Kila mtu alijua kuwa Geb anakwepwa. Na kila
alipofanikiwa kumkuta Nanaa mahali akiwa peke yake kama jikoni, Nanaa
alimuonyesha heshima kubwa. Kama anayeongea na baba mkwe wake. Salamu
aliziitikia kwa heshima sana. Mtoto huyo aliyelelewa uchagani aliweza kutoa
mpaka goti la Kinyakyusa kwa Geb. Heshima asilimia 100 alizitoa, endapo
atamsalimia. Hakutaka kumtizama, wala kuwa naye karibu. Akiingia huku, anatoka
na kwenda sehemu nyingie. Liz anapokuja hapo ndani, ndio ilikuwa kabisaa, Nanaa
hatoki chumbani kwake mpaka asikie anaaga.
Ila akaona upendo kwa mama G, unaongezeka kwake.
Alitaka kuwa naye karibu na kuzungumza naye wakati wote. Udhaifu wa Nanaa ni
kupenda stori. Akajikuta yeye na bibi Fili ndio wapo peke yao mle ndani hawana
wapenzi, ushoga ukaanza. Alianza kuzoeana na bibi Fili wakawa wakipata muda
mwingi wakucheka na kupeana stori za hapa na pale.
Alisaidia kazi za mle ndani, akawa msaada mkubwa
sana. Alifundishwa kupika chakula cha Geb, na chakula cha watu wengine. Kwa
hiyo alipokuwa akitoka kazini tu, alipitiliza jikoni kuandaa chakula. Na
asubuhi hivyo hivyo. Alikuwa wa kwanza kuamka kufanya usafi na kuandaa kifungua
kinywa. Akajitahidi kutoa mawazo yake kwenye kila kitu alichojua kitamtibua, na
kumnyima raha, ila kazi za mle ndani na ofisini tu.
Hakumtafuta tena Zena, wala hakujihangaisha tena
na Geb. Kazi za ofisini akaanza kuzimudu vizuri bila shida kubwa. Akawa msaada mkubwa
kwa Grace na huko ofisini pia. Na kwa kuwa hakuwa na safari yeyote, si kwa
James ambako alishapigwa marufuku, wala kwa rafiki. Nanaa akajikuta ana muda
mwingi tu wa kutosha kuwa mbunifu wa mambo mbali mbali hasa ya pale nyumbani
kufurahisha wenye nyumba wake. Akawafaa sana katika kila eneo.
~~~~~~~~~~~~~
“Bwana nyumba hii siku hizi tunakunywa
chai asubuhi kabla ya kwenda kazini! Tena sio chai na mkate. Tunapata chai ya
kueleweka kama tupo kwa mama lishe! Wakati wale wasichana wa kazi wapo hapa,
ilikuwa fujo tupu! Chakula hamna, sijui walikuwa wanafanya kazi gani humu
ndani!?” Danny alikuwa akiongea wakati anakunywa chai ili awahi
kazini.
“Basi sio utumalizie Danny! Maana nasikia sifa
zako zinasindikizwa na kutafuna.” Danny akacheka sana. “Mikate ipo
mama.” “Mmmh! Na sisi pia tunataka bajia. Wewe kuwa na kiasi bwana!” Danny
alizidi kucheka “Usiwe na wasi wasi mama yangu. Siwezi
kukumalizia.” Nanaa alikuwa akicheka peke yake chumbani.
~~~~~~~~~~~~~
Juma la kwanza likapita tokea Nanaa akatae Ice
cream aliyoletewa chumbani na Geb, na kuacha kuwa karibu naye kabisa. Pakawa
patulivu. Ijumaa Liz akaja kulala, akaondoka jumamosi usiku. Tena aliondokea
hukohuko walipokuwa wametoka na Geb. Walishinda hapo nyumbani siku nzima.
Ilipofika jioni wakamsikia Liz akimuaga Grace wanatoka na Geb kwa ajili ya
chakula cha usiku. Liz alikuwa amependeza sana. Alivaa suruali ya jinsi nyeupe
iliyokuwa imemshika juu mpaka chini, na top nzuri sana ya wazi juu ya rangi ya
kijani kibichi. Ilionekana ya thamani sio ya mtumbani anakonunua Nanaa nguo
zake. Kiatu cha juu kilichofanana na blauzi yake. Aliacha harufu ya pafyumu
nzuri, imeenea nyumba nzima.
~~~~~~~~~~~~~
Siku ya jumapili ambayo Liz anakuwa na familia
yake hafiki hapo nyumbani, Geb alikuwepo tu. Walikwenda kanisani ibada ya
asubuhi sana, Nanaa na yeye akaenda kanisani Mwenge. Kanisa la Mtakatifu
Joseph, kwenye misa ya saa 4:30 asubuhi. Mama G na familia yake waliondoka
asubuhi, wakamuacha Nanaa ndio na yeye anajiandaa. Walirudi mara baada ya ibada
kuisha mchana wakitegemea kumkuta Nanaa nyumbani lakini hawakumkuta hapo.
Wakaona wasimsumbue kwa kumpigia simu. Mama G akashauri aachwe tu asipigiwe
hata simu. Kwa kuwa anapokuwa hapo nyumbani anakuwa na kazi nyingi sana.
Akasema angalau hiyo jumapili aitumie kwa mambo yake binafsi.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo hali
ya Geb ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya. Mama yake akamuona anazunguka mle ndani
kama pia. Lakini akiwa ametulia. Anaingia chumbani kwake, anatoka. Anakaa sebuleni
kidogo, anatoka nje. Grace akamtizama mama yake. “Amekula?” Grace
akauliza kwa kunong’ona. Mama yake akaitikia kwa kutingisha kichwa. “Afadhali.” Grace
akajibu akisikika amepata aghueni.
Mpaka inafika saa 11 jioni, Nanaa hakuwa amerudi
nyumbani. Hakuna aliyemuulizia. Wote wakajikuta wapo hapo sebuleni wanaangalia
tv kimya kimya. Geb alikuwa ametulia kwenye kochi amejiegemeza. Hakuwa amezungumza
na mtu kitu chochote tokea watoke kanisani. Danny alitoka kwenda kuleta
chakula. Alinunua nyama ya mbuzi ya kuchoma, chips kidogo, ndizi za kuchoma
kiasi. Grace akaingia jikoni kutengeneza kachumbari. Tayari michale ya saa
ilikuwa ikigonga saa 12 kamili jioni hiyo wakati Nanaa anaingia.
“Shikamoo mama.” Nanaa akasalimia na kwenda
kukaa pembeni yake. “Marahaba mwanangu. Za huko?” “Nzuri. Nashukuru
nimepata wakati mzuri. Na nyinyi za kushinda?” “Nzuri tu. Tumekuwa hapa siku
nzima. Baada ya ibada tu, tukarudi nyumbani.” Bado alikuwa akiongea Nanaa
na Mama G. Geb na Danny macho walisharudisha kwenye tv baada ya kuhamishia
mlangoni wakati Nanaa anaingia.
“Ngoja nikaoge nipumzike, mama yangu. Nimekuwa na
siku ndefu kweli leo.” Nanaa aliendelea kuongea na mama G kwa sauti ya
chini kama asisumbue wanao angalia tv. “Haya mwanangu Nanaa. Grace
akimaliza kutengeneza kachumbari nitakuita uje ule kabla hujalala.”
“Nimeshakula mama. Asante. Kesho.” Nanaa akasimama. “Haya, usiku
mwema.” “Na wewe mama yangu.” Nanaa akaondoka. Siku hiyo nayo ikaisha bila
Nanaa na Geb kuzungumza lolote hata salamu japo walionana.
~~~~~~~~~~~~~
Siku ya 8 tokea Nanaa aweke mgomo wa Ice cream
ikawa jumatatu. Kila mtu anaenda kazini. Utaratibu wa Nanaa ukawa uleule. Kuamka
asubuhi na mapema, anapika ndipo anarudi kuoga. Kama amewahi kujitayarisha,
akimsikia Grace ameamka, anaenda kumgongea amchukue Fili amwandae yeye. Ili
Grace apate muda wa kujiandaa na kupata kifungua kinywa kabla hawajaenda
kazini.
Hiyo week ikaanza kuwa nzito. Kila kitu kikaanza
kuwa na kasoro kwa Geb. Matatizo yakaanza kwa wafanyakazi wake. Akigundua
unakosa kidogo, anataka wafukuzwe kazi wala sio kupewa onyo. Chakula kikawa
hakiliwi vizuri. Akiondoka na chupa ya uji asubuhi kama kawaida yake, atarudisha
bado imejaa uji vilevile. Inamaana siku hiyo nzima anakuwa hajala kitu.
Jumatatu na jumanne ikawa hivyo hivyo. Jumatatu alirudisha uji, lakini saa
mbili akawepo nyumbani, kwa hiyo mama yake akambembeleza akala chakula cha
usiku. Jumanne mpaka mama yake anaenda kulala, hakuwa amerudi nyumbani.
Ikawa kisirani mpaka kwenye biashara yake.
Ikabidi Grace amwambie mama yao. Siku ya jumatano akampigia simu mama yao, na
yeye akiwa kwenye biashara zake. “Hivi Geb anakula
vizuri?” “Kwani vipi?” Mama yake akauliza. “Zile hasira zake akiwa na njaa naona zimeanza, mama.”
“Anafanyaje?” “Anataka nimfukuze kazi huyu dereva. Anasema si mwaminifu. Wakati
huyu dereva amekuwa naye kwa muda mrefu, mama. Na wote tunamjua sio mwaminifu.
Kuna kipindi nikataka kumfukuza kazi, Geb mwenyewe akamtetea. Akatafuta njia ya
kumfanya asiibe. Ndio tunaitumia wakati wote. Yaani kwa kifupi hamna jipya.
Lakini hamtaki tena. Anasema nimfukuze kazi, wakati huyu dereva anatufaa sana.
Anafanya kazi hata siku za weekend. Ukimpigia simu apeleke mzigo mahali
popote pale, hawezi kukubishia. Anakwenda. Amekuja jana usiku amekuta mlinzi
mmoja ameenda kujisaidia, amekasirika. Anataka nibadilishe kampuni nzima ya
ulinzi.” Mama yake akamtuliza Grace. “Usiwe
na wasi wasi, nitazungumza naye.” Wakakata simu. Siku hiyo nayo
ikaisha.
~~~~~~~~~~~~~
Siku ya alhamisi wakati Grace na Nanaa wametoka
tu kazini wapo njiani, Geb akampigia simu dada yake, kumwambia ametoka kazini
kwake, BOT amepitia hapo ofisini kwa Grace. Yaani kwenye biashara yake. Anaona
kuna uzembe mkubwa sana kwa mtu wa stoo. Ndio maana wanapata hasara. Anataka
Grace amfukuze kazi kesho yake. “Nimekuwa na siku
ndefu sana Geb. Naomba tutazungumza vizuri jumamosi, tukiwa tunapitia kazi yake
pamoja.” Akamkatia simu dada yake bila kuaga. Grace akajua ni
hasira tu.
Grace na yeye akawa ameshakasirika na walikuwa
wamekaribia nyumbani. Waliposogelea tu geti la nyumbani kwao, mlinzi
akawafungulia geti kwa haraka, bila hata kuwachelewesha. Grace akaingiza gari
bila ya kusalimia walinzi pale getini kitu ambacho si kawaida yake. Akaenda
kuegesha gari. Nanaa akamuona ameshuka kwenye gari bila hata kuchukua vitu
vyake mle ndani ya gari. Mpaka funguo za gari aliacha zinaning’inia pale pale
baada ya kuzima gari. Akamuona anashuka kwa hasira.
“Mama! Mama!” Grace alisikika akiita kwa
hasira kidogo. “Nipo jikoni wewe mtoto. Kwani kuna nini?” Grace akaongoza
njia mpaka jikoni alipo mama yake. Mama yake akamuona anaingia kwa
hasira. “Nilikwambia uongee na Geb, naona hujazungumza naye.” “Kuna nini
tena?” “Ananiingilia kazi yangu mama, na si kawaida yake.”
“Nitazungumza naye bwana, tulia.” “Sasa kwa nini hujaongea naye mpaka sasa
hivi?” Mama G akacheka.
“Usicheke bwana mama!” “Kwani amefanya nini
tena?” “Anataka nimfukuze kazi mtu wa stoo.” Mama G akacheka kama
mazuri. “Bwana mama!” “Nilitaka kuongea naye leo. Nikamwambia aje pale
kazini kwangu tule naye chakula cha mchana. Kwa kuwa nimeona hata chupa ya uji
ameacha. Nikajua ameacha kula. Akasema leo yupo busy. Tupange wakati mwingine.”
“Hana ubusy wowote ule. Sasa hivi yuko kazini kwangu. Ametoka kuzungumza na
mimi sasa hivi.” “Basi ujue hapo ananikwepa. Anajua akija hapa nitamkera na
maswala ya chakula. Nikimuacha hivyo, hatarudi hapa mpaka usiku wa saa sita.
Ngoja nimpe lisaa limoja. Nitampigia, nimlazimishe arudi nyumbani, ale halafu
alale.” Grace akatoka akiwa na hasira zake vilevile. Nanaa akajisikilizia.
Akanyamaza. Akaingia chumbani kwake baada ya kula. Akalala. Wala asijue
kinachoendelea.
~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi wakati yupo jikoni, siku ya ijumaa
akiandaa kifungua kinywa, akashangaa Mama G, naye anaingia. “Mbona mapema
mama?” “Geb hayupo sawa. Hali chakula. Halali vizuri. Jana kachelewa kurudi, na
ameshaondoka bila hata kula!” Nanaa akanyamaza. Asijue aongee nini. Maana
alijua hata mama G, anajua kuwa amemnunia Geb. Hawaongeleshani. Mama G
akalalamika hapo jikoni bila kupata uungwaji mkono na Nanaa, mpaka Nanaa
akamaliza kazi zake, akamuacha hapo jikoni.
Hakuna aliyemsikia siku hiyo. Usiku wa saa mbili
wakamuona anaingia. Akasalimia vizuri akaingia chumbani kwake. Mama yake akampa
kama lisaa, akijua anaoga labda atatoka. Lakini kukawa kimya. Akaamua kumfuata
chumbani kwake. Akamkuta amelala. “Pole na
kazi?” Akamuanza. “Asante.” Mama G hakuwasha taa, akamsogelea
mpaka pale kitandani. “Nimekutengenezea mchemsho wa mboga mboga na
samaki.” “Leo nilikuwa na semina kazini. Karibia siku nzima. Wametupa chakula.
Kwa hiyo nimeshiba. Nataka kulala.” “Utakuja tulale
wote?” Kimya. “Geb?” “Unalala saa ngapi?” Akamuuliza mama
yake. “Muda sio mrefu.” “Basi nitakuja.” Mama G akatoka.
Ni kweli alikwenda kulala na mama yake. Lakini
alikwenda usiku karibia panapambazuka. Mama yake alimsikia akipanda kitandani,
akajua hakuwa amelala kwa muda wote alipokuwa kitandani. Akamuhurumia, asijue
amwambie nini muda huo na yeye alikuwa na usingizi.
~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi siku ya jumamosi, akatoka baada ya kunywa
uji. Akamwambia mama yake anakwenda Bagamoyo, atarudi jioni. Akaondoka. Kila
Mama G alipokuwa akimuona Nanaa, alijiongelesha juu ya Geb. Nanaa alijua ni
kama anataka kumfikishia ujumbe fulani lakini alishindwa asaidiaje. Mama huyo
alilalamika jinsi mwanae alivyo na wakati mgumu. Hali vizuri. Halali vizuri.
Lakini hataki kuzungumza naye. Akaendelea kuongea kwa kurudia rudia kama Mungu
angemfanyia muujiza wa kumtumia mtu akaweza kuzungumza na Geb, angeshukuru
sana. Nanaa alijua anatumwa yeye tu. Kwani mama G, anajua wazi hawazungumzi.
Lakini hakujua kama chanzo cha heka heka zote zile za Geb, ni yeye mwenyewe
Nanaa.
Jioni ilipofika Geb akaingia bila salamu,
akaanza. “Nataka kusitisha mkataba na hii kampuni ya ulinzi ya hapa
nyumbani. Wanachukua muda mrefu sana kufungua geti.” Grace na mama yake
wakaangaliana. Akapita kwenda chumbani kwake kwenda kuoga. Nanaa naye alikuwa
jikoni, akasikia. “Hivi mama umesikia lakini?” “Nimesikia. Sasa leo ndio
tutalala hapa bila walinzi. Akitoka huko ndani, wanafukuzwa leoleo wala si
kesho. Subirini muone.” Mama yao akajibu huku cheko limemjaa. Nanaa
akatoka jikoni akaenda kukaa pembeni ya mama G.
“Bwana mama! Acha kufanya utani! Ujue atawafukuza
kweli?” “Tupo wanaume wawili humu ndani. Tutapeana zamu ya kulinda. Acha Geb
awafukuze tu. Waache utani na bosi wao! Kwa nini wamuweke getini muda
mrefu?” Danny kama kawaida yake ya uchochezi. “Naomba nyamaza
Danny.” Mama G na Danny wakawa wanacheka. Nanaa alikuwa amekaa pembeni ya
mama G, akawa anasikiliza tu bila hata kuongeza neno. Geb alitoka chumbani
kwake akasogea pale sebuleni. Alipoonyesha dalili za kutaka kukaa tu, hapohapo
Nanaa akanyanyuka, akaenda zake chumbani kwake.
Mara Zinda akaingia akiwa na maneno mengii,
ikabidi Geb akae tu amsikilize. Stori zikaanza. Vicheko. Mara Liz naye
akaingia. Wakakaa kwenye makochi. Stori zikaendelea. Watu wakasahau hekaheka za
Geb. Kila akikutana Zinda, James, Danny, Malii, Gozi na marafiki zao wengine,
hutaacha kucheka. Sasa hapo alikuwa Zinda na Danny tu, lakini nyumba nzima
ilijaa vicheko. Mama G ndio alikuwa akisikika akicheka kila wakati.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alibaki pale chumbani akijisomea kitabu
chake cha hadithi ya mapenzi cha Endless Love. Alikuwa
amejilaza kwenye kochi la pale pale chumbani kwake. Kwenye simu yake aliweka
miziki iliyokuwa ikimtumbuiza taratibu huku akiendelea kusoma. Alifikia sehemu
nzuri sana ambapo msichana Mercy wa kwenye kitabu hicho ameondoka kwa siri
nyumbani kwa kina Ben, baada ya mchumba wa Ben kumdhalilisha vibaya sana wakiwa
mezani. Mara nyingi Nanaa alijifananisha na Mercy. Jinsi wanavyohangaika kwenye
mapenzi na wote ni kama walikuwa yatima
Uzuri wa Mercy uliosemwa kwenye stori hiyo
ya Endless Love, alijifananisha nao
sana. ‘Kasoro mimi sio mchanganyiko wa damu ya kizungu. Nywele ndio
sitaki hata kujifanisha naye. Zangu kipilipili kisichoweza kuchanika.’ Nanaa
alijisemea na kujicheka. ‘Lakini weupe upo bwana! Hata maumbile yetu!
Japo huyu Mercy mwenzangu anaonekana amezidi.’ Nanaa alijiangalia
kidogo akacheka. ‘Ila na mimi aahaa! Najikubali, hata kama wanaume
wananizingua. Lakini najijua umbile na sura Mungu hakufanya haraka. Alitoa
ujuzi wake japo kwa sehemu.’ Nanaa akajisifia wakati akijilinganisha
na Mrembo Mercy wa kwenye stori huku akicheka.
Wakati amezama kwenye kitabu akiendelea
kumfuatilia Mercy aliyekwisha fika Mlimani city, Nanaa akimuonea huruma Mercy
kuwa peke yake usiku ule. Tena kwenye jiji asilolifahamu. Uzuri ulio bayana
hata gizani! Nanaa alikuwa akiogopa asije akakamatwa na vibaka wakamtendea
ubaya. Hofu ilimjaa Nanaa pale kwenye kochi kana kwamba yupo kwenye tukio la
kweli. Aliendelea kusoma kitabu hicho cha ‘Endeless
Love’ huku akiomba Mungu kuwa Ben apite maeneo hayo ili akutane na
Mercy usiku huo, wazungumze wayamalize. Wapenzi hao warudi wote nyumbani, mambo
yaishe. Alishamchukia Bety. Akamlaumu. Akamfananisha na kina Viola. Aliendelea
kusoma, akili zikawa zimezama kitabuni. Akasahau alipo na matatizo yake yote.
~~~~~~~~~~~~~
Mara akasikia mlango
unafunguliwa. “Nimegonga naona kimya, nimeamua kuingia tu.” Alikuwa
mama G. “Samahani sikukusikia wakati unagonga. Karibu mama.” Nanaa
akashusha miguu kwenye kochi, kumpisha akakaa. “Una mgeni.” Nanaa akakunja
uso. “Mimi!?” Mama G akacheka. “Ndiyo Nanaa. Una
mgeni.” Hakuna aliyejua anaishi hapo. Nanaa hakuwa na marafiki wakufuatana
nyumbani. Na kama ni kaka yake, mama G angesema James anakuita sio mgeni. James
hakuwa mgeni kwenye hiyo nyumba na wala kwenye maisha yake. Mama G akabaki
amekaa kama anawaza.
“Ni nini mama?” “Bado hali ya Geb sio nzuri.
Tokea arudi hajala. Natamani kuzungumza naye lakini nimeshindwa kabisa.” “Kwa
kuwa Liz nimemsikia amekuja, labda atamuweka sawa. Usiwe na wasiwasi mama
yangu.” Nanaa akajaribu kumtuliza, akikwepa huo mpira. “Ngoja tuone
kama Liz atafanikiwa. Lakini Liz huwa hana mtindo wa kumlazimisha chakula.
Anasema kutokula sana ndio vizuri kwa afya yake. Wakati mwenzie sio kwamba yupo
kwenye diet, ni hapendi kula.” Nanaa akabaki kimya. “Lakini
labda leo atanisaidia na kumfanya ale.” Mama G, akatoka akamuacha Nanaa
anajiuliza. Alijua ndio amemtuma hivyo. “Lakini Geb anaye Liz
jamani! Kunihusisha na mimi kwenye maisha yake, sio sawa kwangu!” Nanaa
akajilalamisha, akanyanyuka na kutoka. Alifika hapo sebuleni akakuta ni Zinda
na Liz ndio wameongezeka.
~~~~~~~~~~~~~
Hapakuwa na mgeni. Si Zinda wala Liz waliokuwa
wageni nyumbani hapo. Zinda ni kama kaka yake James kwenye familia hiyo.
Aliingia hapo na kutoka bila taarifa. Alipokuwa akija na njaa, alipitiliza
kwenye friji bila kusubiri kukaribishwa. Wakati mwingine aliwasikia
wakimlalamikia bibi Fili wakiwa huko huko jikoni kwamba wao wananjaa na hakuna
chakula. Tena wakiwa wameshafika mpaka kwenye friji! Hapo ndipo bibi Fili
huenda jikoni na kuwatengenezea kitu cha kula kwa haraka, wanakaa naye wanakula
huku wakizungumza hili au lile.
Liz alijichukulia kama mama mwenye nyumba hiyo.
Mpenzi wa mwenye nyumba. Aliingia hapo na kutoka atakavyo. Tena alipokuja
wakati mwingine alisalimia tu na kupitiliza chumbani au wakati mwingine
alipowakuta sebuleni, hakutoa hata salamu. Alipitiliza chumbani kwa Geb, moja
kwa moja. Kama Geb alikuwepo, alisimama na kumfuata chumbani. Na kama alikuja
Geb akiwa hayupo, basi ujue Geb anakuwa na yeye anakaribia kurudi hapo
nyumbani. Basi watapishana dakika chache sana. Hata dakika 5 hazitaisha, Geb
naye atakuwa anaingia hapo ndani. Baada ya salamu tu bila hata kuambiwa kama
mpenzi wake yupo chumbani anamsubiri, Geb atapitiliza chumbani moja kwa moja
kuashiria waliwasiliana kabla ya Liz kufika hapo. Kwa hiyo mpaka hapo, Nanaa
hakuona mgeni aliyeitiwa.
~~~~~~~~~~~~~
“Habari zenu?” Nanaa
akasalimia. “Salama kabisa.” Zinda akajibu kwa haraka, Liz kama
kawaida yake huwa hujibu pale anapojisikia. Ni kawaida. Wote walishamzoea. Kwa
hiyo yeye hakuitikia salamu ya Nanaa. Alinyamaza tu. Kimya kikapita. “Huyo
mgeni wangu yuko wapi?” Nanaa akauliza huku akimwangalia mama G
aliyemwita. “Ni mimi, Nanaa.” Zinda akajibu kwa upole sana, akasimama.
Alikuwa amekaa karibu na Danny.
Nanaa akakunja uso. “Wewe ndio mgeni wangu
mimi!?” Nanaa akauliza huku anajionyeshea kidole. Watu wote walikuwa
wakiwaangalia. Nanaa alikuwa na haki ya kushangaa. Siku zote alizomuona Zinda
akifika hapo nyumbani, hakuwahi hata kumuona akitafuta hata kuwa na maongezi
naye zaidi ya salamu. Alifika akiwa na habari nyingi za mtaani. Bila salamu
alikuwa akiingia na stori huku akitaniana na kila mtu kasoro yeye. Leo iweje
awe mgeni wake yeye!?
“Ndiyo Nanaa. Nataka kuzungumza na
wewe.” Nanaa akaingiwa na wasiwasi kidogo. “Kaka James ni mzima?” “Mzima
kabisa. Ni mazungumzo yangu mimi mwenyewe binafsi.” Kidogo akavuta pumzi
kama kupata aghueni. “Sawa. Karibu.” Kimya. Nanaa akabaki akimtizama.
Bado walikuwa wamesimama palepale sebuleni watu wote wakiwepo kimya
wamekaa. “Wewe Zinda vipi bwana!? Mbona kimya? Nanaa
anakusikiliza.” Danny alimpiga ngumi ya mguuni. “Kumbe unanisikiliza?
Basi tutoke hapo nje tukakae kabisa.” Nanaa akakubali. Wakatoka nje.
Zinda kwa
Nanaa.
Kimya kidogo kikapita pale walipokuwa wamekaa nje
barazani. Palitenganishwa na vioo na nyavu kuzuia mbu na wadudu wengine kutoka
nje. Baraza lilifunikwa na nondo za urembo wa maua. Kuanzia kwenye dari mpaka
katikati kufikia nusu ya ukuta uliojengwa kwa muundo nadhifu sana. Ndani ya
nondo hizo kulikuwa na vioo pia, ambavyo vilizuia hewa ya AC isitoke nje.
Paliwekwa sakafu yenye marumaru za kuvutia. Kulipangwa makochi mazuri sana ya
rangi nyeusi na meza za vioo ndogo tu kama stuli. Baraza lenyewe lilikuwa na thamani
ya sebule ya mtu.
Nanaa akashangaa Zinda hazungumzi
kitu. “Umetumwa na kaka!?” Nanaa akavunja ukimya kwa kuuliza
swali. “Hapana.” Kimya. Zinda huyu wa leo siye Zinda aliyezoea
kumuona Nanaa. Kwa asili Zinda alikuwa mtundu sana. Kimya. “Kuna nini,
mbona unaniogopesha?” “Usiwe na wasiwasi kabisa. Ni mazungumzo tu.” Kimya.
Nanaa akakunja uso akaona na yeye anyamaze. Akajirudisha nyuma kwenye kochi,
akanyamaza.
“Umesikia Malii anaoa?” Nanaa akamgeukia
Zinda. “Ndiyo.” Nanaa akajibu. Zinda akaendelea. “Tena Fili
anasimamia harusi. Sendoff itakuwa Marangu. Anaoa msichana wa Marangu. Lakini
si unajua Malii na yeye ni mchaga? Wachaga wanapenda kuona wenyewe kwa wenyewe.
Sasa naona mwenzangu ameamua kuaga ukapela, ametuacha sisi, anaoa. Ni hatua
kubwa sana ya maisha. Na mkewe ana kazi. Na mdada mwenyewe sio mbaya, ila hana
rangi kama yako. Ila ni Mmarangu wa nguvu. Kwa hiyo sendoff itakuwa Marangu,
huko Kilimanjaro. Sijui umewahi kupasikia?” Nanaa alikuwa haelewi. Zinda
alianza kuongea kama mashine.
“Nimezaliwa Moshi mjini. Nikasoma miaka 2, katika
shule ya wasichana Ashira sekondari. Ipo Marangu.” Nanaa akajibu kwa
utulivu. “Kumbe wewe ni mwenyeji sana huko? Basi utakuwa mwenyeji wangu.”
“Wapi!?” Nanaa hakuwa ameelewa. “Huko Marangu. Tutaondoka hapa siku
mbili kabla ya sendoff. Tunamsindikiza Malii, kuchukua jiko. Wote tunakwenda.
Au hujasikia?” “Mama na Grace wameniambia, lakini mimi sitakwenda.” Nanaa
akajibu.
“Tungeenda tu ili tuwe pamoja. Umoja ni nguvu.
Nitakununulia gauni na viatu. Nitakununulia cheni na bangili. Lakini vitakuwa
vya dhahabu. Dhahabu itakupendeza sana. Halafu nitakununulia gari. Nyumba yangu
ile niliyokuwa najenga, inakaribia kukamilika. Sasa hivi..” Mara wakasikia
Danny anakohoa sana. Zinda akatulia kidogo.
Nanaa akabaki ametoa macho akimshangaa Zinda.
Alipotulia Danny, Zinda akaendelea. “Kwa hiyo kama nilivyokuwa
nikikwambia. Tukioana tutahamia kwenye nyumba yetu hiyo mpya. Nitaenda kuleta
wadogo zangu kutoka nyumbani. Kwetu ni Tabora. Usifikiri ni kijijini. Hata wao
ni watu tu wa mjini. Kwa hiyo wakija huku mjini, itabidi waanze kusoma hapahapa
mjini. Usiwe na wasiwasi, nyumba yenyewe ni kubwa sana. Najua utawapenda tu.
James anakusifia una roho nzuri na…” “Aibu gani hii jamani!?” Walimsikia
Danny akigomba kwa sauti. Gafla kila mtu akaanza kucheka.
“Wewe Zinda, hebu njoo kwanza.” Danny
alitoka pale barazani. “Hebu njoo. Njoo.” Danny alisisitiza huku akimuita
kwa ishara ya mkono. Zinda akasimama, akamfuata. Wakaingia ndani. Kila mtu
alikuwa akicheka. “Kamleteeni maji ya kunywa.” Nanaa alimsikia bibi
Fili akiongea huku anacheka sana. “Grace, nenda kamleteeni mwenzenu
maji.” Wote waliendelea kucheka. “Kaa hapa Zinda mwanangu. Kaa hapa
baba.” Alimsikia bibi Fili akipiga piga kiti huku anaendelea kucheka.
“Vipi? Kwani nimeharibu?” Zinda
aliuliza. “Kumbe wewe ujanja wote huo hujui kutongoza bwana!? Kelele
nyingi kumbe hujui kutongoza!” Danny alikuwa kwenye mshangao na hasira juu.
Lakini wengine walikuwa wakicheka sana. “Sasa wewe magauni na cheni za
dhahabu za nini Zinda ndugu yangu!?” Danny alimuuliza kwa mshangao mkubwa. “Nitamnunulia!” Zinda
alijitetea akiwa amepoa kama sio yeye. Walizidi kucheka.
“Daah! Ahadi hizo unamwambia mama yako Zinda! Sio
watoto wa mjini. Hayo mambo yamepitwa na wakati. Watu wanataka surprise.
Sasa wewe unaanza kutoa ahadi nyingiii! Tena nyingine zinaogopesha! Hujamuoa
unaanza kumpa na majukumu ya wadogo zako!? Mara unampa ahadi ya gauni, mara
gari, mara bangili. Bangili? Wewe vipi Zinda bwana!?” “Huyu mtoto
ananichanganya bwana!” “Wewe hujui kutongoza bwana. Acha kumsingizia Nanaa.
Hujui uanzie wapi wala uishie wapi. Unaanza kumsifia mchumba wa Malii kwa
Nanaa! Wapi na wapi?” “Si ndio nilikuwa naanza sasa ili nipate
pakutokea?” Zinda alijitetea nakufanya watu wazidi kucheka kasoro Danny
aliyekuwa anamuhoji kwa mshangao.
“Ushafika kwenye ndoa bila kumtongoza, sasa
kitakachofuata ni nini kama sio kifo?” Danny aliuliza nakufanya watu
wazidi kucheka. “Zindaaaa!!” Grace alikuwa akicheka mpaka
machozi. “Huyu hatakaa aoe. Unafikiri mama?” “Taratibu Zinda mwanangu.”
“Eti mama, eeh?” Zinda alitaka kutiwa moyo baada ya shutuma nyingi za
Danny. “Kabisa mwanangu. Lakini nahisi umemuogopesha Nanaa. Ungefanya kama
ulivyosema mwanzo au vile mlivyokuwa mmekubaliana na Danny, kabla ya Nanaa
hajaja. Kuwa leo unamuomba tu muende naye Marangu. Basi. Umetoa ahadi nyingi
mno Zinda mwanangu. Halafu..” Bibi Fili alishindwa kuendelea akaanza
kucheka upya. Zinda alikuwa mpole kama sio yeye.
“Yaani wewe unapitwa hata na Fili bwana! Yaani
huwa nikimsikia mwanangu Fili akiongea na Nanaa, mwenyewe naona nimezaa. Mtoto
anajua kupanga maneno. Hachanganyikiwi kama wewe! Kwanza akijinadi kwa Nanaa,
Nanaa mwenyewe anamkubali mwanangu. Pointi zake zinaeleweka. Wewe unachanganya
mambo kama nini sijui! Hujulikani kama ni mtabiri wa hali ya hewa, au mchimba
madini. Mara uwe kama pedeshee la mjini, mara mshamba wa kijijini kabisaa! Fujo
tupu. Hebu nenda kamwangalieni Nanaa. Weza kuta mtoto wa watu amezimia hapo
nje.” Zinda akatoka kwa haraka.
Akamkuta Nanaa ameinama. “Hajazimia bwana.
Ameinama tu.” “Kachoka! Umemchosha mtoto wa watu.” Watu walizidi kucheka.
“Na nitamwambia James.” “Acha hizo Danny. Ngoja mimi nikazungumze tena na
Nanaa.” “Hakuna. Toka kwetu. Nenda Zinda. Hatutaki tena. Toka.” Danny
akasimama, kila mtu alikuwa anacheka. “Nini bwana Danny! Sasa hivi
nishajua makosa yangu nitarekebisha.” “Hamna. Toka Zinda. Ushamchosha Nanaa kwa
maneno mengi.” “Sasa kwa nini unamjibia Nanaa? Mwache mwenyewe
aongee.” Zinda na Danny wakaendelea kubishana.
“Njoo Nanaa mwanangu.” Nanaa alisimama kwa
haraka aliposikia bibi Fili akimuita. Alishukuru Mungu. Kila mtu alianza
kucheka upya pale Nanaa alipoingia ndani. Zinda naye akarudi ndani kwani bado
alikuwa amesimama mlangoni pale alipoenda kumwangalia Nanaa akamkuta
ameinama.
Danny akamuwahi Nanaa. “Eti Nanaa, unataka
mkufu na bangili?” “Vya dhahabu bwana!” Zinda aliongezea kwenye swali la
Danny, nakufanya watu wazidi kucheka. “Yaani ndio unaharibu zaidi! Eti
Nanaa, unataka dhahabu wewe?” Danny akauliza tena. “Hapana.
Sitaki.” Nanaa alijibu huku akicheka kwa aibu. Alitamani aondoke
pale. “Unataka gauni?” “Na viatu Danny! Wewe vipi bwana? Atavaaje gauni
bila viatu?” “Sawa Zinda. Eti Nanaa?” Watu walikuwa wakicheka mpaka
machozi. Geb pia aliyekuwa amekasirika, ilibidi acheke tu. Liz ndio kabisa.
Mpaka alikuwa akinyanyua miguu juu kwa kucheka.
“Mimi sitaki kitu chochote. Sitaki hata gari na
nyumba. Na sipo tayari kuolewa sasa hivi, bado nasoma. Na sitakwenda
Marangu.” Nanaa alimaliza akaondoka kurudi chumbani kwake huku akicheka na
wengine wakicheka zaidi. “Haya, toka kwetu. Lione! Janaume zima linashindwa kutongoza
na mtoto mdogo! Nimekufundisha maneno yakuongea, unakuja kusema mambo ya ajabu,
tena yazamani! Nani kakwambia Nanaa anataka magauni kama sio kutiana tu aibu
hapa? Wote atatuona tupo hivyo hivyo kama wewe! Atajua kaka yake haoi mpaka leo
kwa kuwa hajui kutongoza kama wewe! Toka bwana. Ushatudhalilisha vyakutosha.
Toka Zinda.” “Daah! Naona kweli niondoke tu.” “Mwache anywe hata maji, Danny.
Mwanangu Zinda amekuwa na wakati mgumu sana.” “Mwache aende mama. Akanywe maji
huko mbele ya safari, sio hapa. Kaniudhi sana. Nimekohoa mara ngapi hapa ili
kumshitua, lakini hasikii. Wewe habari za Fili mwanangu kusimamia harusi
zinahusikaje na kutongoza kwako? Eti mkewe anakazi! Aibu tupu hii. Hebu nenda
kwenu bwana. Toka.” Zinda akatoka akawaacha wanacheka sana.
Kila walipokuwa wakikumbuka waliendelea kucheka.
Hakuna aliyeweza kuangalia Filamu tena. Walikumbushana habari za Zinda na
Nanaa, nakuzidi kucheka. “Naona Nanaa hatakaa akasahau.” Grace
aliongeza huku akicheka. “Maneno mengi vile, kumbe hajui kutongoza!?
Atanikoma Zinda. Amezoea sana kunichokoza. Nishajua pakumpatia.” Grace
aliendelea kucheka. “Halafu mimi nimemfundisha kweli hapa.” Danny alimkata
mkewe. “Basi uulizaji ule wa maswali, nikajua kaelewa. Maana alimtuma mama
kwa ujasiri wote. Eti ‘nenda kaniitie mkweo, nimpange.’ Kumbe
hana lolote!” Liz aliongeza huku akicheka.
“Tena alikuwa akimuuliza mwenzie Danny maswali ya
msingi kweli! Danny naye akarudiarudia kumwambia hilo ongea mwanzo, na hili
mwisho.” “Tena akanijibu ameelewa, bwana! Akaenda kututia aibu!” Danny
alimkatiza bibi Fili. “Ila mimi niliona dalili tokea Nanaa anauliza hapa
mgeni wake yuko wapi. Kama mlimwangalia Zinda, alianza kubabaika tokea mwanzo.
Akawa kama amepata ganzi mpaka Danny alipompiga ngumi.” Grace alichangia
nakufanya waendelee kucheka.
Liz akanyanyuka huku anacheka. “Ngoja
niondoke zangu. Lakini njiani lazima nimpigie Zinda nicheke zaidi.” “Sasa hivi
atakuwa baa. Kwa aibu hii, lazima akanywe ndio aweze kulala.” Danny
alijibu na kuwafanya wazidi kucheka. Liz akatoka, wakasikia gari imewasha,
akafunguliwa geti akaondoka bila hata kuulizia swala la chakula kwa Geb wala
hata kujua alishindaje. Wakashangaa hata hakulala siku hiyo.
Geb na yeye akanyanyuka. “Chakula
baba!” Mama G akamuuliza mwanae kwa upendo. “Nitakula kesho. Sasa
hivi nimechoka naenda kulala.” Geb akajibu huku anaelekea chumbani kwake.
Bibi Fili akawaza kidogo, na yeye akasimama kuelekea chumbani kwa
Nanaa. “Na mimi naenda kulala. Lakini lazima nipitie chumbani kwa Nanaa
mwanangu niangalie hali yake.” Bibi Fili akaondoka. Akabaki Grace akicheka
na mumewe.
~~~~~~~~~~~~~
Akagonga chumbani kwa
Nanaa. “Karibu.” Nanaa aliitika. Mama G akaingia. “Nimekuja
kukuangalia wewe unayekataa bahati ya dhahabu na gari.” Nanaa akacheka
sana. “Mama wewe! Balaa gani hilo!?” “Tumepata kituko cha
mwaka.” Wakacheka kidogo, mama G akaenda moja kwa moja kwa kile
kilichompeleka huko chumbani kwa Nanaa.
“Geb ameenda kulala bila
kula!” Akajilalamisha. “Na sijui ataendelea hivyo mpaka lini? Zinda
ametoa vichekesho pale, naona akajisahau kwa muda. Zinda ameondoka na yeye
akanyanyuka kwenda kulala, na huzuni zake. Nikumuombea tu.” Nanaa
akanyamaza. “Usiku mwema Nanaa mwanangu.” “Asante na wewe mama.” Mama
G akataka kutoka. “Mama!” Nanaa akamuhurumia. “Unajua sina namba
ya simu ya Geb?” “Ni rahisi sana. Unaweza kuishika hata kwa kichwa
tu.” Nanaa akaona mama G amechangamka gafla. Akamtajia ile namba, akatoka
akiwa anacheka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alibaki akifikiria chakufanya. Akaamua
kumtumia ujumbe. ‘Hey! Ni mimi Nanaa.’ Baada
ya muda mfupi sana, akaona Geb amerudisha ujumbe. ‘Mimi
bado ninayo namba yako Nanaa.’ Nanaa akamuhurumia. ‘Pole na kazi.’ ‘Asante.’ Kimya. Nanaa akafikiria
amwambie nini tena. ‘Umeshalala?’ Nanaa
akauliza. ‘Bado.
Na wewe ndio unalala?’ Geb akauliza. ‘Bado
nipo nipo. Nasoma kitabu cha hadithi.’ ‘Kinahusu nini?” Geb
akauliza. ‘Mikasa ya mapenzi. Bado sijamaliza.
Ndio nipo katikati. Unaweza kuja kukiona.’ Hata dakika haikuisha
Geb akawa ameshawasili mlangoni kwa Nanaa.
“Karibu.” Geb akaenda kukaa pembeni
yake. “Kina jina gani?” “Kinaitwa Endless
Love.” Geb akakichukua. “Ni kizuri sana.” Nanaa
akasifia. “Kumbe ndio maana unajifungia mwenyewe huku chumbani
ukifaidi!” Nanaa akacheka kidogo. “Unakipendea
nini?” “Namfananisha huyo msichana na mimi. Maisha yetu naona kama
yanafanana!” “Kivipi?” Geb alidadisi tena huku akijaribu kuperuzi kurasa
za kile kitabu. Alimuona vile alivyochoka usoni.
“Eti Nanaa?” “Naona mapito yake yanafanana na
mimi katika kila eneo la maisha. Lakini naona yeye mwenzangu Mungu alimpa Ben,
mimi Mungu amenipa kaka James.” “Na yeye Ben ni kaka yake?” Geb aliendelea
kudadisi taratibu huku macho yakiwa kitabuni. “Hapana. Ni kijana tu
waliyekutana kwenye hangaika za Mercy. Lakini Ben anaonekana kumpenda sana
Mercy. Mpaka hapo nilipofika, bado hajamwambia chochote juu ya mapenzi. Japo
anampenda na kumuhangaikia sana. Mercy naye hana wazazi kama mimi, anahangaika
pakuishi kama hivi mimi ninavyohangaika pakuishi.” Geb akamtizama. Nanaa
akainama.
“Wewe upo hapa na sisi.” “Hata yeye alikuwa
akipata sehemu anahifadhiwa kwa muda kama mimi. Namaanisha sehemu ya kudumu na
ndugu wanao kuhitaji.” Geb akamtizama tena nakurudisha macho kwenye
kitabu. “Namaanisha nyumbani.” Nanaa akajaribu kutetea hoja yake
zaidi. “Unaweza kupafanya hapa ni nyumbani Nanaa.” Nanaa akacheka
kidogo akainama kama anayefikiria.
Akafikiria maneno ya mama yake mkubwa,
akaguna. “Nyumbani ni pale moyo wako ulipo, Nanaa. Ukiamua kuwa na sisi,
utapafurahia tu hapa na kupafanya ni nyumbani kwenu.” Nanaa akanyamaza.
Ukapita ukimya wa muda. Geb akiwa ameshika tu kitabu, hakuwa akisoma
tena.
“Geb!” Nanaa akamuita kwa upole,
akamgeukia. “Upo sawa?” Akamuuliza kwa upendo huku
akimwangalia. “Sijui Nanaa!” “Pole. Naamini Mungu atakusaidia. Kila kitu
kitakuwa sawa. Usiwe na wasiwasi.” Nanaa aliongea kwa upendo,
akimfariji. “Nakushukuru. Na samahani.” Nanaa alielewa msamaha ule ni
wa nini. Machozi yakaanza kujaa machoni. “Ni
sawa tu.” Nanaa akajibu kwa upole akitaka kumtoa hukumu moyoni. Geb
akabaki akimtizama, Nanaa akainama. Wakabaki kimya kwa muda.
Akajifuta machozi. “Vidonda vya mikononi
vilipona?” Akauliza. Geb akajiangalia viganja
vyake. “Tuone.” Nanaa akamsogelea karibu zaidi. Akamshika mkono wa
kushoto uliokuwa upande wake. Akakiweka kiganja chake, mkoni mwake akawa
amemshikilia. “Mkono huu unaonekana kidonda kimekauka. Tuone mkono
mwingine.” Geb akampa. “Huu bado kidogo. Pole.” Alimpa pole huku
akiangalia vile vidonda mkononi. “Asante.” Geb akashukuru kwa sauti
iliyosikika kutulia.
Nanaa akawa anapitisha kidole chake kimoja juu ya
vile vidonda kama anachora pembeni yake kuzunguka mduara mzima wa kile kidonda.
Taratibu sana huku akikipuliza. “Kinauma?” Akauliza kwa upendo kama
kwa mtoto. “Kikiingia sabuni au kitu cha chumvi chumvi ndio kinauma
zaidi.” Geb akajibu huku na yeye akiangalia vile Nanaa
alivyomshika. “Pole. Utapona tu.” Nanaa akaendelea taratibu. Hata na
yeye alishakuwa na hamu na Geb. Alifurahia kuwa naye pale.
“Naomba nikuletee chakula ule.” Nanaa
akamwangalia tena, macho yakagongana. Mwili mzima wa Nanaa ulisisimkwa pale yale
macho yalipotua kwenye macho yake. “Wewe ulishakula?” Geb
akauliza. “Tulikula na mama.” “Nitashukuru. Nimekuwa na kazi nyingi sana.
Naona nikila, ndio nitaweza kulala vizuri.” Nanaa akafurahia
moyoni. “Pole. Na kweli unaonekana umechoka.” “Asante.” Geb
akajibu akiwa ametulia na mnyenyekevu kama sio yeye aliyekuwa akimsumbua Grace
karibia juma zima. “Basi nisubiri nikakupashie moto chakula. Nitakuletea
hapahapa, pumzika tu.” “Asante.” Nanaa akatoka.
~~~~~~~~~~~~~
Bado Danny na mkewe walikuwa hapo sebuleni. Kwa
kutokumuuliza kitu, Nanaa akajua wanajua Geb yupo chumbani kwake. Akapasha
chakula moto kwa haraka, kwa kutumia microwave. Akaweka kwenye trei. Wakati
anataka kuweka na maji, mama yake akaja jikoni haraka. “Naomba muwekee na
juisi.” Nanaa akacheka na kutingisha kichwa. “Unanicheka Nanaa? Sawa.
Utazaa na wewe. Utaona tu.” “Kwani mimi nimesemaje mama?” Mama G
alionyesha wazi amefurahi. Akachangamka kuongeza kwenye hilo sinia bakuli dogo
la matunda. Kwa hiyo kukawa na mchemcho wa kuku na viazi, bakuli la matunda,
glasi ya maji na juisi. “Asante Nanaa mwanangu.” Nanaa akacheka na
kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
Alimkuta Geb amejiegemeza kwenye
kochi. “Unasinzia?” Nanaa akamuuliza. “Nahisi kuchoka. Sijapata muda
mzuri wakupumzika. Nimekuwa na mambo mengi.” “Basi kula haraka,
ukalale.” Geb mwenyewe alishavuta stuli karibu yake. Nanaa akaweka ile
sinia. Akaanza kunywa juisi, akaja matunda, ndipo akala chakula huku Nanaa
akimwangalia kwa kujiiba. Alionekana kweli ananjaa. Alikuwa akila kwa bidii
zote utafikiri sio yeye aliyekuwa akimkatalia mama yake chakula.
“Tunaondoka alhamisi kwenda Marangu kama
alivyokwambia Zinda. Wote tutaondoka. Kwa nini umekataa kuwa na sisi?” Geb
akavunja ukimya wakati anamalizia chakula chake. Nanaa akanyamaza. “Mama
ameniambia umekataa kwenda. Kwa nini?” Geb akarudia swali. “Nakumbuka
nilikwambia Moshi na Arusha sio sehemu natamani kurudi Geb. Nakuwa ni kama
najitonesha vidonda. Kumebeba historia ngumu sana ya maisha yangu.” “Pole
Nanaa. Japo sifahamu ni kwa nini, lakini hudhani labda ni wakati wa kuandika
historia mpya?” “Sidhani Geb. Kwa sasa sina historia mpya na nzuri ya kuandika
kwenye ule mji.” “Utakuwa na sisi. Na tunakwenda kwenye sherehe. Hiyo pekee iwe
sababu. Tutalala hotelini. Sio nyumbani kwa mtu. Tutakuwa na muda mtulivu
wa kupumzika. Mbali na kazi na kelele za huu mji. Hufikirii chochote mbali na
wewe tu. Nashauri twende wote. Utafurahia tu.” Kwa sauti ile ya utulivu.
Na macho mazuri na laini ya Geb, hata kama ulitaka kusema hapana, mdomo
utatamka ndiyo. Nanaa akanyamaza.
Akamaliza kula. Nanaa akatoa vyombo nje.
Akavirudisha jikoni. Alibakisha maji ya kunywa akasema atayanywa baadaye. Nanaa
alirudi kukaa palepale, pembeni yake. “Twende wote bwana! Naamini tutakuwa
na wakati mzuri sana.” Moyo wa Nanaa ulishalainika tokea zamani, ni vile
tu alizuia jibu lake. “Eti Nanaa? Au basi niseme nakuomba twende
pamoja.” Geb alikuwa akimtizama. “Tutakuwa na wakati mzuri.” Geb
aliendelea kubembeleza. “Naomba usikatae kwanza. Angalau niambie utafikiria.
Bado una siku kama tatu zakufikia maamuzi. Usinikatalie tafadhali.” Nanaa
akacheka kidogo. “Okay.” Geb akaweka kidole chake tena kwenye dimpo
ya shavu la Nanaa, lile lililokuwa karibu yake kama akichezea kidogo
tu. “Okay, unafikiria au umenikubalia?” “Nitakwenda na nyinyi.”
“Asante.” Geb alitabasamu akabaki akimwangalia.
“Nakuona umechoka Geb. Nenda kapumzike.” “Kweli
nimechoka.” “Usiku mwema.” Sio kwa sauti ile kwa Geb. Nanaa aliongea naye
vizuri, tayari akili zake zikawa zimeshatulia. Hasira zikaisha. Akajua kila
kitu kinawezekana hapa duniani. “Asante na wewe, Nanaa.” Geb
akasimama. “Unisalimie Mercy na Ben.” Nanaa akacheka. Akavuta kitabu
chake cha Endless love, akarudisha macho
kwenye kitabu huku amejawa furaha moyoni.
Alifurahia uwepo wa Geb. Hata yeye alikuwa na
hamu naye. Japokuwa hawakuwa wanapata muda mwingi wa pamoja, lakini alifurahia
kila anapozungumza naye na kila anapomtizama yeye. Alicheka na kujishika shavu
ambalo Geb aliweka kidole chake. Hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo. ‘Anaonekana
anapenda kuchezea dimpozi zangu!’ Nanaa alijiambia akiwa bado ameshika
shavu lake. Akasimama na kuhamia kitandani. Akabaki akimuwaza Geb huku
anatabasamu. ‘Liz amebahatika!’ Kidogo wivu ukamuingia.
Akawaza kidogo, akapitiwa na usingizi.
~~~~~~~~~~~~~
-
Ni Liz na Nanaa pekee ndio hawajua tatizo la Geb ni nini. Hasira,
kujizira na kuamua kujiadhibu kwa kiasi kile. Mama yake ameshajua tulizo pekee
analohitaji na kumuweka sawa mwanae latoka kwa Nanaa. Aamua kumuweka Karibu
yake yeye ili asimpoteze katikati ya uwepo wa Liz kwa Geb. Mpaka lini? Je Nanaa
ataendelea kuumizwa hivyo mpaka lini?
-
Safari ya Marangu kule alikokataa kurudi Nanaa, sababu historia
mbaya ni baada ya siku tatu. Geb anaomba safari hii yeye awepo, pengine
wataandika historia mpya. Watafanikiwa? Na Liz naye? Zinda je?
Usikose
Muendelezo wa hadithi hii ya kila mtu anayetaka
kumiliki wake…
0 Comments:
Post a Comment