Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 71. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 71.

Akaanza kuona tai inamkaba. Akailegeza kidogo. “Upo sawa dogo?” Akanyanyua uso kumuangalia kaka yake. “Vipi? Ushamaliza?” “Bado.” Akameza mate na kurudisha macho kwenye ile video. Bado Phina hakuwa ametoka. Wasiwasi ukazidi kumuingia, akajua baba yake atajua Phina alilala pale. “Umeangalia hii video mpaka mwisho?” Akamuuliza kaka yake kwa wasiwasi. Junior akasogea. “Tumeshaangalia. Ndio kiongozi alikuwa akishauri hapa, kuwa njia ya haraka ya kuwadhibiti ni kuwahi kuwashitaki. Sisi ndio tuwashitaki kwa kukuchafua na naona baba ameshaanza kulifanyia kazi.” Jack akamwangalia kaka yake na kurudisha macho kwenye ile video kuona kama Phina alitoka.

“Mbona umepata ushahidi mzuri tu, lakini umejawa wasiwasi?” “Hapana.” Akajibu Jack macho kwenye video. “Ni nini?” “Mbona Phina hatoki, kaka? Maana mimi nilimwambia atoke, nikapitiwa na usingizi. Na Mungu wangu ni shahidi kaka, nilipoamka hakuwepo.” “Mbona alionekana kutoka! Sogeza mbele, nafikiri ni baada ya kama dakika…” “35 hivi baada ya kuingia.” Akadakia yule bosi wake na kurudi kusogelea laptop yake. Acha nikusogezee mbele maana hata sisi pia tulisogeza mbele.” Akavuta ile laptop akasogeza mbele. “Huyu hapa anatoka. Tena inaonekana bado ni usiku, hata lisaa halikuisha! Mwendawazimu kabisa huyu mwanamke. Ameonjeshwa asali anataka kujenga mzinga! Mpuuzi wa mwisho!” Jackson akapumua kwa nguvu kusikia kiongozi wake yupo upande wake.

“Sasa dogo, acha mimi niwaache nikaweke mambo yangu sawa kabla ya safari. Naona mzee ameshaanza mchakato, mtawasiliana naye.” “Nashukuru kaka.” “Halafu hujaniamia Msindai. Ile dili ilitiki?” “Wapi! Nasukumana nao mpaka…” Jack akaona atoke maana walirudi kwenye mambo yao, akabaki kama msikiliza mambo yasiyomuhusu, akatoka taratibu na kuondoka bila yakuaga.

~~~~~~~~~~~~~~

Alipoingia tu ofisini kwake, ujumbe kutoka kwa baba yake na namba ya simu. ‘Mtafute huyu jamaa, ndiye atakayesimamia kesi yako. Weka mazingira ya kukutana naye leo bila kukosa. Nataka mwishoni mwa hili juma, niwe nimefunga hizi kesi zako. Zinanichukulia muda mwingi sana.’ ‘Naweza kukupigia?’ Hakujibiwa, ila baada ya dakika 15 akaona baba yake akimpigia. “Nakushukuru sana baba na samahani kwa usumbufu wote. Ila naamini umethibitisha sijadanganya.” “Umefanya kosa Jackson. Kosa linalonigarimu sana.” “Naelewa baba yangu. Na narudia tena kukuomba msamaha. Naahidi haitakaa itokee tena.” “Kutana na huyu mwanasheria mapema.” “Nampigia sasahivi nikiagana na wewe. Ila naomba nikuulize, baba.” Jack akawahi kabla baba yake hajakata simu maana alijua ni jumatatu inamaana juma ndio linaanza kwa mzee Msindai mwenye majukumu mengi, na hospitali yake kubwa anayoendesha. Hata Jena mwenyewe kuna siku tatu za juma hufanya kazi kwenye hospitali ya baba yake.

“Juu ya nini?” Mzee Msindai akauliza. “Hatima yangu na hii kazi. Nianze kutafuta kwingine?” “Hakuna mtu atakufukuza kazi. Tuliza akili kazini, usiharibu majukumu uliyopewa.” Hilo likamtuliza kabisa Jackson. Akajua kumbe baba yake tokea mwanzo alijua hatafukuzwa kazi! “Jambo la mwisho. Ni juu ya Sabrina. Yeye hajawahi kuniloga.” Baba yake akamuelewa. Lilikuwa ni kama swali akitaka uhakika, lakini kama anayeogopa ukweli, halafu kama anayemtetea. “Nampenda Sabrina tokea chuo na sijawahi kuacha kumpenda.” “Sabrina hajawahi kukuloga, Jackson.” Jack akavuta pumzi kwa nguvu kama aliyetuliwa mzigo mzito. “Nakushukuru baba yangu.” “Acha woga. Ongeza nidhamu kwenye hiyo ofisi.” Simu ikakatwa.

Kwa Waili, Wakili wa Msindai

Aliyemtoa Jasho Jackson.

B

ila ya kuchelewa Jack akampigia simu huyo wakili ila akakuta ameshajua nini chakufanya. “Nilikuwa nikimalizia kuangalia video yako nikilinganisha na malalamiko ya Phina. Nimeshayatoa kopi malalamiko yake yote huko mitandaoni na ninalinganisha na hii video. Baada ya muda mfupi sana Ibra na Phina watapokea barua zao za mashitaka.” “Nashukuru sana. Ungehitaji kuniona?” “Hakuna sababu. Ila ningependa kukusikia wewe binafsi kwanza ndipo nijue ninaendelea vipi kuanzia hapa.” “Unataka kusikia nini?” “Kuanzia mwanzo wako mpaka mwisho. Usiache chochote ambacho unajua kitanisaidia kwa haraka dhidi ya hao watu wawili. Mzee anataka tufunge hii kesi kwa haraka sana.” Jack akavuta pumzi kwa nguvu akifikiria pakuanzia.

Wakati akifikiria, ujumbe kutoka kwa Sabrina ukaingia. ‘Nataka kumtuma Chali apeleke matumizi nyumbani. Kwa jinsi nilivyozugumza na baba, wana hali mbaya.’ Jack akausona na kufikiria kwa haraka akarudi kwenye simu. “Naomba nikupigie baada ya muda mfupi. Nataka kuzungumza na mke wangu.” Kabla Waili hajamjibu, Jack akakata simu na kumpigia mkewe, akimuacha huyo wakili akishangaa. Anawezaje kukatiza mazungumzo muhimu kama hayo!

~~~~~~~~~~~~~~

“Wote mliamka salama?” “Wote tupo salama. Vipi kikao?” Sabrina akauliza. “Kilienda vizuri. Nilikuwa kwenye simu na wakili atakayeniwakilisha kwenye kesi yangu. Ndio nimemwambia anisubiri ili nizungumze na wewe.” “Ushanichanganya! Una kesi gani tena?” “Mzee Msindai amepata ile video. Anataka tumshitaki Phina kwa uongo anaosambaza mtandaoni na Ibra.” “Kwa maana nyingine baba amepata kitu alichokitarajia kwenye hiyo video?” “Sijadanganya, Brina.” Sabrina akaanza kucheka.  

“Umepoteza imani kabisa na mimi!” “Acha kuanza kukasirika bwana Jack! Sasa unasemaje juu ya ujumbe niliokutumia?” “Wewe  mtume tu. Unataka msaada wowote?” “Hapana. Nina kila kitu nilitaka tu kukutaarifu.” “Basi acha niendelee na huyu wakili. Tutazungumza baadaye.” “Asante kwa kujali na kupiga.” “Nakupenda Brina.” Sabrina akacheka. “Ndio utulie.” Sabrina akajibu hivyo na kukata.

Jack akampigia tena. “Tulia Jack, fanya kazi.” “Jana ulinipa wakati mzuri Brina, leo unataka kunichanganya tu, niharibu kila kitu!” “Haya nakupenda Jack, mume wangu. Baba watoto wangu. Mupenzi. Umeridhika?” “Kama unamaanisha!” “Namaanisha Jack. Usikasirike bwana! Tena leo nimefunga kwa ajili yako ili kila kitu kiende sawa. Mungu akufanikishe hata ambako hustahili” Hapo akamtuliza Jack. “Nashukuru Brina. Basi nitakupigia baadaye kukupa taarifa ya kinachoendelea.” “Sawa. Na usiogope.” Akakata. “Jack!” Sabrina akabaki akimfikiria mumewe. “Sasa sijui kama anakumbuka kama yeye ndio amenikosea! Anataka tena mimi ndio niwe nambembeleza tena!” Sabrina akawaza na kucheka akimfikiria mumewe.

~~~~~~~~~~~~~~

Akarudisha simu kwa wakili ambaye hata sura hakuwa akimfahamu. “Nataka kukupa historia fupi kati yangu mimi, Ibra na Phina.” Jack akaanza moja kwa moja mara baada ya Waili kupokea. “Nakusikiliza.” Akamuelezea kuanzia walipokuwa chuoni, walipomaliza na kumtafutia Phina kazi. Urafiki wake ulipoisha na Ibra. “Subiri kidogo Mheshimiwa. Naomba turudi nyuma kidogo. Inamaana kilichomkasirisha Ibra ni wewe kumuoa tu Sabrina, au kulishakuwa na matatizo mengine?” Akauliza huyo wakili.

“Pengine kama mimi sikuyagundua mapema. Ila ninachokumbuka ni yeye kutoafikiana na mimi kumuoa Sabrina, tena akiwa mjamzito wa mimba ya mtu mwingine.” “Kwa maana ingine hata yeye alijua kama unajua kuwa Sabrina ni mjamzito kabla ya kumuoa?” Waili akataka uhakika kutokana na shutuma zinazoendelea mtandaoni. “Ndiyo. Na mimi ndiye niliyemwambia. Kwa hiyo sasahivi wanadanganya kusema eti mimi nilimwambia Phina kuwa nataka kumuacha mke wangu kwa kuwa alinibambikizia mimba! Si kweli. Na yeye Ibra nishahidi yangu maana hicho ndicho kilichomuudhi zaidi akisema inawezekana Sabrina ananiloga. Si kawaida. Na hata kwenye harusi alikataa kabisa kuja.” Akatulia kidogo kama anayeandika.

“Okay. Endelea.” Jack akaendelea kumsimulia mpaka siku wanakutana na Phina nchini Uswiz. “Na kilichoendelea ni kama ulichokiona kwenye video.” “Video haina sauti Mheshimiwa Msindai. Nataka kujua mlichozungumza tokea anagonga mpaka mnaachana.” Ikabidi Jack asimulie tena. Hakuacha neno hata moja japo kwa mkewe hakutaka kumwambia Phina alichomwambia ila kwa wakili wake akaongea yote aliyoambiwa mpaka kumdhoofisha na kumrukia Phina bila kufikiria mpaka alipofunga goli ndipo akili ikamrudia kuwa ameoa, na amefanya mapenzi na mwanamke asiye mkewe.

“Mimi si dhaifu. Ila sijui ilikuaje!” Jack akajitetea na kuendelea kueleza kilichoendelea mpaka Ibra kufanikisha kumleta Phina nyumbani kwake. “Inamaana wewe hukujua kama Phina atakuwepo miongoni mwa marafiki wanaokuja kuwatembelea nyumbani kwako?” “Phina sio rafiki yangu mimi wala wa mke wangu. Mahusiano yaliishia chuoni.” “Ulimtafutia kazi na kulala naye tena baada ya kuoa.” Waili akamrekebisha. “Lakini hapakuwa na muendelezo hata wakuhisi kama anaweza kuja kunitafuta baadaye kwa hitimisho tulilokuwa nalo nchini Uswiz!” “Baada ya mapenzi?” Hilo swali likamuudhi Jack.

“Unataka nikwambie kilichokuwa kikiendelea au?” Jack akauliza kwa jazba kidogo. “Lazima tuwe ukurasa mmoja na uelewe aina ya maswali, maana haya ninayokuuliza unaweza kuulizwa na wakili wa Phina akitaka kuthibitisha anachokizungumzia Phina na Ibra. Kuwa ulimuahidi ndoa baada ya kumuacha mke wako, na ndio maana ulimkaribisha nyumbani.” Akamuweka sawa na kuendelea. “Huyu Phina alikuwa mpenzi wako wakati ulipokuwa na Sabrina. Si ndiyo?” Jack kimya.  

“Kwamba kuna kipindi ulikuwa na hawa wanawake wote wawili kwa wakati mmoja. Na palikuwa hakuna mipaka kati yao. Kwamba Sabrina aliweza kufika ulipokuwa na Phina na Phina hivyohivyo. Si ndivyo?” “Hapana! Sivyo.” Jack akakanusha kwa hasira.

“Sabrina ni mke wangu! Hata kama nimechanganyikiwa kwa kiasi gani, nisingeweza kumleta Phina niliyekosea naye karibu ya mke wangu!” “Lakini kama nilikusikia vizuri na hakuna nilichokosa kutoka kwenye maelezo yako ya muda mfupi uliopita, unaweza kunirekebisha lakini.” “Juu ya nini?” “Kwamba ulishakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Phina, na Sabrina alikuwepo karibu yenu.” Kimya. “Na kwa kuangalia hii video ulionekana wewe mwenyewe kumfungulia mlango.” “Si nimekwambia aliniambia ana kitu muhimu cha kuzungumza na mimi! Au hukusikia?” Jack akauliza kwa hasira.

 “Utanirekebisha tena, Mheshimiwa Msindai. Mlikuwa hotelini, ambako kuna mgahawa sehemu ya chini. Lakini ulikubali mazungumzo yenu myafanyie chumbani kwako ambako kwa maelezo yako, tayari ulikuwa nusu uchi! Ni kama mtu ambaye hukutaka kuweka mipaka kati yenu! Na ni kama ambaye ameshazoezwa, tena na wewe mwenyewe kufika popote pale. Ndio maana hapakuwa na shida kufika nyumbani kwa mkeo.” “Hiyo sio kweli.” Jack akakanusha.

“Narudia tena. Mimi nipo upande wako Mheshimiwa. Lakini nataka ujiandae, haya ninayokuuliza unaweza kuulizwa na wakili wa Phina kuthibitisha kuwa nyinyi bado mlikuwa kwenye mahusiano. Kwa msichana wa kawaida tu, ambaye hampo kwenye mahusiano, asingeweza kumfuata Naibu Waziri kwenye chumba anacholala, tena usiku ambao anajua ameshalala! Isipokuwa hawa watu wapo kwenye mahusiano ya karibu sana. Sijui kama unanielewa?” Kimya.

“Kilichoendelea ndani, baada ya wewe kumfungulia mlango inamaana kilitarajiwa kati yenu wote wawili. Halikuwa jambo geni, na Phina hakuonekana kuvuka mipaka kwa kuwa hakuvunja mlango, wewe ulimfungulia. Hakukubaka au kukufanyia fujo, ila matokeo ambayo inaonekana mliridhia nyinyi wote wawili na ndio maana palikuwa na ukimya kati yenu mpaka swala la ujauzito lilipotokea. Si ndivyo?” Kimya.

“Naomba tuzungumze Mheshimiwa Msindai. Maana hii kesi mzee wako anataka ifungwe kwa haraka.” “Nakusikiliza.” “Kwa hiyo unaelewa ninachozungumzia?” “Sasa unataka kunisikia nikikwambia nini?” Na yeye Jack akamuhoji kwa jazba. “Uelewe kile ambacho kinapelekea jamii kubwa kumuunga mkono Phina. Nimefuatilia posti zake na kusoma kila comments kutoka kwa mashabiki wake. Nataka na wewe uwe upande ambao hujajifunga, ila ukiwa na akili wazi ili tuweze kumaliza hili jambo.” “Mimi nakwambia ukweli wa mambo ulivyokuwa.” “Basi tuendelee.” Jack akataka kumkatia simu ila akakumbuka na yeye yupo kazini, anatakiwa kurudisha majibu ya kueleweka kwa mzee Msindai. Akajaribu kujirudi na kuendelea.

“Ndio akafika na Ibra. Wakamkabidhi mke wangu bahasha na kumwambia Phina ni mjamzito wa mimba niliyompa mimi.” Jack akaelezea kwa ufupi akificha yale waliyoyafanya akisaidiwa na Jacinta. “Kwa hiyo unakubali kuwa Phina alikuwa na mimba yako?” “Hapana! Hata kidogo. Sikumkuta ni bikra na wala sijui kama ni mimi peke yangu ndiye niliyekuwa nikijamiiana naye kwa wakati huo.” “Uliona picha za Ultrasound ya mtoto aliyekuwa amebeba?” “Hapana. Na pia sio kithibitisho kuwa alikuwa ni mtoto wangu na ndio maana nilimwambia nipo radhi kupima DNA mtoto atakapozaliwa kuthibitisha kama mimi ndio baba wa mtoto, lakini sikutaka kufanya naye vipimo akiwa mjamzito kama ni kweli alikuwa mjamzito ili tusimzuri mtoto. Kwa kifupi hakuna aliyethibitisha kama kweli alikuwa mjamzito. Na nikweli nilimwambia tutafanya DNA mtoto akizaliwa. Sasa kama ningekuwa nataka kuanzisha naye familia, ni kwa nini nitake tena kufanya DNA?” “Pengine hukutaka kurudia kosa kama anavyosema ulifanya kosa kwa mkeo, ukamuoa akiwa mjamzito akakudanganya mimba ni yako lakini si yako!” Jack akafunga macho kwa hasira.

Hakujibu. “Mheshimiwa Msindai?” Waili akaita akitaka kujua kama bado yupo au alishakata simu. “Kwa kuwa sio kweli!”  Jack akajibu. “Hakimu na wengine wote hawajui hilo. Sijui kama unanielewa? Anaweza kusema kutaka kufanya DNA ilikuwa ni njia sahihi kwako ili usirudie kosa, uanze naye pazuri.” “Naomba nikuage kwa sasa?” “Sawa. Lakini nilazima kumalizia haya mazungumzo na…” Jack akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~

D

akika 10 hazikuisha, akaona simu ya mzee Msindai. Akajua ameshapata taarifa. Akajaribu kutulia ndipo akapokea. “Kabla hujaongea chochote baba, jua na mimi nimekasirika sana. Wakili uliyenitafutia ni kama ananihukumu na wala si kunisaidia!” “Ulielewa chochote juu ya kutaka kwangu kumaliza hii kesi kabla ya juma hili kuisha?” “Nilielewa baba, lakini..” “Simu inayofuata kutoka kwa Waili iwe yakutaka muongozo baada ya kumalizana na wewe, Jackson. Umenielewa?” “Ndiyo.” “Hakikisha yeye ndiye anayekuaga. Nikimaanisha kusiwe na muingiliano wowote mpaka atakapomaliza yeye.” “Sawa.” Jack akakubali, simu ikakatwa. Akatamani kuirusha ile simu lakini akakumbuka huyo wakili anasubiria simu yake ili arudishe majibu kwa mzee Msindai. Akapoa.

Mtaka Cha Mvunguni, Sharti Ainame.

Kwa Wakili Tena.

Akampigia tena Waili, ikapokelewa kwa haraka kama aliyekuwa akimsubiria na simu mkononi. “Uliishia kukubali kumsaidia mpaka atakapojifungua, ndipo mkafanye DNA.” Bila kupoteza muda Waili akapokea na huo muendelezo. “Lakini ilikuwa ni njia ya kumfanya atulie ili nijipange.” “Narudia tena. Hayo ni maneno yako wewe, lakini vitendo na anachozungumza Phina, ulishakubali hata kulipia kliniki yake, na kumtunza yeye kama yeye akiwa mjamzito.” “Ni kweli.” “Hiyo inamaana mlikuwa kwenye mahusiano ya kama wazazi mpaka ulipomkimbia.” “Ndiyo.” Jack akajibu kwa jeuri na kunyamaza.

“Sasa huu ndio ushauri wangu na nitakutaka usimamie hapo. Chochote kilichoendelea kati yako na Phina baada ya kulala naye Uswiz, futa kana kwamba hakijawahi kutokea wala kuzungumzwa kamwe hapa duniani. Sijui kama unanisikiliza?” Kimya, Jack akisikiliza upande wa pili bila ya kumjibu, yeye akaendelea akijua amekasirika. “Wewe hukujua swala lake la ujauzito wala hukumuahidi kumlea yeye na mtoto. Unanielewa Mheshimiwa Msindai?” “Na swala la kuja nyumbani?” “Hilo nimeshazungumza na mzee, hapa nasubiria waraka nitaletewa mapema tu, kuwa walikuja kukufanyia fujo nyumbani ukiwa haupo, wakatolewa na mlinzi, na uliwashitaki. Safari hii wanapopelekewa shitaka lao la kudanganya na kukuchafua mtandaoni Phina akitumia siri za ofisi, kwa upande wako na hilo litakuwa moja wapo. Watashitakiwa kwa kuvamia familia yako na kufanya fujo nyumbani kwako kisha kukimbilia mtandaoni na kusambaza uongo.” Akamueleza mengi wakijipanga kwa hiyo kesi ambayo inamashabiki wengi, mpaka kweli akaridhika na kumuaga. Jack akabaki ametulia hapo mezani simu mkononi asiamini jinsi alivyopozwa na hiyo starehe ya muda mfupi!

~~~~~~~~~~~~~~

Akabaki akifikiria watu aliowaingiza matatizoni kwa kushindwa kusema hapana kwa tamaa iliyomuwaka na kuituliza kwa starehe iliyogeuka kuwa chungu kuliko shubiri. Akamuhurumia sana Phina. Akajua kwa hakika atalipa anachokifanya, tena atalipa kwa uchungu mkubwa sana. Alijua baba yake hawezi kumsamehe. Lazima atamuadhibu vibaya sana. Akatamani angemuokoa tokea mwanzo hutoka huko anakopitishwa na Ibra, na yeye mwenyewe kujianika mitandaoni. Alimjua Phina. Alikuwa msichana mtaratibu sana, ila akajua kwa kushindwa kwake kusema hapana kwa tamaa ya mwili iliyomuwaka gafla na kumrukia kimapenzi, kumeleta maafa makubwa kwake na kumtibua moyo wake, akajiachia na yeye shetani anatumia uchungu wake na hasira, kumtesa akihaha huko mitandaoni. “Phina yupo kwenye uchungu wa kupoteza mtoto pia na kutolewa kwenye ofisi iliyokuwa ikimneemesha.” Jack akajikuta akimuhurumia badala ya kumchukia vile anavyomchafua. Aliziona siku zake ambazo hatakuwa na hao mashabiki tena, mzee Msindai amemfikisha kwenye adhabu yake! Jack akajikuta akivuta pumzi kwa nguvu na kutulia.

Majuto yakamrudisha kwa mama yake na adhabu anayopokea kutoka kwa baba yao. “Jena!” Japokuwa mengi alijitafutia mwenyewe Jena, lakini yeye alitoa sababu ya anguko lake. Hekaheka anayoingiza familia nzima! Kaka yake aliacha shuguli zake, akaja hapo ili tu kuongeza uzito kwenye mazungumzo yake na bosi wake! Kweli ilisaidia, lakini ni usumbufu wa starehe ya muda mfupi sana aliyoipata. “Jacinta!” Akazidi kuhesabu maafa aliyosababisha hata kwa huyo dada yake na kumuhurumia, akijua yeye ndio miguu na mikono ya baba yao. Inamaana hapumziki yupo kwenye kutekeleza tena kwa haraka kila anachotumwa na baba yao ili kusafisha maafa aliyoyasababisha mbali kabisa na nchi! Hapo ndipo akamfikiria baba yake kwa kumuhurumia. Muda na pesa nyingi anayotumia kwa ajili ya hilo tu! “Umri alio nao alipaswa kupumzika na kutumia uzee wake vizuri!” Jack akazidi kujihukumu.

“Masikini Sabrina wangu!” Akamuhurumia mkewe. Yupo kwenye mfungo akiwa ananyonyesha ili tu kusaidia yeye kusafisha uchafu wake! Aibu aliyomuingiza. Maneno machafu yaliyosambaa mitandaoni wakimfananisha muonekano wake na Phina. “Wamemchafua Sabrina wangu kwa starehe iliyogeuka kuwa chungu kuliko shubiri!” Akawaza na kuumia sana moyoni.

Akatamani hiyo kesi iishe kwa haraka kila mtu apumzike. Lakini hofu nayo ikaanza kumsumbua akijiuliza iweje Phina apate wakili mzuri atakayemuhoji zaidi na alivyohojiwa na Waili! “Akinibana kwa maswali magumu zaidi mpaka nikashindwa kujieleza!” Jack akajiuliza kwa hofu. “Inamaana hii hali haitakaa ikaisha! Bado kutaendele….” Jack akabaki akiwaza siku ya mahakamani. Akaona mamilioni ya watu watakavyojaa na kushuhudia aibu yake. Akazidi kuingiwa na hofu akijutia kumfungulia mlango Phina usiku ule. “Bora ningefanya kama alivyosema Waili. Kwenda kuzungumza naye chini sehemu ya Mgahawani kuliko nilivyomfungulia mlango! Kweli zinaa ni ya kukimbia.” Akazidi kuwaza Jack asijue…

~~~~~~~~~~~~~~

Majuto, ni Mjukuu…

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment