Kabla Jena hajamalizia Jack akasimama kama mshale
akamrukia na kumpiga ngumi tatu mfululizo, mama yao akaingilia, Sabrina
akatoka. “Niliwaonya mumuache Sabrina. Mama na Jena, hakika nawaonya.
Katika kusaidia kwenu katika hili, iwe ni kusaidia kweli, isiwe si kushindana
na Sabrina. Mimi nilifanya kosa, acheni kumuadhibu mke wangu kwa makosa yangu.
Na usinijibu Jena. Sijalala nina usingizi, naweza nikakumalizia wewe hasira
bure!” Jena akanyamaza. Jack akatoka.
Chachu
Ndogo Imechachua Donge Zima.
|
J |
ack akamkuta Sabrina ndani ya gari. “Panda nyuma
ya hii gari.” Sabrina akamuamuru mumewe. “Tunakwenda wapi na kwa nini niache
gari yangu hapa!?” “Nikimalizana na wewe, utarudi kuchukua gari yako. Panda.”
Jack akapanda asijue wanapokwenda ila yeye Chali alishajua maana Sabrina
alimwambia mara tu alipopanda garini wakati Jack akimpiga dada yake ndani.
Chali akatoa gari hapo. Njiani kimya. Jack akashangaa wanaendesha mpaka kituo
cha polisi Ostabay. “Shuka.” Sabrina akaamuru tena. “Kwa nini tupo hapa!?”
Sabrina hakumjibu, akashuka na pochi yake na kufunga mlango.
Sabrina akaongoza njia
mpaka ndani kituo cha polisi, mapokezi. Jack akamfuata. “Mimi na mume wangu
tunataka kufuta kesi na kuondoa restrain Order kwa Constatino Mandari.”
“No way Sabrina! Haiwezekani.” “Usinitanie Jackson. Futa kesi
zote za Tino, na nataka atolewe jela usiku huu.” “WHAT!? Hata kama unaniadhibu
lakini si kwa..” “Ushaona wapi mtu
anaadhibiwa kwa kupata starehe?” Askari wa pale mapokezi wakabaki wanashangaa.
Ni Naibu Waziri wa fedha na mkewe. Kina Msindai!
Sabrina akamvuta mkono na
kumtoa nje kabisa ya pale mapokezi mbali na masikio ya watu. “Kwa maisha
uliyochagua kuishi wewe, ndiyo nayaendeleza. Wewe unalala na wanawake nje bila
kinga. Unataka uje uniue mimi, halafu binti zangu ndio waje wapate shida!” Sabrina
akaanza kugomba. “Yaani mama yako leo amenifungua macho na amenithibitishia
wakina Jeilini hawatakaa kuwa wakina Msindai. Amewakataa. Ndio maana leo
yupo radhi kumpokea mtoto wa Phina, lakini si wangu! Sasa ulitaka wewe
uendeleze umalaya huko nje bila hofu ukijua hata ukifa kesho wanao watapata
pakukimbilia halafu wanangu wao ndio waje wapate shida baadaye, ukiwa mimi mama
yao ushaniua, baba yao umemfunga jela, hawajui ukoo wao kama hivi mama Msindai
anavyotaka mtoto wa Phina ajulikane kwenye ukoo wa Msindai!? Acha ushenzi na
ujinga. Tunafuta kesi zote za Tino. Na sijui utafanyaje Jackson Msindai,
namtaka Tino HAPA. Usiku huu, LEO.” “Tino anakabiliwa na makosa mengi likiwepo
la kukamatwa na madawa ya kulevya.” Sabrina akashangaa sana.
“Umechanganyikiwa Jackson,
wewe!?” “Amekamatwa, sio mimi.” “Sasa nisikilize Jackson. Namtaka Tino ambaye
amefutiwa makosa yake yote likiwepo hilo mlilomsingizia.” “Sio…” “Nisikilize
Jackson, maana katika hili huna chaguzi. Badala ya kupoteza muda hapa, anza kukusanya
jopo lako lote, mjue jinsi ya kumtoa Tino ndani.” “Hayupo hapa.” “Popote
mlipomfungia, utamleta hapa nillipo mimi. Maana hapa sitaondoka bila TINO.
Ukishindwa wewe, mimi nitamtafutia mwanasheria wakumtetea. Waseme leo, ni kifaa
gani hicho maalumu walichonacho uwanja wa ndege wa nchi kama Tanzania, ambacho hawana
nchi zilizoendelea kama Itali, kilichoshindwa kugundua madawa ya kulevya kwenye
sanduku la Tino wkati akiyatoa huko, eti hapa Tanzania ndio waweze kumkamata!”
Jackson kimya akijua akili ya Sabrina bado inafanya kazi japo amekasirika.
“Usinitanie Jackson! Kamlete
Tino hapa, lasivyo mimi na kina Jeiline, tutafika mpaka mahakamani kwa ajili
yake.” Kimya. “Na ujue kabisa Jackson, Tino
akilala ndani, mimi nitakuwa hapa nikimsubiria mpaka atoke. Hata kama
itachukua miaka, nitakuwa hapa. Usilete michezo ya kijinga hapa! Na uanze kwa
kumfutia mashitaka yote, hapa, tena sasahivi. Usitake kunitania mimi!” Sabrina
akazidi kuwaka.
“Unataka wewe watoto wako
uwatunze, au watambue ukoo wao, halafu eti mimi wangu nije kuwaacha hapa
duniani wakitangatanga kama mimi mama yao nilikuwa mjinga tu, sijielewi!
Namshukuru sana mama Msindai na Jena kunifungua ufahamu wangu leo! Sasa kama
wewe unakataa, ondoka niache hapa.” Sabrina akataka kuondoka, Jack akamuwahi. “Sabrin..”
“Acha kuzungumza na mimi. Nataka vitendo tu. Sina shida ya kukusikia.” Simu ya
Sabrina ikaanza kuita akapokea kwa haraka maana ilikuwa ni simu ya nyumbani
kwake.
“Dada, mtoto
analia sana.”
Alikuwa Phina. “Nilikamua maziwa na kuyaweka kwenye
friji kabla sijaondoka. Kwa hiyo mpe hayo maziwa. Pasha moto angalia yasiwe
moto sana akaungua ulimi.” “Tuliyamaliza tokea saa nne.” “Mmmh!” Sabrina
akaangalia saa, ilikuwa ikienda saa sita. “Usiwe na wasiwasi,
baba yake anakuja na maziwa.” “Acha kuadhibu watoto Sabrina. Huyu mtoto
bado ni mdogo, hajaanza kunywa maziwa mengine. Turudi nyumbani, tukazungumze.”
“Wewe ulikimbia nyumba tokea jana! Leo unataka kuniambia nini!?” “Nilirudi ila
sikujua ni jinsi gani ya…” “Basi kwa kuwa leo upo tayari kurudi, nenda na wewe
kalee wakati na mimi nikishugulikia mpango kando kama wewe. Wewe unashugulikia
mipango kando yako huko nje ya nchi wakati mimi nikilea. Sasa na wewe nenda
kalee wakati na mimi nahangaika na mpango kando wangu. Nikimaliza na mimi
nikawa tayari kurudi nyumbani, nitarudi. Ila hapa sitoki bila Tino.” Jack akaondoka
hapo kurudi garini. Sabrina akarudi kwa Phina. “Usiwe
na wasiwasi baba yao anakuja. Na ukiwa na swali lolote la watoto mpigie yeye
simu.” Sabrina akakata simu na kuizima kabisa na kurudi ndani kituo cha
polisi, akaenda kukaa kwenye benchi mbele ya mapokezi, akainama.
“Mama Msindai, karibu
usubirie hapa ofisini.” Mkuu wa kituo alishaitwa na kuambiwa kina Msindai wapo
hapo, akatoka na kubaki hapo mapokezi akijua kwa alichoambiwa na maaskari wa hapo,
watarudi tu. Akawa akiwasuriria hapo. Ndipo aliporudi tu Sabrina, akamuwahi kwa
ukaribisho. “Hapana, nashukuru. Kama hamtanifukuza, basi hapa panatosha.” “Hapa
pako wazi kwa msaa 24. Ila huku ndiko kwenye mazingira mazuri.” “Nashukuru,
lakini acha hapa patoshe tu.” Sabrina akarudi kujiinamia, kumuashiria amemaliza
mazungumzo na yeye.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jack akabaki garini
akifikiria pakuanzia kumtoa Tino. Kitendo cha baba yake kuondoka vile, akigomba
mbele yao, akajua kwa mara ya kwanza amemvunja sana moyo. Akaona asimtafute.
Junior! Akakumbuka Junior aliondoka pale hata hakumtizama wala kuchangia lolote
juu ya hilo. Akaona amtafute Jacinta ambaye yupo jikoni. Akarudi ndani kwa
Sabrina. “Njoo mara moja hapa nje.” Sabrina akasimama na kumfuata.
Waliporidhika wapo mbali na watakaposikika, Jack akaanza. “Inamaana unataka
mpaka Sabina aachiwe!?” “Umenisikia nikitaja jina Sabina usiku wa leo mimi?”
“Kwa hiyo upo radhi ndugu…” “Acha kunipoteza malengo. Futa kesi zote za Tino,
na ninataka hati yake ya kusafikiria ije naye pamoja na mizigo yake yote.” Sabrina
akaweka msisitizo.
“Kwa nini tusishugulikie
haya mambo kesho? Sasa hivi ni usiku sana.” “Tokea lini giza limekuwa tatizo
kwako na kushindwa kufanya yako? Usinitanie Jackson. Na usicheze na upande
ninaokuwepo mimi! Wewe unajua kabisa, walio upande wangu huwa hawashindwi, sasa
usinijaribu nikahamia kambi pinzani. Hutataka kuwa mahakamani ukishindana na
mimi pamoja na kina Keiline! Nakuonya Jackson!” Jack akarudi garini, Sabrina
akarudi kukaa ndani.
Kwa
Jacinta.
Akampigia simu Jacinta.
Ikaita mara kadhaa mpaka ikakata. Akajua ameamua asipokee simu zake. ‘Tafadhali, ni muhimu, lasivyo nisingethubutu kupiga.’
Akaona amesoma hajajibu. Jack akafikiria kitu kinachoweza kumfanya dada yake azungumze
naye. Akakosa. Akafikiria kwa muda ni nini kinamfanya Jacinta kuwa kama
mwanadamu au mwanamke wa kawaida! Maana wote walimjua Jacinta ni katili,
mkorofi haswa. Masikio yake huwa yanamsikia baba yao vizuri na kumuelewa yeye
bila kurudia kuliko mwanadamu mwingine yeyote na huwa hamuogopi mtu ila kuamua
kukustahi tu. Ila Junior huwa wanapatana sana na kuheshimiana tokea wadogo. Ni
kama Junior alishamjualia na akajua jinsi ya kuishi naye.
Jackson akamfikiria dada yake, mpaka akapata jibu.
Akarudi kuandika kwa haraka. ‘Ni jambo la kuhusu Sabrina.’
Hapo Jacinta akampigia. “Sabrina yupo hapa kituo cha
polisi cha Ostabay, amesema hataondoka mpaka Tino atolewe na afutiwe kesi zake
zote na aletwe na mizigo yake yote ikiwepo hati yake ya kusafiria.” “Mwambie
Tino atakuwa hapo baada ya dakika 45.” Simu ikakatwa. Jack akashangaa
sana asiamini anawezaje kumuachia Tino kirahisi hivyo! Akajua kweli Jacinta
amekasirika na anafanya makusudi kumkomoa.
Akarudi ndani, akamuita
tena Sabrina. Sabrina akatoka na kumfuata nyuma. “Tino atakuwa hapa baada ya
dakika 45. Nashauri urudi nyumbani kwa watoto.” “Nitakuwa hapa mpaka nimuone
Tino kwa macho yangu haya ya nyama. Akiwa mzima nitakuwa na mazungumzo naye.
Akiwa mgonjwa nitahakikisha nampeleka hospitalini. Anatibiwa mpaka apone kabisa,
nipate muda wa mazungumzo naye ndipo mengine yatafuata. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi
juu yangu. Inaonekana usiku ndio mzuri wa kufanya mambo kukiwa kumetulia. Ila wakati
wewe unakusanya watoto wa nje, nasikia kuna anayelia kule nyumbani. Jitahidi
kuwahi.” Jack akataka kutoka.
“Nashauri usiondoke bila kufuta
kesi na vipingamizi vyote vya Tino, Jackson. Maana kesho nakwenda naye Ustawi
wa Jamii, na mimi nafanya kama Phina.” “Sabrina umekasirika. Nashauri utulie.”
“Hata kidogo Jackson. Mama yako amenipigia kengele inabidi niamke. Na
nimeshaona hatari ya wewe kuja kuniua nikaacha binti zangu wakihangaika. Katika
hili, hamna hasira hata kidogo.” “Sabrina!” “Nakusisitiza Jackson, futa kesi za
Tino. Sikutishi, nakuonya.” “Kila kitu kimeshashugulikiwa. Tino analetwa hapa
na vitu vyake…” “Basi nashauri uwahi nyumbani. Brandon akianzaga kulia bila
kutulizwa akatulia, anaamsha watoto wote. Hapa tunapozungumza, watakuwa nyumba
nzima wapo sebuleni. Wahi. Na naomba uniachie Chali. Asisogee pale alipo. Tafuta
usafiri mwingine wa kukutoa hapa.” Jack akatoka. Sabrina akarudi ndani.
Sabrina&Tino
Tena .
Sabrina akiwa amejiinamia
askari kanzu wawili wakaingia hapo na Tino. Tino alikuwa amechoka haswa na
mandevu mengi. Wakamfungua pingu. “Mama Msindai!” Sabrina akasimama. Tumeambiwa
tukukabidhi na mizigo yake ipo kwenye gari. “Mimi sitaki tena kesi Sabrina.”
“Sasa hivi ndio unajidai hutaki kesi? Ulipokuwa ukikusanya watu kinyume changu
na mume wangu! Sikukuonya wewe?” Sabrina akamgombeza. “Nimejifunza.” Sabrina
akamwangalia na kurudisha macho kwa wale askari. “Naomba muhamishie mizigo yake
kwenye gari yangu. Twendeni. Na wewe unifuate. Acha kujitilisha huruma hapo
wakati ulijitafutia mtatizo wewe mwenyewe.” Akatoka, wote wakamfuata nyuma.
Wakamkabidhi Tino vitu vyake vyote, Sabrina akawashukuru na kubaki amesimama na
Tino.
“Mimi sitaki tena kesi
Sabrina. Naondoka hapa nchini na hutakaa ukaniona tena. Ila naomba nikuachie
ile nyumba. Na kabla hujakataa naomba nisikilize.” “Nani amekwambia nakataa!”
Tino akashangazwa na hilo jibu. Hakutegemea! Ikambidi kusimama wima na kumtizama
vizuri, aina hii mpya ya Sabrina. “Ulikuwa ukisema?” Sabrina akataka aendelee,
aache kumshangaa. “Ile nyumba baba yangu alinisaidia kuijenga makusudi ili na
mimi niwe na kwetu. Na ndio maana nilimwambia Lela, nitampa kila kitu lakini si
ile nyumba.” “Wakati umemtibua sasahivi? Unataka kuniachia ugomvi?” “Usiwe na
wasiwasi na Lela. Hana chake tena. Tulishamalizana. Max alisema tumchokoze tu
kama kuchokonoa mambo lakini alituhakikishia kwa hakika, hana lake tena. Kwanza
mimi ndio kama namdai. Kwahiyo chukua wewe ile nyumba ili Jeiline na Keiline
wapate kwao.”
“Sasa nisikilize Tino.
Kwanza umeangamiza watu wengi sana kwa upuuzi wako ambao nilishakuonya. Huwezi
kushindana na kina Msindai wewe. Nilikwambia.” “Hakika nimejifunza Sabrina.
Basi. Utakaponihurumia naomba uje unitambulishe kwa wanangu. Lasivyo najiweka
pembeni kabisa.” “Mbona safari hii hujaugua huko ulikokuwa umefungiwa?”
“Jeiline na Keiline ndio wamenifanya nitulie, Sabrina. Wale watoto wamenipa
sababu ya kutoka hivi japo njaa inauma sana. Lakini kila nilipokuwa nikikumbuka
wanangu, nilikuwa nikijiambia nina sababu ya kuwa hai. Sikuruhusu kuugua hata
kidogo. Ila nilifungiwa pabaya sana. Kulikuwa kunatisha, na hofu ya mashitaka
niliyosomewa ndio zaidi!” “Umesomewa mashitaka gani?” Akamtajia Sabrina.
“Sasa nisikilize Tino.
Nimekuombea kwa kina Msindai, haya mambo yaishe. Ila..” “Asante Sabrina. Hakika
ningefia jela! Nakuahidi sitasumbua tena.” “Nisikilize Tino. Nimeona siwatendei haki
wanangu. Kuna leo na kesho. Nataka kina Jeiline wakufahamu kama baba yao na
watambue wanapotoka.” Tino akaanza kulia hapo kama mtoto wa kike. “Nashukuru Sabrina. Nakushukuru sana. Niambie vile
unavyotaka, mimi nitafanya.” “Wewe ndio haupo hapa nchini. Ndio niambie
hii hangaika yote hii, mpaka ukafanikiwa kugeuza ndugu zangu kinyume yangu,
ulipanga nini baada ya kufanikiwa kupata hao watoto?” Sabrina akataka kujua
mipango yake.
“Acha kwanza mimi mwenyewe ndio niombe msamaha
kwa upande wangu kwa kuwa watoto ni damu yangu. Lakini Sabrina, halikuwa wazo
langu. Ipo siku tutazungumza vizuri. Ila kwa mara ingine tena, mlipoondoka
usiku ule pale Vila, mama yako na Sabina walinitaka nirudi usiku uleule kabla
sijaondoka nchini, nikarudi. Walizungumza na mimi mambo mengi sana mpaka
wakanibadili moyo wangu nikaona nakimbia wanangu sababu ya hofu tu. Nikajisikia
nina jukumu la kupambana ili kukomboa wanangu, wakiwa wamenihakikishia Jackson
hawezi kuwa baba mzuri kwa hao watoto. Wakasema hana msimamo. Atakuja kukimbia
watoto kama alivyofanya, kisha wanangu wakapata shida. Waliniambia mengi juu yenu
ya ndani kabisa, mpaka nikakuhurumia, nikakumbuka jinsi ulivyosimama na mimi bila kuchoka wakati sijiwezi, japo Lela
alikuwa akikukatisha tamaa. Lakini bado ukabaki na mimi.”
“Nikajua ile tabia yako
ndio unayoendelea nayo kwa Jack pia, mwishoe wanangu watakuja kuteseka.
Nikajiambia nina jukumu la kusaidia wanangu, ambalo siwezi kulikwepa hata kama
Jack kwa wakati huo anaonekana yupo, lakini na mimi lazima niwepo, ili
atakapokuja kukubadilikia, basi niwepo.” Sabrina akajiambia ndio utabiri
umetimia hivyo. Akajisikia vibaya, akapotelea mawazoni, Tino akizungumza.
“Anyways, nikataka
kuwalaumu kwa kuwa niliwaonya, lakini wakati nimefungiwa hivi nilivyokamatwa,
ndio ni kama nikapata muda wakutulia na kutafakari zaidi. Ni kama na mimi nimeungana nao kukuangamiza,
Sabrina! Nimejichukia sana. Na sikwambii hivi kwa sababu unanipa watoto, ila tu
kukwambia, nilivyofikiria. Nikajiambia nilikuwa nikikimbia bila kufikiria,
nikaungana nao. Ile hali ya utayari wao kuwa kinyume nawe na mimi nikiwasaidia
kimali, ndiyo ikanikumbusha zamani ulipokuja pale kwangu kuja kunisaidia nikiwa
mgonjwa, uliniambia juu yao. Jinsi mahusiano yao na wewe yalivyo na mimi nikaungana
nao. Kwa hiyo makosa ni yangu Sabrina. Acha mimi niombe msamaha. Nimekukosea
tena. Ila lengo ni wanangu, Sabrina.”
“Wale watoto wananikumbusha
haiba ya mama yangu mzazi ndio maana nashindwa kuwaacha. Nahisi kama Mungu
amenirudishia mama kupitia wale watoto. Anti alikuwa akiwaangalia kwenye video,
anasema wapo kama yeye na mama walivyokuwa. Hiyo ndio ikazidi kunichanganya.
Nataka kuwa na mahusiano na wanangu, Sabrina.”
“Kivipi?” “Kwa kadiri
utakavyoniruhusu. Wana vipaji vikubwa sana ambavyo vinahitaji pesa na mtu
anayeelewa kuviendeleza. Nilikuwa natamani hiki ulichosema, lakini sikuwa najua
jinsi ya kukitekeleza.” “Kipi?” “Siku moja niende nao kule kwa ndugu zetu,
niwatambulishe. Wapafahamu tulikotoka na ndugu zao ili wasijikute waajabu
katikati ya familia yenu. Sitajali hata wakiendelea kumtambua Jack kama baba
yao. Sitawaingilia vile watakavyokua, ila nataka wajue nilikosa, nimerudi na
nataka kuwatunza.” “Leo umechoka na kuna mengi utazungumza sababu ya hofu na
mimi sitaki kudanganywa.” “Sita…” “Hapana Tino. Nenda kalale. Pumzika kabisa
ukiwa na uhakika hakuna atakayekugusa tena. Huna kesi inayo kukabili. Kisha
nitafute baada ya siku tatu kuanzia sasa.” “Kwa maana nyingine, kuanzia leo upo
tayari kupokea msaada wowote wa watoto nitakao kupa?” “Kabisa. Na nitataka uwe
na mahusiano nao, ili ikitokea leo na kesho mimi sipo, basi wawe na pakwenda.”
Tino akamtizama Sabrina vizuri.
Sabrina akainama kama
anayefikiria. “Kuna nini Sabrina!?” “Nafikiria maisha ya binti zangu, Tino.
Mimi si Mungu kwamba nitakuwepo hapa duniani milele. Sitaki waje kumangamanga
mtaani wakitesema na wewe umerudi ukiwataka! Siwezi kufanyia hivyo wanangu.
Wewe nenda kapumzike, tutazungumza vizuri.” “Usinielewe vibaya Sbrina, ila
naomba kuuliza kwa uhakika. Hichi unachoniambia umekifikiria vizuri?” “Kabisa
Tino.” “Sabrina?” “Ni kweli na ndio maana nilitaka utolewe na ufutiwe kesi
zote, uwe huru. Nimeona nitajidanganya, na wanangu ndio wataishia kuumia.
Hakika usingekaa ukatoka jela Tino.” “Hilo najua. Najua kabisa.” “Basi ujue upo
huru kwa sababu ya watoto. Nataka uwepo hapa duniani, ili siku moja wawe na
kimbilio.” “Daah! Utanifanya niwe makini sana.” Wakatulia.
“Nakuahidi nitakuwa
makini Sabrina. Kwa hiki unachonipa, sitakuangusha. Najua utafurahi. Nipe namba
yako ili tuweze kuwasiliana.” Sabrina akamtajia. Tino akashika kwa kichwa.
“Sitakupeleka kwako Tino. Ingekuwa hospitalini hapo sawa. Hii gari ni ya
Msindai, siwezi nika…” “Naelewa kabisa. Kama hawatakuwa wamenidanganya, basi
inamaana wamenirudishia kila kitu changu. Nitakuwa sawa tu. Nitachukua taksii
hapa.” “Usiku mwema.” Sabrina akaingia garini akamwambia Chali amrudishe
nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina alifika kwake akakuta
pako kama mchana. Watoto wote wapo sebuleni
na baba yao, wamechangamka, mdogo analia na kunyamaza. Wote wakataka
kumkumbatia alipoingia. “Mama yenu ni mchafu na ninanuka. Subirini hapahapa
nikaoge kwanza. Nakuja.” Sabrina akakimbilia kutoa nguo na kuoga kwa haraka akatoka na kumchukua
Brian aliyekuwa akilia mikononi kwa baba yake. “Haya Jeiline mshike Brayan mkono twende chumbani kwao.”
Jeiline akasimama na kumshika mkono kaka yake. “Keiline wewe mtoto mzuri
ukaniombee maziwa ya Brayan kwa dada, halafu uyalete chumbani kwao.” Keiline
akakimbilia chumbani kwa kina Pina ,
baada ya muda hiyo nyumba Jack akashangaa ipo kimya kama haina mtu. Akavuta
pumzi kwa nguvu na kujiegemeza kwenye kochi. Akapitiwa na usingizi mzito asijue
alipo.
Ilipofika asubuhi Jack
akashitushwa na wasichana wa kazi waliokuwa wameamka wakianza majukumu yao ya
siku. Ikabidi atoke hapo sebuleni kuwapisha wasafishe. Akaingia chumbani kwa
kunyata akamkuta Sabrina ananyonyesha, pako kimya. Hakumsemesha, akaingia
kuoga, akatoka na kuvaa kwa haraka na kutoka hapo.
Kwa Phina.
|
N |
jiani akampigia simu Phina. “Ni nini kinaendelea Phina!? Mbona imekuwa ni kama umekusudia
kuniangamiza kana kwamba nilikubaka au nilikurubuni ili ulale na mimi?” “Mimi
mwenyewe nahisi kama Ibra ndiye anayekuza, Jack. Mimi sikutaka kukuharibia wala
yafike mbali, ila nilipokuwa nikikutafuta, nikakukosa ndio nikampigia simu Ibra
kumuulizia kama ana namba yako ingine.” Jack kimya akimsikiliza.
“Akasema siku hizi kukupata ni shida,
ila naweza kumwambia chochote atanisaidia. Ukweli sikuwa na jinsi Jack. Nikijua
Ibra ni mtu wako na anatufahamu tokea chuo nikamwambia kama tulikutana Uswiz,
tukalala wote, nimeshika mimba.”
“Subiri kwanza
Phina. Wewe unavyoiweka ni kama ulilala na mimi usiku kuchwa na wakati bado
ilikuwa mapema tu. Na baada ya pale nilikwambia wazi kabisa, nimefanya kosa.
Sikutakiwa kulala na wewe kwa kuwa mimi nimeoa, nampenda mke wangu. Nimefanya
kosa ambalo sitataka lijirudie tena. Uondoke urudi chumbani kwako. Nilikuacha
unavaa Phina! Nikapitiwa na usingizi. Lakini nashangaa kukuta picha ulizopiga
na mimi tukiwa tumelala kitandani! Imekuwa kama ulinitega makusudi!” Jack akasikika kulalamika.
“Mimi nakupenda
Jack. Na hilo unalijua tokea chuoni.” “Na ndicho ulichoniambia hata siku ile
uliponifuata chumbani kwangu. Ukanilainisha kwa maneno mengi, akili imekuja
kurudi nimesha msaliti mke wangu! Na wewe nilikwambia ni kosa! Ni kwa nini
unipige picha bila idhini yangu?” “Nahisi ni kutaka kutunza kumbukumbu yetu,
Jack.” “Kumbukumbu yetu unayoitumia kuniangamiza na kuisambaza kila mahali
ukinichafua! Unamfuata mke wangu nyumbani na kumuonyesha picha chafu vile!”
“Hakika ni Ibra. Sio mimi. Ibra ndiye aliyeanzisha hilo na ndiye aliyempa
Sabrina.”
Phina akajitetea.
“Kwanza hakuwa
akiamini kama kweli unaweza kuwa umelala na mimi. Akasema wewe ni muadilifu
sana, huwezi ukalala na mwanamke mwingine ukiwa kwenye mahusiano.” “Lakini
hivyo sivyo anavyosema! Hata kwa Sabrina amemwambia tofauti!” “Na mimi siku ile
pale nyumbani kwako nilishangaa. Ni kama alinibadilikia! Lakini katika kupinga
huko ndio nikamwambia ninao ushahidi, mimi nililala na wewe tulipokuwa nchini Uswiz.
Akitaka aje nimuonyeshe. Nilikuwa nimekasirika Jack, Ibra aliniona mimi muongo.
Nakuzushia tu! Ndio ikabidi kumwambia ninao ushahidi. Ibra aliendesha mpaka
kwangu kuja kuona huo ushahidi. Nikampa simu yangu akawa anaangalia zile picha
zetu. Sasa wakati namwandalia kinywaji niliporudi akaniambia eti ameona
ajihamishie zile picha. Nikamuomba asije kuzisambaza. Akaniambia nisiwe na
wasiwasi.”
Phina akaendelea.
“Sasa juzi
mchana akanipigia simu kuwa amejua pakukupata kwa urahisi, atanisindikiza. Ndio
akanifuata baada ya kutoka kazini, akaniambia twende. Mimi sipafahamu kwako, wala
kwake Ibra. Kwahiyo hata sikujua ni wapi tunaelekea. Nikashitukia tunaingia
nyumba ambayo Sabrina yupo, Ibra akaanza hasira kwa kina Felix na Ney na
kuniambia niseme. Sasa mimi nikasita kuzungumza pale kwa kuwa niliona
hayawahusu pale, ila Ibra yeye akasema kila kitu, nikashangaa ametoa na picha
kabisa. Wakaanza kutukanana na Felix. Felix na Ney wakaanza kumchangia kwa
maneno, wakaanza kurushiana ngumu nafikiri msichana wa kazi akaenda kuita
mlinzi au sijui mlinzi alisikia fujo, ndio tukatolewa wote pale. Ila sio mimi.” Phina akajitetea.
“Sio wewe ndio
ulikwenda Ustawi wa Jamii ukidai haki yako? Wakati mimi sijakataa chochote na
wala sikuwa nikijua kama umeshika mimba! Kwa nini unafanya hivyo Phina?” “Ni
Ibra. Mungu wangu ni shahidi, Jack. Ibra ndiye ananipelekesha mpaka
ananiogopesha! Amejawa na hasira na ninahofia atatumia zile picha vibaya. Ila
tulipotoka pale Ustawi wa Jamii, nilimwambia, atulie, tupunguze spidi.
Tunawasha moto bila sababu. Akasema yeye anaijua nguvu ya kina Msindai.
Wanaweza kunizima nikapotea hivihivi. Mimi nimemwambia kuanzia sasahivi
sitataka kwenda naye popote. Nitakusubiria wewe.” “Labda nikuulize Phina. Baada
ya kushika hiyo mimba, unatarajia nini kutoka kwangu? Maana wewe unajua kama
nimeoa na nampenda Sabrina. Nilichofanya kwako nilikosea. Na nilikwambia Phina!
Sijakurubuni. Sasa wewe ulitaka nini au unatarajia nini kutoka kwangu?” Kimya.
“Tafadhali kuwa
muwazi. Unachotaka ni pesa?” “Unajua sina shida na hela Jack. Mimi pesa ninayo.
Ninachotaka ni umtambue kuwa huyu mtoto ni wetu. Hilo tu. Ujue ni damu yako na
uhusike kama baba, kama hivyo unavyofanya kwa watoto uliozaa na Sabrina.” Jack akahisi giza. “Sitaki mwanangu aje afichwe. Nataka atambuliwe kuwa na yeye
ni Msindai.” Phina akaongea bila kuuma maneno. “Sasa
hii fujo unayofanya ukizunguka na Ibra, tutakuwa na mahusiano gani na huyo
mtoto? Mimba yenyewe hata miezi miwili bado, unafanya fujo nchi nzima!? Unataka
mimi niharibikiwe ili iweje? Unaungana na Ibra kuniangamiza huku unataka mtoto
aje akute baba! Unataka akutane na baba niliyeshindwa majukumu yangu, sina
kazi, siwezi hata kusaidia siku anapohitaji msaada wangu!” “Nimeongea na Ibra. Na nitamuomba leo tukutane tuzungumze ili
afute hizo picha aache kuzisambaza.” Phina akasikika kunyenyekea.
“Nahisi umeshachelewa
Phina. Mimi na wewe hatukuwahi kushindwana jambo. Hata tulipomaliza chuo, japo
nilijua hatutakuwa wote, lakini nilihangaika mpaka ukapata kazi inayokuingizia
pesa nzuri mpaka sasa!” “Na mimi hilo sijasahau Jack. Na nilikwambia sitakuja
kusahau huo wema wako.” “Sasa kwa nini katika hili mimi umenifanyia ubaya?” Jack akauliza kwa kuumia
kama aliyebakwa.
“Ulifungia simu
zangu Jack! Ulitegemea nini?” “Wewe ulitegemea nini Phina? Eti kwa kuwa
tumelala wote mara moja, basi tuanze kuchat na kurudisha mawasiliano kama vile
sijaoa? Hivi unajua shida niliyopata baada ya kufanya lile kosa?” “Mimi sijui
Jack.” Phina
akajibu kinyonge akisikika wivu, kana kwamba hakujua analala na mume wa mwenzie.
“Nina hukumu yakupitiliza. Sabrina amekuwa muaminifu
sana kwangu. Mno. Sikutakiwa kumtenda nilichomtenda.” “Kwa hiyo unanilaumu?”
“Nilikwambia tokea mwanzo, kuwa mimi ndiye niliyefanya kosa. Sikukubaka,
hukunibaka. Nilikosa. Hapakuwa na jinsi baada ya pale eti tukaendeleza
mazungumzo kati yetu, kwa ile hukumu niliyokuwa nayo, Phina.”
“Sasa kuanzia
sasahivi nikiwa na shida nakupataje?” Phina akauliza kwa hasira. “Shida gani tena Phina na wewe umesema huna shida na pesa
unachotaka ni mtoto akizaliwa niwe na mahusiano naye?” “Kwa hiyo ndio
sitakusikia tena mpaka nijifungue?!” Phina akauliza kwa kuhamaki. “Nimetoka
kukuuliza Phina. Unataka nini kutoka kwangu? Ni nini unatarajia kutoka kwangu? Kumbuka
nimeoa, nina familia na nina majukumu ya kazi pia. Ulitaka nifanye nini na huyo
mtoto bado hajazaliwa?” “Kwa hiyo unaamini kama ni mtoto wako?” Ikawa
swali la kama kumtisha tena Jack. Akatae, aanzishe kingine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila Kazi Na
Malipo Yake. Hakuna Kunakopandwa, Kusivunwe Hata Magugu!
Makosa! Makosa!
Makosa!
Nani Atavuna
Nini?
Usikose Muendelezo…
0 Comments:
Post a Comment