Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 7. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 7.

Mawazo yakampeleka siku ya kwanza akitolewa bikra na Alex. Akakumbuka yale maumivu. Akakusanya miguu yake pamoja. Akakumbuka ule utayari baada ya kujishauri kwa muda mrefu kama amkubalie Alex au la. Alex alikuwa mkubwa kwake. Lakini wakati wote alimbembeleza wafanye mapenzi. Ili asimpoteze au akaenda kuridhishwa na mwingine, Nanaa aliyekuwa na shauku ya kutoka kwa mama yake mkubwa. Akaamua kumpa Alex bikra yake. Akamruhusu yeye ndio awe mwanaume wake wa kwanza.

Akiwa anavuja damu pale kitandani wakati Alex amekimbilia dukani kununua pedi, Nanaa aliendelea kugugumia maumivu. Kwani ni kama Alex hakuwa amemuelewa Nanaa, pale alipokuwa akimsihi afanye taratibu. “Naomba uwe mwangalifu Alex. Mwenzio sijawahi kufanya mapenzi.” Akiwa amejawa hofu, binti huyo wa sekondari alimsihi Alex aliyekuwa chuoni. Akiwa na tumaini la kuja kuolewa. Lakini Alex alimwingilia kama aliyekuwa anapambana. Na bado Nanaa alivumilia mpaka mwisho wa Alex akapiga bao. “Nilijua kwa hakika Alex anganioa! Nilijua ni wangu! Lakini aliamua kuzaa na Viola! Nina kasoro gani mbaya hivyo inayowafanya wanaume kunikimbia?” Hakukumbuka kufurahishwa kimapenzi na Alex hata mara moja! Na wakati wote Alex hakuonyesha kama anajali furaha ya Nanaa kwenye tendo hilo. Ilimradi yeye amefanikiwa, aliishia kumshukuru kwa juhudi zake.

Mawazo yakamrudisha kwa Jamal. “Jamal ndio alinionyesha ni kama alikuwa akipunguza haja zake tu, mwilini mwangu. Hapakuwa na penzi lolote pale. Hata nilipomwambia ninafahamu kuwa ana mke, hakuonyesha kujali hisia zangu. Mbona sina bahati? Ni nini wanakutana nacho huko kwenye mwili wangu kinachowachefua na kushindwa kunithamini?” Nanaa aliendelea kuwaza moyoni akijiumiza nafsi yake kwa kujitupia lawama zote yeye kama wanawake wengi wafanyavyo kunapotokea matatizo kwenye mahusiano. Mara nyingi hupenda kujitafuta kosa/tatizo wao wenyewe, hata kama aliyekosea ni mwanaume!

~~~~~~~~~~~~~~

Walikutana na foleni kubwa kwenye njia yakuingilia Tabata. Wakasimama. Ndipo Nanaa akajua wanaelekea Tabata. Alishindwa kuuliza wanaelekea Tabata ipi, kwani hakuwa amemuongelesha chochote dereva wake, tokea amfunge mkanda. “Hivi nilisema hata asante kweli?” Nanaa akajiuliza na kujishangaa. “Ustarabu ni kitu kidogo sana Nanaa jamani! Hata ‘asante’ hukusema!” Akajisuta kidogo. “Nitakuwa nimesema bwana!” Akajitetea tena nafsini mwake. “Hata kama sikusema, nani alimwambia anifuate na mgari wa ajabu? Kwanza abiria huwa hawatakiwi kufunga mkanda. Ajali ikitokea? Au kwa nini basi mikanda iliwekwa?” Nanaa aliendeleza vikao vya mashitaka, utetezi, kujisuta na mengine mengi huko kichwani mwake nakuonekana mtulivu zaidi kwa nje.

~~~~~~~~~~~~~~

Simu ya Geb ikaanza kuita. Nanaa akagutuka kutoka mawazoni, na kujiweka sawa. Alishangaa mlio unalilia kwenye spika za gari. Akatulia kidogo. “Huo sio mziki bwana! Hata kama ni ushamba sio kwa kiasi hiki! Niache kujifanya mjinga wakupita kiasi.” Akaona Geb anabonyeza kwenye kitufe kilichopo kwenye usukani wa hilo gari. “Kuna foleni kweli. Lakini tupo njiani tunakuja.” Geb aliongea. “Amejuaje aliyempigia?” Nanaa akajiuliza huku akitafuta kusoma kama kuna sehemu iliandikwa jina la mpigaji. “Mbona anazungumza naye bila mwenzie kujitambulisha? Au namba imetokea mahali ndio akajua? Lakini wapi sasa!?” Nanaa aliendelea kujiuliza asijue anaonyesha hata nje jinsi anavyochungulia.

 “Kama hutajali naomba upitie matunda sokoni. Nilimtuma Danny, amesahau.” Alikuwa ni Grace. Nanaa akatambua sauti ya bosi wake. “Lakini amemjuaje mpigaji? Maana ameanza kuongea moja kwa moja baada ya kupokea tu!” Akaongeza juhudi za makusudi kuchungulia kwa makini kwenye dashboard kuona kama kuna mahali kunaonyesha namba au jina. “Hamna shida. Tunaweza kupitia sokoni. Lakini ujue tutazidi kuchelewa. Kuna foleni kubwa kweli!” Geb alijibu. “Ni afadhali mchelewe lakini mje na hayo matunda. Fili ameshaanza kuulizia juisi yake. Nimemzungusha lakini naona anaanza kunibadilikia.” “Sawa.” Geb akajibu na kukata simu. Walikuwa wakizungumza kwa kutumia spika ya gari, kwa hiyo hata Nanaa alikuwa akiwasikiliza. Grace aliongea kwa utulivu kama Geb. “Watakuwa wanaishi wote na dada yake.” Nanaa akawaza.

“Naona twende hapo Buguruni sokoni, itakuwa karibu zaidi.” Geb alimgeukia Nanaa, macho yao yakagongana. “Sawa.” Nanaa alijibu na kukwepesha macho kwa haraka. “Lakini alijuaje aliyempigia?” Bado Nanaa aliendelea kujiuliza lakini hakutaka kujiabisha zaidi. Aliona Geb anahama upande mwingine kurudi barabarani ili kuelekea Buguruni sokoni. “Kwani huko kwao hakuna magenge wanayouza matunda!?” Nanaa akaendelea kujiuliza.

Zena Kwa Nanaa Tena.

S

imu yake ikaanza kuita. Yake haikutolea mlio kwenye spika za gari, bali kwenye kipochi chake kidogo alichokuwa amekipakata. Akaitoa ikiwa imeshakatika. Aliposoma jina la aliyempigia, akaguna kwa sauti. “Mmmh!” Geb akamtizama. Ikaanza kuita tena. “We Zena? Umekosea namba au ulitaka kunipigia mimi?” Nanaa aliuliza mara baada ya kupokea. “Nanaa naye!?” “Nini?” “Nakupigia wewe bwana. Za siku?” “Nzuri.” Nanaa akajibu, wazi alionekana bado yupo kwenye mshangao.  “Sasa mbona hata huniulizi na mimi!?” “Nipo bado kwenye mshangao Zena! Siamini kama umenipigia mimi simu!” “Hamna bwana! Nimekuwa na hamu na wewe. Ulishaanza field?” “Wewe Zena? Hebu acha kunidanganya bwana. Niambie una shida gani?” Alizungumza naye akijua walivyojawa hila kwake.

“Nakujulia hali tu shoga yangu.” “Yameanza lini? Kwani Tia ameenda wapi?” “Nanaa naye?” “Zena? Usinifanye mimi mtoto mdogo. Najua unashida. Wewe niambie tu.” “Mpaka naona aibu.” Nanaa akacheka. “Aibu ya nini sasa? Wewe niambie. Mimi nilielewa. Wala usijali.” “Mmmh Nanaa wewe! Kweli?” “Kabisa Zena. Wala usijali. Niliwaelewa kabisa wewe na Tia.” Walifika sokoni.

 Geb aliegesha gari. Akabaki ametulia. Nanaa hakuwa ameelewa ule ukimya. “Naomba usubiri kwanza Zena.” Akamgeukia Geb baada ya kubonyeza sehemu ya MUTE ili Zena upande wa pili asisikie. “Tumefika sokoni. Unaweza kunisubiri tu kwenye gari. Nitajitahidi kuwahi kurudi.” “Hutataka msaada?” Nanaa akauliza. Geb akafikiria kidogo. “Hapana. Nitarudi baada ya muda mfupi sana. Nisubiri tu.” Akashuka na kumuacha Nanaa ndani ya gari.

Akaendelea na Zena. “We Zena?” “Kwani uko wapi?” “Buguruni sokoni. Kwani vipi?” Nanaa akauliza. “Kwanza nikuombe radhi shoga yangu. Nilikukosea.” Nanaa akacheka. “Mbona kama huamini?” “Nakusikiliza.” “Umenisamehe?” “Wewe Zena? Nimekwambia nilielewa. Mbona kama nahisi shida yako ni kubwa sana? Unanianzia mbalii!” “Wala sio uongo shoga yangu. Nimepata mwanaume.” Nanaa akaanza kucheka.

“Usicheke bwana. Sasa Tia yupo mbali. Jamaa mwenyewe anaonekana yupo vizuri. Natamani anioe.” “Hongera Zena.” Nanaa alimpongeza mwenzie bila hila. “Lakini nataka uje leo tutoke wote. Na yeye akiwepo. Kisha kwenye mazungumzo yetu, nitagusia maswala ya ndoa kwa ujumla, halafu wewe naomba uulize maswali kwa makini. Kama swala la kumpima na mengineyo. Sitaki kupoteza naye muda.” “Ujue una kichaa wewe Zena?” “Nisaidie shoga yangu. Mimi kama namuogopa!” “Sasa utaolewaje na mwanaume unayemuogopa? Mtazungumzaje mkisha oana? Au utataka nihamie kwenu?” Zena aliendelea kumbembeleza Nanaa, huku akimsikiliza hoja zake. Baada ya muda Geb akarudi na mifuko mingi ya matunda.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akafungua mlango wa nyuma. “Subiri kwanza Zena.” Nanaa akamuweka tena kwenye Mute na kumgeukia Geb. “Naweza kukusaidia? Naweza hata kuyapakata hapa mbele.” Nanaa aliuliza na kuendelea kutoa ushauri wake wa kizamani! Mambo ya kubeba mizigo ndani ya gari! “Haina haja. Nitayaweka tu hapa kwenye boksi kubwa, yasikuchafue wala kuchafua gari.” Geb alijibu. Akaanza kuyapanga huko nyuma ya gari kwa uangalifu huku Nanaa akimtizama akiwa amegeuka nyuma, akabaki akimtizama vile anavyoyapanga kwa makini na usafi. “Anaogopa kuchafua gari ya dada yake. Wala sio mimi.” Nanaa alijisemea moyoni.

“Labda atakuwa hana kazi ya maana, ndio maana dada yake anamtumatuma.” Nanaa aliendelea kuwaza. “Wakati mwenzake anasoma na kujiendeleza sijui yeye alikuwa wapi!? Kweli duniani watu hawafanani! Yaani hawa ni mapacha, mmoja kafanikiwa, mwingine mzurulaji! Atakuwa na kazi ya kujitengeneza kama mtoto wa kike, na kulala na kila mwanamke anayempitia. Mwanaume gani kucha zimelingana kama anafanya kazi saluni ya kutengeneza kucha! Ananukia kama mtoto wa kike! Mimi mwenyewe mwanamke lakini sinukii hivyo. Nywele utafikiri anafanya kazi kwenye saluni ya kinyozi! Ndevu zimejipanga mstari, utafikiri askari wa Uingereza! Basi kazi yake itakuwa ndio hiyo tu. Kujitengeneza na kuzunguka na gari ya dada yake. Na macho hayo, wanawake watakuwa wanapangwa mstari mpaka wanachoka.” Nanaa aliendelea kuwaza huku akimwangalia Geb aliyekuwa ameinama nyuma ya gari akiendelea kupanga matunda.

~~~~~~~~~~~~~~~

“We Nanaa!? Akamsikia Zena akiita. Akakumbuka kama amemsahau shoga yake kwenye simu. “Zena?” “Uko wapi wewe!? Mbona sikuelewi?” “Nimekwambia nipo Buguruni sokoni.” “Mbona patulivu hivyo? Soko hilo soko gani!?” “Nipo ndani ya gari na wewe.” Zena akaanza kucheka. “Siku hizi shoga yangu umepata bwana mwenye gari lenye AC?” “Leta dharau zako, uone kama nitakusaidia.” Geb akafungua sehemu nyingine kwenye boksi, palepale nyuma ya gari alipokuwepo akatoka na chupa mbili za maji. Akarudi ndani ya gari, akafungua ile chupa ya maji, akamkabidhi Nanaa. “Naona jua kali sana. Karibu maji.” “Asante.” Nanaa alishukuru akapokea yale maji yaliyokuwa baridi. “Karibu.” Geb naye akajibu.

“Asante ya nini na wewe Nanaa?” Zena akauliza. “Siongei na wewe!” Geb akakunja uso. “Sio wewe. Samahani ni...” Nanaa aliongea huku akinyoosha kidole kwenye simu. Geb akaelewa. “Nani? Uko na nani wewe Nanaa?” Zena aliendelea kudadisi upande wa pili wa simu. “Nimesahau kuikausha hiyo chupa. Chukua hii napkins itakusaidia kuikausha hiyo chupa, usilowe.” “Asante.” Baadhi ya matone kutoka kwenye chupa aliyopewa ya maji ya kunywa, yalishaanza kumdondekea Nanaa. Akapokea zile napkins. Geb akafunga mkanda, akaondoa gari.

“Mbona unasena asante kila mara? Umepata bwana mwanajeshi nini? Naona nidhamu imeongezeaka!” “Zena! Naomba nikupigie simu baadaye.” “Nanaa wewe! Tafadhali shoga yangu.” “Si umtafute Tia?” “Tia yuko mbali na ameshaanza field. Hawezi kuja.” “Nitakufikiria.” “Acha kunifanyia hivyo Nanaa. Kwanza Terry anakutafuta.” “Mmmh! Mimi ndio wakula makombo?” Nanaa aliuliza. “Sio makombo. Terry alinikataa kabisa. Anakutaka wewe.” “Naona umesahau shida yako wewe.” “Basi. Naacha habari za Terry. Njoo basi leo nyumbani tuzungumze.” “Kuna mahali nakwenda jioni.” “Mbona sasa hivi mapema tu. Njoo kabla hujakwenda huko. Tupange mambo yetu vizuri. Tena ana best yake na yeye hajaoa. Ukikubali tutoke wote, nitamwambia aje naye. Mambo yao safi. Siwezi kukuunganisha kwa wanafunzi kama kina Terry.” Nanaa akacheka.

“Akikusikia Tia.” Zena na yeye akacheka. “Hawana hela bwana. Kutwa chips mayai! Mtoko huu ni wa uhakika shoga yangu. Tutaenda kwenye mahoteli makubwa ya maana. Usijivunge. Au ushapata bwana?” “Wapi? Nipo tu.” “Basi njoo nyumbani tuzungumze vizuri. Lazima kieleweke.” “Ntakuja baadaye.” “Ndio maana nakupenda.” “Acha kunidanganya. Nitakuwa siji!” “Nanaa naye!” Nanaa akacheka kidogo. “Haya Zena. Nashukuru kunikumbuka. Nitakuona baadaye.” Alimsikia Zena akipiga kelele za kushangilia. Nanaa akacheka na kukata simu.

Alibaki na tabasamu usoni. Gafla akakumbuka mazungumzo yake na Zena. Tabia yake yakumuunganisha na wanaume. “Mungu wangu! Sijui amenielewa huyu?” Nanaa akawaza. Akaamua kumtumia ujumbe Zena baada ya kufikiria tena kidogo. ‘Sina uhakika kama umenielewa vizuri Zena. Naomba usiniunganishe na yeyote, yule. Hata aweje. Bado nipo mapumzikoni. Naomba nikusaidie ishu yako tu, basi. Sitaki mwanaume kwa sasa.’ ‘Nanaa naye!’ ‘Kweli tena Zena. Tafadhali sana. Nimeamua hivyo na naomba ibaki hivyo. Nitakuja kwa ajili yako, basi.” “Lakini…” Wakaendelea kujibizana mpaka wakawekana sawa. Baada ya majibizano hayo ya jumbe na kuridhika kuwa Zena ameelewa, hatamtafutia mwanaume, akarudisha simu yake kwenye pochi. Alishangaa kuona wamesimama mbele ya geti kubwa tu. Akajua wamefika.

Akajua ameongea na Zena kwa muda mrefu, au hawakuwa wakikaa mbali na hapo sokoni. Labda maeneo ya Tabata ya mwanzoni! Pia hakuuliza. Geti likafunguliwa, wakaingia ndani. Nyumba ilionekana bado mpya. Kulimwagwa vitofali vizuri. Kuanzia getini mpaka mlangoni. Baiskeli ndogo ilikuwa pembeni, akajua itakuwa ya Fili tu.

Kwa Mara Ya Kwanza, Nanaa Nyumbani Kwa Bosi Wake.

“Karibu.” Nanaa alifungua mkanda. “Asante. Nikusaidie nini?” “Nisubiri tu twende wote ndani. Nitabeba tu mwenyewe, sio vitu vingi.” Geb alitoa boksi zima. Lilikuwa ni boksi la plastiki, lenye mishikio miwili. Lilionekana ni maalumu kwa kubebea vitu kama hivyo. Akafunga mlango akamkaribisha ndani. Wakaongozana mpaka ndani sebuleni.

“Karibu Nanaa, nipo huku jikoni. Msichana wa kazi ameondoka leo asubuhi, amefiwa. Natayarisha chakula cha mchana, tukishakula ndio tuanze kufunga zawadi.” Nanaa akamfuata Geb huko jikoni kulikosikika sauti ya Grace. “Asante na pole kwa shuguli.” Nanaa akaingia. “Asante mwaya.” Grace alijibu na tabasamu. “Mama yuko wapi?” Geb akauliza mara baada yakutua mzigo. “Alikuwa anasinzia hapa, Fili amempa nyanya, kala nusu, nusu amekufunikia hapo kwenye meza. Ameniambia ukija uile.” Grace aljibu, Geb alinawa mkono akasogelea hiyo sahani. “Halafu nimempatia maparachichi.” “Atafurahi kweli. Alikuwa ananiambia anahamu nayo.” “Tena nimepata yale mazuri anayopenda.” Geb aliendelea kukila kile kipande cha nyanya huku akiongea na dada yake.

“Fili yuko wapi?” Nanaa akauliza. “Yupo na bibi yake huko chumbani. Na anavyopenda kuongea mwanangu yule, sijui kama mama atakuwa ameweza kulala!” Nanaa akacheka. “Ngoja nikamwangalie mama. Nitakuja kukusaidia kutengeneza juisi.” Geb alitaka kutoka. “Ungenielekeza tu mimi, nitatengeneza.” Nanaa akamuwahi kabla hajatoka. “Anza basi kuosha matunda mawili mawili kutoka kwenye hilo boksi. Nikirudi nitakutolea tangawizi na Blenda, nikuonyeshe tunavyosaga. Ni rahisi tu.” Geb alitoka akamuacha Nanaa anaanza kuosha matunda.

 “Pole.” “Nimeshazoea. Wasichana huwa hawakai hapa kwangu, sijui kwa nini! Mwanzoni nilifikiria wanalemewa na kazi, tukawa tunawasaidia, lakini wapi. Nikafikiri ni sababu ya Fili.” “Kwa nini Fili!?” “Mtoto ni mtundu huyo, hujawahi kuona. Yupo kama baba yake. Akianza kuongea mpaka kichwa kinauma na anataka umsikilize. Nahisi ndio maana wanatukimbia, wanachoka! Nikataka kumuanzisha shule mapema ili niwe natoka naye asubuhi na kurudi naye jioni, ili kuwafanya wasichana wa kazi wasitukimbie, lakini Danny hataki aanze shule kabla yakufikisha miaka 5. Kwa hiyo wasichana wa kazi wakitukimbia, inabidi wote tupeane zamu ya kubaki naye hapa. Lakini bibi yake ndio huwa anakuwa naye zaidi, kwa kuwa hachoki.” Nanaa akacheka.

“Kweli tena. Bibi yake anatabia kama za Geb. Huwa hawachoshwi na kelele nyingi, wanawezana naye. Kwa hiyo muda mwingi hata tukiwa na mfanyakazi, bibi yake huwa anachelewa kwenda kwenye shuguli zake. Anamuhudumia Fili. Anahakikisha amemuogesha, anamuacha amekula ndio anaondoka, ili msichana wa kazi asiwe anahusiki sana na mtoto, nayo pia haikusaidia!” “Poleni.” Nanaa akaona ampe pole tu.

“Haya na anko wake pia akaanza kazi ya kufua nguo zote. Mara mbili kwa juma. Tena wakati mwingine akiona nguo nyingi anafua mpaka usiku na kukunja nguo zote, anampangia Fili kabatini kwake, na mimi nakuwa napika chakula cha usiku mara nyingi, ili tu kumpunguzia msichana wa kazi majukumu, lakini pia naona hawakai. Sasa sijui itakuaje, lakini kwa kuwa ametimiza miaka mitano, ni heri aanze tu shule, nitachanganyikiwa bure.” “Pole. Na Danny?” Nanaa aliuliza baada yakuona dad mtoto hayupo kwenye ratiba ya ulezi.

“Huyo sitaki akae na mwanangu siku nzima. Mwanangu anakuwa hana raha! Mkali sana kwa Fili. Anamlea kama mtu mzima bwana! Hapana. Yaani nikimuacha mwanangu na Danny hata masaa mawili tu, tumbo linauma! Kila saa nampigia simu au naomba Geb arudi aje awaangalie. Najikuta kazi zenyewe zilizonipeleka ofisini sifanyi, nina kazi yakumpigia simu Danny, kumkumbusha umri wa Fili. Ndio tumeona tuache kumpa yeye hiyo kazi ya ulezi tubaki nayo sisi tu.” Nanaa alikuwa akicheka sana.

 Geb alirudi akiwa amembeba Fili mabegani. “Usimuweke hapo juu bwana! Ataanguka. Si unamjua hawezi kutulia?” “Nimemtoa kule kwa mama ili apumzike kidogo. Anaruka ruka tu kitandani mama hawezi kulala.” “Tulia basi kidogo Fili mwanangu. Huchoki? Au nimpigie simu dad arudi aje akuchukue?” “Hapana mama. Natulia” “Basi tulia. Tumalize kazi haraka ili tuwahi kwenye birthday yako.” Tayari Grace alionekana kulemewa. Alishika hiki na kuacha nusu.

“Mwache bwana. Mimi si nipo? Hawezi kuanguka. Haya nenda kamsalimie Nanaa, halafu uje ukae hapa kwenye meza.” Alienda kusimama mbele ya Nanaa akabaki akimtizama huku anacheka. “Anajua kuchanganyikiwa vibaya huyu! Sasa unacheka nini badala usalimie?” Mama yake alidakia huku akiendelea na shuguli zake. “Hapo anataka uiname, akubusu.” Geb aliongeza, wakacheka. Fili alienda kuvuta kiti mpaka karibu ya Nanaa, akapanda na kumfikia Nanaa. “Ningeinama tu.” Nanaa akacheka. “Uiname umpunguzie shuguli? Anapenda shuguli huyo!” Grace aliongeza. Fili akambusu shavuni kisha akamkumbatia. “Asante Fili.” Nanaa alishukuru na tabasamu la aibu usoni. Hakuzoea.

“Karibu. Umekuja kuishi na mimi?” Fili akauliza. “Nitakuchukua twende tukaishi wote kwangu.” “Afadhali. Umchukue moja kwa moja. Lakini James anaweza kumrudisha usiku huyo.” Grace aliongeza na kufanya Nanaa acheke. “Wewe ndio uje uishi hapa kwetu.” Fili aliongeza. “Kwa nini?” “Dad amesema nisubiri mpaka nisome, nipate mahela mengiiiii.” Fili alionyesha ukubwa wa pesa anazotakiwa awe nazo kwa kupanua vimikono vyake. “Halafu ndio amesema nikishapata pesa niende kwa anko James, tumlipe hela, nikuchukue. Lakini amesema nikikuchukua nisirudi hapa, nikupeleke kwangu.” Walicheka sana.

“Yaani Danny jamani!” Grace akalalamika akicheka. “Lakini wewe ukija hapa sasa hivi, usimwambie kama mimi ndio nimekwambia uje tuishi wote hapa. Wewe umwambie umeamua kuja kuishi hapa na mimi, wala sijakuita. Halafu hawezi kukufukuza.” Fili aliongeza na kuwafanya wote wazidi kucheka, Geb alikuwa akitingisha kichwa. “Hapa kazi ipo! Akili ya ujanja ujanja kama baba yake. Wewe? Tulikwambia nini juu ya kusema uongo?” “Hapo anko nitakuwa mimi sijadanganya. Nanaa atakuwa ndio amekuja hapa.” Fili alijitetea.

“Kwa hiyo unamfundisha Nanaa kusema uongo?” “Hapana anko.” “Na hapo pia unasema uongo. Si umemfundisha aje hapa asikutaje kwa dad wako kama wewe ndio umemkaribisha?” Fili alinyamaza kidogo kisha akauliza. “Kwani huo ni uongo?” “Sasa je? Hakuna kusema uongo.” “Basi Nanaa. Usiseme tena. Samahani anko.” “Haya, nenda kacheze, usubiri mpaka upate hela kama alivyokwambia dad, ndio utaenda kumlipa anko James, umchukue Nanaa, umpeleke kwako sio hapa. Sawa?” Fili akapooza. “Sawa anko. Kwani utamwambia dad?” Akauliza kwa upole. “Ukirudia tena kumfundisha Nanaa kusema uongo, ndio nitamwambia.” “Mimi sirudii tena. Usimwambie dad wangu.” “Ujue nitakuwa nakusikiliza kila neno unaloongea. Usirudie tena. Haya nenda.” Alishuka kwenye kiti, akatoka.

“Afadhali umemuweza. Fili anaongea jamani! Halafu hasahau jambo kama baba yake. Hapo ataenda kumsimulia kila mtu kuwa anataka kuoa lakini dad amemwambia atafute kwanza pesa.” Wote waliendelea kucheka wakati Grace akisimulia vituko vya mwanae, Geb anatengeneza juisi. “Sasa si atarudi tena kwa bibi yake?” Nanaa aliwakumbusha, Geb akatoka kwa haraka kwenda kumtafuta, akarudi amemshika. “Alishafika chumbani kwa bibi yake nakuanza kumsimulia habari zake zisizo isha. Nimekwambia kaa hapa.” Geb akampandisha tena juu ya meza. “Msimulie Nanaa badala ya bibi.” Fili akaanza kusimulia huku akiruka ruka hapo juu ya meza.

“Utaumia Fili mwanangu! Tulia basi.” “Naweza kuruka hapa, mama. Juu mpaka chini. Muulize anko.”  Fili alimchonganisha anko wake. “Wewe Fili?” Geb alimshitua huku akimkonyeza anyamaze lakini hakunyamaza. “Namwambia ukweli mama yangu. Mwenzio anko sio muoga. Ananiruhusu nipande halafu niruke.” Nanaa alicheka sana. “Geb jamani!” Grace akalalamika. “Hawezi kuumia bwana! Huyu ni Spider man. Acha hofu.” “Usikubali awe anaruka!” “Hana neno bwana. Kwanza hapo pafupi.” Geb alitetea. Alikuwa akimruhusu kuruka kwa siri, akiona mama yake hayupo. Alikuwa akivaa nguo zake za Spieder man na kumuomba anko wake aruke kama Spider man.

 “Kwani ni lazima aruke? Tafuta mchezo mwingine. Umesikia Fili?” “Spider man lazima aruke mama.” “Hapana Fili mwanangu. Mwambie dad au anko wakutafutie kazi nyingine za Spider man, ufanye. Kuliko kuruka. Ukivunjika, mama ataumia sana.” “Basi mama yangu. Nitaruka kidogo tu.” Geb na Nanaa wakacheka. “Kwani lazima kuruka Fili? Acha tu mwanangu. Utaumia!” Mama yake alisisitiza huku akimpa juisi aliyokuwa ametengeneza Nanaa. Alimuwekea kwenye chupa yake maalumu yenye picha za Spider man, akaanza kunywa, ndio akanyamaza. Geb alimbeba na kutoka naye pale jikoni akabaki Nanaa na Grace wakimalizia usafi.

Grace alipanga chakula mezani, akamuita kila mtu aje kula. Wakati wamekaa mezani ili wale, mama yao naye akatoka chumbani. Umbile alifanana sana na Grace kama alijizaa huyo mwanamke, hata rangi alifanana na watoto wake lakini sio yale macho. Nanaa akasimama. “Nilikuwa naambiwa mchumba umefika.” Yule mama alitoa mkono na kumpa Nanaa, wote wakacheka. “Naona sasa hivi kila mtu anamfahamu Nanaa. Kila anayepiga simu, anakaribishwa kwenye birthday na kuambiwa Nanaa atakuwepo. Mwanangu amependa jamani!” Grace alidakia. Wote wakacheka. “Shikamoo mama.” Nanaa alisalimia huku akicheka. “Marahaba. Karibu sana.” Yule mama alikaa.

“Mbona sahani yako haina nyama?” Mama yao akamuuliza Geb. “Nimeshakula zote.” Geb akajibu. “Chukua na hizi zangu.” “Kula bwana mama! Nikitaka nitaongeza. Mbona bado zipo tu nyingi.” “Basi chukua hii moja.” Walibishana kwa muda, mwishowe Geb akachukua nyama kutoka kwenye sahani ya mama yake. “Hajawahi kukua huyo kwa mama. Utawazoea tu. Mama akila kitu, anataka na mwanae ale. Hata kama hayupo nyumbani, anakula nusu, nusu anamuwekea.” Grace alimwambia Nanaa, Nanaa akacheka kidogo na kuinama. “Mvivu sana wakula huyu. Usipomsisitiza kula, ndio basi tena. Hizo nyama zilizofanikiwa kuingia huko tumboni ndio kashamaliza hapo. Huo mdomo hautapitisha tena kitu kingine.” Mama yao alimtetea Geb, Nanaa alicheka tena kidogo na kuinamia sahani yake tena, akaendelea kula bila yakuongeza neno.

 “Watakuwa wanamdekeza ndio maana hataki kutoka nyumbani kwa dada yake, akaishi peke yake ajitegemee. Amenikalia kudeka!” Nanaa aliwaza. Wakala lakini hawakuwa wakizungumza sana, mpaka Danny alipoingia ndio akaanza kuongea nakuwafanya wote waanze kucheka. Kitu kidogo, Danny alikikuza, akakisimulia kwa mbwembwe nyingii na kuwafanya wote wacheke. Fili alianza kusinzia, Grace akambeba kwenda kumuogesha ili amlaze angalau apate usingizi wa mchana. Nanaa alitoa vyombo pale mezani wakisaidiana na Geb.

“Acha niwasaidie tu kusafisha. Sio vingi.” Nanaa alitaka Geb ampishe pale kwenye sinki. “Ni vyakupanga tu hapo kwenye mashine. Huwa mashine inatusaidia kuosha. Labda sufuria ndio zakuziosha. Ngoja nikuonyeshe.” Geb alisuuza kidogo, akavipanga vyote kwenye mashine iliyomtoa macho Nanaa, hakuwahi kuona mashine yakuoshea vyombo. Ili kuepuka mshangao usoni, akaamua aanze kuosha sufuria. “Sasa kwa nini wasichana wa kazi hawakai kama kuna mpaka mashine za kuoshea vyombo!” Nanaa akazidi kushangazwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Simu ya Geb iliita. Akatoa mfukoni na kupokea. “Vipi?” Aliuliza. “Nimetoka kazini, nimechoka.” Akasikia sauti ya kike upande wa pili. “Njoo upumzike hapa kwetu.” “Fili anakelele bwana!” Yule msichana akalalamika, Geb akacheka. “Ameenda kulala, hatakusumbua.” “Acha tu niende kwangu. Nipumzike, nikiamka ndio nijiandae kuja kwenye birthday yake.” “Njoo basi, angalau nikuone, Liz!” Geb akambembeleza. “Kwani una hamu na mimi?” Liz akauliza. “Si ndio maana nataka uje?” Liz alisikika akicheka. “Niache nikalale kidogo, Geb. Nimechoka. Tukitoka kwenye sherehe tutakuwa wote, mpaka utanifukuza.” “Sawa mama. Baadaye basi. Ulale unono.” Liz alisikika akicheka tena. “Asante.” Wakakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mara Grace akaingia.  “Usinge hangaika kuosha hayo masufuria, Geb angeosha tu.” “Hamna shida. Kwanza namalizia.” “Basi ukimaliza uje tukae hapo sebuleni, tupumzike kidogo. Fili amelala.” “Mbona Fili mwenyewe sio mtundu wa hivyo?” Geb na Grace wakaangaliana na kucheka. “Kweli! Nipeni mimi siku za jumamosi niwe nakaa naye.” “Kama ulikuwa unatania ujue ndio imekula kwako. Na hivi sina msichana wa kazi, jumamosi ijayo asubuhi na mapema, nakuletea kwako.” Nanaa akacheka. “Kweli tena, wewe mlete tu. Ndugu yangu ana mtoto wa kiume, yule mtoto ndio mtundu. Huwa kaka akienda nyumbani Moshi kusalimia, huwa anachoka. Anasemaga ameshaona watoto watundu, lakini pale mwisho.” “Mtoto wa Viola?” Grace akauliza na kumfanya Nanaa kushangaa kidogo.

“Kumbe unawafahamu dada zake James?” Wakacheka. “Alishawahi kufika hapa. Zamani kabla ya kupata mtoto. Alimpenda sana Geb, lakini tatizo la Geb kazubaa. Sasa hivi angekuwa na mtoto mkubwa tu na Viola.” Nanaa alitulia kidogo kama anawaza. “Tena hata Vai pia alishafika hapa. Walikuja kumtembelea kaka yao hapa Dar, James akawaleta waje watusalimie.” “Kumbe! Sikuwa nafahamu kama mnafahamiana vizuri hivyo!” “Sana tu.” Grace akaitika bila shaka. Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini. Alikausha mikono, akabaki amesimama kama aliyeduwaa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kumbukumbu za mateso ya nyumbani kwa mama yake mkubwa zilimjia. Vile Viola alivyompokonya mwanaume wake, akazaa naye, huku akipongezwa na mama yake bila kujali machungu aliyomsababishia. Alimkumbuka Alex, ahadi walizokuwa wamewekeana, majina ya watoto waliyokuwa wameamua kuwapa pindi watakapo jaliwa watoto hao. Lakini akaishia kuzaa na Viola!

Alex alifanikiwa kulipa mahari kama alivyoahidi, Viola akabaki akimsubiri amalize chuo ili wafunge ndoa, lakini walikuja kusikia Alex alioa mwanamke mwingine, kwa haraka sana, mara tu baada yakumaliza chuo chake. Ilimchukua muda mrefu kwa Nanaa kuja kurudi nyumbani kwa mama yake mkubwa, Moshi. Kila James alipokuwa akienda kusalimia, Nanaa alikataa kurudi. Alimuomba ampe kwanza muda wakupona. James alikuwa akimletea habari zote ya kinachoendelea nyumbani kwao, lakini Nanaa hakuwa akienda kusalimia na alikata mawasiliano kabisa.

Yalikuwa ni majuma machache sana yaliyopita kabla yakuanza kazi kwa Grace ndipo alipoona ni vyema kuungana na James, kwenda kusalimia nyumbani kwao. Siku alipokwenda kusalimia, alijuta. Asubuhi ya siku inayofuata baada ya kutua tu Moshi, mama yake mkubwa alimuita kutoka chumbani alipokuwa amelala na kumtaka aende hapo sebuleni kwa mazungumzo. Nanaa alivaa, akaosha uso, na kwenda kukaa alipokuwa amekaa yeye na watoto wake. Bila hata kujua linaloendelea kwenye maisha ya Nanaa ambaye hawakuwa wameonana kwa zaidi ya miezi 24, tena waliachana katika hali ya machungu, yule mama alianza kumsema sana Nanaa.

 James na baba yake walikuwa wametoka, kwa hiyo alimsema vile atakavyo. Alimsema Nanaa bila kupumzika tena akitumia maneno machafu ambayo asingethubutu kumsema mtoto wake aliyemzaa. Alimsema vile alivyonyimwa shukurani. Amefanikiwa kidogo tu na kusahau alipotoka. “Usifikiri hapo ulipo umefika mwenyewe! Hata hapo unapoishi sasa hivi ni kwa James, mtoto wangu. Tulimsomesha na kumtunza kwa jasho letu. Sasa hivi wewe usiye na shukurani ndio unafaidi jasho la mtoto wangu! Umekuwa mzigo kwenye maisha yake mpaka anashindwa kumsomesha mdogo wake, anakusomesha tu wewe mtu baki!”

“Huna shukurani kabisa! Umeondoka hapa, unashindwa hata kunijulia hali! Mwenzio anashindwa kusaidia nyumbani kwao, kwa kuwa wewe umekuwa mzigo kwake! Unajidai msomi kwa kuwa umefika chuo kikuu! Tutakuona utafika wapi.” Alimsema Nanaa mpaka aliposikia gari ya mumewe wakirudi nyumbani na James, ndipo akanyamaza na kubadilika kuwa mwema kwake kana kwamba sio yeye na kubadili mazungumzo mara James alipoingia tu ndani.

“Nanaa amemshauri Vai mrudi naye Dar na yeye akatafute shule asome.” Alimuwahi James kabla hajakaa, na tabasamu usoni. James alipoona sura ya Nanaa alijua kilichokuwa kikiendelea na kujua ule ulikuwa uongo. “Mbona baba ameniambia kuwa Vai anataka kuolewa? Sasa anasoma lini na kuolewa lini?” James akauliza huku akikaa. “Kwani mtu akiolewa hawezi kurudi shule?” “Nini kinaanza sasa?” James akauliza tena. “Vyote vinaweza kwenda kwa wakati mmoja.” Mama yake alimjibu. “Basi kama ndio hivyo akasomee kwake na mumewe amsomeshe.” James alijibu.

“Mwanaume mwenyewe hana pesa! Sijui tutaishije?” Vai aliongeza. “Nanaa twende nikakuonyeshe kitu.” James hakutaka kuingilia kabisa. Alishawazira wadogo zake. Alichukia vile mama yao anavyowakingia kifua, hata walipokuwa wakikosea, hakutaka waonywe. “Sasa utaondoka na Vai, ili aanze kujiandaa na safari?” Mama yake alirudia tena. “Hapana.” James alijibu bila hata kufikiria. Kama aliyekuwa ameshaandaa jibu tayari.

“Kwa nini!?” Mama yao aliuliza kwa mshangao na hasira. “Yaani upo radhi kumsaidia huyu mtu baki na sio mdogo wako, ambaye ni  damu yako?! Tumeshamsaidia huyo Nanaa vyakutosha. Ni wakati sasa atafute maisha yake, apishe nafasi ya wenzie wapate msaada. Kwanza bibi yako ana shida.” “Nimeshazungumza na bibi na nimeshamtumia pesa za matumizi.” “Sasa nini kinachokushinda kumchukua Vai?” James alirudi kukaa kwenye kochi.

“Unakumbuka Viola na Vai walishakuja Dar ili waishi na mimi? Unakumbuka kuwa mimi ndiye niliwarudisha? Nilikueleza sababu zote za kwa nini nawarudisha nyumbani. Nilishindwa kuishi nao. Nafasi niliyotaka kuwapa wao, sasa hivi nimempa Nanaa na anaitumia vizuri. Nanaa amekuwa msaada kwangu. Tunaheshimiana. Hawa watoto wako walinitia aibu kwa marafiki zangu, mpaka ikabidi niwafukuze. Kila mwanaume walikuwa wakimtongoza wao, mpaka waume za marafiki zangu waliwatongoza! Kama rafiki zangu wangekuwa watu wasio na ndoa za kueleweka si wangevunja ndoa zao? Na pia hawana uwezo wakufanya kazi za nyumbani kama Nanaa. Wakati naishi nao, Viola na Vai, ilinilazimu kuwatafutia msichana wa kazi wakuwahudumia wao, wakati wao wamekaa tu, wanaangalia tv, mchana na usiku. Shule walikataa, wakaishia kuniingiza hasara zakulipa ada bila wao kuhudhuria darasa hata moja. Nanaa amekubali kusoma. Anahangaika na shule, amebakiza kidogo tu amalize.” James alijieleza kwa kituo bila jazba, ili mama yake aelewe.

“Watu wanabadilika James. Dada zako wamebadilika sana.” “Basi watafute chuo hapahapa Moshi waanze kusoma. Kama baba ameshindwa kuwasomesha, mimi nitatuma hiyo pesa itakayohitajika ya ada.” “Sijashindwa kumsomesha hata mmoja wao hapo. Muulize Viola kama sijambembeleza ajikaze arudi shule. Tena nilimwambia nitamsaidia kumtafuta mtu wakumlelea mtoto wake, wakati anasoma, lakini amekataa. Ni week iliyopita tu nilimkumbusha tena, akakataa. Jana pia nilizungumza nao wote wawili kutaka warudi shule, lakini wamekataa. Sijashindwa kuwasomesha hata kidogo.” Baba yao aliingilia. “Nanaa twende.” James akasimama na kutoka nje kumsubiria Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alikumbuka yale maneno yote. Akakumbuka vile Grace naye alivyosema anawafahamu vizuri sana. Aibu na hofu ikaanza kumwingia. “Sasa sijui walimtaka mume wa Grace, Danny au wote wawili? Aibu gani hii! Kumbe muda wote nipo hapa wananiangalia tu, kumbe wanazijua habari zetu! Sijui niage niondoke?” Nanaa alibaki ameduwaa, huku Grace na Geb wakizungumza palepale jikoni, akasikia wanacheka. Akagutuka kutoka mawazoni.

 “Twende basi.” Grace alitoka pale jikoni, akamfuata nyuma, wakaenda kukaa upande wa sebuleni, Nanaa akiwa amepotelea kwenye mawazo. Zile kumbukumbu za maneno ya mama yake mkubwa zilishamuharibia utulivu wa moyoni. Akabaki kimya nakushindwa kuchangia lolote. Geb naye alitoka akaenda kukaa pale akisaidia kufunga zawadi.

Mara waliona mlango unafunguliwa. “Liz!” Geb alishangaa. “Si ulisema una usingizi?” “Nimekubali ile ofa ya kuja kulala hapa hapa. Shikamoo bibi wa Fili.” Liz alimgeukia mama yao nakusalimia. “Marahaba. Karibu.” Alijibu kwa ufupi tu mama huyo akanyamaza. “Njaa inauma, nina usingizi, sijui nifanye lipi niache lipi?” “Nilikwambia napika. Chakula tumekirudisha sasa hivi kwenye friji. Wewe nenda kale ndio ukalale.” Grace alijibu, Geb akasimama, Liz akambusu midomoni. “Twende nikusindikize ukale, ndio ulale.” Wakaondoka na Geb kuelekea jikoni, akamsikia Liz akiongea na kucheka akiwa na Geb huko huko jikoni. Akajua ni wapenzi.

“Liz! Liz!” Grace akaita kama aliyekumbuka kitu. “Nimesahau kukutambulisha kwa Nanaa. Njoo.” Liz akatoka. “Huyo ndio Nanaa.” “Mchumba wa Fili?” Liz akauliza na kuamsha kicheko. “Amemng’ang’ania! Kabla hajalala alikuwa anamfundisha Nanaa uongo wakumwambia baba yake ili ahamie hapa.” “Aje amlee?” Liz akauliza. “Naona. Maana wasichana wa kazi wote wanamkimbia. Lakini Geb akamgombesha aache uongo, naona akapooza mpaka akapata usingizi.” Wakacheka tena.

“Sasa Nanaa ujiandae. Mume yule hamna kulala sababu ya maneno mengi. Sura ya upole kama mama yake. Akikuangalia hivi na macho yake yale, utafikiri ni malaika ambaye hajaanza kuongea. Lakini ngoja afungue mdomo, ndio utajua ni mtoto wa Danny. Jana amenipigia simu ananieleza habari zako, mpaka nikapitiwa na usingizi. Mtoto hachoki! Kila nikimuaga ananiita, Anti Liz, nimekwambia Nanaa ni mzuri?’ Namwambia ulishaniambia zaidi ya mara hamsini, anasema ‘Ndio unatakiwa usisahau sasa’.” Kila mtu alikuwa akicheka. “Sasa Nanaa ujiandae. Hajuagi kuongea kwa kifupi huyo mumeo, na hachoki.” Liz alirudi jikoni, baada ya kula wakaongozana na Geb chumbani.

~~~~~~~~~~~~~~~

Japokuwa alikuwa akicheka, lakini moyoni alishakosa amani, asijue ni nini kinachomsababishia ile hali. Kama ni maneno ya kashfa aliyokumbuka kuambiwa na mama yake mkubwa, au ujio wa Liz, au aibu ya ndugu zake hapo kwa kina Geb, hakujua ni lipi, lakini moyoni alikuwa amechafuka kabisa. Alibaki kimya mpaka walipomaliza. Grace alikuwa akiongea na mama yake huku Danny akiangalia mpira.

“Naona tumemaliza mapema na bado tuna muda mwingi uliobaki wa sherehe ianze. Naomba niondoke, kuna mahali nataka nipitie kabla ya kuja huko kwenye birthday.” Nanaa aliaga baada yakumaliza. “Basi ngoja nimuite Geb akupeleke.” Grace alitaka kusimama. “Hapana. Mwache tu apumzike. Ningependa kwenda peke yangu.” Grace akacheka. “Haya Mkwe wangu. Lakini usimsaliti tu mwanangu!” Grace alirudi kukaa, akamfanya Nanaa acheke kidogo. “Wala usijali. Nitakuja kwenye sherehe, nicheze naye.” Nanaa alichukua pochi yake akamuaga mama yao na Danny aliyekuwa akishangilia mpira kwenye tv, akatoka na sononeko moyoni.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa mara ya kwanza Nanaa akiwa amekusudia kuachana na mapenzi. Akiwa ameumizwa vyakutosha, anapatwa na hisia za ajabu kwa Geb ambaye anamvutia kwa ajabu asijue ni nini! Hamfahamu Geb hata kidogo, ila kwa hakika anajua ana mpenzi wake, Liz. Liz si msichana wa vichochoroni. Anafahamika mpaka kwa mama yake Geb. Anaonekana kufahamiana na Grace vizuri tu. Na ni Anti wa Fili!

v  Nini atafanya?

v  Je, atatupilia mbali hisia hizo ngeni zinazomliza na kumuumiza moyo?

v  Nini kitatokea kwenye sherehe ya Fili?

v  Na, Je, Zena ataheshimu ombi la Nanaa?

 

Usikose Muendelezo.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment