“Kwa ujumbe?” Danny akageuka
tena na kuuliza. “Nilijua tu hayajaisha! Ukoje Danny lakini?” “Si
unijibu roho yangu itulie?” “Wala haiwezi kukutulia. Mimi nakujua.” “Sasa kama
unajua si heri unisaidie tu.” “Siwezi kuweka hii simu chini kwa kuwa ni mambo
ya kikazi.” “Basi wapigie.” “Kelele Danny. Ni nini lakini?” “Unataka
kunichanganya tu Grace mke wangu.” “Wewe usichanganyikiwe. Tulia tu, endelea
kupiga stori na Geb.” Danny akatulia kama dakika tano. Kisha akageuka
tena.
“Bado
tu!?” Danny akauliza. Grace akanyamaza huku ameinamia simu yake. Danny
akamuona kama anatabasamu huku anaandika kitu. “Grace?” Danny
akaita. “Subiri kidogo Danny.” Grace akamjibu mumewe huku macho yapo
kwenye simu na tabasamu usoni. Nanaa na Geb walikuwa wakiwasikiliza maongezi
yao. Lakini wakawa kimya bila kuingilia.
“Mambo gani hayo ya kikazi
mnazungumza mpaka unacheka!? Anakwambia nini?” Danny akauliza akisikika
tayari amepaniki. “Grace?” Danny aliita tena. “Namalizia sasa
hivi. Subiri kidogo nitakujibu.” “Hapana. Naomba mimi nihamie nyuma.
Simamisha gari Geb.” “Bwana wewe kaa huko huko mbele.” Grace
aliongea kwa upole huku macho yapo kwenye simu. “Hataa! Simamisha gari
Geb. Sasa hivi. Hapa hapa. Nataka nikakae na mke wangu hapo nyuma, tutume wote
hizo jumbe za kikazi.” Nanaa alikuwa anasikiliza.
Akasikia gari linawekwa pembeni ya
barabara, akajifunua. “Nanaa, samahani sana. Naomba uje ukae hapa mbele.
Mimi nataka nikae na mke wangu hapo nyuma.” “Hamna shida.” Nanaa akashuka.
Akakaa mbele, Danny akamsogeza mtoto dirishani, Grace akakaa katikati kisha
Danny dirishani. Safari ikaanza tena. “Sasa mbona hutumi tena hizo
jumbe?” Danny akamuuliza mkewe. “Simu hii hapa kaa nayo. Nilikuwa
situmi ujumbe wowote. Nilitaka kukurusha tu roho ili uhamie tu
hapa.” Nanaa alitamani kucheka lakini alikuwa na mshangao. Lakini Grace
alikuwa akicheka. “Acha bwana Grace!” “Ukiwa mbali siwezi kulala Danny.”
“Sasa si ungesema tu?” “Usingekuja kwa haraka kama hivi. Halafu Geb
asingesimamisha gari kwa haraka. Ukiwa na hasira huwa anakusikiliza kwa
haraka.” Bado Grace alikuwa anamcheka mumewe.
“Lala basi.” “Lakini ujue nimefurahi
umekuja hapa.” “Aaah!” “Aaah nini sasa Danny mme wangu? Hapo ulipo ndio
nitalala haraka sio vile ulivyokuwa mbali.” “Unapenda kunichanganya kweli
Grace!” Danny alisikika ametulia kidogo. “Yaishe basi. Ngoja nilale
kidogo. Nahisi kichwa kimejaa usingizi.” “Lala basi hapa.” Grace akamlalia
mumewe mapajani, akalala. Danny hakuongea tena. Akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~
“Mbona kama
unatetemeka baridi?” Geb alimgeukia Nanaa akaona amejikunja na amekalia
mikono yake. “Hapa mbele ni baridi zaidi.” Nanaa akajibu. “Basi
funga hapo na pale ili upepo usitoke upande wako.” “Haitakusumbua wewe?”
“Hapana. Upande wangu upo wazi. Napata upepo kama kawaida. Umekumbuka
sweta?” Geb akauliza. “Nafikiri nimeweka kwenye begi.” “Tutaingia
hapo Korogwe muda sio mrefu. Tutasimama tuangalie.” “Lakini nipo sawa. Hamna
haja ya kusimama sababu hiyo.” Geb akamwangalia kidogo, akarudisha macho
barabarani.
“Huchoki kuendesha?” Nanaa
akauliza. “Sio kwa safari fupi kama hizi. Huwa tunaendesha na kina Danny,
James na Zinda safari ndefu sana. Wakati mwingine mpaka Mwanza au Tabora
nyumbani kwa kina Zinda. Na huwa napenda kuendesha mimi. Kidogo huwa
wananisaidia. Lakini hapo Moshi ni karibu sana. Sihitaji msaada.” Nanaa
akatulia.
Baada ya muda mfupi akaona kibao cha
Korogwe, akajua wamefika Korogwe. Geb akaingiza gari karibu kabisa na stendi ya
mabasi ya Korogwe. “Twende kule nyuma, tuangalie kwenye begi lako, tuone
kama ulibeba sweta.” Geb akashuka Nanaa akafuata. Akavuta begi la Nanaa.
Lilikuwa limewekwa yale maua kwa juu. Geb akayaangalia. Nanaa akamuona akiyatizama.
Geb alijua wazi amemuona. Akamwangalia kidogo yeye na yale maua. Kisha
akayaweka pembeni kwa uangalifu, na kumsogezea begi lake karibu. Akaangalia kwa
haraka, hakulikuta. “Nitakuwa nimelisahau pale nilipokuwa nakunywa chai.
Nitamwambia mama anijie nalo kesho.” “Basi kwa sasa hivi, ngoja nikupe langu.”
“Hamna haja. Mimi nipo sawa tu.” Danny alikuwa ametulia kimya,
akiwasikiliza. Geb akatoa sweta kwenye begi lake alipokuwa ameweka nguo zake,
akamkabidhi. “Nimekuona unavyotetemeka baridi. Vaa hili sweta.”
“Asante.” Nanaa akalipokea.
“Rudi kwenye gari ukakae. Nitarudi
baada ya muda mfupi tu.” Geb akaondoka. Alikwenda kwenye moja ya duka
lililokuwepo ndani ya stendi. Akanunua kama viblangeti vitatu vidogo. Akarudi
kwenye gari. Moja akamkabidhi Nanaa na Danny. “Mfunike huyo.” Akimaanisha
dada yake. Jingine akatoa kwenye lailoni akamfunika Fili. Fili na mama yake
walikuwa wamelala hawana habari. “Muone alivyolala kama mama yake! Hapo
alipo hana hata habari ya tulipo. Usiku kucha alikuwa akituelezea jinsi atakavyopendeza
kwenye harusi ya Malii. Kama yeye ndio bwana harusi vile!” Danny aliongea
huku anamtizama mwanae. Geb akacheka.
Akamuweka sawa pale kwenye kiti
chake. “Na hicho kiti ulichomnunulia kitamfaa sana. Naona atakalia mpaka
anunue gari yake.” Danny akaongeza. Wote wakacheka. “Na anakipenda
kweli! Akikaa hapo anajiita King Fili.” Geb na yeye akaongeza. Wote
wakacheka mpaka Nanaa. “Fili kwa kujikubali mwanangu huyu! Sijui ni hivyo
anavyodanganywa na mama yake kila mara?” Geb alimuweka sawa na kurudi
upande wa dereva. Safari ikaanza tena.
Sababu ya kijijoto alichoanza kupata
kutoka kwenye sweta na blangeti, akaanza kusinzia. Ni kama alivaa furaha ya
ajabu. “Sweta la Geb!” Nanaa aliwaza huku
akijishika. “Unataka kulala?” Geb akamuuliza. Nanaa akatingisha
kichwa kukubali na tabasamu usoni. “Bonyeza hapo pembeni ili kiti kirudi
nyuma. Ndio utalala vizuri.” Akafanya kama alivyoelekezwa. Hakuwa tena
mbishi. Akafuata maelekezo. Kwa urahisi sana kile kiti kikajilaza. Akajiweka
sawa. Alipitiwa na usingizi kama yupo kitandani. Na kwa kuwa kulikuwa kimya,
akalala usingizi mzito sana. Geb aliwasha radio akawa anasikiliza miziki ya
taratibu. Waliendesha kwa muda, Danny naye akisinzia huku amepakata kichwa cha
mkewe.
~~~~~~~~~~~~~
Simu ya Geb ndio iliyowatoa
usingizini. Japokuwa hakuna aliyezungumza chochote, lakini wote waliamka,
wakabaki kimya. Geb akapokea simu yake. “Nimefika.” Sauti ya Liz
ilisikika. “Pole na safari.” “Asante. Nakusubiri.” “Nashauri ushukue taksii
ikulete Liz. Sisi ndio tunaingia Himo. Hoteli aliyopata Danny, au
tuliyokubaliana wote tulale ni Marangu hoteli kama nilivyokwisha kukwambia.
Sasa mpaka niwafikishe hawa huko Marangu, ndio nije mpaka huko KIA, utasubiri
sana.” “Mbona kama unaonekana hutaki kuja?” “Unatafuta sababu ya kukasirika
Liz. Nimejieleza vizuri tu, tena kifasaha. Muda wa mimi mpaka nije huko halafu
turudi tena Marangu, utajichosha zaidi.” “Sio lazima turudi leo Marangu.
Tunaweza kuchukua hoteli huku huku.” Liz akaongeza wazo la kibinafsi
kama kawaida yake.
“Sidhani kama ni sawa Liz. Nafikiri ni vizuri
tuwe na wenzetu.” “Si tutawafuata kesho!? Tatizo liko wapi? Au kuna kingine
hutaki kuniambia.” “Liz!” “Nini? Maana sikuelewi naona kama unanikwepa, Ge!”
“Kwa nini nikukwepe? Kama ungetaka, ningewaomba hawa watu nilio nao hapa,
tukufuate wewe ndio tuelekee Marangu.” “Tangia lini unataka kuomba ruhusa kwa
watu? Gari yako na pesa ni zako. Huhitaji kuomba ruhusa kwa mtu.” Geb
akanyamaza. Alijua kwa maongezi yale, hata walio lala watakuwa wameamka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa hakutoka ndani ya lile blangeti
alilokuwa amepewa na Geb. Akatulia kimya. Grace akakaa. “Nataka kukojoa,
mama.” Fili alimgeukia mama yake. “Subiri anko asimamishe gari,
nitakupeleka. Njaa inauma?” Fili akatingisha kichwa kukataa. “Nina
hamu na wewe Fili. Mbona umelala sana mwanangu?” Grace aliongea na mwanae
kwa upendo. “Unaumwa?” Fili akakataa. “Umechoka tu?” Fili
akakubali. “Basi anko atasimamisha gari, dad atakupeleka chooni. Au unanitaka
mimi?” “Nakutaka wewe mama.” “Haya. Basi tutaenda wote. Mbusu mama.” Fili
akambusu mama yake. “Umefurahi?” Fili akamuuliza mama yake. Grace
akacheka. “Sana. Nimefurahi mpaka moyoni.” “Basi baadaye nitakubusu tena.”
“Asante mwanangu.” Wote walikuwa wakiwasikiliza.
~~~~~~~~~~~~~
“We Geb!?” Wakasikia
tena upande wa pili Liz anaita. “Naomba nikushauri Geb. Tushushe sisi
hapa. Tutachukua taksii mpaka Marangu. Wewe kamfuate Liz huko KIA. Tutakutana
huko na itakupunguzia shuguli. Halafu pia utawahi kurudi, wote mpumzike.” Grace
alimaliza. Kimya. “Au unasemaje Danny?” Mkewe akamuuliza. “Naona
ni wazo zuri na rahisi. Itakurahisishia Geb.” Kimya, wakaona Geb anatafuta
mahali pakuegesha gari.
“Geb!” Liz akaita tena. “Chukua taksii.
Mwambie dereva akulete mpaka Marangu hoteli. Nitalipia.” “Kwa hiyo hutaki kuja
kunichukua?” “Nikija sasa hivi ujue nitakuwa na watu wengine kwenye gari. Ni
sawa?” “Nitafanyaje sasa? Sitaki kupanda taksii. Kwanza sijui kama nitapata
nzuri yenye hadhi na sijui kama nitapata dereva mwaminifu. Akiamua kunibaka
je?” “Basi tunakuja.” Geb akakata simu.
“Twende nikupeleke
chooni.” Geb alimgeukia Fili baada ya kuegesha pembeni ya kimgahawa
kidogo. “Namtaka mama.” “Mwanangu anahamu na mama yake. Twende
baba.” Grace akamfungua mkanda. “Naombeni mnivumilie kidogo,
nikamchukue Liz uwanja wa ndege.” Geb aliongea huku akimwangalia Danny na
dada yake. “Hamna shida.” Wote walijibu kwa pamoja. Grace akashuka na
mwanae, baada ya muda wakarudi. Safari ya KIA na wala si Marangu ikaanza.
Ukimya mkubwa ulizuka ndani ya gari.
Ni Fili tu ndiye aliyekuwa akiimba nyimbo alizokuwa ameweka anko wake kwenye
gari, mpaka wakafika KIA. Geb alishakuwa ameangalia kwenye simu yake umbali
aliokuwepo hapo Himo mpaka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, akaona itamchukua
lisaa limoja na dakika karibia 30. Akajua wazi anawachosha wasafiri wenzake,
lakini hakuwa na jinsi.
Akasogeza gari mpaka sehemu
alipoelekezwa na Liz. Akamuona amesimama na sanduku moja kubwa, linalofanana na
mabegi madogo mawili. Geb akashuka kwenda kumpokea sanduku ili amsaidie
kupakiza kwenye gari. Akachukua lile kubwa na begi jingine mkono wa kushoto,
Liz akabeba lililobakia. Wakazunguka nyuma ya gari kupakia hiyo
mizigo. “Mbona naona nafasi yangu imerithiwa?” Alihoji Liz wakati
wanapandisha mizigo yake huko nyuma ya gari. “Nitanyanyua hivi viti vya
nyuma nilivyolaza, tutapata tu nafasi.” “Ili nani ake nyuma!?” Liz
akauliza kishari na kuongeza kibabe. “Kama ni mimi ujue sitakaa
nyuma.” Geb akanyamaza.
Sweta La Geb,
Lazua Hekaheka.
Kwa kuwa kila mtu alikuwa akiwasikiliza,
Nanaa akavuta kiti alichokuwa amekilaza. Akakaa vizuri. Akaanza kukunja vitu
vyote alivyokuwa amejifunikia navyo, akafungua mlango akakuta Liz ameshafika
mlangoni anamsubiria atoke pale mbele. “Hee! Mbona kama hilo sweta
nalifahamu!” Liz akahoji kwa mshituko. Nanaa akajiangalia.
“Ameniazima Geb.” “Mmeanza lini kuvaliana nguo na Geb!?” Akauliza
tena. “Nimesahau sweta langu nyumbani, ndio akaniazima hili. Lakini naweza
kulirudisha tu.” Nanaa akajibu kiustarabu.
“Nanaa! Hebu ingia ndani ya gari.” Grace
akaingilia. “Pitia huu upande aliokuwepo Danny. Atakupisha, uruke nyuma.
Geb amenyanyua kiti cha upande huo aliokaa Danny. Njoo.” Nanaa akampita
Liz kwa tahadhari, akazunguka gari akapanda ndani.
Liz kabla ya kukaa pale alipokuwa
amekaa Nanaa kiti cha mbele, akaanza kusafisha. Alikung’uta kwa muda. Kisha
akachukua kitambaa cha kufutia jasho alichokuwa nacho. Kilikuwa kisafi kabisa.
Cheupee. Akakilowesha maji kidogo aliyokuwa akinywa. Kutoka kwenye chupa ya
maji ya Kilimanjaro, akaanza kupangusa kiti kizima. Wote walikuwa wametulia
kwenye gari wakimsubiria asafishe hicho kiti alichokuwa amekalia Nanaa.
“Itabidi tukutolee taulo kabisa.
Maana kabla yakukaa Nanaa hapo, nilikuwa nimekaa mimi.” Danny akarusha
neno. “Hata hivyo nimemaliza. Naona inatosha tu.” Liz akajibu baada
ya kutoa mtandio ambao ulikuwa kwenye kibegi kidogo alichokuwa ameshika mkononi
pamoja na pochi yake, na kuendelea kufuta kile kiti. Geb alikuwa kimya kabisa
akiangalia simu yake. Hakuongeza neno. Aliporidhika na ule usafi, ndipo
akapanda na yeye. Safari yakuelekea Marangu ikaanza. Na hapo tena
waliongeza kama lisaa. Kutoka KIA mpaka Marangu hoteli. Yote hayo Geb alikuwa
akiangalia kwenye simu yake. Akajua adhabu anayowapa wasafiri wenzake. Ukimya
ukatanda.
Wakaendesha kama dakika 10 tu, Liz
akaanza. “Sasa kama na mimi nikipatwa baridi, utafanyaje?” Liz
akamuuliza Geb. “Na wewe umesahau sweta lako?” Geb akamuuliza
taratibu tu. “Mbona swali juu ya swali?” Geb akamtizama Liz kidogo,
akarudisha macho barabarani. “Kwamba unanipuuza au?” Liz akauliza
tena. “Endapo ukisikia baridi, na sweta lako halitatosha, tutajua kitu
chakufanya wakati huo. Ila kwa kuwa sasa hivi upo sawa, naomba tutulie tu.”
“Umejuaje kama sasa hivi sisikii baridi? Kwani Nanaa alikwambia anasikia baridi
ndio ukampa sweta au uliona anasikia baridi ndio ukampa sweta? Eti
Nanaa?” Liz alimgeukia Nanaa aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma ya Danny.
“Kwa nini unafanya hivyo Liz?” “Nini
Grace? Kwa nini asivae sweta la Danny, avae la Geb?” Kimya. “Umeona
eeh! Nina haki ya kuhoji mimi kama mpenzi wa Geb. Sijawahi kuja pale nyumbani
nikamkuta Nanaa amevaa hata t-shert ya Danny. Iweje leo avae nguo za Geb!? Au
basi angalau angevaa sweta lako wewe sio Geb!” “Unanijua mimi huwa siwezi
kuongea sana kama wewe Liz. Ila naomba kuwe na amani. Kwanza sweta lenyewe
Nanaa alishalivua. Kwa nini unaendeleza maneno unayojua yataondoa amani? Naomba
yaishe. Kama ni kosa, basi samehe. Kuwe na amani. Wote tumeshaelewa kuwa
hupendi nguo za Geb zivaliwe na mtu mwingine, basi, hakuna atakaye rudia tena.” Grace
akaongeza kwa upole kabisa.
“Kama huwezi kuongea mbona umeongea
maneno yote hayo? Kilichokushinda kujibu swali langu ni nini?” “Mimi sioni
shida yeyote Liz. Hata sasa hivi Danny akitaka kumpa sweta au Nanaa akisema
anasikia baridi, na sweta la Danny lipo karibu, tutampa tu. Sioni sababu ya mtu
kuteseka na baridi wakati nguo zipo!” “Unaongea tu.” Liz akapinga. “Ni
sweta tu Liz. Tafadhali tunaomba yaishe, kuwe na amani. Tunachotaka ni amani.
Basi.” “Hata mimi nataka amani na kuwe na mipaka. Kila mtu ajue nafasi yake.
Tusiingiliane.” “Sawa Liz, tumeelewa.” Grace akajibu kwa ustaarabu.
~~~~~~~~~~~~~
Hapakuwa na maongezi yeyote. Liz
akaanza kubadili miziki humo ndani ya gari. Mara aweke huu, atoe. Mara azime
redio ya gari, awashe miziki iliyokuwepo kwenye simu yake. Ilimradi wote
walijua mmiliki wa Geb yuko pale. Akafanya hivyo bila kuongeleshwa na mtu,
mpaka walipofika Marangu hoteli. Walikuta wenzao walishafika wamekaa kama kundi
wakipiga stori. Vicheko vilikuwa vimetawala.
Walisalimiana, wakaelekea mapokezi.
Danny alikuwa amechukua vyumba vitatu. Viwili double, na single kimoja. Nanaa
na bibi Fili chumba chao. Danny na familia yake chumba chao na hicho single cha
Geb na Liz. Wakapewa funguo kila mmoja akaelekea chumbani kwake kwa makubaliano
wasikae sana vyumbani, watoke ili waungane na wenzao kwa chakula cha mchana.
Marangu
Hotel.
Mwili mzima wa Nanaa ulikuwa ukitetemeka. Akaingia chumbani kwake,
akajitupa kitandani. “Hivi ni kwa nini nilikubali kuja na kuvaa sweta
la watu!?” Nanaa akaanza kujutia. “Nimedhalilikaje!? Aibu
gani hii niliyoingia!” Nanaa aliendelea kujisikitikia.
Baada ya muda Grace
akagonga. “Twende tukale.” “Naomba mimi nilale tu. Nitakula chakula cha
usiku. Tafadhali Grace.” “Unauhakika? Naweza kukuletea huku huku ndani?”
“Hapana. Hata kaka James nimemjibu hivyo hivyo. Ametoka kunipigia simu
sasa hivi. Nataka kulala tu. Labda usiku ndio nitaweza kuungana na nyinyi.
Tafadhali Grace, naomba uniache tu.” Grace alimpa tabasamu la upole kama
kuelewa anachoongea. “Sawa. Lakini usiku lazima utoke. Usijifungie humu
ndani peke yako.” “Sawa.” Grace akatoka.
Baada ya muda tena kidogo, akasikia
tena mlango unagongwa. Akasimama na kwenda kufungua. Alipofungua tu na kumuona
Geb, akafunga kwa haraka sana. “Nanaa!” Geb alianza kuita kwa upole
huku akigonga taratibu, lakini Nanaa hakufungua. Akagonga kama mara mbili,
Nanaa hakufungua. “Nanaa!” Kimya. Nanaa alibaki amesimama palepale
nyuma ya ule mlango akimsikia Geb akiita lakini hakutaka kufungua mlango.
Nikitendo alichokifanya kwa haraka bila hata kufikiria.
Walisimama pale mlangoni kwa
muda. Geb akiwa kimya nje ya mlango, Nanaa ndani, nyuma ya mlango mapigo ya
moyo yakienda kasi huku akilia taratibu. Geb alimsikia anavyolia kwa sauti ya
chini. Akajaribu kufungua mlango, lakini Nanaa akawa amefunga kwa ndani.
Walisimama pale kwa muda mwishowe akamsikia Geb anaondoka, ndipo na yeye
akarudi kujilaza kitandani huku machozi yakiendelea kumtoka. Alilia asijue
kinachomliza. Kitu kilimkaba kooni akabaki akilia pale kitandani mpaka alipopitiwa
na usingizi.
Usiku Wa Kwanza
Walipofika Marangu.
Aliamka ilishakuwa giza kabisa nje.
Akaangalia saa ya kwenye simu yake, akakuta missed call mbili kutoka kwa kaka
yake. Akampigia. “Nilikuwa nimelala kaka.” “Uje kula.” “Sisikii njaa kabisa, kaka.” “Basi
njoo tu tukae wote.” “Nilikuwa nafikiria labda leo nipumzike tu.” “Hapana. Njoo
tuwe wote. Hatujaonana zaidi ya week sasa! Huna hamu na mimi?” Nanaa
akacheka. “Nakusubiri. Njoo nikupe habari zilizojiri mjini.” “Haya. Nakuja
kaka yangu.” Nanaa akaogoa haraka haraka, akatoka.
Hakupata shida kujua walipo, kwani
walikuwa na kelele kupita kiasi. Hoteli nzima zilisikika kelele za kina kaka
hao wakicheka na kutaniana. Nanaa akasogea mpaka walipokuwepo. Akaangaza macho
akamuona alipokuwa amekaa kaka yake, akamsogelea. “Nitakaa wapi
sasa?” Nanaa akamuuliza kaka yake James kwa sauti ya chini kidogo, kumbe
akasikika. “Kaa hapa kwenye kiti changu. Mimi nitaenda kuchukua
kingine.” Zinda akiwa amelewa sana akajibu yeye. “Tafadhali sana Nanaa,
mama watoto wangu. Kalia kiti hiki roho yangu itulie.” Watu wakaanza kucheka.
“Zinda! Zindaa!” Mmoja wa rafiki
zao alimwita. “Mwimbie basi Nanaa ule wimbo uliokuwa ukituimbia.”
“Nimeutunga maalumu kwa ajili yako mama watoto wangu.” Nanaa akakaa kwenye
kiti alicholetewa na Zinda. Pembeni ya kaka yake. “Kila neno ndani ya huu
wimbo ni lako mpenzi Nanaa. Nimetunga kwa ajili yako. Ni wewe mpenzi
nikupendae. Sinywi wala kula….” “Mimi hapo ndipo anaponichosha Zinda. Maneno
mengiiii. Mpaka unaharibu. Sasa kama hunywi wala kula, umelewaje na una mfupa
wa nyama hapo mkononi? Wewe ungeimba tu, yakaisha. Umeharibu kila kitu. Na
hakuna kuimba tena. Ukiimba tu tunakubeba na kwenda kukufungia chumbani kwako.
Hatutaki umdanganye Nanaa.” Danny alimkata Zinda na kufanya watu wazidi
kucheka.
“Sikudanganyi Nanaa.” “Sasa
umelewaje? Na mfupa huo wa nyama ya mbuzi umefikaje mkononi kwako?” “Kwanza
sijalewa. Pili huu mfupa sio wangu. Wa Malii.” Akaurusha kwa Malii. Watu
walizidi kucheka. Nanaa alibaki ameinama. “Nanaa! Nanaa!” Nanaa
akamwangalia Zinda. “Nakupenda sana Nanaa.” “Asante Zinda.” “Sauti mimi
jamani! Sauti ya Nanaa!” Zinda akalalamika kilevi nakufanya watu wazidi
kucheka.
“Zinda! Ulisema unataka kufanya nini
na sauti ya Nanaa?” Gozi alimuuliza kishabiki. “Nataka kuimiliki
mpaka kifo changu. Nishaongea na James. Katika mahari watakayonitajia nilipe,
nitaongeza nusu yake kwa ajili ya sauti ya Nanaa. Hiyo sauti nilazima nitalipia
tu. Halafu nitamrikodi wakati ananiita jina langu. Niweke kama ringtone
yangu.” Watu walizidi kucheka. “Yaani nyinyi mnanipigia mimi simu,
basi mwenzenu naitwa jina langu na Nanaa. Zinda! Zindaa!” Nanaa aliinama
huku akicheka kwa aibu. Pombe zilikuwa zikimsaidia Zinda. Alikuwa akiongea bila
shida.
~~~~~~~~~~~~~
Muhudumu akamsogelea
Nanaa. “Nimeambiwa nikuulize unataka kula nini?” Nanaa akajua ni Geb
tu. Alishindwa kukataa. Njaa ilishaanza kumuuma. “Kwani kuna chakula
gani?” Kulikuwa na kelele, Nanaa akashindwa kumsikia. Yule muhudumu
akarudia tena na tena lakini Nanaa alipata shida kumsikia na kufikiria ili
kutoa maamuzi. “Naomba tuongozane mpaka jikoni. Nione mlichonacho labda
nitaweza kuchagua.” Akasimama na kuongozana na yule muhudumu. Akafika
jikoni, akapata kitu ambacho aliona anaweza kula wakati ule. Akaweka oda.
Wakati anarudi akiwa mbali kidogo na
lilipokuwepo lile kundi la watu wengine, akamuona Geb akimjia. Akasimama na
kuinama. Geb akamsogelea mpaka karibu yake, akamfunika tena na lile lile sweta.
Lilikuwa la vifungo mbele. “Sihitaji tena sweta. Asante.” Nanaa
akalitoa mwilini mwake. “Sasa hivi unaweza usione umuhimu wake, lakini
unaweza kupatwa vichomi. Nimekuona vile ulivyokuwa umekaa pale, umejikunyata.
Unasikia baridi Nanaa. Vaa hili sweta.” Geb akalirudisha tena mwilini kwa
Nanaa. Akalizungusha juu ya mabega yake. “Mimi sitaki tena sweta lako
Geb. Nikizidiwa na baridi nitajifunika mtandio wangu.” Machozi
yalianza kumtoka tena Nanaa. Akalitoa lile sweta mabegani akalishika mkononi
huku anajifuta machozi.
“Naomba uvae hili sweta, halafu ndio
ujifunike mtandio na kile kiblangeti nilichokununulia ili usiingiwe na
baridi.” Geb akalichukua tena kutoka mkononi mwake. “Naomba mkono
wako wa kushoto.” Nanaa akabaki ameinama
akifikiria. “Nanaa!” Nanaa akaona avae yaishe, kwani Geb
alishazunguka nyuma yake. Akaingiza mkono wake wa kushoto kwenye lile sweta
alilokuwa ameshikilia Geb, akamvalisha na mkono wa kulia, akazunguka mbele
akaanza kumfunga kifungo cha kwanza mpaka cha mwisho huku Nanaa akifuta
machozi. Akalitengeneza kidogo mabegani kwake. Akaridhika.
“Afadhali hivyo. Hapo sasa hata
ukiongezea na mtandio juu itakuwa afadhali.” Geb aliongea huku macho
yakiwa kwenye sweta alilovaa Nanaa. Nanaa akajifuta tena machozi. “Asante.” Nanaa
akashukuru kwa upole. “Karibu. Umepata chakula?” Geb akamuuliza,
Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Umekipenda?” Nanaa akabaki kimya
huku ameinama kama anayefikiria. “Kama haujakipenda, tunaweza kutafuta
chakula kingine nje ya hapa.” “Nimekipenda. Umepata muda wa
kupumzika?” Nanaa akauliza kwa upendo huku akimwangalia. “Nitalala
baadaye.” Geb akajibu.
Alionekana amechoka. “Umeshakula?” Nanaa
akamuuliza tena. “Bado.” Geb alijibu huku akimwangalia. “Naomba
uenda ukale.” Geb alibaki akimwangalia. “Vipo vyakula vingi. Mama
alikutayarishia leo asubuhi. Hutakosa kitu cha kula. Naomba usilale bila
kula.” Nanaa aliongea kwa sauti ya kubembeleza.
Wakagundua lile eneo zima lipo kimya.
Zile kelele za wale marafiki zimeisha. Nanaa akageuka kuwaangalia ili kujua
kulikoni. Akagundua macho ya watu wote yanawatizama wao. Geb alikuwa ametulia
tu. Akawaangalia na yeye, akarudisha macho kwa Nanaa. Nanaa alikuwa
ameinama. “Mimi nitakula. Nenda kakae watakuletea chakula chako.” “Naogopa
Geb. Nimeingiwa na hofu! Najuta kwa nini nimekuja.” Nanaa
alijikuta akiongea huku machozi yakimtoka. “Pole. Lakina huna haja
yakuogopa. Leo ni alhamisi, tuna siku 3 mbele. Jumamosi ndio sendoff yenyewe.
Jumapili tutaenda kuzunguka kidogo Arusha. Tutatafuta hoteli nzuri yakupumzika.
Naamini utafurahia. Halafu jumatatu baada ya kifungua kinywa ndio tutarudi Dar.
Naomba utulie, na ujiwekee akili yakutarajia wakati mzuri. Nina uhakika
utafurahia tu. Sawa?” Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu.
Akatamani asirudi tena pale, arudi
chumbani kwake tu, kwani macho ya watu wote bado yalikuwa yakiwatizama wao.
Lakini akakumbuka kaka yake alimuita. Anarudije tena pale? Anamwangaliaje tena
Liz aliyelalamikia sweta lake halafu ameshuhudia Geb akimvalisha!? “Sasa
kwa nini anivalishe tena wakati mpenzi wake alimkataza?” Nanaa
akajiuliza, akamwangalia Geb, bado alikuwa akimtizama.
“Nanaa!” “Abee.” Nanaa
akaitika. “Naomba nikuombe kitu kabla hujarudi kukaa.” Nanaa akabaki
akimtizama. “Ni sawa?” “Nakusikiliza Geb!” “Naomba siku nyingine
usinifungie mlango nje.” Nanaa alijisikia vibaya sana. Geb aliongea
kiustarabu akiwa ametulia. “Samahani.” Geb alibaki akimtizama na macho
yaliyokuwa yakimchanganya Nanaa. “Sitakufungia tena mlango
nje.” “Asante.” Maongezi hayo Geb aliyaendeleza wakiwa wamesimama
karibu sana na Nanaa, na bado watu wengine waliwatizama na wengine waliinama.
Hapakuwa na mazingira ya kaka na mdogo wake pale. Geb alisimama na Nanaa
wakiongeleshana kwa upendo wa namna yake.
~~~~~~~~~~~~~
Hisia zilizokuwepo ndani mwao ni wao
wenyewe walizijua. Mazingira yote hayakuwa yakiwaruhusu, lakini kila mmoja wao
alishindwa kujizuia. Bado Nanaa alitaka kumuona Geb amepumzika na kula vizuri.
Na Geb bado aliweza kumuweka Nanaa mbele hata pale alipojua atazua maswali
mengi. Anachojisikia Nanaa kwa Geb, hakuwahi kusikia maishani kwake kabla.
Asijue kama ni mapenzi au upendo kwa baba mwenye nyumba wake. Au anamsaidia
shoga yake mama G kumlea kiziwanda wake. Lakini alishindwa kujizuia. Akajikuta
anafanya kile roho yake inamsukuma. Hata pale wengine walipokuwa haelewi,
anawezaje!
~~~~~~~~~~~~~
Muhudumu alipita na chakula akielekea
kule lilipokundi la marafiki. “Twende ukale.” Hakuwa hata anajua
alipokuwa amekaa Geb. Hakuwa amemuona hata Grace na mumewe ila sauti ya Danny
tu. “Twende.” Nanaa alibaki ameinama kama anawaza. “Nanaa!”
“Labda nikale chakula changu chumbani.” “Hapana Nanaa. Twende. James alikuita.
Unakumbuka?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Basi
twende.” Geb alitangulia, Nanaa akamfuata nyuma mpaka pale mezani. Geb
akavuta kiti pembeni ya James. “Njoo ukae hapa.” Nanaa akaenda kukaa,
akainama. Watu wote walikuwa bado kimya. Geb hakuonekana kuwa na wasiwasi
wowote usoni.
Geb akaondoka na kurudi kukaa pembeni
ya Liz. “Kula chakula chako kisipoe.” James akavunja ukimya.
Akamsogezea dada yake kile chakula. “Wewe umeshakula?” Nanaa
akamuuliza kaka yake. “Tokea tunafika hapa, tulikuwa tunakula nyama choma.
Hapa tumbo limejaa. Kula.” Bado watu walikuwa kimya. Hakuna aliyekuwa
akiongea tena. Ilimlazimu Nanaa kula, kwa kuwa ndicho alichoambiwa na Geb na
kaka yake. Lakini chakula kilishakosa ladha kabisa. Ni kama alikuwa akitafuna
makapi.
Mmiliki Wa
Penzi!
“Unajua uliponiambia Nanaa anaishi
pale kwako, nikashituka sana. Nikakuuliza iweje atoke kwa kaka yake, aje aishi
pale nyumbani kwako? Ukanijibu James amemuombea aishi na nyinyi pale kwa muda
tu, wakati anamtafutia kwake. Hilo nikalinyamazia japo naona siku zinazidi
kwenda tu, na yeye yupo palepale kwako hana hata dalili yakuondoka.” Liz
akaendelea. Kila mtu alikuwa akimsikiliza. Kwani alijitahidi kuzungumza kwa
sauti ya kusikika. Na ule ukimya uliokwisha kuwepo, kila neno lake lilisikika vizuri
tu.
“Zinda akaja siku ile nyumbani kwako,
akamuomba Nanaa aje huku kwenye sendoff kama mtu wake, Nanaa akakataa.
Nashangaa jana nakuuliza watu tutakao kuwa nao safarini, ukanitajia na Nanaa
atakuwepo. Nikashangaa zaidi. Nikajiuliza mara mbili mbili. Nanaa alishakataa
kuja huku. Na Grace aliniambia Nanaa amekataa kuja huku kwa kuwa hata Malii
mwenyewe hanamahusiano naye au hawafahamiani. Au sijui ilikuwa sababu gani
aliyoitoa Nanaa lakini mambo yanayofanana na hayo, ameamua hatakuja huku.
Nikaona inaleta maana. Lakini leo yuko hapa. Sasa alikataa nini na amekubali
nini? Kwa nani na kwa nini?” Liz akaendelea bila ya kusubiri jibu.
“Maana naona wewe ndiye unahangaika
naye kupita kiasi! Kila mtu anajua mimi ni mtu wako. Zinda ametangaza kumtaka
Nanaa, tena kwa ndoa. Leo wewe unaniacha mimi hapa nikiwa nimekaa, unaenda
kumvalisha sweta Nanaa!! Tena nikiwa nimeshakukataza njiani wakati tunatokea
uwanja wa ndege! Tena Grace akaongeza kwa sauti kuwa ameelewa kuwa sitaki mtu
avae nguo zako. Na akasema Nanaa alishalivua sweta lako. Sasa nisikilize Geb.
Tusipotezeane muda wala kunyimana raha. Tuambie kama Nanaa ndiye mwanamke wako,
mimi na Zinda tuwaache.” Geb alitabasamu akamwangalia Liz. Alishakasirika
kupita kiasi.
“Usiniangalie kwa dharau Geb.
Nimeuliza swali. Tena vizuri tu. Kwa niaba yangu na Zinda, naomba
ujibu.” Liz akaona aongeze nguvu kwa kumtaja Zinda. “Umeshatangaza
hapa kama tunaishi na Nanaa. Ni kweli James ametukabidhi dada yake. Tayari
Nanaa amefanyika mmoja wa familia yetu. Na nyinyi wote mnajua jinsi
tunavyoishi. Kila kitu tunafanya pamoja, kitu kilichokushinda wewe Liz. Kawaida
yetu sisi ni kufungua mlango kwa kila anayetusogelea. Ilikuwa lazima kuja huku
na Nanaa. Siwezi kuwa na amani eti sisi tupo huku tunastarehe, halafu
tumemfungia Nanaa nyumbani na walinzi! Ilikuwa ni heri hata niahirishe safari
nisije, kuliko kumuacha Nanaa pale nyumbani peke yake. Kwa hiyo ilinilazimu
kumsihi yeye aje na sisi ili na mimi niweze kuwepo hapa na Malii. Hilo ni moja.”
“Ulazima wa yeye kuwepo hapa ni upi?” Liz akauliza tena.
“Naomba nimalize kuzungumza Liz.
Umeuliza maswali ya kiuchonganishi mbele za watu ukitaka kuendeleza ugomvi.
Sasa naomba nikujibu bila kuniingilia. Kwa kuwa unanijua siwezi kubishana, na
siwezi kupigishana kelele. Sikiliza majibu yangu mpaka mwisho. Si lazima majibu
yangu yalete maana kwako na wengineo, lakini najibu kutokana na kile
ulichouliza.” Watu wote walikuwa kimya.
Grace akajua Geb
alishakasirika. “Swala la sweta. Nanaa amesahau sweta lake nyumbani.
Tumegundua hilo tukiwa njiani tena wote wakiwa wamelala, kasoro mimi niliyekuwa
dereva na Nanaa ambaye ilimbidi kumpisha Danny, aende nyuma, Nanaa aje kukaa
mbele. Kwa kuwa Grace alitaka kulala kwenye miguu ya mumewe. Ikabidi
kubadilishana. Nanaa alipokuja mbele, baridi ilimshinda. Ikabidi kusimamisha
gari ili akaangalie sweta lake kwenye begi lake. Ndipo akagundua amelisahau
nyumbani. Ikabidi nimpe sweta langu, kwa kuwa kwanza sikuwa
nikilitumia.” Geb akaendelea.
“Pili sikuona sababu yakuanza kumuamsha
Grace kumuomba sweta ambalo hata sikujua kama na yeye alibeba au la. Tumekuja
kukufuata wewe kule KIA, ukaanza maneno mengi yaliyomuogopesha Nanaa. Kuepusha
ugomvi, akaamua kulivua na kuniachia pale kwenye gari. Kwa sasa James haishi na
Nanaa. Mimi, Grace, Danny na Mama, tunahusika na Nanaa kwa asilimia zote. Sweta
la Nanaa anakuja nalo mama kesho. Siwezi kumuacha Nanaa anateseka na baridi
hapa, eti kwa sababu anakuogopa wewe! Hata kidogo Liz. Nitafanya kile
ninachojua na kuelewa ni sahihi. Bila hila wala kificho.” Geb alijibu
kifasaha, taratibu tu.
“Kwa hiyo sio kwamba ni mapenzi ndiyo
yamekupelekea hivyo?” “Unataka kusikia nini kutoka kwangu, Liz?” “Hilo ni swali
la jibu la ndiyo au hapana.” “Nimeongea kwa muda mrefu sana, Liz. Na wote
mnajua sio kawaida yangu. Nimejieleza kupita kawaida yangu. Kwa heshima yako
na Zinda. Kama mpaka hapo haujaelewa, hata nikirudia, hutanielewa tena.
Naomba niishie hapo.” Geb akanyamaza.
“Na mimi nasikia baridi.” Liz akaendelea. “Ngoja
nikakuletee sweta na kitu chakujifunika.” Geb akasimama na kuondoka kurudi
chumbani kwao.
Baada ya muda akarejea na sweta la
Liz na mtandio wake. Akamvalisha taratibu, roho ikamtulia Liz. “Unacheka
nini sasa?” Wakamsikia Geb anamuuliza Liz. “Nimefurahi.” Geb
akamfunga vizuri, akamfunika na ule mtandio, akampitishia mkono juu yake kama
kumkumbatia kwa mkono mmoja. Akaanza kumsugua viganja vyake kwa mkono wake
mwingine. “Asante.” Liz alisikika akishukuru kwa sauti tulivu. Kidogo
pakapoa.
~~~~~~~~~~~~~
Ukaanza utani wa muda. Angalau watu
wakasahau. “Mimi naenda kulala, kaka.” Nanaa alimnong’oneza kaka
yake. “Mbona mapema?” “Najisikia kuchoka. Nataka kupumzika. Labda kesho
nitajisikia vizuri.” “Haya. Usiku mwema.” “Asante kaka, na wewe pia.” Nanaa
akasimama. “Unaenda kulala, mama watoto?” Zinda alimuwahi Nanaa kabla
ya kuondoka. “Ndiyo Zinda.” “Mbona mapema, mamaa?” “Nimechoka. Nataka
nikapumzike.” “Basi naomba nikusindikize.” Zinda aliongeza. Nanaa akacheka
kidogo. “Nitashukuru.” Watu wakaanza kushangilia.
“Siamini mwenzenu. Naweza nisirudi
kabisa.” Watu walizidi kucheka. “Utaenda wapi?” “Nanaa anaweza
kunihurumia akaamua anibembeleze nilale kabisaa.” “Ukichelewa hata dakika moja,
nakufuata Zinda.” “Nakutania James na wewe! Mbona mkali hivyo kwa dada yako?
Namsindikiza tu narudi.” “Hata ndani usiingie.” “James naye! Nikikaribishwa
ndani je?” “Basi baki hapa.” “Siingii bwana James! Acha roho ya kwa nini!” “Na
urudi Zinda. Sio uende kumng’ang’ania Nanaa. Akiniambia ulimfanyia fujo tu, au
hata ulimuomba uingie ndani, nakutoa meno ya mbele na sitanii.” “James kwa
mdogo wake! Ubinadamu unamuisha kabisa! Sasa mimi si nitakuwa shemeji yako?”
“Wewe msindikize, urudi.” “Sawa mkuu.” Zinda na Nanaa wakaondoka.
Nanaa kwa
Zinda.
“Zindaa!” Nanaa akamwita wakati
wakitembea. “Niambie Nanaa.” “Najua umelewa sana. Unafikiri nikikwambia
kitu leo, kesho utakikumbuka?” “Kabisa. Sijalewa kiasi chakushindwa
kukuelewa.” Nanaa akamwangalia. “Kweli Nanaa. Sijanywa sana.” “Basi
naomba tukae kidogo tuzungumze.” Wakatafuta mahali wakakaa.
“Naomba nikushukuru kwa heshima
unayotaka kunipa. Kwangu sio kitu kidogo. Najua unafahamu kuwa mimi ni kama
yatima. Ndugu niliyenaye ni kaka James tu. Nisipokuwa kwenye maisha ya kaka
James, mimi sina tofauti na mtoto wa mtaani. Kama ulivyosikia nikitangazwa pale
mbele za watu, kaka amekosa pakuniweka kwa sasa, ameniombea niishi kwa muda
nyumbani kwa Geb. Sifurahii hata kidogo haya maisha Zinda. Naumia kuona nakuwa
mzigo kwenye maisha ya watu. Zaidi mvunja amani. Sijui kesho yangu ikoje au
inafananaje? Sijui kesho nitakuwa wapi! Sijui kaka ataamua kunihamishia wapi na
kwa nani!” Nanaa akaendelea.
“Ni maisha ambayo hayana utulivu hata
kidogo. Si akilini tu, hata moyoni pia. Sijui ni nini nataka! Nimefanya makosa
mengi sana kwa kukubali wanaume wengi sana ili wanitoe kwenye hii hali.
Ungekuja miezi michache nyuma, ningekukubalia kwa haraka sana. Kwa kuwa
nilikuwa natafuta mtu wakuninusuru kwenye hii hali. Bila kujali hisia zangu
kabisa. Nimegundua sijitendei haki na wala sitakutendea wewe haki endapo
nitakukubali sasa hivi. Akili, mawazo na hali yangu ya maisha, vyote vinataka
kusema ndiyo kwako. Tena nikung’ang’anie hata kesho unioe. Lakini nimekusudia
kutofanya tena, ‘permanent decision, for temporary situation’.
Najua ipo siku nitatulia tu. Nitaweza kuruhusu hisia zangu kupenda kwa
dhati.” Nanaa akatulia kidogo.
Kisha akaendelea. “Nitaumia sana
kukukubali sasa hivi wakati ninashida. Sijafikiria. Unipe magauni na viatu.
Nyumba na gari, halafu mwili ukishapata hivyo vyote, nafsi ije igundue
haikupendi! Haitakuwa sawa kwako, Zinda. Naomba nikupe jibu la bila kukupotezea
muda, mimi siye mke wako. Siye mwanamke unayetaka kuniweka ndani sasa hivi.
Nitakuumiza Zinda na wewe unaonekana ni mtu mzuri sana. Sijui umenielewa?”
“Nimekuelewa Nanaa. Naweza kukusuburi? Sio lazima tuoane kesho. Ila naomba tuwe
hata kwenye mahusiano.” Zinda huyu siye yule aliyekuwa akifanya mizaa.
Alitulia kabisa.
“Nikwambie ukweli Zinda? Ukweli usio
na kificho. Kichwa changu chenyewe hakina mahusiano hata na mwili wake. Siwezi
kukupa kitu ambacho sina Zinda. Hapana. Naomba wala usinisubiri. Sipo kwenye
nafasi ya kuongeza mtu mwingine au kitu kingine kwenye maisha yangu kwa sasa.
Akili zimevurugika. Tafadhali naomba unielewe.” “Daah! Sawa Nanaa. Lakini
afadhali nimejaribu. Nakushukuru kwa kuwa muwazi kwangu.” “Asante Zinda.
Basi naomba mimi nikapumzike.” “Usiku mwema. Tutaonana kesho.” “Asante na
wewe.” Zinda akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu, akatoa
simu yake akamtumia ujumbe kaka yake. Akamuomba afike chumbani kwake. James
alipopata tu ule ujumbe, akasimama. Akamuona Zinda amerudi amenywea kama sio
yeye. “Mzima kaka?” “Mzima kabisa. Wapi tena?” Zinda alimuuliza
James. “Naenda kuzungumza na Nanaa.” Wote walimuona Zinda vile
alivyorudi kwa upole. Alivuta kiti akakaa, bila kuongeza neno. Watu wakabaki
wakimtizama. Zinda yule aliyekuwa na maneno mengi ya kilevi sie huyu. Kumbe
walevi huwa wanaelewa! Nawaza kwa sauti tu.
“Mbona umekaa gizani peke yako?”
“Nakusubiri tuingie ndani tuzungumze.” Nanaa akafungua mlango wakaingia na
kaka yake. “Vipi mbona kama unalia?” “Nachukia maisha yangu kaka.
Nachukia hivi nilivyo.” “Usilie basi. Acha tuongee. Pole.” “Sifurahii
hivi ninavyozungumziwa mbele za watu. Nakuwa mtu wakutangazwa naishi wapi,
nasaidiwa na nani! Hapa pameshaleta shida kaka. Hapatakuwa na amani tena.
Nataka kuondoka nirudi Dar, nikaangalie vyumba. Nianze kujitegemea. Inatosha
kaka yangu.” “Uondoke kabla ya shuguli iliyotuleta hapa!?” James
akauliza.
“Liz yupo sahihi. Uwepo wangu hapa
hauongezi chochote. Kwa nini niwepo hapa? Tayari Liz amekuwa na wasiwasi na
mimi kaka. Siwezi kusema mengi juu yake kwangu, kwa kuwa akili yangu
haijatulia. Lakini kwa maneno aliyokuwa akiongea hata jana nyumbani na leo
njiani, naonekana nimeshakuwa tatizo tena hapa. Sitaki kuishi kwa kusumbua
watu. Hawa watu nimewakuta wana amani na utulivu. Naomba mimi nisiwe
sababu.” Huwa akili ya James inaacha kufanya kazi pale anapomuona dada yake
huyo akilia.
“Utarudije Dar peke yako?” “Kumbuka
haya maeneo mimi ni mwenyeji kaka. Napafahamu vizuri. Nimesoma hapo Ashira
Sekondary. Nitafika tu Dar. Nitaondoka mapema ili nimuwahi dalali, nizunguke
kabla giza halijaingia.” James alibaki kimya kwa muda. “Kaka!” Akamuita na
kumtoa mawazoni. “Sawa Nanaa. Lakini sipendi hivi unavyohangaika!” “Ipo siku
nitatulia kaka yangu. Naamini hivyo. Acha nihangaike nipate kwangu. Sitaki tena
kuishi kwenye majumba ya watu. Najiumiza tu.” “Nakuelewa. Unayo nauli
sasa?” “Nina pesa kaka yangu. Wala usiwe na wasiwasi.” “Basi
nitazungumza na kina Geb. Nitawaambia mimi ndio nimeamua urudi Dar. Lakini sasa
hivi naomba usilie kabisa. Tumeshafikiria chakufanya. Tutafute sehemu yako.
Huna haja yakulia. Tulia ili uweze kulala vizuri.” Nanaa akatulia.
Akajifuta machozi kabisa.
“Asante sana kaka yangu. Nakushukuru.
Lakini ujue nitaondoka alfajiri sana. Nitaondoka na mabasi ya saa 11, ili
nifike Dar mapema.” “Nitakuja kukusindikiza.” “Sitaki kukusumbua itakuwa mapema
sana.” “Siwezi kukuacha utembee hapa mpaka kituoni halafu usubiri pale peke
yako. Hapana. Lala mapema, nitakuja kukugongea saa 10:45 asubuhi.” “Asante
kaka.” James akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
James naye akarudi akiwa
amepoa. “Kwani nyinyi vipi?” James akacheka. “Tunarudi kwa
mafungu?” Akauliza James kwa utani. “Tena bila Nanaa, halafu wote
mmepoaa. Zinda ameshindwa hata kuongea!” Mmoja wao akadakia. “Nanaa
analala. Yupo sawa tu. Kila kitu kipo sawa.” James akajibu na kujituliza
kitini. Vicheko na stori vikachanganya tena, James akaangalia saa yake,
akagundua anatakiwa kulala na yeye mapema ili asimcheleweshe Nanaa kituoni.
Akawaaga kuwa anakwenda kupumzika. Na wengine wenye wake zao wakatoka mmoja
mmoja kuingia vyumbani mwao. Grace na Danny nao kwa kuwa walikuwa si wakataji
maji, soda zilishawachosha. Wakaenda kulala na mtoto wao.
Nanaa maji
yawa marefu. Aamua kujitoa.
Aliamka alfajiri na mapema. Akaoga
haraka haraka, akavaa suruali yake ya jinsi, akachomekea blauzi yake ya mikono
mirefu, akajitengeneza nywele zake vizuri. Akabaki akimsubiria kaka yake huku
amejifunika blangeti dogo alilonunuliwa mjini Korogwe na Geb. Akakunja vizuri
sweta la Geb, akaliweka hapo kitandani kwani alijua lazima Geb ataliona tu.
Ndicho chumba bibi Fili alitarajiwa kulala pindi atakapo wasili. Yeye alikuwa
akiingia na ndege ya asubuhi hiyo. Grace na Danny ndio waliokuwa wakienda
kumpokea uwanja wa ndege wa KIA.
James hakuchelewa. Alimchukua Nanaa
kwenye gari mpaka kituoni. Walipofika tu na basi la kwenda Dar nalo likawasili.
Kaka yake akamsaidia kuingiza begi kwenye basi. “Naomba uniagie wenye
nyumba wangu.” “Nitafanya hivyo. Usafiri salama, nitakupigia baadaye kidogo.”
“Simu imezima kaka. Niliiweka kwenye umeme usiku kucha, kumbe switch ilikuwa
mbovu. Hata iliyokuwepo imeisha kabisa. Nikifika nitaiweka tena kwenye umeme,
halafu nikupigie.” “Usisahau.” “Siwezi kaka.” James akashuka baada ya
konda wa basi hilo kuingia nakusema wanaondoka. Akasubiri mpaka basi
lilipoondoka, na yeye akarudi hotelini.
~~~~~~~~~~~~~
Maji
yamemfika Nanaa shingoni. Historia imejirudia. Aamua kuondoka.
-
Je, amani aliyotaka iwepo akiondoka itakuwepo?
-
Geb bila Nanaa mjini Marangu!
-
Nini kitatokea huko aendako Nanaa
kutafuta kwake?
-
Na huku nyuma alikokuacha Marangu je?
Usikose Sehemu ya 16.
0 Comments:
Post a Comment