Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 58. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 58.

Jack alitua jiji kuu la Tanzania akiwa na familia yake tayari kwa kuapishwa kesho kutwa yake. Walitaka kufika mapema kidogo ili kupata siku moja nzima ya mapumziko kabla ya shuguli za kuapishwa. Kaka yake na yeye alikuwepo hapo kwa shuhuli za Bunge, kwani bado Bunge lilikuwa likiendelea na bajeti ya wizara yake ilikuwa inakaribia kujadiliwa. Jack alikuwa amejawa furaha ya kupitiliza hata Sabrina alimuona. Jioni Junior akafika kuwaona hapo hotelini. Wakakutania sehemu ya chakula. Akacheka sana alipomuona Sabrina. “Kwani nyinyi mnapanga kuzaa watoto wangapi?” Tayari tumbo la Sabrina lilikuwa likionekana. Na hivi alikuwa na mtoto mdogo, bado tumbo la uzazi lilikuwepo na kuchanganyikana na ujauzito, safari hii ujauzito wake ukawa bayana.

          “Huyu wa mwisho shem. Tumepanga wanne tu.” Junior akacheka akitingisha kichwa kama anayesikitika. “Hamkutaka kusubiria angalau Brayan afikishe…” “Tunataka kusomesha tukiwa vijana.” Akawahi kujibu Jack, wote wakacheka. “Haya hongereni kwa familia nzuri. Ila Sabrina usisahau ulizaa kwa upasuaji. Kuwa makini.” “Yupo daktari anamsaidia kwa karibu. Hata baba anasema ni mzuri. Tusiwe na wasiwasi.” “Mzee ameniambia mnazungumza sana siku hizi.” “Ni kweli, sio kama ilivyokuwa zamani. Nimemuona amebadilika kweli! Alikuwa akinipigia mara kwa mara tokea nilipotoka nyumbani mara ya mwisho. Na huwa anapiga kuulizia hali za wajukuu zake.” “Na yeye ndiye aliyeniambia kama ulimpata Sabrina. Akashauri tukuache kwanza.” “Niliona nimwambie tu. Alikuwa na wasiwasi sana na Sabrina kwa kuwa alizaa kwa upasuaji, halafu akaondoka  na watoto wote. Nilipompata Sabrina ikabidi kumtaarifu kuwa wote wapo salama.” Sabrina alikuwa kimya tu hapo akiangalia watoto wakati wakizungumza.

“Umemwambia mama juu ya hili?” “Hapana. Tokea siku ile pale nyumbani sijazungumza naye tena. Hata hivyo najua atakuwa anajua. Hamna jipya.” Junior akanyamaza kama anayefikiria. Jack akajua kuna anachotaka kuwaambia ila anatafuta hekima ya kuzungumza naye. Nao wakanyamaza kabisa. Ni Junior, waziri, halafu mstaarabu sana. Wakanyamaza mbele yake kama kumpa nafasi. Kisha akaanza. “Sabrina, shemeji yangu, najua hili nilishakwambia. Lakini naomba nirudie tena.” Sabrina akamgeukia vizuri. “Naomba msinichoke.” “Tushauri tu shem. Najua wewe unatuwazia mazuri na ulipo ndipo Jack anataka kuwepo. Kwa hiyo tunakutegemea kwa ushauri, wala usisite kwetu.” “Kweli?” “Kabisa Shem. Wewe unaweza kutushauri kwa chochote. Hata kutukemea kabisa.” Jack akabaki kimya akiwa ameshajua ni nini kaka yake anataka kuzungumzia.

“Basi kwa ruhusa hiyo, acha niseme tu.” Junior akaendelea. “Najua mama amewaumiza sana. Na najua amekosa. Lakini bado ni mama.” “Lakini hanitaki mimi na hawa watoto. Sasa tutafanyaje?” “Sijui Mungu atawasaidia vipi! Lakini nilimsikia Jack akisema ulikubali kuwa haya mapito ni yako wewe na mama.” Sabrina akainama. “Si umekubali niwaambie?” “Ndiyo.” Sabrina akajibu macho chini. “Basi mwache Mungu ashugulike na mama, isiwe wewe. Wewe kama wewe umefanya kwa nafasi yako na kila mtu anatambua juhudi zako na upendo wako kwa Jack. Huna hila. Mwache yeye mama ahusike na Jack kwa vile atakavyoweza. Jack amejifunza kutokana na kilichotokea. Nina uhakika baba ameshazungumza naye sana kama alivyozungumza na mimi, na ameelewa. Jack mwenyewe atakulinda na mama.” Junior akaendelea taratibu tu.

“Binafsi baba alinifundisha sana juu ya ndoa yangu na jinsi ya kuishi na mama. Nafikiri ndio maana mimi na Joy tumebaki salama. Haikuwa rahisi na wala si rahisi. Wote tungetamani ingekuwa tofauti, lakini sivyo. Bado mama ni mama yangu mimi na mama mkwe wake Joy. Haitabadilika. Basi mwache Mungu afanye. Ila kwa kitu kinachotokea kwa Jack kesho kutwa, nina uhakika mama na baba wangefurahia kufanya kama walichonifanyia mimi siku naapishwa kwa mara ya kwanza. Ile furaha niliyoiona kwa mama usoni kwake siku alipokuwepo hapa Dodoma nikiapishwa, namuombea Jack kwako, asije na yeye kuikosa. Imenisaidia sana kwenye huu uongozi na kunifanya nisibweteke nikijua sijiwakilishi mimi tu na Joy, bali na mama yangu pamoja na familia nzima ya Msindai, wananitizama na kunitegemea sana. Namuombea mama Msindai kesho awepo hapa, Sabrina. Ashuhudie kuapishwa kwa Jackson kesho kutwa. Najua yeye anaweza asiseme, lakini najua angetamani na zilikuwa ndoto zake kuwepo hapa wakati Jack akiapishwa.” “Mimi sina shida shem. Hata kama uwepo wangu na watoto wangu utamsumbua..” “Watoto wetu.” Jack akarekebisha.

“Namaanisha hawa asiowataka mam.…” “Hawa watoto wote ni wangu mimi, kaka. Na hapo ndipo inapokuwa tatizo. Mama akiwepo tu kwenye picha, basi kunaanza kuwa na matabaka. Mimi hilo ndilo nisilopenda.” “Naomba utulie Jack. Ninachotaka kusema ni kwamba hili jambo ni la heri sitaki tulifanye liwe sivyo. Mama anakaribishwa hapa. Bila shida kabisa. Ila ikitokea uwepo wangu hapa utamsumbua kama siku ile kwenye harusi ya Pendo na Willy, mimi na watoto tutaondoka bila shida.” “Sidhani kama safari hii tutafika huko.” Junior akamtuliza Sabrina, lakini Sabrina hakujibu. Pakazuka ukimya.

“Acha mimi nirudi chumbani nikambadilishe huyu kaka.” Sabrina akaaga kama kuwapa nafasi. Jack kimya akiwa anajua kabisa anawapisha, Brayan hakuhitaji kubadilishwa. “Basi nitakuja kuwaaga kabla ya kuondoka. Ila mna watoto watulivu!” Wakawaangalia wale mapacha pembeni ya Jack. “Hao hivyo walivyo hapo na hiyo michoro yao, hutawasikia wakizungumza wala kutoka hapo mpaka wamuone baba yao ananyanyuka hapo ndio utawaona ni kama wamekatwa mikono.” Junior akacheka akiwaangalia. “Hapo walipo ni kama hawapo hapa kabisa. Watachora na kupaka rangi zao hapo mpaka wewe ndio utake watoke hapo, lasivyo unaweza wasahau.” “Sasa wanachora nini?” “Jack aliwaagizia hivyo vitabu vyenye michoro kwenye karatasi ya chini. Wanafuatisha kuchora kwenye karatasi ya wazi ya juu yake kisha wanapaka rangi. Naona aliwafundisha jinsi yakufanya, wakaelewa ndio hao. Wanapenda sana.” “Basi nikipaji chao.” Jack na Sabrina wakacheka tu. “Baadaye shem. Wewe weka hekima zako zote kwa baba watoto wangu. Tunahitaji hekima zako.” “Kwa baraka hizo, acha niwe huru.” Sabrina akacheka na kuondoka.

“Mama ananiharibia familia, kaka.” Jack akaanza kulalamika mara baada ya Sabrina kuondoka. “Wewe ndio unajukumu la kumlinda mkeo lakini si mama. Wewe unafikiri wanapatana sana na Joy?” Jack kimya. “Ni hivyohivyo tu. Lakini ilinibidi kusimama kiume haswa na kumuhakikishia mama kuwa Joy ni kila kitu changu,    kwangu na maisha yangu. Nikamchorea mstari ambao nilimuonyesha kila anapouvuka huo inakua ni tatizo. Basi tunaendelea hivyohivyo. Siku nyingine kunakuwa shwari siku nyingine ndio hivyo. Ila Joy naye ameshaweza kumzoea na kumchukulia. Huwezi kumkwepa mama, Jackson. Ni mama yetu na ukiangalia katika yote ni kwa kuwa anakupenda tu. Ila hajui ni jinsi gani yakufanya. Anakosea.”

“Hakika nilipanga kumuacha kabisa.” “Najua. Na ndio maana nakwambia usifanye hivyo. Ila kuwa makini na nini unamshirikisha tena, basi. Jua sasahivi yupo Sabrina, huwezi kumshirikisha mama kila kitu. Na yeye muonyeshe hakuna usiri kati yako na Sabrina. Atakujaribu tena na tena kwa hili na lile. Lakini akishaona unamsimamo. Ataanza kuelewa mipaka yako na kuishi na wewe kutokana na mwanya utakao mpa.” Jack akavuta pumzi kwa nguvu na kutulia.

“Mpigie simu mkaribishe kesho.” “Kaka! Mama atafanya mke wangu aondoke!” “Mkaribishe na Jacinta. Huwa anajua kumtuliza. Na mimi nitakuwepo karibu sana na Sabrina na watoto. Na tukiwa bungeni, nitamwambia Jacinta asisogee mbali na Sabrina mpaka mimi mwenyewe nitakaporudi au wewe utakapoungana nao tena.” “Daaah!” “Mpigie simu.” Jack akatoa tena simu. “Lakini nilimkaribisha baba.” “Najua. Aliniambia na unajua baba hawezi kuja bila mama. Mpigie simu mama.” “Ila Jena simtaki.” “Jackson!” “Jena ni mkorofi kaka. Tutaishia kugombana bure hapa, tena hadharani.” “Wewe utakuwa mbunge wa wapi unakwepa watu? Kiongozi wa namna gani ambaye huwezi kutawala watu wa nyumbani kwako? Jena na ukorofi wake wote, ulishamsikia anamjibu vibaya Joy?” “Si kwa kuwa anakuogopa wewe? Ni wewe peke yako ndio anakuogopa pale nyumbani. Mimi haniheshimu.” “Nilikwambia nini juu ya heshima?” Jack akakasirika na kusimama kwa kuvuta kiti kwa nguvu. Jeiline na Keiline wote wakanyanyua vichwa wakimtizama baba yao kwa pamoja mpaka Junior akashangaa.

“Huo ni ukweli na lazima ubadilike Jack. Acha kukimbiakimbia. Na rudi kukaa, unatia wasiwasi watoto wako.” Jack akarudi kukaa watoto wake wakabaki wakimwangalia. “Tuone mlivyochora.” Wote wakamkabidhi baba yao kwa pamoja. “Mmechora vizuri sana.” Jack akawarudishia, wakaendelea kuchora na kupaka rangi. “Sasa hata wakikubali kuja, watafikaje huku?” “Watakuja na Jacinta, usiwe na wasiwasi.” Kazi ya kupiga simu ikaanza.

Akaanza kwa Jacinta. “Mheshimiwa Msindai?” Jack akacheka. “Hongera sana. Au niseme hongereni sana.” “Nashukuru dada. Sasa ili hii furaha ikamilike, kesho kutwa wakati nikiapishwa lazima uwepo.” “Mbona nilikuwa nakuja bila hata ukaribisho! Na nguo tayari ninayo.” Jack akacheka sana kwa furaha. “Hapa nishakusanya timu yangu yote sema dada mdogo ndio anatufanya tusiondoke leo.” “Claire huyo?” Jack akaliza akicheka. “Huyohuyo! Anamipango mingi kuliko baba yake waziri! Ndio tunamsubiria amalize leo jioni, kesho nambeba na timu ya Joy nzima, tunatua jijini. Tupate nyama choma na kunywa usiku kuchwa, asubuhi bungeni.” “Nashukuru dada yangu. Asante sana.” “Wala usijali.” “Acha nimpigie simu na mama.” “Hiyo hekima. Hapo nakupongeza na ndio unatutangazia upo tayari kwa majukumu mazito.” Jack akanyamaza. “Utakuwa sawa. Mimi mwenyewe nakuja. Kwa hiyo kesho na kesho kutwa itaisha vizuri.” “Naamini hivyo.” Wakaagana.

Akampigia simu mama yake. “Nimeteuliwa kuwa Mbunge wa viti maalumu.” “Hongera sana.” Mama Msindai akajibu. “Kesho kutwa naapishwa. Nilikuwa nakukaribisha.” “Nilijua hutaki nije!” “Ndio nimekupigia mama!” “Kwani wewe huku kuapishwa ndio umejua leo?” “Mama Msindai!” “Inakua kama unalazimishwa mimi niwepo! Kama unaona shida ya mimi kuwepo haina sababu. Maana..” “Mama! Mama! Naomba unisamehe kuchelewa kukutaarifu. Naomba kesho uje, na swala la usafiri dada Jacinta atashugulikia.” “Maana unaweza ona nitaharibu!” “Nimeomba msamaha mama. Na naomba yaishe.” “Yanaisha yote au hili tu lakuchelewa kunitaarifu mimi kama mtu baki wakati ni mama yako? Maana uliniitisha kikao mimi mbele ya ndugu zako!” Jack akamwangalia kaka yake, Junior kimya.

“Nia yangu ilikuwa nzuri lakini ukanitupia mimi lawama! Mimi sina kipimo, na wewe huna kipimo chakumjua mtu. Sasa kwa nini mimi nisiongee moyo wangu pale ninapopatwa nawasiwasi?” Jack akaweka spika kaka yake asikie. “Mimi kama mama lazima nikulinde kwa kila namna. Sasa kosa langu lipo wapi?” “Omba msamaha.” Junior akanong’ona. “Kaka!” Jack akashangaa sana kwa kuumia. Junior akatingisha kichwa akikubali akiweka msisitizo, Jack akatamani kulia. “Mimi mke wangu sio mchawi. Brina ananipenda na ananiombea sana.” “Sasa hayo yakuwa si mshirikina kwa hakika mimi ningeyajua wapi? Kama yalimpata Ngoi, kwa nini mimi nisiwe na wasiwasi juu yako? Kitakachoshindikana kukupata wewe ni nini?” “Basi mama, mimi naomba yaishe. Yaishe yote. Ila naomba muache Brina. Hivi nilivyo mimi, napenda. Hata kama ananiloga, niachwe tu nilogwe.” “Sawa.” Akajibu mama Msindai.

“Kwa hiyo unakuja?” Jack akamuuliza. “Sijui! Napatwa uzito maana ni kama watu wote wananiona mimi sifanyi ilivyo wakati nia yangu ni nzuri.” Gafla mama Msindai akageuka yeye ndio muhanga! Anaonewa! Ikabidi Jack ajishushe kumtuliza ila akisimamia Sabrina ndio yeye, lazima hilo aelewe. Wakaongea hapo karibu nusu saa, mwishoe akachangamka. “Nitakuletea tai na soksi.” “Nishanunua tai. Tafadhali usianze mama!” “Muulize Junior. Kila akiapishwa lazima avae tai niliyomletea mimi.” Akamtizama Junior, akamuona anacheka taratibu akiwa ameinama anatingisha kichwa kwa masikitiko. “We Jack?” “Nipo mama. Sasa kwa nini..” “Muulize hata Joy. Nilishamwambia na yeye akaelewa. Awamu zote mumewe akiapishwa lazima avae tai nilizonunua mimi na soksi pia. Sasa wewe unabisha nini?” “Sawa mama, lakini nilishapanga tai yangu.” “Tai gani hizo za vichochoroni? Unataka kuniharibia utaratibu wangu! Hii tai nilishanunua muda mrefu sana nikijua siku moja utakuja kuapishwa tu. Sasa unataka kunikatili bila sababu?” “Sawa mama. Unakuja na tai pamoja na nini kingine?” “Mimi sina uhakika sana na hiyo suti unayotaka kuivaa siku ukiapishwa.” Junior akaanza kucheka.

“Kwa hiyo na suti pia unataka ulete wewe, yangu nisiivae?” Jack akamuuliza. “Unaposimama pale kesho kutwa ujue unawakilisha kina Msindai wote. Sasa unataka tuonekane sisi wote hovyo? Unavaa suti ambazo hata hazijulikani zimeokotwa wapi! Mpaka unafanya watu wajute kukuchagua bwana! Inakua…” “Sawa mama.” “Basi swala zima la mavazi ni juu yangu. Na umwambie Junior mimi nataka nije nilale huko leo. Ili nijiridhishe kama nguo imekukaa vizuri au la. Kama kunamarekebisho basi siku ya kesho nishugulikie ili kesho kutwa utokee smati.” “Usiwe na wasiwasi. Yako isiponikaa vizuri, ipo hii yangu.” “Mbona unafanya nijirudierudie? Nasema sina imani na hiyo suti yako.” “Sawa mama Msindai. Nitamwambia kaka ahakikishe leo, unalala Dodoma ili unijaribishe suti.” Junior akatingisha kichwa kwa masikitiko akicheka. Wakaagana.

“Mama!” “Ila nimemsikia amefurahi sana. Nashukuru kunitia moyo kumpigia. Aliniumiza sana.” Wakaendelea kuzungumza wawili hao. Ila safari hii angalau kikaongezeka na kicheko. Jena yeye akamtumia tu ujumbe wa kumkaribisha, hakutaka kuzungumza naye alijua wataishia kugombana. ‘Nakuja sana. Wala sipitwi.’ Akarudisha hayo majibu. Akamuonyesha kaka yake. “Huyu usiwe  na wasiwasi naye. Nitazungumza naye hata kabla hajaondoka Dar. Nitamuonya kabisa ili akishindwa, basi asije huku.” “Naomba nisaidie kaka. Brina ameshika mimba akiwa bado na mshono mbichi kabisa. Sitaki waanze kumpandisha tena pressure.” “Usiwe na wasiwasi. Mimi na Jacinta tutajipanga.” Wakaendelea kuzungumza.

Kwa Pendo.

S

abrina akaona ampigie simu Pendo. “Nimekuamsha dada yangu?” “Usijali. Vipi maandalizi huko?” “Tumeshafika Dodoma. Tupo hotelini. Lakini dada, kuna jambo nilikuwa nikisita kukwambia, lakini acha tu nikwambie. Sina nia ya kukutisha ila kukufanya uwe makini na wewe uombe.” “Niambie tu. Ni nini?” “Nimeona roho ya mauti ipo karibu na wewe pamoja na Willy. Nimekua nikiwaombea, lakini hata Jack amenishauri ni lazima nikwambie mwenyewe.” “Sabrina!” “Naomba usiogope dada. Mungu anapotuonyesha jambo si kwa kutaka kutuogopesha ila kutenda kazi na sisi. Naomba uombe na wewe.” “Na nimepoa kweli! Sina maombi yeyote sababu ya hekaheka ya kulea. Nimejisahau.” Pendo akakiri.

          “Na hapo ndipo shetani anapenda kupenyeza yake. Akishaona tumepokea majibu ya maombi fulani, tukabweteka, basi anachokonoa kwingine. Yeye hasinzii wala kulala akijua muda wake wa hukumu umefika. Basi kazi yake ni kuharibu ili watu waanguke na apate wafuasi wengi. Mimi nakuombea dada, lakini naomba mwambie na Willy aombe pia.” “Nashukuru Sabrina. Ila naomba usiache kuniombea. Nimekua mbali na Mungu, ila nakuahidi nitaomba.” Wakazungumza kidogo na kuagana.

Jiji Kuu La Tz.

M

ama Msindai akatua jijini akionyesha alikuwa amejiandaa vilivyo. Junior alimchukulia hoteli mbali na hapo alipokuwa Jack na familia yake. Jack na Junior wakaenda kumpokea na kwenda naye hotelini. Sabrina alimwambia asiwe na wasiwasi yeye atakuwa tu sawa hapo hotelini na watoto, yeye apate nao muda. Basi mazungumzo yakaanza. “Msindai anakuja kesho na timu yake. Amefurahi huyo!” “Baba!?” Jack akauliza asiamini. “Huyohuyo baba yako. Kafurahi sana na kataka nitangulie na suti yake kabisa.” Wakacheka. “Ni hivyo tu anawagonjwa wake leo usiku, kama mnavyomjua hawezi kuwaacha, ila angekuja na mimi.” Zikaendelea stori, pakaonekana pana amani tu wala hapakuongelewa Sabrina wala wanae.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Kesho yake Mzee Msindai, Jacinta, Joy, Jena na watoto wote wa Junior wakatua jijini tayari kwa shuguli nzima ya kuapishwa kwa Jack siku inayofuata. Hapo ikabidi jioni baada ya Junior kutoka bungeni watu wote wakutane sasa kwa chakula cha jioni. Maana Sabrina alibaki hotelini na watoto wake karibu siku nzima Jack alipokuwa hotelini na mama yake wakijaribishana hizo nguo. Ila Junior alishazungumza na kila mmoja wao hapo akiomba amani zaidi kwa Sabrina. Akawaambia mpaka hiyo shuguli iishe, basi Sabrina na watoto wake wote nilazima wawepo ndipo Jack atatulia, lasivyo wataharibu shuguli nzima.

          Jack na Sabrina pamoja na watoto wao wakawafuata walipokuwa wakikutania. Sabrina aliona ni kama wote wanamshangaa ujauzito wake, lakini akaona kama walioonywa hakuna aliyemsemesha. Alisalimia kwa jumla tu, wakakaa sehemu ilipoachwa wazi kwa ajili yake na watoto wao. “Mmependeza na wanao!” Jacinta akawasifia. “Asante wifi yangu. Haya salimieni sasa!” Wakamwangalia baba yao. “Kwani wameanza kuongea?” “Wanajua kusalimia sana tu. Ngoja Jack awaambie naona yeye huwa wanamuelewa vizuri kuliko mimi.” “Au tuinamishe vichwa watushike?” Babu yao akauliza. “Pina dada yao aliwafundisha kusalimia hivyo kwa kushika vishwa, eti Jack akawakataza kusalimia kwa namna hiyo.” Wakacheka. “Sasa wanasalimiaje?” “We Jack, waambie wasalimie bwana. Mbona wanajificha?” Jack akawachungulia kule nyuma yake.” “Haya njooni huku mbele muangalie watu na kuwasalia, hslsfu mkae.” Wakachungulia. “Bwana hawa watoto ni wazuri jamani! Sabrina, hapa ulizaa.” Joy akasifia wote wakacheka.

          “Mimi napenda nywele zao, anti. Wananywele za kizungu.” Claire akafanya wazidi kucheka. “Lazima kusalimia na mseme asante.” Mama yao akaweka msisitizo. Wakasalimia huku macho kwa baba yao. “Salamu za Singida hizi. Ushamba tu sijui wakoje mwaya!” Sabrina akawaambia wanae, wakarudi nyuma ya baba yao. “Mlitaka wanangu wafanyaje sasa? Mmetaka salamu, wamewasalimia. Bado tu?” Jack akalalamika akiwaangalia binti zake wa kizungu. Sabrina aliwavalisha vizuri na kweli walikuwa wamependeza. Wakaendelea kucheka wengine ila mama Msindai na Jena kimya.  

“Watakubali kukaa na mimi hapa karibu na dad?” Claire akauliza. “Labda nihame nao hapo karibu yenu. Lasivyo hawatakubali.” Jack akajibu. “Basi mama wewe na Clei muhamie pale ili watoto waje hapa wakae karibu na mimi pamoja na dad.” Kila mtu akaanza kucheka. Junior akawa akicheka huku akimtizama mkewe.

“Wala sinyanyuki hapa. Mkitaka nyinyi ndio muhame, hee!” “Dad amechoka na kazi, mami. Tusimsumbue.” Claire akamjibu mama yake taratibu akitaka yeye ndio aondoke, kila mtu akazidi kucheka. “Basi wakati nyinyi mnajipanga bora mimi nikaanze kucheza na watoto.” “Utalia Clei wewe!” Mama yake akaanza kumtisha. “Sasa yeye Claire si hataki kuhama mpaka ahame na dad! Mimi nipo tayari kufuata watoto.” “Acha kutaka kumliza mtoto bwana! Yeye ndio amewahi, mwache aende.” Kaka yao, CJ akaingilia. “Clei yeye mchokozi.” “Usilie Claire. Twende wote mimi nikae na wewe ucheze na watoto halafu ukichoka, dad atakupakata.” CJ akaendelea kuzungumza naye taratibu Clei anacheka. “Usimwangalie, niangalie mimi. Anataka uzidi kulia.” “Basi mimi silii.” “Mbona machozi yana…” “Clei wewe utalia wewe mtoto wewe!” Clei akanyanyuka haraka akahamia kwa babu yake.

“Muone! Mwenzio anambembeleza asilie, wewe raha yako ni mpaka alie!” Baba yao mwenyewe alikuwa akicheka taratibu. “Acha kushindana na mtoto. Njoo Claire.” CJ akajaribu kumtuliza. “Na mimi nataka tucheze wote Claire.” Clei akaingilia tena, makusudi tu. “Sitaki kucheza na wewe Clei.” “Junior mkanye Clei, atalia huyu mtoto jamani!” “Sasa mimi si nataka kucheza naye tu! Nimekosea wapi?” “Mimi sitaki kucheza na Clei, nataka kwenda na CJ nikacheze na watoto.” “Yaani mpaka hilo bunge lenu mmalize hapo kina Msindai, na watoto wenyewe hawawataki tena.” Jacinta akaingilia nakufanya mpaka Joy acheke wakawaangalia. Wale mapacha walikuwa wamesimama pembeni ya baba yao wamemshika kila mmoja mkono wake kama asiwakimbie. Kimya, wametulia wanawaangalia vile Claire anavyolia.

 “Vipi yeye mzee mwenzangu?” Mzee Msindai akauliza akimwangalia Brayan pale kwenye kigari chake alipokuwa amelala pembeni ya mama yake. “Kaka yupo tu. Bado mtulivu hivyohivyo.” “Bwana mtoto yule wa kiume wa Pendo anajua kulia mpaka Willy jasho linamtoka.” Wakaanza kucheka kila wakikumbuka mapacha wa Pendo. “Akianza kulia kaka mtu na dada yake anapokea basi hapo Pendo utasikia, ‘mpaka mimi mwenyewe machozi yananitoka!’ Pendo huyo.” Joy akaigiliza sauti ya Pendo nakufanya wazidi kucheka. “Pendo analia, na wanae pia wanalia?” “Wewe si unamjua Pendo asivyopenda matatizo? Basi mama yake amekua kama amehamia pale. Anasema akiondoka tu, simu zinamfuata juu ya wale watoto.” “Na mimi mama K, aliniambia. Anakaribia kumuhamishia mumewe pale. Hana analofanya zaidi ya kulea hao wajukuu.” Wakazidi kucheka.

Mzee Msindai akasimama kwenda kumchukua Brayan na Cleiton naye akamshika shati. “Utamuangusha babu yako bwana!” Baba yake akamuwahi. “Mama anataka kunipiga kwa kuwa kaka mzuri kwa Cl…” “Usinitaje jina langu.” “Na ukimjibu tu unalia.” Mama yake akamtisha tena. Cleiton akajiziba mdomo na kiganja kimoja mkono mwingine amemshikilia babu yake. “Basi mtamuangusha huyo mtoto.” Mama Msindai akaingilia. “Wewe ukitulia hutachapwa.” “Wananionea bure babu! Sijakosa.” “Basi tulia hapa kwenye kiti changu na usinyanyuke. Hakuna atakayekufuata kwenye kiti changu.” “Na kila mtu amesikia. Babu amesema hata mtu asinirushie kiatu.” Walicheka mpaka mama yake akatokwa machozi. Mzee Msindai akaenda kumchukua Brayan, Junior akamuhamishia kiti pembeni ya Cleiton. Baba yao akakaa akiwa amembeba Brayan.  

“Mtulivu huyo!” Jacinta akamsifia Brayan. “Halafu bado ameshikilia sura ya baba.” Junior akaongeza. “Ndio inamaana amefanana na Jack au wewe Junior.” “Mimi nahisi amepitiliza mpaka amebakia kwa baba, jamani! Yaani utafikiri yeye ndio mtoto wa mzee Msindai!” Mzee Msindai akazidi kufurahi. “Basi hapo mmemuweza Msindai. Anaona sifa!” Mama Msindai akafanya wacheke wakimuangalia mzee Msindai. Kweli alionekana anampenda huyo mjukuu wake. Alikuwa amemshika vizuri. Zikaendelea stori wakaletewa vyakula kila mtu alichopenda, kukawa na kula, kunywa na kusaza mpaka waliporidhika watoto wamechoka.

Sabrina akaaga kwamba anakwenda kulaza watoto. Jacinta, Joy na Junior wao walisema wanabaki kunywa. “Mbaki na baba watoto wangu ila mumrudishe salama.” “Unauhakika Sabrina?” Jack akamuuliza kama kweli abaki pale. “Kabisa. Sasa unataka na wewe uende ukalale sasahivi kama Brayan?” Angalau wakacheka wakaamua watoto wote waondoke na Sabrina akapumzike. Junior akatafuta dereva kuwarudisha watoto wake hotelini, CJ kaka yao awaangalie kwa maelezo kwa chochote kuwa kikitokea awapigie wazazi wao simu, hata hivyo hawakuwa mbali na hoteli waliyoshukia hao kina Msindai wote. Kisha dereva alitakiwa kumpeleka Sabrina na wanae kwenye hoteli waliyofikia wao. Wakaondoka na kuwaacha hapo, Mzee Msindai na mkewe, Junior na mkewe, Jacinta, Jena pamoja na Jack. Ndio kukawa kumekuchwa. Wakaaanza kikao kwa upya.

          Penye Amani Na Utulivu, Na Uharibifu Hunyemelea.

W

akati Jack anaingia hapo chumbani kwao hotelini akamkuta Sabrina akizungumza na Pendo. Akaingiwa na wasiwasi kwa sababu kwa muda ule, usiku wa saa saba alitegemea Sabrina awe alishalala. Akajua haitakuwa simu nzuri. Jack akasogea kusikiliza, Sabrina akaweka kwenye spika ili na yeye asikie. Jack akamsikia Pendo akilia. “Najuta Sabrina wewe! Najuta sana. Natamani muda uleule uliponipigia ningeomba. Pale ulivyokata tu simu na mimi nikaingiliwa na vilio vya watoto. Nimekuja kukumbuka ulichoniambia sasahivi Willy alivyopigiwa simu na kutaarifiwa kifo cha kaka yake. Ameondoka hapa mbiombio.” “Poleni dada. Wanasema ni nini?” Sabrina akauliza.

“Gafla tu, hata hakuwa mgonjwa! Yaani ameanguka tu  akiwa anatoka sebuleni usiku huu, anakwenda kulala chumbani kwake. Mkewe anasema alirudi akaishia hapo sebuleni wakawa wakizungumza mpaka wakaamua kwenda kulala. Yaani mkewe anasema amedondoka akimuona hivi! Imekuwa kama aliyesukumwa wakati anaelekea chumbani. Amedondoka na kufariki hapohapo.” “Poleni dada.” Wakaagana lakini Pendo akisikika mwenye majuto.

          “Ni nani!?” “Kaka yake mkubwa Willy.” “Ulipomwambia aombe aliomba?” “Kama ulivyomsikia hapa. Anasema ndio anakumbuka sasahivi baada ya hizo taarifa.” “Inamaana alipuuza!” “Anasema alipitiwa. Nilipomaliza tu kuzungumza naye ile jana, eti watoto wakaanza kulia, akasahau.” Jack akasikitika sana. “Alikuwa na nguvu zake kabisa!” “Namkumbuka yule kaka. Nilimuona siku ya msiba wa mama yao. Alikuwepo pale. Tena amefanana kweli na mzee Ngoi mwenyewe.” Ikawa habari iliyowahuzunisha sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Katikati Ya Mema Na Mabaya Hujihudhurisha.

Sabrina Aliona Roho Ya Mauti, Akawataarifu Waombe. Kukawa Na Kujisahau Kwingi Wakiendelea Kufurahia Majibu Ya Muujiza Wao.

Sasa Je, Hiyo Roho Ya Mauti Iliyofunguliwa, Inakwenda Umbali Gani?

Nani Anaangamia? Nani Anabaki?

Mwisho wa Ubaya ni Nini?

Familia Ya Msindai Nayo Ipo Jiji Kuu La Tanzania Kushuhudia Kuapishwa Kwa Jack. Nini Kitaendelea kwenye siasa za Jack?

Usikose Sehemu Ya 59.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment