“Nimemuahidi nyumba yake
italindwa mpaka atakapokuja kurudi. Nataka utulie Sabrina. Maamuzi yoyote
utakayoyafanya sasahivi, yanatoka kwenye hisia zilizoumizwa na hofu, unaweza
usipatie sana. Tulia. Nataka utulie kabisa, mimi nipo kwenye kutengeneza. Baada
ya miezi sita kuanzia sasa ukiona bado unahitaji Tino awe karibu na watoto,
hapo utakuwa na akili safi ya kujua uweke mipaka gani. Na yeye Tino
nilimwambia. Amepoteza haki ya ubaba kwa hawa watoto, ataishi nao kwa kauli
yako. Kwa hiyo tulia. Fikiria kisha baada ya miezi sita kuanzia sasa,
tutazungumza tena. Sawa?” “Nashukuru, usiku mwema.”
Sabrina akazidi kulia akielekea kwenye gari ya Jacinta akitamani bora
asingepanda humo.
Wakati Jacinta
akimsubiria Sabrina aingie garini, ujumbe kutoka kwa baba yake ukaingia kwenye
simu yake ya kazini, ‘Singida, HAPANA.’ Akaelewa
mara moja. ‘Nimeelewa baba.’ Akarudisha hayo
majibu na kuweka simu pembeni. Sabrina akapanda garini akilia.
“Nisikilize Sabrina. Wewe
una watoto wachanga watupu. Wote wanakuhitaji wewe kama mama. Tulia ulee watoto
wako. Hakuna atakayeruhusu ukapata shida ya kuishiwa pesa. Usiogope. Tulia kwa
kipindi hichi ulichoumizwa, pata muda wa kufikiria ili utoe maamuzi sahihi.
Unanielewa?” Sabrina akatingisha kichwa akilia kwa uchungu akiumia kwa nini
wamfukuze Tino.
Alilia mpaka akafikishwa
kwake, analia na kushindwa kunyamaza. “Nisikilize kabla haujashuka garini. Pina
nenda kampe huyo kaka maziwa ya kaka Brayan, alale ili mama yake naye aje
apumzike.” Pina akashuka garini na mtoto. Wakabaki wao wawili. “Mambo ya Phina
yamemtingisha sana baba. Ni jambo lililotekea bila kutegemea. Analalamika
kumuamini sana Jack, alidhani yupo kama Junior. Sasa, kwa jinsi lilivyolipuka
hili la Phina, na Tino naye akawa anaonekana na watoto mtaani, ikawa ni fujo,
hatujui tutulize wapi, tuache wapi. Na madhara yake si kwenu tu, ni familia
nzima kama ulivyomsikia baba. Katika watoto wa Msindai, Junior amekuwa kioo cha
jamii kwa muda mrefu sana. Hapajawahi kutokea skendo yake hata mara moja. Na
mkewe hivyohivyo. Joy hana mambo mengi. Biashara na kupigizana kelele na wanae
kama vile unavyomuona, hata marafiki hana.”
“Ilibidi kwenu baba
mwenyewe aingilie kati kwa sababu nyinyi wenyewe mlionekana kuharibu zaidi
kuliko kutengeneza. Sijui kama unanielewa?” Sabrina akaanza kujisikia aibu. “Mimi
nitakwambia tu ukweli wifi yangu, nikijua unajua nakupenda. Si ndio Sabrina?” Akajifuta
machozi akikubali. “Mlikuwa mkiharibu zaidi kila inapoitwa leo. Katikati ya
yote hayo eti Tino aliyekuwa amefungwa jela, anatokea Wizara ya Vizazi na Vifo
na barua kutoka kwa Sabrina Msindai, akitaka watoto wabadilishwe majina! Kutoka
kuwa Msindai, sijui waitwe nani sijui! Ilimshitua sana baba na kuamuru Tino
apelekwe alipo.” “Baba alijuaje wifi!?”
“Nakwambia hivi, hakuna jina la Msindai likatajwa mahali kwa hila, asisikie.
Ana masikio kila mahali. Ndio maana ikabidi kuingilia kati yeye mwenyewe alijua
nyinyi wote mnatengeneza mkiwa mmepaniki.” “Nimeelewa.
Na samahani. Ila naomba nikuombe kitu.” Sabrina akajifuta machozi.
“Nini?” “Ikitokea nakufa wifi, naomba angalia wanangu. Popote
walipo, jicho lako liwe kwao.” “Hilo nakubali. Lakini nataka uondoe
mawazo ya kufa ila kuishi ulee wanao mwenyewe. Unanisikia Sabrina?” “Nasikia, ila inatokea. Na inaweza kutokea.” “Hilo
nimekuahidi nitafanya kama na mimi nitakuwa hai. Lakini nataka uanze mabadiliko
yako wewe binafsi. Sasahivi nenda kapumzike. Lala kama mtoto mchanga kabisa.
Usiku wa leo Pina atalea watoto. Nitaenda kuzungumza naye. Nakupa dawa za
usingizi. Kalale kabisa. Naomba jaribu kutulia, upone. Umekonda, umechoka,
usiruhusu watu kukuita kinyago kwa makwazo ya Jack. Hastahili. Unanielewa
Sabrina?” Sabrina akatingisha kichwa kukubali.
“Naomba anza kwa kutoa
hizo nywele kichwani. Hazijakupendeza hata kidogo. Kesho asubuhi badala ya
kukimbilia Singida na kwenda kujionea huruma huko, anza kwa kwenda saluni. Suka
nywele nzuri, pendeza. Jitengeneze, mimi nitakulipia garama nzima, ni ofa yangu.”
Sabrina akacheka akiwa ameinama. “Kesho ni alhamisi. Ijumaa tunatoka kwa
chakula cha jioni. Mimi, wewe, Joy, na Pendo. Bila watoto. Tunakwenda kula na
kunywa mpaka tuchoke ndio tunarudi makwetu. Hakuna kurudi Singida. Kama
hujaelewa, ndio mzee Msindai amekutambua ramsi.” “Kweli!?”
“Wewe mpaka ametangaza wanao ni warithi wake! Unafikiri ni kitu kidogo?”
Sabrina akabaki kimya akisikiliza.
“Kwa mara ya kwanza baba
ametoa wosia wake mbele ya Junior ambaye wote tunajua ndio mrithi wake. Na amefanya makusudi kuwatangaza
mbele ya watu wote mpaka mama mwenyewe amepoa! Wewe na Joy ni Msindai. Baba
anatambua watoto wako wote, Sabrina. Anza kuishi kama unayejielewa, au kama
vile Joy. Hakuna kumpisha mtu hapa mjini. Mjini haondoki mtu labda ndani ya
jeneza.” Sabrina akacheka. “Pambana kufa kupona mpaka wewe ndio ubaki umesimama.
Usikimbie hovyo. Mimi nipo na wewe, na hao warembo wako ni jukumu langu
nalipokea kwa asilimia zote.” Sabrina alifurahi sana, hakutegemea. “Muda na
wakati wowote, nipigie. Unanielewa?” “Nashukuru wifi yangu. Ila kweli natamani
ningeyasikia haya muda mrefu, wifi. Haya yote yamebadili hata mtazamo wangu na
imeniondolea hofu. Nahangaika kwa ajili ya wanangu wifi! Sikutaka kuacha
wanangu hawa wawili pabaya.” “Babu yao achasema tusichanganywe na hiyo rangi
yao. Na wao ni warithi wa Msindai. Sasa kama ni warithi wa Msindai mwenye mali
zote hizo, unafikiri watakuja kupata shida?” “Sasa hivi nimeridhika wifi yangu.
Roho yangu imeanza kutulia. Na hivi na wewe najua umeshawachukua, hata Jack
akiniua kesho sina wasiwasi.” Safari hii Sabrina akasikika ametulia.
“Hawezi. Sasa hivi jicho
la baba lipo kwake mpaka namuhurumia aisee!” Wakatulia kidogo. “Haya twende
ukanywe dawa, nataka ulale mpaka ukorome kabisa. Usiku wa leo watoto wakilia,
si jukumu lako. Kesho saluni siku nzima. Hawa kina Msindai watakua sawa tu,
usitie shaka.” Sabrina akacheka na kushuka garini. Jacinta naye akashuka,
wakamkuta Jack amejiinamia hapo sebuleni. “Nataka usiku wa leo Sabrina alale
kabisa. Nampa dawa ya usingizi, nataka alale atulie kabisa. Hata kama unajambo
lako unataka kuongea, unyamaze Jackson. Maana wewe ni msumbufu.” “Sawa.” “Na
usaidie alale. Sio waanze kumgongea nakuanza kumuamsha wakiuliza maswali ya
watoto. Hakikisha wewe unaweka sawa mambo yote. Asubuhi uondoke hapa pakiwa
pako sawa, maana akiamka, anakwenda saluni. Ijumaa kama ulikuwa na mipango
yako, uahirishe ujue unakibarua chakulea, sisi tunatoka na Sabrina.” “Hata
hivyo sikuwa na mipango mingine.” Jacinta akamtizama kama mchape kofi. Sabrina
akapitiliza chumbani. “Nashukuru dada.” Jack akanong’ona. Jacinta akaelewa
ameshukuru kumfanya Sabrina abaki. “UKOME.” “Nishakoma.” Jacinta hakumjibu
akamfuata Sabrina chumbani.
Sabrina alikuwa amechoka,
zaidi mawazo na mshituko mpaka maziwa yakakata. Na kwa kuwa hakuwa mnywaji
pombe, dawa aliyopewa na Jacinta, ilimchukua kwa haraka sana hata asijue alipo.
Alilala kama mama asiye na vichanga ndani ya nyumba. Alikuja kuamshwa na kilio
cha Brandon, akadhani ni usiku kumbe saa nne asubuhi ya siku inayofuata.
Akataka kutoka kitandani, akasikia kizunguzungu, akarudi kujilaza na kumuita
Pina. “Mlete.” Akashangaa anaingia Jack na mtoto. “Huyu mtoto anakataa maziwa
anayopewa na dada yake.” “Ngoja nijaribu kumnyonyesha.”
“Nikuletee supu? Pina
amekupikia.” Jack akaongea kwa kujali akisikika kujikomba kabisa. Sabrina hakumjibu
akaendelea kumnyonyesha mwanae mwishoe
akamuita Pina na kutaka aingie. “Naona sina kitu cha kumpa huyu mtoto.
Anajibembeleza tu hapa na ziwa. Naomba supu, ingine nifungashie na uji ule
uliokuwa ukinipikia wakuongeza maziwa, nitaondoka navyo. Kisha nipe maziwa ya
Brandon nimjaribishe huyu.” “Amekataa kabisa.” “Wewe nipe mimi nitampa.” Jack
akabaki amesimama hajui chakufanya.
Sabrina akafanya yake,
akapaacha hapo vizuri, mtoto wake akalala akiwa ameshiba, ndipo akaondoka
kuelekea saluni. Alimuacha Jack hapo nyumbani, hata hakumuuliza muajiriwa huyo,
muda huo anafanya nini nyumbani siku ya kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaelekea saluni yake ya
zamani ambayo walikuwa wakimsuka mtindo wake ambao huwa anapendeza, huna jinsi
ukaacha kumsifia. Wakaenda kumtoa zile nywele, kazi ya ukarabati ikaanza. Mpaka
inafika saa nne usiku, Sabrina hakuwa amerudi nyumbani.
Jack akamtumia ujumbe. ‘Upo salama huko?’ Sabrina akasoma akafikiria, akaona
tu ajibu. ‘Bado nipo saluni. Brandon analia sana?’
‘Babu yake amemletea maziwa amesema apewe hayo hayatamsumbua tumbo. Naona
amelala. Nilikuwa nakuangalia tu, kujua kama upo sawa.’ ‘Bado kama lisaa hivi
wanimalize.’ Hivyo tu kujibiwa, kukamfanya Jack afarijike. ‘Sawa. Usiwe na wasiwasi watoto wote wapo sawa. Wewe malizia
tu.’ Hapo hakujibiwa tena. Akatamani amtumie ujumbe mwingine, akaona
asiharibu. Akatulia.
Usiku huo Sabrina alirudi
kwake saa tano na nusu, akamkua Jack sebuleni. Akataka kupitiliza, Jack
akamuwahi. “Umependeza.” Sabrina hakumjibu. Akapitiliza jikoni, akaweka vyombo
na kupitiliza chumbani kwenda kuoga. Alipotoka akakuta Jack amemuwekea supu.
“Naomba unywe hii supu ndio ulale. Baba ameleta kuku wa kienyeji, anasema
itakusaidia.” Sabrina akaiangalia, akaibeba na kutoka nayo pale chumbani,
hakumsemesha kitu. Jack naye akaona anyamaze. Akaenda nayo chumbani kwa Brayan
na Brandon. Akawakuta wamelala vizuri. Akajua wameshiba. Na yeye akakaa kabisa
sakafuni, akaanza kuinywa hiyo supu. Aliposhiba, akajilaza hapohapo sakafuni
akitafakari, akapitiwa na usingizi.
Jack akajua ndio analala
huko, akamfuata. Wakati anatoa vyombo alivyokuwa ameacha pembeni yake, akaamka.
“Nahisi nimechoka. Bado dawa za wifi zinanipa usingizi. Nilikuwa nikisinzia
siku nzima huko saluni.” “Naomba ukalale kitandani, Sabrina. Mimi naweza kulala
hata kwenye makochi.” “Sawa.” Sabrina akanyanyuka hapo na kuhamia kitandani
hata meno hakusafisha. Akalala hivyohivyo.
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi na mapema, Jack
akaingia hapo kwa kunyata ili asimuamshe, akajitayarisha kwenda kazini, akatoka.
Ijumaa hiyo ndiyo ilikuwa ya Sabrina kutoka kwa chakula cha usiku na wifiye
pamoja na Pendo na Joy. Angalau alikuwa amepata kitu cha furaha akikitizamia.
Akawa na kazi ya kutafuta nguo zitakazoendana na kamwili kake. Akatamani
kupendeza zaidi, maana hizo nywele zilishambadilisha. Ungeweza sema ni
mwanamitindo wa kutokea Los Angeles, Hollywood, aliyefanya juhudi za makusudi
kupungua kwa ajili ya hilo jukumu.
Phina.
Cha Mtu,
Mavi!
P |
hina alikuwa na furaha ya kupokelewa ukweni yeye
na mwanae, kwa ahadi ya kufanyiwa babyshower na mama Msindai! Ikawa kama
ndoto ambayo hajawahi hata kuiota. Hana ajualo, akaanza siku yake na amani
rohoni. Ungemuona Phina, ungejua kuna jema tu linaloendelea maishani mwake.
Akaingia ofisini amependeza kwelikweli. Furaha imejaa, anazaa na Jackson
Msindai, shida iko wapi? Mimba hiyo changa ikaanza kutunzwa kwa kula vyakula bora.
Akaagiza hapo vitu vyake alivyoona ni bora kwake na mwanae, baada ya muda akaletewa.
Akaanza kwa matunda, ndipo akaja sasa mayai, firigisi na mengine mengi akitaka
mwanae akue vizuri. Akasukumia na maziwa yaliyowekwa Milo. Phina akaridhika,
siku ya kazi ndipo ikaanza sasa.
Akiwa ndio ameenza tu
kazi akapewa barua. Akaifungua akiwa amekunja uso, haelewi ni ya nini.
Hakuamini alipoisoma. Wizara ilimtaka aripoti Lindi, Nampunga. Phina alishituka
sana, hakutegemea. Akataka kupaniki lakini akakumbuka hayupo tena peke yake.
Akaamua kumpigia simu Jackson Msindai, Naibu Waziri, baba mtoto, ili amsadie. Akatafuta
namba ya Jack kwenye orodha ya majina kwenye simu yake, hapakuwa na hiyo namba
wala jina la Jackson Msindai. Phina akashangaa. Akaona aingie kwenye jumbe zake
za zamani alizokuwa akichat na Jackson, ili amtumie ujumbe kuwa ni jambo muhimu
na ampigie kwa haraka, hapakuwa na chati. Phina alishangaa karibu macho
yamwagike. Akatafuta tena na tena akahisi kuna mazingaombwe kwenye simu yake,
maana hapakuwa na ujumbe hata mmoja kana kwamba hajawahi ku chat na Jack
kabisa!
Akajaribu kukumbuka namba
ya Jack. Kila namba aliyokumbuka na kupiga haikuwa ikienda kana kwamba hiyo
namba haikuwahi kutumika! Akaanza kuingiwa na wasiwasi. Nani wakumsaidia! Akahangaika,
hasira zikampanda. Akakumbuka picha alizompiga walipokuwa wote nchini Uswiz,
akaona huo ndio wakati muafaka wa kuzitumia kama fimbo ya kumsaidia kubaki
mjini. Akaanza kuzisaka. Akashangaa hakuna hata moja kwenye simu yake wakati
hakuwa amezifuta!
Tumbo likaanza kukoroga.
Akakimbilia chooni. Akaanza kutapika. Akajua mambo ya mimba changa. Likazidi
kuuma kama yupo kwenye siku zake. Hajakaa sawa, tumbo la kuharisha likaanza.
Akaanza kuhara mfululizo kama aliyekula kitu kibaya. Mara ya pili anajisaidia,
damu zikaanza kutoka. Alishituka Phina, karibu aanguke chooni. “Inamaana mimba yangu imeharibika!” Akawa
haamini. Kila alipojifuta, akawa anakutana na damu. Akawaambia wenzie wamsaidie
kwenda hospitalini ili kujaribu kuwahi kuokoa hiyo mimba. Mpaka anafika
hospitalini akawa hatapiki tena wala tumbo la kuhara hakuna, limepo kabisa, ni
siku zake tu! Ikawa kama aliyesafisha tumbo, basi. Phina alikuwa akilia kama
amefiwa na mtoto aliyekwisha nyonyesha.
Daktari aliyemuhudumia
akamuuliza “Kwani ulikuwa na mimba ya miezi mingapi?” “Miwili!” “Au ulipitisha
tu siku zako, maana hakuna dalili ya kutoka mimba ila hedhi ya kawaida tu!?”
Phina akazidi kulia. Akasema anao mpaka ushahidi wa ultrasound. “Ilikuwa ni mimba kabisa!” Hapakuwa na chakufanyiwa.
Akashauriwa akapumzike na kutumia dawa za maumivu endapo maumivu yataendelea.
Phina akaondoka hapo hospitalini asiamini kama yamempata hayo! Alishajiona vile
atakavyotembea na tumbo kubwa akijulikana amebeba mimba ya Jackson Msindai.
Alishaona heshima atakayopewa siku ya babyshower yake! Alishaona vile
atalea huyo mtoto na Jackson! Leo anarudi nyumbani hana kitu! Ulikuwa msiba
mkubwa sana kwake. Aliona ndoto zake zikipotelea chooni, akishuhudia kwa macho
yake.
Kitu cha kwanza alipofika
nyumbani kwake ni kutafuta picha za ultrasound kuthibitisha kweli alikuwa
mjamzito. Phina alitafuta mpaka chini ya godogo, kila mahali, hapakuwa na hizo
picha. Akashangaa sana. Akaamua kumtafuta wifi yake Jena angalau azungumze naye
na amsaidie kumuunganisha na Jack, naye Jena hakuwa akipatikanika kwa simu.
Ikawa kama Jack! Hata jumbe walizowahi kuchati na Jena hakuzikuta.
“Mimi sichanganyikiwi
jamani!” Akaongea peke yake. Akaona aingie Istagram ili amtumie ujumbe huko. Napo
hakukuta akaunti ya Dr. Jena Msindai. Akafuatilia post na comment zake na Jena.
Hazikuwepo! Akazidi kuingiwa na wasiwasi akahisi ni mazingaombwe kweli.
Akatamani kumtafuta Ibra, akasita asijue kinachompata yeye na Ibra kilishampata
mpaka kuonekana muongo kwa kila alipokwenda kumchafulia Jackson Msindai, kwa
kuwa hakuwa na ushahidi!
Ijumaa hiyo ikawa chungu
kwa Phina. Amepoteza kazi ya ulaji, halafu uhamisho huko Lindi! “Hakika
siendi. Nani akakae kijijini!” Phina akakumbuka shule aliyonayo kichwani,
akajiambia hiyo, hakuna wakumnyang’anya. Atabanana nao hapohapo mjini asijue
jicho la mzee Msindai lipo naye kuhakikisha anamlipa ubaya kwa kumuanika kila
mahali akiwa anasindikizwa na Ibra, kisha Jena! Mzee Msindai alijimbia
atahakikisha kila anapoomba kazi hapo mjini, hapati, mpaka alipe ipasavyo.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati Phina akiomboleza
kupotelewa na mtoto, Sabrina yeye aliacha wake nyumbani na kutoka na kundi
lake. “Sasa hapo unawakilisha jina Msindai vizuri.” “Kweli wifi yangu?” “Mbona
ningeshakwambia! Si unanijua mimi?” Angalau Sabrina akacheka. “Na wewe
umependeza sana wifi yangu.” “Mwenzio kawaida yangu.” Sabrina alicheka mpaka
machozi, Jacinta kimya. “Wifi!” “Wewe sema ni lini umenikuta hovyo.” “Hata siku
moja.” Sabrina akamjibu. “Ndio ujue ni maamuzi tu. Sijiweki kihasara hasara
mimi! Kwa nini!?” “Nitabadilika wifi yangu.” “Na ubadilike kweli. Mjini hapa,
watu hawana kazi ila kuongea ndio ajira yao. Sasa wewe akili kichwani. Ukienda
saluni wamekutendeza kitu hakijakaa sawa akili mwako, waambie watoe hapohapo.
Usitoke ukiwa unajishuku.” “Wifi!” “Kwani ulikwenda kutengeneza udugu au
kutengenezwa upendeze?” “Nipendeze.” Sabrina akajibu na cheko. “Ndio hivyo.
Wasikutoe kituko.” Akaja Joy, amependeza haswa. Jacinta akaanza kucheka.
“Mumeo amekuona na hilo
gauni?” “Nimetoka hajarudi. Nikaona nijiwahi na gauni langu. Nililinunua gali, lakini
nimeshindwa kulivaa.” Joy akalalamika. “Sasa kwa nini hujawahi kulivaa gauni
zuri hivyo!?” Sabrina akauliza akiwa haelewi. “Si Junior huyo!” “Mumewe ana wivu
yule, usimuone vile. Halafu mkoloni.” Joy akaanza kucheka. “Hataki nivae nguo
za kubana, matako na hips vikachorwa hivi! Hataki.” Sabrina akaelewa maana hapo
hips zote na tako la Joy vilikuwa vikionekana. “Sasa na wewe Jacinta sio umuite
hapa, aje atulipie. Atanikuta na hili gauni, akasirike, usiku wa leo mume wangu
alale amenuna.” “Sasa wewe ulilivalia nini kama si kutaka kumuuudhi mumeo?”
“Sehemu yenyewe hii ya hadhi wifi yangu. Mtoko wenyewe kama hivi ni mpaka wifi
yangu uamue huko kichwani kwake, ndio tunatoka. Nikajiambia acha nipanie.”
Stori zikaanza. Akaja na Pendo. Vicheko vikaendelea hapo.
Mara simu ya Junior
ikaingia kwa Jacinta. “Huyu ukishatoka na mkewe, kazi yake ndio hii.” Jacinta
akaongea na kupokea. “Njoo Mheshiwa Msindai uje ulipe.”
“Mimi nilijua tu. Sasa kwa nini unamuita, mwache akapumzike bwana!” “Kapiga
mwenyewe. Njoo kaka yangu. Tule na kunywa vya mjini.”
Junior akaongezeka. “Mke wangu kapendeza!” Akamsifia. “Asante mpenzi wangu. Pole
na kazi.” “Jacinta, mpigie mzee Msindai mwambie naoa upya. Nataka mahari ingine
ya Joy!” Joy alicheka mpaka machozi. “Unanioa tena!” “Kabisa.” Jacinta
akampigia kweli baba yake.
“Baba mzazi,
inatakiwa mahari ingine ya Joy. Junior anataka umsindikize ukweni, ukamuolee
tena.” “Joy huyohuyo?”
Mzee Msindai akauliza. “Mwambie tena safari hii ajiandae zaidi, maana
ashanizalia watoto watatu.” Junior akajibu, Joy hana mbavu. “Mzee Msindai umesikia?” Jacinta akamuuliza baba yake.
“Acha nijikusanye tena, mama.” Mzee Msindai
akajibu. “Usikubali
mwaya baba yangu. Hawa wawili watakufilisi. Lala baba yangu mzazi. Kesho.”
Jacinta akakata simu, Junior akambusu mkewe. “Kama mzee Msindai ameishiwa, mimi
mwenyewe nitakulipia tena mahari ingine.” Akambusu tena, safari hii mdomoni
kabisa. “Hawa nao wanaboa!” “Acha wivu wifi yangu. Mapenzi kupendwa.” Stori
zikaanza, Sabrina hapo akapoa akimwangalia Joy na mumewe. Ungejua tu Junior
anampenda mkewe.
Walikaa hapo mpaka usiku
mwingi tu, Sabrina mawazo. Bado moyo ulikuwa hauna raha kila akikumbuka yupo
Phina na mtoto wake katikati ya ndoa yake. Aliweza kucheka kidogo, lakini
wakati wote akili zilimkumbusha Phina. “Hivi ndio itakuaje, jamani! Mtoto
akiumwa ndio Jack awe nao mpaka apone!” Hilo swali likaendelea kupita
kichwani mwake. Mwishoe akaaga.
~~~~~~~~~~~~~~
Pendo akamsindikiza mpaka garini. Wakaanzisha
kikao kingine. Sabrina akamsimulia kila kitu. “Nimechanganyikiwa dada, sijui
chakufanya!” “Bora wewe upo hapo na watoto nyumbani. Mwenzio niliachwa na
sikuwa na watoto. Lakini unakumbuka jinsi ulivyonibeba bila kuchoka?” “Sasahivi
ndio nakuelewa dada. Ila naona bora wewe ulikuwa angalau unapata muda wa kulia
unapunguza uchungu. Mwenzio sipumui sababu ya majukumu ya watoto. Usiku wa jana
angalau wifi alinisaidia. Akapanga ile timu yangu, ndio nikaweza kulala mpaka
asubuhi. Nimechoka dada! Zaidi nafsi. Sijui itakuaje! Sijui ndio ndoa yangu
itachukua sura gani! Hata sielewi! Jack anakuwa baba wa mtoto wa Phina pia.
Inamaana anahaki zote za umama kama mimi, na Jackson anatakiwa kuwajibika huko
kama huku kwangu! Haya watoto wote wakiugua kwa wakati mmoja, huyo Jack
anakwenda kwa yupi na yupi atabaki kupewa pole ya kwenye simu! Sijui itakuaje
dada! Nimeazima matatizo yote ya kesho, naishi nayo leo
kwa wasiwasi na siwezi kujisaidia.” “Pole Sabrina.” Pendo akaamua na yeye
amuazime masikio. Atoe la rohoni kama alivyomfanyia yeye wakati ameachwa na
Willy.
“Lakini nashukuru Jacinta
amekubali kupokea wanangu. Ameniambia hata nisipokuwepo hapa duniani, jicho
lake litakuwa na kwao pia. Hilo limenifariji na kuniondolea hofu.” “Mmmh!” Wakazungumza
hapo, Sabrina akaondoka kurudi kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Alifika kwake akamkuta
Jack sebuleni, akamsalimia na kupitiliza chumbani kwa Pina na mwenzie.
“Nimewaletea kuku choma. Wapo jikoni. Mkitaka mle kesho au…” Wote wakaruka
kitandani nusura wamuangushe mlangoni. “Kwani
hamjala usiku, nyinyi!? Mtaniangusha bure mnivunje.” “Kuku wa kuchoma
mpaka asubuhi dada na wewe! Kweli?” Pina akajibu akikimbilia jikoni. “Basi
mtaamsha watoto wote humu ndani!” “Tunakula kimya kimya.” Akajibu Pina akiwa
washafika jikoni na cheko limewajaa wote wawili. “Mfuko huo mwingine sio wenu.
Chakula cha baba.” Jack akasikia ila akashangaa yeye hajakaribishwa. Akatulia
tu.
‘Harusi ya
kesho ni ya familia nzima. Na bado sijapata majibu ya vipimo vyako.’ Ujumbe kutoka kwa baba
yake ukaingia. Jack akajua ndio anatakiwa kwenda na Sabrina. Akatulia akijua
baba yake anasubiria majibu. ‘Kwa kuwa bado sijaenda
kupima, baba. Nitaenda kesho asubuhi.’ Jack akarudisha hayo majibu.
Kimya. Akajua ameyapata. Na lazima kesho aende kupima. Akabaki ametulia kochini
akifikiria.
Wema Hauozi.
S |
abrina akaenda chumbani akatoka akiwa ameoga.
“Nilileta samaki wakuchoma kama vile unavyopenda na ndizi za kuchoma pia. Unataka
kula sasahivi au uwekewe utakula kesho?” “Asante kujali. Lakini naona nile tu
kesho. Usiku umeshakuwa mwingi.” Sabrina akaenda kuweka kwenye friji na kurudi chumbani
kwa watoto. Akataka kumuamsha Brandon anyonye lakini akaona amuache tu. Maziwa
yalishaanza kujaa tena. Hakuwa amenyonyesha kwa msaa mengi. Akachukua vifaa
vyake vya kukamulia, akahamia hapohapo chumbani kwa wanae akaanza kukamua.
Jack akamfuata. Alipoingia tu, akajifunika kwa
haraka. “Kumbe maziwa yameanza kutoka!” “Ndiyo.” Sabrina akajibu nakurudisha
mawazo kwenye kukamua huku amejifunika. Akashangaa Jack haondoki. “Wewe nenda
tu kalale chumbani. Mimi nitalala hapahapa ili akiamka usiku, nimuwahi kujaribu
kumnyonyesha kabla Pina hajampa maziwa mengine. Nataka aendelee na maziwa yangu.
Kwa hiyo nenda tu kalale kitandani, mimi nitakuwa hapa. Usilale kwenye makochi.
Si sawa.” Jack akaenda kukaa pale pembeni yake.
“Sabrina!” Akajaribu
kuita. “Wakati ule tupo chuoni, na ulipokuwa Moshi nilipokufuata, yale maneno
uliyoniambia, hayakuwa yakileta maana mpaka sasahivi!” Sabrina akamwangalia na
kukunja uso. “Nimeingiwa na hofu, Brina! Sina jinsi nikakwambia ukaelewa. Nina wakati
mbaya ambao sijawahi ishi kabla. Najisikia fedheha nashindwa hata kuangalia
ndugu zangu usoni. Nimeingiza kila mtu kwenye shida, Brina. Nimepatwa na ile
hali kama wewe. Moyo unapasuka kila wakati kama kumeangushwa chuma!” Sabrina
akatulia, akajua ndio anamkumbusha jinsi yeye alivyokuwa akimbeba kwenye shida.
“Nimekwama Brina. Sijui
nifanyaje! Dhambi yangu inanililia, nashindwa kutulia.” Jack akatulia kidogo,
Sabrina na yeye akatulia. “Najua kwa swala la mume kwa sasa itakua ngumu,
lakini naomba turudi kuwa marafiki wakubebana!” “Kwa hiyo leo ndio umekuja
kudai fadhila zako?” “Hapana Brina. Hata kidogo. Lakini nipo pabaya! Halafu
mbaya zaidi sina mtu. Nipo kama hivi.” “Na Phina?” “Sina mawasiliano naye na sidhani
kama tutakuja kuwasiliana tena.” “Mpaka ajifungue?” Sabrina akamuuliza kwa wivu.
“Baba ametoka kunitaarifu
kuwa ile mimba iliharibika leo.” Sabrina alishituka nusura amwage maziwa yote.
“Ni nini kilitokea!?” “Hata sijui! Ila baba ananiambi alionekana hospitalini
leo asubuhi akilia anaumwa na tumbo, na kuanza siku zake. Basi.” “Poleni sana.”
Sabrina akajikuta akitoa pole bila hila. Jack akanyamaza. Wakatulia kila mtu
akiwaza lake, Sabrina akakumbuka alikuwa akikamua, akaendelea mpaka akamaliza
bado Jack yupo hapohapo.
“Nenda kalale Jackson. Najua
upo kwenye maumivu ya kufiwa na mtoto wenu, lakini nenda kajaribu kupumzika.
Tena kitandani kabisa, sio kwenye makochi. Itakusaidia. Ile usiku wa jana mimi kulala
vile angalau imenisaidia kidogo. Kajaribu kupumzika pengine kesho utaamka na
akili ya kujua nini mfanye.” “Hakuna maisha kati yangu na Phina. Tafadhali
naomba uamini hatukuwa tumepanga kukutana.” “Si umesema ni bahati mbaya wewe!? Ndio
hiyohiyo bahati mbaya imewakutanisha tena huko Uswiz mpaka na mtoto juu! Sasa
unakataa nini?” “Sasa sasahivi nimtafute tena wa nini? Sikuwa nataka mahusiano
na Phina, Sabrina. Naomba nisamehe. Ilitokea…” “Kwa bahati mbaya.” “Basi mama.
Kama umekataa kunisaidia na mimi, basi Brina. Acha mimi niendelea kulipa garama
ya makosa yangu. Ila ingekuwa mimi nisingekuacha Brina. Japokuwa unakuwa
umeniumiza, lakini huwa sitaki uwe peke yako matatizoni.” Sabrina kimya.
Jack akanyanyuka, na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina akakaa pale
akaanza kuumwa na dhamira. Akakumbuka Jackson alivyombeba wakiwa chuoni.
Japokuwa alimuabisha, lakini akaweka tofauti zao pembeni akamsaidia. Akakumbuka
na kutulia. Kumbukumbu zikamjia jinsi alivyokuwa ameishiwa chuoni, Jack
huyohuyo akawa akihangaika naye mpaka kula yake. Akapoa. Kumbukumbu ikamrudisha
alipokuwa Moshi. Ile hofu aliyokuwa nayo mpaka Jack akaenda kumchukua na
kumsamehe akiwa mjamzito! Akatulia.
Mungu akamrudishia ile
furaha aliyokuwa nayo na kushindwa kuamini Jack kumuoa na ujauzito! Jinsi
alivyombeba na tumbo lake. Heshima aliyompa kwenye jamii kwa kumchumbia kwa
heshima na ujauzito wake. Ikaja harusi ya kifahari! Na Jack kubaki naye
hospitalini baada ya ndugu zake kuona amejifungua watoto wa kizungu. Sabrina
akatulia kidogo. Hasira zikaanza kushuka.
~~~~~~~~~~~~~~
Akatoka, akakuta taa ya
sebuleni imezimwa, akajua Jack amefuata ushauri wake. Ameenda kulala chumbani.
Akajishauri hapo! Ingekuwa sio kukumbushwa fadhila, angelala chumbani kwa
watoto. Lakini usiku huo Jack amerudi kukusanya malipo ya wema wake. Baada
ya muda Jack akamsikia ameingia hapo chumbani. Akajizungusha hapo wee, Jack
kimya akitaka kujua mwisho wake, ila akajua anajishauri. Akaingia chooni.
Akamsikia anaoga tena, wakati alishaoga. Akatulia kabisa, wala hakulala ili
amuone. Akatoka hapo akamuona anapaka lotion, hamalizi. Jack kimya wala
hakumsemesha.
~~~~~~~~~~~~~~
Alichokiunganisha Mungu, Mwanadamu Asikitenganishe.
Inaendelea..
0 Comments:
Post a Comment