Hilo juma zima, Tino
alikuwa akifanya hivyohivyo. Anakuja kuwachukua asubuhi, na kuwarudisha usiku
wakiwa wameshalishwa na kubadilishwa nguo. “Unavyojitahidi! Unawarudisha
wasafi!” “Ungemuonea huruma anti. Kuanzia nawapikia, nawasaidia kula na
kuwaogesha nakuwa naye kwenye video akinipa maelekezo. Mpaka kuzibrashi nywele
zao vizuri na kuzifunga hivyo ni yeye.” Sabrina akaangalia wanae na kucheka.
“Ila leo nimefanya mwenyewe bila msaada wake.” “Sawa. acha wakapumzike.”
Sabrina akaondoka.
Siku Ya
Sita.
T |
okea waachane na shemeji yake siku ile nyumbani
kwao, siku hiyo akaona simu ya shemeji yake inaingia. Akaiangalia kwa muda
akijishauri kama apokee au la, karibia ikatike akapokea. “Unaendeleaje na watoto Shem?” “Tunaendelea vizuri, namshukuru Mungu.” Sabrina akajibu lakini
Junior alisikia sio sauti aliyoizoea. Na yeye akaona ayafanye marefu kuwa
mafupi. “Sasa sitachukua muda wako mrefu. Mimi ni
mjumbe tu, baba ameitisha kikao kingine nyumbani. Leo usiku saa mbili. Ameomba
nikufikishie ujumbe.” “Mimi sidhani kama nitaweza kuhudhuria shem. Naona mimi
inatosha. Nyinyi endeleeni tu.” “Naomba usikatae wito shem. Waswahili wanasema
kataa maneno.” “Hayo maneno machungu ya huko kwenu ndio ninayokataa, shem.
Naishia kudhalilishwa bila sababu shemeji yangu. Acha tu nikae pembeni. Mama
Msindai hatazungumza lugha ingine nikaja kuelewa zaidi ya msisitizo kuwa
amenikataa. Na naona na kijana wake ndio kama hivyo. Jack ameanzisha familia
inayotambulika na kukubaliwa na mama yenu. Mimi nakuja huko kama nani?” Sabrina
akaongea taratibu tu.
“Ingekuwa ni
wakati ule Jack ni mume wangu, hapo sawa ningesema navumilia sababu ya mume
wangu. Lakini…” “Bado Jack ni mume wako. Mlioana ndoa takatifu ya kanisani.”
“Kanisani kule ni ndoa ya mke mmoja, mume mmoja. Siwezi ndoa za mitala, shem.
Nina watoto wadogo sana. Sasahivi nikijiingiza kwenye mapenzi ya kitajiri hayo anayoanzisha
Jack huko, hatujui huko kwa wapenzi wao wengine na wao wanaishije! Mwanamke
anayekubali kulala na mwanaume bila kinga, si inamaana analala na wengine
hivyohivyo bila kinga!”
Sabrina akaendelea taratibu tu.
“Shem, Jack
aliniacha hapa nina homa kali, inapanda haishuki. Natetemeka baridi,
nimeharibikiwa kidonda cha mshono wakujifungua, ameniachia watoto wadogo,
anakwenda kulala nje bila shida! Halafu akaficha. Alishindwa hata kukiri mpaka
Phina alipojitokeza, inamaana hiyo ndio tabia yake. Mwanamke wake
asingejitokeza, hakuna ambaye angejua, na angeendeleza tabia yake hiyo
anayotaka kuaminisha watu ni bahati mbaya. Hizo bahati mbaya zingeendelea tu
kutokea mpaka mnakuja kushitukia tunakufa kwa maradhi! Hapana shem. Nilimpenda
Jack, lakini si kwa kuja kuniua. Hata bibilia inaniunga mkono, jamani! Kosa la
uzinzi! Hilo naruhusiwa kutoka kwenye hii ndoa.”
“Halafu mama
yake hanitaki mimi na watoto niliozaa! Wanatangaza kumpokea Phina na mtoto wake
mpaka huko mitandaoni, mimi wamenikataa kabisa! Nimegeuka mimi kichekesho!
Wamechagua kuniumiza bila sababu, shem! Hapana shemeji yangu. Acha itoshe hivyo.
Kwa nini niendelee kujitesa jamani! Acha tu Jack aendelee na maisha yake yenye
mafanikio na mwanamke wake. Mimi inatosha.” Junior kimya akisikiliza.
“Hata hivyo,
mwambie baba, sisi kesho tunakwenda Singida. Najiandaa usiku wa leo kwa safari
ya kesho na watoto.” “Kwema?” “Nahisi kutakuwa kwema mimi mwenyewe nikienda
huko. Ni mambo ya biashara tu.” “Mimi nimekusikia Sabrina. Pole sana.” “Nashukuru
shem. Muwe na usiku mwema.” Junior akajua ndio anaambiwa anakata simu. “Basi nitamfikishia baba ujumbe. Uwe na safari njema kesho.”
“Nashukuru.” Sabrina akakata simu.
Mzee
Msindai!
Sabrina akiwa chumbani
kwake, akasikia sauti ya mzee Msindai akizungumza na watoto sebuleni kwake. Alishituka
karibu aruke kitandani. Akaangalia saa ya ukutani, akagundua ni saa tatu usiku.
Akavaa kwa haraka na kutoka. “Karibu
baba.” “Asante. Vipi unaendeleaje?” “Tunaendelea vizuri kabisa. Wote hatujambo.
Ila kesho alfajiri tunasafiri.” “Nimeona masanduku yapo mpaka mlangoni!”
Sabrina akanyamaza. “Mwambie dada achukue watoto tuzungumze.” Phina akakusanya
jeshi lote la Sabrina akawapeleka chumbani, Sabrina mapigo ya moyo yakienda
kasi. Amefuatwa na mzee Msindai!
Akakaa kochi la pembeni
ya mkwe wake. “Junior alikupigia simu kukwambia kuna kikao. Tumekusanyika pale
nyumbani, hukutokea, ndio maana nimekuja mimi.” “Samahani baba. Ila nilimwambia
shemeji sitaweza kufika.” “Ndio maana
nipo hapa.” Sabrina akatulia macho chini. “Siku ile ya kutolewa mahari yako
nyumbani kwenu, unakumbuka kuniona mimi?” “Nakumbuka baba.” Sabrina akaanza
kulia na hofu. “Unakumbuka maneno niliyosema?” Sabrina akaanza kufikiria.
“Nilisema nimekuja kuoa kule kwenu. Nilimuolea Jackson mke. Ile mahari ni jasho
langu mimi wala si Jackson. Niliwasindikiza mpaka kanisani. Nikaona baraka mlizopewa
kama mke na mume. Leo unapoitwa mama Msindai, si kwa kukubali kwa Jack. Ni kwa
kuwa mimi nilishakuchunguza hata kabla Jackson hajakutamka nyumbani.” Sabrina
akashangaa kidogo.
“Siwezi nikakubali kila
mtu akaitwa Msindai. Lasivyo kungekuwa na Msindai wengi tu. Lakini wanaotokana
na Msindai mimi, MIMI mwenyewe ndiye ninayechagua. Ndio maana niliposikia
habari za Tino akisumbua, sikutaka kuwa nikipewa taarifa, mimi mwenyewe
nilikuwa mstari wa mbele, ili utulie na ubaki umetulia kama mama Msindai.”
Sabrina kimya.
“Kwa umri wangu huu,
mpaka sasa, sijawahi kuita mtu, akakataa wito wangu kwa sababu mimi kama
mimi huwa sitoi sababu ya mtu kunikatalia jambo. Unanielewa Sabrina?”
Mikono ikaanza kumtetemeka Sabrina akifuta machozi. “Samahani sana baba.”
“Basi. Kila mtu yupo nyumbani, nimewaambia mtu asiondoke, na kikao hakitaanza,
mpaka wewe uwepo.” “Tunaweza kwenda sasahivi. Ila
naomba nibebe huyu mtoto mdogo kwa kuwa sina maziwa. Na siwezi kukamua, maziwa
yananikauka.” Sabrina akaongea kwa sauti ya chini. Basi mbebe na Pina,
ili akusaidie kumshika wakati wamazungumzo. Nitakutaka wewe pale muda wote.” “Sawa baba. Na samahani sana.” “Hilo limekwisha.
Na leo mimi ndio nitakuwa dereva wako.” Sabrina akacheka kwa wasiwasi na kwenda
kukusanya vitu na kubeba mtoto wake na Pina. Wakatoka.
Jungu
Kubwa, Na Ukoko Wake.
S |
abrina alifika hapo akakuta pako kimya. Kila mtu
yupo mpaka Jack! “Lete nikupokee mtoto.” Jack akamuwahi alipoingia na mwanae
mkononi. “Acha nikamlaze maana akiamka hapa, atataka maziwa na mimi sina, ndio
nimetoka kumnyonyesha, ameyamaliza yote mpaka yajae tena, itachukua muda ndio
maana nataka tusimsumbue, akiamka akutane na maziwa.” “Umekonda sana Sabrina!
Unakula wewe?” “Nakula wifi yangu.” “Mmmh! Huo mwili hauwezi kutoa maziwa.
Umekauka sana. Kazana kula, au sasa mwanzishie huyo maziwa mengine.” “Mwanangu bado mdogo wifi. Najitahidi naye hivyohivyo nimsogeze
kidogo.” Sabrina akajifuta machozi. “Basi hataacha kukulia. Ni aidha
wewe ubadilike, uanze kutoa maziwa, au umuanzishie maziwa. Huna jinsi ingine.” Sabrina
akamwangalia mwanae vile alivyolala.
“Naomba nikamlaze hapo
chumbani kwa dada, nakuja sasahivi.” “Kwa nini ukamlaze huko na vyumba vimejaa
hapa ndani!” Mzee Msindai mwenyewe akamuita msichana wa kazi na kumtaka
amwandalie huyo mtoto chumba. Sabrina akashukuru na kumfuata msichana wa kazi.
Kimya. Mama Msindai kama hayupo hapo.
Baada ya muda Sabrina
akarudi na kwenda kukaa pembeni ya Jacinta. “Samahani kuwaweka muda mrefu.”
“Usijali. Hiki kikao ililazimu uwepo hapa ndio maana unaona mpaka Joy yupo
hapa.” Akaanza Mzee Msindai.
Wamjua
Msindai Mwenyewe.
“Wote mliokaa hapa ndani,
ni kina Mzindai kwa kuwa MIMI Msindai niliruhusu muwe kina Msindai.” Mama
Msindai akamwangalia na nyusi akapandisha juu. “Wengine kwa kuolewa na
wengine kwa kuzaliwa. Jinsi nilivyoenda
kukuposa wewe Sabrina, ndivyo nilivyofanya hivyohivyo kwa Joyce. Na Joy
amefanyika binti yangu tokea siku ile, na ndivyo ilivyo hata kwako wewe
Sabrina. Kitu ambacho nyinyi hamjui, nilimjua Sabrina na kumchunguza hata kabla
Jackson hajaja kumtambulisha hapa nyumbani.” Wote wakamtizama.
“Ilikuwa hivyohivyo kwa
Joy. Na ninafanya makusudi kabisa kwa sababu sitaki aina nyingine za
Msindai kwenye hii familia isipokuwa nyinyi. Jackson na Junior mnanielewa?” Wote
wakaitika kuwa wameelewa.
“Jena!” Jacinta akafurahi sana akajua
usiku huo atakipata. “HURUHUSIWI. Huna ruhusa,
wala mamlaka yakukaribisha mtu yeyote kwenye hii familia bila idhini
yangu. Unanielewa?” Kimya. “Jena?” Akamuita kwa ukali. “Wewe ni Jena Msindai
mpaka sasa kwa kuchagua kwako vinginevyo ungekuwa mtu mwingine kwenye familia
ingine. Acha ndoa za kaka zako.” “Msindai..” “Ninaongea mama J. Tafadhali
nisiingiliwe.” Jacinta akatamani kupiga vigelegele.
“Kitendo cha kuwa
mtandaoni, ukimkaribisha Phina kwenye hii familia, bila idhini yangu, UMEKOSA sana.
Umeingiza hii familia aibu na wote sisi umetufanya tuonekane tumekubaliana na
maisha ya kinyama aliyoamua kuishi Jackson.” Jack akainama. “Hata Jackson
mwenyewe, HARUHUSIWI
kukaribisha
mtoto yeyote kwenye familia yangu, kama hajatokana na Sabrina, tena ndani ya
ndoa yako. Mtoto yeyote utakayezaa nje ya Sabrina, niliyekwenda mimi kukuolea, tafuta
jina na ukoo wakumtambulisha, lakini kwa Msindai mimi, NIMEMKATAA. Unanisikia
Jackson?” “Ndiyo baba.” “Unanisikia Jena?” Kimya.
“Katika hili sina utani
Jena. Nataka nikusikie. Kama hutanisikia, nitakutaka uondoke hapa ndani, wewe
si mmoja wa Msindai anayetokana na mimi.” “Msindai unakwenda mbali.”
“Hujanielewa mama J. Mimi ndiye Msindai, nachagua nani anaingia kwenye hii
familia na si vinginevyo. Anayeshindwa, anaruhusiwa kuondoka, ila ujue Jena, nitakupokonya
majina yangu yote. Ukitoka kwenye huo mlango bila kunitii, ujue huna cheti hata
chakuzaliwa chenye jina la Jena Msindai.” “Msindai!” Mama Msindai akashangaa
sana. “Kama huamini, mwambie Jena atoke kwenye huo mlango sasahivi. Nimenyamaza
lakini naona mnataka kuharibia kila mtu!” Mzee Msindai akaendelea kugomba.
“Wewe Jena hujui hata
maisha ya ndoa ni nini, upo mitandaoni unashangilia uchafu huo?” “Na
nilimuonya. Muulize mama, mpaka mimi nikampiga hapa. Nikamwambia aache
kumuadhibu mke wangu kwa makosa yangu. Sasa mimi namjua Jena. Alichokifanya
mtandaoni, ni kunikomoa mimi, makusudi tu.” “Umedhalilisha familia
nzima! Simama Jena.” Baba yake akarudia, safari hii kwa amri zaidi mpaka Jena
akasimama. “Umenielewa au unaondoka?” “Nimeelewa.” Jena akajibu.
Jena akaanza kusomewa
hukumu yake.
“Kuanzia leo, huruhusiwi kuwa na akaunti yeyote ile ya social media. Na
akaunti uliyokuwa nayo Istagram
imefungwa. Huruhusiwi kuchangia chochote mitandaoni.” “Baba J, hapo
umezidisha.” “Hakika katika hili sina utani na sitabadilika. Akishindwa yupo
huru akawe kingine lakini si mmoja wetu. Siku atakapomtangaza mwanamke
mwingine yeyote, popote pale, bila idhini yangu, mbali na Joyce na Sabrina, nitakuadhibu
vibaya sana.” Jacinta alitamani asimame ashangilie.
“Labda uwe kwa jina
jingine si Msindai. Umenielewa Jena?” “Ndiyo.” “Na uwe na adabu kwa wake za
Msindai, sisi wote sasahivi tunaonekana ni wanaume tusiojua majukumu! Yaani
sisi wanaume watatu hapa ndio tumegeuka gumzo huko mitandaoni! Hapana Jena.
Usiwahi kurudia. Ukiona wifi zako wapo sehemu ambayo huwezi kuwa nao pamoja,
usifike. Na wewe hatutakulazimisha ufike. Natangaza ramsi, leo tunakuruhusu
kutokuwepo katikati yetu. Ukijisikia kuja, basi uje na adabu zako zote.
Ukishindwa, usifike. Kaa kwako. Unanielewa Jena?” “Ndiyo.” “Rudi kukaa.”
Akakaa.
Mzee Msindai akaendelea. “Swala
la watoto.” Jacinta akamtizama Junior. Junior kimya japo alimuona dada yake.
“Narudia tena. Mtoto yeyote, aliyezaliwa ndani ya ndoa ya Msindai, ni Msindai.
Awe wa kijani, bluu, njano, rangi yeyote ile ni Msindai. Unanielewa Sabrina?”
Wakajua zamu yake na yeye imefika.
“Ndiyo baba.” “Watoto
uliozaa ndani ya ndoa ukiwa Msindai, mimi nikalipa mahari kwa jasho langu bila
kusaidiwa na mtu hata shilingi, watabakia Msindai. Hilo hata Tino
nimemwambia.” Sabrina alishituka mpaka mate yakapita kwenye njia ya hewa. Akapaliwa
na kuanza kukohoa mfululizo. Jacinta akaenda kumletea maji. Akanywa
wakimsubiria mpaka akatulia. “Pole.” Jack akarushia pole yake. “Asante.”
“Nimezungumza naye na nimemuonya vikali sana. Nimemwambia, siku atakayothubutu
kuwabadilisha wajukuu zangu majina, hata kwa kuongeza herufi yake kwenye majina
yao, nimemwambia nitamuadhibu vibaya sana. Na nikamwambia hakuna
atakapojificha akataja jina la Msindai hata kwa kunong’ona, nisisikie kama
alivyofanya leo. Popote hilo jina linapotajwa kwa hila, linagusa
antena zangu, na ninasikia.” Sabrina kimya.
“Unanielewa Sabrina?”
“Ndiyo baba.” “Jamani, msichanganywe na rangi ya wale watoto. Hata Tino
nimemwambia hili. Wale watoto nilibeba mimi mwenyewe wakiwa hata hawajafikisha masaa
24 hapa duniani! Niliwabeba mimi kwa mikono yangu, nikawakaribisha kwenye hii
familia. Hakuna atakayenipokonya.” Sabrina akaanza kulia tena taratibu.
“Kama alivyo mrithi
Claire kwenye hii familia, ndivyo alivyo Jeiline na Keiline. Na Tino
nimemwambia. Atakachorithi mtoto wa Joyce kutoka kwenye mali zangu, ndicho
atakachorithi mtoto wa Sabrina. Hiyo nawaambia mimi nikiwa hai. Unanisikia
Junior.” “Ndiyo baba.” “Jeiline na Keiline, hawatabadilishwa majina yao ya
mwisho, hata kwa idhini ya Sabrina mama yao mwenyewe, mpaka watakapoolewa, au
watakapofika umri wa kuwa wakubwa, wakaamua wenyewe. Hapo hatutakuwa na
upinzani. Lakini si sasahivi. Ni kina Msindai. Unanisikia Junior?” “Ndiyo
baba.”
“Yanayoendelea mkiwa
hapa, ndani ya nyumba hii, sina mamlaka nayo kwa kuwa ni kwa mama yenu.
Lakini haibadilishi uhalisia wa mambo.” Jacinta akajua zamu ya mama yao lakini
yeye anaambiwa kiutuuzima. “Wote mliokuwepo hapa ni kina Msindai. Na kina
Msindai, tuna nia mamoja. Tunaweza kuwa na mapungufu yetu, lakini linapofika
swala la kupigana nje, tunasimama pamoja mpaka Jackson alipoleta utaratibu wake
mwingine.” Wakajua zamu ya Jack.
“Nimemuonya, na
ninarudia kumuonya. Maisha anayotaka kuyaishi nikiwa hai, hataruhusiwa
kuyaishi. Unanisikia Jackson?” “Nimeelewa baba.” “Uelewe na usiwahi kusahau.
Labda na wewe ubadilishe, usiwe Msindai. Nitakufuta kila mahali na hutakaa
ukawa hata na cheti cha darasa la saba. Mpaka chakuzaliwa nitachukua, kwa kuwa
ni mali yangu. Itabidi uanze upya, ukiwa na jina jingine. Kuanzia leo.” Hukumu
yake ikaanza. “Utapewa namba mpya ambayo kwa muda mpaka mambo yatakapokuwa
sawa, hutampa mtu mwingine yeyote zaidi marafiki zako. Itabakia nyumbani na
kazini. Ujue itakuwa ikifuatiliwa. Safari za kikazi ambazo si lazima wewe uende,
tutakuombea ruhusa ubaki ukifanya majuku yako hapahapa nchini, kwa muda mpaka
mambo yako yakae sawa. Rudi nyumbani baada ya kazi. Unanielewa Jackson?” “Ndiyo
baba.” Jackson akaitika kwa haraka kwa unyenyekevu.
“Kwa wengine wote, nimeeleweka?” “Tunaruhusiwa
maswali?” Akauliza mama Msindai. “Kwa nini hili langu halijajibiwa kwanza?” Kila
mtu akamshangaa mzee Msindai. Alimbadilikia kila mtu mpaka mkewe. “Eeeh!
Msindai vipi leo!?” “Nauliza, katika niliyozungumza mimi, nimeeleweka?” Akaweka
msisitizo. “Mimi nimeelewa baba.” Jacinta akajibu. “Na
mimi nimeelewa baba, na naomba msamaha. Naahidi nitaongeza umakini.”
Akaongea Sabrina na machozi kibao. “Hilo ndilo nilitaka kulisikia kutoka kwako.
Jua unalea watoto uliozaa wewe, lakini si wako peke yako. Huwezi kufanya
kile unachotaka! Hapana Sabrina.” “Nimeelewa baba.”
“Kama ni hivyo nashukuru.”
“Na mimi nimekuelewa
baba. Kina Msindai wengine tutakao pokea kwenye hii familia ni kutoka kwa kina
CJ, Cleiton, Brayan na Brandon.” “Naona hapo nimeacha maagizo yangu sehemu
sahihi. Na ibaki hivyo.” “Sawa baba.” Junior akaitika. “Mmmh!” Mama
Msindai akasikika akiguna. Hakuna aliyemwangalia.
“Namalizia juu ya Phina.” Mzee Msindai akaendelea
na hukumu ya Phina. Kila mtu akataka kujua. “Jackson na wengine wote. Mimi
nikiwa hai na nikiwa nimekufa, Phina haruhusiwi kukanyaga hapa.” “Heee!” Mama
Msindai akashituka sana. “Hana adabu. Hana maadili, hawezi kuwa mmoja wetu. Ni
mwizi asiye na aibu. Ameitia familia yangu aibu na kunifedhehesha vibaya sana. Amenichafua
kila mahali na yupo mtandaoni akijisifia uovu wake kwa ndoa ya mwenzie!
Sitamtaka hapa kwangu na popote nilipo mimi. Siku nitakayokusikia umerudi
kulala na yule mwanamke, usiwahi kurudi hapa Jackson. Nitakuweka mbali kama
nitakavyomuweka mbali Phina.” Hapo kila mtu akaingiwa hofu. Nitahakikisha
hakuna atakayemsikia tena. Kama vile jina la Msindai lilivyomuinua juu, ndivyo
litakavyomshusha chini. Unanielewa Jackson?”
“Nimeelewa baba na naomba
msamaha kwako na wote. Najua nimewaingiza aibu na kuifikisha familia hapa
tulipo. Nimekosa baba. Naahidi haitakaa ikatokea tena.” Kimya. “Nimekosa baba.
Najutia kosa langu, ni hivyo siwezi kurudisha siku nyuma nikarekebisha.
Nimekosa baba yangu. Sio kitu hata kilikuwa kichwani kwangu kwamba nilikuwa
nikipanga. Hata na mimi sijui ilikuwaje, naahidi kuongeza…” Brandon akaanza
kulia kwa ukali. Akalia tena na tena mpaka baba yake akashindwa kuzungumza.
“Baba, naomba mimi nikamchukue.” “Sabrina, huyo mtoto hashibi. Kilio hicho si
chakutoka usingizini. Mtoto huyo ananjaa. Unanisikia?” Jacinta akamuuliza kwa
msisitizo.
“Najitahidi kunyonyesha.”
“Sidhani kama kwa sasa unamaziwa yakumtosha huyo mtoto. Lazima kumuongezea
chakula wakati wewe ukirudisha mwili. Au ukubali tu kuwa alivyonyonya Brayan si
Brandon, basi aanze kupewa maziwa mengine. Au baba wewe unasemaje?” Jacinta
akamuuliza baba yake kama mtaalamu wa watoto. “Kwa hivyo alivyo mpaka aje
arudishe maziwa yakumshibisha huyo mtoto, itakuwa muda mrefu na mtoto
ataendelea kuteseka. Nenda kamtulize kwanza.” Sabrina akaenda.
“Ona ulipomfikisha mkeo!
Sabrina alipendeza na mwenyewe anaasili ya maziwa mengi kwa wanae. Uchafu wako
unatesa mpaka watoto wako! Wewe unaacha mkeo anakuwa kichekesho mitandaoni kwa
kushindwa kuwa mwanaume kama Junior! Mchafu, unalala hovyo, unajaza wanawake
wajawazito mitandaoni!” “Huyu mtoto ameomba msamaha jamani!” “Hapana mama. Acha
kumtetea Jackson. Amekosa SANA. Na kama si baba kutaka kuzungumza leo hapa na
Jena, hakika nilipanga kumfuata nyumbani kwake nikazungumze naye.” Junior
akaendelea. “Jena, angalia maneno ya kinywa chako tafadhali. Acha chuki
kwa wake zetu. Hawaishi na wewe, ni nini kinakusumbua wewe?” “Kwani..”
“Ukinijibu tu, leo mimi nitakupiga.” Mpaka Joy akashituka. Junior
alibadilika kama baba yake.
“Umekosa adabu kabisa
wewe! Unatangaza mtoto wa uzinzi mitandaoni wakati wewe umeshindwa hata kutunza
mwanaume hata mmoja?” Jena akaanza kulia. “Junior unapitiliza!” “Hapana mama.
Huyu ndiye amefikisha familia hapa. Amemtia hofu Sabrina, mpaka akaanza kuwatafutia
watoto wake baba, akihangaika usiku magerezani!” “Mbona
hamumsemi mama yeye aliyesema huyo mtoto anatakiwa kutambuliwa hapa na
akaribishwe kama Msindai?” “Jena acha mdomo wewe.” “Mimi nilifanya kutokana na alivyosema mama. Nikamtafuta
Phina na kuzungumza naye kutokana na alivyosema mama, lakini sasahivi mimi ndio
naonekana mbaya.” “Mbaya sana wewe Jena.” Jack na Jacinta wakamchangia.
“Mnafiki tu. Ulienda
kumtafuta Phina ukitaka kunilipiza kisasi sababu nilikupiga.” “Mbali ya hivyo,
amekakaa tu kuvunja ndoa za wenzie!
Mdomomdomo tu.” “Mdomomdomo gani na wewe Jacinta
kama si..” “Sasa leo umeonywa. Na UBADILIKE. Badilika kabisa, wake za
wenzio wapumzike. Tukienda kuoa majumbani kwao tunakuwa wema, wakishaingia tu
humu ndani ndio tunageuka mwiba! Acheni watoto wawatu watulie makwao jamani!
Acha kuunganisha waume zao na wanawake wengine. Junior kashamuoa Joy, mwach...”
“Kwani mimi nimemuunganisha Junior na nani?” “Jack! Jack ndiye anayekuuma mpaka
unashangaza hata mashoga zako! Acha kujidhalilisha Jena. Wewe mtu mzima, tulia.
Ni hilo tu mimi nilitaka kukwambia. Kakae ufikiri.” “Sina muda wa kipuuzi.”
“Hakika nakushauri utulie na utafakari Jena. Umevuka mpaka ambao huna nafasi
nyingine ya kukosea.” Baba yake akaweka msisitizo, wakanyamaza.
Sabrina akatoka na mtoto.
“Vipi?” “Kweli naona nikamuanzishie tu maziwa mengine. Hajapata kitu,
amejibembeleza tu na nyonyo amelala, hana muda mrefu ataamka tena.” “Hapa sisi
tumemaliza mama. Naweza kukurudisha nyumbani.” “Naona nitakusumbua baba. Acha
nimuombe mnyonge wangu.” Jacinta akacheka na kutingisha kichwa. “Mimi naweza
kurudi nao nyumbani.” “Nataka kuzungumza na wifi. Wewe endelea tu na ratiba
zako.” Sabrina akamkatalia mumewe. “Nisindikize wifi yangu najua na wewe
natakiwa kukupa maelezo.” “Haya twende.” “Pina beba vitu turudi nyumbani.” Akatulia
kidogo, kisha akasema.
“Mimi nashukuru kwa kila
kitu. Asante baba. Asante kunisamehe. Ila nilitaka kuwaaga rasmi. Sisi kesho
asubuhi tunaondoka, tunarudi Singida.
Tutakuwa huko nikiendelea kufanya biashara zangu. Hapa mjini naona sitapaweza.”
Wote kimya. Sabrina akamgeukia mzee Msindai. “Naomba kukuuliza swali baba yangu.”
“Karibu.” “Naomba iwe hapo nje.” Mzee Msindai akasimama wakati anataka kutoka, mkewe
akaanza kulalamika macho kwenye simu.
Na mama Msindai hakuachwa
salama. “Mbona simu zangu zote hazifanyi kazi!?” “Eneo zima la kuzunguka huu
uzio, hapatakuwa na mawasiliano ya simu pamoja na internet.” “HAPANA Msindai!
Haiwezekani uniadhibu mimi kama mtoto mdogo!” “Kwa hiyo hakuna simu
itakayoweza kufanya kazi mara unapoingia pale getini, isipokuwa yangu na
Jacinta tu kama na yeye atatumia ya kazini.” Akamalizia mzee Msindai. “Hakika
huwezi kunifanyia hivyo.” “Nashauri utulie mpaka nitakaporekebisha hii hali. Kila
mahali kumechafuka. Hatuwezi kuzuia haya madhara kama wote humu ndani tukiwa
wasemaji. Naomba mpaka nitakaporekebisha madhara aliyoyasababisha Jackson, mimi
peke yangu ndio nibakie msemaji wa hii familia. Na Junior, endapo nitamtuma
mimi.”
“Unanivunjia heshima
Msindai!” “Ukitulia, utakuja kugundua nipo kwenye kutengeneza, na simu zako na
marafiki zako zinanishika miguu. Kwa kuwa wapo kukuchota maneno na kuyasambaza.”
“Hapana Msindai! Mimi ni mtu mzima, najua nini chakuzungumza na nini chakuto….”
“Unakumbuka majibu yako ya kwanza kabisa kwenye simu ya mtu aliyekupigia
kukutaarifu habari za mwanao huyo, alizozisikia kutoka kwa Ibra na Phina huko Ustawi
wa Jamii?” Mama Msindai akatulia kidogo akijaribu kuvuta kumbukumbu. Wote
kimya.
“Mwanamke wa kwanza
kabisa aliyekupigia simu akikwambia anataka kukusaidia kama mzazi akitaka
kuzuia mambo yasiende mbali. Unamkumbuka?” “Mbona nilimjibu vizuri tu!?” “Kama
ulimjibu vizuri ni kwa nini mama Mkapa na yeye alikupigia akikushauri mmalize
mambo kinyumbani? Hilo moja, pili, umeshajiuliza yeye mama Mkapa aliyajua wapi
hayo kwa muda mfupi vile? Na kama aliyemwambia alikuwakilisha vizuri kwake, kwa
nini akupigie na kukusisitiza umalize mambo kinyumbani?” Mama Msindai akakunja
uso.
“Naomba tumalize haya
mazungumzo baadaye, ili mimi nikaongee na Sabrina, akawahi kumpa mtoto
chakula.” “Kwa hiyo nikitaka kuzungumza na simu zangu inabidi nitoke hapa?” Hukumu
ingine kwa mama Msindai. “Utachukua likizo kwa muda, utulie humu
ndani.” “Hakika huwezi kunifungia humu ndani Msindai, eti kwa sababu ya makosa
ya Jackson! Sitakubali.” “Tayari kuna ulinzi getini. Siruhusu mgeni
yeyote humu ndani wala mtu kutoka mpaka nitakapoweka mambo sawa huko
mtandaoni.” Mzee Msindai akatoka nje.
“Hakika baba yenu hawezi
kunifanyia hivi mimi! Hawezi kunifungia mimi humu ndani! Junior, nenda
kazungumze na baba yako. Mwambie..” “Kabla hujaanza kutishia mama, jua baba
amesikilizishwa majibu yako yote ulipozungumza na yule mwanamke aliyekupigia
simu. Na baada ya kuachana na wewe, alipompigia mama Mkapa pia baba
amesikilizishwa mazungumzo yao. Yule mama hakusemi vizuri. Anasema unamtetea
kijana wako kwa tabia zake chafu. Anasema hukujali swala la kwa nini amelala
nje ya ndoa, bali ulionyesha unalalamikia kusingiziwa kwake mimba na mengine
mengi. Ni mbaya mama!”
“Na mbaya zaidi ni kama
mkalithibitisha hilo kwa kuongeza swala la Phina. Jena ameenda kukuwakilisha
kwa Phina pia.” “Acha kunisingizia Jacinta.” “Wewe unafikiri ni kwa nini baba
amekasirika? Huyo shoga yako Phina, anatangaza amepokelewa na mama yake Jack na
wifi yake. Na wewe umemwambia mama atamfanyia babyshower. Pinga nikamuite
baba.” “Lakini ndivyo mama alivyosema! Mimi nilizungumza na Phina mambo yote
aliyoongea mama.” “Mnafiki mkubwa wewe na mbea! Hata kama nilisema, nani
alikutuma ukaongee mambo ya ndani, huko nje!?” “Ulisema Phina ameshakuwa mmoja
wa familia. Hata kama wamekasirika, lakini Phina amembeba Msindai, na ni
mtoto wa humu ndani. Wewe utampokea kwa baraka zote na utamkaribisha. Ulisema
hutamtupa huyo mjukuu. Bisha mama.” Wakaanza kubishana hao wawili wakijua
wameshakamatwa. Jack kimya ameinamia magoti, kichwa chini.
Sabrina alipoona
hawamalizi, akamuita msichana wake. “Pina tangulia kwenye gari ya anti Jacinta.
Nakuja, sisi tuondoke.” “Nipe vitu vyenu nitangulie navyo kwenye gari. Mimi
mwenyewe natoka hapa. Sitaki kusikiliza ujinga huu.” Jacinta akachukua kibegi
cha mtoto mkononi kwa Pina aliyekuwa amebeba mtoto na begi. Wakatoka. “Usiku
mwema jamani.” Sabrina akaaga nakutoka. Joy akabaki ameinama, hakuzungumza neno
hata moja tokea anaingia hapo. “Twende Joy.” Junior naye akaondoka na mkewe.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina akamfuta mzee
Msindai mpaka alipokuwa amesimama. “Nimeshajichanganya baba yangu, hata sijui
nitafanya nini!” “Juu ya nini?” “Hiki ulichokuwa umekizungumza leo, natamani
kama ningekisikia muda mrefu. Niliingiwa na hofu juu ya hatima ya binti zangu,
ikabidi kuomba au nisema kudai Tino atolewe, ili angalau awepo ikitokea nakuja
kufa kwa maradhi basi yeye awepo kulea watoto ambao nilijua hapa wamekataliwa.
Tino alipotolewa, nikamrudishia watoto na baraka kwamba, hata hivi anavyotaka
kuondoka, anaweza kwenda nao, ila awarudishe baada ya juma moja. Tukakubaliana
hivyo. Sasa sasahivi nitafanyaje?” “Kabla sijakujibu swali lako, naweza
kukuuliza swali na naomba uwe muwazi tu.” “Sawa.” Sabrina akakubali akiwa na
wasiwasi. Huyo mzee alibadilika usiku huo akawa Mafia wakutisha.
Alitembeza hukumu hapo, kila mtoto akabaki kupokea hukumu yake mpaka kumshangaza
Sabrina, hiyo mamlaka kubwa hivyo anapata wapi! Alidhani
“Bado unataka ndoa na
Jackson?” Hapo Sabrina akaanza kulia tena. Mzee Msindai akabaki kimya akimsubiria
amalize, ampe jibu lake.
“Wewe unataka nini?”
“Nimezungumza sana na Tino, na naona ameongeza adabu. Ameahidi kufanya
nitakachomwambia. Naomba safari hii achukue watoto, atawarudisha.” Akamuona
mzee Msindai anafikiria. “Nitakwambia habari zitakazokushitua na kukuumiza
kidogo.” Sabrina akatulia akimwangalia. “Nimemuondoa Tino hapa nchini.” Sabrina
alishituka sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment