Heka heka kabla ya Safari ya Moshi kwenye harusi ya Malii.
Siku moja
kabla ya safari, yaani siku ya jumatano, Grace alimwambia Nanaa wawahi kutoka kazini
ili wakajitayarishe na safari ya kesho yake. Mara baada ya kufika tu nyumbani
Nanaa aliingia chumbani kwa bibi Fili hakumkuta. Akampigia simu. “Natafuta
vitu vya kula Geb njiani. Bila hivyo hatakula kitu ataishia kunywa maji tu. Na
safari yenyewe ndefu.” “Afadhali. Wewe si umeshaweka mizigo yako tayari? Maana
Grace amesema tunaondoka alfajiri sana.” “Mimi safari ndefu siziwezi, mwanangu.
Magoti yananisumbua. Nitawafuata na ndege ya ijumaa asubuhi.” “Mama wewe
jamani! Kwa nini hukuniambia!?” “Nilijua nikikwambia utagairi kwenda na wenzio.
Nenda kajichanganye bwana.” Nanaa akanyamaza. “Utakuwa
sawa. Narudi muda sio mrefu. Ninamalizia. Nikija tutakuja kuzungumza vizuri.”
“Usichelewe mama bwana. Kwanza nishakosa raha.” Bibi Fili akacheka na
kukata simu.
Bibi Fili
akarudi. Nanaa akatoka chumbani kwake haraka baada yakusikia sauti yake,
akamfuata chumbani kwake. Akamkuta bibi Fili anacheka mwenyewe chumbani
kwake. “Ujue ulichonifanyia sio vizuri mama wewe!” “Ningekwambia ungekataa
kwenda. Lakini kesho kutwa tu mbona tutakuwa wote na wewe!? Kachukue chumba cha
watu wawili. Mimi nikitua tu uwanja wa ndege, nakufuata tukae wote.” Nanaa
akajitupa kitanda cha jirani akionekana kuishiwa nguvu. Walishazoeana na Bibi
Fili, wakawa kama marafiki wa karibu sana. Kila alipotongwazwa huko, alimwambia
bibi Fili na kumtaka ushauri.
Bibi Fili
kwa muonekana alikuwa kama Grace, mkimya. Lakini kumbe akiamua kukuzoea, alikuwa
mzungumzaji mzuri tu. “Acha wasiwasi wewe. Ngoja nikusimulie habari ya
Viola. Leo Grace kanikumbusha wakati nipo kazini mchana, tukacheka sana.”
“Alifanyaje?” “Alikuja hapa kusalimia. Akampenda sana Geb. Akahangaika naye
wee. Kama unavyomjua Geb. Akiamua kukupuuza, utachoka tu mwenyewe. Kila
akijaribu hivi, Geb kimya kama hajui. Akaona Geb hana muelekeo, akahamia kwa
Danny.” Bibi Fili akaanza kucheka yeye mwenyewe, Nanaa akimwangalia.
“Sasa
akili za Danny wewe si unazijua? Akawa mwanzoni hajaelewa kama Viola anamtaka.
Mimi kama unavyonijua, mtazamaji tu. Nikawa namuona vile anavyohangaika na hawa
wanaume wa humu ndani. Safari za humu ndani hazimuishi. Kila siku anakuja hapa
nyumbani kusalimia. Akaanza urafiki na msichana wa kazi wa humu ndani ili apate
sababu ya kuja kulala hapa. Safari za kulala hapa zikaanza. Habanduki. Si
mchana si usiku yupo humu. Anamuwinda Danny na Geb. Lakini Geb akawa
ameshamjua, akawa anamkwepa.” Nana alijisikia vibaya sana.
“Wewe hujachunguza vizuri. Danny hataki awepo
nyumbani eti mkewe yupo jikoni masaa kwa masaa! Heri akanunue chips yai, au aje
na nyama choma au rosti, mle kuliko mkewe ashinde jikoni wakati yeye yupo.
Hathubutu. Au yale mambo ya mkewe amuache kitandani asubuhi kama wanawake
wengine. Aamke, amuache kitandani ili amwandalie kifungua kinywa, hataki.
Anataka alale na mkewe, waamke, waoge pamoja, ndio waende naye jikoni. Apike
kidogo tu, atoke wakae wote. Na kitafunio cha haraka anachopikaga Grace ambacho
anajua hakichukui muda mrefu huko jikoni ni chapati za maji tu. Sasa na zenyewe
huwa zinachosha. Akipika kitu kigumu, ujue Danny yupo kazini. Basi apike
haraka, akirudi amkute amekaa kama vile. Sio eti hajamuona mkewe siku nzima
wakiwa kazini, halafu aje hapa mkewe yupo busy jikoni, hapo hamuwezi kuelewana
hata kidogo na Danny.” Nanaa akacheka.
“Basi, turudi kwenye stori yangu. Grace
anamuuliza mumewe umeona nyoka? Anasema hapana. Nakwambia Danny anapiga kelele
kwelikweli anamtaka James aje pale haraka. Wote tukaingiwa na wasiwasi tukasema
labda kapatwa na kichaa. Bahati nzuri ilikuwa siku ya sikukuu, watu hawaendi
kazini, hakuna foleni. Kwa hiyo James akaja kwa haraka akamkuta bado yupo juu
ya kitanda. James anamuuliza vipi? Akaanza kumuuliza James kama anakumbuka vile
alivyohangaika kumpata Grace. Sasa James anamwambia anakumbuka, kwani
vipi? Danny kakazana, eti James atuelezee shida alizopitia mpaka akakubaliwa na
Grace. Basi James akasimulia kwa kifupi wakati huo bado kasimama juu ya kitanda
kabisa, hataki kukaa. Watu wote tumetoa macho tunamwangalia. Grace amemletea
maji ili anywe, hataki. James akamaliza kusimulia huku anamkatisha kila mara
anamkumbusha hiki au kile. Anamwambia anasahau. Basi James akawa anarudia
kueleza mpaka akamaliza. Wote tumesimama tunataka kujua mwisho wa yote ni nini
kinaendelea? Maana habari za Danny na Grace kila mtu anazijua.” Mama G
akacheka tena.
“Sasa kwa nini alitaka kaka asimulie
tena?” Nanaa akahoji. “Sikiliza sasa. Baada ya kuridhika, akamwambia
afungue mlango wa bafuni. James si akamkuta dada yake yupo uchi huko bafuni.
Akafunga mlango haraka kwa mshituko. Sisi hatuelewi. Tunamuuliza James, kwani
kuna nini huko bafuni? James kakaa kitandani ameinamisha kichwa kama mgonjwa.
Grace akamuuliza tena Danny. Safari hii kwa ukali. Si ndio akaanza kusimulia
kisa kizima kuwa Viola amemfuata hapo chumbani anamtaka kimapenzi.” Nanaa
akakumbuka vile Viola na Vai walivyorudishwa nyumbani kwa haraka wakati Nanaa
alivyokataliwa kuja nao huku jijini kipindi amemaliza kidato cha 6.
“Danny akaanza, ‘Huyu mtoto anakichaa kibaya
sana. Grace mwenyewe wala sijamfaidi. Yaani yale matusi yakunikataa wakati
namtongoza wala bado hayajaisha moyoni, eti na yeye anataka kunitoa humu ndani!
Unataka kuniponza wewe?’ Yaani badala ya kusikitika, tukajikuta wote
tunacheka mbavu hatuna. Vile anavyosimulia na anavyotetemeka, utafikiri
amepigwa shoti ya umeme. Grace akamuuliza sasa kwa nini anaongelea juu ya
kitanda? Anasema alikuwa anaweka msisitizo, ili James aje haraka, amchukue
mdogo wake pale ndani, asimletee balaa.”“Maskini kaka yangu!” Nanaa akamuhurumia
James.
“Nakwambia James alitia huruma. Akawa mwekundu
kama nyanya. Ungemuhurumia. Alikuwa hawezi kumtizama mtu machoni. Alijisikia
vibaya sana. Ungekuwepo, ungemuhurumia zaidi. Aliomba msamaha kwa Grace, mpaka
akapiga magoti. Sasa Danny naye badala amfariji mwenzie James, amekazana kumshutumu
eti yeye ndio amemtuma mdogo wake. Basi James yupo amepiga magoti anatubu huku
anajitetea na Danny naye anaendelea kumlaumu tu. Mpaka Grace alipomgombeza
Danny ndio akanyamaza. Sasa jioni yake ndio tulicheka mpaka
machozi.” Nanaa akajifunika uso wake na mto.
“Aibu gani hii! Sasa wewe mama ulipomuona
mwanzoni akiwa anahangaika na Geb, kwa nini hukumkataza?” “Mimi! Akaa.
Nanyamaza kimya, ili kila mtu yakija kumshinda baadaye asije nilaumu.
Najiangalizia kimyaa kama sipo.” “Sasa na kwa Danny? Kwa nini
hukumwambia mkewe?” “Niambiwe mchonganishi, navunja ndoa za watu!? Tena na
Grace mwenyewe aliniuliza hivyo hivyo. Nikamwambia kama yeye anajidai yupo busy
haoni na anashindwa kumchunga mumewe, atajijua mwenyewe. Viapo alitoa yeye
mwenyewe kanisani. Halafu aje ashindwe kuvitekeleza, atake watu wote tumchunge
mumewe! Aku! Apunguze shuguli, amlinde mumewe.” Nanaa alikuwa anacheka
nakujisahau kama watu wengine wanawasikiliza.
Waliendelea kucheka mpaka Grace naye
akaingia. “Jamani mnacheka nini? Niambieni na mimi.” “Acha umbea wewe
Grace. Nenda kalale na mumeo.” Mama yao akamjibu akiendelea na shuguli
zake. “Si mnisimulie tu!” “Acha umbea wewe mtoto. Danny atakuja sasa hivi
kukufuata. Sitaki mnijalie humu ndani kwangu, nataka kulala. Ondoka. Nanaa na
wewe nenda kamalizie kujiandaa. Acha kupenda umbea. Kwanza mimi natoka mara
moja. Narudi tena dukani, kuna kitu nimesahau kununua.” Nanaa alitoka huku
akiendelea kucheka.
****************************
Grace
akarudi chumbani kwao alipokuwepo mumewe na Fili wakicheza tv games. Fili
alikuwa akishangilia anavyomfunga baba yake. Ilikuwa game ya mpira wa kandanda.
Walikuwa wakicheza wawili tu hapo chumbani. Nanaa akaingia chumbani kwake. Mama
G, na yeye akaondoka na gari yake. Kulikuwa kumetulia sana. Bado Geb hakuwa
amerudi kutoka kazini. Nanaa akaanza kuwaza afungashe nini cha muhumu.
Mara
wakasikia mlango wakuingilia ndani unafunguliwa. Sauti ya Liz na
Geb. “Nimekwambia usiwe na wasiwasi Liz. Kwa nini unataka kujinyima raha
bure?” “Kwanza kwa nini tuondoke na gari tusipande ndege? Mimi sipendi wala
sijazoea usumbufu.” “Tukiondoka na ndege, tutatumia usafiri gani kutuzungusha
tukifika huko Moshi? Tumekubaliana na Danny mara baada ya sendoff, tuzunguke
kidogo. Hata tukiweza twende mpaka Arusha. Tutakuwa wengi, nina uhakika
utafurahia tu.” “Hayo ndio yanayonichosha. Watu wengi kila mahali! Hamna sehemu
ya utulivu ya kwetu sisi wenyewe! Kila mahali watu! Na leo tena unasema
tutakuwa na watu humo kwenye gari. Hamna sehemu ya kupumzika jamani!? Watu kila
mahali!” “Tunaondoka na hii SUV ya viti nane. Na tutakuwa watu wa humu humu
ndani tu. Hatuwezi kubanana.” “Kila mtu anaharufu yake Geb. Tukichanganya
harufu ya kila mtu humo ndani kwenye gari, na safari yenyewe mpaka Moshi!
Nitatapika njia nzima.” Liz aliendelea kulalamika.
Nanaa aliyekuwa chumbani
kwake aliweza kusikia kila kitu. Hakujua Grace na mumewe kama na wenyewe
wanasikiliza. Hamu ya safari ikamwisha kabisaaa! Akaamua asiende. Akaacha
kukusanya vitu vya safari. Akaamua asubiri patulie, atoke akapike chakula cha
kula nyumba nzima usiku huo. Kwanza safari yenyewe ni ya Moshi. Hakutaka kwenda
tena huko na kujiongezea matatizo. Geb alimwambia ajiandae kwenda kuandika
historia mpya. Lakini mpaka hapo, akajua historia lazima itajirudia tu. Asiongeze
idadi kwenye gari ya watu na kuongeza harufu nyingine. Akajituliza.
Bado Liz
aliendelea kulalamikia hili na lile. Kila Geb alipompa suluhu ya hili,
aliongeza tatizo jingine. Mara Nanaa akasikia mlango wa chumbani kwa kina Grace
unafunguliwa. Akajiweka sawa kusikiliza kitakachoendelea. Ukimya wa Geb na Liz
ukazuka. “Samahani Geb na Liz. Naingilia mazungumzo yenu. Kama harufu
unazozungumzia wewe Liz ni ya hii familia yangu na Nanaa, wala kusiwe na shida.
Danny ameamua tuendeshe gari yetu tu. Kwa hiyo nyinyi nendeni wawili tu.” “Hata
mkinielewa vibaya ni poa tu.” “Wala hakuna anayekuelewa vibaya Liz. Sisi
tunaelewa. Na tuna amani.” “Mnaelewa nini sasa?” Liz akauliza kwa ushari.
“Hivi mbona kama hujanielewa? Nimekupa suluhu ya
tatizo lililokuwa likikukera. Tena kwa amani tu. Kwa nini unatafuta tatizo
jingine? Kama hujaelewa chochote nilichosema tokea nimewafuata hapa, elewa
hivi, sisi tutaendesha gari yetu. Mimi, Danny, Nanaa na Fili. Basi.” Grace
alijaliwa sauti ya upole sana, japo ilisikika ya uvivu zaidi.
“Maana mnaweza msinielewe! Lakini mimi
sijali.” Liz akaongeza. Grace hakusikika kujibu. “Kwanza nashangaa
kwa kumbi zote zilizojaa hapa mjini eti mtu anaenda kufungia harusi au sijui
sendoff huko milimani! Na sisi eti tunaenda! Kwa lipi haswa? Ndio maana nasema
haya mambo yakuoa hujajiandaa kipesa sio mazuri. Harusi sio dharula. Ni kitu
mtu anatakiwa kujipanga kabla. Sio kushikana mashati, eti
mnachangishana!” Liz akaendelea.
“Watu wanawekeza mpaka kwenye misiba yao kabla
hawajafa! Ili ukifa usisumbue watu na maiti yako. Sembuse harusi! Tena ya watu
mnaokubaliana na kupanga tarehe! Panga harusi ukiwa na pesa yako sio unapanga
harusi kwa pesa za watu wengina! Mtu akiwa na pesa yake si anatafuta ukumbi na
hoteli sehemu za kueleweka? Kama ndugu zake wako mbali na mjini, anawaleta
mjini na kuwaweka mahotelini. Harusi ikiisha kila mtu anarudi kwake, sio lazima
kuendelea kufuatana nyuma. Hayo ndio maisha na hiyo ndio habari ya mjini. Sio
mnafunga safari kufuata harusi ya kijijini! Kwa nini!? Mimi hata
sielewei!” Nanaa alimsikia Liz akiendelea kulalamika. Aliongea kwa kutumia
lugha ya kingereza kwa muda mrefu, huku akiweka maneno machache sana ya
Kiswahili. Na kilikuwa kingereza kizuri. Maneno aliyatamka kifasaha kama mzawa
wa huko nchini Uingereza. Nanaa akabaki akitamania.
Cha ajabu hakumsikia Geb, wala Grace wakijibu
tena na wote walikuwa maeneo hayo hayo. Nanaa aliendelea kusikiliza maneno ya
kingereza yanayotolewa kwa jazba. Mara akasikia hatua za Grace zikimfuata
chumbani. “Nanaa!” Mlango ukafunguliwa. “Usiende kupika. Mama
amesema atatuletea kitimoto na ndizi. Wewe endelea kujiandaa. Akirudi, nitakuja
kukuita.” “Asante.” Nanaa akashukuru, Grace akatoka na sura yake tulivu.
Akamsikia akiingia chumbani kwake. Kidogo wakasikia Geb na Liz nao wanaingia
chumbani kwa Geb.
Mara akasikia gari ya bibi
Fili. Nusura aruke pale alipokuwa amekaa. Akaona atulie kwanza kwani alimsikia
Fili akiwa amefungua mlango kwa haraka, anakimbia huku akiita bibi Fili. Bibi
Fili akaingia. “Umeniletea pipi yangu?” Fili akauliza. “Nipokee
kwanza. Mbona hivyo Fili?” “Nataka kujua kwanza bibi.” “Nimeleta.” Bibi
yake akajibu. “Hivi nilikwambia kuwa nakupenda?” Fili akamuuliza bibi
yake. “Mmmh!” Nanaa akamsikia bibi yake ameguna, akacheka peke yake
pale chumbani. “Kweli tena bibi Fili. Mimi nakupenda sana.” “Wewe mapenzi
yako hayatabiriki bwana!” “Mimi nakupenda wakati wote. Ni mama tu ndio huwa
ananilazimisha kulala naye. Lakini mimi ningekuwa nalala na wewe kila
saa.” Grace akatoka.
“Ujue wewe Fili nakusikia
wewe! Na nisikuone kitandani kwangu tena. Ukalale huko huko unakomdanganya bibi
yako.” Fili akaanza kucheka. “Basi bibi. Wewe tutalala wote kesho.
Leo nalala na mama yangu.” “Kila siku habari ni hiyo hiyo! Mpaka ufukuzwe huko
chumbani kwa watu, ndio kimbilio linakuwa mimi.” “Sasa si kwa sababu nakupenda
wewe.” “Mmmh!” Bibi Fili akaguna tena.
“Nanaa yuko wapi? Mwiteni
aje kula.” Aliposikia tu hivyo, akatoka haraka. “Halafu hii chupa
mbona ina uji? Huyu Geb mbona hajanywa? Au hayupo? Lakini kama nimeona gari
yake hapo nje!” “Yupo chumbani na Liz.” Grace alijibu huku akiandaa
chakula. “Oooh!” Mama G akaitika. Nanaa akaingia. “Mbona
sura imepooza tena, wakati nilikuacha na furaha?” Mama G alimuhoji Nanaa
mara alipoingia pale jikoni. “Nimepata dharula mama. Naona sitaweza kwenda
tena Marangu.” “Mmmh! Dharula hiyo dharula gani? Mbona gafla!? Nimekuacha hapa
hata lisaa saa halijaisha, tayari umepata dharula!?” “Kweli mama. Natakiwa
kwenda kuangalia chumba kesho. Dalali kanipigia simu sasa hivi. Kanipatia chumba.” Grace
na mama yake wakabaki wakimwangalia Nanaa.
“Itabidi tu kwenda hiyo
kesho. Lasivyo huyu dalali atakigawa chumba. Heri tu kesho nikifuatilie,
nifunge mkataba kabisa.” Nanaa aliendelea kujitetea. Grace na mama yake
wakaangaliana. “Basi kazi mtakuwa nayo huko njiani.” Mama G
akasema. “Wala si kidogo.” Grace akajibu akikumbuka hasira za kaka
yake, kama Nanaa asipokwenda. Lakini Nanaa hakuelewa ni nini wanachoongelea.
Akanyamaza.
Danny akatoka. Wakaanza
kula. Lakini kulikuwa na ukimya wa namna yake sio kama siku zote. Walikula
kimya kimya mpaka wakamaliza. Kila mtu akaaga kuwa anakwenda kulala mapema
tayari kwa safari kesho yake. “Msihangaike kuosha vyombo. Mimi nitaosha na
kusafisha hapa. Nyinyi kawahini kulala. Mpumzike kwa safari kesho.” Nanaa
aliongea huku akikusanya vyombo kurudisha jikoni. Danny na familia yake
wakaondoka kuingia chumbani kwao. Bibi Fili naye akaingia chumbani kwake.
Wakamuacha Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~
Wakati
Nanaa yupo jikoni, Bibi Fili akamfuata. “Geb anatatizo moja.” Nanaa
akageuka kumwangalia. Alikuwa anatoa uchafu kwenye vyombo vichache walivyolia
chakula, ili avipange kwenye dishwasher, akaacha. “Tatizo
gani?” Nanaa akauliza. “Unapomuahidi kitu, anapenda utimize. Ni heri
usimuahidi kabisa. Yaani ukiona hutaweza kufanya jambo analokuomba, ni heri
usimkubalie tokea mwanzo. Anaumia vibaya sana, ukiahidi halafu
usitimize.” Yule mama aliongea kwa kifupi tu, akatoka pale jikoni
akamuacha Nanaa.
Nanaa
alibaki akiwaza pale jikoni. Alijua wazi mama yule anampa yeye ule ujumbe.
“Sasa mimi nina umuhimu gani wa kwenda jamani!? Si atakuwa na ndugu zake na
mpenzi wake!? Mimi ninaulazima gani?” Nanaa aliendelea kujitetea
mawazoni. Akasikia Geb ametoka na kuita. “Mama!” “Nipo huku
chumbani.” Geb akaenda chumbani kwa mama yake. Nanaa akaendelea kusafisha.
Baada ya muda akasikia mlango wa jikoni
unafunguliwa. “Nanaa!” Akageuka alikuwa Geb na uso uliopooza zaidi si
kawaida yake. “Abee!” Nanaa aliitika kwa upole. “Mama ameniambia
hutuendi wote tena!” “Nilimwambia kuwa dalali alinipigia simu akaniambia kesho
nikaangalie chumba.” “Ni kweli?” Geb akauliza, Nanaa akabaki kama amepigwa
na butwaa. “Nanaa?” “Hapana sio kweli.” Nanaa akajikuta
anajisalimisha.
“Najua umechoka. Lakini naomba ujikaze kunywa
hata uji tu. Usilale na tumbo tupu.” Nanaa akaendelea
kusisitiza. “Nakushukuru Nanaa. Asante.” “Kwa hiyo umekubali
kula?” Nanaa akauliza, Geb akacheka kidogo. “Uji,
tafadhali.” “Yes!” Nanaa akafurahi sana mpaka Geb akajua. Akacheka.
Kwa haraka kama asimcheleweshe kurudi huko
chumbani, akammiminia uji kwenye bakuli kubwa huku Geb akimwangalia. Akamuwekea
kwenye sinia lake pamoja na maji na matunda. “Ukimaliza wewe weka hata nje
ya mlango wenu. Usihangaike kurudisha huku. Mimi mwenyewe nitakuja
kutoa.” Geb akamtizama. “Asante Nanaa. Nakushukuru. Ila nitarudisha
tu mimi mwenyewe. Wewe nenda kapumzike.” Akamkabidhi. “Usiku mwema
Nanaa.” “Na wewe pia, Geb.” Akamtizama kidogo, nakutoka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
aliamka alfajiri sana. Akamkuta bibi Fili jikoni. “Hivi mama wewe ukoje
lakini!?” Wakaanza kucheka. “Kwani mimi nimesemaje? Si nilimwambia tu
kuwa huendi!” “Sasa kwa nini umwambie?” “Ulitaka kufanyeje?” “Nilipanga asubuhi
hii wakati watu wote washapanda ndani ya gari ndio niseme.” “Halafu mwanangu
asafiri bila raha? Aka mwenzangu! Ndio kiziwanda changu huyo.” “Sasa mimi nina
umuhimu gani huko kama sio kuongeza tu idadi!?” “Bwana wee, wewe nenda bwana.
Tena mumeo Zinda atakuwepo huko huko.” Walianza kucheka mpaka wakajisahau.
“Mtoto mbaya wewe! Sasa kwa nini ukatae gari?”
“Sio gari tu mama na wewe, na nyumba!” Nanaa
akaongeza. “Gauni.” Mama G akaongeza. “Na viatu mama! Kwa raha
zangu.” Nanaa alitembea mbele ya Mama G, huku anaringa kidogo. Yule mama
akawa anacheka. “Nanaa wa dhahabu!” Mama G akaongeza. “Kumbe!
Sasa hivi ningekuwa nimejaa madhahabu. Shingoni na mkononi.” Bibi Fili na Nanaa
waliendelea kucheka pale jikoni mpaka wakaamsha kila mtu."
“Hivi nyinyi huwa mnacheka nini hakiishi jamani!?
Mnajua saa hizi ni saa ngapi?” Grace aliingia pale jikoni akilalamika. “Umbea
wako ndio umekuamsha wala sio sisi. Usiye lala na mumeo ukatulia ndani ni
nini?” “Kelele!” Grace akamjibu mama yake. “Mama huyo!” Nanaa
akajitetea. “Aliye na kazi ya kucheka hapa jikoni ni nani kama sio wewe Nanaa?
Acha kunisingizia bwana.” Grace alianza kusaidia kazi pale jikoni.
“Heri huyo Geb mumtengenezee uji mwingi. Hatakula
njia nzima.” Grace aliongeza. “Mama amemnunulia vitu vya kula njiani.
Karanga na korosho.” “Nitamtengenezea na fruits salad. Akale mbele ya safari.
Naomba msisitize. Unanisikia Grace? Lasivyo mtafika mmwage vyakula vyote.”
“Wewe mwekee kwenye cooler box na hotpot. Unamjua Geb. Akiwa na hasira anaweza
asile njia nzima. Akiwa anakupigia simu msisitize wewe mwenyewe. Mimi anaweza
hata asinijibu. Si unamjua mwenyewe?” “Bora viingie kwenye gari. Nitakuwa
nampigia mwenyewe nimkumbushe. Na wewe Nanaa naomba uwe unamkumbusha.” “Kwani
Nanaa anaenda tena!?” Grace akashangaa.
Mama G akaanza kucheka. “Si mama
huyo!” “Alimuahidi yeye mwenyewe huyo Geb.” Mama G
akaongeza. “Na ukimuahidi Geb kitu, lazima utimize. Ni heri kama huna
uhakika, umkatalie tokea anakuomba. Anaumia sana ukija kubadilika baadaye. Na
yupo hivyo tokea mtoto.” Grace aliongea kama mama yake. “Lakini
nimemuomba tuondoke wote. Nipande gari yenu nyinyi.” Nanaa
akaongeza. “Mmh! Mbona tena mnaendesha magari mawili wakati aliniambia
mtaondoka na gari ile kubwa. Kwa nini kumkimbia mziwanda wangu!?” Grace na
Nanaa wakaangaliana. Kisha wakanyamaza. “Nishaelewa.” Mama G, alijua
tu baada ya Grace na Nanaa kuangaliana. Wakanyamaza.
Harufu ya manukato ya Liz ikaanza kuenea taratibu
pale ndani. Akatoka na funguo zake. “Nakwenda kuhamisha mizigo yangu
kwenye gari yako.” Walimsikia akimuaga Geb. “Sawa. Lakini si utarudi
ndani ili tunywe kwanza chai?” “Sio lazima.” Liz akajibu na kutoka nje.
Geb akaingia. “Shikamoo mama.” Akamsalimia mama yake. “Marahaba.
Mlilala salama?” “Ndiyo. Za asubuhi?” Akiwa anamaanisha salamu kwa Nanaa
na Grace. “Kwetu tumeamka salama.” Grace akajibu huku akitoka. “Ngoja
nikamuamshe Fili, tujiandae na sisi tuondoke.” “Si tutaongozana?” Geb
akamuwahi dada yake. “Vyovyote tu. Hamna shida. Ila ujue sisi bado. Mpaka
huyu kaka aoge, tulazimishane kula, na mimi nijiandae,
tutawachelewesha.” Grace akajibu. “Hamna tunapowahi. Vizuri tuondoke
kwa pamoja.” Geb akajibu.
“Hilo ni swali ambalo ukipenda, utanipa jibu
baadaye kama uliamua kuja na ndege au la. Lakini mimi nitaondoka na gari kubwa,
pamoja na kina Danny. Unanijua mimi huwa sio mtu wakubadilika badilika Liz.
Nilipewa na Danny jukumu lakufanyia hiyo gari service ili iwe tayari kwa safari.
Nimefanya hiyo kazi. Leo asubuhi siwezi kuamka eti nimwambie Danny apandishe
familia yake kwenye gari ambalo halijafanyiwa service kwa safari ndefu, halafu
eti mimi na wewe tunaendesha gari lenye viti nane! Tupo peke yetu njiani! Si
sawa na sitafanya hivyo. Nashauri uje na ndege. Na kama utapata gari ya
kukodisha pale uwanja wa ndege, uchukue utufuate Marangu au ukitaka mimi naweza
kukufuata. Huna haraka ya kuamua. Utanijulisha kwa simu.” Watu wote
walikuwa kimya.
Nanaa alipomsikia Geb ameweka tu kituo kwenye
maongezi yake, akatoka pale jikoni kimya kimya, akarudi chumbani kwake
akinyata. Mama yao alikuwa akiendelea kupika huku akitayarisha
matunda. “We Geb! Hebu kaniletee ile cooler kutoka kwenye gari yako.
Nataka niweke kila kitu tayari. Nisiwacheleweshe.” Mama yake akamtuma kwa
kuamuru kidogo. Geb akajua ameshakasirika na yeye. Alisikika kwa sauti ya amri,
wala si utani kama alivyokuwa na Nanaa pale jikoni. Geb akatoka. Wakasikia Liz
anatoka na yeye.
Nanaa akaingia kuoga haraka haraka akaanza kuvaa.
Wakati anamalizia, Geb akaingia. “Nimefuata mzigo wako. Umeshaweka kila
kitu?” “Nafikiri kila kitu kipo tayari.” Nanaa alijibu huku akiangaza
macho kama kuangalia kama amesahau kitu. “Nataka nikapange kwanza mizigo
yote kwenye gari.” “Umeshakula?” “Nitakula nikiridhika kila kitu kipo kwenye
gari, zaidi mizigo yako wewe.” Nanaa akacheka. “Hukawii kubadili
mawazo wewe!” “Sibadiliki tena bwana!” “Wewe nipe mzigo nikaweke kwenye gari
ndio tukae chini tule.” Nanaa akamalizia kuweka vitu baadhi, akafunga
sanduku hilo dogo, Geb akatoka nalo.
Walikaa wote mezani, wakaanza kula. Kilikuwa
kifungua kinywa kikubwa kama chakula cha mchana. Nyama iliyokuwa imebakia jana
yake, ilipashwa moto. Kukawepo na chapati nzuri sana za kusukuma. Mchuzi wa
maharage na chai iliyowekwa viungo. Baadhi ya matunda aliyobakisha Mama G,
baada ya kumuwekea Geb ya kula safarini, aliyaweka hapo mezani. Geb alikunywa
uji wake kama kawaida yake. Mama yao akawaambia lazima waombe kabla ya safari.
Wakashikana mikono, bibi Fili akaomba. Safari ikaanza.
Safari ya
Moshi kwenye harusi ya Malii.
Alikuwa akiendesha Geb. Akakaa mbele yeye na
Danny. Nanaa na Grace walikaa kiti cha pili, Fili katikati yao. Kwa kuwa Liz
hakuwepo, wakalaza viti vya mwisho kabisa. Wakapanga mizigo yao humo nafasi
ikawepo tu yakutosha. Waliondoka jijini saa 11 asubuhi. Hakuna aliyeuliza alipo
Liz wala Geb hakutaka kuzungumzia hilo. Walipoanza kuliacha jiji la Dar,
wakaanza kupigiana simu na kukubaliana wasubiriane mjini Kibaha ndipo waendelee
na safari.
Walipofika Kibaha, wakatafuta mahali wakaegesha
magari yao. Nanaa alishangaa kuona magari zaidi ya nane yakiwa yanaongozana
kumsindikiza Malii kumchukua mke Marangu. Geb na Danny wao ndio walishuka
kwenye gari kuzungumza na wenzao. Baada ya muda mfupi wakarudi ndani ya gari
safari ikaanza tena. Nanaa alianza kusikia baridi. Geb aliwaomba radhi kwa
kuwasha AC kali. Akasema kila akiendesha anapenda kuwe na baridi kwenye gari,
ili asilale. Walimvalisha Fili sweta, Nanaa akajifunika mtandio wake, akalala.
Danny na Geb ndio walikuwa wakiongea njia nzima
huku wanacheka. Nanaa alishituka kutoka usingizini baada ya Danny kucheka kwa
sauti. Akatoka ndani ya mtandio wake taratibu, akamkuta Grace ametulia kama
hayupo pale. “Mama alisema tumkumbushe Geb kula karanga au ndizi za kuiva.
Hakunywa uji mwingi.” Nanaa alinong’ona. “Nilisha sahau.” Grace
alijibu na tabasamu. Akachukua ndizi, akamenya kidogo akamgusa kaka yake
mgongoni. “Chukua hii ndizi ule.” Geb akapokea. “Asante. Nilifikiri
umelala.” “Nasinzia tu lakini usingizi hauji. Danny anacheka kwa sauti
kweli!” Grace akalalamika. “Mmmh! Wewe si mlalaji bwana. Mbona
mwanangu kalala?” “Nina usingizi sana. Lakini wewe ndio unaniamsha.” “Eti
Nanaa?” Danny alimchokoza Nanaa. Nanaa akabaki akicheka bila kujibu.
Akajirudisha ndani ya mtandio wake akarudi kulala.
“Sasa ngoja tukaone fujo zake huko Moshi.” “Wala
hatutafika Moshi. Subiria tu, utamuona.” Danny alimjibu mkewe. “Katuzungusha
jana kama wendawazimu! Mpaka James akaamua atuache madukani. Eti anatuambia
tumwangalie kwa jicho la Nanaa. James anamwambia hatuwezi. Yeye achague nguo
anazotaka, tuondoke. Kanunua suti ya pesa kibao sababu ya Nanaa. James
anamuuliza atakula nini kama anatupa pesa yote hiyo kwenye suti? Akatuambia
hiyo ni pesa iliyokuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya pombe kwa mwaka mzima.
Sasa ndio ameamua kuwekeza kwenye muonekano wake mpaka ahakikishe amemuweka
Nanaa ndani.” Walizidi kucheka.
“Zinda ni chizi jamani! Sasa magauni na viatu vya
Nanaa?” Grace akauliza huku wote wanacheka. “Wewe utamuweza Zinda na
fujo zake. Fujo tu. Alikuwa anasema kuanzia sasa, matendo yake yataongea.
Hataki tena maneno mengi.” Waliendelea kuongea na kucheka mpaka walipofika
Segera wakaamua wote wasimame.
~~~~~~~~~~~~~
James na yeye alikuwa kwenye msafara. Alipanda
gari moja na Malii, Zinda, Kamali, na Jonas. Walifika Segera bado ni mapema tu.
Wengi wao wakataka wapate supu. “Utataka kula kitu?” Grace akamuuliza
Nanaa. “Bado najihisi tumbo limejaa.” “Hata mimi.” Grace
aliongeza. “Tushukeni tunyooshe miguu. Tumuamshe Fili ajisaidie
kabisa.” Danny alishuka akaja upande wa mkewe. “Shuka nikusaidie
kumbeba huyo.” Grace akashuka akampisha mumewe. Akamfungua mkanda mwanae,
akamtoa pale kwenye kiti chake akamuweka pembeni ili aamke. Fili akafungua
macho. “Vipi?” Baba yake akamuuliza. “Namtaka mama.” “Mama yako
huyo hapo chini ya gari. Twende.” Fili akachungulia kuhakikisha, akamuona
mama yake ndipo akatulia.Wakaondoka Danny na familia yake.
Wakabaki Geb na Nanaa mle ndani ya
gari. “Twende Nanaa.” Geb alizima gari akamgeukia. “Naona
nyinyi nendeni tu, mimi nitabaki humu humu ndani ya gari.” “Kwa
nini?” Nanaa akakosa jibu. “Twende tukakae na wenzetu. Usikae humu
ndani peke yako.” “Nikuwekee matunda ule?” Geb akafikiria kidogo. “Au
nikupe korosho?” Nanaa akaongeza swali jingine kabla Geb
hajajibu. “Naomba korosho tafadhali.” Nanaa akafungua mfuko maalumu
aliotayarishwa na mama G, kwa ajili ya mwanae huyo anayesumbua kula. Akatoa
korosho, akampa. “Mbona nyingi?” Geb alilalamika kidogo huku
akipokea. “Unahitaji kula Geb. Hukunywa uji vizuri, na wewe unaendesha
safari ndefu. Utachoka. Kula tu, zikibaki nitarudisha. Chukua na hili kopo la
soda.” Geb alitoa tabasamu na kupokea. “Asante. Twende
basi.” Geb akasisitiza.
Geb akamwita wakati anafunga mfuko. “Nanaa!”
“Abee!” Nanaa akaitika na kumwangalia. “Nimefurahi
umekuja.” Nanaa akainama huku anacheka. “Twende.” Nanaa akashuka
akawa anamfuata Geb kwa nyuma yake kidogo.
~~~~~~~~~~~~~
Mara akasikia watu wanacheka. Akaangalia pembeni
akamuona Zinda anamsogelea na maua mkononi. Nanaa alitamani kugeuka upepo. Kila
mtu alikuwa anacheka huku wakiwaangalia. Akasimama, Zinda akamsogelea mpaka
pale. “Haya ni yako Nanaa.” “Acha kupiga goti kama mtoto wa kike Zinda!
Wewe ukoje bwana?” “Sijapiga goti bwana Danny!” Zinda
akajitetea. “Umepiga goti, wote tumekuona.” Kila mtu akamshambulia
Zinda. “Tumekuona bwana, acha ubishi Zinda. Magoti kama mtoto wa
kike!” James alikuwa akicheka sana. “Usicheke James. Anatia aibu
kweli!” “Sikujua kama hali ni mbaya hivi! Na hapo kanywa bia mbili za haraka
haraka, akafunga na tai, ili aweze kutoa hayo maua!” James aliongeza
nakufanya watu wacheke upya, Danny akabaki anatingisha kichwa.
“Sasa kutoa maua tu, unakunywa bia mbili na
kufunga tai. Siku ya kumkabidhi hilo gari si utafunga baa zote
mjini?” Kila mtu alikuwa anacheka sana. “Daah! Hapa kazi
ipo.” Grace alikuwa anacheka mpaka anafuta machozi. Nanaa akamtizama Geb.
Akakuta anamwangalia kwa utulivu. Macho yao yakagongana. Nanaa akainama.
“We Zinda! Nini bwana? Umeng’ang’ania maua kama
wewe ndio umepewa?” “Danny naye hana subira! Acha nikusanye nguvu, kaka!” “Basi
sisi tunaondoka. Hatuwezi kulala hapa Segera.” Kila mtu alikuwa anacheka.
Walikuwa wametoka kwenye magari yao, wanaangalia vituko vya Zinda na Danny. Danny
akamsogelea akiwa bado amembeba mtoto wake, akampiga ngumi ya begani. Maana
alibaki kama ameganda. “Zinda!” Danny akamuita kwa
ukali. “Nanaa! Nanaa mama watoto…” Zinda akaanza tena. “Anaanza
kuharibu tena!!” Danny alimkatisha. “Danny mbona huna subira kaka?
Naanzia mbali. Subiri. Nitashika tu kasi.” “Sasa Nanaa mama watoto ndio nini
Zinda? Mpe maua. Basi.” Kila mtu alikuwa akicheka sana.
“Mimi naona hili zoezi tuliahirishe. Mnamchosha
dada yangu bure!” “Mimi si nilikwambia James? Akawa ananibishia, anasema
nimeongeza. Sasa umeona mwenyewe?” “Kweli hii aibu ya mwaka!” “James! Mimi na
wewe tumetoka mbali sana mtu wangu. Usininyime dada yako.” “Nanaa huyo hapo.
Hujanyimwa chochote.” “Basi ngoja nikaongeze bia nyingine narudi sasa
hivi.” Zinda akaondoka na maua yake mkononi. Watu walizidi kucheka.
Baada ya utani wa muda mrefu, huku Geb akicheza
mpira na Fili akiwa kama hayupo pale. Bila kuchangia neno lolote bali kumtizama
tu Nanaa, wakaamua waondoke tena. Wakati Geb anawasha gari Zinda
akawakimbilia. “Danny! Washikaji wameniambia kama haya maua hataondoka
nayo Nanaa hapa, basi mimi nipande tu basi niwafuate. Wamenishusha kwenye gari
yangu bwana!” “Sasa hapa kwangu unataka nini wakati Nanaa yupo hapo kiti cha
nyuma? Wewe mpe bwana tuondoke. Unatuchelewesha.” Wakasikia honi. Wakajua
wanampigia Zinda.
Zinda akakohoa mara kadhaa. Akatoka pale kwenye
dirisha la mbele alilokuwepo Danny, akarudi dirisha la nyuma alilokuwepo Nanaa.
Akakohoa tena. “Sasa Nanaa, ni hivi. Moyo wangu umevutiwa sana na wewe.
Pokea maua haya, ishara ya upendo wangu kwako.” “Daah! Malii hana mistari mingine
tena yakusema siku ya harusi yake!” Danny alifanya Geb na Grace waanze
kucheka. “Nanaa! Naomba pokea tu hayo maua. Lasivyo tutalala hapa.” Danny
alimgeukia na kumsihi. Nanaa akayapokea. “Asante Zinda.” Nanaa
alishukuru huku akicheka kwa aibu.
“Umeyapenda mama watoto wangu? Eti Nanaa?”
“Nimeyapenda ni mazuri.” Nanaa alijibu huku akiyaangalia yale
maua. “Basi moyo wangu umefurahi sana. Nime..” “Aaaahhh.” Danny
alikohoa kwa kumkataza. Zinda akatulia kidogo. “Au nihamie humu kwenye gari
yenu ili niwe na Nanaa?” “Hapana Zinda. Ondoka. Hatukutaki humu ndani.
Tena ondoka haraka kabla hujaharibu zaidi. Toka, rudi kwenye gari yenu.” “Sawa
kaka.” Zinda akaondoka akaacha kila mtu akicheka huku wanachungulia kwenye
magari yao. Wakaanza kushangilia. Zinda akawapungia mkono zaidi ya mara tatu.
Akimuaga Nanaa. “Daah!” Danny alisikitika.
“Sasa maua kayapata wapi?” Grace aliuliza
huku akicheka. “Nakwambia jana katuzungusha mjinga yule! Halafu sasa
mbishi. Hataki tumshauri, huku anauliza.” Walizidi kucheka. Waliendelea
kuongea mpaka simu ya Geb ilipoanza kuita.
~~~~~~~~~~~~~
Ikaita tena, akapokea. “Nimepata ndege. Naondoka mchana. Itabidi uje unipokee.”
“Sisi bado tupo njiani Liz.” “Mnategemea kufika saa ngapi?” Liz
akauliza. Geb akafikiria kidogo. “Geb!” Liz
akaita. “Sijui. Sina uhakika. Lakini nashauri kama
utawahi kufika kabla yetu, chukua taksii ikupeleke mpaka Marangu hoteli. Sisi
wote tumekubaliana kukutana hapo. Ila sisi tukiwahi kufika, nitawashusha hawa
hotelini kisha nitakufuata uwanja wa ndege.” “Ningependa wewe
unifuate Geb.” Liz aliongeza. “Sawa.
Nitajitahidi nisikuweke sana hapo. Uwe na safari njema utakapo anza safari.”
“Asante.” Liz akajibu, na kukakata simu. Pakazuka ukimya. Nanaa
akajirudisha ndani ya mtandio wake, akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~
Ndio
kwanzaaaa mambo yameanza. Je, historia mpya ya Marangu imeanza kuandikwa
njiani?
Geb
anaeleza furaha yake kwa Nanaa. Safari imeanza kwa utulivu, Nanaa akiwa nyuma
yake. Je, furaha hiyo itadumu? Atafanyaje na wanawake wawili kwenye hoteli moja
huko mjini Marangu?
Zinda
naye amegaramia sana hiyo safari kwa ajili ya Nanaa. Mipango mingi aliyoipanga
na James kaka yake Nanaa, pamoja na Danny kwa ajili ya Nanaa tu. Ameanza kwa
maua. Huku muonekano ukikubali kumuuza. Je atafanikiwa?
Baada
ya kuombwa na Danny, Nanaa ndio akapokea maua kutoka kwa Zinda, macho kwa Geb.
Wanaume wawili mbele yake. Zinda anayemuhangaikia na muwazi mpaka kwa kaka
yake, au Geb mpenzi wa Liz?
Liz naye
mwenye mpenzi, yupo angani kumfuata mpenzi wake huko mjini Marangu. Hachezi
mbali na Geb. Amekaba kila mahali. Japo hafurahii kuwepo huko, lakini ameamua
kwenda tu.
-
Je, nani ni wa nani?
-
Nani atammiliki nani huko waendako?
-
Nini kitatokea?
Usikose
Visa na mikasa ya mjini Marangu kwenye Sehemu ya 15.
0 Comments:
Post a Comment