Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 57. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 57.

Walifika Singida muda mzuri tu kwa ndege wakakodi taksii tena mpaka nyumbani. Sabrina alimuona jinsi Jack alivyobadilika. Alipoa sana. Hakurudia hali yake ya zamani kabla ya yote hayo. Alikaa na watoto kwenye ndege, lakini hapakuwa na vile vicheko. Sabrina akawa mwenye wasiwasi. Ila hakujua kinachomfanya awe hivyo zaidi ni nini! Kwa hakika alijua amechukia kukuta watoto wamerudishwa kwa Tino. Hilo alijua limemuudhi haswa. Lakini hakujua na kukosa ubunge nako kunachangia au mama yake! Ikawa ni hali ya kumkisia tu bila kujua kwa hakika.

Watoto wote walikuwa wamelala wakati wanaingia hapo nyumbani kwao. Wakasaidiana kuwaingiza ndani na kuwalaza. Mizigo yao ilibahatika kuondoka siku iliyopita na basi la mwisho kabisa kutoka Dar. Jack akajua itakuwa imeshafika, akachukua gari kuifuata, Sabrina alipojiridhisha amebaki peke yake, akapiga magoti hapo chumbani, na kuanza kulia mbele ya Mungu. Alijawa hofu juu ya ndoa yake. Jack alikuwa mtu wa kusamehe kwa haraka na kumtaka kimapenzi wakati wote. Lakini walilala hotelini hata hakugusia kabisa swala la mapenzi. Alikuwa amepoa kupita kawaida yake. Akakumbuka mara zote alizomuomba msamaha tokea wapo Dar, hakusema kama amesamehe.

Sabrina anayependa kumpa Yesu mtatizo yake, akamwambia mpaka hapo ameharibu, hajui chakufanya, anaomba msamaha na msaada. Akajifikisha maeneo yake ambayo hapo huwa hakosei. Magotini. Akatubu kwa machozi na kuomba rehema, Mungu asimchoke, amkumbuke tena, amrehemu na kumrudisha moyoni kwa Jack. Akaomba mpaka akakumbuka anajukumu hapo kama mama na mke, na hana msaada. Akanyanyuka na kuanza majukumu ya kinyumbani, zaidi kupika.

Jack alipitia na sokoni. Kwa hiyo akachelewa kidogo kurudi. Akamkuta Sabrina ameunganisha masalia ya kwenye friji na stoo, anapika. “Nisadie nini?” Jack akauliza baada ya kuingiza kila kitu ndani na kupanga. “Labda kuniangalizia Brayan. Anaweza akawa ameamka na kutulia tu.” “Ndio mpole hivyo?” “Wewe utamuona. Kama haupo makini, ni rahisi kumsahau.” Jack akaondoka. Ila chakushangaza hakurudi tena jikoni kama Sabrina alivyozoea. Alivyotoka kumuangalia mtoto akaenda kukaa sebuleni.

 Sabrina wakati akipanga vyakula mezani, akamuona amekaa sebuleni amejiinamia wala hajawasha tv. Akamuacha akijua watoto wanakaribia kuamka. Mazungumzo yeyote watakayoanzisha, hawatamaliza kabla yakuingiliwa na watoto.  Na kweli haikuchukua muda mrefu watoto wote wakaamka. Wakasaidiana kimya kimya mpaka watoto walipoenda kulala, na yeye Jack akajiwahi kuoga na kujiweka kitandani. Akamkuta kitandani amejilaza hata simu amezima. “Nimezungumza na Pina, nimemuomba arudi atusaidie kazi.” “Umefanya vizuri. Tutahitaji msaada.” Akajibu hivyo, Sabrina akaona bado mazungumzo kati yao yamekua mazito.

Akajiweka kitandani na yeye baada ya kuoga bila kuzima taa. “Jack, umeshalala?” “Nipo. Nafikiria inamaana nisingekufuata inamaana mpaka leo ningekuwa hapa peke yangu! Na nikiangalia mazingira niliyoyakuta pale, ni kama nimewaingilia Brina. Maisha yenu yalikuwa yakiendelea kama kawaida, tena vizuri kabisa bila mimi. Nahisi ndio maana mama yako amenichukia sana. Ananiona mimi mvurugaji.” Jack akazungumza akilalamika.

“Najua nimekosa na nimekuumiza, Jack. Lakini naomba utulie na ujaribu kufikiria tu. Weka hasira pembeni na ufikirie. Fikiria tu tafadhali.” Jack akamwangalia. “Hivi kweli wewe ulifikiri nilikutafuta kweli ili unipe nguo za Brayan, kweli?” Jack akatulia kidogo bila ya kujibu. Baada ya muda akamuona anakunja uso kama anayepingana na jibu lake. Sabrina kimya akimtizama pale alipojilaza kitandani kwa huzuni. Kisha akajibu. “Lakini ndivyo ulivyoniambia Brina!” “Kwa hiyo wewe unavyofikiria kule Dar hakuna nguo za watoto wa kiume mpaka Singida?” Jack akanyamaza.

“Unakumbuka wewe uliondoka na kunitelekeza na watoto wote ukaendelea na mipango yenu na mama yako?” “Ukisema hivyo inasikika vibaya!” “Ndivyo ilivyokuwa, Jack. Sasa ningejuaje kama umeamua kuturudia mimi na makinda yangu?” “Wewe Sabrina! Si ilikuwa ni...” “Mimi ningejuaje mipango yako na mama yako? Kama ni moja kwa moja au utaturidia? Sikujua safari hii mama yako amefanikiwa lipi na kwa undani gani kwako! Kumbuka maneno machafu aliyoyasema juu yangu, halafu nikaja kukuona upo naye. Ulikuja kwa Pendo, nikakuona mara moja tu, tena hukuzungumzia chochote kwenye swala la Ubunge. Hata hukutaka kujieleza lolote juu ya hilo. Sikujua umeamini nini na utaamua nini juu yangu na wanangu! Halafu ukweli nilikuwa nikiumwa na niliumia Jack. Nikaona nije huku, nikuache tu mpaka umalize, uje ututoe mimi na wanangu kwenye hii nyumba. Sikupanga hata kukaa kwenye Villa, na Mungu ni shahidi.” Sabrina akaendelea.

“Sasa siku ile ya harusi nilipoondoka pale, hata hukunifuata nyuma, nikajua moja kwa moja umekubaliana na mama yako mimi ni mzigo. Umekusudia kuachana na mimi.” “Nilitaka kukufuata lakini Pendo akanirudisha na kutaka kuniambia ukweli.” “Sasa mimi sikujua yote hayo. Nilijua moja kwa moja uliamua kuachana na mimi. Na naomba ukumbuke historia yangu, Jack. Wanaume wote huwa napambana kuwasaidia kwenye ndoto zao, wakishafanikiwa huwa wananitupa. Mimi moja kwa moja nikajua na wewe utakuwa hivyohivyo. Nilitoka pale nikaenda sehemu kuomba. Nikiwa sijui tena chakufanya, nikijua umekusudia kuachana na mimi. Nilikaa pale kwa muda mrefu sana, nikimuomba Mungu lakini ukweli nilikuwa nimepoteza dira. Baada ya kujihisi nimechafuka na maumivu ya tumbo kunizidia, nikaamua kurudi kwa dada Sabina, maana nilipanga tulale pale na watoto pamoja na mama, kesho yake nije huku.”

“Nilifika pale, sikuwakuta. Nikakaa nje tu mpaka wakarudi. Nilipowashika kina Jeiline nikapata harufu ya Tino. Nikajua walikuwa na Tino maana nilishapata habari za kutaka kujirudi kwake, lakini mimi nilimkatalia. Sasa muda ule nikijua umeamua kuachana na mimi, halafu nilikuwa mgonjwa, sina pakwenda.” “Na huku?” “Sasa huku ningerudije wakati tukio la harusi kwa Pendo kutonifuata likawa limeshanithibitishia unaniacha? Watoto watatu, sikuwa na pakuwaweka na wewe hukuwa hata ukikosea kwa ujumbe angalau kutujulia hali! Nikajua umeingiziwa maneno, safari hii yamekuingia.” “Nahisi hapo ndipo nilipokosea.” Jack akakiri.

“Basi nikajiambia ni bora nimtumie Tino aniweke mahali wakati nikijipanga upya. Mungu nishahidi Jack, sikuwa hata na mpango wa kurudiana na Tino, na wala hakuna lililokuwa likiendelea kwa muda wote tuliokuwa pale. Kwanza ananiogopa mno. Hapakuwa na jingine isipokuwa kuomba kuona watoto tena wakati mwingine hata alikuwa akimtuma mama amuombee kwa jinsi anavyoniogopa. Yaani jana, kwa mara ya kwanza na wewe ukiwa pale kwenye Villa ndio angalau nimeweza kukaa naye chini kuzungumza naye. Tangu anitelekeze yule kiumbe, sijawahi kupata naye muda wakuzungumza naye. Moyo wangu ulisita kabisa kuwa naye karibu kwa muda mrefu. Alichokuwa akifanya ni akifika pale, akiniomba kitu nikiwa chumbani, nikimruhusu anatoka. Au akinikuta nina maumivu alikuwa akiogopa hata kunisogelea, anamtuma mama.” Jack akawa anasikiliza tu.

“Tino kama yeye kwa hakika nilikuwa nikimtumia na yeye nilimwambia kabisa kuwa namtumia kujipumzisha. Haikuwa siri hata wazazi niliwaambia ananilipa kwa kumtumikia alipokuwa yeye mgonjwa, hii ni safari yangu na mimi anilipie pale nikijiuguza.” “Lakini alihusika na wanangu, Brina. Mpaka kuwalisha?” “Nisikilize Jack, na naomba uamini. Hiyo picha iliyokuingia kichwani haikuwa hivyo. Hapakuwa na maisha ya Tino na hao mapacha wako. Haikuwepo kabisa. Unaposikia aliwalisha, sio kwamba ilikuwa ni mpango ulikuwa ikifanywa ili awalishe au asaidie kazi zao. Kwanza Tino sio kama wewe, hayawezi. Anachopenda ni zile show pale. Atayarishiwe watoto ndio atoke nao. Ni mtu wakutumikiwa. Nahisi pengine atakuwa alimkuta mama akiwalisha, akasaidia kwa vijiko vichache tu. Hapakuwa na maisha yaliyokuwa yakiendelea kama familia pale.”

“Ninachojuta na nafikiri ni kosa nililifanya kwa kuwa nafikiri nimekosa imani na Tino kabisa.” “Kosa gani?” Jack akauliza. “Najuta kule kumtuma mama kila mahali awe na Tino anapokuwa na watoto. Na nafikiri huko ndiko alikomuingia mama moyoni. Maana nilikuwa sina amani ya kumuacha peke yake na watoto wetu. Kwa hiyo nikawa nikimuomba mama atoke nao. Halafu sio mara nyingi. Alikuja mwanzoni aliponisaidia hoteli, nilipohamia kwenye Villa na yeye akaondoka. Nilimsikia akimwambia mama, tena mimi nilikuwa chumbani, kuwa anasafari ya kwenda kwenye kuuza picha zake mnadani. Hata sikujua ni nchi gani, ila aliondoka. Amerudi nafikiri hata siku saba hajamaliza. Ameomba wale watoto kama mara tatu tu. Na jana tena lakini ndio wanao wakamgomea, ndio maana akawarudisha.”

“Kwa hakika nilihitaji kupumzika Jack, kwa kuwa sikuwa nikijua hatima yetu japo nilihisi kwa asilimia 79 utakuwa umeniacha. Sasa nafanyaje na watoto watatu ambao hata bibi yake huyu Brayan amemsusa? Ndio sikuwa najibu, nikajiambia nikapumzike kidogo, nijiuguze, nipone ndipo nijue chakufanya. Wapi pakuanzia, sikuwa nikijua ila nilishakusudia Tino hatarudi kuwa mbadala hata iweje. Japokuwa anajitilisha huruma, lakini ni mtu mwenye roho mbaya sana. Ni chui mwenye ngozi ya kondoo. Nilimuona wakati tukiwa Moshi. Na ni mtu anayeweza kubadilika vibaya sana pindi anapoamua jambo lake. Hata kama usingenirudia Jack, Tino asingekuwa mbadala.”

Anyway, katika hizo asilimia chache zilizokuwa zimebakia kwako ndio nikajiambia nikujaribishie swala la nguo kwanza nione msimamo wako.” “Sabrina!” “Nishakataliwa sana Jack. Sikuwa tayari kwa wakati huu kukataliwa tena. Nilijiambia nikiona majibu yako hayaeleweki, basi natulia Dar na wanangu, nianze tena maisha mengine.” “Mimi na wewe mpaka kifo Brina. Na wewe nilikwambia.” “Hayo maneno yanasikika vizuri sana siku ya harusi, lakini kuja kuyaishi ndio mambo kama haya yaliyotupata mimi na wewe. Wakati mwingine ni rahisi kuyatilia shaka.” “Mimi nitayashikilia mpaka kifo.” Sabrina akamwangalia nakuendelea.

“Swala la kukublock kwenye simu. Ni kosa. Lakini Jack, ukitulia na kufikiria, sijakublock.” “Unawezaje kusema hivyo?!” “Najua usingependa kusikia hili, lakini na kwako nilifanya kama kwa Tino. Simu yangu ilikuwa hewani tokea namzaa Brayan, naruhusiwa na kutoka hospitalini kwenda kwa Pendo, mpaka siku ya harusi ya Pendo, natoka pale nakuhamia kwenye hoteli. Haikuwahi kutokuwa hewani. Lakini Jack, ni mara ngapi hata ulinitumia ujumbe kunijulia hali mimi na watoto?” Jack akababaika sana mwishoe akakumbuka.

“Lakini nilikuja siku ile pale kwa Pendo, mpaka nikakuomba nichukue watoto niende nao! Ulikataa lakini nilikuja kuelewa baadaye ni kwa nini ulikataa. Ila siku ile unanikatalia watoto sikuwa nikijua ni  kwa nini. Na mimi nikaendelea kukasirika na kushindwa kujua hata nikikutafuta nakwambia nini?” “Sasa umekubaliana na mimi sio kwamba nilikufungia mawasiliano ila hapakuwa na mawasiliano kati yetu kutokea mwanzo? Nilichofanya ni kupumzisha tu simu za watu ambao nao niliona nipumzike, zaidi wa huku Singida. Sikujua nawaambia nini nikiwa sijui hatima yetu! Sikutaka niongee jambo likaja kukuharibia, ndio maana nikaona nitulie tu. Hata kama utaniacha, basi wewe nitakayekuacha huku ubakiwe na hekima ya kuzungumza juu yangu na watoto.” “Nakushukuru kwa hilo, ila nahisi nilifeli tokea mwanzo kwenye swala la mawasiliano na wewe, Brina.” “Ni kweli. Na mimi najutia maana hata dada Pendo alinisihi sana nikwambie. Nikidhani nitakuchanganya, kumbe naharibu zaidi. Naomba unisamehe Jack, mpenzi wangu. Mimi nakupenda sana na nimekuchagua wewe. Nisingekutafuta kama sina mpango wa kurudi huku. Na huo ndio ukweli.” Akamuona ameridhika.

“Naomba na mimi unisamehe Brina. Nilikukosea. Sikupaswa kukufanyia nilichokufanyia. Ila ujue sikuwa na mpango wa kukuacha hata kama ningefanikiwa huo Ubunge wa EALA. Na naomba uniamini japo najua unaweza kusema naongea hivi kwa kuwa nimekosa.” “Kwangu yameisha. Na wewe?” “Yameisha. Ila naona kuanzia sasa, tubadilike jinsi tunavyoishi na watu, turudi kama zamani. Mambo yetu ni sisi tu. Sio kama sasa hivi. Tumejianika vibaya sana. Kila mahali tunaonekana hovyo! Nimejichukia sana.” Sabrina akatoka hapo kitandani na kuzima taa akijua wameshapatana.

“Sasa mimi nilijua tunapata penzi la upatanisho! Si unajua jinsi inavyokuwa nzuri? Mkigombana halafu mnamalizia kwa…” “Unakumbuka chochote tulichoambiwa na daktari juu ya mapenzi baada ya kuzaa kwa upasuaji?” “Yale mambo ya baada ya majuma 6 ujue ni kwa wale wanaume walevi na wale waliorafu. Kuhofia kuumiza wake zao. Mimi mstaarabu Brina.” Akajua akili zimeshamrudia. Jack wa zamani amerudi. Yashaisha. Akamshukuru Mungu kwa moyo wake huo wakumpenda na kutaka mambo yaishe waendelee.

“Acha kunishika Jack bwana!” “Kwani wewe huna hamu na mimi?” “Ninayo ila sasa ujue mshono wa ndani haujapona. Japo nje inaweza kuonekana kama nimepona.” “Acha niwashe taa basi niangalie hata huo mshono.” “Iwe tu kuangalia Jack. Usiende mbali. Sijajikinga na chochote kile. Ukianza tu mambo yako hapa nashika mimba usiku huu huu. Naomba kuwa mvumilivu.” “Mimi siwezi kuvumilia.” “Jack!” “Kweli tena. Yaani mara ya mwisho ni vile ulivyoniaga hapa siku unakwenda Dar, napo havikuwa vya muda mrefu ulisema ushachelewa.” “Lakini usiku wake si tuli..” “Acha kukumbushia mambo ya zamani, Brina! Mimi hali mbaya. Nitulize hata kidogo tu.” Jack akawasha taa na kurudi kitandani.

“Hapana Jack. Ushaanza kunishawishi, na mimi najiona kama sina nguvu nyingi za kukukatalia. Bora hata nisikuonyeshe.” Jack akacheka sana. “Tena leo ningekupa yale mambo yako yote unayapenda mpaka unaniita jina langu.” Sabrina akacheka, nakucheka sana. “Yote?” “Hakika nisingekubakisha. Kwanza ningekupa kwa pole ya kujifungua na kujiuguza mwenyewe. Halafu kukushukuru kusimama na mimi japo nimeshindwa mambo ya ubunge.” “Hujashindwa bwana.” “Sawa Brina wangu. Lakini ujue usiku wa leo ungepoozwa vilivyo.” Jack akajiweka kitandani na kupiga magoti mbele ya alipokuwa amekaa Sabrina. Akaanza kumbusu. “Ningekushukuru kwa kurudi na mimi huku, kunichagua na kuni…” “Huko huo mkono unapokwenda, utulie hukohuko usitoke.” Jack akaanza kucheka.

“Vipi yale majuma 6?” “Huyu daktari asinitanie kabisa. Wewe endelea kunishukuru. Ila na wewe sio fujo sasa mpaka usiku wa leo tuhamie hospitalini!” “Mie mstaarabu. Taratibuuu…” yakaanza mapenzi usiku huo. Jack na mkewe ambaye hana hata kitanzi. Akajiachia wakati mwanae hata hajafikisha siku 30. Lakini kweli Jack akawa mstaarabu haswa, alihakikisha hamuumizi. Baada ya hapo stori zikaanza sasa. Jack akimpa kinachoendelea hapo.

“Sasa hakuna kupaniki. Tutembeze siku tatu za mfungo.” “Si unanyonyesha wewe?” “Usijali. Mwanao atapata chakula.” “Na wewe?” “Nitakuwa nikinywa chai tu. Siku tatu mpaka tumsikie Mungu akitupa dira.” “Nakushukuru Brina. Asante mama.” “Tulale, kesho uende kazini kama kawaida.” “Nilikuwa nikifikiria nichukue likizo nikusaidie kazi.” “Usijali. Pina atakuja kesho kutwa kutusaidia. Tuendelee na maisha yetu kama kawaida.” Wakazungumza na kupanga mengi, wakalala.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jack akiwa anajua amebakiwa na Sabrina tu, hakuna tena cha mama, akaongeza mapenzi kwa mkewe. Sabrina naye akijua anasubiriwa viharibike kwa Jack achekwe kwao, akaongeza umakini kwa Jack. Wakashikana wawili hao, ule ukaribu wake na Pendo ukawa kidogo umepungua. Pendo amempata Willy wake, akawa na muda mwingi na mumewe si Sabrina tena. Sabrina naye alipoona Jack amepunguza ukaribu na kina Willy, ikawa shida kupiga simu kwa Pendo zaidi Jack akiwepo. Akahamishia mtindo wa kuomba kwa Jack. Yale mazoea ya kupiga simu na kuomba mara kwa mara na Pendo ikawa ni Jack sasa. Mara waombee watoto, mara mambo ya chama, wakati mwingine biashara zao. Ikawa wao wawili zaidi, Pendo yupo likizo na mambo ya Mungu, anafurahia majibu ya maombi yake. Analea ndoa na mimba.

Sabrina hakuharakisha kutoka ndani mpaka siku 40 za tokea ajifungue zilipoisha ndipo akatoka. Akaanza taratibu kwenye mambo ya chama ila akakuta ukinzani mkubwa sana. Uzuri wanawake wa pale hawakuwa wakipikika chungu kimoja. Kwa hiyo wakati akijaribu kujirudi, akagundua wenyewe kwa wenyewe walishagombana, hawasemeshani, hawawezi kufanya tena kazi pamoja. Mashitaka yakaanza kwa Sabrina. Hilo nalo akaona ni muujiza. Hapakuwa na jinsi ya kutapanya pesa kwa sababu bado Jack alikuwa lazima aweke saini ili kutoa pesa. Kwa hiyo hata huyo mpinzani alipokuwa akiwachanganya, hawakuweza kuiba pesa.

 Sabrina akarudisha nguvu kwenye mambo ya chama haswa, akifanya kwa juhudi huku akikataa majungu. Hakuwahi kutaka kumsema huyo mpinzani mbele ya hao watu akijua jinsi wanavyopenda kusambaza maneno. Akawa na kazi ya kuwasikiliza na kujitahidi kuwarudisha kazini bila mafanikio makubwa sana kwani haikuwa rahisi kama mwanzo. Kulikuwa na mgawanyiko mkubwa sana. Huyo mpinzi alishafanikiwa kuwaingia akilini na kuifanya kazi yao kuwa ngumu zaidi kuliko mwanzoni walipokuwa hawana upinzani wa ndani. Kila siku wakawa wakikutana na jambo zito na gumu huko chamani. Lakini Sabrina hakuwa akikata tamaa mpaka akawa anamshangaza sana Jack.

 “Mama unapambana! Kila siku najiambia pengine safari hili litamkatisha tamaa Brina wangu ataacha kabisa mambo ya chama kwa sababu mimi mwenyewe nilikuvunja moyo na mambo ya mama kutaka kushinda, nikajua huu ugumu tunaokutana nao sasahivi, utaona ni mimi na mama yangu ndio tulikufikisha hapa, utaamua kuacha lakini nakuona kila siku ukikutana na jambo unatafuta njia, huachi!” “Kwanza naomba uelewe kitu kimoja Jack. Sishindani na mtu yeyote, zaidi mama yako. Kokote utakapofanikiwa kutimiza ndoto zako, sina shida ilimradi ufanikiwe wewe. Mimi nakujua na nimetambua kitu Mungu ameweka ndani yako ndio nafanya kazi na Mungu kuhakikisha unafanikiwa kufika pake alipokusudia. Siwekezi nguvu ili ufanikiwe kupitia huku iwe eti ni mimi! Hapana Jack. Mimi sina huo uwezo wa kukufanikisha ila Mungu wako mwenyewe aliyekupa kicho kipaji.” “Basi mimi mpewa kipaji naona nishachoka Brina. Hakika nimekinahiwa. Hila na vijambo haviishi! Kila siku kuna hili! Najiambia hivi ni kwa nini nahangaika hivi! Sioni sababu.”

“Mimi mwenyewe nilifika hapo. Lakini kuna mambo mawili Jack. Kwanza, tunalipa garama ya makosa yetu wenyewe. Isingekuwa siri zako na mama yako, tusingekuwa hapa leo.” “Nimekuahidi hamna tena siri. Kwanza sasa hivi nimetulia na wewe tu, hata sizungumzi na kina Msindai labda baba tu tena mpaka apige mwenyewe.” Sabrina akashangaa kidogo, lakini akaona aendelee na lake.

“Ninachotaka kukwambia, tunalipa garama. Tulifungua mlango sisi wenyewe, huyu mpinzani wako akaingia. Kwa wewe kuweka usiri wako, na mimi kufunga mawasiliano hata na viongozi tulioacha huku. Ikawa ni kama tumewatelekeza. Tukamwacha huyu mpinzi akawa kiongozi wao, sisi tuko likizo. Shetani haitaji siku nyingi kuharibu, kama kujenga. Ameingia na kufanya uharibifu wake kwa muda mfupi sana wakati sisi wenyewe tukiwa tumetengana. Mungu anaamuru baraka kwenye umoja. Imeandika hata kwenye Zaburi 133. Ipo baraka katika umoja wetu mimi na wewe. Mungu alipoona mwanzoni ule umoja wetu, na juhudi zetu mimi na wewe, akaweka baraka zake. Tulipotengana tu, na shetani naye akaingia.” “Sirudii tena.” Jack akaongeza.

“Basi lazima kumuonyesha Mungu tulikosa na tumekusudia kutorudia tena.” Sabrina akaendelea. “Kwa hakika tumesamehewa. Lakini tumwambie Mungu kwa maneno na vitendo kuwa tunastahili na tunaweza nafasi ya pili kama ataturudishia tena. Sisi hatuna kimbilio jingine kama wengine, isipokuwa Mungu. Njia yetu ni nyembamba na imesonga. Kiongozi wetu ni Yesu. Lazima tubakie hapo na tukubali kufundishika. Tunyenyekee hapahapa, tufundishike mpaka ajue na kuona kweli tumetia adabu. Na tunastahili kwa makubwa.  Hapa hatutatoka kwa maombi tu ni mpaka kumuhakikisha Mungu akitukabidhi kitu kikubwa sana, basi tunauwezo wa kutenda naye kazi. Na hatutakimbia tena. Ukikimbia tu, atampa mtu mwingine bila shida.” “Basi natulia mama.”

Na kweli wakatulia wakaendelea kutumika kwa shida hivyohivyo wakiambiana waliyataka wenyewe. Wanavuna walichopanda. Ukaribu wao ukaongezeka. Hawakumsikia mama Msindai, mama Sabina na watu wote wa nyumbani kwa kina Sabrina, wala Tino mwenyewe. Msichana wao wa kazi, Pina, naye alirudi na kuwa msaada mkubwa sana kwa Sabrina, akimsaidia swala la watoto wakati yeye Sabrina akizunguka kwenye biashara zao pamoja na mambo ya chama bila kukata tamaa huku akimuomba Mungu na kumshangaza zaidi Jack. Maombi ya kufunga na kuomba kati yao likawa jambo la kawaida mpaka Jack akaanza kuelewa mambo ya Mungu kwa ukaribu. Japokuwa hapakuwa na mabadiliko makubwa huko chamani,  mambo ni kama yaliendelea kuwa magumu tu, lakini jinsi Sabrina alivyokuwa akizungumza naye, Jack mwenyewe akabakia akifanya kazi na Sabrina tu na kumuunga mkono japo hapakuwa na tumaini tena. Ni kama Jack alishaona mwisho wa kushindwa mwanzoni ila hakumwambia Sabrina ili asimkatishe tamaa.

 Ugumu wa maisha haukusikika kati yao kwa juhudi alizoongeza Sabrina akitambua anao watoto wawili wa ziada, hakutaka kumlemea Jack. Hakutumia pesa ya Tino, kwani alimuachia mama yake kile begi alichotaka Tino akichukue Sabrina akisema kina kadi za benki za watoto na vitu muhimu vitakavyomsaidia kwa malezi. Siku Sabrina anaondoka pale kwenye Villa, alimwambia mama yake amrudishie Tino. Na hakutaka kujua kama alimrudishia au la. Akaachana nao kabisa.

Ila hakuna kati yao aliyekuwa na hamu ya kurudi tena Dar wala kuwasiliana na watu wa nyumbani kwao. Kila mmoja kati yao ni kama alikinahiwa na hekaheka za jijini la Dar. Wakatulia kabisa Singida. Ila kila walipopata pesa ya ziada, hawakuacha kulipa deni kwa ajili ya mkopo wa nyumba waliyonunuliwa na Junior na mkewe huko Dar. Walipeleka pesa benki kimya kimya na kutunza resiti.

Kwa Pendo.

M

ungu alimsaidia Pendo akafikisha miezi 9 bila shida, nao huo ukawa muujiza mwingine. Sabrina alimwambia Pendo yeye atakwenda kutembelea tu watoto, sio kuwepo siku ya kujifungua kwa sababu ya wegazi wake. Inamaana akiondoka yeye, abebe watoto wote watatu na msichana wa kazi. Akamwambia Pendo wakifika huko watajikuta wakilea timu ya watoto wake nakushindwa kuangalia watoto wapya. Hata hivyo Pendo alikuwa na uungwaji mkono mwingi. Watoto wake walikuwa wakisubiriwa kwa hamu na kila mtu! Nyumba yake isingetosha na Sabrina alimwambia huo ni wakati wake na yeye wakulelewa na watoto wake tu. Kwamba macho na masikio ya kila mtu yanatakiwa yawe kwake yeye tu na wanae. Pendo asiye na mengi akawa akicheka tu bila shida.

Kukiwa kunaonekana kuna amani na utulivu, shetani naye akihangaika kivyake, muda wa Pendo nao ukafika, naye akajifungua bila tatizo bila shida. Kwa salama kabisa akiwa na mumewe hospitalini. Sabrina na Jack na wao wakawepo kwa njia ya video kushuhudia safari nzima mapaka hao watoto wakazaliwa. Ukweli walikuwa ni watoto wazuri sana. Kwa afya na muonekano pia walikuwa wakivuti kuangalia. Wazuri kwa muonekano kama Pendo na Willy wenyewe. Ilikuwa furaha yakupitiliza kwa wawili hao. Muujiza ambao hawakuutegemea. Na kweli mtoto wa kike walimuita Sabrina na wakiume Samweli kama alivyopanga mama yao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina akiwa anatoa salamu za pongezi kwa Pendo, tayari alishajigundua ni mjamzito. Walipopiga mahesabu na Jack, wakagundua ni siku ya kwanza waliporudi hapo nyumbani wakafanya mapenzi ndio siku hiyohiyo Sabrina alishika mimba. Kabla Brayan hajatimiza miezi miwili, mama yake alishashika mimba, na ina mwezi mmoja tayari. “Iweje sasa mshono ufunguke, tumbo lipasuke halafu…” “Naomba usiniingizie hofu bwana Jack! Wewe tulia.” “Iweje..” “Haitakua chochote. Nitakua sawa. Na kama wewe unaogopa, usiniambie. Unataka kunitia tu hofu, wakati haitasaidia tena.” “Basi usiogope.” “Wakati wewe mwenyewe humaanishi? Ona ulivyoingiwa hofu! Ningejua nisingekwambia kama mimba ya Brayan.” “Hapo ungeniudhi kupitiliza.”

 Safari hii hawakuchelewa kwenda kwa daktari. Halikuwa jambo la hatari sana, ila waliambiwa wawe makini tu na daktari kuwa karibu ya Sabrina. Sabrina akawa na kazi ya kliniki zake kama mama mjamzito na za Brayan mtoto mchanga na mapacha wake. Alikuwa akienda kliniki anacheka mwenyewe kama mazuri. “Hii ni aibu ya mwaka! Tunaonekana kabisa ni wazazi tusiofikiria.” “Hapana bwana. Huu ndio uzazi wetu wa mpango. Tunazaa na kumaliza, halafu tunalea.” “Hakika huyu ndio wa mwisho Jack.” “Na mimi nakubaliana na wewe. Wanne inatosha.”

Maisha yao yakaendelea kimya kimya wala wasimwambie mtu chochote kinachoendelea kwao. Jack akawa kimya na familia yake. Mambo yao wao wawili tu. Sabrina hakuwa amemsikia mama yake na wala yeye hakumtafuta hata Sabina. Ikawa hivyohivyo kwa upande wa Jack. Kimya maisha yao yakiendelea na watoto wao, msichana wa kazi akiwa msaada mkubwa kwa Sabrina.

Mungu Wa Yote Katika Yote

S

iku moja Jack alipokuwa kazini akapata simu kuwa kulikuwa na nafasi ya ubunge kwa viti maalumu, raisi hakuwa ameijaza, yeye ameteuliwa na raisi kuijaza nafasi hiyo. Alipata ububu nakushindwa kuongea. Mpaka anayempa maelezo na kumwambia siku ya kuapishwa kwake anakata simu, Jack ndio akawa kama amerudiwa na akili. Akatulia kwa muda, akagutuka na kutaka kumpigia simu kaka yake kwanza, ila akaoana mpigie kwanza Sabrina mkewe anayehangaika naye kumuombea. “Brina!” “Tokea wanao waanze kuita ‘dad’ na kujua ‘hodi’, naona wamekuwa kama wewe! Hakuna kupumzika!” Jack akacheka nakushindwa hata kumwambia alichompigia simu maana Sabrina alimtanga na maneno.

“Pokea video nikuwekee uwaone. Wamenikuta nikiomba hapa, naona wameanza na ‘dad’ na maneno mengine mengi. Sina ninachowaelewa, nimebaki nimewakodolea macho, pengine wewe dad mtu unayezungumza nao kila wakati utawaelewa.” Jack akawa anacheka na kuweka video. Akaanza kuzungumza nao. “Naomba niwapeleke sebuleni, muendelee kuzungumza mimi nimalize maombi Jack. Kuna kitu kinaendelea kwa kina Pendo, nasikia kuwaombea.” “Ni nini tena?” “Sasa tutazungumza vipi wanao wamejaa kwenye simu?” Jack akawaangalia wanae, nakuzidi kucheka maana walichukua simu ya mama yao, wao ndio wakawa wamejaa hapo, hata hakuwa akimuona mama yao ila wao.  “Nakuja. Nina habari njema.” “Sasa wewe usikate. Zungumza nao hapo sebuleni, mimi niombe tena kidogo.” Akawatoa hao watoto hapo, akarudi chumbani kuomba.

Baada ya muda Jack akaja. Sabrina akatoka. “Kuna nini, mbona mapema?” Jack akamsimulia juu ya ile simu aliyopata. “Jackson Msindai!” “Kweli tena. Siamini Brina.” “Umemuuliza Shem kama ni kweli?” “Bado. Nilitaka kuzungumza na wewe kwanza. Inamaana na kazi hapa ndio basi.” Jack akawa anacheka kwa furaha. Akampigia kaka yake. Junior akamwambia na yeye alisikia fununu lakini akataka asikie yeye mwenyewe kwanza. Na atakuwepo Dodoma wakati wakipishwa. Akampa pongezi na kumueleza mengi. Mpaka wanakata simu, Sabrina akawa anajua mumewe ameshapewa ubunge. “Wewe ni Mungu, badala yako hakuna mwengine.” Akasikika Sabrina akianza kushukuru na kumtukuza Mungu. Jack akidhani milango ya hapo ya miaka miwili ijayo kuja kugombania hapo Ubunge imeshafungwa, Mungu wala hasikii tena, kumbe Mungu anawawazia makubwa na mazuri zaidi, tena kwa haraka.“Kweli tumshukuru Mungu. Mwenzio nilishakata tamaa, nikawa nikifanya bora liende. Nilikuwa nakusubiria tu na wewe uchoke, tuondoke kwenye huu mji tukaendeleze maisha Dar, niachane na siasa kabisa.” “Tungepishana na majibu yetu.” Wakashikana mikono wawili hao na kumshukuru Mungu mpaka wakamaliza.

“Afaddhali tunahama hapa.” Akaanza kushangilia tena Jack ambaye alishachoka huo mji. “Kaa hapa chini Jack, acha kukimbiakimbia kila wakati.” “Hakika naondoka Singina, Brina. Hatuna haja ya kubaki hapa! Kwa nini!?” “Naomba usijisahau Jack. Huu ubunge ni wa kuteuliwa. Aliyekupa, anaweza kukupokonya muda na wakati wowote akiamua. Hilo ni moja. Nakuomba uvumilie ili hii iwe njia ya kwanza ya kukupatia cha kwako, yaani ubunge wa hili jimbo, kama kaka yako alivyojipatia ubunge kwenye jimbo lake kwa kuchaguliwa na wananchi. Ukifika hapo, basi ujue hakuna mtu wa kukupokonya. Hiyo moja, lakini pili, kuendelea kuishi hapa japo umekuwa mbunge iwe njia ya kurudisha mioyo ya watu wa hapa, kwako. Wathibitishie kwamba haukuwa na nia ya kuwakimbia tokea mwanzo. Wewe ni Mbunge wa viti maalumu, lakini pia unakwenda kuwawakilisha wao. Kwamba upo pamoja nao kwa nyadhifa yoyote ile utakayoshika. Tukiondoka tu sasahivi, uchaguzi ujao hatutashinda.”

“Brina! Hutamani kuishi Dar?” “Mimi natamani kuishi na wewe, popote ulipo na Mungu alipotupa.” Hapo akamgusa Jack mpaka akarudi kukaa. “Kweli Brina?” “Wewe sio Junior Msindai, Jack. Junior yupo mbali sana kwenye siasa. Ameshajijenga na amethibitishwa na Mungu mpaka Mungu ameridhika naye ndio maana unamuona mpaka baba yako anamsifia kila wakati. Wewe bado upo chini. Tafadhali tuendelee kujijenga kwenye huu msingi. Hapa ni kwetu na Dar ni kwetu. Hatuna haraka ya kukimbilia popote. Mungu ameweka mkono wake hapa. Tusikimbie.” “Kweli Mungu alikusudia kukuweka kwenye maisha yangu Brina. Ingekuwa mwingine angetamani kwenda kuishi kwenye ile nyumba kubwa na nzuri kule Dar. Au angetamani yale maisha kule. Lakini naona mwenzangu unafikiria mbali kuliko mimi! Basi tutabaki hapahapa kama ulivyosema. Ila tujiandae kwenda Dodoma kuapishwa. Tunabeba watoto wetu wote. Tunaenda nao.” “Kwahiyo kazi tena basi?” “Ndio nimepewa kazi ingine mama. Ila sio uhasibu.” “Hongera muheshimiwa Msindai.” Sabrina akamfanya Jack ajisikie vizuri sana. “Sasa hii pongezi urudie nikishaapishwa. Sasahivi twende ukanipe pongezi ya vitendo. Au umefunga?”

“Usiku. Usiku lazima nikupongeze. Acha sasahivi niombe Jack. Ipo roho ya mauti naiona kwa kina Pendo. Sijui kama ni kwa familia yake moja kwa moja na Willy, au familia ya Ngoi? Sijui. Nipo kwenye kumsihi Mungu awalinde na kuwaepusha na roho ya uharibifu inayowanyemelea.” “Umemwambia Pendo mwenyewe?” “Hapana. Ila nitamwambia. Najua bado yupo kwenye kusherehekea uzazi.” “Uzazi huo mpaka leo miezi mitatu! Mungu anaona ameshamaliza mapumziko, arudi kazini.” Sabrina alicheka sana hakutegemea Jack aseme hivyo.

“Basi hapa kwa kuwa hakuna mapenzi, acha nikasubirie barua ramsi ya kuteuliwa, ndipo na mimi nifanye taratibu za kuacha kazi. Nataka nipaache pale vizuri mpaka atakaekuja nyuma yangu atambue Jackson Msindai alikaa hapa na alipatendea haki pale kwenye ile ofisi, sio nitoke kama nakimbizwa.” Jack akatoka, Sabrina na yeye akarudi kwenye maombi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment