Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 69. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 69.

Sabrina akabaki akimwangalia mumewe. Jack akameza mate kwa wasiwasi kama anayetafuta pakuanzia, kisha akapata. “Unajua hao walinzi wanawasiliana na..” “Jacinta?” Sabrina akamuuliza. “Na mimi nilihisi hivyo, lakini sasahivi sijui itakuwa ni baba! Mpaka nahisi kuwa Jacinta ndiye anayetumwa kazi za baba! Hana analofanya yeye mwenyewe ila kwa kupitia baba.” Sabrina akafikiria kwa haraka. “Kwa hiyo hapa ameshajua kama baba yupo hapa?” Sabrina akauliza, Jack akamkabidhi simu yake.

“Soma huo ujumbe wa pili.” Sabrina akasoma. ‘Sabina hatatoka sasahivi, kwa kuwa nipo kwenye kutuliza fujo aliyoanzisha mtaani. Tutazungumzia hilo patakapotulia.’ Ujumbe huo ukaishia hivyo. Sabrina akamaliza kusoma mpaka mikono ikaanza kutetemeka. Akamrudishia simu Jack. “Sabrina?” “Naomba ukale Jack na umwambie baba anisubiri.” “Unakwenda wapi?” “Kuzungumza na Mungu wangu. Hapa nilipo, sasahivi, nilipita nilipokuwa Moshi. Nilikuwa sijui chakufanya, Mungu akanitendea. Sasahivi pia sijui chakufanya Jack.”

“Niliacha kuzungumza na Mungu wangu tokea usiku aliponifuata Phina hapa. Nimepoteza mawasiliano kabisa na Mungu. Acha nimlilie yeye ambaye hajawahi kuninyamazia. Yeye ambaye hajawahi kunichoka. Anayeweza kunibeba kwenye magumu. Anayenitumia suluhu ya mambo magumu na mazito ambayo hata wanadamu hawana majibu nayo. Acha nirudi kwake. Naamini atanijibu tu, naomba muda.” “Basi na mimi uniombee kikao cha kesho, Brina. Tafadhali mke wangu.” “Si uombe mwenyewe!” “Wewe unataka mbingu nzima inyamaze na maombi yote yasijibiwe.” “Mungu hajakukasirikia Jack.” “Basi wewe zungumza naye kwa niaba yangu. Wewe huwa Mungu anakusikia Brina. Ona tu kwa leo jinsi ambavyo tayari nilivyopata uungwaji mkono! Sasa mwambie huyo Mungu na kesho awepo kwenye kikao.”  Jack akatoka na kumuacha Sabrina akimwangalia.

Kwa Mungu Wa Yasiyowezekana!

A

lipojiridhisha amebaki peke yake, Sabrina akarudi sehemu anayoimudu ambayo ameshajua hana mipaka ya kuzungumza. Hana hukumu kwakuwa hukumu yake ilishafutwa msalabani. Msamaha ni wa uhakika. Ni kiasi cha kurudi tu na kuita Baba! Akapiga magoni pembeni ya kitanda ila akainamia magoti kwamba hata ukiingia chumbani hutamuona. Akaanza kama kawaida yake. Kutubu kusikoisha na kumlilia Mungu asimuache. Akamkumbusha jinsi alivyompitisha kwa hili na lile akiwa hana tumaini kabisa. Akaomba hapo zaidi ya lisaa ndipo akamaliza.

Alitoka hapo na nguvu ya ajabu moyoni akiamini kila kitu kinawezekana. Akapata utulivu mzuri nafsini mwake. Akakuta baba yake ameegemea kwenye kochi, amelala usingizi mzito. Akaenda kumuandalia sehemu ya kulala, akamuamsha. “Nenda kajilaze kitandani kidogo. Ukiamka ndipo tuzungumze.” Hakubisha. Sabrina akamuongoza njia mpaka kwenye hicho chumba, akashukuru na kulala. Akamkuta Jack ametulia kimya sebuleni. “Umependa chakula?” “Nimependa. Nashukuru.” Wakabaki wakiangaliana.

“Nini?” “Nikikwambia uje upumzike hapa, utakubali? Nakuona unashuguli nyingi Brina! Huwa unapata muda wa kupumzika kweli!” Sabrina akacheka na kwenda kukaa hapo pembeni ya Jack. Akavuta pumzi kwa nguvu, akatulia. “Unataka ukajipumzishe kidogo?” “Hiyo timu yako inaamka sasahivi. Watataka kula, kuogeshwa, na mengine kibao, Pina peke yake hawezi. Acha nikae tu hapahapa.” Wakatulia.

~~~~~~~~~~~~~~

“Unafikiri wazazi wamejua?” Sabrina akamwangalia. “Na maanisha kwa hili lililotokea kwangu na Phina?” “Sijui Jack.” “Itakuaje kama wamejua?” Sabrina akakunja uso. Akafikiria, akamwangalia Jack. “Naomba kuanzia sasa, tujibu kile kinachotujia. Tusiazime matatizo ya kesho. Kama sasahivi, naomba jiandae vile utakavyozungumza kesho mbele ya kaka yako na bosi wako, Waziri wa Fedha.” “Lakini la Sabina ni la sasahivi.” “Bado halijaja. Tunahisi ndicho kilichomleta. Hajasema. Naomba tutulie Jack.” “Na kama ndicho kilichomleta?” Sabrina akajua ameshaingiwa hofu. “Naomba ya Sabina niachie mimi na familia yangu. Na usiniulize tena maana sina jibu lolote. Nitajibu kutokana na atakachoniambia baba. Kwa hiyo tulia.” Jack akajirudisha nyuma ya kochi akajiegemeza.

~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakati wanakula, baba yake akatoka huko chumbani akimuita Sabrina. “Nipo huku sebuleni baba. Nikutayarishie maji uoge?” “Naona tuzungumze kwanza.” “Unataka nije huko chumbani?” “Naona huku itakua pazuri.” Akamgeukia Jack. “Twende.” “Brina! Hataona nawaingilia?” “Wewe si mume wangu na mahari alipokea! Sasa siri ipo wapi? Twende.” Wakaongozana. Na kweli baba yake akaonekana kama kutofurahia ujio wa Jack.

“Wewe zungumza tu baba. Wala usiwe na wasiwasi. Hata kama asingekuwepo hapa, ingenilazimu baadaye kumwambia, labda iwe ni mambo yetu ya familia. Hayahusiani na ndoa yangu.” “Mchanganyiko.” “Basi usiwe na wasiwasi. Wewe zungumza tu baba. Mambo mengi ya nyumbani yeye aliyajua hata kabla yangu. Mipango ile iliyokuwa ikiendelea mkijipanga kinyume yangu, yeye alikuwa akijua hata kabla yangu. Kwa hiyo hakuna siri.” Baba yake akatulia kwa muda akiwa amekaa hapo kitandani. Sabrina naye kimya kama anayempa nafasi. Jack naye akatulia.

“Hali ya nyumbani sio nzuri.” Akaanza tena. Sabrina kimya. “Kama unavyojua tulikuwa tukimtegemea sana Sabina.” Kimya. “Ndipo akaja kuongezeka na Tino.” Wote kimya wakimsikiliza. “Tino alikuja kuwa msaada mkubwa sana pale nyumbani. Sasa mama yako alikuwa na jinsi ya kuwasiliana naye hata anapokuwa nje ya nchi. Sasa hapa majuzi Sabina alipofungwa, mambo yakawa magumu sana pale nyumbani tukawa tumeishiwa kabisa. Mama yako akamtafuta Tino kuomba msaada. Lakini mambo naona hayakwenda vizuri.” “Unamaanisha nini?” Hapo Sabrina akauliza akitaka baba yake awe muwazi zaidi.

“Tino ameanzisha malalamiko. Anamlaumu sana mama yako na Sabina kumponza kwenye swala la watoto wake.” “Ni watoto wangu mimi.” Hapo Jack akadakia. “Kwa uharaka mtakao tumia kuupokea huo ukweli na Tino mwenyewe, itawasaidia sana. Kitendo cha kuendelea kuwatambua binti zangu kama ni wa Tino wakati hata nyinyi wenyewe mlimtelekeza Sabrina, mimi nika…” “Jackson!” Sabrina akashangaa sana.

“Hapana Sabrina. Nimenyamaza naona naonekana mjinga. Napokonywa haki yangu hivihivi najiona! Mnanidhulumu bila sababu!” Jack akaendelea. “Mlikuwa wapi jamani kipindi chote Sabrina ameondoka nyumbani, ametelekezwa na mimba mpaka mimi nikamfuata? Mbona mnakuwa wepesi wakusahau? Mnapata wapi haki yakugawa binti zangu vile mnavyopenda nyinyi? Eti Sabrina?” Sabrina akashangaa na yeye anajumuishwa. “Ni wapi baba akikosa anapokonywa watoto?” Sabrina alibaki ametoa macho.

“Na nyinyi wazazi, mnapata wapi ujasiri wakuingilia familia ya mtu na kuanza kugawa watoto wao jamani? Mmenikosea sana. Mmevuka mipaka ambayo hakuna mila wala kabila au hata sheria yeyote ile hapa duniani inawapa ruhusa ya kufanya mnachonifanyia na binti zangu. Si sawa, na mimi nawasemelea kwa Mungu. Hakika katika hili, Mungu aingilie kati na ahukumu kwa haki. Mmenitenda isivyo sawa kabisa.” “Jack, umekasirika na…” “Hapana Sabrina. Kukasirika si neno sahihi. Nimeumia. Naumia sana.” Sabrina akashindwa hajui aseme nini mbele ya baba yake.

“Nimelea wale watoto tokea wanazaliwa! Mimi ndio mtu wa kwanza kuwashika tokea waje hapa duniani! Tena wakati huyo Tino akiendeleza starehe zake na mambo yake huko nje ya nchi akikwepa kuwajibika! Leo imekua ni kama pipi! Nawekewa mdomoni na kutolewa kwa vile mshika hiyo pipi anavyojisikia! Sina uhakika kama kesho watakuwa wangu au la! Wamekua ni fimbo kwangu! Lakini kumbukeni Mungu anaona.” Jack akanyanyuka na kuondoka. Pakazuka ukimya.

Adui Wa Mtu.

“Ila ni afadhali hivyo alivyoondoka ili nikwambie ukweli Sabrina. Nilishindwa kuwa muwazi. Ninapokwambia hali si nzuri, namaanisha hali si nzuri kwa sababu kama nilivyokwambia. Tino amewageuka kabisa mama yako na Sabina. Kumbe tena kuna pesa ya watoto ilikuwa benki, wao wakaitafuna yote.” “Kwani wewe hukuwa ukijua?”  “Wewe unamjua mama yako na Sabina. Ni marafiki wa karibu sana. Wanafichiana siri na mimi huwa wananikwepa kwa kuwa huwa nawaambia ukweli. Hata safari hii ni kama nimesikia kwa bahati mbaya kwa kuwa mama yako alinisihi niwepo wakati akizungumza tena na Tino maana ni kama mara yao ya mwisho alikataa kabisa kuzungumza naye. Ndipo Tino akaomba sasa aniambie ukweli.” “Ukweli gani?”

“Kuanzia mwanzo jinsi walivyomshawishi kuanzisha vita na Jack mpaka kufika walipofika hapo. Tino anasema amekuja kuchunguza juu ya familia ya Msindai. Amegundua ni familia inayoogopewa na watu wanaowafahamu undani wao, na baba yao ndio mkongwe wa mambo ya hii nchi. Kumbe huyo mzee Msindai ni hatari sana sivyo kama hivyo anavyoonekana. Ametumia neno kuwa ni kama Joka kali sana linalotisha. Anasema ni kama mti ulioweka mizizi yake hapa nchini tokea enzi za awamu hizo za Mwinyi. Amejaa kila mahali na ana mizizi ya miaka kwa karine. Tino anasema huyo mzee ameshikilia Usalama wa Taifa ipo kiganjani, wote waliopo ni mtandao wake yeye huyo Mzee. Anaogopewa sana. Kila unapolitaja hilo jina sehemu, watu wa Usalama wanakunyaka. Inavyosemekana yeye mwenyewe huyo mzee ndiye muongoza mambo.” Baba Sabina akaendelea kwa sauti ya chini, kama asiyetaka kusikika.

“Anasema yeye alipokutanishwa na huyo Mzee, alihisi ndio mwisho wa maisha yake. Anasema anatisha kuliko atakavyoeleza na mama yako na Sabina ndio wamemuingiza chini ya mkono wa huyo mzee, hatakaa akapata binti za…” Hapo akasita.

“Ameomba, tusimtafute tena. Amesema yeye anakusubiria wewe tu. Na amesema, chochote tunachotaka kwake, iwe kimetoka kwako kwa sababu ametuona sisi wote sio waaminifu. Tulimtumia vibaya ili kujinufaisha. Anasema haamini mtu yeyote pale nyumbani kwetu na hao watoto. Anasema yupo radhi kuweka hata kwa maandishi kuwa kamwe, mabinti zake wasije wahi kulelewa pale nyumbani, bora kwa kina Msindai wanaoonekana kutumia nguvu nyingi kulinda wanae, kuliko sisi tunapigania pesa zake kwa jina la wanae.”

“Anasema kitendo cha kukamatwa kikatili kiasi kile kwa ajili ya binti zake, na vitisho alivyopewa na mzee Msindai mwenyewe, amekifikiria, amewaheshimu sana kina Msindai. Anaona hata akiondoka hapa duniani, au hata asipoona hao watoto milele, anajua kwa hakika wanae watapata kile ambacho yeye alikosa akiwa mtoto. Familia inayowahitaji, kwa kuwa mzee Msindai mwenyewe amemwambia, hakuna mwanadamu atampokonya wale watoto. Ni wake yeye mzee Msindai. Ni kina Msindai na si vinginevyo. Anasema hilo lilimtoa hapa nchini kwa amani kabisa, akijua wanae wapo upande sahihi.” Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu.

“Hichi alichokizungumza Jack hapa, hata Tino ametuambia. Sisi ni wazazi wa ajabu kwa kuwa aliishi na wewe, alishatuona jinsi tulivyokutenda. Akajutia jinsi alivyosahau ubaya wetu, akaungana na mama yako pamoja na Sabina kukuangamiza tena. Tino ameonya mawasiliano na sisi. Na amesema tukiendelea kumtafuta, atatushitaki.” Sabrina akashangaa ila akaona anyamaze.

“Ubaya wa yote haya, unafika kwenye maamuzi ya mama yako. Na ndio maana leo nimekuja kuzungumza na wewe japo sikupanga kuongea na ya Tino, ila nimejikuta nikikwambia tu.” Sabrina akakunja uso. “Anauza kidogo tulichonacho kwa ajili ya ushirikina.” Sabrina akashituka sana. “Anamloga nani sasa?!” “Amekuwa kama amechanganyikiwa! Yeyote aliye kinyume naye. Na anafanya dawa, Sabina atolewe. Sasa mimi namwambia, anamaliza kidogo tulicho nacho, mbona Sabina mwenyewe hatolewi! Kutwa anakuja na mahitaji mapya ya mganga yanayomlazimu kuuza vitu vya pale ndani au vya Sabina mwenyewe.” “Subiri kwanza baba. Upo hapa kuniambia mama ananiloga?” Kimya.

Sabrina akajua ni kweli. “Sasa mimi nimemfanya nini mama mpaka kutaka kuniloga?” “Anakulaumu kwamba wewe ndio chanzo ya yote. Kwamba umeshindwa kumtii. Kama ungemtii tokea mwanzo, inamaana Sabina asingefungwa, na sasahivi Tino angekuwa upande wetu.” Sabrina akachoka kabisa.

“Nakuomba uwe makini Sabrina. Ni hilo tu mama.” “Wala usiwe na wasiwasi baba yangu. Mtetezi wangu, Yu hai. Na najua hata mpaka sasahivi tunavyozungumza hapa ni kwakuwa Yeye yupo vitani kwa niaba yangu. Ila tu, wewe ndio ukamwambie mama, kama nilivyomuonya kwa Sabina, wakakataa kunisikiliza, na safari hii mwambie namuonya tena. Aache anachokifanya. Anacheza na mboni ya jicho la Mungu.” “Wala hajui kama nipo hapa. Mimi nimetoka tu nyumbani na ndio maana nilitaka kugeuza palepale getini ili asijue kama nipo hapa.” Sabrina akazidi kuumia.

“Kwamba mlipanga hapa kwangu msiwahi kukanyaga!?” “Anasema hujawahi kutukaribisha.” “Naomba katika hili uwe mkweli baba. Si mama aliyekataa kuwa karibu na mimi akisema namtaka aje ili anisaidie kunilelea watoto wa Msindai?” Baba yake kimya. “Au umesahau baba?” “Nakumbuka.” “Sio nilikuja nyumbani kwa wema, akakataa kunipokea mimi na wanangu, hata ndani hajatukaribisha! Tena ni kama alirudia maneno yaleyale, kuwa namtaka ili aje anisaidie kulea! Nilitakiwa kufanya nini na yeye hanitaki?” Kimya.

“Mmenikataa bila sababu, baba! Lakini mimi namuachia Mungu. Kama kuna nilipowakosea, basi naomba radhi kwenu wazazi wangu, na kwa Mungu. Ila kama ni chuki tu, basi Mungu aje awe muamuzi wetu. Ila muonye mama. Mwambie anacheza na mboni ya jicho la Mungu. Anapigana vita na Mungu aliye hai wala si mimi. Kwa kuwa uhai wetu sisi, yaani mimi, mume wangu na wanangu wote, umefichwa ndani ya Kristo Yesu. Si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndani yangu, na hao wote niliokutajia. Jack na watoto wetu, nawabeba magoti kila iitwayo leo. Ni hilo tu.” Sabrina akahitimisha bila hofu ndani yake kana kwamba ameambiwa mama yake anamuombea. Halikumtisha hata kidogo.

“Mimi naomba uoge, ule cha usiku, ndipo ulale. Uondoke hapa kesho. Chalii atakapokuja hapa kesho, ndiye akurudishe nyumbani. Sasahivi imeshakuwa usiku sana.” “Nashukuru mama.” Akakubali bila yakupinga. Sabrina akatoka na kurudi hapo na taulo la baba yake. “Kila kitu kipo bafuni baba. Nitakuletea tisheti angalau safi ubadili.” Baada ya kumuweka sawa baba yake akamfuata Jack chumbani.

Makosa!

A

kamkuta amekaa. “Nisikilize Jack. Wewe ulilala na Phina, ukaficha kabisa, mpaka Phina alipokuja kujitokeza na mimba yako. Kitendo cha kuyafanya yote hayo na maisha hapa ndani kuendelea kama kawaida mpaka kuja kwa Phina, binafsi kiliniogopesha sana. Mbaya zaidi ni kama ukapotea hapa, nakuja kukutana na wewe, siku mama yako anashangilia mtoto wa Phina, na alikataa wangu hata wasifike kwake! Hebu tuwe wa kweli Jackson, ingekuwa wewe umevaa viatu vyangu, inamaana ungetulia tu na kuona ni jambo la kawaida? Kuwa mkweli Jackson.” Jack akanyamaza.

“Naomba ongea Jack. Mimi sina kazi. Sijui maisha yangu ya kesho yakoje! Wanangu hawajapokelewa kwenu! Mimi si Mungu kwamba nina uhakika wa maisha ya milele hapa duniani. Nina watoto wawili ambao huwezi kuwaficha hata gizani, wanao ni wazungu haswa. Wewe uliyewapokea, umeanzisha familia huko nje, halafu umepotea. Sijui unalala wapi! Kwa Phina au...” “Mimi nilikuwa nikilala hapo sebuleni na ofisini, Brina. Sijawahi kulala nyumbani kwa Phina!”

 “Hayo ndio unayazungumza sasahivi! Mimi ningeyajuaje? Nilifanya kile nilichojua kitasaidia wanangu. Hata kama sasahivi kinaonekana ni kitu kibaya, ila nakwambia ukweli kabisa Jackson, sijutii. Na nahisi hata tukija kupita hapo tena, tufanye baba hajawatambua kama hivi, najihisi kabisa ningefanya hivyohivyo kwa sababu ya wanangu. Sioni muujiza wa eti nitulie nikiwa na amani eti kwamba ningekufa, eti Phina aje anilelee hao wanangu wa kizungu huku amezungukwa na Jena pamoja na mama Msindai! Hakika hapana Jackson, na katika hilo naomba unielewe kabisa.”

“Wala si adhabu, lakini mimi huwa sijidanganyi. Nikiwaza jambo nalichukulia hatua, kwa kuwa namjua mwanadamu alivyo. Wangemfunga Tino, mimi sipo hapa duniani, vibinti vyangu ndio vingegeuka vichokoraa! Hapana. Haikuwa adhabu kwako, ila msaada kwa watoto. Hilo naomba uelewe Jackson.” “Kwa hiyo sasahivi umeridhika kama ni kina Msindai?” “Sasahivi si kwa kile tu alichokisema baba, na Jacinta pia. Amekubali kuchukua wanangu kama wake. Hivi nilitaka utulie, niweke kwa maandishi kabisa.” “Sabrina!” “Kwa nini unakimbia ukweli Jackson? Wazazi wangapi wanakufa gafla na kuacha watoto wakihangaika kwa kuwa wameshindwa kuacha wosia wakueleweka? Tutapungua wapi kuweka mambo yetu sawa, halafu tusife mpaka tukazeeka?” Jack akatulia.

Kisha akauliza. “Lakini sasahi si umeshanisamehe kila kitu kimerudi kuwa kama zamani?” “Nikuulize swali Jackson?” “Acha kuniita hivyo, Sabrina bwana! Najua bado…” “Wewe tulia nikuulize swali.” “Lakini nishaanza kuhisi sio swali zuri.” “Nitakuuliza tu hata kama unakwepa. Tufanye hii hali imegeuka. Mimi ndio nilifanya kama wewe hivyo. Kwamba ulipokuwa safari, ‘kwa bahati mbaya’, nikakutana na Emma. Yule mpenzi wangu wa kwanza. ‘kwa bahati mbaya’ Nikalala naye na kushika mimba kama hivyo Phina…” Jack akasimama kabisa akiwa ameshabadilika sura. “Acha kusema hivyo.” “Subiri kwanza Jack.” “Hapana. Nimekataa.” “Unakataa nini sasa wakati hujasikia swali zima?” “Najua unachotaka kusema na naomba tusizungumzie hilo. Nishaomba msamaha yameisha. Au umerudisha mawasiliano na Emma?” Jack akambadilikia.

“Hivi umeona jinsi mwanao anavyoninyonya kama mbuzi? Hayo mawasiliano na…” “Naomba utulie Brina. Sio kuanza kulipiziana kisasi. Wewe ni mcha Mungu. umesamehe…” Ikabidi tu Sabrina acheke. “Usicheke Brina! Sio kitu kizuri.” “Yaani wewe leo ndio unakumbuka kama mimi ni mcha Mungu!?” “Mimi najua wewe ni mcha Mungu, hutakiwi kulipiza kisasi. Hata bibilia imekuonya. Na usifikiri nilikuwa nimeficha siri ya kulala na Phina kwa sababu nilikuwa nafurahia! Nilikuwa nikiteseka sana moyoni. Naomba wewe usipite hapo. Sio wakati mzuri. Nakuonya Brina.” “Wala usihangaike kunionya. Mimi sijuagi kuiba. Ndio maana nilipokuwa na Emma, japokuwa alikuwa akininyanyasa, nilikukataa wewe. Mimi sijuagi ‘bahati mbaya’ za kuiba nje ya …” “Basi mama. Twende kwa mgeni.” Jack akatoka hapo mbio asije tibua jingine. Sabrina naye akatoka.

Aluta Kontinua.

W

alipofika tu sebuleni ile wanakaa vizuri wakashitukia na mzee Msindai naye anabisha hodi mlangoni na kuingia. Wote wakasimama. “Karibu baba.” Sabrina ndiye akamkaribisha maana Jack alipatwa kama mshituko alipoiona sura ya baba yake. “Asante mama. Ila nikuombe radhi, nimekuja na mgeni mwingine bila ya taarifa ukinipa baraka zako, nitaomba aingie ndani. Nataka tufanye kikao kidogo hapa nyumbani kwako. Tuwekane sawa.” Mapigo yakaanza kwenda kasi kwa wote wawili. “Karibuni tu.” Wasiwasi ukazidi kuingia wasijue huyo mgeni ni nani. Sabrina akahisi pengine ni mama Msindai.

Mzee Msindai akapiga simu na kuongea kwa kifupi tu. “Unaweza kumuongoza njia ili aingie ndani.” Wakabaki wote wamesimama, mwishoe mzee Msindai akagutuka alipogundua kama wamesimama. “Tafadhali naomba tukae.” Wote wakakaa, hata hakuwa amemsalimia baba yake Sabrina pale mezani. Kimya.

Baada ya muda mfupi, akagonga kijana mgeni kabisa pale na kuingia ndani. “Karibuni ndani.” Huyo mgeni mwenyewe aliyeingia akaangalia nje na kuwakaribisha watu wengine wa nje kama waliokuwa wameongozana ila wenzie wakabaki nje. “Sasa hivi ndio unajidai muungwana! Ulipokuwa ukinilazimisha kupanda gari na kunivuta kwa nguvu!” Nusura Sabrina aanguke kwa mshituko. Ilikuwa sauti ya mama yake. Akaingia ndani akimalizia kulalamika. Sabrina akabaki ametoa macho. Akaingia na baba mtumzima kidogo. “Nashukuru sana, Majid. Sasa unaweza kutupisha. Tukiwa tayari nitakujulisha.” “Bila shaka mzee wangu.” Huyo aliyeshukuriwa kwa jina la Majid, akatoka, akabaki amesimama mama Sabina na huyo mzee mwingine.

“Naomba mkae chini.” Akashangaa mama yake ameingiwa hofu ya gafla baada ya kumuona mzee Msindai. “Baba Sabina najua unakula, ila…” “Hata. Nimeshamaliza.” Akasimama kabla hata mzee Msindai hajamaliza sentensi yake na kusogea pale. “Tafadhali naomba ukae, ili tuzungumze, tuwekane sawa.” Akaanza mzee Msindai, Sabrina kimya kama ameona msukule.

“Nina maswali nataka kuwauliza nyinyi wazazi wa Sabrina kwanza, mbele ya Sabrina mwenyewe kabla hatujaendelea. Na naomba majibu ya waziwazi kabisa bila kuficha ukweli.” Chumba kizima kimya wakimsikiliza mzee Msindai. “Nilipokuja kuoa kwenu, nilitanguliza maswali kujua taratibu zenu nzima. Kwa heshima kubwa sana tulimtuma Sabrina mwenyewe kuwauliza. Maana hatukuwa na muda wa Mshenga. Kulikuwa na uharaka. Jack alitaka kuoa. Lakini pia tukaona Sabrina awe wakili wetu. Akarudisha majibu akisema yanatoka kwenu, labda isiwe hivyo, Sabrina hakufika kwenu, na alitupa majibu yasiyotoka kwenu, leo nitataka kujua ukweli. Ila Sabrina alirudisha majibu kwa Jackson, Jackson akawakilisha kwangu, ndipo nikaja nyumbani kwenu. Mpaka hapo, kuna hatua yeyote niliruka? Na Je, majibu aliyonipa Sabrina, yalitoka kwenu? Naomba aanze kujibu baba Sabina kwa kifupi tu.” “Majibu aliyokupa Sabrina yalitoka kwetu. Na hakuna hatua uliruka.” Akajibu. “Na mama Sabina je? Kwa hatua tu ya kwanza, kuna sehemu nilikosea? Maana nimeshajua Sabrina hakudanganya. Alirudisha majibu kutoka kwenu.” “Sijui.” Mzee Msindai akatulia kidogo akimtizama.

“Nafikiri hapakuwa na kosa.” Mama Sabina akarekebisha kwa haraka. “Unafikiri, au unauhakika? Na naomba uwe mwangalifu sana na majibu yako mama Sabina.” “Kwa wakati ule hapakuwa na kosa.” “Nashukuru.” Akaendelea mzee Msindai. “Siku nilipokuja kuwalipa malipo yenu yote mliyotaka nilipe ili kuweza kumchukua binti yenu, baada ya kuwakabidhi kila kitu mlichohitaji. Niliuliza mbele ya watu waliokuwepo pale, na ilichukuliwa kwenye video, ushahidi upo, nilitaka kujua kwa hakika kama katika orodha yenu, kama kuna kitu hata kimoja kilipungua siku ile. Tena nikaomba kwa kurudia kabisa, mpate muda wa kukagua mahari ya Sabrina, isijekutokea kuja kudaiana baadaye. Tukatoa nakala mbili ya orodha nzima ambayo Sabrina alitupa kutoka kwenu. Moja tukakukabidhi baba Sabina, ingine akaishika Junior. Kijana wangu mkubwa, akawa akisoma, na dada yake anatoa vitu. Nikakuomba kwa kila kinachotamkwa kwenye ile orodha, na mkakabidhiwa, basi uweke alama kuonyesha mmepokea. Je, unakumbuka kukosekana kitu hata kimoja?” “Hapana.” Baba Sabina akajibu kwa haraka tu.

“Tuliondoka na Sabrina siku ile. Je, kabla ya kuondoka na binti yenu unakumbuka mimi kumuombea Jack ruhusa ya kuondoka na mkewe nikiwa nimewaambia kabisa, kwa taratibu za kimila, tulikamilisha, na Sabrina ni wa Jack. Mnakumbuka kutupa baraka zenu kuondoka na Sabrina?” “Nakumbuka mzee Msindai. Nakumbuka kabisa.” Akaendelea kukubali baba Sabina.

“Kwa maana iliyo rahisi na nyepesi, tuliingia mkataba ambao haukuwa na hila wala vificho kati yetu. Nililipa kila kitu kilichotakikana, mkanikabidhi binti yenu rasmi. Si ndivyo?” “Kabisa.” Akajibu baba Sabina. Mkewe kimya.

“Sasa, kwa nini sasahivi mnarudi kinyumenyume na kunipokonya haki yangu, tena bila hatia?” “Mimi nilichokuwa nikitaka ni watoto wa Tino. Hilo tu.” Akajibu mama Sabina kwa ujasiri wote. “Ni vile hukutaka kujibu maswali yangu. Mliponipa Sabrina aje awe Msindai, kulikuwa na sharti lolote ambalo nililikiuka?” “Naongelea…” “Nijibu swali langu.” “Sharti kama masharti ya kuolewa kwa Sabrina hukuvunja, ila sasa Sabrina alikuwa na watoto wa watu!” “Watoto wa nani?” Akauliza mzee Msindai na kuendelea. “Naomba kabla hamjajibu hili, acha niongeze mfano ambao najua mtaelewa kwa haraka. Si nyinyi mlikuwa wafugaji? Si ndio baba Sabina?” “Kabisa. Tena kwa muda mrefu tu.” Akaafiki baba Sabina kwa haraka.

“Acha swali langu liwarahisishie kujibu kwa huu mfano ninaojua mtauelewa kwa haraka sana.” Mzee Msindai akaendelea. “Ikitokea mmenunua ng’omba jike ambaye ana mimba changa tu. Mmemaliza malipo yake yote na mkakabidhiwa ng’ombe wenu, mkarudi naye nyumbani kwenu na kuanza kumtunza kama ng’ombe wengine kwenye zizi lenu. Mkalisha. Alipougua mkamtibu mpaka muda wa kuzaa ulipofika, akazaa. Mkiwa na ng’ombe mliyenunua ambaye mtakubaliana na mimi, ni wenu sasa, na huyo ndama aliyezaa, mnafurahia maziwa mengi na faida za yule ng’ombe, halafu Aliyewauzia anarudi na kudai ndama. Akisema ndama ni wake, anataka kupewa yule ndama aliyezaliwa kwenu kutokana na yule ng’ombe aliyewauzia. Kama ilishawahi kutokea popote hapa ulimwenguni, basi tufanye kama inatokea kwenu nyinyi wawili, mngemtoa huyo ndama kwa kuwa mlinunua ng’ombe aliyekuwa na mimba ya huyo ndama?” Kimya.

“Eti baba Sabina? Ulishawahi kuona hilo linatokea popote? Hata kwa kusoma tu mahali. Ushawahi sikia hilo?” “Hapana.” Akajibu baba Sabina, mkewe kimya. “Jamani, watoto wowote walio zaliwa ndani ya ndoa, kwa ridhaa ya wanandoa, ni wa wanandoa. Kama Tino alikataa kujihusisha na hawa watoto tokea mwanzo alipoambiwa wapo, kwa nini nyinyi kurudi kinyumenyume, kwa uchochezi, mkivuruga amani, kutaka kumpa wajukuu zangu? Mwenyewe kwa kauli yake alikataa na kusema watoto si wake, ni wa Sabrina! Wewe haki yakuingilia ndoa ya kijana wangu unapata wapi mama Sabina? Au acha nikusikilizishe majibu ya Tino mwenyewe.” Mzee Msindai akatoa simu yake.

“Aa..” “Subiri kwanza mama Sabina, maana nataka tuwekane sawa kabla sijaweka hitimisho ambalo hapatakuwa na nafasi ya kiukwaji baada ya hapa. Maana mimi si mzuri sana wa kupokonywa vilivyo vyangu. Sijui kukubali. Na huwa sipendi kudhulumiwa. Ninatumia akili na nguvu zangu zote kuhakikisha sidhulumiwi kwa kuwa na mimi huwa simdhulumu mtu. Ndio maana kama ukigundua, nafanya vitu vyangu kwa umakini sana, hatua kwa hatua ili kusitokee makosa kama haya.” Haikuchukua muda, ikaanza kusikika sauti ya Max na Tino.

Yale mazungumzo yalisikika kana kwamba walikuwa wakizungumza kwenye kipaza sauti. Akawasikilizisha mpaka mwisho. “Je, mngependa mrudie kusikiliza au mmeridhika wenyewe kusikia kutoka kwenye kinywa cha Tino mwenyewe? Au mngependa kusikia ni sababu gani ilimpelekea yeye mwenyewe kwa ridhaa yake kukubali kuwa watoto si wake?” “Maadamu umeanza, tumalize tu.” Akajibu mama Sabina.

Mzee Msindai akafanya mambo machache kwenye simu yake, akaweka sauti. Yakasikia mahojiano kati ya watu wawili. Sabrina akagundua sauti ya pili. “Hiyo sauti inafanana sana na yule daktari aliyelipwa na Tino kunitoa mimba.” “Kwa kuwa ni yeye.” Mzee Msindai akajibu na kuwasha tena ukiri wa yule daktari akikiri kuanzia mazungumzo yake na Max, mpaka kuja kukutanishwa na Tino, ndipo sasa akapelekewa Sabrina mwenyewe amtoe mimba. Na makubaliano yake na Sabrina mpaka akashindwa kumtoa mimba.

“Haya yote yalikuwa yakiendelea, nyinyi wazazi hamna habari! Hamjui binti yenu alipo mpaka aliporudishwa nyumbani kulipiwa mahari, bado hamkuwa mkijua kama ni mjamzito! Lakini mimi nilikuja kulipa mahari yake nikijua Sabrina alikuwa mjamzito, tena mimba haikuwa ya Jackson! Haikuwa rahisi kufikia hayo maamuzi jamani! Lakini ni moja ya vitu vilivyonifanya nimuheshimu sana Jackson. Wakatulia kwenye ndoa yao mpaka mlipoanza nyinyi kuchokonoa mambo.” “Aliyeanza ni Jackson mwenyewe pale alipowatelekeza.” Akajibu mama Sabina kwa jeuri.

“Mama Sabina unaongea nini wewe!? Unajua maana ya kutelekezwa?” Akauliza mzee Msindai. “Sabrina ndiye aliyeondoka na watoto wote, akafunga simu zote, akabaki akitafutwa bila mafanikio mpaka mume wake alipopata fununu anakwenda kwa Pendo, ndipo akamfuata nyuma kujua alipo yeye na watoto.” Mapigo ya Sabrina yakaanza kwenda kasi.

“Na alipokuwa kwa Pendo, je?” Bado mama Sabina alikataa kushindwa. “Unakumbuka kuniona mimi na vijana wangu pale kwa Pendo au umesahau?” Miguu yote ya Sabrina ikafa ganzi akashindwa hata kusogea. “Ni lini na wapi ambako Sabrina alitelekezwa?” Kimya. “Kutelekezwa ni kuachwa mahali, peke yako bila msaada. Kwa upande wa Sabrina, angeachwa peke yake na watoto wote bila msaada wowote ule. Lakini Sabrina alichagua kuwepo kwa Pendo, wote tukaliheshimu hilo na ndio maana uliniona nilikuwa nikija pale kila siku usiku kuangalia wajukuu zangu. Sijawahi kukosa hata mara moja mpaka Sabrina mwenyewe alipoondoka na watoto wote. Tena bila hata taarifa kwa yeyote yule!” Kimya. Mapigo ya moyo ya Sabrina yakienda kasi. Mzee huyo alimnyamazia, kumbe hilo nalo lilimkera.

“Narudia tena, kosa langu mimi nilipi, kuja kunidhulumu haki yangu? Mnakuja kugawa wajukuu zangu kwa mtu ambaye hakuwahi kuwataka ila tamaa tu! Tino ndiye aliyemtelekeza Sabrina, huko Moshi. Akiwa mjamzito, akamuacha akiwa ameridhika kabisa ameua watoto! Sasa nauliza, iweje leo mnipokonye mimi watoto, mumrudishie mtu ambaye alitaka wauwawe!?” Kimya. “MMENIKOSEA SANA.” Akaongeza mzee Msindai na kuendelea.

“Baba Sabina na mama Sabina, narudia tena, mmenikosea sana. Kama ambao mmekusudia kunikosea na kutaka kuendelea kunidhulumu, bado nakuona mama Sabina unaendelea kunitangazia vita kwa kwenda kuloga kijana wangu.” Sabrina na Jack walishituka sana. “Nimemleta na huyu mganga wako hapa ili akawe shahidi wa hiki ninachozungumza, kwa kuwa ukiri wake na yeye umesharikodiwa na nimeshafungua kesi. Mnanidhulumu bila sababu! Nilioa kwenu kwa heshima kubwa sana. Leo kuzunguka kwa waganga mkitaka kumuangamiza kijana wangu, ni kosa ambalo sitakubali.” Jack aliingiwa hofu mpaka akapatwa baridi kali. “Mnataka kuniua mimi!” Jack akajikuta akiuliza kwa hofu.

Mkewe kimya akijua utabiri wa mama Msindai, kuwa wanamloga kiziwanda wake, shetani ameamua kuukamilisha kwa kuuthibitisha kipindi hicho anachomuombea mumewe, na kuona amefanikiwa kuwaleta pamoja! Amerudisha ule utengano, akaleta umoja. Familia imeamua kusimama pamoja kumsaidia Jack, shetani amesikia, anatumia kumuanika mama Sabina, ili tu kuleta mafarakano, na kuendelea kuangamiza. Sabrina akajua shetani bado yupo kazini.

~~~~~~~~~~~~~

Akiwa Ametoka Tu Kuomba, Ungetegemea Amani Na Utulivu, Lakini Bado Shetani Anatupa Makombora Yake Ya Nguvu! Sabrina Ameshindwa Kutulia. Kila Siku Na Kila Saa Lipo Jipya Lakupambana Nalo.

 Nini Kitaendelea?

Usikose Muendelezo Kujua Mama Sabina Ameshikwa Vipi Uchawi? Mzee Msindai Amemtoa Wapi? 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment