Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 3. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 3.

Nanaa alitua jijini Dar akiwa na James, ambaye alikodisha nyumba ya vyumba viwili na alikuwa akitumia gari ya kampuni akiwa jijini. Gari yake hiyo aliitumia siku za weekend tu kwenye shuguli zake binafsi. Alibahatika kazi kwenye kampuni moja ya simu kama muhandisi. Alisomea mambo ya “Eletronics Engineering”. Kwa hiyo alikuwa na kazi nzuri, na maisha yakueleweka. Lakini kwa kuwa alikuwa na akili ya maendeleo, bado alikuwa kwenye kuwekeza. Kwa hiyo hakuwa na pesa nyingi mkononi. Lakini alijitahidi kuishi maisha ya kawaida tu kama mtu msomi mwenye mshahara mzuri.

Alikuwa na kijana aliyekuwa akifika kumsaidia usafi nyumbani hapo, lakini Nanaa akaanza kushika usukani. Alimfulia, akampikia kaka yake na bado aliweza kufanya usafi ndani na nje ya hiyo nyumba ndogo, bila shida. Kwa kuwa walikuwa wakielewana tokea zamani, furaha na amani havikukosekana ndani ya hiyo nyumba yao.

James alitoka asubuhi na mapema, na kurudi usiku. Wakati mwingine alichelewa kurudi na kumkuta Nanaa alishalala, ila ameachiwa chakula mezani. Alimsaidia Nanaa kufanya maombi ya kujiunga katika vyuo mbali mbali pale jijini, na kumsisitiza kuomba na chuo kikuu cha Dodoma pamoja na Mzumbe. “Huwezi jua utabahatika wapi. Tupia ndoano kila mahali.” James alimtia moyo. Na kweli Nanaa alituma maombi kwenye vyuo vingi tofauti tofauti. Akafanikiwa kupata nafasi katika chuo kikuu cha Mlimani. James alimsaidia kufuatilia mkopo, Nanaa akapata mkopo wa asilimia 80, James akaahidi kumalizia.

Chuo Kikuu Cha Mlimani.

S

hule ya Nanaa ikaanza. Akabadilika, kama siye Nanaa aliyekuwa akiishi mkoani Kilimanjaro. Akanoga na kuiva kwa joto la jiji. Nanaa huyu ni Nanaa aliye huru. Anayejifikiria mwenyewe. Kutoka kwenye manyanyaso mengi. Kazi nyingi mfululizo, leo yupo hosteli! Peke yake. Anajiwazia yeye tu. Kuanzia akiamka asubuhi mpaka usiku anakwenda kulala, jukumu lake likawa ni shule na yeye peke yake. Pesa ikaanza kuingia. Kutoka  bodi ya mikopo na kwa kaka yake. Akaanza urembo wa nywele na kucha. Akatafuta sehemu wanazouza mitumba, akaanza kuvaa vizuri. Akawa anapendeza na kuvutia.  Wakati wote utakaomuona Nanaa aliye msafi. Kuanzia kichwa ambacho alikisuka wakati wote. Kama si rasta, basi alishonea weaving. Hakuacha nywele zake hivi hivi. Alizaliwa na kipilipili kikavu sana. Kwa hiyo wakati wote alizisuka nywele zake. Miguuni na mikononi, safi wakati wote.

Urembo, uzuri na unadhifu wa Nanaa haukujificha kwenye macho ya wengi. Hata wenzake wakaanza kumsifia kuanzia rangi ya mwili wake, umbile na kila kitu mwilini mwake kilipewa sifa. Wanaume wakaanza kuvutiwa. Kila mmoja aliyebahatika kumuona, alitaka na kuota kumiliki penzi la Nanaa. Kuanzia wenzake wa mwaka wa kwanza mpaka wa ngazi za juu. Kila mmoja akajitosa kwa wakati wake. Wakimtaka Nanaa aliyeumizwa kimapenzi. Huku akiwa na hofu ya kuumizwa tena, lakini bado shauku ya kuja kuwa na kwake na wake, haikumwisha moyoni. Ni kweli Alex alimuumiza, “lakini si wanaume wote ni wabaya bwana!” Nanaa alijipa moyo.

Haiba yake ya kupenda kucheka na kuwa msikilizaji mkubwa ikawavuta hata wakina dada wa darasani kwao. Akajikuta ameingizwa katikati ya marafiki wawili wa muda mrefu. Zena na Tia. Waliokuwa wameanza urafiki wao tokea shule ya sekondari. Wakatengeneza kundi dogo la marafiki watatu. Akawa Nanaa, Zena na Tia. Na wote wakajikuta wamepata chumba kimoja ‘main campas’, Hall 3. Lakini siku za weekend mara moja moja na likizo Nanaa alikuwa akirudi nyumbani kwa James. Kipindi cha mitihani alikuwa akipotea kabisa hapo nyumbani. Lakini James alikuwa akielewa na kufurahia juhudi za dada yake. Alimsisitiza kutulia na kuweka akili chuoni.

Penzi La Zac Chuoni.

K

adiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kusitasita kwenye njia mbili katika kufungua moyo kwa mwanaume mwingine. Mara ajitie moyo, mara ajikatishe tamaa, ilimradi tu. Lakini Zac akawawahi wenzake. Yeye akawa king’ang’anizi kweli kweli. Hodi na zawadi tofauti tofauti na za mara kwa mara kwa Nanaa, chumbani kwao hazikukoma.  Kama Zac hakumkuta chumbani hapo, basi aliacha zawadi hizo chini ya mto anao lalia Nanaa, kitandani kwake. Ilimradi tu kuonyesha kumjali na kuwa anamfikiria wakati wote.

Yeye alikuwa mwaka wa mwisho, wakati Nanaa ndio yupo mwaka wa kwanza. Hilo nalo likaongeza nafasi ya kuanza kufikiriwa yeye zaidi ya wengine wote. Nanaa akaanza kumpigia mahesabu. “Naona huyu atanifaa. Si kwa kujali huku!” Nanaa alijiambia huku akicheka moyoni na tabasamu kubwa usoni, mara baada ya kurudi chumbani kwao na kina Tia kumwambia ana mzigo chini ya mto, kitandani kwake. Uliokuwa umeachwa na Zac masaa machache yaliyopita.

Wenzake wote walikaa huku wamemkodolea macho, kuona kile alichokuwa ameletewa safari hiyo. Nanaa akatoa kwa madaha yote. Zilikuwa chocolate nzuri aina ya ‘Godiva’.  Zilibeba umbo la moyo mkubwa na ndani yake zilipangwa chocolate 32 zenye ladha tofauti tofauti ikiwemo caramels, dark chocolate, milk chocolate na truffles. Kila mtu alitoa macho. Hata Nanaa mwenyewe alishangaa. Ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuletewa zawadi ya chocolate. Kwake pia yalikuwa mageni. Akajisikia vizuri mbele za wenzake. Akaanza kuwagawia ili nao waonje.

“Kweli huyu ndio wakunioa. Kwanza atamaliza chuo mapema, kabla yangu. Atapata kazi, na kutafuta sehemu yetu ya kuishi pamoja mara baada ya harusi yetu. Yaani hapa namaliza chuo, naenda kwangu sio narudi tena kwa kaka.” Nanaa akaendelea kumpigia mahesabu usiku huo huku akila chocolate zake.

Ujumbe wa shukurani kwa chocolate nzuri alizofurahia yeye na wenzake kwa Zac, ndio ukawa mwanzo wa mawasiliano na penzi zito kati yao. Shule na mapenzi vikaanza kwenda pamoja. Zac alionekana kumpenda sana Nanaa. Kama kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mwanaume anayemjulia. Hakutaka amuone Nanaa akiwa mnyonge. Wakati wote alipokuwa naye, alimuweka mikononi mwake. Popote na mbele ya yeyote, alimkumbatia Nanaa na kunyesha mvua ya mabusu.

Nanaa alipoona Zac ni mwaname wakueleweka, akamsimulia kaka yake, James juu yake. “Mbona sasa humleti nyumbani?” James akauliza. “Tumepanga akimaliza chuo, ndio tujitambulishe rasmi kwa pande zote.” Nanaa aliongea na tabasamu usoni. “Kumbe mpo serious!?” James alishangaa kidogo. “Huyu anaelekea kaka. Ameapa kunioa, na ananipenda sana na kunijali kuliko nilivyowahi kufikiria. Naamini safari hii Mungu amenifuta machozi.” James aliuona uso wa dada yake vile ulivyojaa furaha ukionyesha kutulia, akajua ni kweli amepata kijana wakueleweka.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakati penzi la Zac likiendelea, na urafiki na  rafiki zake hao wawili, Zena na Tia pia ukaendelea. Vyote vikanoga kote kote, Nanaa akaishi maisha ambayo hakuwahi hata kudhania anaweza kuyaishi. Furaha ya ajabu, kila kitu kikiwezekana. Alipokuwako Tia, ndipo utampata Zena na Nanaa. Waliongozana kila mahali. Wakati Nanaa yupo na Zac, Zena hakuwa amepata mwanaume bado, ila Tia alikuwa na mpenzi wake, Evan aliyekuwa akisoma SUA, mjini Morogoro. Wakati mwingine alikuwa akija jijini kutembea nyumbani kwao na kuona rafiki zake pia hapo Chuo kikuu cha Mlimani na IFM. Tia, Nanaa na Zena hawakuacha kujumuika na Evan na kundi la marafiki zake. Kama ni siku za weekend, basi watatoka kwenda kwenye kumbi na sehemu za starehe pamoja, wao kama kundi. Umjini nao haukukawia kwa Nanaa, kwa haraka sana akachangamka kama mtoto wa jiji.

Ikitokea kama wanatoka siku za weekend au kwenye vilikizo vifupi ambavyo kaka yake anajua angekuwepo nyumbani kwake, na Nanaa akajua kuwa watachelewa kurudi, au watapanga kwenda mahali watachelewa, basi alimtaarifu kaka yake, na kuishia kulala chuoni bila kurudi nyumbani kwa kaka yake. Na mara nyingi Evan anapokuwa jijini, basi Tia ambaye na yeye alifaulu kutokea shule ya wasichana Iringa, na wazazi wake walikuwa wakiishi Iringa mjini, alitumia siku hizo bila shida, kulala popote anapotaka Evan mpaka Evan atakaporudi chuoni.

Evan na Tia.

E

van mtoto wa jijini. Alizaliwa jijini Dar. Lakini shule ya secondary alisomea Tosamaganga, Iringa. Enzi hizo shule hizo mbili, Iringa girls na Tosamaganga walikuwa maswahiba. Ikitokea kuna mziki kwenye shule hiyo ya wasichana wa sekondari ya Iringa, basi shule ya wanaume watakayo karibishwa ni Tosamaganga. Na hivyo hivyo upande wa shule hiyo ya bweni ya wavulana, Tosamaganga. Wasichana wao walijulikana kama ‘Iringa girls’.

Wakati Tia na Zena wanakaribishwa kidato cha 5, kama ilivyo ada. Sherehe nzuri ya shule ilifanyika. Shule ya wanaume Tosamaganga ikakaribishwa ili kuja kucheza mziki shuleni hapo. Na hapo ndipo Evan na Tia walipokutana kwenye mziki. Yeye Evan akiwa kidato cha 6. Japokuwa wote wawili hawakuwa na watu wakucheza nao, washamba kabisa. Zena mtoto aliyetoka kwenye nyumba ya wazazi walioshika dini, Tia mtoto hapo hapo Iringa. Lakini hakuwahi hata kuingia Club. Wakakusudia siku hiyo wasipitwe. Japo waingie kuosha macho. Kujua kinachofanyikaga humo ndani ya mziki.

Walipofika kwenye mziki ndipo Evan akatokea na kumuomba Tia wacheze pamoja. Zena na Tia waliangaliana na kucheka kwa aibu. Kisha Tia akamgeukia tena Evan na kuuliza akiwa hana uhakika sana, kwani hata wao wenyewe walijua kati ya wasichana wote waliokuwepo pale ndani, wao walikuwa wasichana wa kawaida sana kuliko wenzao. “Unamaanisha mimi!?” Tia aliuliza huku akijinyooshea kidole na cheko limemjaa. Evan alicheka kwa kujiamini. Mikono mfukoni. “Ndiyo. Nimeomba tucheze wote.” Tia alimgeukia Zena kwa mshangao. Akiwa haamini.

Evan hakuwa amekurupuka hata kidogo. Yeye na marafiki zake, walishamuona Tia na Zena wakiwa wamekaa peke yao wanacheka kitoto huku wakishangaa jinsi wengine wanavyocheza. Walionekana ni wasichana wenye mambo ya kitoto. Evan aliwaambia wenzake anakwenda kuzungumza na mmoja wao bila kuamua ni yupi kabla. Lakini kadiri alipokuwa akiwasogelea, ndipo macho yake yakavutiwa na Tia. Na huo ndio ukawa mwanzo wao.

Zena na Tia.

Tia na Zena walikutana siku ya kwanza kabisa walipowasili shuleni hapo. Zena akiwa anatokea jijini Dar, na Tia mjini Iringa. Wote waliletwa na baba zao. Wakati wazazi wakilipia ada ya shule, wakajikuta wamebaki wao peke yao. Ikabidi wasalimiane. Wakajikuta wote wanapenda kucheka hata pasipo sababu. Kule tu kujitambulisha mimi naitwa Zena, natokea Dar, tayari cheko. Bila kujijua na Tia naye akaanza kucheka wasijue wanacheka nini. Mvua ilikuwa ikitaka kunyesha. Wazazi walipomaliza taratibu zote za kuwasajili watoto wao wakataka kuwaaga. Baba yake Zena kuwahi usafiri ili akajipumzishe hotelini, na baba yake Tia kwenye gari lake.

Walipotoka na kukuta watoto wao wakicheka kama ndege, ikabidi wafahamiane. Mzee Hiza, ambaye ndiye baba yake Zena aliposema anakimbilia hotelini kabla hajalowa, ndipo baba yake Tia, Mzee Sonzigwa alipomwambia, kamwe mkewe hatamsamehe, kama akisikia aliacha mgeni akalale hotelini na si nyumbani kwao. Hapo ndipo Zena alipojua wapi Tia alipata utundu. Mzee huyo alikuwa mzungumzaji tofauti na baba yake, Mzee Hiza, swala 5. Alikuwa mtulivu sana. Kikubwa alichoweza kufanya ni kushukuru na kucheka tu.

Mzee Sonzigwa alimchukua baba yake Zena, wakaondoka na kuwaacha binti zao wakipelekwa bwenini na kiranja aliyekuwepo zamu siku hiyo. “Baba yako anaonekana mpole!” Tia alisifia. “Sasa ngoja uje ukutane na mkewe. Ndio utauliza walikutana wapi.” Tia akacheka. “Kwani yukoje?” Tia alihoji huku akijiandaa kucheka. “Unamjua kasuku?” Tia aliangua kicheko bila kutoa jibu. “Basi ndio Mama Hiza. Hakuna asiyemjua pale mtaani kwetu. Kwanza hakujaliwa aibu. Hana cha mgeni wala mwenyeji. Akianza jambo, hamalizi. Mshari, hujawahi ona. Usithubutu ukamuanza. Utajuta.” Tia alizidi kucheka. “Sasa baba yako anasemaje?” “Kama vile ulivyomuona. Yeye ilimradi aswali. Basi. Anabaki akimsikiliza tu mkewe. Humuwezi mama Hiza. Watoto wote wanao anza kuongea pale mtaani wanajua kutamka mama Hiza bila kukosea.” Urafiki ukanoga kati yao. Wakajikuta darasa moja mpaka wakafaulu chuo kikuu. Hawakufanya kosa. Wakahakikisha wapo chumba kimoja hapo Hall 3. Na kukusudia kumuongeza Nanaa kwenye kundi lao.

~~~~~~~~~~~~~~

Kwa kuwa walikuwa watundu sana na wachokozi, hawakuacha kumtania Nanaa. Walipenda umbile lake na hawakuacha kumtupia neno kila Nanaa anapoingia darasani kana kwamba hawakuwa wakitoka chumba kimoja. Mbaya zaidi, awe amechelewa na wao  wawe wamewahi lecture. Wataanza, “Jamani mmemuona Nanaa ameingia?” “Nanaa wa ukweli.” Tia atarusha neno jingine kumuunga mkono shoga yake Zena.  “Nanaa wakuvutia bwana!” Zena ataongeza. “Hana atakachoweka mwilini, Nanaa kikamchukiza.” “Nanaa Mashallah!” “Nanaa wa dimpozi.” “Nanaa wa mitego!” “Nanaa wakuumiza mioyo!” “Nanaa ndoto ya wengi!” Zena na Tia watapokezana maneno huku watu wakicheka, na Nanaa akicheka na kutingisha kichwa. “Hivi nyinyi mlifikaje hapa Mlimani?” Mara zote Nanaa aliwauliza.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku moja, kabla ukaribu wao haujachanganya, bali kulala chumba kimoja tu. Wakimuona Nanaa akiwasikiliza na kucheka wakiwa chumbani, na darasani kuwa kama hayupo. Zena na Tia walimwandikia Nanaa barua, na kuamua kuisoma mbele ya darasa zima wakati profesa aliyetakiwa kuingia kwenye kipindi, kuahirisha kipindi hicho. “Jamani! Kuna barua rasmi kwa Nanaa. Sisi kama wapenzi wa Nanaa, tutaisoma.” Zena aliongea kwa sauti kufanya wale waliokuwa wanataka kutoka darasani wasubiri na kuwasikiliza. Nanaa alijiweka sawa, akabaki akiwatizama. Tia na Zena walijulikana kwa vituko. Swali likawa, wakiwa wao wawili peke yao, wanaweza kuzungumza kitu cha maana?

“Kwa Nanaa! Kutokana na tabia ya wanaume wa hapa mjini, kupenda wasichana kama wewe. Na mimi ndugu yako Zena, kushindwa kubahatika kumvutia hata mmoja wao. Kamati ya Tia na Zena, imetafakari kwa kina. Imefikia maamuzi yafuatayo.” Tia na Zena wakatizamana. Wote wakiwa wamesimama mbele ya ukumbi huo wa lecture. Wakaweka sura za kazi. Tia akiwa msomaji, Zena akampa maji, kama kusafisha koo, kisha Tia akaendelea. “Tumeazimia yafuatayo. Nanaa atakuwa rafiki wa Zena. Haraka iwezekanavyo. Tia akiwa katikati yao. Kwa haraka sana, ni lazima Nanaa ahakikishe kila anapokwenda kula, maktaba, au kutembea kokote kule, lazima Tia na Zena wawepo.” “Umesahau kuweka, endapo ataweza kuniunganisha na kaka yake, basi afanye hivyo mara moja. Ili kunusuru hali ya upweke, na kunitoa nyumbani kwa mama Hiza.” Zena aliingilia na kuongezea huku akiwa uso usio na masihara hata kidogo. Watu walizidi kucheka.

Wakiwa mwaka huo huo wa kwanza, tena wote wakiwa wageni hapo chuoni, bado wakiogopana hapo darasani, wakipeana heshima, hawajuani vizuri, Zena na Tia, binti hao waliokwishajulikana ni watundu wa kupindukia, walinyimwa hofu kwa yeyote, wakafanikiwa kumvuta Nanaa katikati yao na kumfanya rafiki. Maisha yakazidi kuleta ladha kwa Nanaa. Marafiki waliomfanya acheke wakati wote na mpenzi Zac! Hakuna jinsi ungemwambia Nanaa amekosea maisha au alizaliwa kwa bahati mbaya, akakubali.

~~~~~~~~~~~~~~

Evan alipokuwa akija kwa Tia hapo chuoni, alikutana na Zena na Nanaa. Utundu mwingi, maneno yasiyoisha na stori nyingi vuliwavutia hata rafiki wa Evan pia. Wakikosekana kina dada hao kati yao, lazima wauliziwe ndipo kikao kinanoga. Evan alikuwa akifika chuoni hapo na gari la baba yake akiwa na rafiki zake. Basi kitawekwa kikao mahali. Watacheka mpaka wanaagana au wakati mwingine aliwatoa wote watatu na kwenda kukutana na marafiki zake huko club. Starehe zinaendelea.

Mwanzoni Nanaa alijitahidi kutolemea upande mmoja. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda na penzi lilivyozidi kuwa zito akajikuta upande wa Zac unaanza kupendelewa zaidi. Ikawa ikimlazimu wakati mwingi wa weekend, ambapo alizoea kuwepo na kina Tia na Zena, kuwepo Mabibo hosteli ambako alikuwa akiishi Zac mpenzi huyo mpya.

Walipokuwa wakimlalamikia, alijitahidi kutoka nao japo kwa masaa machache na kurudi kwa Zac. Ikitokea wamechelewa kutoka kwenye starehe, Nanaa na Zena watarudishwa hosteli. Siku inayofuata kama bado ni weeked, basi Zena atarudi kwa mama Hiza, Nanaa kwa kaka yake au kwa Zac. Wakati Tia akitumia siku hizo, mchana na usiku na Evan. Maisha yakaendelea.

Wakati mwingine watatu hao walipochoka na kusoma, walikwenda kwa Mama Hiza kwenda kucheka. Wakazoeleka nyumbani kwa kina Zena. Na kila walipokuwa wakiondoka mama Hiza, mjuzi wa vitafunio hakuacha kuwatengenezea vitu kadhaa vya kurudi navyo chuoni. Walimpenda mama huyo kwa stori nyingi na vichekesho. Wakati mwingine wa weekend kabla hawajatawanyika, walimpigia simu kujua kama yupo nyumbani au la. Basi akiwaambia yupo, wote wataingia kwenye gari mpaka Tanki Bovu, nyumbani kwa kina Zena. Kwenda kumsalimia mama Hiza, japo kwa dakika chache tu ndipo Nanaa aende kwa kaka yake au Zac. Tia aende kwa Evan au alale hapo hapo na Zena mpaka jumapili usiku.

Basi hapo mama Hiza atawasimulia habari za mtaa mzima. Nani kaachika, nani kafumaniwa, nani anamuhisi mchawi wake. Nani anayejidai anaswali sana lakini mmbeya. Habari zote za mtaani hapo atawasimulia kina Zena mpaka watakapo ondoka. Na alikuwa na uwezo mkubwa sana wakusimulia. Hata jambo likiwa dogo kwa namna gani, lakini mama huyo atalikuza kwa kadiri ya muda wao. Atalisimulia jambo hilo kwa mbwembwe zote, nakuwafanya wacheke mpaka watoe machozi. Na wakati wote mumewe hubaki kimya akimsikiliza na kumtizama kama yuko karibu nao. Maisha yakawa mazuri na yakupendeza.

~~~~~~~~~~~~~~

 Wakati wanakaribia kumaliza mwaka, wakiwa wanakaribia mitihani, Nanaa kumaliza mwaka wa kwanza, Zac kumalizia mwaka wake wa tatu na wa mwisho chuoni hapo, Nanaa kama kawaida yake, alifika nyumbani kwa James siku ya ijumaa baada ya mtihani wake uliokuwa umemlaza macho. Alimsaidia kusafisha na kumpikia kama kawaida huku akimsubiri kaka yake arudi kutoka kazini. James alirudi nyumbani kutokea kazini akidhani Nanaa atalala siku hiyo, lakini kumbe alifika tu kuaga.

“Hivi nimekuja kukuona na kukuaga, kaka yangu. Mitihani imekaribia. Baada ya siku 8 tu, tunaanza mitihani ya kufunga mwaka. Hutaniona kwa majuma matatu na siku kadhaa. Nataka nikatulie kabisa chuoni. Ila nikimaliza tu mitihani, nitarudi hapa nyumbani.” “Si leo ulale? Nitakupeleka kuona movie.” “Acha nijikaze kaka yangu. Nikimaliza mitihani tutazurula wote mpaka uchoke wewe.” James akacheka, Nanaa akachukua mkoba wake na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Nia ya Nanaa haikuwa kurudi hostel kusoma kama alivyomuaga kaka yake. Ilikuwa kwenda kumsurprise mpenzi wake Zac aliyekuwa akimtegemea siku inayofuata ya jumamosi. Walikubaliana kutoka pale hostel na kwenda kujifungia mahali. Wakatumie siku ya jumamosi na jumapili pamoja kabla hawajaingia kipindi hicho kigumu cha mitihani ambacho alijua itakuwa ngumu kuonana mara kwa mara. Nanaa alikwenda mpaka hostel za Mabibo ambako alikuwa akiishi Zac, bila hata kumtaarifu mpenzi wake kuwa anakwenda siku hiyo si kesho yake kama walivyokuwa wamekubaliana.

Nia alitaka kumfurahisha kwani siku iliyopita alimbembeleza sana Nanaa, waanze mapumziko yao siku hiyo ya ijumaa, lakini Nanaa akakataa akimwambia ana mtihani mmoja siku hiyo ya ijumaa mchana na angekuwa na vipindi mfululizo mpaka usiku, kwa hiyo atakuwa amechoka sana. Akamuomba mpenzi wake aliyekuwa amemwambia anahamu naye sana, amvumilie mpaka kesho yake ili apumzike usiku huo. Wakikutana awe na nguvu. Kwa shingo upande Zac akakubali. Lakini baada ya mtihani huo wa mchana, maprofesa wa vipindi vya jioni wakaahirisha vipindi. Ndipo Nanaa akaonelea aende kwa kaka yake. Amsaidie kazi na kwenda kumsuprise mpenzi wake. Waanze mapumziko mapema.

~~~~~~~~~~~~~~

Zac alikuwa na rafiki mfanyakazi. Bachela, aliyekuwa akiishi peke yake kwenye nyumba yake maeneo ya Makongo juu. Mara nyingi aliwaachia chumba kimoja watumie hapo nyumbani kwake kila walipohitaji. Kwa hiyo weekend hiyo, Nanaa na Zac walipanga kuwepo huko.

~~~~~~~~~~~~~~

Alishuka kwenye daladala na lengo la kuelekea moja kwa moja chumbani kwa Zac na rafiki yake akiwa amejawa furaha zote akimfikiria vile Zac atakavyofurahi kumuona usiku huo wala si kesho yake. Wakati anakaribia jengo ambalo lina chumba chao akakutana na rafiki yake Zac ambaye anaishi naye chumba kimoja, Felix. Wakasalimiana na Felix na kutaniana kidogo, kisha wakaongozana moja kwa moja chumbani kwao huku wakiongea na kucheka.

Walipofika mlango wa chumbani kwao, wakasikia mziki mkubwa ndani. Kitu ambacho si kawaida yao. “Jamaa katoka nini? Maana namjua Zac, hapendi kelele.” Felix aliongea huku akifungua mlango. “Labla aliacha radio wazi kukuashiria yupo maeneo ya karibu.” Nanaa aliongeza huku akiwa na shauku ya mlango ufunguliwe waangalie ndani. Na alijiambia yupo tayari kusubiri kama Zac hatakuwepo. “Atakuwa ameenda kufuata chakula hapo Cafe.” Felix Akaongeza baada ya kufanikiwa kufungua mlango na funguo, kisha kuchomoa funguo mlangoni ili waingie ndani.

Alipomaliza kuchomoa funguo, wakaingia ndani bila hata kugonga wakijua kwa kelele zile, Zac asiyependa kelele, hawezi kuwepo ndani. Wote walibaki wameduwaa mara baada ya kuingia na kumkuta Zac  na msichana mwingine aliyekuwa kwenye kundi moja la kujisomea, Ndina na Zac wapo kitandani, uchi na wao wakiwashangaa.

~~~~~~~~~~~~~~

Ndina hakuwa mgeni kwa Nanaa. Walifahamiana na Nanaa. Mara nyingi Nanaa alimkuta na Zac na marafiki zao wengine wakijisomea pamoja. Kama hawakuwa maktaba pamoja, basi chini ya mdigrii wakisoma. Hata mara nyingine aliwakuta cafteria wakila pamoja mara baada ya  lectures au wakiwa wamemaliza kujisomea. Zac hakuwahi kusita kumbusu Nanaa mbele ya Ndina na marafiki zake wengine. Walishawazoea na kuwaelewa. Kwani mara nyingine Nanaa alipowakuta mahali wakisoma, Zac alitengeneza nafasi pembeni yake, nakumtaka Nanaa akae hapo akimsubiria wakati wao wakimalizia kusoma. Basi hapo Zac ataendelea kusoma na wenzake huku amemkumbatia Nanaa. Mara nyingine alimtupia mabusu ya hapa na pale. Ilimradi tu, kuonyesha mapenzi kwa Nanaa. Na kundi lao zima walimfahamu Nanaa kuwa ni wa Zac rafiki yao. Kwa hiyo hata alipokuwa akimkuta Zac na Ndina peke yao, haikumsumbua kwani waliheshimiana sana na Ndina!

Halafu sasa, Ndina alikuwa msichana wa kawaida sana ukimlinganisha na Nanaa. Hakuwa na vitu vya ajabu ambavyo mtu au hasa wanaume wengi wa kiafrika wanaweza kuvitaja na kuvisifia kama jinsi Nanaa alivyo. Mara nyingi Nanaa alipokutana naye mara baada ya salamu, hapakuwa na maongezi mengi. Kwani Zac alimtawala Nanaa wakati wote. Kwa hiyo Nanaa hakumuona Ndina ni hatarishi hata kidogo!

~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alibaki ametoa macho huku maswali mengi aliyotamani kuuliza yakibakia kupiga kelele ndani yake bila mtu wa pembeni yake kusikia. Ndina alishavuta shuka pembeni yake akajifunika nakubaki kimya. Felix yeye aliweza kusogelea radio iliyokuwa na mziki mkubwa, kelele nyingi zaidi pale ndani, akaizima. Nanaa alimwangalia wakati akisogelea radio. Chuki ikamwingia. “Inamaana hata Felix alikuwa akijua? Mbona haonekani kushituka ila kusikitika tu?” Akaanza kujisikia vibaya, akijihisi ni mjinga mbele ya kundi zima lakina Zac. Akidhani walikuwa wakiwajua wote wawili wanapitiwa na Zac. Swali la kuwa aliyeingilia mapenzi ya mwenzake, likaanza kukosa jibu kwa Nanaa. Ni yeye au Ndina!

“Nilijua kwa hakika wewe ni wangu Zac!” Ndilo neno pekee aliloweza kutoka mdomoni mwa Nanaa. Aliongea kwa masikitiko makubwa kutoka moyoni. Zac alijua historia ya Nanaa na Alex. Vile alivyomsaliti. Akamuahidi kumuenzi na kumpa mapenzi ya kweli. Hakutaka kuendelea kujidhalilisha pale mbele yao, akaamua kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Haikuwa mara ya kwanza kwa Nanaa kumsaprizi Zac. Lakini lilikuwa ni jambo ambalo hata Zac alikuwa akilitegemea hasa siku za ijumaa. Alijua wazi Nanaa huwa anakwenda kwenye chumba hicho kumsubiria endapo atachelewa kurudi hapo Mabibo hostel. Naye Zac hakuwa akichelewa. Kila ijumaa baada ya vipindi, aliwahi kurudi hostel akijua aidha atamkuta Nanaa au atamsubiri. Mara nyingi walitumia usiku wa ijumaa pamoja. Kisha siku ya jumamosi, Nanaa alikuwa akirudi kwa kaka yake kama kawaida.

Kwa kuwa nyumbani kwa kina Felix ilikuwa hapo hapo jijini, basi mara nyingi walijikuta wapo peke yao hapo chumbani. Basi siku hizo za Ijumaa walikuwa wakizitumia chumbani hapo, kitanda hicho hicho alichomkuta Ndina yupo uchi usiku huo aliomkatalia yeye Zac na kumwambia atakuwa amechoka mpaka kesho yake ndipo wakajifungie Makongo Juu kwa rafiki yake mwingine Zac, ambapo walikuwa wakipata uhuru wote, ndicho kitanda hichocho na yeye alikuwa akikitumia na yeye akiwa uchi na Zac. Ikamuuma sana Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~

Alitoka hapo asijue ni kama alimfumania Zac na Ndina, au alibahatika kujua ukweli! Hakujua kama amekamatwa na wivu au aibu! Chuki au amejidhalilisha! Kila alipojifananisha na Ndina, bado alijiona ni bora kuliko yeye. Mawazo yakampeleka vile anavyojituma kitandani kumridhisha Zac, “na bado analala na Ndina!? Kwa..”  Nanaa akataka kujinyeshea mvua ya maswali, lakini akasikia sauti ya Zac ikimwita kwa mbali kama anayemkimbiza.

Kwa haraka sana alijionya hata asisimame. Akaongeza mwendo akielekea zilipo daladala, barabarani bila hata kugeuka. Kumbe baada ya kutoka tu pale chumbani, ni kama akili ikamrudia Zac waliokuwa kimya pale kitandani na Ndina. Felix aligeuka na kuendelea na shuguli zake palepale chumbani. Wala hakutoka kuwapa nafasi. Akavuta suruali yake. Akavaa kwa haraka na kuanza kumkimbiza Nanaa bila shati. Kifua kikiwa wazi kabisa.

Alimuona Nanaa akiongeza mwendo kwa mbali kukiwa na giza tayari. Aliendelea kumkimbiza bila viatu mpaka kituo cha daladala akiomba msamaha na kusema ni bahati mbaya. Lakini Nanaa hakujibu kitu.  Akapanda ndani ya daladala huku akikumbuka vile alivyosalitiwa na Alex pia, daladala iliondoka, Zac akiwa amepiga magoti nje ya daladala hiyo akiomba Nanaa ashuke ili wazungumze. Hakumjibu kitu, alibaki ameinama nakushindwa hata kumwangalia Zac nje ya dirisha. Wasafiri wengine walibaki wakichungulia dirishani wakishangazwa na Zac.

~~~~~~~~~~~~~~

Hazikuwa siku nyingi zilizopita tokea Nanaa na Zac wawe na wakati mzuri wa pamoja. Ilikuwa weekend iliyopita tu, pale James alipomwambia Nanaa amsindikize au warudi wote nyumbani, mkoani Kilimanjaro, Moshi, kusalimia wazazi. Nanaa akamkatalia kaka yake na kumsihi sana aende yeye mwenyewe, yeye atakuja kurudi kwa mama yake mkubwa wakati mwingine.

Kwa kuwa ilikuwa katikati ya muhula, James akaonelea ni sawa kumuacha. Asimlazimishe na kuishia kuchanganywa na mama yake mara baada ya kufika huko kwao, akaja kushindwa shule. James alisafiri yeye mwenyewe. Aliondoka siku hiyo ya Jumamosi alfajiri sana. Nanaa akampigia simu Zac na kumuelezea kila kitu. Zac akamuomba wakutane Makongo Juu kwa rafiki yake, kwa kuwa Felix alikuwepo pale hosteli. Hakwenda kwao. Kwa kuwa James alikuwa akirudi siku ya jumatatu, Nanaa aliondoka hapo nyumbani siku ya jumamosi asubuhi na kwenda kujifungia na Zac mpaka siku ya jumatatu ndipo alipotoka hapo na kwenda kwenye kipindi kilichokuwa kikianza saa nne asubuhi.

 ~~~~~~~~~~~~~~

Aliondoka, lakini akiwa ameumia kupita alivyowahi kuumizwa kabla. Moyo ulikuwa unauma kama umechomwa mkuki. “Mbona alionekana kuridhishwa na penzi langu! Wakati wote aliniambia mimi ni mzuri kitandani. Anapenda jinsi ninavyomfanyia kitandani. Na umbo langu linazidi kumsisimua kila nikiwa mtupu mbele zake!” Nanaa aliendelea kuwaza hapo ndani ya hiyo daladala asijue ashuke wapi! Arudi kwa kaka yake au hostel.

~~~~~~~~~~~~~~

Nini kitaendelea kwa Nanaa?

Usikose Muendelezo.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment