Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 62. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 62.

Sabrina alikuwa amekufa ganzi miguu haiwezi kusogea. Akili imegoma hata kufikiria! Masikio yakawa hayasikii kabisa, akawa amepigwa na bumbuwazi. Alikuwa akiona ni kama dunia iliacha kuzunguka kwa muda. “Dada, mtoto analia! Ameamka, nimembadilisha, ila anaendelea kulia, nahisi ni njaa.” Ikabidi Phina amshitue tu, maana alikuwa kama hayupo pale wakati kilio cha mwanae kilikuwa kikisikika kwa sauti ya juu tu. Ndipo akagutuka na kumsikia Brandon akilia. Akasimama hapo kochini na kukabidhiwa mwanae. Hiyo nyumba ilikuwa imejaa watoto, kila akipita yupo mtoto. Akamchukua na Brayan aliyeanza na yeye kumlilia akiwa anaelekea chumbani. “Huyu atakuwa na usingizi Phina. Naomba uje umbadilishie nguo zake za kulalia hapa chumbani wakati nikimnyonyesha mdogo wake. Akilala ndio uje umchukue.

Ney&Felix.

L

ilikuwa ni tukio ambalo hata wao hawakuwa wamelitarajia hata kidogo.  Walichokuwa wamejiandaa nacho ni wakati nzuri wakukutana baada ya majukumu mengi ya mjini kwa Ney, Felix na Jack. Pamoja na kupotezana kwa muda mrefu na Ibra. Japokuwa hao wawili walikuwa wakifanya wizara moja na Jack, lakini Jack alirudi kuwa bosi wao tena. Busy, kukutana naye si kama ilivyokuwa chuoni. Ibra yeye alipotea hawakumsikia kwa muda mpaka alipompigia Felix yeye mwenyewe. Ila wote walichukulia ni ubusy wa maisha. Kila mmoja mjini kuhangaika na maisha, wakajua na yeye yupo busy na wao wakawa busy. Amani ikaendelea kila mmoja na majukumu yake.

Walipomaliza Chuo wote hawakupangiwa Wizara ya Fedha hapo Dar, kama walivyokuwa wakitamani. Wao watatu walikwenda kuripoti na kufanya kazi kwenye vituo vyao vya kazi japo wawili hao hawakupenda, lakini si Jack. Felix alipangiwa Gundu. Watoto hao wajiji walikuwa wakimcheka sana maana hawakujua hata Gundu ilipo. Lakini Felix alikwenda. Akafanya kazi miaka miwili ndipo akapata uhamisho kurudi Dar. Ibra yeye alipangiwa Mpiji, alikasirika nakuona amedharauliwa. Hakutaka hata kwenda. Akajiingiza kwenye biashara. Neema yeye akapangiwa Mkuranga. Akawa na kazi nyingine ngumu ya kwenda asubuhi Mkuranga na kurudi kwake Chang’ombe usiku kwa karibia mwaka. Haikuwa rahisi hata kidogo, lakini alikusudia kubaki Wizarani akiamini atakuja kurudi tu alipopataka. Akaendelea hivyo bila kulalamika na kweli akaja kufanikiwa kurudi jijini. Jack na yeye alipangiwa Singida ila yeye ni kwa kutaka kwake. Kaka yake Junior ndiye aliyemsaidia mpaka akapangiwa huko, kwani alitaka kwenda Singida kupafahamu zaidi. Alikuwa na malengo nako ya Ubunge kama hivyo.

“Hakika Jack atanilaumu sana.” Felix akampigia Ney mara tu walipoondoa magari yao hapo nyumbani kwa Msindai kwa kufukuzwa na askari wanaolinda hapo. “Ila Jack amefanya uchafu wa kupitiliza. Hakika sikumtegemea!” “Yeye ni binadamu bwana! Kukosea kumo. Halafu si umeona Phina mwenyewe alivyozidi ku...” “Acha ujinga Felix. Unatetea nini? Kwa hiyo atakuwa akilala na kila mwanamke aliy..” “Basi na sisi tusianze kugombana Ney. Nishauri chakufanya.” Akamtuliza maana na Ney alishaanza kuwaka. “Kwa kuwa wewe ndio umemletea ile fujo mle ndani na kumsogezea janga kwa mkewe, muwahi kabla hajarudi nyumbani.” “Acha masihara Ney!” “Kumbe! Wewe unataka afike pale kwake na kukuta ile hali wakati sisi tulijua!” “Aisee kweli.” Felix akaona ampigie simu Jack.

Mjumbe Hauwawi.

J

ack alipokea simu ya Felix bila yakuchelewa. “Nakaribia nyumbani mzee, mbona huna subira?” “Aisee egesha pembeni, usiende nyumbani kwako kwanza mpaka tuzungumze.” “Kuna nini wewe?” “Acha ubishi Jack. Hili unatakiwa kulisikia ukiwa huendeshi kaka.” Jack akiwa haelewi akatafuta mahali pazuri na kuegesha gari. “Kuna nini Mkuu?” “Wewe ulipolala na Phina, mkiwa Uswiz, ulijua kama anakupiga picha?” Jack alishindwa hata kujibu. Felix akaona aendelee. “Sasa ile ya Ibra kunitafuta ili nimlete kwako ilikuwa njia ya kupajua kwenu, ili waje na Phina maana Phina anasema umemfungia simu zake zote hakupati ili kukwambia ni mjamzito. Hapa tunapozungumza mkeo amepewa picha mlizokuwa kwenye chumba mlicholala huko Uswiz na Phina. Mimi na Ney tulikataa kuziangalia, ila ameachiwa mkeo. Hapa tumetolewa na askari wako tena kwa mtutu maana tulianza kushikana na Ibra. Alikuwa akikutukana matusi mabaya mpaka wafanyakazi wako wote wa nje na ndani na watoto wakaja pale sebuleni wakawa wakitusikiliza, ikabidi kumtuliza kwa ngumi.” “Mungu wangu!” Hivyo ndivyo Jack alivyosikika.

“Ibra mshenzi sana. Amenitumia mimi kutimiza azma yake! Halafu anaonekana anatumindi sisi kuwa Wizarani pamoja wakati yeye mwenyewe alikataa kafanya kazi serikalini, sasahivi anaona tunamdharau! Anatukana kama mwehu! Na anawaambia wanawake zako kuwa huo ndio mchezo wako. Ukiwa na Phina unakuwa na Sabrina, ukiwa…” “Sio wanawake zangu. Mke wangu ni mmoja tu, Sabrina. Phina ilikuwa mara moja tu na hata yeye nilimwambia nilifanya kosa na.…” “Sasa hapo kaka umeangukia pua. Hiyo mara moja naona ukafanikiwa na mtoto.”

“Phina ni mjamzito na mkeo kapewa mpaka kopi za ultrasound. Na amesema yupo tayari kufanyiwa DNA hata kesho ili kuhakikisha kuwa mtoto aliyebeba ni wako.” “Mungu wangu!” “Na naona ujiandae kiongozi. Hayo madai wanayokutaka, mpaka nikamwambia Ibra anataka kutajirika kwa jasho lako! Amemwambia Sabrina, mtoto wa Phina anataka akue kwenye mazingira mazuri kama yale wanayokulia watoto wako pale nyumbani kwako na Sabrina. Halafu Jack.” Felix akaendelea kufikisha ujumbe.

“Wamekupa siku tatu tu wanataka wakusikie. Tena wakusikie na mipango inayoeleweka kwa mtoto wako na Phina lasivyo wamesema wanakupeleka Ustawi wa Jamii, na utawasikia magazetini wakidai haki yao. Nimeona nikuwahi usije kufika nyumbani, moto ukawaka, ukashindwa kuupata huu ujumbe nakushindwa kuutekeleza kwa wakati waliokupa, halafu wakakuchafua magazetini. Fanya ufanyalo hili ulimalize kinyumbani, kaka. Mtafute Phina.” Kimya. Jack akishindwa hata kujibu. Felix akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jack na yeye akapata kama hali iliyompata Sabrina. Alibaki hapo garini zaidi ya lisaa, hajui alipo, hajui chakufanya. Ila yeye aliona tofuati. Dunia nzima ilikuwa ikizunguka kwa spidi ya ajabu sana mpaka akafunga macho ili kujaribu kujituliza. Napo haikusaidia. Huko mawazoni ikawa mbaya zaidi. Kila kitu kikawa kimepinduka. Juu chini na kikienda kwa mwendo kasi kuliko gari ya mashindano. Akafungua tena macho. Alibaki pale hajui chakufanya mpaka saa nane usiku wa giza nene na saa mbili alikuwa akitakiwa tena ofisini.

Akajua muda huo Sabrina atakuwa amelala. Akarudi nyumbani. Akakuta ile bahasha pale sebuleni kwenye kochi. Akaichukua mikono ikitetemeka kama anayeiba akihofia kukamatwa, kumbe inamuhusu. Kweli Phina alikuwa amempiga picha wakiwa wameonekana kitandani, ila yeye ndio alikuwa amelala usingizi kabisa, pembeni ya Phina. Jack akazirudisha kwa haraka kwenye bahasha yake na kwenda kuziweka kwenye gari yake. Akarudi kukaa hapo sebuleni. Aliposikia mtoto wao akilia, akanyata na kutoka kabisa hapo ndani na kurudi kazini muda huohuo akijua Sabrina ataamka tu.

Siku hiyo Jack hakusikika na yeyote hata kwa salamu kutaka kujua familia yake inaendeleaje. Aliingiwa hofu kwa Sabrina, alishindwa hata kutaka kumsikia. Aliogopa hata kuiona sura yake! Alikuwa akitetemeka kila akimkumbuka Sabrina. Alikaa ofisini siku nzima na wala Sabrina hakumtafuta.

Adui Wa Mtu.

K

inyume na walivyosema nyumbani kwa Jack, hata mbele ya Felix na Ney, hata siku tatu walizompa Jack hazikutimia, jioni ya siku inayofuata, wawili hao wakatokea ofisi za Ustawi wa Jamii. Huko nako Ibra akazungumza mengi mno akisema wanakusudia kumshitaki Jack kwa kumtelekeza Phina akiwa amebeba mtoto wake. Siku hiyo ilivyo mbaya kwa Jack, akitaka kufikiria ajue ni jinsi gani atalikabili hilo, akaamua kwa siku hiyo afunge simu kabisa atulie. Kumbe na watu wa Ustawi wa Jamii wakawa wakimpigia simu bila mafanikio. “Na nyinyi mmekuwa mashahidi! Si mmeona hapatikanini kwa simu? Sisi tunaenda kufungua mashitaka polisi.” Ibra akazidisha jazba.

 “Jamani mimi nafahamiana na mama Msindai. Acheni nizungumze naye kwanza kabla haya mambo hamjafikisha mbali. Nipeni muda tafadhali.” Mama mmoja mtu mzima ambaye naye walimkuta tu hapo kwa bahati, akaingilia. “Tusipowasikia na nyinyi mpaka kesho, sisi tunakwenda mbele, kudai haki. Maana najua kwa kuwa wao wameshika hii nchi basi mnajisikia kuwabeba tu.” Ibra akatishia. “Wala hatutafika huko. Usiwe na wasiwasi.” Wakaondoka.

Kwa Mama Msindai.

Ilishakuwa jioni, akaanza kwa kumtumia ujumbe mama Msindai. ‘Mama Msindai, najua unaweza usiwe unanikumbuka kwa karibu. Lakini nina jambo zito, naomba tafadhali tuzungumze kwa haraka.’ Hapohapo mama Msindai akampigia. “Nazungumza na nani?” Huyo mama akajielekeza lakini mama Msindai akashindwa kabisa kumkumbuka. Lakini akamwambia anamfahamu kupitia mama Mkapa. Kuna kipindi walikutana kwenye washa aliyokuwa ameandaa mama Mkapa mwenyewe. Akamtambulisha kwake ndipo akamuomba namba kipindi yupo waziri wa afya. Lakini hakuwahi kumtafuta.

“Yaani leo nikiwa kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii niliposikia jambo linalokuhusu, nikasema ulinipa namba yako kwa heshima, sio vibaya leo nikaitumia kwa jambo la msingi, kukusaidia!” “Jambo gani hilo?” “Ndicho nataka kuzungumza na wewe kwa kuwa nimewaambia mimi nakufahamu, nimeomba kuzungumza na wewe kabla mambo hayajapelekwa mbali kwa kuwa na mimi ni mzazi.” “Kuna nini, mbona husemi!?” Mama Msindai akasikika kupotezewa muda.

“Amekuja msichana, amejitambulisha kwa jina la Phina, anasindikizwa na kijana, aliyejitambulisha kwa jina la Ibra, akasema ni kama kaka yake Phina, tokea chuoni. Na kwa aina ya mazungumzo yao, inaonekana walisoma na kijana wako huyu Naibu Waziri, Jackson Msindai.” “Wote hao wawili nafikiri ndio hao ninao wafahamu. Ibra ni rafiki wa karibu sana wa Jack.” “Mmmh! Si kwa alichokisema anakusudia kukifanya endapo Phina hatapewa haki yake.” Hapo akamtia wasiwasi zaidi mama Msindai.

“Hapo unanichanganya!” “Inavyoonekana Phina yupo kwenye mambo ya protocal, sijui mipango huko serikalini.” “Nafahamu, Jack alimuomba kaka yake amsaidie kumtafutia hiyo kazi, ndio akapewa hiyo nafasi. Kuna nini?” “Anasema kama miezi miwili iliyopita, na yeye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wameandaa safari ya Naibu waziri wa fedha na kamati yake walipokwenda nchini Uswiz kwenye kikao. Anasema Jack alifika huko akakutana naye, wakalala chumba kimoja mpaka asubuhi, nafikiri mpaka hapo wewe mtu mzima umeelewa kilichoendelea kati yao.” Mama Msindai kimya mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi. Huyo mama akaendelea.

“Sasa Ibra analalamika anasema ilipofika asubuhi kijana wako akiwa amemtumia Phina usiku kuchwa, eti asubuhi ndipo akamfukuza, tena vibaya sana. Na kuanzia hapo akawa amemfungia simu zake. Hata Phina alipotaka kumwambia alishika mimba, hakuwa akimpata Jackson.” Mama Msindai kimya.

“Mama Msindai, nashauri hili jambo mlimalize kinyumbani. Hawa vijana wanaonekana wapo tayari kuzungumza na vyombo vya habari wakihofia usalama wa Phina kwamba ikitokea anajulikana anadai haki yake chochote kibaya kinaweza kumpata kikisababishwa na nyinyi.” “Kwanza kuna uthibitisho gani wa hicho anachokisema huyo Phina?” Mama Msindai akauliza akisikika kumtetea mziwanda wake. “Mama Msindai, hawa vijana wamejiandaa aisee. Inaonekana huyu binti alipiga picha za kutosha tu wakiwa wamelala na kijana wako huko hotelini nchini Uswiz. Na zina tarehe mpaka muda.” “Kwa hiyo ndio inamaanisha ni mimba ya Jackson!?” Mama Msindai akazidi kuhoji kwa hasira.

“Ndio nilikuwa nikienda kwenye point ya pili. Wana picha za ultrasound za huo ujauzito ambao una majuma saba unakwenda nane.” “Sasa picha hizo ndio zitathibitisha kuwa mtoto ni wa Jackson!?”  Mama Msindai akazidi kuhoji. “Ndio nilikuwa nikiendelea kuzungumza! Mimi nimewaomba muda wa kuzungumza na wewe ili kukusaidia na mimi nikiwa mzazi kama wewe tu, mwenye vijana kama wako. Sina nia mbaya. Ni mjumbe niliyejitolea ili tu kuwatuliza pale Ustawi wa Jamii, ili na nyinyi mjue jinsi ya kujipanga.”

“Nilitaka kuwatuliza tu, maana nilikuwepo hapo wakati wakivuta watu kwa kuongea kwa jazba, zaidi yule kijana anayesema ni kaka yake Phina, Ibra. Amesema yupo tayari Phina kupimwa DNA hata kabla mtoto hajazaliwa. Mimi nikamuuliza anayajua madhara ya kumchokonoa huyo mtoto huko tumboni ili kufanyiwa hiyo DNA kabla hajazaliwa? Akasema ameshafanya uchunguzi wake, ameshazungumza na Phina na yeye Phina ameelewa. Wameshajua njia salama za kufanya hiyo DNA ambayo haitamdhuru huyo mtoto anayemuita Msindai. Haitakuwa hapa nchini, amesema siku hizi Jackson anayo pesa. Watataka njia salama kwa mtoto wao. Na kama mkikata apelekwe nje ya nchi kwa hivyo vipimo ili kuthibitisha kuwa ni mtoto wa Jackson, basi amesema wataomba mahakama imsaidie Phina. Narudia tena, mimi ni mjumbe tu mama Msindai. Nimeona nikusaidie kabla mambo hayajakwenda mbali. Maana wanalalamika kwamba walianzia nyumbani kwa kijana wako, hawa…” “Unamaana kwa mkewe!?” Hapo mama Msindai akashituka sana.

“Walivyosema walimkuta mkewe, kijana wako hakuwepo. Wamezungumza na mkewe na kumuachia maagizo yote pamoja na hizo picha. Huyu Ibra anacholalamika ni kuwa inamaana Kijana wako amewadharau. Amepata ujumbe lakini bado ameshindwa kuwatafuta. Wao walitegemea hata usiku uleule angemtafuta Phina wazungumze, lakini imekuwa kimya. Wao wanahesabu kuwa ni dharau. Ndio maana wamekuja hapa na wapo tayari kwenda mbele ya haki zaidi. Ni hilo tu.” “Nashukuru. Asante. Nikutakie jioni njema.” Akakata.

Kwa Mzee Msindai.

M

zee Msindai akiwa katikati ya kuona wagonjwa wake ambao ni watoto, akaona simu ya mkewe. Kabla hajatoa salama. “Saa mbili kamili, nataka kukuona hapa nyumbani wewe na watoto wako wote bila kukosa.” “Leo nina wagonjwa mpaka saa nne, mama! Kwa nini…” “Na Msindai, namaanisha saa mbili kamili na watoto wako wote. Nisipomuona mtoto hata mmoja hapa!” Mama Msindai akaweka mkwara. “Junior ndio amerudi leo, mama. Hata nyumbani hajakwenda. Kwa nini hicho…” “Hawa watoto wananidharau mimi! Junior hapokei simu zangu lakini anazungumza na wewe! Na Jacinta hivyohivyo! Jackson ndio simu zake zote hazipo hewani. Msindai onya watoto wako!” “Saa mbili na nusu tutakuwa hapo mama. Lakini wewe ni mzima?” Simu ikakatwa.

Kabla hajasahau akampigia simu Jacinta haikuita hata mara mbili, akapokea. “Baba mzazi!” “Naomba muunganishe na Junior.” Mzee Msindai akaendelea na mtoto aliyekuwa naye hapo akimuhudumia. Jacinta akamuunganisha kaka yake kwa haraka. “Mama yenu ameagiza saa mbili na nusu amuone kila mmoja wenu pale.” “Kuna nini tena baba jamani! Mimi ndio nimerudi tu, hata sijamuona mke wangu!” Junior akalalamika. “Linaonekana ni jambo la msingi hawezi kusubiri. Na Jacinta.” “Nipo baba.” “Jackson hapatikaniki kwa simu. Naomba taarifa zimfikie, na hakikisha saa mbili na nusu yupo nyumbani.” ‘Sawa baba.” Jacinta akakubali. “Sasa mimi nipo na kijana mzuri sana hapa. Anataka niendelee kuzungumza naye. Nitawaona nyumbani.” Hiyo simu nayo ikakatwa. Junior akajua ndio ni lazima kuhudhuria kikao.

Kwa Sabrina.

Akiwa ananyonyesha mwanae, ukaingia ujumbe kutoka kwa mama mkwe. ‘Kuna kikao cha familia saa mbili na nusu usiku wa leo. Tafadhali fika bila kukosa.’ Sabrina akasoma na kutulia akifikiria. Akataka asiende, lakini rohoni akasukumwa kwenda. Akajibu. ‘Sawa mama.’ Hapakuwa na ujumbe mwingine. Na yeye akatulia tu. Mpaka hapo hakuwa amemuona Jack.

Bahari Imetibuka.

K

wa makusudi kabisa, Sabrina akachelewa kwenda kama kwa dakika 10 hivi hakutaka awahi hapo ajikute na huyo mama peke yake, wengine hawajafika. Kwa kuwa aliwajua familia hiyo ni watunza muda, akajua baada ya hizo dakika kumi, wote watakuwa hapo. Dereva akamshusha nje. Akakuta magari yote mpaka la Jack. Akaingia. Tokea yupo mlangoni alikuwa akimsikia mama Msindai akigombesha wanae. Sabrina akajivuta taratibu alipoingia tu hapo mzee Msindai akamuwahi. “Karibu mama.” “Asante baba. Shikamoo.” “Marahaba. Umeacha wapi wenye mji?” “Nimeona nikija na ile timu yote, hatutasikilizana hapa. Brayan siku hizi anapatwa wivu akiona nimemshika mdogo wake. Analia na yeye anataka nimbembe.” “Amepokonywa ziwa je! Lazima alie wivu.” Akadakia Jacinta na kufanya kidogo atulie.

“Wengine wote shikamooni. Mama samahani nimechelewa kidogo.” “Hamna shida tunaelewa. Na wala hujachelewa sana. Maana nilikuwa nikizungumzia swala la mawasiliano. Naona kuna kupuuzwa.” “Kwa hilo tumelielewa mama. Na tumeomba msamaha.” “Hamjaomba msamaha. Acheni kunifanya mimi mtoto mdogo. Mnapuuzia simu zangu halafu..” “Sabrina mama, kaa. Kaa chini.” Mzee Msindai ikabidi aingilie. Jack alikuwa ameinama.

“Asante.” “Karibu Shem. Umetukuta katikati ya kikao. Karibu sana.” Akaenda kukaa pembeni ya Jacinta ambako kulikuwa na nafasi, Jack alikuwa ameinamia magoti, anachezesha mguu mmoja kwa wasiwasi. “Mama, samahani kwa kutopokea simu. Nilikuwa katikati ya mambo mengi. Nimetua tu nchini na kukimbilia mambo ya ofisi hata nyumbani sijafika.” “Mimi nilikuwa na vikao siku nzima. Na asubuhi pia natakiwa kuwahi Pugu. Hivi itabidi kuwahi kuondoka.” “Muongo Jacinta. Anachaguaga simu za kupokea. Tunakujua sana tu.” Jena akaingilia. Jacinta hata hakumjibu. “Kwani mimi simjui! Anachagua simu ipi apokee na kwa wakati wake yeye ndio anaweza kurudisha simu uliyompigia.” “Samahani mama.” Jacinta akamuwahi ili asiendelee kulalamika.

“Wala humaanishi! Unanifunga mdomo tu ili nifanye haraka uondoke.” “Mtoto ameomba msamaha mama, si..” “Hata iweje hutaacha kumtetea Jacinta, wewe! Hata kama ana kosa, basi unaona bora wewe ubebe kosa lake yeye aachwe. Lakini hivyo unavyofanya Msindai si sawa.” Mzee Msindai akanunua ugomvi. “Hawa watoto wananidharau mimi na wewe unajua, huwakemei! Junior anarudi tu hapa nchini anakutafuta wewe kukupa ratiba zake zote, mimi hajanijulia hata hali wakati hajawasiliana na mimi kwa muda mrefu sana!” “Nilikupigia simu juzi usiku mama! Labda kama umesahau.” “Juzi usiku ndio leo?” “Nimeomba msamaha mama yangu.”

“Hata mimi naomba tena msamaha mama. Halafu nina swali.” “Jacinta wewe mtoto!” Mama yake akamnyoshea kidole kumuonya kwa ukali. “Jamani baba!” Jacinta akamgeukia baba yake akitaka tena utetezi. “Sio ungemsikiliza swali lake kwanza!” Kama kawaida yake hapo mzee Msindai akaingilia tena. “Najua swali lake. Hapa ni nyumbani kwangu. Mimi ndio nimewaita. Naongoza mimi kikao. Sitaki kuulizwa kama hili ndilo nililowaitia. Nachagua ni wapi nianzie na wapi nimalizie.” “Kuwa huru mama. Hapa kwako na sisi watoto wako, lazima tukusikilize.” Jena akawakera kwa makusudi. Sabrina kimya. Alishaijua hiyo familia. Akabaki ametulia tu. Jacinta akajirudisha nyuma, akatulia. Mama Msindai akalalamika mpaka akamaliza.

“Sasa tumepata tatizo linaloonekana limekwenda mbali tena kwa kasi. Nishapata simu zaidi ya tatu kwa muda mfupi tu. Inaonekana inasambaa vibaya sana.” Hapo wote wakaongeza umakini. “Jack ameingia matatizoni.” Hapo akamuumiza Sabrina. Kwa jinsi alivyoongea, ni kama ilikuwa ajali! “Matatizo gani!?” Akauliza mzee Msindai na wote kumgeukia Jack. Alionekana amejawa wasiwasi haswa, mguu anachezesha bila kutulia.

“Na katika hili lazima kusimama kwa pamoja. Sisi wote tuwe pamoja. Nikimaanisha mpaka Sabrina anatakiwa awe ukurasa mmoja, na asimame upande mmoja na Jack, ili kulinusuru hili jambo “Naomba muache Sabrina, mama.” Jack akaingilia. “Kama ungekuwa unataka kumlinda tokea mwanzo, usingefanya umalaya hovyo.” Hapo akamtibua mama yake. “Ulipokuwa ukilala na wanawake bila kinga, ulitegemea nini?” “Ni bahati mbaya mama! Sio kwamba ni kitu nilipanga ndio kikatoke!” Jack akajiteta. “Twende taratibu. Kuna nini kinaendelea!?” Akauliza mzee Msindai.

“Nimetoka kuzungumza sasa hivi na mama Mkapa. Yani hii habari imeenea na yeye amenipigia simu akimiambia lazima tukae kama familia tulizungumze na tuwe ukurasa mmoja. Phina huyo aliyepewa mimba na Jack, na Ibra huyo anayemsindikiza Phina kila mahali, wamekusudia kumuangamiza Jackson kabisa. Walianza jana usiku nyumbani kwa Jack mpaka wakampa mkewe uthibitisho wa Jack kuwa na huyo Phina huko Uswiz walipokuwa wamelala mpaka akashika hiyo mimba. Na picha hizo za Ultrasound za ujauzito zinazoonyesha umri wa huo ujauzito kulinganisha na tarehe za kwenye picha zao huko Uswiz. Sasa aliyenitafuta wa kwanza ni mtu aliyemsikia Phina na Ibra huko Ustawi wa Jamii wakilalamika kuwa Jack amefungia simu za Phina zote baada ya kulala naye.” Mama Msindai akaeleza yote mpaka mwisho.

“Wanaonekana wanasambaza haya maneno makusudi eti wanahofia tusije kuwaziba mdomo.” “Tafadhali sana mama J. Siku nyingine unaponiitisha kikao cha dharula na watoto, kiwe kikao cha dharula kweli.” Mzee Msindai hapo akawaka mpaka akashangaza wanae. “Hii ni dharula Msindai!” “Dharula ni ile niliyoacha watoto wagonjwa, ili kuja hapa kuzungumzia starehe za mtu mzima huyu aliyeamua kuishi kama mnyama tu!” “Usiseme mtoto ni mnyama, Msindai! Hili jambo limetoea. Bahati mbaya zipo na Jackson sio wa kwanza. Mtoto atakayezaliwa ni Msindai kama kina CJ. Atataka kujua familia yake na kukuzwa kama watoto wote wa wakina Msindai humu ndani, ajue ndugu zake na asili yake.” Hapo akawa kama amewasha taa ambayo hakuwa hata akiifikiria kwenye fahamu za Sabrina. Akakaa sawa akimtizama mama Msindai anachokizungumza.

“Na Phina mwenyewe anaonekana yupo tayari kuwa mmoja wa hii familia. Mtoto wake awe Msindai kwelikweli. Kwa hiyo lazima kuwa upande mmoja kujua jinsi ya kulikabili hili. Kulimaliza kifamilia.” “Narudia tena mama J. Umenikosea na hili sitalinyamazia. Hatuwezi kuokoa kazi ya mtu ambaye amekataa kuwajibika kwenye jamii, huku tukiharibu kwa wengine. Uliponipigia simu nilikwambia kabisa, ninao wagonjwa wakuwaona mpaka saa nne usiku. Inamaana usiku huu sisi tukiwa hapa tukijadili starehe zake huyu aliyechagua kuwa mbinafsi, akifuatisha tamaa zake za mwili kama mnyama tu, bila kujali familia yangu nzima ya Msindai, yupo mama anahangaika usiku huu na mtoto mgonjwa! Nimerudisha watoto wagonjwa kwa ajili ya upuuzi huu! Isiwahi kurudiwa tena.” Hapo kila mtu akajua kwa mara ya kwanza mzee Msindai amekasirika kupitiliza. Hakuna aliyewahi kumuona hivyo, hata mama Msindai hapo akanyamaza.

Akanyanyuka, akachukua funguo zake za gari na kutoka. Pakazuka ukimya. “Jamani, nilikuwa safari kwa muda mrefu, sijamuona mke wangu. Nimemuomba anisubiri, asilale mpaka nifike. Naomba na mimi niwahi nyumbani.” Junior akasimama. Hiyo haikuwa ishara nzuri kwa Jack hata kidogo. Junior hajui kumnawia mtu mikono. Inamaana katika hilo hakuwa na la kusema. “Na mimi kama nilivyosema mwanzoni, kesho natakiwa PUGUUUU!” Jacinta naye akasimama.

“Kwa hiyo mnamkimbia mtoto?” “Kwa jinsi nilivyokusikiliza tokea mwanzo, wewe mama hutahitaji msaada wetu hata kidogo. Unaonekana ushafikiria hiki alichofanya Jack. Umeshamtetea, usha.” “Sija..” “Si umetaka kusikia? Basi subiri.” Jacinta naye akawa mkali gafla. “Mbele ya mkewe hapa, umesema yeye sio wa kwanza. Phina ametaka kuwa mmoja wa familia yeye na mtoto wake. Sisi tuwe ukurasa mmoja ili kuunga mkono hiki kitu. Kuna nililoongeza hapa au unataka sisi tubishe, halafu na wewe ubishe kwa hasira mwishoe wewe ndio uonekane mshindi, kwa kuwa kile ulichotaka kimekua?” Jacinta akauliza kwa ukali kabisa.

“Familia umesema ni yako. Umetoa muongozo kile unachotaka kifanyike, tena kwa baraka zako. Ulitaka wote tukwame hapa tukibishania starehe za mwanao huyo! Na kukusaidia tu, mimi sitaingia aibu kwa starehe za Jack, wala haitakuwa Junior. Junior anajulikana kwa kuthibitishwa na kila mtu, halali na mwanamke isipokuwa mkewe na ndio maana iliposikika tu mipango ya Max na mkewe, watu walinifuata haraka kuniambia wanataka kumuharibia kiongozi. Uungwaji mkono niliopata mpaka mimi mwenyewe nikashangaa. Watu wanajitolea kwa Junior kupita nitakavyokwambia wote mkaelewa. Linapofika swala la Junior mpaka mimi huwa nashangaa, na wala sihangaiki. Watu wanamuhangaikia mimi naletewa ripoti tu. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi juu yetu. Kila mmoja atabeba msalaba wake mwenyewe.” Jacinta akachukua pochi yake na kuondoka. Akafuata Junior, akatoka kwa haraka kama akimbie.

Akabakia hapo mama Msindai, Jena, Jack na Sabrina. Sabrina kimya. “Sasa wanazira nini? Kwani wao hawakosei! Wanajidai watakatifu!” Jena akaanza. “Hata wakizira huyo mtoto atazaliwa na yeye atakuwa Msindai tu.” “Na hilo ndilo nilitaka tuwekane sawa, lakini naona kama…” “Wewe mama usiyumbe. Maji yashamwagika, hayazoleki. Sisi nikuendelea. Mimi mwenyewe nitamtafuta Phina. Kwanza msichana mwenyewe mzuri yule. Moyo wake safi, hana shida. Nitazungumza naye na kumkaribisha kwenye familia. Hata babyshower ya mtoto mimi nita…” “Acha kuzungumza ujinga Jena!” “Ujinga ni upi kati yangu mimi niliyekubali ukweli bila shida au nyinyi mnayetaka kufanya mambo yakuzwe? Na kwa taarifa yako tu, kwa kadiri unavyojichelewesha kwenye kukubali ukweli, ujue unajiharibia mwenyewe. Pokea mtoto wako, tunza damu yako.” “Jena yupo sahihi.” Mama Msindai akadakia.

“Jamani wakati nyinyi mnapanga mipango ya Phina na Msindai mpya, naomba mimi nikaendelee na yangu. Ila naomba nitoke na Jack kidogo.” “Sasa unaondoka na Jack…” “Atarudi wala usiwe na wasiwasi Jena.” “Mimi sina wasiwasi ila..” Sabrina akachukua pochi yake wakati anataka kutoka, Jena akamuwahi tena. “Unadharau na utaona tutakachomfanyia Phina. Wewe si ulikuwa ukiringa kama vile ni mwanamke peke yako kwa Jack? Sasa Jack mwenyewe amekuonyesh....”

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Itaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment