Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 61. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 61.

Kwa Sabina.

Sabina akiwa ofisini kwake, siku ikiwa imeanza kama kawaida, akasikia ana mgeni mapokezi. Akatoka akiwa hana hili wala lile kumbe arobaini zake zimefika. Alipofika tu mapokezi akadakwa na askari. Wakamfunga pingu na kumwambia yupo chini ya ulinzi. Kabla akili haijakaa sawa, Sabina akavutwa vibaya sana na kupakizwa kwenye difenda ya polisi, watu wote wasielewe. Ni Sabina, mdada wa kuheshimika sana hapo kazini! Alipoingia tu garini akafunikwa kichwa asiweze kuona atakapopelekwa. Askari mmoja akaamuru pochi yake na vitu vyake vingine vyote viletwe hapo. Wafanyakazi wenzake wakasaidiana kukusanya vitu vyake vyote na kuwakabidhi hao askari lakini lengo ni kupata simu yake ili kujua mawasiliano yake na Tino. Walipojiridhisha kwenye hivyo vitu ipo simu yake, ndipo wakaondoka.

Gari ilitolewa pale kama amekamatwa jambazi sugu anapelekwa kufungiwa. Akiwa hajui ni kwa nini anakamatwa, maana ni kweli walijitahidi sana kuwa makini kwenye mipango yao wakijua wanasikilizwa, Sabina asijue watu wa Usalama wa Taifa wapo kila mahali na huwezi kuwatambua kwa kuwaangalia. Japokuwa alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni ya kutoka nje ya nchi, lakini walikuwepo pia watu wa Usalama wa Taifa wakifanya nao kazi wasiwajue. Na wenyewe walikuwa wakiendelea kumchota taratibu kujua kila kitu kinachoendelea na yeye alikuwa akisema kwa kujisifu, asijue alikuwa akijishitaki wakati wote.

Sabina alipelekwa sehemu na kufungiwa kwenye chumba, asijue alipo ila hofu. Aibu ya kutolewa vibaya sana mbele ya watu akiwa ofisini! Akabaki akitetemeka kwa hofu zaidi ile yakuvutwa na kutupiwa kwenye hicho chumba chenye giza, kikatili. Wakati amekaa hapo chini sakafuni, akaingia mtu na kuamuru taa iwashwe. Ikawashwa. Alionekana mtu mwenye mamlaka mpaka akamtisha Sabina. “Upo chini ya ulinzi kwa kosa la kula njama za kufanya uhalifu. Unajihusisha na mtuhumiwa anayeshikiliwa na makosa makubwa na hatari sana kwa jamii ikiwepo kusudio la kutaka kua. Njama ya kumuangusha kiongozi mkubwa sana, aliyeaminiwa na raisi wa nchi yetu. Kwa kuwa yeye ameshikiliwa yupo ndani, anashindwa kuhitimisha nia yake, wewe ndiye anayekutumia kufanya uhalifu huku nje. Kutaka kuangamiza watoto wasio na hatia pamoja na uchochezi.” Sabina alikuwa akilia sana huku akibisha.

Akamtolea picha zake akiwa gerezani akizungumza na Max. Zaidi ya mara moja. Siku zote alizokuwa akienda kumtembelea Max, alikuwa akipigwa picha akiwa na Max mwenyewe na wakili waliyemtafutia Max. “Je, unapinga kwamba huyu sio wewe?” Sabina akaendelea kujitetea huku akilia akisema safari zote alizokuwa akimtembelea Max, zilikuwa za kirafiki tu. Akaanza kusikilizishwa mazungumza yao alipokuwa akimtembelea Max huko rumande. Sabina hakuamini vile alivyokuwa akijisikia vizuri bila shida wakati akimshawishi Max akubali kusimama na Tino, apinge shutuma zote anazotuhumiwa na aseme anamjua Tino na Sabrina kwa muda mrefu.

Alimtaka aseme kuwa alikuwa nao hao wawili tokea mwanzo wa mahusiano yao, pale Lela alipomtelekeza Tino. Tino alimpenda sana, ila Sabrina ndiye aliyekuja kumgeuka Tino pale alipoondoka tu nchini kwenda kwenye matibabu, na kumpa watoto Jack. Akajisikia vile anavyomuhakikishia Max kuwa endapo atamsaidia Tino katika hilo, na akaweza kupata watoto wake, basi Tino atalipia garama zote za mwanasheria wa aina yeyote anayemtaka yeye, atakayemtetea mpaka na yeye akashinda kesi dhidi ya Msindai pia.

Kisha akajisikia tena vile alivyomwambia Max kuwa, Tino ameahidi kumlipa yeye malipo makubwa zaidi pindi atakapopata watoto wake. “Mimi ndiye ninayemuwakilisha Tino hapa nchini. Sasahivi anafanya chochote ninachomwambia mimi. Ukikubali tu, ujue maisha yako yamebadilika Max. Usiogope.” Akajisikia vile alivyokuwa akiweka ushawishi zaidi na zaidi ili Max amkubalie. Hapo Sabina akaongeza sauti kama aliyefiwa na mama yake mzazi.

Kisha akasikilizishwa tena mazungumzo kati yake na Lela pia. Sabina akajisikia vile alivyokuwa akimchochea Lela, akimwambia kishabiki kuwa asikubali hata kidogo. Hata kwa kuandamana, adai haki yake. Tino amlipe zaidi ya alivyolipwa wakati wa kutengana. Hapo Sabina akazidi kulia na kuogopa zaidi. Hata yeye alijisikia vile alivyokuwa akizungumza kama aliyepagawa akichochea mambo ambayo hata hayakuwa yakimuhusu! “Wewe ni mvunjaji wa amani, kwenye nchini yenye amani. Wewe ni mchochezi. Unakula njama na wauaji.” Sabina alikuwa akilia, akashindwa hata kujitetea zaidi maana alipewa ushahidi ambao hakuwa hata akihisi kama walikuwa wakirokodiwa na watu wa Usala. Ukweli walijitahidi kuwa makini ili hicho kinachotokea, kisitokee. Wakasahau kina Msindai masikio yao yapo kila mahali, ni kiasi cha kusikiliza tu.

Yule aliyekuwa akimsomea mashitaka akatoka na kuamuru taa izimwe tena kitu kilichomuongezea hofu zaidi. Alikuwa akitetemeka kwenye chumba hicho kibaya, ila kilikuwa na baridi ya kawaida tu, lakini yeye alihisi ni kama amewekwa kwenye friji. Giza na akawa peke yake asijue alipo. Alikuwa akitetemeka kana kwamba amepigwa shoti ya umeme mpaka meno yalikuwa yakigongana.

Mama Kundi.

J

acinta alipoachiwa afanye vile anavyojua yeye kuharakisha mambo, hakutaka kuchelewa zaidi. Wakati askari wake wakimkamata Sabina, tayari alishatuma wengine Dodoma. Wakamfanyia kama walivyomfanyia Sabina. Mama Kundi akiwa ofisini, hata kazi zenyewe hakuwa akifanya kwa hofu na mawazo ya kile kinachowakabili yeye na mumuwe, askari wakamtia pingu. Ila sasa yeye ikawa tofauti. Aliwekwa nyuma ya gari, safari ikaanza. Alishangaa ule mwendo kasi, asijue anapokwenda ila akashangaa hawafiki. Baada ya masaa kama mawili kupita ndipo akili ikamjia kuwa, anarudishwa Dar. Mama huyo alikuwa amejawa hofu kupitiliza kwani yeye alishayajua makosa yake, ila akashangaa ni kwa nini hakuwa amekamatwa bado mbali ya kuhamishwa kituo cha kazi!

          Siku hiyo ndio akajua arobaini zake zimefika. Akatulia hapo garini akitamani mauti imfike, shutuma zake zisije someka magazetini. Alikuwa akilia akihurumia watoto wake na aibu watakayoingia. Uzuri walikuwa na watoto wakubwa na wanaojua maisha. Waliwaacha pazuri kimali. Ila aibu ya wazazi wao baada ya uovu waliokuwa wakipanga kuja kuwekwa hadharani, huyo mama alisononeka na kujuta sana. Kwa upande fulani yeye alijua hiyo siku ingeweza kufika ila akawa akimsihi Max asimamie kwenye kuomba msamaha na kukiri kutorudia tena, asijue Sabina na wakili waliyemtafutia mumewe waliuza sera zao mpaka mumewe akapotea lengo. Kwa mara ingine tena, Max anamuingiza matatizoni.

          Gari iliendelea kwenda mpaka akasikia likisimamishwa kwa ajili ya kuongezwa mafuta. Akaulizwa kama angetaka kujisaidia. Akakataa. Baada ya hapo, gari liliondolewa hapo ikaendeshwa kwa masaa kadhaa, mpaka sehemu fulani. Ikasimamishwa tena, wakaingia askari wengine wawili hapo nyuma alipokuwa ametupwa tu, na kuachwa peke yake amelala chini na pingu zake mkononi kwa muda wote tokea wanatoka Dodoma. Kisha hiyo gari ikaondolewa tena. Aliweza kuona kwa kuchungulia kwa chini ya ile soksi aliyokuwa amefunikwa kichwani, wale askari walikuwa wamesimama kabisa. Gari ikaondolewa tena kwa mwendo kasi mpaka baada ya kama dakika 45 hivi, akaanza kusikia hiyo gari ikipigwa honi mfululizo kama inayotaka ipishwe barabarani. Akajua wameshaingia Dar na ndio maana waliongezeka askari wenye risasi kuongeza ulinzi. Mama Kundi alikuwa akitetemeka vilivyo asiamini kama na yeye amegeuka kuwa kama jambazi!

          Na yeye akashushwa na kwenda kutupiwa kwenye chumba chenye giza. Hata alipotolewa ile soksi kichwani, hakuwa akiona kitu. Alikaa hapo akitetemeka kwa hofu mpaka baada ya masaa kama manne mbeleni. Akaingia mtu hapo ndani na kuamuru taa iwashwe. “Uko chini ya ulinzi kwa kosa la kukusudia kutenda kosa la kumsingizia UBAKAJI, kiongozi aliyeteuliwa na raisi, na kupewa majukumu mazito ya kiserikali.” Mama Kundi alikuwa akitetemeka nakushindwa hata kujibu. Na yeye wakamsikilizisha mazungumzo yake na mumewe siku Max alipompigia akiwa na hasira ya Jackson uwanja wa ndege. Yule mama alijisikia vizuri kana kwamba walikuwa wakizungumza kwenye kipaza sauti. Akajisikia jinsi alivyokataa mwanzoni na kumuonya mumewe. Mumewe akasikika kuweka ushawishi mpaka akakubali kabisa mipango ya kumtoa Waziri Misindai mjini. Hapo mama Kundi alilia sana. Yule aliyemsomea mashitaka akatoka na kuamuru taa zizimwe tena. Akabaki peke yake.

Tino.

S

iku Tino anatua nchini hakuwa akijua kama anasubiriwa vilivyo. Usalama wa Taifa walikuwa hapo muda muafaka wakisubiria ndege yake ifike. Akiwa uwanja wa ndege akisubiria mizigo yake ili atoke uwanjani hapo, akasogelewa na askari wanne. “Wewe ndiye Costantino?” Tino akashituka kidogo. “Tufuate.” “Mnanipeleka wapi!?” “Tumesema ongozana na sisi. Au unataka tukuvute?” “Hapana! Kwani nimefanya nini!?” “Twende.” Wawali wakatangulia, Tino akafuata, wengine wawili wakafuata nyuma. Tino alijua mambo yameshaharibika, na yeye arobaini zake zimetimia.

Wakamuingiza kwenye moja ya chumba hapohapo uwanja wa ndege ambapo nje kulikuwa na mbwa  wakubwa wale wapolisi wanao tumiwa kunusa ili kujua kama kuna kitu kimefichwa mahali hata kama ni ndani sana. Akakuta masanduku yake yote yapo juu ya meza. Akazidi kuchanganyikiwa. “Haya ni  masanduku yako?” “Ndiyo! Kuna nini!?” “Hati yako ya kusafiria inaonyesha sasahivi unatokea nchini Italy. Na umeingia nchini na kutoka kwa muda mfupi sana zaidi ya mara 5. Unaweza kueleza unajishugulisha na nini?” “Kwanza kwa nini mnihoji juu ya maisha yangu binafsi!? Inawahusu nini?” Wakaangaliana kisha wakamtizama kwa cheko la kejeli kama vile kumwambia tutakuonyesha.

Akafunguliwa sanduku lake moja, vitu vyake vyote vikatupwa mezani kishwa akaonyeshwa kuwa chini kabisa kulichanwa. “Sisi ndio tulichana hapa baada ya mbwa kupata harufu ya hii na mashine kuthibitisha kuwa umeficha bidhaa haramu.” Akaonyeshwa mfuko wenye madawa ya kulevya. “No way! Hayo sio madawa yangu.” “Lakini umesema masanduku ni yako. Si ndivyo?” “Hilo sanduku ni langu lakini madawa si yangu!” “Kwa hiyo haya madawa yamejiingiza tu humu ndani?” “Hapana. Yupo aliyeyaweka hapo lakini sio mimi.” Tino akazidi kuingiwa hofu. “Costantino upo chini ya ulinzi kwa kosa la kuingiza chini madawa ya kulevya.” Tino akafugwa pingu na kutolewa pale kama mtuhumiwa na yeye akaenda kufungiwa sehemu peke yake.

Yeye walimfanyia tofauti. Sababu alianza kwa jeuri, walimuacha siku hiyo nzima bila mtu kumzungumzisha. Na siku ya pili nayo ikaisha akiwa peke yake. Gizani haswa hajui kama huko nje ni mchana au usiku. Hofu iliyokuwa imemkamata Tino, alishindwa hata kufunga macho gizani. Baada ya siku tatu kujua jeuri yake imeshuka na ameelewa ipo nguvu kubwa juu yake hapo nchini ndipo na yeye akafuatwa na mtu yuleyule aliyewasomea mashitaka Sabina na Mama Kundi.

Likaanzwa kosa la kuingiza madawa ya kulevya nchini. Hilo alionyweshwa ushahidi wa picha. Sanduku lake lilivyochanwa, akaonyweshwa madawa ya kulevya yakiwa kama yamefichwa chini kabisa ya hilo sanduku lake. Tino akazidi kuingiwa hofu na kujua hana jinsi ya kujitetea tena maana wazi yale madawa yalionyeshwa ni kama kweli yametolewa kwenye sanduku lake bila ubishi.

Akasomewa shitaka la kusudio la kutaka kuua watoto aliokuwa amebeba Sabrina. Akaonyeshwa ushahidi wa malipo aliyomlipa yule daktari wakiwa moshi na ukiri w daktari mwenyewe. Akasikilizishwa mazungumzo yake na Max alipomshawishi arudi nchini kudai watoto, akakataa akisema watoto ni wa Sabrina. Lakini akaja kuitishia familia ya Msindai mpaka wakamuwekea restrain order, ila baadaye kukiuka onyo hilo la kutosogelea watoto wa Sabrina na Jackson Msindai. Akaambiwa tarehe na muda aliochukua watoto wa Sabrina akisaidiwa na Sabina kinyume na matakwa ya wazazi wao. Akaonyweshwa picha zake akiwa na hao watoto siku na tarehe yenyewe ikionekana pichani. Tino alishituka, hakulitegemea hilo. Asijue utafiti ulifanyika mpaka wakajua hoteli waliyokwenda siku hiyo, na kuamuru hoteli kuangalia kwenye kamera zao za ulinzi wakitishwa kuwa wao ni Usalama wa Taifa. Walipowaona wakatoa hizo picha kama ushahidi. Hapo walizidi kumuogopesha Tino.

Lakini akajikaza na kujitetea. “Jackson Msindai alitelekeza watoto wangu. Nyinyi mlitaka niache damu yangu ipate shida kwa kuhofia restrain Order? Kipi bora, mimi kuwa jela, au kuwa huru na kuendelea kutesa watoto ambao nilishatenda kosa?” “Utapata nafasi ye kujitetea mahakamani. Hiyo ni haki yako ya msingi, lazima utapewa.” Akamjibu hivyo na kuendelea na kosa jingine.

Akamtajia kosa la kumsaidia kifedha, akiwa ameshamtafutia na kumlipa wakili atakayepinga mashitaka ya muhalifu Max. Yeye Tino akitaka Max awekwe huru ili amsaidie kuendelea kuifanyia fujo familia ya Jackson Msindai akitaka kuiba watoto wake ili baadaye, yeye na Max sasa, waje watimize kusudi la kutaka kuua watoto hao. Akaonyeshwa picha alizotumiwa mwanzoni kabisa na Max, wakati mapacha wa Jack ni wadogo na ukiri wake mwenyewe kuwa watoto si wake ni wa Sabrina. Akaonyeshwa kopi ya restrain order aliyopewa na kusaini kuwa alipokea onyo hilo alilopewa, baada ya kujipinga yeye mwenyewe aliposema, watoto si wake ni wa Sabrina lakini akarudi kudai watoto hao kwa vitisho. Akaonyeshwa tena picha ambazo alishawahi kwenda kumtembelea Max rumande. Mpaka anamaliza kumsomea mashitaka yake, Tino akajua ndio mwisho wake wa uhuru hapa duniani.

Kwa Sabrina.

S

abrina akawa kama amejionya, akataka kutulia kabisa asiharibu hiyo mimba. Akawa mtu wa kulala kama vile alivyokuwa akifanya Pendo. Hajigusi kwa chochote, na hatoki hapo ndani. Alikuwa amebakisha siku kama tano tu ili afikishe majuma 38 ambayo daktari alimwambia hawatasubiria uchungu, ila kutoa huyo mtoto. Akawa na kazi ya kula na kulala tu. Hata simu akafunga kabisa ili asisikie lolote isije kujipandisha pressure. Siku mbili kabla hajaenda hospitalini kujifungua, usiku ikabidi azungumze na Jack. “Tokea najifungua mapacha mpaka Brayan, hapajawahi kutokea amani ninapokuwa hospitalini nikijifungua. Nimekuwa nikifuatwa na maneno yakuniumiza tu bila sababu. Safari hii tulikataa babyshower tokea mwanzo na wakaelewa. Sasa naomba ukawaongezee na hili, SITAKI mtu kule hospitalini.” Jack akashangaa sana.

“Haiwezekani Sabrina!” “Hakika hakikisha inawezekana Jackson. Na katika hili sitaki utani wala masihara. Wanataka mtoto, wasubiri nijifungue. Mungu akinitoa chumba cha upasuaji salama, na mtoto akatoka salama, tutarudi hapa. Ndipo waje hapa waone mtoto. Najua hapa hata wakiwa na lakunisema, watayakusanya yote, watasubiri wakanisemee makwao sio hapa kwangu.” “Na baba kuangalia mtoto?” “Tungekuwa Singida angefanyaje?” Jack kimya akifikiria.

“Maana hii mimba nilishika tukiwa Singida na tukasema tunyamaze waje washitukie tuna mtoto mwingine. Sasa kilichobadilika hapa ni nini?” Jack kimya. “Mimi sitaki fujo Jack. Kwanza ni mtoto wa nne. Najua kila kitu. Halafu Mungu amenipa Pina, ananijulia mimi na makinda yangu yote. Huyu msichana mwingine atafanya kazi za humu ndani akisaidiana na kaka. Nishapanga timu yangu, wote wameelewa. Sitaki msaada wa mtu mwingine yeyote yule maana ndio wanakuja kunisimanga baadaye. Mungu amenihurumia amenipa hao watu, inatosha.” “Chakula?” “Nitakula cha hospitalini pamoja na uji atakao kuwa akinipikia Pina na kumpa Chali au wewe uniletee hospitalini. Nimemaliza.” “Hata Pendo pia?” “Huyo nishazungumza naye na ameniunga mkono kwa asilimia 100. Wanachofanya wakija hospitalini nikiwa najifungua ni kunitesa tu. Sitaki mtu. Mungu atamsaidia mwanangu atazaliwa salama hatahitaji hekaheka za madaktari kama za Brayan.” Jack akapoa.

“Hakika naomba uniahidi utalisimamia hilo Jack.” “Sasa hata mama nisimwambie?” “Utampelekea watoto. Lasivyo nikwambie kabisa Jack, kesho mimi naondoka nakwenda kujifungulia Singida, nikatulie kabisa kule. Sitaki fujo mimi.” “Basi nitawaambia kama unajifungua ila nitawaambia wasije hospitalini.” Sabrina akanyamaza.

“Sasa mbona hujibu?” “Nishaona wewe utanisumbua. Acha tu kesho mimi niondoke. Nakwenda kuzungumza na yule daktari wangu wa Singida, anisaidie kujifungua. Nikipata nguvu ndio nakuja huku.” “Basi Sabrina.” “Unataka kunichanganya bila sababu Jack. Kuna ulazima gani wakuwaambia kuwa najifungua kama vile yupo mtu ananijali sana, kwamba atakuulizia Sabrina yuko wapi, kama si kutaka kunijazia watesi wangu pale hospitalini?” “Lakini ni kama wamebadilika.” “Basi ndio wasubirie na wewe utulie.” Akanyamaza.

“Jackson Msindai?” “Basi hata tuagane.” “Hapana Jack. Wewe unakwepa kuahidi tu. Niambie kama umeelewa na ume..” “Sasa si tuagane kwanza?” “Hapana. Tunaagana hapa kila siku na hatumalizi! Leo tufunge huu mjadala.” “Sawa nimeelewa. Hutasumbuliwa.” “Acha kujibu harakaharaka ili uanze michezo yako bwana, Jack!” Jack akaanza kucheka. “Michezo yetu mama. Mbona unajitoa wakati na wewe nakuona siku hizi mpaka asubuhi unakumbushia kuagwa!” Sabrina akacheka sana. “Naona kila siku hali inabadilika! Hakika sitoki chumba cha upasuaji bila kufunga kizazi, lasivyo baada ya miezi 9, habari hii itajirudia.” Wakakubaliana na Jack itoshe hivyo. Mungu amewapa watoto wanne, itoshe. Wawili hao makubaliano hayo yakasindikizwa na penzi, wakiambiana wanaagana. Maana Sabrina anakwenda kujifungua kwa upasuaji kwa maana ingine inabidi wasubiri mpaka apone.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye mida ya saa nne asubuhi siku ya kujifungua kwa Sabrina, Jack akiwa anatokea kazini akamfuata hospitalini maana Sabrina alipelekwa na dereva tu, akamwambia amuache hapo. Lakini Chali alikuwa akipatana na kila mtu hapo kwa Sabrina. Akamwambia atamsubiria mpaka aone atakapolazwa ili apate mtu wa kumtuma kabla hajapelekwa wodini. Sabrina hakukataa akajiambia inawezekana hayo ndiyo maagiza aliyopewa, asimuache hapo peke yake. Chali alikaa hapo na Sabrina mpaka akapewa kitanda, akaenda kukaa naye mpaka Sabrina alipomwambia arudi nyumbani pengine Pina atakuwa akimuhitaji amtume, ndipo Chali akaondoka. Ilipofika saa nne sasa ndio Jack naye akaingia.

 “Sasa wewe sahizi huku, na kazi?” “Sikutaka uwe peke yako!” “Mimi nipo mzima kabisa, nilikuwa na Chali hapa tunaongea. Ameondoka muda si mrefu ili nipumzike. Wewe nenda kazini.” “Hapana bwana Sabrina! Hata kama ni kazi ndio hata nisiwepo hapa!” “Hata ukiwepo hapa, kwenye chumba cha upasujia hutaingia na kwa jinsi nilivyoambiwa nafasi yangu ni mpaka saa nane. Leo dakatri ana watu wengi wakuwazalisha. Sasa utakaa hapa mpaka saa ngapi?” “Nakuonea huruma, Brina wangu. Umekataa watu.” “Mwenzio nina amani na Mungu wangu. Nishaombea kila kitu, hapa nilikuwa nimelala ili nisifikirie chakula.” “Njaa imeshaanza?” “Nafikiri kile kitendo cha kuambiwa nisile chochote ndio kinaniongezea njaa.” “Pole.” “Acha kuniangalia kwa huruma bwana!” “Sasa unataka nifanyaje? Nikusaidie nini?” “Hakuna kwakweli. Kama huna lakufanya sasahivi huko kazini, basi tukae tu. Ila kama una mambo mengi, nenda kapunguze uje hata hiyo saa nane.” “Basi muda ukibadilishwa niambie. Si unajua hapo kazini sio mbali na hapa, nitakuja mara moja.” “Nakuaminia Mheshimiwa Msindai.” Jack akacheka.

“Huogopi?” “Naomba uondoke Jack. Unataka kuanza kuniingizia hofu zako.” “Nakuuliza tu!” “Sitaki. Mimi nakujua wewe. Hapo ushawaza pengine naweza kufa huko chumba cha upasuaji, usinione tena ndio maana umekimbilia hapa.” Jack akapoa.

Akajua ni kweli. “Njoo Jack.” Akamsogelea karibu. “Wewe tuliomba jana usiku. Ukamwambia Mungu mengi. Kwa nini unakosa imani?” “Nina imani na hofu pia, Brina! Aisee utoke huko.” “Mungu atanisaidia. Vipi lakini?” Zikaanza stori, wala Jack hakuondoka.

Wakakaa hapo mpaka mida ya saa 6 Sabrina akaja kuchukuliwa kupelekwa chumba cha upasuaji wakicheka tu na Jack. Akamsindikiza mkewe mpaka nje ya mlango akamwambia anamsubiria yeye na Brandon, mtoto wao wa mwisho. Japokuwa watu hawakuja hapo, lakini kila mtu nyumbani kwa kina Jack alijua siku hiyo Sabrina anajifungua. Mzee Msindai akawa ameshatayarisha daktari wa mtoto wa kumuangalia pindi atakapozaliwa na kuomba apewe taarifa zake.

Baada ya muda mtoto akatolewa ndipo baadaye Sabrina naye akatolewa. “Umemuona Brandon?” Sabrina akauliza akisikika bado ana madawa ya usingizi mwilini. “Nimemuona. Naona amefanana na wewe huyo! Sura kama dada zake!” Sabrina akacheka wakati wakimrudisha chumbani kwake. “Vipi maumivu?” “Nimeanza kuyasikia.” “Tukimuweka tu kitandani tutamchoma sindano ya maumivu.” Baada ya kumuweka sawa na kumchoma sindano, wauguzi wakatoka. “Nasinzia Jack.” “Lala.” “Na wewe usisite kuondoka. Nikiamka nikawa na shida nitabonyeza kengele, watanisaidia tu, usiwe na wasiwasi. Acha nipumzike.” “Basi nitarudi jioni na uji.” “Sawa.” Sabrina akarudi usingizini.

Alikaa pale hospitalini akisaidiwa na wauguzi kwa siku tatu ndipo akaruhusiwa kurudi nyumbani na mtoto wake. Hakuna aliyefika hapo hospitalini kumuona isipokuwa Jack tu ambaye alikuwa akipita asubuhi na chakula na kurudi tena jioni akitokea kazini. Wanakaa hapo wanazungumza na kumsaidia kutembea kidogo kisha anaondoka usiku kurudi nyumbani kwa watoto mpaka akaruhusiwa.

Aluta kontinyua…

B

rondon alikuwa ameshafikisha miezi miwili, lakini bado Sabrina akawa mtu wakukaa ndani kwani aliugua sana baada ya kujifungua. Akaanzishiwa madawa ya makali ya antibiotic ili kuua infection, kwahiyo ndio akawa kama ndio amepona tu. Siku hiyo akiwa amejipumzisha tu nyumbani Jack akampigia simu kumtaarifu kuwa kina Ibra watafika hapo nyumbani kuwaona. “Sikujua kama mmerudi kuwasiliana na Ibra!” Sabrina akashangaa sana. “Maana si alikuwa hataki mimi niwe na wewe ndio mpaka akashindwa hata kuhudhuria harusi yetu na kukata mawasiliano na wewe muda wote huo! Sasa leo anakuja kutuona kwa lipi!?” “Mimi mwenyewe nilishangaa. Ila Felix ndiye aliyeniambia kuwa ni Ibra mwenyewe ndiye aliyempigia simu na kumwambia imekua muda mrefu hajawasiliana na sisi, anaomba yeye na Ney wamsindikize kuja kutuona. Ndio ikabidi Felix ampigie simu Ney kumuuliza kama leo ananafasi ya kuja huku, Ney akakubali bila shida.” “Makubwa!” “Hutaki wageni mama Msindai?” “Mimi nashangaa tu. Maana sijamsikia huyo mtu hata kwa kuropokwa nilipo mimi!” “Na mimi ndio leo nimemsikia tena. Kila kitu kikiwa sawa mida ya saa mbili nitakuwa nimeshafika hapo.” “Haya waambie wakaribie tu.” “Ila usijichoshe sana. Watakula watakachopika kina Pina.” “Usijali.” Wakazungumza yao, wakaagana.

Ikabidi Sabrina kutoka kitandani akijua ana wageni jioni hiyo, lazima kupikwe vizuri na maandalizi yakae ya kigeni. Akatoka kutoa maagizo nini kipikwe na kitayarishwe kwa ajili ya wageni watakaowatembelea usiku huo. Ukweli Sabrina alikuwa na wasichana wa kazi wazuri, waliojua kujipanga kiasi chakumpa pumziko zuri huyo mzazi mwenye mapacha wa nje na ambaye ndio alikuwa akirudisha nguvu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika mida aliyojua wageni wanakaribia kurudi na mumewe, Sabrina akatoka kuangalia vyakula. Akasaidia kupanga ndipo akarudi kuoga na kujitengeneza vizuri angalau na yeye afananie na ile nyumba. Wanae wakawa wasafi, wakatoka kusubiria wageni. Wakaanza kuingia Neema na Felix. Zikaanza stori Sabrina akicheka hana mbavu wakikumbushiana mambo ya chuoni na habari za mtaani. Mwisho akaingia Ibra na Phina. Japokuwa hawakuwa wakimtegemea Phina hapo, na hata Sabrina mwenyewe alishangaa ujio wake pale, mpenzi huyo wa zamani wa baba mwenye nyumba hiyo lakini  Sabrina akawa muungwana, akasimama kabisa na kuwapokea kwa furaha zote, bila hila.

Felix na Ney wakawa kama bado hawajaelewa. Ibra alipiga simu akisema yeye ndio anaomba wamsindikize hapo kusalimia familia ya Jack, sasa anawezaje kufika nyumbani kwa Jack na mpenzi wa Jack wa zamani! Hicho kikawasumbua kidogo. Lakini walipoona Sabrina hajajali, na wao wakaona wanyamazie. “Mama wewe umependeza. Tena umependeza mnoooo!” “Acha kunisanifu bwana Sabrina!” “Eti Ney, huyu Phina hajapendeza kweli?” “Sasa anakataa nini? Basi umetisha! Acha kujishaua.” “Achana na Ney. Mwaya umependeza na unazidi kuvutia. Karibuni mkae, tuendelee kucheka.”  

“Naona mzee ulijificha!” Felix akamrushia neno Ibra. “Maisha tu. Vipi Ney?” “Nipo Ibra. Tupo na serikali yetu.” “Naona huko mnagawana tu mihela ndio maana hamtukumbuki!” “Wewe si ulikataa serikalini mzee! Malalamiko ya nini?” Felix akaingilia bila nia mbaya, ila utani tu. “Kwa hiyo sasahivi unaona sisi tunalia tu njaa, hatuna maana?” Kidogo vicheko vikapungua. “Maana mmeshapata nyinyi, wengine mnatuona..” “Mbona povu mkubwa wakati mimi nakutania tu!?” Felix akauliza na cheko la mshangao kidogo.

“Phina zungumza mama, upo sehemu sahihi. Sema tuondoke. Naona wanaleta dharau kwa kuwa wanajiona wao wamepata, siku hizi mambo yao wao safi, wanakula na wakubwa wa hii nchi, ndio wengine hatuna maana! Yaani Jack ndio wakukataa kupokea simu zangu mimi!? Yaani mimi ili kumpata yeye ni mpaka wewe!” Hapo wakajua hao wawili hawajaja kwa wema. Utani ukaisha kabisa, wakanyamaza kuwasikiliza. “Sema Phina tuondoke zetu.” Wote wakamgeukia Phina kusikia hicho anachotaka kusema.

“Au labda nimsubirie Jack mwenyewe, nizungumze naye yeye? Hapa naona kama si sehemu yake!” “Sehemu ingine ipi na bosi wao hawa analeta dharau! Ongea usiogope.” Akawa kama anampandisha morari, ila Phina amejawa hofu, akainama. Kimya wakimtizama yeye na kuwasikiliza. Phina aliponyanyua kichwa kuwaangalia, akakuta wakimtizama kumuonyesha wanamsubiria yeye aongee lililowaleta na kutaka kuja kuzungumza na Jack tu! Akaanza taratibu. “Mimi sio kwamba ni mvurugaji. Ni vile Jack amenifungia simu zangu na sina jinsi ya kumpata.” “Basi unabahati nzuri. Amerudi nchini. Yupo hapa mjini! Muda si mrefu atakuwa hapa.” Sabrina akamtuliza bila hila. Kidogo Phina akapoa.

“Acha kusita Phina! Ni haki yako. Unaogopa nini? Hata kwa wazazi wake mimi nimekwambia nitakupeleka. Waache dharau.” “Kwani kuna nini? Kama kuna jambo ambalo unaona naweza kukusaidia, tafadhali usisite Phina. Sisi tumetoka mbali. Na tumesaidiana katika mengi.” Sabrina akajaribu kumtuliza ili azungumze lakini akadakia tena Ibra. “Mengi sana, nashangaa eti sasa hivi ndio wanaleta dharau!” “Kiongozi vipi mbona jazba tena!?” Felex akauliza na Ney akaanza kucheka. “Acha hasira Ibra. Kama kuna jambo la kuzungumza, acha tuzungumze kwa amani.” “Amani ipi wakati Jackson anatumia madaraka yake vibaya, kisha analeta dharau?” Kimya wakimpa nafasi huyo Ibra maana alionekana analo jambo analotaka lazima Phina aliseme, lakini ni kama Phina naye anasita. “Sema usiogope, Phina.” Akazidi kumsisitiza Phina.

“Kuna nini Phina?” Sabrina akamuuliza Phina kwa upendo tu akimbembeleza. “Jack kampa mimba Phina, halafu anamkimbia!” Ibra akajibu kwa haraka, moyo wa Sabrina ulishituka kama kumeanguka chuma sakafuni. Akaona kama giza kwa sekunde kadhaa. “Anatafutwa, halafu anafungia namba za Phina zote! Anatumia watu tu vile atakavyo! Amelala na Phina usiku kuchwa, eti asubuhi ndio kama anakumbuka alifanya kosa, anamfukuza Phina! Uzuri Phina alimpiga picha na ushahidi anao wakiwa hotelini Switzerland walipokutana na Jack.” Ibra akasimama na bahasha kubwa tu aliyokuwa ameishika tokea wanaingia hapo akaenda kuiweka pembeni kwa Sabrina kama kumpa ushahidi.

“Huo ndio ushahidi wa Phina. Mpe mumeo anayejua kuchezea wanawake vile atakavyo. Alipokuwa na Phina, akawa na wewe pia. Nikamuonya Jack, hakunisikia. Akakuoa. Sasahivi yupo na wewe, analala na Phina. Si ushenzi huo? Sasa mwambie Jack aanze kuweka mikakati juu ya mtoto wa Phina. Tunampa siku tatu tu awe amewasiliana na Phina na kuweka mipango ya kueleweka lasivyo sisi tunatangulia Ustawi wa Jamii kudai haki zetu, na atasikia habari zetu magazetini.” “Labda mimi nikuulize Ibra, wewe unaongea hapa kwa jazba kama nani?” “Hayakuhusu Ney.” “Mbona mimi ndio naona kama wewe Ibra ndio hayakuhusu?” Akadakia Felix.

 “Twende Phina. Ila Sabrina, jua mtoto wa Phina naye anataka alelewe kama hivi hao watoto wako wanavyolelewa hapa. Wawekewe ulinzi kama huo waliowekewa watoto wako na aishi kwenye nyumba kama hii.” Felex akakasirika sana. “Wewe ni mshenzi Ibra na naona maisha yamekupiga mjomba, unataka uponee hapahapa kwa Msindai.” Nusura ngumi zianze. Matusi yakaanza hapohapo mpaka wasichana wa kazi na watoto wakajongea hapo sebuleni kujua kulikoni. Sabrina kimya palepale alipokuwa amekaa.

“Umenitumia mimi kukusogeza kwenye familia ya watu ili mje kufanya fujo! Yeye Phina hakujua analala na Jack mume wa mtu na ana majukumu mengine mbali ya kupokea simu zake malaya huyu.” Felix alikuwa amekasirika kwelikweli akigomba, Ibra naye anamtukana Jack matusi ya nguoni hapohapo mbele ya mkewe na watoto wake kama aliyekuwa na hasira kali sana kwa Jack. Chakushangaza Felix ndiye aliyekuwa akigombana naye, lakini yeye anamtukana Jack mpaka mlinzi akaingia na kuwatoa wote mpaka kina Ney.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Nini Kitaendelea? Usikose Muendelezo.. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment