S |
iku ya tatu usiku wakiwa bado hawajafungua
wakisindikizwa na mchungaji aliyewajua hao watoto tokea enzi za uhai wa mama
yao na yeye marehemu mama yao alikuwa akitumika kwenye kanisa analochunga huyo Mchungaji, akiwa na yeye amefunga, wakaongozana kwenda nyumbani kwa mzee Ngoi
na mkewe Zelda. Kwa hakika Zelda alishituka sana. Akataka kumshawishi Ngoi
awafukuze kwa kuja bila taarifa, lakini ilivyo ya kushangaza kwa mara ya kwanza
Ngoi akawa kinyume naye. Akamwambia angependa awasikilize.
Wakakaribishwa ndani. Hilo
likawa kosa, hata maji walikataa kunywa, wakasema wanaanza kwa maombi. Maombi
yaliyopigwa hapo ndani, Ngoi na mkewe wakaanza kulipukwa mapepo. Zelda akawa
anataka kukimbia kichaa. Wakamkamata na kumfunga kamba. Kazi ya kumuombea Ngoi
ikaanza. Akatolewa mapepo akawekwa huru asielewe kinachoendelea. Hawakutaka kupoe.
Wakaendeleza maombi ya nguvu ndipo Zelda akaanza kulipuka mapepo mengine
yaliyoanza kuzungumza na kufanya msiba uanze upya. Alikiri mengi
mno yaliyowaliza ndugu hao mpaka Ngoi mwenyewe. Prisca akamuomba mchungaji
amuulize ni wapi anaficha uchawi wake. Kila alipokuwa akisema, wanaenda kutoa
hirizi na madawa. Alikuwa amechimbia madawa kwenye kila kona ya hiyo nyumba.
Zelda akiwa bado
amefungwa kamba akilia kama kichaa huku akiwaonya wasithubutu kuangamiza kitu
hata kimoja wapo, lakini mchungaji hakumsikiliza. Wakakusanya yote mpaka madawa
na hirizi alizokuwa ameficha ndani na kuchoma moto, watoto wao wakimchukua
video kwa kila ukiri aliokuwa akikiri na kila mahali aliposema amefukia au
kuficha hizo dawa, walikuwa wakienda kufukua uchawi huku wakichukua video.
Ilikuwa wote wafe kasoro
Willy. Zelda alisema yeye Willy hakuwa kinyume naye, alikwenda mpaka kwenye
harusi yao. Ila aliyekuwa akifuata kufa ni Prisca. Ikazidi kuwaumiza na kujuta
kutochukua hatua mapema, pengine wangebakiwa na ndugu zao! Walipochoma kila
kitu ndipo sasa ikaanza kazi ya kutoa hayo mapepo ya Zelda mpaka akawekwa huru.
Ngoi alikuwa akimuogopa mkewe kupita kiasi. Hakutaka hata amsogelee.
Walichofanya ni kumpeleka polisi usiku huohuo.
Kwa kuwa walijua kesi za uchawi ni ngumu
kuendeshwa kwa sheria za nchi, basi wakatoa ushahidi wote mpaka wa video ili tu
kusaidia kuhukumiwa kwake kihalali. Kesi ya Zelda ikaanza. Wakimshitaki kwa mauaji
aliyokiri mwenyewe kufanya kwa njia ya kutuma mapepo kuua. Wazazi wake
Zelda wakaja hapo wakiwatisha kuwa kitawapata kitu kibaya kama hawatamtoa
Zelda. Nao wakawashitaki na hivyo vitisho vyao. Wakapewa onyo kisheria na
kuambiwa chochote kitakachoipata hiyo familia tena, hata kwa bahati mbaya, basi
wao watakamatwa na kushitakiwa kuhusika moja kwa moja. Wakapoa.
Hakuna aliyesikia kilichowapata hiyo familia
wasitake kuwasaidia kwa hali na mali, mpaka maombi, na kisheria pia. Wakapata
uungwaji mkono mkubwa, Zelda hakuweza kutolewa hata kwa dhamana. Kesi yake
ikawa ikiendelea, yeye yupo rumande ila mtoto wake alichukuliwa na mama yake
Zelda. Willy akaahidi nilazima baba yao atakuwa akimtunza huyo mtoto na
kuhakikisha anakua vizuri na kusoma bila shida. Hilo likakaa sawa. Wakashukuru
sana wasiamini kama hawatamtelekeza huyo mtoto.
Mungu Wa
Yasiyowezekana Kwa Akili Za Kibinadamu..
S |
abrina alipofikisha mimba ya miezi saba, mumewe
akateuliwa kuwa naibu waziri wa fedha baada ya aliyekuwa naibu waziri kutolewa
na raisi. Jack alikuwa akifurahia asiamini kama yote hayo yanamtokea yeye.
Safari hii wakaenda kuapishwa ikulu. Jack akakusanya tena timu yake mpaka Dar. Na
walishukia nyumbani kwao kwani walishaanza kujaza nyumba yao kwa thamani za
ndani wakitaka kuwa wakiitumia pindi wanapokuwa jijini maana kuendelea kushukia
majumbani kwa watu ikawa shida, familia yao ishakuwa kubwa. Kwa wakwe bado
hawajapatana na Sabrina, wakaona bora wawe na kwao, iishe hivyo. Ikawafaa sana
kwa wakati huo pia. Na kama kawaida yake, mama Msindai akaleta yeye nguo za
Jackson. Wala Sabrina hakulalamika. Akamuacha tu afanye kile anachotaka kwa
huyo mwanae.
Baada
ya shuguli hizo zote, wakajua nilazima sasa kuhamia Dar kwa kuwa sasa majukumu
ya Jack kikazi yalimtaka awepo huko. Ikawa ngumu sana kwa Sabrina. “Itakuaje
kule Singida, Jack?” “Tutarudi kuzungumza nao na kuwaambia majukumu
yanatushikilia huku lakini mimi bado ni mbunge wao, nawawakilisha huku. Na
tutakuwa tukirudi kuwatembelea mara kwa mara. Na wewe utaendelea kufanya nao
kazi kwa karibu.” Wakaweka mipango iliyofanya hata Sabrina kujiridhisha kuwa
wameacha jimbo kwenye hali nzuri. Walipotulia, wakarudi Singida kuwaaga na
kuzungumza nao vizuri. Ikawa ni jambo la kuwahuzunisha kuwakosa huko Singida
lakini pia lakuwafurahisha wakijua wamepata uwakilishi mzuri huko bungeni.
Kila Kitu
Mwangani.
B |
ado Sabrina hakuwa amewasiliana na nyumbani kwao
ila habari za mafanikio ya mumewe haikuwa siri. Hata wao walijua mafanikio ya Jack
waliyembeza aliposhindwa ubunge wa Afrika ya Mashariki. Madaraka ya Jack
yakaibua kuchimbuliwa kwao. Minong’ono juu ya familia ya Jack ikaanza. Kitendo
cha kuonekana na aina ile ya watoto ndio iliyoibua minong’ono mitandaoni.
Familia yenye watoto wa kizungu wakati hapakuwa hata na mweupe kwa wazazi hao! Nani
kati yao alizaa na mzungu ndipo akaja nao kwenye ndoa!!!?? Naibu waziri au Sabrina?
Ukawa utata. Ilianza minong’ono ya chinichini tu, ila iliweza kusikika, na
hapakuwa na jibu.
Picha
za mapacha zikaanza kuenea na kufananishwa mpaka wakajua ni watoto wa Sabrina.
Nani baba yao!? Nalo likawa jambo lakutafutiwa majibu. Lakini sasa unampata
wapi Sabrina kujua habari zake? Hajaajiriwa popote, na sio mtoto wa jiji,
hakuna anayejua habari zake kwa undani. Hana Instagram wala Facebook.
Habari zake zikaanza kusakwa bila kuchoka. Nani yupo karibu na familia hiyo
inayoweza kutoa mambo ya ndani! Kwa upande wa familia ya Msindai ikawa ngumu
kuingia ili kuweza kutoa mambo ya familia ya Naibu waziri mpya, ikaanza kusakwa
familia ya Sabrina. Amezaliwa wapi! Ndugu zake kina nani! Ilimradi tu kujipatia
habari. Mswahili mnyime chakula lakini si neno.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado Max alikuwa kifungoni
na kesi yake haikuwa imesomwa. Hajahukumiwa bado, kila wakati kesi yake ilikuwa
ikisogezwa mbele. Mkewe alishahamia Dodoma, akisubiria kustaafu aondoke
serikalini na kiinua mgongo chake sio mikono mitupu.
Adui Za Mtu
Ni Wale Wa Nyumbani Kwake.
{Mathayo 10:36}
A |
lipofikisha majuma 36 ya ujauzito wake, Sabrina bila
hila akijua akifikisha majuma 38 lazima kufanyiwa upasuaji mwingine na akajua
hataweza kutoka ndani kwa muda mrefu akijiuguza kidonda na kulea hao mapacha
wake wa nje, akaamua kwenda kuona wazazi. Nyumbani ni nyumbani, wazazi ni
wazazi. Akaamua kwenda kuwaona na kuweka amani. Akakusanya watoto wake na
dereva maana ni kweli mambo yalibadilika kati yao. Mapenzi ya kila wakati
wakishikana huku na kule, kuongozana kila mahali, yakapungua, Jack alishapewa
majukumu mazito, hawezi kuzembea kwa sababu hakutaka kuharibu kwa la unaibu
waziri, akitaka kuja kuaminiwa na makubwa zaidi. Akaongeza nidhamu ya kazi
zaidi ya kawaida yake. Kwa hiyo mtindo wakufuatana kila mahali ukakoma. Mara
chache tena ikilazimu ndipo utawakuta pamoja.
Sabrina alijifungasha
vizuri akiwa amewanunulia wazazi wake zawadi za kutosha, akaondoka mjini muda
mzuri tu akielekea Chalinze nyumbani kwao. Ilikuwa siku ya jumamosi. Akashangaa
mazingira ya nyumbani kwao! Kulionekana kumebadilika sana. Hali ya neema ya
ajabu! Nyumba iliwekwa geti zuri na la kisasa. Akashangaa kidogo na kumpongeza
Sabina nafsi mwake. Akamwambia dereva asubiri pengine watafunguliwa baada ya
kupiga honi. Wakatulia garini wakisubiria kuona. Na kweli akaja kijana ambaye
Sabrina hakuwa akimfahamu, akafungua geti wakaingia ndani. Macho ya Sabrina
yakapokelewa na barabara iliyotandazwa mawe mazuri kuanzia hapo getini
walipoingia mpaka kwenye ngazi za nyumba! Ngazi zenyewe ni kama zilijengwa mpya
sio alizoacha Sabrina za kawaida tu. Halafu ngazi hizo zilijengwa na
kuzungushiwa rembo nzuri za vinguzo vyenye muundo mzuri za kuvutia pamoja na
rangi yake. Halafu sakafu ikajengewa marumaru za kisasa, safi. Kuanzia ngazi ya
chini mpaka kuingia ndani. Sabrina akashangaa sana.
Dereva akamsaidia
kushusha watoto, Sabrina akawaambia wale wakubwa mapacha wambebee pochi yake
waanze kuingia ndani wakati akijaribu kumuweka sawa Brayan ambaye hata mwaka
hakuwa ametimiza. Ila dereva akamtoa kwenye kiti chake, Sabrina akawa amemshika
mkono akimtaka atembee mwenyewe sio kumbeba. Basi akawa akijivuta taratibu
kutokana na tumbo lake na hatua za Brayan.
“Umeona yanakushinda
huko, yamewalemea, ndio unajidai kurudi ulikokua umetususa!” Sabrina
akatoa macho kwa mwanae na kumuangalia mama yake aliyekuwa akizungumza bila
karibu hapo barazani. Sabrina akahisi pengine anazungumza na mtu kwenye simu au
mtu mwingine, sio yeye. “Shikamoo mama.” Sabrina akasalimia na kurudisha macho haraka
kwa Brayan asije akaanguka. “Mimi naona tubebane tu. Lasivyo tutafika huko
mwakani.” Sabrina akamwambia Brayan na kumnyanyua mwanae. Kuangalia, bado mama
yake anawatizama.
Akacheka.
“Unavyotushangaa! Umependeza mama Sabina.” “Ulivyotususa, ulifikiri
tutaaibika?” Sabrina akakunja uso. “Kwamba gafla mimi nataka muabike!?” Sabrina
akauliza na tabasamu la mshangao. “Kumbe! Ulivyotutupa, ulidhani tutayumba!
Mungu wetu yupo Sabrina. Na tumeyaanza maisha kabla wewe hujaja hapa duniani.
Ona kinachokutokea sasa hivi! Yamekushinda huko ndio unarudi huku kuomba
undungu! Undugu hauombwi wakati wa shida. na kwa taarifa yako tu, kama
umeshindwa wewe kututambua sisi kama ndugu zako, sio waonavyo walimwengu.
Habari zako zinatafutwa ulikozaliwa. Sasa hata ukitukimbia sisi kwa sababu
unatuona si wasomi na hatufai kama kina Msindai, lakini jua bado sisi ni wazazi
wako. Ulizaliwa hapa na kukuzwa hapahapa. Hapa ni mtakuja. Hata uende
wapi, hapa ni mtakuja tu.” Sabrina na wanae wakabaki hata kwenye ngazi ya
kwanza hawajapandisha. Mama Sabina anaongea kwa jazba kupita kiasi, Sabrina
haelewi.
“Kwanza hata hao kina
Msindai hawakutaki. Unaa..” “Mama Sabina, huyu mtoto hata ndani hajaingia mke
wangu! Ona hali yake! Ni mjamzito huyo na ana mtoto mkononi, kweli unashindwa
kumpokea wakati amekuja nyumbani kutuona!?” “Amekuja kutuona au kaja kutusanifu
na kutufunga mdomo! Sasa hapa lazima haki itendeke. Tino apate haki yake. Hatuwezi
kunyamazia ukweli huku mkitesa watoto wake wakati yeye mwenyewe yupo na ana uwezo
wa kuwalea!” “Acha nikupokee mtoto.” Dereva akamsogelea na kumuomba Sabrina kwa
heshima. Sabrina akageuka. “Nashukuru. Naomba nisaidie kurudisha wote ndani ya
gari, hapa jua kali sana.” Sabrina akamkabithisha Brayan kwa huyo dereva ambaye
wanae walishazoea kumuita anko Chali. “Jeiline, mama, nenda kwa anko Chali, atakusaidia
kupanda kwenye gari. Mnisubirie nakuja sasahivi. Sawa Keiline?” Wakakubali na
kuanza kumfuata Chali. “Hata ukiwakimbiza hapa…” “Subiri kidogo mama.
Sitaondoka hapa mpaka umalize dukuduku lako. Lakini naomba nitoe wanangu juani.
Tafadhali mama yangu.” Akamgeukia dereva. Alipomfunga Brayan kwenye kiti chake,
akaanza kuingiza wale mapacha garini. Alipoingia na yeye na kuwasha gari,
Sabrina akamgeukia mama yake.
“Nakusikiliza mama, japo
kwa hakika hata sielewi ni nini unazungumzia!” “Utajijua!” Mama yake akajibu.
“Jamani wazazi wangu mimi nilikuja kuwaona, ni hilo tu sina jingine. Nilitaka
kuwajulia hali nikijua Mungu akinipa uzima nikijifungua,..” “Ili nije
kukusaidia kulea watoto wa watu wasio na utu! Binadamu walionyimwa utu,
wanatumia vyeo vyao vibaya! Wanamfunga mtu aliyekuwa akitaka kumsaidia Tino!
Kwa kosa lipi mno! Sasa na sisi kwa kuwa Tino ametuonyesha utu na
ubinadamu, anatambua sisi ni ndugu za watoto wake, anajali na kukumbuka
nyumbani sio huyo mwanaume ana kazi ya kukuzalisha tu, hajui kama una wazazi!
Sasa na sisi kama familia, tutasimama na Tino mpaka apate haki yake. Popote na
kwa yeyote yule, tutazungumza ukweli.” Kidogo ni kama Sabrina akaanza kuelewa.
Akaangalia yale mazingira
kisha akarudisha macho kwa wazazi wake. “Kwa hiyo haya mabadiliko ninayoyaona hapa,
ni kazi ya Tino hii?” Sabrina akauliza. “Yeye ndiye aliyebaki mwenye uti je!
Ulifikiri na yeye atakuwa kama huyo mwanaume wako wa magazetini tu, wala
chamaana hatuoni!” “Sawa mama. Nyinyi endeleeni na Tino.” “Unatudharau ukidhani
tutashindwa hiyo kesi? Sasa Sabina amekubali kutoa ushahidi wote. Na mimi
nitaeleza jinsi huyo Jackson alivyowatelekeza watoto wa Tino zaidi ya mwezi, hajui
walipo, wanakula nini wala wanavaa nini mpaka Tino akaingilia kati kuwasaidia.
Hakika tutasema.” “Haikufika hata mwezi mama yangu!” “Utajijua mwenyewe. Lakini
na mimi nilikwepo, shahidi wa Tino. Nitasema ukweli wala sitaogopa. Alikutelekeza
na watoto mpaka Tino akaja kukusaidia. Aliposhindwa ndio akajirudi na
kumpokonya mwenzie watoto wake.”
“Huyo mwanadamu gani kama
si mnyama tu! Yakimuendea sawa anawatelekeza. Yakimdodea anarudi! Ona ulipofikishwa.
Tumbo linakulemea na watoto wote upo nao peke yako, yeye anazungushwa kwenye
magari ya kifahari! Sasa safari hii ujue wazi kabisa, Tino anachukua watoto
wake.” Sabrina hata hakuwa akijua kama kuna kesi inayoendelea dhidi yao.
Akabaki kimya akimsikiliza. Baba yake naye kimya. Mama huyo akaongea mpaka akayamaliza.
Alipoona Sabrina kimya na hakuna uungwaji mkono kutoka kwa mumewe, akataka
kurudi ndani.
Sabrina akamuita. “Naomba
unisikilize kidogo tu mama yangu.” “Kwa lipi?” “Sina jipya mama yangu. Ila nilitaka
kuwapa angalizo.” “Hututishi.” “Hata kidogo mama. Mimi sina nguvu. Nilishashindwa
muda mrefu sana ndio maana nilimuachia Yesu wangu atawale na anipiganie.” “Huo
ni unafiki Sabrina. Kama wewe kweli unamjua huyo Yesu, basi mpeni Tino haki
yake.” “Baba, naomba wewe unisikilize ili badaye kusiwe na majuto.” “Uta..”
“Hapana mama. Kama wewe huwezi kunisikiliza, tafadhali mwache baba anisikilize. Nisikilize tu baba
yangu.” Sabrina akasihi.
“Najua Sabina anategemewa
sana hapa nyumbani. Ni nguzo yetu tokea zamani.” “Kumbe unalijua hilo na…” “Mwache
amalize.” Baba yake akaingilia. “Nawasihi wazazi wangu, hata kwa kupiga magoti
nitapiga, mwambieni Sabina asijiingize kwenye vita na Jack.” “Atamfanya nini?”
“Baba na mama. Hata kama mmezoea kunipuuza, lakini naomba isiwe katika hili.
Tafadhali sana wazazi wangu. Baba, mwambie Sabina, asianze vita na Jack. Hata
nyinyi, chochote mnachopanga kinyume na Jack, acheni kabisa. Acheni vita
ya Tino, apigane mwenyewe, nyinyi isiwahusu.” “Huyo Jack atatufanya
nini? Ni kwa kuwa amekua naibu waziri wa fedha ndio anakuchanganya
akili?” Mama yake akaendelea kupayuka.
Sabrina akamgeukia baba
yake. “Baba, umenisikia? Vita yeyote mnayopanga dhidi ya Jackson, mjue
mnapigana na kina Msindai wote. Nimeishi na wale watu, nimewasoma. Katika
mapungufu yao yote ambayo mnayajua wanayo wao, basi iwe ya ndani wenyewe kwa
wenyewe watakuwa sawa na kuyanyamazia, ila si nje. Huwa hawakubali mmoja wao
ashindwe. Ukimgusa Jack, umegusa kina Msindai wote na kwao si kitu kidogo hata
kidogo, Kwa kuwa unawachafulia jina lao ambalo wanalilinda kwa sababu wana malengo
nalo kwa mpaka watoto wao. Unapomuona Jack leo ni kiongozi, hajajikuta tu, wazazi
wangu. Wale wanaandaliwa kuwa viongozi tokea watoto wadogo. Uongozi wa hii nchi
kwao si kwa Jackson na kaka yake tu, ni mpaka watoto wao. Macho na masikio yao
yapo kila mahali wakilindana mchana na usiku. Popote linapotajwa jina la
Msindai inakuwa ni kama umegusa antena zao, wanasikia na hawapuuzi.” Sabrina
akaendelea.
“Baba, mnamtegemea sana Sabina.
Nakusihi baba yangu, mwambie Sabina aachane na kina Msindai. Hata kama ameanza,
akatangaze huko kuwa, ameacha. Hamtawaweza kina Msindai.” “Sisi
tunatetea haki ya Tino.” “Sawa mama. Lakini hakika hii siku ikumbukwe. Msije
sahau kama niliwaonya. Baba umenisikia?” “Acha kututisha Sabrina. Unataka
kutufunga mdomo ili…” “Kuwaokoa, ili mbakie salama.” Sabrina akamalizia kwa
mama yake na kuendelea. “Mimi sijui huwa Tino anawaambia nin…” “Ukweli.
Ukweli mtupu. Ameongea ukweli na ameomba msamaha mpaka kwa vitendo. Ndio maana
anajenga hapa ili ikitokea watoto wake wanatelekezwa tena, wasihangaike. Yeye
ni binadaamu.” “Hakika Mungu awasaidie wazazi wangu.” Sabrina akawahurumia
sana.
“Atusaidie mara ngapi?”
Mama yake akaendelea. Sabrina akatulia kama anayefikiria mbele ya wazazi wake.
Akatulia kabisa kwa muda akiwa ameinama, mama yake akizungumza kishabiki. Akaongea
mengi kwa jazba akiropoka. “Kama hayo unayozungumza mama ni ya kweli na ndiyo yanayoendelea
huko mitandaoni na mtaani, basi..” “Inamaana wewe Sabrina ndio unasikia haya!?”
“Kabisa baba na Mungu wangu nishahidi, mpaka naogopa. Mimi nilitingwa na
shuguli nyingi kwa kuwa tulihamia hapa nikaacha mambo yangu Singida hayajakaa
sawa. Nikawa nipo hapa na kule nikihangaika kule kupaweka sawa maana niliacha
hata biashara zetu hazijakaa sawa. Sasa akili ikawa Singida japo niko huku
nikifanya mambo kwa haraka ili nitakapojifungua, nipate muda wa mapumziko. Na
nikajiambia leo lazima kila kitu kisimame, nije niwaone kabla lakutokea
likatokea nikajifungua, nikashindwa kuja kuwaona. Haya mama anayoongea hapa,
sina hata habari nayo! Na ndio maana najiambia kama mama haongezi chochote, ni
kweli kama ilivyo, basi kwa ukimya wa wakina Msindai, ujue si jambo zuri.”
“Muongo. Kaja kutuchota.” “Subiri kwanza mama Sabina.” Muwe akamtuliza.
“Twende taratibu Sabrina.
Inamaana mumeo hajakwambia chochote juu ya haya?” “Jack hawezi kuniambia baba
kwa sababu kama unavyoniona. Nilipata huu ujauzito mshono ukiwa mbichi kabisa. Huyu
unayemuona hapa ni dereva tuliyepewa na Jacinta, dada yake Jack. Sina
ninapokwenda bila huyu kaka mpaka nimeogopa kwa sababu ya cheo cha Jacinta.
Inawezekana kwa hicho kinachoendelea, huyu ninayedhani mimi kama ni dereva,
wala si dereva yupo hapa akilinda hawa watoto wa Jack.” “Wengine ni wa Tino.
Usije jisahau.” “Vile atakavyokuaminisha Tino ukaamini, sina jinsi ingine
nikakuweka upande mwingine ukakubali mama yangu. Lakini ninachotaka kusema,
Jack hataki nipandishe pressure kabisa nafikiri ndio maana wananificha na mimi si
mtu wa kushika simu kujua kinachoendelea mitandaoni. Kwanza kushika simu kwenye
ni shida. Hapa kwenyewe nilipo hata sijui simu yangu ilipo, mpaka naanza
kujilaumu najiambia itabidi nibadilike.”
“Kujibu swali lako baba
yangu, sijui. Nipo hapa kuwaona tu. Sijui chochote, na Jack yupo kimya juu ya
hili ila sasa ndio mmenifanya nifikirie. Kumeongezeka umakini sana pale
nyumbani. Hata aina ya ulinzi sio kama zamani. Mimi nilidhani ni kwa kuwa Jack
amekua Naibu waziri amepewa ulinzi na serikali, kumbe ni kuzuia hao watu wa
habari wanaokuja huku kwenu, wanaotaka kunihoji mimi wasitusogelee pamoja na
huyo aliyekuwa mke wa Tino, Lela ambaye mmesema ananitafuta kujua ukweli juu ya
watoto wa Tino. Sasa hivi ndio naelewa huo umakini wa wakina Msindai.” Sabrina
akafikiria tena kidogo na kuzidi kufunguliwa macho.
“Wazazi wangu, hiyo vita
mliyoanzisha na kina Msindai, hawatakubali. Na inamaana hata hapa
nyumbani wanajua kinachoendelea.” “Watatufanya nini?” “Msipoachana nao,
kwa hakika mtajua kwa vitendo.” Sabrina akamgeukia tena baba yake ambaye naye
ni kama aliingizwa kwenye jambo hajui chakufanya tena. “Baba, kila linapofika
kwenye swala la Msindai hata mmoja wao, ile familia hawafanyi kama hivi
sisi. Huwa wanaweka tofauti zao pembeni, wanasimama pamoja. Usimuone yule mzee
ni mkimya vile, yule mzee ni mtu wa usalama wa taifa wa miaka mingi mno. Anajua
mambo ambayo yatakushangaza, baba yangu.”
“Anawafundisha mpaka
wajukuu zake jinsi ya kumjua mtu mwenyewe kwa uhalisia ni kwa kumsikiliza kwa
makini, na kutopuuzia taarifa yeyote ile anayotoa mdomoni mwake hata kama ndogo
ya kiasi gani. Kwa kumsikia mwenyewe akiwaambia wale wajukuu zake, neno lolote
linalotoka kinywani mwa mwanadamu, halijatoka mdomoni bali moyoni.
Anawafundisha wale watoto wadogo kuwa wakimsikia mtu yeyote akizungumza kwenye
mazungumzo yasiyo rasmi kama hotuba zilizoandikwa na kuandaliwa, ila yale
mazungumzo ya kirafiki tu, basi kunyamaza ili kusikia moyo wa huyo mtu. Mpaka
akanifanya niwe makini sana kuzungumza nao wale watu. Na kuna jambo
anasisitizia wanae, taarifa yeyote wanayosikia, wasiwe wepesi kujibu na
kuchukulia hatua.”
“Huwa anarudia kusema bila
kuchoka, hata kwenye kuapishwa kwa Jack mara hii ya pili baada ya kutoka Ikulu,
tulipokusanyika kama ndugu tu, Junior akamuomba tena aongee chochote cha
kumjenga Jack, yule mzee akarudia tena, akasema siri ya kushinda jambo
ipo kwenye kutulia, kufikiria hatua zote utakazochukua ndipo kuchukua hatua. Yeye
anasema, kuchukua hatua za haraka ambazo hazijafikiriwa, mara nyingi ndipo
kushindwa kirahisi. Ni maneno ya yule mzee kwa kumsikia mwenyewe, mbele ya
wajukuu zake na wanae. Yule mzee sio mkimya na mjinga wazazi wangu, ila yupo
makini mno, na analinda familia yake kuliko nitakavyowaambia au mtakavyomuona
yupo mkimya vile mbele ya watu. Si mjinga. Amewafundisha watoto wake kutokukurupuka
kwenye lolote. Hiki mnachowafanyia kina Msindai, na mnaona wapo kimya, sio
kwamba wameshindwa! Hata kidogo. Wapo kwenye mipango yao na sidhani kama
itawaletea nyinyi matokeo mnayotarajia.” “Wat..” “Subiri kwanza
mama. Nakaribia kumaliza.” Sabrina akamkatiza mama yake kwa haraka.
Akaendelea taratibu tu. “Wazazi
wangu, najua mimi nimekuwa mtoto ambaye hamridhishwi na mambo yangu. Ndio maana
mpo tayari kusimama na mtu baki kama Tino ili tu ashinde dhidi
ya upande niliopo mimi. Lakini naomba mchukulie ujio wangu huu ni Mungu
amenituma kwenu. Si safari hii na si katika hili. Nitafuteni kuniangamiza
mimi kama Sabrina lakini si kwa vita na kina Msindai. Nawahakikishia wazazi
wangu, hamtashinda.” “Hii nchi ni ya haki. Sheria itasimama na haki
itatendeka.” “Sawa mama. Jambo la mwisho, nilikuja na zawadi. Je, mtazipokea?”
“Ili mje mseme hamkutelekeza nyumbani! Mnatujali kama Tino? Maana siku zote
mlitutupa, Tino ndiye anayetujali. Leo mnajirudi ili kupata ushahidi wa kuja
kusema eti na nyinyi mlikuwa mkitujali?” “Kama nimekuelewa vizuri mama, ni
umekataa kupokea vitu nilivyokuja navyo. Si ndiyo?” “Hatuna shida. Kamwambie
mumeo, amekumbuka shuka kumekuchwa.” “Kwa hiyo hutakuwa na shida hata
ukiona nakwenda kumpa mama Jabiri huyo jirani yetu? Maana nilinunua, nikaombea
kuwa iwe baraka kwa mpokeaji.” “Hatuna shida.” “Mama Sabina!” Mumewe akashangaa
sana kuwa wanawezaje kukataa!
Wakati akikataliwa zawadi
zake za vyakula dereva naye alikuwa amemfuata tena. Sabrina akageuka
alipomsogelea zaidi. “Simu yako ilikuwa ikiita sana, mwishoe nimepigiwa mimi.
Ni mumeo anataka kuzungumza na wewe. Anakwambia pokea simu.” “Nashukuru. Nakuja
sasahivi, acha niage tuondoke.” Akabaki amesimama. Sabrina akamgeukia
akimshangaa kwa nini haondoki! “Nimekwambia nakuja. Wewe tangulia tu kwenye
gari.” “Ameniambia nirudi na wewe kwenye gari. Nafikiri sababu ya jua.” Akajua
Jack ameshajua kinachoendelea. “Haya wazazi wangu. Mimi naondoka na kuwaacha na
amani ya Bwana.” “Ilikuwepo na itaendelea kuwepo.” Sabrina akaondoka hapo kwao
hata ndani hajakaribishwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaingia garini akakuta
Jack amempigia zaidi ya mara tatu. “Naomba tushushe hivi vitu hapo kwa jirani.
Siwezi kurudi navyo nyumbani.” Akamuona yule dereva kama anasita kumwambia
kitu. “Ni nini? Niambie tu Chali.” “Nina familia kubwa hapo kwangu, mama
Msindai! Ni kama ukoo mzima umehamia hapo mpaka namuhurumia mke wangu. Kama
nyumbani wamekataa, basi naomba na mimi kidogo.” “Basi ni vyako vyote. Mungu
alikusudia kukubariki wewe. Ila naomba uturudishe sisi nyumbani kwanza ndio
upeleke hivi vitu kwako.” “Mungu akubariki.” “Amina.” Akaamua kurudisha simu ya
mumewe.
“Sikujua kama leo
unakwenda nyumbani!” Jack akawa kama analalamika. “Sikupanga
kukaa muda mrefu. Nilitaka kuwaona kabla sijajifungua.” “Pole.” Sabrina
akataka kama kumuuliza lakini akasita na kunyamaza. “Kwa
hiyo mnarudi nyumbani?” “Naona nikapumzike tu.” “Upo sawa lakini?” “Nafikiri.”
Akajibu Sabrina na kutulia. “Basi nitakuona jioni,
tutazungumza vizuri.” “Sawa.” Sabrina akakata simu akiwa na maswali
mengi hajui aanzie wapi kuuliza na hakuwa akijua kama mambo ndio yapo yalivyo!
Akataka kujilaumu, lakini akaona haitasaidia. Akaumia sana kuona familia yake
inavyojipanga kushindana naye wala si kumtetea.
Dereva akaendelea
kukanyaga mafuta kuwatoa huko Chalize kuwarudisha nyumbani. Sabrina aliomba
hata redio izimwe. Dereva akaizima, kukawa kimya kabisa. Akarudisha kiti nyuma,
akabakia amejilaza hapo akisugua tumbo lake taratibu. Wanae wote wakapotelea
usingizini, kukaendelea kuwa kimya hapo garini. Dereva akaendesha taratibu kwa
makini mpaka kwake. Bado ilikuwa mapema tu mida ya saa saba mchana wakati mlinzi
akiwafungulia geti. “Naomba niitie kina dada, wawachukue hawa wote.” “Wewe
hushuki?” “Hapana. Nataka nikamuone daktari mara moja.” “Kwema?” “Kwema tu.”
Sabrina akajibu na kurudi kujilaza kitini, kimya.
Wakaitwa wasichana wa
kazi, wakachukua watoto. Wote wakiwa bado wamelala. Sabrina akatoa maelezo na
kuondoka na dereva, mpaka hospitalini. “Wewe niache hapa. Endelea na shuguli
zako. Nikimaliza nitakuita.” “Unaweza kukisia muda?” “Sijui. Lakini wewe usiwe
na wasiwasi. Unaweza hata kwenda nyumbani ukashusha mizigo yako. Nitakutaarifu
kutokana na nitakavyozungumza na daktari.” “Sawa. Nakushukuru sana dada yangu.”
“Karibu.” Dereva akaondoka Sabrina akaingia ndani, akamwambia mtu aliyemkuta
hapo mapokezi kuwa hajisikii vizuri, anahisi pressure ipo juu, anaomba kumuona
daktari, zaidi daktari anayemuona kwa maswala ya ujauzito. Akaambiwa yupo
kliniki na kina mama wengine, ila anaweza kuanza kupimwa.
Akakubali, vipimo
vikaanza. Kupimwa, pressure ikawa juu sana. Wakamwambia daktari ambaye huwa anamuona
kwa kliniki za ujauzito. Akafika hapo alipopumzishwa Sabrina, kitanda cha
sehemu ya mapokezi tu. “Huyu mtoto bado kidogo, mama Msindai.” “Basi nipe dawa
nipumzike kabisa. Nimekuwa na hekaheka nafikiri ndio maana imepanda. Nikitulia
itatulia.” “Nitakupa dawa na nitawaambia wakuwekee maji. Nataka ulale mpaka
yaishe kabisa. Halafu nitakuja kukupima tena baadaye.” “Sawa.” Akamtumia ujumbe
yule dereva afike hapo kumchukua saa 11 jioni kisha akatulia kabisa ili
asisababishe madhara kwa mtoto wake. Alipopewa tu dawa akalala kabisa hata
hakutaka kujua linaloendelea duniani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ambacho hakuwa akijua
Sabrina, moto ulishawaka na mama Msindai alikuwa kooni kwa wanae mchana na
usiku. “Sikuwaambia mimi hawa watoto wa kizungu
watatuletea matatizo?” “Hakuna tatizo mama. Naomba utulie. Hii fujo yote
inakaribia kufika ukingoni. Na safari hii tumeamua kuikomesha kabisa.” “Hakika
Mungu akusaidie Junior. Hii familia inaangamia mikononi mwako hivihivi!”
“Hakuna kuangamia mama. Tafadhali nipe muda wakurekebisha bila simu za kila
wakati! Unanifanya nashindwa kufikiria.” “Siwezi nikatulia hivihivi sijui
kinachoendelea!” “Basi naomba muda, nitakuwa nikikupa muendelezo kwa kila hatua
nitakayokuwa nikifikia.” Junior akamuaga mama yake. Na kumpigia simu
Jacinta.
“Umefikia wapi?
Nashindwa kufanya kazi sababu ya simu za mama.” “Mimi nimeacha kupokea simu
zake mpaka nikamilishe hili. Nilifikiria huyu askari kanzu atoke huko jela
mwishoni mwa juma hili, ili kujua msimamo wa mwisho wa Max atakapozungumza na
huyo mwanasheria wake.” “Mbona ni kama ulisema amejiridhisha kuwa Max amekataa
kuwapa ushirikiano?”
Junior akasikika kuchoka kusubiri. “Anasema ni kama
wanaanza kumshawishi na anashawishika zaidi kutokana na ndugu wa Sabrina
kuonekana kutoa ushirikiano. Wanaye mngojea ni Tino ambaye inasemekana
anatarajia kurudi siku za karibuni. Hawajampa tarehe kamili. Ila ndugu wa
Sabrina ndio wanaomshawishi na wamemwambia safari hii Tino pia yupo upande wake
na wao wanao ushahidi wa kutosha kumtetetea.” “Daah!” Junior akachoka
kabisa.
“Nilikwambia
jana, Junior. Pengine umesahau.” “Nina mambo mengi Jacinta! Tafadhali nisaidie
hili liishe nimtoe mama mgongoni kwangu.” “Nyinyi mmetaka kulimaliza moja kwa
moja bila madhara, Junior. Mngekubali kutumia njia yangu, sasahivi tungekuwa
tumeshasahau.” “Daah!” “Hawa watu wanataka kuharibu. Lazima kuwadhibiti. Sasa
kama wewe na baba mnataka kwa njia zenu, juwa itachukua muda mrefu. Lazima kuwa
wavumilivu. Ukitaka vya haraka, mwambie baba mniachie mimi.” “Acha nifikirie,
jioni nitakupigia simu.”
“Sawa.” Jacinta mjeshi, hacheki na kima, hajui
kubembeleza. Junior mtaratibu, anataka mambo kwa hekima kama baba yake na
Jacinta alimjua kaka yake akawa akimchukulia taratibu na kufanya vile
anavyotaka yeye akijua mwishoni atachoshwa tu. Akamuacha mpaka asalimu amri
mwenyewe. Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni Sabrina akarudi
nyumbani na kupitiliza kuoga ndipo akaomba aletewe watoto wote. “Huyu
ummemlisha nini mbona kitumbo kimejaa hivi! Eti Brayan.” “Pina ametoka kumpa
uji sasahivi.” Sabrina akabaki ametulia hapo kitandani wanae wakicheza mpaka
Jack aliporudi. “Vipi?” “Sasahivi nipo sawa. Nilijipandisha pressure. Nafikiri
mshituko na kuumia.” “Nisikilize Sabrina. Usinichukie kwa sababu sikutaka
kukuumiza. Nilijua ungejua mipango ya kwenu yakutaka kumsaidia Tino kupata
watoto ingekuumiza sana.” “Najuta Jack! Najuta sana. Nahisi mimi mwenyewe ndiye
niliyesababisha kumleta Tino karibu yao.” “Hata kidogo. Mwenzio nimejifunza
kutoka kwa kaka kuwa makini. Acha niwatoe hawa nje, tuje tuzungumze.” Jack
akacheza na wanae kidogo, akawatoa nje na kuwaambia wasubirie wakiwa na michezo
yao.
Akarudi kwa Sabrina.
“Tino ndiye aliyemtafuta Sabina kwa mara ingine tena akamkabidhi begi lenye
vitu alivyotaka wapewe watoto, ukakataa, akalichukua mama yenu.” Sabrina
akatulia akisikiliza. “Ukiwa kwenye harusi ya Pendo huna taarifa, Sabina na
mama yenu walikutana na Tino ambaye tayari anayo restrain order. Si
ndivyo ulivyoniambia?” “Lakini nilikaa Villa na hotelini kwa pesa ya Tino,
Jack. Usilisaha hilo. Ni kama mimi mwenyewe nilijirudisha tena kwa Tino!
Najitetea vipi?” “Hizo taarifa zilishafutwa. Hakuna sehemu inayoonyesha ulikaa
Villa wala hotelini.” “Jack!” Sabrina alishituka mpaka akakaa.
“Si kazi ndogo. Sabina,
mama yako na Tino walirudi pale hotelini na kwenye Villa kutafuta ushahidi
kuonyesha nilikutelekeza wewe na watoto ndipo Tino akawasaidia.” “Jack!” “Kweli
tena. Sijui ni kwa nini ndugu zako wanataka kuniangamiza, Sabrina.” “Ni njia ya
kunikomoa mimi tu. Ukiona jinsi Tino alivyotengeneza pale nyumbani! Unaweza
potea. Amewabadilisha kwa mahela anayowapa, nafikiri ndio maana
wanamng’ang’ania.” “Ila Sabrina, mwisho sio mzuri. Nasikitika kusema hivi kwa
kuwa ni ndugu zako, lakini mwisho si mzuri hata kidogo. Hivi tunavyozungumza,
yupo mtu wa usalama wa taifa yupo alikofungwa Max, kama na yeye ni muhalifu, akifuatilia kila
kitu.” “Jackson Msindai!” “Kabisa Sabrina. Hawa watu wamepanga kutuangamiza, baba
hawezi kukubali. Wanafuatiliwa kupita kiasi. Namsikitikia Sabina. Amejiingiza
pabaya mno. Hawawezi kumuacha.” Jack akaendelea.
“Walimpa kila sababu
ajitoe ili asiangamie na Tino pamoja na Max, lakini inavyoonekana yeye Sabina ndio
yupo mstari wa mbele, akiunganisha pande
zote ambazo zipo kinyume yetu. Mara kwa mara anaonekana huko rumande
akimshawishi Max, akiwa ametumwa na Tino.” Sabrina akaumia sana. “Hivi
tunavyozungumza, Sabina amemtafuta aliyekuwa mke wa Tino.” “Lela?” “Nafikiri
huyohuyo. Sasa kwa kuwa nafikiri wamegundua simu zao zinasikilizwa, wameacha
kuzungumza kwa simu. Lakini Sabrina, hili nakwambia wewe kwa kuwa
imeshajulikana kuwa unajua, nimeombwa kuzungumza na wewe ili tuwe ukurasa
mmoja. Tafadhali usipandishe pressure kwa ajili ya haya.” “Wewe niambie tu. Maana
mama alizungumza hata juu ya Lela, lakini akiwa na jazba sana. Na naumia kuona
kumbe ni Sabina mwenyewe ndiye aliyemtafuta Lela! Hakika ndugu zangu
wananichukia Jack. Nilijua chuki dhidi yangu imeisha, nipo upande woa, lakini
hili limewaanika wazi kabisa! Wamemchagua Tino, Max na wengine dhidi yangu!
Tena Sabina ndio mstari wa mbele akishindwa hata kuwasiliana na mimi nikijua
yupo busy na kazi kumbe ana muda wa kuzunguka ili kuniangamiza!” Sabrina
akazidi kunung’unika.
“Nikikwambia Sabina
anafuatiliwa, ni anafuatiliwa kila aendapo. Walikutana na huyo aliyekuwa mke wa
Tino. Sabina amemwambia kuwa Tino alimsaliti wakiwa kwenye ndoa, akazaa na
wewe. Kwa hiyo amshitaki Tino.” “Sasa mbona tena wanageukana na Tino?” “Wajanja
sana. Hiyo ni akili waliyopewa na Max wakiwa na wakili wao. Bila kujua, Max aliporudi
ndani huko rumande waliposhikiliwa na huyo askari kanzu, akamueleza kila kitu,
mipango yote wanayopanga. Ndio maana sasahivi kila wakienda kumtembelea Max, na
huyo askari kanzu anatembelewa. Anakaa nao karibu kujua wanachopanga na
kuwarikodi. Sasa tulitaka kuachana na Max ila baada yakupewa onyo kali. Max
alionekana kukataa mwanzoni. Ila sasahivi ni kama ameanza kushawishika ndio
sasa na yeye kesi yake inataka kusomwa ili ahukumiwe kwa makosa yake.
Nasikitika kwa kuwa hata mkewe hatabaki salama.” “Jamani Tino anaangamiza wengi!”
Sabrina akasikika kuumia zaidi.
“Sana Sabrina. Kaka na baba
wamesema wanataka haki itendeke bila kuonewa mtu wala kuachwa mtu ili kukomesha
hili kabisa.” “Mzee Msindai!” “Ni vile mama hajui kama baba anashugulikia hili
kwa undani. Nikikwambia amefanya, ni zaidi nitakavyokwambia na baba huwa akifanya
jambo anafanya kikamilifu mpaka likamilike sio nusunusu. Akikwambia anaweka
kikomo, ujue anaweka kikomo. Ameshampata yule daktari. Amehojiwa kisheria
kabisa. Ameeleza kila kitu juu ya mipango waliyokubaliana na Max juu ya kuuwa hawa watoto. Na amefungiwa
mahali mpaka kesi ikamilike.” “Jackson!” Sabrina akazidi kushangazwa jinsi
mambo makubwa na mazito yanavyoendelea yeye akiwa hana hata habari!
“Baba hataki kufanyike kosa. Wakimfikia na
kumbadilisha mawazo au hata kumdhuru ili ashindwe kutokea mahakamani kutoa
ushahidi wake!” Sabrina akabaki ametoa macho. “Amekusanya ushahidi wote tena
kwa haraka na kumkabidhi wakili wetu. Aliyekuwa akisubiriwa ni Jacinta, upande
wa Max na kujaribu kumtoa Sabina. Lakini kwa jinsi nilivyoona, imeshindikana.
Sabina amekusudia kwelikweli. Na inavyosemekana amewahakikishia mama yenu yupo
tayari kutoa ushahidi pia, ili kumsaidia Tino kwamba wakati mimi
nimewatelekeza, eti yeye na Tino ndio walikuwa wakiwalea wewe na watoto.” Sabrina
akazidi kuumia. “Naomba turudi kwenye swala la Lela.”
“Ndio hivyo walivyokuwa
wamepanga kama kumtibua Lela. Max amewahakikishia popote kwenye harufu ya pesa,
Lela anakuwa kama mwendawazimu hawezi kutulia. Kwa hiyo wamemchokonoa tu, ili aanzishe
tena kesi ya madai. Itabidi uchunguzi ufanyike ili kujua kama kweli Tino alizaa
nje ya ndoa. Watatafutwa watoto walipo. Mahakama itaamuru watoto wafanyiwe
vipimo ili kujua kama kweli ni wa Tino, si itabidi sasa DNA ifanyike kwa kuwa
mahakama imeamuru! Ikishajulikana ni watoto wa Tino ndio sasa wao waendelee kuanzia
hapo mpaka Tino aje apate watoto. Kwa hiyo Lela atakuwa ni kama anachokonoa tu.
Sasa inavyosemekana, au walivyosikia hao watu wakati Sabina akizungumza na Lela
ni kuwa, Lela akutafute wewe, akuulize. Na ndio maana nimetumwa kukwambia ili
ujiandae.” “Mimi sitaki kukutana na Lela. Sitaki kabisa Jack. Kwa sababu najua
anachotaka ni kujua kama kweli nilikuwa na mahusiano na Tino na kama nilizaa
naye. Sipo tayari kulijadili hilo tena. Na yeyote yule, sitaki. Nataka nitulie
kabisa mpaka siku za huyu mtoto kufika, azaliwe.”
“Leo niliingiwa hofu
nilipoona pressure ipo juu na daktari kuniambia mtoto bado!” “Daktari!?”
“Ilibidi kwenda mimi mwenyewe kujisalimisha Jack. Nilitoka nyumbani nikiwa
nimechafuka kwelikweli. Ile kukaa njiani mpaka hapa nikiwafikiria watu wa
nyumbani kwetu, ikanipandisha pressure ikabidi kwenda tu hospitalini. Ndio
nikaambiwa pressure ipo juu, na mtoto hayupo tayari.” “Kwa nini hukuniambia?”
“Nilitaka anipe dawa, nilale kabisa. Sikutaka kuzungumza na yeyote yule.
Tafadhali na wewe nisaidie Jack. Niweke mbali na hao watu au kesi, angalau
mpaka nijifungue salama. Haya mambo yapo tu. Hizi kesi zipo tu. Lakini
nikimpoteza huyu mtoto ndio nimempoteza kabisa, hasara yangu mimi.” “Ni hasara
yetu. Na mimi nataka mwanangu azaliwe salama. Ila nakuelewa. Nitamwambia kaka
wakuache mpaka mwisho kabisa itakapolazimu. Hata kama itabidi kuivuta hii kesi,
iendelee kuvutwa tu, ili utulie tupate huyo mtoto.” Sabrina aliingiwa na hofu
hakujua kama mambo ni makubwa kwa kiasi hicho.
“Nikuulize kitu Sabrina?”
“Juu ya nini?” “Ujue Tino atafungwa na anaweza akahukumiwa kifungo cha maisha
kwa kusudio la kutaka kuua?” “Hakika sijali Jack. Acha Mungu ashugulike nao.
Sina kosa, ni kwa nini wanataka kuniangamiza bila sababu? Tino hakutaka hawa
watoto kabisa. Kwa nini leo anafanya hivi? Na upande wa Sabina, yeye ni dada
yangu mimi, kwa nini asinisaidie kama hivi wewe unavyosaidiwa na watu wa
nyumbani kwenu! Wote wamesimama na wewe hata kama wanaona hustahili, lakini wapo
kukusaidia. Kilichowashinda wao kunilinda ni nini mpaka wakamuacha Mungu wangu
ashuke, apigane vita yangu? Acha Mungu ajitukuze hata katika hili Jack.
Sikutaka kuua viumbe wake, ndio ilikuwa kosa langu! Acha ashuke yeye mwenyewe
Mungu anitetea. Wamemtafuta Mungu mpaka ameitika. Acha ashugulike nao. Na leo
nimemuonya baba nikimwambia amwambie Sabina aache hila. Sasa sijui!” “Nahisi
wameshachelewa.” Hilo likamshitua Sabrina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kikulacho
Ki Nguoni Mwako. Kila Pande Imejipanga. Nani Mshindi?
Nani Mwenye Kisu Kikali? Usikose Muendelezo
0 Comments:
Post a Comment