Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 68. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 68.

Jacinta akaona awe muwazi zaidi pengine Sabrina hajapata kila kitu. “Kwa hiyo unajua kama amesema ni Jack ndiye aliyemfuata chumbani kwake na kumtaka kimapenzi akimwambia amechoshwa na ndoa yake, ilianzishwa kwa uongo, ukimdanganya kuwa una mimba yake, mpaka wakaja kuzaliwa watoto wakizungu, ndipo akajua wewe ni muongo. Phina anatangaza kuwa Jack amemwambia kuwa anajutia kukuchagua wewe, anaomba nafasi ingine kwake na yupo tayari kuanzisha naye familia, wazae watoto wao sio wakusingiziwa. Kwamba ndio sababu Phina alijiachia kwake mpaka kushika mimba kwa kuwa Jack alimuhakikishia ndoa na wewe imeisha. Unajua hayo?” “Wifi yangu, NAJUA. Nimeona na ninajua jinsi walivyopata taarifa za watoto wangu na naona jinsi wanavyozitumia vibaya.” “Kwa hiyo kumbe ni kweli Sabrina unajua kila kitu!” Junior akashanganzwa sana.

 “Shem najua. Safari hii nilijiambia sitapitwa na kitu hata kimoja. Nina uhakika kwa asiliamia 100 bila hata Jack kukanusha kwangu, Jack hajazungumza na Phina juu ya kina Keiline. Kwa kuwa nayajua mahusiano ya Jack na wale watoto. Hata ukimuamsha Jackson usingizini, ukamuuliza kwa haraka baba ya wale watoto wakizungu ni nani, hatamtaja Tino, ila yeye mwenyewe. Najua kwa kuishi na Jack, kwa hiyo najua kwa hakika, hata kama alikuwa na shida ya kiasi gani ya kulala na Phina, hilo asingeweza kusema kwa kuwa yeye Jack halipo akilini mwake hata kidogo. Phina amemsingizia Jack. Hayo mambo ya Tino na watoto hajayapata kutoka kwa Jack. Ila nahisi, sina uhakika, nahisi kuwa habari za watoto wetu wamezipata kwa Lela, aliyekuwa mke wa Tino, ambaye na yeye hajasikia kutoka kwa Tino ila aliambiwa na Sabina.” “Upo sahihi kabisa.” Mzee Msindai akaafiki.

“Asante baba. Mimi nilijua kwa hakika Jackson hajazungumza hayo yote na Phina. Ni habari ambazo ninauhakika sasahivi wanazisaka kwa kila jinsi, ili kuzitumia vibaya. Kwa upande wa Phina ni ili kuendelea kutengeneza stori yake. Na kwa upande wa Ibra ni ili kuendelea kumchafua na kumvuruga Jack.” “Sio na wewe!?” “Sio mimi hata kidogo wifi. Mimi shida yangu ni Jack. Nimeshajua bado mume wangu ananipenda na anataka familia, sina hofu na ungurumaji wa shetani. Na ninajua inaweza kuwa mbaya zaidi ya hapo kwa kuwa sasahivi Phina yupo kwenye uchungu wakumpoteza mtoto wa Jack, aliyejua ni kama alikaribia kumpata tena mume wangu. Tena safari hii akiwa na mtoto wake! Kwamba watakuwa na mahusiano yasiyovunjika tena, kwa kuwa wamezaa!”

“Kwa hiyo najua sasahivi ataweza kuongea chochote na kufanya chochote kwa kuwa yupo kwenye hasira na uchungu. Na Ibra akimsaidia kukusanya taarifa zetu ili kupanga jeshi kinyume na Jack. Hilo halinisumbui jamani. Nayajua maneno ya mkosaji jinsi yanavyoweza kuwa machungu kuliko chubiri, na sumu kali kuliko sumu ya nyoka. Najua kwa kupita kwenye hizo hali. Najua jinsi mwanadamu anavyoweza kugeuka akawa mkali na hatari kuliko simba. Ni nguvu ya ajabu sana mwanadamu alipewa na Mungu. Hiyo sina wasiwasi hata kidogo. Namwacha ahangaike tu huko mitandaoni na popote pale anapotaka yeye, mimi sitajali ilimradi Mungu amenirudishia mume wangu, inatosha.” Sabrina akaendelea.

“Shida yangu mimi ni hali aliyonayo Jack. Tafadhalini naombeni mumsikilize na mume wangu.” Sabrina akamgeukia baba yao. “Baba, hata kwa magoti mimi nitapiga. Najua alichokifanya Jack. Wala mimi si mjinga. Najua amekufedhehesha sana, na kwa mara ya kwanza ameharibu sifa nzuri ya familia. Ila baba, shetani anatumia hili tukio kama fimbo ya kumchapa kila mmoja wetu hapa. Tafadhalini nawasihi, kama mnaweza kumsikiliza Phina, basi mpeni na mume wangu nafasi awaeleze upande wake. Na mjaribu kuvaa viatu vyake pale alipo sasahivi. Tusiruhusu akaingilia hata kazi yake.”

 “Hivi unajua cheo cha mumeo ni chakupewa, shem?” Junior akaendelea kama ambaye bado hajamuelewa Sabrina vizuri au anahisi Sabrina hajaelewa uzito wa hilo jambo. Akaendelea kumuweka sawa kwa maswali yatakayomfanya afikirie, kama anayetaka Sabrina aelewe taarifa sahihi kabla hajaongea sana.

“Kwamba aliyempa anaweza kumpokonya wakati wowote kwa kuwa hii ni siasa, Sabrina! Acha nikwambie ukweli Sabrina. Kitendo alichokifanya Jack si kigeni katikati ya watu wanao tuzunguka. Nawaona wakifanya hayo tunapokuwa tukiishi huko Dodoma kipindi cha Bunge, na hata kwenye hizi safari zetu tunazokwenda nje ya nchi. Kwao ni jambo la kawaida sana kulala hovyo na wanawake, hata wenyewe kwa wenyewe, kwao si jambo la hatari.  Ila matokeo yao wao hayana madhara kwenye siasa zao na wengine. Lakini hapa, katika hili la Jack, unamgusa moja kwa moja Raisi aliyempa haya majukumu! Anachafuliwa yeye moja kwa moja kuwa mfanyakazi wake anaharibu, tena anaharibu vibaya akitumia mali ya umma! Sasa wewe fikiria, amchafulie hivyo, na yeye ana mpango wa kurudi tena madarakani, unafikiri Jackson atabaki salama?” Junior akamuuliza tena taratibu tu.

“Nimeshalifikiria hilo na hata Jack pia. Lakini ni BORA apoteze hiyo kazi lakini si sisi tuliokaa kwenye hii meza.” Kila mtu pale mezani akamshangaa Sabrina, mpaka Joy mwenyewe ikabidi amuangalie vizuri. “Jamani, hiyo itakuwa mbaya zaidi.” “Kwa maana nyingine hata akipoteza hayo madaraka wewe huna shida?” “Hata hilo na yeye aliniuliza wifi yangu. Mimi nitakuwa muongo, eti leo Unaibu Waziri huu aliopewa Jack juzi, ndio iwe ngao ya familia yetu! Hakika sijali. Kipato kitapungua, lakini mkumbuke tulipotoka mimi na Jack jamani! Singida kule, na watoto wetu wote! Kasoro huyu Brandon ndiye hakuwepo. Lakini tulikuwa hivihivi na hatujawahi kulala njaa, wala kuhisi kupungukiwa. Haya majukumu aliyopewa sasahivi sikatai yameongeza kipato, lakini sio kila kitu jamani! Eti kiasi ya kwamba eti sasahivi ndio tukose utu! Tupaniki na kumtupa Jack kwa sababu ya hofu ya kupoteza haya madaraka tu!”

“Hapana jamani! Mimi naombeni tuanze na Jack kama Jackson Msindai kwanza. Yeye mwenyewe na mtu wake wa ndani, acheni mengine yajijibu kwa kadiri ya muda unavyokwenda. Nashukuru ushauri wa baba, sitajibu mtu. Mimi huwa namwangalia Mungu wangu. Hata katika hili atajibu tu. Atamsamehe Jack na atamrejeshea furaha aliyopoteza alipofanya kosa. Ni hilo tu. Naombeni mumsamehe Jack. Kabla ya kuwaza na kushugulikia watu ya nje, naombeni tumfikirie Jack mwenyewe, kwanza. Naombeni macho yetu yarudi kwa Jack mwenyewe.” Sabrina akaendelea bila kuchoka.

“Shem, naomba nyosha tena mkono, niokotee mume wangu pale alipoanguka, ili asimame tena. Naomba usimuache chini. Tafadhalini sana. Ni hilo tu.” Sabrina akawafanya watulie na kujirudi. Maana wote walikuwa wakihangaikia mambo ya nje na kumsahau Jack mwenyewe. Pakatulia hapo mpaka muhudumu akarudi kuuliza tena vinywaji. Mzee Msindai akataka aongezewe juisi, akaondoka na kuwaacha kimya.

~~~~~~~~~~~~~

Jack naye akawa anarudi na Brayan akilia. Sabrina akasimama kuwafuata. “Sasa kaka mkubwa naye analia nini?” “Ameanguka.” Claire akajibu. “Ila mimi nimemfuta vizuri, kumtoa mchanga.” “Wewe ni dada mzuri Claire. Asante.” Sabrina akambeba. “Nionyeshe ulipoumia.” Brayan akamuonyesha akilia. “Pole kaka mzuri. Pole sana.” Akawa anambembeleza. “Mimi nahisi huu ni usingizi Jack. Tule, turudi nyumbani wakawahi vitanda vyao, kabla timu nzima haijaanza kilio.” Wakarudi hapo mezani.

“Mkeo amekuagizia chakula. Tunaweza kuzungumza wakati tukisubiria?” Jack hakuamini. “Kabisa kaka. Nashukuru sana.” Akajikuta akishukuru bila hata kujua anaitiwa nini. “Sasa huyo aliyelala si…” “Mlete mimi ni mbebe.” Mzee Msindai akawahi. Jack akamkabidhi baba yake na kuondoka kwa haraka akimfuata kaka yake. Pakazuka ukimya wakimwangalia Sabrina akipanga watoto wake hapo mezani. Wakamsikia Jacinta akicheka. “Naona Sabrina kazi ya umama unaiwezea! Umetuliza ghasia yote kila mtoto ametulia anakuangalia!” Sabrina akacheka. “Ndio ofisi yangu mwenzio.” Sabrina akajibu akicheka

“Ila hawa wawili wanakusikia Sabrina!” “Sana. Kwa hilo namshukuru Mungu, Joy. Hakuna utakachowaambia ukarudia sana. Imenisaidia kulea hawa mapacha wangu wa nje kiurahisi. Hata dada zao hawapati nao shida. Wanasema chochote unachowaambia kufanya, ilimradi wakuelewe tu. Watafanya bila shida.” Jeiline na Keiline walikuwa wamekaa kwenye kiti wakimwangalia mama yao kila anachokifanya, wametulia kimya. Mpaka chakula kilipoletwa, zoezi la kula likaanza, Jack na kaka yake hawakuwa wamerudi.

Waliporudi tu Sabrina akamuomba Jack wao waondoke. “Nimeomba wakufungie chakula.” “Nashukuru.” Jack akasimama kwa muda kama aliyetaka kuzungumza jambo, akagairi akaishia kuaga tu. Mzee Msindai akasimama na mtoto. “Naona sisi watatu tutangulie kwenye gari.” Wakaelewa anamaanisha yeye, Brandon na Jack. Wakijua anataka kuzungumza na Jack. Sabrina akaona asubiri kidogo kama kumpa nafasi. Akarudi kukaa akimshukuru Mungu kuwa wamemsikiliza na wanampa nafasi Jack.

Mzee Msindai Kwa Jack.

M

zee Msindai alipomfunga mtoto kitini akamwambia Jack awashe gari, ndipo wazungumze nje. Jack akawasha gari akaacha inawaka na A/C akatoka kuzungumza na baba yake. “Sijui umezungumza nini na mkeo! Lakini amekutetea sana, Jackson. Na ameomba nikusaidie. Sasa, kabla hatujaendelea mbele baada ya hapa, nakupa nafasi ya mwisho ya kuniambia ukweli bila kunidanganya. Kwa sababu utakaponiambia neno lolote sasahivi, huna nafasi ya kurekebisha tena, na nitakuadhibu vibaya sana.” Hofu ikamuingia Jack. Akameza mate akimtizama  baba yake na yeye mzee Msindai akatulia akimwangalia. “Sidanganyi chochote baba. Na wala Sabrina sijamdanganya ili aniamini. Nimesema ukweli.” Jack akajibu midomo ikimcheza mbele ya baba yake. Mzee Msindai akabaki akimwangalia machoni kama anayemsoma. Jack naye akatulia akijikaza kumtizama.

“Kwa maana nyingine, nitakapoletewa video iliyorikodiwa na kamera zilizokuwepo nje ya vyumba vya hoteli mliyolala nchini Uswiz, siku ulipolala na Phina, nitamuona yeye akiingia chumbani kwako na sivinginevyo?! Na kabla hujajibu, nakuonya Jackson, uwe na uhakika. Kwa sababu nitatumia muda na pesa nyingi sana kuhakikisha naipata hiyo video.” “Labda kama wai wai…” “Jackson?” Baba yake akagomba kwa sauti. “Kama hawajabadilisha, hakika agiza baba. Mimi nasema ukweli. Na hakikisha ni kweli ni chumba changu wasije…” “Nimeianza hii kazi kabla hujazaliwa.” Mzee Msindai akamjibu hivyo na kuondoka akionekana anatoa simu yake ili aanze mawasiliano.

Shetani Hana Zawadi Ya Bure

Kidogo Jack akashukuru Mungu akahisi pengine hiyo video inaweza kuwa mtetezi wake kufuta shutuma mpya za Phina hata kwa mkewe. Maana alijua kwa hakika asubuhi hiyo atakuwa amemmaliza kabisa kwa kila mtu hata wale waliokuwa wamebakiwa na asilimia chache za imani kwake, watakerwa zaidi. Kwani asubuhi hiyo mitandaoni, alitoka na jipya akisema anataka kuongea ukweli wote wa kilichoendelea kati yake na Jack huko nchini Uswiz.

Akaeleza kuwa Jack ndiye aliyemfuata chumbani kwake akiwa amelala. Akamlilia shida kwenye ndoa yake, kuwa watoto hao wakizungu ndio wanaleta shida. Kwamba Sabrina aliingia kwenye ndoa akiwa amemdanganya Jack kuwa  mimba ni yake. Siri ilifichuka walipozaliwa watoto wa kizungu. Na fujo inayoendelea kwenye ndoa yake kwa sababu ya Tino aliyejitokeza kama baba wa hao wa watoto wakizungu.

Kwamba imezua tatizo kwenye ndoa yake, Jack ndio anataka kumuacha Sabrina. Hataki kuingia kwenye vita na Tino. Anataka kuoa tena. Na alimuomba yeye rasmi aanze naye upya kwa kuwa walishakuwa na mahusiano ya kimapenzi, na yeye hakuwahi kumsaliti kama Sabrina. Ndipo Phina alipojiachia mpaka kushika mimba.

Akaendelea kueleza kupokelewa kwake ramsi na wakweze, wakimkaribisha yeye na mtoto kwenye familia ya Msindai. Na ahadi hata ya babyshower ambayo haikuwa hata siri huko mtandaoni. Wifi yake Dokta Jena Msindai aliliweka wazi bila kificho. Na alimfuta yeye kibinafsi na kumwambia mama Msindai ndiye atakayemfanyia babyshower ya huyo mjukuu aliyembemba kama njia yakumkaribisha mtoto kwenye familia.

Huku Nyuma Walipoachwa na Sabrina.

“Kila nikizidi kukufahamu wifi yangu, nazidi kuelewa kwa hakika ni kwa nini Jack alikung’ang’ania akuoe wewe!” Sabrina akacheka tu. “Kweli Shem. Umefanya wote sisi tujirudi. Sijui upande wa Jacinta, ila kwa jinsi nilivyomuona baba, haya mazungumzo nafikiri wote tulihitaji kuyasikia Shem. Ni jambo lililotupata kwa mshituko. Hakuna aliyetegemea. Tukajikuta tukisumbuliwa na habari za mitandaoni, tukamsahau Jackson mwenyewe.” “Ila kwa upande wangu aliniudhi zaidi nikijua ameanza umalaya.” Jacinta akaongeza. “Hilo nalo.” Junior akakubaliana na dada yake.

“Kwa sababu madaraka na pesa huo vina mtindo wa kumuanika mtu na kumfichua kabisa. Hata kama alionekana anatabia fulani, akishapata nafasi, ndio anaanza kutoa makucha yake. Hilo mimi lilinikera sana. Halafu akaniudhi zaidi akionekana tena hajui chakufanya! Hapo ndipo nikachukia kabisa. Yaani ameanza uchafu wake, halafu hajui jinsi ya kuishi nao huo uchafu! Hapo ndipo aliponikera nikawa nikimkwepa kabisa. Maana nilijua akinisogelea, naweza kumchapa makofi bure kama mtoto mdogo.” Jacinta akaongeza na kuendelea.

“Lakini hiki ulichokizungumza, na mimi nimekua kama Junior. Nimeshukuru kukisikia. Kwa asilimia kumbwa sana kimenituliza. Hata sasahivi ninapo shugulika na hili jambo zima, la huyo Phina, nishaona utofauti. Si kwa..” “Kupaniki.” Akadakia Junior. “Kabisa Junior. Si kwa paniki au hofu. Na mimi naanza kumuona ni kama mfa maji tu. Na nakwambia ukweli, sijui labda iweje, inaweza isiwe kubwa kama tunavyotaka kujiogopesha.” “Na hata ikiwa kubwa wifi, bado nawaomba mbaki na Jack.” “Sabrina alivyomng’ang’ania mumewe!” Joy akafanya wacheke.

“Kwa kuwa namjua Jack wangu jamani! Hajabadilika ila amekosa tu.” “Basi shem. Tumekusikia.” Wakazidi kucheka. “Nawashukuru sana. Asante shem na samahani kuwaharibia mapumziko yenu.” “Na kweli umeyaharibu!” Joy akadakia. “Joy naye! Huwa waungwana wanasema usijali!” “Mimi najali. Junior wangu huwa simpati kwa muda mrefu na jumatatu usiku anasafiri tena!” Junior akazidi kucheka akimwangalia mkewe. “Basi ondokeni sasahivi na nyinyi msitukere. Msichomalizaga nyinyi ni kipi mno! Mapumziko hayaishi!”  “Kwanza hapa kikao kimeshaisha. Twende Joy.” Junior akasimama kabisa.

“Wazazi nyinyi hata sijawapatia mfano! Watoto wenu bado wanakula, nyinyi mnataka kukimbia!” “Nani anataka kurudishwa na anti Jacinta nyumbani?” Junior akauliza. “Mimi naweza kurudi na anti.” CJ akajibu taratibu tu kama aliyeelewa nia ya wazazi wao kwa haraka. “Na wewe Claire mwanangu mzuri hutaki..” “Hakika siamini! Kweli nyinyi mnauza watoto!” Jacinta akawashangaa Junior na Joy, wao wakazidi kucheka. “Baki na anti na umwambie akupitishe kule madukani kwenye vibanio vizuri. Mkanunue na ice cream ndio mrudi nyumbani. Umesikia Claire mtoto mzuri?” “Mimi sinunuliwi kitu?” Cleiton akauliza baada ya Claire kutingisha kichwa akikubali. “Na wewe Cleiton mwambie anti atakununulia chochote unachotaka.” Wakaondoka kwa haraka, Jacinta akiwaangalia. Sabrina hana mbavu, kwa kucheka.

“Huna neno wifi yangu?” Sabrina akamuuliza akicheka. “Tufanye nina neno. Ushawaona wazazi wenyewe?” Sabrina akazidi kucheka. “Msiwe na wasiwasi wanangu. Tukitoka hapa, tunaenda kuangalia movie, tunanunua na popcon kabisa. Tunakula popcon huku tunaangalia movie. Tukichoka tunaenda madukani, halafu ndio nawarudisha nyumbani. Au mnasemaje?” Wote wakakubaliana na anti yao, babu yao akawa anarudi.

“Mbona Junior na mkewe wameacha watoto?” “Nawapeleka movie na kumnunulia Claire vibanio vya nywele.” Mzee Msindai akacheka akikaa. “Nakushukuru baba yangu, acha sisi twende, hawa wakalale.” “Karibu mama. Na tunashukuru na wewe kwa kila lililoendelea hapa. Mfike nyumbani salama.” Jacinta akamsaidia kubeba watoto na mizigo, wakaenda garini. Wakamkuta Jack garini amekaa, kimya. Wakapandisha watoto garini, Jacinta akaenda upande wa dereva alipokaa Jack. “Kula na ulale vizuri ili uwe na uwezo wa kufikiria. Umezeeka gafla!” “Sasahivi naweza hata kulala!” “Ndio UKOME.” “Nilishakoma dada.” Jacinta akamuangalia na kuondoka bila yakujibu.

Shetani Hanaga Usingizi!

W

akati wanaingia getini, Sabrina akamuona baba yake amesimama na walinzi. Hakutegemea kumuona baba yake nyumbani kwake! Akamwambia Jack amshushe. Akasimamisha gari, Sabrina akashuka, yeye akavuta gari ndani na kuita wasichana wakazi watoke wachukue watoto maana wote walishakuwa wamelala. Na yeye akarudi getini alipomuacha mkewe akawakuta kwenye mazungumzo. Akapenyeza salamu na kumkaribisha baba mkwe huyo ambaye hawakuwa wameonana kwa muda mrefu. “Karibu ndani.” Mzee alionekana amechoka haswa. “Naomba tukazungumzie ndani baba.” Sabrina akaweka msisitizo na kutaka kutangulia. “Mimi sitakaa sana, nilitaka tu…” “Kwa hiyo unataka uishie getini!?” Sabrina akashangaa sana.

“Kwa nini iwe hivyo!? Kuna uadui gani huo mkubwa kati yangu mimi na nyinyi wazazi wangu mpaka nikifika kwenu mshindwe kunikaribisha ndani, na mkija kwangu pia mshindwe kuingia ndani!?” “Ni vile nimekuja bila miahadi sikutaka kusumbua. Ila nilikuwa na jambo muhimu sana nataka kukutahadharisha. Na ninaharaka yakurudi nyumbani. Wala si kwa ubaya kati yetu.” “Sasa ndio unataka hilo ‘jambo muhimu’ tulizungumze hapa nje tumesimama wimawima?! Kwa haraka gani hiyo hata ndani usiingie?!” Jack alipoona Sabrina ameshawaka akaona aingilie. “Tafadhali karibu ndani. Husumbui mtu yeyote. Jisikie upo nyumbani, karibu. Sio sawa uishie nje.” Wakaongozana mpaka ndani.

“Karibu mzee wangu. Sisi tulikuwa tumetoka, acha tuangalie chakula ndani.” Akamtizama Sabrina kama anayetaka aongozane naye. Sabrina akaelewa na kuongozana nae chumbani. “Naomba tulia mama.” “Kwa nini wananifanyia hivyo!? Nilichowakosea mimi ni nini jamani!?” “Naomba tulia, tujue kilichomleta. Tafadhali mama.” Sabrina akatulia. Akatoka kwenda jikoni, akamwambia msichana wake wa kazi aanze kuandaa meza kwa chakula cha baba yake, yeye akarudi chumbani kubadili nguo.

~~~~~~~~~~~~~

Alichoshangaa Sabrina, alipomkaribisha baba yake chakula, hakujivunga hata kidogo. Akahamia mezani kula. Alionekana na njaa na amechoka. “Mama anaendeleaje?” Sabrina akatupia hilo swali wakati akimpangia mumewe chakula sehemu ya sebuleni. “Hali sio nzuri.” “Mgonjwa?” Sabrina akauliza. “Mmmh!” Akamsikia akiguna tu na Sabrina akanyamaza kama kumpa nafasi amsikie. Maana mara ya mwisho alimfukuza hakutaka hata aingie ndani. Sabrina alipoona hazungumzi akaenda kumuita mumewe chumbani ili atoke aende kula maana wakati wao wakila, yeye alikuwa kwenye mazungumzo na kaka yake. Akamkuta amejiinamia.

~~~~~~~~~~~~~~

“Ni nini tena!?” “Daaah! Kwanza sijui umezungumza nini na kina kaka, naona nimepata uungwaji mkono mzuri. Ameniambia kesho atakuja ofisini kunichukua, tukazungumze na Waziri wa Fedha mwenyewe. Atamuomba leo, ili kesho anipe nafasi yakunisikiliza upande wangu ili atushauri. Baba ametoka kunitumia ujumbe kuniambia ushauri wa Junior ni mzuri, nitengeneze mazinga yakutekeleza hilo kutokana na muda wa Junior kabla hajasafiri.” “Sasa mbona ni jambo zuri na wewe unaonekana kukosa tena raha?” “Kwa upande huo hamna shida. Kwanza nakushukuru. Asante Brina. Umerudisha mioyo yao kwangu! Naona hata kaka amenipa pole na kunitia moyo. Na baba anashugulikia video ya Uswiz iletwe.” Hapo akamchanganya Sabrina.

“Sijaelewa! Video gani tena?” “Si unajua haya mahoteli makubwa huwa yana Surveillance cameras?” Sabrina akabaki ametoa macho. “Kwamba yanarikodi matukio yote kila wakati ndani na nje ya hoteli. Sasa baba anataka kuagiza rikodi ya siku na muda ule wa usiku kwenye gorofa nililolala mimi na gorofa aliyokuwepo Phina ili kuthibitisha hicho alichosema Phina kuwa eti mimi ndiye niliyemfuata chumbani kwake na kumwambia maneno yote hayo. Najua na wewe umemsoma leo asubuhi mtandaoni. Unajua shutuma zake mpya.” “Unauhakika baba hatakuta vinginevyo?” Hilo swali likamuumiza Jack.

 “Kwa hiyo huniamini?” “Mimi nakuuliza Jack. Maana najua ukimdanganya mzee Msindai, safari hii hatakusamehe. Nilimuona ni kama amelainika baada ya mazungumzo yetu jioni hii, sitaki umtibue zaidi.” “Sidanganyi Brina! Mungu wangu ni shahidi, yeye ndiye aliyenifuata chumbani kwangu. Tena ndio vizuri hata baba athibitishe sio kwamba nililala chumbani kwake usiku kuchwa kama anavyodai yeye.” Jack akaongea kana kwamba kulala na mwanamke asiye wako kwa muda mfupi ni bora kuliko kulala naye usiku kuchwa! Sabrina akamwangalia akaona amuache tu. Aendelee asijetoka kwenye pointi.

Akarudia swali lake.  “Ndio nauliza, tatizo ni nini tena? Maana ni kama hayo yote yanakwenda sawa!” Jack akamwangalia na kutingisha kichwa kama anayesikitika. “Ni nini Jackson!?” “Nina wakati mgumu Brina! Naomba usikasirike zaidi na kunikimbia. Nitarukwa na akili uki…” “Jackson Msindai, baba yangu yupo sebuleni na yeye anasema kuna jambo anataka akanitahadharishe, na  chakula chako kipo tayari kinaendelea kupoa. Tafadhali nipunguzie hii hali ya wasiwasi unayotaka kuniongezea.” Jack na yeye akasimama kama mkewe na kuzidi kumtia wasiwasi.  

~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea….

(Thank You God For The Gift Of Life. Nov 7th)

{Ufamle Wako Uje, Na Mapenzi Yako Yafanyike Hapa Duniani Nilipo Mimi, Kama Huko Mbinguni} 

{HAPPY BIRTHDAY TO ME}

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment