Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 72. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 72.

 Nyumbani Ni Nyumbani.

Chali alirudi nyumbani moja kwa moja akataka kuzungumza na Sabrina. “Mwambie azungumzie dirishani, mimi nanyonyesha huku chumbani kwa watoto na mtoto ndio ameanza tu, siwezi kumkatisha.” Sabrina akamtuma Phina. Baada ya muda akamsikia Chali dirishani. “Mama Msindai upo?” “Nakusikiliza Chali. Kwema?” Akamsikia akicheka ila si kicheko cha furaha. “Nini tena!?” “Bwana safari hii mimi nimepokelewa mpaka nimekaribishwa ndani!” “Haiwezekani!” “Na chai nimekunywa.” Sabrina akacheka. “Nani kakukaribisha?” “Alianza mzee. Nikahofia mama asije akatoka na kunikimbiza. Lakini yeye ndiye aliyeniletea chai. Ila hali sio nzuri mama  Msindai. Wazazi wanaonekana walihitaji kweli msaada.” Sabrina akatulia.

“Kuna wadogo zako wapo shule, nafikiri ndio nilikuwa nikitumwa kwako na baba, hana ada.” Sabrina akanyamaza. “Wanahitaji pesa mbali na vyakula. Na sidhani hata kama wana umeme pale. Kwa ufupi hali mbaya mpaka ikabidi nimuachie mzee pesa kidogo wakati akinisindikiza.” Sabrina akaumia sana. “Ulimpa kiasi gani?” “Naomba nisikwambie, wale ni kama wazazi wangu pia. Lakini jua wameishiwa kabisa. Mama anasema ilibidi kuokoteza vifuu vya nazi atumie kama mkaa ili kunipikia hiyo chai. Sasa unajua mtu mzima mpaka aongee hivyo, inamaana hali si nzuri.” “Nashukuru Chali.” “Na cha mwisho, nafikiri kwa hali ilivyo, hata ukiwapigia au ukienda, nadhani safari hii utapokelewa tu.” “Naona nianze kwa  kupiga.” Chali akaondoka na kumuacha Sabrina akifikiria familia yake.

Akajua wamepoteza msaada kutoka kwa Sabina na huyo Tino. Kaka yake tokea zamani hakuwa mtu wa kusaidia nyumbani. Akajua kwa hakika hali ya kwao sio nzuri. “Sabina atatolewa lini?” Hilo likabaki swalli aliloogopa kuliuliza kwa sauti kwa kuwa bado hakujua akija kutolewa, atafanya nini cha kuvuruga zaidi! Akabaki akiwaza huku akinyonyesha mwanae.

Aliyetangulia, Katangulia tu.

I

likuwa bado ni mapema tu wakati Ibra na Phina wapo sehemu wakila na kunywa pamoja na wapambe wao. Ibra alisikika akizungumza kwa sauti ya juu iliyojaa ushindi. Akawasogelea mtu aliyetumwa. “Ibrahimu Kondo?” “Nani anauliza?” Akauliza Ibra kwa kiburi. “Mjumbe. Nimepewa hii barua yako nikufikishie, inakuhusu.” Akabaki ameishika, Ibra hajapokea. Akaiweka mbele yake kwenye meza iliyokuwa na vinywaji. “Saphina Shija?” Phina akamwangalia. “Na wewe huu ni ujumbe wako. Ni muhimu kusoma maana..” “Kama unatoka kwa kina Msindai waambie hatutaki misamaha ya vificho. Sisi tumetoka hadharani, wasijifiche, wajibu hadharani kwa heshima ya jamii nzima. Waache dharau.” Akaongea Ibra kwa ujasiri na kiburi.

“Si dhani kama ni jambo baya kupokea ujumbe. Nafikiri sauti zenu zimefika mbali, ndio wanataka kuwasikiliza. Bado nashauri msikatae huo ujumbe.” Wakaanza kushangilia, yule mjumbe akaondoka akaacha wakipongezana. Moja kwa moja wao wakajua wamewafikisha kina Msindai magotini, maana bado Phina alikuwa akipokea pole huko mtandaoni, na kujibu maswali.

Wakamtia morari Ibra mpaka akafungua barua yake. Gafla wakamuona amebadilika sura mara aliposoma tu kichwa cha habari kwenye waraka uliokuwa ndani ya bahasha. Ilikuwa ni shitaka kutoka kwa Jackson Msindai yeye kama Jackson na Naibu Waziri. Alipewa siku 4, ikiwepo hiyo siku ya jumatatu, ajiandae na ushahidi wake wote ili kufika mahakamani siku ya ijumaa, kujibu shitaka lake la kumchafua mtandaoni kwa habari za uongo yeye kama Jackson Msindai, kisha Naibu Waziri. Na shitaka jingine ni kumvamia mkewe na watoto nyumbani kwake, na kufanya fujo mpaka kutolewa na askari. Ibra akatulia na kubadilika sura kabisa. “Nini!?” Wapambe zake wakamuuliza maana ni kama aligeuka kuwa shujaa kwenye jamii gafla. Akijisifu kuwa hababaishwi na cheo cha mtu ila haki tu.

“Phina wewe yako inasema nini?” Bado Phina alikuwa akisoma yake. “Nilikwambia Ibra, kadiri yule mwanasheria anavyochelewa ndivyo anavyotuweka sisi pabaya! Ona sasahivi sisi ndio tutasimama sehemu ya watuhumiwa na si yeye Jack!” Phina akaongea akilalamika macho kwenye waraka wake. “Acha nimpigie. Usipaniki.” Ibra akatoa simu na kuanza kumpigia simu mwanasheria ambaye walishazungumza naye juu ya hilo tokea mwanzo hata Phina hajambadilikia na kurudi upande wa Jack. Walimfahamu kwa jina lake la kwanza, Lioni. Mara ya kwanza simu ya Lioni iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Alipopiga mara ya pili ikaita mara mbili na kukatwa.

Akasimama kabisa na kutoka pale katikati ya kundi ili akampigie simu nje, sehemu tulivu. Hilo zoezi likaendelea kwa mara tatu mbeleni. Simu inaita kidogo na kukatwa. Phina akamfuata. Akamkuta bado akipiga simu. Alipojaribu kupiga tena, ile simu ikawa haipatikaniki tena. Haipo hewani! Ibra akashangaa sana. “Mbona simuelewi huyu Lioni?” “Labda yupo na mteja.” Phina akajibu kwa wasiwasi. Wakaamua kwenda kumfuata ofisini kwake. Wakaondoka hapo baa bila hata yakurudi ndani kuaga wenzao.

Aliyeshika Mpini.

Chakushangaza wakamkuta Lioni amekaa ofisini kwake, hana hata mteja. Tena alimwambia sekretari aliyewapokea mapokezi awaruhusu waingie ofisini kwake moja kwa moja. “Vipi, mbona hupokei simu zetu!?” “Kaeni na fungeni mlango.” Phina na Ibra wakakaa wakiwa na mshangao usoni.

“Ni nini kinaendelea Lioni!?” Ibra akaendelea kuhoji. “Mimi nitakwenda moja kwa moja kwenye pointi wala sitawapotezea muda wenu kwa kuwa sikutaka tuzungumze kwenye simu. Haya mlipaswa kuyasikia tukiwa tunatizamana kama hivi. Kwanza wekeni simu zenu hapa juu ya meza nihakikishe hamnirikodi.” “Acha kututisha bwana!” “Basi ondokeni.” “Acha masihara!” “Hakika siwatanii. Si mlisema huyu Phina alimpiga picha Jackson Msindai akiwa amelala?” Wote kimya. “Kwa hiyo mnataka mnichezee akili na mimi mnirikodi, halafu mkanifanyie kama mnachomfanyia Jackson Msindai!” Wote wakashituka na kushangaa jinsi anavyowabadilikia.

“Wewe tulikuja kwako tukitaka kukupa kazi ndio maana tulikwambia mambo ya ndani, leo unayatumia kinyume chetu!?” “Acha masihara kabisa Ibra. Kama huyu Phina aliweza kumfanyia mwanaume aliyekuwa naye kwenye mahusiano ya muda mrefu, mpaka akaja kumtafutia kazi, wamelala naye akijua ni mume wa mtu, wakaambiana mambo ya ndani kwa kiasi hicho, kwamba kulikuwa na mahusiano mazito kati yao, lakini bado ameweza kumfanyia anayomfanyia huko mtandaoni, atashindwa vipi kwangu mimi ambaye hata hanifahamu!?” Hilo likamuuma sana Phina, akanywea na kuinama kabisa. Lioni akaendelea akiwakazia macho kama asiyetaka utani nao.

 “Ninachotaka kuwaambia ni cha undani tena kama kuwasaidia tu nyinyi wawili. Siwaamini ndio maana sitaki kuja kubadilikiwa baadaye. Mkaja kuniangamiza mimi. Maana kuna waliomea kwenye hii nchi mpaka kuota mizizi kama mti wa muarobaini. Kwamba mizizi yao inaogopewa kila mahali, na ikipita chini ya nyumba yako, haitoi tu nyufa, inapasua kuta. Sasa uchaguzi ni wenu, mnaweka simu au mnatoka?” Ikabidi Phina na Ibra kuweka simu zao mezani. Lioni akaziangalia kabisa kama anayezikagua, akajiridhisha zimezimwa.

“Nianze na Phina. Mpaka sasahivi unao ushahidi wowote ule kwa shutuma zako unazoziendeleza mtandaoni?” “Mpaka sasa ni kama nimekwama ndio maana tumekutafuta, maana nimetoka kupokea barua ya mashitaka niliyopewa inatoka kwa…” “Wakili wa familia ya Msindai INAKUSHITAKI, Moja, Upande wa Jackson Msindai anakushitaki wewe kama Saphina Shija ukiwa na Ibrahimu, ulikwenda nyumbani kwake na kumfanyia fujo mkewe mpaka mkatolewa na askari.” Lioni akamalizia shitaka la kwanza vizuri kana kwamba yeye ndiye aliyeandika shitaka hilo na kuwashangaza wote wawili. “UMEJUAJE!?” Wote wakauliza kwa pamoja.

“Subirini kwanza. Hiyo ni kwa Jackson tu, na si bado Phina unayo mashitaka mengine kama ya kusema uongo mtandaoni na kumchafua mkewe, watoto na yeye mwenyewe Jackson Msindai kama mume na baba wa familia?” Phina kimya. “Si pia Phina umeshitakiwa kwa kutumia nafasi uliyopewa na serikali, kutoa siri za viongozi wa nchi, uliokuwa umepewa dhamana na Wizara uliyokuwa ukifanyia kazi, ili kuwahudumia kikazi, ila badala yake unatumia siri za ndani za Wizara ukiwa umejua wapi walikuwepo kikazi, nini walifanya siku nzima, umetumia hizo taarifa vibaya, kumchafua bwana Msindai kama Naibu Waziri? Ukaingia chumbani kwake, na kupiga picha unazotangaza wewe mwenyewe mtandaoni kuwa ulimpiga na zimeibiwa. Unashitakiwa kwa kutumia wadhifa wako vibaya, kuchafua ofisi zao na kutoa mpaka siri za ndani na mipango ya serikali? Mpaka hapo nimedanganya?” “Lakini..” “Subiri Phina. Kwenye hiyo barua hujapata shitaka pia kutoka kwa Jena Msindai AKIKUSHITAKI kwa kumsingizia mtandaoni na kumfuata kazini kumfanyia fujo?” “Haiwezekani! Kumbe ndio mashitaka ya Phina hayo!?” Ibra akashangaa sana.

“Kwani Phina hajakwambia?” “Hapana!” Phina akabaki kimya. “Mbali ya hayo ya Jackson Msindai, Jena naye anamshitaki kwa kumtupia shutuma za uongo huko mitandaoni.” “Lakini ninao ushahidi wa watu ambao pia waliona likes zake kwenye comments zangu na comment yake pia.” Phina akajaribu kujitetea. “Kumbe huna taarifa?  Jena anasema akaunti zake zote walizi hack. Kwamba kuna mtu alikuwa akitumia akaunti zake zote mitandaoni ndio maana alipogundua, amezifunga zote.” “Kuna mchezo wanatuchezea tu, si bure.” “Ibra, umejiingiza kwenye vita mbaya sana mpaka nakuhurumia.” “Hakuna watakachonifanya. Hii ni nchi yenye uhuru wa kuongea.” “Umeongea pabaya, kaka. Mimi mwenyewe nimeosha mikono yangu!” “Usiniambie kama na wewe Lioni wamesha kununua!” Ibra akauliza kwa kuumia.

“Nikuulize swali Ibra? Na ufikirie kwa makini kabla hujajibu.” “Juu ya nini!?” “Na Phina unaruhusiwa kumsaidia kujibu.” Wote wakaongeza umakini. “Mlishasikia vita yeyote. Mtu yeyote hapa nchini, au Raisi yeyote aliyekwisha kuwepo madarakani, mkubwa wa polisi au yeyote yule hata mwanasiasa mashuhuri, akigombana hadharani na mtu wa Usalama wa Taifa?” Pakazuka ukimya. “Kwa ukimya huo, mjue nyinyi wawili mmekanyaga kwenye moto.” Lioni akajiweka sawa.

“Ingekuwa vinginevyo ningewashauri mkimbie, lakini hamna pakukimbilia. Na kwa taarifa yenu tu, hakuna atakayekubali kuwasimamia kesi yenu, kwa sababu hakuna aliye tayari kuhama hapa mjini. Kila mtu anataka kulisha familia yake sio kuanzisha vita na watu wa Usalama wa Taifa. Kama hamniamini, tokeni hapa, katafuteni wakili mwingine, kampuni ingine, ila si kwenye hili jengo. Hili jengo letu wote, hakuna atakayechukua kazi yenu hata kwa mamilioni ya pesa. Haya jamani, kwaherini.” Kimya.

“Tafadhalini naomba niendelee na majukumu yangu.” “Umejishusha sana thamani, Lioni! Sikujua kama na wewe unaweza kununulika kirahisi kwa kiasi hichi! Jamii nzima ipo nyuma ya Phina ikimuhurumia!” “Sawa Mkuu. Lakini mwenye macho huwa haambiwi tazama. Dada Phina, kila la kheri.” Akasimama kabisa na kuwafungulia mlango, akiwaashiria watoke. “Hivi watu kama nyinyi mkiwa mnapokea rushwa, sisi wanyonge tunao tafuta haki zetu tuende wapi?” “Umejiingiza kwenye vita isiyokuhusu Ibra. Wewe si mnyonge, ila ni shabiki niliyekutahadharisha kutokea mwanzo kabisa uliposema unazo picha za Jackson Msindai, amelala na Phina, na amempa mimba ila anamkimbia. Nilikuomba ushahidi, ukashindwa kutoa ushahidi ila maneno tupu.” “Si kwa kuwa wameiba!” “Unao ushahidi wa hilo unalotaka kulianzisha tena?” Kabla hajajibu akamuongezea swali jingine. “Basi hata kama ushahidi huna, hiyo kesi ya kuwa uliibiwa, uliiandikisha polisi?” Kimya.

“Jamani mnanipotezea muda. Naombeni mnipishe nifanye majukumu yangu. Phina, nashauri ujiandae haswa. Shutuma ulizotupa huko mitandaoni zimefika kwenye masikio hatari sana. Na sijui mlipata wapi hiyo akili ya kusambaza mambo hadharani! Mmejitega wenyewe! Ndio mnatakiwa ushahidi wa kila mlilosema. Mbaya sana, HAMNA!” “Ibra alitaka nisikike.” “Ndio umesikika, unapewa nafasi ukasikilizwe vizuri. Naomba mnipishe.” Phina akatoka akamuacha Ibra akimwangalia Lioni.  Mwishoe Lioni akaamua arudi kukaa, akainamia mafaili yake akaendelea na kazi kana kwamba Ibra hayupo pale.

~~~~~~~~~~~~~~

Phina na Ibra wakaanza kuzunguka kutafuta wakili wakuwawakilisha hiyo siku ya ijumaa. Kila walipoenda jibu kubwa walilopata ni kwa wakati huo wanamajukumu mengi, hawataweza kuchukua kazi mpya kwa haraka. Ibra akawa mtu wa kumtia moyo Phina kwamba asiogope, hakuna watakachowafanya. “Uzuri kesi ipo mahakamani. Hata hakimu akiwa mla rushwa kiasi gani, kesi yetu imefuatiliwa sana mtandaoni. Jamii nzima ipo upande wako Phina, ikikuunga mkono na kukuhurumia kwa unyama uliofanyiwa. Ni kuhamasisha tu watu mtandaoni kuja kwa wingi mahakamani ili hata haki isipotendeka, watutetee.” Hilo likamtia moyo Phina.

Wakarudi nyumbani kwa Phina wakiwa wamechoka, wakaanza kuandika tena mtandaoni kuwa mawakili wote wa jijini wamekula rushwa, hawataki kuwatetea wao wanao gandamizwa. Wakatoa malalamishi yao wasijue wanazidi kuharibu na kuchafua ofisi za wanasheria pia. Watu wakazidi kuunga mkono wakitoa mifano yao na wao jinsi sheria inavyopendelea wenye uwezo na mengine mengi kila mtu akitoa lililokwisha kuwapata na kutopewa haki zao.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku zikazidi kwenda kila mtu akijipanga kivyake. Sabrina akawa na kazi ya kusoma mtandaoni na kuendelea kufunga na kumlilia Mungu wake huku Jack akimshirikisha kila kitu kinachoendelea kwa upande wa Msindai. Yeye kama Sabrina akawa na maombi juu ya mumewe na kesi inayomkabili dhidi ya Phina, na mambo ya familia yake yaliyokuwa yamejikoroga na kujikanganya mpaka akawa hajui hata mwisho wao ni upi. Sabina yupo jela. Kama asingekuwepo jela, inamaana angekuwa uraiani akisaidia kumshinda yeye. Mama yake amekamatwa ndani ya nyumba ya mganga wa kinyeji akitaka mumewe afe. Akabaki akilia mbele za Mungu hajui aseme nini juu ya familia yake. Alishamtumia baba yake pesa siku ileile ya jumatatu Chali aliporudi kutoka kwao na kueleza shida ya nyumbani kwao.

Kimeumana!

Kwa Phina&Ibra.

S

iku ya jumatano Phina na Ibra nao ikabidi kurudi Ustawi wa Jamii kushitaki na kuomba msaada wa mtu wa kuwawakilisha. Huko ndiko waligombana mpaka wakaondoka bila kuagana. Kwanza walimshangaa sana Phina. “Wewe si ulirudi hapa na kukanusha mambo yaleyale ambayo unasambaza huko mtandaoni!?” “Jack ndiye aliyenituma.” “Wewe binti unacheza mchezo hatari sana. Kwa nini unachanganya hawa wanaume kwa kiasi hiki!? Ulikuja na Ibra, mkamsema vibaya sana Naibu Waziri Msindai ambaye inasemekana alikuwa rafiki wa karibu sana na huyu Ibra.” “Ni enzi hizo.” “Sawa. Lakini mwenzio huyu alirudi tena hapa kukanusha yote mliyolalamika na kumshitaki Mheshimiwa Msindai! Tena yeye mwenyewe alituambia hata picha mlizotuonyesha ni za kutengeneza tu! Na Mheshimiwa Msindai ni mpinzani wako wa tokea zamani, hajui ni kwa nini wewe unamchukia kwa kiasi hicho!”

“Haiwezekani Phina!” “Ni vile nilivyokwambia Jack alinidanganya.” Phina akajaribu kujitetea lakini wazi alionekana kupatikanika. “Ndio uje unichafue kwa kiasi hicho!?” “Tena si hivyo tu maana na mimi nilikuwepo hapa.” Akadakia mwingine. Wakaeleza yote aliyokanusha Phina, tena kwa undani zaidi kama waliokuwa wakitaka kuwafarakanisha. “Halafu leo nashangaa mmekimbilia mtandaoni, hakika wewe binti ni mwaribifu na kina Msindai hawatakuacha salama. Leo unazungumza hiki, kesho unakuja kufuta! Umeanika mambo ya undani kama sio mwanamke wewe!” Akaongea kwa kuumia mama mtumzima kidogo waliyemkuta hapo hata siku ya kwanza walipokwenda kushitaki. “Ndio kazi zao hawa. Ndoa hawataki, wanasubiri kutuibia waume zetu na kujaa nao mtaani! Sisi tunakazi ya kuwalisha na kuwatumikia, wao wanakimbilia suruali tulizofua sisi. Wewe unajifananisha na mwanamke aliyefikishwa kanisani wewe! Ona ulipo na alipo mwenye mume!” Phina akaondoka bila ya kuongeza neno, na Ibra hivyohivyo, ila akiwa amekasirika vibaya sana.

Kwa Kina Msindai.

Siku ya alhamisi mzee Msindai akataka wakutane wote na huyo wakili. Kikao nyumbani kwa mama Msindai. Sabrina alikuwa amefunga tokea siku ya jumatatu. Ilikuwa asubuhi mida ya saa tatu akaona simu ya mzee Msindai ikiingia. Alishituka maana hakuwa amemsikia huyo mzee tokea siku alipotoka kumshika mama yake uchawi. Akapokea kwa haraka. “Shikamoo baba.” “Marahaba mama. Wajukuu wote hawajambo?” “Wote wazima.” Akajibu na kutulia. “Kesho ni siku ya mahakamani, nafikiri umeshaambiwa na Jackson.” “Ndiyo baba.” “Sasa simu hii nimekupigia kukuomba rasmi kama unaweza kuongozana naye.” “Huko mahakamani!?” Sabrina akauliza kwa kushangaa na mshituko mkubwa mpaka mzee Msindai akasikia.

“Ndiyo.” Akajibu mzee Msindai kwa kifupi na kumpa muda wakujibu. “Mashabiki wote wa Phina wale waliokuwa wakinitukana mtandaoni watakuwepo kesho. Wanasema watakuja kumuunga mkono Phina. Halafu…” Sabrina akasita akisikika amepaniki. Akajikuta machozi yakimtoka. Hakutaka kwenda kuonekana huko mahakamani mbele ya mashabiki wa Phina. Mzee  Msindai kimya upande wa pili. “Unafikiri ni muhimu na mimi kuwepo huko?” Akauliza na kukumbuka hapohapo kuwa anazungumza na mzee Msindai aliyemuomba amsamehe mumewe na amsaidie. Akajirudi kwa haraka. “Nitakuwepo baba.” Na machozi akajifuta. “Nashukuru sana. Sasa jioni tunatakiwa kukutana na wakili wake huyo Jackson. Nimemuomba tukutane nyumbani. Na Junior nimemuomba awahi kurudi nchini ili kesho na yeye awepo mahakamani na Jackson. Mimi sitaweza kuwepo mahakamani.” Sabrina akaona jinsi mzee Msindai alivyolichukulia hilo jambo kwa uzito.

“Nyumbani tunatakiwa tuje saa ngapi?” “12 na nusu nataka kila mtu awe ameshafika.” “Basi sitachelewa.” “Haya mama. Uwe na siku njema.” Sabrina akakata simu na kubaki akiwaza akitamani kikombe kingemuepuka asionekane na mashabiki wa Phina, ana kwa ana. Wabakiwe kumsema tu ila si kumuona uhalisia wake. Akajisikia kunyong’onyea. Akajisikia duni! Akaona ni kama anaenda kujianika zaidi. Alikuwa amefunga kula ila kunywa tu, akiombea hiyo siku ya kesho. Ukweli alikonda zaidi ya kawaida yake. Leo kuambiwa atokezee mahakamani na mumewe! Jack alikuwa amependeza na kuvutia kama Naibu Waziri haswa, Sabrina hakuwa hata na nyama ya nyongeza. Ikabidi kuanza kusaka nguo na kutafuta kujitengeneza.

 Kwa Mama Msindai&Jena.

M

zee Msindai akampigia simu Jena akamuunganisha na mama yake. “Nipo katikati ya kazi. Jena, upo na mama yako hapo.” Akaanza mzee Msindai. “Nakusikiliza baba.” Jena akajibu kwa heshima zote. “Wakili niliyekutafutia wewe na Jackson, ameshauri Sabrina ni lazima awepo kuonyesha yupo pamoja na mumewe katika kila jambo. Nimezungumza na Sabrina amekubali kutokea mahakamani kesho. Lakini kama nilivyowataarifu, nilazima tukutane jioni na huyo wakili, tuzungumze na kujipanga ili kuwa upande mmoja. Na Sabrina atakuwepo hapo nyumbani.” Wote wawili wakaelewa.

“Mimi nimeshakuahidi baba, sitarudia tena.” “Ninachotaka atulie, kesho aonekane yupo na mumewe si kwa kulazimishwa ila ni kwa kuwa anapenda kuwa na mumewe. Sabrina ndiye aliyeturudisha sisi wote kwa mumewe akimuombea msamaha kwangu, Junior na Jacinta. Yeye mwenyewe ndiye aliyetubu kwa makosa ya mumewe na kunifanya na mimi nijirudi na kufikia uamuzi huu. Amekusudia kusimama na mumewe. Sasa naomba usiku wa leo, kusiwepo mazingira ya kuharibu hiyo hali ndani yake. Sijui kama mama Junior umenisikia?” “Ndiyo.” Akajibu mama Msindai kwa kifupi tu. “Jena?” “Na mimi nimebadilika baba na …” “Jena? Nataka kusikia juu ya Sabrina, tafadhali. Nipo kazini.” Mzee Msindai akaongea kwa ukali haswa akisikika hataki kupotezewa muda. “Nimeelewa baba. Na sitaongea jambo la kuudhi mtu yeyote.” “Basi ni hilo tu. Muwe na siku njema.” Simu ikakatwa kwa wote wawili.

~~~~~~~~~~~~~~

Maombi Ya Sabrina Kwa Mumewe Yamepokelewa Kwa Uzito Mkubwa Sana. Amepata Uungwaji Mkono Na Mzee Msindai Mwenyewe.

Na Mzee Msindai Amekusudia Kufunga Kesi Siku Ya Ijumaa. Anapanga Timu Yake Vilivyo Kuhakikisha Hakuna Kosa Linatokea Siku Hiyo.

Je, Atafanikiwa?

Bado Phina Anao Mashabiki Wake Mtandaoni, Amepungukiwa Wakili Wa Kusimama Naye Mahakamani Kupambana na kina Msindai.

Je, Nini Kitaendelea?

Usikose Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment