Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 56. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 56.

Sabrina akapika mpaka akamaliza, pakiwa kimya vilevie, akajua Jack amelala na watoto huko chumbani. Akamuwekea chakula baba yake  na kwenda kumuangalia. Chakushangaza akamkuta Jack amekaa tu pembeni ya kitanda amejiinamia. Sabrina akaenda kukaa pembeni yake. “Nilijua umelala?” Jack akamwangalia tu. “Twende tukale au unataka nikuletee hapa?” “Nimekasirika sana, siwezi kula.” Sabrina akakaa vizuri na kumwangalia vizuri.

“Sasa umekasirika nini?” “Kila kitu. Nimekasirika na nahisi umeniadhibu au umenilipa kisasi kwa kumrudisha Tino kwa wanangu makusudi.” “Sio kweli Jack!” “Ni hivyo tu. Ukijua wazi nilimfukuza huyu mtu, tena kwa kumpa mpaka restrain order, wewe unakwenda kinyume yangu na kumpa watoto kwa baraka za wazazi wako!? Umenidhalilisha kupita kiasi Brina. Katika yote ningetegemea, ila si kwenda kinyume nami kwa kiasi hicho! Na sijajua ni ujumbe gani unataka kunifikishia?” “Tafadhali usiende mbali Jack. Uliondoka na sikujua kama unger…” Jack akasimama. “Si umetaka tuzungumze? Sasa mbona unaondoka?” “Nimekasirika na kuumia sana Brina. Kwa sasa siwezi kuzungumza na wewe chochote, tukaelewana. Acha nikatembee kidogo.” Jack akataka kutoka akawa kama amekumbuka kitu, akageuka.

“Ni kama nahisi nilijipa au ulinipa nafasi ambayo nahisi siyo! Na kama ndiyo basi ni kwa vile upendavyo wewe. Unanipa hiyo nafasi na kunipokonya vile unavyopenda au kujisikia wewe. Nikiwepo ni sawa. Nikiondoka basi pengo langu linaweza kuzibwa bila shida, tena na yeyote yule hata kwa mtu kama Tino! Unanifungia mimi simu zangu kila wakati unapojisikia kutozungumza na mimi, bila kunifikiria mimi, lakini si kwa watu wengine wanao kuumiza! Umeniacha mimi mpweke kule, huku ukilea na Tino! Mmeanzisha familia yenu na wazazi wako wakiwepo, huna wasiwasi! Unatangaza kumsamehe Tino, huku mimi umenifungia simu zangu? Kwamba mimi dhambi zangu NI KUBWA MNO, huwezi kusamehe ila Tino yeye umeweza kumsamehe na mnaendeleza maisha ya kitajiri huku! Mpaka naanza kuamini ni kweli nimependa nisipopendwa.” Jack akarudia maneno ya mama yake na kutoka.

Kitendo cha kuona watoto wake begani kwa Tino wamelala na Tino kusema mpaka aliwalisha asubuhi hiyo, kilimuuma sana Jack nakushindwa kujizuia. Akasahau hata makosa yake na kuona Sabrina amemtenda ubaya wakupitiliza kwa kumkaribisha Tino kwa undani kiasi kile, mpaka kumpa watoto!

Sabrina akahisi baridi inapita kuanzia juu mpaka chini kama vichomi, akashindwa hata kusogea pale. Hakutegemea Jack aliyecheka naye alipoingia hapo kwa mara ya kwanza, angembadilikia kwa kiasi hicho! Ni kama amebadilika gafla! Asijue alichokiona kwa mapacha wake wakiwa na Tino ndio kimemvuruga. Akabaki amekaa kama sanamu. Alikaa pale bila hata kusogea mpaka akamsikia mama yake na Sabina wamerudi, akatoka. “Mbona umepoa hivyo!?” Mama yake akamuuliza. “Nipo tu sawa mama yangu. Sasa na nyinyi mbona mmerudi mapema wakati nimesikia mnakwenda madukani?” “Kwanza nisifie.” Sabrina na Sabina wakacheka. “Umependeza mama Sabina.” “Sasa upendezaji huu Sabina ameona nisiupotezee mtaani, usiku anitoe mimi na baba yake. Nimeona nije nipumzike, jioni tunatoka. Uzazi mzuri mwanangu!” Akajisifia mama Sabina akitegemea Sabrina aendelee na cheko lakini akamuona Sabrina kama hayupo tena pale kimawazo, na akili imevurugwa. Akamuangalia Sabina kumuona kama na yeye amemgundua mdogo wake, kama hayupo sawa.

“Vipi wewe Sabrina?” Ikabidi Sabina kuuliza asijue moto uliokuwa umewashwa hapo muda mfupi uliopita. Baba yao kimya. “Kuna nini tena!?” Mama yao naye akaongeza swali alipomuona hata mumewe amepoa, na chakula alichowekewa pia hajagusa. “Mimi naona haya mapumziko yetu yameshaisha, sisi kesho tunaondoka.” Sabina na mama yake wakashangaa sana. Hawakutegemea kabisa. “Wewe Sabrina, unaacha pesa yote hiyo iliyolipiwa hapa!?” “Sina jinsi dada. Lazima niondoke. Jack yupo hapa, nimerudi naye, nimemkuta akinisubiria kwa Pendo. Hali si nzuri, nahisi sikufikiria vizuri kuja kukaa hapa. Nimemuumiza sana Jack.” “Mbona yeye alikutelekeza? Sasa hivi yamemshinda ndio…” “Ni nani ambaye hajawahi kunitelekeza?” Sabrina akamuuliza dada yake.

“We Sabrina?” “Tuwe tu wakweli dada. Nani ambaye hajawahi kunitelekeza? Lakini si wote mpo hapa na mimi? Tena wote wamekua wakinirudia mambo yangu yakishakuwa mazuri. Lakini Jack amekuwa akinirudia nikiwa matatizoni na yeye ndio nimekua nikimtenda vibaya kuliko wote! Linapofika swala lake huwa sijui ni kwa nini najisahau nashindwa kufanya maamuzi sahihi! Halafu yeye huwa anaacha kila kitu, na kunifuata! Hapo alipo amenifuata mimi na watoto hata kazini hajaaga amenikimbilia huku ambako nimetangaza msamaha kwa kila mtu, huku nikiwa nimemfungia yeye.” “Lakini ulitaka mapumziko Sabrina!?” “Wala usinifariji dada. Nimekosa. Jack ni mume wangu. Mapumziko ni mpaka kifo. Halafu ukweli Jack hakuwahi kunichosha ila kunibeba kwa hali na mali. Kusema nimejificha huku eti napumzika, nimekufuru dada. Sikufikiria vizuri. Acha niondoke tu, nikajaribu kutengeneza kama sijachelewa.” Akawageukia wazazi wao.

“Ila baba na mama, mimi nashauri nyinyi mmbaki, muendeleze mapumziko mpaka muda uishe, ndipo muondoke. Msiiachie hii pesa hapa.” “Mmmh!” Sabina akaishia kuguna. “Naomba mnisaidie kukusanya vitu vyetu kokote vilipozagaa humu ndani. Nawasiliana na dada Pendo, twende jioni tukawaage, kesho tuondoke.” “Na mimi nakuunga mkono.” Wote wakamgeukia baba yao.

“Nafikiri na sisi kama wazazi hatukufikiria vizuri.” “Juu ya nini!?” Mama Sabina akauliza kwa mshangao na ukali kidogo kama anayejua ni nini anachouliza ila tu jazba. “Hiki tulichokifanya hapa! Hakikuwa sahihi, mama Sabina. Sabrina ameolewa. Tulimuozesha huyu kwa heshima kabisa. Kukaa naye hapa bila kuzungumza na mumewe haikuwa sawa.” “Sasa yeye si alikuwa amemtelekeza! Tungefanyaje?” “Huyu kijana alikuja na wazazi wake mpaka nyumbani kwetu, akatimiza taratibu zote za ndoa, mama Sabina. Tusilisahau hilo. Akalipa mahari kabisa. Tulipaswa kufanya mambo kiutu uzima, sio kuishia barabarani.” “Mimi sijaishia barabarani. Yeye Sabrina alisema anataka kupumzika ndio atajua chakufanya! Sasa tungemuacha hapa peke yake na mume alikuwa haonekaniki, anaendelea na mipango yake na mama yake huko? Pengine ameona ameshindwa huko ndio amejirudi, lakini hana wakumlaumu ila yeye mwenyewe.” Akajibu mama Sabina kwa jazba na kumuumiza Sabrina.

“Jamani wakulaumiwa ni mimi mwenyewe, wala si Jack au nyinyi. Mimi ndio nilikosea. Sikufikiria vizuri, na tokea mwanzo nilishindwa kuzungumza na Jack kumuweka wazi ni nini kiliendelea kati yangu, mama yake na dada yake, tulipokuwa hospitalini, yeye akiwa hayupo. Nafikiri hata dada Pendo alisema, kama utakumbuka mama. Mimi ndio nikasema tumuache, tusimchanganye kumbe ndio nimemchanganya zaidi na kumuumiza kwa maamuzi yangu ya tokea mwanzo. Tafadhali msinunue matatizo yangu. Hili nahusika nalo mimi mwenyewe, tena moja kwa moja. Kama mtabaki mbaki, ila mimi naondoka, narudi kwangu.” Sabrina akataka yaishe.

“Hata hivyo umeshapumzika vyakutosha.” Mama Sabina akajibu kwa hasira akichukia kuona anataka kupokonywa tonge mdomoni. Alishaonjeshwa maisha ya  kitajiri hapo, hakuwa tayari kuyaachia. Akapumbazwa na wema wa Tino aliowaonyesha muda mfupi tu aliokuwa nao hapo. Pesa alizokuwa akimpa hata yeye mwenyewe huyo mama, akaona Jack anataka kumrudisha Chalinze mapema sana! Hakuwa tayari kwani alishanogewa na maisha ya Tino, yakitajiri, aliyokuwa akiwapa hapo, akasahau anawajibika yeye kama mama.

Sabrina hakumjibu tena akarudi chumbani. “Sasa mtafanyaje mama?” Akamsikia dada yake akiuliza. “Mihela yote hii tuiachie hivihivi eti kwa sababu yeye Jack amemaliza yake na kuamua kurudi sasahivi! Hapana kwakweli. Hatuwezi kuyumbishwa kama watoto wadogo. Mimi hapa siondoki mpaka tumalize muda wetu. Hatuwezi tukawa tukichezea pesa kwa kiasi hiki. Hili ni jasho l…” “La Tino.” Sabrina akatoka chumbani akiwa na nguo chafu za wanae na kumjibu hivyo mama yake.

“Kwani hilo ndio tumelijua leo?” Akauliza mama Sabina kwa jazba. “Tokea tunahamia hotelini, na Jack yupo kwenye mambo yake ya kinyang’anyiro tulikuwa tukijua ni jasho la Tino na tukakaa kule kwenye lile lihoteli na kuhamia hapa bila shida. Leo kashindwa na yakumshinda ndio aje atuvuruge na sisi? Mbona tokea mwanzo asiache kila kitu kama kweli yeye ‘muachaji’ na kukufuata tokea wakati ule upo mgonjwa, kidonda cha kujifungua ndio kibichi kabisa, upo pale kwa Pendo, nikihangaika na wewe, iwe sasa hivi?” Mama Sabina akauliza. “Nakuuliza wewe Sabrina. Kama yeye muachaji kweli kama unavyosema huwa anaacha mambo yote na kukukimbilia, mbona asiyaache ya Ubunge wa huko Afrika ya Mashariki akakufuata pale kwa Pendo, ndio anakufuata sasahivi, kama si kuchanganyana tu?” Sabrina akazidi kuumia na kujilaumu kuweka mambo yake na Jack hadharani zaidi kwa familia yake. Akaona hapo asijibu.

“Naomba nitafutie tu tiketi za kesho dada yangu, niondoke kesho.” “Kwa hiyo unaacha vitu vyote hivi? Maana kwenye ndege huwezi kubeba vyote! Acha kuondoka kwa kukimbiakimbia wewe Sabrina. Alikuacha, amerudi. Basi sasa hivi ndio muondoke ukiwa na wewe upo tayari! Usikubali kukimbizwa hovyo!” “Mizigo mingine nitaiweka kwenye mabegi, na maboksi, itatufuata kwa basi. Tutakutana nayo hukohuko mbele ya safari.” “Makubwa!” Sabina akajibu vile lakini Sabrina akawa ameshaamua, mandalizi yakuondoka hapo yakaanza. Hakutaka kuzungumzia tena mambo yake na Jackson.

Sabrina akaingia bafuni kufua nguo za wanae. “Hakika hapa siondoki mpaka mwisho.” Akamsikia mama yake akiongea kwa kupania, akisikika mwenye hasira mpaka akamshangaza Sabrina. “Anamuacha mwanaume anayejielewa, wamaana hivi, anahangaika na mtu ambaye hana hata msimamo!” Sabrina akashangaa sana na kuumia. Kwamba gafla Jackson Msindai hana maana isipokuwa Tino! “Ndio ujue kila mtu na akili yake mama. Hata kama Tino alikosa, lakini amejirudi. Na Tino ana watoto naye wawili! Tena damu inayofanana na kwao kabisa! Huyu kijana mwingine hata maisha yenyewe bado hayajamkalia sawa, anahangaika hajui pakushika!” “Siasa zenyewe ndio hizo. Kupata na kukosa.” Akamsikia mama yake ameongeza kwa Sabina. “Na ndio kakosa sasa.” Sabina akaongeza kishabiki.

“Halafu analoshindwa kukumbuka na anajidanganya huyu mdogo wako kwa maneno ya huyu kinaja asiyejielewa, anasahau kuwa huko ukweni hawamtaki yeye na hao wanae pia. Mama Msindai hataki hawa watoto hata wakanyage nyumbani kwake! Sasa badala aende na mwenye watoto, ambaye ameshasema huko amejijenga na maisha huko ni mazuri, anataka kujichanganya, yamdodee tena, arudi nyumbani na watoto! Kama sio kuandikiwa kukosa huko ni nini?” Akamsikia mama yake akiongea kwa sauti ya chini kama kawaida yake anavyomuona mjinga, fungu la kukosa. “Ndicho anachokitaka na atakipata tu. Mwache amwache Tino aondoke adhani yeye na hao watoto ndio wamaana sana, aendelee kumringia Tino. Wenzake wanalilia hizo bahati!” Akaongeza tena Sabina kwa sauti ya kumteta kama asiwasikie.

 “Halafu mama huyu Tino analiliwa na wanawake kibao!” “Kijana mzuri je? Mzuri na pesa anayo. Kinachomshinda kutulia na baba watoto wake, wakalea watoto na kukuza watoto kama wazungu wenzao ni nini kama si kuchanganya tu watoto?” “Wazungu wa Singida?” Akauliza Sabina kwa kejeli na kucheka. “Hebu niambie jamani kama si balaa hilo ni nini? Kwanza kumbe hata nywele zao zenyewe hawajazijulia mpaka alipokuja baba yao mzazi! Kawaletea wanae vitu vya maana, angalau watoto wamefanania na utajiri wa kwao! Eti sasahivi anataka kuwarudisha kwenye vumbi huko, kama si kuzisaka shida ni nini?” Sabrina akaumia sana wasijue amewasikia vile walivyokuwa wakimsema kwa kunong’ona.

“Twende ukanichagulie nguo nzuri, tutoke, Sabina mwanangu.” “Mama huyumbishwi?” Akamsikia dada yake akiuliza na kucheka kishabiki. “Hata kidogo! Kwa kipi mno? Hanitoi hapa kwa kunikimbiza. Kwanza Tino alisema atakuja kutuaga na kutushukuru rasmi kwa kusaidia kumlelea wanae. Sasa unafikiri atakuja na maneno matupu ya siasa hapa?” Sabina akazidi kucheka. “Akijidai kuondoka tu na wanae, mimi nitakuja tukae wote kwa hizo siku zilizobaki. Bahati kama hizi haziji mara mbili.” “Kumbe! Akisema cha nini, wenzie wanalia tutakipata lini.” Mwishoe akawasikia wamehamia chumbani huku wakiendelea kumsema.

Akaendelea kufua mpaka akamaliza, Jack hakuwa amerudi na wanae wakawa bado wamelala. Akatoka kwenda kumtafuta. Akamkuta amekaa sehemu, humohumo ndani ya uzio wa Villa, lakini peke yake. Na yeye akaenda kukaa pembeni yake.

“Naomba turudi na watoto nyumbani.” Jack akamwangalia. “Namaanisha Singida. Nimeshaanza kufungasha ili kesho tuondoke.” “Nashindwa kurudi mle ndani.” Sabrina akawa ni kama amemuelewa. “Kukaa mle ndani nasikia ni kujidhalilisha kwa hali ya juu. Yaani na mimi nakuja kula na kulala kwa Tino! Natunzwa mimi na wanangu na mwanaume kama Tino? Hata kama sina uwezo kama wake, ni bora niondoke mimi ambaye sina uwezo, niwaache.” “Tutaondoka wote.” “Mimi sina pakwenda. Sina mahela ya kukodi hapa.” “Kuanzia sasahivi popote unapokwenda, ujue tunakufuata wewe.” Jack akamwangalia na kunyamaza.

“Hata kama chini, twende tukalale wote. Popote pale. Sasa hivi tutakuwa tukipanga mambo yetu pamoja. Na tabia ya kukublock naacha kabisa.” Jack kimya. “Nisamehe mume wangu.” Hapo akamgusa Jack. “Sasa ndio tunakwenda wapi?” Jinsi alivyouliza, Sabrina akajua hasira zimeanza kupungua. “Au tukalale kwa dada Pendo?” “Hapana. Pendo alinitukana. Ananiona mimi mjinga. Sijielewi. Sitaki kurudi tena kwake nikiwa na shida.” Katika mtu wa mwisho kutaka kugombana naye ni Pendo. Sabrina alishampenda Pendo na kuona wanaendana katika kila jambo. Ila akaona kwa wakati huo aache tu asimtibue zaidi.

“Na kwa Sabina pia sitaki. Namuhesabu dada yako ni msaliti mkuu na amenidharau kupita kiasi. Hawezi kumrudisha Tino kwako wakati akijua mimi ni mumeo! Hata kama ulimjua Tino kupitia yeye, lakini angetambua nafasi yangu na kuiheshimu. Hiyo ni dharau ya hali ya juu.” “Basi kwa kuwa tuna watoto, siwezi kukwambia twende tukalale pale kwetu ambako hakuna hata kiti cha kukalia. Ingekuwa ni mimi na wewe tu, ningekwambia twende tukalale hata chini. Lakini kwa kuwa tuna watoto, nashauri twende tukatafute hoteli ya uwezo wetu, kesho turudi kwetu, Singida.”

“Unauhakika?” “Kabisa Jack. Mimi nilitaka tu kupumzika. Nishapumzika vyakutosha, turudi nyumbani tukaendelee na mipango yetu.” “Wala si kuendelea. Huko Singida nako kumeharibika, hakufai! Nimeharibu kupita kiasi mpaka nafikiria kurudi kutafuta kazi nzuri huku Dar. Tena safari hii sitaki tena serikalini. Nitafute kwenye kampuni nzuri nilipwe vizuri huku Dar, si huko Singida kuendelea kudhalilishwa.” “Ni nini tena?” “Hili swala la Ubunge wa EALA, imekuwa kama mkosi Sabrina. Nimejichafua kupita kiasi. Nimerudi chini kabisa. Kama unadhani kuna kuendelea, basi ujue hali ni mbaya kuliko vile ulivyonikuta mwanzo kabisa ulipohamia Singida.” Akamuelezea kila kitu jinsi mpinzani wake anavyomchafua. “Sasa ubaya ni  kwamba ni vita ya ndani kwa ndani! Heri ingekuwa anatoka chama pinzani. Ila ni ndani! Amegeuza watu wote wapo upande wake!” Akasikika amekata tamaa kabisa. Sabrina akazidi kujilaumu.

“Nisikilize Jack. Shetani ni kama simba angurumae. Na huwa akinguruma, anaogopesha sana. Lakini hana lolote, ni kelele tu. Ila sisi tunaye Simba wa kabila la Yuda. Yeye akinguruma, kila kitu kinakaa sawa.” Jack akamwangalia. “Usitishwe na kelele ya ‘kama simba’. Si simba huyo. Anakutisha tu ukimbie. Ni kelele tupu.” “Sabrina! Ame…” “Nakwambia acha kutishwa na kelele, Jack. Hizo ni kelele, na kamwe hatutakimbia mji kwa ajili yake. Tutaondoka Singida, Mungu akimaliza shuguli zake kwenye ule mji kwa kututumia sisi. Mungu akisema tuondoke, tutaondoka. Lakini si kwa kutishwa. Hatutakimbia, wala kutishwa. Hata wifi Jacinta nilimwambia. Sijamalizana na Singida. Na mimi si mtu wa nusunusu. Nikimalizana na Singida, ndipo nitaondoka. Tena tukiwa na baraka za Mungu, lakini si vinginevyo.” “Hata mimi uliniambia hivyo. Lakini ilikuwa kabla ya huyu mpinzani!”

“Tuliliweza lile jimbo likiwa na yule mpinzani aliyetawala kwa kura za wananchi wengi, kwa miaka mingi tu. Halafu eti leo tuje kukimbizwa na huyu mpuuzi ambaye hajawahi kufanya chochote pale! Acha kutishwa Jack. Kwanza hukufanya kosa. Ubunge wa EALA sio siri. Majina yalitangazwa tokea hata uchaguzi wenu kufanyika. Ilijulikana na kila mtu kasoro kwetu ambao hatukuwa mitandaoni. Sasa siri hapo iko wapi?” “Anasema mimi sikuwaambia pale jimboni.” “Tokea lini wewe umekuwa ukiwaambia mipango kama si kuwaletea matokeo mazuri tokea mwanzo? Eti Jack?” Jack akaanza kufikiria. “Miradi yote tuliyofanya pale Singida, ulikaa na mtu wa chama mkapanga ndipo mkachukua nao hatua au waliyaona tu matokeo mazuri? Wao wanajuaje kama ulikuwa ukihangaikia huu Ubunge kwa faida yao pia? Kwamba kama ungeshinda inamaana ungekuwa na nguvu, pamoja na uwanja mpana wa kuwawakilisha kimataifa?” Hapo akaanza kubadili hata mtazamo wa Jack mwenyewe.

“Kukimbia ni kuhama mji kisha kwenda kugombania kwingine. Sisi tulikuwepo pale, miradi ikiendelea, na wewe ukihangaika kutuwakilisha kimataifa. Hilo ni kosa au ushamba wake huyo anayekuchafua, asiyejua mambo?” “Sasa kama unayajua yote hayo kwa nini ulinifungia simu zangu ukaniacha mimi naabika sina majibu ya kueleweka? Ulinitelekeza Brina.” “Nimekosa Jack. Nakuahidi sitarudia tena. Najutia vibaya sana. Nahisi mimi nimechangia kufungua huo mlango wala si wewe. Nisingepotea kwa muda wote huo, tusingetoa huu mwanya. Lakini naamini Mungu ataturehemu tu. Turudi nyumbani kwetu Singida, tukaendelee wala tusikimbie.” Jack akatulia.

“Twende. Huna haja yakuingia ndani. Nabeba vitu vyetu, naingiza kwenye gari na watoto wetu, naaga, tunaondoka.” Jack akabaki akifikiria. “Twende Jack. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Mungu atatusaidia. Hakuna kukimbia.” “Hata hapa sitakimbia. Japokuwa ndugu zako wameniumiza, twende tu nikakusaidie kukusanya vitu, tuage na kumshukuru mama kukusaidia kulea, tuondoke na watoto wetu.” Wakarudi pale walipokuwa wakiishi kina Sabrina.

Bado baba yake alikuwa amekaa sebuleni, Sabina na mama yake wapo chumbani. Jack akapitiliza chumbani wala hakukaa hapo. “Sisi tunaondoka baba.” Sabrina akaaga. “Sasa hivi?!” “Ndiyo.” “Unataka nikusaidie nini?” “Jack atanisaidia baba yangu. Wala usihangaike. Kwanza wala si vitu vingi sana.” Mama yake akatoka. “Yaani gafla mnaondoka sasahivi?!” “Ndiyo.” Sabrina akajibu. “Mnakwenda wapi sasahivi watoto wote wamelala?” “Tutajua huko mbele ya safari, mama.” “Huko nikusumbua watoto Sabrina. Nakwambia ukweli wala sitakuficha. Kuwa mama mwenye msimamo. Ukiyumba wewe ujue unayumbisha watoto. Huwezi ukawa wewe ni mtu unayeyumbishwa tu.” “Wewe usiwe na wasiwasi mama yangu. Hawa watoto watakuwa tu sawa. Acha tusaidiane, tutoke.”

“Utakuja kunikumbuka Sabrina wewe! Tena ukiharibikiwa safari hii ujue unao watoto watatu! Uliachwa nao hao, ukajionea mwenyewe! Sasa wewe chezea bahati, kama hujalia tena peke yako.” “Mungu atanirehemu.” “Si ndio amekurehemu! Unataka rehema hizo upewe mara ngapi? Ulitelekezwa hapa. Tino amekusaidia. Kweli unataka uondoke hapa bila hata kumpa nafasi aage watoto wake! Ubinadamu huo uko wapi, Sabrina wewe? Utalaaniwa bure, bila sababu.”

“Hebu subiri kwanza mama. Mbona gafla swala limekua Tino tu? Mbali na Tino kulipia hapa, msaada gani mwingine aliotoa? Kaja juzi tu hapa kakuta watoto wakubwa kabisa hawa, imekua nachezea bahati!? Bahati hiyo ni ya vyanuo vya kuchania nywele hizi za hawa watoto?! Kama watoto wangekuwa wanakuzwa kwa vyanuo na shampuu za nywele tu, si kila mtoto angekuwa na hali kama za kina Jeiline?” Sabrina akawa amekasirika kabisa. “Hawa watoto wamekua au wapo hivyo walivyo na sabuni za Jack, na mbona kila mtu alikuwa akiwasifia! Leo kaja Tino, na maneno ya kujitilisha huruma, na vijisenti vyake ndio imekua nongwa?” “Wala si vijisenti.” “Basi hata kama ni milionea, simtaki. Acheni nikaharibikiwe mwenyewe na watoto wangu, pamoja na Mungu wangu. Kama mnawasiwasi na kuja kuachwa tena na hawa watoto, nikaja kuwa mzigo kwenu, msiwe na wasiwasi. Sitarudi tena na wanangu huko nyumbani. Nitahangaika nao mimi mwenyewe. Hata nikiwa na shida sitawasumbua tena. Nitahangaika mimi mwenyewe na Mungu wangu ambaye huwa haniachi na wala hajawahi kunichoka. Hamtapata mzigo tena kutoka kwangu. Endeleeni na maisha yenu, acheni mimi ambaye situmii akili nikahangaike kivyangu.”

“Nani amekwambia hutumii akili?” Akauliza Sabina. “Nimewasikia sana wewe na mama mkisema situmii akili. Naachia bahati ya Tino. Niacheni na ujinga wangu na wanangu.” “Utatukumbuka Sabrina wewe?” “Wala sijawahi kuwasahau dada yangu. Nawajua vizuri sana.” Sabrina akaondoka hapo maana walishaamsha watoto wote, akasikia wakizungumza ndani na Jack. Akajua sababu ya kuongea kwa sauti ya juu ameamsha wanae. Jack hakuingilia kabisa japo alisikia kila kitu. Akajisikia fedheha ya hali ya juu. Ila hakuwa na jinsi. Wakakusanya vitu vyao vyote, wakatoka hapo baada ya Sabrina kuwaachia funguo zote za hiyo Villa na maagizo ya kuparudisha pindi watakapokuwa tayari. Ndipo wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walitafuta hoteli ya kawaida tu. Jack akawaacha hapo na kutafuta vifaa vyakufungia mizigo yao maana vitu vingine walikuwa kama wamevitupia tu kwenye gari. Akarudi na masanduku pamoja na mabegi. Ikaanza kazi ya kufungasha tena. Walipomaliza kuweka mizigo yao vizuri. Jack akatoka tena na mizigo waliyotaka iondoke na basi na kwenda kuituma kituo cha mabasi ili iondoke kwa basi. Kisha kutafuta tiketi zao sasa za ndege. Jack hakutaka kutumia tena mtu yeyote kumsaidia. Akayafanya yote yeye mwenyewe ndipo usiku sasa wakaelekea nyumbani kwa Pendo kumrudishia gari yake na Sabrina alimwambia nilazima akamuage.

Jack alifika na kukaa sebuleni na wanae akiwa ameshachukua namba ya simu ya mwenye taksii na kumwambia akiwa tayari atampigia afike hapo nyumbani kwa Pendo kuwachukua. Pendo na Sabrina wakaingia chumbani kuteta kama kawaida yao.

“Mbona sasa kama mnaondoka mbiombio? Shuguli zimemuisha mumeo na mama Msindai ndio katulia sasa?” “Nilimuomba mwenyewe kwa Mungu huyo. Mungu akanipa kwa upendo na heshima kubwa sana. Acha tu niende dada yangu. Hata hivyo nishapumzika vyakutosha.” “Nimemuona alivyotulia pale sebuleni. Sasa mama yake?” “Amesema anamwacha kwa muda kwanza. Naona mara ya mwisho hawakuachana vizuri. Mimi nilimwambia sitajali, hata kama anataka kwenda na Brayan kumsalimia, nitamfungashia maziwa ya mtoto aende naye akamsalimie bibi yake, naona amekataa. Nimemuacha.” “Yanawarudi wenyewe. Nasikia wageni wenyewe aliokuwa amewaalika kwenye babyshower ya Brayan walimsusia. Akajidai kukusingizia wewe.” “Dada!” “Kweli tena. Ni kama akaingia mkosi baada ya pale hospitalini. Dakika za mwisho kabisa, kila mtu akawa anampa udhuru. Nancy kayasikia huko mtaani.” Pendo akamsimulia  mengi, Sabrina akashangaa na kunyamaza tu.

Mwishoe Jack akaita taksii, wakaagana hapohapo, Sabrina na familia yake wakaondoka kurudi hotelini. Kesho yake tena wakaita taksii ikaja kuwachukua na kuwapeleka uwanja wa ndege. Sabrina akarudi Singida na familia yake bila kuwasiliana tena na ndugu yeyote upande wa Msindai wala kumsikia Sabina na mama yake. Waliondoka kimya kimya. Hiyo nayo ikawa mara ya pili tena Sabrina kuondoka jijini akiwa amejifungua bila maelewano mazuri na mama yake mkwe. Mwanzoni alidhania ni kwa sababu ya watoto ambao si wa Jack, safari hii akamzalia Jack mtoto wa kiume pia haikusaidia. Bado mama Msindai hakutaka kumsogeza karibu yake. Ila safari hii ndio ikawa mbaya zaidi. Ikawa ndugu upande wa mke, mama mkwe na shemeji, wamemchukia mume, hawamtaki tena Jack. Wanamtaka Tino aliyerudi na ahadi pamoja na pesa nyingi. Na ndugu upande wa mume nao, mama mkwe na wifi wamemchukia mke. Kwa hiyo Jack akaona hata asiendelee kumvuruga kaka yake. Akaona maamuzi yake yanaishia kuleta kutoelewana kati ya mama yake na kaka yake, pamoja na Jacinta pia. Akaona safari hii awaache kabisa. Wakaondoka jijini kimya kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ugomvi Wa Wapendanao Ukishirikishwa Nje, Wao Wakisameheana, Huacha Madonda Nje.

Nini Kitaendelea?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment