Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 73. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 73.

 

Sabrina akaweka mambo sawa hapo ndani na kutoka kwa haraka kukimbilia saluni. Uzuri nywele alizokuwa amesuka kichwani kwa kadiri inavyokaa kichwani kwa muda mrefu, inajaa na kupendeza zaidi. Akaenda kuibadili rangi na kuongeza rangi ya dhahabu kidogo zaidi kwenye ncha. Kisha ikaoshwa na kurudishiwa mawimbi yake madogo. Ile rangi ya dhahabu ikachanganyikana na nyeusi. Halafu kwa kuwa alikuwa amekonda, akataka iachiwe tu, usibanwe kuziba uso ulioonekana zaidi kukonda. Kwa hiyo ile nywele ikashuka vizuri mpaka chini ya mabega. Ungependa kumtizama Sabrina jinsi alivyopendeza. Akatengeneza kucha, nyusi, ilimradi tu kesho yake atokee vizuri. Aliporidhika ndipo akarudi nyumbani maana Jack alimwambia atampitia ndipo waende naye kwao.

Jack alitoka kazini akaambiwa yupo chumbani na ameomba asigongewe kwa muda. Akajua anaomba. Na yeye akaliheshimu hilo akabaki sebuleni ameinama akimuhurumia mkewe. Akakaa hapo kama dakika 20 mbeleni, ndipo akatoka. “Vipi?” “Safi tu. Upo sawa?” “Kabisa. Nipe kama dakika 15 hivi, nipange timu yangu ndipo tutoke.” “Acha na mimi nibadilishe nguo kabisa.” Wakajiandaa wakati wanatoka Jack akamwangalia.

“Umependeza sana, lakini umechoka Brina wangu! Unakula kweli?” “Kesho ndio nitakula. Wala usijali. Nipo tu sawa. Twende sisi walengwa tusije chelewa.” Wakatoka. “Nakuahidi sitarudia tena Brina. Nimejifunza kwa uchungu sana.” “Nakuombea Jack.” Hivyo tu akajibu na kunyamaza. Wakatulia mpaka kwao, Sabrina akiendelea kuombea hata kikao cha jioni hiyo.

Wakati wanafika nyumbani kwao gari la Jacinta na la Junior nayo yakawa yanaingia. Sabrina akashuka na kuwasubiria. “Sasa sikiliza Sabrina, sio nilikwambia uwe unapania kila mahali!” Sabrina alicheka mpaka akainama. “Kwani nimependeza sana!” “Sana shem. Upo mzima lakini?” Junior akaongezeka. “Nipo mzima kabisa, shikamooni.” “Marahaba, ila midomo imekukauka bwana!” “Nakunywa maji sijui kwa nini! Labda kwa kuwa nailamba sana.” Sabrina akajibu akijilamba tena. Jack na yeye akasalimia. “Sasa mzee Msindai leo sijamsikia vizuri.” Junior akanong’ona. “Kumbe na wewe umemgundua eeh?” Jacinta akamuuliza kaka yake kwa kunong’ona. “Nimemsikia. Sasa naomba tuingie ili saa 12:30 itukute tumekaa sebuleni kwake, hivi nilimtanguliza Joy mapema, nikamwambia asichelewe, leo upepo sio mzuri sana.” Wakaingia wote wanne.

Wote wakasalimia. Walimkuta mzee Msindai, mkewe, Joy na Waili pia alishafika. “Jena bado hajafika?” Akauliza Junior akikaa. “Ameniambia yupo kwenye foleni, lakini anakuja.” Akajibu mama Msindai. “Pole na kazi, baba.” Junior akaendelea. “Asante.” “Wakati tunamsubiria Jena, nikuletee chai, baba mzazi?” Jacinta akamuuliza. Mzee Msindai akatulia akifikiria, wakajua kweli hayupo sawa. “Amekataa. Dada amemuuliza mara mbili na kuamua kumletea kabisa kwenye sinia lake, amekataa amemwambia arudishe. Ndio maana unaona wote tuna vinywaji yeye hana.” Akajibu mama yao kama anayejitetea. “Wakati wote chai huwa haikudanganyi baba yangu, mimi. Mimi naomba nikuletee.” Jacinta akasimama bila kusubiri jibu, akaenda kuleta sinia lilelile lililokuwa limepangwa tayari sukari, kijiko chake, chupa ya chai na kikombe anachokipenda kutumia mzee Msindai wakati wote wa chai.

“Mpaka hiki kikombe kikiisha, utajisikia vizuri.” Akammiminia kwenye kikombe na kijiko kidogo kimoja cha sukari kama kawaida ya baba yake. “Asante mama.” Mzee Msindai akashukuru. “Junior, naomba mpigie Jena, mwambie watu wote tupo hapa tunamsubiria yeye.” “Sawa, baba.” Junior akasimama na kutoka hapo kwa haraka. Baada ya muda mfupi tu akarudi. “Naona anaingia getini.” Kimya. Jack akabaki ameinama.

Sabrina akamsugua mgongoni na kucha, akamgeukia akiwa vilevile ameinama. “Nikuombee chai?” Sabrina akamuuliza kwa kunong’ona. “Hapana. Asante. Wewe hutaki?” “Tena ipo nyingi tu huko jikoni. Tumeandaa kabisa na chakula ili mle mkiondoka hapa mmeshiba ni kwenda tu kulala.” “Asante mama. Shem nikuletee na wewe kikombe? Najua wifi yangu yeye atataka glasi ya wine.” “Hapa nilikuwa najikaza tu. Maadamu umeamua kutukarimu wifi yangu, glasi itahusika.” Jacinta akadakia yeye. “Basi na mimi niombe glasi. Joy atakuwa dereva wangu leo.” Sabrina akasimama akicheka.

“Na wewe Joy?” “Kama hujaelewa ndio nimeambiwa mimi nisinywe ili nimuendeshe.” Wote wakacheka. “Sijasema hivyo bwana Joy!” “Wewe ushanichagua nikuendeshe, sasa mimi nakunywaje?” “Labda kwa sababu ya majukumu yako ya kesho.” Kila mtu akazidi kucheka. “Wewe huendi kazini kesho?” “Asante baba.” Joy akafanya wazidi kucheka. “Mimi nakunywa glasi mbili tu, baba. Haziwezi kunishinda kuamka asubuhi.” Angalau kidogo kukachangamka. Waili kimya.

Jena akaingia. “Samahani baba. Nimekutana na foleni, nimechelewa.” “Kwa kuwa umechelewa kuanza safari ya kuja hapa.” “Nilikuwa na mgonjwa baba yangu. Niliona ni bora…” “Ndio maana nimesema hukuchelewa barabarani ila ulichelewa kutoka kazini, na wakati nilishakwambia umuhimu wa hiki kikao! Junior mwenyewe imembidi aahirishe majukumu yake, leo awepo nchini kwa ajili ya hili! Ninapotoa muda na kutaka wote muwepo si kwa sababu nimebuni tu muda, Jena. Kila mmoja yupo hapa akiacha majukumu mazito yanayotukabili kwa kuokoa fujo ulizomsaidia mdogo wako kuziendeleza huko mtandaoni.” Watu wakajua huo usiku ushakuwa mchungu kwa hao waliotajwa.

“Samahani baba yangu. Leo sikutaka kukuudhi zaidi. Nilijua kwa hakika mimi ndio ningekuwa wa kwanza hapa. Nisamehe baba.” Jena akajishusha na kusikika kama Jacinta kwa baba yake. “Sasa na wewe Sabrina si unywe hiyo chai, itapoa! Yamoto itasaidia maziwa. Midomo imekukauka sana. Kunywa. Au nimwambie dada akuletee yamaziwa?” Mpaka Jacinta akakunja uso. “Nashukuru mama, asante. Naona hii ya rangi anayopenda baba itanifaa na mimi. Nashukuru.” “Ongeza kula. Kazi yakunyonyesha dume sio kazi ndogo!” Mama Msindai akaendeleza kuongea na Sabrina ili kumtuliza mumewe. “Na naona ana kazi ya kula tu, mpaka mashavu yamekutana na shingo!” Sabrina akajibu kidogo pakatulia.

“Ila umependeza! Umekua kama kamodo!” Mpaka Jack akanyanyua uso na kumtizama Jena. Junior na Jacinta wakabaki wamehamaki. Ni kama Sabrina na yeye hakutegemea akashindwa kujibu kwa haraka. “Halafu aina hiyo ya nywele pia nzuri! Imekupendeza sana wifi yangu. Na kwa kukuomba msamaha nimekuletea pochi nzuri hiyo! Najua lazima utaipenda tu. Sema nimeiacha kwenye gari kwa haraka ya kuwahi hapa ndani.” “Mimi naomba kwa heshima zote, baba, mruhusu huyu maneno mengi akalete hiyo pochi.” “Jacinta unanianza!” “Wewe usitake ugomvi na mimi, kalete pochi.” “Sasa unafikiri nadanganya?” “Wewe ungeacha maneno mengiiiii! Muombe baba, ukalete hiyo pochi kama kweli ipo.” Junior naye akaongeza kwa Jacinta. Akamwangalia baba yake. “Naomba ufanye haraka Jena.” Jena akasimama kwa haraka na kutoka nje.

“Hakika ningejua leo, ningekuja na mwamvuli wangu.” Mpaka Joy akacheka. “Kwamba mvua itanyesha, wifi?” Joy akauliza akicheka. “Tena ile ya radi kabisa!” Junior akazidi kucheka. Kweli Jena akarudi na mifuko mizuri tu ameshika mkononi. “Hii hapa pochi ya wifi yangu, Sabrina. Na vibanio vya anti zangu wale mapacha wa Msindai. Keiline na Jeiline.” “Baba ataniazima mwamvuli wake.” Wakazidi kucheka. “Na sijamaliza. Hivi hapa ni vya mrembo Claire. Na huu mfuko huu pia ni wa....” Akachungulia ndani. “Eehee! Hizi nguo za ndani za dada Claire na hizi nyingi za mapacha wetu. Jeiline na Keiline.” “Asante Jena mdogo wangu.” Junior akashukuru, Joy akabaki ametoa macho.

“Leo mpaka nimeitwa mdogo wangu!” “Uwe unaleta hivi zawadi mara kwa mara dhambi zako zinakuwa zinasamehewa.” Watu wote wakacheka. “Mimi nimeshasema nimebadilika. Halafu haka kamfuko kadogo haka, ka mamilioni ya pesa, ni kababa mzazi.” Mzee Msindai akacheka na kutingisha kichwa. “Hapa mimi leo siondoki baba. Nalala hapahapa. Kesho navaa nguo za mama kwenda kazini.” Jacinta akafanya wakazidi kucheka. “Wifi unaogopa hata kutoka?” “Hakika leo ni mvua ya mawe!”

“Sijali maneno yako Jacinta. Hii saa ya baba. Baba yangu amenihangaikia sana, mpaka nimepata ile nafasi!” Mpaka mama Msindai akasimama na kushangilia. “Kweli Jena?” “Waziri wa Afya mwenyewe amenipigia simu, wameniambia katika wanawake tuliofanya usahili, mimi peke yangu Reseach yangu imepita. Ila kwa ajili ya kushika hiyo nafasi, nahitajika kwenda kusoma kwa miezi 6 tu kama kujiweka sawa, nikirudi ndio nakabidhiwa rasmi kitengo cha mambo ya moyo kwa upande wa watoto.” “Sasa utakwenda!?” “Sina kinachonizuia mama yangu. Kwa nini nisiende tu? Nitakwenda. Nimefurahi, nikasema nitamwambia baba nikija sio kwa simu, maana ndiye aliyehangaika na mimi kwenye kukusanya Data, kupitia Reseach Papers zangu, akizisahihisha bila kuchoka. Kila niliporekebisha makosa na kumrudishia asome tena na tena wala hajawahi kunikatalia, mpaka akaridhika. Halafu bado akanifanyia mazoezi kitu cha kuzungumza nao hao walionifanyia usahili ili kuwavutia na wanichague mimi. Akawa akinifanyia mazoezi mpaka nikaweza. Asante baba.” “Hongera sana.” Mzee Msindai akampongeza na kupokea hiyo zawadi ya saa.

 “Na nikirudi tu nchini tunafungua kitengo chetu cha mambo ya moyo kwa watoto pale kwenye hospitali ya baba!” “Mama huyu kapata mukari mpaka anapangia mahesabu pesa ya baba bila kumuuliza mwenyewe kama yupo tayari na kitengo cha mambo ya moyo!” “Aliniambia baba mwenyewe wakati nilipoenda kusomea mambo ya moyo. Aliniambia nikifanya vizuri huko chuoni, anaweza kuongeza kitengo cha mambo ya moyo pale hospitalini kwake, halafu akaniachia mimi nikiendeshe. Ila niliporudi nchini ndio nikawa na mambo mengi. Ila sasahivi nishakuwa mtoto mzuri. Sasahivi sifanyi tena mambo yakumuudhi bab..” “Na kila mtu.” Wote watatu wakadakia kwa pamoja.

“Wewe unakera kila mtu Jena.” “Jacinta ujue wewe umenikazania wewe! Unataka kunianza! Baba unamuona Jacinta?” “Sasa nyinyi wawili msianze kuchafua hali ya hewa hapa.” Mama Msindai akawawahi. “Ni Jacinta huyo! Anataka kunikorofisha bila sababu! Mtu nishasema nimebadilika lakini…” “Hata ukipewa kitengo na baba pia, ubakie hivyohovyo. Usirudi kule kubaya. Maana sio uwe mwema sasahivi ili kumfanya baba akuamini, halafu ukishakabidhiwa kitengo huko kwenye hospitali ya Msindai…” Jena akaanza kulia. “Kwa nini hamumpi mwenzenu nafasi jamani!? Eti Junior?” “Mimi namtahadharisha mama.” “Hapana Junior. Mtieni moyo. Sio mumzodoe. Amejirudi kwa kila mtu, bado mnashindwa kutambua jamani! Si sawa.” “Nimekosa mama. Samahani.” Junior akajirudi kwa haraka.

“Jena mdogo wangu, naomba msamaha.” “Wewe hunipendi Junior, tokea zamani unampendelea Jacinta. Mnanitenga kwenye kila kitu! Kila nikifanya jambo zuri wewe huoni, unaona mambo ya Jacinta tu, tokea zamani sisi ni wadogo. Mimi sijui niliwafanyia nini!” Jena akaongea kwa uchungu akilalamika na kulia. “Kila jambo unamsifia Jacinta, lakini sio mimi! Halafu kwenye kila jambo la Jacinta unakuwepo lakini mambo yangu mimi huwa unatoa udhuru.” Akendelea kulalamika. “Kila mtu alikuja kwenye mahafali yangu ya kuhitimu mambo ya moyo, lakini wewe hukuja Junior. Na nilimwambia mama kabisa, ingekuwa ni Jacinta, ungeahirisha kila kitu kuhakikisha unahudhuria.” Akatoa mifano mingi akisema Junior anavyompendelea Jacinta kuliko yeye.

“Kila siku unaonekana unatoka na Jacinta, mimi hamniiti! Mnanitenga kama mimi sio ndugu yenu! Mnanifanya nakuwa peke yangu naishia kuwa na mama tu! Kila siku, kila mahali unakuwa na Jacinta sio mimi.” Jena akaendelea kulia akilalamika. Jacinta naye akanyamaza kimya akiendelea kunywa. “Basi Jena, mdogo wangu. Kwanza nashukuru kuniambia. Naomba msamaha, na ninakuahidi nitaongeza umakini kwako. Ila ujue Jacinta huwa sitoki naye. Jacinta anatoka na mke wangu, halafu anaishia kunipigia simu…” “Aje alipe.” Akamalizia Joy, wote wakacheka.

“Kweli baba. Yaani ukitoka na Jacinta ujue umetoka na Junior. Wine zikishamuingia tu kichwani, simu kwa kaka yake.” “Na samaki wa kuchoma kwa baba yake.” Mama Msindai akaongeza na kufanya wazidi kucheka. “Samaki wa kuchoma na ndizi, hivyo vinaagizwa akishalewa. Sasa Junior huwa anamwambia, baba sasahivi atakuwa ameshalala. Hapo huna utakachomwambia wifi yangu. Ataagiza viletwe, na maagizo yake ni yaleyale, kamkabidhi mlinzi getini, akagonge usiku huuhuu dirishani kwa mzee Msindai, amwambie kitoweo kutoka kwa mama mzazi.” “Basi hayo maagizo hata saa sita usiku utayasikia dirishani. ‘Kitoweo kutoka kwa mama mzazi.’ Basi najua yupo baa tu.” Akamalizia mama Msindai wakazidi kucheka.

“Mimi naomba Jena mdogo wangu, unisamehe. Si nimesema nitaongeza umakini?” “Ndiyo.” Jena akajibu. “Basi tunaanza na kwenda kukupongeza kwa kupata kitengo. Unachagua popote unapotaka, safari hii Jacinta atalipia.” Kidogo kukaanza kutulia. “Na mimi naomba nikushukuru Jena. Binafsi nimechukulia ni jambo la kipekee na nimefurahia sana kwa zawadi yangu, na asante kwa zawadi za kina Jeiline na Keiline pia. Asante sana.” Sabrina akashukuru. “Karibu.” Jena akaitika akisikika ametulia.

~~~~~~~~~~~~~~

“Haya, naomba tuokoe muda, tumruhusu Waili aendelee. Kwanza tumeshatumia muda wake mwingi sana.” “Hakuna shida kabisa mzee wangu. Maana hiki kilichoendelea hapa ni muhimu sana. Kuwa ukurasa mmoja kwanza nyinyi kama familia. Zaidi kwa mke wa Jackson.” Sabrina akakunja uso kidogo. “Mnaweza msitambue umuhimu wake kesho, lakini kwa hiki kilichotokea kwa mumewe, uwepo wake yeye kama mke pale mahakamani, unanguvu sana.” Waili akaendelea.

“Kama mtakumbuka mwaka 1998, ile skendo aliyoipata aliyekuwa Raisi wa wakati ule nchini Marekani.” “Raisi Bill Clicton na yule mwanadada Monica Lewinsky?” Akadakia kwa haraka sana Junior na kuongeza. “Mimi nakumbuka na mpaka vile mkewe alivyosimama naye.” “Sawasawa Kiongozi. Na ile ilipunguza sana makali ya lile kosa lake. Jackson atakapotokea kesho na mkewe ambaye walijaribu kumchafua na kuwachonganisha mtandaoni, ile kuwaona tu pamoja wakiwa kwenye hiyo tu hali ninayowaona nayo hapa sasahivi. Hata bila kuzungumza kitu juu yao, itasaidia sana. Maana sehemu yenye upendo huhitaji kupatetea sana. Watu watawaona tu, na kuwadhoofisha walio kinyume nanyi. Nianze na Dokta Jena Msindai.” Akamtambua kwa heshima.

“Kama tulivyozungumza na yeye mwenyewe nataka na sisi hili litukae kichwani zaidi Jackson, kuwa hakuwahi kuandika kitu mtandaoni, akaunti zake zote walizi hack. Kwa hiyo huyo mtu aliyekuibia akaunti zako ndiye aliye kuwa akizitumia huko mtandaoni mpaka ulipojua ndipo ukazifunga zote. Sijui kama tupo pamoja?” “Nimeelewa. Hata hivyo mimi sikuwa mtumiaji sana wa akaunti zangu. Kwa hiyo nimeelewa.” “Kuna swali?” “Ndiyo.” Jack akadakia na kufanya wote wamgeukie yeye.

 “Karibu.” “Huyu Jena alimfuata Phina. Sijui walikutana wapi! Sijui nani waliwaona pamoja!” Jack akazidi kuweka hali ya wasiwasi akionekana wazi binafsi ameingiwa hofu ya kesho yake huko mahakamani.

“Jena na Phina hawajawahi kukutana. Unakumbuka Jena?” “Nakumbuka.” Jena akajibu. “Kivipi tena!?” “Jackson, naomba zingatia upande wako tafadhali. Ya Jena wewe hufahamu kama hivi unavyoniuliza, tafadhali ibakie hivyo.” “Ikitokea wananiuliza?” Jack akamuuliza Waili kwa mshangao mkubwa kama anayezungumza asichojua! “Nikuulize swali mheshimiwa Msindai?” “Tafadhali niite Jackson.” Jack akawa ameshakasirika.

“Samahani.” Sabrina akamkatisha. “Naomba utulie Jack. Nafikiri huyu wakili yupo hapa kukusaidia, na nahisi kama sijakosea anataka kukupunguzia mzigo. Naomba usikasirike.” “Nafikiri mkeo amenielewa kwa haraka sana.” “Ameanza na mimi muda mrefu sana, wewe hujui tu Sabrina. Imekua kama ananiadhibu! Maswali yake kwangu ni ya kunihukumu, kuliko kunisaidia!” Jack akazidi kupandisha hasira akiendelea kulalamika.

“Ameharibu siku yangu nzima kwa kunihoji kama yeye ndiye anayemtetea Phina na sio mimi! Na mimi nimechoka jamani! Ananihoji kama mimi ndio mtuhumiwa wakati anatakiwa kuwa upande wangu!” “Baba, naomba nizungumze na Jack kwa muda mfupi tu hapo nje. Hatutachelewa.” Ikabidi Sabrina kuingilia kati. “Sawa.” Ile mzee Msindai anamalizia kukubali, Jack alishafika mlangoni. Sabrina akanyanyuka na kumfuata. Ukimya ukazuka hapo ndani

~~~~~~~~~~~~~~

Usikose Sehemu Ya Mwisho Ya Simulizi Hii Kujua Hatima Ya Hukumu Ya Kila Mtu Na Makosa Yake.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment