Usiku huo haukua mzuri tu kwa Nanaa, hata Geb alilala kama katoto
kachanga. Tokea walipotua Marangu mpaka siku ya jumapili asubuhi wanaondoka
Marangu mtoni, Geb hakuwa akila wala kulala vizuri. Usiku huo wa jumapili
kuamkia jumatatu, ulisindikizwa na ujumbe kutoka kwa Nanaa, ‘Usiku mwema
Geb. Mungu akusaidie upate usiku mtulivu na upumzike. Kesho uamke ukiwa na
nguvu mpya.’ ‘Asante na wewe Nanaa. Nitakuona kesho.’ Sio kuwa Nanaa alikuwa mbali. Ni chumba kinachofuata tu.
Ndani ya nyumba yake. Lakini ile kujua Nanaa yupo hapo nyumbani kwake, akili
yake ilitulia kabisa. Geb alisoma ule ujumbe kwa kurudia rudia, mpaka akapitiwa
na usingizi. Kwa sababu alikuwa ameshiba, hata hakugeuka usiku.
~~~~~~~~~~~~~~
Kila mtu aliamka akajitayarisha
kwenda kazini, lakini isivyo kawaida ya Geb hakuwa ameamka. Grace alitoka
chumbani akiwa yupo tayari yeye na Fili. Akamkuta Nanaa
ameshajiandaa. “Nisubiri nimlishe huyu mara moja ndio tuondoke. Mwalimu
wake anasema hataki kula akiwa shuleni. Nahisi anakuwa na michezo
mingi.” Grace aliongea huku akijaribu kumuweka mwanae kitini ili amlishe
kwanza kabla hajampeleka shule. Nanaa akanyamaza.
Mama G naye akaamka akajitayarisha.
Akatoka chumbani muda mmoja na Danny. Nanaa akasikia wakisalimiana koridoni
wakija pale sehemu ya kupata kifungua kinywa. “Wewe! Mbona umesimama hapo
na wasiwasi?” Mama G akamuuliza Nanaa. “Njoo nikwambie
kitu.” Nanaa akamshika mkono na kumvutia jikoni. “Unamfahamu
Geb?” Nanaa akaanza kumuuliza mama G, akabaki akimwangalia. “Nijibu
bwana mama!” “Simfahamu.” “Mimi sijui nianzie wapi bwana!” Nanaa
alionekana ameshachanganyikiwa. “We Nanaa? Hebu niangalia
kwanza.” Nanaa akamwangalia. “Haya ongea.” “Sijui nianzie wapi sasa!”
“Ujue Grace atakuacha wewe, shauri yako! Endelea kujizubaisha.” “Ndio shida
yangu hiyo. Lakini sijui nimwambie nini? Sasa kwa nini umechelewa kuamka bwana
mama?” Mama G akaanza kucheka.
“Usicheke kwa sauti sasa!” “Kwa hiyo
leo hutaki kwenda na Grace?” “Shhhhhhh! Punguza sauti mama! Grace bosi wangu.
Na natakiwa kazini saa 2. Lakini mimi sitaki kwenda naye.” “Unataka kwenda na
Geb?” Mama G akauliza. “Unaona unavyoelewa haraka!” Nanaa
akaendelea. “Mwenzio Geb ameniambia kuanzia leo tutakuwa tukienda naye
kazini na kurudi pamoja. Ila akichelewa kutoka, ndio niwe narudi na Grace.
Lakini nisilale mpaka yeye awe amerudi. Nikakubali. Sasa unakumbuka uliniambia
ukimuahidi kitu Geb lazima utimize?” “Nanaa wewe! Acha kuniingiza kwenye
mipango yako! Mbona wakati ulipokuwa ukikubali hukunishirikisha?” Nanaa
akacheka.
“Sasa hapo ndipo unapotakiwa kucheza
karata zako vizuri. Usiniharibie kazi kwa bosi wangu, halafu tumpe kiziwanda
anachotaka. Yaani akiamka hapo, anikute nikimsubiria hapa. Kumbuka leo ni
jumatatu. Natakiwa niwepo kazini muda mfupi sana kuanzia sasa. Sasa wewe nenda
kanirekebishe mambo hapo kwa bosi wangu. Nashauri ‘play mama
card’. Lazima atakusikiliza tu. Haya nenda.” Nanaa alikuwa
akinong’ona. Mama G akaanza kucheka mbavu hana.
“Nanaa wewe ni mtundu sana!” “Sasa
wewe unafikiri nitafanyaje kwa hali hii? Nianze kuomba ruhusa mapema hivi!? Si
nitafukuzwa kazi? Halafu namwambiaje Grace?” “Mbona mke wangu muelewa
sana?” Danny akadakia akiwa yupo sehemu ya kulia chakula. Grace akaanza
kucheka. Nanaa akabaki ameshika mdomo. Mama G alikuwa anacheka mpaka anatoa
machozi. “Uwiii mimi! Sitakaa nikatoka chini ya hii meza mama.” Nanaa
akanong’ona. “Hapo ndipo utakapo fukuzwa kazi sasa. Na huyo Geb unayetaka
kumsubiria akiamka hatakuona huko chini ya meza. Utakosa vyote,
kote.” Danny akajibu tena, nakufanya kila mtu azidi kucheka.
“Haya Danny ondoka zako. Nenda
kazini.” Grace akamfukuza huku akicheka. “Kwani na wewe Grace, bosi
wangu umesikia kila kitu!?” Nanaa akauliza kwa aibu akiwa
jikoni. “Kuwa unataka kumsubiria Geb?” Danny akauliza huku akitoka.
Kila mtu alikuwa akicheka. “Sio mimi, ni Geb mwenyewe!” Nanaa
akajitetea. “Wewe msubirie tu. Mimi nitaanzia ofisini kwako kupokea pesa
zote za tokea tuondoke mpaka jana jumapili. Wala usijali.” “Mwaya mama hajui
kunong’ona!? Siku nyingine nakutoa nje ya nyumba kabisa!” Mama G alikuwa
akicheka na kushindwa kuongea.
Mara Geb akatoka chumbani kwake akiwa
bado na nguo za kulalia. “Asante kwa kumruhusu Nanaa.” Geb
alimshukuru dada yake huku akielekea jikoni. Nanaa aliposikia hivyo,
akakimbilia nyuma ya mlango akaufungua mpaka mwisho akajificha. Mama G akazidi
kucheka. “Shhhhh!” Geb akaingia jikoni. Kwa kuwa mlango ulikuwa
umefunguliwa mpaka mwisho na mama yake alikuwa amesimama hapo akicheka peke
yake, Geb alikwenda moja kwa moja nyuma ya mlango akamchungulia
Nanaa. “Uliamka salama?” Akamuuliza palepale alipokuwa amejificha.
Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Tunaondoka sasa hivi. Sitakuchelewesha
sana kazini. Usiwe na wasiwasi.” “Kwani na wewe umesikia?” Nanaa
akamuuliza, Geb akabaki akicheka. “Bwana hujasikia. Eti Geb?” Geb na
mama yake walibaki wakicheka.
“Toka sasa uje unywe chai. Kila mtu
kashasikia.” Mama G akavuta kiti akakaa. “Ni mama ndio hajui
kunong’ona!” Geb alibaki kucheka. Grace akaondoka mapema na mwanae. Kwa
kuwa alikuwa akimshusha kwanza shule ndio aende kazini. Ilikuwa bado ni saa 12
asubuhi, bado hata saa moja haijafika. Wakati wote walikuwa wakitoka mapema
sana ili kuwahi foleni.
~~~~~~~~~~~~~~
Maisha yakaanza kati ya Geb na Nanaa.
Geb ndiye alikuwa dereva wa Nanaa. Kumpeleka na kumrudisha jioni. Siku hiyo ya
jumatatu alimfuata kazini muda wa mchana. Akamtoa kwa chakula cha mchana.
Alimtafutia mgahawa mzuri. Wakaenda kukaa na kula chakula kizuri cha mchana,
akamrudisha ofisini kwake na yeye akarudi kazini kwake. Jioni alirudi tena
kumchukua. Lakini kabla yakuondoka, alihakikisha anapata muda pale ofisini
kwake. Akapitia kazi zake zote alizozifanya kwa siku ile. Akamshauri hili na
kumtengenezea lile, ndipo wakaondoka kurudi nyumbani.
Alifanya hivyo jumatatu, jumanne na
jumatano pia. Alihakikisha kila anapofika hapo, anaingia ndani, ofisini kwa
Nanaa na kupitia kazi zake. Ilimradi kuhakikisha kazi yake haina lawama kwa
yeyote. Nanaa alikuwa akifurahia na kuuliza maswali mengi ili kuwa bora zaidi
ya muhasibu wao aliyekuwa likizo.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nikuombe kitu Nanaa?” Geb
alianza siku hiyo ya jumatano asubuhi wakiwa wanakwenda kazini yeye na
Nanaa. “Unataka nini?” Nanaa akauliza kwa upendo. “Naomba
unisindikize Bagamoyo siku ya Ijumaa.” Nanaa akafurahia akataka kukubali
kwa haraka, lakini akakumbuka kitu. “Ningependa twende wote Geb. Lakini
ijumaa ni siku ya kazi. Tena ndio nakuwa nafunga mahesabu ya juma zima. Na
unajua ijumaa Grace huwa anawahi kutoka kazini. Labda ingekuwa siku ya
jumamosi, ningekusindikiza. Unaenda kikazi?” “Nimepata dereva mgeni. Nimeambiwa
mzigo upo tayari. Ukiendelea kukaa hapo muda mrefu, utaharibika.” “Ni
nini?” Nanaa akauliza tena. “Matikiti maji. Yasipoenda kuchukuliwa
ijumaa, mwenye shamba anasema itabidi ayauze kwa hasara, ili yasimuharibikie.
Na huwa tunapenda matikiti yake. Yana maji mengi na matamu. Lazima mimi
niyapate. Nataka kumtuma huyohuyo dereva mgeni. Lakini lazima mimi mwenyewe
niwepo ili nikaangalie upakizwaji wake. Sitaki ayafikishe hapa yakiwa
yameharibika.” Nanaa akanyamaza.
“Ningefurahi tungeenda
wote.” Akamtupia tena jicho. “Hata mimi Geb.” “Kama tatizo ni Grace
tu, usiwe na wasiwasi.” “Hapana. Sio Grace tu, lakini ni majukumu yangu.
Sipendi niwe naomba ruhusa mara kwa mara halafu anaishia yeye kufanya kazi
zangu na zake!” “Usiwe na wasiwasi. Nitazungumza na Grace, apokee pesa yote.
Halafu jumamosi tutaenda kuweka mahesabu yote sawa. Yeye hatafanya kitu zaidi
ya kupokea pesa tu.” Nanaa akafurahia hilo wazo. “Asante. Na
ninakuahidi jumamosi nikiamka tu, nitakimbilia kazini nikakamilishe. Sitaharibu
kazi.” “Utaniacha tena!?” Geb akauliza na kumtupia tena macho wakiwa bado
barabarani. Nanaa akacheka kwa aibu kidogo. Huwezi kutofurahia kuangaliwa na
Geb. Akarudisha macho chini kwa haraka kama kukwepesha.
“Najua siku ya jumamosi ndio siku
yako yakupumzika. Nikiwahi kutoka kwenda kazini, nitarudi mapema hata kabla
hujaamka.” “Nisubiri tutakwenda wote.” Nanaa akatoa tabasamu
lakuridhika. “Basi sawa. Nitakusubiri mpaka uamke ndio twende
wote.” Wakajikuta macho yamegongana na tabasamu usoni.
~~~~~~~~~~~~~~
Hakuna ambae hakuona furaha ya Geb.
Alibadilika akawa mtu mwenye furaha kila wakati. Akili ilikuwa imetulia.
Chakula kinaliwa bila shida. Hakuna kununa wala kulalamika. Asubuhi alitoka na
Nanaa, na hata jioni walirudi pamoja, japo wakati mwingine kwa kuchelewa. Kila
Geb anapokuwa akipanga kukosa siku moja ya kazi ndani ya week, alikuwa
akichelewa kurudi nyumbani. Ilimlazimu kufanya kazi zaidi ili kupunguza
majukumu ya siku hiyo ambayo asingekuwepo kazini na asilemee wenzake.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo ya jumatano baada yakutoka
kazini Geb alimpitisha mahali kula ice cream. Walikaa hapo wakiongea na
kucheka. Geb alikuwa akimwangalia kwa kumtamania sana. Vile alivyokuwa akicheka
na mashavu kubonyea, ilimfanya Geb kucheka na yeye huku akimwangalia. Kitu
kidogo tu, Nanaa alikuwa akicheka na kumfariji Geb. Kwa siku hizo chache tu
tokea aanze kwenda na Nanaa kazini au kuwa naye karibu, tayari maisha yake
yalibadilika. Utulivu wa akili na amani ya moyoni aliyokuwa nayo Geb, aliomba
iwe hivyo daima. Asijue amempokonya mama yake rafiki.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwani muda mwingi Nanaa alikuwa
akiongea na mama G ambaye alikuwa peke yake mle ndani. Geb alikuwa busy na Liz.
Grace na familia yake. Na wote wawili, Danny na Fili walitaka kumuona Grace
kila wakati. Walikuwa wakishindana kumuita. Nanaa na mama G walikuwa
wakiwasikiliza na kucheka. Ikitokea Grace ananyanyuka tu na kuhamia sehemu
nyingine, Danny na mtoto wake wataanza kumtafuta. Kwa hiyo muda aliokuwa akiupata
Grace na mama yake ulikuwa mfupi sana. Mara zote ungemkuta Grace na hao watu
wawili. Danny na Fili. Hata kama Danny atakuwa anacheza game na mwanae kwenye
tv, lakini watataka Grace awepo hapo pembeni yao. Akinyanyuka tu, mchezo nao
ujue umeisha.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nataka nimpelekee mama ice cream.
Kwa hiyo tuwahi kurudi nyumbani kabla hajalala.” Nanaa alimwambia Geb.
Wakamalizia za kwao, wakanunua na ya mama G, wakaondoka kuelekea nyumbani. Geb
alichelewa kutoka kazini, akamkuta Nanaa akimsubiria tu ofisini. Hakutaka
kuondoka na Grace mapema. Akampeleka kwenye icecream, mpaka wanafika nyumbani,
tayari ilikuwa saa 3 na robo usiku. Moja kwa moja chumbani kwa bibi Fili.
“Nimelala Nanaa. Wewe vipi bwana?”
“Kama ndio hivyo sikupi zawadi niliyokuletea. Endelea kulala.” Nanaa
akajidai anataka kutoka. “Njoo mwanangu Nanaa.” Geb akawasha taa.
Wakacheka. “Unapenda zawadi mama wewe!” “Nipe basi hiyo zawadi, acha
kuniweka roho juu!” Nanaa akampa ile ice cream. “Haya ndio majaribu
haya! Sasa ice cream hii saa hizi!? Wakati nimekwambia kabisa nimeambiwa kama
nataka haya magoti yapone, basi nipunguze huu mwili.” “Basi nirudishie
nikakuwekee kwenye friji mpaka kesho.” “Aiii! Sitaweza kulala. Heri tu
niile.” Wote wakazidi kucheka. Geb akajirusha kitandani kwa mama yake,
Nanaa akakaa kitanda cha pembeni.
“Muone alivyojawa furaha.” Mama
G akamchokoza Geb. “Ni kawaida yangu.” Geb akajibu huku akicheka. “Mmmh!” Mama
yake akaguna. “Mmekula sasa?” “Bado.” Nanaa akajibu. “Mbona
mmechelewa hivyo?” “Mimi ndio nimechelewa kutoka kazini.” “Sasa wewe Nanaa si
ungerudi na Grace? Umekaa mwenyewe kazini mpaka saa hizi!?” “Nilimuomba
anisubiri. Kwani umechoka?” Geb alijibu na kumuuliza Nanaa. Nanaa
akatingisha kichwa kukataa. “Mmmh!” Mama G akaguna huku akiendelea
kula ile ice cream yake akiwatizama kwa zamu. “Sasa unaguna nini
mama?” Geb akamuuliza huku anacheka. “Nasafisha koo.
Niache.” Wakacheka.
“Inanisaidia kujua…” Nanaa
akanyamaza na kuanza kucheka. Mama G akabaki amemkodolea macho. “Bwana
mimi naenda jikoni kumchukulia Geb chakula.” Nanaa
akasimama. “Umeanza mwenyewe! Kaa hapo chini uyamalize.”
“Nini?” Nanaa akauliza huku akijua mama G anachouliza. Ila alitaka
kumzungusha tu. “Huko kukaa kazini unamsubiria Geb. Inakusaidia nini wewe?
Usiyerudi hapa nyumbani ukapumzika wakati unamsubiria hapa kama si kuchoshana
tu?” “Mama wewe! Kuchoshana? Usiseme hivyo!” Geb na mama yake waliangua
kicheko. Nanaa akatoka anakimbia kuelekea jikoni kuleta chakula.
Alikuta mama yake alishampikia Geb
chakula chake na kipo chakula cha nyumba nzima. Akapakua chake na cha Geb
akarudi chumbani wakawa wanakula huku wanaongea.
“Ijumaa naenda na Nanaa
Bagamoyo.” Geb akamwambia mama yake. “Kazi ipo.” Mama G akaongea
huku akiendelea kula ice cream yake. Wakacheka. “Tunaondoka saa
ngapi?” Nanaa akauliza huku akicheka. “Nikishakunywa uji wa Bibi Fili ndio
tunaondoka.” “Mbona hiyo biashara nilishamkabidhi Nanaa? Yeye ndio anakibarua
cha kuupika huo uji kila siku asubuhi.” Mama yake akajibu. Geb
akamwangalia mama yake. “Unaniangalia nini sasa? Siamki siku hizi asubuhi
asubuhi. Nanaa ndio anaamka, anakupikia huo uji. Anakuwekea kwenye bakuli na
mwingine kwenye chupa wa kunywa kazini.” Geb akainamisha kichwa kwenye
mkono wake.
“Aibu zako! Baba mzima unakunywa uji
mpaka leo!” “Ni wewe mama ndio umenianzishia kunywa uji.” “Si kwa kuwa huli!
Yaani alikuwa anarudi hapa nyumbani hajala siku nzima. Alibaki mifupa tu
huyu.” Nanaa alikuwa akicheka taratibu huku anakula. “Nakula bwana
mama. Mbona nakula ugali?” “Lakini hutaki mchuzi utakao kuwa na kitunguu au
karoti.” “Lakini nakula na mboga za majani.” Mama yake akaguna. “Nini
sasa?” “Na hivyo vyakula vyenyewe vipikwe humu ndani na dada yake au mimi,
lakini si vinginevyo.” “Nyamaza mama bwana! Nanaa atanikimbia bure.” “Kwani
unafikiri hakujui kuwa unashida ya kula? Anakujua sana.” “Eti
Nanaa?” Nanaa alibaki akicheka tu.
“Wewe ukitaka aendelee kuongea huko
mtakapo kuwa, hakikisha anakula mara kwa mara.” “Mama! Nyamaza bwana.”
“Ukimuona maneno hayatoki ujue ni njaa tu. Beba karanga zakutosha. Korosho
zake. Halafu usisahu ile chupa ya uji, juice na maji ya kunywa. Hapo mtawezana.
Halafu sio ubebe tu halafu usimpe, ujue hatakukumbusha mpaka mnarudi hapa.
Utarudi navyo. Vitu vyake vyakula ni vitu vidogo vidogo, tena uwe unamkumbusha
kula. Mshikishe mkononi kabisa. Yaani hakikisha vimefika kwenye mkono wake,
hapo ndipo vitaingizwa mdomoni, lakini si vinginevyo.” “Mama! Usimfanye Nanaa
akagairi kwenda na mimi bwana! Hali sio mbaya hivyo. Huwa nakula
bwana.” Geb alijitetea. “Basi wewe usimpe, halafu utakuja kuniambia
kama alikula.” “Nitakula bwana.” Geb alizidi kujitetea.
“Huwa hali. Hata tukiwa kazini,
atanifuata tukale, lakini yeye hali. Jumatatu tulipotoka hapa.” “Siku ile
uliyokuwa hutaki kuondoka na bosi wako?” Wote wakacheka. “Wewe ndio
uliharibu mama. Huwezi kunong’ona!” “Mmmh! Mbona sasa Danny alisikia maneno
yako na si yangu?” “Mimi sijui! Lakini akanifuata mchana tukale. Mimi nikajua
maana ya twende tukale, ni tunaenda kula wote. Yaani na yeye atakula.
Nikashangaa anaagiza chupa ya maji baada ya kunisisitiza mimi niagize chakula
kwanza. Nikadhani ataagiza chakula baadaye. Unajua tukaondoka hajala! Akasema
anawahi ofisini, atakula chakula hukohuko ofisini.” “Ndio kawaida yake kama
humjui.” Geb alikuwa anacheka tu.
“Sasa jana akaja tena. Nikamwambia
kama yeye hali, ni afadhali tusiende. Akasema atakula. Ujue mama akaagiza
matunda tu. Mbaya zaidi wakaleta hayo matunda yamekatwa. Yaani mama, yalikuwa
yanavutia kama nini pale kwenye sahani. Mimi mwenyewe niliyatamania. Unajua Geb
aliyatazama yale matunda kwa muda, kisha akaniangalia. Alipoona namtizama.
Akamwita muhudumu. Akamwambia amletee matunda mazima na kisu. Hataki
yaliyokwisha kukatwa.” “Siamini Nanaa kama na wewe unanigeuka!” “Ni kweli Geb,
unashida ya kula.” Hapo alipokuwa, Geb alikuwa akila bila shida. Kitandani
kwa mama yake. Alikaa vizuri akawa amepakata sinia lake la chakula.
“Sasa akayala hayo
yaliyoletwa?” Mama G akauliza. “Sasa matunda yenyewe aliyoagiza sasa.
Tango, karoti, parachichi na nyanya.” “Na usifikiri ameagiza hapo kwa bahati
mbaya? Aliagiza hivyo makusudi ili wamwambie kimoja wapo hakipo, aseme basi.”
“Uzuri vyote aliletewa, tena baada ya muda mfupi sana. Ikaanza kazi ya
kuviosha.” Mama G akaanza kucheka. “Chupa ya kwanza ikaisha,
akaagiza ya pili.” “Hapo ujue alikuwa anavuta muda ili umalize akwambie
twende.” “Sasa na mimi nikawa nimeduaa namtizama.” Geb na mama yake walizidi
kucheka.
“Ni kKwa kuwa hujamjua tu. Kila mtu
anamjua Geb. Ndio mtindo wake huo. Wala hakuwa akifanya usafi wa hayo matunda.
Alikuwa anapoteza muda tu, umalize muondoke asiyale hata hayo matunda.” “Basi
nitabadilika.” “Mmmh! Usimdanganye mwenzio. Tangia mtoto mdogo ndio yupo hivyo
hivyo. Nishampa madawa ya kuongeza hamu ya kula mpaka nikachoka. Si madawa ya
mahospitalini, si miti shamba! Amekunywa mpaka nikasalimu amri. Watu
wakaniambia akikuwa atabadilika, lakini sioni dalili. Namwambia akiona anachoka,
hawezi kuongea, ajue ni njaa. Ale. Wapi! Basi huwa nikiona yupo kazini,
ananipigia simu mara kwa mara na kulalamikia mambo yake mengine, najua ni
hasira za njaa tu. Maana akishiba huyo, hana shida na mtu. Hata umkanyage
makusudi, hutamsikia akiongea. Kimyaa.” Geb alikuwa akicheka.
Safari Ya Bagamoyo.
G |
eb alishazungumza na Grace juu ya kutokuwepo Nanaa kazini siku ya
ijumaa. Kama kawaida ya Grace, hakuwa na neno akijua kazi za Nanaa, atazifanya
tu Geb mwenyewe. Kwa kuwa ni biashara yake, hatakubali kitu kiharibike. Siku ya
ijumaa asubuhi, Nanaa aliamka asubuhi kama kawaida yake. Akapika uji na chapati
kwa ajili ya watu wote watakapoamka. Akakusanya vitu alivyonunua Mama G kwa
ajili ya kula Geb njiani. Akaweka kwenye kibegi kidogo cha chakula ambacho Geb
huwa anasafiria, na mama yake ndipo anapoweka vyakula vyake, na yeye akavipanga
kama alivyofundishwa na mama G. Alipohakikisha kila kitu ambacho angehitaji
njiani kipo tayari akavichukua na kuweka kwenye meza iliyokuwepo karibu na
mlango. Ili wakitoka wasisahau. Wakati anasafisha jikoni, Geb akatoka chumbani
akiwa ameshajiandaa. Wakati Geb akinywa uji, yeye akarudi chumbani
kujitayarisha. Wakatoka nyumbani saa 12 asubuhi.
Mwanzo
Mwingine Mpya.
“Si utakuwa na usingizi? Vuta kiti
nyuma ulale kidogo.” “Maisha yangu yote nimeshazoea kuamka kabla ya saa 11
asubuhi. Sikumbuki kuamka kabla ya hapo. Kwa hiyo nipo sawa tu.” “Haiwezekani!”
“Kweli tena, tokea nipo mtoto.” “Na mchana huwa unarudi kulala?” Nanaa
akacheka sana. “Urudi kulala mchana halafu nani atafanya kazi?” Geb
akamwangalia na kubaki akishangaa.
“Sasa kwa nini ulikuwa unaamka
mapema?” Geb akaendelea kuhoji. “Nilikuwa naamshwa kusaidia kazi, au
kuwaandaa kina Viola kwenda shule. Labda kuhakikisha kabla hawajaamka nguo zao
zimepigwa pasi, soksi zote zipo tayari, viatu visafi, na chai ipo tayari ndio
unawaamsha. Kama watataka kuoga asubuhi, si unajua Moshi kuna baridi? Basi
unakuwa ulisha wachemshia maji yakuoga, ili waoge. Wakishamaliza kunywa chai,
unaosha vyombo, ndio na wewe ujiandae haraka uwahi shuleni.” Geb aliulimia
sana, kwani kina Viola ni umri sawa na Nanaa. Lakini Nanaa alikuwa anacheka
kama kawaida yake.
“Sasa kwa nini usizifanye hizo kazi
ukitoka shule?” “Ilikuwa inategemea. Wakati mwingine Viola na mdogo wake
walikuwa wakitoka shule, wanaenda tuition. Mimi nawahi kurudi nyumbani kupika.
Wakirudi wanakuwa wamechoka. Labda wanasema wanataka kula kwanza. Kwa hiyo
inabidi kuwatayarishia chakula. Wakimaliza kula, unamsaidia dada kuosha vyombo.
Maana kazi ya kupika mara nyingi ilikuwa hivi, mchana nikiwa shule ni dada ndio
anapika. Jioni nikitoka shule napika mimi na kuosha vyombo vya usiku.
Kutayarisha vitafunio vya asubuhi ilikuwa inategemea. Kama mimi na dada
hatujachoka sana, tunapika usiku ili tukiamka inakuwa kupika tu chai. Mama
Mkubwa hakuwa anataka chai iliyo lala. Tukichoka sana, ndio tunaamshana asubuhi
na mapema zaidi. Mimi napika kitafunio, yeye anafanya kazi
nyingine.” Nanaa akaendelea.
“Haya, turudi ratiba ya usiku, kama
nilivyokwambia mimi ndiye nilikuwa mpishi wa usiku. Napika, nawatayarishia
mezani au sebuleni walipokaa. Unawasubiria wale. Wakati wao wanakula labda na
mimi nakula kama sijachoka sana au siumwi ndio nitakula. Lakini mara nyingine
wakati wakila kama nimechoka, nasafisha jikoni kupunguza kazi huku
unawachemshia maji ya kuoga na kuwawekea kwenye ndoo mpaka kiasi cha kuwatosha
wote. Wakishakula hiyo usiku, unatoa vyombo na kuwapelekea hayo maji bafuni ili
waoge. Wakati wanaoga ndio unakusanya nguo zao za shule kwenda kufua, na kuosha
vyombo. Hapo inakuwa usiku tayari, na mimi nakuwa nimeshachoka, nataka kwenda
kulala, tayari kwa asubuhi.” Geb alizidi kushangaa.
“Kwani walikuwa na sare ya shule moja
tu?” “Mbili. Lakini Mama mkubwa hakuwa anataka kulaza ndani nguo chafu au
vyombo vichafu. Lazima mkienda kulala, mnaacha nyumba yote safi. Hata na mimi
ilikuwa inanisaidia kufua nguo chache kuliko nikizirundika zikawa nyingi.”
“Ngoja kwanza Nanaa. Ulikuwa ukiwafulia wote?” “Ndiyo! Sasa unafikiri nani
atafua?” “Wao wenyewe au msichana wa kazi!” Nanaa akacheka.
“Pale ndani tulikuwa tunafuga kuku,
ng’ombe na mbuzi. Kwa hiyo dada alikuwa akikamua kila siku asubuhi na jioni
akisaidiana na baba mkubwa. Mama mkubwa alikuwa akinunua tu majani, hapakuwa na
kijana wakufuga. Ila kusafisha banda walikuwa wanalipa kijana wa jirani anakuja
kusafisha. Ila ikitokea huyo kijana hajaja labda amepata dharula, ndipo
tutasaidia. Kwa hiyo dada alikuwa akimka asubuhi kama mimi. Anakwenda kwenye
banda la kuku kuokota mayai. Kuosha vyombo vyao na kuwaekea chakula na maji.
Pakianza kupambazuka, anahamia kwenye banda la ng’ombe kukamua. Wakati huo na
mimi nafanya kazi za ndani.”
“Kwa nini kina Viola walikuwa
hawakusaidii lakini!?” Geb akamkatisha. “Walikuwa wakilalamikia baridi ya
asubuhi na jioni. Hawawezi kukaa nje au kushika maji ya baridi. Na mara zote
walikuwa wakitoka shule wanakuwa wamechoka.” Geb akamwangalia Nanaa
akanyamaza akaendelea kuendesha.
“Lakini Geb, namshukuru sana Mungu.
Katika yote hayo, niliweza kusoma. Japokuwa sikuwahi kufaulu sana darasani,
lakini nilikuwa nikipita kwenye hayo madarasa kimiujiza ujiza tu. Sikuwahi kuwa
na masomo ya ziada, tuition. Sikuwahi kuwa na makundi ya kujisomea, au muda
wakukaa chini kurudia nilichofundishwa darasani. Kama sikuelewa darasani, ndio
basi tena. Sikutani na hayo madaftari mpaka nikiwa darasani. Lakini Mungu
alikuwa akinipitisha kwa namna yake.” Geb akamwangalia na kunyamaza.
“Hakuna kipindi ulikuwa
ukichoka?” Baada ya muda Geb akauliza. “Kuchoka na kazi, hapana. Kwa
kuwa sikuwa najua maisha mengine mbali na yale. Nimezaliwa hapo, na kukua hapo.
Hata wakati wao walipokuwa wakisafiri labda wanaenda kwa bibi kijijini, kama
nitachukuliwa mimi, basi ujue ni kwenda kuwasaidia kazi. Kwa hiyo hata
tunapokuwa huko kijijini ratiba inaweza isibadilike sana. Au naweza
nikaongezewa majukumu mengine kwa kuwa dada anakuwa amebaki yeye nyumbani. Na
kama nitabakishwa mimi, ujue dada wa kazi atakwenda nao. Kwa hiyo majukumu yote
ya pale ndani nabakiwa nayo mimi. Tokea ninakuwa nilikuwa nikifanya kazi hizo
hizo. Masaa ya kulala ni yaleyale. Na maisha hayakubadilika sana, mpaka
tulipokuwa wakubwa ndipo mambo yalipobadilika.” Nanaa akatulia kidogo kama
aliyekuwa akijaribu kujituliza.
“Yalibadilikaje tena!?” Geb
akauliza. “Tokea zamani, kulikuwa na hii shauku ya ‘sense of belonging’. Sujui kama utanielewa. Yaani ile shauku ya kutaka kuhisi
ninahitajika mahali, au kwetu ni sehemu fulani. Yaani na mimi nihesabike kama
ni mmoja wa familia hiyo sio mzigo. Yaani ni kama nilikuwa natamani itokee siku
moja mtu ananiambia ananihitaji mimi.” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.
~~~~~~~~~~~~~~
Geb akakumbuka mkasa aliomsimulia.
Kuanzia yupo tumboni wazazi wa mama yake walimfukuza mama yake Nanaa, hata
mwanaume ambaye alisadikika ni baba yake Nanaa, alimkana mama yake alipopelekwa
mjamzito akiwa na mama yake mkubwa. Na hata baada ya Nanaa kuzaliwa akiwa mtoto
mdogo kabisa ndio amezaliwa tu baada ya kifo cha mama yake, mama yake mkubwa
aliporudishwa nyumbani kwa huyo mwanaume, wazazi wa huyo mwanaume pia walimfukuza
mama mkubwa akiwa na Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Pole
Nanaa.” Geb alijikuta akitoa pole baada ya kumbukumbu hiyo kujirudia
akilini mwake. “Yaani habari au jambo la kwanza nahisi nililolielewa tokea
napata akili zangu na mama mkubwa alihakikisha analiweka sawa, kuwa pale
ninapoishi sio kwetu, nasaidiwa tu, na mimi ni mzigo. Yaani hilo ni jambo
nilikuwa nikiambiwa nafikiri kila siku, mpaka majuzi nilipoenda kumsalimia kwa
kaka James, aliniambia. Mama mkubwa alihakikisha ninaelewa hilo. Hakuacha
kunilalamikia kuwa anahangaika sana kuniweka pale. Baba mkubwa alishakataa
kunisaidia kwa lolote. Kwa hiyo niliishi hapo kwao, mama mkubwa ndiye aliyekuwa
akinihudunia kwa kila kitu. Lakini Geb, hakika nilikuwa nikilipia ule msaada
kwa machungu sana. Hata akikupa shilingi yake, atahakikisha atakuelezea jinsi
alivyoipata kwa shida. Jinsi ambavyo anamahitaji mengi, lakini inamlazimu
kunipa mimi. Na mara zote alikuwa akijiambia mbele yangu kuwa mimi ni mzigo
ambao hajui atautua lini.” Nanaa aliongea huku akitokwa na
machozi. “Pole sana Nanaa. Naomba usilie.” Geb akajaribu kumtuliza.
Akatulia kidogo.
“Unajua, nilizaliwa mwaka
mmoja na Viola. Mama yangu akafa akiwa anajifungua kama nilivyokusimulia. Kwa
hiyo anasema tokea nazaliwa mpaka leo, nimekuwa tatizo ambalo hajui Mungu
atampumzisha lini. Anasema hakuwa akilala tokea mimi nazaliwa kwa kunibadilisha
nepi na kuninyonyesha. Ilibidi kuninyonyesha kama Viola kwa kuwa anasema
nilikuwa mlizi sana. Anasema nilikuwa nikilia usiku kucha. Kwa hiyo anasema
hakuwa akilala kwa ajili ya kunibembeleza na kuninyonyesha. Na anasema
mpaka leo halali akifikiria jinsi ya kunilea. Anasema ni mzigo ambao hajui ni
lini Mungu atampumzisha nao. Na ndio anasema sasa hivi ndio imekuwa mbaya
zaidi.” “Daah! Pole sana. Pole Nanaa. Naomba usilie.” Geb
alizidi kuumia.
Nanaa akatulia kidogo. “Kwa
nini anasema sasa hivi imekuwa mbaya zaidi wakati hauishi naye tena?!” Geb
alikuwa na maumivu yaliyompelekea kutaka kujua zaidi. “Anasema alijua kaka
ndio angekuwa msaada pale nyumbani, lakini anaumia kuona misaada ya kaka yote
inahamia kwangu sio kwao. Nimechukua nafasi yake kwa kaka. Kaka hawezi kusaidia
ndugu zake, wala hawezi kuoa, eti kwa ajili yangu. Anasema nimekuwa tatizo
ambalo halijawahi kuisha na wala hadhani kama itakuja kuisha mpaka naona nije
kuwa na kwangu, na maisha mbali na yeye na watoto wake. Hapendi kabisa hivi kaka
James anavyonisaidia. Anaumia sana. Kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo
nahisi nachoka moyoni. Sijui nifanyeje kujikwamua! Nimejitahidi kwa kadiri ya
uwezo wangu, lakini naona juhudi zangu zinagonga mwamba. Nikijitahidi hivi,
najikuta kama siharibu kwa wengine basi ujue nitaumia vibaya sana.” Nanaa
akatulia kidogo.
“Nimekuwa nikifanya kila niwezalo
kuondoka pale nyumbani, au kutafuta mtu ambaye angalau atanipokea. Lakini wapi!
Nimeishia kujidhalilisha tu. Wakati mwingine nilikuwa nikifanya mambo ya
ajabu, ili tu kuridhisha wanaume, wanichukue. Nakumbuka bado nilikuwa mdogo tu.
Tena sekondari, wakati nikimkubali mwanaume ambaye alikuwa mkubwa kwangu. Tena
alikuwa akisoma chuo kwa matumaini kuwa akimaliza chuo, akipata kazi, anichukue
ili nitoke pale kwa mama mkubwa. Ndiye alikuwa mwanaume wangu wa kwanza
kabisa.” “Alex?” Geb akadakia kwa kuuliza. Nanaa akashituka
sana.
Maana Geb aliuliza kana kwamba yeye
ndio James. Yaani ni kama watu waliokuwa wakifahamiana tokea zamani. Akamgeukia
vizuri. “Umemjuaje!?” Geb akacheka. “Ukumbuke nimesoma na James,
na ni rafiki wa karibu sana kwetu kama ndugu. Lile kundi lote pale, wengi
tulikuwa pamoja tokea sekondari halafu wengine tukakutana tena chuoni. James
anakupenda sana, huwa haachi kukuongelea.” Nanaa
akashangaa. “Ananiongelea kwenu!?” “Kabisa. Na ukitaka kuona ubaya wa
James, mtu akuguse wewe lakini si vinginevyo.” Nanaa akabaki na maswali
kidogo. Asijue aendelee vipi.
“Kwa hiyo alituambia vile Viola
alivyozaa naye Alex na mama yao kuona ni sawa tu.” Geb alielezea historia
nzima kwa kifupi na kumfanya Nanaa abaki anashangaa. “Kumbe unanifahamu
hivyo!!?” Nanaa akazidi kushangaa. “Sio sana. Endelea.” Geb
alijibu huku akicheka.
“Lakini Geb, Viola hakuniumiza kama
Alex. Yule kaka nilijitoa kwake kupita kiasi. Yaani ndiye mwanaume wangu wa
kwanza kulala naye. Nilikuwa naenda umbali wa kudanganya nipo shule, kumbe
nipo naye kwenye nyumba za kulala wageni, kumridhisha yeye ili anipende tu.
Huku nikimuomba aje anioe. Shida yangu ilikuwa nitoke tu pale kwa mama mkubwa
nimpunguzie mzigo. Na nilikuwa nikimwambia kila kitu! Yaani alikuwa akimjua
Viola, tabia zake, kila kitu. Lakini alikuja kuzaa na Viola, na akawa anakuja
palepale nyumbani, ananiona vile ninavyomuhangaikia na Viola aliyekuwa mjamzito
wa mimba yake.” Nanaa akafikiria tena kidogo.
“Haya, sikukata tamaa.
Nilipofika chuoni tena nikakutana na kijana mwingine aliyekuwa mwaka wa pili.
Tukaanza mahusiano. Jinsi alivyokuwa akionyesha kunipenda, nikajua atanioa
kabisa. Yaani Geb, yule kaka alikuwa akinipenda na kunijali kupita matarajio
yangu. Alikuwa akiishi Mabibo hosteli, na mimi nilipata chumba Main Campus.
Lakini kila siku atataka kujua nimeamkaje na kunitakia usiku mwema. Uzuri
wangu, niliujua kama upo mwilini mwangu kutoka kwake. Sikuwahi kujithamini
mpaka nilipokuwa na yule kaka. Alikuwa akinisifia kila kitu changu. Tukiwa peke
yetu hata mbele za watu. Angalau watu wakaanza kuniangalia kwa tofauti.
Alinyanyua uthamani wangu. Kutoka mavumbini, na mimi nikajiona mtu. Nikajua kwa
mara ya kwanza maishani, nimepona.”
“Naye nikaja kumfumania na msichana
aliyekuwa akijua kabisa tunamahusiano. Walikuwa darasa moja na kwenye kundi
moja la kujisomea. Lakini nikawafumania. Sasa nikawa najiuliza, kama alikuwa na
mahusiano na yule dada waliyekuwa wameanza naye tokea mwaka wa kwanza, kwa nini
alinifuata tena mimi! Yaani ni kama alikuwa akinichezea tu! Si mwili wangu tu,
mpaka hisia zangu. Tena bila huruma! Huku akijua ni kiasi gani nilikuwa
nikimuhitaji.” “Huyo alikuwa Zac?” Geb akauliza, Nanaa akamgeukia na
kubaki akimtizama. Geb akacheka.
“Kwa hiyo wewe unafahamu kila kitu
changu!?” Geb akazidi kuckeka. “Nilikwambia huwa sisahau kitu, Nanaa.
Sasa wakati upo kwenye mahusiano na Zac, James alituambia kuwa amefurahi
angalau ulipata mwanaume mwingine anayeonekana kukupenda na kukuthamini sana.
Alikuwa amekuahidi akimaliza chuo atakuoa.” Nanaa akanyamaza kwa muda,
akabaki akiwaza.
“Nakusikiliza, Nanaa. Shauku yako
ndio ikaishia hapo?” “Hapana, Geb. Sikutaka kukata tamaa, nikaja kuangukia tena
kwa mwanaume mwingine.” Nanaa akacheka. “Unacheka nini?” “Najicheka
mwenyewe! Yaani sijui nikuchanganyikiwa au vipi? Nilijitupia kwa Jamal kama
mwendawazimu.” “Jamal si ni mwislamu?” “Kumbe! Yaani nilikuwa hata tayari
kubadilisha dini ili tu aje anioe.” Geb akamwangalia.
“Najua utaniona nimechanganyikiwa,
lakini ndivyo ilivyokuwa. I was that desparate. Kutaka kutoka kwenye
maisha ya zamani, kuingia kwenye maisha mapya. Nikajitupia kwa Jamal, akili
zote na mwili, tena bila kufikiria. Hatukukaa hata muda mrefu sana na Jamal,
tena hata sikumtambulisha kwa kaka, ndipo nilipokuta ujumbe kutoka kwa mkewe.
Alikuwa mtu wa Tanga, ana mke na mtoto. Mkewe anamtafuta kule, kumbe yupo huku
na mimi. Niliumia sana, nikimuhurumia mkewe. Alikuwa akimsubiria nyumbani,
mtoto mgonjwa, kumbe yeye yuko na mimi huku anastarehe. Aliniudhi, sikutaka
hata kumuangalia mara mbili, nikaondoka.”
“Sasa si ndio kitu ulikuwa unataka?
Mtu anayekuhitaji wewe kuliko mtu mwingine?” “Geb! Sio kihivyo. Yaani amuache
mwanamke wake, aliyemuoa na kumpatia mpaka watoto, aje kwangu! Nitampa nini
ambacho amekosa kwa mkewe? Halafu nilijua wazi ipo siku ambayo angenifanyia
kama alivyomfanyia mkewe, endapo angepata mwanamke mwingine wakunizidi mimi au
atakayeweza kumpa kile nitakachoshindwa kumpa. Nilitamani kuwa na mtu wangu.
Mimi mwenyewe. Sio wakumpokonya mtu.” “Ulitamani?” Geb akauliza
lakini Nanaa akanyamaza kwa muda.
“Eti Nanaa? Shauku imeisha?” Geb
akaendelea kudadisi taratibu. “Niliachana kabisa na hayo mambo, Geb. Nilikuwa
natafuta kwa juhudi zote, nimeishia kuumizwa tu, bila mapenzi ya kweli.
Nimetumiwa kwa faida za watu wasiojali hisia zangu. Nimeamua kupumzika labda
shule yangu ndio itakuwa mkombozi. Kabla yakufunga chuo hapa majuzi, alikuja
kaka mwingine, akitaka mahusiano. Achilia mbali kina Jeff na wengineo. Yule
kaka alikuja na ahadi nyingi zinazosikika vizuri. Akawa akiwahonga rafiki zangu
ili kunifikia, lakini kila nilipojitahidi kufungua moyo wangu kumpokea,
nilishindwa kama ninavyoshindwa kwa wengine sasa hivi. Nafikiri nimekinahiwa.
Sitaki tena. Nimegundua sina nilichobakiza kumpa mtu akaridhika na mimi.
Sitaki kuchezewa tena na wala sitaki kumtumia mtu.” Nanaa akafikiria.
“Nimeamua kusitisha zoezi la
ukolewaji.” Nanaa aliongeza huku akitoa tabasamu lake la huzuni. “Na
imenibidi niwe hata muwazi kwa Zinda.” “Zinda ameumia sana.” “Nafahamu Geb.
Lakini nilimwambia ni heri aumie sasa hivi ili aje apate mwanamke atakayempenda
na kumliwaza, kuliko sasa hivi nimkubalie kwa kuwa nataka nyumba na gari!
Hapana Geb. Nina shida ambayo najua Zinda angeweza kunisaidia. Tena
aliniambia yupo tayari hata kama sio ndoa, basi tuwe kwenye mahusiano naye ili
tuwe pamoja. Ni kitu kizuri sana kwangu kwa sasa hivi. Lakini sikutaka
kumfanyia hivyo Zinda.” Nanaa akaendelea.
“Sitaki awe msaada sasa hivi, halafu
nikaja kufanikiwa baadaye, nikagundua nilikuwa naye kwa ajili ya pesa au msaada
aliokuwa akinipa tu. Nikajikuta hana tena matumizi kwenye maisha yangu.
Nikaamua kumuacha. Ingemuuma zaidi. Ni heri nivumilie shida za sasa, natumaini
muda sio mrefu nitapumzika tu. Kitu cha kwanza nipate kwangu, shule iishe,
kisha nipate kazi. Naamini kutakuwa na utulivu kwangu na kwa wanao nizunguka
pia. Nitapumzisha wengi.” Nanaa akamalizia hivyo, akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~
“Wakati mwingine mahusiano ya muda
mrefu, huleta mapenzi ya kweli.” “Na mimi nilijua hivyo. Lakini si umesikia
historia yangu na wanaume niliokuwa nao? Wakati mwingine haitokei hivyo. Halafu
pia nimechoka Geb. Huo mchezo nimecheza sana na sijaona matokeo yake. Nimeona
ni heri nipumzishe hisia zangu. Sijitendei haki. Ndio maana hata uliponitumia
ujumbe, kuuliza ninaendeleaje, sikutaka hata kuweka ule ujumbe, nikafuta
palepale. Najua ulifanya kiuungwana tu.” “Ki vipi?” Geb akauliza.
“Unajua kama vile unavyokutana na mtu
barabarani, unamuuliza tu ‘Mambo!’ Sio kwa kuwa unataka kujua
yanayoendelea kwenye maisha yake, bali ni kama salamu tu. Na unakuwa hutegemei
aanze kukuelezea matatizo yake au furaha yake, unampita tu baada ya
kusema ‘mambo’, ukitegemea atakujibu tu ‘safi’ hata
kama ni mgonjwa au anamatatizo. Sijui kama unanielewa?” “Kwa hiyo hivyo ndivyo
ujumbe wangu ulivyomaanisha kwako?” Geb akauliza.
“Kwa kusema ukweli ndivyo hivyo.
Hapakuwa na cha ziada nilichofikiria. Kwa kuwa hukuonyesha kunijali mimi kama
Nanaa. Niliondoka na kukuacha ofisini nikikwambia sijisikii vizuri. Hukuonyesha
hata kujali kama ninaumwa nini, au nitafikaje nyumbani wakati
nilikuaga nikikwambia sijisikii vizuri. Halafu eti nafika nyumbani
ndio unanitumia ujumbe! Kweli Geb? Nimeshapita huko. Nimejifunza mambo mengi,
tena kwa machozi, ambayo hakuna aliyewahi kuyafuta. Moyo wangu umejaa madonda
ambayo nayauguza kwa shida sana. Naamini ipo siku yatapona. Kwa hiyo nipo
makini sana na kila neno na kila mtu, ili nisizidi kuumia. Kwa kuwa sasa hivi
najijua mimi ni nani na nini nataka. Kama nimeshindwa kupata kutoka kwa mtu
mwingine, afadhali nijipe mimi mwenyewe. Matatizo mengine sikujitakia.
Ningetamani na mimi ningekuwa na familia kama watu wengine, lakini sikujaliwa,
na sijui kwa nini! Ila matatizo mengine nakubali kabisa nilijitakia, wala sina
wakumlaumu. Sasa siwezi kuendelea kujiumiza.” Ukimya mkubwa ulipita, Geb
hakujibu kitu, akaendelea kuendesha.
Baada ya muda, Geb akavunja
ukimya. “Samahani kwa kushindwa kuonyesha kujali siku ile
ofisini.” Geb akaongea kwa upole, Nanaa hakutegemea, akabaki na
kigugumizi. “Nanaa?” “Haina shida Geb. Nimeshazoea. Hata hivyo sikutegemea
kitu cha tofauti kutoka kwako. Kwa hiyo ni sawa tu.” Nanaa akajibu, Geb
akamwangalia. Akajishangaa machozi yanatoka. Akajifuta kwa haraka, akaamua kubadili
mazungumzo.
“Huko Bagamoyo unakuwa na mashamba
yako ya Matikiti maji, au wakati wote unaenda kununua kwa wakulima?” “Bado
sijafikiria kuwa na mashamba. Sina muda wakutosha kuanza kulima au kuwa
mkulima. Kwa hiyo huwa nategea kipindi cha mavuno ndio huwa nakwenda. Leo
asubuhi nimetuma lori likafuate mzigo. Kwa hiyo huwa wakati mwingine napenda
sisi wenyewe kwenda kusimamia. Hasa nikiwa na dereva mgeni kama nilivyokuwa
nimekwambia juzi. Dereva huyu aliyekwenda huko ni mgeni kabisa. Ndio mara yake
ya kwanza. Sijamfahamu anatabia zipi. Kwa hiyo lazima kuwepo.” Akatulia
kidogo.
“Halafu najikuta mimi ndio nalazimika
kwenda kwa kuwa Grace anahitajika sana na familia yake.” “Nimeona. Yaani hata
akiwepo pale ndani, Danny na Fili wanamfuata nyuma kila mahali!” Nanaa
akaongeza. Wakacheka. “Kwa hiyo hata mikoani huwa naenda mimi mwenyewe.
Kama tunataka mzigo mkubwa zaidi ya ule tuliozoea kuchukua, nakwenda kutafuta
wakulima wapya na kukubaliana nao kabisa. Ili tukituma dereva anakuwa na kazi
ya kubeba tu, sio kuhangaikia tena kutafuta mzigo.” “Ooh! Kwa hiyo huwa
unasafiri mara kwa mara?” Nanaa akauliza tena.
“Sio sana. Inategemea na wapi
nachukua mzigo, na ni mzigo gani. Kwa mfano mchele huwa najua bei zake, na nina
watu wengi nafahamiana nao kwa muda mrefu. Nikitaka zaidi, sina haja ya kwenda.
Nawaomba wakulima ambao nimekuwa nao kwenye biashara kwa muda mrefu,
waninunulie kwa wakulima wengine wanitumie, kisha ninawalipa. Kwa hiyo kuna
mikoa mingine nimeshatengeneza mahusiano ambayo yananirahisishia. Halafu kama
unavyojua, katika maisha lazima ukubali kuamini mtu fulani. Lasivyo utateseka
sana.” Nanaa akanyamaza akijua anajaribu kumfikishia na yeye ujumbe.
Akamtolea karanga
akampa. “Asante.” “Nikupe na maji au juisi?” Nanaa
akauliza. “Maji tafadhali.” Akatoa na kumkabidhi. “Asante.”
“Karibu.” Geb akaendelea kula huku akiendesha. “Nikuulize kitu,
Nanaa?” “Niulize tu” “Unapoamka asubuhi na kunitayarishia kifungua kinywa,
unaona unalazimika kwa kuwa unaishi pale au?” Nanaa alishituka sana,
hakutegemea hilo swali. “Naomba uwe tu mkweli, haitabadilisha chochote.”
“Sijawahi hata kufikiria! Labda sasa hivi nianze kutafakari.
Lakini..” Nanaa akasita.
“Lakini nini?” “Pale kwako ni tofauti
Geb. Mama yako na Grace wamenionyesha upande mwingine kabisa wa maisha. Naogopa
kusema zaidi ili nisijiwekee tumaini ambalo halipo. Lakini kuna jinsi
wananichukulia, sijisikii kama ni mzigo nikiwa pale kwako.” “Lakini si unajua
lazima ufungue tena moyo wako? Huwezi kuishi hivyo Nanaa. Watu wakikuonyesha
upendo, lazima kuutambua huu ni upendo na kuupokea. Lasivyo utazidi kujiumiza.”
“Naogopa Geb!” “Lakini hivyo hujisaidii, na itakuchukua muda mrefu sana
kupona. Huwezi kutoka hapo. Kuna watu wengine Mungu anawaleta kwenye maisha
yako, kukufariji. Lakini usipokuwa mwangalifu, unaweza kuwafungia watu wote
mlango.” Nanaa akanyamaza.
“Sitaki uishi pale, na kufanya kitu
chochote kwa ajili ya kulipa fadhila. Hata usipofanya jambo lolote, ukaamka na
kujishugulikia wewe mwenyewe na kuondoka pale, nakuhakikishia kabisa, hakuna
atakaye kulaumu Nanaa. Mama na Grace watakupenda kwa upendo uleule wanao
kupenda sasa hivi.” “Unajuaje?” “Nanaa! Lazima ukubali sio watu wote watakao
kuja kwenye maisha yako, watataka kukutumia tu. Wengine watakuja kwa nia nzuri
na watakupenda wewe kama Nanaa. Labda nikupe mfano utakao kusaidia. Najua kwa
sehemu umeanza kumfahamu Liz ni mtu wa namna gani.” “Unamaanisha Liz mpenzi
wako?” Nanaa akauliza ki uchokozi tu, na Geb akajua. Akamtazama kidogo na
kurudisha macho barabarani.
Akaendelea. “Sasa Liz alisoma na
Grace darasa moja. Wakajikuta wanakuwa marafiki. Alishamfanyia Grace mambo
mengi sana yakumuumiza, lakini bado wakabaki kuwa marafiki na kumkubali Liz kwa
tabia zake kama alivyo. Kipindi mimi nipo chuoni nje ya nchi, wakati Grace na
mama wapo kwenye shida sana, bado Liz alikuwa rafiki wa Grace. Liz amezaliwa
kwenye familia yenye uwezo sana, na wapo watoto wakike wawili tu. Nikikwambia
wana uwezo, ni watu wenye uwezo. Liz hajui shida hapa duniani. Anaendesha
magari tokea hata hajafikisha miaka 18. Namaanisha magari ya nyumbani kwao, sio
yakuhongwa. Anapesa yakutosha. Walikuwa marafiki na Grace tokea zamani kama
nilivyokwambia, lakini hata Grace alipokuwa na shida, Liz hakuwahi kumsaidia
hata mara moja.” Nanaa alikunja uso akiwa haamini.
“Anasema wakati wapo chuoni, wakati
mwingine walikuwa wakienda kula pamoja, kundi la marafiki, Grace anashindwa
kujinunulia chakula, wenzake wanampunguzia chakula sehemu ili ale, lakini sio
Liz. Liz haelewi kwa nini mtu anakosa pesa. Inakuaje mtu analipwa na chuo,
halafu akose pesa ya kujinunulia chakula. Anaposema kwa nini watu wanazaliwa
milimani au wanaishi milimani, sio kuwa anatania au anakejeli, ni kweli
haelewi. Na kingine Liz ni muwazi sana. Hawezi kuficha hisia zake. Anaongea
kile anachofikiria akidhani ni jambo la kawaida tu au na wengine walitakiwa
waelewe hivyo. Anashangaa pale wengine wasivyofikiria kama yeye.
Haelewi.” Nanaa akainama huku akimfikiria Liz.
“Amesoma bila shida na kupata kazi
bila tatizo lolote. Sio kama mimi nilivyokwambia ilibidi mama kuniombea mpaka
vyeti na mimi kuzunguka karibia mji mzima kutafuta kazi! Sio Liz. Alikuwa
anamalizia chuo, akiwa na ahadi ya kazi tayari. Ana ndugu na marafiki
wanaoshika nyadhifa kubwa sana hapa nchini. Amezaliwa kwenye pesa, na yeye
sasa hivi anaingiza pesa nzuri tu bila shida. Huwezi kumueleza mtu anakosaje
pesa akaelewa. Anaishi kwenye jumba la thamani. Kubwa na wapo wao tu. Familia
ya watu wanne. Hawajawahi hata kuona ndugu analala nyumbani kwao. Amekuwa
akiona wageni wakija kutembea kwao wametokea nchi za nje, si kijijini na
wanalala hotelini. Na kama watakaa kwa muda mrefu, watawakodishia nyumba
mahali. Zile nyumba ambazo zipo full furnished. Kwa hiyo haelewi
inakuaje watu wengi wanaishi nyumba moja.” Nanaa akacheka taratibu kama na
yeye asiyeelewa asichoelewa Liz.
“Kweli tena. Haelewi kwa nini mtu
atake kupumzika aende sehemu kama Marangu! Au useme unakwenda likizo kijijini.
Haelewi kwa kuwa hana marafiki wa namna hiyo na wala hajawahi kukaribisha
mazungumzo ya matatizo kwenye maisha yake. Yaani kwa Grace ilimbidi tu kwa kuwa
mwaka wa kwanza walijikuta wamepewa chumba kimoja. Japokuwa hakuwahi kulala
chuoni hata siku moja sababu ya mazingira yale ya hosteli yalimshinda, lakini
alikuwa akiacha madaftari yake chuoni na kusoma na kina Grace darasa moja na
kundi moja. Alikuwa akiendesha gari ambalo hata maprofesa pale chuo wakati ule
walikuwa wakishangaa. Tena jipyaa. Sio lililotumiwa huko Japan. Anaingia chuoni
asubuhi, na kurudi kwao usiku. Anaweza kukufanyia kitu, ukabaki huelewi. Lakini
sio yeye. Yeye anaona ni kawaida tu. Kila mtu anamfahamu hivyo Liz.” “Kwa hiyo
unachojaribu kuniambia na mimi ni kujaribu kumuelewa mpenzi wako na kumpokea
kama wengine?” Tayari wivu ulishakuwa ukimtesa Nanaa.
Geb akamtizama kidogo, kisha
akaendelea. “Katika yote hayo, bado Grace anamtamka Liz kama rafiki yake na
akaja kumtambulisha kwangu, na kuniambia ananipenda. Yaani akaniunganisha naye.
Tumeanza mahusiano, ndio baadaye anakuja kuniambia tabia za Liz na kuniambia
nisimshangae, ndivyo alivyo. Na nikikwambia ni rafiki yake, ni marafiki. Hata
kitendo cha Liz kunilalamikia mimi kwa nini ninaishi nao, Grace na mumewe,
Grace anakijua, alishamsikia akinilalamikia tukiwa jikoni, anataka Danny na
familia yake waondoke pale ndani. Grace akaingia nakucheka tu. Baadaye
nikajaribu kuongea na Grace kama kumtuliza kwa yale mazungumzo aliyotusikia
tukizungumza na Liz, chakushangaza yeye ndio akanituliza. Aliniambia nisiwe na
wasiwasi, yeye anamuelewa Liz vizuri kuliko mimi ninavyomuelewa. Alishaishi
naye chuoni kwa miaka 3. Hamsumbui. Nilishangaa kidogo, ndipo na mimi nikajifunza
kuwa kuna watu kwenye maisha, wanapendwa vile walivyo. Sijui unanielewa?”
“Nimeelewa.” Geb akamwangalia.
“Umenielewa kweli?” “Nimeelewa Geb.”
“Basi naomba uanze kuishi pale nyumbani ukiwa unajisikia uhuru wote. Usifanye
kitu ambacho hujisikii kufanya. Nakuhakikishia hakuna atakaye kulaumu.” “Lakini
sijafanya kitu chochote ambacho nimelazimishwa Geb. Yote ninayofanya sasa hivi
ni aidha ni kwa kuwa nipo hivyo, yaani sijui jinsi ya kufanya vinginevyo, au
nafurahia kufanya.” “Kama nini unafurahia kufanya?” Geb alitaka kujua
zaidi, ili ahakikishe asemayo kama ni kweli.
“Kukupikia chakula au kukufanyia wewe
kitu ambacho kinamsaada. Yaani kuona nafanya kitu, halafu naona mtu mwingine
anafurahia, najisikia vizuri. Hata kama sitashukuriwa, lakini najiona sio mtu
wa hasara.” Geb akamwangalia na kutabasamu.
“Kweli tena! Kwa mfano, mwanzoni
hukuwa ukijua kama mimi ndio nakupikia chakula, au uji. Lakini kule kukuona
unakula, nakufurahia kama amekufanyia mama yako, kwangu ni furaha tosha. Siku
ya kwanza kumuomba mama yako nikupikie, aliniambia nijaribu, tusikwambie,
kama utaona tofauti na hautakula, ataendelea kupika yeye mwenyewe. Lakini
kama utakula bila kulalamika, ataniachia. Akaanza kuniachia kukupikia uji
kwanza kabla ya chakula. Siku ya kwanza nilipopika mimi uji, ukauchukua kwenda
nao kazini, hukunywa ule wa kwenye bakuli kwa kuwa ulichelewa kuamka. Ukasema
utakula ukifika kazini. Ukaondoka na ule wa kwenye chupa. Uliporudi jioni mama
akakupokea chupa, kisha akaniita jikoni akaniambia umeupenda ule uji ndio maana
uliumaliza wote.” Nanaa akatabasamu kisha akaendelea.
“Siku nyingine akaniachia nikupikie
mchemsho wa samaki na ndizi. Lakini alikuwa ameshanifundisha jinsi ya
kukupikia. Nakumbuka ilikuwa siku ya jumamosi mchana. Ukala, ukatoka na Fili
kwenda kucheza mpira na wenzako. Ilipofika jioni ukampigia simu mama yako
ukamwambia njaa inauma, lakini unataka ukirudi, ukute chakula kama alichokupa
mchana. Mama yako akaniita na kuniambia utakuwa umekipenda sana, kwa kuwa huna
tabia yakurudia chakula, labda uji. Ndio akaniachia hiyo kazi mimi.” Geb
alikuwa akimsikiliza kwa makini tu.
“Lakini Geb, nasema kweli, kwa mara
ya kwanza maishani nilijiona ninamanufaa. Kaka James anakuwa ananishukuru sana,
mpaka wakati mwingine nilikuwa najisikia vibaya. Tokea tupo nyumbani kwao, kila
kitu nilichokuwa nikiwafanyia ndugu zake, hata mama yake, walikuwa wakikosoa.
Tena kwa kunigombesha sana au kupigwa, lakini sio kaka. Tena wakati mwingine
alikuwa akinipa mpaka pesa kunipongeza kwa kazi nzuri ninayofanya, na kuniambia
ninunue chochote ninachotaka. Sawa, nilikuwa napata pesa yakujinunulia vitu
vyangu binafsi, lakini kwa upande mwingine nilikuwa nikijiambia labda nakuwa
nakosea, yeye ananitia tu moyo. Sasa kuona nafanya kitu pale nyumbani kwako, na
wewe unakikubali, halafu hujui kama ni mimi ninafanya, nafurahia sana Geb.
Sijali kama unajua kama ni mimi au la, kwa kuwa najua mimi ni mpita njia tu,
nitaondoka hivi karibuni na mnaweza msinikumbuke tena, lakini huwa natamani
muda wa kukupikia ufike, nipike ili nimpokee hiyo kazi mama yako
anayeonekana kuridhika na ninachofanya halafu na wewe ule bila shida.
Inanifariji kwa upande fulani.” Nanaa akacheka kidogo.
“Haya, kingine najiona nafanya kitu
cha maana vile Danny anavyoshukuru kwa kupata kifungua kinywa tofauti tofauti
kila siku asubuhi. Alimwambia mpaka kaka, kaka akanipongeza. Na wakati mwingine
Danny huwa anambebea na yeye kaka. Kwa hiyo kaka naye anapata kitu cha kula
kazini.” Nanaa akaendelea.
“Kingine ni vile Grace anavyoniomba
nimsaidie kumuogesha au kumlisha mtoto wake. Naona ameniamini, au amefurahia
ninavyomfanyia mwanae, na mengine mengi tu. Pale kwako kunanisaidia kwa upande
fulani. Najua hata nikiondoka pale, kutakuwa na kitu kingine kimejengeka kwenye
nafsi yangu tofauti nilivyojengwa na maisha tokea nakua.” Geb akamtupia
jicho kidogo akaendelea kuendesha.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya ukimya kidogo, Nanaa
akatupia swali. “Kwa hiyo umeelewa kwa nini sikujibu ujumbe
wako?” Geb akatulia kidogo. “Nafikiri nimeelewa. Lakini imeniumiza.”
“Kwa nini tena!?” Geb akanyamaza kidogo kama anayefikiria kitu. Kisha
akaongeza, “Unajua nakumbuka maongezi yote yaliyokuwa yakiendelea siku
ile? Kila neno nililokwambia na vile ulivyonijibu, Nanaa.” Nanaa
akamwangalia.
“Sijui kama wewe unakumbuka? Lakini
mimi nakumbuka vizuri tu. Ulinyanyuka gafla, nikakuuliza, ‘vipi?’ Unakumbuka
jinsi ulivyonijibu?” Nanaa akanyamaza. “Ulinijibu kwa ukali, Nanaa.
Uliniambia ni muda wa kula, unaenda kula, kisha ukaondoka hapo hapo. Baada ya
muda ulirudi, nilikuona kabisa haupo sawa, nikakuuliza tena, ‘kwema?’,
ukanijibu kwa kifupi sana, ‘najisikia vibaya, naenda kupumzika’.
Hapo hapo ukachukua pochi yako na kuondoka. Ningefanyaje?” “Angekuwa Grace au
Liz, ungefanyaje?” Nanaa alitupia swali la harakaharaka, nakumfanya Geb
ashindwe kujibu. Waliendelea kuendesha kimya kimya mpaka walipofika.
Wakiwa
Bagamoyo!
“Naomba kabla hujashuka, umalizie
hizo karanga, Geb. Zimebaki kidogo tu hapo.” “Asante. Nilishazisahau. Nisaidie
chupa nyingine ya maji ili nisafishe meno baada ya hapa, ili nisishuke na meno
yaliyojaa karanga.” Nanaa akacheka. “Naona huyu dereva mpya amejitahidi! Sijui
amefika saa ngapi! Anamalizia kupakia. Naona hatutakaa sana.” “Namimi naomba
nishuke.” Geb akacheka. “Mbona unanicheka?” Nanaa akauliza.
“Utachafuka.” Nanaa akajiangalia. “Haina shida. Nikirudi nitaoga. Sitaki
kukaa humu ndani kama mtalii.” Geb alitabasamu huku akimwangalia na
kumalizia kunywa maji yake. “Basi twende.” Wakashuka pamoja.
Geb alisalimiana na wenyeji wake na
kurudi kwenye lori kusaidia kupakia. Nanaa na yeye akaanza kusaidia. Alikuwa
akikusanya matikiti maji yaliyosambaa, na kuwasogezea karibu. Baada ya masaa
mawili wakawa wamemaliza kabisa. “Pole.” Nanaa alimsogelea
Geb. “Asante. Pole na wewe.” “Kumbe ukija huku na wewe huwa unafanya kazi!
Nilijua huwa unasimamia tu.” Geb akatabasamu. “Wakikuona na wewe
unafanya kazi na wao wanapata moyo, wanaongeza juhudi.” “Lakini umelowa!”
“Nimekuja na nguo zakubadilisha.” “Kumbe unakuwa unajua!?” Geb akatoa
tabasamu jingine kama kawaida yake.
“Lazima. Huwa sipendi kufika sehemu
nisimame tu. Napenda kufanya nao kazi.” Akajibu na kumuuliza Nanaa
swali. “Umechoka?” “Bado nina nguvu tu. Kuna sehemu nyingine ya kwenda
kupakia?” “Hapana. Hapa ndio mwisho, na naona lori lenyewe limejaa.” “Kwa hiyo
hapo unakuwa umeshapata wateja?” “Kwa huo mzigo, ndiyo.” “Hongera.” “Asante.
Lakini sio mara zote inakuaga hivyo. Si unaona hata kwenye ripoti ile
niliyokusaidia kutengeneza tukampa Grace, nilionyesha kuna hasara?”
“Nakumbuka.” “Basi ujue kuna mzigo uliokuwa umeharibika. Wakati mwingine dereva
anaweza kuharibikiwa na Lori porini, matunda yote yakaharibika. Au
ukatokea uzembe pale ofisini kama nilivyokuwa nikimwambia Grace. Mtu wa masoko
asifuatilie wateja kwa wakati, mzigo ukafika, ukawa hakuna pakwenda kwa haraka,
ukaishia kuharibika tu.Tunaongeza hasara. Kwa hiyo ndio biashara.” Nanaa
alibaki akiangalia lile lori.
“Unaratiba gani baada ya
hapa?” Geb akauliza. “Yule dalali amenitumia ujumbe. Ameniambia kuna
chumba amepata kule mitaa ya Savei karibu na chuo. Amesema kama naweza kwenda
leo, ingekuwa vizuri, ili nikakiangalie. Lakini nimemwambia nipo mbali kidogo,
sijui ni muda gani nitarudi. Ameniambia muda wowote nitakapofika mjini,
nimtafute anaweza kunipeleka.” Geb alibaki akimwangalia. “Lakini
haina haraka, amesema hata kama ni usiku atanipeleka tu. Kwa hiyo haina
haraka.” Geb alivuta pumzi kwa nguvu. Akazishusha kwa wakati mmoja.
“Naomba nisubiri kidogo. Nataka
niagane na huyu dereva, nitarudi sasa hivi.” “Sawa.” Geb akaenda
kuzungumza na yule dereva huku Nanaa akimwangalia. Alitoa pesa akamkabidhi.
Wakazungumza kidogo, Geb akarudi na matunda. “Nimembembea Fili matunda ya
juisi. Twende.” Wakaingia kwenye gari.
“Asante.” Geb
akashukuru. “Kwa nini?” “Kusaidia kazi.” Nanaa akacheka. “Karibu. Na
mimi nimefurahia kuja huku.” “Sasa hivi bado mapema sana. Tunaweza kwenda
mahali tukakae kwa muda mfupi, ndio turudi nyumbani?” “Sawa.” Geb akaondoa
gari. Wakaendesha umbali kama wa dakika 20, ndipo wakaanza kuona mahoteli.
Aliingia kwenye hoteli moja nzuri, akaegesha gari. “Tuingie humu, lakini
mimi nitaanzia chooni kwanza. Nijisafishe kidogo, halafu nitabadili tisheti.
Nimejichafua. Naona mwenzangu ulikuwa mwangalifu.” Nanaa akacheka
kidogo. “Nikusubiri hapa hapa ndani ya gari?” “Kama hutajali. Sitachelewa
sana.” “Sawa.” Geb alichukua kibegi kidogo nyuma ya gari, akaondoka.
Na kweli baada ya muda mfupi, akarudi
akiwa anaonekana msafi, amebadili na kuvaa tisheti nyingine. Alionekana alijisafisha
vizuri maana hata uso ulionekana umetulia. “Twende ndani.” “Nishuke
na uji?” Geb akafikiria kidogo. “Nikikosa kitu cha kula humo ndani,
ndio tutarudi kuja kuuchukua. Nataka kunywa baadaye.” Nanaa akashuka,
wakaongozana mpaka ndani. Alitafuta sehemu wakakaa. “Pazuri sana. Sijawahi
kufika sehemu nzuri kama hii.” Nanaa akasifia, Geb akacheka kidogo. “Usinicheke
bwana! Unafikiri maeneo kama haya huwa nafikaje sasa?” “Nakuelewa.
Napapenda hapa, huwa pametulia.” Muhudumu akawasogelea kutaka kujua
wanataka kula nini. “Mimi bado nimeshiba, Geb. Nimekula sana korosho na
ile soda yote nilimaliza, njiani.” “Unauhakika?” Geb
akauliza. “Kabisa. Nikisikia njaa nitaagiza.” Nanaa
akajibu. “Basi. Asante. Tukihitaji kitu tutafuata tu. Asante
sana.” Geb akamshukuru yule muhudumu, akaondoka na kuwaacha wawili.
~~~~~~~~~~~~~~
Kila mtu alikuwa kimya akiangalia
sehemu yake. “Nanaa!” Geb akaita, Nanaa akageuka. “Naomba
unisamehe, kwa kutokujali uliponiambia hujisikii vizuri siku ile ofisini.
Nisamehe kwa kukuacha ukaondoka bila kujali. Samahani.” Nanaa aliona
machozi yanatoka. Akajifuta mara kadhaa. “Samahani. Sikufanya vizuri. Na
najua angekuwa Grace au Liz kama ulivyosema, ningefanya tofauti, lakini
nilikosea. Samahani. Haitakaa itokee tena. Wakati mwingine nitakuwa
makini.” Ilimgusa sana Nanaa. “Kwa hiyo naomba unisamehe.” Nanaa
alitingisha kichwa kukubali huku akikausha machozi. “Asante.” Geb
akashukuru, wakatulia tena.
“Nikuombe kitu kingine?” Geb
akauliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Naomba usiondoke
nyumbani.” Nanaa aliinama na kukunja uso. “Naomba tuishi wote, mpaka
chuo kikifungua ndio unaweza kuchukua chumba pale ‘Main campus’, tukakiweka kwa
ajili ya siku za mitihani au siku unazotaka kuwepo chuoni kwa ajili ya
kujisomea na wenzako. Lakini kwa sasa naomba tuishi wote.” “Sidhani kama ni
sawa, Geb. Acha tu niondoke, nitakuwa nikirudi kuwasalimia.” “Kwa nini?” Nanaa
akabaki kimya.
“Eti Nanaa?” “Sijui niseme nini
Geb. Lakini naomba uwe na amani. Umeshanisaidia, au nimeshasaidiwa vyakutosha.
Ngoja na mimi nianze maisha yangu. Naomba usijisikie kama unajukumu lakutimiza
kwenye maisha yangu. Huku kukufahamu kwa muda huu mfupi tu, umeacha somo
kwenye maisha yangu. Na ninakushukuru. Naona na mimi nikatumie yale
niliyojifunza kwenu. Naamini na mimi nitakuja kuwa msaada siku moja kwa mtu
mwingine.”
“Mbona hata sasa wewe ni msaada
kwetu. Huwezi jua faraja unayoileta pale nyumbani. Mama anakupenda Nanaa.
Amepata rafiki wakuzungumza naye. Grace anakuwa busy sana na mtoto wake
na mumewe. Muda mwingi anajikuta anakazi, au hao watu wawili wanamuhitaji, hana
muda na mama kama ulivyoona. Halafu hata hivyo karibuni sana wanaondoka. Nyumba
yao imebakia padogo sana kukamilika, watahama. Tutabakia wapweke
kweli.” Nanaa akacheka kidogo. “Liz si atakuwepo?” Nanaa
akatupia swali na kumfanya Geb atulie kidogo. “Naona kama mama amekuzoea
wewe zaidi.” Nanaa akamwangalia, nakunyamaza. “Eti, Nanaa?” “Kwa hiyo
unataka nibaki kwa ajili ya mama yako?” Nanaa akauliza, lakini Geb
hakujibu. Akanyamaza.
Walizungumza mambo mengine. Baada ya
muda, Nanaa akasema njaa imeanza kumuuma. Walimuita muhudumu, wakaagiza
chakula. Geb alitaka ugali, nyama choma, na kachumbari. “Lakini usiweke
kitunguu wala karoti. Iwe nyanya, tango na limao tu.” Nanaa
akacheka. “Usinicheke bwana Nanaa. Huoni nimeagiza chakula?” “Kuagiza ni
hatua ya kwanza, na nzuri sana, tena huwa unapenda kweli kuagiza. Kikija na
kukiweka mdomoni ndipo kazi ilipo.” “Basi leo nitahakikisha kinaingia mdomoni.”
“Tutaona.” Geb akacheka. “Na wewe utakula nini?” “Nyama ya kuchoma na
ndizi za kukaanga. Naomba na kachumbari kama ya Geb lakini mimi weka
karoti.” Muhudumu akaandika, na kuondoka.
Chakula kikaletwa. Nanaa akamuona
vile Geb anavyokiangalia, akajua hatakula. “Geb! Naomba kabla hujakikataa
hicho chakula kwenye akili zako, jaribu kukiweka kidogo tu mdomoni. Naomba
usishibe kwa macho.” Geb akacheka. “Ulijuaje? Nishaangalia hii kachumbari
ilivyowekwa hapo, ikanikinahi kwa haraka sana. Nyama yenyewe ni kama imekaushwa
sana, ugali kama umepoa!” “Naomba jaribu kuchukua hatua nyingine. Naomba jaribu
kuweka mdomoni. Jaribu tu. Halafu uniambie na mdomoni kinakuaje.” Geb
akacheka huku akikiangalia kile chakula.
“Kwani nikikuagiza kuku wa kuchoma
itachukua muda gani?” Geb akamgeukia muhudumu. “Nakuomba ujaribu
kidogo tu. Nakuomba Geb. Najua utaagiza tena huyo kuku, itakuwa tena kama hiyo
nyama ya ng’ombe, hutakosea sababu. Unakumbuka majuzi mchana? Uliponifuata
kazini, tukaenda kula chakula cha mchana?” Geb akacheka. “Wale
waliacha nyama ina damu bwana!” “Unakumbuka uliagiza nyama ya ng’ombe tena?
Ukashindwa. Ukaomba kuku wa kuchoma. Pia ukashindwa. Ukataka tena samaki.
Akaletwa. Vyote ukaishia kuviangalia kwa macho bila kuweka mdomoni. Tukaishia
kuondoka hujala, lakini umelipia vyakula vya watu karibia watano.” Geb
alibaki akicheka.
“Kumbe siku ile ulikuwa ukiniangalia
tu. Leo umeamua kunitolea uvivu?” “Leo umefanya kazi ngumu sana, unahitajika
kula. Naomba ujikaze kula hata kidogo. Utaenda kuongezea na uji kwenye
gari.” Geb alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha huku akiangalia kile
chakula chake. “Sawa. Nitakula hiki hiki.” “Kwa hiyo nisilete tena
kuku?” Muhudumu akamuuliza Geb, Nanaa akabaki akimwangalia,
akacheka. “Hapana. Nitakula hikihiki chakula. Asante.” Muhudumu
akaondoka.
“Chakula ni kizuri Geb.
Jaribu.” Geb alianza kula taratibu. Nanaa alikuwa akimwangalia. “Vipi
nyama?” “Sio mbaya. Ni laini kwa ndani, tofauti inavyoonekana.” “Na ugali ni
baridi sana? Kama nibaridi naweza kuwapelekea, niwaombe watupashie.” “Naona
inatosha. Asante.” Geb alijibu kwa tabasamu. Alionekana anafanya kazi
asiyoipenda kabisa. Heri ile kazi yakupandisha matunda kwenye Lori alionekana
amechangamka sio kama kula kile chakula pale. Lakini alijitahidi, akala zaidi
ya nusu. “Naomba nikamalizie na uji. Hiki chakula kilikuwa kingi
sana.” Nanaa akacheka. “Hata hivyo umejitahidi.” Geb akacheka.
Nanaa akamaliza chakula chake
chote. “Umeshiba?” Geb akauliza. “Sana. Nahisi nikipanda tu
kwenye gari, nitalala.” Geb akacheka. “Unaniacha niendeshe mwenyewe?”
“Nakutania bwana! Mimi si ndio nakulinda?” “Kama unanilinda mbona unafikiria
kunikimbia sasa?” Nanaa akainama. “Usiondoke bwana Nanaa. Naomba
tubaki wote. Wewe huoni ukiwa na mimi unavyonihimiza kula? Unanipikia vizuri,
unanisindikiza huku. Nakuwa sipo mpweke. Usiondoke bwana.” “Kwani huwa hujagi
huku na Liz?” Geb alicheka kwa sauti mpaka akapaliwa na maji.
“Liz!?” Akazidi
kucheka. “Ndiyo.” “Kwanza umeona mwili wake? Hathubutu kuja shamba.
Anajipenda na kujithamini sana Liz. Sehemu kama zile hawezi kukanyaga. Kwanza
kumwambia aje huku ni kumtusi. Kila kitu kinachoingia mwilini kwake lazima kiwe
ni cha thamani. Kila anapoenda ujue nisehemu ambayo ni mazingira yanayoendana
na mwili wake. Kila week, lazima mwili wake auweke kwenye sauna, na kufanyiwa
masaji. Na akikosa hata mara moja tu, anajua kuwa week hiyo amekosa, na ni mara
chache sana. Sasa mwili kama huo, huwezi kuupeleka shamba au kuuweka karibu na
moto. Yaani aanze kumpikia mtu! Yeye mwenyewe hawezi kujipikia, anaogopa moto,
halafu umwambie ampikie mtu mwingine! Hathubutu, na atahisi umeamua kumtukana
vibaya sana. Hata kitendo cha kuja kule Marangu, nilimsifu sana. Kwake yale ni
mazingira hatarishi. Na sio kwamba anajidai, ndivyo alivyo.” Nanaa
akacheka kidogo na kuzidi kumtafakari Liz.
~~~~~~~~~~~~~~
Alikuwa ni binti mweusi. Mwili mzima.
Rangi moja tu. Laini hata kwa kumtizama kwa macho, alionekana laini. Alikuwa na
umbile namba 6 isiyo kubwa hata kidogo. Alikuwa na kamwili kazuri sana. Hakuna
muda wala wakati ungemkuta Liz ni mchafu. Na wakati wote alikuwa kwenye kiatu
cha juu. Hata kama ni sandals tu. Ilikuwa lazima iwe ya juu. Tena kucha safi
wakati wote. Nanaa hakukumbuka kumuona amekaa mahali bila kupishanisha miguu
yake. Popote alipokaa, alikunja 4. Tena alikaa vizuri, si kihasara. Wakati
wote, mabega yake yalikuwa yamenyoka. Usingemkuta amepindisha mgongo hata akiwa
amekaa kwenye kochi alinyooka vizuri. Ni kweli kila kitu chake kilikuwa kisafi
na cha thamani. Lazima ungependa kumtizama tu.
Jinsi alivyotembea na kujiweka,
utajua anajielewa. Mikono yake ilikuwa mizuri na laini. Rangi yake ya weusi
ilimkaa vizuri na alihakikisha kila anachokivaa, kinaendana na rangi yake hiyo.
Hakukumbuka kuona hata kipele mwilini mwa Liz. Kila alipomkumbuka Liz, Nanaa
akacheka. Hakukumbuka kumuona akifanya kitu chochote hata alipokuwepo pale
ukweni. Na hakuwa mnafiki. Kila kitu aliuliza kilipo. Si kwamba hakujua
vinapowekwa, bali alitaka aletewe alipo. Na akagundua ni kweli pale ndani kwa
kina Geb wanamjua. Kwani kila alipoulizia kitu, aliona kama sio Geb anasimama
kumletea, basi shoga yake Grace atakwenda kukifuata hicho kitu na kumpelekea
alipo yeye. Nanaa akacheka tena.
~~~~~~~~~~~~~~
“Unacheka nini?”“Namfananisha
Liz na watoto wa mama mkubwa. Wanafanana hivyo hivyo. Kama sasa hivi namfikiria
kaka jinsi anavyoishi nao pale nyumbani kwake, nashindwa jinsi yakumsaidia kwa
kuwa mama mkubwa amenikataza kwenda. Atakuwa anachoka sana. Kuwapikia,
awasafishie, na bado awapeleke kila wanapotaka kwenda! Nahisi ataisha mwili
wote.” Nanaa aliongea akionekana kumfikiria kaka yake.
“Unajua nilipohamia kwake, alikuwa
anaishia kulala kwenye makochi? Anasema chumbani kwake pia alikuwa anapaona
mbali kwa kuchoka.” “Na James anajua kujituma sana. Si kazini, si kwenye
biashara zake. Anajua kujituma bila kuchoka.” “Namuombea Mungu aje kumpata mwanamke
mzuri, atakayempenda na kumthamini. Anastahili.” “Kwa hiyo mimi
sistahili?” Geb akauliza akisikika kumuonea wivu James.
“Unamfikiria James tu! Mimi nakuomba
ubaki na mimi, unanikatalia!” Geb aliongea kwa kulalamika
kidogo. “Wewe unaye Liz, Bibi Fili na Grace. Wote hao wanakulea kama
yai. Huhitaji mtu waziada kwenye maisha yako Geb. Lakini sio kaka. Kaka yupo
peke yake.” Geb alicheka sana.
“Umesema wananilea kama yai?”
“Kabisa. Wakiwa wanamzungumzia Geb, unaweza kufikiri wanamzungumzia mtoto wa
chini ya miaka 10. Kila mtu anawasiwasi wa ulipo, umekula nini, au ulisikikaje
mara ya mwisho kwenye simu. Kama uliongea kwa huzuni au furaha. Mara ya mwisho
wa kusikika ni saa ngapi! Hayo yote ndio mazungumzo ya Grace na mama
yako.” Geb alicheka sana.
“Yaani wewe huna haja ya mtu mwingine
kwenye maisha yako, Geb. Na ndio maana unauwezo wa kuishi na Liz bila shida na
wala usione kama umepungukiwa. Kwa kuwa umezungukwa na watu wanaokufikiria wewe
wakati wote. Lakini sio kaka. Hamna anayemjali yeye kama James. Wakati wote
nyumbani kwao wanamuomba pesa. Hawajali kama anazo au hana. Hawajali kama yeye
mwenyewe ni mzima au la. Akipigiwa simu mpaka utamuhurumia. Wakati wote ni simu
za matatizo. Na lazima asaidie. Asiposaidia kosa la kwanza na kubwa ni
kuendelea kumsaidia Nanaa.” Nanaa alikuwa akiongea kwa upole na
masikitiko.
“Ataambiwa Nanaa anamkosi, hakuna
mahali anapoishi mtu akafanikiwa, au Nanaa ana roho ya chuma ulete. Ndio maana
eti anafanya sana kazi lakini haoni matokeo mazuri. Maneno mengii, mpaka
utamuhurumia kaka. Na hapo anakuwa ametoka kuwatumia pesa hata week haijaisha!
Na mama mkubwa bado anabiashara zake, na zote zinamwingizia pesa. Japokuwa baba
mkubwa alistaafu, lakini pia anabiashara zinazomwingizia pesa. Ila baba mkubwa
yeye ni afadhali. Huwa hamuombi kaka pesa. Akipiga ni kutaka kumjulia hali
mtoto wake, ni mara chache sana kuomba pesa. Tena huwa anakopa, na kurudisha.
Sasa unakuwa unamfikiria, mpaka unakuwa na shida unashindwa kumwambia jinsi
tulivyo wengi tunaohitaji msaada kutoka kwake. Huwa naamua kunyamaza tu na
shida zangu.” Nanaa aliongea kwa kumuhurumia kaka yake. “Naomba
Mungu anisaidie nimalize shule, labda na mimi naweza kupata kazi yakumsaidia
kaka yangu, na yeye siku moja akapumzika.” Geb alikuwa akimsikiliza tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Walirudi kwenye gari, walipokaa tu,
kabla Geb hajawasha gari alimgeukia Nanaa. “Naomba usitafute chumba sasa
hivi. Naomba tubaki wote.” “Hapana Geb. Acha tu nianze maisha yangu. Pesa
ninayo yakujilipia na kuanza maisha. Nikikwama nitawaomba msaada. Nishasadiwa
sana, tena kwa manyanyaso makubwa sana. Sikunyimwa chakula wala sehemu ya
kulala. Hivyo havikuwahi kuwa tatizo kwenye maisha yangu. Lakini nilivipata kwa
garama kubwa sana. Huwezi kujua ni mara ngapi nilikuwa nikilala bila kula na
mimi ndio nilikuwa mpishi. Si kwa kuwa nilikuwa nanyimwa chakula, lakini kile
chakula kinakuwa kwenye sahani na maneno mengi sana Geb. Mbali na kuchoka
mwili, nafsi pia ilikuwa inachoka, naishia kwenda kulala tu bila
kula.” Nanaa akaanza kulia.
“Unalia usiku kucha. Hakuna wakukubembeleza,
hakuna wakukupa pole. Tena hata hapo kitandani kwenyewe unafuatwa na maneno
mengi, tena ya kweli tupu. Uchovu pekee ndio unakufanya ulale. Hujui unaumwa
lini, hujui unapona lini. Ukisema unaumwa, unaambiwa unadanganya ili usifanye
kazi. Hamna dawa, hamna pole. Sina shida ya kuendelea kusaidiwa, Geb. Sina
sababu yakuniweka nyumbani kwako. Naomba usijisikie ni kama nakimbia msaada, au
unalazimika kunisaidia. Nakuahidi nikikwama nitakutafuta nikuombe msaada,
lakini sasa hivi nipo sawa tu. Acha watu wote wapumzike na mimi niwe na
kwangu.” Nanaa alikuwa akiongea kwa uchungu huku akitokwa na machozi. “Nashukuru
kwa moyo wako wa ukarimu, Geb. Lakini nimeamua kuanza kujitegemea, acha na mimi
niwe na kwangu. Nianze maisha yangu. Inatosha.” Geb alijivuta kwenye
kiti chake akabaki amefunga macho.
“Unataka kuondoka lini?” Geb
akafungua macho baada ya muda na kutupa hilo swali. “Nikipata tu chumba,
nitaondoka. Ninazo pesa kiasi za kodi na kujinunulia vitu vya kunisogeza mpaka
nimalize chuo.” “Kwa hiyo unanikimbia, Nanaa?” “Hunihitaji Geb. Mengi
ninayokufanyia hata hukuwa ukijua kama ni mimi nilikuwa nikikufanyia. Ulijua
ni mama yako ndiye anayekufanyia. Na mama yako hajashindwa kukufanyia kitu hata
kimoja wapo. Ni mimi tu ndiye nilimuomba nifanye kwa kuwa nilijiona naamka
asubuhi sana, halafu sina kitu cha kufanya. Wakati yeye analalamika magoti
yanamuuma. Inamlazimu kuamka, akupikie halafu arudi tena kulala. Lakini bado
kuna vitu vingine huwa anataka akufanyie yeye mwenyewe. Haridhiki hata Grace
akikufanyia. Ni lazima akufanyie yeye mwenyewe. Kwa hiyo sina sababu yakuwa
pale. Naongeza idadi ya watu tu mle ndani, tena bila sababu. Kitu
kinachomuumiza Liz mpenzi wako.” Geb akamgeukia akamwangalia.
“Kama unataka kunisaidia, na kama
utakuwa kwenye nafasi ya kunisaidia, nikimaliza chuo, nitawaomba tena kazi. Si
mtaniajiri?” Nanaa akauliza, Geb kimya. “Kama nafasi ipo lakini. Na
mimi nilikwambia nitakwenda mkoa wowote ukinipa kazi, kasoro Moshi na Arusha
tu. Hata ukitaka kuniajiri kijijini nikukusanyie mazao, mimi sina neno.
Ilimradi pesa iingie.” Geb aliwasha gari wakaondoka bila ya kujibu kitu.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
wanarudi, hapakuwa na maongezi mengi. Nanaa alimmiminia uji kwenye kikombe
kirefu kinachokaa vizuri kwenye gari yake, Geb akaendelea kunywa huku
anaendesha. Safari hii Dalali akapiga simu. “Kuna chumba kingine nimekipata
mitaa ya Sinza.” “Sinza itakuwa garama sana na itanilazimu kuchukua daladala
mbili kufika chuoni. Kwani kile cha Savei imekuaje tena?” “Mwenzangu amempeleka
mtu huko, na ninaona wamekubaliana pesa.” “Usifanye hivyo bwana! Mbona na mimi
nilikwambia ninayo pesa? Ninayo kodi hata ya mwaka mzima.” “Lakini haupo dada
yangu. Fimbo ya mbali haiuwi nyoka.” “Hapa nipo njiani nakuja. Baada ya muda
mfupi sana nitakuwa hapo Mwenge, unipeleke. Hata ukitaka niwalipe pesa yenu
leo, nitafanya hivyo. Ila naomba usikiuze hicho chumba mpaka na mimi nikione.”
“Basi nakusubiri hapa Mwenge. Ukifika unipigie.” “Nitafanya hivyo, asante.
Lakini zungumza na mwenzako sasa hivi, mwambie asikiuze kwanza.” “Sawa.” Nanaa
akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nimekuponza?” Geb
akauliza. “Kwa nini?” Nanaa akauliza na yeye. “Umenisindikiza
huku, umekosa chumba.” Nanaa akacheka. “Wewe huwajui madalali. Hiyo
ni lugha yakunionyesha ananihangaikia sana ili nimuongezee pesa. Anaweza akawa
yupo sahihi, au ni lugha tu. Naomba unishushe Mwenge, nikamalizane naye kabisa.
Nitarudi nyumbani baadaye. Nitajitahidi kuwahi kabla baba mwenye nyumba wangu,
hajalala.” Nanaa aliongea kwa utani lakini Geb hakucheka, alimwangalia tu
akaendelea kuendesha.
“Sasa mbona umekasirika badala ya
kufurahi pamoja na mimi!?” “Natakiwa kufurahia nini? Kwamba unaondoka nyumbani
kwangu?” “Ufurahie kuwa nimepata chumba, naanza kujitegemea. Hakuna usiku wa
machozi tena. Nitakuwa kwangu.” “Naomba mimi hiyo kazi ya kukufuta
machozi.” Geb alimfanya Nanaa acheke sana. Alicheka mpaka akainama.
“Kama kweli vile!” “Kwa hiyo
huniamini?” Geb akauliza, Nanaa akamwangalia akamuona
anamaanisha. “Naomba usifanye hivyo Geb. Please.” “Kwa nini?” “Hapana.
Nimeshaumizwa sana hisia zangu. Naomba na wewe usiwe miongoni mwao. Usinipe tumaini
ambalo halipo.” “Unajua Nanaa, ni lazima ufike mahali ufungue moyo wako tena?
Ili kuamini mtu fulani, na kupenda. Nilishakuwa hapo ulipo. Tena mwenzio
nilikaribia kuchanganyikiwa.” “Hata mimi nilikaribia kuchanganyikiwa Geb.”
“Hapana Nanaa. Mimi namaanisha kukaribia kurukwa na akili kabisa.
Nilikwambia habari ya kufeli chuo. Basi amini nilifeli. Nikikwambia nilifeli,
nilifeli masomo yote. Nilikuwa sielewi tena sababu ya mapenzi.” Nanaa akamtizama
vizuri.
“Sijisifii kwako, lakini mimi Mungu
alinijalia akili ya ajabu. Sijawahi kupata alama chini ya 100, tokea naanza
shule mpaka namaliza. Kwa kuwa huwa sisahau kitu na nilijaliwa uwezo mkubwa
sana wakufikiri. Ukiniambia jambo, linaenda kukaa kichwani, halitoki.
Inanisaidia kwa upande mwingine, lakini inanitesa sana. Na ndio sababu yakutaka
kujiua niliposalitiwa na mpenzi wangu wa kwanza. Yale maneno aliyokuwa
akiniambia, ahadi tulizokuwa tumewekeana, zilikuwa zikijirudia kana kwamba ndio
alikuwa akiziongea na mimi wakati huo. Nilikuwa silali, wala kula. Halafu yeye
anaendelea na maisha yake kana kwamba hakuna kilichotokea!” Geb
akaendelea.
“Mimi ndiye nilikuwa mwanaume wake wa
kwanza. Tokea sekondari nilikuwa naye. Tulipofika chuo, akapata mwanaume
aliyekuwa akisomea mastares, shahada ya pili. Hivi unajua yule binti aliniacha
bila hofu wala kujiuliza! Si unajua pale Mabibo hosteli watu wa Mastars
walikuwa wakipewa vyumba vyao? Sasa yule binti alihamia kwa yule jamaa, akawa
anaishi naye. Jamaa alikuwa na gari, yaani alikuwa anamaisha fulani hivi. Watu
wakawa wananiambia vile wanavyomuona anatoka na jamaa na kuingia bila aibu na
tulikuwa tukifuatana naye kila mahali pale chuoni. Yaani watu walikuwa
wanatujua sisi ni wapenzi. Hapakuwa na mahali utamuona Geb bila yule binti. Si
asubuhi si usiku kasoro darasani tu. Tulikuwa kama kumbikumbi. Pale Mabibo
hosteli walikuwa wakitujua. Wenzangu walinipa jina la chizi kupenda. Nilimpenda
yule msichana kama mwehu.” Geb akajicheka.
“Nilikuwa namfuata chumbani kwa yule
jamaa, nampigia magoti. Namuomba anirudie. Yule jamaa alinipiga marufuku
kuingia kwenye lile jengo lao, kwa hiyo nilikuwa nakaa pale nje, hata masaa
manne, nikijiambia labda atatoka nijaribu kuzungumza naye, anirudie. Sijui
niliingiwa na nini!? Nilikuwa kama nimerukwa na akili. Kina James, Zinda, Malii
na Danny, walikuwa wakija kunitoa pale, nakunirudisha chumbani kwangu.
Wakiondoka tu, na mimi narudi kukaa pale nje. Nilijidhalilisha vyakutosha tena
bila kuchoka wala kujali. Ndio kina James na Danny ikabidi kwenda
kumwambia mama. Maana tulikuwa tumemaliza mitihani, lakini mimi sitaki kuondoka
chuo. Tena yote hayo yalitokea kipindi cha karibia na mitihani.”
“Kuna somo yule jamaa alikuwa
anawafundisha kundi la huyo binti. Kwa hiyo wakati mwingine yule binti
alikuwa akienda na marafiki zake kusoma, na mimi nakuwa na kina Danny. Muda
ukifika, naenda kumfuata, tunarudi chumbani kwangu. Sasa akaanza vituko, hataki
nimfuate tena, au anakwenda yeye mwenyewe kwa huyo jamaa bila marafiki zake,
mpaka akahamia kabisaa.” “Pole Geb. Kwa hiyo ikawaje?” Geb akajicheka tena.
“Ndio mama ikabidi aje pale chuo,
anichukue. Grace yeye alipata chumba Main Campus, kwa hiyo alikuwa akiishi huko
na wenzake. Mama akanirudisha nyumbani. Nilikuwa ninahali mbaya sana Nanaa.
Ndio kipindi hicho hicho mama na yeye akaokoka kwa ajili yangu. Mama alikuwa
akiniombea bila kuchoka. Matokeo yakatoka, mimi nikawa nimefeli kabisaa, yeye
yule binti amefaulu. Lakini usifikiri sikuwa namfuatilia nyumbani kwao?
Nilikuwa naenda mpaka kwao, kumbembeleza. Maana nyumbani kwao wote walikuwa
wananifahamu.” Nanaa alibaki anashangaa.
“Baada ya muda akahamia kwa huyo
jamaa, tena alikuwa mfanyakazi, ameajiriwa. Kipindi cha likizo au tuseme chuo
kikifungwa, jamaa alikuwa akirudi kazini. Haya, nikapeleleza mpaka nikaja
kupajua nyumbani kwa huyo jamaa. Nikaenda. Lakini nikamkuta yule binti, ana
mimba kubwa tu. Ndio nikasalimu amri, nikamuaga rasmi na kumuacha. Lakini
niliumia sana. Kwa kuwa aliniacha bila kosa! Labda kwa kuwa sikuwa na pesa.
Sijui! Ndio maana nachukia sana umasikini. Napenda kulala, sana.” “Grace
aliniambia.” Wakacheka.
“Napenda na nina furahia kulala. Na
ndio maana nimetumia pesa nyingi sana kwenye kitanda na mashuka ya kitanda
changu, kwa vile ninavyothamini usingizi. Najua mama amekwambia huwa nalala
naye.” Nanaa akacheka huku akikubali. “Mama hana siri!
Ananidhalilisha sana. Lakini ngoja niendelee, ndio maana hata
yeye nimehakikisha anakitanda kizuri, ili nikienda kulala kwake, nilale
sehemu nzuri. Napenda sana usingizi. Lakini kila nikifikiria pesa, yaani
nikiona kuna jinsi yakuingiza pesa, huwa najilazimisha kuamka. Starehe yangu ya
kwanza ni kulala. Lakini ikifika kwenye pesa, huwa usingizi inabidi
kusubiri.” Nanaa akacheka.
“Kwa hiyo Nanaa, usifikiri sielewi
unachoongea. Naelewa sana. Mimi nilitoka hapo kwa maombi ya mama yangu. Alikuwa
akinishika mkono hata nikiwa usingizini, ananiombea. Lakini ni lazima ifike
mahali, uchore mstari na uruhusu watu kwenye maisha yako.” Nanaa
alifikiria kidogo. “Nitajitahidi Geb. Lakini naogopa sana. Nimekuwa makini
kupita kiasi. Mimi nakiri kuwa sijawahi kupenda hivyo. Yaani ilikuwa ni kama
natafuta mkombozi tu kwenye maisha yangu. Mtu wakunitoa pale kwa mama mkubwa,
na kuishi na mimi. Sikuwa na vigezo vingii. Sijui mrefu, mwenye pesa, mweupe,
au mweusi. Sikujali hayo. Ilikuwa yeyote atakaye nijia.” Nanaa akafikiria
kidogo.
“Lakini sasa hivi nimeamua kuchunga
moyo wangu, naogopa hata kufikiria kumwingiza mwanaume moyoni. Yaani hata wazo
likinijia tu, najionya kwa haraka sana. Nahisi nitakufa, Geb. Sitaweza. Hawa
wanaume wote walionitenda niliumia hivyo, sasa ije itokee nipende kama wewe
ulivyompenda huyo binti, si ndio nitakufa?” “Sasa hivi utafanikiwa Nanaa. Kwa
kuwa utaanza mahusiano mengine ukiwa umetulia, huna haraka au haupo desparate.
Toa nafasi yakupendwa tu.” Nanaa akacheka sana.
“Unavyoongea kama rahisi vile!” “Ni
rahisi.” “Mmmh! Haya bwana. Naanza kutoa hiyo nafasi. Sasa sijui nitoe tangazo
kwenye vyombo vya habari na social media, ili waanze kuja!? Au nimtafute Zinda
kwanza?” Geb akamtizama. “Anza kuwa makini na watu wanokuzunguka
kwanza. Usikimbie, tulia. Unaweza kuweka mawazo na macho yako mbali, ukawapita
walipo karibu yako.” Nanaa akanyamaza.
Nanaa &
Geb.
Nanaa
agundua Geb anamfahamu zaidi ya alivyofikiria. Geb anataka Nanaa aendelee
kuishi naye wakati Liz bado yupo ndani ya picha. Hatoi maelezo yakumtosheleza
Nanaa kumfanya akubali kubaki nao pale nyumbani kwake. Hofu ya kuumizwa tena
inazidi kumtesa. Ni kama kwa mara ya kwanza maishani, vitu vyote alivyokuwa
akivitamani sana vinafunguka kwa wakati moja. Anapata matarajio ya kupata
nyumbani kwake na mwanaume ambaye hana uhakika naye, Geb yupo pembeni yake
akimsihi tu abaki.
-
Aende wapi?
-
Achague kuhama akaanze maisha yake, au
-
aendelee kubaki na Geb ambaye anafunguka nusu nusu.
-
Kwa nini?
Usikose
mwendelezo ….
0 Comments:
Post a Comment