Sasa jumapili hiyo iliangukia mwishoni mwa mwezi.
Antii alikuwa akienda kutoa misaada hospitalini. Nanaa akaona ni jambo la
kujifunza na yeye, ajiunge naye. Wakaongozana na kumsaidia kugawa vitu. Baada
ya siku ndefu ya misa, huko kanisani na kutembelea wagonjwa hospitalini,
walirudi wote wamechoka, wakajitupa kwenye kochi wakasinzia.
Baada ya
kurudi kutoka Marangu.
Waliwasili nyumbani mapema tu. Hata chakula cha
mchana walikila nyumbani. Mama G akaanza kumsaka Nanaa kwa simu. Akawa
hapatikaniki mchana kutwa. Aliiacha simu yake nyumbani, kwani iliishiwa chaji
baada ya kusikiliza miziki usiku kucha akiwa analala. Akaona hamna haja ya
kuibeba. Akaicha nyumbani kwa Antii. Asijue kama kuna mtu atamtafuta. “Kwanza
nani? Kina mama G sasa hivi wapo Arusha na wanae wanafurahia utajiri Mungu
aliowapa. Kaka atakuwa ameenda kumuona baba mkubwa. Hakuna wakunitafuta.” Nanaa
akawaza na kuitupia simu yake kitandani na kuondoka.
Aliporudi nyumbani, akaiweka kwenye umeme pembeni
yake, akalala. Asijue anavyotafutwa. Yupo ambaye alishachanganyikiwa tokea mama
yake alipomkosa kwenye simu kwa mara ya kwanza walipofika tu nyumbani. Chini
palikuwa hapakaliki, usingizi hauji. Kila mtu alikwenda kulala kupunguza uchovu
wa safari na kuamka alfajiri siku hiyo, kumuwahi Nanaa jijini Dar. Walipokula
tu, kila mtu akaelekea chumbani kwake kulala.
Mama G hakulala. Kila wakati Geb aliingia
chumbani kwake na kumuulizia kama amempata Nanaa. “Hivi unajua hata dakika
moja haijaisha tokea ulipoingia hapa chumbani na kuniuliza swali hilo
hilo?” Geb akanyamaza, nakutoka. Baada ya dakika tano akarudi tena
chumbani kwa mama yake. “Mimi naona upande hapa kitandani, uendelee
kumpigia simu kwa kutumia simu yangu. Wakati mimi nalala kidogo. Akipokea,
uniamshe.” “Sasa unalalaje mama kwenye hali kama hii!?” Geb akauliza kwa
hasira na kulaumu. “Nimechoka Geb mwanangu! Nimepiga simu zaidi ya mara
kumi! Na nimemuachia ujumbe, akiwasha simu yake tu, ataona ujumbe na
atanipigia. Naomba tusubiri. Atapiga tu.” Geb akajilaza pembeni ya mama
yake.
“Unaweza kukuta simu yake iliibiwa au hana
pesa.” Mama G ndio alikuwa anapitiwa na usingizi. “Umeniamsha Geb
jamani! Kwa nini unakosa subira bwana?” Mama G akalalamika. “Naomba
uondoke na usirudi tena humu ndani mpaka nitakapokuita. Haya
toka.” Akaamua kumfukuza. Geb akatoka. Lakini hata mama G mwenyewe
akashindwa kulala kwa kumuhurumia. Akatoka na yeye. Akamkuta amekaa sebuleni
peke yake. “Atapiga. Usiwe na wasiwasi.” Akamfariji wakati
anakaa. “Njoo ulale hapa karibu yangu. Sitakuongelesha tena.” Mama G
akacheka. Akaenda kweli kulala kwenye kochi refu alilokuwa amekaa Geb.
~~~~~~~~~~~~~
Alishituka kutoka usingizini, akaiwasha simu
akiwa amejilaza palepale kwenye kochi. Mara simu ya mama G, ikaingia. Akaipokea
kwa haraka na sauti ya kiusingizi, kabla hajamwamsha na Antii aliyekuwa
amelala, kwenye kochi la pembeni yake. “Mama!”
“Maajabu, unalala saa hizi! Kwani wewe mgonjwa?” Nanaa akacheka
kidogo. “Mwenzio nilikuwa hospitalini kuona
wagonjwa na kuomba nao. Nilimsindikiza Antii.” “Bora. Tumerudi.” “Poleni na
safari.” “Asante. Lakini nataka tuzungumze Nanaa.” “Unataka nije sasa hivi!?
Naona giza limeshaanza kuingia. Nitakuja kesho.” Nanaa asijue jinsi
alivyokuwa akisubiriwa na kutafutwa kwa muda mrefu.
“Hapana. Njoo leo. Tena sasa hivi.
Chukua taksii mimi nitalipa.” Nanaa akaanza kucheka. “Sasa
unacheka nini?” “Mwenzio huko bado sijafikia. Yaani nizungushwe na taksii hapa
mjini!? Kwani daladala zimeisha? Nakuja, lakini si kwa taksii.” Mama
G akaanza kucheka. “Mimi nitalipia bwana! Chukua
taksii Nanaa.” “Utanifanya nisilale usiku bure! Niwe na kazi ya kuota usiku
kucha! Acha tu nipande daladala tu.” Mama G akacheka tena. “Nanaa wewe mtundu sana. Sasa kwa nini uote?” “Si
kupanda taksii! Yaani eti Nanaa ajikute tu amepanda kwenye taksii! Halafu
anaendeshwa na mtu atakayemlipa baadaye! Mama wewe hunitakii mema!” “Si mimi
nitalipa?” “Acha tu nije na daladala mama yangu. Nishazoea.” “Usichelewe sasa.”
“Wewe unanijua. Nusu saa tu, nitakuwa hapo. Niombee usalama tu huko
barabarani.” Wakacheka kidogo. Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~
Akaingia kuoga. Akabadilisha nguo. Akavaa gauni
la kawaida tu refu mpaka chini. Mtoto huyu wa kichaga ni wa ajabu. Umbo lake la
tofauti. Alipendeza na gauni lake la kawaida tu. Mikono mifupi mpaka chini
kidogo ya mabega. Alijaza gauni hilo kwenye maeneo ambayo ungependa kutizama.
Akatoka. Antii alikuwa anakoroma. Akaanza kucheka. “Nanaa unanicheka?”
“Sasa ulalaji gani huo wa kukoroma hivyo Antii jamani!?” “Nimechoka bwana.
Mbona umetokelezea? Unaenda kwa James?”
Ikabidi Nanaa akae chini amuelezee stori ya Mama
G, na wanae. Akaeleza kwa kifupi mpaka simu ya mama G aliyompigia muda mfupi
uliopita, kutaka kufika mara moja pale kwao ili wazungumze. “Kwa hiyo
naweza kurudi na mabegi yangu.” “Wewe njoo nayo tu.” Wakaagana, Nanaa
akatoka akiwa na furaha.
Kwa Geb!
Ilikuwa siku ya jumapili. Hakupata shida ya
kupata daladala. Akapanda daladala zilizomfikisha mpaka kituo kilichokuwepo
karibu na nyumbani kwa Geb. Tabata Barakuda. Akatembea mpaka getini. Akabonyeza
kengele. Mlinzi akamuuliza kwa kupitia spika iliyokuwepo kwenye nguzo nje,
pembeni ya geti. “Naitwa Nanaa. Mama G,
ananitegemea huko ndani.” “Subiri.” Mlinzi alimjibu kwa kutumia
spika hiyo. Nanaa akajua ni mpaka apige simu ndani, akiruhusiwa ndipo
atamfungulia geti.
Alisimama pale kwa muda mfupi tu, akasikia geti
dogo likifunguliwa. Akasogea akijua ni mlinzi. Macho yake yakagongana na Geb.
Akashituka sana, akarudi nyuma kidogo. Hakutegemea kuiona sura ya baba mwenye
nyumba getini. Kwani haikuwa kaiwada ya hapo. Unafunguliwa geti na kuingia
ndani. Utakutana na wenyeji ndani ya nyumba. Sio ufuatwe nje, getini.
Akababaika sana huku Geb akimwangalia. “Samahani
nimekuja mida hii. Najua ni usiku. Na giza limeingia. Mmetoka safari, mmechoka.
Lakini Mama ndiye aliyeniita. Nilimwambia nije kesho, lakini amesema nije
tu leo. Nitajitahidi nisikae sana. Sitachelewa kutoka ili na nyinyi mpate muda wa
kupumzika.” Nanaa aliongea kwa muda mrefu, akijitetea, huku Geb
akimwangalia.
Geb alijua amepaniki kumuona pale. “Lakini naweza
kurudi tena hata kesho. Mapema kidogo. Au nitamwambia mama tuzungumze tu kwa
simu.” Nanaa akaendelea tena akionyesha kutaka kuondoka. “Hamna
shida. Nimefurahi kukuona. Karibu ndani.” Kidogo Nanaa akatulia akifikiria
jibu la Geb huku akimwangalia kutaka uhakika na alichomwambia.
Alikunja uso kidogo, Geb akamuona. Pale nje ya
geti lake, Geb alijengea mataa makubwa yenye mwanga mkali, mweupe kwa ajili ya
usalama. “Karibu ndani.” Akampisha
getini. “Asante.” Akaingia ndani akiwa na wasiwasi. Akili zake
zilishindwa hata kufikiria kwa nini Geb yupo pale. Na kwa nini yeye ndio
anamfungulia geti na sio mlinzi! “Labda kwa kuwa ni usiku sana.” Nanaa
akawaza. Palikuwa na umbali kidogo kutoka getini mpaka kufikia nyumba.
Akanyanyua uso kumtizama wakati wakitembea. Geb
naye akamwangalia. “Pole na safari.” Ndilo neno lililofanikiwa kutoka
tena, mdomoni kwa Nanaa. “Asante.” Geb akajibu, wakaendelea kutembea
kuelekea ndani
~~~~~~~~~~~~~
Alikuta
watu wote sebuleni. Kidogo akaingiwa na wasiwasi. “Nilijua mtarudi
kesho!” Nanaa aliongea huku akimsogelea mama G
taratibu. “Tuliahirisha. Sababu yako.” Nanaa akaanza kucheka
taratibu. “Ulinimiss?” Alimnong’oneza mama G, wakati anakaa. Mama G,
akacheka kidogo. “Muone!” “Sasa kwa nini hamkwenda kutembea Arusha?
Ungepata sababu yakuniletea zawadi!” “Hata hivyo nimekuletea zawadi.”
“Mmmh! Unanidanganya mama kunirusha roho!” “Kweli.” “Zawadi gani ya kutoka hapo
Moshi?” “Utaiona. Ngoja kwanza tuzungumze.” Nanaa akaangalia wengine,
akaona wametulia wanawasikiliza wao. Hapakuwa na kuangalia tv. Kwanza haikuwa
hata imewashwa. Akaingiwa hofu. Akatulia.
“Mbona sasa umeingiwa woga?” Mama G, alimwangalia
Nanaa alishapooza. “Sijui!” Nanaa alijibu kwa upole. “Wala
usiogope Nanaa. Ni mambo machache tu yakuwekana sawa.” Nanaa akajiweka
sawa. “Hatukufurahia jinsi ulivyoondoka na kutuacha Marangu.” Nanaa akainama. “Huwa
tunazungumza sana mimi na wewe. Tena mara nyingine tunaagana kwenda kulala,
lakini ukifika chumbani ukikumbuka kitu, unanipigia simu. Tunazungumza hata
lisaa, ndipo tunaagana tena. Kwa nini uliondoka Marangu bila kunijulisha wakati
tulipeana mipango mingi sana mimi na wewe?” “Kaka…” Nanaa akasita, kisha
akaanza tena kwa kujirudi.
“Nilikosea mama. Lakini ni maamuzi yalikuwa
ya haraka tukashauriana na kaka niondoke tu. Lakini mama, nia ilikuwa nzuri tu.
Kuleta amani. Sikuwa na nia mbaya. Kama
nilikosea, au kama mimi na kaka tulikosea kuamua vile, naomba radhi, nilikosa.
Mtusamehe.” Tayari machozi yalishaanza kumtoka Nanaa. Kama
alivyomwesi kucheka, ndivyo alivyokuwa mwepesi kulia. Hisia zake zilikuwa
karibu sana.
Wote wakanyamaza wakisutwa moyoni. Nanaa
alijirudi, yeye ndio akawa anawaomba msamaha. “Nilifanya
maamuzi ya haraka, mama yangu. Halafu sikutaka mimi ndio niwe sababu ya
kuharibika jambo zuri kama lile. Ndio maana nikaamua kuondoka kwa haraka. Kama
nilikosea, naombeni mnisamehe.” “Nia ilikuwa nzuri Nanaa. Lakini
kulikuwa na njia nyingine ya kuleta amani, kuliko ulivyoondoka.” “Kwani niliharibu zaidi?” Nanaa akauliza kwa
upole. “Ndiyo Nanaa.” Mama G akajibu.
“Oooh! Naomba nisamehe mama yangu.” Nanaa akamshika
mkono. “Nisamehe mama. Sikukusudia
kuwaudhi.” “Mimi ni mama yako Nanaa. Lazima ujifunze kuniambia
chochote kile.” “Nilifikiria hivyo mama.
Lakini nikawa hata sijui nikwambie nini! Nilishika simu mara kadhaa nikitaka
kukupigia, lakini nikashindwa. Nikasema nikutumie ujumbe ili nikuombe ushauri.
Niliandika jumbe karibia tatu. Nikaishia kuzifuta tu. Nilishindwa, nilikuwa
sijui nitakwambia nini! Wazi nilijua mimi ndio tatizo mama yangu. Mimi ni
mpitaji tu hapa kwenu. Na tokea nimefika hapa kwenu, nilichokikuta kikubwa ni
amani. Sijawahi kusikia hata kupishana kwa maneno kati yenu. Mimi huwa najijua
mama. Au kama mama mkubwa alivyosema, mimi ni tatizo. Kila ninapoenda lazima
kuwe na tatizo. Nikajua nikiondoka, utakuta amani. Na wewe upate wakati mzuri
wa kufurahia na kusherehekea. Sikukusudia baya mama. Nimekosa, naomba
mnisamehe.” Nanaa alikuwa akiongea kwa kunyenyekea huku akilia.
“Hapana Nanaa. Usikubali huo uongo. Wewe
sio tatizo. Umekuwa faraja kubwa sana hapa kwetu. Umeongeza kitu kingine kati
yetu. Kwanza nimehesabu ni kama nimepata mtoto mwingine.” Nanaa
akatabasamu huku anafuta machozi. “Kweli kabisa. Wote tumekuelewa. Na pole
kwa yote yaliyokukuta huko njiani mpaka ulipofika hotelini na kukufanya
uondoke.” Nanaa alinyamaza akabaki ameinama huku anafuta machozi
yaliyokuwa yakiendelea kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
Simu ya Nanaa ikaanza kuita. Akaingalia kwa
muda. Akafuta machozi akaipokea. “Ulifika salama?
Maana usingizi umeniishia ndio nikakumbuka umeniaga unakwenda Tabata na utarudi
na mizigo.” Nanaa akacheka. “Nilifika
salama. Pole na uchovu.” “Asante. Niliamka mapema sana. Nikufuate na gari?”
“Wala usihangaike. Wewe pumzika tu. Hata hivyo sio mizigo mingi Antii. Nitapandisha
tu kwenye daladala. Ila usilale tena, ukanifungia mlango.” Antii
alisika akicheka. “Nimekwambia usingizi umeisha.
Utanikuta nipo macho nasafisha na kumwagilia mboga zangu.” “Usiku huu!?” Nanaa
akashangaa kwa sauti huku akiangalia muda kwenye simu yake. “Si unataka nikusubiri wewe?” Nanaa
akacheka. “Haya mwagilia. Nakuja muda sio mrefu,
sitachelewa.” Wakakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
“Kwa hiyo mama umenisamehe?” Nanaa
alivunja ukimya. “Yameisha Nanaa.” “Basi nimefurahi. Siku nyingine nitakwambia.
Sitaondoka bila kukuaga.” Mama G, akatabasamu. “Na wengine naomba
mnisamehe. Nilikosea.” Geb, Danny, Grace akiwa amempakata Fili walikuwa
kimya wamekaa wakiwasikiliza.
“Mimi naelewa Nanaa. Pole na
wewe.” Grace akaongeza. Nanaa akatabasamu akainama. “Unajua Nanaa,
mimi huwa sio muongeaji sana. Na kukiwa na hali ya kutokuwa na amani, ndio
kabisaa. Huwa siwezi kabisa kuongea. Nikijitahidi sana, nikulia basi. Maneno
haya machache huwa yanaishaga kabisa kila panapokuwa hamna amani. Kwa hiyo
wakati mwingine unaponiona nimenyamaza, sio kwa kuwa sijui au sielewi
kinachoendelea, ila ni kwa kuwa naishiwa. Sijui niseme naishiwa nguvu! Sijui
niseme nini! Lakini kunyamaza kwangu hata siku ile usiku, nilikusudia kupunguza
maneno mengi ili kutulie. Lakini sio kwa kuwa nilifurahia mkasa mzima. Hapana.
Kwa hiyo naomba na mimi unisamehe tu pale unapoona ulitakiwa kutetewa, halafu
ukaona kuna ukimya.” Grace aliongea kwa upole kama kawaida yake. Ongea
yake yenyewe ni kama alishachoka kabla hata hajafikisha neno la pili.
“Kwa hiyo naomba unisamehe. Na kama mama
alivyosema, ukiona kitu hakipo sawa, mwambie tu. Usiache kumwambia mama.” “Mimi
mnanijua nilivyo na maneno mengi na hasira. Kwa hiyo huwa naona ni heri kuongea
na mtu kama Geb, au rafiki zangu. Kwa kuwa wameshanijua. Na wanajua mpaka sauti
yangu. Kwa hiyo wanajua nikiongea hivi, wanisaidie kwa haraka ili nisipandishe
hasira zaidi. Huwa siwezi hata kidogo kuzungumza na mtu anayenijibisha.
Ndio maana huwa nikishakujua huwa unajibishana, huwa sipendi ukaribu na wewe,
hasa nikiwa nahasira. Labda ndio maana nampenda mke wangu. Mtu mkali sana huwa
simuwezi. Au mwenye maneno makali huwa simuwezi.” Danny akamkatisha mkewe
na kuendelea.
“Kwa hiyo na mimi naomba unisamehe kama uliona
nimenyamaza. Ni heri vile nilivyonyamaza, kuliko ningenyanyua mdomo wangu.
Ningeharibu zaidi. Wote hawa wananijua. Ndio maana huwa hawashangai wanaponiona
nyakati nyingine huwa nakuwa kimya. Wananijua. Muulize hata kaka yako akiwa
ametulia. Atakwambia juu yangu. Ananifahamu, na huwa anashukuru Mungu
kunapokuwa na ugomvi, halafu nanyamaza. Huwa mimi sio msaada mzuri sana. Huwa
naharibu, badala ya kusaidia.” Nanaa akacheka huku ameinama.
“Hamna shida, nimeelewa.” Ukimya ukazuka.
Geb akiwa kimya. Walitegemea aongee kitu. Lakini hakuwa amezungumza jambo
lolote tokea wametoka Marangu. Alijibu baadhi ya maswali wakiwa njiani tena
pale alipoulizwa. Tena alichagua nini chakujibu. Mengine hakujibu kabisa.
Alionekana ana mawazo mengii.
“Naomba niwashukuru kwa kunihifadhi kwa kipindi
hiki. Nimepata sehemu nyingine yakuishi mpaka nitakapopata chumba au mpaka chuo
kitakapofungua. Asanteni kwa kila kitu. Nataka kuwahi kuondoka kabla daladala
hazijai...” “Subiri kwanza Nanaa. Kwa nini unatuacha sisi, unaenda kuishi
kwengine? Heri ingekuwa unarudi kwa James!” Mama G, alimbadilikia
Nanaa.
“Sio kwa nia mbaya mama. Siwezi kurudi tena kwa
kaka. Mama mkubwa ameniomba nimpe nafasi ili na yeye aweze kujifikiria, na
pengine atafikiria swala la kuoa. Amenikataza
hata nisiwe nakwenda pale na kumsaidia kaka kazi. Anasema ndio maana anashindwa
kuona umuhimu wa mwanamke. Amesema nisirudi tena pale, na yeye hataondoka mpaka
ahakikishe kaka ameoa. Ndio pengine ataniruhusu kurudi tena pale. Kwa sasa ndio
tumempata huyo mama, mtu wa kwetu. Ameonyesha anaweza kunihifadhi kwa muda
wowote nitakao taka mimi.” “Kwa nini uondoke hapa?” Mama G
akauliza. Wakati anaweka tu kituo kwenye swali lake, wakasikia gari inaingia
getini. Wote wakajua atakuwa ni Liz tu.
~~~~~~~~~~~~~
Kwani kwa yeye Liz mlinzi wa getini hakuhitajika kuuliza
ndani kama anaruhusiwa kuingia au la. Magari yake yalifahamika. Kwa hiyo kila
gari linalosimama pale getini, namba ziliingizwa kwenye komputa. Zilizoruhusiwa
kuingia, geti lilifunguliwa bila kuonana na mlinzi, lakini kama namba yako
haikuwa kwenye kompyuta ya getini, utasikia sauti ya mlinzi kwenye spika ndogo
ya kwenye nguzo ya chuma iliyokuwepo hapo nje. Akikuuliza wewe ni nani na
unamtaka nani. Ndipo utaambiwa usubiri mpaka ruhusa itolewe ndani ndipo
utafunguliwa geti. Lasivyo hutaingia kwenye hiyo nyumba. Na wakati wote kamera
za nje na ndani ya kuzunguka hiyo nyumba, zilikuwa zikionyesha kwenye screen ya
chumba kidogo hapo ndani ya geti, walipokuwa walinzi.
~~~~~~~~~~~~~
Ukimya ukazuka, akaingia Liz, mpenzi wa
mwenye nyumba. Aliingia akionekana na haraka kidogo. Aliwakuta watu wote
wamekaa palepale sebuleni. “Za safari jamani?” Liz alisalimia bila
kusimama wala kumwangalia mtu, akapitiliza chumbani kwa Geb. Hakuna
aliyeitikia. Mama G akamtizama Geb, Geb akaelewa macho ya mama yake. Kwani
macho hayo yalikuwa wakati mwingine yakizungumza nao yeye na Grace, tokea
wakiwa watoto, bila hata mama huyo kufungua kinywa, aliweza kufikisha ujumbe
kwa macho tu. Na walimuelewa mama yao kwa kumuangalia machoni na kutekeleza kwa
haraka sana. Geb akasimama taratibu na kumfuata Liz chumbani.
Akafungua mlango na kusimama mlangoni akiwa
anamwangalia Liz. “Vipi?” Walimsikia Liz akimsemesha Geb. “Safi
tu.” Liz akaanza kupekua. “Unatafuta nini nikusaidie?” Geb
akauliza. “Ndio nimetua na ndege sasa hivi. Lakini nimeona kabla ya kufika
nyumbani, nije kuchukua vitu vyangu. Niliviacha hapa mara ya mwisho
nilipokuwepo hapa. Usiku kabla ya safari.” “Ni nini?” Geb akauliza. Kimya,
Liz akaendelea kutafuta. “Labda ungeniambia, ningekusaidia kutafuta.”
“Yaani unanifukuza, unatamani nitoke hapa sasa hivi!?” Liz akauliza
kishari. “Mimi ndio nalala hapa. Inawezekana wakati nasafisha, kuna mahali
nimekuhifadhia vitu vyako.” Kimya, Liz akaendelea kupekua.
“Mbona sasa sioni mkufu wangu?” Liz
akauliza. “Niliuvua nikauweka hapo mezani na hereni. Nilipoamka nikachukua
hizi hereni nikasahau mkufu. Na mkufu wenyewe nilipewa zawadi na mama
yakumaliza darasa la saba. Ni wa muda mrefu na umebeba historia ya muhimu sana
kwenye maisha yangu. Siwezi kuupoteza maana pia ni ile dhahabu nzito ya thamani
kweli kweli.” Liz alisikika ameshapaniki.
“Kwani nani mwingine huwa anaingia
humu?” Liz akauliza. “Tuangalie vizuri, Liz. Kama uliacha hapa,
utakuwepo.” “Kwa hiyo unaniita mimi muongo?” “Namaanisha kama uliuacha hapa,
lazima utakuwepo. Hakuna mgeni aliyekuja tokea uondoke, na wala hakuna mwizi
humu ndani. Tuendelee kutafuta. Ninauhakika tutaupata tu.” “Wewe unawajua watu
wote humu ndani? Unajua tabia zao? Mbona sikuelewi!? Unatetea nini sasa!?
Hakuna mwizi! Wewe unashinda nao humu ndani?” Liz aliendelea kuropoka.
Grace alinyanyuka akaamua kwenda kumlaza mtoto,
akawafuata huko chumbani. “Naombeni na mimi nisaidie kutafuta huo mkufu,
kutulie humu ndani.” “Unamaanisha nini? Kwamba mimi napoteza amani ya hapa?”
“Nisikilize Liz. Mimi sitaki maneno mengiii. Shida ni mkufu uonekane au ni
nini? Kama ni mkufu tu, naomba tuutafute. Utakakuwepo tu. Hiki chumba
anasafisha Geb mwenyewe. Hakuna mtu mwingine anaingia humu ndani.”
“Unajuaje?” Liz akauliza.
“Kwa hiyo unafikiri mimi na mama au Danny ndio
tumekuibia huo mkufu?” “Kwani ni nyinyi tu ndio mnaishi humu ndani? Mbona siku
zote naacha vitu vyangu humu ndani na ninavikuta? Iweje leo sivioni? Nanaa
aliondoka Marangu tokea siku ya ijumaa. Ulikuwa naye?” Grace aliumia
sana. “Liz wewe!? Naomba nyamaza. Tafadhali sana nyamaza.” Grace
hakutaka kuongea naye zaidi, akaanza kumsaidia Geb kutafuta huo mkufu. Grace
alivuta droo zote kwenye kabati la Geb, akamwaga vitu vyote kitandani, nakuanza
kuchambua kitu kimoja baada ya kingine bila mafanikio.
“Mlikuwa mnaniona mimi muongo. Sasa uko wapi huo
mkufu? Na hapa ndio sehemu ya mwisho kuwa nao.” Waliendelea kutafuta
wakati Liz amesimama. Chumba cha Geb kilikuwa kina kapeti kubwa chini ya
kitanda. Geb akainama kutafuta uvunguni. “Huu hapa mkufu wako.” Geb
akanyanyuka na ule mkufu. Liz akauchukua na kutoka pale bila ya kuongeza neno.
Hakusema hata asante, akaondoka. Alipita pale sebuleni bila hata kuaga.
Mkufu ulipopatikana tu, na Liz kuondoka, Nanaa
naye akasimama, akaingia kwenye chumba alichokuwa analala. Akaanza kukusanya
mizigo yake huku akilia. Machozi yalikuwa yakimtoka mfululizo huku kwikwi
imemng’ang’ania kooni. Alijua wenyeji wake watakuwa wameshapata jibu la kwa
nini anaondoka. Akasikia mlango unagongwa taratibu. “Karibu.” Nana alimkaribisha huku analia
sana. Alikuwa Geb. Alipomuona tu ni yeye, akasogea mbali zaidi huku ameina
akilia.
“Nanaa!” Geb alimsogelea karibu, lakini
Nanaa aliendelea kulia huku akirudi nyuma kama kumkwepa. “Nanaa!” Akasogea
tena kama amkumbatie, lakini Nanaa akamkwepa. “Hapana
Geb. Naomba unipishe. Nataka nimalizie kukusanya mizigo yangu niwahi kuondoka.” “Nanaa
please!” “Hapana Geb. Naomba usiniongeleshe
chochote. Nataka kuondoka. Nimepata sehemu nyingine ya kuishi. Acha niende
tu.” Nanaa aliendelea kulia huku ameshika baadhi ya nguo zake
mkononi. Alichukua moja wapo ya nguo hizo, akajifutia machozi na kamasi
zilizokuwa zikimdondoka. Alikuwa ameshafika mwisho kabisa kwenye ukuta.
Geb akamsogelea mpaka pale akamvuta karibu yake
akamkumbatia. Alimkumbatia kwa kupishanisha mikono yake juu ya mgongo wa Nanaa,
na kubaki ameegemeza kichwa chake juu ya kichwa cha Nanaa. Alisikika yeye
kupata nafuu kubwa kuliko hata Nanaa mwenyewe aliyekuwa akilia. Alikuwa
amemkumbatia kwa nguvu sana, hata Nanaa alisikia ile hali. Akamuhurumia.
Mwishowe akaanza kusugua mgongoni kwa Nanaa kwa kutumia mkono wake moja. Faraja
aliyokuwa akiipata Nanaa, alitamani asinyamaze aendelee kulia ili aendelee
kubembelezwa vile. Lakini taratibu hasira zikapungua. Akajikuta amenyamaza.
Wote wakifurahia ile hali ya utulivu pale.
Geb alirudisha mikono yeke kama ilivyokuwa
mwanzoni. Akamkumbatia tena Nanaa. Wakajikuta wamenyamza na kutulia. Wakajikuta
nyuso zao zimegeukiana kwa karibu kabisa. Nanaa akipata sawia pumzi ya Geb,
kadhalika Geb vilevile aliweza kupata pumzi ya kujaribu kutulia kwa Nanaa.
Ukapita muda kidogo, Nanaa akakumbuka Geb ni wa Liz. Akajitoa mikononi mwake,
akasimama pembeni kidogo akainama.
Geb alimshika mkono akamvuta mpaka pale
kitandani, akamuomba wakae. “Naomba nikuombe radhi, Nanaa. Pole na
samahani sana.” Nanaa alianza kulia taratibu huku ameinama akichezea
kifungu cha moja ya nguo aliyokuwa ameshika. “Nikwambie tu ukweli Nanaa,
ni heri vile nilivyonyamaza tokea mwanzo kuliko ambavyo ningetoa hata neno moja
kinywani mwangu. Hakuna mtu yeyote kati yenu ambaye angekuwa tayari kupokea
neno lolote kutoka kinywani mwangu. Ingekuwa mbaya zaidi.” Nanaa hakuwa
ameelewa.
“Sielewi
Geb.” Nanaa aliongea kwa upendo huku akifuta machozi. “Ukikaa
hapa kwa muda kidogo, pengine utanielewa.” Nanaa akainama kama
anafikiria. “Huna haja yakuondoka hapa. Kwanza wewe ni mwanafunzi, kodi
yakulipia chumba utapata wapi?” “Grace
ananilipa mshahara. Ninazo pesa na kaka amesema nikiacha kazi, chuo kikifungua,
ataendelea kunipa pesa. Ninazo pesa. Acha tu niondoke hapa, ili nisiharibu
mahusiano yako. Sitaki kuwa mvunja amani au mahusiano ya watu. Mimi ni mpita
njia tu, Geb. Kama nisipoondoka leo, basi lazima itakuwa kesho. Basi ni heri
iwe leo kabla sijaharibu zaidi.” “Mapenzi ya kweli huwa hayavunjwi
na nguvu ya nje Nanaa. Labda ndani. Ikitokea wapendanao wamechokana. Hizo
nyingine ni sababu tu.” Nanaa akahisi anafikishiwa ujumbe yeye. Kwani Geb
alibaki akimtizama.
~~~~~~~~~~~~~
“Hawezi kuwa ananizungumzia mimi. Itakuwa
anamuongelea Liz.” Nanaa
akawaza wakati amekwepesha macho yake baada ya kumsikiliza Geb. “Kwani
mimi ni mpenzi wake? Atakuwa anaongelea Liz tu.” Nanaa akaendelea
kujitetea. “Lakini amesema mapenzi ya kweli hayavunjwi na nguvu ya nje.
Hajasema mpenzi wa kweli. Lakini kwani mimi nimesema wapi kama nampenda?” Nanaa
akaendelea kuwaza huku akichezea kile kifungu. “Lakini kuna kitu cha
tofauti ninachojisikia nikiwa na Geb. Nashindwa kujizuia kabisa!” Nanaa
akawaza tena. “Itakuwaje nikiondoka halafu nikawa nakimbia nafasi ya
pekee kwa Geb?” Bado Geb alikuwa ametulia kana kwamba anampa nafasi ya
kufikiria.
~~~~~~~~~~~~~
“Utajuaje sasa kama lipo penzi la
kweli?” Nanaa akajikuta anaendelea kuwaza. Safari hii swali likatoka kwa
sauti. Akashituka kidogo. “Sio kwamba nakuuliza wewe. Nahisi nimeropoka
tu. Nimewaza kwa sauti.” Nanaa aliendelea kujitetea. “Maana wakati
mwingine unaweza kuta hiyo nguvu ya nje, ndio ishara ya kuwaonyesha kuwa
hamtakiwi kuwa pamoja. Ishara ya kushituliwa ni muda mwafaka wakutoa mawazo
potofu.” Nanaa akaendelea kuongea.
Mwishowe akajishitukia. “Samahani. Ulikuwa
unaongea wewe. Nakusikiliza.” Geb akatabasamu. Alifurahi kujua ujumbe wake
umefika. “Penzi la kweli kama lipo, lipo tu Nanaa. Na upendo huwa umebeba
sifa nyingi sana. Moja wapo ni subira. Upendo unatabia ya kuvumilia. Ukiona mtu
anasubira na mwenzie ujue lipo penzi la kweli.” Nanaa akainama. Geb
akatulia akabaki akimtizama.
Akamsikia anavuta pumzi kwa nguvu. Akajiweka
sawa. Nanaa akamwangalia. “Mbona midomo imekukauka Geb? Umechoka. Uliweza
kupata muda wa kupumzika kweli?” “Hapana. Imekuwa safari ngumu zaidi ya
nilivyotarajia. Nimejuta kwa nini nilikulazimisha twende wote. Najua utakuwa
umenichukia kwa hilo.” “Hapana Geb. Naomba usijilaumu kabisa. Najua nia yako
ilikuwa nzuri. Lakini nafikiri na mimi nilikata tamaa mapema. Natamani
ningekusikiliza siku ile usiku uliponiambia nivumilie. Labda siku zilizobaki
zingekuwa nzuri. Lakini Geb, sikutaka kukuweka kwenye wakati mgumu. Nilikuona
ulivyokuwa ukifanya kazi kwa bidii hapa ili ukapate muda wa mapumziko kule
Marangu na baadaye Arusha. Sikutaka mimi, na tatizo langu la sweta, ndio nikawa
sababu yakutokufanya usipumzike na mpenzi wako. Nilipokwambia nimeogopa. Ni
kweli niliogopa Geb. Nikaona ni heri niondoke, niwape nafasi.” “Haikusaidia Nanaa.
Ndio iliharibu akili zangu kabisa.” Nanaa akamuhurumia.
Akajikuta amemvuta mkono wake. Akaushika
kwenye viganja. “Pole Geb. Na naomba unisamehe nilishindwa kukusikiliza.
Hakika nilifanya kwa ajili yako. Nilitaka..” Akasita. “Ningejua kama
haitasaidia, hakika nisingeondoka. Kama ningejua kama kubaki kwangu ni bora
kuliko kuondoka, hata kama ningeendelea kunyanyasika kihisia, hakika ningebaki
Geb, ili wewe upumzike. Samahani sana. Wakati mwingine
nitakusikiliza.” Geb alifurahi sana kusikia hivyo. “Asante
Nanaa.” Wakatulia.
Nanaa akagundua bado ameshika mkono wa Geb.
Mpenzi wa Liz. Akauachia kwa haraka. Aliuvuta na kuukumbatia bila
kufikiria. “Samahani.” Geb akamwangalia na kutoa tabasamu. “Sasa
utakula nini?” Nanaa akauliza. “Si ndio mmefika sasa
hivi?” Asijue wenzie walianza safari alfajiri, wakimuwahi yeye hapo Dar.
Watu wengine walikuwa hata hawajaamka wakati Geb anaegesha gari nje ya nyumba
yake asubuhi hiyo na kumuomba mama yake ampigie Nanaa simu.
Geb alibaki kimya. Hakujua hata amwambie nini!
Kwamba alikuwa anashindwa hata kupumua, mpaka alipomkumbatia pale. Au amwambie
ameendesha gari huku mawazo yakiwa kwake! Amwambie nini wakati bado Liz
anatambulika kama mpenzi wake? Akaona anyamaze tu. “Najua
hakutakuwa na chakula. Naomba nikuletee hata maji na matunda uanze kula.
Wakati nakupik..” Nanaa akakumbuka anatakiwa kuondoka. Tena na daladala
ambazo anahatari ya kuzikosa mida hiyo. Ilikuwa jumapili, siku ambayo usafiri
unakua sio mwingi kama siku za kazi. “Ingekuwa mapema kidogo,
ningekutayarishia chakula haraka haraka, wakati unakula matunda. Lakini inabidi
niwahi kuondoka ili nisikose daladala na nisimcheleweshe Antii
kulala.” Geb alikuwa ametulia tu wakati akijikanyaga kanyaga na mipango
mingii.
~~~~~~~~~~~~~
“Naomba nipe muda mfupi tu nikwambie kitu
kimoja. Labda itakusaidia na wewe ikakubadilisha mawazo.” Nanaa akajiweka
sawa kumsikiliza. “Naweza kuzungumza? Sitachukua muda mrefu sana.” “Hamna
shida. Nakusikiliza Geb.” Alishasahau haraka yakuondoka aliyokuwa nayo.
“Okay. Nataka ujue kuwa, hivi unavyoniona nilivyo, uzima wangu, shule niliyo
nayo na maendeleo yeyote niliyo nayo, ni kwa kuwa kuna garama kubwa sana
imelipwa.” Geb akaanza hivyo.
“Simaanishi garama ya fedha tu. Namaanisha, ipo
garama kubwa sana mtu amelipa kunifikisha hivi unavyoniona. Amenilipia garama
kubwa sana ambayo hailipiki kwa fedha. Kuna kipindi nilipoteza tumaini
maishani, nilikuwa nakaribia kujiua. Sikujua kama mpaka leo nitakuwa hai na
kuwa hivi nilivyo leo. Lakini unamuona vile alivyo mama? Kama hataki kuhusika
na maamuzi yangu! Hata yale mabovu na yakijinga ninayofanya sasa hivi. Lakini
mama anauwezo wa kuniambia nifanye chochote kwenye maisha yangu, na ikanilazimu
kutii, sio kwa kuwa ni mama yangu tu, lakini ni kwa umbali aliofika na mimi
kwenye maisha yangu mpaka leo.” Geb akaendelea.
“Alifanya mambo ambayo kila nikikumbuka, inabaki
kuwa fundisho. Alikuwa halali mchana na usiku akiniombea na kuhakikisha
ananihangaikia kupata ada nyingine, tena pesa nyingi sana, ili anirudishe
shule. Kwa kuwa shule ya kwanza nilifeli kwa ujinga wangu. Tena akiwa alinionya,
mara kwa mara. Kwa kurudia rudia akiniambia niwe mwangalifu. Lakini
sikumsikiliza, mpaka nikagonga mwamba. Ndipo yakabaki majuto. Nilikata tamaa,
lakini sio yeye. Nilikuwa nalala masaa 24, sitaki kutoka kitandani. Mama
alikuwa ananiacha hapo kitandani, anaenda kunitafutia pesa, akirudi jioni, ndio
anipikie, anifulie, na kubaki akiongea na mimi.” Geb aliguna huku akivuta
hisia.
“Usiku kucha mama alikuwa na mimi. Halali mpaka
ahakikishe mimi nimelala. Alikuwa akiniombea bila kuchoka. Wakati mwingine nilikuwa
naamka usiku, namkuta amepiga magoti kitandani kwetu, anaomba. Unakumbuka vile
ulivyokuwa umeshika huu mkono wangu wa kulia?” Nanaa akatabasamu kwa aibu
na kuinama.
“Basi ndivyo mama alivyokuwa akiushika huo mkono
akiomba hata nikiwa usingizini. Alihangaika hivyo mpaka nikaamua na mimi
nimuunge mkono kujaribu tena. Aliniambia nisikate tamaa, nina maisha marefu, na
mazuri sana mbeleni, ambayo Mungu amenikusudia. Kwa wakati ule, hayo maneno
hayakuwahi kuleta maana hata kidogo.” Geb akaendelea.
“Kwa ufupi nilipata tena shule nyingine ambayo
mama aliuza kila kitu chake, kuhakikisha namaliza ile shule. Tena niliamua
kusoma shahada mbili kwa wakati mmoja, na zote hizo, mama ndio alikuwa akilipia.
Shahada moja nilisoma madarasa ya Online kwenye chuo kimoja nchini Marekani, na
ilitaka pesa nyingi, na shahada nyingine nilisoma palepale nchini India.
Nilikuwa nikiingia darasani kama wanafunzi wengine. Kwa hiyo na hapo pia
nilikuwa nikilipa pesa kamalifu. Tena kubwa kama International Student.
Yaani mwanafunzi ambaye anatoka nje ya pale kwa hiyo ada yetu ilikuwa kubwa
kuliko wazawa. Na pesa zote hizo za ada alikuwa akilipa mama. Nikikwambia
aliuliza kila kitu, ni aliuza kila kitu mpaka vitenge vyake. Kutoka kwenye
maisha mazuri aliyokuwa ametuacha nayo baba, mama akarudi kuwa fukara. Watu
wakimcheka. Tulikuwa tukiishi kwenye nyumba yetu, lakini mpaka mimi namaliza
chuo miaka minne, tukajikuta kwenye chumba kimoja cha kupanga. Tunaishi wote,
na dada yangu Grace.” Nanaa alikuwa akimsikiliza Geb. Macho yake
yalimfanya Nanaa kuendelea kutulia. Na alikuwa akiongea kwa utulivu wa aina
yake.
“Somo jingine alinifundisha Grace. Aliolewa na
Danny, kwa mapenzi tu. Danny ni rafiki yangu mimi. Lakini alimpenda Grace
karibia kuchanganyikiwa. Hakuwa na pesa, ila penzi tu. Grace akiwa anafuatwa na
wanaume wenye pesa, tupo kwenye shida, pengine angeolewa na mwanaume mwenye
pesa labda angetutoa pale kwa wakati ule. Lakini akabakia na Danny tukihangaika
kwa muda mrefu tu. Maana na mimi nilipomaliza chuo, sio kwamba nilipata kazi
moja kwa moja, hapana. Nilirudi, nikakaa nyumbani kwa muda. Nikihangaika mimi
na mama. Tena nikiwa nimeshamfilisi vyakutosha. Nilirudi nikawakuta hawana
kitu. Mimi nina vyeti vizuri, lakini havina kazi. Yaani nimemrudishia mama
makaratasi. Kumwambia juhudi yake yote, pesa yake yote aliyokuwa akinitumia, ni
yale makaratasi yasiyo na kazi kwa wakati ule.” Geb akatulia kidogo.
“Hapo napo nikajaribiwa sana Nanaa. Lakini sio
mama yangu. Alikuwa akinipa moyo na kuniambia Mungu anaangalia kile nilicho
nacho mkononi, ili akitumie. Hapo sielewi Nanaa. Nina makaratasi. Kazi
sipati, mama ananiambia nisubiri. Mama akaanza kuombea tena vile vyeti.
Kama mwehu vile! Nakumbuka kumsikia kwenye maombi akimwambia Mungu, kama
alivyomuuliza Musa, yule wa kwenye bibilia. Samahani lakini mimi sio mzuri sana
wa mambo ya bibilia.” Nanaa akacheka.
“Lakini alikuwa akimwambia Mungu kama vile
alivyomuuliza Musa ana nini mkononi, Musa akamjibu kuwa alikuwa na fimbo tu.
Tena fimbo chafu ya kuchungia kondoo. Lakini akawa jasiri na kuitaja mbele za
Mungu, na bado Mungu aliitumia ile fimbo kutenda maajabu yanayosimuliwa mpaka
leo. Kwa mataifa na mataifa, akawa anamsihi Mungu kuwa, aangalie kile
nilichokuwa nacho mimi mkononi.”
“Akawa anamkumbusha kuwa nina vyeti mkononi.
Akamwambia Mungu anaomba hivyo vyeti avitumie. Usifikiri lilikuwa ni jambo la
siku moja! Mama alikuwa anaomba hayo maombi mchana na usiku mpaka nikajua na
kuyakariri hayo maneno. Haikuwa kazi ya muda mfupi. Na usifikiri nilikuwa
nikiomba naye. Mimi nilishakata tamaa. Nikaona ni mchezo wa kuigiza. Lakini sio
yeye. Aliendelea hivyo mpaka nilipopata kazi BOT. Hakuna aliyeamini kati yetu.
Lakini vile vyeti vikaleta kazi yenye kipato kilichofungua milango mingi
sana.” Geb akatulia kidogo.
“Haya. Turudi kwa dada yangu. Grace naye
kama nilivyokwambia. Kipindi hicho cha shida, akajikuta anaolewa na Danny,
mwanaume asiye na kitu.” Geb akacheka kidogo. “Yaani badala
yakupunguza tatizo, ndio tukaongeza tatizo jingine. Maana Danny naye
akaongezeka kwenye familia. Hana pesa na ni mwanafunzi. Tena akiwa hana vipindi
chuoni ndio anakuja kula hapo nyumbani, na kulala hapo hapo kwenye hicho chumba
kimoja na sebule, ndio alale na mkewe hapo. Lakini hawa watu wanapendana sana
Nanaa. Na wametoka mbali sana.” Geb akaendelea.
“Haya, Grace akapata kazi. Haikuwa ikimlipa sana,
lakini ilimsaidia Grace akumtunza mumewe na sisi. Siku alizojua Danny
anamitihani chuoni, alikuwa anampikia vyakula vingi, anamfungashia ili akifika
chuo, ale kwa hizo siku ambazo hatakuwepo nyumbani. Maisha yakaendelea kwa
muda. Mama naye akawa anahangaika kivyake. Akipata pesa, alete nyumbani kidogo,
nyingine alipe madeni ya pesa alizokopa kipindi nasoma. Na mimi nahangaika
maofisini kutafuta kazi. Asubuhi mpaka jioni. Wakati mwingine ilikuwa
ikinilazimu kutembea ili kubania pesa. Natembea umbali mrefu tu, siwezi hata
kumudu pesa ya kupanda daladala. Ukipata kazi, mshahara hautoshi. Ni vile
vikazi wanakwambia unaongeza ujuzi. Pesa wanayokulipa ni nauli tu.” Nanaa
akamwangalia Geb, akawa haamini. Geb aliyekaa hapo pembeni yake, amejaa neema
na amezungukwa na neema tupu. Hafananii na anayoelezea.
“Maisha yakaendelea hivyo mpaka mimi nikapata
kazi. Haya, bahati nzuri kwa Grace akashika mimba ya Fili. Akaugua sana sababu
ya ule ujauzito. Wakamfukuza kazi. Lakini Mungu alitusaidia wakati huo na mimi
nikawa nimeshapata kazi. Ndio na mimi nikampokea Grace na mama ambaye wakati
huo alikuwa na vibiashara vyake vilivyokuwa vikitusaidia kulipia hicho chumba
na sebule.” Geb alivuta pumzi.
“Kwa nini nimekwambia yote haya? Ni kwa kuwa nataka
uone jinsi maisha yalivyo mchezo wa ajabu. Ukikosea kidogo tu, ndio basi. Kama
mimi nisingekubali kupokea msaada wa mama, nikakataa kurudi shule, wote hawa
wasingekuwepo hapa. Na kama Danny asingekubali kudhalilika kwa muda, kwa
kuendelea kutunzwa na Grace, ili kuhakikisha anamaliza ile shule yake na
kuendelea kusoma, hivi leo Danny angekuwa labda aliamua kuacha shule wakati
ule, angetafuta kazi ya kawaida sana ili kumlea Grace. Kuna kipindi
alishawishika kukatisha masomo ili atafute kazi, amchukue Grace na mtoto wake,
lakini mama alimkatalia katakata, akamwambia lazima asome mpaka amalize shule
yake. Asingekubali yote hayo, sasa hivi Danny asingekuwa na shahada mbili na
wala asingekuwa akiingiza pesa anayoingiza sasa hivi. Tena Mungu amemuheshimu
Danny, analipwa kwa dolla akiwa nchini Tanzania. Danny analipwa mshahara mzuri
sana.” Nanaa hakuwa hata akijua kuwa Danny na porojo zote zile kumbe na
yeye mambo yake safi!
“Mama na Grace walikubali kutulipia sisi watoto
wakiume garama kubwa sana, kutufikisha hapa tulipo. Wapo hapa nyumbani kwangu
sasa hivi sio kwa sababu hawana uwezo wakupanga. Wanajenga. Aina ya nyumba
Grace anayotaka au niseme nyumba ya ndoto zake, inawagarimu sana ndio maana
wanachukua muda mrefu kumaliza. Hatukuona sababu wakalipie nyumba nyingine
yakupanga, wakati hapa pako. Tunakwepa nini sisi watu tulioishi hivi kwenye
chumba kimoja! Tena hivi hivi kama unavyotuona, ila Fili ndio alikuja
kuongezeka baadaye. Lakini tulikuwa hivihivi. Mtu anayekuja sasa hivi kwenye
maisha yetu itamuwia ngumu sana kutubadilisha, kwa kuwa tunayajua maisha kwa
vitendo, kwa kuyaishi sio kusimuliwa.” Geb akatulia kidogo.
“Mungu anapokutumia msaada, usikatae Nanaa. Hujui
ni kwa nini upo hapa. Lakini kikubwa ni kwamba, sasa hivi unahitaji msaada,
sisi tupo kukusaidia. Tumia hii nafasi kwa kadiri ya uwezo wako. Usikubali
kashfa, kejeli na dharau zizuie kufikia ndoto zako. Unajua kwa nini James
anakupenda sana?” Nanaa akatingisha kichwa kukataa, huku machozi yakimtoka.
“Alikuwa akitusimulia maisha yako yote, na vile
ambavyo uliendelea kujitahidi kufika hapo ulipo. Anasema wewe ni role modal
wake. Kila akisikia kukata tamaa, anayaangalia maisha yako na changamoto
unazopitia na bado unaamka asubuhi na kuendelea, wakati dada zake wanakila kitu
lakini wameshindwa kuendelea na maisha. Usikubali watu unaokutana nao njiani
wakukwamishe Nanaa. Hujui jinsi maisha yako yalivyo fundisho kwa wengine.
Umebakiza kidogo tu umalize shule. Jikaze mpaka uone mwisho wake. Leo unakutana
na changamoto hii hapa kwetu, hujui huko unapokimbilia usiku huu utakutana na
changamoto gani. Utakimbia mpaka lini Nanaa?” “Nilikuwa
nakuhofia wewe, Geb.” Nanaa aliongea kwa upole huku akimtizama Geb.
“Sikutaka
kukuharibia.” “Kwa hiyo unaondoka kwa ajili yangu?” “Niliona vile ulivyonipokea kwa upendo. Wote mnaishi na
mimi vizuri. Najua maisha ni magumu. Lakini wewe unanitunza hapa bure kama mtu
ninayekuhusu! Wakati hunifahamu kabisa. Sina jinsi ya kukulipa isipokuwa
kukupunguzia matatizo.” “Kwa kunikimbia kila mahali?” “Sikujua nifanye nini? Nataka kukusaidia na wewe.” “Sasa
unajuaje kama maamuzi yako huwa yananisaidia?” “Sijui
Geb!” “Ndio ungeniuliza mimi mwenyewe ili ujue nini
nataka.” Nanaa alinyamaza kwa muda. Akajikausha machozi. Akatulia tena.
Akanyanyua uso na kumwangalia akiwa
ametulia. “Kwa hiyo unataka nini?” Nanaa akauliza. Geb akatoa
tabasamu. “Nataka usinikimbie. Usihame hapa na kwenda kuishi nyumba
nyingine, labda chuoni.” “Nitakuwa nakuja kuwatembelea Geb. Itarahisisha maisha
yetu wote. Hapa patakuwa na amani, na mimi nitakuwa na amani.” “Hapana Nanaa.
Naomba usihame. Sio sawa. Umeshafikiri utakuwa na maisha gani hayo? Unahama
nyumba moja hadi nyingine! Mpaka lini? Kwa James inaeleweka. Na hapa je?” “Hapa
sitakiwi Geb. Nitaishi hivi mpaka lini?” “Sisi wote tunaoishi na wewe tunakutaka
ubaki na sisi. Kila mtu alikataa kwenda mapumzikoni Arusha sababu wewe
hukuwepo. Tunakuhesabu kama mmoja wetu.” “Naomba unisamehe Geb. Ni kweli
niliondoka ili kukuletea amani na mpenzi wako. Sikukusudia kuharibu.”
“Nimeelewa Nanaa. Lakini kama mama alivyokwambia, tuwe tunazungumza.” Geb
akaweka msisitizo.
“Nataka yale unayomwambia James, na mimi uwe
unanishirikisha kwa kuwa sasa hivi tunaishi wote. Haupo na James. Unaishi na
mimi. Najisikia vibaya, au najihisi kushindwa pale unapokuwa unaishi hapa,
halafu matatizo yako unayatuma kwa James! Yaani mimi nasikia matatizo yako
kutoka kwa James, wakati mimi ndio naishi hapa na wewe! Sioni kama ni sawa
Nanaa.” Nanaa akanyamaza.
“Tunaishi wote hapa, naomba na mimi unihusishe
kwenye maisha yako. Naweza nisiwe msaada kama James, lakini naamini tukiwa
pamoja hatutashindwa kitu.” Nanaa alianza kulia tena huku ameinamisha
kichwa chake kwenye magoti yake. Geb aliweka mkono wake mgongoni kwake akaanza
kumbembeleza tena taratibu. Alipitisha mkono taratibu mgongoni kwa Nanaa mpaka
akatulia. Akatoa uso magoti, akamwangalia. Akakuta Geb akimtizama kwa
karibu. “Asante.” Nana akashukuru
kwa upole. “Karibu.” Geb akajibu na uso mtulivu huku akimtizama.
Nanaa akacheka kidogo. “Nini?” Geb
akauliza natabasamu usoni. “Sikuwahi kupata bahati kama hii.” “Bahati
gani?” “Mtu kuomba kujua matatizo yangu!” Geb akacheka. “Na yalivyo
mengi! Nahisi utajuta kama wenzako.” Geb aliweka kidole chake kwenye dimpo
ya Nanaa. “Nilijaliwa tunda la uvumilivu. Kwa hiyo wewe yalete tu hayo
matatizo.” “Haya, tutaona na wewe utaishia wapi.” “Usiseme hivyo sasa. Niombee
niweze. Usiwe kama mtazamaji wa mpira. Hutaacha kuona kasoro. Nimekwambia
tutatue pamoja.” Alimsugua mgongoni kwa nguvu kidogo, Nanaa
akacheka. “Sawa. Na ninakushukuru sana.” “Kwa hiyo si tumekubaliana
unabaki?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali.
“Asante Nanaa. Basi twende tukafuate mizigo
yako.” “Nina wazo la tofauti.” “Wazo gani?” “Leo niende nikalale na Antii.
Nipate muda wa kuzungumza naye. Halafu kesho nikitoka kazini nitarudi hapa moja
kwa moja.” “Naomba urudi nyumbani Nanaa. Tafadhali naomba iwe leo. Mimi
nitakupeleka. Nitasubiri hata kwenye gari. Zungumza naye mpaka uridhike, halafu
turudi wote nyumbani.” Nanaa aliinama akifikiria.
“Tafadhali Nanaa.” Kwa sauti ile ya Geb.
Mikono mizuri ambayo ikikushika lazima ufarijike. Macho yake ndio ungetamani
hata akushike na kukumbatia. Ilikuwa kama barafu moyoni. Hakuna jinsi Nanaa
angemkatalia Geb. Labda ndio maana alijikuta akikubali kila kitu hata kama
amekusudia kukataa. “Nanaa, please!” Geb aliendelea kubembeleza.
Nanaa akajikuta anatingisha kichwa kukubali huku akimwangalia. Kama angekuwa
mwanaume mwingine, ule ndio ulikuwa wakati wa busu. Lakini Geb hakuwa mtu wa
papara. Kila kitu alikuwa akikipigia mahesabu.
“Basi twende sasa hivi.” Akamshika mkono,
Nanaa akatoka pale kitandani. Akamtengeneza nywele vizuri kama kumuweka sawa,
akamfuta machozi vizuri kama anavyomfanyia Fili. Nanaa
akacheka. “Asante.” Akashukuru. “Karibu.” Geb akajibu.
Akamtizama kidogo. “Gauni imekukaa vizuri.” Nanaa akajiangalia.
Akajicheka na gauni yake ya mtumba. “Asante. Lakini gauni yenyewe ya zamani!”
“Bado inaonekana nzuri mwilini mwako.” Geb alisisitiza sifa
zake. “Asante.” Akajibu kwa aibu huku akicheka. Wakatoka pale
chumbani. ‘Kumbe huwa ananiangalia!’ Nanaa akawaza.
~~~~~~~~~~~~~
“Mama yuko wapi? Lazima
nimuage?” Nanaa akamuuliza Geb, lakini Grace aliyekuwa sebuleni akasikia
akawafuata pale koridoni. “Unaondoka Nanaa? Naomba usiondoke bwana! Tubaki
wote. Usitukimbie, tuvumilie tu. Sisi tunakupenda na tunataka
ubaki.” Grace akaongea kwa upole. Wakamsikia Mama G na yeye anatoka
chumbani. “Usiondoke Nanaa.” Mama G naye akaongeza. “Naenda kuchukua
tu vitu vyangu, halafu narudi. Nitakaa hapa mpaka tutakapo pata chumba changu.
Kaka amesema akirudi kutoka safari ataongeza juhudi ya kunitafutia chumba
changu, na yule dalali niliyekuwa naye amenipa moyo. Amesema nitafanikiwa tu.
Nisubiri. Kwa hiyo nitakuwa hapa nikisubiria. Sitahamia tena kwa Antii.”
“Afadhali. Ulitaka kunitia presha.” Nanaa akacheka.
“Asanteni jamani. Asanteni kunisamehe na
kunipokea tena. Nashukuru.” Wote walijua Nanaa hajui moto aliowasha kaka
yake huko Marangu. Kama angejua yeye ndio anastahili kuombwa msamaha,
asingerudia rudia kuomba msamaha. Lakini Mama G alifanya makusudi, kumuwekea
hukumu ili kumfanya arudi kuishi pale ndani.
“Mimi naenda kulala. Nimechoka.” “Geb hajala
mama. Njaa inamuuma.” Nanaa akajikuta anaropoka. Kama ndiye anayewajibika
na Geb. Grace na mama yake wakaangaliana. “Namaanisha hakuna uji wake ili
niweke kwenye kikombe, twende huku anakunywa huko njiani?” Nanaa akajishitukia,
akaongeza kwa aibu kidogo. “Au nipike mara moja kabla hatujatoka? Najua
mmetoka safari, mmechoka.” “Ujue tumefika hapa tokea asubuhi? Hata chakula cha
mchana tumekula hapa.” Nanaa akashangaa na kumgeukia Geb aliyekuwa kimya
nyuma yake.
“Sikujua! Maana nimeona Geb
amecho...” Akasita kama anayefikiria kitu akaelewa kwa haraka, akamgeukia
tena Geb. “Pole.” Akaongea kwa sauti ya chini na kumuhurumia.
Akakumbuka alivyomwambia tokea alivyoondoka, kichwa chake kilivurugika.
“Nilikutafuta sana. Karibia siku nzima nilikuwa nakupigia wewe simu.” “Pole
mama yangu. Simu iliishiwa chaji. Nikaicha nyumbani hata sikwenda nayo
kanisani. Nilijua sina wakunipigia. Nikaipuuza simu na kuiacha nyumbani kwa
Antii. Tulipotoka kanisani, tukaenda kuona wagonjwa
hospitalini.” Nanaa alijieleza huku akimfikiria Geb kwa kina na
kumuhurumia.
“Basi sisi tupo hapa tokea asubuhi. Na uji upo
kwenye chupa yake huyo. Nilipika tu tulivyorudi. Lakini hakuwa tayari kunywa.” “Asante
mama yangu. Ngoja basi nikamuwekee kwenye kile kikombe kirefu kinachokaa kwenye
gari yake. Anywe njiani wakati ananisindikiza kufuata mizigo yangu kwa
Antii.” Nanaa akaongea huku anaelekea jikoni.
Akawaacha wanaangaliana, yeye hana habari. Grace
akatoa tabasamu kwa mama yake. “Nitamsindikiza Nanaa.” Geb alipita
kati kati yao huku na tabasamu usoni. “Muone anavyocheka! Kama sio yeye!
Unashida ya roho wewe!” Mama G akarudi chumbani kwake. Grace akarudi kwa
mumewe sebuleni.
Nanaa akamimina uji kwenye hicho kikombe kirefu
cha Geb, akatoka jikoni akiwa ameshika chupa ya uji mkono wa kushoto na kikombe
cha uji mkono wa kulia. Akamkuta Geb akimsubiria pale sebuleni. “Nikupokee?” Geb
akamuuliza. “Lakini uwe makini. Ni wa moto sana. Au tukae ule kwanza? Nitakuwekea
kwenye bakuli kubwa, upoe kwa haraka.” Danny na Grace walikuwa
wakiwasikiliza, lakini wote wamegeukia tv. “Twende tu. Utapoa njiani.
Asante.” Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
“Na wewe umekula?” Geb akauliza wakati
wapo njiani. “Sijala tokea asubuhi. Lakini sisikii njaa.” “Ulikuwa
ukifanya nini leo?” “Antii huwa anakuwa anakwenda kutembelea wagonjwa
mahospitalini mara kwa mara. Lakini kila mwisho wa mwezi akipata pesa anakwenda
kuwapelekea mahitaji yao muhimu huko hospitalini. Sasa leo baada ya kutoka
kanisani, nikamsindikiza. Nimependa. Ni kitu kizuri. Nimemwambia nitakuwa
nakwenda naye kila mwisho wa mwezi, asiniache. Nitakuwa na mimi nanunua vitu,
naongozana nae.” Geb akamwangalia nakucheka kidogo.
“Unafikiri Geb? Imenibadilisha sana mtazamo wa
maisha yangu. Ile ni therapy tosha ya maisha. Huhitaji therapist.
Ukidhani wewe unashida, basi nenda mahospitalini. Utajisikia kujisuta. Mimi
nimetoka pale, nikamuomba Mungu msamaha.” “Safi sana. Itabidi tuwe tunaenda
wote.” “Kweli Geb?” “Kweli. Sasa ni nani ambaye hataki kujiona hana
matatizo?” Nanaa akacheka kidogo kisha akafikiria.
“Wewe huna matatizo Geb.” Geb
akamwangalia. “Najaribu kuangalia maisha yako, naona mkono wa Mungu katika
kila eneo la maisha yako.” “Basi utakuwa hujanifahamu vizuri.” “Niambie
unashida gani Geb? Kama ni mali, Mungu amekubariki. Hilo halina swali. Upande
wa mpenzi, pia Mungu amekupa mwanamke mzuri, msomi na anajielewa. Tena
mnapendana sana. Hapo napo hakuna mjadala.” Geb akamtizama Nanaa.
“Haya. Tukirudi kwenye familia, kitu
kinachotamaniwa na wengi. Hapo napo Mungu amekubariki. Unafamilia ya watu
wanaokupenda na mnaelewana sana. Binafsi sijawahi ona familia kama yenu.”
“Ikoje?” Geb akauliza. “Familia iliyofanikiwa katika kila eneo na bado
mkabaki kuwa wanyenyekevu kama vile! Mnaheshimiana na mpo kitu kimoja. Mtu
akija pale kwenu, anaweza kufikiri nyinyi wote watatu ni watoto wa mama mmoja!
Mpaka Danny. Halafu mnapenda watu.” Geb akacheka. “Kazi ya mama
G hiyo.” Akamsifia mama yake. “Hata nyinyi wenyewe mnaonekana
mnamsikiliza. Sio kama watoto wengine. Haya, turudi kwa baraka Mungu
alizokupendelea na kunifanya nikwambie huna shida.” Geb akacheka tena.
“Nini tena?” “Unamarafiki wazuri wanao kuheshimu
Geb. Wote wanakuheshimu sana japo mwenyewe ukiwa katikati yao huzungumzi sana.
Lakini ukiwasikia wakikusema, wanakusema vizuri. Hata wafanyakazi wako, au
wenu, wote wanakusema vizuri. Wanakusifia sana wewe na Grace. Haya niambie Geb,
shida yako wewe ni nini?” Geb akamtizama na kurudisha macho
barabarani. “Niambie tu Geb. Wewe unashida gani?” “Siwezi kukwambia
mpaka unipe maelezo ya kwa nini hukujibu ujumbe wangu.” Nanaa akacheka
sana.
“Geb wewe! Husahau tu?” “Ndio maana ulikuwa
ukinikwepa ili nisahau nini?” Nanaa alicheka tena. “Mwenzio nina sifa
yakutosahau mambo. Sasa sijui kama ni sifa nzuri au mbaya. Kwa hiyo kabla ya
kujua matatizo yangu mengine, ujue una deni kwangu. Lakini sio leo. Tutatafuta
siku nzuri, ambayo sijachoka na kichwa changu kimetulia. Tutapata muda mzuri wa
kuzungumza.” “Pole. Ni kweli unahitaji kupumzika. Umekuwa ukiendesha wakati
wote.” Nanaa aliongea asijue yanayomchosha kijana huyo. Geb akamtizama
tena kidogo, akarudisha macho barabarani na kunywa uji wake kidogo.
~~~~~~~~~~~~~
Alikuwa na njaa yakupitiliza. Kwa asili alikuwa
mvivu wa kula. Lakini kila alipokuwa na jambo zito moyoni, chakula kilikuwa
kikigoma kabisa kupita mdomoni kwake. Hasa jambo linalomuhusu Nanaa. Hakujua
jinsi yakufanya linapokuja swala la Nanaa, ambaye alimjali kuliko hata Liz
mpenzi wake. Na Nanaa alifanya bila hila. Akajikuta furaha yake nikumuona Geb
anafuraha tu, bila kutaka sifa au kujipendekeza.
~~~~~~~~~~~~~
“Na ili usinitoroke tena au usiwe
unanikimbia, nitahakikisha tunakuwa karibu na tunaonana kila siku.” Nanaa
akacheka. “Wakati wewe huwa unawahi kuondoka asubuhi na wakati mwingine
unachelewa kurudi nyumbani?” “Kuanzia kesho, tunaondoka wote kwenda kazini.
Kama nachelewa kutoka kazini, nitazungumza na Grace aweke utaratibu mzuri
kazini. Ili akiwa anatoka, muwe mnatoka naye. Sio kurudi tena nyumbani usiku,
tena peke yako kwenye madaladala.” Nanaa akacheka kwa kuridhika.
“Halafu..” Geb alitaka kuendelea, lakini
Nanaa akamuwahi. “Nisilale mpaka urudi kutoka kazini?” Nanaa
akamalizia. Kama aliyekuwa anasoma mawazo yake. Geb akacheka. “Utachoka?” Geb
akauliza, Nanaa akatingisha kichwa kukataa. “Kwanza ndio itakuwa vizuri.
Unajua kwa nini?” Akamuuliza Geb wakati ananyanyua kikombe chake kupata
funda jingine la uji. “Sijui ni kwa nini itakuwa vizuri.” Geb akajibu
baada ya kumeza. “Itanipa nafasi yakujua kila siku, siku yako
ilikwendaje. Na kama umekula au la.” Geb akacheka. “Asante
Nanaa.” Pakazuka ukimya mpaka Geb alipomuuliza nyumba ya huyo Matroni.
“Si tutaingia wote?” “Kama ndio unavyotaka.
Lakini naweza kusubiria tu kwenye gari.” “Basi wewe pumzika kwenye gari wakati
unamalizia uji wako. Najua umechoka na una njaa. Sitachelewa.” “Usiwe na
wasiwasi na mimi. Hakikisha unaacha mazingira mazuri. Kuwe na amani.”
“Sawa.” Geb alifika mpaka kwenye jengo la hiyo hosteli ambayo nyuma yake ndipo
alipokuwa akiishi huyo matron, kwenye nyumba ndogo tu. Akaegesha gari yake.
Nanaa akashuka.
Na kweli baada ya muda mfupi akarudi na begi lake
alilokuwa nalo safarini. “Sikumkuta. Nimempigia simu na kumuaga.
Ameniambia yupo sehemu hawezi kuongea. Sasa sijui ni wapi! Antii anashuguli
kweli! Sijui amepatwa na dharula gani tena!? Maana aliniahidi atanisubiri. Ila
nimemwambia nitarudi kuongea naye siku ya jumamosi.” “Sawa.” Geb akaondoa
gari.
“Naona umechoka! Twende ukapumzike.”
“Hapana, kawaida tu. Tena afadhali sasa hivi nimekunywa huu uji, nimepata nguvu
kidogo. Twende tukatafute chakula.” “Kwani nyinyi hamkula?” “Unajua tulirudi na
mama. Ilibidi kusimama zaidi ya mara nne ili kunyoosha miguu.” “Kwa nini
hakurudi tena na ndege!?” Geb akanyamaza.
Nanaa akajua anakitu anaficha. “Geb?” “Hali
haikuwa nzuri Nanaa. Ikabidi mama awepo na sisi kwenye gari.” Ni kama
alielewa nusu ya lile jibu. Akajisikia vibaya sana. “Nimejisikia vibaya
sana Geb. Kweli sikukusudia kuharibu.” “Naomba usijilaumu Nanaa. Sidhani kama
unahusika moja kwa moja. Ni kama wote tulimiss uwepo wako pale. Wote tulitaka
uwepo pale. Hatukulaumu.” Nanaa akatulia kidogo.
“Kwa hiyo mlikula?” Akakumbuka swali
lake. “Tuliokota okota vitu njiani. Naona kila mtu ameshiba.” “Twende
tukanunue nyama choma. Si unajua jana ilikuwa mwisho wa mwezi? Nimelipwa
mshahara wangu. Sasa nisindikize nikanunue hiyo nyama choma na ndizi. Halafu si
unajua inavyonukia? Tunaweka pale sehemu ya kulia chakula, karibu na sebuleni.
Ili inukie nyumba nzima. Wataamka wenyewe waje kula.” Geb akacheka.
“Wewe unafikiri wenzio wanapenda kula kama wewe?”
“Ujue ni wewe peke yako hapa duniani usiyependa kula? Hakuna mtu asiyependa
chakula. Labda awe mgonjwa. Sasa twende nikakuthibitishie. Halafu utaona kama
haitafanya kazi.” “Sawa Nanaa.” Kweli wakafanya kama Nanaa alivyosema.
Lakini Geb alilipia yeye hakutaka Nanaa atoe pesa
yake. Wakafika nyumbani wakakuta kila mtu yupo chumbani kwake. Nanaa akakiweka
kile chakula mezani. “Wewe kaa hapo kwenye kochi, halafu nyamaza kimyaa.
Utaona mwenyewe. Usimwite mtu yeyote” Geb alicheka akatingisha kichwa,
akavuta kiti palepale pembeni ya Nanaa. Wakakaa nakutulia.
“Mbona hawaji sasa?” Geb
akauliza. “Wewe subiri.” Nanaa akanong’ona. Baada ya dakika 5 akatoka
Danny, akijidai anafuata maji ya kunywa. Nanaa akamkanyaga Geb kama
kumkonyeza. “Njaa inauma kweli!” Danny akajiongelesha. “Mbona
kunanukia hivi?” Grace naye akatoka. “Nanaa amerudi?” Mama G,
naye akatoka chumbani. Nanaa akaanguka kicheko. “Nyama choma huwa
haidanganyi.” Geb alikuwa akimwangalia Nanaa huku anacheka.
“Mlitutega?” Mama G, akauliza. “Hasa
wewe mama.” “Ujue wewe Nanaa akili yako haikutoshi? Na kwa taarifa yako wala
hujanipata.” “Mmmh mama! Kweli?” “Kweli tena. Mimi nimetoka kuja kukuangalia
kama umerudi.” “Haya mama yangu. Kaa tule. Nilijua mmelala bila kula. Tumenunua
chakutosha watu wote.” “Mbona tunashukuru.” Grace akaongeza huku
wakiendelea kucheka. Wakakaa.
Mara Geb na Nanaa walipotoka tu, mama G badala ya
kulala, akaingia jikoni na kumpikia mwanae mchemsho wa ndizi na kipande cha
samaki walichokuwa wameacha kwenye friji. “Mlipoondoka, nilitaka kulala.
Lakini nikakumbuka huyo Geb, hajatia kitu chochote cha maana tumboni, zaidi ya
siku mbili.” Mama G akaanza. “Nanaa! Kamletee chakula chake hapo
kwenye hotpot kwenye meza ya jikoni.” “Asante mama.” Geb
akashukuru.
Nanaa akaenda kufuata hicho chakula jikoni.
Lakini kama kawaida, akakipanga vizuri kama siku zote. Alikimimina hicho
chakula kwenye bakuli kubwa. Maalumu la Geb. Akamimina juisi kwenye glasi ya
Geb, akaweka hapo kwenye sinia. Kulikuwa na zabibu kwenye friji. Akaziosha kwa
haraka, akaweka kwenye kibakuli cha Geb cha matunda. Akampelekea pale alipokuwa
amekaa. Alisahau napkins na kijiko. Akarudi kwa haraka jikoni. Akaenda
kuchukua. Akamwekea hapo kwenye sinia. “Karibu.” Nanaa
akamkaribisha. “Asante.” Wote walikuwa wakisubiria hapo mezani. Mama
G akamwambia Nanaa aombee chakula na kumshukuru Mungu kuwarudisha nyumbani
salama. Nanaa akaomba kwa kifupi tu. Wote wakaanza kula kwa pamoja pale
mezani. Nanaa akitaniana na mama G.
~~~~~~~~~~~~~
-
Utulivu na amani vimerejea nyumbani kwa Geb. Wamefanikiwa kurejesha
uwepo wa Nanaa na cheko la Geb. Kila mtu alianza kuelewa kwa nini nafsi ya Geb
inavutiwa na Nanaa. Ni kama alikuwa akipata kwa hakika anachokita au mtu yeyote
anachostahili maishani, kutoka kwa Nanaa. Kujaliwa kwa dhati.
-
Yote aliyomtajia Geb, kuwa Mungu amembariki nayo, hayakuwa
yamekamilika kama yeye hayupo kwenye picha nzima. Kuna jinsi alifikia nafsi ya
Geb, hakuna mtu wala pesa iliweza kufika huko. Tena kwa kukana nafsi yake. Hata
kama akiwa ameumizwa na wivu ukimwendesha kwa kasi, lakini linapofika swala la
Geb, Nanaa aliweka kando hisia zote, nakutaka kumuona Geb yupo sawa. Yeye kama
Geb. Alimuonyesha kujali kwa namna yake.
-
Sasa Geb ameweka mkakati mpya wakumfanya Nanaa awe karibu naye zaidi
ili kuridhisha nafsi yake. Alimwambia, akiendelea kuishi pale, ataelewa zaidi.
· Je,
watafanikiwa kueleweshana kile kinachoendelea mioyoni mwao wakati tayari ni
kama Geb alitamka mbele ya marafiki zao na Liz kuwa
anamsaidia tu Nanaa?
· Itakuaje
wakati Liz bado yupo kwenye maisha ya Geb?
0 Comments:
Post a Comment