Nanaa
hakumsikia tena Geb. Siku hiyo ikaisha. Jumanne mpaka ijumaa zikawa siku ndefu
kupitiliza akitamani atokee tena au angalau kumsikia tu. Lakini hakuonekana
pale ofisini wala hakusikia lolote linalomuhusu Geb. Ijumaa wakati anafunga
mahesabu ya siku, akaona Zena anampigia simu. Akacheka kwanza. Akajua ni mambo ya
Jeff tu. Akapokea. “Vipi shoga yangu?” Zena
akaanza kwa upendo “Kama mtu vile!
Ukitaka kuniunganishia kwa mwanaume, unakuwa unanipenda kweli!” Zena
akacheka. “Tutoke kesho basi.” “Nimemkatalia
Jeff.” “Kwa nini Nanaa? Hawa vijana ni watofauti.” Zena akamwaga
sifa nyingi weee, akimuuza Jeff.
Lakini bado moyo wa Nanaa ukakataa kabisa. Umeshaonjeshwa
hisia tofauti baada ya kuwa karibu na Geb! Akaona hapana. Anajipunja. Mbali na
kutafuta bora mwanaume, akajua ipo hisia tamu, unaweza kuipata kwa mtu. Hajajisikia
hivyo kwa yeyote yule! Kwa nini ajifunge tena kwa Jeff! Akaona asipoteze muda
zaidi, akamkatalia Zena. “Basi naomba tutoke kwa
ajili yangu tu. Nisaidie shoga yangu. Safari hii umenikatalia pabaya kweli! Ni
best wake Yasini. Tutoke tu tumsikilize.” “Zena akitaka jambo lake!” “Nihurumie
shoga yangu. Ndio kwa mara ya kwanza napata mwanaume wa maana na yeye ana
rafiki wa maana anakutaka wewe!” Zena
akajihuzunisha mpaka Nanaa akamuhurumia.
“Sawa. Kesho. Lakini isiwe usiku.”
“Usiwe na wasiwasi. Mimi mwenyewe nitazungumza na kaka James kukuombea ruhusa,
wala usijali.” Nanaa
akacheka. “Atakuchoka kaka yangu na maombi yako
yasiyoisha.” Zena akacheka. “Tukitoka
jioni ndio vizuri. Sio mchana jua kali bwana.” “Basi nitazungumza na kaka.”
“Lakini tupendeze kama kawaida yetu.” “Wala usijali.” “Nakuaminia Nanaa.” Nanaa
akacheka na kukata simu.
Changamoto
Za Maisha.
A |
limaliza
shuguli zake, akatoka ofisini ikiwa mapema tu. Akapanda daladala mpaka
nyumbani. Akashangaa kumkuta kaka yake yupo nyumbani, kitu ambacho sio
kawaida sana. “Leo mbona mapema? Shikamoo.” “Marahaba. Kuna kitu nilitaka
kuzungumza na wewe kabla hujakwenda kulala.” Nanaa akakaa. “Mama
anakuja kesho na Viola. Amenipigia simu kuniambia mtoto wa Viola ni mgonjwa na
ameambiwa huku ndiko kwenye daktari mzuri wa watoto. Nimejua ni uongo tu, kwa
kuwa najua wapo madaktari wazuri tu KCMC. Lakini sikutaka niwape sababu. Sasa
najua hapa pataanza kuwa padogo sana kwako. Naona nikutafutie chumba karibu na
maeneo ya chuo au karibu na hapa.” “Mmmh!” Nanaa aliishiwa nguvu kabisa.
“Pole.” “Sasa kipindi hicho tunatafuta chumba,
nitaishije nao hapa?” Nanaa alishakosa raha. “Nimezungumza na Grace pamoja
na Danny. Nimewaomba wakuhifadhi kwa muda wakati nahangaikia sehemu yako
yakuishi.” Nanaa akaumia moyoni akijisikia bado yeye ni mzigo wa kutafutiwa
sehemu ya kuwekwa kila wakati, akabaki ameinama akiwaza. Alishatulia nafsini
mwake, akifurahia maisha yake na kaka yake. Gafla anatolewa tonge mdomoni! Hakuwa
tayari kutoka hapo na kuanza kupya. “Ni mambo ya muda tu Nanaa. Namuamini Mungu
ipo siku utapumzika.” Nanaa akanyamaza.
“Kina Grace ni watu wazuri sana. Hutapata shida.”
“Unafikiria niondoke lini?” “Mapema kesho asubuhi, ili msikutane humu ndani
hiyo jioni wakifika hapa. Unaweza kuja kuwasalimia tu, lakini sio kuja kukaa
nao hapa. Watakuvuruga sana.” “Nakushukuru kaka yangu. Asante
kunifikiria.” Nanaa akashukuru na kuondoka hapo. Akaingia chumbani kwake.
Alijikuta machozi yakimtoka.
Alianza kukusanya vitu vyake vyote bila kusahau
hata kimoja. Akaweka kitandani. James akagonga na kuingia. “Nimekuletea
haya mabegi mengine. Najua utahitaji.” “Asante.” Nana
aliendelea kukusanya na kuweka kwenye mabegi huku akifuta machozi, mpaka
alipomaliza. James alikuwa amekaa kitandani akimwangalia. “Usiwe na
wasiwasi. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Naamini
hivyo kaka yangu.” “Ukiwa kwa kina Grace nitakuwa sina wasiwasi.
Najua utapata utulivu, ila mimi ndio unatakiwa unihurumie.” Nanaa alicheka
huku akifuta machozi. Alikumbuka uvivu na uchafu wa Viola. Vile mtoto wake
alivyo mtundu, maneno mengi ya mama yake. “Nitakuwa nakuja kukusaidia
usafi siku za jumamosi.” James akacheka, akatoka pale chumbani bila
kuongeza neno. Alijua wazi haitasaidia.
~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi ya saa nne, Grace alikuja na mtoto wake. “Yaani
mapema hii tayari umeshaivisha!?” Alimshangaa Nanaa. “Namuonea huruma
kaka. Yaani atoke kazini halafu asikute chakula! Hapa nimeshamfulia kabisa na
kumwandalia chumba cha wageni.” “Ndio maana James anakupenda! Unamfikiria sana
kaka yako.” “Sio kama yeye anavyonifikiria mimi. Kaka ananipenda sana. Bila
yeye nina uhakika nisingekuwa hapa.” Nanaa aliongeza na kumgeukia Fili
aliyekuwa kimya.
“Mbona Fili wangu leo hana raha?” “Danny
amemchapa mwanangu! Yaani alikuwa akilia njia nzima! Amenyamaza tu hapo nje
kwenu. Ilibidi nikae naye atulie kwanza ndio tuingie ndani. Nimemwambia wanaume
huwa hawalii mbele ya wachumba, akanyamaza.” Nanaa akacheka. “Jamani
Fili wangu! Pole. Kwani alifanyaje?” Fili bado alikuwa na hasira. Alikuwa
akihema kwa hasira. “Eti Fili? Tumwambie Nanaa?” Fili akatingisha
kichwa kukataa huku anataka kuanza kulia tena. “Basi Fili. Nyamaza mtoto
mzuri.” Nanaa alimbeba.
“Twende tuwahi. Nimemuacha Danny nyumbani. Leo
hakwenda kazini. Nikusaidie kubeba nini?” “Wewe rudi na Fili tu kwenye gari.
Nitaleta tu.” “Unauhakika?” “Sio vitu vingi. Nenda tu umfanye Fili wangu
atulie.” Grace alitaka kutoka na mtoto wake lakini Nanaa akamuwahi. “Grace!” Nanaa
akamwita. “Nashukuru kwa kukubali kunihifadhi. Nitajitahidi kutafuta
sehemu ya kuishi kwa haraka.” “Wala usijali. Sisi wenyewe pale tunahifadhiwa na
Geb.” “Geb! Geb mdogo wako!?” Nanaa alishituka mpaka usoni
akaonyesha. Hakujua kama pale ni nyumbani kwa Geb.
Historia Ya
Geb, Grace & Danny.
G |
race
akacheka baada yakuona ule mshangao usoni kwa Nanaa. Ikabidi arudi kukaa kwenye
kochi, akampakata na kumkumbatia mtoto wake. “Unajua Nanaa, maisha ni kitu
cha ajabu sana. Lakini unatakiwa usikate tamaa.” Nanaa alirudi kukaa na
yeye. “Wapo wenye wazazi wote na bado wanataabika maishani. Sisi tulizaliwa
kama watoto wa nje ya ndoa tu. Mama alizaa na mume wa mtu. Lakini yule baba
hakukataa kututunza. Kwanza tunafanana naye mno. Haya macho unayaona kwangu
mimi na Geb, ndivyo alivyokuwa baba yetu. Vile unavyomuona Geb, kila kitu
anafanana na baba. Mama anasema mpaka anavyokaa, anavyofikiria, jinsi alivyo,
mpaka anavyotembea ni baba mtupu. Ni kama alivyokuwa baba. Kwa hiyo hapakuwa na
jinsi yakutukataa. Alitutunza mpaka tulipofika kidato cha kwanza,
akafariki.” Nanaa alikuwa ametulia kabisa akisikiliza.
“Alimjengea mama nyumba huko maeneo ya Kibamba.
Tukawa tukiishi hapo mpaka kifo chake. Hata baada ya kufariki, watu walitaka
kutunyang’anya lakini baba akawa ameacha barua kwa watu wamuhimu, akisihi vitu
vile aachiwe mama. Baada ya purukushani nyingi, huku mama akilaumiwa kuwa aliiba
mume wa mtu, akashinda kesi, maisha yakaendelea.” Grace akatulia kidogo
kama anayetafuta pumzi. Kwa asili alikuwa mvivu wa kuongea. Nanaa akahisi kama
amemaliza. “Lakini mbona ndio kama ameanza!” Nanaa akajiuliza.
“Nikuletee maji ya kunywa?” “Nipo sawa tu.
Asante.” Akaendelea. “Kwa asili Geb anaakili sana ya mahesabu au
akili za mambo ya sayansi tofauti na mimi. Mimi nilisomea mambo ya lugha,
mwenzangu akachukua sayansi. Tukafaulu kwenda kidato cha kwanza. Yeye akaenda
shule ya bweni Iliboru, mimi mama akataka nibaki naye nyumbani nikasomea
Jagwani sekondari. Tulipomaliza kidato cha nne, mwenzangu akachaguliwa kusomea
PCM, mimi HGL. Geb akapata msichana tuliyekuwa tukisoma naye sisi shule moja.
Alikuwa akiitwa Frida.” Grace akaendelea.
“Geb ni mpole sana na anajua kupenda kupita
nitakavyo kwambia. Mama akamkataza yale mahusiano, na kumwambia itamuathiri
masomo yake, lakini Geb hakusikia. Wakaendelea, Geb akamaliza kidato cha 6,
akachaguliwa chuo kikuu cha Mlimani kusomea mambo ya Eletronics. Akajikuta tena
yupo na kina Danny na James, au tuseme lile kundi ulilolikuta pale siku ya
birthday ya Fili.” Nanaa akacheka kwa aibu. Akakumbuka mkasa wake na Jeff
mbele yao.
“Utawazoea tu. Wachokozi sana. Mimi mwenyewe huwa
wananichokoza mpaka leo.” Nanaa akacheka. “Vituko vyao haviishi kwa
kuwa ni kama wamekua pamoja. Kuanzia wapo kidato cha kwanza walipokuwa Iliboru
mpaka leo. Sasa mimi na yule msichana wa Geb, Frida, pia tukapangiwa chuo kikuu
cha Mlimani. Tulipoingia tu pale chuoni, tukiwa wote mwaka wa kwanza yule
msichana akaanza kumsumbua sana Geb. Kalikuwa kadada karembo kwa kweli. Akaanza
fujo. Mara awe na mwanaume huyu, mara afumaniwe, ikawa fujo tupu. Geb naye akawa
amempenda yule msichana kupita maelezo. Akimuomba tu msamaha, Geb anasamehe,
wanaendelea. Shule ikaanza kumuia ngumu, Geb. Akawa kama amechanganyikiwa na
yule binti. Mitihani ya kuingia mwaka wa pili, Geb alifeli mitihani yote
kabisa. Nikikwambia yote, namaanisha yote na wakati aliingia pale chuoni na
Division 1, ya “A” tupu.” Nanaa alikaa vizuri.
“Mama akaanza kuzungumza naye, kumfanya atulie.
Mungu akabariki, akatulia, akamkubalia mama kurudi tena shule. Akaanza kutafuta
tena chuo kingine kwa kutumia tena matokeo yake ya kidato cha 6. Mungu
akasaidia, akapata chuo mwaka huohuo nchini India. Akaamua kwenda kusomea mambo
hayo hayo ya Electronics. Sasa hapo baba hatuna, mama ndio tunayemtegemea kwa
kila kitu. Na yeye mwenyewe mama kipato chake hakikuwa kikubwa chakuweza
kumsomesha Geb nje ya nchi. Alikuwa na duka anauza yogurt na maziwa kidogo.
Halafu akaendeleza biashara ya kufuga kuku aliyokuwa akifanya tangia baba yupo
hai. Alikuwa akiuza, lakini sio kwa kiwango cha juu. Kwa hiyo hata pesa
tuliyokuwa nayo, ilikuwa ya kawaida tu.” Grace akaendelea.
“Lakini mama akawa amekusudia Geb
lazima asome. Kufupisha habari, ilimlazimu mama kuuza lile shamba, ng’ombe wote
aliokuwa ameachiwa urithi na baba. Akauza na ile nyumba ya urithi pia,
ili kupata pesa yakumfanya Geb amalize hiyo shule. Ukweli mambo yakatubadilikia
sana. Maisha yakawa magumu. Ilitulazimu kuhamia kwenye chumba kimoja na sebule,
ili mama aweze kubana matumizi ili Geb amalize shule yake. Mimi nilikuwa
nalipiwa na serikali. Kwa hiyo ikawa ni kazi ya kumsaidia Geb tu.” Grace akacheka
kidogo.
“Vipi?” Nanaa akahoji. “Nakumbuka yale
maisha. Yaani ilikuwa Geb akiwa likizo akirudi hapa nchini, anakuja hapo
tunaishi naye. Tukawa tunaishi humo kwenye hicho chumba kimoja na mama. Mama
yetu ni muhangaikaji sana, akikwambia kitu hakiwezekani, ujue ni kweli amefika
mwisho. Akawa anamtumia pesa Geb. Kila pesa anayotaka Geb, bila kuuliza, mama
akawa anamtumia. Sasa hatujui Geb alikuwa akifanyaje huko chuoni, lakini
alirudi baada ya mika 4, ana shahada mbili tena zote ni nzuri zakueleweka.
Maisha yakaendelea hapo kwenye hicho chumba kimoja na sebule, tena uswahilini
tu. Mimi nikawa nimepata kijikazi cha kawaida sana, kinachotusaidia wote pale
nyumbani, huku Geb akitafuta kazi, na mama anahangaika kivyake. Hatukuhama pale
tunapoishi. Tukaendelea kuishi hapo mpaka Mungu alipomsaidia Geb akapata kazi
BOT.” Nanaa alizidi kushangaa.
“Nikikwambia ni Mungu, ujue na amini kuwa ni
Mungu tu. Hatukuwa tunamfahamu mtu yeyote huko BOT. Aliona tu tangazo, akatuma
maombi kama kujaribu. Wakampigia simu kumuita kwenye usahili. Nakumbuka siku
anakwenda, mama akamshika mikono, akamuombea. Basi akaenda. Kwenda kufanyiwa
usahili, wakampenda. Mwaka wa kwanza tu wa Geb kuanza kazi hapo, ndipo maisha
yakaanza kubadilika. Turudi kwa Danny.” Grace akacheka.
Nanaa naye akaelewa. Mumewe alikuwa mtundu
sana. “Katikati ya hizo shida zote hizo, Danny naye akawa ananisumbua kweli
anataka kunioa. Kazi hana, na hataki kutafuta kazi, anataka arudi shule. Nikawa
namkwepa. Lakini kama unavyomjua Danny, hakwepeki. Yaani pale kwenye ile nyumba
ya kupanga, kila mtu alikuwa anatufahamu mimi na Danny. Alikuwa anakuja pale,
ananibembeleza na maneno yake hayaishi.” Nana alianza kucheka.
“Mama akawa anamwambia kwa nini asimalize shule
ndio arudi tena? Hataki. Anasema yeye anawajua vijana wa mjini, watamzidi
mahesabu. Anataka vyote viende pamoja. Anioe na andelee na shule. Yaani Danny
nyie! Hapo anafanya fujo zote hizo, hana hata mahari!” Nanaa alikuwa akicheka
mpaka basi.
“Sasa wale wapangaji wakawa wanamuuliza, anataka
kumuoa Grace wakati mahari hana wala hana pakuniweka? Akawa anawaambia yeye
atanioa tu, halafu mama aendelee kunitunza.” Nanaa alizidi kucheka. “Yaani
wewe muone Danny vile vile. Watu wakawa wanamwambia huo sio utaratibu. Ukioa
unatakiwa umchukue mke wako. Ujue Danny hana aibu nyie jamani!” Grace
alianza kucheka kila akimkumbuka Danny. “Ikawaje sasa?” Nanaa
akauliza.
“Mmh! Kwanza namshangaa anavyomwambia mwanae
akioa asimlete mkewe hapo nyumbani. Ujue Danny alining’ang’ania mpaka ikabidi
nikubali tu. Yaani alikuwa anatoka shule, anakuja kunisubiri nyumbani. Sasa na
mimi nilikuwa nikijua yupo nyumbani nilikuwa najificha. Alikuwa haondoki mpaka
anione. Na hapo fujo hizo alizianzia tokea tupo chuo. Kila mtu alikuwa
anatufahamu mimi na Danny! Nikimwambia simtaki, anaweza kupiga magoti eti hata
cafteria mbele za watu, eti ananibembeleza!” Nanaa alizidi kucheka.
“Wewe muulize James vituko vya Danny na mimi.
Tuliacha historia pale chuoni. Kila ninavyomkataa ndivyo alivyokuwa
akijitangazia mimi ni mke wake. Basi kwa kifupi ndani ya shida zote za kuishi
chumba kimoja, pesa zote zikienda kwa Geb, Danny naye akahamia hapo hapo
nyumbani akawa analala kwenye makochi na Geb. Geb akiwa shuleni, yeye ndio
anarithi yale makochi. Hapo wala hajakaribishwa wala hatuna mahusiano.
Anajikaribisha mwenyewe. Mimi na mama tulikuwa tunamshangaa yupo ndani, maisha
yake yanaendelea kama kawaida, yaani yupo kama kwao! Upande mwingine alikuwa
rafiki wa Geb, upande mwingine alikuwa anasema haondoki hapo mpaka anioe. Mama
anamuuliza akinioa ataniweka wapi? Akawa anamwambia mama bila aibu wala
hofu, eti akinioa tutaendelea kuishi hapo hapo.” “Haiwezekani!?” Nanaa
alikuwa anacheka haamini.
“Wewe muone Danny vile vile. Akili zake
anazijua yeye mwenyewe. Na si unakumbuka ile timu ya wale wanaume pale?” Nanaa
akaitikia. “Basi wote walishawahi kuishi hapo kwenye kile chumba.”
“Haiwezekani!? Mliishije?” “Wala sijui Nanaa! Na Danny ndiye aliyekuwa
akiwakaribisha hapo wasome. Eti hawezi kusoma mbali na mimi.” Nanaa
alizidi kucheka.
“Basi, baada ya purukushani nyingi, tukaoana na
Danny bila hata kulipa mahari wala sehemu ya kuishi. Tena hapo ukumbuke mimi
nilikuwa ndio nimemaliza shahada yangu ya kwanza ya miaka mitatu, yeye
anajiandaa kwenda kusomea shahada yake ya pili, chuo kikuu cha Mlimani. Yaani
ni kama mwanafunzi tu. Maana ukumbuke pia nilimuacha anamalizia mwaka wake wa
4. Yaani mwanafunzi asiye na mbele wala nyuma, wakati hapo nilikuwa natongozwa
na watu wenye magari yao na maisha yakueleweka. Halafu alichokuwa akinikera
zaidi ni vile ambavyo shule yake haiishi, ni shida tupu! Mipango mingii kama
mwanae Fili.” Wote walicheka.
“Haya, turudi kwa Geb. Si nilikwambia alipata
kazi BOT?” “Ndiyo” “Basi, baada ya muda akaanza kuingiza pesa nzuri.
Mimi nikashindwa kazi kwa kuwa nilishika mimba ya Fili nikawa mgonjwa kweli
kweli, nikafukuzwa kazi. Tukarudi sifuri mimi na Danny wangu. Danny anasoma,
mimi nipo nyumbani. Geb anaakili sana. Akaanza kufanya biashara na kazi. Hata
ile kampuni ninayoiendesha sasa hivi ni yake.” Nanaa alizidi kushangaa.
“Alikuwa anakusanya mazao mikoani, anakuja
kuyauza huku mjini na Baressa. Alinunua lori lake, akawa anaenda vijijini
anapata mazao kwa bei nafuu, anakuja kuuza huku mjini kwa bei ya juu kidogo kupata
faida. Sasa faida ikawa kubwa kwa haraka. Kwa kuwa yeye halimi wala haangaiki.
Kazi yake ni kwenda kununua tu. Akafungua tena sehemu kubwa yakuuza mchele.
Akamuweka mama asimamie. Anachukua mchele Morogoro na Kyela, anasambaza hapa
jijini. Akaongeza lori jingine lililokuwa linaenda kufuata matunda Lushoto,
analeta Dar. Anauza pia kwa Baressa na masokoni kwa jumla. Pesa ikawa
inaingia kila kona huku anaendelea kuwekeza kwenye mazao, lakini bado anafanya
kazi yake BOT.” “Kwa hiyo mpaka sasa hivi unasema Geb anafanya kazi BOT!?” Nanaa
akauliza akionekana ni kama amechanganyikiwa kabisa.
“Anapenda sana kazi yake anayoifanya. Kwa hiyo
anafanya vyote, ndio maana namsaidia kusimamia biashara. Hivi tunavyozungumza
yupo safarini kibiashara. Akipata mwanya tu kazini kwake, anahamisha akili
kwenye biashara. Na yupo makini sana kwenye mambo yake. Ana uwezo mkubwa sana
wa kupanga mambo yake na kufanikisha.” Nanaa alizidi kushangaa.
“Mambo yalipoanza kuwa mazuri, yeye na mama
wakahahama. Wakapata nyumba ya kupanga. Mimi na Danny tukabakia pale kwenye
kile chumba chakupanga. Hapo mimi namlea Fili nipo tu nyumbani sina kazi, Danny
yupo bado shule. Sasa Geb alipoona mtoto amekuwa mkubwa kidogo, ndio akaniambia
nisitafute tena kazi, nimsadie ile biashara. Tunachukua mazao mikoani, na kusambaza
hapa jijini. Mambo yalipokuwa mazuri, akanogewa na kuanza kuuza na nchi za
jirani. Alijaribu kidogo, akapata masoko, akaanza kununua sukari kutoka Mtibwa
kwa bei nafuu, anauza nje ya nchi wakati watu wa hapa wanaingiza sukari kutoka
nje. Maajabu! Lakini anyway, ikawa faida kwetu.” Bado Nanaa alikuwa
kwenye mshangao. Geb aliyedhani anamtumikia tu dada yake na kuuza sura, siye
huyu anayesikiliza habari zake.
“Akaanza kujenga pale pale Tabata. Ndani ya mwaka
mmoja jirani yake akamwambia ameshindwa kumalizia nyumba yake, anunue. Nyumba
yenyewe ni ile nyumba tunayoishi sasa hivi. Ilikuwa imefika kwenye bati. Geb
akainunua, akamalizia kwa haraka, akahamia hapo na mama, wakati akimalizia
nyumba yake taratibu. Ile nyumba ipo kwa pembeni ya nyumba tunayoishi sasa
hivi, ni ya Geb pia. Sema alijenga ukuta mrefu sana huwezi kupaona. Walipakana
na huyu mzee aliyemuuzia hii nyumba, ndio maana alijenga ukuta mkubwa ili
wasiingiliane, akaishia kupamiliki kote.” Nanaa alipooza sura. Hakutegemea
kama Geb, ndio anapesa vile. Tayari akajua si saizi yake tena.
“Sasa turudi kwangu. Geb akawa ananifundisha ile
biashara huku anaendelea na kazi yake. Mimi ikawa inaniwia vigumu kazi na
mtoto. Wasichana wananisumbua mchana na usiku, na bado Danny yupo shuleni
siwezi kumtegemea. Ikawa ni kazi yakupokezana kumlea Fili. Mara tusikie msichana
anamtesa mtoto, Geb anaenda kumchukua anakaa naye kidogo, mara anampeleka
kazini kwa mama, mara mimi. Ikawa fujo isiyoeleweka, ndio Geb akasema kwa kuwa
tunalipia pale walipotuacha. Halafu chumba chenyewe ni kimoja tu ndio
tunatumia, ni heri tuhamie kuishi naye pale iwe rahisi kumlea yule mtoto kwa
pamoja. Ndio tena tukahamia pale wote, na Danny wangu nyuma.” Nanaa
akacheka.
“Anafujo nyie Danny! Usimuone vile. Lakini mama
anampenda Danny, kama nini sijui! Akikaa kidogo tu anamuulizia Danny. Anampenda
kupita kiasi, sijui anampendeaga nini! Sijui ni kule kumdanganya danganya?
Haishiwi maneno ya kuongea na watu.” Nanaa alizidi kucheka.
“Haya, Geb akatupa gari moja, ndio tukawa
tunatumia. Mungu bariki wametuvumilia, mpaka Danny amemaliza shule yake,
amesaidiwa na James kupata hiyo kazi. Tunamshukuru Mungu analipwa pesa nzuri
sana. Tumechanganya pesa ninayolipwa na Geb, na yeye mshahara wake, ndio na
sisi tunajenga sasa hivi. Tumefika mbali, Mungu akisaidia mwakani tunahamia
kwetu. Kwa hiyo unaona? Imechukua muda mrefu, lakini kwa kuwa bado tuna
malengo, hatukati tamaa. Isingekuwa Geb, naona wote tungeaibika hapa mjini. Kwa
hiyo na sisi tunawekwa pale na Geb kama wewe tu. Fanya yako, Mungu
akikufungulia mlango, unatoka.” “Sasa mmemwambia Geb mwenyewe kama na mimi
nakuja pale? Tusijekuwa tunamlemea.” Grace akacheka.
“Cha kwanza, vile unavyomuona Geb alivyo, ndivyo
hivyo hivyo alivyo mpaka moyoni. Mkarimu sana na hana neno. Yeye ilimradi
msimtoe mama kwenye ile nyumba, basi. Hawezi kuishi popote bila mama. Na urefu
wote ule, mara nyingi analalaga kitandani kwa mama wala hatumii chumba chake.
Labda mpaka Liz aje pale.” Nanaa alicheka kidogo kwa hofu. “Amesafiri,
atarudi leo usiku. Tutamwambia tu wala usijali.” “Au labda nisubiri mpaka
mumwambie?” Nanaa alishaingiwa na hofu.
“Hana neno kabisa, usiogope. Mwenye neno ni Liz.
Liz huwa hapendi watu wengi pale ndani. Hajalalamika moja kwa moja, lakini
kwenye mazungumzo yake utamsikia akigusia jinsi anavyopenda nyumba yenye
utulivu. Nafikiri ndio kitu kinachowafanya washindwe kuendelea na Geb.
Alivyolelewa Liz, ni tofauti sana na sisi. Liz tulisoma naye mimi, kwao ana uwezo
mkubwa wa kifedha. Hata alipomaliza tu chuo, alitafutiwa kazi haraka na wazazi
wake. Hajuagi shida hata kidogo. Halafu wamezaliwa wawili tu kama sisi. Halafu
wakaishi yale maisha ya kizungu, hakuna wegazi. Kwa hiyo inamsumbua kiasi
fulani kuona Geb anajaza watu nyumbani kwake, nafikiri ndio maana hataki
kujiingiza zaidi kwa Geb. Hataki mzigo. Lakini sio Geb. Geb anaelewa maisha na
anapenda sana kusaidia. Furaha yake nikuona kila mtu anafanikiwa, na ndio maana
anaweza kuishi na kila mtu. Wala usiogope. Kwanza mama mwenyewe anakusubiri nyumbani.
Anakusifia, anasema unaonekana ni mtoto mzuri.” Nana akacheka
kidogo. “Twende. Utakuwa na Bibi Fili, usiogope.” Wakasaidiana
kuingiza mizigo kwenye gari, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Wakati wapo njiani Nanaa akiwaza maisha yake,
simu ya Zena ikaingia. “Haya ndio majaribu. Wakati nina shida, ndio
Jeff anatokea! Nikimkubali naweza kuolewa, nikapumzika na shida za kuzunguka
kwenye majumba ya watu. Nikapata kwangu.” Nanaa akawaza. Akapokea ile
simu. “Zena!” “Naamini bado hujabadili mawazo.
Jeff amefurahi sana kusikia umekubali.” “Lakini Zena, leo sio siku nzuri.”
“Nanaa! Naomba usianze.” “Kweli Zena. Nipo kwenye wakati mgumu sana.” “Basi
nakuja kwa kaka James tuongee.” “Huwezi amini Zena, ndio ninahama pale.” “Kwa
nini tena?” “Ni habari ndefu. Naomba kukusimulia wakati mwingine. Hapa ndio
nipo njiani.” Zena akashangaa sana.
“Makubwa! Sasa unahamia wapi?” “Tabata
Barakuda.” “Duuu! Shoga pole.” “Kwa kuwa bado mapema, nikiweka mambo sawa
nitakutafuta. Sitaki kukuharibia kwa Yasini. Ila nikishindwa, nakuahidi kesho
lazima tutaonana.” “Sawa kipenzi. Nashukuru kwa hilo. Maana ni kweli nimempenda
Yasini. Naomba Mungu atujalie. Ananipenda.” Nanaa akacheka. “Nimemuona. Hongera Zena. Nawaombea kila la kheri. Na mimi
nitajitahidi nisikuangushe.” “Asante.” Wakakata simu. Nanaa
akanyamaza kwani Grace na yeye alikuwa kimya kama kawaida yake.
~~~~~~~~~~~~~
Alifika nyumbani kwa Geb, akakuta anasubiriwa kwa
hamu. “Karibu tukuonyeshe chumba chetu.” Bibi Fili aliongoza njia
wakati Danny akisaidia mizigo. “Kitanda chako kitakuwa kile pale, hiki
kikubwa ni changu. Maana napataga wageni hapa, wanaojua kujikaribisha wenyewe!
Unaweza ukalala peke yako, usiku mnajikuta mko wawili, tena wakati mwingine mpaka
watatu.” Nanaa akacheka, akakumbuka Grace alimwambia Geb huwa analala na
mama yeke.
“Wengine wakigombeshwa usiku, pia wanakuja
hapahapa.” Bibi Fili aliongeza, wakacheka. “Huyu bwana
huwa hatulii! Akianza fujo zake, lazima kumfukuzia huku huku kwa bibi yake.” Danny
aliongeza huku akimuangalia Fili. “Nitakuwa nikilala naye.” Nanaa
aliongeza. “Wala hutaweza. Anaanza kulala kichwani, mkiamka yuko miguuni.
Usiku kucha Danny ana kazi ya kumpanga hapo kitandani. Akichoka ndio anamuhamishia
huku kwa bibi yake.” Grace aliongeza. Waliendelea kuongea hapo hapo
chumbani huku wakicheka na kutaniana kidogo. Kilikuwa chumba kikubwa na kizuri
sana. Kisafi na kitanda cha bibi Fili kilionekana cha tofauti. Kizuri na
mashuka yake pia yalikuwa mazuri. Kilionekana cha gharama sana.
“Ngoja nikampikie. Akija hapa atakuwa na njaa
kweli.” Bibi Fili akasimama. “Si alisema anakuja usiku?” Grace
akauliza. “Kanipigia simu muda sio mrefu, kasema yupo Chalinze na njaa
inamuuma.” “Mpaka Geb alalamike njaa!” “Ujue hapo ana siku mbili hajaweka kitu
mdomoni.” Mama yake alimalizia na kusimama. Nanaa akamfuata nyuma.
“Unataka kupika nini?” Nanaa akauliza. “Wala
hutaweza kunisaidia. Geb anasumbua sana kula. Anachagua chagua kweli! Na
akiweka kitu mdomoni tu, akisikia kina ladha sio yake, hali.” Nanaa
akacheka kidogo. “Nachemsha chemsha tu, lakini hataki kuona nyanya,
kitunguu wala karoti kwenye chakula chake. Kwa hiyo lazima nisage kila kitu. Na
hataki mafuta mengi.” Mama yake aliongeza.
“Nitampikia na uji wa ulezi. Nitaweka kwenye
chupa. Halafu namchemshia ndizi na kipande cha kuku. Basi.” “Basi ngoja
niangalie ili siku nyingine nikusaidie.” Nanaa akaongeza. “Hayo ndio
maneno.” Wakaingia jikoni. Mwanzoni Nanaa alikuwa akimuogopa sana yule
mama. Alionekana mkimya kama Geb. Wakaishia kuwa kimya hapo jikoni mpaka walipo
maliza. Nanaa akasaidia kusafisha, wakatoka.
Mwenye Nyumba, Nyumbani
Kwake.
I |
lipofika
saa nane mchana, Geb akaingia. “Mama yuko wapi?” Ndio ilikuwa salamu
yake mara alipoingia tu ndani. “Nipo huku chumbani, njoo.” Nanaa
alikuwa na bibi Fili hapo chumbani. Akajiweka sawa. Akajivuta nyuma kabisa,
akatulia akiwa amejiegemeza ukutani. Geb akaingia na kujirusha kitandani kwa
mama yake. “Njaa inauma, mama.” Geb alilalamika huku amejilaza kifudi
fudi, pembeni ya mama yake amefunika uso kwenye mto. “Pole na safari.”
“Sijalala vizuri. Nimechoka. Tangia nimeondoka hapa nilikuwa nazunguka tu. Nina
usingizi.” Geb aliendelea kulalamika kama mtoto mdogo. “Sasa ndio
uamke ukale kabla hujapitiwa na usingizi hapo!” Geb akanyamaza.
Mama yake akajua atalala kama asipomsisitiza
kuamka. “Umemuona Nanaa lakini?” Geb akaruka na kukaa kama mshale.
Nanaa akacheka. “Pole na safari.” “Asante. Sikuwa nimekuona!” Wote wakacheka,
Geb akasimama na kutoka bila kuaga. Mama yake akaanza kumcheka. “Kaingia
aibu leo! Ngoja nikamsimamie ale. Anaweza kwenda kulala bila ya kula.” “Mama!” Walimsikia
Geb akiita. “Nakuja.” Mama yake akaitika na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
“Tutakuwa tukiishi na Nanaa.” Alimsikia
mama yake akizungumza na Geb wakati anakula. “Kwema?” Geb
akauliza. “Mama yake mkubwa anakuja leo na Viola. James hakutaka wamsumbue
pale.” Kimya. Geb hakujibu. Nanaa akapatwa na wasiwasi. “Lakini
James ameomba tumuhifadhi kwa muda mfupi tu wakati anamtafutia chumba chake
kabla chuo hakijafungua. Anatafuta chumba karibu na maeneo ya chuo. Amesema
akipata tu chumba, hata kesho atamuondoa hapa. Ilikuwa gafla ndio maana
hatukukwambia. Nikaona nikusubiri mpaka urudi.” Mama yake aliendelea
kujieleza kwa mwanae.
“Haina shida kabisa. Mlifanya vizuri
kuwasaidia. Hii nyumba ni kubwa, hawezi kuongeza chochote akiwepo hapa.” “Na
mimi nilifikiria hivyo hivyo. Maana tunakuwa na wasichana wakazi mpaka wawili,
na bado tunatoshea.” “Sasa kwa nini hukumpa chumba chake?” “Tumeona mpaka uje
mwenyewe.” “Mama jamani!” “Hata hivyo kile chumba kingine ambacho
nilidhani kingemfaa yeye, bado kina vitu vingi. Hapakuwa na muda wakukisafisha.
Hamna shida nikilala naye kule chumbani kwangu.” “Kesho nitamtengenezea kile
chumba, ili awe huru.” Alivyoongea vile Geb, angalau Nanaa akatulia.
“Vipi lakini safari yako?” “Mambo yameenda
vizuri. Nimepata mtu aliyeniunganisha na mkulima mwingine. Lakini ilibidi
tumfuate mbali kweli! Ndio maana sikulala vizuri. Jana niliamka asubuhi sana na
tukarudi usiku. Lakini nimefanikiwa, asante kwa kuniombea.” “Afadhali. Utukufu
ni kwa Mungu.” Mama yake akasikika na sauti ya furaha iliyojaa shukurani.
“Utakuja chumbani kwangu?” Geb akamuuliza
mama yake. “Kwani si uje tu ulale pale pale?” “Mbele ya mgeni! Njoo bwana mama.
Nataka nikusimulie kitu.” “Muongo Geb. Una habari gani kama sio unataka niwepo
tu pale ili ulale?” Geb akacheka. “Shauri yako, utapitwa!” “Huna
lolote.” “Sawa mama. Lakini sio baadaye uanze kulalamika mbona sijakwambia!” “Haya.
Nenda kaoge ukimaliza, uje uniite.” Nanaa alibaki pale pale chumbani
akiwasikiliza huku anacheka kimya kimya.
~~~~~~~~~~~~~
Maisha yamemsukumia Nanaa
mpaka ndani ya nyumba ya Geb ambaye ameanza kupata habari zake zilizomvunja
moyo. Geb si saizi yake. Anahamia nyumbani kwake akiwa tayari amejawa hofu
naye. Mtazamo wake juu ya Geb umebadilika kabisa. Geb aliyempenda alidhani ni mlala
hoi. Sasa hivi amejua Geb sio kijana wa kutumwa tumwa. Anajielewa kimaisha, na
anampenzi anayejielewa kimaisha pia. Heshima imerudi kuwa 100.
Je, ni nini kitaendelea ndani
ya nyumba hiyo?
Je, yale aliyokusudia shetani
kumtesa nayo Nanaa kwa kumtoa nyumbani kwa kaka yake kwa machozi, yatageuka kuwa mema hapo
baadaye?
Baada ya Nanaa kujua ukweli
juu ya Geb, na Jeff bado kumtaka na kuonekana amebeba suluhisho kubwa la tatizo
la maisha yake. Anauwezo wa kukata kiu yake iliyokuwa ikimfanya avulie nguo kila
mwanamme. Zena anamuhakikishia kuwa Jeff si mchezeaji. Mfano mzuri wa kuigwa
upo kwa Best friend wake, Yasini, mpenzi wa Zena. Anataka kuoa kiukweli. Si
kumchezea.
Je, Nanaa atamkubali Jeff ili
amuoe na kuepusha kutangatanga. Hasa baada yakugundua kwa hakika Geb si saizi
yake na pale kwa Geb, mpenzi wake Liz hatafurahia uwepo wake?
Usikose kusoma visa na mikasa
itakayoendelea humu.
0 Comments:
Post a Comment