Jack akatumia akili ya
haraka kumjibu maana alishatoka kwenye mapenzi akimbembeleza, akaanza jazba. Akajua
hatima yake nzuri inategemeana na huyo Phina. Akitulia, patatulia.
“Nisikilize Phina.
Huyo mtoto awe ni wangu au asiwe wangu, cha muhimu ni usalama wake. Hichi
anachokwambia Ibra mfanye, mimi sitakataa, ila si salama kwa mtoto. Kwa kuwa
mimi nililala na wewe, na umesema mimi ni muhusika, kwa sasa nakubali
kuwajibika kwa vile utakavyotaka wewe, ila tafadhali kuwa muungwana kama
Sabrina alivyokuwa muungwana kwako wakati tupo wote kule chuoni. Sabrina
alikuheshimu sana akijua nipo na wewe kwenye mahusiano.” Jack akasikika
kusihi.
“Naomba hilo
tulifanye kuwa kila ukitoka kliniki unachoambiwa juu ya mtoto, basi uwe
unanijulisha. Na ikitokea unaugua, unahitaji msaada, nijulishe. Hii simu
sitafunga tena.”
Hapo akamgusa Phina. “Nashukuru Jack. Na ninakuahidi
nitazungumza na Ibra na nitahakikisha anafuta picha zote. Na mida ya saa nne
nitatoka kazini kwenda Ustawi wa Jamii kufuta kila kitu.” “Utahakikisha vipi
kama Ibra amefuta picha?” “Acha nifikirie. Maana bila mipango yakueleweka,
anaweza kunigeuka, akakataa na kuamua kutumia zile picha vile anavyotaka yeye.”
“Na huo ndio wasiwasi wangu, kama hatujachelewa.” “Naamini hilo nitalimaliza.”
“Nafikiri na mimi ninahaja ya kukutana naye, tukazungumza. Nafikiria hivi.”
Jack akapata wazo.
“Safari hii usimfuate
peke yako ila usimwambie. Muombe mkutane naye sehemu. Kisha mimi na wewe twende
wote. Usigusie swala la kutotaka kuendeleza mikakati yake, wala swala la picha
mpaka tutakapokutana naye pamoja.” Hapo Phina alishakuwa mama watoto wa Jack, akaona
anajaliwa na Jack, hakuna atakachoambiwa na Jack akakataa. Anataka mahusiano na
baba mtoto wake! Akakubali bila shida. Wakajipanga kama kitu kimoja, ndipo wakaagana.
Kwa
Jacinta.
J |
ack akafikiria na kuamua kumtumia ujumbe dada
yake. ‘Dada, najua nimekuangusha vibaya sana. Naomba
msamaha. Ila nipo kwenye kutengeneza. Na safari hii nitatengeneza mimi mwenyewe
bila kumtumia mama. Ila nahitaji msaada wako.’ Akatuma huo ujumbe.
Kimya. Ila akaona amesoma. ‘Naomba kuzungumza na wewe
dada yangu. Ukinitupa tu, ujue safari hii nitaumiza vibaya sana familia yangu.’
‘Nitakupigia baada ya lisaa.’ Alipopata hayo majibu, akafurahi sana. Akaondoa
gari mpaka kazini.
Baada ya dakika 45,
akaona simu ya Jacinta ikiingia nusura aruke kutoka kitini. Akaomba faragha
ofisini kwake, waliokuwepo ndani wakatoka. “Nashukuru
kunipi..” “Nenda kwenye pointi tafadhali. Usinipotezee muda.” “Nataka
kukusimulia kilichotokea.” “Acha kuniambia uchafu wako Jackson! Wewe ni mchafu
unashindwa hata kufikiria familia yako! Hata kama wewe ni malaya wa namna gani,
unalala hovyo tu bila kinga!?” “Ni kitu kilichotokea mar…” “Unahitaji
nikusaidie nini?” Jacinta akasikika kikazi haswa mpaka Jack akarudiwa na
hofu.
“Ibra
alijichukulia picha alizopiga Phina nikiwa nimelala kutoka kwenye simu ya Phina
na kujihamishia kwenye simu yake. Phina anasema anaonekana ni kama analengo la
kutaka kuzitumia vibaya. Nimemwambia Phina amuombe tukutane naye, asimwambie
kama mimi nitakuwepo. Kama tumvamie tu. Ndio naomba askari ambao watatusaidia
kupokonya simu yake illi kuzifuta.” “Akiwashitaki kwa kumpokonya simu?” Hapo Jack akakwama.
“Umelala kweli wewe?
Au unausingizi unaokufanya unashindwa kufikiria! Maana naona unaongea ujinga!”
“Nisaidie dada. Nimekwama na sikukusudia kuzaa na Phina.” “Nakuuliza hili swali
nataka ulifikirie kabla hujanijibu na kama huna jibu, ni bora unijibu baadaye.”
“Juu ya nini?”
Jack akauliza kwa wasiwasi. “Unataka kuzaa na Phina?”
“Hapana dada na wewe unaju..” “Jackson Msindai, unaongea sana bila kufikiria. Unataka
mtoto na Phina? Jibu lako nipe ukiwa umetulia. Na naomba usionekane TENA na
Phina sehemu yeyote ile.” “Sawa dada.” “Nitumie namba yake ya simu na ya Ibra.
Huwa hatupokonyi watu simu ili kufuta taarifa.” Simu ikakatwa na
kumuacha Jack akitafakari. Lakini kwa haraka sana akamtumia Jacinta namba ya
simu ya Phina. Akabaki akifikiria. Jibu alilojibu kwanza, hakuwa na wasiwasi
nalo. Anauhakika nalo. Ila agizo la kutoonekana Tena na Phina, analitekeleza
vipi wakati Phina ametulia akijua anakutana naye ili amsindikize kwa Ibra!
Akili ya Jack ikawa ikichemka akijitahidi kucheza karata zake kwa akili ili
asiharibu zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia simu Phina. “Ibra anatumia namba gani?” “Anazo mbili. Unazitaka?” “Zote tafadhali.”
Hapohapo akamtumia. “Umeshamtafuta?” “Hapana. Nimeona
nianzie pale Ustawi wa Jamii kwanza. Nipaweke sawa ndipo nimtafute.” “Unawekaje
sawa?” Jack akaendelea kumchota taratibu. “Naenda
kufuta kila kitu tulichosema jana. Zaidi mambo aliyozungumza Ibra. Nataka
kuwaambia haikuwa idhini yangu. Yeye ameongea tu. Mimi sitaki kesi.”
“Nakushukuru sana Phina. Asante.” “Samahani Jack. Nimeumia kuona imekua hivi!
Nimekumbuka jinsi ulivyonisadia kupata hii kazi na mengine mengi. Sikukusudia.”
“Haina shida. Naomba kuanzia sasa tuwe upande mmoja.”
“Nitakutaarifu muda na sehemu tutakayokutana na Ibra, ili tuwe na wewe pia.
Angalau nikuone, nikuombe msamaha unione ninavyo maanisha.” Phina
akaonyesha utayari wa kuwa huo upande mmoja na Jack. Jack na yeye akawa
akimsikiliza na kumuitikia kwa makini ila kichwa kikichemka jinsi ya kumtoka
bila kuharibu hiyo hali ya utulivu aliyoipata mpaka utayari wa kwenda
kurekebisha huko Ustawi.
“Sawa. Ila
naomba usikasirike ikitokea nashindwa kufika Phina, mama. Nina mambo
yananishikilia hapa ofisini. Sitaki kuharibu na hapa.” “Usijali hata kidogo,
Jack. Nakuelewa kabisa baba watoto wangu.” Hapo moyo wa Jack ukawa kama wa Sabrina. Mpaka
akaelewa anavyosema Sabrina moyo unapasuka inakuwa kama chuma kimeanguka sakafuni!
“Baba watoto wake! Mungu nisaidie!” Akachoka kabisa na kuzidi kuingiwa
hofu kana kwamba hakuyapanda, hapo anavuna! “Sawa. Tutawasiliana.”
Jack akamjibu lakini huku akiyafanya yote. Mpaka wanaagana na Phina,
alishamaliza kumtumia dada yake hizo namba na kumjibu ujumbe wake. ‘Nitakujulisha kazi itakapokamilika.’ ‘Asante dada. Na bado
jibu ni lileile, sikuwa nimekusudia kuendesha familia mbili.’
Hakujibiwa. Ila aliona ujumbe umefika.
Phina.
K |
uanzia Phina anatoka nyumbani kwake, hakujua kama
kuna watu wanamfuatilia na kuripoti kwa Jacinta. Akaingia Ustawi wa Jamii, kuzungumza
nao. Wakati anakaa tu, akaingia msichana mwingine na yeye akakaa sehemu
nyngine. Phina akajieleza akikanusha kila kitu walichosema jana yake mpaka
akawashangaza wale aliowakuta pale mwanzo. “Au umetishwa!?” “Hivi mnavyoniona
naonekana ni kama mtu niliyetishwa?” Phina ametoka kuzungumza na Jack, wana mipango
yakulea mtoto, roho safi. “Yale mambo ni ya yule niliyekuja naye. Kwanza hata
sio kaka yangu! Ana bifu na Jackson Msindai. Anataka kumuharibia, ndio
akaniambia nije tumuharibie. Jack alikuwa mpenzi wangu wa chuoni.” “Kwa hiyo
zile picha mlizopiga Uswiz ni…” “Mjini hapa mama yangu. Mambo yanatengezwa.’
Phina akaongea mengi mpaka akawaweka sawa, Ibra akabaki kichekesho. Akatoka
hapo akiwa ameridhika amemtengenezea Jack, atamfurahisha.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamtumia ujumbe Ibra
akimuomba wakutane kwa chakula cha mchana. Akakubali kwa haraka sana. Wakapanga
muda na sehemu. Hapohapo Phina akamtumia ujumbe Jack kumtaarifu kila kitu. Jack
akashukuru Mungu hilo la Ustawi wa Jamii limekaa sawa. Sasa kukutana ndio
akatafuta hekima yake ili asije kutibuka tena atakapoona hajatokea. Akijua wazi
hatakwenda, lakini akamwambia kwenye mida ya saa nne atampa jibu la hakika kama
atakwenda au atamuomba yeye amuwakilishe. Phina akazidi kufurahia akijua
wapo ukurasa mmoja na Jack, kumbe Jack yupo kwenye mikakati ya kujitoa kwake
moja kwa moja. ‘Usijali Jack. Mimi naelewa. Wewe chapa
kazi.’ Akamrudishia hayo majibu.
Hata hivyo kwa asili
Phina alikuwa mtaratibu. Mzuri sana wa sura na umbile pia. Kwa muonekano ukweli
alivutia kwa haraka sana. Jack akamtumia dada yake muda na sehemu watakayokutana
Ibra na Phina. Akaona ujumbe umefika, lakini hapakuwa na majibu. Alitegemea. Akatulia.
Sikio
Halizidi Kichwa.
I |
lipofika mida waliyokubaliana kukutana, Phina
akaenda hapo, akamkuta Ibra akimsubiria. “Vipi mrembo?” “Mimi naendelea vizuri.
Za tokea jana?” “Nzuri tu, lakini nilikuwa nazungumza na jamaa hapa kwa simu,
anaonekana anaweza kutusaidia swala la Jack.” “Kwa njia gani?” “Hata kwa kumshitaki
kisheria! Yeye si anajidai mjanja? Sasa sisi tumuwhi kisheria. Tunamshitaki
kuwa Jackson Msindai anatumia mali ya serikali kufanya…” “Subiri kwanza Ibra. Kwani
kimetokea nini kati yako na Jackson!?” Mpaka ikabidi Phina kuuliza maana Ibra
alionekana amebakiwa na ajenda moja tu maishani. Ajenda, ‘Angamiza Jackson
Msindai’!
“Jamaa mshenzi yule!”
“Amekuudhi nini hicho ambacho upo tayari kumuharibia kwa kiasi hicho?” “Usitake
kuniambia kama umebadili mawazo, Phina!” “Sio kubadilli mawazo ila nataka tu
kujua mlipokosana na Jack kwa kiasi hiki ulicho tayari kumuona ameharibikiwa
mpaka amefika chini kabisa!” “Nisikilize Phina, mimi nakusaidia wewe.” Phina
akakunja uso kama akimshangaa.
“Katika mazungumzo yangu
ulinisikia nikisema Jack alinibaka!” “Phina wewe vipi!?” “Hapana Ibra. Katika
vita yako na Jack, jua na mimi utaniangamiza tu. Unapotaka kumshitaki kutumia
mali ya umma kufanya uchafu wake, ujue aliyefanya naye uchafu ni mimi. Jack
atakapofukuzwa kazi au atakapoharibikiwa, inamaana na mtoto wangu
ataharibikiwa.” “Wamekufikia nini ndio maana unaongea hivyo!? Wamekuahidi
nini?” Ibra akaanza kupandisha hasira zaidi kana kwamba ni kaka yake kweli Phina!
“Hapana Ibra. Wewe
fikiria tu bila jazba. Sina mahali nilipolalamika juu ya kubakwa. Na sio kwamba
nimekutana na Jack, nikamwambia swala la ujauzito, akanikana. Nimefikiria
nimeona nakwenda mbali mpaka napotea lengo.” Wakaanza kubishana. Wasijue yupo
mtu meza ya karibu kabisa na wao, ameshaingia kwenye simu zao, ameshapata
mafaili ya picha, anaendelea kufuta vitu kwenye simu zao, wao wakiendelea kubishana,
hawajijui.
“Hapana Ibra. Mimi
mwenzio bado nampenda Jack.” “Kwa hiyo unajidanganya kwa kubeba huyo mtoto ndio
atakurudia?” “Hata asiponirudia lakini nitabaki mama watoto wake, daima. Kwamba
nimepata sababu ya kuwa na Jack kwa karibu kama mzazi mwenzie. Nampenda Jack, na
Mungu amenisaidia atakuwa baba mtoto wangu, nataka afanikiwe zaidi. Nakuonya
achana na mambo yangu na Jack.” “Basi wewe achana nayo, mimi naendelea
kivyangu.” “Unaendelea vipi na mimi mlengwa nishakwambia sitaki! Wewe
vipi Ibra!?” Ibra akanyanyuka na kuondoka hapo kwa hasira kabisa mpaka akamshangaza
Phina.
Alichokuwa hajui Ibra mpaka
hapo ananyanyuka na kuondoka kwa hasira akipania kwenda kumuharibia Jackson
Msindai, hana ushahidi tena wa kuwa Jack alilala na Phina. Kitendo cha kukaa tu
hapo, nyumba yake, gari na hiyo simu vilivamiwa kama nyuki bila yeye kujua. Na
walihakikisha wanatafuta mpaka chini ya godoro! Kwa makini ili akirudi asijue
kama kuna mtu aliingia hapo kwake. Gari yake ilipekuliwa kila mahali. Uzuri
nyumbani kwake alikuwa akiishi peke yake. Ikawa rahisi.
Picha zilizokutwa
zikachukuliwa na gari yake kufungwa pamoja na nyumba kurudishwa kama alivyoiacha
kwani huwa wanapiga picha kabla hawajagusa. Kwa hiyo wanaporudisha
wanahakikisha hata kama uliacha kijiko kichafu kitandani, basi utakikuta
vilevile kana kwamba hakuna aliyepita hapo kumbe ilifanyika kazi kwa kina bila
kupuuzwa sehemu yeyote mpaka ndani ya mto, lazima mkono upite na jicho
lihakikishe hakuna wanachokitafuta.
~~~~~~~~~~~~~~~
Phina akamtumia ujumbe
Jack. ‘Nimetoka kuzungumza na Ibra. Hatujaishia pazuri
na ameshatafuta mtu atakayemsaidia kukushitaki.’ Jack akasoma huo ujumbe
akatulia kidogo kama dakika kumi hivi, kumuonyesha kweli yupo busy, wakati hapo
akili yake haifanyi kazi kwa hofu ya mkewe na aibu aliyotia familia. Alikuwa
akisubiria safari moja ya nje ya nchi ambayo hakuwa na uhakika kama atapewa
yeye au atasafiri Waziri mwenyewe. Akatamani iwe ni yeye angalau atoke hapo
nchini, akapumue kwa muda. Pengine ataweza kulala kitandani, maana hakuwa akilala
kitandani kwa hofu ya mkewe. Akajiambia akipata usingizi hata wa masaa 6 tu
mfululizo, pengine akili itafanya kazi. Akabaki akifikiria hapo mwishoe akamrudishia
ujumbe. ‘Usijali. Rudi kazini ukatulie kabisa. Usijipandishe
presha. Inatosha.’ ‘Nashukuru kujali, Jack. Asante na samahani.’ “Usijli.”
Phina akafurahi akarudi kazini roho imetulia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jack alikuwa amekaa
ofisini kwake hana afanyalo isipokuwa macho kwenye simu akimsubiria dada yake
na kujua kama anasafiri au la. Akiwa mawazoni, ujumbe kutoka kwa Jacinta ukaingia.
‘Labda kuwepo na picha nyingine sehemu ingine, lakini
hizo picha zimefutwa kwenye simu zao. Mpaka nakala alizokuwa ameficha nyumbani
kwake na kwenye gari lake zote zimeharibiwa.’ Jack akapumua kwa nguvu, wakati
akitaka kumshukuru dada yake akapata wasiwasi mwingine. ‘Kama je zimebakia kumbukumbu huko studio alipoenda kutoa kopi?’
Jack akamuuliza dada yake. ‘Wapi?’ Hapo Jack
akajua hilo swali linataka majibu ya uhakika. Akamtafuta tena Phina kujua ni
wapi walienda kutoa zile picha, akawa hajui. ‘Nimekwama
dada. Phina hajui.’ ‘Angalia kwenye bahasha au nyuma ya picha walizokuletea.
Wanaweza wakawa wameacha jina la hiyo kampuni. Iwe haraka kuwahi kabla hazijatolewa
nyingi zaidi tukashindwa kudhibiti.’ Jack akakimbilia kwenye gari
kuchukua ile bahasha. Bahati nzuri dada yake alikuwa sahihi. Akamtumia. ‘Hizo picha zisiwahi kuonekana na jicho lolote, hata lako.’
‘Naziharibu sasa hivi.’ Ujumbe ulifika ila haukujibiwa.
Jioni akiwa amebaki peke
yake ofisini ukaingia ujumbe mwingine. ‘Na studio pia
zimeharibiwa. Isiwahi kutokea tena kuniomba nifaye ujinga kama huu. Iwe
mwisho.’ ‘Nashukuru dada na nakuahidi haitatoke...’ ‘Na baba ameamuru yule
daktari wa Moshi aachiwe huru. Kesi zako zote hataki kuzisikia tena. Zimefutwa.’
Jack akaumia sana, akajua baba yake ndio anamnawia mikono. ‘Nilikosea sana dada yangu. Najuta. Najua nimeabisha familia
na nimeharibu familia yangu mwenyewe. Lakini naahidi nitarekebisha.’ Huo
ujumbe haukujibiwa tena. Akabaki pale akifikiria kitu chakufanya.
Nyumbani kumekuwa moto.
Anamuogopa Sabrina, kuliko alivyowahi dhania anaweza muogopa mwanadamu. Akajua
Tino ndio amerudishiwa watoto. Akatamani ingekuwa ni kosa jingine amefanya ili
ampigie simu kaka yake apate hekima zake, lakini naye akamuogopa. Akaona
atulie. Dhambi yake aliyofanya mbali, nje ya nchi kabisa, ikanuka kuliko
waasherati wote na wazinzi wote aliowahi kuwafahamu. Akajifananisha na mfalme
Daudi wa kwenye bibilia, alipolala na mke wa Uria. Mungu akamuadhibu vibaya
sana. Jack akajua na yeye anapata aina ileile ya adhabu aliyopewa mfamle Daudi {2Samweli12:12,18}. “12.Na
mimi niliyofanya sirini, hakika Mungu ameniadhibu hadharani.” Jack akawaza.
“18.Na mimi nimepoteza binti wazuri,
wawili!” Kila Jack alipohesabu starehe aliyopata alipomuweka Phina
kitandani mpaka anamalizana naye, na madhara anayoendelea kuyapata, akazidi
kuingiwa hofu. “Hakika hii ni laana kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa maombi ya
Sabrina. Mungu nisamehe.” Hapo mpaka Jack akatubu.
Akabaki akisuburia muda
aliojua Sabrina na wanae watakuwa wamelala, ndipo na yeye akarudi nyumbani. Akafanya
hivyo kama siku mbili mfululizo. Anakwenda usiku mwingi na kuondoka alfajiri,
tena analala kwenye kochi.
Tino.
B |
aada ya siku tatu kama alivyoambiwa na Sabrina,
Tino akamtumia ujumbe Sabrina. ‘Tunaweza kukutana
tukazungumza?’ ‘Saa ngapi na wapi?’ Sabrina akarudisha majibu. ‘Muda wowote ambao utakufaa kwako wewe na watoto. Kuna
chakula nataka niwapikie, ni Pasta tu, chakula cha kiitaliano. Mje kula hapa
nyumbani kama kuwakaribisha rasmi Jeiline na Keiline kwenye familia. Kama ni
sawa lakini.’ ‘Basi nitawaleta na njaa, mida ya saa 10 jioni wakiamka,
nitakuacha nao mpaka kwenye saa moja hivi ndipo nitarudi kabla hawajaanza kulia
usingizi. Na hapo ndipo tutapata muda wa mazungumzo.’ Tino akapoa
kidogo, inamaana Sabrina amejitoa kwenye huo ukaribisho. Akatulia kidogo ila
baadaye akajibu. ‘Hata hivyo nashukuru Sabrina. Asante
kunipa nafasi na watoto.’ Sabrina akasoma huo ujumbe, akajua amemuelewa.
Akatulia akifikiria bila yakumjibu tena.
Ilipofika mida ya saa 10:30
jioni, Sabrina akawa amewasili nyumbani kwa Tino. Siku hiyo alimruhusu Chali
mapema sana. Akamwambia kwa siku hiyo kazi yake imeisha, anaruhusiwa kuondoka.
Sabrina akawa akiendesha wanae mwenyewe. Mlinzi akafungua mlango wakamkuta Tino
ndio anatoka mlangoni. Alishanyoa, akarudi yule Tino wakuvutia. Sabrina akavuta
gari mpaka karibu kabisa ya aliposimama. “Sasa hao wananjaa. Kila mmoja wao
anakibegi chake hapo. Wakianza tu kulia, nipigie. Nitakuwa saluni. Nikimaliza
nitakuja.” “Sasa mbona wananiangalia tu hawataki kutoka kwenye viti? Watakubali
kweli?” “Zungumza nao kwanza. Hawawezi kushuka tu. Halafu pia bado wana usingizi.”
“Basi anza kuwaambia wewe Sabrina.” Sabrina akawageukia wanae nakucheka.
“Wanavyokuangalia! Keiline?”
Keiline akamgeukia mama yake na Jeiline akamgeukia pia. “Anko Tino ana kitu
kizuri anataka kwenda kuwaonyesha. Mnataka kwenda kuona?” Wote wakatingisha
kichwa kwa pamoja kukataa. “Mnataka kwenda na mami?” Wakakubali. “Basi acha
niweke gari vizuri nishuke nao, wakichangamka ndio niondoke ili upate nao muda.
“Nashukuru. Lakini kwani huwa wanakataa watu?” “Nilidhani wewe wangekukumbuka.
Nahisi sababu ya kukaa tu ndani, hawajazoea watu. Acha niweke gari vizuri
nishuke nao.” Tino akafunga huo mlango wa nyuma walipokuwa wamekaa hao watoto,
wamefungwa kwenye viti vyao Sabrina akasogeza gari.
Kaegesha vizuri na
kushuka na wanae. Wakaingia wote ndani, akakaa nao chini kabisa na kuwaambia
watoe michoro yao waanze kuchora. Tino akabaki akiwaangalia. “Wamekua! Wameweza
kuzungumza?” “Wanaongea wakiamua. Ila wanaelewa kila kitu na wakitaka kitu chao
watakwambia tu. Wanatumia vitendo zaidi kuliko maneno.” Tino akabaki
akiwaangalia. Kila mmoja wao akafungua begi lake na kutoa vifaa vyake. Tino
akashangaa sana. “Hivi vitu umepata wapi Sabrina!?” “Jack huyo. Kila akienda
safari, anarudi navyo. Ila Tino, hawa watoto wanakipaji cha ajabu sana mpaka wanatushangaza!
Chagua kitu chochote unachotaka. Kiweke mbele yao, halafu waambie wakichore.
Utashangaa.” “Kweli Sabrina?” “Wewe si utakua nao hapa, wajaribishe na usiwe na
haraka. Kwa muda wao watarudi na kuchora.” Tino akafurahi sana.
“Wakati wanachora,
unaweza kuja hapa sehemu ya kula tuzungumze kidogo au watalia?” “Ilimradi wajue
nipo, hawatakuwa na neno. Tena ngoja niwaambie. Wamesahau kusalimia.” Akageukia
wanae. “Keiline, mmesalimia?” Wakaangaliana, halafu wote kwa pamoja wakasema,
“Shikamoo anko Tino!” Tino akashangaa mpaka akafunika mdomo. “Sabrina! Inamaana
walikusikia…” “Na kuelewa pale garini. Kwahiyo walivyotingisha kichwa kukataa,
haukuwa usingizi. Kweli walikuwa hawataki.” “Ungewalazimisha?” “Wana machozi
hao, hujawahi ona. Na wakilia utasikia uchungu maana wanalia kwa huzuni mpaka
dada yao anawajua! Hataki walie.” Sabrina akaanza kucheka akiwaangalia.
“Na mbona unamuita sana
au unamuanza Keiline katika kila jambo?” “Upo makini, Tino!” “Nimekuona tangia wakati
ule kwenye Villa.” “Alinifundisha Jack, akasema Keiline ndiye mtiifu na
mwitikiaji wa haraka. Hata wakitoka hapa wakaenda chooni. Ukimuita Keiline,
atakuja kwa haraka sana. Ila ukimuita Jeiline, unaweza ukarudia hata mara tatu
ndio anakuja. Na ujue wanafuatana kila mahali. Kwa hiyo ndio siri hiyo.”
“Oooh!” “Waitikie sasa salamu yao halafu waulize maswali. Nikiondoka, jifunze
wanachofanya, halafu fanya nao ila usiongee sana. Ukizidisha tu maneno,
wanaondoka na kukuacha.” Tino alicheka sana.
“Kweli Sabrina?” “Wajukuu
wote wa Msindai wamewajua. Michezo yao hawa, hawataki maneno mengi. Ukiongea tu
sana, wanaondoka kimyakimya. Kwa hiyo mara nyingi wanakuwa wao peke yao.” Tino
akawasogelea karibu na kuwatizama kwa kutulia. Wakamwangalia. “Gosh! You girls
are so beautiful!” Tino akajikuta
akiwasifia tu hao watoto jinsi walivyo wazuri! Wakacheka wote kwa pamoja.
“Kwani wameelewa!?” “Sijui!” “Kwani mnawaongelesha lugha gani?” “Unanitania
wewe Tino? Kiswahili.” Akarudisha macho kwa wanae. Akakuta wakimwangalia. “Nimefurahi
kuwaona tena. Nilikuwa na hamu na nyinyi!” Wakatulia wakimwangalia. “Endelee na
mnachofanya, acha nizungumze na mami, halafu nakuja mnifundishe mnachofanya.” Wakakubali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakahamia sehemu ya kulia
chakula. “Kabla sijaanza mengine naomba nikwambie swala la hii nyumba. Ni kweli
nimekusudia kuwapa hawa binti zangu. Nilisaidiwa kujenga na baba yangu, na mimi
nawaachia. Sitaishi tena hapa nchini. Nimeamua. Naona huko nilipo ndio nafanya
vizuri kuliko hapa. Nataka wanangu wawe na kwao. Hapa palinifaa sana nilipofukuzwa
nyumbani kwa baba na mkewe. Nimeishi hapa kwa miaka mingi sana. Pamefanyika
kama nyumbani.” “Nashukuru Tino.” Tino akasimama kuelekea chumbani kwake, akarudi
na kilekile kibegi alichokuwa amempa Sabina.
“Ulivyokikazania hicho
kibegi!” “Ilibidi nikakifuate Chalinze japo nafikiri upande wa pesa, hapako
vizuri.” Sabrina alimjua dada yake. Akajua yeye na mama yake watakuwa walizitumia
zote. “Nilikwenda benki, hali si nzuri. Sasa sijui kama kuna mtu aliiba taarifa
au vipi, lakini nimekuta pesa zimetumiwa vibaya sana. Ila nimeshazifunga.
Nataka kukuomba kama utanipa hawa. Niende nao kesho huko benki. Niwafungulie
akaunti zao.” “Kesho saa ngapi?” Tino mwenyewe akashangazwa na utayari wake.
Alibadilika sana Sabrina.
“Ni wewe tu na muda
wako.” “Lakini Tino, hizo kadi za benki safari hii nataka zitunzwe sehemu
ambayo haitaguswa mpaka itakapolazimu sana.” Sabrina akafikiria. “Nimeyajua
maisha kwa picha ya tofauti. Huwezi kuyatabiri ndio maana imebidi nijiandae.
Nilipojifungua mtoto wangu huyu wa mwisho, niliugua sana.” “Pole. Nini?”
“Nilipata infection, nilikuwa nikipandisha homa, nilidhani ningeondoka. Sasa
nafikiria siku nikiondoka, hawa watoto wakizungu, watakwenda wapi! Ndio imebidi
nijirudi japo wewe ni mtu wa mwisho kabisa natamani kukaa na wewe kama hivi na
kuzungumzia jinsi ya kuwalea hawa.” “Bado hujanisamehe tu, Sabrina!?” “Hakika
ni kwa kuwa wewe ni baba yao Tino, na wamezaliwa wapo hivyo kama walivyo na
kugoma kuchukua uswahili kabisa. Lakini wewe!” “Basi Sabrina. Naomba
usipandishe hasira.” “Na kweli.” Sabrina akasimama.
“Sijamaliza.” Sabrina
akamgeukia. “Unafikiri unaweza kuja kunipa siku moja niende nao Italy.”
“Nilikwambia siku ile usiku kuwa, nataka wafahamu walipotoka. Kwa hiyo ndiyo.
Ila bado hawana hati za kusafiria.” “Ukinipa mimi taarifa zao zinazotakiwa huko
wizarani, nitashugulikia hizo hati kwa haraka sana.” Sabrina akakunja uso. “Kwani
ulitaka kwenda nao lini?” “Wakati wowote utakapokuwa tayari.” “Hawa watoto
hawajakuzoea Tino, na bado wanahitaji msaada. Mimi nakujua wewe ni mtu
wakutumikiwa. Watateseka sana ukiwachukua sasa hivi. Tafadhali acha wakuzoee
kwanza.”
“Nisikilize Sabrina. Tino
uliyekutana naye wakati ule si huyu. Hakika nimebadilika na nimeacha ubinafsi.”
“Hilo ulitakiwa kulishugulikia kwakweli. Kama umefaulu hapo, hongera. Maana…”
“Utapandisha hasira Sabrina. Hapo paache hivyohivyo. Ninachotaka kusema ni
kwamba, hawa watoto ndio wamesababisha nitoke kifungoni safari hii nipo mzima.
Ni kama sasahivi naishi kwa ajili yao. Nakuahidi nitajifunza kuwa baba mzuri
kwao. Nielekeze tu. Na ukiwa unanipa nikiwa hapa, basi wakilia nitakuwa
nikikupigia mpaka wanizoee.” “Hapo sawa. Una kingine? Maana nataka kwenda
saluni.” “Hiki kingine naomba ukae.” Sabrina akarudi kukaa.
“Hali ya wazazi kule si
nzuri.” Sabrina akabaki akimwangalia. “Umenisikia?” “Nakusikiliza.” “Waliambiwa
kwa barua kuwa Sabina ameshikiliwa na kufungiwa sehemu sababu ya aina yake ya
makosa. Mchochezi na mvunja amani. Anapanga mbinu za uvunjaji amani. Hawataweza
kumtoa mpaka siku ya hukumu yake. Ametengwa na jamii. Wazazi wanalalamika
kwamba si sawa. Kwa nini iwe hivyo kwake?” “Sasa si washitaki serikali?”
Sabrina akauliza kwa ukali. Tino akajua tayari amemtibua.
“Nilikwenda pale
nyumbani…” “Wameniambia Sabrina. Wamenisimulia kila kitu.” “Na unajua kwamba
wewe ndio unahusika kuwafikisha wote pale walipo? Maana wewe unaneema yako
mpaka huwa namshangaa Mungu. Linapofika jambo lako, huwa Mungu anaweka
mazingira mpaka anakutoa kwenye mdomo wa simba. Ona ulipo sasahivi na walipo mashabiki
wako.” “Ila Max na mkewe sijahusika Sabrina. Wao wenyewe walinitafuta na
kupanga mipango kinyume na kaka yake Jack.”
“Sabina?” “Nilikwambia
Sabrina. Na usifikiri siku ile nilikuwa nikizungumza kwa kuwa nilikuwa
nikijitetea! Ni kweli. Sikuwa nimekudanganya.” “Juu ya nini?” “Kweli unataka
kujua kwa undani?” “Umeanzisha mwenyewe. Ndio useme sasa.” “Tokea waliponiita
siku ile kule kwenye Villa na kuniambia niliyokwisha kukwambia, mimi nilibaki mtoa
pesa tu, lakini nilikuwa nikitembea kwenye mipango ya Sabina mpaka mimi
nikamwambia tupunguze mwendo ni kama tunakwenda mbali sana. Akasema
ameshawasoma kina Msindai, anajua aliposhindwa Max, yeye hawezi kuanguka kama
Max. Nifanye anachoagiza, yeye na mama watanisaidia kupata mtoto.”
“Mpaka kujenga pale kwenu
ni wazo lao wenyewe wakisema ni moja ya ushahidi kuonyesha kuwa mimi najali
nyumbani kwenu kuliko mumeo. Basi mimi nikawapa hiyo pesa. Lakini Sabrina, Sabina
yupo nilipomuonya atakuwepo kama hajajipanga vizuri. Akanihakikishia kwamba,
hawatamuweza. Nakuhakikishia Sabrina, nilimuonya Sabina.” Sabrina akazidi kuumia.
“Basi, watoto wakianza kulia, nipigie. Vinginevyo nikimaliza saluni, nitakuja
kuwachukua.” “Sawa.” Sabrina akatoka akiwa amezidi kuumizwa. Nyumbani kwao
vita. Ukweni vita. Mume ambaye ndiye aliyekuwa ngao yake, ndiye huyo! Akatoka
hapo na maumivu kweli.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akaenda saluni
kujitengeneza. Hakuwa amekwenda kwa muda mrefu kidogo. Akaona atulie hapo.
Wakaanza kumshugulikia. Akataka asuguliwe mpaka miguu. Akatulia hapo akiwa
amepotelea mawazoni hata asijue kinachoendela hapo saluni. Nani anasemwa, nani
anasifiwa. Yeye kimya mpaka wakamaliza, ilikuwa saa mbili usiku. Akarudi
nyumbani kwa Tino, akakuta watoto walishalala, wamemuegemea Tino. “Sasa kwa
nini hukunipigia?” “Nasikia raha hivi walivyonilalia. Nilikuwa naogopa hata kusogea
wasije wakaamka. Nimeongea kwa video na anti na ndugu wote wakiwasalimia hawa
naona mpaka chaji imeniishia, simu imezima.” “Walikula vizuri?” “Naona chakula
chenyewe nilichowapikia hawajapenda. Anti amekiona anasema ningefanya Pasta
laini zaidi na ningeongeza sauce pengine wangekula.” Sabrina akacheka akiwaangalia
vile walivyolala. “Watakwenda kuongezea na maziwa ndio watalala vizuri mpaka
asubuhi.” Tino akasaidia kuwapandisha garini, Sabrina akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka wanafika nyumbani
ni saa nne na nusu na Jack naye akawa anaingia getini. Akawa ameshampigia simu
Pina na mwenzie watoke kumsaidia kubeba hao watoto. Jack akabaki kwenye gari akiangalia
kinachoendelea. Akagundua ni watoto wa kike tu, na ndio wanarudi mida hiyo na
mama yao. Inamaana alikuwa kwa Tino. Jack akaumia sana. Ingekuwa siku chache zilizopita
angeuliza na kukemea, gafla akahisi amepoteza mamlaka kwenye familia iliyokuwa
ikimtizama kama kichwa cha familia. Akatulia hapo garini akifikiria mpaka
wakaingia wote ndani na yeye ndipo akaingia na kukaa sebuleni kama mgeni rasmi.
Sabrina akarekebisha
mambo yake na watoto. Akarudi sehemu ya kula akakaa na kuanza kula. “Kesho
nasafiri.” “Hata kama mama yako amekwambia anatambua watoto unaozaaa huko nje,
nakushauri ukumbuke kinga. Utakufa ukiwa umemuachia mama yako watoto kila kona.
Fanya umalaya ukiwa na akili timamu. Sio kwa kuwa mwanamke amekubali kulala na
wewe, basi ndio unajiachia tu hovyo ukijua hata ukizaa kama paka, mama yako
atakusaidia kulea.” “Sa…” “Acha kunijibu. Nakusisitiza, kumbuka KINGA. Hata
kama starehe zimekunogea huko, kumbuka mpaka sasa una watoto watatu. Brayan,
Brandon na huyo wa Phina. Kuwa mwangalifu.”
“Usifurahie vile dada
yako anavyokushangilia na kumwambia mwanamke wako eti atamfanyia babyshower na
yeye Phina anashangilia huko mitandaoni akijiona mshindi, ukadhani ni sifa.
Unaendelea kumwaga mbegu hovyo. Utakufa uache hawara zako na watoto bila baba.
Shauri yako.”
“Nilimuonya Jena aachane
na mambo ya babyshower. Sasa kama yeye…” “Hilo tu ndilo unaona ndilo lakuelewa?
Elewa swala la kinga, Jackson Msindai. Babyshower ya Phina, haina madhara, ila
haitakuwa na maana kama hata huyo mtoto atakuja kuzaliwa, halafu aje asikukute.
Binadamu wazuri ukiwepo. Hata Jena anashabikia sasahivi ili tu kuniumiza. Sasa
usifikiri ushangiliaji huo au juhudi hizo zitaendelea ukiwa wewe mwenyewe haupo!
Hamu ya ushindani itamuisha kwa kuwa watakuwa wamekuzika. Kwa hiyo huko Mungu anakokutuma
akiwa amekuamini, na wewe unaamua kuanzisha agenda zoko nyingine,
ndio nakusisitiza, KUMBUKA KINGA.” Sabrina akasimama na kuondoka hapo hata
chakula hakumaliza.
Jack akatamani kama
akamtafute Jena usiku huo, lakini akajua ataishia kumpiga mpaka amuumize kwa
kummalizia hasira. Alikuwa na safari aliyokuwa akiitamani mpaka akamuomba bosi
wake yeye ndio aende akamuwakilishe, bila shida Waziri akampa yeye. Jack
akalifurahia hilo akijua anaondoka kesho yake, anakwenda kupumzika kwa muda na
kumuacha Sabrina pengine atatulia lakini imekuwa tofauti. Safari yenyewe
imegeuka kuwa chungu kupita alifadhania. Anaacha kwake moto unazidi kuwaka na
dada yake akisaidia kuchochea kuni. Inamaana hata akirudi, atakuta mambo
palepale, hapajapoa.
Safari zote zinakuwa
nzuri na anaagwa kwa maombi, ila safari hii maneno machungu! Akabaki pale kwa
muda, akaamua kuingia chumbani na kuanza kufungasha, Sabrina kitandani
amejilaza, macho kwenye simu.
Akaanza. “Mwanamke wako amejaa
huko Instagram akisaidiwa
na wifi yake Jena. Dada Pendo amenitumia. Ameshatuma picha za Ultrasound na
tarehe ambayo wanapanga na Jena kufanya babyshower.” Jack akasimama wima kwa
mshituko, hakutarajia. “Unataka kuona au ndio unakwenda kuchezea tumbo lenyewe live?”
Sabrina akamkejeli akicheka kwa uchungu. “Siendi na Phina.” “Kwa hiyo safari
hii unaenda na mwingine tena!?” Jack kimya. “Mheshimiwa Msindai, utajaza
wajawazito huko Insta,
mpaka mfungue nchi yenu wenyewe.” Jack kimya.
Sabrina akarudisha simu
yake pembeni ya kitanda, akatulia. Jack akaendelea kufungasha. “Ni safari ya
siku 6 tu, nitarudi Brina. Na tutazungumza vizuri.” “Unataka unisimulie jinsi
ulivyomfaidi mrembo Phina, wakati mimi nikijiuguza hapa nyumbani peke yangu? Nilikuwa
nimejawa hofu ya kifo kwa kujifungua kwa upasuaji na kupata infection kali,
nahofia na kukuhurumia kukuachia watoto peke yako, kumbe mwenzangu huna hata
wasiwasi maisha yako yanaendelea, tena si
kama kawaida, kwa starehe tupu! Hakika Mungu aingilie kati katika hili.”
“Sabrina, ilitokea bahati mbaya, sio kitu nilipanga mke wangu. Naomba
usinilaani!”
“Mtoa laana ni Mungu
Jackson. Wala si mimi. Ila ujue umepoteza vigezo vyote vyakuwa baba kwa binti
zangu. Wewe endelea kukusanya watoto huko nje, mwache Tino na yeye achukue
wake, mambo yaishe. Unaniacha mimi naugua hapa na katoto kachanga, bado Brayan
mdogo kabisa ananililia hajui kama naumwa au nina mdogo wake, na wewe unajua
tulizaa karibu karibu, ukaniacha hapa, unakwenda kuendeleza umalaya wa kizembe huko
nje! Hakika Mungu aingilie kati.”
Sabrina akatoka kabisa hapo.
Jack akajua hicho
alichokiona huko Istagram ndio
kinamuumiza zaidi. Akaamua na yeye aangalie. Akachukua simu ya Sabrina na kutafuta
ujumbe aliotumiwa na Pendo. Akakuta ni kweli mpaka na tarehe na jina la ‘wifi
Jena’ halafu Jena Msindai aka like ile post na comment.
Akabaki amesimama pale na simu mkononi. Sabrina hakurudi mpaka asubuhi
anaondoka, akasikia Brandon amelia kidogo, akatulia. Akajua Sabrina yupo
chumbani kwao. Akaenda. “Mbaki salama.” Hakujibiwa. Akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment