Nanaa akajiandaa, nakutoka. Alimkuta bibi Fili
anamsubiria Geb sehemu ya kulia chakula. Geb alikuwa akioga chumbani
kwake. “Mbona umependeza hivyo?” “Naenda kukutana na rafiki zangu mara
moja. Nimekuwa nikiwaahirisha kila wakati.” Danny akakohoa. Alikuwa sebuleni
na mkewe, wanaangalia tv. Nanaa akacheka na kuinama. “Umependeza kweli
Nanaa! Au ndio na safari ya kwa Jeff?” Bibi Fili akaendelea kuhoji
kichokozi. “Na yeye pia atakuwepo mama.” Nanaa alijibu kwa aibu
kidogo. “Sitakawia kurudi. Nataka na wao nikawashirikishe swala la uhitaji
wangu wa chumba. Pengine wanaweza kunisaidia kwa haraka.” “Sawa.” Nanaa
akasogea pale sebuleni.
“Umependeza sana Nanaa.” Grace akamsifia. “Asante.” Alijibu
kwa aibu. “Nitarudi baadaye.” “Unataka usindikizwe?” Grace
akauliza. “Hamna haja. Nitachukua daladala hapo barabarani.” “Sawa. Uwe na
wakati mzuri.” Danny akaanza kucheka. Nanaa akatoka bila hata kugeuka huku
akicheka na yeye. “Anaonekana ni binti mtulivu sana.” Alimsikia bibi
Fili akisifia. “Na ni mzuri pia.” Akamsikia Grace ameongeza.
Nyongo
Mkalia Ini.
“Naona Jeff amekaza kweli! Mpaka amekubaliwa!” Danny
aliendeleza maongezi. “Nani?” Geb alitoka akakuta wanaongea huku
wanacheka. “Nanaa katoka.” “Sio katoka bwana Grace! Wewe vipi? Sema katoka
na amependeza kweli kweli. Halafu kamuaga mama anaenda kumshirikisha Jeff, hana
sehemu ya kuishi. Kama namuona Jeff atakavyofurahi.” “Danny nyie! Nanaa anaenda
kwa rafiki yake. Tena walikuwa wakizungumza kwenye gari wakati namleta hapa.” Grace
akatetea.
“Eti mama, Nanaa hasema kuwa na Jeff atakuwepo?” Danny
alitaka uungwaji mkono kutoka kwa mama mkwe wake. “Kasema hapa. Na
alivyopendeza vile! Lazima huyo Jeff ampishe kwenye nyumba yake. Kwa uzuri na
utulivu ule! Lazima maombi ya Jeff yatakuwa yamejibiwa.” Waliendelea
kutania, lakini wasijue wanazidi kumchanganya Geb.
Huku kwa
Geb!
H |
akwenda
kulala kama alivyomwambia mama yake. Akaanza kusafisha chumba alichosema
angesafisha kesho yake akipumzika, kwa ajili ya Nanaa. Grace alivyosikia kukuru
kakara nyingi, akaamua kwenda kusaidia. Geb alikuwa kimya kupita kawaida yake.
Swali moja, alichukua zaidi ya dakika tano kulijibu. Kwa kuwa Grace anamfahamu
pacha mwenzie, akaamua amuache tu. Wafanye kazi kimya kimya. Alihangaika Geb,
mpaka Grace alimuonea huruma. Akasafisha kila mahali tena kwa mikono yake
mwenyewe. Akahakikisha anafuta vumbi kila mahali na kusafisha choo cha humo
ndani. Chumba kikadekiwa vizuri. Ikaja kazi ya kupanga sasa. Akatoa mashuka
masafi na kumtandikia Nanaa. Akaenda chumbani kwa bibi Fili, akahamisha mizigo
yote ya Nanaa. Akampangia kwenye hicho chumba.
Mama yake akahamia kukaa kwenye makochi baada ya
kuona shuguli zimekuwa nyingi, hasira kwa mziwanda zimeanza. Akajua hakuna
kulala tena. Wakabaki wanaangaliana na Grace. Aliingia na kutoka. Mara abebe
hiki arudishe kile. Ilimradi tu kukamilisha hicho chumba cha Nanaa.
Huko kwa
Nanaa!
Na yeye baada ya purukushani za panda shuka
kwenye daladala hii kuingia ile, akawa amewasili Sinza Pub. Akakuta wote
wanamsubiria. Jeff akamvutia kiti, akakaa. “Mbona sasa unanishangaa?”
“Ndio kupendeza gani hivyo?” Zena alimnong’oneza. “Si umesema
tupendeze!?” Wakacheka. “Umependeza sana Nanaa.” “Asante.” Akashukuru
na ndipo akasalimia wengine. Jeff na Yasini.
“Unisamehe Jeff. Mambo yamekuwa yanaingiliana.”
“Nini tena?” Jeff akauliza. “Nahangaika sehemu ya kuishi. Bado sijatulia.”
“Pole. Ungependa nikusaidie?” Jeff akauliza. Nanaa akacheka. “Msaada
mkubwa ninaotaka kwa sasa ni niwe na kwangu. Kama ukisikia kuna chumba
kinakodishwa, tafadhali nijulishe.” “Mimi ninayo sehemu kubwa tu yakuishi.
Nakukaribisha.” “Asante.” “Mbona unacheka kama huamini?” “Nimekushukuru jamani
Jeff! Natakiwa nifanyeje?” “Sasa shukurani hiyo utahamia au vipi?” “Kwa sasa
ninapo pakujishikiza. Natafuta kwangu.” “Hata kwangu panaweza kuwa kwako.” Jeff
akaendelea. Muhudumu akawasogelea.
“Nasikia njaa! Sijala tokea jana mchana
nilivyokula kazini. Nilipika tu kwa kaka, lakini sikula.” “Pole. Basi tuagize
mbuzi wa kuchoma. Si utapenda?” Jeff akauliza. “Mimi ni kama fisi kwa
nyama.” Nanaa akajibu, wakacheka. “Naomba usichelewe dada yangu.
Natakiwa kuondoka hapa kabla ya saa 12.” “Usijali. Nitahakikisha oda yenu
inakuwa mbele.” “Nitakushukuru.” Wakaendelea kuongea na kucheka. Ni kweli
Yasini alionekana kumjali Zena. Nanaa akabakia akiwatizama kwa kuwatamania.
“Hongereni. Naona mpo vizuri! Na mmependezeana.” Nanaa
akasifia. “Namshukuru Mungu kwa kweli. Nafurahia kampani ya Zena. Hana
makuu.” Yasini akasifia. Zena akacheka kwa aibu na deko kidogo.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa akaanza kuwaza maisha yake. Alipotoka,
alipo ambapo maisha yanaendelea kumchanganya na kujichanganya. Anapoelekea ndio
ukawa mtihani. Karata chache alizonazo mkononi alitakiwa azicheze kwa makini
mno. Lasivyo ataharibu kabisa. Akabaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~
“Mbona upo mbali?” Swali la Jeff likamtoa
mawazoni. “Nipo hapahapa jijini.” Nanaa alijibu huku akitoa tabasamu.
Wazi alionyesha ametingwa na mambo. Hajui afanye nini! Ni kama jibu amelipata.
Lakini moyo wake unasita. Akabaki njia panda.
Vinywaji vilishaletwa, wakabakia kusubiria
chakula. Wakawa wanaendelea na vinywaji, huku stori za hapa na pale
zikiendelea. Walipokuwepo jana yake. Walifurahia nini. Wapi watakwenda baada ya
pale. Nanaa alikuwa kimya tu akisikiliza na kucheka. “Nilifikiri tutakaa
mpaka usiku! Ili tuwe wote.” “Ningependa kufanya hivyo. Niongozane na nyinyi
kila mahali, lakini naishi kwa watu. Au ndio nimehamia kwa watu. Lazima niweke
heshima. Siwezi kuanza kurudi usiku nyumbani kwa watu.” “Upo sahihi.” Jeff
akakubaliana naye.
Chakula kikaletwa, wakaanza kula. Nanaa
akaangalia saa yake, akamalizia soda, akaamua aondoke. “Jamani
nawashukuru.” “Unaondoka sasa hivi Nanaa!?” “Nawahi daladala.” Nanaa
alishasimama, na pochi yake akaiweka begani. “Naomba nikusindikize.” “Kweli
Jeff? Naona bado unakula.” “Usiwe na wasiwasi. Twende.” Wakatoka wao
wawili tu.
Jeff Atupia Ndoano Kwa Nanaa
Wakiwa Garini.
“Naomba uniahidi utafikiria ombi langu.” Jeff
aliongea mara baada ya kuondoa gari. “Ombi gani tena? Maana kama kutoka
kwa ajili ya chakula cha mchana, nimeshatimiza.” Jeff akacheka. “Kweli
hunitaki kwenye maisha yako Nanaa! Hivi ndio umeshatoka na mimi?” “Jamani
Jeff!” “Kweli Nanaa hii ndio picha uliyonayo ya kutoka na mimi?” Nanaa
akanyamaza. “Huwa wanasema, usikatae wito. Kataa maneno. Lakini naona
mwenzangu unanikatalia vyote!” “Akili yangu haijatulia Jeff. Bado sijapata
maisha ya kueleweka.” “Kwa nini usije kutulia kwangu kwa muda mpaka utakapo
jipanga?” “Sikufahamu Jeff!” “Na unampango gani juu ya hilo?” “Sijui! Sitaki
kuongezea kitu kingine kitakachonifanya nishindwe hata kumaliza yanayonitinga.”
“Kwa nini umeanza kunifikiria vibaya, wakati hata hujanipa nafasi?” Kimya.
“Unajuaje labda chanzo cha kunifahamu ndio ukawa
mwanzo wa ufumbuzi wa maswala yako? Huwa wanasema, ‘Two are better than one.’ Hujasikia
hilo, kuwa wawili ni bora kuliko mmoja?” Nanaa akacheka. “Wawe
wamepatana na kuelewana. Unaweza kukuta ndio wanaongezeana matatizo zaidi
maishani.” Jeff akamtizama na kuendelea kuendesha. “Mbona sasa
kimya?” “Nimeishiwa hoja Nanaa. Kila ninachoongea, unapinga! Nimekubali
kushindwa.” “Usinielewe vibaya.” “Sawa Nanaa.” Wakaendelea kuendesha,
Nanaa akimuelekeza.
“Nakushukuru kwa kunirudisha.” “Anytime.” Jeff
alijibu kwa kifupi tu na kunyamaza. Nanaa akajua ameshakasirika. Akacheka
kidogo na kugeukia pembeni huku akifikiria. “Nini sasa?” Jeff
akamuuliza huku akiendelea kuendesha kwa makini. “Nikitulia nitakutafuta
Jeff. Nakuahidi hivyo.” “Unajuaje kama wakati huo bado nitakuwa nataka
kukwambia hichi ninachotaka kukwambia wakati huu?” Nanaa akapooza.
~~~~~~~~~~~~~
“Nisije kuwa napiga teke bahati!” Nanaa akawaza akiwa
anafikiria. “Geb!” Wazo likamjia, akajicheka. “Mimi na
yule kiumbe! Haitakaa ikatokea. Tena heri nijiachie. Ana Liz kwenye maisha
yake. Tena asiyetaka wegazi. Heri nimchangamkie Jeff.” Nanaa akaanza
kushawishika.
~~~~~~~~~~~~~
“Kama nilikusikiliza kwa makini, basi huu ndio
mtaa wenyewe.” Jeff alimtoa kwenye mawazo. “Ndio hapa hapa. Lakini
nyumba ipo kwa nyuma ya hiyo barabara inayongia kulia. Sio mbali. Naweza
kutembea hata ukinishusha hapa.” “Usijali. Naweza kukupeleka tu. Labda iwe
unaogopa.” “Hapana. Nyumba yenyewe ina ukuta na geti, hakuna atakayejua hata
kama nililetwa na gari. Twende tu.” Jeff akafuata hiyo barabara mpaka wakakaribia.
“Ni nyumba ile pale.” “Kumbe unaishi kwenye geti kali?” Nanaa
akacheka. “Unaishi na nani tena?” Jeff akauliza. “Yule dada,
ambaye ni bosi wangu. Alisoma na kaka. Ndio kama ameniombea kwao.” Geb
hakutajwa. “Oooh!” Jeff akaitika.
Ilishakuwa saa 12:20 jioni wakati Jeff anaegesha
gari nje ya geti la Geb. “Nakushukuru sana Jeff.” “Anytime!” Jeff
akajibu na kunyamaza. Nanaa akabaki akifikiria pale pale kwenye kiti kabla ya
kushuka. Jeff naye akabaki akimtizama. Nanaa alikuwa kwenye wakati mgumu sana.
Hajui chakufanya. “Nitakupigia.” Nanaa alivunja ukimya. Jeff
akacheka. “Kweli nitakupigia.” “Sawa.” Jeff akajibu na
tabasamu. “Mbona kama huniamini tena?” “Kwa nini tena? Mbona mimi
nimekubali yote! Au nilitakiwa kufanya nini?” Nanaa akanyamaza kwa
muda. “Najua nimekuwa kama… kam.. Ila naamini umenielewa.” Nanaa
alianza kujing’ata ng’ata. Jeff akabaki akimtizama tu. Wazi alionekana
alishakata tamaa. “Usiku mwema.” Nanaa akaamua kuaga. “Na
wewe Nanaa.” Akashuka.
~~~~~~~~~~~~~
Alimkuta Grace anaandaa chakula jikoni. “Pole
na kazi.” “Asante. Vipi huko?” “Kwema tu. Mama ameshakwenda kulala?”
“Nimemuomba akae na Fili huko chumbani ili nipike. Fili akiwa na mimi anadeka
kweli! Siwezi kufanya kitu chochote. Anataka niwe na yeye tu.” Nanaa
akacheka. “Niachie basi mimi nimalizie kukupikia wali. Naona umeshaivisha
mboga zote.” “Hapa nilikuwa nawaza kama nipike wali au nimtume Danny akanunue
chapatti kule kwenye mgahawa wa mwarabu. Wanakuwa na chapati nzuri.” “Basi
wakati unafikiria hivyo, ngoja nipike wali wa maua hata kidogo tu. Mtachanganya
na chapati.” “Hayo ndiyo mambo.” “Lakini nataka nikamsalimie mama kwanza.
Najisikia vibaya nimechelewa!” “Wala usijali na wala hujachelewa. Bado mapema
kabisa.” Wakatoka wote wakaongozana mpaka chumbani kwa bibi Fili.
Alimkuta Geb na Fili wote wapo kitandani kwa bibi
Fili. Fili anaongea, wao wanamsikiliza ila Geb akiwa amefunika uso na mkono
wake. “Samahani nimechelewa.” “Mbona mapema tu! Umepata muda wakutosha na
wenzako kweli? Ni kama umekimbia kimbia tu.” Bibi Fili akauliza. “Nimeona
kwa leo inatosha.” “Naona mambo sio mabaya Nanaa mwanangu.” Nanaa akacheka
na kuuliza. “Kwa nini mama?” “Umesema kwa leo inatosha.” Nanaa
akajisikia aibu. “Namaanisha jumamosi ijayo nitawahi kutoka hapa na kuwahi
kurudi.” “Jeff huyo!?” Nanaa akacheka mpaka akatoka pale chumbani.
“Nanaa! Njoo nikwambie kitu.” Nanaa
akarudi. “Abee mama!” Nanaa aliitika. Bado Geb alikuwa amelala
chali, vilevile amefunika uso kwa mkono mmoja kama aliouegemeza huo mkono juu
ya kipanda uso chake, ukafunika sehemu ya macho, na kiganja kuning’inia pembeni.
Kimya, hata hakumsemesha Nanaa tokea aingie pale.
“Geb amekutayarishia chumba chako. Twende
nikakuonyeshe.” Nanaa akabaki kama haamini. “Mimi!?” Bibi Fili
akacheka kidogo. “Samahani mama. Sijak..” Akashindwa kuendelea,
akanyamaza na kuinama. “Ndio ujue tunataka ubaki hapa. Twende nikakuonyeshe.” Bibi
Fili akatoka pale kitandani, wakaongozana mpaka kwenye hicho chumba.
Kilikuwa kikubwa, kisafi, kitanda kimetandikwa
vizuri, na vitu vyake vyote vilikuwa humo. “Naona mmenitandikia mpaka na
kitanda!” “Grace na Geb ndio walikuwa wanasaidiana.” Nanaa alisimama pale,
akashangaa machozi yanamtoka. “Asanteni mama.
Nashukuru kunipokea. Nitajitahidi kutafuta chumba kwa haraka ili niwapishe
hapa.” “Wewe usijali. Tulia
hapa mpaka utakapo jiweka sawa.” “Asante
mama yangu. Nashukuruni sana.” “Sasa nimesikia kuna wali
maua.” Nanaa akacheka nakufuta machozi. “Nausubiri kwa hamu.” “Sawa
mama yangu. Ngoja nikapike.” Mama G akatoka. Nanaa akabadili nguo kwa
haraka. Alivaa gauni la kawaida tu. Akarudi jikoni.
~~~~~~~~~~~~~
Bado Geb alikuwa amejilaza kwenye kitanda cha
mama yake, akiwa kimya vile vile. Tayari walishajua hasira zile ni za wivu, na
hawezi kujisaidia. Mama yake akarudi tena pale kitandani. Hakuwa ameongea kwa
muda mrefu na wala hakuwa amefungua macho japo alijua wazi hajalala. “Upo?” Mama
yake akamchokoza. Geb hakufungua macho, kimya. “Geb Magesa! Najua
hujalala.” Mama yake akaendelea. “Nenda basi kanywe hata maji huko
jikoni.” Kimya. “We Geb!” Mama yake akaita kwa ukali.
Akafungua macho. “Lazima utoke hapo kitandani. Kulala hapo haitakaa
ikasaidia kitu. Haya nyanyuka.” Geb akatoka pale kitandani. Akiwa ameelewa
mama yake alichomwambia.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alishaanza kutayarisha vitu vya kupika.
Alitaka kupika wali wa kukaanga na kitunguu maji, na kitunguu swaumu. Ili
baadaye aje aweke njegere na karoti. Kulikuwa na tui la nazi limebaki kwenye
friji, akajua atalitumia hilo hilo. Akalitoa na kuweka jikoni ili lipate moto,
huku akianza kukaanga kitunguu. Moto aliweka mdogo, ili aweze kuendelea kutayarisha
vitu vingine kama kumenya vitunguu swaumu, njegere na karoti huku akipika.
Aliendelea kufanya mambo yake kwa haraka ili asiunguze na asicheleweshe
chakula.
Geb akaingia. Nanaa alishindwa hata kugeuka
sababu ya ubusy wa pale jikoni. Akaendelea kushika hiki, koroga pale, kata
hiki, punguza moto upande huu wa jiko hilo refu la gesi lenye sehemu 4 za
kupikia. Akili zote zikawepo pale jikoni asiunguze chakula cha kwanza kupika
ugenini. Wala asijue ni nani ameingia na nani ametoka.
Geb akasimama pale kwa muda. Akahisi kupuuzwa.
Akatoka kwa hasira za wivu na kurudi kwa mama yake. Akajitupa kitandani. “Nimeshakunywa
maji.” “Geb Magesa!” Mama yake akajua mambo hayakwenda kama
alivyotaka. “Kwani wewe huwezi hata kukata kitunguu, jamani!?” Geb
akacheka kama aliyepata wazo, na kutoka tena pale kitandani. Alimsikia mama
yake akimcheka nyuma. Akarudi na kumbusu. “Muone!” Mama yake
alimtizama kwa macho ya kumsuta. Geb akacheka na kurudi tena jikoni.
Geb kwa Nanaa.
A |
kafungua
tena mlango, pia Nanaa hakugeuka. Akajisogeza. “Naona upo busy! Nikusaidie
nini?” Nanaa akageuka, akamuona Geb. “Pole na safari.” “Asante.”
“Umepata muda wakutosha wa kupumzika?” Nanaa akauliza kwa kujali na kumfanya
Geb ajisogeze karibu zaidi ya pale alipo. “Nitalala baadaye.” Nanaa
bado alikuwa akichanganya viungo. “Kunanukia vizuri.” Geb
akasifia. “Utakula kidogo?” Nanaa akauliza huku akicheka. Akijua wazi
Geb hawezi kula. Geb alitabasamu nakushindwa kujibu. “Kwanza ulikula chakula
mama alichokupikia?” “Nilikula. Naona inatosha. Baadaye naweza kuongezea uji
kidogo, naona itatosha tu.” Nanaa akamwangalia.
“Ulisafiri lini?” “Niliondoka alhamisi.” Geb
akajibu. “Niliona kimya!” Nanaa aliongea kwa kulalamika kidogo. “Kwa
nini hukuuliza?” “Sina namba yako Geb.” Geb akamwangalia. “Nilikuomba
msamaha. Unakumbuka?” Geb akacheka kidogo. “Hukuona umuhimu wa kuwa
na namba yangu Nanaa. Kama ujumbe haukuleta maana, ungefuta ujumbe na kutunza
namba.” “Nikikwambia najutia, utaamini?” Geb akatabasamu kama asiyeamini.
“Kweli. Hata siku ile uliponishusha nyumbani,
nikataka kukuuliza kama mlifika nyumbani na mtoto salama, lakini
nikashindwa. Jumapili siku nzima nilikuwa nataka kukujulia hali lakini
nilishindwa. Sikuwa na namba yako. Nikajua labda hata ungenitumia ujumbe
mwingine. Lakini nikaona kimya!” “Ningejuaje kama wa safari hii
ungejibiwa?” Nanaa akanyamaza kidogo kama anayefikiria, kisha akakubaliana
na hoja yake. “Ni kweli. Lakini nimefurahi umerudi salama.” Nanaa
akarudi kupika.
Geb akabaki amesimama pembeni yake akimwangalia.
Alipochanganya kila kitu kwenye sufuria, akafunika na kupunguza moto. Alikwenda
kwenye friji akamimina juisi kwenye glasi akamkabidhi Geb. “Asante.” Geb
alipokea na tabasamu la furaha ya kujaliwa na Nanaa. “Ametengeneza
Grace.” Nanaa aliongeza. Wakakaa pale pale jikoni.
“Mbona sasa wewe haunywi?” “Nimeshiba. Nimekula
muda sio mrefu.” “Ulienda kukutana na Jeff?” Geb akauliza swali la moja
kwa moja. Nanaa akababaika kidogo. Akashindwa jinsi ya kujibu, akaona anyamaze. “Nilifikiri
nilisikia ukisema moyoni hujisikii. Mambo yalibadilika?” Geb
akaendelea kudadisi. “Jeff ni rafiki wa mpenzi wake Zena, ambaye ni rafiki
yangu mimi. Na walikuwa pamoja.” “Kwa hiyo ulikwenda kwa Zena, ndio ukakutana
na Jeff bila kujua?” Nanaa alijua anategwa. “Nilijua na Jeff
angekuwepo, Geb. Nikaona ni wakati muafaka wa kuwashirikisha uhitaji wangu wa
chumba. Endapo watasikia sehemu kuna chumba kinapangishwa, basi waniambie.”
“Kwa hiyo?” Geb akaendelea kuhoji.
“Wameniambia kuna nafasi mahali.” “Kwa Jeff?” Geb
akarusha swali jingine, Nanaa akanyamaza. “Nanaa? Ni Jeff ndiye aliyekwambia
ananafasi ya kukuweka?” Geb akarudia tena. “Ndiyo. Alisema
anasehemu kubwa tu yakuishi. Naweza kwenda kuishi naye kwa muda wakati nikijipanga.” Geb
akabaki akimtizama. Walikuwa wamekaa karibu, kwenye meza ya jikoni. Nanaa
akainama.
“Nanaa?” Geb akamuita kama kutaka aendelee.
“Nilimkatalia Geb.” “Kwa nini ulikataa?” Geb aliendelea kuhoji. “Simfahamu
na yeye pia hanifahamu!” “Kwa hiyo mmepeana muda wa kufahamiana?” Nanaa
akanyamaza kwa muda huku ameinama akichezea ganda la kitunguu swamu. Akanyanyua
macho, akakuta bado Geb akimtizama. “Nilimkatalia msaada wa kuhamia
nyumbani kwake. Nilimwambia kwa sasa ninapo sehemu yakujishikiza. Ila msaada
ninao hitaji ni kusaidiwa kutafuta kwangu. Kwa hiyo kama akisikia kuna chumba
kinakodishwa mahali, anifahamishe.” “Unafikiri itakuwa na tofauti gani kama
yeye akikusaidia kutafuta hiyo sehemu? Si yatakuwa ni yaleyale tu! Atakuwa
anafahamu unapoishi, au kule kujua yeye ndiye amekutafutia sehemu unayoishi!
Kwanza utajuje kama atakapokutafutia sio nyumbani kwake? Yaani ukajikuta
unaishia kuishi naye nyumbani kwake!” “Sikuwa nimefikiria hivyo.” Wakanyamaza
kidogo, Nanaa akanyanyuka kwenda kugeuza wali.
Akasafisha ile sehemu aliyokuwa akitumia. Huku
Geb ametulia kimya kwenye kiti akiendelea kutafakari. Nanaa akaanza kusuunza
vyombo alivyokuwa akitumia huku akivipanga vizuri kwenye dishwasher. “Naona
wali unakaribia kuiva.” Akamgeukia Geb aliyekuwa amekaa tu pale kwenye
kiti akinywa juisi yake taratibu.
“Onja hata kidogo.” “Umeweka vitu vingi sana
Nanaa! Mimi nikishaona karoti hivyo. Au njegere zinaniangalia kwenye wali,
nachanganyikiwa kabisa nakushiba hapo hapo.” Nanaa akacheka. “Kidogo
tu. Funga macho, halafu fungua mdomo, mimi nitakuwekea. Tafuna, halafu
uniambie.” “Nanaa!” “Kweli tena.” “Basi toa karoti, njegere. Hakikisha kitunguu
hakiingii kwenye kicho kijiko kimoja utakachokiweka mdomoni kwangu.” “Sasa hapo
si utakuwa unakula wali mweupe, wakati mimi nimepika wali maua!?” “Mimi hata
wali mweupe huwa sipendi.” “Basi.” Nanaa akageuka.
“Lakini sio kwamba sitaonja huo unaopika!” Akamsikia
Geb akiongea kwa haraka kama aliyejirudi na kusimama. “Sio lazima. Ni sawa
tu.” Nanaa alijibu kwa upole. “Nataka kuonja.” “Kwa nini, wakati
umeshasema hupendi? Acha tu.” “Nanaa!” Geb akamsogelea. “Naomba
kuonja.” Nanaa akamgeukia. “Hamna haja. Kweli tena. Ni sawa tu.”
“Nanaa! Labda kama unaninyima.” “Unajua siwezi kukunyima Geb. Lakini
nimejua sio kitu ambacho ungependa hata kujaribu! Yaani umeshakataa kwa
kukiangalia tu. Na kitu chochote ukishakikatia tamaa mawazoni, huwezi kukikosea
kasoro. Ukila tu huo wali, hutakosa sababu. Acha tu.” Geb alijiona
amekataa bahati ya kulishwa. Tayari alishaanza kujutia kukataa bila kufikiria.
Akajua hasira za wivu ndizo zilizokuwa zikimsumbua wakati akijibu. Hofu ya kuwa
Jeff anamzidi mahesabu ilimwingia. Anaonekana anataka kumtoa Nanaa pale ndani! Hilo
lilimuudhi zaidi Geb na kushindwa kujizuia.
“Samahani Nanaa. Nimekukatalia bila kufikiria.” Nanaa
akatabasamu. “Ni sawa tu. Usijali.” Alijibu kwa upole. Wakabaki kimya
hapo hapo karibu wakiwa wamesimama. Nanaa ameangalia chini, Geb akimtizama
karibu yake. Ukimya wa muda ukapita, Nanaa akagutuka. “Ngoja nianze
kupakua, niweke mezani. Njaa zitakuwa zinawauma.” Akageukia kwengine
nakuanza kutoa vyombo kwenye makabati, akatoka navyo nje na kumuacha Geb
amesimama palepale. Akaanza kupanga kwenye meza ambayo huwa wanakula kwa
pamoja. Akaandaa kila kitu hapo mezani mpaka akaridhika.
Ndipo akaenda kumuita bibi Fili au Mama G kama
wengi walivyozoea kumuita, wote wakakaa mezani. “Naona kinavutia kwa
macho.” Nanaa akacheka. “Asante mama. Lakini mimi bado nimeshiba.
Nitakula kiporo kesho kama kitabaki. Naenda chumbani kuoga. Nitoe harufu ya
vitunguu.” “Sidhani kama utabaki.” Mama G akajibu na kufanya Nanaa
acheke. “Asante Nanaa. Naona wali unavutia!” Grace naye akashukuru
wakati anampakulia mumewe. “Asante kushukuru. Nitakuwepo hapo chumbani.
Nitatoka kusafisha meza na vyombo.” “Wala usijali. Tutamalizia tu.” Nanaa
akaondoka.
Kiujazacho
Moyo.
S |
iku
inayofuata ilikuwa jumapili. Nanaa akaamua kurudi nyumbani kwa kaka yake ili
kusalimia wageni. Hakumkuta kaka yake, akajikuta ameishia mikononi mwa Mama
yake mkubwa na Viola. Alijuta hata kwa nini alikwenda bila taarifa. Walimpa
wakati mgumu sana. Mama yake mkubwa alimsema kwa maneno ya kumnyanyasa mpaka
alipomaliza roho yake ikatulia. Akamfukuza rasmi hapo nyumbani kwa mwanae
James.
Nanaa akatoka akatafuta sehemu karibu kidogo na
kituo cha daladala, akakaa hapo akiwaza. “Jeff anaweza kuwa suluhisho
la kudumu. Nikimkubali, naweza nikapata mkombozi wangu. Nikaepuka
maneno.” Nanaa akawaza akiwa amekereka sana rohoni. “Lakini
nikiwa na Jeff, sijisikii vizuri kama ninapokuwa na Geb, mchumba wa mtu!” Nanaa
akajirudi na kuanza kujichanganya tena mawazoni. “Alikuwa wapi huyo Jeff
siku zote jamani!?” Akalalamika. Alikaa pale akiwaza bila kufikia
muafaka, mwishowe akaamua kurudi nyumbani kwa Geb akajifikirie zaidi.
~~~~~~~~~~~~~
Aliingia ndani mida ya saa 11 jioni, akawakuta
wote wamekaa sebuleni. Mpaka Liz alikuwepo. Tena alikaa pembeni ya Geb. Fili alikuwa
amepakatwa na baba yake. Aliingia hapo akionekana kabisa hana furaha. “Kwema?” Grace
akamuwahi. “Kwema. Nimchukue Fili nikamuogeshe?” “Geb alishamuogesha,
amekula, hapo baba yake anambembeleza alale, kesho shule.” “Ooh! Nimemchelewa
Fili wangu!” “Nenda kachukue chakula, nimekubakishia.” “Labda nisafishe tu,
sitakula.” Nanaa alimjibu Grace huku akielekea jikoni. Alikuta jiko
limeshasafishwa, akatoka. “Naona kupo kusafi. Basi na mimi naenda kulala.”
“Mbona mapema? Njoo tukae kidogo.” Nanaa akasimama pale kimya kwa muda
kama anayejishauri, lakini alijawa simanzi moyoni, akashindwa kujichanganya nao. “Naomba
mimi nitangulie tu. Naona nimechoka!” Nanaa akajibu kwa upole, akaelekea
chumbani.
~~~~~~~~~~~~~
Picha ya Liz akiwa amekaa pembeni ya Geb ilipita
kwa haraka mawazoni. Akatulia. Kisha maneno ya mama yake mkubwa yakaanza
kumrudia na kukubali kuwa kweli yeye ni tatizo sugu. Aliona hastahili kuwepo
pale. “Naona nimeanza hata hisia zisizo sahihi kwa mchumba wa mtu!
Wenyewe wanapendana! Mimi nimejaa humu ndani. Geb anahangaika kutengeneza
chumba, akashindwa hata kupumzika!” Aliona vile anavyosumbua watu,
akazidi kujisikia vibaya. Lazima kutafuta suluhu ya kudumu.
Akaingia kuoga, akatoka na kubaki amejilaza
kitandani. Baada ya kuwaza hili na kushindwa kupata majibu, huku Jeff
akionekana ndio suluhisho la kudumu akaamua alale tu. “Sijui nimpigie
Jeff? Nitamwambia nini? Nirudie maisha yaleyale ya zamani? Kukimbilia wanaume
sababu ya sehemu ya kuishi?” Nanaa akaanza kulia gizani. Wivu wa
kumkuta Liz pembeni ya Geb, na maneno ya mama yake mkubwa yalizidi kumliza.
Asijue atafanyaje. Alilia huku akiangalia simu yake akitamani ampigie simu
Jeff, lakini moyo ulizidi kusita. Alilia taratibu pale gizani, asijue
chakufanya.
~~~~~~~~~~~~~
Akasikia hodi mlangoni, akakaa na kujiweka
sawa. “Karibu.” Mama G akafungua
mlango. “Mama!” Nanaa akafuta
machozi. “Niwashe taa?” Mama G akauliza kiustarabu. “Washa tu.” Akawasha akamsogelea kitanda
alipokuwa amelala Nanaa. Akaweka juisi kwenye mezani ndogo iliyokuwepo pembeni
mwa kitanda. “Mbona unalia?” Akamuuliza. “Sijui nifanyaje mama! Hata sielewi.” Mama G,
akakaa. “Nini kinakusumbua?” Akauliza kwa utulivu, akisikika kujali.
“Nachukia haya maisha yangu mama.
Nitakuwa hivi mpaka lini? Nitazunguka kwenye majumba ya watu mpaka lini?
Natamani kutulia. Natamani na mimi kuwa na kwangu. Jeff….” Akakwama. “Nakusikiliza
Nanaa. Ongea tu usiogope.” “Jeff anaonekana ni
muugwana na ana uwezo mzuri tu. Anaonekana angeweza kunioa. Nikaanza
maisha yangu nakuacha kusumbua watu wengine.” Nanaa alijieleza huku
machozi yakimtoka.
“Umeshafikiria baada ya ndoa? Yaani ameshakuoa,
amekupa sehemu ya kuishi. Maisha yako yatakuaje?” Mama G akauliza
swali la msingi akionekana ametulia kabisa. “Hilo
ndilo tatizo, mama yangu. Nimekuwa nikifanya kosa hilo hilo. Kukubali wanaume
sababu ya kupata kimbilio. Nimechoka mama yangu. Nikaamua kupumzika. Nitulie
pale kwa kaka. Lakini sasa hivi tena ndio mambo yametibuka. Mama mkubwa
amenifukuza rasmi pale kwa kaka. Hataki hata nirudi kusalimia. Nitafanyaje? Na
Jeff naye ndio anaonekana mkombozi wangu. Lakini mama, moyo wangu umemkataa
kabisa yule kijana. Sijui nitafanyaje?” Nanaa alikuwa akiongea naye
kana kwamba wanafahamiana kumbe ni kufika mwisho, hana jinsi.
“Samahani mama. Najua nakwambia
mambo yasiyo kuhusu. Lakini sina mtu wa kuzungumza naye?” “Nisikilize Nanaa. Kwanza
nimefurahi kuwa umeweza kuniamini na kunishirikisha. Pili, kuna usemi huwa
wanasema, ‘Don’t make permanent decision for temporary problem’.
Unanisikia Nanaa?” “Nakusikiliza mama.” “Ehee!
Tulia kabisa. Mungu amekuleta hapa kwa makusudi. Nakuomba hapa uwe huru.
Usijisikie kuwa una haraka yakuondoka. Utakapokuwa tayari ndio uondoke. Kwanza
wewe bado mwanafunzi. Fikiria shule na hiyo kazi uliyopewa. Basi. Naamini Mungu
atakupa maisha mazuri tu. Umesikia mama?” Bibi Fili alijaribu kumtuliza.
“Nashukuru mama. Asante.” “Yatapita tu haya. Tena
naona una mwanzo mzuri kuliko watu wengi sana. Vumilia, na ujipe muda.
Usikimbilie kufanya maamuzi utakayojutia baadaye.” Nanaa akatingisha
kichwa. “Tumuombe Mungu pamoja. Tumruhusu Yeye ndio awe msaada wako.
Kisha jiruhusu kuipokea siku ya kesho ukiwa na amani.” Nanaa alitoa
tabasamu. “Asante mama yangu.” “Haya
kaa vizuri tuombe.” Bibi Fili akamshika mkono Nanaa, akamuombea. Ilikuwa
sala fupi, lakini ilimfariji sana Nanaa.
“Asante sana. Umenitua mzigo mzito. Nilikuwa
sijui chakufanya!” mama G akatoa tabasamu la faraja. Kama mama kwa mtoto
wake wakumzaa. Hakika hakujua alichokifanya kwa Nanaa. Ndio mama wa kwanza
aliyeweza kukaa naye chini na kumfariji kwa kiasi kile. Yale maombi yalikuwa
kama barafu nzuri ndani ya moyo uliokuwa mzito ndani ya Nanaa. “Basi
kunywa hiyo juisi, ndipo ulale.” Mama G akatoka, na kumuacha Nanaa
amefarijika. Kwanza ni kama alimsaidia kumpa majibu ya maswali yake. Juu ya
Jeff na hisia zake. “Sina haraka tena. Nitamtafuta Jeff, nimpe nafasi
ya kumsikiliza. Kisha nimkatalie rasmi. Nijiruhusu kufikiria, na kujipanga bila
mtu nyuma yangu.” Nanaa aliwaza. Akalala akiwa na furaha.
Jumatatu!
Aliamka asubuhi hiyo akiwa na furaha zote. Alishafarijiwa
yeye sio mzigo pale na wenyeji wake zaidi mama G, amemuhakikishia anahitajika
pale sio kama alivyofukuzwa kwa kaka yake. Aliandaa kifungua kinywa, wakati
akimwangalia Mama G akimwandalia Geb uji wake. Akamsaidia Grace kumwandaa Fili,
wakaondoka mapema yeye na Grace na mwanae. Alifika kazini akiwa ametulia.
Akafanya shuguli zake, akaamua kumpigia simu Jeff!
“Unacheka nini sasa?” “Sikutegemea!”
“Kwa nini?” “Basi tu. Mzima wewe?” “Mzima. Naomba tukutane jumamosi.” Nanaa akaomba kwa
kujiamini akitegemea kusikia muhemko kutoka kwa Jeff lakini chakushangaza, ikawa
kimya. “Jeff!” “Nakusikiliza mrembo.” “Ndio
nimemaliza. Kama bado utataka kuniambia ulichotaka kuniambia. Na kama bado
sijachelewa.” Jeff akacheka. “Nimegairi
Nanaa.” Moyo wa Nanaa ulishituka, hakutegemea. Jeff akaendelea taratibu
tu. “Naona niache tu.” Nanaa alishindwa
hata chakujibu. Akabaki kimya mpaka Jeff akahisi simu ilikatika. “Nanaa upo!?” “Nipo Jeff. Samahani sana. Lakini naamini
utakuwa umepeta sikio jingine la kukusikiliza.” “Naamini hivyo. Asante.” “Haya.
Kila la kheri.” Nanaa akakata simu, asiamini.
~~~~~~~~~~~~~
“Daah! Mlango umeshafungwa hivyo. Sijui
niseme nimechezea bahati!?” Siku ikaanza kuwa ngumu. Kukataliwa kubaya! Jeff
alimfungia vioo kwa haraka sana. Hakutaka kuzungushana naye zaidi. Nanaa
alitamani yeye ndio awe wakumkataa, kuliko vile alivyokataliwa. Akamkumbuka
Geb. Akakumbuka Liz amekaba. “Nijipumzikie tu.” Akaazimia.
~~~~~~~~~~~~~
Jeff hakutaka kuzungushwa na
Nanaa. Mapemaaa, ameshamfungia mlango na nyumbani kwa kaka yake amefukuzwa
ramsi na mama yake mkubwa. Liz naye amekaba penzi la Geb. Mpaka Jumapili siku
hizi yupo nyumbani kwa Geb.
Je, amechezea bahati?
Usikose Makubwa, Yakusisimua,
Kushangaza, Kuburudisha, Kujifunza huko MBELENI.
0 Comments:
Post a Comment