Wakati Wa Mungu.
iku
inayofuata walikutana kwenye viwanja vya bunge ikiwa mapema tu. Kila mtu
alikuwa amependeza kwa shuguli nzima. Jack akawapa habari za kifo cha mtoto wa
kwanza wa Ngoi. Junior akapiga simu kwa Willy wote wakatoa pole wakiwa
wamebakisha muda mfupi waingie bungeni. Ukweli ilisikitisha. “Kesho tutakuwa hapo kukuunga mkono Willy. Poleni sana.”
Junior akamalizia ili waingie ndani, wasichelewe. Wakaagana na kuanza kuelekea
ndani.
Wakamuona
Jack anamvuta mkewe pembeni. “Umeipenda hii suti?” “Nimeipenda na umependeza
sana Mheshimiwa Msindai.” Jack akacheka. “Asante Brina.” “Asante ya nini
tena!?” “Kunifikisha mpaka hapa. Hakika usingekuwa wewe watu wote hawa
wasingekuwepo hapa leo wakifurahia hivi. Ushauri wako wakuendelea kubakia
kwenye siasa kule Singida ndio umenisogeza hapa. Nakushukuru.” “Karibu.”
Angalau hilo likamfurahisha Sabrina. Katika wanaume wote aliosimama nao, Jack
amemtambua.
“Hayo
mabusu mheshimiwa Msindai ungeyaendeleza ukitoka huko kuapishwa.” Jacinta
akafanya wote wakawageukia wakamkuta Jack akiwa anambusu mkewe. Sabrina
akacheka na kusogea. Jackson akawaaga
wanae vizuri na kuwaacha mama yao amewashika mkono, akaingia sehemu nyingine
akiwa na kaka yake, waziri Msindai wakati wageni wao wakielekea sehemu wanayofikia
wageni hapo bungeni.
Jackson
Msindai akafanikiwa rasmi kusimama ndani ya bunge, akiwa anakaribia kuwa
mmoja wao. Ikawa ni ndoto yake iliyotimia akiwa anajua kabisa aliyefanya yote
hayo ni Sabrina. Alikaribia kupishana na huo muujiza akiwa amefunga, ameomba na
mkewe, wakasubiri bila kuona mabadiliko yeyote huko chamani. Jackson ambaye
alitegemea mfungo wake ulete matokeo ya haraka ikawa sivyo mpaka akakata tamaa
na kutaka kuachana kabisa na mambo ya siasa. Lakini kumbe pale alipokuwa
akipatizama yeye, sipo Mungu alipokuwa amemkusudia kwa wakati ule. Mungu
alimuwazia mema zaidi, tena kwa haraka. Ikawa amepata zaidi ya alivyoomba tena
kwa haraka sio kusubiri mpaka wakati wa uchaguzi mkuu miaka ijayo, ndipo
agombanie tena.
Vikafanyika
viapo hapo, Jackson Msindai akaapishwa rasmi kuwa mbunge wa Bunge la Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania. Baada ya hapo ikawa tafrija fupi. Ukweli kulikuwa na
amani. Hapakuwa na maneno maneno. Ikawa kama mama Msindai naye anajihami na
Sabrina. Sabrina naye hata hakumsogelea. Jacinta akawa karibu naye kila wakati.
Wakati wanakaribia kuondoka Sabrina akacheka na kumuangalia Junior.
“Nini?”
Junior akauliza na tabasamu. “Mimi nina swali linalonisumbua kidogo, shem.
Nilikuwa nikisubiria wakati Claire hayupo nikuulize.” Wakamuangalia Claire pale
alipokuwa na watoto wa Sabrina na Clei wakiendelea na yao. Wakawa wakicheka
zaidi kumcheka Claire. “Mwanangu mtu mzuri sana tu, ila Clei ndio anamchokoza.”
Joy akafanya wacheke zaidi. Junior akamgeukia Sabrina. “Karibu.” “Eti mimi
nimekuona. Sijui kama nipo sahihi! Katika kila ugomvi wa Claire na Cleiton,
huwa huingilii kabisa. Hata mziwanda wako alie, hutawaingilia utambembeleza tu.
Ni kwa nini?” “Asante Sabrina. Na mimi nilishamlalamikia huyu Junior.
Nikamwambia akimkemea Clei mara moja tu, ataacha kunilizia mwanangu. Clei
ananifanya mimi kama bibi yake, ananichezea hanisikilizi.” Joy akalalamika.
“Ngoja
nikwambie ukweli Sabrina. Katika kila baraka Mungu anayokupa, kuna jinsi ya
kuishi nayo. Junior mume wa Joy wa kabla hajawa waziri, sie mume huyu aliyekuwa
waziri. Kuna garama zake tunalipa ambazo kama mimi na yeye Joy hatujakaa sawa,
tukakubaliana, familia yetu ingeyumba sana. Na wewe utakuja kuona. Jack yule
aliyekuwa muhasibu wa Singida, hatakuwa huyu aliyeapishwa leo. Ni jambo zuri,
lakini hii baraka itakuja na mabadiliko mengi sana, lazima ujiandae haswa.” “Ni
kweli mwaya.” Hapo hata Joy akakubali.
“Maisha
ya Jack sijui kubeba watoto na kukumbatia hivi kila wakati, yatapungua kwa
asilimia karibu na 80 kwa sababu ya majukumu atakayokabidhiwa. Kipo kipindi
hatakuwepo nyumbani, itakulazimu kulea peke yako. Hayo anayokufanyia sasahivi
kwa ukaribu hivyo, hataweza kuyafanya japo atatamani. Vipo vipindi utauguza
watoto peke yako. Kwa asilimia 88 utaishia kulea hao watoto peke yako, kwa
maisha yao ya kila siku. Ndicho kinachotokea kwangu na Joy. Hata nikiwa pale
Dar, nakuwa na majukumu ambayo yananinyima muda wa kuwa na watoto kwa karibu
kama hivi Joy. Napata nao muda mfupi sana, na sitaki nikiwa nao niwe mtu wa
kesi tu.” “Lakini kweli. Maana unaweza kujikuta watoto wanakuona kama mwalimu
mkuu wa shule zile tulizosoma sisi za kuchapwa sio kama hawa watoto wa siku
hizi wanaonywa kwa maneno tu.” Jacinta akaongeza na kucheka wakikubaliana naye.
“Ewaa!
Yaani wewe ukirudi nyumbani ni kesi na adhabu tu! Watoto hawajakuona muda
mrefu, wanahamu na wewe, na wewe unarudi nakuanza mashitaka na adhabu! Hakuna
mahusiano mengine isipokuwa kujibu mashitaka! Hapana. Mimi huwa namwambia Joy
awaadhibu yeye mwenyewe anayeishi nao kila siku. Anajua wapi pakukemea na
wakati gani wakupooza. Sasa mimi nikiwaadhibu, naondoka nikiwa nimegombana nao,
nakuwa sina muda mwingine wakutengeneza mahusiano mengine.” “Cleiton atasikia
kila kitu lakini si kwenye swala la Claire jamani! Sijui yukoje yule mtoto
jamani!” Wakacheka.
“Lakini ukweli, wao wenyewe. Huyu Joy na
Claire hawawezi kuwa sehemu bila Cleiton.” Wakaanza kucheka. “Huwa wanamuita
wao wenyewe.” CJ akaongeza, Joy akazidi kucheka. “Nyumba inapooza bwana!”
“Umemsikia sasa Joy mwenyewe?” Junior akauliza. “Wanaweza wakawa na safari zao
wao wawili, Joy na Claire, lakini hawawezi kwenda bila Clei. Hata kama mwanangu
anashuguli zake, basi watambembeleza mpaka waongozane nae.” “Nikienda sehemu
ananisaidia kuniangalizia mwanangu wakati nafanya mambo yangu.” Wakazidi
kucheka.
“Kwa
hiyo shem ushawaona hawa ni waarabu wa pemba?” Sabrina akauliza akicheka.
“Haswaa! Wanajuana kwa vilemba. Huyu Joy hawezi kuwa popote bila Clei. Popote
alipo Joy, atamtaka na Clei awepo. Muda na wakati wowote Clei akiwa hayupo
shule, ukipiga simu basi ujue atakuwa yupo na mama yake. Na hapo ujue lazima
Claire naye yupo hapo akinyonya vidole vyake huku akimshikashika mama yake.
Sasa na yeye Clei akiwa katikati yao hawa, hana chakufanya kwa kuwa michezo
yake na Claire haiendani, basi mchezo wake ni vile anavyomchokoza mwenzie,
akilia ndio anaona raha. Wakimfukuza ni dakika 10 tu.” “Tena hizo ni nyingi
dad. Wao wenyewe huwa wanamuita.” CJ akaongeza nakufanya wazidi kucheka.
“Kumbe!”
“Muulize Joy huyu hapa. Hawajiwezi bila Clei. Lakini kingine na kikubwa mimi
shida yangu si Cleiton. Shida yangu ni huyu dada yao. Claire. Claire anakipaji
cha uongozi kama huyu anti yake. Mbali na vilio vya Clei, muulize CJ jinsi
anavyojua kujipangia mambo yake na kuyasimamia mpaka huwa anatushangaza.”
“Kwani si ndiye aliyetufanya tusije huku siku moja na mama! Anasema alikuwa
tayari ameshamuahidi rafiki yake atahudhuria birthday yake, eti alishanunua
mpaka zawadi, lazima yeye aende huko. Halafu alivyo sasa, ananiambia.” Jacinta
akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko. Wakaanza kucheka.
“Eti,
wewe anti tangulia tu na kina bibi. Usimuache Clei. Halafu utatutafutia usafiri
mimi na mama pamoja na CJ utufikishe Dodoma kesho yake.” Walicheka sana.
“Nikampigia simu baba yake. Nikamwambia mwanae ananipanga! Na kashaniagiza
kesho nimtafutie usafiri wake, mama yake na CJ. Ila Clei naweza kutangulia naye
tu.” Wakazidi kucheka. “Akiwa na jambo lake, hana kusitasita.” “Halafu ni msafi
sana, kila kitu chake anapangilia vizuri huwezi kukuta vitu vyake vinazagaa
hovyo.” CJ akaongeza. “Na kweli anti yangu ni msafi haswa. Anajipenda kweli!”
“Namuona. Kila wakati vitu vyake visafi kama mama yake.” Sabrina akaongeza.
“Mwenyewe anasema yupo kama anti yake wala si mimi!” Joy akaongeza.
“Basi hata akiwa shule yupo hivyohivyo. Very
smart mpaka huwa anasifiwa. Mungu akimjalia, anaweza kuwa kama anti yake
Jacinta.” “Mimi nimemwambia nataka awe zaidi yangu.” Jacinta akafanya wacheke.
“Na mwenyewe anapenda sana kuongoza hata shuleni kwoa ni kiongozi. Sasa huwa
namwambia watu kama kina Cleiton wapo wengi tu kila mahali. Lazima yeye
mwenyewe ajue jinsi ya kumkabili kama anti yake anavyoongoza wanaume wenye kila
haiba na hashindwi.” “Lakini anasema Clei amezidi sana.” Joy akamtetea
nakufanya wazidi kucheka.
“Shemeji
yangu unahekima!” “Inabidi kumuandaa! Yeye amezaliwa mwanamke mwenye kipaji cha
uongozi. Atafanyaje akiwa analia mbele yao huku ananyonya vidole?” “Jamani
mwanangu ataacha kunyonya vidole! Bado mdogo.” “Sawa Joy.” Junior akakubali
bila shida. “Ni vile anampenda.” Sabrina akaongeza. “Tena nakwambia anampenda
sana Clei. Japokuwa hakawii kumliza, lakini hasikii raha bila ya kumuona.
Nikimuita sasahivi hapa Clei, nikampa kitu cha kufanya hapahapa, dakika tano
nyingi. Claire ataacha kila mchezo pale na kuja kumfuata hapa. Yeye mwenyewe
anamfuata Clei. Sasa ndio nimemuachia kuwa Clei iwe ni jukumu lake mwenyewe.
Hawezi kumkwepa Clei kama vile uwe bosi kwenye ofisi, halafu upate watu wa
chini yako wabovu. Utaacha kazi?” “Hapana.” Akajibu Sabrina.
“Basi
ndio nimemuachia Clei awajibike naye yeye mwenyewe. Lazima kesi zake ajue jinsi
ya kuzikabili yeye mwenyewe. Hatuwezi kumsaidia kukabiliana na kila matatizo
kwenye maisha yake. Atahangaika naye hivyohivyo mpaka atakuja kummudu tu. Na
akisha mmudu basi ataacha kulialia hovyo. Atakua hamsumbui tena. Ila Clei
akizidisha kwa mdogo wake huwa CJ naye anammudu Clei, anajua jinsi ya
kumtuliza.” “Tena wakati mwingine anamsikiliza CJ kuliko mimi, mpaka mimi huwa
ndio maana namrushia viatu maana kumkimbiza simpati.” Wakazidi kucheka.
Wakapata
wakati mzuri ndipo wakaondoka hapo na mumewe kurudi hotelini. Walikuwa wakikaa
hapo kwa siku ambazo bunge linaendelea. Safari hii Sabrina aliaga chamani huko
Singida. Hakutoroka na bado alikuwa akiwasiliana nao kwa simu. Ila hawakuwa na
uhakika kama Jack na mkewe watakuja kurudi tena Singida. Likabakia fumbo huko
Singida japo Sabrina na Jack waliwahakikishia pale ni nyumbani lazima warudi
tu.
Siku
inayofuata Jack na familia yake wote wakaondoka Dodoma kwenda Dar. Ila Jack na
Junior walikuwa wakienda msibani kwa siku moja tu kisha kurudi tena Dodoma
kuendelea na shuguli za Bunge. Sabrina akabakia hotelini na wanae wakimsubiria
Jack arudi, amalize shuguli zake za Bunge warudi kwao Singida.
Hakuna
Msiba usiokuwa na Mwenzie.
J |
ack na Junior wakarudi hapo Dodoma wakiwa bado
hawajamzika kaka yake Willy. Waliamua kusubiria ndugu wengine kwa mazishi.
Sabrina akawa akibakia hotelini wakati Jack akihudhuria vikao vya bunge.
Alijawa furaha huyo, Sabrina akawa akimcheka tu. Juma hilo nalo likaenda
Sabrina akiwa anapata mapumziko yake na wanae. Juma lilipofikia ukingoni,
wakiwa wametoka kumzika tu mtoto wa kwanza wa mzee Ngoi, Patric, dada yao
mkubwa, Stella, akiwa anaoga bafuni, kutoa vumbi la makaburini, na yeye
akaanguka na kufa papohapo huko bafuni. Nazo zikawa habari za kushitua sana.
Huyo dada alikuwa na pressure inayopanda, akahisiwa pengine ilikuwa juu ila
akashindwa kutumia dawa zake sababu ya msongo wa msiba wa kaka yake.
Pendo
akampigia tena simu Sabrina. Akamuelezea kila kitu. “Lakini
dada, naomba muombe. Msipuuze. Hii roho ya mauti umefunguliwa, ipo kuangamiza.
Tafadhali mwambie Willy asipuuze. Ombeni ulinzi wa kimungu.” “Inahuzunisha wewe! Stella ameacha binti wazuri! Mmoja
anaenda chuo kikuu mwaka huu! Hata hajamuona mwanae akimaliza jamani! Inauma
sana. Japokuwa Stella hakuwa akinipenda lakini bado wanae wanamuhitaji,
Sabrina!” Akalia hapo Pendo, Sabrina akimtuliza.
Baada
ya ndugu kukusanyika, naye huyo dada akazikwa. Likawa jambo la kuumiza na
kushangaza kila mtu. Vifo viwili vyakufululiza! Sabrina akaona sio sawa.
akampigia mama yake Pendo. “Mama, naomba unisikilize.
Najua kwa sasa Pendo ametingwa na uzazi pamoja na ulezi, lakini ipo roho ya
mauti inayotembea kwenye familia ya Ngoi. Niliiona kabla ya kifo cha yule kaka
yao Patric. Nikamwambia Pendo, lakini alisahau. Naomba zungumza nao, Willy akae
sawa na Mungu, ili apate ulinzi wa ki Mungu. Na kama upo karibu na Prisca naye
uzungumze naye amkimbilie Mungu.” “Na mimi nilihisi sio kawaida jamani! Vifo
mfululizo hivyo! Nitazungumza na Pendo pamoja na Willy. Hiki sio kitu cha
kawaida jamani! Wataisha wote!” Wakazungumza na mama Kenton mpaka
Sabrina akaridhika kuwa huyo mama amemuelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya Bunge kuisha Jack na Sabrina wakarudi Singida. Safari hii wakapokelewa kama
mashujaa kwelikweli. Hakuna aliyeamini kama wangerudi, wasijue bado Jack
anamasilahi makubwa sana kwenye hilo jimbo na Sabrina analishikilia hilo jimbo
kwa maombi. Safari hii waliporudi chamani hata wale waliogeuzwa mioyo
wakawa upande wa Jack. Jack huyu aliyerudi ni Mheshimiwa Jackson Msindai. Heshima
ikaongezeka na bado akawa akitoa ushirikiano wa karibu sana hapo chamani na
kwenye ofisi alikokuwa akifanyia kazi kuhakikisha anapaacha salama. Hilo nalo
likamuongezea heshima.
Falme Zote Zipo Kazini Zikitenda Kazi Na Watu.
B |
ado walikuwa wakipokea pole za kuondokewa na
ndugu zao hao wakubwa kwa kufa kwa kufuatana, bila kupumzika. Mtoto watatu wa
Ngoi naye akiwa baa na rafiki zake wakinywa, gafla akaanguka na kufa papohapo.
Ukawa mshituko mkubwa, kwani alinguka mbele ya wenzake wakadhani ni pombe
imemzidia. Kumuangalia pale chini ikawa ameshapoteza uhai. Usiku mkewe akiwa
anakaribia kulala, akiwa ameshazoea tabia ya mumewe kuchelewa kurudi nyumbani,
akapigiwa simu na marafiki zake waliozoea kunywa naye kuwa mumewe amepelekwa
hospitalini akiwa si mgonjwa ila maiti. Usiku huohuo Willy akapigiwa tena simu.
Na Pendo naye akampigia Sabrina. “Naomba tuombe wote
sasahivi Sabrina. Inakua kama tunapigwa na upofu hivi, tunasahau kuomba kabisa.
Inakua kabla hatujakutana wote na kuomba, basi jambo lakutuchukua akili
linatuingilia, tunashindwa kuomba, basi ndio tunasahau mpaka mtu anaanguka tena
na kufa! Wanaanguka kama upupu jamani! Sasahivi amebakia Willy wangu tu na
Prisca! Hapana Sabrina. Lipo jambo.”
“Tutaomba dada, lakini nakusihi sana mwambie Willy asimame
kama yeye mbele za Mungu ili Mungu mwenyewe aweke ulinzi wake kwake. Shetani
hana kazi ingine isipokuwa kuua, kuharibu na kuangamiza. Sina jinsi nyingine ya
kuwasihi ila hiyo. Dada, shetani anawinda watoto wa Ngoi. Ni kwa nini, mimi na
wewe hatujui.” “Mimi mpaka namuhisi ni
Zelda. Na hivi alizaa mtoto wa kike na akaona sasahivi ni kama watoto wa Ngoi wamemgeuka,
ndio anawatoa wampishe.” “Basi usipuuze dada, OMBENI.
Roho ya maangamizi imetumwa kwenye hiyo familia. Hakikisha haipiti nyumbani
kwako.” “Naomba tumuombee sasahivi Willy
wangu. Tafadhali Sabrina.” Wawili hao wakaanza maombi kama zamani.
Hilo
juma Pendo na Sabrina wa zamani wakarudia maombi yao ya zamani. Kila siku
walikutana kwa simu na kuomba. Japokuwa Prisca hakuwa akimpenda Pendo na wote
walijua, lakini Pendo alimpigia simu na kumtaka afike kwake wazungumze. Pendo
akazungumza naye taratibu kwa kina mpaka Prisca akakubaliana naye waombe
pamoja. Prisca naye akaingia kwenye kundi la Sabrina na Pendo. Maombi
yakaendelea huku bado wanasubiri kuzika. Willy na yeye akaanza kuomba na mkewe.
Mtindo wa kusema wapo busy, ukakoma. Mungu akawekwa mbele.
Hapohapo msibani,
nyumbani kwa marehemu walikuwa wakianza kuomba hapo, mpaka wanasahau kama ni
msibani. Mke wa marehemu kaka yao Patric, shemeji yao mume wa Stella, na watoto
wao, mke wa huyo marehemu, kina Pendo, Willy, na Prisca walikuwa wakiomba haswa
hapo msibani. Wakawa wakiomba ulinzi wa Mungu huku wakivunja roho ya mauti.
Walikuwa wakisubiria mida ya usiku ambapo wale wageni wanao ondoka hapo msibani
wakiondoka, basi wao wenyewe na watu wao wa karibu ndio inapoanzishwa sala
ya nguvu, mpaka kunapambazuka. Walifanya hivyo mpaka walipozika. Zelda hakuwa
akilala msibani. Na walimuona hapo kama mara moja tu, akarudi siku ya mazishi.
Na walipozika akaondokea hukohuko makaburini hakurudi tena hapo msibani.
Baada ya kumzika huyo
kaka yao, siku inayofuata Willy akampigia simu baba yake akiomba ndugu wakutane
nyumbani kwao, yaani kwa mzee Ngoi kwa ajili ya mazungumzo. Lakini Zelda
akakataa akiweka ugumu akisema kuwa hataweza kukaribisha wageni hapo nyumbani
kwake kwa kipindi hicho. Akatoa sababu nyingi zisizo na mashiko. Willy hakutaka
kubishana naye, akashukuru na kukata simu. Lakini baada ya kukata tu simu Willy
akawaambia ndugu zake waliokuwa wakisubiria jibu wakiwa wamekusanyika hapohapo
msibani kwa maombi kuwa watakwenda hivyohivyo ila kwa kumshitukiza yeye ambaye
ndio mlengwa mkubwa. Walitaka mazungumzo lakini lengo kubwa ni kufanya
maombi na yeye Zelda akiwepo.
Wakatangaziana siku tatu
za mfungo. Familia nzima wakaingia mfungoni wakijitakasa na kutaka kujisogeza zaidi
patakatifu kwa Mungu kwa ajili ya ulinzi wakijua vita inayowakabili mbeleni.
Kuanzia familia ya marehemu kaka yao Patric mpaka familia ya mtoto wa mwisho
ambaye ni Prisca, walikubaliana wote na watoto wao wafunge isipokuwa wale
watoto wadogo kabisa. Mpaka watoto wao wakakubali. Wote wakaingia mfungoni, Sabrina
naye akawasaidia. Akaungana nao kwenye maombi. Wakawa wakijiandaa kwa maombi
kama wanao kwenda vitani kumbe kwenye nyumba waliyozaliwa na kukulia watoto hao
wanao uwawa mchana na usiku, ila safari hii Zelda akiwa mama mwenye
nyumba siye mama yao aliyechimba hilo kaburi na kuishia kuingiza wanae mwenyewe
wala si Pendo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose Muendelezo
Kujua Nani Anabaki Kwenye Familia Ya Ngoi, Nani Anamfuata Marehemu Mama Yao
Pamoja Na Ndugu Zao waliotangulia Mbele Ya Haki!
Hatima Ya
Yote Ni Nini?
0 Comments:
Post a Comment