Maisha
yakaanza ndani ya nyumba hiyo. Kulikuwa na amani na utulivu wa aina yake. Kama
Danny asipokuwepo nyumbani, basi ni Fili ndio alikuwa akichangamsha nyumba,
lakini wengine wote walikuwa wakimya. Akaanza kujiwinda na Geb. Hakutaka kuwa
karibu naye kabisa ili asijiumize nafsi yake. Geb alikuwa akiibua hisia ambazo
zilimfanya kumtaka zaidi. Nanaa akaona hatendei haki hisia hizo mpya na ngeni.
Kwani Geb alikuwa ni wa Liz. Na Liz mwenyewe alikuwa akikaba kweli kweli.
Siku hiyo ya jumatatu jioni waliporudi nyumbani
baada ya kazi. Nanaa akiwa anatayarisha chakula cha usiku jikoni, Bibi Fili
naye anaoga baada yakutoka kwenye shuguli zake, wakamsikia Liz na yeye
ameingia. “Naona umetoka dry clener!” Alimsikia Grace
akimuongelesha. “Hapana. Nilipitia nyumbani kuchukua baadhi ya nguo zangu
za kuvaa kazini week hii nzima. Nikilalaga hapa, halafu kuamka kwenda kuvaa
nyumbani, nachelewa kazini. Nimeona heri niwe natokea hapahapa kwenda kazini.
Halafu weekend hii Geb amesema hatasafiri. Tutakuwepo wote nyumbani.” Moyo
wa Nanaa ulipasuka. “Liz anahamia hapa!!!” Akajiuliza. “Lakini
ni kwake. Sasa si nilisikia hapendi watu wajazane hapa ndani?” Nanaa
akajiuliza. Gafla amani ikatoweka moyoni mwake, asijue chakufanya. Pakwenda
hana, analazimika kuwepo pale kwa wakati ule. Akabaki akiwaza pale jikoni yeye
mwenyewe.
Akatayarisha chakula. Akala huko huko jikoni.
Kingine akakipanga vizuri mezani. “Chakula tayari.” Akamsogelea Grace
akamwambia kwa sauti ya chini. “Una mkono mwepesi! Hapa ndio nilikuwa
najipanga kuja kukusaidia.” Nanaa akacheka. “Usicheke Nanaa! Nilikuwa
nakuja.” “Wala usijali. Ilikuwa ni kuunga tu njegere. Nyama zile tulizokaanga
jana bado zilikuwa nyingi. Nimepasha tu. Na nimeona chapati alizoleta Danny
bado za moto. Kwa hiyo wala sijachukua muda mrefu.” “Pia nashukuru. Nimejikalia
kizembe, utafikiri nimetoka shamba!” Nanaa akacheka. “Basi usiku
mwema. Kuna kitu nataka kufanya huko chumbani kabla sijalala.” “Haya mwaya.
Usiku mwema.” “Na nyinyi pia.” Nanaa akaenda kumuaga Mama G, akaingia
chumbani kwake.
Jumanne nayo alifanya hivyo hivyo kuingia
chumbani kabla hata Geb hajatoka kazini. Na jumatano nayo akafanya hivyo hivyo.
~~~~~~~~~~~~~
Alhamisi usiku Zena akamtafuta kumwambia akaribie
kwenye birthday party ya Yasini. “Ni wapi tena
Zena!? Mwenzio nimeamua kutulia.” “Mbona nimeelewa. Hata Jeff ametusimulia kila
kitu, wote tumeelewa. Nataka tu uje uniunge mkono. Sitaki nijikute peke yangu
nikiwa nimezungukwa na marafiki wa Yasini tu.” “Kwa hiyo mtafanyia wapi hiyo
sherehe?” Nanaa akahoji akionyesha wazi hataki kwenda. “Tutaelekea Kigamboni. Tutaondoka saa nne, na kurudi jioni.
Nakuomba usinitupe Nanaa.” Baada ya kubembelezwa sana na kupewa
mipango yote, Nanaa akakubali. Hata hivyo alijua itamsaidia kuwa mbali na ile
hali pale.
~~~~~~~~~~~~~
Ijumaa kabla hajaingia kulala, akamfuata Mama G,
chumbani kwake. “Niambie mwanangu Nanaa.” Nanaa akatabasamu,
akasogea. “Unakumbuka habari za yule rafiki yangu Zena?” Nanaa
akauliza. “Yule ambaye mchumba wake ni Yasini, rafiki wa Jeff?” Nanaa
akacheka kwa sauti. “Mama! Husahau?” “Nasahauje wakwe? Haya, kuna nini
tena?” Nanaa akavuta pumzi. “Kesho ni birthday ya Yasini. Wanaenda
kufanyia Kigamboni. Wamenialika. Wamekubaliana kukutana pale kivukoni saa 3:30
asubuhi, ili saa 4 waanze kuelekea huko. Kwa hiyo nilitaka kukutaarifu hivyo.” Mama
G, akajua Nanaa akiondoka hiyo kesho hapo, kazi itakuwepo!
“Sawa. Utataka kusindikizwa, au watakuja
kukufuata hapa?” “Nimemwambia Zena asisumbuke. Nitakutana nao kivukoni. Kwa
hiyo naweza kutoka mapema kabla hamjaamka. Ila nitahakikisha nimeacha kila kitu
tayari.” “Wewe nenda kapumzike na wenzako. Mambo mengine tutafanya tukiamka.”
“Haya mama yangu. Usiku mwema.” “Mbona mapema?” “Nimeanza kuandika ripoti. Ndio
inanichukulia muda mwingi huko chumbani.” “Haya mama. Usiku mwema. Na uwe na
wakati mzuri na wenzako kesho.” “Asante mama yangu.” Nanaa akaelekea
chumbani kwake.
Jumamosi Ya
Heka Heka Baada Ya Nanaa Kutoka.
K |
esho
yake asubuhi Nanaa akaamka mapema. Akaandaa kifungua kinywa cha kila mtu.
Akapika mpaka uji wa Geb, ndipo akarudi chumbani kwake. Akaoga vizuri na kuanza
kujitengeneza. Kama kawaida yake ya kupenda kuvaa vigauni. Akavaa gauni zuri.
Refu mpaka chini. Lilimkaa Nanaa vizuri mpaka mwenyewe alijua, akabaki
akicheka. Alilichagua hilo makusudi kwakuwa lilikuwa kata mikono juu.
Ilishikiliwa na kamba nzito zilizokuwa zimepita juu ya shingo. Sehemu kubwa ya
mgongo ilikuwa wazi. Kwahiyo rasta zake akazibana kiasi zile za mbele, za nyuma
akaziachia kufunika ule uwazi wa mgongoni. Akafurahia na rangi ya hilo gauni
sababu ya jua kali. Akajua litamfaa na joto la jiji hilo.
Hereni zake za bati tu. Kubwa na duara
zilizokuwa zimechomvya kwenye maji ya dhahabu, nakuzifanya uhisi ni dhababu
tupu kama ukiangalia kwa haraka, zilimkaa vizuri sana. Alichukua kofia maalumu
ya beach, akaining’iniza kwenye kimkoba chake kama cha mkeka. Miwani ya jua
akaining’iniza mbele ya gauni yake kwenye ile ‘V’ iliyotengenezwa
kutokana na ile mikanda iliyopita shingoni. Akavaa zile zile sendozi zake
zilizokuwa na shanga nyingi nyeupe. Akajua zitaendana na gauni hilo lililokuwa
na rangi nzuri iliyokolea bluu kama maji ya bahari.
Usiku kucha alikuwa akipaka rangi kucha
zake. Mara afute, apake tena, mpaka akaridhika. Kwa hiyo kucha za miguu zikawa
zinavutia kwenye zile sendozi zake. “Hapa ningekuwa na gari!” Nanaa
akawaza. “Nitajichafua tu, kwa kutembea hapa mpaka kituoni.” Nanaa
alijiongelesha. Akataka kusahau rangi ya midomo anayopenda kupaka. Nyekundu.
Akaweka huku akifurahia jinsi alivyozidi kuwaka.
~~~~~~~~~~~~~
Alipojikubali kuwa amependeza na hana
chakuongeza mwilini mwake, akaamua kutoka. Wakati anatoka chumbani akakumbana
na Danny koridoni. “We Nanaa? Unaenda wapi asubuhi yote hii wakati bosi
wako kalala ndani!?” Nanaa akacheka kidogo. “Naelekea Kigamboni
kwenye birthday.” “Mmmh! Birthday ya asubuhi hiii!?” “Tutashinda huko siku
nzima. Hata hivyo tunatakiwa kuondoka pale kivukoni saa 4 asubuhi. Lakini
sababu ya daladala, imenibidi kuwahi kidogo.” “Khaaa! Naona kweli umekamia
hiyo birthday! Sio kwa kupendeza hivyo bwana!” Nanaa akataka kuondoka huku
anacheka.
“Nanaa!” Nanaa akageuka. “Nisubiri
nikusogeze. Mimi mwenyewe naenda kazini leo.” “Asante. Utakuwa umenisaidia.”
“Basi nifungie vitafunio vyangu. Harufu nzuri imeenea mpaka chumbani!”
“Nimepika sambusa.” “Acha masihara Nanaa! Sambusa!?” Nanaa akacheka. “Mimi
naona nile tu hapahapa. Nikienda nazo, James atanimalizia.” “Nimepika nyingi.
Naomba mbebee na yeye.” “Kama ndio hivyo sawa. Tena tenganisha kabisa, na weka
majina yetu juu. Ili akimaliza zake, akatulie ofisini kwake.” Nanaa
akacheka na kuingia jikoni.
“Umeamsha nyumba zima Danny. Kwani huwezi kuongea
sauti ya chini?” “Wewe umeamshwa na Sambusa bwana! Acha kunisingizia Grace.” Mkewe
akacheka na kuelekea jikoni. “Kwa mwendo huu tutanenepa humu ndani mpaka
tupasuke.” Grace akabaki akimtizama Nanaa. “Mbona unanishangaa?
Nimetisha? Niambie ukweli.” “Sidhani kama utarudi leo. Ndio umependeza hivyo!” Nanaa
akacheka sana. “Ukichelewa tu, sisi tunakufuata.” “Nitajitahidi
nisichelewe sana.” “Wala usijali. Wewe nenda kafurahie na wenzako.” Akajua
tayari bibi Fili amemwambia.
Huko Kwa Nanaa!
D |
anny
alimpeleka mpaka Kigamboni. Akamshusha. Alikuwa amewahi kidogo. Mara akaja
Yasini na Zena. Wakasalimiana. Baada ya muda akaja Jeff na msichana mwingine.
Nanaa akabaki amepigwa butwaa. Wakawasogelea wakasalimiana. Jeff akamtambulisha
yule msichana kama ‘girlfriend’ wake. Wakasalimiana na Nanaa. Wakaja
tena marafi zao wengine wawili. Baada ya muda, wakajikuta wameshakuwa kundi
kubwa. Nanaa akapanda kwenye gari la Yasini na Zena. Jeff na msichana wake
wakaingia kwenye gari yao. Na wengine hivyo hivyo, wakavuka.
Kwa
haraka sana, Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini. Alijuta hata kufika pale.
Na walipofika kule, ni kama Jeff alikuwa akimfanyia makusudi. Mabusu ya hapa na
pale kwa huyo msichana hayakuisha. Alimlisha mbele za watu! Alitaka kukaa naye
kiti kimoja huku amemkumbatia. Kila mtu aliona vituko vya Jeff na msichana huyo
mpya. Ni kama alimfanyia makusudi Nanaa.
Huku kwa
Geb!
M |
aongezi,
sifa na shamra shamra za Danny kwa Nanaa, ni kweli ziliamsha kila mtu pale
ndani. Geb alibaki amelala pale kitandani kama amemwagiwa maji. Akili
ilishavurugika. Alilala pale kwa muda, kisha akaamua kutoka nje kabisa. Akaanza
usafi wa nje ya nyumba yake. Ilifika saa nne asubuhi watu wote wakawa wameamka
wanakunywa chai, lakini Geb alikuwa anazunguka nje. “Nenda kamuite aje kunywa
uji.”“Mie mama? Akuu! Wewe unamjulia mwanao. Nenda mwenyewe.” Grace
akajitoa mapema. Walikuwa wakinong’ona kwa kuwa Liz alikuwepo.
Akatoka mama G. Akamkuta jasho linamtoka kama
maji! Anasafisha sehemu ambazo ni safi. Akasimama pale akimwangalia. Akamuona
anaenda stoo, akatoka na jembe mkononi. “Una chimba shimo?” Mama yake
akatupia neno kuchokoza. “Nataka kupanda miti.” “Wazo zuri ili tupate
vivuli.” Akaanza kuchimba mashimo kama makaburi.
“Kwani miti hiyo unayotaka kupanda hapo, ni
mirefu ya kiasi gani?” Kimya. “Naona kama mashimo hayo ni marefu sana
Geb, mwanangu.” “Sitaki mizizi ije kuungua na jua.” “Wazo zuri.” Akatulia.
Akaona anaendelea kuchimba. “Nikuletee uji wako hapa nje?” “Mpaka nimalize.”
“Nashauri ule kwanza. Hayo mashimo ni marefu sana.” Kimya. “Kwani
unapanda miti mingapi?” Kimya. Geb akaendelea kuchimba. Jasho lilikuwa
likimwagika kama maji. “Hivi ulisema ni miti gani tena?” Kimya. “Utapanda
mbegu au miti ile mikubwa kama mibuyu? Maana hayo mashimo!” “Mama!” Geb
akagomba. “Basi baba nanyamaza.” Akatulia kidogo. “Ngoja nikakuletee
uji unywe ili upate nguvu.” “Sitakula sasa hivi. Natoka kwenda kufuata hiyo
miti.” “Kumbe hiyo miti yenyewe pia huna!?” Geb akatupa jembe kwa hasira
akarudi ndani.
Mama yake akamfuata nyuma. “Uji huu hapa
mezani.” Mama yake akarudia. “Nimekwambia SINYWI.” “Oooh! Nimekumbuka
umeniambia ndio unaenda kufuata miti.” Liz akatoka chumbani akiwa ndio
ameamka. Alionekana ameoga vizuri na amependeza. Nyumba nzima ilikuwa ikinukia
manukato yake. “Unakwenda wapi Geb?” Liz akauliza kwa upendo. “Nitarudi
sasa hivi.” “Nilifikiri leo tunapumzika kama ulivyosema!” Geb hakujibu.
Akatoka akiwa ameshika funguo zake za gari. Wakasikia akiondoka. “Sasa
ananuna nini!?” Liz akauliza kishari. “Mimi mambo ya visirani asubuhi
asubuhi siyawezi!” Liz akaendelea. Grace alikuwa amenyamaza kimya mezani
akimlisha mwanae, kama hayupo pale. “Siku ndio imeanza.” Mama G,
akaongea na kurudi chumbani kwake.
Baada ya lisaa, wakasikia gari ya Geb inaingia.
Wote wakajua amerudi. Wakatulia. Wakasubiri labda ataingia ndani, lakini muda
ukazidi kwenda kimya. Fili akataka mama yake atoke naye nje amwangalie
anavyoendesha baiskeli. Grace na mwanae wakatoka. Wakakuta mashimo mengi urefu
wa Geb mwenyewe. Grace akabaki ametoa macho. Liz akatoka. Grace naye akaona
akamtoe mama yake. Akamkuta chumbani. “Wewe mama! Hivi umeyaona hayo
mahandaki hapo nje!?” “Nimeyaona. Amesema anapanda miti. Nahisi ni mibuyu!” Wakacheka. “Nenda
kazungumze naye mama! Ataanguka azimie.” “Wewe kwa nini usiongee naye? Si kaka
yako!” “Si unamjua Geb. Hatakaa anijibu kitu. Nenda kampelekee hata maji!” Wakatoka.
Grace akampelekea mama yake jagi la maji na
glasi. Wakacheka pale sebuleni. Wakati wanataka kutoka nje, wakasikia Liz akigomba
nje. Grace akamvuta mama yake. “Subiri kwanza wamalize.” Grace
akanong’ona. Liz aliongea kama dakika 10 bila kujibiwa kitu. Wakamsikia anarudi
ndani huku anaongea kwa hasira. Na yeye akachukua funguo zake za gari, akatoka.
Baada ya kama dakika 3, akarudi tena ndani. Akakusanya nguo zake, akaanza
kuweka kwenye gari yake. “Huwezi kunibabaisha mimi!” Liz alikuwa
akiongea kwa hasira na jazba. Aliingia mara mbili na kutoka mpaka akamaliza,
wakasikia milango ya gari inafungwa kwa nguvu, akaondoa gari karibu agonge
geti.
Waliposikia kimya, ndipo na wao wakatoka.
Akasogea mpaka kwenye shimo alilokuwa ameingia Geb. “Maji ya kunywa haya.” Mama
G alikuwa akimchungulia kule ndani ya shimo alipokuwepo. Kweli mashimo yalikuwa
marefu. “Sina kiu mama. Naomba niache.” “Najua huna kiu. Lakini naomba
kunywa haya maji Geb. Jua kali na wewe unashinda juani. Utaanguka kwa
kizunguzungu.” “Nimegundua nimeyashimba marefu sana, nataka kuyafukia kiasi, ndipo
nipande.” “Miti yenyewe iko wapi?” “Si hiyo hapo pembeni!” Mama G
alipoiangalia, ilikuwa ni miche. Hata haijafikia urefu wa mkono wake.
Akajua kazi ya kufukia tena inaanza. Alikuwa
amechimba mashimo matatu, marefu sana. “Naomba kabla hujafukia hayo
mashimo, kunywa maji.” “Nimesema sina kiu.” “GEB MAGESA!” Mama
G akaita kwa ukali. Geb akajua ameshambadilikia. “Kwani ni lazima mama
jamani!?” “Ndiyo.” Mama G akajibu kwa ukali na kibabe. Geb
akatoka huko shimoni. Mama yake akampa maji, akanywa glasi moja tu, akarudi
kuendelea na kazi yake ya kufukia yale mashimo. Grace akamtizama mama yake.
Wakaangaliana, akaendelea kucheza na mwanae.
Akafukia yale mashimo yote. Jua lilikuwa kali
sana. Alikuwa amelowa chapachapa kwa kuwa udongo ulikuwa mkavu haswa.
Alipomaliza kuyafukia, akaenda upande mwingine, akachimba mashimo mengine.
Lakini ya safari hii aliyafanya mafupi. Akapanda ile miti. Wakajua amemaliza.
Wakaona ametoka tena na gari. “Sasa sijui
anakwenda wapi!?” Grace akauliza kwa kumuhurumia kaka yake. “Siku
mbona ndio imeanza! Baba yake alikuwa hivyo hivyo. Akianza mambo yake ya wivu,
basi hatakuuliza. Anaanza kazi kwenye hiyo nyumba. Asubuhi mpaka usiku.” “Sasa
ulikuwa unafanyaje?” “Inategemea. Kama amenikera au ananisingizia mahusiano,
namuacha ahangaike mpaka atulie mwenyewe. Wakati mwingine nikimuhurumia, naenda
kuzungumza naye. Anatulia. Sasa huyu Geb, anasumbuliwa na mengi. Mwache
ahangaike mpaka akili yake ikae sawa. Hajui anataka nini.” Grace akaguna.
~~~~~~~~~~~~~
Danny akarudi. “Mbona ukoka umechimbuliwa
tena wakati uligarimu pesa nyingi sana kupandwa na kutunzwa mpaka kufikia hivyo!?”
“Kuna shuguli hapa. Hujawahi kuona.” Mama G, akajibu. “Kwema?” Danny
akaendelea kuhoji. “Geb kaamka na matengenezo ya nyumba, hapa!” Danny
akaanza kucheka. “Huyo ni Nanaa tu.” “Kumbe umejua!?” “Mimi nilijua.
Na nilifanya kusudi kongea kwa sauti asubuhi, ili ajue Nanaa anaondoka.” Grace
akampiga ngumi mumewe. “Hivi wewe ukoje Danny jamani!? Unaona raha hivyo
anavyohangaika?” Danny akacheka na kuruka pembeni.
“Sasa, sasahivi kaenda wapi?” “Ndio tumekaa hapa
barazani, tunasubiri tuone. Hajala kuanzia kifungua kinywa wala hajataka kula
chakula cha mchana. Maji yenyewe kanywa glasi moja, tena baada ya kuwa mkali.”
“Ngoja na mimi nikae, nishuhudie.” Akaenda kuchukua chakula ndani, akatoka
kula pale barazani kulikokuwa kumezungushiwa vioo, kwenye ukuta ulikuwa
umejengwa vizuri sana nakupendezesha hilo baraza. Kwa hiyo AC ya baridi ilikuwa
ikipuliza. Fili akapitiwa na usingizi pale pale.
Kwa Nanaa!
N |
anaa
alipoona vitimbwi haviishi, akamuita Zena pembeni. “Samahani Nanaa!” Zena
akamuwahi kabla hata Nanaa ahajasema kitu. Nanaa akacheka. “Sasa mpenzi,
acha mimi niondoke.” “Hata mimi nilitaka kukwambia hivyo hivyo. Haya mambo ya
ajabu kweli! Mpaka nimejisikia vibaya! Lakini usije ukafikiri nimehusika.”
“Wala usijali. Mimi naelewa. Hata yeye nimemuelewa tu. Naomba niagie Yasini.
Mwambie zawadi yake inamngoja ng’ambo ya bahari.” Wakacheka, Nanaa
akaondoka bila kuaga mtu.
Kwa Geb!
Mara Geb akarudi na makopo ya rangi. Danny na
Mama G, wakaanza kucheka kimya kimya. “Leo patamu hapa!” Danny
aliongea kishabiki. “Mama wewe! Muwahi bwana.” Mama G akaendelea
kucheka taratibu. “Nenda bwana mama! Usimfuatilishe Danny.” Mama G,
akatoka pale. Akamfuata. “Unabadili rangi ya geti au ukuta?” “Vyote?” Akajibu
Geb kwa kifupi.
“Unapaka nyeusi!?” Mama yake akaendelea
kuhoji taratibu lakini kwa mshangao baada ya kugundua ni rangi nyeusi. “Ndiyo.
Nataka ukuta mweusi, na geti jeusi.” “Mmmh!” Ilikuwa saa tisa
mchana. “Si ungepumzika mpaka jua litue?” “Sijachoka mama. Naomba niache.” Grace
na Danny walikuwa wakiangalia. “Naona kuna brashi mbili, ngoja nikusaidie
kupaka.” “Hapana mama. Naomba niache.” “Nikuletee maji ya kunywa tena?”
“Sitaki mama. Naomba niache. Nataka kuwa peke yangu.” “Haya baba.” Mama G
akaondoka taratibu.
Nanaa Arudi
Na Kuokoa Jahazi.
Mara Nanaa akaingia. Akamkuta Geb amelowa jasho
yupo karibu na getini. Amechoka mpaka usoni. Anajifuta jasho kwa mikono yake.
Akamsogelea. “Pole na kazi.” “Asante.” Nana akabaki akimtizama.
Alikuwa ameinamia yale makopo ya rangi anahangaika nayo. Kina Grace walikuwa
bado wakimwangalia kwa mbali wakiulizana, kama anataka kuchanganya au kumwagia
kwenye geti.
Mama yao akasema hawezi kumwagia. “Nyinyi
hamjajua. Pale anapiga mahesabu jinsi gani yakufanya ile kazi kuwa ngumu zaidi
ya vile.” Danny alizidi kufurahia. Grace akamfinya. “Sasa unafurahia
nini?” “Nyinyi si mnanionaga mimi chizi kupenda? Sasa leo muone mwalimu wa
machizi.” “Usiseme hivyo Danny bwana! Mimi namuhurumia Geb. Najua anashindwa
chakufanya. Anaona yupo huku, na kule anapoteza.” “Ndio atie akili. Sasa
tusubirie tuone. Nanaa kawasili.” Grace alimwangalia mumewe asimmalize.
Mama G, na yeye akajiweka sawa.
~~~~~~~~~~~~~
“Geb!” Nanaa akamuita taratibu. Geb
akamtizama. “Vip, upo sawa?” Nanaa akamuuliza kwa kujali. “Umeweza
hata kula?” Nanaa akauliza tena kwa upole. “Nimekuwa na kazi nyingi.”
“Pole.” Nanaa akabaki akimwangalia. “Umekuwa na wakati mzuri huko?” Geb
na yeye akauliza. “Hapana.” Nanaa akajibu bila kufikiria. “Ni
nini?” Geb akauliza tena. “Aaah! Mambo ya kitoto tu. Nimeamua
kurudi.” “Pole. Umekula sasa?” “Hapana. Nilikuwa nimekasirika, nikashindwa
hata kunywa soda. Haya maji nimenunua njiani sababu ya jua kali.” Nanaa
akaanza kutokwa na machozi.
Geb akakaa vizuri. “Pole. Usilie sasa. Ni
nini?” “Mambo ya kitoto tu. Hayana hata
maana.” “Mbona yamekuumiza sasa?” Nanaa akaanza kujifikiria ni
nini cha kusimulia na nini cha kuacha. Kwanza ni Jeff. Halafu amsimulie Geb!
Atamwambia nini? Kwa haraka sana atasema ni wivu. Akaamua abadili mazungumzo.
Akajifuta machozi.
“Kama unataka kupaka rangi, naweza
kukusaidia.” Nanaa akaona atoe msaada. “Jua kali sana. Labda baadaye.
Kwanza umeipenda hii rangi?” Geb akamuuliza Nanaa huku akimuonyesha ile
rangi ya maji, nyeusi. “Unataka kupaka wapi?” Nanaa akamuuliza huku
akimsogelea karibu zaidi. “Ukuta na geti.” “Kwa nini unataka
kubadili hii iliyokuwepo? Inaonekana bado mpya tu na imependezea. Sidhani kama
hiyo nyeusi itapendezea ukuta. Labda geti.” “Basi heri niache tu. Mpaka hii
ichakae ndipo nifikirie tena.” Hata Nanaa alikuwa akitokwa jasho.
Akaona malengelenge kwenye mikono ya Geb. “Tuone.” Akamvuta
mkono wake akawa ameushika anaangalia. “Mbona vidonda vikubwa hivi!?” Nanaa
akamuuliza huku akiviangalia vile vidonda. Wala asijue mama yake Geb na kina
Danny wapo barazani wanawaangalia. “Vinauma?” Nanaa akamuuliza kwa
upendo. “Vikiingia jasho ndio vinauma.” Geb alijibu huku akifikiria.
Ndio hisia za maumivu zilianza kumjia. Kabla ya kuja Nanaa, hakuwa akisikia
chochote kile. Si njaa, si kiu, si maumivu wala kuchoka. Bado alikuwa na nguvu
nyingi tu ya kuendelea.
“Pole.” Nanaa akatoa mtandio wake kutoka
kwenye mkoba aliokuwa nao, akampa. “Futia jasho.” Geb akacheka. “Mbona
mtandio wenyewe msafi hivi!?” “Nitafua tu. Ni heri kutumia huu mtandio kuliko
hivyo unavyojifuta kwa mkono. Jasho linaingia kwenye vidonda. Utazidi
kujiumiza.” Geb akaupokea akaanza kujifutia jasho.
Akafungua
chupa ya maji ya baridi aliyokuwa nayo. “Nipe huo mkono wako wa kulia
kwanza. Naona ndio una kidonda kikubwa.” Geb akaunyosha mkono na kufungua
kiganja chake. Nanaa akammiminia yale maji ya baridi kwenye lile lengelenge
kubwa lililogeuka kidonda. Mikono hiyo ya BOT, iliyozoea kucheza na kompyuta
muda mwingi, leo ilipitishwa kwenye shuruba, ikasalimu amri.
Akaona Geb anacheka. “Umeona eeh?”
“Napata nafuu kubwa. Huu ubaridi wa maji unapoozesha maumivu.” Geb
alisifia anachokifanya Nanaa. Wakacheka. “Umetembea sana?” Geb akauliza
huku akiendelea kujipangusa jasho kwa kutumia mkono wake wa kushoto. Aligeuza
ule mtandio upande mwingine, uliokuwa mkavu, akaendelea kujipangusa. “Sio
sana, ila jua kali! Leo nimetamani kama ningekuwa na gari langu.” Nanaa
aliongea na kujicheka. “Eti hata pakulala sina, nataka gari!” “Ungenipigia
simu nikufuate.” “Kwanza niliacha bado mmelala, pili nilikwambia sina namba
yako Geb. Tatu hata kama ningekuwa na namba yako ya simu, nisingethubutu
kukupigia na kukuvurugia mapumziko yako na Liz. Najua leo ni weekend.
Mngehitaji muda usio na mwingiliano wa mambo yasiyo maana.” “Kuomba lifti
sio kitu cha maana!?” Geb akauliza. “Inategemea na muombaji
Geb. Kumbuka ni mimi Nanaa.” Nanaa alijionyeshea kidole kinyonge.
“Ningekufuata Nanaa.” Nanaa akajicheka.“Huniamini?” Geb
akauliza, Nanaa hakujibu. Akachukua mkono wake wa kushoto, akaanza kuumwagia
maji kama alivyofanya kwenye mkono wa kulia. “Nanaa?” Geb aliita kama
kumkumbushia swali lake. Akayamalizia yale maji yote kwenye ule mkono. “Twende
tukale Geb.” “Huniamini?” Nanaa akamwangalia, akaona amekusudia kupata
jibu. “Nakuamini lakini mimi mwenyewe nisingeruhusu ufanye hivyo.” Geb
alibaki akimtizama. Nanaa akatoa tabasamu lake la upole huku akiachia mkono wa
Geb taratibu.
“Twende Geb.” “Maji uliyokuwa unanimwagia
yamenifanya nitamani kuoga mwili mzima na maji ya baridiii.” Nanaa
akacheka. “Asante kwa kujali.” “Karibu.” Nanaa akajibu na cheko
lililofanya dimpozi zake machavuni zikae vizuri. Geb alikuwa akimwangalia kwa
kumu admire sana. Kama kitu kizuri cha thamani anachokitamani.
Nanaa akainama.
“Hata mimi nataka nikaoge kwanza. Lakini tuyatoe
haya makopo hapa katikati ya barabara. Mtu akitaka kutoka au kuingia,
atashindwa.” Nanaa alitoa wazo. Kuepuka kuendelea kuangaliana pale juani,
akainama na kunyanyua makopo mawili ya rangi. “Tukayaweke stoo.” Geb
akatoa wazo. Wakawaona wanaanza kuyabeba yale makopo kuyapeleka stoo. Geb
alinunua makopo 10 ya rangi.
~~~~~~~~~~~~~
Kila mtu akahema. “Daah! Nanaa angechelewa
kidogo tu, tungejishindia geti jeusi na ukuta mweusi.” Mama G, akaanza
kucheka. “Danny huwa ananiudhi mimi jamani! Ukoje huna huruma?” “Unafikiri
pale anakuwa anachoka? Yaani wivu mzuri sana. Pale alikuwa anajiona ndio
anaanza.” “Na angemaliza mapema, angeanza kazi nyingine.” Mama yao
akaongeza. “Natamani siku nyingine akumbuke kuchimba shimo la taka,
refu.” Grace alimrushia mumewe kiatu cha mwanae kilichokuwa karibu.
Danny akakwepa. Mama G, na Danny walikuwa wakicheka taratibu ili Geb asisikie
maana walikuwa wanapita mbali kidogo, kuelekea stoo kubwa ya nje. Kuyapanga
yale makopo ya rangi.
~~~~~~~~~~~~~
Uchokozi ukawazidi yeye na mama G, kupokezana maneno,
wasijue wenzao walishamaliza. Mara wakaona wanaingia. Wakanyamaza kwa haraka.
Danny akatoa simu yake akajidai anasoma ujumbe. “Hiyo ni kalenda Danny!” Geb
akajua wala hasomi kitu kwani macho yake yalitua kwenye kalenda ya simu
akashindwa hata kuhamisha macho. Geb akamkamata. Akang’ata meno kwa
nguvu. “Mmmhhh! Lazima kujua tarehe Geb. Mambo ya majira. Kiangazi, masika
na… ” Geb akatingisha kichwa, akaingia ndani. “Uchokozi mpaka
umekamatwa. Muone. Ujanja wote umekuisha.” Mkewe akamcheka.
Mama G ndio alikuwa hana mbavu kwa kucheka. Nanaa
akamsogelea. “Kumbe mlikuwa mmekaa hapa!?” Nanaa akauliza huku
akimwangalia mama G. “Sio muda mrefu sana. Ila tumeona kila kitu.” Danny
akajibu yeye kwa haraka. Nanaa akacheka. “Shikamoo Mama!” “Mbona umewahi?”
“Mambo hayakwenda kama nilivyodhani. Nikaona nirudi tu nyumbani.” “Afadhali.
Kuna chakula ndani. Nenda ukale.” “Asante mama.” Na yeye akaingia ndani.
~~~~~~~~~~~~~
Alikuta Geb amesimama nje ya mlango wa jikoni
akisoma ujumbe. Nanaa akampita, akatangulia jikoni. Haraka sana Geb akamfuata.
Wakasahau swala la kuoga kwanza. “Nini kinaanza? Uji au chakula?” Nanaa
akamuuliza mara alipoingia. “Uji kwanza, halafu ndio chakula.” Akaanza
kumtayarishia. Kwa kuwa alikuwa mvivu wa kula, mama yake alihakikisha kila kitu
anachokula, lazima kisindikizwe na bakuli la matunda. Kwa hiyo na yeye,
akamuwekea kwenye sinia yake hiyo maalumu aliyomuona mama yake akimpangia
mwanae chakula. Akamimina uji kutoka kwenye thermos na kuweka kwenye bakuli
lake maalumu la kunywea uji. Akafungua friji, akakuta mama yake alishamwandalia
matunda. Akayaweka kwenye hilo sinia. Akaongeza glasi ya maji na napkins tatu,
juu yake akaweka uma, kijiko na kisu. Akamsogezea pale. “Karibu.”
“Nashukuru Nanaa. Asante.” “Karibu.” Na yeye akajiwekea chakula kwenye
sahani, akaenda kukaa pembeni yake pale pale jikoni. Wakaanza kula.
“Wamekuudhi nini huko?” Geb
alimgeukia na kumuuliza. “Hata sio mambo ya maana.” “Nataka kujua Nanaa.” Nanaa
akafikiria ni nini chakumwambia. “Sijui niseme nini? Lakini ni juu ya
Jeff.” “Na yeye alikuwepo!?” “Ndiyo. Lakini kwa kuwa nilimkataa, akaja na
msichana mwingine. Akawa anafanya vitimbwi kama kunikera tu.”“Uliona wivu?”
“Hapana Geb! Najua alifanya kusudi kuniumiza, kwa kuwa na mimi nilimuumiza kwa
kumkataa. Tena baada ya kufanya juhudi na kunisisitizia yeye sio tapeli kwangu.
Anania ya dhati. Naelewa kwa nini amenikasirikia. Au kuja na msichana mwingine
pale. Ni kama kunionyesha aliyokuwa akiyataka kwangu sio uongo. Maana alianza
hata kusema pale mbele ya watu kuwa anafikiria kufunga ndoa haraka. Hayo yote
alikuwa akinithibitishia mimi kuwa hakuwa akidanganya au akitaka kunidanganya.
Lakini..” Nanaa akasita.
“Lakini nini?”Geb akataka aendelee. “Najiuliza
sijui nimepiga teke bahati au la!” “Kwamba unajutia?” Likarushwa swali
jingine. “Kwa sasa sijutii Geb. Kwa kuwa najiona sipo tayari kabisa kwenye
swala la mahusiano. Ila najua siku moja nitahitaji kuwa na mtu. Sasa iweje kama
Jeff ndio alikuwa mtu sahihi kwangu, halafu nilishamfukuza?” Geb akanyamaza.
“Lakini moyoni nilishindwa kumpokea kabisa!”
“Basi ujue siye Nanaa. Jipe muda kila kitu kitakuwa sawa.” “Naona nifanye tu
hivyo. Hata hivyo naona nimeshachelewa.” “Ikitokea anakupigia simu na kutaka
mrekebishe?” “Hilo ndilo tatizo Geb. Moyoni nimeshindwa kumpokea kabisa. Japo
naona ni kama ameshika majibu ya maswali mengi au ni kama atakuwa ni msuluhishi
wa matatizo yangu.” “Ki vipi?” “Sijui Geb! Hata sijui niseme nini?” Geb
alibaki akimtizama kwa muda.
Akamaliza uji wake wote. “Tunaweza kutoka
kidogo?” Nanaa akamtizama kwa makini, kama aliyeshindwa kuelewa. “Na
Liz?” Nanaa alijikuta akiuliza bila kufikiria. “Liz anahusikaje na
kutoka kwetu?” Nanaa akanyamaza baada ya kuropoka. “Nanaa?”
“Nilimsikia akisema weekend hii ulimwambia mtakuwa pamoja. Alisema ulimuahidi
mtakuwa naye kwa kuwa hutasafiri. Ndio maana nauliza.” Nanaa akajitetea,
Geb akasimama. Akaweka sinia alilokuwa akitumia lililokuwa na bakuli la uji na
matunda akaweka kwenye sinki. Akabaki amesimama kama anayefikiria kitu cha
kuongea huku akiangalia vile vyombo pale kwenye sinki. Akashindwa chakuongea,
akaamua kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa akahisi amekosea. Akaingia kuoga. Akabadili
nguo. Safari hii alivaa kigauni kifupi mpaka katikati ya magoti. Akajitengeneza
kidogo, akavaa na hereni zake zile zile za duara zilizofanya uso wake uzidi
kuvutia. Aliporidhika, akaenda kugonga mlangoni kwa Geb. Geb akafungua. Akabaki
amesimama mlangoni akimwangalia. “Naomba lifti.” Geb akacheka na
kujiweka vizuri pale mlangoni. Nanaa alijua wazi amefurahi kumuona pale. Na
anafurahia anachokiona mbele yake. Yeye.
Akakumbuka alimwambia akimuomba lifti atampeleka
popote pale. “Sawa. Nisubiri nimalizie kuvaa.” Geb alikuwa ndio
ametoka kuoga. Alikuwa amevaa jinsi na singlendi tu. “Utanikuta jikoni
nakupashia moto chakula chako. Ukila ndio tutatoka.” “Sawa.” Geb
alishafurahia mpaka uso wake ulionyesha kuna furaha moyoni mwake. “Nanaa!” Geb
akamuita. Akageuka kabla hajapotelea jikoni. “Umependeza.” Nanaa akacheka
na kujitazama. Kwa hakika alikuwa akivaa vitu vya rahisi sana. “Kila kitu
huwa kinakupendeza.” Geb akaweka msisitizo kumuhakikishia huwa anaangalia
kila anachoweka mwilini mwake. “Asante.” Nanaa akashukuru na cheko la
aibu kisha akageuka na kupotelea jikoni.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda Geb alitoka akiwa na furaha, sio
kama yule aliyeamka asubuhi. Akaingia jikoni, akamkuta Nanaa anamsubiria. “Sasa
kwa kupendeza huko, unataka nikupeleke wapi?” Nanaa akacheka. “Kaa
chini kwanza ule wakati nakusimulia habari ya tunapokwenda.” Geb
akakaa. “Ehee!” Akataka Nanaa aendelee. “Kuna mahali mpenzi wake
Tia, anaitwa Evan alitupeleka. Wakati wao wanakula na kunywa na kuzungumza
mambo yao, nikawaomba nitembee mimi mwenyewe kuosha macho. Nikatoka na kutembea
kama umbali wa dakika 10 mbeleni. Nikagundua kijiwe changu.” Nanaa
akacheka kidogo.
“Pazuri, patulivu. Nilijikuta peke yangu.
Nikajisifu kuwa labda mimi ndio wakwanza kupagundua hapo au hamna watu wengi
wanaofika hapo. Nikaamua siku nyingine nije kurudi peke yangu. Nikatafuta siku
nyingine, nikaenda peke yangu. Nilikaa zaidi ya masaa 4, bila kukutana na mtu
yeyote hapo. Basi nikajua ndio sehemu yangu.” “Wapi?” Geb aliendelea
kudadisi huku anacheka. “Sitakwambia mpaka twende ukajionee mwenyewe. Unaweza
usipapende sababu tu ya jina la mtaa au hoteli, wakati hilo eneo langu,
nililoligundua ni zuri.” Geb akacheka huku akimwangalia Nanaa, msichana
aliyeshindwa kushibisha macho yake.
“Pazuri! Wewe kula nikupeleke, halafu utakuja
kuniambia kama hutakuwa ukiwa ukienda peke yako kila unapotaka muda mtulivu.”
“Sawa.” Geb akakubali. Hakujali eneo. Popote kule, ilimradi awe na Nanaa.
Vilisikika vicheko huko jikoni. Angalau mama G na Grace wakatulia mioyo.
Cha Mtu
Mavi!
Wakati Geb anamalizia kula, wakasikia Liz
ameingia. Danny akafuata nyuma. “Ngoja niangalie kama kuna mpira. Njoo
mama.” Grace alijua ni umbea tu wa mumewe. Na lazima mama yake awepo, ili
wakonyezane. Grace yeye akabakia palepale nje amempakata mwanae. Mama G
akaingia, akaenda kukaa kwenye kochi karibu na Danny. Wakawasha tv kwa sauti ya
chini ili wasikie kinachoendelea.
“Geb!” Walimsikia Liz akipita kuelekea
chumbani kwa Geb huku akimuita. Geb akamwangalia Nanaa, akamuona vile
alivyonyong’onyea. Tabasamu lote lilimwisha. Zile dimpozi alizokuwa akifurahia
kuzitizama wakati anaongea hapo jikoni hazikuwepo tena. Alibaki akichora
mezani, gafla akamuona ananyanyuka na kutoka pale jikoni. Akarudi chumbani
kwake.
“Geb!” Liz akaita tena. “Nipo huku
jikoni, nakula?” “Hee! Kwa nini ule jikoni kama msichana wa kazi!?” Liz
akaingia. “Ulimaliza kazi?” Akamuuliza Geb. “Ndiyo. Vipi?” “Kuna
kitu nataka nikakuonyeshe.” “Nimechoka sana Liz. Nataka kupumzika.” “Mimi
nitakuendesha. Wewe utakaa tu wala hutafanya kitu.” Geb alitulia kwa muda
kama anayefikiria. “Hutachoka Geb! Nakuahidi. Na ukirudi huko,
utanishukuru. Ni kitu sahihi kwa kazi ngumu uliyofanya leo.” Kimya.
Wadada wawili wote wanataka kumfurahisha weekend hiyo. Wote
wanamuhakikishia furaha mara yakufika huko. “Nani mwenye kisu kikali?”
“Uliniahidi leo utakuwa na mimi Geb! Nimeahirisha
mambo yangu yote leo, ili tuwe wote. Naomba usinigeuke tafadhali. Wewe sio mtu
wakutoa ahadi ukashindwa kuzitimiza.” Geb akawa amebanwa, akashindwa cha
kujitetea. Asubuhi alimwambia ana kazi. Lakini sasa hivi amemkuta msafi na hana
kisingizio chochote. “Basi subiri nimalize kula.” “Utanikuta basi hapo sebuleni.
Si unanijua mimi na jiko? Hatuna urafiki ki hivyoo!” Liz akatoka na kwenda
kukaa sebuleni wakati Geb anamalizia kula pale jikoni.
~~~~~~~~~~~~~
Liz akajiweka kwenye kochi na miguu kakunja
4. Miwani yake nzuri sana ya jua, aliweka kichwani ikashikilia nywele zake
ambazo kwa asili alijaliwa nywele nzuri. Japo ziliongezwa umaridadi na aina ya
dawa aliyokuwa anaweka kichwani. Nakuzifanya nywele hiyo nzito, ianguke
mabegani kama sufu. Inang’aa hata gizani. Kuonyeshwa huwa inashugulikiwa
kitaalamu.
Alivaa pensi yake nyeupe na blauzi ya kata
mikono, nyepesi. Ilifanana na sendozi ndefu za wazi alizokuwa amevaa. Huwezi
ukamkuta Liz mahali ukachoka kumtizama. Ungeweza kusema ni mwana mitindo huko
Hollywood, mjini Los Angeles. Hajikosei. Kila kitu kizuri na garama. Aliupenda
huo mwili wake, wenye rangi nyeusi kamili iliyong’aa kama alikuwa akipiga msasa
ngozi yake kila mara. Msafi kuanzia nywele, mpaka ukucha wa mguu. Ni ngumu
kujua kama huwa anakutana na vumbi. Kimwili chake kizuri. Alipo Liz, utajua
kuna neema ya uchumi, elimu na afya njema.
~~~~~~~~~~~~~
Akatoa simu yake akaanza kuitumia bila kumsemesha
Danny wala mama G. Akainamia simu yake akaendelea na shuguli zake kwenye hiyo
simu, wakati mama G na Danny macho yapo kwenye luninga. Harufu na uwepo wa Liz vikatawala
pale ndani akimsubiria mpenzi wake.
Geb alimaliza kula, akatoka. Akaangalia ile hali
pale sebuleni. Mama yake, Danny na Liz, akabaki akifikiria. Liz akanyanyua
macho na kumtizama mpenzi wake. Yeye hakumnyima tabasamu. “Utafurahia na
utanishukuru. Twende.” Liz alionekana amechangamka kweli tofauti na
alivyoondoka. Wakatoka.
Nanaa akajicheka. Akaamua alale tu ili asianze
kuwaza jinsi siku yake ilivyozidi kumsisitizia kuwa yupo mpweke na kila
mwanaume ana mwanamke wake. Mungu bariki, akalala hapo hapo. Bila shida.
~~~~~~~~~~~~~
Wakati amepotelea usingizini, akasikia mtu
anagonga mlango. Akahisi ni ndoto, lakini akaendelea kusikia mlango unagongwa
taratibu. Akajua ni chumbani kwake. Akafungua macho, giza lilishaingia nje.
Akajua amelala na kupitiliza. Akasimama kwa haraka, akajiweka sawa, akaenda
kufungua mlango. Akakuta Geb amesimama mlangoni. “Ulikuwa umelala?” Nanaa
akatingisha kichwa kukubali na tabasamu la kinyonge. Bado alikuwa amevaa vilevile
kama alivyokuwa amejiandaa kutoka naye masaa machache yaliyopita.
“Nimekuletea Ice cream.” Nanaa akatoa tena
tabasamu la kinyonge akainama kama anayefikiria. Geb alibaki amenyosha mkono
kumkabidhi kopo lake dogo la Ice cream. “Nanaa!” Geb aliita kwa
upole. “Abee!” Nanaa akanyanyua uso akamwangalia. “Hii ni ice
cream yako, nimekuletea.” Geb akarudia kana kwamba hakuwa amesikiwa tokea
mwanzoni. “Nakushukuru, lakini hapana.” Nanaa
alijibu kwa upole huku machozi yakiwa yamejaa ndani ya macho yake. Yakafanikiwa
kujaa mpaka kuchirizika nje ya macho yake yaliyokuwa yamejaa huzuni.
Akajifuta. “Usiku mwema Geb!” Akamuaga
kwa sauti ya chini kabisa, kama kunong’ona huku akiangalia chini. Akafunga
mlango. Akarudi kulala, alimuacha Geb amesimama palepale nje ya mlango wake na
ice cream mkononi.
~~~~~~~~~~~~~
Mapenzi yamtatiza Geb. Yu
njia panda. Liz au Nanaa?
Nani wa Nani?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment