Alifika pale akaangaza macho, akamuona Geb amekaa
na Liz, ila Danny na familia yake hawapo. Akawasogelea na
kuwasalimia. “Tunaweza kuzungumza hapo pembeni?” James akiwa
anamwangalia Geb. “Ni nini hicho ambacho hamtaki mimi nikisikie?” Liz
akadakia. Kama kitu kikampanda James. Hasira ikawaka moyoni. Alimwangalia Liz,
Geb akasimama. “Hee! Yaani wewe umetukuta tumekaa hapa na Geb, unamchukua
mpenzi wangu unataka kwenda kuzungumza naye bila mimi! Kivipi?” “Ni nini
Liz!?” Geb akamuuliza kwa kushangaa. “Unashangaa nini na wewe? Tupo
hapa mapumzikoni. Tulikubaliana tuje hapa kama couple ili kupumzika.
Mambo yenu ya siri na biashara, yasubiri mkirudi Dar. Acha kuharibu mapumziko
yetu James. Kama huwezi kuzungumza hapa, basi naomba uondoke usitake kubugudhi
watu. Huo ni ustaarabu tu ambao kila mtu anatakiwa awe nao.” Kidogo James
alianza kuelewa kile Nanaa alichokuwa akikipitia akiwa na Liz. Alimtizama
kidogo tu, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Sababu ya hasira, akaamua kutoka kabisa pale.
Zinda aliona akiondoka, akamuwahi. Akamuita kwa sauti. “Wapi tena
James?” “Nafika mara moja Moshi mjini. Naenda kumuona baba.” “Acha na mimi
niunge msafara.” “Na mimi.” “Hata sisi tunataka tukazurule mjini
leo.” Kila mtu alitaka kuongozana na James. “Ndio vizuri chakula cha
mchana, tukakile mjini. Kuna mahali nitawapeleka, wanapika kitimoto hiyo! Dar
nzima hamna kitu nzuri kama hiyo.” “Acha hizo James.” Baada ya ubishi wa
muda, wakitajiana sehemu ambazo walishakula kitimoto ya nguvu jijini Dar, huku
wengine wakikataa na kutoleana kasoro ya hizo sehemu, James akabakia mshindi
kuwa, anako wapeleka ni bora zaidi. “Mtu kwao bwana!” Wakakubaliana
watoke kwa pamoja, kasoro Geb na Liz walibaki kimya wamekaa tu.
Wakati wanasubiriana sehemu ya kuegeshea magari,
wakaona Danny na familia yake wanaingia. James akawasogelea mpaka pale kwenye
gari. Akamsalimia mama yao bado wakiwa mlemle ndani ya gari. James alikuwa
upande wa dereva ambaye alikuwa Danny kwa wakati huo, ila gari la Geb. Geb naye
aliyekuwa akizungumza na simu na mama yake, walipofika pale, akakata simu na
kusogelea gari. Liz akabaki amekaa pale pale.
James Awajia
Juu Kina Magesa
“Afadhali wote mpo hapa. Nataka kuzungumza na
nyinyi.” James alianza. Walio kwenye gari wakashuka ili kumsikiliza
James. “Kwema James? Halafu mbona naona watu wengi halafu mwanangu Nanaa
simuoni?” “Hilo ndilo nililotaka tulizungumze.” “Vipi tena!?” Danny
akauliza. “Nimemsafirisha Nanaa leo asubuhi kurudi Dar. Nimeamua hivyo.
Ameondoka na basi la saa 11 asubuhi. Mungu akipenda kwenye mida ya saa 5 hivi
atakuwa amefika Dar. Funguo zenu za chumba hizi hapa.” Kama waliomwagiwa maji,
wakabaki wametoa macho.
“Kwa nini umefanya hivyo James? Tena bila
kutuambia!” Aliuliza Geb, huku akilaumu. “Unafikiri hapa nafanya
nini?” James alijibu kwa hasira, na wote wakajua. Ule muonekano wa jana
aliorudi nao baada ya kuzungumza na dada yake, wakajua ulibeba
hasira. “Hapa ndio nawaambia! Ulitaka nifanye nini wakati kila nikitaka
kuzungumza na wewe, mwanamke wako amekukaba huwezi kufanya chochote?” “Sio
kweli James. Nim..” Geb alitaka kujitetea lakini James
akamuwahi. “Nisikilize Geb.” James akajiweka sawa, uso ukiwa mwekundu.
Wakajua tayari za kichaga zimepanda. Masikio na macho yalishakuwa mekundu haswa.
“Mimi na wewe tumetoka mbali sana. Tokea tupo
tunakunywa uji wa shule na kusubiria ugali na maharage. Tokea hujaanza kushika
pesa, mimi nilikuwepo. Tokea hata hujaanza kuendesha hayo magari ya thamani, mimi
na wewe tumekuwa marafiki. Marafiki wa katika shida na raha. Tatizo lako ni
langu, langu ni lako. Tokea tunakuwa, sisi ni marafiki tuliogeuka tukawa kama
ndugu. Na tunaheshimiana sana. Hatujawahi kupishana hata mara moja. Hujui
ninakuwa vipi linapokuja swala la Nanaa. Umenielewa Geb?” James alikuwa
mkali. Alibadilika kama sio yeye.
“Huwa ninamlinda Nanaa na yeyote yule anayetaka
kumuumiza. Hata ikibidi kumlinda na mikono ya mama yangu mimi mzazi, huwa
nafanya hivyo. Hakuna mwanadamu anaweza kumnyanyasa Nanaa mbele yangu,
nikatulia. Jana mnamuacha Nanaa anadhalilishwa pale mbele za watu sababu ya
sweta!? Nyinyi wote watatu! Danny, Grace na Geb mmenyamaza kimya mnaacha dada
yangu anadhalilika sababu ya sweta tu!? Sasa hivi kila mtu anajua kuwa Nanaa
amefukuzwa kwangu, mnamsaidia nyinyi! Ameenda kulala, baada ya manyanyaso yote
yale na kumtangaza kuwa anashida, wewe Grace ulijisumbua hata kidogo kwenda
kumtizama amelalaje?” Kimya.
Akamgeukia Geb. “Na wewe Geb umekaa umemkumbatia
mwanamke wako pale, umejali hisia za Nanaa baada ya maneno yako na mwanamke
wako? Leo asubuhi nakuita kiustarabu tu, nataka tuzungumze, mwanamke wako
anakukataza na wewe umekaa pale kimya! Sasa hivi ni saa saba mchana. Ukiwa
umetangaza kuwa Nanaa ni jukumu lenu au lako, sijui! Umehangaika hata kujua
Nanaa alipo? Umemuona akiwa anapata hata kifungua kinywa? Eti sasa hivi
nawaambia Nanaa amerudi Dar, ndio unajidai kuniambia kuwa sikufanya vizuri!
Mlitaka abaki hapa ili iweje? Muendelee kumnyanyasa dada yangu kwa sweta!? Sijaona
hata anayemjali Nanaa hapa kati yenu. Na kwa majibu aliyonijibu mimi Liz sasa
hivi, na wewe Geb kubaki kimya kama fala, inawezekana unafanya hivyo hivyo kwa
dada yangu.” Watu walishakusanyika kusikiliza.
“Acha kutukana James!” Geb alijaribu
kumuonya. “Nimekutukana Geb. Fanya unachotaka.” James akamsogelea karibu
kishari. “Huwezi kuendeshwa na Liz, mwanamke aliyetukuta sisi tokea
wadogo, na atakuacha tu wewe kama hujui. Anakung’ang’ania sasa hivi kwa ajili
ya hayo magari yakifahari unayobadilisha sasa hivi. Akiona hapati anachotaka
atakuacha kama hakujui. Unashindwa kutumia akili kwenye mambo ya msingi ya
maisha kama haya!? Umekuwa kama mjinga!” James akaendelea.
“Wewe ndio wakuamuliwa na Liz uzungumze na mimi
niliyekuwepo kwenye maisha yako wakati hata yeye pia alikuwepo lakini alikuwa
kama hakuoni! Kama kweli anakupenda, kwa nini asingekutongoza wakati ule
tupo wote pale chuo kikuu cha Mlimani wakati sisi tunakula kwa mama lishe, yeye
anaendesha gari kwenda kula kwenye mahoteli ya nje? Liz si alikuwepo kipindi
hicho!? Kwa nini sasa hivi ndio anakutongoza na kukung’ang’ania kama anakupenda
kweli? Sisi wote tumekuwa na wewe Geb, hatujawahi kutengana. Hata ulipokuwa nje
ya nchi, bado tulibaki kama familia moja. Leo Liz ndio anakuamulia uzungumze na
mimi au la! Kama sio amekugeuza kuwa fala ni nini?” James alikuwa
amekasirika anatamani kurusha ngumi.
“Naomba usiniingize kwenye mazungumzo yenu James.
Niache. Mahusiano yangu mimi na Geb hayakuhusu.” “Nitakupasua huo mdomo Liz
wewe! Usithubutu kunijibu hata kidogo. Kaa mbali na mimi kabisa. Maskini wa
nafsi wewe.” “Maskini mimi au wewe James? Sijawahi kuwa na shida na wala
sina shida. Wewe ndio unahangaika. Na kwa taarifa yako kama mlikuwa mkisubiri
Geb aniache, mtasubiri sana.” “Nani akusubiri wewe? Huwezi wala hutakaa kuwa
kwenye maisha ya mtanzania yeyote hapa Tanzania. Labda ubadilike.” James
akamgeukia vizuri Liz.
“Umekuja unabinua midomo kama unaingia chooni!
Kila kitu unakilalamikia! Kila mtu anashangaa kwa nini umekuja kama hukuwa
unataka kuja. Unamkera kila mtu Liz. Na usifikiri ulimdhalilisha dada yangu kwa
sweta. Ulijidhalilisha wewe mwenyewe na hii familia yako ya kina Magesa.
Mpumbavu tu wewe. Wivu tu.” “Sina wivu na wala sio mpumbavu.” James
aliruka akataka kumkamata Liz, Liz akakimbia kwa haraka. Danny akamshika James
alipotaka kumkimbiza.
“Nitampasua mdomo mimi!” Zinda
akasogea. “Naomba tuondoke James. Tafadhali.” James alikuwa anawaka
kama moto. “Sitaki mtu anishike. Niache Danny, tafadhali. Nyinyi si mmekuwa
mamilionea? Wengine wote tunashida tu. Tunategemea rehema zenu? Usiniguse
Danny. Watu wanawasema pembeni kwa kuwa wanawaogopa kuwaambia kwa sababu ya
vijisenti mlivyopata juzi wakati sisi tunawaona hapa! Mimi siangalii pesa Geb
na Danny. Mnanijua. Utu kwanza.” Akajitoa mikononi kwa Danny kwa nguvu.
“Mmepata pesa, mkaanza kujifanya mmekuwa
wazungu nyinyi! Mmesahau tulikuwa tunalala chini pamoja, tunasubiri mama G,
atupikie chai ya rangi tuwahi mitihani chuoni? Mmesahau tulipotoka nyinyi!?
Mnamnyanyasa Nanaa, mtoto yatima? Kama nyinyi mmetoka kimaisha, atashindwa vipi
kutoka Nanaa? Acheni dharau na manyanyaso ya waziwazi jamani! Mnacheza na Mungu
nyinyi. Mungu ni baba wa yatima. Aliyewapa nyinyi, ndio aliyetunyima sisi.
Lakini hatujui kesho ya Nanaa. Acheni .”
“James! James! Niangalie mimi.” Malii akamuita.
James akageuka. “Kilichotuleta sio hiki bwana. Tumekuja kuchukua mke, turudi
zetu mjini. Naomba yaishe. Twende zetu tukapige maji ya mjini. Tuwanyweshe
washikaji mbege halisi ya JIJI letu. Tukirudi, tunalala mpaka kesho tuchukue
mke, jumapili tunarudi mjini. Tutapata muda wa kuzungumza na Nanaa, tutamuomba
radhi. Wote tuliona alivyodhalilishwa jana. Lakini Nanaa ni familia, kaka.
Wakati wote mambo ya familia ni magumu, ila hatujawahi kushindwa kuyamaliza.
Tupo wote miaka na miaka. Tumefanya mengi pamoja. Naamini hatutashindwa
kumchukua Mmarangu wangu kesho, tumuhamishie mjini kwenye makochi masafi na
kumbi nzuri kama alivyosema Liz. Tuvumiliane tu. Mapenzi hayachagui. Unaweza
kupenda mjini na kijijini.” Malii akaongeza.
“Ila naomba ombi moja Geb.” Malii akamgeukia Geb, baada yakuona James ametulia. “Kama Liz hapafurahii hapa atusaidie hivi, aondoke. Au ajitahidi kuficha hisia zake. Kila mtu ana macho na kila mtu anahisia zake. Tafadhali sana, tunaomba kwa heshima zote, asikanyage hisia za wengine. Naona kila mtu yupo nafuraha hapa. Hata hawa wake zetu tulio oa pwani na kule bara ndani ndani, wamepafurahia hapa Marangu. Basi, ni hilo tu kaka. Amani na tujali hisia za kila mmoja wetu."
"Safari bado ndefu sana hii. Wengi wenu hapa bado hamjaoa. Leo ni mimi tupo hapa
Marangu, kesho ni mwingine. Weza kuta itakuja kutulazimu kwa wengine kwenda
hata na mtumbwi huko ukweni. Lakini kwa kuwa sisi ni ndugu, mama yetu mmoja.
Huyo hapo Mama G, amehangaika kutukusanya tokea watoto. Basi naomba amani
idumu.” “Samahani sana Malii. Samahani kaka.” James
alishatulia. “Naelewa kaka. Ila naomba kikao kihamie mjini basi. Kwenye
kiti moto ya dunia.” Kidogo pakatulia.
“Mama pole na safari. Nimefurahi sana kukuona
huku milimani.” Malii akamsogelea na kumkumbatia mama G. Kila mtu akampa
mkono Mama G, aliyekuwa amenyamaza kimya muda wote akisikiliza. “Sasa wewe
nenda kapumzike. Jioni tukirudi, utupe neno la busara.” “Msilewe sasa. Hasa
wewe Malii. Kesho ni siku muhimu sana kwako.” “Na umuhimu huo ni wewe kuwepo
hapa. Ukishuhudia na mimi mwanao napata mke. Unakumbuka ulivyokuwa
unatutengenezea kahawa usiku ili tusome kipindi cha mitihani? Sasa shule
imeisha, shuhudia nachukua jiko.” Mama G, akacheka kidogo.
“Haya. Njooni wote tushikane mikono tuombe. Hili
jambo ni la baraka sana. Tusikubali shetani aliharibu.” Wakakusanyika
wote, wakatengeneza duara kubwa, wakashikana mikono. Mama G akaanza kuomba.
Aliomba toba kwa watoto wake hao wote. Akawatakasa kila mmoja, huku akimsihi
Mungu awasamehe. Akamshukuru Mungu kwa ulinzi wake juu ya vijana wake hao, na
mke mtarajiwa wa Malii, kijana wake. Akaomba amani na ulinzi kati yao, huku
akisihi Mungu amlinde Nanaa popote alipo na amfanikishe. Akamaliza.
Mpaka anasema amina, kila mtu akawa ametulia.
Wakaanza kupiga makofi. “Afadhali umekuja mama.” Kila mtu alirudi
kumpa mkono mama G. “Haya. Na mimi nimefurahi kuwaona. Ila nataka muwahi
kurudi na muwe waangalifu huko mabarabarani. Madereva wote msinywe. Mtakuja
kunywa hapa mkirudi. Umenisikia James? Wewe unayewapeleka wenzako usiweke pombe
mdomoni.” “Nimeelewa mama. Saa 12 jioni nawarudisha. Ngoja nikamsalimie Mzee.”
“Haya. Fikisha salamu zetu. Tafadhali macho yako yote yawe kwa Malii. Arudi
akiwa na meno yake yote.” Wote wakacheka. Wakaingia kwenye gari,
wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Alibaki Mama G na wanae. Akamwangalia
Geb. “Mbona midomo imekukauka? Umekula wewe?” Akamuuliza Geb kisha
akamgeukia Grace. “We Grace?” “Hajala tokea jana njiani alipopewa vitu vya
kula na Nanaa. Korosho na soda tu.” Grace alijibu huku anarudi kwenye gari
kuchukua mizigo ya mama yake. “Hata macho hayo yanaonekana hujalala
vizuri. Twende ukale halafu ulale kidogo.” “Sisikii njaa mama. Kwanza pole na
safari.” “Asante.” “Vipi magoti?” Geb akamuuliza mama yake, huku
akimuangalia magotini. “Aaah, hivyo hivyo. Lakini usiwe na wasiwasi.
Safari ilikuwa nzuri. Fupi. Hata lisaa halikuisha huko angani. Twendeni ndani
nikainyooshe kidogo.” Wakaongozana mpaka kwenye chumba ambacho alitakiwa
alale na Nanaa.
Wakalikuta lile sweta kitandani. “Sweta
lenyewe ndilo hili lililozua kizaizai!?” Mama G akalinyanyua akalitazama
na kulitupa tena palepale kitandani. Kila mtu akanyamaza. “Kilichowashinda
kumjulia hali Nanaa, nyinyi ni nini?” Mama G akauliza huku
akikaa. “Usiku sisi tulikuwa tumechoka mama, na asubuhi tuliamka mapema
ili tukuwahi wewe uwanja wa ndege.” Mama yao akamgeukia Geb aliyekuwa
amenyamaza kimya. Akajua hataongea. “Njoo ujilaze hapa.” Bila aibu
wala kubisha, Geb akapanda kwenye kilekile kitanda alichokuwa amekaa mama yake.
Akajilaza vizuri pembeni yake na kugeukia ukutani.
“Naomba hilo blangeti hapo.” Mama G alimtuma
Danny. Danny akavuta blangeti kutoka kwenye kitanda kingine, akamkabidhi mama
yao. Akamfunika vizuri Geb. “Hajala huyo mama. Tokea jana hajaweka kitu
mdomoni.” Grace alimuwahi mama yake kabla hajamfunika vizuri. “Wewe
unamjua Geb. Hawezi kula akiwa kwenye hali hiyo. Mwache alale kidogo. Akiamka
ndio atakula.” Alimjibu Grace huku akiendelea kumfunika.
~~~~~~~~~~~~~
“Nitolee simu yangu kwenye pochi nimpigie Nanaa.” Grace akatoa simu. Akamkabidhi mama yake baada ya kupiga simu ya Nanaa. “Mama!” Nanaa akapokea. “Umefika salama?” “Ndiyo. Nashukuru Mungu nimefika salama. Pole na safari.” Nanaa akajibu. “Asante. Mbona nakusikia kama upo kwenye basi tena!?” Mama G, akauliza. “Nipo kwenye daladala mama yangu. Dalali ameniita nikaangalie chumba maeneo ya Mwananyamala. Ndio nipo njiani. Na simu inaishiwa chaji. Naomba mwambie kaka James nilifika salama, asiwe na wasiwasi. Nikirudi nyumbani nitaichaji kisha niwapigie tena, tuzungumze vizuri.”
“Sasa utalala wapi na mimi nyumba nilifunga. Sikujua kama utarudi.” “Usiwe na
wasiwasi mama yangu. Nitapata tu mahali pakulala. Naomba nikuage kwa sasa ili
simu isiishe chaji kabisa nikashindwa kuwasiliana na dalali.” “Naomba usisahau
kunipigia Nanaa. Sitalala mpaka nikusikie.” “Usiwe na wasiwasi mama!” “Hapana
Nanaa. Nitataka kujua upo wapi, na unalala wapi. Kama ulikula na kama
ulifanikiwa.” Wakamsikia Nanaa akicheka. “Haya mama yangu. Basi nitajitahidi tuwasiliane. Uwe na
wakati mzuri. Nyoosha miguu upumzike kesho ukacheze kwenye harusi.” Mama
G akacheka kidogo. “Asante mwanangu. Nasubiria
simu yako.” “Usijali.” Nanaa akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
“Nanaa anamoyo mwepesi huyu
mtoto!” Mama G, aliwaza kwa sauti. “Nimemsikia anacheka mwenyewe!” Grace
akaongeza. “Anapenda kucheka kama nini sijui! Namtania namwambia ndio
maana mashavu yake yamebonyea. Kila kitu yeye kucheka.” Kidogo
walifarijika baada ya kuzungumza na Nanaa.
“Ila niwaambie ukweli kabisa wanangu. Kama
tukishindwa kumtunza Nanaa, mjue wazi tumeshindwa kutunza baraka za Mungu. Na
hatutabaki kama hivi tulivyo. Wote mlikosea jana. Mlikosea sana. Lazima
tukubali kosa na mjue James alikuwa sahihi japo aliongea kwa hasira. Baraka
mlizonazo leo, hamjui mlizitoa wapi. Danny, uliweza kukusanya wale vijana wote
wale, ukatuletea nyumbani. Yatima na walio na makwao palepale jijini, walipaita
kwetu ni kwao. Ni nyinyi mliwafanya wanipende na kunithamini. Ni nyinyi ndio
mliwageuza kutoka kuwa marafiki mpaka wakawa ndugu.”
“Kundi lote lile ni sisi tumelikusanya na
kuwaunganisha. Wamekuwa kama kondoo wetu. Wewe Danny ndio wamekuchagua kama
mwenyekiti wao. Umekuwa ni mchungaji wao, halafu gafla mnawaacha! Mnajitenga
nyinyi wenyewe! Lazima kutatokea vurugu sana. Kuweni makini kwa kila jambo. Wanawaangalia
kwa karibu sana. Na si kwa mabaya, ni kwa kuwa wanawapenda. Hakuna hata mmoja
wao pale anayetaka kuwapoteza nyinyi. Ndio maana popote mlipo, au popote
mnapoishi, wanawafuata. Na hawajihesabu ni wageni kwenu. Ndio maana wanaingia
na kutoka pale nyumbani, watakavyo. Naombeni msijisahau sasa hivi.” Wote
walikuwa wamenyamaza.
“Mmesikia?” Mama G akawauliza. “Binafsi
nimeelewa mama. Na ninakiri ni hasira tu ndizo zilinifanya ninyamaze. Kama
ningeendelea kuongea jana, au ningefungua mdomo wangu, ingekuwa mbaya zaidi
mama yangu. Wewe unanijua. Usingekuta hii hali ya leo. Au haya yaliyotokea leo,
ingekuwa mbaya zaidi yake. Kumbuka na mimi ni yatima kama Nanaa. Nilikuwa
nikitangatanga kwenye majumba ya watu kama Nanaa. Mpaka mliponifungulia mlango
kama hivi Nanaa. Kwa hiyo naelewa, na ninajua ugumu anaopambana nao
Nanaa.” Danny aliongea kwa hisia zote.
“Mimi unanijua mama. Nikiongea sana kichwa
kinauma au maneno yanakwama na ninaishia kulia kama mjinga. Nilifanya kwa
sehemu niliyoweza mpaka tukafika hapa. Japo nahisi sijui sikusaidia sana au
nilichelewa! Sijui. Lakini namuelewa Nanaa. Ni kweli alikuwa na wakati mgumu.
Na niliumia sana jana usiku. Ni kweli alidhalilika. Nakiri
tulikosea.” Grace aliongea upande wake.
“Na kwa upande wa Geb, mimi namfahamu Geb. Heri mimi nikiwa na hasira huwa naweza hata kuongea kidogo. Geb alikuwa kwenye nafasi ambayo kunyamaza pekee ndio ilikuwa suluhisho sahihi. Sio kwamba namtetea. Jana angeongea zaidi, ingekuwa mbaya zaidi. Nilimsifu jinsi alivyoweza kunyamaza. Japo nilijua alikuwa anaumia sana moyoni. Hata kule kuongea pale mbele za watu na kutoa yale maelezo yote yale, ilimlazimu. Na nashukuru alijibu. Ingekuwa mbaya zaidi kama angenyamaza."
"Kwa kujibu kwake
jana, Geb alituliza ugomvi mkubwa sana ambao Liz alikusudia kuzua chuki kubwa
sana katikati ya hawa marafiki. Geb hakuwa amekusudia kumdhalilisha Nanaa. Wote
tunajua jinsi anavyompenda Nanaa. Lakini mama, walimbana kwenye kona, ilikuwa
hamna jinsi lazima ajieleze vile tu. Lasivyo wangemuona msaliti.” Kama kawaida
ya Grace kumtetea mdogo wake.
“Tukirudi nyumbani, tutapata muda na Nanaa.
Tutazungumza naye. Ninamfahamu Nanaa. Ataelewa tu. Huwa hawezi kuweka kinyongo
yule mtoto. Atasamehe tu.” Mama G, akamalizia. Wakatulia kidogo kila mtu
akiwaza lake.
“Basi kwa kuwa bibi amekuja, wewe kaa hapa
na bibi. Sisi tunakuja sasa hivi.” “Namtaka mama.” “Kwani Fili vipi bwana!?
Unataka kuharibu safari yangu nzima!” Mama yao alianza
kucheka. “Kamganda mke wangu tokea jana! Sina raha!” “Muache mtoto Danny.
Mimi namwambia labda sababu yupo kwenye mazingira mageni, halafu hakuna watoto
wengine. Anaogopa.” “Sasa anachoogopa hapa ni nini wakati bibi yake huyu hapa?
Yaani amepooza kabisa! Haongei, anamtaka mama yake amkumbatie wakati wote
bwana! Sina raha na mke wangu!” “Mmemwangalia homa lakini?” Bibi yake
akauliza.
“Danny amempima, hana homa.” “Eti Fili.
Unaumwa?” Bibi yake akamuuliza kwa upole. “Namtaka mama.” “Yaani hiyo
sentensi inazidi kuniudhi! Ameikazania tokea jana! Kama ananikomoa
vile!” Grace na mama yake wakaanza kucheka. “Si ukae hapo kidogo tu,
tunakuja sasa hivi. Umesikia Fili mwanangu?” Danny aliendelea kubembeleza,
lakini Fili akanyamaza. “Usiwe na wasiwasi Fili mwanangu. Ongea na bibi
kidogo tu, tutakuja. Sawa? Mfundishe ule wimbo wako wa shule.” Fili
alianza kutoa machozi.
“Hii safari kweli imeingiwa mkosi.” “Usiseme
hivyo bwana Danny! Hii sio kawaida ya Fili. Lazima kuna jambo tu. Ngoja nilale
naye hapo kitanda cha pembeni. Akilala nitakufuata.” “Nasubiria hapahapa.
Hukawii na wewe kulala kama jana usiku. Jana nimejikuta nimelala
peke yangu usiku kucha! Fili kalala na mke wangu. Leo umuache hapo sisi
twende.” Grace alianza tena kucheka. “Hata mimi nilikuwa nimechoka na
safari, wala sio Fili peke yake.” Mama G alikuwa akicheka huku ameinamia
simu yake. Danny akakaa. Grace na yeye akapanda kitandani akamkumbatia mwanae
wakalala.
Nanaa huko
Jijini.
Nanaa alikutana na dalali. Bei ikamshinda.
Ilikuwa vyumba viwili na sebule. Inajitegemea jiko na kila kitu. Alimwambia
yule dalali asingeweza. Bei nikubwa sana kwake. Na anatarajia kurudi chuoni
baada ya muda mfupi. Asingependa sehemu itakayomlazimu kuchukua daladala mbili
hasa kodi ikiwa juu kiasi kile. Nyumba ilikuwa nzuri ya kisasa. Isingeendana
kabisa na hadhi ya Nanaa kwa wakati ule.
Akakumbuka ofa ya Zinda. Kupewa gari na nyumba.
Ndoa ya haraka. Au wawe wote kwa wakati huo. “Nikimkubali Zinda,
sitahangaika tena!” Umasikini ukaanza kumsumbua Nanaa. “Nimejizubaisha
kwa Jeff, mpaka akapata mwingine. Nina tatizo gani mimi!?” Nanaa
akaanza kujichukia. “Lakini hapana. Acha nijikane, mpaka nione huo mwisho
wangu.” Wakaagana na dalali kwa makubaliano ya kumtafutana tena pindi
atakapo pata sehemu nyingine inayoendana na yeye.
Nanaa Nyumbani
Kwa Antii.
Wapi pakwenda baada ya hapo ndio ukawa mtihani.
Kama kawaida ya wachaga kusaidiana popote walipo. Nanaa akamkumbuka matroni wao
wa pale chuoni. Alikuwa mama wa kichaga, aliyetokea kumpenda sana Nanaa.
Japokuwa hakuwa akimjua baba yake, lakini alijua mama yake ni mchaga kwa
hakika. Akajenga mazoea na yule mama akimtambua kama mchaga mwenzake. Kwa hiyo
Nanaa hakuacha kuwa akipita hapo kila anapoelekea chumbani kwake na kumpa
salamu. Jina la Antii likawa la kawaida kwao. Wakawa wanaitana Antii yeye na
matroni.
Nanaa akaona ndiye mtu wakumpigia. Japokuwa simu
yake ilishaonyesha dalili zote za kuzimika, lakini hakupata shida wala kutumia
muda mrefu wa kujieleza kuwa anatafuta mahali pakulala usiku huo.
Akakaribishwa. Alifika nyumbani hapo. Antii alikuwa mzungumzaji, Nanaa
mchekaji. Stori zikaanza, Nanaa kucheka tu wakati wote. Mpaka wanaagana kwenda
kulala, hakuwa ameulizwa kulikoni japo alikwenda na begi lake. Mama huyu wa
kichaga hakuwa ameolewa. Japo alikuwa na watoto wakiume wawili na wakike mmoja,
ambaye alikuwa anasoma hapo hapo chuoni, lakini alikuwa likizo na kaka zake,
huko migombani kwa bibi na babu yao. Nanaa akajikuta na yule mama tu mle
ndani.
Antii alikuwa ni matroni wa hosteli za wasichana
palepale chuo kikuu cha Mlimani, lakini pia anabiashara zake zinazomwingizia
pesa. Anasomesha watoto wake yeye mwenyewe na mkubwa alishaoa. Maisha yake
yalikuwa yakuhangaika kuanzia saa 11 asubuhi yupo macho mpaka usiku
anakimbizana na pesa ya jiji la Dar. Alishamwambia Nanaa asubuhi anawahi
mahali, akiamka yeye ajitengenezee chakula na maisha yaendelee kama kawaida,
asimsubiri.
~~~~~~~~~~~~~
Usiku alijisahau kuchaji simu yake, sababu ya
stori. Akalala akiwa hoi. Hata mama G, hakumtafuta tena. Asubuhi akiwa peke
yake pale ndani ndipo akakumbuka anatakiwa kumtafuta kaka yake James na Mama G,
kuwaambia alipo. Akawasha simu mara ilipojaa. Tayari ilikuwa saa tano.
Wa kwanza kumpigia simu akawa kaka yake. “Mbona unanitia wasiwasi?” “Pole kaka. Nipo kwa Antii. Si unakumbuka nilikwambia alivyo muongeaji? Tulilala saa sita kwa stori.” “Na unavyopenda stori wewe!” “Kama ulikuwepo. Nilikuwa nina kazi ya kucheka tu.” “Lakini nimefurahi kama umepata wakati mzuri. Sasa umemwambia nini?” Nanaa akamuelezea kaka yake habari za chumba kwa ufupi.
“Lakini
Antii hata hajauliza. Yeye kafurahi kuniona tu. Akaanza stori zake. Lakini
kaka, itabidi nizungumze naye atakaporudi. Ili aniweke mpaka nitakapopata
chumba changu. Ni mama mzuri. Mtu wa nyumbani. Kama nilivyokwambia,
ananipenda tokea zamani. Haachi kunitafuta na kunijulia hali na maendeleo
yangu. Sidhani kama atajali nikijishikiza hapa kwa muda mpaka nitakapo pata
chumba changu.” “Sawa kama atakubali kuishi na wewe. Itakua jambo zuri.
Utanijulisha basi atakavyo kwambia.” “Haya kaka. Asante.” “Unasalimiwa na Mama
G.” James akamuwahi kabla hajakata simu. “Mwambie
nitampigia kwenye simu yake.” Nanaa akakata simu.
Akampigia mama G. “Pole
mama yangu.” “Mmmh! Umeniweka roho juu wala sijalala.” “Mbona sauti yako nzuri
kama uliyelala usingizi mzuri?” “Si ndio sauti yangu ilivyo!?” Nanaa
akacheka sana. “Unavyojisifia!” “Kumbe. Hebu
niambie kama ulifanikiwa.” “Vyumba ni ghali, mama! Sio kama nilivyojipanga.
Nimepelekwa sehemu jana, pazuri, lakini pesa nyingi. Hata hivyo ni pakubwa
sana. Mimi na mabegi yangu tu, mmh! Tutapwaya.” Wakacheka.
“Sasa, sasa hivi uko wapi?” Mama G akauliza tena. “Nipo kwa mama mmoja amenihifadhi. Ni mama mzuri sana.
Nimelala nacheka tu.” “Na unavyopenda stori wewe!” “Kama ulikuwepo! Nilikuwa na
kazi yakucheka tu hapa. Ametoka muda si mrefu, tulikuwa tukicheka hapa.
Haishiwi vituko.” “Nimefurahi kusikia una furaha Nanaa.” “Mimi mzimaa. Wewe
furahia harusi. Nitakupigia ukirudi.” “Unanipigia au unarudi nyumbani?” “Naona
nitaendelea kuishi na huyu mama tu. Ila mkirudi, naomba unijulishe ili nije
kuchukua mizigo yangu.” Kimya.
Nanaa akaangalia simu kujua kama ilikatwa. “Mama!” Akaita. “Nakusikiliza.”
“Basi tutawasiliana. Nikuache ujumuike na wanao. Angalia tu Zinda asije kukupa
pombe.” “Hapa nimeshaanza kulewa.” “Mama wewe!” Nanaa akashituka
sana “Nakutania bwana!” “Haya mama yangu. Have
fun. Baadaye.” “Sawa.” Mama G, alikata simu lakini kila mtu
alimuona alivyobadilika sura.
“Nanaa hajambo?” Grace aliyekaribu naye
akauliza. “Mzima. Anacheka tu kama kawaida yake. Atakuja kuchukua mizigo
yake tukirudi sisi nyumbani. Amepata sehemu nyingine yakuishi wakati anatafuta
chumba chake. Analalamika vyumba ni garama. Nimeumia sana. Najiona kama sipo
tayari kuachana na yule mtoto! Sijui nikumzoea sana!?” Grace akanyamaza,
Danny hakuongeza neno. Geb naye alikuwa akisikia kila kitu kwani hakuwa mbali
nao. Akanyamaza tu.
~~~~~~~~~~~~~
Kuanzia asikie Nanaa anahama nyumbani kwake, Geb
hakutia hata maji mdomoni. Hata kwenye sherehe alikuwa kimya. Bila kula wala
kunywa. Watu walisherehekea, lakini Geb alikuwa kimya. Grace akajaribu kumpa
hata soda, lakini hakuinywa. Mama G alikuwa upande wa wazazi wa Malii wakiongea
na kucheka mpaka sherehe ilipoisha.
Baada ya sherehe kuisha Grace akamuita mama yake
pembeni, kabla hawajaingia kwenye gari kurudi hotelini. “Ujue tokea mtori
uliomlazimisha Geb kula mchana, akala vijiko sijui vinne sijui vitano, ujue
hajatia kitu kingine mdomoni?” “Haiwezekani! Hata kwenye sherehe!?” “Nimempa
soda, akaipokea na kuiweka chini ya kiti. Mpaka tunatoka pale, hakuiweka hata
tone mdomoni.” Mama G, akanyamaza.
“Sasa na wewe kwa nini uliongea pale mbele yake
kama Nanaa anahama nyumbani, mama jamani!? Si ungesubiri mpaka turudi nyumbani!”
“Nahisi nikujisahau bwana! Nitazungumza naye tukifika hotelini.” “Sidhani
kama kuna safari ya Arusha tena!” Grace akaongeza. “Atafia njiani kama
asiporudi na kumuona Nanaa. Heri kesho alfajiri tugeuze.” Wakaingia kwenye
gari. Geb alikuwa amembeba Fili muda wote wa sherehe, akawa ameshatangulia naye
kwenye gari. Alikuwa amesinzia muda wote wakati amempakata.
Walifika wote ndani ya gari, Geb akawasha gari na
kuondoka bila ya kuongea chochote. Danny na mama G wakaendeleza stori za kwenye
sherehe. Walisimuliana vituko vilivyotokea kwenye shuguli nzima, wakawa
wanacheka wao wawili tu. Geb na Grace wakiwa kimya. Walipofika hotelini kabla
ya kushuka kwenye gari mama G, akaanza. “Nashauri Danny uwaage wenzenu
usiku huuhuu, ili kesho alfajiri sisi tuondoke hapa turudi nyumbani.” “Wazo
zuri mama.” Danny akaafiki. Akamchukua mtoto wake na mkewe, wakaondoka na
kumuacha Geb na mama yake kwenye gari.
~~~~~~~~~~~~~
“Nitazungumza na Nanaa, ili asihame. Tuendelee kuishi naye.” Mama G akavunja ukimya wakiwa wamebaki wao wawili kwenye gari. Geb akamgeukia mama yake. “Unafikiri baada ya yote haya atakubali na wakati nimemsikia akisema amepata sehemu nyingine ya kuishi, na kaka yake ameshamkubalia?” Geb akauliza akionyesha kukata tamaa. “Wewe ushawahi kuona nimekuahidi kitu halafu nikashindwa kukutekelezea?” “Nahisi nimeingiwa na hofu mama. Hali haikuwa nzuri. Halafu siku..” Geb akakwama.
“Grace na Danny wamenieleza kila
kitu. Wewe usiwe na wasiwasi. Nataka utulize mawazo. Upate mapumziko mazuri.
Kama hakuna jingine litakalozuka, ikawa ni haya tu yaliyotokea njiani na hapa
hotelini, nakuhakikishia Nanaa atarudi nyumbani.” Geb akavuta pumzi kwa
nguvu, akazishusha taratibu kama kujituliza “Asante mama.” Geb
akashukuru.
“Twende chumbani kwangu ukanywe soda na karanga.” “Sijisikii kula mama. Naomba nilale tu.” “Basi kama ndio hivyo, mimi sitazungumza na Nanaa.” “Mama!!” Geb akamshangaa mama yake. “Sasa kwa nini huridhiki moyoni wakati nimekwambia kesho Nanaa atalala nyumbani?” “Sasa si mpaka akubali?” “Kwa hiyo huniamini?” Mama G akamuuliza.
“Basi
mama. Twende nikanywe hiyo soda.” “Nimesema na karanga.” “Tumbo limejaa mama
yangu. Lipo kama lina gesi, acha nikanywe tu soda.” “Usinichezee akili Geb! Nimesema
hilo ndilo sharti langu. Hutaki kula, basi.” Geb akacheka kidogo na
kutingisha kichwa. “Unavyoninyanyasa mama wewe!” “Kumbe!” “Haya twende
mama yangu.” Mama G aliwapenda wanae. Alitaka kuwapa chochote wanachotaka.
Akishindwa, basi anakimbilia kufunga na kuomba. Atamlalamikia Mungu kwa machozi
mpaka afanikishie wanae. Na watoto wake walimjua hivyo.
~~~~~~~~~~~~~
Kwa shutuma
zote zile, Nanaa atakubali kurudi kuishi nyumbani kwa Geb tena akiwa amepata
sehemu nzuri na tulivu ya kuishi?
Usikose Sehemu ya 17.
0 Comments:
Post a Comment