Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 6. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 6.

 

Nanaa akajituliza mpaka mwaka huo wa pili ulipoisha. Hapakuwa na mapenzi tena. Alishakinahiwa. Jamal ndio alimchefua kabisaa. Mawazo yakawa shuleni, na Mungu akamfanikisha hapo. Hakukamatwa somo hata moja. Na yeye akawa amefaulu vizuri sana. Tena kwa alama za “A” tupu. Kwa hakika hata James akafurahi na kujisifu kwa wenzake. Lakini  Nanaa akatakiwa kwenda field kabla yakurudi chuo kumalizia mwaka wake wa mwisho.

Wapi akafanye field! Akaanza kuhangaika kutafuta maofisi ambayo angefanya field hiyo lakini angalau wamlipe pesa kidogo ya kumsaidia hata nauli na hata wakiweza kumuajiri mpaka chuo kifungue, lakini akakosa. Hapo ndipo ikambidi azungumze na kaka yake, ili amsaidie kumtafutia sehemu  yakufanya field. James akamwambia ampe muda kidogo wa kutafuta.

Baaada ya kama siku mbili akamwambia amefanikiwa kumpatia kazi mahali. Amepata ahadi ya kazi kwa muda ambao muhasibu wa hiyo ofisi atakapokuwa likizo ya uzazi. Nanaa alifurahi sana na kumshukuru Mungu wake.

~~~~~~~~~~~~~~

S

iku hiyo ya jumamosi asubuhi Nanaa alisikia watu wakicheka na kaka yake sebuleni kwao. Ndio na yeye alikuwa ameingia tu chumbani kwake baada ya kumaliza shuguli zake. Akaona atoke aangalie ni kina nani wanao mfanya kaka yake acheke hivyo. Alikuta ni mtu na mkewe. Wakitaniana sana na James. Akajua lazima watakuwa marafiki wa James. “Njoo Nanaa usalimie na uongee vizuri na Grace. Ndiye atakuwa bosi wako. Hakikisha unamuelewa usibaki unayashangaa hayo macho yake, akamaliza kuongea hujaelewa kitu.” Nanaa akamtizama Grace vizuri. Kweli alikuwa na macho yakuvutia. Akacheka.

“Usicheke mtoto wa kichaga. Tumekuja mjini kuzisaka pesa. Changamka na usipumbazwe na hayo macho na sauti hiyo, ukashindwa kuomba pesa kubwa. Maana wakati tupo pale chuo kikuu cha Mlimani, huyo Grace alizungusha vichwa vya wasomi wenye shahada zao, wafanyakazi, maprofesa,  na wafanyabiashara wa jiji. Watu wazima tukabaki kama wehu. Muulize Danny. Mimi mwenyewe nilitaka kuoa, lakini nikashindwa. Kila alipokuwa akiniangalia, maneno yalikuwa hayatoki. Mwenzangu Danny akaamua kufa kiume, lakini karibia tumkimbize Mirembe kwa kuchanganywa na Grace.” Wote walianza kucheka tena. Lakini Nanaa akawa ameshapata utambulisho wakujitosheleza. Danny ni mume wa Grace bosi wake. Marafiki wa kaka zake waliosoma pamoja.

“Achana nao hao. Wanapenda kunichokoza tu. Tutaelewana Nanaa, usiogope.” Grace alijibu huku akicheka. “Ashindwe kuelewa Danny mpaka leo, ataelewa mdogo wangu huyo? Kwanza hayo macho kwa mara ya kwanza yakikuangalia unakuwa kama unapumbaa hivi. Sasa Danny ndio alikuwa anatuchosha. Pesa hana, anamtaka Grace. Ukiangalia mgongo wa Grace, Danny alikuwa anazidi kuchanganyikiwa. Basi tukajua pakumpatia Danny. Tukitaka kumchanganya, tunamtisha, tunamwambia tumemuona Grace amepakizwa kwenye gari zuri sana, halafu huoni ndani, vioo vyeusi. Basi weee, Danny anapagawa!” James aliongeza nakuwafanya wazidi kucheka.

“Nakwambia nilipambana mpaka nikafanikiwa.” Danny akaongeza.  “Na usifikiri akikwambia alipambana anadanganya? Nilikuwa sina raha. Alikuwa ananisumbua kupita maelezo. Yaani namgombesha mbele za watu, labda asubuhi, lakini mchana utamuona huyo amerudi. Angekuwa hasomei Eletronics huyu, watu wangesema hana akili vizuri.” Grace alijibu kwa sauti yake ya upole. “Mimi nakwambia vile ulivyokuwa ukinigombesha huku unanifukuza, nilikuwa nasikia raha. Nilikuwa narudi kwa kina James nawaambia Grace ameniongelesha.” Walizidi kucheka.

“Yaani anagombeshwa, lakini yeye anasikia raha. Danny mjinga sana huyu! Yaani mpaka tulikuwa tunamuhurumia.” “Halafu sasa suruali yake ni moja tu ya jinsi. Tisheti tu ndio alikuwa anabadili. Marafiki zangu walikuwa wananicheka. Halafu alivyo sasa Danny, anakufuata mpaka kwenye lecture, mbele za watu. Eti ananijulia hali! Nilikuwa nakasirika mpaka basi.” Grace aliwafanya wazidi kucheka. “Mvumilivu hula mbivu. Huoni niliibuka mimi mshindi? Namiliki chombo mwenyewe. Nimewapiga bao watu na pesa zao.” Mumewe akajibu.

“Hawa wawili hawa, na wenzao wenye akili kama zao, walisoma sekondari pamoja. Wakachaguliwa hapo chuo kikuu cha Mlimani. Wakawa  chuo kimoja, mwaka mmoja, darasa moja, na sasa hawa wawili katika kundi lao, wanafanya kazi sehemu moja. Hawana jipya. Wananikera na macho yangu, sina raha. Huyo James kaka yako, na wenzake, walikuwa wanamsindikiza Danny kunitongaza. Basi James na wenzake walikuwa wanasimama mbali kidogo, wanatuangalia mimi na Danny tunavyoongea. Walikuwa wananiudhi kundi lao hawa! Sina hamu. Twende mwaya Nanaa tukazungumze hapo nje. Maana yule muhasibu wangu amepitisha siku za kujifungua, muda wowote ule anaweza akajifungua, nikabaki nahangaika. Ofisi yenyewe sio kubwa, lakini yeye ndiye anamajukumu mengi.” Wakatoka nje. Kuzungumza.

Grace alizungumza naye taratibu. Kwa kumsikiliza tu, Nanaa akavutiwa na bosi Grace. “Sasa upo tayari kuanza kazi lini?” Grace akauliza. “Hata kesho. Sina kitu chakufanya sasa hivi.” “Mbona wewe utanifaa! Ndio vizuri uanze mapema akuelekeze kila kitu, ili ikitokea anajifungua, tusikwame.” Nanaa akafurahi sana. Wakakubaliana mshahara, Grace na mumewe wakaondoka.

“Naona ulivyofurahi.” James alimchokoza dada yake. “Kasema atanilipa.” Nanaa alijibu huku akicheka. “Ni watu wazuri sana, hawana shida. Nina uhakika utafurahia kufanya kazi na Grace. Ni dada muungwana sana.” “Ni kweli ulitaka kumuoa? Mzuri kweli!” James akacheka. “Hapana. Huwa tunapenda kumchokoza tu. Danny, mumewe ni mtundu sana. Halafu Grace ni mpole. Wakati mwingine tunamchokoza tu ili aongee. Tokea shule huwa tunapenda vile anavyoongea kwa upole. Usipomchokoza Grace, hazungumzi hata. Atabaki kimya tu.” “Kwa hiyo Danny ni rafiki yako tokea zamani?” “Danny ni mtu wa watu sana. Alikuwa au tuseme ni  rafiki wa kila mtu. Alituunganisha marafiki tuliokuwa tukisoma pamoja tokea sekondari. Tukajikuta tuna kundi letu. Utakuja kuwaona wengine. Danny hawezi kupoteza mtu. Mmoja wetu akipotea tu, atamtafuta mpaka tujue alipo. Mwishowe tumejikuta lazima kukutana mara kwa mara. Tulipotezana kwa muda, wakati yeye alipoamua kurudi chuoni kufanya shahada ya pili. Akawa kimyaa. Alipomaliza akatukusanya tena. Ameajiriwa pale ofisini kwetu. Hata mwaka hajamaliza pale kazini, lakini kila mtu anamfahamu. Mpaka wafagizi wanamjua Danny. Kila anapopita anatengeneza marafiki anaowafanya wawe karibu yake. Mtundu sana na haishiwi maneno.” Waliendelea kuzungumza wakicheka vituko vya Danny alivyokuwa akisimulia James.

Mwanzo Mwengine Mpya.

N

anaa akaanza kazi kipindi huyo muhasibu anafunga mahesabu na kutengeneza ripoti ya mwezi. Walifanya kama siku mbili tu, Nanaa akiweka juhudi na kuuliza maswali mengi kadiri awezavyo. Akijua ile si field tu, sasa ni kama kazi. Na kama akiongeza juhudi, ni sehemu anayoweza kurudi kuomba ajira pindi atakapomaliza chuo.  Mshahara wa mwanzoni tu ulimvutia. Akajua akirudi na vyeti, basi mambo yake yatakuwa safi. Kabla huyo muhasibu hajakamilisha ripoti, na Nanaa kuona inakuaje mpaka mwisho, chupa ya uchungu ikavunjika wakiwa ofisini. Wote walifurahi kwa kuwa huyo mtoto alikuwa akisubiriwa na watu wote pale ofisini lakini sio Nanaa. Yeye alitaka waendelee kuwa naye ili amfundishe mpaka mwisho ili asije haribu, lakini ndio katikati ya mafundisho, chupa ikavunjika. Grace alimkimbiza hospitalini huku akiwa amempigia simu mumewe awafuate hospitalini. Nanaa alibaki pale hajui chakufanya.

~~~~~~~~~~~~~

Alikaa hapo mpaka jioni wakati anakaribia kufunga, akasikia sauti ya mtu akiongea nje ya ofisi yao, akiwa mapokezi.  “Sasa hivi siwezi kufanya kitu cha maana G. Nimechoka na nina mambo mengi. Akili haijatulia. Kwa nini nisije siku ya jumamosi?” Alimsikia mtu akiongea taratibu kama Grace. Lakini huyu  sauti yake ilikuwa nzito, nzuri ya kiume. Akasikia kimya kama mtu anayesikiliza upande wa pili. “Bwana wewe ni muoga tu, G. Unaweza.” “Siwezi. Wewe msaidie.” Nanaa alishitukia yule mtu amefungua mlango amemsimamia mbele ya meza yake na sauti ya Grace ikasikika kutoka kwenye simu. Moyo wa Nanaa ukapasuka. Akabaki kimya asijue kwa nini! Akabaki ameduaa.

“Labda jumamosi. Leo nitakuharibia kazi. Jumamosi akili itakuwa imetulia, au usubiri baada ya week ijayo.” Yule kaka aliendelea kuongea kwenye simu huku akivuta kitabu cha invoice mbele ya meza ya yule muhasibu, akaanza kuangalia taratibu. “Kwanza wala huna transanctions nyingi! Acha uvivu G. Fanya mwenyewe.” Waliendelea kuzungumza, Grace akisikika akimsisitiza yeye ndio afanye. “Basi nitakuja hiyo siku ya jumamosi, wewe zungumza naye muelewane. Nikifanya leo, nitamchanganya tu.” Grace aliendelea kuzungumza upande wa pili. “Sawa. Hamna shida.” Akaitikia na kukata simu, na kumuangalia Nanaa.

Nanaa hakuhitaji utambulisho, alijua wazi ni kaka yake Grace bosi wake. Walifanana sana na Grace. Macho yao yalikuwa yakifanana sana. Makubwa kiasi na yakusinzia. Aliongea kwa utulivu kama Grace, yaani haiba ya utulivu kama Grace. Mweusi na nywele nyingi zilizoonekana alifanya juhudi za makusudi kuzitengenezea mustachi mzuri kuzunguka midomo yake na usoni. Nanaa alibaki akimtizama.

“Naitwa Geb, kaka yake Grace.” Akampa Nanaa mkono na kuendelea. “Alitaka nimalizie kazi ya muhasibu wake, lakini leo nimechoka sana. Nikisema nikae hapa, nitashindwa kukuelekeza vizuri. Ingekuwa nafanya peke yangu, hapo sawa. Lakini inaonekana G, anataka nikufundishe na wewe.” “Kwani ni ngumu sana? Naweza kukuangalia wakati wewe unafanya. Huna haja yakuongea sana.” Nanaa aliuliza, yule kaka akakaa kwenye kompyuta ya yule muhasibu na kuanza kuangalia bila kujibu kwa muda.

“Huyu mwenzako nilitumia karibia mwaka mzima kumuelekeza kutengeneza hii ripoti tu. Mpaka kipindi fulani nikawa natengeneza mwenyewe. Nafikiri kama nikuweza vizuri, amefanikisha kama ripoti mbili za mwisho, nyingine zote ilikuwa lazima nizirekebishe sana. Ni kama nilikuwa nafanya mwenyewe tu.” Aliendelea kuperuzi kwenye kompyuta ya huyo muhasibu huku Nanaa amekaa meza ya pembeni isiyokuwa na kompyuta.

“Yaani mpaka hapa tu, naona nitahitaji siku nzima. Vitu vingi sana havijakamilika.” Aliendelea kuperuzi huku Nanaa akiwa kimya. “Daah! Kuko hovyo sana.” Aliendelea kuzungumza mwenyewe akiendelea kuperuzi.

Akaingia dereva wa hiyo kampuni. “Mzima bosi?” Geb alisalimia. “Kumbe mkuu mwenyewe upo hapa?” “Nipo.” Geb alijibu na kurudisha macho kwenye kompyuta. “Kama upo basi ipo neema. Maana nina mzigo hapa, natakiwa kumkabidhi muhasibu kisha anikatie kiasi.” “Usinitie matatizoni bwana. Mimi sina pesa. Na sitaki kukaa na pesa ya mtu.” Geb alijibu huku akiendelea kuangalia kompyuta kwa makini.

“Unanikatalia bure bosi wangu. Najua wewe huna shida na pesa ndogo ndogo kama hizi.” “Unamuongelea Geb wa jana, leo hali mbaya. Mpigie simu bosi wenu umuulize chakufanya.” Yule dereva aliendelea kuzungumza na Geb wakionekana kufahamiana. Kwani walitaniana kidogo, mwishowe Grace alimpigia simu Nanaa. “Pokea pesa kutoka kwa huyo dereva, kisha uumpe elfu 10. Hakikisha mnaandikishana na anaweka saini sehemu kuthibitisha amepokea hiyo pesa ya malipo yake na amekupa pesa yote ya ofisi.” “Sawa nitafanya hivyo. Kwani hutarudi tena?” Nanaa akauliza. “Nitakuwepo hapo kesho. Geb bado yupo?” “Yupo.” “Sawa. Analalamika amechoka, hawezi kukusaidia kufunga mahesabu. Anataka kuja kufanya jumamosi. Utaweza?” “Saa ngapi?” “Atakwambia mwenyewe. Hapendi kufanya kazi siku za jumamosi asubuhi asubuhi, kwa hiyo haitakuwa asubuhi sana, usiogope.” Nanaa akacheka kidogo. “Sawa.” Alimuelekeza kidogo Nanaa, wakaagana.

Yule dereva aliondoka na kumuacha Nanaa na Geb pale ofisini. Geb alipiga simu kitengo cha stoo kuomba transctions zote. “Mbona nilishatuma?” Dada aliyekuwepo kwenye kitengo hicho alijibu. “Ni sawa kama nikikuomba utume tena?” Geb aliomba kiustarabu sana. Nanaa akabaki akimwangalia kwa kujiiba. “Sawa. Nitafanya hivyo.” “Asante sana na samahani kwa usumbufu.” “Hamna shida.” Akakata simu na kusimama.

 “Nilikwambia naitwa Geb?” “Ndiyo.” “Samahani. Akili zimechoka. Sasa bosi wako ameniambia huwa hufanyi kazi siku za jumamosi. Mimi nitakuwepo hapa asubuhi ya saa nne. Ukiweza kuja kutizama ninachofanya ni sawa. Ukishindwa, nitakuelekeza wakati mwingine. Haina haraka.” “Sawa.” Geb alimtizama kwa macho yaliyomfanya Nanaa abaki ameduwaa, asijue kama aliulizwa swali na kama alijibu sahihi. Akakumbuka kaka yake alimwambia asili ya macho yale yakikuangalia kwa mara ya kwanza, hupumbaza.  

Nanaa akajiweka sawa baada ya kuona bado anamtizama. “Si umesema jumamosi utakuwa hapa, saa nne ya asubuhi?” Nanaa akauliza kama kupata uhakika. “Ndiyo. Na wewe umesema sawa. Sasa sawa hiyo nitegemee utakuja au utataka kujifunza wakati mwingine?” “Nitajitahidi kuwepo.” Nanaa akaongeza. “Basi usiku mwema. Tutaonana Mungu akipenda.” Geb akatoka. Ndipo Nanaa akapumua kwa nguvu kama aliyepata aghueni. Alihisi tokea Geb amtazame ni kama alishindwa kupumua. Akabaki anababaika. “Si kwa macho yale. Daah!” Nanaa alijiambia huku akijicheka.

~~~~~~~~~~~~~

Isivyo kawaida yake, Nanaa ambaye hakuwahi hata kumfikiria mwanaume kwa umbile, akajikuta anabaki na taswira ya Geb. Kutoka kwenye kuapa hataki tena mwanaume, lakini akajisikia shauku ya kutamani jumamosi ifike haraka akamuone tena Geb. Hiyo ilikuwa siku ya jumatano Geb alipowatembelea ofisini. “Hivi hata jina nilimtajia kweli? Sijui ameoa au ana mpenzi? Daah! Yule akikutamkia ndoa, unasamehe hata mahari.” Nanaa aliwaza wakati amejilaza kitandani kwake. Alitamani Geb arudi tena pale ofisini au ajue habari zake zaidi, lakini hakujua amuulize nani.

~~~~~~~~~~~~~

Siku ya jumamosi ilipofika, Nanaa alimka asubuhi na mapema nakuanza kujiandaa. Kila nguo siku hiyo haikumpendeza. Alivaa yakumbana, “Mmh! Ataona najirahisisha sana.” Akavua na kuvaa kubwa kidogo. “Hii hapana. Hata kiuno changu hakionekaniki! Wakati hiki ndicho kinawachanganya wengi!” Akacheka na kuvua. Alihangaika kuvua na kuvaa, mpaka akaishia kuvaa gauni la kawaida tu kwa kuwa muda ulikuwa umeisha, akaona atachelewa na kuonekanika sio msomi.

 Alitoka akiwa na haraka, akabahatisha daladala mpaka ofisini. Akakuta walinzi tu, na watu wa stoo waliokuwa wakipokea na kutoa mizigo. Aliingia ofisini kwa muhasibu akakaa akisubiri mpaka saa nne na nusu ndipo akamsikia Grace na Geb wanaingia.Walipita moja kwa moja ofisini alipo Nanaa, wakiwa na mtoto mzuri sana wakiume, mwenye macho yanayo fanana na wao. Rangi yake pia alikuwa mweusi kama wao. Nanaa akabaki akijiuliza kama ni mtoto wa Geb au Grace.

Alimsalimia Nanaa kwa heshima akabaki akimwangalia. Nana akacheka. “Wewe vipi Fili?” Grace alimuona vile alivyobaki akimkodolea macho Nanaa. Akampa ishara ainame ili amnong’oneze. Grace akacheka na kuinama kumpa sikio. Yule mtoto alimnong’oneza kitu Grace nakumfanya acheke sana. Akatoa simu na kupiga, kisha akaweka sauti kubwa.

Alipopokea tu, Grace akaanza . “James! Umepata shemeji.” “Nani?” Upande wa pili aliuliza ambaye ni James, kaka yake Nanaa. “Fili amesema Nanaa ni mchumba wake.” Wote walicheka mpaka Geb. “Kwa kuwa naonana na Danny jioni, mwambie Fili nimemkabidhi. Nitamalizana na dad hukuhuku.” Ndipo Nanaa akajua kuwa yule ni mtoto wa Grace wala si Geb. Roho ikatulia. “Labda bado hajaoa.” Nanaa akawaza kwa haraka huku akicheka.

Nanaa alikuwa akicheka kwa aibu kwani bado Grace alikuwa akicheka huku akimwangalia mwanae. Akampigia simu Danny mumewe na kumsimulia. “Mwanao anataka kumuoa Nanaa.” “Sasa huko ndiko kuingizana umasikini. Mwambie kabla hajafikiria kuoa atafute kwanza kazi, ili apate pesa ya kumlipa James ya mahari. James atataka nyumba yangu bure.” Grace aliendelea kucheka na mumewe akilalamika.

Baada ya muda Danny akamuunganisha James kwenye simu wakawa wote watatu. “Hapa nishaanza kutafuta mteja wa nyumba yangu ile mbavu za mbwa. Mahari ya Nanaa ni mjengo wako Danny.” James aliongea mara baada ya kupokea simu. “Si nilikwambia Grace? Mtoto anataka kuniingiza umasikini huyo. Mahari yenyewe si umesikia?” “Acha kumuogopesha mwanangu bwana James! Hata kwa mkopo sisi tutaoa tu.” Grace alimtetea mwanae. “Tena Grace uishie hapo hapo. Mwambie Fili kama anamtaka Nanaa, awe na pesa yake. Mtoto anataka vitu vizuri huyo! Hajui vizuri garama?” Wote walicheka. “Mpango wangu ilikuwa nimpeleke huyo Fili kijijiniii. Nikamchukulie mke kwa joo mbili tu, basi.” Danny aliongeza. Waliendelea kutaniana, huku vicheko vikiendelea. Ikabidi Grace awaage.

~~~~~~~~~~~~~

Akamgeukia Nanaa. “Huyu anaitwa Geb. Mdogo wangu.” “Kaka yako bwana!” Geb alimkatisha. “Kwa kupenda ukubwa huyu! Mimi ndio mkubwa, nimempita kwa lisaa lizima.” Ndipo Nanaa alipojua kuwa ni mapacha. “Kwani ukiniita kaka unapungua wapi, G?” “Haya. Na hivi unanisaidia, acha niwe mpole. Huyu ni Geb, anko wa Fili. Ndiye anayenisaidia mambo ya mahesabu kwenye maisha yangu yote. Usifikiri ni hapa ofisini tu.” Nanaa akacheka kidogo kama asiyesadiki. “Usifikiri nakutania. Nachukia sana hesabu, lakini yeye ni mtaalamu sana wa mambo ya mahesabu tokea watoto yeye ndio alikuwa mwalimu wangu. Halafu huwa hachoki kufundisha. Atakuelekeza mpaka wewe mwenyewe ndio utachoka. Nitakuacha naye hapa. Ukichoka wewe uondoke tu, maana yeye anaweza kulala hapahapa.” “Siwezi kulala bwana. Saa kumi jioni mwisho. Naenda mazoezini.” Geb alidakia tena huku macho yakiwa kwenye makabrasha yaliyokuwepo hapo juu ya meza.

“Haya Nanaa, kazi kwako. Mtumie vizuri kumuuliza maswali yote, ili jumatatu ukiachiwa ofisi, usipate shida.” “Sawa, asante.” Nanaa alishukuru. “Nitakuja baadaye kumchukua Fili twende wote mazoezini. Au unasemaje?” Geb alimtizama Fili, akampa 5. “Ewaa! Ujiandae na uvae kabisa ile jezi yako na viatu. Nikija tu, tunaondoka.” Wakaona Fili anababaika wala hafurahii tena kwenda mpirani na anko. “Nini?” Geb akamuuliza. “Unabaki naye?” Fili akauliza nakuwafanya wote wacheke. “Yaani huyu mtoto kama Danny!” Geb alicheka huku akitingisha kichwa. “Nanaa yupo kazini. Anatoka jioni. Ukimtaka umtafute kesho, hafanyi kazi. Sawa?” Geb alimjibu Fili. “Sawa.” Fili alijibu kwa kuridhika kwa ahadi ya kuonana na Nanaa kesho yake.

“Tutamtafuta kesho?” Wakati wanatoka walimsikia Fili akimuuliza mama yake na kumfanya Nanaa na Grace wacheke. “Wewe Nanaa umemchanganya mwanangu. Wala hakuwa hivi!” Grace aliongea huku akifungua mlango wakutoka nje ya ofisi, wakasikia wakifunga nakutoka.

~~~~~~~~~~~~~

Palipita hali ya ukimya kidogo, Geb akiendelea na shuguli zake, na Nanaa akifikiria chakufanya. “Nimeshajisahau! Naendelea bila kukuonyesha. Sogeza kiti uone jinsi ninavyokusanya kila kitu, na kupangilia mpaka kupata ripoti nzima.” Nanaa akasogeza kiti na kukaa naye meza moja, kazi ikaanza. Kulikuwa na utulivu wa namna yake pale ofisini. Mara kadhaa Geb alitaka kujua kama bado wapo pamoja au alimuacha mbali, na mara zote Nanaa alisema anaelewa.

“Kama una swali lolote, usisite kuniuliza.” Geb alimgeukia kuona kama bado Nanaa yupo au alishahama pale. Yale macho alitamani yaendelee kumuangalia kwa muda. “Naelewa.” Nanaa alijibu kwa utulivu. “Na ujue mwezi ujao hii ndio kazi utatakiwa kufanya. Kwa hiyo uelewe kweli kweli. Ukiwa na swali uliza. Usisite. Na hakuna swali dogo au kubwa. Yote ni ya msingi.” “Sawa.” Nanaa akajibu akijaribu kutulia.

Nyongo Kutumbuka Pabaya!

Waliendelea na kazi pakiwa na utulivu wa namna yake. Nanaa akifurahia kuwepo pale kwa wakati huo wala asijue ni furaha ya kuelewa kazi au ni mwalimu mwenyewe ndiye anayefurahia uwepo wake! Lakini akajisikia kutulia rohoni kwa namna yake mpaka akajishangaa! Ilipofika saa 7:30 mchana, Grace akampigia kaka yake. “Nikuletee chakula?” “Nataka nimalize kabisa. Nikila sasa hivi nitapata uvivu.” “Ndio maana hunenepi!” “Niwekee chakula changu, nikirudi nitakuja kula.” “Mama anasisitiza uwahi kurudi. Usikae huko ukajisahau kula.” “Sasa unataka nikumalizie kazi yako au unataka nije kula?” Grace alisikika akicheka.

“Liz amesema atakuja baadaye.” “Mfanye anisubiri, asiondoke mpaka nije.” “Changamsha mikono sasa.” “Sitachelewa.” “Vipi Nanaa?” “Yupo. Anaonekana kuelewa.” “Mruhusu akale.” “Sawa. Nitakuona baadaye, lakini usisahau kumfanya Liz anisubiri.” “Nitampa hiyo kazi Danny. Amuongeleshe mpaka umkute.” Geb alicheka kidogo na kukata simu.

Baada ya Nanaa kusikia kuna Liz tu, alichafukwa na roho kupita kiasi. Hasira za kusalitiwa zikampanda. Kumbukumbu za juhudi zake kujitoa kwa wanaume nakuishia kujidhalilisha zikamjia. Akaamua atoke pale. “Vipi!?” Geb aliuliza baada ya kuona Nanaa anavuta kiti chake kwa nguvu na kusimama bila taarifa. “Ni muda wa kula, si ndio?” Nanaa akauliza kishari kidogo. Geb akabaki akimtizama. “Nakwenda kula.” Nanaa akaaga nakutoka bila kuongeza wala kujibiwa.

Hakuna chakula kilichopita kooni, akajikuta akitokwa na machozi asijue ni kwa nini. Aliingia chooni akakaa humo kwa muda, akarudi tena jikoni akatengeneza chai, lakini akaishia kuimwaga kwenye sinki. Alishikwa na hasira za ajabu, akashindwa kujizuia. Chuki kwa wanaume ikamwingia, akaamua kurudi ofisini.

Alifungua mlango akapokelewa na macho matulivu ya Geb. “Kwema?” Geb akauliza kwa utulivu. “Najisikia vibaya, naondoka naenda kupumzika.” Alijibu kwa kifupi. Akachukua kipochi chake, nakutoka. Geb alibaki ameshangaa. Lakini lilikuwa jukumu lake kumaliza kazi aliyokuwa amepewa na dada yake. Akabaki akifanya ile kazi, asielewe kilichompata mwanafunzi wake. Kilikuwa kitendo cha muda mfupi. Hakujua kama ni maumivu ya gafla au alikuwa nayo kwa muda mrefu! Anamuuliza nani na Nanaa alishaondoka! Akabaki haelewi.

~~~~~~~~~~~~~

Alitoka pale akarudi nyumbani. Akashukuru kutomkuta James nyumbani, akaingia chumbani kwake nakuanza kulia. Alilia kana kwamba Geb alikuwa mpenzi wake akamfumania. Na wala hakuwahi kulia vile hata alivyowafumania wapenzi wake wote. Alilia kwa kusononeka kutoka moyoni, huku akikubali kushindwa.

Alilia kukosa ambacho wala hakuwahi kumiliki na wala hakuwa akimfahamu Geb! Labda ni juhudi alizoweka kwenye kuvaa akitaka kumfurahisha? Ni kweli Nanaa kwa mara ya kwanza amependa? Amependaje mtu kwa kumuona tu? Hamfahamu Geb. “Sasa kwa nini nilie wakati hanifahamu na mimi simfahamu? Ana maisha yake na mimi ninayo yangu. Huu ni ujinga.” Aliwaza na kujikashifu. Akaamua kulala tu.

~~~~~~~~~~~~~

Sababu ya kulia muda mrefu, alipitiwa na usingizi mzito mpaka akaamshwa na simu ya James. “Pole. Nasikia uliondoka kazini ukiwa unaumwa. Vipi?” James akauliza. “Sasa hivi najisikia vizuri. Nilipatwa na kizunguzungu cha gafla, tumbo lilikuwa linauma.” “Unataka nije nikupeleke hospitalini?” “Hapana kaka yangu. Nimepumzika angalau sasa hivi najisikia vizuri.” “Pole sana.” “Asante.” Ukimya ulizuka kidogo.

“Unauhakika utakuwa sawa bila kwenda hospitalini?” Bado James alionyesha wasiwasi. “Usiwe na wasiwasi. Nikijisikia vibaya nitakupigia. Lakini sasa hivi najisikia vizuri.” “Basi nitamjulisha na Grace. Amenipigia simu akiwa na wasiwasi.” Nanaa alijisikia vibaya kwa jinsi alivyoondoka, hata yeye hakujua kilichompata. “Naomba uniombee msamaha. Niliondoka gafla.” “Afadhali uliwahi kuondoka kuliko kuzidiwa ofisini. Basi pumzika, usihangaike na kupika. Mimi nitakula hukuhuku, nitakuletea na wewe.” “Asante. Lakini usiwe na wasiwasi, nipo sawa tu.” “Sawa. Basi pumzika.” Nana akavuta pumzi akajirudisha kujilaza vizuri.

Wakati amejilaza hapo kitandani ujumbe ukaingia. ‘Vipi, unaendeleaje? Geb.’ Nanaa aliusoma ule ujumbe na kuufuta palepale bila hata kutaka kujibu. “Hayamuhusu.” Akajisemea na kuiweka simu yake pembeni kwa hasira. Akarudi kulala mpaka James alipokuja kumgongea kuwa amerudi na chakula. Aliamka kula na kurudi kulala. Siku inayofuata alilala karibia siku nzima. Aliamka jioni na kujikuta peke yake, James hayupo. Akapika na kuosha vyombo, akarudi chumbani kwake.

Ilipofika usiku akasikia sauti ya Grace, Danny na James wakiingia huku wakicheka kwa sauti ya juu. “Nenda kamuamshe tujue anaendeleaje?” Alimsikia Grace akimtuma James. “Una wasiwasi wakupoteza mfanyakazi nini?” Danny aliuliza huku akimcheka mkewe. “Ninavyomuhitaji huyo Nanaa! Sitaki yule dereva awe analala na pesa. Ataanza kuzitumia. Nenda bwana James.” Alimsikia James akisogelea chumba chake huku akicheka. “Nanaa! Bosi wako amekufuata.” Nanaa akafungua mlango. “Nilikwambia uwaambie najisikia vizuri, kaka! Wasiwe na wasiwasi.” “Wewe njoo uwasalimie, labda wataridhika.” Nanaa akatoka kuelekea sebuleni akiwa na majuto na alichokifanya siku iliyopita.

“Tumekuletea na mchumba wako. Labda utapona.” Grace alimuwahi Nanaa mara alipotokea, akacheka. Fili alikuwa amepakatwa na Geb kwenye kochi dogo, wametulia kimya. Halafu Grace na Danny wamekaa kwenye kochi kubwa. “Nimepona. Nilimwambia kaka James akwambie, ili usiwe na wasiwasi.” “Afadhali. Pole sana. Tulikuwa tunamwambia James, tunaanza kupunguza mahari, tumekuletea Ice cream.” Nanaa akacheka, akaenda kupokea kopo dogo la Vanilla Ice cream. “Sijui kama utapenda! Tumechukua tu.” “Asanteni sana kwa kujali, na poleni kwa usumbufu.” “Hamna shida. Kwanza ndio tumepata sababu ya kuja hapa.” Danny alidakia nakumfanya James acheke.

“Sasa unataka nini hapa kwetu?” James akauliza huku akicheka. “Si basi tu. Kwani hujawahi kuona wale watu wasiopenda kwao?” Danny aliongeza nakufanya wote wacheke kasoro Geb, alibaki akimbembeleza Fili aliyekuwa amelala kifuani kwake. Aliendelea  kupitisha mkono wake mgongoni kwa Fili taratibu. Nanaa alijifanya kama hajamuona na wala na yeye hakuzungumza chochote, alibaki kimya tu akibembeleza mtoto.

 Jumatatu.

A

lifika ofisini siku ya jumatatu akaendelea na shuguli zake kama kawaida. Ilipofika mchana, akasikia sauti ya Geb akiwa ameingia hapo ofisini akiongea na dada yake wakiwa mapokezi. “Utakuwa hunidai.” Alimsikia Geb akimwambia Grace. “Mbona nakushukuru! Nimeipitia ripoti nzima, naona mambo sio mabaya.” “Lakini bado nikiangalia nafikiri unaweza kutengeneza faida kubwa zaidi, G.” “Umeniambia. Tupate basi muda tuzungumze zaidi ili unishauri chakufanya.” Geb akaaga, na kuondoka bila hata kusogelea ofisi ya Nanaa, akamsikia Grace anakuja ofisini kwake. “Geb ametuletea Bank Statement ya mwezi uliopita. Naomba uitunze, atakuja kudai wakati wakutengeneza ripoti.” “Sawa.” Nanaa akaipokea na kuiweka kwenye faili lake husika.

Yalipita majuma mawili mfululizo bila kumuona Geb pale ofisini wala hakutuma tena ujumbe. Nafsi ikaanza kutapatapa. Akatamani kumfahamu zaidi kama anakofanya kazi, na mambo mengine mengi lakini akaishia kujiambia haina sababu. Akabaki anataka, hataki

~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo ya ijumaa wakati anakaribia kutoka, akiwa anarudisha mafaili mengine pale mapokezi, akamuona Grace anaongea na simu kwenye mlango wakutokea nje ya ofisi. “Nanaa!” Grace akamuita. Nanaa akamsogelea. “Kesho ni birthday ya mchumba wako. Tutamfanyia sherehe ndogo tu. Unaweza kuja na James kama huna kitu kinachokufunga.” “Saa ngapi?” “Saa kumi na nusu jioni. James anafahamu hoteli ambayo huwa tunafanyia. Nitamwambia mje naye.” “Anapenda zawadi gani?” Nanaa akualiza. “Mmh! Wala usihangaike. Ana michezo mingi sana, naona hata mingine hachezei. Wewe njoo tu.” “Nije mikono mitupu!?” Grace akacheka kama anayefikiria.

Akawa amepata wazo. “Basi njoo nyumbani uje unisaidie kuandaa zawadi zakuwapa  watoto watakao hudhuria hiyo party, halafu tutaondoka wote kuelekea huko kwenye sherehe na hizo zawadi.” “Hapo sawa.” Wote wakacheka. “Mnakaa wapi?” “Nitamtuma Danny au James wakulete nyumbani. Usiwe na wasiwasi. Utafikishwa tu.” Nanaa alifurahia kuona amepata kitu chakufanya siku inayofuata.

Jumamosi.

Siku hiyo alimka na furaha akiwa anakumbukumbu za kualikwa kwenye shuguli ya Fili. Aliamka asubuhi na mapema akafua nguo zake na za kaka yake. Akasafisha nyumba, baada ya kuandaa kifungua kinywa, akabaki amekaa chumbani kwake akimsubiria James aamke ili ajue ni saa ngapi atampeleka nyumbani kwa Grace. Alimsikia James ameamka, anamwita. Akatoka. “Nahisi Grace atakutaka mapema. Danny amenipigia kuniambia msichana wao wa kazi ameondoka leo asubuhi.” “Utanipeleka?” “Ngoja nile kwanza. Nimeamka na njaa. Nitakupeleka kwenye saa tano hivi.” Nanaa akarudi chumbani kwenda kujitayarisha, akamuacha James anapata kifungua kinywa huku akiongea na kucheka kwenye simu.

~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa tano na nusu, Geb aliwasili pale. “Niambie Mkuu!” James akamuanza. “Nipo kaka. Nimetumwa kumfuata Nanaa.” “Pole kwa usumbufu. Kuna mahali natakiwa kwenda sasa hivi. Nikaona mpaka nimalize huko, nije nimchukue hapa na kumleta huko kwenu, nitachelewa.” “Hamna shida.” Geb akajibu na kutulia.

James akaenda kumuita Nanaa ambaye tayari mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio baada yakusikia sauti ya Geb ndani ya nyumba yao. “Nilimuomba Grace amtume mtu akufuate. Kuna mahali natakiwa kwenda. Geb ndio amekuja kukuchukua. Tutaonana jioni kwenye shuguli.” “Hamna shida.” Nanaa alitoka akamkuta Geb amekaa kwenye kochi akimsubiria.

Hakuwa amemuongelesha tokea siku alipomuacha ofisini, tena kwa hasira na hata alipofika siku ile akiwa na familia ya dada yake, Nanaa hakumsalimia. “Habari yako?” Nanaa alisalimia. “Nzuri.” Geb alijibu kwa ufupi tu. “Mimi nipo tayari.” Nanaa akaongeza, Geb akasimama. “Sasa kaka?” Geb alimgeukia James. “Tutaonana jioni. Acha mimi nikasake pesa.” James akajibu. “Sawa. Baadaye basi.” Geb aliaga nakutoka, Nanaa akamfuata nyuma baada ya kuagana na kaka yake.

~~~~~~~~~~~~~~

Alikutana na gari ya rangi ya silver, aina ya ‘Cadillac Escalade, SUV’ ikisubiri nje. Nanaa alibaki ametoa macho. Hakuwahi kuona gari nzuri vile. Akabaki anashangaa. Alisikia Terry na Evan pamoja na marafiki zake wakishindana kutajiana aina ya magari ambayo ndio ndoto zao. Na kama endapo watafanikiwa kimaisha watanunua magari hayo. Nanaa hakuwa hata anaelewa hayo majina. Hakuwa kwenye ulimwengu huo wakuwaza aina ya magari wakati hata pakulala ilikuwa shida! Hakujua aina ya magari, na hakuona umuhimu wa mtu kupoteza pesa nyingi eti kwa ajili ya kununua tu gari, mpaka alipokutana na ile gari pale nje. Ndipo akaelewa kwa nini kuna aina ya magari, na watu wanapenda aina fulani.

Wazo la kwanza alifikiria kama angepiga picha kwenye lile gari. “Hata nikipiga picha itasaidia nini? Niache ushamba.” Nanaa akajisuta. “Khaaa! Sio kwa uzuri huu wa gari jamani!” Alibaki akikodoa macho. Geb alipoona amezubaa pale nje, akarudi upande wa abiria. Mlango wa mbele, akamfungulia mlango. “Karibu.” Akamkaribisha kama kumtaka waondoke. “Asante.” Akasogea. Tayari miguu ilikuwa ikicheza. “Ndani litakuaje? Hizi nguo haziendani na hili gari hata kidogo!” Nanaa aliendelea kuwaza wakati anasogelea mlango. Akaingia, Geb akafunga mlango.

Geb alijua wazi Nanaa amebabaika na lile gari. Alitegemea. Akamcheka moyoni kwani alishindwa kuzuia mshangao wake. Alishangaa mpaka mdomo aliacha wazi. Geb hakujua kama Nanaa alijijua jinsi alivyoachama mdomo na kutoa macho baada ya kuona lile gari. Alicheka tena moyoni, akatulia tu usoni.

Alimsubiri ajifunge mkanda ndipo aondoe gari. Nanaa hakujua hata kama anatakiwa kujifunga mkanda. Akabaki ametulia kwenye kiti huku akishangaa ile dashboard/mbele ya gari kwa ndani. Akagundua safari haijaanza. Wapo pale pale. Akamgeukia dereva wake. “Nasubiri ufunge mkanda.” Haraka sana, Nanaa akajiangalia gauni alilokuwa amevaa. Lilikuwa la lastiki kiunoni. Ni kweli lilikuwa na vijinyuzi vyembamba pembeni. Vyakupitishia mkanda wa gauni. Lakini hakuwa amevaa mkanda. Alivaa bila mkanda. Lilikuwa la kuchanua chini. Kigauni cheusi. Polka dots za gold. Kilikuwa kina mikono mifupi iliyoshuka chini kidogo ya mabega. Kilimwagika vizuri sana chini ya kiuno.

“Sikupataga mkanda unaofanana na hili gauni.” Nanaa akajitetea. Bado Geb alikuwa akimtizama wakati anajiangalia na kuendelea kuvuta lile gauni na kulikusanya chini ya mapaja kama kulikalia. “Kwa hiyo hapa sina mkanda.” Aliendelea kujieleza, akionekana kupaniki tayari. “Namaanisha mkanda wa gari. Kwa ajili ya usalama wako barabarani.” Geb aliongea kiungwana. “Oooh! Mkanda wa gari. Nil..nil …nilifikiri..” Akaanza kupambana kuvuta mkanda wa hilo gari pembeni ya hicho kiti alichokuwa amekalia. “Nikusaidie?” Geb akauliza baada yakuona anatumia nguvu nyingi kwa kuvuta mkanda ambao hata Fili huwa anavuta bila shida.

~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alijisikia aibu mara mbili. Sio kosa lake. Amepanda wapi gari zuri hivyo? Kaka yake James ana gari nzuri. Lakini ni ya kawaida tu, na huwa Nanaa mwenyewe hapandi mara kwa mara kwa kuwa James anatumia gari ya ofisini siku za kazi, na hawaongozani na Nanaa. Wanafanya kazi pande mbili tofauti za Dar. Ofisi za kina James zipo njia yakuelekea Kawe kutokea Morocco. Na ofisi ya kina Nanaa, ipo Kariakoo karibu na Fire. Siku za weekend James anakuwa na mishuguliko yake na gari yake, Nanaa anabaki nyumbani. Akiwa na safari basi daladala itahusika.

Mwanaume mwingine aliyekuwa naye na mwenye gari alikuwa Jamal. Jamal alikuwa na gari aina ya Mark 2. Nayo ilikuwa ya kawaida sana.  Tena ilionekana ni ya zamani. Jamal aliinunua kwa mfanyakazi mwenzake akiwa ameshaitumia kwa miaka mingi tu. Na huyo mfanyakazi mwenzake alinunua ikiwa imeshatumika hata huko Japan aliko iagiza. Vioo vilishaharibika. Hakumbuki hata kama lilikuwa na mkanda. Milango ya hilo gari ya Jamal ilikuwa lazima ufunge kwa nguvu. Tena wakati mwingine mara mbili au tatu.

~~~~~~~~~~~~~~

Akaendelea kupambana na mkanda wa kiti chake mpaka alipochoka. Akakubali kushindwa. Geb alikuwa ametulia kimya, akimsubiria achoke ndipo amsaidie. Kwa kuwa alijua kwa uvutaji ule, lazima mikanda iji lock. Kwa hiyo alimuacha apambane mpaka aache ndipo arudie tena kuuliza kama angetaka msaada. “Naona mikanda mibovu.” Nanaa aliongea kwa upole, baada ya kupambana na ule mkanda na kushindwa.

Geb akamsogelea. Mapigo yake ya moyo yakaanza kwenda kasi. “Ananipa pole kwa kunibusu!?” Aliwaza harakaharaka huku mapigo ya moyo yakienda kasi wakati Geb akijivuta upande wake. Akanyoosha mkono kwa tahadhari kama asiyetaka kumgusa. Akavuta ule mkanda kwa urahisi sana, akamfunga. Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu. Akajiweka sawa pale kitini huku aibu imemlemea.

~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye nyumba aliyopangisha kaka yake, hapakuwa na geti. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kuingia na kutoka bila shida. Hakujua aseme nini tena. Alishajidhalilisha vyakutosha. “Sio kosa langu. Sijazaliwa kwenye magari. Hata yeye kuna mambo hajui. Kwani yeye ni Mungu kuwa anajua kila kitu? Wala sio jambo la ajabu nililolifanya!” Nanaa alijitetea kwenye nafsi yake. “Lakini nisingesingizia kuwa mkanda ni mbovu! Gari yenyewe inaonekana mpyaaa! Aibu gani hii! Lazima nibadili mazungumzo. Kuondoa hii aibu.” Akawaza kama ajieleze juu ya ujumbe ambao hakujibu au vile alivyomuacha pale ofisini bila maelezo ya kutosha, na pia akamfuata nyumbani kwao, akashindwa hata kumsalimia! “Labda nitulie tu.” Nanaa akaendeleza kikao kichwani mwake, akijiuliza na kujijibu.

Akajifunga mkanda wake na yeye, kisha akaondoa gari bila ya kuongeza neno wala kuuliza swali, aliendelea kuendesha akiwa ametulia kimya kana kwamba yupo peke yake garini. “Itakuwa gari ya dada yake hii! Grace anapesa sana.” Nanaa aliendelea  kuwaza wakati Geb akiendelea kuendesha. Akakumbuka ripoti ya mwezi uliopita ilivyoonyesha faida kubwa waliyoingiza. “Hakika Mungu amembariki yule dada.” Nanaa akaendelea kuwaza.

Alishangaa kuona wanapita Ubungo, wakielekea njia ya Mabibo Hosteli. Akamkumbuka Zac, mpenzi wake wazamani. Kidogo akaanza kukosa raha. Akajiweka sawa na kugeukia dirishani. Akaegemeza kichwa vizuri hapo dirishani, akabaki akiangalia nje ya dirisha. Mawazo yalimpeleka moja kwa moja mpaka siku alipomfumania Zac. “Mmmh!” Alipumua kwa nguvu huku ameshika shavu. Geb akamtizama, lakini akagundua hayupo pale kimawazo maana hata kubabaika pale kitini kuliisha. Akatulia kabisa macho nje gari.

~~~~~~~~~~~~~~

Usikose Muendelezo….

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment