Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 67. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 67.

Mwishoe ndio akapanda kitandani. Jack akavuta pumzi kwa nguvu. Akatamani angezungumza naye hilo muda mrefu kidogo pengine wasingefanya maafa yote hayo. Akatulia. “Jack! Umeshalala?” “Bado.” “Ulitaka nikusaidie nini? Au ulitaka nifanye nini?” “Naomba kesho unisindikize harusini.” Mpaka Sabrina akashangaa. “Jackson! Unataka nitoke hapa tuongozane ili nikaendelee kuchekwa! Nikifananishwa na Phina? Nimekonda kupitiliza, mpaka naitwa kinyago! Na wangenine wanasema ulichoka kula makapi, ndio maana ulikwenda kula…” Sabrina akaona asimalizie kujitusi. “Hapana Jackson. Niombe kitu kingine.” “Phina si mwanamke wangu, na wewe unajua nakupenda Brina. Phina alikuwepo, lakini nikasubiri mpaka nikakuoa wewe! Kulikuwa na sababu gani ya kukuoa wewe kama namtaka Phina niliyekuwa nikijua alipo na mpaka namba yake ya simu nilikuwa nayo?” Hapo Sabrina akatulia.

“Umesahau Phina tulikuwa naye chuoni na mimi ndiye niliyemsaidia kutafuta kazi aliyo nayo?” Kimya. “Kwa maana nyingine, nilijua Phina yupo, ila nikakuoa wewe. Na kama ningekuwa nataka mwanamke mnene, basi Pam uliyenikuta naye kule Singida sasahivi angekuwa mke wangu au hata huyo Phina mwenyewe. Lakini mbona nilikuoa wewe? Tuwe wakweli Sabrina, wakati wote mimi ninaokurudia, unakuwa matatizoni na unakuwa umekonda sana tu!” “Mmmh! Naona leo umeniamulia.” “Nakwambia ukweli ili urudishe mawazo kwenye mahusiano yetu. Najua umekasirika, lakini pia najua unajua kama nakupenda Brina. Sijakosea kukuoa wewe. Nakupenda vile ulivyo mke wangu. Sema nimekosa. Nimejikwaa ambako sikutegemea. Naomba unisamehe. Na tafadhali kesho naomba nifichie aibu yangu. Nisindikize harusini. Angalau baba anione nipo na wewe pengine anaweza hata kupokea salamu yangu vizuri.” Hilo likamshitua kidogo Sabrina.

“Kwani na mzee Msindai atakuwepo!?” “Familia nzima inatakiwa kuwepo. Ni mtoto ambaye baba alimsimamia ubatizo. Kwa hiyo mzee Msindai ni baba wa ubatizo na alikuwa akimtibu wakati mtoto mpaka amekua. Kwa hiyo ndio naomba tuongozane.” Sabrina akanyamaza. “Na swala la wembamba, nilikuoa hivyohivyo ila sema sasahivi umepungia zaidi, tena ni kidogo tu. Wala haina tofauti na unavyokuaga.” “Mimi sijaelewa aina hii ya msamaha jamani!” Angalau wakaanza kucheka.

“Naona unataka kujipa sifa zisizo zako mama. Mimi nakupenda hivyo ulivyo. Nabeba na kuhamisha nitakapo bila kutokwa jasho ila kufaidi tu. Halafu asilimia kubwa ya tutakao wakuta pale walikuwepo kwenye harusi yetu, na wanamjua Sabrina wangu alikuwa mwembamba tokea mwanzo. Hao wa mitandaoni achana nao. Hawatujui. Ni mashabiki tu, kazi yao kuniharibia.” “Umeharibu wewe mwenyewe, wala si watu! Nani..” “Basi mama. Basi. Huko unapokwenda ni kurudi nyuma. Utapandisha hasira halafu tutaanza upyaaa. Acha tuendelee hapahapa. Kwa hiyo?” “Tutakwenda lakini kwa mashariti.” “Gani tena!?” “Sitakwenda after party.” “Hata kama Jacinta atakuwepo na Junior?” Hapo Sabrina akatulia kidogo na kuanza kushawishika. “Si unajuaga inavyokuwa nzuri? Tena..” “Mwenzio nina watoto wadogo, Jack. Nitawahi kurudi ninyonyeshe. Wewe nenda tu. Uwe na amani. Kafurahie na wenzio.” “Basi tutarudi wote. Wakatulia. Sabrina akageukia upande mwingine akalala. Jack aliogopa hata kumgusa asije haribu. Akajisogeza pembeni kabisa na yeye akalala.

Jumamosi.

Sabrina alimuacha Jack kitandani akiwa amelala hana habari. Akamuelewa maana na yeye alikuwa amechoka akili, hakuwa akipumzika kwa mawazo akijua Phina na mwanae wameingilia ndoa yake. Hata akilala alikuwa akilala usingizi wa mang’amung’amu. Usiku aliompa Jacinta, alilala kama mtoto mchanga. Akajua ndio anachokipata mumewe. Mazungumzo waliyoyafanya, yamempa pumziko la akili. Akamuacha apumzike na kutaka kila mtu awe kimya humo ndani ili alale.

Akiwa chumbani kwa wanae wakiume, ametoka kumuogesha na Brayan, Jack akaingia. Ilishakuwa saa nne asubuhi. “Huyu mbona yupo uchi? Si umuite Pina akusaidie?” “Michezo mingi! Ila namtafutia nguo, nitamvalisha sasahivi.” “Natoka. Sitakawia kurudi.” “Na mimi nitatoka baadaye kidogo niende saluni nikatengenezwe kwa harusi.” “Nahisi nitakukuta. Sitakawia. Mzee Msindai anataka nikaache damu hospitali ya Usalama wa Taifa. Sikawii maana wananisubiri.” Sabrina akashangaa. “Damu ya nini tena?!” Akajiuliza ila akaona anyamaze tu. Jack akatoka.

Ndoa Na Iheshimiwe Na Watu Wote.

J

ack na mkewe wao hawakwenda kanisani. Waliamua kwenda ukumbini tu. Ulipofika muda wa kwenda ukumbini, wakatoka. Sabrina alipendeza sana. Walimtengeneza vizuri, hata kule kukonda kukampendeza. Na Jack alivaa suti nyeusi nzuri. Akapendeza maana  alipitia kufanyiwa na usafi wa kichwa. Kwa hiyo wote wakatoka wasafi. Ungejua yapo mafanikio kwao. Walinukia neema tupu. Jack akatoka kama Naibu Waziri kwelikweli na mkewe. Walifika ukumbini wakatafuta meza ya Msindai. Jacinta alifurahi sana kumuona Sabrina. “Hapa Jack asipoangalia ataporwa mjini! Umependeza sana Sabrina, wifi yangu! Upo kama kabinti kasikokuwa na mtoto hata mmoja! Kama mwana mitindo ulioshushwa kutokea Los Angeles!” Sabrina alicheka sana. “Asante wifi yangu. Shikamooni.” Akasalimia wengine hapo mezani. “Bi mdogo naona mambo yako si mabaya.” “Na wewe umependeza Joy. Na shem pia. Wote mmependeza.” Junior akaitikia. Jack kimya.

“Baba na mama wako wapi?” Akauliza Sabrina. “Mzee Msindai yule kule mbele kwenye meza ya wazazi, naona hajaja na mkewe.” Akajibu Jacinta na kuendelea kunywa. Hata Jena hakuwepo. Stori zikaendelea hapo mezani. Jack na mkewe kimya. Maharusi wakaingia, sherehe ikaanza rasmi. Kila mtu kula na kunywa na MC mcheshi basi kukawa na kucheka. Ila Sabrina akawa amepoa tu. “Unasikia baridi?” Jack akamuuliza kwa kumnong’oneza sikioni. “Naona hapa ukumbini wamewasha AC kali!” Sabrina akalalamika. Jack akasimama akavua koti lake kisha akamfunika vizuri. “Asante. Lakini si na wewe utasikia baridi?” “Nipo sawa.” Akavuta kiti cha Sabrina karibu na kiti chake. Kisha akampitishia  mkono juu. Sabrina hakukataa. Akajisogeza karibu, akawa kama amemuegemea mumewee upande mmoja, Jack akamkumbatia vizuri. Wakatulia. Ila Sabrina akasikika kuvuta pumzi kwa nguvu kisha akatulia. Wao wawili wakawa wala si wazungumzaji, ila watizamaji tu. Kimya.

   Kilipofika kipindi cha waalikwa kucheza, baada ya maharusi kufungua kwa mziki wa taratibu, Junior akasimama na kumshika mkono mkewe na kumuongoza njia pale mbele ili wacheze na maharusi. Junior akamshika mkewe vizuri, Joy akamkumbatia mumewe, wakaendelea kucheza. Wakatulia wakiwaangalia wanao cheza. Jack akambusu mkewe sikio ambalo lilikuwa upande wake mpaka Sabrina akasisimkwa, akacheka na kumwangalia. Hakutegemea! “Twende na sisi tukacheze.” Sabrina akajishauri akisikiliza huo wimbo, ukamvutia. Akatingisha kichwa kukubali. Jacinta kimya akiendelea kunywa taratibu.

Akatoa koti la mumewe, Jack akalivaa na yeye akamungoza njia mpaka pale mbele. Sabrina hakujivunga, akamzungushia mikono yote juu ya shingo, Jack alifurahi akatamani kumuuliza baba yake kama anaona! Akamkumbatia na yeye vizuri, wakaanza kucheza. Kweli walipendeza. Alivaa gauni lililomkaa vizuri sana na likaenda na mwili wake. Walionyesha hadhi waliyonayo kwa wkati ule. Sabrina alivaa nadhifu sana kama mumewe. Pendo huwa ananunua nguo kwa mwanamke anayetoa nguo, viatu na vitu vingine kutoka nje ya nchi. Alimuunganisha na Sabrina na yeye akawa mteja mzuri sana wa huyo mama. Kwani na wao huwa wananunua bila kukopa, hulipa siku wanapochukua kitu wanachokipenda kutoka kwa huyo mama. Basi kila anapoingiza mzigo mpya nchini  Pendo na Sabrina wanakuwa miongoni mwa wateja wake wa kwanza kuwaambia ili wachague wao kwanza kabla ya wengine. Kwa hiyo hiyo nguo Sabrina aliinunua tu na kuiweka kabatini ikisubria siku ya
kuvaliwa maana alimuitia mzigo mpya na hilo gauni akamwambia alimchukulia maalumu kwa ajili ya kamwili kake kadogo. Ndipo Sabrina akalilipia na kuliweka tu kabatini.

Siku hiyo alilivaa na kiatu cha juu. Nywele ikatengenezwa vizuri. Sabrina alipendeza sana. Jinsi Jack alivyokuwa amemkumbatia, mpaka Sabrina akajilaza kifuani wakati wakiendelea kucheza.

Mzee Msindai akaenda kumchukua Jacinta wakacheze naye. Na wao wakaenda kucheza palepale pembeni yao. Wakacheza nyimbo nyingine mbili ukiwepo wa ‘It wasn’t easy, but it’s worthy’ uliopigwa na mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili nchini Marekani, mwanamama Cece Winans. Mzuri sana, aliuimba kama Yesu akiongelea kazi nzima ya msalaba, lakini ukaendana kabisa na wanachopitia Jack na Sabrina. Kwamba, ‘Haikuwa Rahisi, Lakini Inastahili’. Ukisikiliza kwa haraka bila kusikiliza maneno yake unaweza usielewe kama ni wa Mungu unasikika kama wimbo wa taratibu tu kama nyimbo nyingine za kimapenzi, lakini ulibeba maana kubwa na nzito, ulifanya wasikilizaji maneno kwenye nyimbo kutulia na kutafari zaidi.

Don't think for a moment, I never felt the pain, You can't imagine, The hurt and the shame, They put the nails through my hands, Pierced my side, please, understand

It wasn't easy, but it was worth it, It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it, It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it, I didn't have to do it, But I did it anyway

'Cause I really love you, So much I took your place, I died for your sins, Yes, I'm the one, Don't take it lightly what I've done, It wasn't easy, but it was worth it, oh, It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it, It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it

I left my throne, My purpose was the cross, Shed innocent blood, I paid the cost

It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it (but it was worth it), It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it, It wasn't easy, it wasn't easy, It wasn't easy, but it was worth it, It wasn't easy, it wasn't easy (it was worth it, yes it was), It wasn't easy, but it was worth it

It was worth it, ooh, No, it wasn't easy, no, it wasn't easy

But it was worth it, Ooh-oh

Wakaucheza huo wimbo vizuri na kufuatisha maneno mpaka ulipoisha. Ilipoanza Twist, Sabrina akajitoa mikononi kwa Jack, wakaondoka hapo sehemu ya kucheza wakicheka, kwamba wamesalimu amri, wawaachie wawezaji. Wazazi wengi wakasimama kuingia kucheza kwa furaha zote. Enzi zimerudishwa! Wakarudi kukaa “Naomba urudi kukaa kama vile ulivyokaa mwanzo.” Jack akamsihi mkewe. Sabrina akamgeukia. “Sasahivi sisikii joto. Nipo tu sawa.” Sabrina akajivunga. Jack akamwangalia, Sabrina akatoa tu tabasamu na kurudi kuangalia waliokuwa wakicheza. Akamsikia Jack amejivuta mpaka kwenye bega lake, akamuegamia yeye. Akamchungulia pale alipojiegemeza. “Nakupenda Brina.” “Najua.” Jack akamvuta mkono akaanza kuchezea pete zake, wakatulia. Sabrina akageuka na kumbusu kichwani maana bado alikuwa amemuegemea. “Nashukuru mama.” Sabrina akacheka, wakatulia.

Wakashitukia mzee Msindai amewasimamia. Wote wakasimama kama watoto wa shule ya msingi waliofumaniwa. “Shikamoo baba.” “Marahaba mama. Umekula vizuri?” “Naona nimezidisha.” Mzee Msindai akacheka. “Nakusanya maziwa ya kaka mdogo.” “Unajuhudi ya kunyonyesha! Lakini hiyo ni nzuri sana.” “Asante baba yangu. Naona na wale kuku wa kienyeji ulioniletea wanasaidia kuongeza maziwa. Asante sana.” “Karibu. Wewe Twist hujui kucheza?” “Hata kidogo. Naweza kuanguka kabisa! Umependeza sana baba.” “Asante. Suti hii zawadi kutoka kwa Jacinta. Naipenda sana. Huwa navaa kwenye vitu muhimu kama hivi.” “Basi acha na mimi nije kukununulia ingine. Ziongezeke.” “Afadhali nipate nzuri ingine ya kubadilisha.” Wakacheka kidogo, Jack kimya. “Tutembee kidogo.” Jack akajua ni yeye anaambiwa atoke wakazungumze nje. “Nitarudi, Sabrina.” Akavua koti lake na kumvalisha mkewe, baba yake akatangulia nje. Wakamuacha Sabrina hapo mezani peke yake, wengine wote wakicheza mbele. Jack na baba yake nje kabisa ya ukumbi. Sabrina kimya akijiangalizia tu.

Baada ya muda Jack akarudi akiwa amepoa haswa. Akajua mazungumzo kati yao bado hayaendi vizuri. Akarudi na kutulia kupita kawaida. Sabrina akamuona mzee Msindai anapita kurudi alipokuwa amekaa. Sabrina naye akamuacha tu.

Kila Kosa Na Garama Yake. Hata Kama Mungu Amesamehe, Huwezi Kuepuka Kulipa Garama.

Wakati wapo njiani kurudi nyumbani baada ya harusi kuisha, akatoa bahasha na kumkabidhi Sabrina. “Asubuhi nilikwenda kupimwa. Baba alitaka niende nikaangalie afya yangu.” Hilo halikuwa jambo baya, hata Sabrina hapo akafurahia. “Mbona umepoa sasa? Umepata matokeo mabaya!?” “Fungua usome.” Sabrina akaingiwa hofu akafungua na kusoma. Akaona kila kitu kipo Negative kwamba hana ugonjwa wowote. “Sasa mbona umekosa raha kwenye majibu mazuri hivi!?” “Phina amerudi. Safari hii anamadai mengine.” “Ni nini tena!?” Sabrina akamuuliza akiwa na wasiwasi.

“Amemtafuta Jena mpaka kazini kwake. Amemwambia anampango wa kunishitaki mimi kuwa natumia madaraka niliyopewa na Raisi, vibaya. Narubuni wanawake kwa kutumia cheo nilichopewa. Nikishalala nao, nawatelekeza. Ananishitaki kwa kumtelekeza yeye akiwa mjamzito, mpaka akaugua na kumpoteza mtoto wetu. Anasema japokuwa ushahidi ulipotezwa, yeye Jena atabaki kuwa shahidi wake maana alishamfuata. Akakubali kuwa mtoto ni wa Msindai. Akamuahidi yeye na mama kumfanyia babyshower na kumkaribisha ramsi kwenye familia. Anasema anao mashahidi waliosoma comment ya Jena, na ku like post yake ya babyshower kuashiria kweli alikuwa mjamzito wa mtoto wangu.” Sabrina akashituka sana. Akatulia kwa muda akifikiria.

Mwishoe akaona aulize tu. “Sasa baba ameshaurije?” “Daah!” Jack akasika kuumia zaidi. “Niambie tu.” “Hivi tunavyozungumza, Ibra na Phina wamerudi  kuwa timu moja. Maana mwanzo..” Ikabidi Jack amuelezee Sabrina sasa kuanzia mwanzo walipoungana na kumfuata nyumbani mpaka mwisho jinsi walivyofuta ushahidi kwenye simu zao na kuchukua hata nakala za picha walizokuwa wamechapisha. Sabrina akazidi kuwaogopa hao kina Msindai. Ikabidi akae sawa asikilize zaidi.

“Sasa kama ulivyosikia siku ile pale nyumbani, simu yangu ilibadilishwa, na inafuatiliwa. Sasa nafikiri katika yote hayo, kupoteza mtoto na kuhamishwa kituo cha kazi, inavyosemekana Phina akaanza kunitafuta bila mafanikio. Nasikia ijumaa alikuja mpaka pale ofisini, akaambiwa hawezi kuniona mpaka miahadi. Ndipo nasikia akamtafuta tena Ibra ili aungane naye kuendeleza mipango yake ile ya kwanza. Safari hii nasikia Phina amemuahidi Ibra kumpa ushirikiano wote.” “Naomba nikuulize kitu Jack. Na naomba uwe mkweli.” “Niulize tu.” Sabrina akamwangalia kwa muda, mpaka ikabidi Jack atoe macho barabarani na yeye amwangalie.

“Niulize tu Brina. Na nakuahidi sitakudanganya kama najua jibu lake.” “Ni nini ulimuahidi Phina huko mlipolala?” “Acha nikwambie ukweli Sabrina. Hapakuwa na kutongozana, wala mazungumzo. Mpaka nahisi Phina alinitega jamani! Maana unajua yeye alikuwa miongoni mwa watu wanaoandaa safari za Wizara. Alijua kama tutasafiri mimi na wenzangu. Wao walitangulia huko kuanza kuweka mipango. Kwa hiyo alijua nani atalala wapi.” “Wewe ulijua kama yuko huko?” “Mungu wangu nishahidi Sabrina. Sikuwa nikijua kama yuko huko na hata kama alihusika na mipango ya malazi yetu huko.”

Anyways. Tulipofika kesho yake tulikwenda kwenye mkutano kama kawaida, nikarudi chumbani baada ya kukaa na wenzangu baa. Mimi nikachoka, kwa sababu mimi sinywi. Nikala, nikaamua kwenda kulala. Wakati nishavua nguo kabisa, nipo kitandani, Phina akaja kunigongea. Kwanza nilishituka. Sikutegemea kama angekuwepo kule maana waliokuwa wameongozana nao nilishakutana nao wote. Akasema kuna sehemu yeye na mwingine walikwenda kama matembezi ndio maana wakati sisi tukisalimiana na wenzake, sikumuona. Basi, akasema kuna kitu anaomba azungumze na mimi. Tena Mungu nishahidi. Nikamwambia kabisa sipo vizuri, kwa kuwa nilishapanda kitandani kulala. Akasema hatanichukulia muda mrefu. Nikamwambia asubiri hapo mlangoni. Nikarudi kuvaa pensi, nikamkaribisha.”

“Siwezi kukwambia aliyoniambia, lakini nikaja kushitukia nimeshalala naye. Nikamwambia kabisa, nimefanya kosa, sikutakiwa kulala naye. Nikamwambia mke wangu ni mwaminifu sana na ananipenda, sikutakiwa kumfanyia hivyo. Nikamuomba avae, atoke. Unajua ni ile aina ya milango ukitoka, huna haja yakufunga tena kwa ndani. Inajifunga tu yenyewe ila kuingia ndio mpaka mtu wa ndani akufungulie, au utumie kadi. Kwahiyo nikamuacha akivaa ili atoke, nafikiri nikapitiwa na usingizi. Nilikuwa nimechoka Sabrina. Siku ilikuwa ndefu.” “Na umetoka kufanya mapenzi.” Sabrina akamalizia. Hapo Jack hakutaka kuchangia kabisa ili papite kwa haraka. Akaendelea kwa haraka.

“Basi nafikiri alipoona nimelala ndipo akanipiga picha.” “Kwa hiyo si kwamba mlilala mpaka asubuhi!?” “Hapana! Tena hata yeye nilimuuliza ni kwa nini anatangaza kana kwamba nililala naye usiku kuchwa? Ni kama hakunipa jibu la kueleweka. Ila kama nilivyokwambia, sikutaka kumbana sana, nikitaka atulie, awe upande wangu, ili kufuta hizo picha na kumtuliza. Sasa sasahivi ndio nasikia wapo na Ibra. Wameshafikia magazeti zaidi ya matatu.” “Mmmh!” Sabrina akaishia kuguna.

“Sasa baba anasema amefanikiwa kufuta hiyo habari kwenye magazeti makubwa, ila ya Udaku imeshindikana, ndio maana ameniomba nizungumze na wewe mapema. Ujue kesho hiyo habari itakuwa imeenea.” “Sasa baba anataka mimi nifanyaje?” “Kwanza ujue ili isikushitue kama walivyokushitukiza mwanzo, wote tukapaniki.” Sabrina akapoa, akakumbuka jinsi ilivyoingiwa hofu mwanzoni.

“Anasema mambo mengi yanaweza kuchimbuliwa. Mengi mno. Yangu, yako mpaka watoto pia. Anachosema tunaweza kuja kujaribiwa kumjibu yeyote yule. Ameomba kama utaweza, unyamaze kabisa. Hata usijaribiwe kujibu hata kwa hekima. Halafu tuache tuone watasababisha madhara makubwa kiasi gani. Anasema tunaweza kutumia nguvu kubwa kupambana na hili, kumbe madhara yake yanaweza yasiwe makubwa sana. Kwa sababu sasahivi hawana tena ushahidi. Watakachoweza ni kunichafua na mengine ambayo hatujui.” Sabrina akanyamaza. Akajivuta mwisho kabisa wa kiti, akatulia.

“Najutia Sabrina. Najutia sana.” “Najua Jack. Na pole.” Jack hakuamini. Akamwangalia. “Namaanisha. Najua hata kama wewe ni malaya wa kiasi gani, lakini najua usingekuwa mjinga, kukubali kuingiza familia nzima matatizoni kwa kiasi hiki.” Jack akaumia sana. “Kwa hiyo wewe unaamini mimi ni malaya?” “Samahani imetoka mdomoni vibaya, Jack. Lakini najua unaelewa namaanisha nini. Kuwa wewe si mjinga kujiingiza matatizoni kwa kiasi hiki.” Wakatulia.

“Najua sasahivi ndio unaweza kurudi Singida kabisa! Maana kuanzia kesho, mjini hapa patachafuka kwelikweli.” Jack akawa kama anamjaribu tu kujua atasema nini. Sabrina hakujibu. “Maana nasikia amesema hana chakupoteza tena. Kumbe mwanzoni hakutaka Ibra aseme si kama alivyoniambia akiniaminisha anataka asiniharibie mimi, kumbe alikuwa akijilinda na yeye kikazi na kujua nitazaa naye. Sasa nasikia amesema kwa kuwa na kazi pia amepoteza, hataogopa hata akiitwa kwenye kuhojiwa popote kule, atakwenda kuongea yote.” “Ameamua kutokwenda huko Lindi?” “Unajua yupo na Ibra ambaye na yeye aligoma kutoka hapa mjini. Kwa hiyo atakuwa amemshauri tu asiende, atafute kazi hapa mjini.” Sabrina akatulia mpaka nyumbani.

Alipofika tu, wakina Pina wakatoka mbio. “Tukupokee dada?” “Mna njaa zisizowaisha nyinyi! Na safari hii sijaleta kitu. Nimetoka kwenye harusi.” “Dada naye! Si ungebeba hata kipande cha keki!” “Songa ugali ule wewe mtoto. Acha njaa zisizoisha.” Sabrina akapitiliza chumbani kwake. Akaenda kuoga, kazi ya ulezi ikaanza. Kunyonyesha na kukamua. Jack akamfuata tena. “Naomba safari hii usikaukwe maziwa kwa mshituko, Sabrina.” “Hapana. Nashukuru kuniambia mapema.  Kwanza imenisaidia kujua moyo wako na kunituliza. Mwanzo ulinikimbia Jack, ikanichanganya zaidi nikijua umekusudia kurudiana na Phina! Na nikajua ulianzisha tabia ya kulala na wanawake huko nje.” “Huo udhaifu wa kukimbia na kuingiwa hofu, najua nilikuahidi nitabadilika, lakini nafikiri niongeze juhudi kuweza kukukabili kipindi cha matatizo tuwe tunazungumza nisiwe nakuacha ukiwa huna taarifa kamili.”

“Nilikuwa nikitaka kukwambia safari hii sitapata mshituko kama mwanzo mpaka kukaukiwa maziwa kwa kuwa sasahivi ni kama akili imeshajindaa kupokea chochote, maana nishafikiria mabaya zaidi. Akili imejiandaa na mpaka ambayo wewe hujayasema pale garini, mimi nishayafikiria na akili imeyapokea. Kwa hiyo hakuna kitakachonishitua tena.” Ikabidi Jack aingie na kukaa hapohapo chumbani kwa watoto wao wakiume.

“Kama nini tena ulichofikiria!?” “Kuvuliwa madaraka!” “Umefikiria mbali! Maana na hilo baba ameniambia nijiandae nalo endapo itakuwa skendo kubwa. Sema nilikuwa naogopa kukwambia.” Sabrina akanyamaza na kuendelea kunyonyesha mtoto aliyekuwa amelala huku akivuta. “Nimekuangusha eeh?” “Nafikiri zaidi Mungu aliyekuamini.” Sabrina akajibu na kunyamaza. Jack naye akabaki ameinamia magoti anawaza. Kimya.

~~~~~~~~~~~~~~

Akasubiri mpaka mkewe akamaliza shuguli zake hapo chumbani, akawa na kazi ya kumfuata mpaka jikoni alipokuwa akisafisha vifaa alivyotumia kukamulia maziwa. Anamfuata nyumanyuma ila kimya. Sabrina akamuacha tu mpaka akamaliza na wakahamia chumbani. Kimya tu. Akaweka mambo yake sawa, Jack yupo tu. “Naomba lala Jack.” “Nakusubiria wewe.” “Mimi namalizia kujisafisha, nitoe harufu ya maziwa, ndio nije tulale.” “Nimefurahi ulivyosema hivyo.” Sabrina akamwangalia na kuelekea bafuni.

Akatoka bado yupo. Akapanda kitandani. “Utarudi Singida?” “Kwani huko ndio hakuna magazeti?” “Lakini kweli. Kwa hiyo utafanyaje?” Akavuta pumzi kwa nguvu na kubaki akifikiria. “Unazidi kunichukia eeh?” “Hapana Jack. Umenifanya nikumbuke hapo ulipo. Mimi nimeshakua hapo Jack. Mara mbili. Ila hapo ulipo sasahivi, ndio panafanana na Dodoma kabisa, kule chuoni. Kila anayekutizama, unahisi anakuona upo uchi.” “Kweli aisee! Au anakuhukumu! Mpaka hao wasichana wako wa kazi naona hata wanavyoniangalia sio kama zamani. Sasa sijui ni kweli au mawazo tu!” “Inaweza kuwa kweli au ni hofu tu.”

“Sasa ulifanyaje?” “Ni wewe Jack! Huoni jinsi nilivyojirudi kwa haraka? Ulinitoa mavumbini. Chini kabisa. Ndani ya masaa 24 ukanirudisha juu kabisa na ukabadilisha historia yangu pale chuoni. Haikuniondolea ile aibu ya kukataliwa na Emma vibaya vile, lakini angalau nikaonekana ni wathamani. Kwamba hata kama Emma amenidharau, lakini bado mtu kama wewe unaniona wa thamani. Ilinisaidia sana.”

“Hata mimi umenisaidia sana jinsi ulivyokuja na mimi kwenye harusi. Nimeona hata jinsi baba alivyozungumza na mimi safari hii imekua kwa heshima. Imekua kama aliyekuwa akinitaarifu kinachoendelea bila ule ukali na uchungu kuona nimemuangusha, na kushindwa hata kunitizama. Nakushukuru Brina.” “Na mimi nimepata wakati mzuri, Jack. Nilikumiss mpenzi wangu. Mwenzio nilijua nimeshakupoteza huko kwa Phina!” “Tafadhali nisamehe Sabrina. Nisamehe.”

 “Wewe niambie kile unachotaka nifanye. Nitafanya tu.” “Usiende Singida. Nimejiambia hata kama nitapoteza hii kazi, nitatafuta kazi hapahapa Dar, tutaishi tu. Au unaogopa?” “Hata kidogo Jack. Mimi tena! Nitakuwa muongo eti kwa hapa tulipo ndio nijidai eti naogopa maisha! Nimetoka pabaya sana, na wewe unanijua. Hapa nilipo ni bora mno. Hata kama tutashuka wakichukua hayo majukumu ya Unaibu waziri, lakini najua hatutashindwa maisha.”

“Halafu acha nikusaidie jambo. Hapo ulipo sasahivi, acha kufikiria mambo mengii ukijiogopesha. Ushafika mwisho wa baya zaidi. Kufukuzwa kazi.” “Hilo wala halikuwa baya la mwisho, Brina. Baya langu la mwisho ni wewe. Kazi hainisumbui hata kidogo. Nimesoma mimi Sabrina, eti! Halafu nimeshakuwa na uzoefu wa kazi. Siwezi kukosa kazi. Wala siogopi ila nasikitika tu, maana tulifika mbali haswa! Nachukia kuanza upya! Tena nikiwa nimeshajiingiza doa ambalo mtu anaweza kulitumia hata kisiasa kuwaambia watu wasinichague kwa sababu hiyo, kutumia mali ya umma vibaya nikirubuni wanawake!” “Naomba tulale Jack. Acha mengine yajijibu yenyewe. Kuna garama ya kulipa, hiyo huwezi kukwepa. Jiandae tu. Ni kwa namna na jinsi gani, muda utajibu hayo. Sasa hivi acha tulale, mwenzio nina kachanga. Sasahivi ataamka anataka kunyonya. Acha nipumzike kidogo.”

“Nashukuru Brina. Asante kukubali kusimama na mimi.” “Sasa wewe ulifikiri nitakukimbia?” “Sijui!” “Nilikwambia naogopa utaniua kwa magonjwa. Sasa ungeniua kwa magonjwa vipi kama nilikuwa na mpango wa kukuacha? Ni kwa kuwa sikuwa na uhakika na wewe Jack, ndio maana nilikuwa nikijiandaa hata kwa binti zangu. Lakini mimi sijui kumkimbia mtu wakati wa matatizo, mpaka ungenifukuza mwenyewe kama alivyofanya Tino na Emma. Ila ni kweli nilikuwa sijui itakuaje kwenye aina ile ya ndoa! Na mtoto! Ndio maana nikaona ni bora niende Singida, nikupishe ufikirie.” “Wewe siwezi kukuacha hata iweje.” Sabrina akanyamaza. Wakalala.

Jumapili.

A

lipoamka na kuweka mambo sawa, akaanza kupiga simu. Akaanza kwa Joy. “Bi mdogo hujambo?” “Njooni basi kwangu leo kwa chakula cha jioni. Mkija mnakuta kipo tayari mnakula ili muwahi kuondoka kwa ajili ya kuwahi usingizi wa Claire.” Joy akaanza kucheka. “Shida yangu ni shem, Joy. Najua nikimuomba yeye peke yake ndio aje sitakuwa nikimtendea haki. Nilimsikia jana akimwambia baba, leo anataka kupumzima tu nyumbani na familia, hatoki.” Joy akabaki akifikiria. “Mbona unapatwa uzito?” “Kwa kuwa leo tulipanga tusitoke kabisa, hapa bado tupo kitandani.” Sabrina akafikiria kwa haraka, akasema basi niruhusu mimi nije nizungumze naye hapohapo kwako. “Hapo nitakupenda. Nilishaanza kujisikia vibaya kukukatalia.” “Usijali. Wewe wangu. Muda gani mzuri ataweza kupokea wageni? Nitakuja peke yangu wala siji na timu yangu.” “Kama ni hivyo kuanzia saa 10 sio mbaya.” Akamuaga Joy na kuangalia muda. Akajua mzee Msindai atakuwa ameshaamka.

~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia na kupokea kwa haraka tu. Akasalimia. Akamuuliza habari za watoto, akamjibu. “Leo mnakwenda ibada ya saa ngapi?” “Kama kawaida yangu, mama. Ulitakaje?” “Basi nimepatia. Hapa naandaa timu yangu yote, leo tutakuja kuabudu huko na nyinyi. Ila shida yangu baada ya hapo nataka kuzungumza na wewe pamoja na wifi Jacinta, najua shem alisema leo hatakuja kanisani naona yeye nitamfuata nyumbani nikazungumze naye. Sitachukua muda wenu mrefu. Ni mazungumzo mafupi tu.” “Ni kweli najua Jacinta atakuja kanisani, ila Junior alisema leo hawatakuja. Ila ili haya mazungumzo yawe mazuri, tukitoka twende tukale sehemu. Wajukuu wacheze wakati sisi tukizungumza.” Hilo likakaa sawa.

Kitu ambacho hakujua Sabrina, alitengeneza mazingira ambayo Jacinta na baba yake walikuwa hawajui ni jinsi gani kuyafanya yawe hivyo. Angalau familia yao ionekane pamoja.

~~~~~~~~~~~~~~

Hapohapo mzee Msindai akampigia Junior. “Naomba kwa leo tu, nikuombe ubadili mipango yako. Najua ungetamani kupumzika, lakini hili ni la muhimu. Sabrina, yeye mwenyewe amenipigia simu akiomba akutane na mimi pamoja na Jacinta. Lakini wewe alipanga kukufuata nyumbani. Nilipomuomba tutoke kwa chakula baada ya ibada, anaonekana amelifurahia hilo. Nilitaka angalau tuwe pamoja wote kujaribu kuponya kulikoharibika.” Junior akaelewa kuwa angalau waonekane kama familia moja ili hata kama shutuma mbaya zimesambaa, basi jamii ione maisha yao yanaendelea kama kawaida.

“Ametoka kuzungumza na Joy, ila akampa mipango yetu ya leo. Hatukupanga kutoka baba. Nimekuwa na mambo mengi, sijatulia na familia yangu, ndio leo nilitaka kupata nao muda.” “Inaeleweka kabisa. Basi nikuache upumzike.” Mzee Msindai akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina na Jack walikwenda kanisani ambako anasali mzee Msindai, mkewe, Jena, pamoja na Jacinta. Ila mama Msindai hakuwepo wala Jena. Ni Jacinta na baba yake tu. Wakaungana nao hapo kanisani na familia ya Jack. Baada ya ibada ndipo wakaenda kula ambako walikutana na familia ya Junior. Hata iweje, Junior hawezi kumkatalia jambo baba yake. Japokuwa hawakwenda kanisani, lakini waliwakuta sehemu ya chakula. Wakaunganisha meza, wakaa.

Yalikuwepo mazungumzo ya kawaida tu tena Sabrina aligundua ni mazito kama kila mtu anatafuta chakuongea wakati wakisubiria chakula. Sabrina akamuomba Jack kwa kumnong’oneza kuwa, aende na watoto upande wa baharini wachezee maji wakati wakisubiria chakula. Jack akashangaa kidogo. Kwa nini yeye ndio aondolewe hapo! Ila akatii, hata hivyo kuwa katikati yao ni kitu ambacho ilishakuwa ni kama adhabu. Aliogopa watu wa nyumbani kwao kupita kiasi.

~~~~~~~~~~~~~~

Walipojikuta peke yao Sabrina akaanza. “Samahani baba yangu, imekua kama nimewaitisha kikao bila idhini yako.” “Usiwe na wasiwasi. Kwanza ni kama hiki kikao mimi ndiye niliyeitisha ili kukusikiliza. Karibu.” “Nashukuru.” Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi baada ya kujikuta watu wazima hao na nyadhifa zao wakimsikiliza yeye. Akacheka kidogo kwa wasiwasi kujituliza. “Ongea mama Msindai, tunakusikiliza. Usiwe na wasiwasi.” Jacinta akamtia moyo, angalau wote wakacheka.

“Labda nianze kwa kuomba msamaha kwa niaba ya Jack.” Wote wakashangaa, hawakutegemea. “Jack amekosa. Amekosa sana na ametushangaza sisi wote na kuumiza familia. Lakini baba, shem na wifi yangu, Jack anajutia sana. Ana wakati mgumu ambao tusipomsaidia, ataharibikiwa kabisa. Ameingiwa hofu yakupita kiasi. Nafikiri ni kwa kuwa Jack si mkosaji.” Wote kimya. “Najua nyinyi mnamjua Jack, lakini mimi namfahamu Jackson kwa mahusiano ambayo nyinyi hamtakaa mkamfahamu. Na hiyo ni tokea chuoni. Ukweli alichokifanya Jack si kawaida yake hata kidogo. Sasa hivi yupo kama alivyo kwa sababu si mzoefu wa hiki alichokifanya, na nafikiri shetani alipata mwanya hapo, akaona atumie huo mwanya kumuangamiza Jack na kutuvuruga.” Sabrina akaendelea. Wote kimya wakimsikiliza.

“Tulipokuwa chuoni, Jackson alikuwa akililiwa na kupiganiwa na wasichana wazuri sana zaidi ya Phina. Mchana na usiku walikuwa wakimtaka. Na walikuwa tayari kulala naye kabisa. Lakini Jack alikuwa na msimamo katika hilo mpaka akampata Phina, na kuanza naye mahusiano. Akatulia na Phina tu. Na hilo ndilo lililokuwa likimtofautisha Jack na wanaume wengi pale chuoni ila zaidi yeye kwa kuwa alikuwa ametokea kwenye familia yenu hii. Jina kubwa. Pesa na usafiri mzuri ambao pia ulimtofautisha na kila mtu pale chuoni, lakini Jackson akabaki akijiheshimu, hajajichafua kwa mambo ya wanawake. Hata alipokuwa na Phina, mpaka mimi namaliza chuo, sikuwahi kumsikia amefanya alichokifanya. Alitulia na Phina tu japo wanawake wengine waliendelea kumjaribu. Si kwa kuhisi ni kwa kusikia wasichana wa pale chuoni wenyewe walivyokuwa wakimpangia mbinu mbalimbali za jinsi ya kumtega Jackson Msindai, lakini walishindwa.” Sabrina akaendelea.

“Jackson sio muhuni, ni muadilifu. Hata Ibra anajua hilo sema amepanga kumchafua tu. Na hata Phina mwenyewe anamjua Jackson si mtu anafanya alichokifanya kwake kwa sababu hata alipokuwa  na yeye, mimi nilikuwepo karibu na Jack akinisaidia kwa hali na mali, na kila mtu alijua kama Jack ananipenda mimi, lakini baba, mimi ni shahidi wa Jack. Japokuwa alinipenda sana, nikarudi kwake, Jackson hajawahi kumkosea Phina na wengi walitegemea kwamba kile ndio kipindi pengine Jackson anaweza kuendesha mahusiano ya aina mbili au kumsaliti  Phina. Lakini hakufanya hivyo.”

“Na Singida hivyohivyo. Alikuwa na Pam, mimi nikiishi naye nyumba moja, lakini hakuwahi hata kukosea kunijaribisha kimapenzi japo nilionekana nipo huru. Jackson hajawahi kuharibu hata kwa bahati mbaya huko Singida. Alikuwa na mwanamke mmoja tu, Pam. Na hiyo si kwa kuambiwa na Jack, ni kwa sifa nilizozikuta Chamani. Jack hajui, wala hajawahi kufanya hiki alichokifanya. Ndio maana mimi nilipaniki na mimi nikakosea, nikijua ameamua kurudiana na Phina na kuanzisha familia ingine, ndio maana nilikuwa radhi kuondoka kurudi Singida ili kumpa nafasi yeye binafsi na mimi kujiponya nafsi yangu. Nisishuhudie kuwa mwanamke wa kwanza kuachwa na Jackson Msindai katikati ya mahusiano. Najua ni ubinafsi, nilikosea niliyoyafanya, naomba msamaha.” “Pole sana mama.” “Nashukuru baba. Ila.” Akamgeukia Junior.

“Nakusihi shem msamehe Jack. Huko kunyamaza, ni adhabu inayomuumiza kupita kiasi.” “Kama naweza kujibu katika hili.” “Karibu shem.” “Asante Sabrina. Mimi nimejifunza kutoka kwa baba, na imefanyika kuwa tabia yangu. Kama sina kitu sahihi chakusema, au kama sijui kitu, siwezi kusema, ni bora kunyamaza. Na baba nilimwambia, kwa mara ya kwanza, sijui nizungumze  nini na Jack. Pengine bado nipo kwenye mshituko! Sijui! Lakini nimekosa kitu chakuzungumza naye kabisa. Na ukumbuke na mimi nina kijana mkubwa tu Sabrina. Anazungukwa na jamii hiihiii. Ni kiasi cha muda tu, atakuja kujua. Muulize baba huyu kama sikumpigia simu kumuomba ushauri nizungumze vipi na CJ endapo atasikia na kutaka kujua ni nini kilitokea kwa anko wake! Kwa hiyo nipo kwenye wakati ambao na mimi sijui chakusema!” Sabrina akatulia kidogo. Pakatulia.

“Pengine nikuombe shem, wifi na baba, mumsikilize.” Kimya. “Tafadhalini msikilizeni tu. Na yeye msikie upande wake, pengine itamsaidia yeye na nyinyi kujua mumsaidiaje. Nyinyi ndio watu muhimu sana kwa Jack. Nimeishi naye, nimemuona. Anaweza asiwaambie, lakini Shem na wifi, Jack anawaangalia na kuwaheshimu sana. Kipimo chake cha ukamilifu kwenye mambo yake ni nyinyi. Ndoto za Jack sio kuwa kitu kingine ila kuwa kama wewe, shem. Anajua amekosa sana. Na mimi najua amekosa na ameniumiza, lakini naombeni mumsamehe mume wangu. Mtizameni kama zamani. Naomba mumfungulie mlango wa mazungumzo. Najua mpo busy, lakini hii itamsaidia.” Sabrina akaendelea kumbembelezea mumewe.

“Jack ana majukumu mazito ambayo hajawahi kuharibu. Ni mchapa kazi tokea tupo Singida au niseme chuo. Ukimpa jukumu yule, hajui kuharibu. Nahofia shetani asije akaendelea kujipati utukufu katika hili ambalo wengi wanamuangalia. Nimeweza kumtizama na kuzungumza naye kwa kumpa muda aongee, yupo kwenye hali mbaya. Kichwa chake hakipo sawa. Tusipo msaidia sisi sasahivi, Jack ataharibu na kazini. Amejawa hofu na wasiwasi kupita kiasi. Kwa kichwa kama kile hakiwezi kufanya kazi ngumu kama anazozifanya, akafanikiwa.”

“Labda mimi nikuulize swali Sabrina. Mumeo amekwambia kinachoendelea sasahivi? Nikimaanisha unajua kinachoendelea hata asubuhi hii?” “Najua wifi.” Hilo jibu likawashangaza na Sabrina akawaona kama ambao hawamsadiki kama anajua kwa undani huo. “Naweza nisiwe na taarifa kamili, lakini imebidi kuanza kumfuatilia Phina huko Istagram. Amefungua akaunti mpya ambayo ametangaza kuwa hiyo inalindwa kitaalamu hakuna mtu anaweza kumfutia tena vitu vyake. Asubuhi hii amepost tena huko Ista na nimesoma gazeti lililoweza kurusha malalamiko yake yeye kama mtoto wa kike akigandamizwa kwenye jamii. Nimeona na post zake zote na jinsi watu wanavyomuunga mkono katika malalamiko yake. Nimeona wifi yangu. Nimesoma na safari hii ninafuatilia kwa karibu sana.” Bado wakahisi anamtetea Jack akiwa hajapata lalamiko jipya aliloazisha Phina huko mtandaoni, analolisimamia na kupatwa uungwaji mkono zaidi wakimchafua Jack, ambalo hilo ndilo limeumiza zaidi familia yake, zaidi mzee Msindai.

.~~~~~~~~~~~~~~

Ni Nini Kitaendelea?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment