Alipomaliza
kuzungumza na Tino tu, akaelekea jikoni bila ya kumsemesha Jack. Na yeye Jack akasimama kwa haraka na kumfuata. “Naomba
tulia Jack, ili nipike.” “Kwani wewe ulikuwa hata ukiniwaza?” Sabrina
akaendelea nashuguli zake. “Mimi nilikuwa naangalia simu usiku kuchwa, Brina!
Najiambia pengine Brina wangu hasira zitakuwa zimeisha, sasa hivi anahamu na
mimi. Nikawa nikikutumia ujumbe mchana na usiku!” Sabrina kimya. “Bado
umekasirika?” “Hapana Jack.” “Kwa hiyo umenisamehe na bado unanipenda?” Sabrina
akaendelea na shughuli zake.
“Hata
iweje, sitakaa nikakuficha kitu tena, Sabrina wangu. Siri ni kati yangu mimi na
wewe tu. Kwanza tutakuwa hatuwaambii watu mambo yetu.” Sabrina kimya. “Nimekoma
Brina. Halafu hata ubunge wenyewe nilikosa. Sasa hivi sitaki tena mambo ya
siasa. Nakutaka tu wewe Sabrina wangu. Au unasemaje?” “Maswala ya kazini umeyaachaje
Jack?” “Nimeyaacha na sijali. Nimekufuata wewe.” Sabrina
akamwangalia na kuchoka kabisa. “Kwa nini hukuomba ruhusa hata ya bila malipo?”
“Hivi unajua inachukua muda mrefu kujibiwa? Na mimi sikuwa na muda wa kusubiri
nilijua nikija kukupoteza tena safari hii, naweza nisikusikie tena.” “Hivi
ukoje Jack wewe jamani?!” “Sasa wewe kwa nini uliniblock kila mahali? Nilijua
ndio unaniacha moja kwa moja!” Jack akaendelea.
“Nimeingia
aibu Brina! Ubunge wenyewe nimekosa!” “Sasa aibu ya nini tena?” Sabrina
akamuuliza huku akiendelea na mapishi. “Huoni ni kama nimejidhalilisha tu?
Nahisi Mungu amenilaani. Wanasema laana ya mke inashika, Sabrina! Mungu
amenilaani na kunidhalilisha ndio maana nimekosa.” “Nisikilize Jack. Wewe
hujaalaniwa na yeyote kati yangu na Mungu. Na mimi sioni kama umejidhalilisha
hata kidogo.” “Kweli Sabrina, au unanitia tu moyo?” Sabrina akamgeukia vizuri
Jack.
“Lipi
bora, kujaribu na kushindwa au kutojaribu?” “Lakini si kwa jinsi kama hii!
Mpaka nikakuudhi!” “Mimi sikukasirika kwa wewe kugombea huo, Jack! Kwa kuwa
sipo kwenye mashindano na mama yako. Siku ile nilikuwa nimeumizwa na maneno
mabaya sana ya mama yako pamoja na Jena. Sijali kama utabadili mawazo. Nafanya
kila kitu kwa ajili yako nikitambua kile Mungu ameweka ndani yako. Ukisema leo
hutaki tena ubunge, mimi sina neno. Lakini isiwe sababu ya kukata tamaa. Hapo hapana.
Umejaribu huko, bado zipo nafasi nyingi tu. Inawezekana hiyo siyo njia Mungu
aliyokuandikia Jack.” “Kweli Brina?”
“Kabisa.
Wewe sio Mungu kwamba unajua kila kitu! Unajaribu huku ukimtumaini
Mungu. Ukikosa, unajaribu tena mpaka mlango wako aliokusudia Mungu ufunguke.
Kile alichokuandikia Mungu lazima kitatimia tu. Usikate tamaa.” Hapo akamtuliza
Jack. “Nashukuru Brina. Nilikuwa nakuonea aibu nikajua utakuwa ukinicheka!”
“Jack! Kwa nini? Hata kidogo! Kushindwa kwako wewe ndio mimi.
Haijalishi njia gani unatumia. Iwe mama yako, kaka yako, yeyote ile, ilimradi tu kufanya jambo sahihi.
Umefanya jambo sahihi lakini halikuwa lako. Basi, tushukuru katika hilo
na kusubiria jingine.”
“Mwenzio
nilijua umeniacha.” “Nilitaka kupumzika. Nikajua mambo yako na mama yako
nikiwepo, naweza nikakuchanganya, bora nikuache na mimi nitumie muda huo kupumzika. Nilikuwa naumwa sana, nikaona
nikiendelea vile, sitakuwa msaada kwa yeyote.” “Sasa hujakasirika
nilivyokuficha?” “Umenishangaza sana na kuniumiza. Ila nimeona na wewe ni
binadamu tu kama wanaume wengine waliozoea kuniumiza na kujirudi.” Hilo
likamuuma sana Jack.
“Usiseme
hivyo Brina!” “Kweli Jack. Ungekuwa ukiniheshimu kweli, na kunipenda
kwa dhati, ukijua mimi nipo na wewe ukurasa mmoja, nakuwazia mema wala
si mabaya, nipo Singida, mkoa ambao hata sikuwaza kuja kwenda, ila naishi kwa
ajili yako, kama ungethamini hilo, usingenificha. Ni ile hali ya
kunidharau kama wengine wote ukijua utarudi kwa wakati wako, utanikuta, utatoa
sababu nzuri iliyokusababisha ukafanya ulichokifanya, kwamba makosa hayakuwa
yako, mtu mwingine ndiye amekusababisha ufanye ulichofanya, kisha ukataka
yaishe kwa wakati wako wewe unapoona inafaa kujirudi kwangu, kisha na mimi
nielewe tu, nikubali yaishe tuendelee. Si ndivyo hivyo unavyotegemea au
nimekosea?” Kimya.
“Hapa
umerudi na sababu kuwa mama Msindai ndiye amekufanya ufanye mlichofanya.
Uliniacha na watoto nyumbani kwa Pendo kwa siku za kutosha tu, nikiwa mgonjwa
na mtoto mchanga, ukaendelea na mambo yako bila hata ujumbe kunijulia hali,
mpaka ukamaliza, ndipo uliponitafuta kama wengine wote waliopita kwenye maisha
yangu, ndivyo hivyohivyo ulivyonifanyia Jackson. Huna tofauti ila sema kwako
imenishangaza zaidi. Imekuwa mshituko mkubwa sana kwangu, kwa kuwa wewe nilijua
upo tofauti Jack! Hata Tino nilimwambia, wewe sio kama wengine. Ila umeishia
kuwa kama wengine tu.” Hapo Jack akaishiwa nguvu na kupoa kabisa. Sabrina
akaendelea kupika.
Tino
akapiga simu. Sabrina akapokea. “Nipo hapa nje.”
“Unataka nije kukusaidia?” “Hapana. Nataka kujua kama naruhusiwa kuingia?”
“Karibu Tino! Sasa hao kina dada si wamelala?” “Nitawabeba tu, ni kama
wanasinzia.” “Wamechoka. Walete walale.” Baada ya muda Tino akagonga na
mguu, Sabrina akakimbia kwenda kufungua mlango, akakuta amewabeba wote wawili.
“Waone! Ujanja wote umewaishia.” Waliposikia sauti ya mama yao, wakatoa vichwa
begani kwa Tino, na ndipo wakamuona Jack kwa nyuma. Wakaanza kumlilia wote
wawili.
“Hata
mimi nilikuwa na hamu na nyinyi. Njooni.” Jack akaenda kuwapokea wote wawili na
kuwabusu wakilia. “Msilie sasa. Mnausingizi?” Wakabaki wakimwangalia Jack na
machozi mpaka mashavuni. “Wamekula?” Jack akauliza akiwaangalia watoto.
“Wamekula kidogo. Watakuwa wameshiba, tuliwalisha uji mwingi asubuhi. Hata
nilipowaongezea...” Jack akaondoka wakati Tino hata hajamaliza! Sabrina
akamwangalia, akajua amekasirika.
“Acha
nikachukue mizigo yao kwenye gari.” “Mimi nipo huku jikoni, napika.” Tino
akatoka na kurudi na mizigo ya watoto, akaiacha sebuleni na kumfuata Sabrina
jikoni, Jack akiwa chumbani na watoto. Wakasikia mlango mkubwa ukifunguliwa.
“Sabrina?” “Shikamoo baba. Nipo jikoni. Mbona mapema?” “Naona Sabina
amewaongelesha hao vinyozi mpaka wakalainika, nimenyolewa kwa haraka,
nimemaliza, nikaona nirudi tu. Mama yako na Sabina nimewaacha hukohuko,
wamesema wakimaliza wanakwenda madukani.” “Basi kaa niivishe sasa hivi, ule.”
“Wala usiharakishe kwa ajili yangu, labda wengine. Mimi bado nimeshiba.” “Sawa
baba yangu.” Sabrina akarudi jikoni alipokuwa amemuacha Tino.
Ukweli, Mchungu.
“Naweza kujaribu kuja jioni nione kama naweza
kupata nafasi ya kuwaaga?” “Sijui kama Jack atatoka nao au la! Na kwa sasa hivi
alivyo sidhani kama ni wazo zuri kumuuliza. Ila umekuwa nao siku nyingi Tino!”
“Daah! Najuta Brina! Najuta sana. Napatwa uzito wakuondoka, na kazi zinanisubiri.
Hapa nilikuwa nikifanya kazi usiku ili mchana niwe nao hawa. Na bado naona
haijatosha! Unafikiri nikija kurudi tena wakati mwingine nitapata nafasi kama
hii?” “Siwezi kukuahidi. Sitaki kukupa tumaini ambalo linaweza lisiwepo.” Tino
akatulia kidogo.
“Lakini
Sabrina, kila siku namshukuru Mungu nilikosea nikiwa na wewe.” Sabrina
akanyamaza. “Kwa hakika namshukuru Mungu. Ingekuwa mtu mwingine angefuata
ushauri wangu, hiyo furaha tunayoipata sasa hivi tusingekuwa nayo. Asante
sana na samahani. Ila ujue najutia.” “Lakini labda mimi nikuulize
Tino, unajutia nini? Upande upi haswa?!” “Kila kitu Sabrina.”
“Kwa kuwa leo tunazungumza, hebu fafanua kidogo. Kuwa tu muwazi. Maana
umezungumza kwa kurudiarudia kuwa unajuta. Ni nini unajutia?”
Sabrina akamuuliza bila jazba.
“Maamuzi
niliyoyafanya nilipokuwa na wewe Sabrina. Huwa nakaa peke yangu, au nakuwa
nimelala, nikikumbuka yote yaliyoendelea Moshi, huwa nashituka kama narushwa
gorofani jinsi moyo wangu unavyovurugika! Nikikwambia hali niliyonayo nilikwenda
mpaka kwa wataalamu wanisaidie, ujue sidanganyi. Lakini mwishowe imenibidi tu
kurudi japo mliniwekea restrain order, lakini nilijiambia nilazima nije
kukiri kosa.” “Naomba tukae kidogo Tino. Tafadhali, ili tuzungumze, maana
nahisi unachanganya habari ambayo haipo. Njoo hapa kwenye meza, sehemu yakulia
chakula.” Sabrina akazima kabisa jiko na kuhamia mezani, baba yake akiwa sehemu
ya sebuleni.
“Twende
taratibu tu. Maana hatugombani. Leo tumepata huu wasaa, tuwekane sawa. Pengine
kuna kitu wewe unachanganya hujaelewa au ni mimi.” Tino akatulia. “Uliponiacha
hospitalini Moshi, ulisema unakuja hapa Dar, kwenye maswala yako ya kupigania
mali zako, kisha kwenda kutibiwa nchini Italy. Hutaki ijulikane kama nina mimba
yako au hata kama tulikuwa na mahusiano mengine yeyote yale bali kukufanyia
kazi kama Lela alivyonipa ajira ya kukuuguza tu, ili asije akashinda kesi. Na
ukasema waziwazi kabisa, huna muda wakulea. Unataka ukatibiwe mkono,
ambao ndio chanzo chako cha pesa. Maswala ya watoto au mtoto kwa wakati
ule tukijua ni mmoja, ulisema hutaki. Si mara moja, ni kwa kurudiarudia
ulisema hiyo kauli, tena ikaanza kwa ukali kabisa ukinifoka kwa nini sitaki
kutoa mimba! Ukanichukia kabisa, hutaki tuzungumzie chochote hata kukujulia
hali isipokuwa kutoa mimba.”
“Haya.
Ukawa hutaki hata kukaa sehemu niliyopo au nikufuate popote kwa hasira kwamba
ni kwa nini nang’ang’ania mimba ambayo wewe hutaki! Tukaendelea
ukiwa kimya kwangu, mwingi wa hasira na kunikwepa. Ukifungua mdomo au
ukiniona swali likawa nimefikia wapi juu ya kwenda kutoa mimba.
Haya, ukabadilika jinsi ya utakaji wa kutolewa mimba. Ukaja kwa kunibembeleza
sasa, ukinisihi nitoe mimba, ili tuachane ukiwa umeridhika, hujaacha
kitu kwangu. Kwa kurudia rudia hayo maneno ukinieleza hutaki kuniacha na
mimba itakayojulikana wewe ndiye uliyenipa. Si ndivyo ilivyokuwa au
umesahau?” Tino akawa mwekundu kabisa, kimya.
“Kuthibitisha
ulichopanga na kuniambia ni kweli ulikusudia, uliniacha hospitalini ukiwa umejiridhisha
nimeshatoa mimba na umetengeneza ushahidi kuwa mimi nilikuwa mfanyakazi wako
tu. Ukanisainisha karatasi yakuwa nilikuwa nikikufanyia kazi na si vinginevyo,
na kuwa nilipokea malipo yangu kwa hundi kabisa ili kubakiwa na ushahidi kuwa
nilipokea ile pesa au benki ionyeshe
hundi yako ilitoka kwenye akaunti yako kuingia kwangu kama niliyekuwa nikikufanyia
kazi tu! Sijui kama unakumbuka hayo yote Tino?” Kimya.
“Kuendelea
kuthibitisha unamaanisha, hukunitafuta tena. Sikubadili namba ya simu kwa zaidi
ya miezi miwili nafikiri mpaka akaja kunichukua Jack pale Moshi, tena nakumbuka
njiani ndipo nilitoa ile namba. Lakini kwa kipindi chote hicho hukuwahi hata
kuuliza ninaendeleaje?! Hata kwa
ujumbe tu, hukukosea.” “Lela alikuwa akikutafuta sana ili umsaidie kumtetea.
Akawa anawinda simu yangu na akapata watu wa mtandaoni wanaofuatilia simu
zangu.” “Tino! Kweli hiyo ndio sababu yakushindwa kumjulia hali mtu kama mimi
kweli! Vipo vibanda vya simu vingapi hapa jijini, au watu wangapi hapa Dar
ambao ungeweza hata kuazima tu simu ukanijulia hali? Na kama kukumbusha tu
Tino, uliweza kudai gari yako ukiwa uliniacha hospitalini. Tukawasiliana kuwa
yule uliyemtuma kuja kuchukua gari amefika, na nikakutaarifu kuwa
nimeshamkabidhi gari yako. Katika mazungumzo hayo Tino, ulishindwa vipi hata tu
kuulizia hali yangu? Si kama mpenzi, ila tu ubinadamu! Au umesahau haya
ninayokwambia?” Sabrina akauliza taratibu tu.
“Tafadhali
nijibu Tino, usijekuwa unajutia kitu kisicho.” “Nilikuwa kwenye hali mbaya
Sabrina. Unakumbuka hata ile hali ilinipata siku ile tuliagana wewe unakwenda
saluni mimi polisi? Nikashindwa kabisa kufikiria? Nahisi akili yangu haikuwa
sawa Sabrina. Hata maamuzi yangu mengi niliyafanya wakati ule hayakuwa sahihi
nikishindikizwa na Max tu au yeye akiniongoza vile atakavyo. Na ndio maana hata
nilipofika Italy ikabidi kupelekwa kwa daktari wa mambo ya saikolojia
kutibiwa.”
“Mmmh!
Kwa hiyo hata mazungumzo mengi tuliyozungumza mimi na wewe wakati tupo pale
hotelini hayakuwa yakitoka kwako kama Tino huyu ambaye akili yako sasa hivi
unasema imetibiwa, ila yalitoka kwa Tino ambaye akili ilikuwa imechanganyikiwa?
Kwamba yote na vyote tulivyofanya pamoja, nilikuwa nipo na Tino ambaye hakuwa
na akili timamu, ndivyo hivyo?” Sabrina akahoji.
Tino
kimya. “Sasa hebu jiulize Tino, kama ulipatwa na tatizo la akili, uliwezaje
kumshinda Lela aliyekuwa amejiandaa vile, huko mahakamani mpaka ukapata mali
zako zote na kuachana naye bila hata kulipwa fidia yeyote ile na wakati alikuwa
mkeo wa zaidi ya miaka miwili?” “Max ndiye aliyekuwa akiendesha mambo yote.”
Sabrina akamwangalia huku amekunja uso. “Kweli Sabrina.” “Mimi sijui unapenda
kujiaminisha nini ili kujipa amani kwenye maamuzi yako uliyoyafanya na
unayoendelea kuyafanya, ila huwa watu wanasema, na nafikiri ndivyo na wewe unavyoishi
kuwa, maishani huwezi kupata kila kitu Tino.”
“Ulipiga
mahesabu yako vizuri sana. Tena kwa kunitamkia waziwazi kuwa hutakuwa na muda
na mimi wala watoto.” “Sabrina!” “Unakataa nini Tino?! Hukuniacha Moshi wewe
ukisema hutakuwa na muda na..?” “Nilikwambia ni kwa sababu nataka nikatibiwe,
na ningerudi kukutafuta.” Sabrina akacheka kwa kuumia sana. “Kweli Sabrina.
Nakumbuka kukwambia hivyo.” “Sasa akili yako haikuwa ikifanya kazi katika lipi
na lipi ilikuwa ikifanya kazi? Mbona umekusudia kugawa yale matukio kwa mafungu
ili tu kujipa amani?” Kidogo hasira zikaanza kumpanda Sabrina.
“Ulifanya
mambo yako kwa umakini sana Tino. Jack anakuja kunichukua pale Moshi, wewe
ulikuwepo nchini, na kesi ulikuwa umeshashinda na imefungwa! Uliishi Dar, mimi umenitelekeza
Moshi, na haukuwa mume wa Lela! Wewe sema umepatwa tamaa baada yakuona hawa
watoto.” “Sio tamaa.” “Nitamaa tu Tino. Unataka upate vyotevyote kwa
gharama hata waliyolipa watu wengine, kitu ambacho sidhani kama ni sawa.
Hawa watoto wamezaliwa wakisubiriwa na Jack kwenye chumba cha
kujifungulia. Wafika hapa duniani, amewashika yeye kwanza hata kabla yangu!”
“Gharama
aliyowalipia Jackson hao watoto niliozaa wakizungu, wewe ulishindwa Tino.
Jackson amepoteza mahusiano muhimu sana na mama yake, sababu ya hao
watoto. Wapo hivyo walivyo kwa kukuzwa na mshahara wa uhasibu, tena
wa serikalini, halafu wilayani Singida, sio Dar, ni Singida.
Mshahara huo anaolipwa Jack ndio umewafikisha hao watoto hivyo! Watoto
wawili, Tino! Jackson anawalisha na kuwavalisha kwa kamshahara kadogo
anakolipwa. Hao watoto unawaona hivyo walivyo wakivutia ni kwa kulelewa na Jack.
Jackson anaajira ya jumatatu mpaka ijumaa. Saa moja na nusu anatakiwa ameshatoka
nyumbani. Na jioni akirudi nyumbani kutoka kwenye kazi ya uhasibu ni kazi ya
watoto mpaka kuwaogesha na kulea mpaka anawaweka kitandani kipindi nipo
mjamzito! Jack analea hao watoto kwa jasho lake. Kwa hali na mali bila msaada
wa yeyote yule ila kabiashara tulikokaanza tena kachanga hata hakajafika umri
wao hao watoto. Wanaishi kwa jasho la Jackson.”
“Wakati
wewe unasoma na kutafuta leseni za kimataifa huko nje ya nchi, huyu Jackson
alikuwa akibana kapesa kake, ili mimi na hawa watoto tuishi vizuri. Alichagua
kufanya kile ambacho wewe ulikataa kufanya Tino! Tena kwa kunitamkia zaidi ya
mara moja, ukimaanisha kabisa. Kuwa, HUNA MUDA WA FAMILIA KWA WAKATI HUO ILA
MALI NA KUJITIBU. Uliniacha bila hata kujua naendeleaje, ila Jackson
alinichukua akaanza kulea mimba yao hawa, nikijua ni mmoja tu. Nilichanganyikiwa nakulia, nilipojua ni mapacha, nikijua
sina uwezo, na Jack ni kijana tu. Lakini huyu Jack akaniambia nimbembee tu,
yeye atalea, nisiwe na wasiwasi hatashindwa kulea hawa watoto.” Sabrina
akajifuta machozi.
“Mama yake Jackson anadhani namloga mtoto wake, kwa
mapenzi aliyonayo kwa hawa watoto! Si kawaida! Anawajali, kuliko nafsi yake
mpaka mama yake anaumia. Na mimi naelewa. Jackson sio milionea. Hana biashara
ya maana, hata tuliyoanza bado haitulipi kihivyo ila mwajiriwa tu, tena wa
serikali. Mimi sina kazi namtegemea huyohuyo Jack! Hata mimi mtu angemfanyia
hivyo huyu Brayan wangu, ningeumia.” Sabrina akajiweka sawa.
“Sijui
kama unanielewa Tino? Mama yake anatafuta njia yakurudisha akili ya Jackson,
ili aweze kufikiria kama hivyo wewe, Tino! Haamini kama Jack ni mzima
kwa anayoyafanya kwa hawa watoto. Na hajifanyi wala kujitahidi, ni wake.
Tokea wapo tumboni, Jack alikuwa akiwaambia anawasubiria kwa hamu, ila
hatukujua kama watazaliwa wakizungu! Ndugu zake walimkimbia hospitalini huyu
Jack baada yakuzaliwa hawa watoto wakizungu, Tino! Nikisema kikimbiwa
namaanisha kukimbia kabisa, tena kwa maneno mabaya sana yakumkatisha tamaa.
Lakini Jack alibaki na sisi pale hospitalini mpaka tuliporuhusiwa. Akatuchukua
tena sisi wote watatu na kuturudisha nyumbani kwake ambako anatangaza ni kwetu
wote.”
“Tumenunua
nyumba hapa Dar, anashughulikia hati ya nyumba iwekwe jina langu kwa ajili ha
hawa watoto! Jack anasema kuna leo na kesho. Hataki akija kuondoka hapa duniani
hawa watoto wakapata shida, au hata baadaye wakija kukua, wapate sehemu ya
kurudia. Nyumbani kwao!”
“Hapo
walipo anajua wanalazwaje kitandani ili wasiumie usiku au wasihangaike.
Akikohoa hata mmoja wapo hapo, Jack anajua kikohozi cha kila mmoja wao hao kwa
majina kitu ambacho hata mimi mama yao mzazi sijui! Kwanza sijawahi ona
umuhimu. Akikohoa hata mmoja wao hao usiku chumbani kwao au hata mchana wakiwa
sehemu, Jack atakwambia ni nani anakohoa, na atamwita. Akija ni kweli ni yeye ndiye
aliyekuwa akikohoa huko walipokuwa. Anaamka katikati ya usiku, tukiwa
wote tumelala, kwenda kuwaangalia jinsi walivyolala. Kila siku usiku
lazima awaangalie wakiwa wamelala, nakuwafunika au kuwaweka sawa. Mimi mwenyewe
siwezi!”
“Ninachotaka kukwambia Tino, huna haja
yakujutia. Ni maamuzi. Na kila maamuzi yanazo gharama zake. Jack analipa
gharama mpaka hivi sasa tunavyozungumza, analipa gharama yakunipokea mimi na
hao watoto. Hao watoto wamemtoa Jackson kwenye familia iliyokuwa ikimpenda
sana. Mama anayemjali kupita nitakavyokwambia. Jack ni wale watu wanaozungumza
na mama zao hata mara tatu kwa siku. Nimemkuta Jackson hajui hata bei za nguo
za ndani. Mama yake anamnunulia na kumtumia popote alipo. Lakini yote hayo
ameyapoteza kwa kuwachagua hao watoto. Na kumuona leo hapa, inamaana
bado amewachagua tena wao, wala sio familia yake!”
“Tafadhali usiseme unajuta
Tino, kwa kuwa ulichagua ulichonacho. Mungu amekupa, tena amekupa kwa
uaminifu mkubwa sana. Una afya njema, ajira nzuri kwenye kampuni ya kimataifa,
unauza picha zako kwenye soko la kimataifa! Vilevile kama ulivyoniambia huna
nafasi kwa wakati ule sababu ya kutaka ulichopata! Tafadhali usikufuru!
Mimi na wewe tunamlaumu Max, lakini wote tunajua Max anahusika kwa asilimia
ndogo sana, kama washauri wengine wowote wale ambao tunaamua kutofuata ushauri
wao. Ila tupo hapa, mimi na wewe, kwa maamuzi yetu au chaguzi zetu tulizofanya
tukiwa pamoja. Wewe ulichagua ulichochagua, na mimi nikachagua nilichochagua.
Mungu ameweka mkono wake kwenye kila chaguzi zetu, akatupa na watu wakusimama
na sisi, sasa kwa nini tena kurudi nyuma na kuchanganya watu?”
“Hiyo sio nia yangu Sabrina.” “Tafadhali
naomba niambie nia yako, Tino. Tafadhli sana. Nia ni nini?
Ni kusafisha dhamira yako au?” “Kusaidia.” “Unamsaidia nani?” Sabrina akauliza.
“Watoto wawili sio kazi ndogo, Sabrina! Acha nisaidie?” “Kwa nini umchague Keiline
Jackson Msindai na Jeiline Jackson Msindai na sio vituo vya watoto yatima vilivyojaa
kote ulimwenguni?” Hapo Sabrina akauliza swali lakini kufikisha ujumbe. “Eti
Tino? Kwa nini uchague kusaidia watoto wa familia yetu?” Kimya, macho mekundu haswa.
“Najua hili usingependa kulisikia
Tino, lakini watoto ulioacha kwangu, TULIUA Moshi na ushahidi
wote wa tulichofanya pale kwenye ile hospitali inayoua watoto upo na
Jackson. Anao.” “Naomba usiseme hivyo Sabrina.” “Sina jinsi nyingine rahisi ya
kukwambia Tino, ukaelewa, na kuendelea na sisi kuanzia hapa, usipokuwa na
uelewa huo. Ukielewa hivyo, nahisi
mbeleni mnaweza mkakutana na Jack, angalau mkaelewana.
Lakini si kwa uelewa mwingine wowote ule.” “Nipeni hata masharti.”
“Nilikwambia, leo Jack hayupo vizuri. Jibu lolote atakalokujibu leo,
hutalipenda. Tafadhali mwache. Shukuru muda uliopata nao, basi kwa sasa itoshe
tu.” “Haiwezi kuwa basi Sabrina! Tafadhali nisaidie.” “Sawa Tino. Ila kumbuka
na hili, nimekuonya. Jack amepoteza mambo na vitu vingi sana sababu ya
hao watoto.” “Mimi sitaki ugomvi ila naomba.”
“Kama mimi nimemuelewa Sabrina. Labda
niingilie na kukusaidia Tino.” Wote wakamgeukia baba yake Sabrina aliyekuwa
amekaa kimya sebuleni akisikiliza muda wote. “Kwamba kwa sasa, itoshe
tu. Acha mpaka wakati mwingine tena. Na yapo madhara ya kulazimishia
mambo kwa wakati usiofaa. Nashauri utulie.” “Naondoka kesho mzee wangu.
Sijui nampataje Sabrina!” “Na kwa sababu yeyote ile, hata kwa kukosea Tino, usiwasiliane
na mke wangu.” Jack akatoka chumbani na hilo onyo.
“Sikutishi,
ila nakuonya ili usije kulaumu baadaye. Hiki nilichokikuta hapa kwa mke
na watoto wangu, ni mara ya kwanza na HAITAKAA ikatokea tena. Kumtafuta
Sabrina kwa kutumia yeyote yule kwenye familia yao, mkawasiliana
nyinyi wawili au kupitia mtu yeyote kwenye familia yao kwa sababu yeyote
ile, huko nikunitangazia vita mbaya sana. Na sitakubali kushindwa.”
Sabrina kimya, ameinama akijua na yeye anafikishiwa ujumbe wake.
“Sabrina ni mke wangu wa ndoa ya
kanisani na nililipa mahari kabisa kwamba hakuna mwanaume mwingine
atasogelea nyumbani kwao tena juu ya Sabrina, mimi nilifunga hiyo biashara tena
kwa heshima zote na ushahidi upo wa kukabidhiwa Sabrina kihalali na
wazazi wake au ukoo wao wote waliridhia mimi Jackson Msindai, kumchukua Sabrina
mpaka kifo.” Na baba yake Sabrina akafikishiwa ujumbe wake. Kimya yeye na
binti yake waliompokea Tino kinyume cha Jackson Msindai.
“Ulimuacha
vibaya sana Sabrina, nilimkuta mpweke na amejawa hofu pamoja na majuto.
Tumejenga familia yetu kitu ambacho hukutaka. Acha kuchanganya
watu!” Jackson akasogea karibu.
“Nilikwambia
Tino, na ninarudia. Litakapofika swala la familia yangu, nitanguruma,
hakuna mwenye sikio akaweza kunisikiliza. Nampenda mke wangu, napenda watoto
wangu. Nywele zao na hiyo rangi waliyobeba, isikuchanganye hata kidogo.
Hawa mabinti wawili ni kina Msindai kama Brayan. Na kukusaidia
tu, SIJASHINDWA kutunza familia yangu, kwa hiyo tunza pesa yako.” “Sitaki
kukuudhi Jack. Nakushukuru kwa kila kitu.”
“Unanishukuru kwa lipi NILILOKUTENDEA?!” Jack akawa mkali haswa
mpaka sauti ilisikika ni ya ukali.
“Sikujui, hunijui. SINA chako. Sijakusaidia chochote kile. Mimi naendesha familia yangu! Nilimuonya Max asimsogelee mke wangu, hakunisikiliza. Unajua kilichompata Max?” Sabrina kimya. “Naomba tusifikishane huko Jack. Na samahani kama nimekuudhi. Naona kweli niondoke. Samahanini sana.” “One Man’s Trash, is another Man’s Treasure. Uliona ni takataka yakutupa, ukatupa. Mimi nikachukua akiwa yupo peke yake, Moshi. Peke yake hakuna hata anayemjulia hali Sabrina! Nilimkuta mpweke kama yatima jangwani! Sasa hivi unaona vinang’aa, vinapendeza, ndio unarudi kinyumenyume kuleta vurugu? Ulikuwa wapi siku zote hizo? Unamdanganya Sabrina unaumia? Kwa lipi!?” “Naomba niondoke jamani. Samahanini sana.” “Na usiwahi kusahau, macho yaliyokuwa yakimtizama Max, mpaka kumtia nguvuni, sasahivi yamehamishwa kwako wewe, Tino. Usinijaribu tena. Hii iwe mara yako ya mwisho.” "Najua na ndio maana unaona nimefuata kila sharti la Sabrina. Nimekuwa nikirudisha watoto kwa wakati aliotaka yeye Sabrina." Tino akajaribu kujitetea asijue anazidi kumuudhi Jack.
"Tino nakuonya wewe! Hakika NAKUONYA. Na leo hata Sabrina atakua shahidi wa hili. Hata kwa kushawishiwa na Sabrina mwenyewe, huruhusiwi kugusa binti zangu kwa kuwa wewe ni muuwaji na ushahidi ninao. Nikianzana na wewe kisheria, adhabu utakayohukumiwa wewe, kwa huruma sana ni kifungo cha maisha kama si kunyongwa. Tafadhali waambie ukweli hao wanao kusogeza karibu na binti zangu. Waambie ulikusudia kuwauwa, ila Mungu akawalinda. Uliwafikisha mpaka kwenye kifo, na ukaridhika kuwa wamekufa. Nakuonya, na onya wanaokusaidia kukusogeza kwa binti zangu." Tino akaondoka kwa haraka. Jack akarudi chumbani,
Sabrina jikoni. Baba yake Sabrina na yeye akapokea ujumbe wake na familia yake wote. Jack aliwasema kwa
heshima na mafumbo lakini alielewa na Jack akajua atafikishia wengine ujumbe. Maana ni kweli walimtelekeza Sabrina. Jackson anamfuata
Sabrina, Moshi, hakuwa hata na mawasiliano na ndugu zake hata mmoja! Leo wanakusanyika
hapo chini ya Tino! Jack alikasirika sana. Pakazuka ukimya mkubwa haswa
hapo ndani, hata tv haikuwashwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment