Geb
akatafuta mahali akakaa. “Tukae hapa.” Nanaa naye akaenda kukaa
pembeni yake, wakatulia kidogo. “Vipi shule lakini?” Geb
akauliza. “Tupo field, kwa sasa. Tukirudi ndio mwaka wa tatu na wa mwisho,
tunamaliza.” Nanaa akajibu. “Una mpango wa kuendelea kusoma?” Geb
akauliza tena. “Mimi sio mpenda shule.” Geb akacheka. “Kweli
tena. Hata hapa nilipofika ni kwa sababu ya kaka James. Sasa kuja kurudi tena
kusoma shahada ya pili! Hapana kwa kweli.” “Utataka kufanya nini
ukimaliza?” “Hata sijui! Nilikuwa na mipango mingii, lakini yote imevurugika.
Nahisi nitajua mbele ya safari.” Geb akamwangalia.
“Nini kimevurugika?” “Kila kitu. Naomba Mungu
asaidie tu, nikimaliza shule, nipate kazi, maisha yaanze.” “Una mpango wakuishi
wapi? Namaanisha utatafuta kazi maeneo gani?” Geb aliendelea kudadisi.
Nanaa akatulia kidogo kama anayefikiria. Akajibu kwa upole. “Popote pale
nitakwenda kufanya kazi au nitatafuta kazi, isipokuwa Moshi na Arusha.” Geb
aliweka uso wa kuuliza kidogo kisha akatupia swali jingine. “Kwa nini
hupataki Moshi na Arusha?” Nanaa akanyamaza, akabaki kimya.
“Eti Nanaa?” Geb akauliza tena. Alikuwa na
sauti nzuri iliyotulia na kumfanya mtu yeyote apende kumsikiliza. Labda ni
Nanaa tu! Lakini alijisikia vizuri kuwa karibu na Geb. “Hiyo mikoa
sitamani kuja kurudi tena. Imebeba historia mbaya tupu ya maisha yangu”
“Ikitokea unapata kazi huko, je? Tena kwa ahadi ya pesa nyingi.” “Mmmh!
Sitakwenda.” Nanaa akajibu kwa hisia za majonzi akiwa ameinama kama
amekumbushwa mbali. “Kweli umepachukia!” Kwa muonekano ule, Geb
mwenyewe akaamini kuwa Nanaa amekusudia kutokuwepo huko.
“Lakini si unajua ukishindwa hiki unapanga
tena mipango mingine? Usiache kujiwekea malengo, kwa kuvunjika kwa malengo
uliyokuwa umejiwekea zamani.” Geb akajaribu kushauri. “Wakati mwingine
unakata tamaa au unajishuku pengine unaweka malengo yasiyowezekanika maishani.
Unaamua kuacha tu. Usubiri litokee lakutokea, upambane nalo mbele ya safari.
Kuliko kuumia kila wakati.” “Pole. Lakini ipo siku nitataka uniambie hiyo
mipango iliyogoma kutimia.” Nanaa akacheka kidogo, akainama kama
anayefikiria.
“Wewe mipango yako yote inatimia?” Safari
hii Nanaa naye akauliza swali nakumfanya Geb acheke huku akifikiria
kidogo. “Daah! Swali zuri sana. Japokuwa sikuwahi kuulizwa kabla na na..” Geb
akababaika kidogo. “Lakini labda niwe muwazi.” Akaendelea. “Siwezi
kulalamika. Ni mambo madogo madogo tu ambayo naweza kurekebisha. Yapo ndani ya
uwezo wangu. Siwezi kulaumu. Namshukuru Mungu kwa hilo.” “Hongera.” Geb akacheka
na kumwangalia. “Natakiwa hongera eeh?” “Kabisa. Niwachache sana wanaoweza
kufikia ndoto zao.” Geb akatabasamu na kujibu. “Asante. Namshukuru
Mungu kwakweli.” Ukimya wa muda ukapita tena.
“Unafurahia kufanya kazi na Grace?” Geb
akauliza tena. “Ukweli hana shida. Ilimradi ufanye tu majukumu yako.
Kwanza anachoka kuongea na kusikiliza maneno mengi. Mpole kama wewe!” Nanaa
alijibu na kumfanya Geb acheke. “Umejuaje kama ni mimi mpole? Au kwa kuwa
sijalalamika kwa kutojibu ujumbe wangu?” Nanaa akacheka kwa aibu
nakujificha uso.
“Eti Nanaa?” “Samahani.” “Kabla yakuomba msamaha,
niambie kwa nini hukunijibu.” Nanaa akanyamaza kama anayefikiria. “Eti
Nanaa?” “Ni habari ndefu. Lakini unisamehe tu.” Walijikuta wakiangaliana.
Nanaa akataka kujaribu kukwepesha macho lakini akakuta bado Geb akimwangalia kwa
utulivu. “Ni mambo mengi, Geb.” Nanaa alijilalamisha kwa upole. “Yanayohusiana
na ule ujumbe niliokutumia au ni kitu kingine? Maana nilitaka kujua
unaendeleaje na kama ulifika nyumbani salama. Basi. Nikaona umesoma ujumbe
wangu, halafu kimya. Hukurudisha majibu Nanaa!” Nanaa akainama.
“Ukweli niliingiwa na wasiwasi. Ikabidi kukufuata
nyumbani kujua unaendeleaje. Tena wala hukunisalimia mimi! Au kuna kitu
nilikuudhi tulipokuwa wote pale ofisini?” Nanaa akajisikia vibaya sana
moyoni. Japokuwa siku ile usiku walipoenda kumtizama nyumbani baada yakuondoka
ofisini bila kuaga na kumuacha Geb haelewi, aliyezungumza ni Grace na Danny tu.
Geb alikuwa kimya. Kumbe yeye ndiye aliyekuwa na safari ya kwenda kumuona! Grace
na mumewe walikuwa wasindikizaji tu!
“Nilikuudhi nini?” Geb akauliza kwa
kubembeleza. “Hapana. Hakuna ulipokuwa umekosea. Ni mimi mwenyewe tu.
Naomba unisamehe.” Nanaa alimwangalia tena. Angemuudhi mtu yeyote, lakini
sio Geb. Kijana mgeni kwake, lakini akajikuta ameshateka moyo na fahamu zake.
“Siweze kusamehe kama sifahamu kosa, Nanaa. Kama
ni kitu cha kurekebisha, si niafadhali tujue turekebishe ili isitokee tena?” Nanaa
akanyamaza. “Eti mchumba wa Fili? Au Jeff ameshamzidi mahesabu?” Nanaa
alijikuta akicheka kwa sauti. “Kumbe na wewe ni mchokozi hivyo!” Geb
akacheka. “Mimi sio mchokozi. Najiandaa kwa harusi.” “Kwani na wewe
ulisikia mazungumzo yangu na Jeff?” Nanaa akauliza kwa aibu huku akicheka.
Geb alibaki akitabasamu tu. Nanaa akapata jibu lake moja kwa moja.
“Usiniambie kama na wewe ulisikia!?” “Mlikuja
kuongea nyuma yetu. Tena Danny alikuwa akionyesha kitu alichokuwa akifanya
Fili. Wakawa wamepingiana pesa na Zinda. Kuna mtoto mmoja hivi, bonge kidogo.”
“Ni Tyrii?” Nanaa akauliza. “Ehee! Umeshawajua!?” “Kumbuka nilicheza
nao muda wote.” Wakacheka.
“Sasa Tyrii alimsukuma kwa makusudi Fili. Wote
tukaona. Fili akakasirika sana. Zinda akasema nilazima Fili atampiga ngumi. Ila
Danny akasema mwanae sio mgomvi kabisa. Zinda akambishia. Ndio Danny akasema
tunyamaze kimya tuone kama mwanae atamrudishia au la. Wakapingiana dau.
Tukakubaliana tunyamaze kimya tuangalie tuone. Kwa hiyo wote tulikuwa kimya
tukifuatilia hilo tukio zima. Na wakamwambia mama yake asiende kuwaingilia.
Sasa wakati tunawaangalia watoto, na nyinyi mkaja nyuma ya ule uzio mkaanza
kuongea. Basi tukawa tunaangalia watoto, huku tunawasikiliza.” Nanaa
akaziba uso huku akicheka kwa aibu.
“Mungu wangu! Kwa hiyo mkasikia kila kitu?” Nanaa
akauliza tena huku ameficha uso. “Naona jamaa amekazana na Fili naye yupo
na mipango iliyokamilika. Mahari mpaka sehemu ya kukuweka. Sasa sijui nani
ataibuka na mke!?” Nanaa akacheka tena. “Naona safari hii
nimebahatika. Nimempata mchumba Fili anayenipenda, na kujivunia mbele za watu.” Geb
akamtizama, na kuuliza, “Kwani safari zingine hukubahatika?” Nanaa akapooza
usoni, akatingisha kichwa kukataa. Cheko likaisha. Huzuni ikamjaa kadiri
alipokumbuka wanaume aliokwisha kuwa nao kwenye mahusiano ndivyo furaha
iliendelea kupotea mpaka usoni akaonyesha.
Taratibu Geb aliona machozi yanachirizika pembeni
ya mashavu ya Nanaa. Akayafuta kwa haraka na kurudisha tabasamu lake la
kumtuliza tu. Lakini wazi alionekana kuna huzuni nyuma ya hilo tabasamu. “Pole
Nanaa. Basi safari hii, tutahakikisha Fili anakufikisha kanisani.” Nanaa
akacheka tena. “Geb wewe ni mchokozi bwana, kama Danny!” “Mimi nakwambia
ukweli, sikuchokozi.” “Haya bwana!” Geb alimtizama kidogo, nakuangalia
pembeni huku akitabasamu.
“Unacheka nini sasa?” Nanaa akamuuliza pale
alipomuona anatabasamu. “Ukicheka unapendeza. Una dimpozi nzuri sana,
Nanaa.” Geb alimgeukia na kumtizama wakati anamsifia. Nanaa alibabaika
kidogo, akajishika machavuni. “Zipo hapa bwana! Unajishika wapi huko?” Geb
aliweka kidole chake kwenye kishimo kilichopo kwenye shavu la kulia la Nanaa,
Nanaa akacheka. “Ewaa! Hapo ndio zimetokea vizuri.” Geb akasifia
tena. Kule kushikwa tu na Geb, Nanaa alijisikia vizuri sana.
Machungu Ya Kuzaliwa Kwa Kifupi
Ya Nanaa Kwa Geb.
“Sijui hata nafanana na nani?” Nanaa
alijiongelesha. “Najua mama yako alifariki, lakini hukuwahi hata kuona picha
zake?” Geb alimfanya Nanaa amwangalie kwa mshangao. “Umejuaje!?” Nanaa
akauliza kwa mshangao. “Kaka yako anakupenda sana, Nanaa. Huwa
akizungumzia habari za ndugu zake, haachi kukutaja na wewe. Kwa hiyo nakufahamu
kwa kiasi.” Nanaa alibaki hajui aseme nini. Kwa kuwa hakujua Geb
anamfahamu kwa lipi.
“Eti?” “Ninazo picha za zamani za mama yangu.
Lakini sifanani naye hata kidogo! Sasa sijui kwa kuwa alifariki akiwa
bado mtoto mdogo!? Lakini hatufanani kabisa, hata sifanani na ndugu zake! Labda
hii rangi kama ya kaka. Lakini nipo watofauti kabisa. Nimejaribu kujifananisha
hata na bibi, lakini sijioni kabisa kwake. Isipokuwa rangi tu. Bibi mzaa mama
ana rangi kali sana. Ndio maana wote mpaka kina Viola, mtoto wake, kaka, mimi,
kina mama zetu, wote tumechukua rangi ya bibi. Lakini sioni kingine. Nahisi
nitakuwa nafanana na upande wa baba yangu.” “Ulifanikiwa kumuona baba yako?” Geb
akauliza.
“Kuna kipindi nilitamani kumtafuta, lakini mama
mkubwa aliniambia sio jambo sahihi, kwa kuwa alikana mimba yangu, na hata wazazi
wake walimfukuza mama yangu na kumuonya asiwahi kurudi tena. Na hapo mama
alikuwa amefukuzwa nyumbani kwao. Mama mkubwa anasema mama alipofukuzwa kule
nyumbani kwao, na kwa huyo mwanaume, akawa hajui pakwenda. Ndio akamchukua
yeye. Lakini alipomuuliza zaidi juu ya baba yangu, mama alishindwa kueleza
zaidi alikuwa akilia tu. Akasubiri labda akijifungua ndipo anaweza kumuuliza
tena, lakini wala hakutoka kwenye chumba cha kujifungulia. Akafa bila kueleza
zaidi juu ya baba yangu. Sasa kwa kuwa bado mama hakuwa namawasiliano mazuri na
wazazi wake, au niseme zaidi bibi ambaye ndiye aliyekuwa mzazi wa pekee
aliyekuwa akiwalea kina mama. Bado alikuwa na hasira na mama, hata baada ya
mazishi, bibi alinikataa kabisa. Hakutaka hata nirudishwe kule kijijini, nyumbani
kwake. Akamwambia mama mkubwa kwa kuwa yeye alifanya kosa lakumpokea mama, yeye
ndio anipeleke kwa baba yangu, sio pale.” Nanaa akaendelea.
“Anasema aliponirudisha kule kwa upande wa
aliodhania ndio baba yangu, na wao walinikataa kabisa. Wakamfukuza mama mkubwa
akiwa na mimi. Hata hivyo mtoto wao, yaani yule baba ambaye ni mwanaume
aliyekuwa ametajwa na marehemu mama, mwanzoni wakati mama mkubwa alipoenda na
mama akiwa mjamzito, alisema mama alikuwa na wanaume zaidi yake. Sasa kwa nini
achaguliwe yeye kupewa huo mzigo, ambao ni mimi? Ndio mama mkubwa akakosa nguvu
ya kuniacha pale, anasema akahangaika sana kutafuta mtu anayetaka mtoto wakati ule,
akakosa. Akatafuta hata kunipeleka kwenye vituo vya watoto yatima, akashindwa.
Walimwambia kwa wakati ule kituo hicho kilikuwa kimejaa, na hawana fedha, na
mimi sio kwamba ni yatima nisiye na ndugu. Nipelekwe kwa ndugu zangu.” Geb
akashangaa.
“Kwa nini yeye hakuta kukulea mwenyewe!?” Geb
akauliza kwa kumuhurumia. Nanaa akanyamaza kidogo, akainama kama kuzuia
machozi. “Tokea nazaliwa mpaka leo, mume wake hakuwahi kunipenda.
Alihesabu mimi ni mzigo mzito ambao hakutaka kujihusisha nao, na wakati huo na
wao walikuwa na mtoto mdogo Viola. Kwa hiyo baada yakushindwa pakunipeleka,
ndio nikaishia kwao. Kwa kifupi mpaka hivi leo, hatukuwahi kujua baba yangu ni
nani.” Nanaa alitoa tabasamu lililoonyesha limejaa maumivu.
“Pole sana. Sikuwa nikijua kwa undani hivyo!”
“Ndio hivyo. Sasa imekuwa kama ni roho chafu nilizaliwa nayo! Nakuwa nakataliwa
na kila mtu! Kila ninaposhika, hapashikiki. Nimebakiwa na kaka tu. Inaniingizia
hofu ya kuendelea kukaribisha watu karibu yangu. Nimeona hata nikiwakaribisha
kwenye maisha yangu, nawachefua kwa haraka sana.” Geb alimuhurumia
asisadiki anayosema Nanaa. Yeye asingechefukwa kama angebahatika kuwa karibu
yake. Aliwaza Geb.
Kabla hajaongea kitu, wakasikia Geb
akiitwa. “Geb!” Wakashitukia Grace anakuja huku akiita. “Vipi?”
“Mpeleke mwanangu akalale bwana! Danny anazidi kuongea hataki turudi nyumbani!
Mbu watamng’ata!” Wakasimama. “Mnisamehe kama nimewakatisha.” “Hamna
shida. Hata mimi naona niombe lifti tu kwa Geb. Nataka nikapumzike.” Nanaa
alijibu kiustarabu tu. Alikuwa kwenye wakati mzuri sana. Geb alionyesha yupo
tayari kumsikiliza. Pole za hapa na pale zilikuwa zikimliwaza. Na kufurahia
kuwa karibu yake, asitamani watoke pale.
“Sasa Geb?” Ilibidi Grace amuulize Geb
aliyekuwa ni kama yupo njia panda. Amepokonywa tonge mdomoni, hakujua ajibu
nini kwa haraka. Ni kama alitaka kuendelea kuwepo pale. “Tafadhali
Geb!” Grace akajaribu kubembeleza. “Sawa. Ngoja nikamchukue. Vipi
mama?” “Naona ana kazi yakucheka tu! Si unamjua anavyopenda porojo za Danny?
Sasa wamekutana na James. Zinda ameshalewa! Na wengine ndio wanazidi kuagiza,
naona tutakesha leo.” “Basi namuacha. Nitamshusha Nanaa nyumbani kwao, ndipo
niende nikamlaze Fili. Nimuogeshe kwanza kabla yakumbadilisha nguo?” Walianza
kuondoka kurudi ndani hotelini. “Fanya chochote utakachoweza. Maana amejaa
michanga mpaka kichwani!” “Uzuri akilala huwa haamki, nitamuosha kidogo.” Walikuwa
wametangulia Grace na Geb, Nanaa akiwafuata nyuma taratibu. Ukweli Grace
alivutia kumwangalia. Nanaa alikubaliana na kaka yake, James.
~~~~~~~~~~~~~
Alimpokea mtoto kutoka kwa shemeji
yake, Nanaa akaaga kwa kaka yake, wakaondoka. Njiani kulikuwa na utulivu
kidogo. Lakini ukimya huu haukuwa kama ule wa mwanzoni. Grace aliwakatisha
mazungumzo yaliyoibua hisia za huzuni katikati yao. Nanaa alijiegemeza vizuri
kwenye kiti, akabaki akiangalia nje ya dirisha. Geb alimtupia macho mara kadhaa
kama anayetaka kuongea kitu, akajikuta anakwama, hajui aongee nini.
Atafutaye Hachoki.
A |
kiwa amepotelea mawazoni kwenye gari hilo ambalo Geb ni dereva,
simu yake ikaanza kuita. Nanaa akaingalia kwa muda, akaipokea. “Ni mimi Jeff!”
“Nilihisi tu.” Nanaa akacheka kidogo. “Vipi? Ulishatoka kwenye sherehe
au nikufuate?” “Asante kwa kujali Jeff, lakini nimepata lifti. Hapa nipo njiani narudishwa
nyumbani.” “Ulikuwa na wakati mzuri huko?” Jeff aliendelea kudadisi
taratibu kuonyesha kujali. “Siyo mbaya. Nimefurahia.”
“Ulikula?” Nanaa akacheka. “Ulikataa kula mchana. Ndio maana
nauliza.” “Hapana Jeff. Sikula. Bado nilihisi tumbo limejaa. Mchana nilikula
chakula kingi. Na mbaya zaidi ilikuwa ugenini. Kila nikifikiria hivi
nilivyoshiba mpaka sasa, nahisi nilitia aibu huko ugenini. Sijui kama wenyeji
wangu walishiba!” Akamsikia Jeff akicheka na yeye. “Inawezekana
una tumbo lenye shukurani tu.” “Haya bwana. Nipe moyo tu.” Wakatulia
kidogo.
“Jeff!” Nanaa akaita. “Nipo Nanaa.”
“Nilifikiri umekata.” “Bila kukuaga?” Nanaa akacheka. “Siwezi kufanya
hivyo.” Geb alikuwa akiwasikiliza maongezi yao. Lakini alikuwa kimya
tu. Wala hakuonyesha kama yuko pale. “Asante kwa kupiga.” Nanaa
akashukuru. “Mbona kama unaniaga?” “Hapana.” Nanaa alijibu kiungwana. Lakini
alijua wazi mazungumzo ya muda mrefu akiwa na Geb pale kwenye geri, sio
ustaarabu. “Unaweza kuendelea kuzungumza?” “Naomba nikupigie kesho.” “Upo
sehemu ambayo huwezi kuongea?” Nanaa akatulia kidogo.
“Unakumbuka nilikwambia nimepewa lifti?
Sasa tupo njiani ndio narudishwa nyumbani.” “Oooh! Sawa. Basi nitasubiri simu
yako kwa hamu.” “Lakini unakumbuka nilisema kesho?” Jeff
akacheka. “Sawa Nanaa.” “Muda gani ni mzuri?” Nanaa
akauliza tena. “Iwe tu kabla ya lunch. Ili usije ukashiba sana, ukashindwa kula na
mimi dinner.” Nanaa akacheka. “Sawa. Nitafanya hivyo. Usiku mwema.”
“Asante. Na wewe Nanaa.” “Asante.” Akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
Hakuna aliyemuongelesha mwenzake tena
pale ndani ya gari. Hata hivyo walikuwa wamekaribia kufika nyumbani kwa James.
Geb alisogeza gari karibu kabisa na nyumba. “Nashukuru kwa lifti na
kunisikiliza. Samahani kama nilikwambia mambo yasiyokuhusu.” “Hata kidogo. Na
mimi nimefurahia wakati mfupi, tuliokuwa nao.” Nanaa akacheka. “Sio
mfupi hivyo. Nimeongea vyote hivyo! Mpaka nimeishiwa maneno.” “Mmmh!” Geb
alijifanya kama anafikiria. “Nini?” “Sikumbuki kusikia maelezo ya
kutojibiwa ujumbe wangu.” Nanaa alicheka tena.
“Hivyo hatukuongea.” “Basi huwezi
kuwa umeishiwa maneno. Bado nasubiri maelezo.” “Lakini si umeshasamehe?” “Mpaka
nijue sababu.” “Haya bwana. Muwe na usiku mwema.” Geb alikuwa
akimtizama na tabasamu lililomfanya Nanaa azidi kufurahia na kusahau hata kama
dunia inazunguka. Kwamba masaa yanasogea. Alitamani kuendelea kuwepo na Geb.
Kitu ambacho hakuwahi kusikia kabla, na wala hakuwa tayari. Lakini akajikuta
inamtokea “Na wewe pia. Usiku mwema.” Nanaa akashuka akiwa na
furaha moyoni. Akasubiri afungue mlango, akaingia ndani bila ya kugeuka nyuma
tena, ndipo Geb alipoondoka.
Kwa Nanaa.
Hakutaka kuharibu ile furaha na
chochote. Akaoga haraka haraka akakimbilia kitandani huku akicheka. “Sasa
nacheka nini?” Nanaa akajiuliza kwa sauti. “Furaha hii ni ya Geb!?
Mmmh! Acha kabisa Nanaa. Mchumba wa mtu huyo! Labda Jeff. Lakini Jeff
anaonekana muungwana! Mmmh! Ni wale wale tu. Kaona pipi kwenye karatasi, na
yeye anataka kufungua aonje ladha. Sidhani. Nimpe nafasi nione? Lakini mbona
nilipokuwa naye sijajisikia hali niliyojisikia wakati nipo na Geb? Labda Jeff
ndio amenifanya nianze kujisikia vizuri hata nilipokuwa na Geb nikafurahia kwa
sababu tayari Jeff aliku…” Nanaa aliendelea kuwaza.
Kwa Geb.
Geb aliondoka pale akielekea kwao
njiani akikumbuka dimpozi za Nanaa. Akacheka. “Anavutia!” Akasifia
moyoni na kucheka. Akakumbuka kicheko kizuri cha Nanaa. Kuna wakati alicheka
huku machozi yakimtoka. Pia Geb akavutiwa zaidi. “Sio kwamba anavutia
tu, lakini pia..” Geb akatulia kwanza. Akakumbuka mazungumzo kati
ya Nanaa na Jeff. Akavuta pumzi kwa nguvu.
“Lakini hamna kitu. Sina haja
yakutilia shaka.” Akajiliwaza. Lakini akakumbuka vile Jeff alivyong’ang’ania
na kurudi kuomba namba ya simu. Isitoshe akapiga! Geb akakumbuka ni kama kwenye
mazungumzo aliyosikia yakiendelea ndani ya gari, Nanaa aliahidi kumpigia simu
kesho yake. “Tena ni kama Jeff amesema kabla ya lunch ili asishindwe
kula naye dinner! Sikumsikia Nanaa akikataa. Ni kama…” Geb aliendelea
kuwaza.
Siku Ya Jumapili Baada Ya Birthday
Ya Fili.
W |
alimuona Geb anaingiza simu yake mfukoni na kuitoa kila mara. Mama
yake akaona, akanyamaza. Grace naye akaona, mwanzoni akanyamaza. Alipoona na
hasira zinaanza, na hata muda wa kula ukaanza kusogezwa mbele, Grace akamfuata
mama yake chumbani kwake. “Kwani leo vipi?” “Mimi mwenyewe nimejibiwa
majibu mafupi. Nimeona ninyamaze tu, nije kujituliza kitandani kwangu. Kwani
Liz anakuja saa ngapi?” Mama yao akauliza. “Leo jumapili mama!
Unajua Liz anatumia siku ya leo na familia yake. Labda kuwe na dharula.” “Naona
inakaribia kuwa dharula.” Grace akacheka na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~
“Mbona ni kama alifurahia kuwa
na mimi?” Geb akabaki akijiuliza. “Au ni mawazo yangu tu? Nini
kilichonipelekea kudhani alifurahia mazungumzo yetu!?” Geb alianza
kujisuta. Lakini akakumbuka vile Nanaa anavyomtizama na kucheka kila alipokuwa
naye. “Mmh! Labda nimewaza kwa haraka. Nilimsikia akicheka hata na
Jeff. Kwa asili, Nanaa anapenda kucheka.” Geb alizidi kunyong’onyea
kila alipokuwa akiitizama simu yake na kukosa jumbe za Nanaa. Alitoa sauti
kwenye simu yake ili kama Nanaa akituma ujumbe mtu asijue. Lakini tena akaona
aweke tu sauti ili Nanaa akimtafuta hata kwa kuomba radhi na kutoa maelezo ya
kwa nini hakujibu ujumbe wakujuliwa hali siku ile, asichelewe kujibu. Akabaki
anahangaika na simu yake.
“Tokea enzi za Frida, tena nikiwa
mtoto, mpaka sasa, Nanaa ndio msichana pekee amenipuuza kwa kiasi hichi!
Angejua msafara wa wanawake wanaotaka hata kupata namba yangu ya simu, hakika
angeshukuru hata kupata ujumbe kutoka kwangu.” Geb
aliendelea kuwaza.
“Hamna haja yakujiumiza kichwa. Sina
sababu yakusubiria simu yake. Naachana naye kabisa. Siwezi kujikosesha raha
bure! Kwanza ilikuwa nafanya kiuungwana tu. Kwa kuwa aliondoka akisema
hajisikii vizuri nikiwa naye. Kama anaona hamna umuhimu wakuwasiliana na mimi,
basi. Ulazima unaletwa na nini?” Geb aliendelea kujiuliza,
kujifariji, kujitia moyo na kujiwekea mikakati ya kupuuza majibu kutoka kwa
Nanaa. Lakini hakuacha kutupia jicho kwenye simu yake kila mara.
Alikumbuka wakati mfupi
aliopata na Nanaa. Cheka na dimpozi zilizokuwa zikitokea mashavuni kwake.
Akakumbuka vile alivyokuwa akimtizama wakati anacheza na watoto. Akajikuta
anacheka peke yake na kutoa tena simu na kuangalia kama alimtafuta hata kwa
salamu. Shauku yakutaka kumuona tena ikaongezeka.
~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Nanaa yeye akaamka na
kuandaa kifungua kinywa chake na kaka yake. Kwa kuwa aliona kaka yake bado
amelala, akaona aue ndege wawili kwa jiwe moja. Akatengeneza chapati za
kusukuma. Akapasha moto mchuzi wa nyama ya kuku na njegere vilivyokuwa kwenye
friji. Akaweka kwenye hotpots. Alitengeneza chai nzuri ya tangawizi, hiliki na
mdalasini. Akaweka kwenye chupa ya chai, akampangia kaka yake mezani.
Alirudi kuoga, akabaki amekaa
kitandani anajipaka mafuta huku akiwaza na kucheka. “Geb!” Wazo
likamjia. “Natamani ningempigia! Lakini naanzia wapi!? Heri ningekuwa
nimemjibu ujumbe wa kwanza. Au jana ningemalizana naye juu ya kwa nini
sikumjibu ujumbe wake. Pengine leo ningekuwa huru hata kumuulizia hali.
Ningejidai kumuuliza kama walifika nyumbani salama na mtoto!” Nanaa akaendelea
kuwaza. “Ni kama nimeshakuwa na hamu naye tayari!” Nanaa
akajicheka na kujisuta.
~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Jeff naye akawa anasubiria
simu ya Nanaa, kila wakati macho kwenye simu. Yeye akajishusha. Mtaka cha
uvunguni, hana uawanaume, shuruti ainame. Ujumbe kutoka kwa Jeff
ukaingia. “Oooh Jeff!” Nanaa akakumbuka wakati ameshika simu
yake akitaka kusoma. “Nimemsahau kaka wa watu wakati nilimuahidi
kumpigia! Ngoja nisome.” Akafungua ule ujumbe. ‘Uliamka
salama?’ Nanaa akasoma na kubaki hajui kama amjibu au apige tu. “Sipo
tayari.” Akajiambia.
Wakati anajishauri, akaona simu ya Jeff
inaingia, akapokea. “Nimeona umesoma ujumbe wangu.” Nanaa akacheka. “Ndio nilikua
nafikiria nijibu nini?” “Umeshajua?” “Najiona sipo tayari kutoka, Jeff. Moyo
wangu umesita kabisa.” “Kwa nini usije kunisikiliza tu? Nipe nafasi ya
kunisikiliza. Ndipo ukatae.” “Basi naomba isiwe leo.” “Lini?” “Weekend ijayo.
Jumamosi.” “Kweli?” Nanaa akanyamaza huku akiuma meno.
“Nanaa?” “Kweli.” “Usinidanganye.”
“Nitakutafuta Jeff.” “Sio kunitafuta kwa kunipigia simu tu, tunatoka.” “Basi
nitakupigia kwa uhakika kama itawezekana au la.” “Nanaa! Mbona tunaenda mbele
na kurudi nyuma!?” “Kwa kuwa sipo tayari Jeff. Kweli sipo tayari hata kidogo.
Sitaki.” “Basi. Naomba nisikulazimishe.” Alisikika akiongea kwa sauti ya
kukata tamaa. “Utakapokuwa tayari, naomba unikumbuke.” “Sawa, asante.” Nanaa
akakata kwa haraka bila kupoteza muda.
~~~~~~~~~~~~~
Alimuhurumia, lakini akaamua ajipe
nafasi. Anachojisikia kwa Geb, hakijawahi kutokea kabla maishani mwake. “Sitaki
kujichanganya. Nikaanza huku, kumbe moyo wangu haupo. Hata hivyo sina haraka. Akitaka
kusubiri, anisubiri. Kama hawezi basi.” Nanaa akakubaliana na wazo
lake. Akatupa simu pembeni. Akaendelea na shuguli zake.
~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa kina Geb, ilipofika mchana
Grace akamuhurumia mdogo wake. Akaamua kumpigia simu Liz ili kumfanya aje hapo
nyumbani, amtulize Geb. Asijue yanayomsibu pacha mwenzie. “Vipi?” “Nipo
na familia Grace. Tumetoka kanisani, tumekuja hapa Sea Cliff, kupata chakula
cha mchana.” Liz aliongea sauti yakutotaka kusumbuliwa. “Ninahamu na
Samaki wa kuchomwa!” Grace alipata sababu ya haraka. “Basi
nitakununulia. Nikuletee. Lakini naweza kuchelewa.” “Hamna shida.” Grace
akashukuru mtego wake umefanikiwa.
Kitu kisicho cha kawaida, Geb alirudi
chumbani kulala. “Amekunywa hata uji?” Grace akamuuliza mama yake. “Kanywa
kidogo. Inaonekana kuna kitu kinamsumbua. Vipi huko kazini?” “Kila kitu kipo
sawa!” Grace akajibu. “Sasa ni nini!?” Mama yake akahoji
tena. “Labda ni vile Liz alivyomuacha jana pale kwenye sherehe ya Fili.
Nimezungumza naye, amesema anakuja.” “Afadhali aje, watu tucheke. Khaa!” Grace
akatoka chumbani kwa mama yake.
~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika mida ya saa 9 mchana, Liz
akaingia na samaki wa kuchoma. Danny akampokea na kuanza kula na mkewe palepale
sebuleni. “Geb yuko wapi?” Liz akauliza. “Kamwangalie chumbani
kwake, amelala.” Grace alishukuru Mungu. “Naona nimuache tu,
nisimsumbue.” “Kwa nini!?” Grace akauliza kwa mshituko kwani lengo ni Liz
aje pale, amtulize mdogo wake. Liz akafikiria kidogo. Akamwomba Grace watoke
nae nje.
“Kwani vipi?” “Kwani huko kazini
mambo yakoje?” Liz akauliza swali kama la mama yake. “Kwema tu. Kwani
vipi?” Grace akauliza kutaka kujua zaidi. “Mmmh! Geb amebadilika
kidogo. Week hii nzima nimekuwa nikimbembelezea mapenzi. Ananipa sababu. Sasa
jumamosi jana, akanipigia simu nije. Nikakataa kwa kuwa nimechoka. Lakini
akasisitiza nije tu. Nikaja nikiwa natumaini angalau nitaambulia kitu.
Nimeingia kuoga, natoka, Geb amelala kitu ambacho si kawaida yake. Tumeamka,
kabla hata muda wa shuguli kuanza, nimemshika, unajua alinikatalia! Akasema
hajisikii. Nikambembeleza, akasema labda kwa kuwa hajala vizuri. Tujaribu
baadaye. Tumekuja pale kwenye shuguli pia ameshindwa kula. Namuuliza mbona
hali? Kama unavyomjua Geb, kujibu anapojisikia. Hakunijibu Grace. Namuaga kuwa
nakwenda sehemu usiku ule, hata kuonyesha kujali wakati mchana wake au week
nzima nimekuwa nikimbembelezea mapenzi. Mtu anayejali si angekuwa na wasiwasi
labda nakwenda kwa mwanaume mwingine? Naona nimuache kidogo.” Grace
akatulia.
“Au unashaurije?” Liz alimtaka
shoga yake ushauri. Grace akabaki akiwaza kidogo. “Wewe Grace?” “Si ndio
nawaza!” “Sasa unawaza nini wakati ni mdogo wako, unamjua vizuri!?” Hilo
ndilo lilikuwa tatizo. Grace alimjua vizuri sana Geb. Akaogopa kumpa ushauri
kwa vile anavyomfahamu mdogo wake. “Naona kweli umpe muda. Labda mgonjwa
au uchovu. Au kuna kitu anapanga kichwani, kinashindana na pesa yake. Na Geb
akianza mipango yake mikubwa, kichwa chake huwa hakiwi sawa.” “Afadhali
kunituliza. Nilianza kuhisi ananikwepa!” Grace na yeye alijua hivyo hivyo.
Lakini hakutaka yeye ndio amuumize Liz. Akaona amtulize tu, watajua mbele
ya safari.
~~~~~~~~~~~~~
Badala ya kuondoka, uzalendo
ukamshinda mtoto wa kike. Akaonelea aingie tu chumbani kwa Geb. Akamkuta ndio
anatoka. Wala hakuonyesha dalili yakumtaka arudi naye ndani. “Umependeza
sana Liz.” Geb akamsifia. “Asante. Jumapili yako ikoje?” “Nimeshinda
kitandani tu.” “Kwema?” Liz akauliza. “Yeah! Kwema tu. Twende.”
“Wapi?” “Sebuleni. Nataka nikale. Sijala.” Liz akaumia mpaka usoni
akaonekana. Hakutegemea kuitiwa sebuleni na si kitandani. “Leo ni jumapili
Geb! Nipo hapa! Chumbani kwako! Unafikiri nimekuja kuzungumza na kina Grace
kweli? Niambie ni nini kinaendelea Geb!” “Mbona kila kitu kipo sawa tu! Kwa
nini unafikiri hivyo?” “Unanikwepa kimapenzi.” Geb aliinama na kuanza
kumbusu. Alimvutia kitandani akaandelea kumbusu.
Alimbusu kwa muda kisha akamuweka
sawa, na kumuuliza. “Umefurahi sasa?” “Nakutaka zaidi Geb. Please.” Liz
akabembeleza akiwa ameamkwa tamaa kwelikweli. “Tafadhali Geb.” Isivyo
ya kawaida, alimuona akivuta pumzi kwa nguvu kama anayejishauri. Akamvua nguo
na kufanya naye mapenzi. Haikuwa kama alivyozoea Liz, lakini angalau
alishukuru. Geb alimfanikishia yeye tu, akaacha.
“Mbona unatoka kitandani wakati
haujamaliza?” “Unakumbuka nilikwambia sijala? Nataka kwenda kula.” “Kwani kuna
kitu nimekuudhi?” Liz akauliza kinyonge. “Hapana Liz. Acha kuwaza
hivyo! Ni njaa tu. Wewe umefurahia?” Liz alitoa tabasamu la
kuridhika. “Nashukuru kwa kidogo ulichonipa.” “Utaniua Liz!” Kidogo
wakacheka. Walizungumza kidogo, angalau ile hali ya wasiwasi kupita kiasi
ikampungua Liz hata na Geb. Wakatoka wote wametulia.
Siku Ya Jumatatu Yake.
A |
subuhi kama kawaida yake, akawahi ofisini. Kwenye saa mbili na
nusu, Grace akaingia na habari za kuwa Fili ameanza shule rasmi. Akamuonyesha
Nanaa picha alizompiga mwanae. Akiwa anatoka nyumbani mpaka yupo
darasani. “Mchumba amependeza!” Nanaa akasifia, Grace akacheka. “Alikuwa
akiimba njia nzima. Amefurahi kweli.” Wakaongea kidogo. Grace akarudi
ofisini kwake.
Ilipofika mchana, wakati kazi
zimechanganya, Grace akapigiwa simu shuleni kwa kina Fili. Nanaa akashitukia
Grace amemsimamia ofisini kwake, akiwa hana raha. “Vipi?” Nanaa
akauliza. “Fili huyo! Yaani leo ndio ameanza shule, siku ya kwanza, hata
masaa saba hayajaisha tangia awepo hapo shuleni, tayari nimepigiwa simu
natakiwa niende.” Nanaa akacheka. “Amefanyaje?” “Sikutaka hata kujua!
Naona niende tu, nitajua huko huko.” “Pole.” “Sitakawia kurudi.” Grace
akatoka kwa haraka ili akajue kinachoendelea huko shuleni kwa mwanae.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda wakarudi. Yeye
anacheka, mwanae analia. “Wamemfanyaje tena!?” Nanaa akauliza kwa
wasiwasi. Lakini Grace alishindwa hata kuongea kwa kucheka. “Nyamaza
mwanangu, eeh!” Kila Grace alipokuwa akimwangalia Fili alizidi
kucheka. “Njoo Fili mtoto mzuri.” Nanaa alisimama akaenda kumchukua
akampakata. Akasikia mlango unafunguliwa bila hodi.
Alikuwa Geb, aliingia huku na yeye
anacheka kama dada yake. “Muone alivyopooza! Kama sio yeye!” Geb
aliongea huku cheko limemjaa. Walizidi kucheka yeye na dada yake wakati Fili
analia. “Nimekuletea Ice cream yako na ya Nanaa. Njoo uchukue.” Geb
alimuita Fili, lakini Fili akakataa.
“Kwani analia nini?” Nanaa
akauliza tena. Hakuwa amepewa jibu tokea wanaingia. Grace na Geb walikuwa
wakimcheka Fili. “Si Danny huyo! Kamwambia mtoto ataende shule, atasoma
sana, atapata pesa nyingii, halafu atamlipa anko James, amchukue Nanaa, aende
naye kwake. Sasa mwalimu wake anasema tangia amefika shule, hataki kucheza
wala kuimba, anataka afundishwe kusoma tu. Mwalimu anamwambia sio muda wote ni wakusoma,
anatakiwa atoke na nje acheze na wenzake, hataki. Kakataa mpaka kula! Sasa mwalimu
anasema tangia afike, hajafanya kitu chochote yeye anasoma tu vitabu.
Imefika mchana wanatakiwa kulala, amekataa anasema apewe hela yake.” Nanaa
na yeye akaanza kucheka akawa ameshaelewa.
Wote wakajikuta wanacheka bila
kujizuia, lakini sio Fili. “Sasa mwalimu anamuuliza pesa gani? Fili
amekazana, dad amemwambia akisoma sana, atapata pesa nyingi sana, kwa hiyo yeye
ameshasoma, anataka apewe pesa nyingi sana, hataki kulala. Yeye mchana analala
na Bibi Fili na usiku analala na Mama Fili. Hajaenda pale kulala wala kucheza
au kula. Yeye ameenda kusoma na kupata pesa, basi. Kama ni chakula amemwambia
yule mwalimu kuwa Bibi Fili anampikia uji mzuri na dad amemkataza kula kwa
watu. Na kama ni michezo yeye ana michezo mingi sana nyumbani kwao na anachezea
timu ya mpira wa kikapu ya anko Geb. Yeye amekwenda pale kusoma na kupata pesa.
Sasa ashasoma, apewe pesa yake nyingi, aondoke.” Geb na Nanaa walikuwa
wakicheka mpaka machozi.
“Hataki kunipa pesa yangu!” Fili alizidi
kulia. Geb akaenda kumbemba. “Nyamaza mtoto mzuri.” Geb akaendelea
kumbembeleza. “Hivi baba yake yuko njiani. Nimemwambia aje, amuelezee
mwanae vizuri, aelewe. Maana yeye ndio ameyataka yote haya.” Grace
aliendelea, kidogo wakamsikia Danny ameingia anaongea. “Yuko wapi Dume
langu?” “Njoo huku ofisini kwa muhasibu.” Grace alimuita mumewe.
Danny aliingia tu na kuanza
kucheka. “Pole mwanangu. Njoo.” Danny alimpokea kutoka kwa Geb, huku
akicheka. “Usilie sasa na wewe! Wanaume huwa hatulii!” Danny
akamkoromea mwanae. “Amekataa kunipa pesa nyingi, wakati mimi nilishasoma sana.” Walizidi
kucheka. “Sasa anko Geb ameniambia amekuletea ice cream yako. Chukua ice
cream kutoka kwa anko, halafu twende tukazungumze ofisini kwangu. Anko James
anakusubiri. Anataka tukakueleweshe vizuri kwa vitendo. Una akili sana Fili,
najua utazidi kuelewa. Sawa?” Fili akatingisha kichwa kukubali.
“Kwa hiyo unaondoka naye?” Grace
akamuuliza mumewe. “Anavyosubiriwa huko, kama shujaa! Kila mtu anataka
kumuona Fili, Dume langu.” “Hapo atakuwa amesimulia kila mtu! Danny jamani!”
“Dume langu hili! Kwanza anamsikiliza dad wake, pili akiweka malengo
anahakikisha yanatimia, haruhusu vitu vya kijinga viingilie malengo yake.
Wanataka kumdanganya mwanangu kwa uji na michezo wakati kwao vyote vipo!? Sasa
leo lazima upate zawadi. Sawa?” Danny alitoka akiwa amembeba mtoto wake,
huku akijaribu kumtuliza.
Akawaacha wote wanacheka. “Huko
ofisini wataenda kukoma! Wakutane nao hao wawili! Itakuwa ni stori tupu leo,
hawatafanya kazi mpaka muda wakufunga ofisi ufike. Ngoja na mimi nikamalizie
nilichokuwa nikifanya.” Grace alinyanyuka akatoka pale, akamuacha Nanaa na
Geb.
~~~~~~~~~~~~~
Furaha ilimjaa Nanaa, asijue ni nini! “Nimekuletea
Ice cream. Uliisahau siku ile ya birthday ya Fili.” Nanaa akacheka. “Nilisahau
hata kama nilitaka kuagiza Ice cream! Asante. Lakini usingesumbuka kuleta.”
“Grace alinipigia simu akanielezea kisa cha Fili. Akasema wapo njiani na bado
analia. Nikaona nimtulize kwa ice cream, ndio nikaamua nikuchukulie na wewe
pamoja na chakula. Najua hujala.” “Na chakula!?” “Mbona huamini?”
“Sikutegemea! Asante kwa kunifikiria. Nashukuru sana.” Nanaa alifurahi
mpaka akatamani kuruka ruka.
~~~~~~~~~~~~~
Labda hujaelewa. Chakula kimeletwa na
Geb! Wakajikuta hawajui waseme nini tena. Nanaa alijawa na furaha akabaki na
tabasamu usoni huku akiangalia vile vitu alivyoletewa. Kiliwekwa kwenye boksi
zuri, lunch box, na kubebwa kwenye mfuko wa maana. Kwa hiyo akajua ni
chakula kilichotolewa kwenye mgahawa wamaana! Sio kibandani, kwenye vumbi.
Inamaana imefanyika juhudi za makusudi, kununuliwa na kuletwa pale kwake.
~~~~~~~~~~~~~
“Vipi kazi lakini? Mambo
yanaenda?” Akabadili mazungumzo. “Hivyo hivyo nakazana.” “Taratibu
utaelewe tu.” “Naogopa kuharibu nikamudhi Grace, akashindwa kunipa kazi
nikimaliza shule.” Geb akacheka kidogo. “Basi ndio ukazane ili
usiharibu soko.” “Samahani. Nimefurahi mpaka nimeshindwa kukupokea!” Geb
akacheka. “Karibu ukae hata kidogo! Ule ndio urudi kazini.” Nanaa
akampokea kile chakula na ice cream. Akaweka mezani. “Nina haraka natakiwa
niwahi sehemu. Tutawasiliana.” “Nakushukuru sana. Asante.” Nanaa
alishindwa kujizuia. Alihisi asante pekee haitoshi. Alibaki akichekacheka
nakushukuru. “Nimefurahi san! Asante.” Akarudia tena. Geb akacheka na
yeye. “Karibu.”
Hakika Geb aliona furaha ya Nanaa
usoni. Hakujua kama furaha ile ni ya chakula tu, au alikuwa na furaha yake
tokea mwanzo! Akatabasamu. “Kazi njema.” Geb akamuaga. “Na wewe
pia.” Geb akatoka na kuacha Nanaa anafuraha sana moyoni, asiamini kama
bado Geb alikuwa akifikiria anachokipenda. Alileta aina ya Ice cream ile ile
ya ‘Vanilla’ aliyomwambia anaipenda. Halafu akamletea na chakula!
Nanaa alitamani kupiga mayowe kwa furaha. Alibaki akicheka cheka tu.
~~~~~~~~~~~~~
Si kwamba Grace hakuona chakula
alicholetewa Nanaa. Aliona na harufu ya kuku wa kuchoma ilienea ofisi nzima.
Watu wakaanza kulalamika kuumizwa pua. Grace mwenyewe akabaki na
mshangao. “Geb!” Grace alikaa ofisini kwake akawaza. “Geb
Magesa, anakwenda kununua chakula na kumletea Nanaa! Mmmmh!” Grace
alifikiria kidogo. Akataka kumpigia simu mama yake ampe umbea. Akaona anyamaze
kwanza mpaka aelewe vizuri. Maana hata yeye mwenyewe hakuwa ameletewa kitu
chochote chakula. “Halafu na mabadiliko Liz aliyoyaona je!? Inawezekana
Nanaa ndio sababu!?” Grace akajiuliza. Akapiga mahesabu ya siku
alizokutana Nanaa na Geb, akagundua ndio muda ambao Liz alimwambia Geb
amembadilikia. “Mmmmhhh!” Grace akaguna huku akimfikiria mdogo
wake.
~~~~~~~~~~~~~
Nini kitaendelea kati ya Nanaa na Geb katikati ya penzi la Liz, Jeff na Zinda ambaye naye ameanza?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment