Viola alichanganyikiwa baada ya Alex kufika hapo nyumbani.
Alitawala mazungumzo yote, huku akionyesha uzoefu wa mambo kadhaa. Alitaka
kujua malengo yake baada ya kumaliza chuo. Nini kilimpelekea kusomea mambo ya
mahesabu. Changamoto gani anapata katika kusomea fani hiyo. Viola akiwa
amechangamka, aliendelea kuhoji maswali mengi ya msingi ambayo hata Nanaa
mwenyewe hakuwahi kumuuliza Alex!
Alipoona mapokezi ni mazuri nyumbani
kwa kina Nanaa, akaanza kumtembelea kila jumamosi. Analala hotelini na kuondoka
siku ya jumapili au jumatatu asubuhi. Furaha na amani vikatawala kwa muda. Kila
anapokuja nyumbani basi Viola hakukosa mazungumzo ya msingi kwa Alex. Gafla
akageuka yeye kuwa msichana wa maana kwa Alex kuliko Nanaa. Mara Nanaa akaanza
kuona mawasiliano yanakuwa mazito kati yao. Alex akaacha kuonekana pale
nyumbani lakini Viola furaha kwake ikaongezeka. Akaanza kudanganya kwa baba
yake huku mama akimkingia kifua kuwa kila siku za ijumaa huwa anamtuma kijijini
kwa bibi yake na kurudi jumapili usiku au jumatatu na wakati mwingine alimuaga
baba yake kuwa anakwenda kutafuta chuo mikoa mingine basi na kupotea zaidi pale
nyumbani.
Alitangaza pale nyumbani kwao kuwa,
kwa mara ya kwanza maishani amepata mwanaume wa ndoto yake. Alisema ameshatambulishwa
mpaka upande wa huyo mwanaume, ni watu wenye uwezo sana. Ilikuwa furaha kwa
Mama Mkubwa, kwani ni kweli Viola alibadilika. Kila aliporudi safari alirudi na
vitu vipya na vya maana, akiwa amejawa furaha.
Juhudi za kumtafuta Alex ziliendelea
huku akiambiwa yupo na hili au lile atapiga simu baadaye. Vicheko vilitawala
mle ndani, asijue anayechekwa ni yeye. Maswali ya kuulizwa Alex alipo huku
akichekwa hayakuisha, na yeye hakushindwa kumtafutia sababu ya kuwapa ndugu
zake ili tu kuonyesha yeye na Alex wapo vizuri, ila Alex ametingwa tu. Asijue
linalo endelea.
“Atakuwa kapata mwanamke mwingine
anayempenda.” Mdogo wake Viola, yaani Vai alikuwa akimwambia Nanaa huku
akimcheka pale alipokuwa akimtetea Alex kuwa yupo busy. “Hapana. Alex ni
mwaminifu sana. Ni ubusy tu.” Nanaa aliongea kwa uhakika, akimtetea mpenzi
wake mbele ya Viola ambaye ndio alikuwa amerudi kutoka safari ya siku tatu
ambayo Nanaa alimsikia mama yake akimwambia baba mkubwa kuwa amemtuma Viola
kijijini kwa bibi yao. “Ubusy huo ubusy gani bwana!? Wewe kubali kuwa
umeachwa. Sababu hazikuishi!” “Amesema atakuja ijumaa ijayo.” Wakamcheka
kwa sauti ya juu, na kugonga mikono wakimcheka Nanaa bila huruma akiwa
amewapelekea chakula cha mchana, hapo sebuleni walipokuwa wakiangalia luninga.
Viola alimtaka awapelekee chakula pale pale, akisema kwa nyodo kuwa amechoshwa
na usiku mrefu, uliopita, uliokuwa umejaa starehe nyingi. Hakutaka kunyanyuka
na kwenda kula mezani.
“Sasa mnacheka
nini?” Nanaa akauliza wakati Viola ameenda kuongea na simu yake
nje. “Njoo nikuonyeshe anapokuwaga Alex.” Vai alimwita Nanaa. Alitoa
simu na kuanza kumuonyesha picha za Alex akiwa na Viola, na nyingine hata yeye
alikuwepo. “Hizi za jumamosi ya juzi. Niliwafuata hotelini, Alex akatutoa.
Wenzio wapo kwenye mipango ya harusi, hata mama anajua. Hapa wanasubiri Alex
amalize tu chuo, aje kutoa mahari.” Nanaa alihisi yupo ndotoni. “Na
kwa taarifa yako zaidi, Viola kaamua kumbebea mimba kabisa ili asije badili
mawazo. Kwa hiyo andika maumivu.” Nanaa alikaa chini. “Yaani Viola amembembea
mimba mpenzi wangu!?” Nanaa aliuliza na kufanya amcheke zaidi. “Sema
aliyekuwa mpenzi wako, wewe Nanaa. Mbona huelewi?” Nanaa alinyanyuka na
kuondoka.
Kisicho
Ridhiki Hakili!
V |
isa vikaanza. “Sasa unanuna nini? Kama mwenzio amebahatika
kupata mwanaume mzuri si ushukuru Mungu, badala ya kumnunia? Kama hakuwa andiko
lako, basi! Maana mwenzio tayari mjamzito.” Mama Mkubwa alikuwa akiongea
na Nanaa alipomkuta jikoni akiosha vyombo. “Huna shukurani wewe mtoto.” “Mbona
mimi sijasema kitu, mama mkubwa?” “Mbona Viola anasema humsalimii? Akikuita
msaidie, huendi. Mama yako alikuja hapa na ujauzito wako, tukamsaidia bila
kujali alikobebea mimba! Hatujui kama ilikuwa mimba ya mume wa mtu au la.
Lakini nikamsaidia bila kujali. Leo mwenzio amebahatika, unamfanyia roho
mbaya!? Shukurani yako iko wapi wewe?” Gafla kitendo cha Viola binti
aliyemaliza kidato cha 6 tu, nakushika mimba, kikaonekana cha kusifiwa.
Kazi ya kumuhudumia Viola, mjamzito,
ikampata Nanaa. Alex anapokuja kumsalimia Viola mpenzi wake, pia Nanaa
alitakiwa amuhudumie huyo Alex, tena bila kinyongo. Alitakiwa aonyeshe heshima
kwa Alex kama shemeji yake. Hakuruhusiwa kumsemesha, ila kumtengea kinywaji na
chakula kisha kuondoka. Viola alimpiga marufuku Nanaa mbele ya Alex kuwa asimtafute
tena mpenzi wake, hawataki usumbufu.
~~~~~~~~~~~~~
Matokeo yakumaliza kidato cha sita
yalipotoka, Nanaa akapata daraja la pili, Viola daraja la nne. Ni kama hapakuwa
na jambo zuri lililokuwa limemtokea Nanaa. Mama Mkubwa aliumia sana. Akabaki kuzungumza
kwa mafumbo. “Katika maisha huwezi kupewa vyote. Heri yako mwanangu
umebahatika kuolewa na mwanaume anayekupenda. Wakwe zako wanakujali na
unatarajia mtoto.” Hayo ni maneno kutoka kwa mama Mkubwa. Hapakuwa na
pongezi kwa Nanaa, ila manyanyaso. Hapo ndipo alipoona upendeleo wa wazi wazi
na kujiona kweli yeye si mtoto wa pale ndani.
Wenzake walianza kutuma maombi ya
vyuo mbali mbali lakini Nanaa alishindwa. Kwani aliacha kupewa pesa, akawa yupo
tu nyumbani akimtumikia Viola mchana na usiku. Hakuna hata aliyezungumzia mambo
yake ya shule tena, bali majukumu. Ampikie nini Viola au alipewa ratiba ya siku
nzima ya jinsi ya kumuhudumia Viola. Napo hapo alilala akiwa hoi. Maana mara
nyingi Viola alibadili mawazo ya kila chakula alichotaka Nanaa ampikie. Anaweza
kutaka ndizi na nyama ya ng’ombe. Nanaa anapompikia na kumpelekea, anaweza
kusema hakitaki tena kile chakula, anataka chakula kingine au kumlazimu kufuata
aina ya chips fulani mbali sana na hapo nyumbani, tena pengine ni usiku.
Ilimradi tu, atumikiwe na mwenzie.
~~~~~~~~~~~~~
James mtoto mkubwa alikuwa amemaliza
chuo na kuajiriwa jijini Dar. Aliishi Dar kwa muda mrefu tu. Tokea yupo chuo
mpaka ameajiriwa. Kwa umri, aliwapita mbali sana dada zake. Halafu kwa asili
James alibeba haiba ya kiutu uzima. Alijiheshimu sana. Kwa hiyo hata hapo
nyumbani aliheshimiwa kama anavyoheshimiwa baba yao.
Alifika nyumbani hapo mida ya usiku.
Aliwaambia ilimbidi kwenda kazini asubuhi ndipo akaanza safari. Kwa muda mfupi
tu alipoingia pale ndani, akahisi mambo hayakuwa sawa. Ilikuwa saa tano na nusu
usiku wakati anamaliza kula. Alikuta watu wote wakimsubiria kasoro Viola. Kama
kawaida, Nanaa ndiye aliyekuwa akimuhudumia kaka yake. Wakati anatoa vyombo na
kusafisha meza, James akaongea kwa sauti. “Nina hamu sana na supu ya
makongoro ya Kiboriloni. Kesho asubuhi ujiandae Nanaa. Nataka
unipeleke.” Nanaa akafurahi sana kusikia atapata muda wa faragha na
mkombozi wake.
~~~~~~~~~~~~~
Halikuwa jambo la ajabu kwao kwa
James kumtaka Nanaa ndio amsindikize. James alijulikana kwa kumpenda na kumjali
Nanaa tokea mtoto, kama yeye ndio dada wakuzaliwa tumbo moja. Wakati mwingine
alifika hapo nyumbani kwenda kumuona tu Nanaa. Hata hivyo, yeye ndiye aliyekuwa
amemlea Nanaa, kama yaya wake, tokea anatolewa hospitalini baada ya kifo cha
mama yake. Mbali ya kumpa hilo jina alilosema ndilo jina mama yake alimwambia
huyo mtoto akizaliwa atamwita hivyo, pia ndiye aliyeshika usukani wa kumlea
Nanaa. Alijua kula na vaa ya Nanaa, tokea hata Nanaa hajakatika kitovu cha
kuzaliwa.
~~~~~~~~~~~~~
Kwa uongeaji ule, ndio alikuwa
akitangaza kuwa Nanaa hatakuwepo asubuhi ya siku inayofuata. Kwa maana
nyingine, alikuwa akimtaka mama yake asimpangie Nanaa majukumu mazito
yatakayomchelewesha yeye na Nanaa kutoka. Ujumbe ulifika bila shida. Nanaa
akaachwa bila jukumu lolote kwa siku inayofuata. Hata hivyo mtetezi wake
alikuwepo. Hakuna anayemgusa wala kumsema kama James anakuwepo nyumbani.
Aliachwa kabisa.
Wakaagana na kwenda kulala. Aliamka
asubuhi nakufanya shuguli chache kumsaidia msichana wa kazi ambaye ndio rafiki
yake wa karibu. Ndiye waliyekuwa wakilala naye na kuzungumza mambo
mengi. Kwanza ni kama wote walikuwa kwenye nafasi moja wakitumika humo ndani
kuanzia asubuhi mpaka usiku wanapomaliza kazi zote. Walijikuta wapo karibu kwa
kuwa iliwalazimu kufanya kazi pamoja ili kupata muda wakupumzika.
Alipomaliza shuguli zake za asubuhi,
akarudi chumbani kujiandaa. Akamsikia James anamwita kwa sauti. “Nipo huku
chumbani kaka.” “Twende!” Nanaa akatoka. Wakasalimiana kidogo, wakatoka
wao wawili tu. Mdogo wake wa mwisho, Vai alipotaka na yeye aongozane nao, James
alimkatalia bila kung’ata maneno tena mbele ya wazazi wao. Akisema waziwazi
anataka muda na Nanaa tu.
~~~~~~~~~~~~~
“Vipi?” James alimtupia swali
mara tu baada ya kukaa. Kutokana na makuzi aliyokuzwa yakuto kusikilizwa pale
anapoishi, yeye kama msikilizaji wa mambo ya watu na kupokea amri tu, Nanaa
hakuwa muongeaji sana. Wakati wote alikuwa kimya akisikiliza au kucheka tu. Na
ilimlazimu kuwa mtaratibu ili asiingie matatizoni, lakini si kwa kaka yake
James. Hakuwahi kumficha James jambo. Na yeye ndiye aliyekuwa akimsikiliza
Nanaa. Alijua maisha magumu ya Nanaa, kwani alizaliwa James akiwa na akili
timamu. Alimuona vile mama yake Nanaa alipokuja pale nyumbani kwao akiwa
mjamzito. Manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa wazazi wake, na hata Nanaa
mwenyewe alipozaliwa, yote hayo James aliyajua kwa kuyaona.
Kwa hiyo akajenga upendo wa ajabu
sana kwa Nanaa. Alimkingia kifua Nanaa tokea mtoto mpaka amekuwa. Na wote
walijua. Ukitaka kumuudhi James, mguse Nanaa. Hapo ndipo alimbadilikia kila mtu
mpaka hata mama yake mzazi. Baba yake ndio hakutaka ukaribu na Nanaa kabisa.
Usingeweza kuwakuta wawili hao sehemu moja wakiwa wanazungumza. Kama watakuwa
kwenye banda la ng’ombe wakifanya kazi, basi kutakuwa kimya kabisa. Kila mmoja
akifanya kazi yake. Na ilikuwa mara chache sana. Ni kama alikuwa akimkwepa
Nanaa. Hakumtaka kabisa karibu yake.
Njia Za
Mungu Si Za Wanadamu.
W |
akati Nanaa na Viola walipokuwa wachanga kabisa, alipoona Nanaa
analia sana na hakuna wakumbembeleza, James akajifunza kumbembeleza mpaka
akajua mbinu zote za kumtuliza Nanaa. Akatatua kero kubwa sana iliyokuwepo kwa
wazazi wake. Kwa hiyo kila Nanaa alipokuwa akilia, yeye ndio aliitwa
kumbembeleza au walimsikia akikimbia kutafuta kilio cha mtoto huyo. Hata kama
ni usiku, James akimsikia tu analia, ataamka na kuhakikisha anamtuliza Nanaa
mpaka anatulia. Akajifunza mambo yote ya watoto wachanga. Hakupata shida.
Kwa kuwa tayari alishamuona mama yake
akimlea mdogo wake Viola. Na kwa kuwa uhitaji wa malezi ya Nanaa ulitokea,
James akaongeza umakini kwenye kutizama kila kitu mama yake anachomfanyia mtoto
huyo mchanga, ambaye alimtafuta kwa shida sana na kumlea kwa mapenzi yote,
Viola. Akaiga kila kitu na kuhamishia kwa mtoto huyo aliyekuwa ameachwa mkiwa,
Nanaa. Kwa muda mfupi sana, akamudu kila kitu na Nanaa akajisikia salama
mikononi mwa James, mtoto wa kiume, mwenye umri wa miaka 11 tu. Akawa kama
ndiye mama yake.
Akajua kumlisha. Kumbadilisha nguo na
nepi, pamoja na kumsafisha. Kila alipomuona ameachwa bila uangalizi mzuri,
James alichukua hatua kwa haraka sana bila kuuliza. Kama akimkuta amelowa au
amejichafua, basi James mwenyewe ndiye aliyekuwa akihusika. Akilia Nanaa, James
hakupata shida. Alishajua hata na sauti zakumtuliza mtoto. Sauti ipi aitumie
wapi, neno lipi lakuzungumza wapi. Kama alivyomuona mama yake anamfanyia mdogo
wake Viola. Na Nanaa akamtambua James. Kwa sauti, harufu yake na sura.
Akishikwa tu na James, alitulia kwa haraka sana. Ikajulikana James ndio kazi
anayopenda na kufurahia. Kwa hiyo kila Nanaa alipotakiwa kuhudumiwa, aliitwa
James.
Jioni alipokuwa akitoka shule,
alifanya kazi zake za shule kwa haraka ili apate muda na mtoto. Alijua kitu
baba yake anachotaka ni kufaulu vizuri shuleni na kwenye maisha. Sasa ili
asimtenganishe na Nanaa, James akaongeza juhudi zaidi shuleni ili kusiwe na
lawama. Maana baba yake alishamtahadharisha kuwa atakuwa mjinga kama akiendelea
kuwa kama mama wa Nanaa. Alimlaumu sana mama yake kumruhusu James kuwa karibu
na marehemu Wini kutokea mwanzoni. Akahisi James hatakuwa kama watoto wengine
wakiume. Hakuwa na muda na marafiki wala michezo ile ya watoto wa umri
wake.
Maisha yake yalibadilika mara Nanaa
alipozaliwa. Alibeba sura ya utu uzima, na majukumu yakamwingia. Na kwa kuwa
alipendwa sana hapo nyumbani, aliendekezwa tokea mdogo. Mpaka baba yake alikuwa
akimsikiliza sana James. Alipoona hatari ya Nanaa kugawiwa kwa watu wa nje
tokea mtoto, akawaomba wazazi wake wasihangaike tena kumgawa Nanaa, akawaahidi
kuwa yeye atamuhudumia. Hayo aliyaongea akiwa bado na umri ule ule miaka 11.
Baba yake alipomuuliza swala la shule. Akaahidi kuleta matokeo mazuri sana
nyumbani.
Na kweli, Mungu akamfanikisha sana
katika hilo eneo. James akazidi kufaulu shuleni. Wakakosa chakuzungumza. Kila
alipotoka shule, alikimbilia ndani kwa Nanaa. Atamchukua Nanaa na kuanza
kucheza naye wakati anakula. Kama akimkuta kama nepi imejaa, au mchafu na njaa,
atamsafisha na kumlisha kwanza ndipo na yeye akae chini ale. Wakati anafanya
kazi zake za shule, atamuacha Nanaa pembeni yake akicheza. Na hapo hutamsikia
Nanaa akilia. Kutakuwa na utulivu wa namna yake. James anafanya kazi zake za
shule huku akizungumza naye kumfanya atulie na kucheka. Nanaa akaijua sauti ya
James na kumsikiliza kwa makini sana kama mtoto kwa mama.
Siku ambazo haendi shuleni, ndio
ikawa salama kwa Nanaa. Kuanzia asubuhi utamkuta Nanaa msafi sana. Atasafishwa
na James, na kulishwa. Nanaa akawa akimfahamu James hata akipita kwa mbali.
Kama akiwa anacheza mahali, akimuona tu James, au akisikia sauti yake hata kwa
mbali, mambo yote yatasimama. Atatambaa na kumfuata popote anapoenda au alipo.
Alipoanza kutembea ndio ikawa zaidi. Angalau mama mkubwa akawa anapata msaada
wa mtu mwingine kumtoa Nanaa karibu yake na mwanae.
Ilikuwa huzuni na uchungu kati ya
James na Nanaa pale James alipofaulu na kuchaguliwa katika shule ya bweni ya
wavulana Iliboru. Ilibidi James kwenda kuanza kusoma kidato cha kwanza shuleni
huko na kumuacha Nanaa akiwa bado anahitaji uangalizi wa karibu. Kila alipokuwa
akipata nafasi, alirudi kwenda kumuona Nanaa. Wakati mwingine alidanganya
shuleni ni mgonjwa sana, ili arudi nyumbani awe na Nanaa angalau kwa siku
chache tu.
Rafiki zake wote James walimfahamu
Nanaa kwa kumsikia tu kutoka kwa James mwenyewe. Hakuna jinsi James ataongea
stori zake, asisimulie habari za mdogo wake kipenzi Nanaa. Lakini anapoanza
kumuelezea, au jinsi anavyomuelezea Nanaa, utafikiri ni mama anayeeleza habari
za mtoto wake. Mungu alitengeneza connection au muunganiko ya ajabu sana
kati ya James na Nanaa. Hata Nanaa alipovunja ungo, mtu aliyemwambia ni James.
James ndiye aliyekuwa akimtunza kwa karibu tokea zamani. Kila alipokuwa akipewa
pesa zake za matumizi, alimgawia Nanaa kiasi na kumnunulia vitu vidogo vidogo
alivyojua anahitaji. Yeye ndiye aliyekuwa akimnunulia mpaka nguo za ndani. Kwa
hiyo alipomwambia tu James kuwa amevunja ungo, akakimbilia dukani kwenda
kumletea pedi. Kila alipokuwa mwezini James alijua na kuwa akimnunulia mahitaji
yake yote, kumsitiri dada yake huyo, asiaibike. Ikawa kama mtoto kwa mama.
Kila shule zilipokuwa zikifungwa iwe
likizo ndefu au fupi, James alikimbilia nyumbani kuwa na Nanaa. Wakakuwa wakiwa
na mahusiano ya kipekee na kila Nanaa alipopewa nguo za James amfulie,
alihakikisha anampa pesa kidogo kama shukurani tofauti na wengine ambao
walikosoa kila kitu Nanaa alichokuwa akiwafanyia.
Na hata Nanaa alipokuwa akipika,
James alipita jikoni kuomba supu ya nyama kabla haijaungwa na kukaa naye jikoni
akizungumza naye hili au lile ndipo aende kwenye mizunguko yake. Kwa hiyo
ikajengeka tabia. Kila anapochemsha nyama, Nanaa alimuwekea James supu na nyama
kidogo pembeni, ndipo anapounga mchuzi wa nyumba nzima. Hata kama alichemsha
maharage, basi alimuwekea mchuzi wake pembeni kabla hajaunga. James akawa ndio
kiongozi wa Nanaa. Kwani alimlea tokea anazaliwa. Tena alimlea kwa karibu. Ile
ya kumuogesha na kumbadilisha mpaka nepi. Kwa hiyo alifuata mahusia ya James na
ndiye akawa kama mzazi wa pekee kwake.
~~~~~~~~~~~~~
“Ni nini kinaendelea?” James
akamuuliza tena Nanaa, wakiwa kwenye kimgahawa hicho, pembeni ya soko hilo
kubwa la Kiboriloni, wakipata supu. Nanaa alimueleza James kila kitu. Kuanzia
mahusiano ya wizi aliyokuwa nayo na Alex. Muda alioutumia kwenye mahusiano,
makubaliano yote waliyokuwa wamekubaliana, vile alivyompeleka pale nyumbani na
kuishia mikononi kwa Viola.
“Naumia sana kaka yangu. Alex na
mama mkubwa ndio wananiumiza zaidi. Alex kwa kunigeuka. Ahadi zote alizonipa
mimi ndizo hizo hizo anazitimiza kwa Viola! Mama mkubwa akijua wazi ubaya
alionifanyia Alex na Viola, amewapa baraka zake zote! Yaani mimi ndio nadeki
matapishi ya Viola! Yaani namuhudumia kwa ujauzito aliopewa na aliyekuwa mpenzi
wangu! Si sawa kaka. Na ninahisi ananifanyia makusudi kabisa. Viola anaweza
kunipigia simu usiku, wakati nimelala, eti niamke nikampelekee maji ya kunywa
chumbani kwake. Siku akikosa yeye usingizi, najikuta ninakesha naye usiku kucha
mpaka yeye alale. Nikishindwa kuamka mapema akiwa ameniita, anakwenda
kulalamika kwa mama mkubwa, basi hiyo siku itakuwa mbaya zaidi kwangu.” Nanaa alikuwa
akiongea huku akitokwa na machozi.
James aliumia sana. “Unajua
sikuwa najua kama Viola ni mjamzito! Ndio maana ananikwepa sana. Hataki hata
kupishana na mimi tokea jana nilipofika pale nyumbani. Nikajua labda ni kwa
kuwa niliwafukuza kule kwangu na kuwarudisha huku nyumbani. Tena kwa hasira
sana na kumuonya mama wasiwahi kurudi tena Dar, nyumbani kwangu. Sasa
nikashangaa leo asubuhi mama ananiambia eti Viola amepata safari ya gafla,
amesafiri. Kumbe ananificha ujauzito wake! Kwa nini mama anatoa baraka zake kwa
Viola mtoto mdogo? Na shule?” James akauliza kwa hasira kidogo.
Akiwa anataka kuuliza kwa nini
aliwafukuza Viola na Vai, nyumbani kwake Dar, akaona ni heri aeleze shida zake
kabla James hajaondoka hapo Moshi kurudi kwake Dar. “Matokeo yetu
yametoka, kaka. Yeye amepata daraja la 4, mimi la pili. Kinachoniuma zaidi ni
kule kusimangwa mimi na matokeo yangu, halafu yeye anapewa sifa zote! Wenzangu
wote wameanza kutuma maombi ya chuo kaka, lakini mimi nimeshindwa. Sina pesa
kaka yangu. Mama mkubwa anasema amefika mwisho, na Vai naye anatakiwa aende
shule. Wakati najua wazi Vai amekataa shule.” “Nini!?” James alizidi
kuchanganyikiwa. Asiamini yanayo endelea hapo nyumbani kwao. Wazazi aliojua ni
wakali sana kwake na Nanaa, ni kama wamebadilika kabisa! Au sio hao wanao lea
wadogo zake!
“Vai ameacha shule. Wamekuja
kugundua hata mitihani ya kidato cha nne hakufanya. Alikuwa anadanganya kuwa
anasubiri matokeo, kumbe alishaacha shule muda mrefu tu. Aliwaandikia barua
shuleni kwao. Akijidai yeye ndio mzazi, kuwa anahamishwa shule. Akafanya
taratibu zote za uhamisho. Akatoa namba ya simu ya mwanaume wake, huko shuleni,
akijidai baba mkubwa amebadili namba na anataka ahame shule akamalizie kidato
cha nne shule nyingine. Sijui aliandika shule gani huko ya bweni! Ila kila barua
zilipokuwa zikija pale nyumbani za uhamisho aliokuwa ameshugulikia wakati
anamaliza muhula wa kwanza wa kidato cha nne, akawa anazifungua mwenyewe,
anazichoma moto. Kwa hiyo shuleni wakajua wamewasiliana na wazazi wake na
wamekamilisha taratibu zote za uhamisho, kumbe ni yeye.”
“Shule zikafungua ili amalizie hiki
kidato cha nne, akawa anatoka nyumbani asubuhi kama kawaida. Tena akiwa amevaa
sare zake za shule na kurudi jioni. Hakuna aliyekuwa akijua alipokuwa akienda,
lakini mpaka akamaliza muhula. Ada akawa amepewa, na michango isiyoisha akawa akiomba
pesa hapo nyumbani kwa baba mkubwa, halafu anarudisha risiti za shule kama
kawaida. Kumbe hata shuleni kwenyewe hakuwa akienda katika kipindi chote hicho
mpaka wenzake wakamaliza kidato cha 4. Baba Mkubwa alimpiga karibu ya kumuua.
Akatoroka pale nyumbani kama mwezi, akarudi. Amesema kabisa yeye hataki
shule.” James alibaki kimya kwa muda. Nanaa alimuona amebadilika mpaka sura
yake.
“Wewe unataka
kuendelea na shule?” “Natamani kaka. Sina jinsi nyingine ya kujikwamua maishani
ila shule. Halafu sio kama nimefaulu sana, nahofia kukosa nafasi za chuo kama
nitaendelea kuchelewa. Mwaka huu watu wamefaulu sana.” James akafikiria
tena kidogo. “Jiandae, wakati naondoka kesho kutwa, tunaondoka
wote.” Nanaa hakuamini. “Lakini mama mkubwa hawezi kukubali, kaka.
Nani atafanya kazi pale ndani? Yule dada wa kazi anakaribia kuondoka. Amesema
mwezi huu ndio mwisho, na yeye anaenda kuolewa.” “Usiwe na wasiwasi. Wewe
jiandae. Mambo mengine niachie mimi.” Wakatoka pale James akiwa
amekasirika na kuumia sana moyoni, lakini akawa mtulivu mbele ya Nanaa.
Alimwambia wakazunguke madukani
kidogo. “Una kitu chochote unahitaji?” James akamuuliza. “Nina
shida na begi, kaka. Sitakuwa na sehemu ya kubebea vitu vyangu.” “Unataka begi
kubwa au dogo?” “Kwani nitarudi lini?” Nanaa aliuliza kwa
wasiwasi kidogo akitamani kuambiwa asirudi tena pale kwa mama yake
mkubwa. “Wewe tu.” James alijibu kwa kifupi na mafumbo. “Kwa
hiyo hata nikitaka kuishi na wewe huko huko ni sawa?” James akacheka. “Mpaka
utakapo pata kwako. Sio ubweteke.” “Mbona nakuelewa kaka. Ulisema hakuna
kutulia mpaka nipate changu.” “Kumbe bado unakumbuka? Endelea kupambana. Sasa
chagua begi unalotaka na kitu kingine kimoja kama zawadi yako ya kufaulu kidato
cha sita.” “Kweli kaka? Kwani hapo ndio nimefaulu?” “Umefaulu vizuri tu.
Hutasumbuka sana kupata chuo. Hongera.” Nanaa aliipokea hiyo pongezi kwa
shingo upande akijua vile James alivyo na akili ya darasani, akajua pale anampa
tu moyo. Wakati wote alikuwa akipata alama za A tu darasani. Hakumbuki
vinginevyo.
Kila matokeo yake yalipokuwa
yakitoka. Ripoti zake zilipokuwa zikitumwa nyumbani, baba yake alikuwa
akizifungua na kumkabidhi James mwenyewe. Na yeye alikuwa lazima ampelekee
Nanaa amuonyeshe. Wakati wote alimwambia Nanaa, na yeye anaweza kufaulu vile
vile. Alikuwa akimuonyesha mpaka mitihani yake. Vile alivyokuwa akifaulu
vizuri. Nanaa akawa anapata moyo, anajua ataweza tu.
~~~~~~~~~~~~~
Hakujua kaka yake alifanyaje, au alizungumza
nini na mama yake, lakini wakati wamekaa mezani wote wakila, James akaingia na
baba yake usiku ambao kesho yake walijua anaondoka. Alikuja siku ya ijumaa
usiku, jumamosi hiyo ndio alikuwa anazunguka na Nanaa mjini. Jumapili
walipotoka kanisani, alimuomba baba yake amsindikize kwa bibi yake huko
kijijini. Walishinda huko kwa bibi yake siku nzima ndipo wakarudi usiku,
akasema anaondoka siku ya jumatatu asubuhi.
Akamuita Nanaa. “Nataka leo uwahi
kulala, tunaondoka kesho asubuhi sana. Hakikisha unabeba vitu vyako vyote.
Nataka ukifika kule utulize mawazo shuleni. Sio tena safari za kurudi huku
kufuata vitu ulivyosahau.” Nanaa alitamani kushangilia, lakini palikuwa na
ukimya mkubwa sana hapo, kila mtu akiwasikiliza.
“Unanisikia Nanaa?” James akauliza
kimamlaka. “Nimesikia kaka.” “Haya, naomba umalize kula hapo, kisha
unyanyuke. Nenda moja kwa moja kwenye gari na wala si jikoni kuanza kuosha
vyombo au kuanza shuguli tena. Chukua begi nililo kununulia la zawadi yako ya
kufaulu vizuri kidato cha sita. Lipo nyuma kabisa ya gari. Kakusanye vitu vyako
vyote. Weka kwenye hilo begi, halafu uje uniite. Nitalibeba usiku huu huu,
nikalifungie kwenye gari. Bakisha nguo za kuvaa kesho safarini tu. Mizigo yote
italala kwenye gari. Umesikia?” “Sawa kaka.” Chakula hakikulika tena kwa
furaha. Hakutegemea kama ataruhusiwa kuondoka kwenye ile nyumba.
James anaingia na kumtangazia uhuru!
Ahadi ya maisha mapya na kutimiziwa ndoto za kuendelea na shule! Bado kwake
ilikuwa ni ndoto. Pale pale akasimama. “Chukua funguo za gari hizi hapa.” James
akamrushia. Nanaa akadaka. “Nilikwambia begi lipo kwenye trunk?” “Ndiyo,
kaka.” Nanaa akaitikia kwa furaha zote. “Haya, God’s
speed! Fanya kwa haraka uwahi kulala. Nataka tuwahi sana kuondoka. Kesho
mchana, natakiwa niwepo ofisini kwangu.” Sio kwamba ni begi jipya ambalo
Nanaa hakulijua. Ni lile lile alilomnunulia walipoenda naye madukani. Lakini
walikubaliana walifiche mpaka safari itakapokuwa tayari. Na ni kama James
alikuwa akitangaza uhuru wa Nanaa kwa wazi na kwa wote.
Nanaa alikimbilia kwenye gari ya kaka
yake. Ilikuwa ni gari aina ya Toyota RAV4, ya kisasa iliyokuwa ndio imetoka
wakati huo. Ya rangi ya silver. Safiii. Ikionekana inatunzwa vizuri. Hata hivyo
alimjua kaka yake kwa usafi. Akafungua gari huku haamini kama kweli kwa mara ya
kwanza maishani atatoka katika ule mji wa Kilimanjaro. “Mmmh! Ngoja
nijitulize kwanza. Chochote chaweza tokea, nikazuiliwa kuondoka na kaka. Mungu
nisaidie.” Nanaa akawaza. Akatoa begi lake akarudi ndani akiwa mtulivu
kama hakuna kinachoendelea rohoni mwake.
Akarudisha funguo kwa kaka
yake, akakimbilia chumbani. Alikusanya kila kitu chake mpaka jiwe la kusugulia
miguu, akaweka kwenye kilo begi. Hata hivyo hakuwa na vitu vingi sana. Alishakwenda
shule zote alizowahi kusoma akachukua matokeo yake, akisubiria muujiza wa
kupata pesa aanze kutuma maombi vyuoni. Lakini akashindwa mpaka James alipokuja
na kumwambia wanaondoka wote. Alivitazama vile vyeti, akaviweka kifuani,
asiamini kama yale makaratasi aliyoyakumbatia, ambayo ndio vyeti vyake vya tokea
shule ya msingi, ndio vimefanyika tiketi ya kumtoa hapo kwenye hiyo
nyumba. “Naenda Dar mimi Nanaa, mtoto wa Wini! Kweli shule umekuwa
mkombozi wangu.” Nanaa aliendelea kuwaza. Akavibusu vile vyeti.
Akavitazama kana kwamba vitazungumza jambo lolote. Akajicheka na kuviweka ndani
ya hilo begi.
Aliporidhika kuwa vitu vyake vyote vipo ndani ya hilo begi,
akatoka nalo. “Nilikwambia uniite Nanaa! Wewe vipi? Utavunja
mgongo.” James alisimama kwa haraka mara alipomuona Nanaa anatoka na begi
lake. “Nimeona sio zito.” “Ngoja nikusaidie. Wewe nenda kaoge, upumzike.
Mimi nitaliweka kwenye gari. Asubuhi ya saa 10, nitakuja kukugongea. Uwe
tayari. Hata chai tutakunywa njiani, usije kuamka na kuanza kupika
tena.” Nanaa akacheka. “Muone alivyo furahi.” “Asante kaka.” “Si
unakumbuka nilikwambia shule itakutoa chini na kukuketisha na wakuu? Sasa hayo
ndio matunda yake. Hongera sana.” James aliendelea kujivunia Nanaa mbele
ya wazazi wake, Vai na msichana wa kazi. “Asante kaka,
nimeona.” Nanaa akaitika huku akicheka. Ile nyumba ikageuka kuwa kama kuna
msiba. Watu wote walikuwa kimya wakimsikiliza James na Nanaa. Nanaa alikuwa
anacheka mpaka dimpozi zake zilikuwa zikionekana.
~~~~~~~~~~~~~
Hakuna aliyeweza kumgusa Nanaa, kama
James akiwepo. Walishamjua anamtetea Nanaa tokea mtoto. Alimzungushia wigo wa
ulinzi na utetezi ambao huwezi hata kumuonya Nanaa, akiwepo yeye. Hakuna
aliyemuona anastahili kuzungumza na Nanaa ipasavyo. Alijua ni uonevu tu kwake.
Lakini yeye mwenyewe alikuwa akizungumza naye sana. Na mara nyingine alikuwa mkali
sana kwake lakini hakutaka mtu mwingine aingilie. Alikuwa akisema hakuna
anayemfahamu Nanaa, kwa hiyo huwezi kurekebisha kitu usichokifahamu. Kaka huyo
mtulivu, aliyebeba haiba ya utu uzima, watu waliujua ukali wake James, pale
unapomgusa Nanaa. Aligeuka kuwa kama mbogo, na mama yake alijua. Kila
anapokuwepo James, Nanaa aliachwa kabisa.
~~~~~~~~~~~~~
Msichana wa kazi alimfuata Nanaa
chumbani huku akilia. “Unaniacha Nanaa! Na mimi naondoka kesho tu,
wewe ukiondoka.” Nanaa alianza kucheka. “Ukiondoka watachanganyikiwa.” Nanaa
alishabikia. Wala hakumkataza asiondoke. Usiku huo ukawa wakuagana. Nanaa
alikuwa amechagua zawadi ya taulo kubwa jeupe. Ndilo aliloomba kaka yake
amnunulie. Kwani alikuwa akijifutia khanga wakati wote kila akimaliza kuoga. Kwa
hiyo akatamani taulo jipya. Akajimbia zawadi yake ya kufaulu kidato cha 6,
kutoka kwa kaka yake ni taulo tu. Na kweli James akamnunulia pamoja na hilo
begi. Kwa hiyo usiku huo wa furaha, Nanaa alioga na kujifutia taulo jipya,
kubwa na jeupe. Tayari moyo wake ukaanza kuonja raha ya kule aendako.
~~~~~~~~~~~~~
James alikuja kumgongea Nanaa saa
11:30 asubuhi. “Mbona umepooza tena!?” James akamuuliza Nanaa. “Ingia
huku chumbani kaka.” Nanaa akamvuta mkono James, akaingia ndani akafunga
mlango. “Ujue nimeamka asubuhi kujiandaa, sijamkuta Maria, huyu dada wa kazi!
Nimeenda kumwangalia mpaka kwenye banda la ng’ombe, hayupo. Nimerudi humu ndani
kuangalia begi lake. Ona. Hamna vitu vyake hata kimoja! Ametoroka. Jana alikuwa
akilia hapa kuwa namuacha peke yake, hataweza kazi.” Nanaa alikuwa akinong’ona. “Sasa
hayo sisi hayatuhusu. Twende ukawaage. Tuondoke sasa hivi.” Nanaa akaanza
kucheka taratibu. “Kaka wewe! Nani atawasaidia kazi? Ujue Vai na Viola
hawajui hata kuosha vyombo?” “Najua. Si walikuja kuishi na mimi Dar. Sasa
unataka kubaki uwasaidie?” “Akuuu!” Nanaa akajibu kwa kukataa huku
akipandisha mabega. James akacheka. “Ndio tuondoke sasa.” Wakatoka.
Hatimaye Mji Mwingine,
Maisha Mengine,
Changamoto Nyingine.
Hakuwa akiamini wakati kaka yake
akitoa gari pale kwenye nyumba aliyolelewa na kukuzwa kwa masimango mengi.
Asiamini kama siku hiyo ndio mwanzo wa kuachana na Viola, Alex, baba mkubwa na
mama mkubwa. Nanaa alibaki akiangalia dirishani huku machozi yakimtoka. Hewa
safi iliyokuwa imeenea humo ndani ya gari ya kaka yake, ilimtuliza roho yake na
kujua kwa hakika anaenda kuanza maisha mapya na mazuri.
Njia nzima alikuwa akijaribu
kuainisha aina ya changamoto ambazo labda atapambana nazo huko jijini Dar,
akajikuta anajiaminisha kuwa ataweza tu. “Kama nimeweza kuishi pale kwa mama
mkubwa, naamini hakuna nitakaposhindwa kuishi.” Nanaa aliendelea kuwaza
wakati kaka yake akiendelea kukanyaga mafuta kuwahi jijini Dar. Maisha yakaanze
kwa Nanaa na yeye awahi kazini siku hiyo ya jumatatu.
~~~~~~~~~~~~~
Maisha mapya yaliyojaa
tumaini jipya kwa Nanaa, yanamsubiri mbeleni. Hatimaye anatolewa Moshi na
kuhamishiwa jijini Dar.
v
Changamoto gani zinamsubiri jijini?
v
Ni kweli mema matupu ndiyo yanamsubiri mbeleni baada ya kutoka kwa
Mama yake Mkubwa?
v
Akiwa analia peke yake akidai, ‘lakini Alex Ni Wangu!, huku akideki matapishi ya
Viola, akiwa amebeba mtoto wa Alex huyo huyo, mwanaume wake wa kwanza,
aliyemtoa bikra, kwa ahadi kemkem hasa ya ndoa aliyokuwa akitamani Nanaa,
unafikiri kweli bado ananafasi yakupenda tena?
Usikose Sehemu ya 3 na
nyingine nyingi zilizosheheni Visa na Mikasa ya Maisha.
0 Comments:
Post a Comment