“Naomba tulia, fuata
ushauri wake mpaka tuone mwisho wake. Unanielewa? Au wewe unafurahia hii
hekaheka ya kila siku familia yetu sisi ndio inakaliwa vikao?” “Ndicho
kinachoniumiza na kuona nimekuingiza wewe matatizoni zaidi!” “Kwa upande wangu
naomba usijali. Naomba wewe tulia, tumalize hili. Mbona litapita tu na watu
watatulia! Naona hili Mungu anaanza kulitumia kwa wema. Kile shetani
alichokusudia kutuangamiza nacho, Mungu ataendelea kukitumia tu. Naomba mpe
Mungu nafasi atusaidie. Tafadhali Jack.” “Sawa.” Wakarudi ndani, Jack
akaonekana ametulia kabisa.
~~~~~~~~~~~~~
“Upo tayari?” Waili
akamuuliza mara tu alipokaa. “Ndiyo.” “Kutokana na yote uliyozungumza, je, unazungumzia
nini juu ya ujumbe aliotuma dada yako, Dokta Jena Msindai huko mtandaoni
akimkaribisha Phina kwenye familia kwa niaba ya mama yenu?” Pakazuka ukimya
mkubwa hapo ndani, kila mtu kimya wakitaka kumsikia atakavyojibu juu ya hilo. “Mheshimiwa
Msindai?” Kimya. “Jamani, nawaandaa kwa maswali ya kesho maana Jena ni mmoja wa
shahidi wa Phina. Na atakapolazimisha lazima uhojiwe, ujue mahakama
itakulazimisha usimame kizimbani na ujibu. Tafadhali nataka kusikia jibu lako
Mheshimiwa Msindai ili nijue jinsi ya kurekebisha.” “Kwa nini hilo
hatukuzungumza mchana, Waili?” Jackson akalalamika.
“Halafu nimesema niite
Jackson.” Akagomba, Sabrina akamshika na kumwangalia kama kumkumbusha atulie. “Ndio
maana tupo hapa ili wote tuwe ukurasa mmoja. Jena nimeshazungumza naye na wewe
hivyohivyo. Hili linawahusu wote wawili ndio maana nataka mlijibu ili kesho
msijichanganye.” Waili akaweka msisitizo. Jack akabaki ameinama. “Lazima kuna
jibu la kwanza lililokujia kichwani lakini unapingana nalo mpaka linakuudhi,
Jack. Naomba mpe hilohilo yeye atakurekebisha.” Sabrina akamuongelesha taratibu
nakumfanya Jack atulie tena akifikiria. “Jackson?” Waili akamuita kama
kumkumbusha swali lake. “Naomba mpe muda tafadhali. Atakujibu tu.” Sabrina
akaingilia kwa heshima, wote kimya wakijiangalizia.
Akamkwangua taratibu na
kucha nyuma ya mgongo. Safari hii hakuna aliyeona maana walikaa karibu, na
mkono wake ulikuwa nyuma yake muda wote. Akamuangalia mkewe, akavuta pumzi kwa
nguvu kisha akajibu. “Cha kwanza sijui unazungumzia nini!” “Safi sana.
Lakini linaweza kuja swali kwa namna nyingine, Je, uliona huo ujumbe wa
ukaribisho wa dada yako huko mtandaoni?” “Hapana.” “Bwana Msindai, naomba
kukumbusha upo chini ya kiapo.” “Nafahamu.” Jack akajibu kwa kujiamini. “Narudia
tena. Je, unajua kama dada yako alimkaribisha Phina kwenye familia?” “Hapana.”
“Je, umesikia fununu zozote juu ya hilo?” “Ndiyo.” “Umechukuliaje?” Waili
akamuuliza tena kama wapo mahakamani kweli. “Kama uongo mwingine wowote ambao
Phina ameutumia kunichafua mimi na familia yangu.” Mpaka Waili akatabasamu akitingisha kichwa
akiashiria kuridhika.
“Safi sana. Mpaka hapo naona
tupo sawa. Kwamba katika hilo, hata ukiulizwa kwa kuzungukwa, tafadhali usitoke
hapo. Na usijisahau ukakaa hivyo ulivyokaa sasahivi hata mara moja. Wewe ni
Naibu Waziri Msindai. Kaa kimamlaka kama vile alivyokaa kaka yako.” Wote
wakamgeukia Junior. Junior akacheka. “Nimeshazoea kukaa hivi.” “Basi hata
nyumbani ni hivyohivyo mpaka Cleiton anamuigiliza baba yake akiwa hayupo.”
Wakacheka. Jack akanyoosha mgongo na kutengeneza mabega vizuri. Lakini akakaa
kwa kuegemea kwenye kochi ila si kihasara au kinyonge kama alivyokuwa ameinama.
Akazungumza na Jena pamoja na Jack akiwafanyia mazoezi mpaka akaridhika.
“Mzee naona sisi tupo
tayari.” “Hapatakuwa na kushitukizwa kesho?” “Labda kuwe na jipya ambalo mimi
mpaka sasa silifahamu. Lakini kama ni hayahaya tu, hapatakuwa na lakutushinda.”
“Jamani, mimi nina swali lakini si kwa ugomvi. Baba naomba kuuliza.”
“Ukishasikia hivyo tu, ujue kuna anachotaka kusema na anajua atanikera tu,
ndio anaomba ulinzi wa baba yake. Jacinta mtoto wewe!” “Basi mama. Ila ujue ni
katika kutaka kusaidia tu.” “Sasa si tupo kwenye kutengeneza hapa! Ukimzuia
kuuliza, tutajuaje mawazo yake?” “Mimi nayajua sana mawazo ya huyo mwanao.
Najua sana anachotaka kuuliza.” “Basi mama.” “Basi mpe jibu na wote tusikie ili
tubakie upande mmoja!” “Majibu yangu atayasikia kesho. Nishazungumza na Waili,
tumeshaelewana. Au sicho ulichotaka kusema?” “Basi mama.” “Sema kama nimekosea
na usitunge kingine.” Jacinta akaanza kucheka.
“Mbea huyu!” “Sasa mbona
kama ni jambo la kheri halafu…” “Na usingemtetea, mimi leo ndio ningesema mvua
itanyesha!” Wote wakaanza kucheka. “Haya, hili limekaa sawa, twendeni tuhamie
mezani.” “Jamani mimi naomba sisi tuondoke. Mke wangu amefunga tokea jumatatu!”
Kila mtu akashangaa. “Jack jamani! Watu wakifunga hawatangazi!” “Sasa
unataka kubaki hapa watu wakila ili ufanyaje na sisi tumesharuhusiwa?” “Subiri
kwanza Sabrina. Unafunga na wewe unanyonyesha!” “Ila nakunywa chai.” “Kwa nini
unafanya hivyo!?” “Ananiombea mimi.” Jack akajibu wote wakamgeukia yeye.
“Baba kama sisi
tumemaliza naomba mke wangu akapumzike.” “Ndio maana umechoka Sabrina!
Utafungua lini sasa?” Sabrina akaanza kucheka. “Wifi anavyouliza kwa uchungu!”
“Wala si uchungu huo, ni aibu zake. Maana amekutuma pombe.” “Wala si mimi,
mumeo huyo.” Jacinta akakanusha. “Sio Jacinta wewe uliyetaka wine na mimi ndio
nikatuma glasi yangu?” Junior akashangaa kusingiziwa. “Ila ametumiminia wote
hapa!” “Ona mnavyoshikana uchawi wenyewe kwa wenyewe! Mungu amewaona kwa
kuninyima na mimi nisinywe.” “Wewe ukinywa unakuwa msumbufu sana bwana! Glasi
mbili tu utafikiri umefunga baa nzima! Bakia dereva wa mumeo tu.” Wakazidi
kucheka.
“Shem tusamehe bwana.”
“Wala msijali. Ila naomba sisi tutangulie, sasahivi nitakuta timu yangu yote ipo
sebuleni inanisubiria, macho mlangoni. Phina ashanipigia simu kama mara mbili
hapa. Ujue hapo ameishiwa maziwa ya Brandon.” “Mimi mpaka nahisi Phina huwa
anamwaga maziwa ili dada yake arudi akae na Brandon. Maana ukitaka kutulie pale
ndani, basi Brandon awe mikononi kwa mama yake. Panapoa na kila mtoto atalala.
Sasa nahisi anamwaga ili Sabrina akiwa anatoka, asikawie kurudi.” “Ila Brandon
anamwili mkubwa yule. Inawezekana anamaliza kweli maziwa.” “Afadhali umwambie
wewe baba. Mpaka ameanza kumchukia Pina! Wakati mwanae akianza kunywa maziwa,
hapumziki mpaka chupa itoe hewa ndio anatulia, tena anaweza kulia kwanza ndipo
alale. Brandon si mvivu wa kula. Bora sisi twende.” “Nyinyi nendeni.” Mzee
Msindai akawaruhusu.
“Ila naomba nimchukulie Jack ndizi.” “Yeye muombewaji
hajafunga!?” Sabrina alicheka mpaka akakaa. “Sabrina naye! Ni siku moja tu!”
Jack akalalamika. “Yaani huyu mkitaka mlale mpaka kuchwe, ni ale kama mwanae
Brandon. Lasivyo mbona hamtalala! Usiku kuchwa anakusemesha mpaka umpe chakula,
ndio analala. Eti yeye anasema hawezi kuomba na njaa. Bora ashibe ndio anaweza kuzungumza
na Mungu.” Wakazidi kucheka.
“Ila Singida niliwahi
kufunga bwana!” “Mimi naomba nichukue tu ndizi hapa, ukale, ulale vizuri kesho
uamke na nguvu. Utafunga kesho kutwa.” “Bora.” Mama yake akaongeza akielekea
jikoni kumpakulia kiziwanda chake chakula, wengine wakicheka. “Huwa nafunga
bwana! Sema Sabrina naye hana subira. Ukimlalamikia kidogo tu kuwa njaa inauma
mpaka usingizi hauji, eti yeye anakupa chakula bwana!” “Wewe si mfungaji bwana.”
“Mbona angenitia moyo mimi ningefika tu asubuhi!” Wakazidi kucheka. “Muulizeni
uji nilimpikia saa ngapi kama si saa sita ya usiku kwa kushindwa kulala! Kila
saa ananiamsha na kunilalamikia. Nikaona tutakesha tukilia njaa, na kuomba
hatuombi.” Sabrina akajibu akiwa anaelekea na yeye jikoni kufuata chakula.
“Wewe Sabrina sio
mvumilivu bwana.” “Aibu zako! Baba mzima unaombewa kama maiti!” “Basi leo
sili.” “Utakula sana, ili tulale. Wewe kama unataka kumthibitishia wifi wewe ni
mfungaji, funga kesho kuamkia jumamosi.” “Sasa hapo nitakuwa nikifunga nini
kama si kuweka tu ushindani ambao Mungu hapendi! Si bora kuacha tu!” Kila mtu
akacheka baba yake akimwangalia.
“Haya, Jackson Msindai,
twende. Sisi tunashukuru sana Waili. Asante kusimama na sisi. Wengine wote
usiku mwema. Mama asante kwa chakula.” “Basi hiyo kesho mje mfuturie hapa nyumbani.”
Pakazuka ukimya wote wakamgeukia mama Msindai. “Sasa mnashangaa nini? Tena njoo
na watoto wote ili ule ukiwa umetulia.” “Hata mimi kesho nafunga mama, naomba
nije kufuturu hapa kwako.” Jacinta akadakia. “Watu wasiopenda kupika makwao!”
“Nitafunga mama.” “Hata mimi na wanangu tutafunga kesho. Kwa hiyo kule kwetu kesho
hakuna kupikwa. Junior kesho kula kwa mama Msindai. Ukitoka kazini wewe njoo tu
hapa moja kwa moja.” “Mpaka nijute! Ukaribisho huu wa Sabrina tu, wengine
mnaleta mpaka waume zenu!” “Mama Msindai basi mimi nitakuletea vinywaji mama
yangu, ili usipate shida ya kukarimu wageni.” Junior akaongeza.
“Nyinyi njooni wote na
wajukuu zangu, tuje kula na kumshukuru Mungu pamoja.” “Na hivi kesho kutwa ni jumamosi, hawaendi
shule, mbona tutakuja!” Wakakubaliana kuwa kesho yake watakuwa hapo kwa mama
Msindai, ila Sabrina alifurahi sana. Kwamba mpaka mama Msindai amewakaribisha kina
Jeiline! Akabaki kumshukuru Mungu, wakaondoka.
Mahakamani.
S |
abrina aliamka kabla ya mumewe akaelekea sebuleni
kuomba. Aliomba Sabrina kwa machozi akimsihi Mungu atende muujiza huko
mahakamani. Yale shetani alikusudia kwa ubaya, basi Yeye Mungu mwenyewe
akageuze kwa wema. Akatubu kwa ajili ya familia nzima ya Msindai.
Alipokuja kumuombea mama yake Jack, akatulia kwanza akikumbuka kilichomtokea
usiku uliopita nyumbani kwa wakweze. Akatafakari na kuishia kusema, ‘Wewe ni Mungu,
badala yako hakuna mwingine. Hugeuza mioyo ya wafalme kuwageukia wanyonge!’
Akabaki magotini kwa Mungu wake akaomba na kushukuru, ndipo siku yake ikaanza.
“Nataka nianzie kwanza
ofisini. Naomba tuwahi kidogo.” Jack akamfuata jikoni. “Au wewe utangulie
nitakufuata mahakamani.” “Unataka kuanza kunichanganya tena, Brina!” “Sasa
unachanganyikiwa nini? Bora tukutane mahakamani kuliko tuanze kwenda wote mpaka
ofisini kwak..” “Basi bwana Brina!” “Sasa unakasirika nini Jack?” “Uliniahidi
mwenyewe leo tutakuwa wote, unaanza kunigeuka! Mwisho utasema tena umeshindwa
kuja mahakamani.” Watoto nao wakaanza kuamka.
Keilini na Jeiline wakaja
hapo jikoni. “Mbona leo mapema hivi!?” Akawanyanyua wote wawili, wakambusu na
kujilaza mabegani. “Eti?” “Wewe ndio utakuwa umewaaamsha. Unalalamikia vitu
ambavyo..” Sabrina akanyamaza. Jack akatoka nao na kwenda kukaa nao sebuleni
wakawa wamemlalia. “Sabrina, hawa bado wanausingizi. Nashauri wapewe maziwa,
warudi kulala.” Sabrina akatoka kuwaangalia. “Eti Keiline bado unausingizi?” Wakabaki
wakimwangalia. Akamuita dada kuwachukua wao wakaanza kujiandaa, baada ya nusu
saa wakatoka hapo pamoja.
~~~~~~~~~~~~~
Kesi yao ilikuwa
ikisikilizwa saa tatu na nusu asubuhi. Watoto wa Msindai wote walifika hapo
kasoro dakika 15. Mama Msindai aliletwa na dereva, wakakutana wote na wakili
wao. Mzee Msindai na Joy hawakuwepo. Ila Waziri Msindai naye aliletwa na dereva
bila kuchelewa. Kulikuwa na ulinzi wakutosha maana mashabiki wa Phina walionyesha
utayari wa kufika hapo kumuunga mkono mahakamani. Kama kawaida Jacinta alikuwa
amependeza haswa. Familia ya Msindai wote wakaenda kukaa pamoja ila Jack na
Jena wakaenda kukaa mbele upande wa washitaki, wakatulia.
Baada ya muda wakiwa
wamechelewa, saa nne kasoro, wakasikia shangwe nje, wakajua wamefika. Hakimu
alitaka kuahirisha kesi lakini Waili akamsihi aongeze muda kidogo ili
kuwasubiri. Wakaingia hapo mahakamani. Jack kimya hata hakugeuka wakati Phina
na Ibra wakiwa na wakili wa serikali wakiingia pamoja na mashabiki wao. Ilibidi
wapewe wakili wa serikali. Akaomba dakika 10 pamoja nao ndipo waanze. Hakimu
muendesha kesi akaahirisha na kusema kesi yao itaanza kusikilizwa saa nne
kamili.
Jack akasimama. “Wapi
tena!?” “Naenda kwa mke wangu! Wewe hujasikia ni mpaka saa nne kamili?” “Bado dakika
13 tu, Jackson!” Jack akamwangalia Waili kama anayemwambia ninayo saa, akatoka
pale mbele na kwenda alipokaa Sabrina akiruka watu waliokaa mwanzo, Jacinta na
kaka yake ili kumfikia mkewe na wenyewe wakampisha, mpaka akamfikia. Akaenda
kukaa katikati ya Sabrina na Jacinta. “Vipi?” “Nimekuja kukuangalia wewe.”
“Mimi nipo sawa.” Wakabaki wakiangaliana. “Utakuwa sawa Jack. Usiogope?”
Sabrina akaendelea kunong’ona akimfariji. “Natamani hii leo ipotee iwe kesho
tayari.” “Lazima tuimalize leo.” Akatulia. Sabrina akamshika mkono na
kumuegemea begani. Jack akamchungulia. “Nimefurahi upo hapa na mimi.”
Akampitishia mkono juu, Sabrina akajisogeza vizuri, akawa kama amemkumbatia
mkewe aliyekuwa amejiegemeza ubavuni, wakatulia. Mama Msindai kimya upande
mwingine mpaka hakimu aliporudi kuendesha kesi.
Saphina Shija.
Waili akamgeukia Jack.
Akasimama akimuachia mkewe taratibu na kurudi pale mbele. Kesi ikaanza. Waili
akaeleza mashitaka yote anayowashitaki Phina na Ibra. Ikaanza zamu ya Phina
kuhojiwa. Akaeleza kila kitu kama alivyowaaminisha watu mtandaoni kuwa Jack
alimfuata chumbani kwake, akamueleza matatizo aliyonayo na mkewe na kutaka
kuanzisha naye familia. Lakini aliposhika mimba, Jackson akamkimbia kitu
kilichozua matatizo ya kiafya kwake kwa msongo wa mawazo mpaka akapoteza mtoto.
Wakili wake akamuuliza maswali rahisi tu ili kutengeneza upande wake mpaka
akamaliza.
Akaeleza juu ya Jena na kile alichomwambia juu ya mama Msindai kutaka kumfanyia kitchen party kama ishara ya kumkaribisha kwenye familia. Lakini baadaye naye Jena akamgeuka. Wakili wake akaomba shahidi wa kwanza aliyeona post ya Jena aende. Akaenda wa kwanza na wapili wote wakasema waliona comment na likes za Jena. Akaitwa sasa Jena. Jena akaapishwa na kuanza kuhojiwa.
Jena
Msindai!
Jena akiwa ametulia
kabisa akaeleza kama alivyopanga na Waili. Kuwa akaunti yake iliibiwa, kuna mtu
ambaye alikuwa akiitumia bila yeye kujua. “Kwa hiyo unataka kusema hukuwa
ukijua kilichokuwa kikiendelea?” “Hapana! Mpaka nilipokuja kupewa pongezi ya
mtoto mpya atakayeongezeka kwenye familia yetu ndipo ikabidi kuanza kufuatilia
na kuzifunga kabisa hizo akaunti.” Sabrina alibaki akimwangalia Jena vile
anavyokanusha bila hofu.
“Wakina Msindai ni
wakristo jamani! Hatuna ndoa za wake wawili! Halafu hata iweje, mwanamke
kama Phina wa mitandaoni huyu, anayetoa mambo mazito yanayotakiwa kuwa
ndani, hawezi kuingia kwenye familia kama yetu ya kina Msindai, ambayo
tumeaminiwa kubeba siri za serikali jamani!” Pakaibuka kelele. Hakimu akataka watulie.
“Ni kweli! Mwanamke ambaye yupo mtandaoni akijianika mchana mpaka usiku,
akishindwa hata kutunza siri za ofisi yake tu, atawezaje kusogezwa kwenye
familia ya kina Msindai ambayo tukikaa sisi wanne tu, tunawakilisha wizara nne
tofauti tofauti! Hii serikali si itakuwa kama ipo uchi tu mbele ya kila mtu!”
Jena akaongea kijasiri kabisa bila ya kupepesa macho.
“Wake za Msindai
wametulia jamani! Mshawahi kuwasikia mitandaoni?” Jena akaendelea bila kutumwa.
Kelele zikaibuka zaidi. “Wake za Msindai wanajielewa! Na wana vifua vya kubeba
mazito ya ndoa na nchi. Huwezi kuwakuta mitandaoni wakianika mambo. Huyu Phina
hata ajilize vipi, haiwezi familia yetu na wala Jack sio mjinga kumsogeza
kwenye familia yetu. Ndio maana japokuwa yeye alikuwepo, akamuoa Sabrina. Ni
kwa kuwa tunajua ni wanawake gani wakuingiza kwenye familia. Nimemaliza.”
Zikaibuka fujo nyingine akaitwa Jackson.
Jackson
Msindai.
Akaanza kumuhoji wakili
wa Phina. “Ulikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Phina?” “Ndiyo.” Jack
akakubali. “Kwa hiyo unakubali shutuma alizokutupia?” “Si ndio maana leo tupo
hapa? Namshitaki kwa mashitaka yote yaliyosomwa mwanzoni. Phina alikuwa kwenye
mahusiano na mimi tulipokuwa chuoni, lakini si mama watoto wangu na sikuwahi
hata kumfikiria kwenye maisha yangu ya baadaye. Hana hata kigezo kimoja cha kuwa
mwanamke ambaye anaweza kuwa na mimi maishani, ndio maana baada ya chuo tu niliachana
naye.” Ukaibuka mzozo wa chinichini, hakimu akataka upande wa kina Phina
watulie akiwaambia lasivyo atawatoa nje. Ibra akawatuliza, wakatulia.
“Unakubali kufanya naye
mapenzi mlipokuwa nchini Uswiz kikazi?” “Labda niweke jambo moja sawa.” “Jibu
swali.” Upande wa kina Ibra wakashangilia sana. “Ndio najibu!” “Jibu ndiyo
au hapana?” “Siwezi kujibu ndiyo au hapana wakati swali lako si sahihi!
Limegawanyika na unataka kunitega!” Wakaanza kubishana, Jack akisaidiwa na Waili
na wakili wa wakina Phina, mpaka Waili akasimama, ikabidi kumsogelea hakimu.
“Naomba Jackson ajibu swali.” “Hajakataa kujibu swali lakini rekebisha swali
lako! Unauliza swali huku ukimsingizia!” Waili akatetea. Wakabishana tena hapo
mbele ya hakimu, mwishoe Jack akaambiwa ajibu swali.
“Nilijamiiana na Phina tulipokuwa
nchini Uswiz lakini haukuwa muda wa kazi. Ninachofanya baada ya majukumu yangu
ya siku, ni juu yangu mimi.” “Kwahiyo unajua kama baada ya kujamiiana na Phina
alishika mimba?” “Hapana.” Ukaibuka mzozo mkubwa sana. “Jackson, naomba
kukukumbusha upo kwenye kiapo.” “Nafahamu na ninasema ukweli. Kwa sababu tokea
alipokuja chumbani kwangu akinitaka nifanye naye mapenzi akinikumbusha mambo
mengi na kunililia, nilianguka na kulala naye. Baada ya pale nilimwambia
kabisa…” Ukaibuka mzozo, hakimu akamwambia Phina, asipotuliza watu wao,
watatolewa pale. Kwa mara nyingine tena Ibra akawatuliza lakini akaongeza
kuwa Jackson anasema uongo.
“Mimi ninao ushahidi na
ndio maana na yeye aliambiwa alete ushahidi wa anachokisema.” “Ushahidi gani?”
“Acha nimalizie ninachoongea ndipo nitaleta uthibitisho wangu. Phina amemfanyia
fujo mke wangu akisindikizwa na Ibra kwa uongo anaosambaza Phina.
Amekuja nyumbani kwa mke wangu na watoto wakiongea uongo! Kana kwamba haitoshi,
wakaenda kunichafua Ustawi wa Jamii. Kesho yake akiwa peke yake, yeye mwenyewe Phina
akarudi kukanusha yote aliyozungumza Ustawi wa Jamii akisema ni Ibra
ndiye alimshindikiza. Akafuta kesi. Baadaye tena, Phina huyohuyo
akatokezea mitandaoni akilalamikia kitendo tulichofanya si kwa kubakwa, ni yeye
mwenyewe kunifuata chumbani kwangu, na pia baada ya hapo nilimwambia wazi
kabisa tulifanya kosa. Mimi nimeoa na ninampenda mke wangu, sikupaswa
kuangukia kwenye ushawishi wake. Phina akaondoka chumbani kwangu…” “Wewe ndio ulimfuata
chumbani kwake na…” “Unaongea nini Ibra!?” Jack akamuuliza, Ibra akaanza
kupayuka, hakimu akaingilia na kuwatuliza. “Naomba kuthibitisha hayo
anayozungumza bwana Msindai.” Waili akasimama na kuomba kuweka hiyo video.
Pakatulia.
Uhalisia Mchungu!
I |
le video ikawekwa. Ikaanza kuonyeshwa hoteli
yenyewe kwa nje, kisha vyumbani. Mapigo ya moyo ya Phina yakaanza kwenda kasi.
Akaonekana Phina anatoka kwenye chumba. Akaelekea kwenye Elevator/ lifti
huku akijitengeneza vizuri. Lifti ikamchukua mpaka gorofa aliyokuwepo Jackson
Msindai. Kweli akaonekana amegonga kwa muda. Kisha akaonekana anazungumza akiwa
bado amesimama nje ya mlango uliokuwa bado umefungwa, akasubirishwa kidogo.
Akaonekana anasubiria nje ya mlango huku akitengeneza matiti yake kuyafanya yaonekane
vizuri kwa nje, na kuweka nywele vizuri wakati akisubiria.
Baada ya muda Jack
akamfungulia akionekana anachungulia sio kutoka kabisa. Wakazungumza kidogo.
Japokuwa maneno hayakusikika, lakini akaonekana Jack kurudi tena ndani. Hapo
kukawa na kusubiria tena. Phina akaonekana nje ya mlango kuendelea kujiweka
sawa. Akarekebisha matiti yake tena na tena akiyanyanyua juu zaidi. Akayachungulia
mara ya kwanza, akaonekana kutoridhika. Akasogea pembeni ya mlango. Akayapanga tena
mpaka akaridhika ndipo akarudi tena mbele ya mlango. Akaweka sawa nywele zake, akasubiria
tena, ndipo mlango ukafunguliwa. Safari hii Jackson hakuonekana hata
kuchungulia ila Phina kuingia ndani. Pakatulia. Sabrina akatulia kimya
akiangalia na yeye kama wengine wote hapo mahakamani.
Baada ya muda Phina akaonekana
kutoka hapo ndani peke yake bila Jack kuonekana tena. “Kwa hiyo pia sio kwamba
ulilala mpaka asubuhi!?” Ibra akasikika na swali la mshangao wa wazi kabisa.
“Wewe ndio uliyekazania tokea mwanzo. Mimi sikusema ni mpaka asubuhi!” Phina
akapinga, ukaibuka mzozo mwingine. “Demu kaonjeshwa asali, anataka kujenga
mzinga!” Wakaanza kucheka kwa sauti. “Jamaa kamkoleza vya fasta, anataka ndoa!”
Wakazidi kucheka. Sabrina akainama. Kejeli zikaendelea.
“Umedanganya Phina! Ulisema
yeye ndiye aliyekufuata chumbani!” Wakili wake akajikuta na yeye anaongea kwa
sauti. “Sasa ndio mjue aina ya mtu ambaye mnamtetea na kumuhurumia. Phina
alijua mimi nimeoa. Yeye alitaka nimtafute baada ya pale wakati tuliagana
vizuri na kama mlivyoona, alitoka chumbani kwangu vizuri tu. Sikumbaka!
Sikumuahidi chochote kile! Huo uongo anaosambaza juu ya mke wangu na watoto wetu,
amesikia wapi? Maana mimi sikuzungumza naye chochote zaidi ya kumsikiliza yeye,
kikatokea chakutokea, nikamwambia nimekosea kujamiiana naye, na nikamuomba
atoke chumbani kwangu. Maneno yote anayosambaza huko mtandaoni ameyapata wapi
na mkiangalia muda aliongia chumbani kwangu na kutoka, nisingeweza kuzungumza
yote hayo na bado tukajamiiana! Phina amesema uongo, amemchafua
mke wangu na familia yangu, sitakubali.” Phina akabaki ameinama, watu
wakizomea.
Mwishoe hakimu akaamuru
askari wawatoe nje wale wote waliokuja kushabikia. Palipotulia Ibra na yeye
akasomewa mashitaka yake. Akamuuliza kama na yeye analo la kujitetea juu ya
mashitaka yake, akashindwa kabisa kwani ni kama Phina alimmaliza. Ushahidi wa Msindai
ulioonekana pale, uliwafunga mdomo na kuwamaliza kabisa, wakashindwa hata
kueleza mengine. Jinsi mambo yalivyokuwa yakiendeshwa hapo mahakamani, ungegundua
tu ni kesi ilikusudiwa kufungwa siku hiyo.
Hukumu ya Ibra na Phina.
Ibra akahukumiwa kwa makosa
mawili. Uchochezi na Kula njama za kutenda kosa. Yote hayo
yakawekwa pamoja, akapewa miaka 8 jela. Hawakuamini. Maana ilikuwa kama utani
tu. Muda mfupi uliopita alikuwa shujaa mtandaoni, mpaka kujipatia mashabiki
gafla mambo yamemgeukia! Na Phina naye akasomewa makosa yake. Akishitakiwa kutoa
siri za serikali. Kuchafua Wizara ya Fedha akisema. Kusema uongo
na uchochezi kwa umma, akitumia mitandao vibaya. Phina akaunganishiwa
makosa yote akapewa miaka 15. Phina alilia kama mtoto mdogo. Wakatolewa hapo na
pingu. Wakabaki kina Msindai wamesimama.
~~~~~~~~~~~~~
Wakati wakina Msindai
wanasogea mbele kumshukuru Waili, yeye Jack akatoka pale mbele bila shukurani
kwa wakili wake, moja kwa moja kwa Sabrina. Akamkuta amekalia mikono yake,
amejiinamia. “Brina!” Akamuita. Akatulia kwa muda ndipo akamgeukia taratibu,
akamuona machozi yamejaa machoni. Akatoa tabasamu na pongezi. “Hongera Jack.” “Brina!” Jack akawa ameishiwa
nguvu baada ya kuona sura ya mkewe. Sabrina akacheka na kuinama.
Japokuwa video ilizimwa,
mambo mengine yakaendelea mpaka hukumu, lakini bado yeye aliachwa
hotelini Uswiz. Bado ile video ilikuwa ikiendelea kichwani mwake na mengine
mengi ambayo hata hayakuonyeshwa kwenye ile video, yeye Sabrina alikuwa
akiyaona yanayoendelea nyuma ya pazia. Mumewe uchi kitandani na mrembo Phina.
Kumbukumbu ikamjia
walipokuwa chuoni na kuwafumania wawili hao. Vile mpaka Jack akatoka kumkimbiza
akamuacha mrembo Phina kitandani akilalamika, akaishia kumkuta darasani na homa
kali, akampeleka hospitalini. Akamuuguza mpaka akapona, akisaidiwa na Phina
huyohuyo! Sabrina akajisikia wivu wa ajabu kana kwamba ndio imetokea,
kumbe muda ulishapita!
“Nakuja sasahivi.” Sabrina akasimama, wakati kina
Msindai wakiendelea kushangilia ushindi na Waili pale mbele. Jack akamfuata
nyuma. “Brina!” “Nataka kutumia choo, Jack. Nakuja sasahivi.” “Unanidanganya,
Brina. Naomba uje.” Sabrina akabaki amesimama. “Ni bora ulie hapa nilipo,
kuliko chooni peke yako.” Jack akamsogelea na kumshika mikono yote miwili.
Bado kulikuwa na watu
wengi tu nje kila mmoja akisema lake, wao bado walibaki ndani mahakamani. “Nakupenda
Brina, na unajua nimekosa mpenzi wangu. Nimejifunza na nakuahidi aina hizi za
video hutakaa ukaziona tena.” Sabrina akatingisha kichwa kukubali. Kabla hata
hawajazungumza jingine, wakawasogelea kina Jacinta. “Jamani, hili limeisha,
acha mimi niwahi kazini.” Jacinta akaaga. “Na mimi acha niwahi majukumu yangu.”
Junior naye akaaga. “Nashukuruni jamani. Asante kaka. Jacinta dada yangu, tutazungumza
vizuri jioni tukikutana kwa mama.” “Usijali.” Junior akajibu kwa niaba ya wote.
Waili naye akasogea. “Waili, asante.” Jack akashukuru. “Tunashukuru Waili.”
Sabrina naye akashukuru na kumpa mkono. “Nenda ukale sasa. Hili limeshapita.”
Sabrina akacheka tu. Waili akawaaga na kuondoka.
Askari wakaja kuweka
mazingira ya kina Msindai kutoka, wakataka Jacinta kiongozi wao ndio aondoke wa
kwanza. “Tafadhali naomba mama Msindai atolewe kwanza hapa, kisha afuate Waziri
Msindai, ndipo Naibu Waziri na mkewe.” Jacinta akawatambua vizuri na kwa
heshima hao kaka zake. Kikazi akionyesha yeye kama mtu wa Wizara ya Ulinzi na
Usalama, anawajibika kwa viongozi wa nchi yake kwanza. “Jena akishaondoka hapa,
ndipo na mimi nitoke.” Akaamuru Jacinta. Ikasogezwa gari ya mama Msindai.
Dereva wao wa familia ndiye aliyekuwa akimuendesha. Mama Msindai akatolewa
ndani akisindikizwa na askari. Alipoondoka, akaja kufuatwa Junior. Na yeye akakuta
gari yake imeshasogezwa mpaka mlangoni, akapanda dereva akaondoa gari. Akafuata
Jackson na mkewe. Ikawa hivyohivyo. Wakaondoka ndipo na Jena naye akasindikizwa
na askari mpaka kwenye gari yake. Alipoondoka ndipo Jacinta naye akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Njiani Jack akamuona
Sabrina anatoa simu. Akampigia mzee Msindai ikaita mara kadhaa ndipo
ikapokelewa. “Samahani baba tunakusumbua!” “Hata
kidogo. Nilikuwa kwenye simu na Waili kunijulisha kilichoendelea.” “Basi
nikuache uendelee, lakini mimi na Jack tulitaka kukushukuru kwa kila kitu.
Asante baba yangu.” “Karibu mama. Tutazungumza zaidi mkija nyumbani. Tuwe
tunakunywa chai huku tukiongea.” Sabrina akacheka na kuaga.
~~~~~~~~~~~~~
“Nakushukuru kusimama na
mimi Brina. Samahani najua sio rahisi.” “Tushukuru hili limepita.” Wakatulia. “Inabidi
mimi kurudi kazini.” “Basi tutakutana kwa mama Msindai jioni.” “Sio
mtanisubiri?” “Inabidi niwabebe na kina Pina ili vikianza vilio kule,
tusaidiane.” “Nisubiri, tutamchukua tu Pina. Mimi mwenyewe nitakuwepo kusaidia.”
“Sawa.” Safari ya kutafuta Wizara ya Fedha ikaendelea ili kumshusha Jack.
“Nikuulize kitu, Brina?”
Sabrina alikuwa amepotelea mawazoni akamwangalia. “Hivi nikipanga tusafiri mimi
na wewe tu, unafikiri itawezekana?” Sabrina akabaki akifikiria. “Hata siku
mbili tu.” “Watoto nawaachaje, Jack? Hawa wasichana hawana akili ya kufikiria
hata kwa masaa mawili tu. Hata ukiwapa maagizo ya masaa matatu tu nikiwa naenda
saluni, nikitoka hata dakika 20 haziishi simu za maswali ya maagizo yaleyale
niliyowaachia zinafuata. Kwa siku mbili nzima, watachanganyikiwa.” “Acha na
mimi nifikirie.” “Halafu maziwa ya Brandon?” Sabrina akakumbuka kikwazo kingine.
“Anaweza kunywa yale maziwa aliyokuwa akiletewa na babu yake. Hawezi kufa kwa
siku mbili, bwana! Angalau na wewe utoke kidogo ukapumzike.” “Mimi sijachoka
Jack. Nipo sawa kabisa.” “Sawa. Basi angalau tupate muda wetu sisi wawili tu.”
Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu na kutulia mpaka walipofika na kumshusha Jack,
yeye akarudishwa nyumbani.
Kwa Mama Msindai.
W |
akati wakila na kunywa wajukuu wamejaa kwenye
hiyo nyumba ya mama Msindai, Sabrina akamsogelea mzee Msindai. “Naomba
tuzungumze kidogo.” Wakawaona wanatoka bila ya kuaga. Waliporidhika wamebakia
wao wawili huko nje, Sabrina akaanza. “Najua mimi na Jack tumekuwa na hekaheka
hujapumzika baba yangu. Lakini naomba kujua hatima ya Sabina.” Sabrina
akaendelea. “Wazazi wanahangaika nyumbani, na Sabina ndio tegemeo lao tokea
zamani.” Akamuona anafikiria.
Sabrina naye akanyamaza
kabisa kumpa nafasi. “Nataka kesi ya Max na mkewe ifungwe kwanza ndipo
nifikirie juu ya Sabina. Kwa kuwa sina uhakika endapo nitamtoa Sabina sasahivi,
kabla ya hukumu ya Max na mkewe, ataanzisha nini kingine chakuvuruga. Sijui
kama unanielewa?” Sabrina akajikuta machozi yakimtoka. “Nilimpa Sabina nafasi
zaidi ya nitakavyoweza kukwambia ili atulie na aache mambo kama yalivyo, lakini
alionekana alikusudia kuharibu, na mimi sipo tayari kuharibikiwa mambo mkononi.
Sijui kama unanielewa?” Sabrina akatingisha kichwa kukubali.
“Alifika umbali wa hatari
sana akisaidiwa na mama yenu ambaye alikuwa tayari kwa kifo cha Jackson!
Tafadhali kwa sasa endelea kusaidia nyumbani huku nikiweka mambo sawa. Kuwepo
kwa Sabina nje ni kunishika mimi miguu. Sitaweza kusogea kwa haraka kwa kuwa
bado sina imani na mama yenu kujua kama kwa hakika ameamua kuachana na nia yake
yakumuangamiza Jackson au la! Kwa hiyo macho yangu yote yapo kwake kuhakikisha
harudii tena kumloga Jackson. Sasa siwezi nikamtoa na Sabina ambaye itanilazimu
na yeye niweke macho yangu kwake huku nikitaka kukamilisha na la Max! Naomba
univumilie kidogo zaidi.” “Sawa. Hata hivyo
nakushukuru kutuvumilia. Ila naomba uniamini sijawahi kumloga Jackson.”
Sabrina akaongea na kujifuta machozi.
“Hilo najua kwa hakika.
Sina shaka nalo. Na hata mama najua ameanza kipindi hiki ambacho Sabina
amefungwa, na kumpoteza Tino. Hata kutaka kumuua Jack, ni ili wewe ujikute peke
yako, uje urudiane tena na Tino, mlee watoto. Na hilo sitakubali
Sabrina.” “Hata mimi sitafanya hivyo, baba. Nampenda Jack. Na hata kama Mungu
akimchukua Jack, sitarudi kuolewa na Tino hata iweje. Ni mtu mwenye roho mbaya
sana. Nina uhakika yeye hawezi kuwalea Brayan na Brandon kama hivi Jack anavyowalea
Jeiline na Keiline. Kwamba hata leo Mungu angebadilisha tukio, yeye
akawa Jack, asingeweza kufanya kama Jack. Kwa hiyo huko sitarudi tena.”
Sabrina akaendelea.
“Na naomba nikushukuru
kumsamehe mama na kutokuwaambia watu wengine. Zaidi mama Msindai.
Nimegundua hafahamu. Najua asingewahi kuja kuniamini tena na Jack.” “Tulia tu.
Baada ya muda mfupi kama halitaanzishwa jingine, kila kitu kitakuwa
sawa.” “Nakushukuru sana baba. Asante.” Sabrina akarudi ndani.
~~~~~~~~~~~~~
Alipokuwa akiingia
mlangoni Jack akampokea kwa macho, akagundua mambo hayakwenda sawa. Akarudi
kukaa karibu ya mumewe, akatulia kabisa. “Pole Brina.” Jack akamnong’oneza.
Sabrina akatoa tu tabasamu. Mzee Msindai naye akaingia. “Nikusaidie Keiline?” “Naona
wanasinzia, waache walale kabisa. Au unataka tuondoke?” “Hapana. Tukae kidogo,
naona stori zimenoga!” Hilo likamfurahisha hata mzee Msindai na wengine waliokuwa
wakiwasikiliza na kujua kwa hakika kinachoendelea. Kila mtu alijua Sabina yupo
jela na Sabrina anamuombea atolewe. Kitendo cha kurudi amepoa, wote wakajua
mzee Msindai amemkatalia. Ila bado akaonekana kutii na kuendelea kutulia! Hilo
likawashangaza kidogo ila likawapendeza wote zaidi Jack, akajisikia kujivunia
mkewe. Stori zikaendelea yeye akinywa chai, kina Jacinta, Joy, mama Msindai na Junior
wao wakinywa wine.
“Huu muda wa Brandon
amelala, acha sisi tupendane na Brayan wangu.” Sabrina akasimama ili kumtafuta
alipo. “Pumzika Sabrina na wewe! Mbona ametulia huko chumbani na kina Clei!” Joy
akamzuia. “Nakuwa na hamu naye! Brayan mkimya sana, kama si makini rahisi
kumsahau. Najua sasahivi amekaa tu amepoa mahali. Sasa kabla Brandon hajaamka
na kuniganda, huwa wenyewe tunapata muda na mwanangu. Acha nimchukue nimshike
kidogo.” “Mama wewe unashuguli!” Sabrina akacheka na kwenda kumchukua Brayan.
Na kweli akamkuta amekaa chini ametulia kimya wenzie wanacheza. Akamuhurumia.
“Twende mwanangu.
Wamekusahau?” Sabrina akambeba na kutoka naye. “Nimemkuta mwanangu amekaa peke
yake, wamemsahau!” Wakamwangalia jinsi alivyotulia. “Wanao wote wapole Sabrina
akasoro mmoja tu ndio yupo kama baba yake!”
Jacinta akafanya wacheke. Jack akatingisha kichwa akicheka. “Uchekaji
wako Sabrina sijaufurahia sana. Ni kama unakubaliana na Jacinta vile!” Wakazidi
kucheka Sabrina hakumjibu mumewe ila kuendelea kumkumbatia Brayan. Akamuona
anasinzia. “Alikuwa amechoka huyu.” Sabrina akaongea akimbusu na kumuweka
vizuri. “Lala kaka mzuri.” Akafunga macho.
Zikaendelea stori
wakinywa mpaka dada akawaletea nyama. “Mchomaji huyu alikusudia kutunyima hii
safari ya pili! Na mimi nikasema siondoki hapa mpaka alete.” Jacinta akaongea
akichukua zake na kuweka pembeni. “Nyama inachomwa mwaka mzima!” Junior naye
akalalamika akichukua zake. “Mimi naona nyinyi wawili leo watoto wenu
watayarishiwe chumba walale hapa. Si waondokaji nyinyi!” Jena akaongea
akimaanisha Joy na mumewe. “Mama Msindai akitufukuza tu hapa, tunahamisha
kikao. Au unasemaje Jacinta?” “Wewe tu. Leo mpaka pakuchwe.” Jacinta akajibu na
kipande cha nyama akaweka mdomoni. “Nitawaachia nyumba, mimi sitakesha.” Yeye
mwenyewe mama Msindai alikuwa akinywa kama wanae hao wawili. Jena, Jack na baba
yao hawakuwa wakinya pombe kabisa.
Ilipofika saa sita usiku
Jack akaaga yeye mwenyewe. “Naona sisi itoshe kwa leo. Watoto wote wamelala!”
“Sabrina nilikuwa na mzigo wako. Nisubiri nikupe.” Mama Msindai akasimama.
Junior akamfanyia ishara Jacinta kuwa anyamaze kabisa. Jacinta akaendeleza
stori akicheka na Joy maana hao wawili walipatana haswa na umri walilingana.
Jacinta na Joy. Sabrina akabaki akimwangalia Jack. Jack akamwangalia na
kuendelea kukusanya vitu vya watoto. Akamwambia dereva wa mama Msindai
atangulie na Pina pamoja na mapacha. Pina akaondoka na mizigo yote, Sabrina akabaki
amempakata Brayan akicheka moyoni akimsubiria mama Msindai arudi na hizo zawadi.
Bado hakuwa anaamini. Mama Msindai! Alijua adhabu aliyopewa na mumewe ndio
angemchukia yeye zaidi, lakini ikawa kinyume.
“Ni kitu kidogo tu. Nguo
za kulalia wajukuu na wewe hereni hizi. Hii dhahabu nzuri sana. Uvae ukiwa
nyumbani. Usiwe unakaa na masikio bila kitu.” Sabrina akasimama na kumkabidhi
Jack mtoto ili apokee. “Nashukuru sana mama yangu. Mungu akubariki. Nimefurahi
sana.” Wakacheka. Sabrina akapokea. “Acha nizivae sasahivi.” Wakaendelea
kucheka. Ila wakajua yote hayo ni kwa kuwa mzee Msindai aliingilia kati na
kuwaonyoosha mpaka wakarudi kwenye mstari. Sabrina yeye akabaki akimshukuru
Mungu wake.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya mwezi kesi ya
Max na mkewe ikasomwa. Max akahukumiwa miaka 15 jela, mkewe miaka miwili tu.
Hilo likaisha salama. Jack akiendelea na shuguli zake kama kawaida na yeye
Sabrina akiendelea kutunza nyumbani kwao kifedha na vyakula akimtuma Chali.
Yeye mwenyewe hakurudi kwao. Baada ya juma moja mbele baada ya hukumu ya Max na
mkewe, Sabina akatolewa. Kama aliyekuwa ameonywa, hakuzungumza
chochote juu ya alipokuwepo na kilichoendelea huko alipokuwa. Ila
alikonda sana. Akawa amepoa kuliko kawaida. Aliporudi kazini kuomba arudishwe
kazini, wakashindwa kumpokea, nafasi yake ilishajazwa na mtu mwingine. Akaona
arudi kwao kwanza mpaka arudishe mwili na akili. Akawa kama amepatwa msongo wa
mawazo. Kula na kulala bila kuzungumza chochote, mama yake akimuhudumia.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya miezi 6 na siku
10 tokea Tino aondolewe nchini mzee Msindai akamfuata Sabrina nyumbani kwake.
Jack alikuwepo, ila akaomba atoke nje azungumze na Sabrina. “Unakumbuka
nilikupa miezi sita yakufikiria kisha unipe jibu juu ya Tino?” “Samahani
kuchelewa kujibu kwa wakati baba yangu. Naona inaleta shida kwenye ndoa yangu. Naona
niache tu.” “Unaachaje?” Sabrina akatulia akifikiria. Mzee Msindai kimya.
Sabrina akamwangalia.
“Nata..” Akasita. “Jack
amenikataza kuonana tena na Tino. Sijui jinsi ya kuwasiliana naye.” “Ulitaka
kumwambia nini?” Sabrina akasita. “Wewe niambie kile ulichotaka Tino asikie.”
“Kuwa baba yao kina Jeiline amekataa nao kabisa na amesema hata akifa leo, yeye
Tino sio baba yao na hatakuwa baba yao.” Sabrina akaendelea.
“Jack ameandikisha hilo
kwa Waili, baba. Na amemuweka Junior kuwa shahidi wake. Anasema Italy sio kwa
kina Jeiline. Na hata nikiachana naye, bado watoto ni wake kwa kuwa hata mimi…”
Sabrina akasita.
“Kwa kifupi ndio hivyo.
Jack amekataa na watoto wake. Hata salamu ya Tino kwa wanae Jack, amekataa. Kwa
hiyo kama angekubali nikutane na Tino, hayo ndio ningemwambia Tino. Jack hataki
kumuona karibu ya wanae huyo Jack. Na nakala ya hayo yote niliyokwambia,
amemtuma Chali siku chache zilizopita amewapelekea wazazi Chalinze.” “Je, na
wewe umeamuaje?” Mzee Msindai akamuuliza kutaka kujua. “Hapakuwa au hakuna nafasi
ya kuamua tena, baba! Jack amesema huo ndio uwamuzi wa mwisho na
kunithibitishia hilo ndio akamuita Waili pale nyumbani na shem akawa shahidi.
Kwa hiyo hilo tumefunga baba yangu. Jack hataki tena na binti zake.” “Basi mimi
nitamfikishia huo ujumbe Tino.” “Nashukuru baba.” “Hilo limekwisha. Na
tumelifunga milele. Naomba hili lisiwahi kuzungumziwa tena Sabrina.” “Sawa
baba. Sitarudia tena.” Mzee Msindai akarudi ndani kuaga na kuondoka. Ilichukua
kama dakika 10 kutulia na kurudi ndani kwa mumewe.
~~~~~~~~~~~~~
Karibu na uchaguzi, Sabrina akabeba tena
watoto wake na kuhamia tena Singida kuanza kampeni akimsaidia mumewe. Safari
hii Sabrina hakuwa mjamzito, Brandon mtoto wa mwisho ana miaka miwili, ikawa
rahisi kuzunguka na mumewe akiomba kura. Wakashikana Jack na Sabrina wakimuomba
Mungu na kufanya kampeni bila kuchoka mpaka Jack akafanikiwa kuchukua jimbo
hilo. Hapo ndipo Sabrina akatulia sasa na kurudi Dar kulea kwa nafasi. Jack
anaapishwa kuwa Mbunge wa hilo jimbo, ana watoto wanne tayari. Hao warembo wa
kiitaliano na wake wakiume wawili. Brayan na Brandon.
~~~~~~mwisho~~~~~
0 Comments:
Post a Comment