Wakati yupo njiani kuelekea kwao, Zena akampigia
tena simu kumsisitiza asichelewe na kumwambia wakutane Mlimani city, asiende
nyumbani kwao. Nanaa akakubali. Akafika nyumbani kwao, akaoga kwa haraka. Kutoa
jasho na vumbi la Kariakoo, akatoka kuelekea Mlimani City.
Walikubaliana wakutane nje ya duka la nguo la
Maikos. Nanaa alisimama pale, akampigia simu Zena. “Nimefika.” “Subiri dakika moja tu.” Nanaa akakata simu.
Akamuona Zena anakuja na vijana wawili. Nanaa akacheka na kutingisha
kichwa. “Sasa unacheka nini?” Zena akauliza. Nanaa akamvuta pembeni
kwa nguvu. “Maneno yote yale kumbe nia yako nikuja kuniuza mimi na wala
huna ishu unayotaka nikusaidie!” “Sio kwa mtu mbaya Nanaa shoga yangu. Njoo
nikutambulishe. Utampenda.” “Wewe ni muongo Zena. Sijui kwa nini nilikuamini!”
“Chonde shoga yangu. Naomba usiniabishe hapa.” Nanaa hakuwa akiamini
aliweza vipi kumuamini Zena, tena kwa uongo wa kijinga kama ule!
Zena na yeye akamvuta kumrudisha kwa wale
vijana. “Huyu anaitwa Yasini, ndie rafiki yangu. Na huyu ni rafiki yake
anaitwa Jeff.” Akawageukia wale vijana wawili. “Huyu ndiye Nanaa.
Shoga yangu kipenzi. Tupo sisi watatu. Tia tu ndio amekosekana hapa.” Nanaa
hakuwa akiamini. Alibaki akimtizama Zena. “Tumefurahi kukufahamu Nanaa.” Jeff
akaitika. “Asante.” Nanaa alishindwa hata kujibu na mimi nimefurahi
kuwafahamu, akaishia kusema ‘asante’ tu. Kwani hakukusudia kuangukia kwa
mwanaume mwingine kwa wakati huo. Hasa wanaume aliokuwa akiunganishwa na Zena!
~~~~~~~~~~~~~~
Na Zena huo ndio ulikuwa mchezo wake. Mwanaume wa
mwisho alimfanyia hivyo hivyo. Alimwita Nanaa mahali akimwambia amekwama
mahali. Wamekula yeye na Tia, lakini wakagundua hawana pesa ya kulipa. Wanaomba
awafuate kwenye huo mgahawa. Nanaa akaacha shuguli zake zote, akapanda daladala
mpaka Sirender Bridge pub, ili kunusuru mashoga zake. Alipofika pale akapiga
simu kuwaambia hawaoni. Zena kwa ujasiri wote, akamwambia atafute meza akae,
wameenda chooni mara moja watatoka. Tena hapo ni baada ya kumuuliza aina ya
nguo alizokuwa amevaa.
Baada ya Nanaa kukaa kwenye hiyo meza, akashitukia
anafuatwa na kijana, aliyemsalimia kwa kumtaja jina kana kwamba wanafahamiana.
Akiwa kwenye mshangao, yule kijana ndipo akamwambia ameunganishwa na Zena.
Anatafuta mchumba aliyetulia aoe. Nanaa hakuwa akiamini mchezo
aliomchezea Zena. Akajua wazi alishakula pesa ya yule kijana. Tena ndio
walikuwa wamemaliza mitihani, Nanaa ametulia kwao.
~~~~~~~~~~~~~~
“Tunaweza kwenda kula sehemu?” Yasini
akauliza kiungwana. Nanaa akacheka kwa kuguna. “Samahani. Mimi nimetoka
kula muda si mrefu. Na baada ya muda mfupi sana kuanzia sasa, natakiwa kwenda
mahali.” “Una miahadi ya saa ngapi?” Jeff akauliza na yeye. “Baada ya
dakika 45 kuanzia sasa.” Nanaa akajibu. “Basi haina shida. Kama ni
sawa na tunakuomba twende hapo ‘Saad restarant’. Muda ukifika,
nitakupeleka.” Nanaa alicheka akifikiria, lakini ikabidi akubali.
Waliingia hapo kwenye hiyo restaurant, wakatafuta
meza wakakaa. Walionekana ni vijana waungwana na watu wazima walio tulia. Wao
waliagiza chakula na vinywaji, Nanaa akaagiza maji ya kunywa ya baridi.
Akaletewa kwenye glasi. Wakaanza kula. Hapakuwa na maneno mengi sana. Yalikuwa
mazungumzo ya maana tu. Jeff akamuuliza Nanaa ni wapi anafanya field yake. Kama
anapafurahia. Wanamlipa kutokana na kazi wanazompa. Anampango wa kufanya hapo
kwa muda gani. Hayo yote yalikuwa maswali waliyouliza Jeff na Yasini kwa
kupokezana.
Jeff mwenyewe ndiye aliyemkumbusha Nanaa juu ya
miahadi yake. Nanaa akashangazwa. “Sitaki sisi ndio tuwe sababu ya
kutokufanikisha miahadi yako.” “Nashukuru.” “Kama ni sawa, tunaweza
kukupeleka mpaka huko. Vinginevyo tutakuchukulia taksii.” Jeff aliongea na
tabasamu usoni. “Sio sehemu ya siri. Nimealikwa kwenye birthday ya mtoto
wa bosi wangu. Anatimiza miaka 5. Kwa hiyo mnaweza kunisindikiza tu, kama
mtapenda. Lakini nina uzoefu mzuri sana na daladala.” Nanaa aliongea
kwa tabasamu. “Basi kwa kuwa tuna usafiri, nafikiri tukusindikize tu.”
Wakasimama wote kwa pamoja. Wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Jeff na Yasini walitangulia mbele, Nanaa na Zena
wakabaki kimya. “Hebu niambie shoga yangu. Hapo vipi?” “Ukoje wewe Zena!?”
“Acha hasira, niambie ukweli. Huyu wa safari hii muugwana.” “Sasa wewe
huyu Yasini si mkristo? Utamwambia nini mzee Hiza?” “Hapo ndipo atakapojua
penzi halina dini. Nilivyompenda huyu kaka! Hamna mtu ataniambia kitu nikaelewa.
Labda na yeye ajekugeuka tapeli kama Dula.” Nanaa alimwangalia Zena mtoto
wa ustadhi, asiamini. Baba yake alijulikana mtaani kwa kushika dini. Alikuwa
Mzee mstaarabu na mwenye maadili. Swala 5, zisizopungua kila siku.
~~~~~~~~~~~~~~
Jeff na Yasini walikaa mbele, Nanaa na Zena
wakakaa nyuma. Sehemu yenyewe waliyokuwa wakifanyia shuguli nzima ya Fili
ilikuwa Masaki. Wakaondoa gari kuelekea Masaki. “Umefurahia chakula,
Zena?” Yasini alikuwa ndiye dereva, alirusha swali. “Ndiyo.
Nashukuru.” Zena alijibu huku akimkonyeza Nanaa. Akionyesha wazi
amefurahia lile swali la kuonyeshwa kujaliwa. Nanaa akatabasamu. “Hongera.” Alinong’ona. “Asante
shoga yangu. Mungu kanipumzisha!” Wote wakacheka kwa pamoja. Nanaa akaanza
kujifikiria maisha yake. Akapotelea mawazoni.
“Si ndio hapa?” Jeff akauliza swali
lililomtoa mawazoni Nanaa. “Sijawahi hata kufika! Kama nyinyi ndio mnasema
ni hapa, basi itakuwa hapa. Nawashukuru sana na nawatakia wakati mzuri.” Nanaa
akashuka. Kabla hajafunga mlango, Jeff akamuita. “Abee!” Nanaa
akarudisha kichwa ndani. “Naomba tuzungumze kidogo.” Nanaa akamtizama
Zena, akarudisha macho kwa Jeff. Akakuta anamtizama. “Sawa.” Akakubali.
Jeff.
W |
akasimama
pembeni kidogo ya gari. Mbele ya uzio wa michongoma. “Naomba kesho
tuonane.” Jeff akavunja ukimya mara baada ya kuridhika wako peke
yao. “Mimi sijui Zena amekwambia nini juu yangu. Lakini sina mpango wa
kuolewa hivi karibuni.” Nanaa alikataa haraka sana. Jeff akacheka
kidogo. “Sijasema nataka kukuoa Nanaa! Nimeomba tukutane kesho.” Nanaa
akaingia aibu tena, akacheka kidogo. “Samahani. Nahisi kwa sababu
namfahamu Zena, ndio maana nimekuwahi mapema. Sitaki kukupotezea muda.” “Hata
mimi nisingependa kupotezewa muda.” Nanaa akainama na kufikiria.
“Nanaa?” “Nafikiria Jeff!” “Nini?” Jeff
akauliza tena. “Najiona sipo tayari na hizo heka heka! Na wewe unaonekana
ni mtu mstaarabu, pengine ungenielewa tu. Sipo tayari kwa mahusiano aina yeyote
ile.” “Mbona vipingamizi vingi Nanaa? Nimeomba tutoke. Kwa nini usikubali,
ukasikia ni kwa nini nataka tutoke kabla hujaanza kuweka vipingamizi?” Nanaa
akacheka tena kidogo. Lakini wazi alionekana hafurahii.
“Ulitaka twende wapi?” “Tutoke kwa chakula cha
usiku.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu. “Naishi na kaka yangu Jeff!
Siwezi kutoka usiku. Nitamwambia nakwenda wapi na wewe sikufahamu?” “Basi
tufanye iwe mapema.” “Labda hujanielewa. Ninaposema naishi na kaka yangu.
Namaanisha ndiye kama Mungu wangu wa pili hapa duniani. Ndiye mama yangu.
Nikisema mama, namaanisha ndiye aliyenilea tokea siku nimezaliwa natolewa
hospitalini mpaka hivi sasa. Kuninyonyesha, kuniogesha nakunivalisha mpaka
nepi. Ni kama baba kwangu, kwa kuwa ndiye anayehangaika kula. Kulala
kwangu. Ndiye anayehangaika na kuvaa kwangu tokea mtoto mpaka hivi sasa. Ni
kama baba anayesumbukia na soma yangu pia. Amechukua nafasi ya dada pia kwa
kuwa ndiye anayenishauri kwa karibu. Na ndiye mtu wa pekee katika maisha yangu
ambaye yupo karibu yangu tokea nazaliwa mpaka sasa. Siwezi kufanya lolote hasa
nikiwa nyumbani bila kumshirikisha yeye kwanza. Sasa hata nikikubalia tutoke
mapema, namwambia nini juu yako Jeff wakati wala sikufahamu?” Nanaa
alizidi kumsisitiza Jeff, ili tu amuache.
Lakini bado Jeff alipambana. “Unaweza
kumuaga tu na kumwambia kuna mtu nakwenda kuonana naye. Mwambie utamwambia
zaidi juu yangu baada ya mazungumzo yetu ya kesho tukitoka. Tukishakutana.
Tukazungumza. Ukajua unipe nafasi gani kwenye maisha yako, utakaporudi nyumbani
unaweza kumwambia chochote kile juu yangu. Lakini baada ya mazungumzo yetu.
Ninachoomba ni unipe tu nafasi Nanaa. Tafadhali.” “Mmmh!” Nanaa akaguna.
Wazi alionyesha hataki.
“Vipi?” “Sijui kwa nini Jeff, moyo
wangu unakataa! Naomba nipe muda wa kufikiria tafadhali.” “Unafikiria nini
wakati hata hujui ni nini nataka kuzungumza na wewe!? Si ungenisikiliza kwanza
ndipo uniambie kama utataka kufikiria?” Nanaa akaulia.
“Tafadhali Nanaa!” “Sijui Jeff! Naomba nifikirie
hata huko kutoka. Sijajiandaa. Naomba nikutafute nikiwa nipo tayari. Tafadhali
Jeff. Najua ni nini nazungumzia. Nahitaji muda.” “Unaniahidi kunipigia?”
“Nafikiri.” “Nanaa!?” Jeff akamwita kwa masikitiko. “Sijui Jeff!
Labda. Sitaki kukupa ahadi za uongo. Mimi sio muongo Jeff.” Bado moyo wa
Nanaa ulikuwa mzito.
“Nanaa please!” “Kwa nini unanisihi wakati hata
hunifahamu? Umetajiwa tu na Zena. Unajuaje kama mimi ndio mtu sahihi unayetaka
kumwambia hicho unachotaka kuongea tukikutana?” “Hilo swali naomba nilijibu
tukitoka wote.” Nanaa akacheka akionyesha wazi cheko lile sio la furaha.
Hata uso wake ulionyesha kutokukubaliana.
Wakasikia mtu anakohoa upande wa pili wa ule
uzio. Wote wakageuka. “Pole Danny mwanangu. Upepo huo!” “Asante mama
yangu. Upepo mkali kweli!” Danny akajibu. Wakasikia watu wakianza kucheka.
Ndipo wakajua kuna watu walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa akainama. Jeff
akacheka. “Nitasubiri simu yako Nanaa.” Jeff akaaga. “Asante kwa
lifti. Nitakutafuta.” Jeff akaondoka. Nanaa alibaki akiwaza.
Birthday ya
Fili.
“Uwiii! Danny si mume wa Grace? Sasa si watakuwa
wamesikia kila kitu?” Nanaa
aliwaza akiwa amesimama pale pale. “Njoo tu Nanaa. Hatujawasikia kabisa.
Kwanza hatukuwa tukiwasikiliza.” Nanaa alitamani kuanguka. Akasikia sauti
za watu wakizidi kucheka. Nanaa akajua wapo kundi la watu. “Nyamaza Danny!
Utamfanya ashindwe kuja.” Alisikia sauti ya Grace. “Uwiii! Kwani na
kaka James yupo hapo?” Nanaa akauliza. “Yupo. Lakini hajasikia kama
utatoka kesho usiku.” Danny alijibu na kufanya wazidi kucheka. “Uwiii!” Nanaa
akazidi kulalamika kwa sauti. “Njoo Nanaa. Achana na Danny!” Alisikia
sauti ya kaka yake akimuita huku akicheka sana.
“Njoo mara moja kaka!” Nanaa akamuita kaka
yake, lakini akasikia wanazidi kucheka. “Nenda kamlete mkwe wangu,
James.” Alimsikia Grace akiongea. James akazunguka uzio, akatoka kwenye
kigeti kidogo. Alitoka akicheka. “Usicheke kaka!” “Usiwe na wasiwasi.
Twende.” “Naona aibu kweli! Natamani niondoke tu.” Nanaa alijaribu
kunong’ona zaidi, lakini bado akasikika. “Wala usione aibu Nanaa. Nimekwambia
hakuna aliyesikia.” Danny alidakia tena, vicheko vikazidi kuongezeka.
Nanaa akajifunika uso. “Danny nyamaza bwana! Ujue Nanaa akiondoka hapa,
mwanao hatakata keki? Wewe fanya mchezo.” Hata James mwenyewe alikuwa akicheka
sana. Akamshika mkono Nanaa, akaongoza njia mpaka ndani.
Alikuwa akitembea nyuma ya James. Aliishiwa nguvu
baada ya kukuta hilo kundi la watu waliokaa hapo. Alishindwa kujua akifika hapo
aanze vipi. Mungu bariki Fili akawa amemuona kabla hajawafikia. Akaanza kupiga
kelele huku anamkimbilia Nanaa. Nanaa akasimama. “Nanaa! Nanaaa!” Nanaa
akafungua mikono kama kumlaki. Maana Fili alikuwa akija kwa mwendo kasi.
“Usimchafue bwana!” Grace alimuwahi kabla
Fili hajamkumbatia Nanaa. “Hamna neno. Mwache tu.” Fili alikuwa
amejaa michanga mpaka kichwani. “Umechelewa. Lakini bado sijakata keki.
Leo Mama ameniruhusu kunywa soda wakati nakusubiria.” Fili alianza. “Kumbe
ulikuwa ukinisubiria mimi?” “Ndiyo. Kwani ulikuwa hujui? Nilimwambia anko Geb
akupigie, akasema unakuja sasa hivi.” Fili aliendelea. “Mwache hata
akae basi! Unamdaka na maneno mengii. Ataondoka sasa hivi.” Alimsikia
Danny akiongea. “Eti utaondoka, Nanaa?” Fili akauliza kwa upole.
“Njoo ukae hapa mwaya. Huyo atakuchosha
tu.” Grace alisimama huku akimuonyeshea pakukaa. “Eti utaondoka?
Maana nimewaambia rafiki zangu wote kuwa unakuja. Wakataka kukuona. Sasa
utaondoka kabla hawajakuona?” Fili alirudia tena kuuliza akionyesha
wasiwasi. “Hapana. Siwezi kuondoka, mpaka niwaone rafiki zako, tucheze
wote ndio nitaondoka. Na hii ndio zawadi yako.” Fili akacheka akionyesha kufurahia
zawadi aliyopewa na Nanaa. “Asante sana Nanaa.” “Karibu na samahani kwa
kuchelewa.” “Mimi nimeshakusamehe Nanaa.” Fili akajibu huku macho yapo
kwenye zawadi. Wakacheka wote.
Nanaa akasogelea lile kundi la watu wazima
waliokuwa wamekaa, wakiangalia watoto wanavyocheza. Bado alikuwa amembeba Fili
wakati akifungua mfuko uliokuwa na zawadi yake.“Nanaa ameniletea mpira wa
Spider Man!” Fili alifurahia sana. “Nilikwambia nini juu yakufungua
zawadi hapa? Nitakufinya masikio mimi! Kwa nini husikii?” Danny
alimbadilikia mwanae. “Si ni ya Nanaa tu, ndio nimefungua!” Wote
walicheka.
“Fili! Fili!” Liz akamuita. “Eeeh!” Fili
akaitika. “Unaitikaje kama mtoto wa kike wewe? Sema ‘naam’!” Danny alimgombesha
tena. “Naam!” Fili akarekebisha haraka sana. “Sasa lini unamuoa
Nanaa?” Liz alimuuliza kumchokoza tu. “Dad amesema mpaka nipate hela
nyingi, nimlipe kwanza anko James, halafu nimchukue Nanaa, niende naye kwangu,
nisirudi naye nyumbani.” Kila mtu alianza kucheka.
“Wewe Fili! Ndio nilivyokwambia hivyo?” Danny
alimuuliza nakumfanya Fili afikirie kidogo. “Umeruka kitu kimoja.” Akajaribu
kumsaidia. “Ehe, nimekumbuka. Dad amesema, nisome sana,
nipate pesa nyingi, nimlipe anko James, akinipa Nanaa, niende naye nyumbani
kwangu, nisirudi naye nyumbani kule kwa dad.” Kila mtu alikuwa
anacheka sana.
“Itabidi ukazane sana. Bado una safari ndefu mno.” Rafiki
mmoja aliongeza. “Shule yenyewe bado hujaanza!” Mwingine
alichangia. “Sio mbali sana. Dad wangu amesema naanza jumatatu.
Ameshanitafutia.” Kila mtu alikuwa akicheka. Ni kweli Fili alikuwa
mzungumzaji. Tena anaongea kwa ufasaha, bila woga. Mama yake alikuwa
akitingisha kichwa.
“Bibi Fili amesema atanisindikiza kumlipa anko
James pesa. Mimi sijui kuendesha gari, sioni mbele.” Watu walizidi
kucheka. “Kumbe mama wewe ndio dereva?” Danny akauliza. “Nimepewa
hiyo kazi. Amesema yeye hafikii sehemu ya kukanyaga mafuta na kuweka breki. Kwa
hiyo mimi nimsindikize kwa anko James.” Mama Grace na Geb, au Mama G kama
wengi walivyozoea kumuita, alijibu nakufanya watu wazidi kucheka. “Bwana
mwanangu amejipanga! Lazima atamuoa Nanaa.” Grace akaongeza. “Tena
Jeff akae mbali kabisa!” Danny alifanya Nanaa afunike uso kwa aibu. “Bora
umemkatalia.” Danny aliongeza nakufanya watu wazidi kucheka.
Mama G ndio kabisa mpaka machozi.
“Nina mpango wakuacha kazi, nasubiri mahari yangu
kutoka kwa Fili.” James alidakia. “Ujipange mwanangu. Huyo anko James
anapenda pesa kuliko benki!” Danny aliongeza. “Nitampa. Nitakuwa nazo
nyingi sana.” Fili alijibu kwa kujiamini na kufanya watu wazidi
kucheka. “Mmemsikia Dume langu? Nipe namba ya simu ya Jeff nizungumze
naye.” “Bwana Danny muache Nanaa.” Grace alimwambia mumewe anyamaze huku
yeye mwenyewe anacheka. “Lazima taarifa zimfikie Jeff king’ang’anizi.
Jamaa kakaba kweli! Kila akikataliwa hivi, anang’ang’ania tu. Haelewi!” “Ndio
ikabidi uokoe jahazi Danny mwanangu?” “Kabisa mama. Mtu gani hataki kuelewa!?” Wakazidi
kucheka huku Nanaa amejificha nyuma ya Fili na yeye anacheka taratibu kwa aibu.
“Twende Nanaa tukacheze.” Fili
alimuokoa. “Bwana wewe nenda kacheze na wenzako, mwache Nanaa apumzike.” Danny
alimkoromea tena mwanae. “Acha tu niende naye. Leo ni siku yake, mwache
afurahi.” Nanaa akamshusha, akamshika mkono. Wakaanza kuondoka huku wengine
wakicheka. “Najua kuogelea, dad alinitafutia mwalimu akanifundisha
kuogelea. Halafu pia najua kucheza mpira wa kikapu na miguu. Nachezea kwenye
timu ya mpira wa kikapu ya kina anko Geb. Mimi ndio mfungaji wao.
Kila jumamosi jioni huwa naenda naye mpirani. Wananitegemea mimi hapa.” Geb
alitingisha kichwa huku akicheka na wengine. Fili akaendelea. “Halafu huwa
nacheza mpira wa miguu na dad wangu pale pale nyumbani. Najua pia kukimbia.
Mama yangu ananisifia najua sana kuruka Kamba. Pia…” Fili aliendelea kujisifia
kwa Nanaa.
“Daah! Mwaangu kachanganyikiwa kabisa. Msikieni
anavyojinadi kwa Nanaa. Vitu vyote leo anajua kuvifanya yeye, wakati muoga
kweli wa maji!” Danny alifanya watu wazidi kucheka. “Bwana mwanangu
ameweza kuogelea. Mwalimu wake anayemfundisha kuogelea anamsifia kweli!” Grace
alimtetea. “Mmmh! Mbona mimi nilivyompeleka mazoezini alikuwa analia mpaka
ulipongea naye kwa simu, ndio akakubali kuingia kwenye maji? Kioga kweli,
utafikiri kitoto cha kike!” Danny alimjibu mkewe. “Sasa wakati ule si
alikuwa bado hajazoea? Siku hizi mjuzi kweli. Muulize Geb ambaye pia huwa
anampelekaga kwenye mazoezi ya kuogelea.” “Hana lolote huyo mwanao. Maneno
mengii, muoga kama mama yake!” Danny alizidi kuchekesha watu.
Atafutae Hachoki.
N |
anaa
alianza kumsukuma Fili na rafiki zake kwenye bembea. Walipeana zamu, Nanaa
akawa anawasukuma kwa zamu. Mara akamuona tena Jeff amerudi na kuingia mpaka
ndani. Akamuangalia Jeff, kisha akawaangalia wale waliokuwa wamekaa pale. Kina
Danny. Akaona wote wameinamia simu zao. Kama hawajamuona Jeff. Nanaa
akamsogelea akiwa amembeba Fili. Lakini wazi alijua kwa uinamaji ule, wote watakuwa
wamemuona Jeff. “Vipi?” “Nimekumbuka sijachukua namba yako ya simu, na
Zena amesema hawezi kunipa. Nikuombe mwenyewe.” Nanaa akacheka kwa aibu.
Akijua wazi kina Danny wanasikiliza. “Au basi chukua namba yangu mimi ya
simu. Kama unaona shida kunipa yako.” Jeff aliongeza. Na yeye alijitahidi
kuzungumza kwa sauti ya chini.
“Hamna shida. Hapa nilipo sina simu. Nimeiacha
pale mezani. Nacheza na watoto. Chukua tu ya kwangu. Utanitumia ujumbe ili niwe
na ya kwako pia.” Nanaa alijibu taratibu. “Asante. Nitafanya
hivyo.” Jeff alionekana kufurahia hilo wazo. Akatoa simu yake kwa haraka. “Sasa
sio na wengine muanze kukariri namba ya simu ya Nanaa. Mwenyewe ameamua kumpa Jeff
tu.” Danny aliongea kwa sauti. Mpaka Jeff akacheka. “Kwani huwezi
kunyamaza Danny jamani!?” Grace alimfinya. “Mimi nawajua binadamu mke wangu.
Bahati ya Jeff wanaweza kuikalia mlango wazi. Kabla hajafanikisha dinner
ya kesho, wakamuwahi kwa lunch.” Watu walizidi kucheka mpaka wengine
walikuwa wakitokwa na machozi.
“Ningekuwa mimi Jeff, ningempa Nanaa simu aandike
tu. Asiitaje. Wote waliokaa hapa, ni watu wa namba tupu. Tokea wanaanza kuongea
mpaka leo wanacheza na namba tu. Yaani wapo hapa mjini wanalipwa kwa kuchezea
namba kwenye maofisi ya watu. Nakuhakikishia Jeff, hawatashindwa
kukariri hizo tarakimu 10 tu za namba ya simu ya Nanaa. Ni ushauri tu kaka.
Unaweza kuuchukua au kuuacha. Na ujue wengi wao hapa, bado hawajaoa na hawana
hata wachumba! Sasa juu yako Jeff.” Danny aliongeza. Nanaa na Jeff
walishindwa hata kuongea, wakabaki wanacheka. Nanaa akiangalia chini, Jeff
akiwatizama.
“Au kuondoa mzizi wa fitina, chukua hii kalamu na
karatasi Jeff. Mimi nawajua binadamu. Hapo wote wasikio wazi. Wewe unaandika
kwenye simu, wenzio kichwani. Halafu ulogwe ukosee namba hata moja hapo,
utaandika maumivu. Maana hivi vichwa hapa, mimi navijua. Vina historia
yakutokusahau. Heri kuandika tu kimya kimya. Hata Nanaa akikosea kuandika hata
tarakimu moja tu, potelea mbali. Wote mkose. Kuliko wewe uliyehangaika vyote
hivyo eti ukose, halafu majamaa hapa yapate!” Danny akasimama na
kumpelekea Jeff kalamu na karatasi.
“Mimi nakukabidhi wewe mwenyewe. Uamuzi ni wako.”
“Nakushukuru.” Jeff alishukuru huku akicheka. “Tupo pamoja
kaka. Wema ndio asili yangu.” Danny alijibu kiungwana sana huku
akijisifia. Mama G, alikuwa akicheka mpaka machozi. Jeff akamkabidhi Nanaa ile
kalamu na karatasi. Nanaa akapokea, akaandika ile namba kisha akamrudishia Jeff
ile kalamu na karatasi, yeye akarudi upande walipokuwepo watoto na kuwaacha
wazazi wao wakizidi kucheka. Jeff akamrudishia Danny kalamu yake. “Asante.”
“Karibu Mkuu. Kila la kheri. Naamini hujapewa namba za gari.” Danny
akapokea kalamu na kumpa mkono. Mpaka Jeff akacheka. Akaondoka na kaucha huku
nyuma wanazidi kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa akamrudisha Fili kwenye bembea. Akaendelea
kumsukuma. Fili alisikika akicheka kwa furaha. “Hivi nimekwambia kama
umependeza sana?” Fili alisikika akimuuliza Nanaa nakufanya mpaka Nanaa
mwenyewe acheke. “Asante Fili.” “Umependeza sana. Gauni yako nzuri.
Nitamwambia mama yangu atupige picha. Halafu dad akaitoe tuiweke ukutani.
Nikihama na wewe, nahama na picha yangu.” Safari hii mpaka Danny alicheka kwa
sauti ya juu. “Bwana mwanangu amekazana!”
Walitoka kwenye mchezo huu, na kuhamia kwenye
mchezo mwingine huku Fili akiendelea kumsifia Nanaa, akionekana kufurahia uwepo
wa Nanaa kwenye party yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Wala Nanaa hakuwa amevaa nguo ya ajabu sana.
Alivaa gauni lake alilokuwa amelipata mtumbani. Lenye viboksi vyeusi na vyeupe
kote. Kata mikono lakini lina kiungio kiunoni. Kwahiyo kiuno chake kilibanwa
vizuri na kushuka mpaka chini kabisa. Liliendana na umbile lake zuri na likaonekana
la heshima. Alivaa na sendozi zake za kimasai zilizojazwa shanga nyingi nyeupe.
Alishazivua pembeni ya kiti alichokuwa amekalia kaka yake ili aweze kutembea
mchangani kwa uhuru.
Kama kawaida, alikuwa amesukwa rasta ndogo ndogo.
Lengo kubana matumizi. Wakati wote alisuka rasta ndogo ndogo ili zikae muda
mrefu. Zisimgarimu kwenda saluni mara kwa mara. Na pili zilimrahisishia kila
asubuhi anapokwenda kazini. Kwa hiyo usingemkuta Nanaa na kipilipili chake
kikavu. Wakati wote alisuka nywele zake. Hapo napo alibana mtindo wa butterfly.
Pande mbili ambayo moja ilikuwa ndogo, mstari wa pembeni na kuzivuta mpaka
katikati huku nyuma zimeanguka mpaka mgongoni.
Hereni zake za duara kubwa kiasi, alizokuwa
amenunua kwenye urembo tu, tena kwa bei rahisi sana. Lakini zilimkaa vizuri
sana na ule mtindo wa nywele ambao hata upepo uwe mkali vipi, bado kichwani
alibaki msafi na gauni halikumfanya awe uchi. Japokuwa alionekana amevaa vitu
vya hali ya chini sana, cheap, lakini bado alipendeza. Ungetaka
kumwangalia tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Walikuwa watoto 15, kutoka familia tofauti
tofauti, na wazazi wao walionekana kufahamiana vizuri. Danny ndiye alikuwa
akiwachekesha wazazi wao. Geb naye alikuwepo. Alikuwa amekaa pembeni ya Liz,
ametulia kama kawaida yake. Akajikuta macho yake yakihama na kwenda kila
anaposogea Nanaa. Alitulia akabaki akimtizama kwa utulivu, kama anayetafakari
kitu.
“Mwenzetu umepotelea wapi?” Liz alimshitua
Geb. “Nipo tu, nasikiliza.” Geb akajibu. “Mama Fili anakuuliza.” Geb
hakujua hata kama aliongeleshwa. Akamwangalia dada yake. “Keki vipi?” Grace
akarudia. “Unataka sasa hivi?” “Ndiyo. Naona njaa zitaanza kuwauma sasa
hivi, wadai chakula kabla ya keki. Nataka wakate keki kwanza ndio wale.” “Basi
ngoja nikamuombe yule muhudumu anipe. Nilimuomba anihifadhie kwenye friji.” Geb
akasimama. “Usisahau kuja na juisi yake huyu. Akili zikitulia,
ataikumbushia. Ni heri uilete tu moja kwa moja ili usifanye safari nyingi za
kwenda na kurudi.” “Hamna shida.” Geb aliondoka kwenda kufuata keki na
hiyo juisi ya Fili.
Zinda Naye.
“James!” Mmoja wa kijana aliyekuwepo pale
aliita. “Vipi Zinda?” “Sasa si unajua mimi pesa ipo? Sihitaji kukusanya
kama Fili. Au kuomba namba kama Jeff. Mimi mtoto wa nyumbani. Tumetoka mbali
sana mimi na wewe. Tumalizane kabisa.” Watu walianza kucheka tena. “Wewe
tu. Changamka. Si umemuona mwenzio Jeff karudi?” James akajibu, Geb
akarudi na keki akaiweka mezani.
“Tena Jeff mwenzio kakazana kweli! Si ulisikia
mama?” Danny alimuuliza Mama G nakumfanya acheke tena. “Kila
alivyokuwa anakataliwa, jamaa amekazana!” Danny aliongeza. “Yaani
nina uhakika Nanaa ni mke wangu mimi. Wengine wanahangaika tu.” “Sasa si
umfuate pale? Maneno mengii. Au unaogopa?” Danny akamuuliza. “Kukataliwa
kubaya!” Wote wakacheka.
“Jikaze kiume, Zinda.” “Ngoja nivute pumzi.” Zinda
alijisogeza kwenye kiti. “Vipi Mkuu? Mbona unatoa jasho wakati upepo
mkali?” Geb aliuliza na kuamsha kicheko kingine. “Anataka kumzidi
mahesabu mwanangu na Jeff. Sasa anapanga maneno ya kumwambia Nanaa. Maana
amesikia ya mwenzake Jeff, hana hali. Akirudi kwa Fili, yeye ndio anamikakati
mpaka ya mahari. Halafu mke anacheza naye.” Danny akajibu. Wote wakacheka.
“Nawaambieni kweli, Nanaa mke wangu mimi.” “Kwani
kuna aliyekukatalia hapa, Zinda? Wewe si uende!” Danny alifanya wote
wazidi kucheka. “Eti bibi Fili?” Zinda akamgeukia mama G. “Nenda tu
baba. Mwenye kisu kikali ndio mla nyama.” Mama G, alijibu, wote wakacheka.
Mara wakamuona Nanaa na Fili wanarudi pale
walipokuwa wamekaa. “Ehee! Huyo anakuja.” Zinda akajiweka sawa,
wengine wakakwepesha macho wakijidai hawakuwa wanamwangalia. “Anataka nini
huyo?” Danny akauliza walipo wasogelea. “Anataka kutumia choo. Sijui
ni wapi?” Nanaa akauliza. “Ngoja nikusindikize Nanaa.” Zinga akadakia. “Sio
mimi, ni mtoto!” Nanaa alijibu kwa upole akishangaa nakufanya kila mtu
acheke. “Sasa Zinda unachanganyikiwa nini? Nanaa kasema wazi kabisa, ni
Fili!” “Si ndio na mimi nimesema niwasindikize, au nyinyi mmesikiaje?” Kila
mtu alizidi kucheka.
“Wewe mpeleke mtoto chooni, acha kujitetea!
Umesema umsindikize Nanaa.” Danny hakuwa anajua kunyamaza, watu walizidi
kucheka. “Muone na huyu anavyo ruka ruka. Nilikwambia nini juu ya kubana
mkojo?” Danny alimuuliza mwanae kwa ukali. “Ulisema nisibane mkojo.
Nikisikia tu mkojo, niache michezo niende chooni kwanza.” “Sasa kwa nini
unaruka ruka?” “Si ruki ruki.” Fili akajitetea. “Nilikwambia nini juu
ya kusema uongo?” Aliendelea kumuhoji mwanae. “Nisiseme uongo hata
kidogo. Ni heri niingie matatizoni kuliko kusema uongo, hata
mdogo.” Fili alimjibu baba yake kwa upole na kuacha kuruka ruka.
Alionekana huwa ana mmudu Fili cha utundu. Watu wakazidi kucheka.
“Mmpelekeni mwanangu chooni jamani! Atajikojolea!” Grace
akalalamika. “Anko Geb, nipeleke chooni.” Fili akamgeukia anko wake. “Nipeleke
au naomba unipeleke!?” Danny akamkoromea tena. “Anko Geb naomba
nipeleke chooni.” Fili alirudia tena kwa upole. “Kwa nini mimi
nisimpeleke huko chooni?” Nanaa alitaka kupunguza shuguli
nyingi. “Hapana. Wewe utanipeleka choo cha kike.” Watu walianza
kucheka upya, na wote walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa bado hakuwa akimuelewa.
Tokea anamtoa kwenye mabembea alitaka apelekwe kwa Geb, au baba yake ndio
wampeleke chooni.
“Kwani choo cha kike kina nini!? Mimi nitakuwa na
wewe. Sitakuacha Fili.” Nanaa alimuongelesha kwa upole na upendo. “Hapana.
Dad alisema hakuna kuvaa tena diaper, wala kukojoa nikiwa nimechuchumaa au
kukaa kwenye choo. Nikojoe choo cha kiume, tena nikiwa nimesimama.” Watu
wote walicheka mpaka Nanaa alishindwa kujizuia akacheka mpaka machozi, lakini
Fili alikuwa ametulia akionekana anajikaza tu lakini amebanwa na mkojo.
“Bwana Geb mpeleke mtoto chooni! Atajikojolea!” Grace
alilalamika tena, Geb akasimama huku anacheka. “Twende. Na hakuna kubana
tena mkojo.” Geb alimshika mkono na kuondoka naye. Kila mtu alibaki akicheka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Twende tukacheze Nanaa.” Zinda akaanza
tena, nakufanya watu wazidi kucheka kasoro Nanaa alikunja uso na tabasamu la
mshangao. “Zinda vipi leo?” Danny aliuliza huku akicheka sana. “Namaanisha
twende tukacheze na watoto, bwana! Kwani nyinyi mmesikia nini?” “Mimi nashauri wewe
leo uache tu. Ishashindikana. Utaishia kumtukana Nanaa mwenyewe bure! Maana
mara umwambie umpeleke chooni, mara mkacheze, hujielewi kabisa!” “Nafwata
ushauri wako Danny. Naona kweli leo bahati sio yangu. Upepo unavuma pabaya.” Walizidi
kucheka, lakini Nanaa hakuwa ameelewa akaona aondoke kabisa pale arudi kwa
watoto.
“Naomba James unikaribishe nyumbani kwako.” Zinda
alimgeukia James. “Ushindwe hapa, nyumbani utaweza? Sitaki wageni nyumbani
kwetu. Wewe malizana na Nanaa hapahapa. Ukija nyumbani ni kulipana tu kama
Fili.” James alijibu. “Mimi bado naona mwanangu ndio Dume. Kwanza
kashatongoza mapemaa. Kajinadi mpaka Nanaa mwenyewe amemkubali. Hang’ati
maneno. Na ameshaweka utaratibu wa kulipa mpaka mahari! Msimzibie mwanangu
bahati yake. Katafute kwengine.” Danny alifanya watu wacheke zaidi.
Geb alirudi na Fili. “Njaa imeanza kumuuma
huyu. Anataka juisi yake.” Danny akataka kumpa chupa yake ya juisi. “Usimpe
bwana Danny! Hatakula wala hataweza kukata keki, ataishia kulala na chupa ya
juisi mdomoni. Njoo kwanza hapa mwanangu.” Fili alimsogelea mama yake
kinyonge, akionekana ameshachoka. “Njaa inauma?” Fili akatingisha
kichwa kukubali. “Wee!” Danny alikuwa kama anamkumbusha mwanae kitu,
haraka Fili akakumbuka na kujirudi. “Ndiyo mama, njaa inauma.” “Mwache
bwana Danny! Amechoka.” “Hakuna tabia za kuitikia na kichwa. Kwani yeye mtoto
wa kike?” “Amechoka!” Grace akamtetea. “Ndio akae hapo apumzike,
asubirie chakula.” Danny aliongeza. “Huo utakuwa mtihani. Akae chini
huyo! Hawezi. Kateni tu hiyo keki, ale, akacheze. Akitoka hapo, nikulala.” Liz
aliongeza.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakawaita watoto wote, Nanaa akawakusanya na
kurudi nao pale. Wakamwimbia Fili, akakata keki. Alimlisha Nanaa wa kwanza,
mama yake, dad, Bibi Fili na anko Geb. Wakaagiza chakula, Nanaa akaona ni heri
aenda kukaa kwenye meza ya watoto kuliko kukaa pale na kina Danny. Akajua
watazidi kumchokoza. Akamuaga kaka yake. “Kaka! Naenda kuwalisha
watoto.” Nanaa alimuaga kwa sauti ya chini ili asisumbue
wengine. “Poa poa.” James akiwa amenogewa na porojo za Danny,
akakubali bila kupinga. Nanaa akamchukua Fili wakaondoka.
Kilipoletwa chakula cha watoto Nanaa akaanza
kuwagawia wote. Na kuanza kumlisha Fili huku akisimamia na watoto wengine wale
wapunguze michezo. Wengi wao walikuwa na njaa. Kwa hiyo wakala bila shida.
Wakamaliza kwa haraka bila Nanaa kutegemea. Akabaki akibembelezana na Fili pale
mezani.
“Na wewe utakula nini?” Alishitukia Geb
amemsimamia nyuma yake. Akageuka, macho yao yakagongana, haraka sana Nanaa
akarudisha uso pale mezani. “Nimemwambia muhudumu asubiri kwanza,
asiniletee cha kwangu mpaka watoto wamalize kula.” Nanaa alijibu huku
amekaa, na kumpa mgongo Geb. “Ungekula sasa hivi, tunakaribia kumaliza
shuguli nzima.” “Basi nitaenda kufuata ndani.” “Unataka kula nini? Mimi naweza
kwenda kukuchukulia.” Geb aliendelea kusisitiza taratibu. “Usihangaike.
Nitakwenda tu.” “Sio usumbufu hata kidogo.” Nanaa alifikiria
kitu gani chakula, akajikuta hajui achague nini, akabaki kimya
akifikiria nini ale.
Grace na mama yake wakasogea pale. “Bibi
Fili! Njoo tule wote.” Fili alimuwahi bibi yake. “Mwenzio nimemaliza
chakula changu. Na wewe maliza cha kwako.” Bibi yake alisogea mpaka pale
mezani. “Sidhani kama atakula vizuri. Danny amempa keki kubwa sana.” Grace
na yeye akasogea. “Lakini anakula. Anakaribia kumaliza.” Nanaa akamtetea. “Basi
atakuwa alikuwa na njaa sana.” Grace alivuta kiti, akakaa.
“Unataka kula nini ili nimuite muhudumu
akuletee?” Grace naye akauliza. “Nahisi kushiba.” Nanaa akajibu. “Basi
agiza, mwambie akufungie ubebe. Ukale nyumbani ukisikia njaa.” Grace
akavuta sahani ya Fili akaanza kumlisha yeye. “Labda hivyo. Ngoja niende
hukohuko ndani ili niangalie wanavyakula gani.” Nanaa akasimama. “Usije
kulipia lakini. Geb ndio atalipia vyakula na vinywaji vyote.” Grace
aliongeza wakati anamnyanyua Fili ili ampakate. “Ameshaanza kusinzia huyu.
Inabidi tuondoke.” Grace alimbusu mwanae, Fili akajilaza kifuani kwa mama
yake. “Hivyo unavyomkumbatia, ujue ndio hatakula tena.” Bibi yake
aliongea huku akikaa kwenye kiti alichokuwa amekalia Fili.
Nanaa aliingia ndani ili kuchagua chakula,
akamuona Geb naye anamfuata. Alisimama sehemu wanayo agiza chakula akabaki
akisoma Menu, ili aagize. Geb naye akasimama pembeni yake. Nanaa alisoma mpaka
mwisho bado hakuona kitu chakuagiza. “Unaweza kulipia tu. Sidhani kama
nitakula.” “Hujapenda kitu hata kimoja wapo hapo?” Geb akauliza. “Nahisi
bado nimeshiba.” “Ungechukua chakula chochote tu, watakufungia vizuri
utakula baadaye.” “Ili nisikucheleweshe kulipia, ungelipia tu vyakula vya watu
wengine, halafu nikiamua baadaye kuchukua kitu chochote, nitalipia mwenyewe.” Alimsikia
Geb akicheka kwa kuguna kidogo, akageuka kumwangalia.
“Sina haraka yakulipia Nanaa. Ila sitaki
uondoke bila kula kitu chochote.” “Mbona wewe sijakuona ukila? Umekula
kweli?” Nanaa alimuuliza kwa kujali. Hata huwezi kujua alionaje kama Geb
hakula wakati alikuwa kwenye meza ya watoto na Geb alikuwa katikati ya meza
iliyojaa marafiki zao. “Mama alinipikia uji, nikanywa kabla hatujaja hapa.
Bado nimeshiba.” “Bado unakunywa uji mpaka leo!?” Nanaa alijikuta akiropoka
kwa kushangaa sana, nakumfanya Geb acheke kidogo. “Naomba hilo swali
umuulize Bibi Fili. Na mimi huwa nashangaa hivyo hivyo.” “Sasa kwa nini na wewe
usibebe chakula? Baada ya muda utasikia njaa. Uji huwa haukai muda mrefu
tumboni.” “Hapa naona wanavyakula vya kukaanga tu. Na mimi huwa sipendi vyakula
vyakukaangwa na mafuta mengi, kama chips au hao kuku. Nakinahiwa kwa haraka
sana. Nikifika nyumbani naweza kula chakula alichopika Grace mchana. Kwa hiyo
mimi nipo sawa tu.” Yalikuwa ni maongezi ya mara ya kwanza waliyozungumza
kwa muda mrefu kwa kuangaliana.
Nanaa alikuwa akimsikiliza huku akitizama macho
yake. “Haya macho si mchezo!” Nanaa aliendelea kuwaza moyoni
wakati bado akimsikiliza. “Kwa hiyo utachukua nini?” Geb aliendelea
kuuliza. “Nitarudi baadaye wakati tunaondoka. Nahisi nitachukua tu Ice cream,
nikale nyumbani.” Nanaa akageuka tena kama kusoma tena ile Menu
kujiridhisha. “Huwa unapendelea Ice cream gani?” Geb alihoji
kiustarabu. “Vanilla ndio napenda zaidi.” Nanaa alijibu na kumgeukia
tena. “Kwa nini umeuliza!?” Nanaa akamuuliza na tabasamu lenye
mshangao kidogo. “Nataka tu kujua.” Nanaa alitabasamu tena kidogo,
akageukia tena ule ubao mkubwa uliokuwa umening’inizwa juu kabisa. Ulikuwa
umebeba Menu zote. Akageukia upande palipo Ice cream na bei zake. Akaangalia kwa
muda kisha akageuka na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Alitoka na kukuta baadhi ya wazazi walishaondoka
na watoto wao, lakini James na kina Danny bado walikuwa wakiongea na kucheka kana
kwamba ndio wamefika hapo. Danny alikuwa amempakata mtoto wake, Fili,
amelala. “Naomba nikupokee.” Nanaa alimsogelea Danny. “Mzito
huyu! Wewe muache tu hapahapa. Pumzika.” Danny alimjibu Nanaa huku
akimwangalia mtoto wake aliyekuwa amelala. “Maneno yote yamemuisha kwa
kuchoka.” Liz aliongeza huku akisimama.
“Geb yuko wapi? Nataka kuondoka.” Liz
aliuliza huku akiangaza macho kumtafuta Geb. “Grace! Umemuona wapi Geb?” Grace
alikuwa ndio anarudi kutoka kusindikiza wageni wengine waliokuwa wamekuja
kwenye sherehe ya mtoto wake. “Unataka muondoke?” Grace akauliza
akiwasogelea. “Nataka kumuaga.” Liz alijibu. “Mwangalie ndani,
atakuwa analipia.” Grace alijibu na kwenda upande walipokuwa wakicheza
watoto ili kujaribu kusafisha kabla yakuondoka. Nanaa akamfuata ili kumsaidia.
Waliendelea kuokota huku wakihifadhi baadhi ya vitu walivyosahau watoto.
“Najua utakuwa umechoka, lakini nakushukuru.
Umenisaidia kucheza na watoto. Wamefurahi.” Grace alimshukuru Nanaa wakati
wakiendelea kusafisha. “Na mimi nimefurahi. Napenda sana watoto.” “Mimi
napenda watoto, lakini wasiwe watundu kama Fili. Jamani mtoto ananichosha akili
huyo! Nafikiria kama mimi mama yake ananichosha hivi, sijui inakuaje kwa
wasichana wa kazi!” Nanaa alicheka. “Unafikiri nakudanganya? Mimi
napenda akiwa ameanza kuchoka, hapo sina neno. Na anapenda kulala kama mgonjwa.
Hajiwezi kwa usingizi!” “Labda anakuwa anachoka sana.” Nanaa alijibu huku
akicheka. “Kwa shuguli zile, lazima achoke. Ukimuona amekaa chini
ametulia, ujue Danny yupo, au ana njaa au usingizi umemlemea. Basi.” Nanaa
alizidi kucheka.
“Hakuna urefu asioweza kupanda. Hakuna neno
asiloweza kuongea. Hakuna jambo asilolielewa. Na hasahau. Anarudia neno kwa
neno. Sasa akianza kusimulia habari zake, namtuma kwa Geb, yeye huwa hachoki
kumsikiliza. Halafu anamjulia. Sasa mimi siwezi. Nakuwa na mambo mengi
yakufanya na kuwaza. Sasa ubaya wake ni kila akizungumza kidogo, anakuuliza
maswali kutaka kujua kama unamsikiliza au umempuuza. Na anajua.” Nanaa
alizidi kucheka.
“Niwasaidie nini?” Geb aliwasogelea. “Afadhali
umekuja. Msaidie hapa Nanaa, mimi nikakae. Nimechoka. Liz ameshaondoka?”
“Ameondoka, kuna mahali amesema anataka kwenda.” “Ana mambo mengi shoga yangu
yule! Sasa usiku huu anaenda wapi?” “Sijamuuliza.” Geb alijibu kwa upole
na kwa ufupi tu. Akaendelea kukusanya takataka. “Mmh!” Grace aliguna
na kuondoka. Akawaacha Nanaa na Geb. Kimya kikazuka. Wakaendelea kukusanya
mpaka wakamaliza. “Hivi ni baadhi ya vitu walivyoacha watoto.” Nanaa
alimkabidhi. “Asante, na tunashukuru kwa kuja.” Nanaa akatabasamu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naona kikao ndio kimeanza rasmi.” Geb
aliongea huku akiangalia meza waliyokaa kina Danny na rafiki zake waliobaki
pale bila watoto. Walikuwa wakicheka huku wakiongea kwa sauti ya juu. “Unamaana
hawataondoka pale sasa hivi?” Nanaa akauliza. “Sio leo. Huwa wanakaa
muda mrefu sana. Una haraka yakutaka kuondoka? Naweza kukurudisha nyumbani.” Geb
akauliza na kumwangalia vizuri. “Hapana. Naweza kumsubiri tu kaka. Sina
pakwenda.” “Basi tukazunguke kidogo, ndio turudi kukaa.” Nanaa akamwangalia
vizuri.
“Unamaanisha na mimi?” Akauliza kutaka
uhakika. Maana alijua huwa anajichanganya sana kila anapokuwa na Geb. Hakutaka
kufurahia safari isiyo muhusu. Geb akatabasamu. “Ndiyo.” “Wapi?” Nanaa akauliza
tena. “Hapo nje ya uzio, kumepakana na bahari. Au umechoka?” “Hapana.
Tunaweza kwenda tu. Labda kama wewe ndio umechoka.” Tayari alishaanza
kujichanganya. Akasahau kama Geb ndiye aliyemwambia watembee kidogo. “Mimi
nipo sawa kabisa. Nililala muda mrefu mchana.” Geb alijibu huku akitoa
tabasamu. “Nisubiri nikaweke hivi vitu kwenye gari. Grace atawarudishia
wazazi wao akipata nafasi.” “Sawa.” Geb aliondoka, akamuacha Nanaa
amesimama akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~~
“Atakuwa alilala na Liz, pale
nilipowaacha nyumbani kwa dada yake.” Nanaa aliwaza huku wivu
ukimtesa. “Wanaonekana wanapendana! Alimuomba aje pale akisema anahamu
naye.” Aliendelea kukumbuka. “Wote wanaonekana wanajielewa.
Liz anaonekana ni msichana msomi, anapesa, na mzuri. Ni haki yake kumuhitaji.” Wivu
ulishamjaa kwa mwanaume asiye wake. “Liz anakaumbile kazuri! Hana nyama
uzembe. Kila kitu chake ni cha kiasi mwilini mwake. Mpaka rangi ya mwili wake
inavutia.” Nanaa aliendelea kusononeka akiwa amesimama pale peke yake
akimsubiria Geb. Hamu ya kuzunguka naye ikaanza kumuisha. “Nitakuwa
najiumiza bure.” Nanaa aliendelea kusononeka.
~~~~~~~~~~~~~~
Namzungusha Nanaa baharini kidogo.” Alimsikia
Geb akiwaaga lile kundi la vijana waliokuwa wakiongea na dada yake. “Afadhali,
ili asichoke.” Grace akajibu. “Unataka twende wote, mama?” Geb
alimuuliza mama yake. “Nimechoka bwana! Acha niendelee kusikiliza stori,
nicheke.” Mama yao alijibu huku akionekana anafurahia sana kinachoendelea
pale.
Geb akamsogelea Nanaa, aliyekuwa amepooza. “Upo
tayari?” Geb akamuuliza huku akimwangalia, Nanaa alitingisha kichwa
kukubali, wakaondoka. Ukimya mwingine ukazuka wakati wakiendelea kutembea nje
ya uzio, mchangani. Mawimbi ya bahari yalipigwa kwa nguvu na upepo, lakini giza
lilishaingia, ilikuwa ngumu kuyaona.
Walitembea kwa muda kidogo, hakuna
aliyemuongelesha mwenzake. “Tusiende mbali sana. Kunakuwa na wahuni wengi mida
hii.” Geb alivunja ukimya. “Unasikia baridi? Naona upepo mkali kweli!” Akauliza
tena. “Hapana, nipo tu sawa.” Nanaa akajibu kwa kifupi,
akanyamaza. “Unataka tukae kidogo au umechoka unataka kurudi?” Geb akaendelea
kumuuliza taratibu. “Vyovyote tu, nipo sawa.” Geb akamwangalia kama
aliyegundua kitu cha tofauti, kisha akaona aulize. “Upo sawa? Mbona kama
umekosa raha gafla?” “Nipo tu sawa.” Nanaa alijitahidi kutoa tabasamu, lakini
Geb akabaki akimwangalia akionyesha wazi amelikataa tabasamu feki.
~~~~~~~~~~~~~
Kwa mara ya
Kwanza Nanaa anapata nafasi ya kuwa na Geb. Maongezi yao ya kwanza ambayo
angalau yalichukua muda mrefu kidogo, yalijawa kujaliana. Kila mmoja akitaka
mwenzie asilale njaa. Sasa wapo peke yao ufukweni. Nanaa aliyejawa na wivu kwa
mwanaume asiye wake. Huku akikataa wanaume wanao mbembeleza, atatumiaje nafasi
hiyo hapo ufukweni.
Usikose Sehemu
ya 9.
0 Comments:
Post a Comment