Hakuacha
kumtumia ujumbe Sabrina kila siku asubuhi kumjulia hali yake na watoto. Na kila
siku ikawa kazi ya kuangalia hizo jumbe kama zimefika. Juma la pili lilipoisha
akaongeza ujumbe wa usiku. Kumtakia usiku mwema yeye na watoto. Nia ni kupata
kitu cha kuangalia kwenye simu yake, na sababu ya kujua kama Sabrina amefungua
simu yake. Akaendelea kusubiria mchana na usiku bila kuona kama jumbe zake
zimefika.
Zilipita
siku 21 bila mawasiliano kati yake, Sabrina, mama yake wala ndugu zake. Kukawa
kimya kabisa, ila baba yake hakuacha kumpigia kumjulia hali. Angalau mara moja
kwa juma na hawakuwa watu wa mazungumzo marefu, ila salamu tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
moja usiku akiwa ametoka kuoga, akasikia ujumbe umeingia. Akakimbilia simu
akiwa na taulo tu. ‘Sisi tunaendelea vizuri, namshukuru
Mungu. Naulizia kama Singida kuna mtu. Naona nguo za kaka nilizokuwa nazo
zimeanza kuwa ndogo. Sasa kabla ya kufanya manunuzi mapya, nilitaka kujua kama
naweza kupata nguo zake na za dada zake. Ikishindikana, hamna shida. Nitafanya
manunuzi mengine.’ Jack alisoma na kukaa kitandani. Zilishapita siku 25
tokea amuone Sabrina. Nyumba ilijaa vitu vya familia, lakini alikuwa peke yake.
Akampigia
lakini hakupokea ila akamtumia ujumbe. ‘Kaka na dada
zake wamelala. Siwezi kuongea. Tafadhali nijulishe kwa ujumbe tu.’ Jack
akasoma na kupiga tena na tena lakini haikupokelewa. ‘Naomba
pokea simu, Brina.’ ‘Sio lazima Jack. Nitanunua upya. Usiku mwema.’ ‘Tafadhali
toka hata nje tuzungumze.’ Jack akaona amemtumia tena ujumbe wa pili. ‘Kaka na dada zake wamelala. Siwezi
kuongea. Tafadhali nijulishe kwa ujumbe tu.’ ‘Nilisoma huo ujumbe,
Brina. Naomba tuzungumze.’ Hakupata ujumbe mwingine ikawa kimya. Akapiga
tena, simu haikuwa hewani.
Jack
akasubiria kuona kama atapigiwa tena, ikawa kimya. Kesho yake asubuhi akatumia
akili akamtumia ujumbe. ‘Ulitaka kupataje hivyo vitu?
Mimi nipo Singida ila ijumaa nitakuwa Dar. Unataka kuvipata kabla au unaweza
kusubiri nikaja navyo Dar? Na kama kuna vitu vingine ungehitaji, niandikie,
niviweke pamoja.’ Huo ujumbe
haukuonyesha kufika mpaka usiku akapata majibu. ‘Nashukuru.
Ni vya watoto tu. Wanakuwa kwa haraka vikikaa muda mrefu vinaweza visiwafae
tena.’ ‘Nivilete wapi?’ Jack akauliza kwa haraka. ‘Kwa Pendo tafadhali. Nitavifuata kwake.’ ‘Nimwambie lini
utavifuata?’ ‘Nitazungumza naye. Sina uhakika. Pengine ijumaa au jumamosi.’
‘Sawa. nisalimie wanangu.’ Kimya na ujumbe haukufika. Akajua ameshazima
simu, ila furaha aliyokuwa nayo, akajiambia hataondoka nyumbani kwa Pendo mpaka
amuone Sabrina.
Atafutaye, Hachoki.
|
J |
ack
aliondoka asubuhi siku ya ijumaa kuelekea Dar, na basi tu akiwa na mabegi
kadhaa yaliyojaa nguo za watoto wake. Akatua jijini Willy akaenda kumpokea
kituo cha mabasi, jioni hiyo. Walijua atakuwepo nyumbani kwao. “Vipi maisha ya
ubachela?” “Naomba usinidhihaki Willy.” Willy akaanza kucheka. “Mbona hasira
Jack na haupo hapo kwa bahati mbaya ila maamuzi tu!?” Jack hakumjibu hilo ila
kuuliza jingine. “Sabrina amefika leo pale kwa Pendo?” “Mimi nimetokea kazini
ndio nimekupitia hapa kituo cha mabasi. Kwa hiyo sijui.” “Kwani hujazungumza na
Pendo?” “Mpaka muda mfupi niliotoka kuzungumza na Pendo, na yeye hajamuona wala
kumsikia Sabrina kama mimi tu, tokea siku ile ya harusi akimwambia anakwenda
kupumzika kwa muda, anamuombea, na atamtafuta mapumziko yakiisha. Basi.” Jack
akanyamaza.
Walifika
nyumbani kwa Pendo wakamkuta amejilaza chumbani kwake. Willy akamsaidia Jack
kuingiza mizigo yake mpaka kwenye chumba alichokuwa akilala Sabrina na wanae. Wakati wapo humo ndani ya hicho chumba
wakamsikia Pendo akicheka mlangoni. “Hiki chumba nacho kinakaribia kuitwa mtakuja.”
Jack akamgeukia vizuri. “Umezungumza na Sabrina?” Jack akauliza. “Sabrina
alilala chumba hikihiki karibia siku 5 wewe ukiwa kwenu hata kumtumia ujumbe
wakumjulia hali ukaona shida, sasa hivi unataka kusumbua tu watu. Chakula kipo
mezani. Nenda kale. Twende zetu Willy.” “Na mimi nilikuwa nimemkasirikia
Sabrina kwa kujua amenigeuka bila kujua ukweli.” Akajitetea Jack.
“Wewe
mwanaume gani, au baba gani unanuna kama toto dogo na kuzira mpaka watoto! Hiyo
ni akili kweli au ujinga huo?” Pendo akamuuliza. “Mama yako anammalizia hasira
Sabrina kwa watu kumsusia shower, kwa kushindwa kwake mwenyewe! Halafu
anamsingizia Sabrina kumbe hata mgeni rasmi aliyetaka awepo siku ya shughuli
alighairi, halafu eti anasingizia babyshower haikufanyika sababu ya Sabrina!”
“Sijaelewa Pendo.” “Ndio utajijua mwenyewe wewe usiyetaka kutumia akili ila
hisia.” Pendo akaondoka, Jack akamkimbilia.
“Nini
wewe?” “Umezungumza na Sabrina lini?” “Leo. Na kesho mida ya saa nne anakuja
hapa kuchukua mizigo yake. Tulia.” “Nampenda Sabrina.” “Basi vitendo vyako
vinazungumza tofauti.” Pendo akamjibu na kugeuka. “Kwa hiyo wewe unapenda mimi
nikiachana na Sabrina?” Pendo akamgeukia na kumwangalia kwa sekunde kadhaa,
akaondoka zake akijisukuma na tumbo lake bila ya kumjibu
Mtakuja...
Siku Inayofuata.
|
K |
wenye
majira ya saa tatu na nusu wala si saa nne Sabrina akawa anaingia hapo getini kwa
Pendo. Sifa akafurahi kumuona. “Umependeza dada! Hizo nywele umesuka si itakua
garama sana?” “Na muda mrefu haswa. Kwa hiyo kama umezipenda ujiandae kukaa
chini.” “Mmmh! Itakua mihela mingi. Akuu!” Sabrina akamcheka Sifa jinsi
alivyojilalamisha. “Nimemsikia dada akizungumza chumbani, atakua ameshaamka,
ngoja nimuite.” “Sasa na wewe unamwagilia maua jua lishatoka!?” Sifa akachekaa.
“Leo nimepitiwa na usingizi. Nikupokee mtoto?” “Mwache tu, alichomwa sindano
jana, naona hajisikii vizuri. Acha tuendelee kupendana tu.” Sifa akaingia ndani
na kibegi cha mtoto na pochi aliyompokea Sabrina, akaenda kumgongea Pendo,
akatoka kwa haraka.
“Mama
huko ulikojificha naona kumekupenda! Umependeza Sabrina!” “Asante dada.
Ninapumzika vizuri, halafu huyu kaka mpole, kwa hiyo uzazi mzuri. Nakula
vizuri, napumzika vyakutosha. Naona na wewe unazidi kuongezeka!” Wakacheka
wawili hao kwa furaha. “Ndoa tamu.” Wakaendelea kucheka. “Kabla sijakaa,
niambie mizigo yangu kama ililetwa? Maana nguo za huyu kaka sikuwa nazo nyingi,
na hata nilizoziacha Singida nahisi ni kubwa, maana bibi yake aliniambia
nisinunue nguo, yeye atanunua. Nikaanza kununua za miezi minne kwenda juu tena
kwa hamu tu. Sasa siku ile nilipowaacha kwenye tafrija yako, nikasema nisifanye
haraka, nikakosa mengi. Nikamtumia ujumbe mama Msindai kumuuliza kama hiyo shower
bado ipo, kimya.” “Haiwezekani Sabrina?!” Pendo akashangaa sana.
“Kwamba
huamini kama nilimtumia ujumbe? Tena nilipoona kimya nikampigia kabisa ila
hakupokea.” “Sabrina wewe!? Na maneno yote yale machafu aliyokutupia na
kukuzulia bado ulimtafuta?” “Mimi ndiye mbaya wake lakini si mjukuu wake dada.
Lakini nilipoona hajanipokea simu yangu wala kujibu ujumbe tena, nikaona nitulie
tu. Nikajua na yeye amesusa mtoto kama mwanae. Nimenunua nguo baadhi, lakini
naona nahitaji zaidi. Ndio nimeomba zile za Singida ziletwe nichambue.
Nikikosa, nimnunulie nyingine.” “Mmmh! Sabrina wewe una moyo wa ajabu! Mimi
nisingeweza.” “Nafanyaje dada, si mtoto wangu peke yangu. Lakini kama hivi
wamemsusa, basi. Nalea mwenyewe na Mungu wangu hajaniacha wala kunipungukia.”
“Nakuona ulivyopendeza.” Wakacheka kwa kushangilia.
“Mama,
umependeza haswa! Naona na mwili safari hii umekubali.” Wakacheka zaidi. “Nashukuru dada yangu lakini
kwa uzazi wa wale mapacha nao ilikuwa hivihivi. Mwili ulikuja, wakati
nashangilia kunenepa, ukanywea wote. Hapa nahesabu tu siku.” “Wakati ule
ulikuwa mzazi na hekaheka za huko Singida. Safari hii huna la kukuzungusha,
mwili na wenyewe utabaki tu.” “Na kweli dada. Nahisi safari hii Mungu ameamua
kunipumzisha kitajiri haswa!” Wakacheka tena na kugonga kwa ushindi. Willy
akatoka chumbani. “Mzima Sabrina?” “Mimi mzima Willy, namshukuru Mungu. Vipi honeymoon
imeisha?” “Haiishi.” Willy akajibu na kumfanya Sabrina na Pendo kucheka zaidi.
“Warembo
wako wapi?” “Wapo na Tino. Leo ameomba ashinde nao, maana kesho anaondoka. Ndio
na bibi yao amepata nafasi ya kwenda saluni, na mimi wamenishusha hapa, ndio
maana nimewahi mapema, nimeomba lifti wanilete hapa. Naamini sijawaamsha au
kusumbua.” “Hata kidogo. Karibu.” “Subiri kwanza Sabrina. Tino, Tino?” “Huyohuyo dada, mwingine nani? Kajirudi
na msamaha mpaka kwa wazazi ameomba msamaha, nikajiambia kwanza mimi mwenyewe
mkosaji namba moja na wakati wote Mungu amekua akinisamehe. Amekua akinifutia
midhambi yangu na kunirehemu. Nawezaje kubakia na Tino moyoni nikimchukia na
kweli wanae ninao! Nikamwambia Mungu yeye ndio ashugulike naye, mimi nimtue tu,
nimalize kinyongo naye kwanza hata jinsi ya kupata hao watoto wote tulikuwa
tukimkosea Mungu, lakini amenirehemu. Wale watoto hawajawahi hata kuugua
wakanywa dawa! Wazima. Sasa huyo si Mungu tu.” “Kweli mwaya.” Pendo akaafiki.
“Halafu
dada, watoto wenyewe wanakataliwa huko kwengine, na kufukuzwa waziwazi,
hawatakiwi! Nawezaje kuwang’ang’ania mimi mwenyewe, nitaweza wapi dada? Kuna
leo na kesho. Siku chache zilizopita hapa ilionekana waziwazi, nikaachwa hapa,
kila mtu akashuhudia. Sasa nijidai kichwa ngumu, nimeachwa peke yangu,
nafanyaje?” “Lakini kweli mwaya.” Pendo akaendelea kuafiki.
“Najua
leo mnapumzika, wala sitaki kumpunja Willy kwa kuchukua muda wenu. Mimi
nitarudi jumatatu dada, wakati Willy yupo kazini, tuzungumze vizuri. Nipe
mizigo yangu niondoke.” “Jack yupo.” Sabrina akanyamaza. “Alikuja jana usiku.”
Kimya, na Willy kimya. “Sabrina?” “Hata sijui dada!” Kisha akamgeukia Willy. “Samahani
Willy, naomba mwambie Jack nimekuja kuchukua mizigo kama alifanikiwa kuja nayo,
mimi niondoke, mtoto akapumzike.” “Mzima lakini?” “Mzima. Ila jana tulimpeleka
kupata sindano ya chango, naona ndiyo ilimpa homa kidogo, ndio maana unaona tumekumbatiana
hivi.” Wakamchungulia, alikuwa amelala kifuani kwa mama yake amebebwa, kwa
kufungwa mbeleko maalumu ya kubebea, ila amemuweka kwa mbele. “Mwanangu huyu si
mlizi. Akilia ujue kuna jambo. Usiku hakulala vizuri, na vilio vya hapa na
pale, na ameamka akilia kidogo ndio maana unaona tupo kwenye kupendana hapa.”
“Sasa
hivi anayo homa?” Akatoka Jack na hilo swali, Sabrina akajua alikuwa
akisikiliza. “Nampa dawa kila baada ya masaa 8 ili kufanya isipande tena.”
Akajibu Sabrina macho kwa mwanae wala si Jack ambaye hakuwa amemuona kwa muda
mrefu. “Amekua!” Pendo akasifia huku akimchungulia pale alipofungwa kifuani na
mama yake. “Hana utani na chakula huyu. Ni mlaji mzuri sana na mlalaji, ndio
maana bibi yake anasema anakuwa na mwili.” Jack akasogea mpaka pale alipokaa
Pendo na Sabrina aliyekuwa amempakata huyo mtoto lakini bado amemfunga na mbeleko
hapo kifuani kwake.
“Kweli
amekua.” Jack akataka kumchukua.
“Nashauri ungemuacha kwa sasa. Analialia na si kawaida
yake. Hajatulia vizuri. Hapo amepitiwa na usingizi muda si mrefu ndio maana
unaona nasita hata kumtoa hapo kifuani.” “Nina hamu naye, acha nikupokee tu, akilia
nitambembeleza.” Sabrina akafungua ile mbeleko, akamkabidhi. “Basi wakati wewe
umemshika, acha mimi nikangalie nguo zake. Kubwa nitaziacha hapahapa kwa dada,
nitakuja kuchukua wakati mwingine.” Sabrina akaelekea kwenye chumba alichojua
Jack ndipo alipopewa hifadhi.
Jack
akamfuata nyuma. “Swala la Ubunge binafsi sikujua kama kulikuwa na hila nyuma
yake, Brina.” Akaanza Jack akimfuata Sabrina nyuma, wala hakugeuka. “Mama
alinishauri kwa hekima kwamba nisikwambie ili nisikuvunje moyo kwa juhudi
unazoweka kule Singida. Niingie kwenye kinyang’anyiro tu. Nikishinda ndipo nikwambie
ili tuwe na chaguzi mbili.” “Begi lipi ndilo lenye nguo za watoto?” Sabrina
akamuuliza. “Jeusi.” Akajibu Jack na kuendelea.
“Yaani
mimi siku ile pale hospitalini sikujua kama yalishasemwa maneno mabaya, na mama
hataki watoto wafike nyumbani kwake, ndio maana na mimi nikakasirika kuona
unanibadilikia kwa hasira kiasi kile na hutaki kunisikiliza, wakati mimi najua
mama aliweka mipango mikubwa kwenye shower yake huyu, bila kujua kumbe
na wageni wenyewe walishatoa udhuru. Kwamba hata shower yenyewe isingefanyika
hata kama ungekuwepo au pengine ingekuwa ni watu tu wa familia, asiniambie
hivyo. Akabaki kusema wewe ndio umesababisha isifanyike.” Sabrina kimya.
Akiendelea na alichokuwa kifanya.
“Unanisikiliza
Sabrina?” “Ulichukua nguo zote za Brayan, sehemu zote nilizokuelekeza?” Sabrina
akamuuliza na yeye. “Kwani tunahamia huku Dar?” Sabrina akasimama na
kumwangalia vizuri. “Nilikuelekeza sehemu zote nilizoweka nguo za mtoto, Jackson.
Ulichukua?” “Ukiniita hivyo jina langu lote najua umenikasirikia. Unakuwa kama
unanisomea hukumu. Najua.” “Umechukua nguo zote au umeacha?” “Nimeacha nyingine
nikijua tunarudi.” “Sasa zile ulizoziacha ndio za muhimu zaidi, maana hizi
ulizoleta ni za umri mkubwa. Sizihitaji.” “Kwani tunarudi lini nyumbani kwetu?”
Jack akauliza.
“Sijui
wewe, lakini mimi, nikizungumzia mimi nawakilisha...” “Watu watatu. Najua.”
“Hapana. Watu wanne.” Sabrina akamrekebisha. “Tupo mapumzikoni.” Sabrina
akamalizia. “Mapumziko yetu yanaisha lini?” Jack akauliza swali
akijiongeza na yeye. “Yetu sisi ni kwa mwezi mzima, yakiisha hayo ndipo
nitajua chakufanya. Sijui wewe!” “Kwa maana nyingine umebakiza siku kama 6 tu
umalize hayo mapumziko. Na mimi nakusubiria hapahapa Dar, yakiisha hayo
mapumziko ndipo tujue chakufanya pamoja. Kama tunabaki wote hapa Dar, au
tunarudi Singida.” Akamuona anarudisha nguo kwenye begi alilokuja nalo mpaka
akamaliza.
“Haya
namuomba mtoto, sisi tuondoke, nikamnunulie nguo.” “Tunaondoka wote Sabrina.
Tukapumzike wote mpaka huo mwezi ukiisha ndipo tujipange tena upya
lakini nilitaka unisikilize.” “Nikwambie ukweli Jack, sina shida yakujua
mipango yako na mama yako. Hainihusu hata kidogo. Sijui kama
unanielewa?” “Nilitaka kukwambia kilichotokea!” “Sihitaji Jackson.
Tafadhali mimi naomba mtoto niondoke. Acha kunipotezea muda na kutaka kunichanganya.
Nina vichwa vitatu vinanitegemea mimi, kila siku wanayopewa na Mungu. Mimi
nikiyumba tu, na kumuongeza na mama yako kwenye mipango yangu, tutajikuta wote
tunakwama tukisubiria amri kutoka kwa mama yako. Mimi sina huo muda. Mpo
watoto wanne kwa mama yenu, nafikiri mnatosha kumsikiliza na kufuata hekima
zake. Naomba na mimi usiniingize huko tafadhali. Sitaki na sitafanya hivyo. Au
niseme sitakuruhusu. Namuomba mtoto.”
“Basi
tuendelee na mipango yetu. Mimi na wewe na familia yetu.” “Jackson Msindai,
acha kunipotezea muda na kuniyumbisha tafadhali. Kama unataka kubakia na mtoto,
sawa. Nakuachia ila ujue bado ananyonya na sijatembea na maziwa yake. Sasa je,
nikuachie mtoto au unanipa mimi niondoke hapa? Siku ya leo ni ya Pendo na
mumewe, wenzetu bado wapo honeymoon. Naomba usiniharibie ratiba yangu. Nishamwambia
dada Pendo leo nakuja kuchukua tu mizigo, sitakaa.” “Basi nisubiri tuondoke
wote.”
“Unakwenda
wapi!?” “Huko kwenye mapumziko.” “Hapana, huwezi. Kwa sababu kama ileile
iliyokushinda kuwepo hapa kipindi natoka hospitalini.” “Pale nilikuwa...” “Naishi
kwenye villa ya vyumba viwili tu. Chumba kimoja natumia mimi na watoto wangu
wote, na kingine nilimuomba baba aje akae na mama, ili mama atulie, anisaidie
kulea watoto. Sina nafasi ya kukuweka.” “Nitalala kwenye makochi.” “Hapana
Jackson. Hapa nako kulikuwa na makochi lakini ulishindwa kulala. Acha kuwa myumbaji.”
“Basi naenda kukodi Villa ya vyumba vitatu, wote tuhamie hapohapo.” “Sina
sababu yakuhama mimi. Sitahama.” “Basi twende wote, nikakodi Villa yangu
ya peke yangu, ila karibu na nyinyi. Au hutaki Tino akatuona tupo pamoja?
Ulimwambia nimekuacha ili mrudiane?” Sabrina akamwangalia na kuchoka kabisa.
“Maana
naona unanikwepa, na maisha yako sasahivi ni Tino tu. Sasa mimi sijasema nataka
nikaishi na wewe pamoja na huyo Tino. Nachukua Villa ya pembeni yenu ambapo
sipafahamu. Ninachokuomba ni unifikishe mpaka hapo mnapoishi na mimi nikakodi
Villa yangu. Nalo hilo pia hutaki?” “Basi naomba ufanye haraka, tuondoke.”
“Sawa. Umekula lakini?” “Ndiyo.” “Basi nisubiri nikusanye vitu, tuondoke.”
Akamkabidhi Sabrina mtoto pale alipokuwa amekaa, akaanza kukusanya vitu vyake.
“Mimi
nipo tayari, sijui tunaondokaje hapa?” “Mimi, nilimuomba Tino asiwe
mbali na hapa ili nikichukua vitu, anisaidie kunirudisha.” “HATUTAONDOKA
na Tino hapa.” Jack akaongea kwa sauti ya juu kwa hasira. “Sawa.” Sabrina
akabaki akimwangalia. Akaonekana akifikiria kidogo, kisha akatoka. “Willy!” Akamsikia
akiita. Willy akaitika. “Naomba nisaidie tena usafiri.” “Wewe ni msumbufu Jack.
Mimi naomba Sabrina uchukue gari yangu, atumie akiwa hapa mjini na watoto. Nitazungumza
naye mwenyewe juu ya kurudisha.” Pendo akajibu kabla ya Willy. “Asante Pendo.”
“Sitaki Jack. Na sijakupa wewe gari, ni Sabrina.” Jack akarudi chumbani
alipokuwa amemuacha Sabrina na mtoto.
“Tumepata
usafiri.” “Sawa.” Jack akaanza kubeba mabegi yote. “Mimi naomba mizigo
uliyonijia nayo hapa Dar niiache hapa kwa dada Pendo. Sina nafasi yakujaza
mizigo nisiyotumia.” “Nitaiweka kwenye Villa nitakayokodi mimi, au umesahau siku
hizi tuna mahela yakuishi kwenye Villa mbili hapa mjini? Bado nyumba tuliyonunua
ya hapa Dar inatusubiri na Singida pia?” Akamuuliza kwa kejeli akiwa
amekasirika. “Sawa Jack. Wewe beba mizigo unayotaka.” “Nabeba yote.” Sabrina
akatoka na kurudi sebuleni alipokuwa amekaa Pendo na Willy.
“Dada,
acha sisi twende, nikajaribu kumlaza huyu kaka, nitakuja jumatatu.” “Basi
nitakusindikiza na madukani, usiende peke yako.” Wakaanza kucheka. “Mimi
mwenyewe nilikuwa na hamu na wewe dada yangu. Nitakuja kukufuata basi
jumatatu.” “Hayo ndio maneno.” Sabrina akatoka, Pendo akimsindikiza. Jack
akarudi ndani kumuaga Willy, kisha akatoka kumfuata Pendo na Sabrina ambao
walishafika garini. “Kapumzike dada. Tutaongea zaidi jumatatu Mungu akipenda.”
“Sawa.” Pendo akarudi ndani.
“Tunaelekea
wapi?” Sabrina akamuelekeza. “Unanitania au kweli!?” “Ndipo ninapoishi.
Nilitaka kupumzika.” Jack akamwangalia na kuendelea kuendesha mpaka kwenye hizo
Villa. “Kweli wewe unayo pesa! Au ndio mambo ya Tino haya?” “Naomba unisikilize
Jack. Nimetaka mapumziko ya mwezi tu katika maisha yangu. Mbali na kelele
pamoja na masimango. Nimebakiza siku chache sana, unafikiri unaweza kusubiri au
mimi na watoto tuondoke tena?” “Hata maswali ya kawaida...” “Naomba uyatunze
utakuja kunihoji wakati mwingine isiwe sasa.” Jack akatulia.
“Na
kukusaidia tu, ofisi za wanapokodisha hizi Villa, tumeziacha kule getini,
upande wa kushoto. Naomba unishushe mimi na mtoto karibu na mlango,
nikambembeleze nione kama atalala, wakati wewe ukishughulikia Villa yako.”
“Mimi sidhani kama nitapamudu hapa. Na hivi nitakaa hapa bila likizo ya kazini,
naweza nikajikuta nafukuzwa kazi. Kwa hiyo twende tu hapo kwenu, nitalala hata
jikoni.” Sabrina hakumjibu. Alitegemea yote hayo. Akamuelekeza mpaka kwenye
kinyumba wanachoishi.
“Ndio
mnalipia kiasi gani hapa?” “Wewe ni msumbufu bwana Jack! Ni kwa nini huwezi
kuwa msikivu?” “Hata swali kama hilo nilakutunza!?” “Nenda ofisini ukaulize.”
Jack akanyamaza. Wakafika, Sabrina akashuka na mtoto hata pochi hakuchukua.
“Karibu.” “Sasa mbona ukaribisho wenyewe ni kama hujafurahia?” “Nazungumza kwa
sauti ya chini sababu ya mtoto Jack! Acha kulalamika kama mtoto mdogo bwana!
Karibu.” “Sasa mizigo yangu ndio niweke wapi?” “Popote unapotaka wewe.” “Chumba
chetu na watoto ni kipi? Nisije nikaweka chumbani kwa wakwe.” “Jikoni ni
pale ndani.” Jack akaanza kucheka.
“Kweli
sitakiwi humu ndani!” “Si ulisema mwenyewe!” “Ni kiuungwana tu! Hapo ulitakiwa
wewe uniambie, ‘hapana mume wangu, tutajibana tu na watoto’! Mapenzi yote yale
yamekwenda wapi Brina wangu?” “Naomba punguza kelele, Jack. Huyu mtoto hajalala
vizuri usiku.” “Sawa. Kwa hiyo akilala ndio tutapata muda wetu?” Sabrina
hakumjibu akapitiliza chumbani.
Akaingiza mizigo yote hapo chumbani,
Sabrina kimya akibembeleza mtoto. “Nimekumiss Sabrina.” “Acha kelele Jack,
bwana!” “Mbona sasa hata mtoto mwenyewe unayembembeleza ameshalala! Pata muda
na mimi Sabrina! Hujui hata nilikuwa naendeleaje! Nilikuwa na hali gani! Kwa
nini mimi hunijali tena?” “Najuta kukutafuta Jackson Msindai jamani! Heri
ningemaliza likizo yangu ndio nikakutafuta jamani!” “Nijali hata kidogo tu!”
“Unaendeleaje Jackson?” “Usiniite hivyo. Niite vile vizuri kwa upendo.” “Basi
nenda kasubiri hapo sebuleni, mimi nimlaze mtoto.” “Kwa hiyo unakuja tupate
muda wetu kama familia?” “Naomba toka Jack.” “Ukichelewa mimi narudi. Maana
nahisi nimeshasahauliwa. Sijaliwi tena!” Akakaa.
“Kweli karibu mwezi mzima hujui nilipo
wala nakula nini, Brina jamani! Maisha yangu yamekuwa mabaya. Naishi peke yangu
kwa kosa dogo tu. Mimi nilikasirika nikaenda kulala kwa mama, lakini nilikuja
kukuangalia. Ila nikasafiri. Mimi hunipendi Brina. Sio kama mimi
ninavyokupenda. Siwezi kuishi bila wewe, hata nikiwa nimekasirika, nataka niwe
na wewe tu. Hata ukinitendea jambo baya la namna gani, mimi nakutaka tu wewe.
Mimi sio kama wewe Brina. Siwezi kuku block kwa kuwa nataka kukusikia tu
wewe. Mimi nakupenda wewe kuliko mtu mwingine yeyote hapa duniani. Lakini wewe
hunipendi Brina.” Sabrina akabaki akimtizama tu, na mtoto mkononi.
“Unaweza
kulala bila kujua kama mimi ni mzima au la! Nimekula au la! Maisha...” “Naomba
ukanisubiri hapo sebuleni, ili umalizie malalamiko yako Jack. Acha nimlaze
mtoto kukiwa kimya ili asiamke wakati namuweka chini.” “Na mimi nataka
kujaliwa. Unanipuuza Brina.” “Haya nenda, nakuja kukusikiliza.” Akatoka na
kurudi. “Hivi hata ulishakuwa na wasiwasi kujua mimi naendeleaje au niko wapi?” “Nilikuacha mikononi
salama kwa mama yako, Jack. Naomba tulia kule kwenye makochi.” Hapo
akapoa kidogo akatoka, lakini akamsikia akiendelea kulalamika kwa sauti ya
chini kama mtoto mdogo. Sabrina alimjua Jack, akajua ameongeza mtoto mwingine
hapo kwenye Villa.
“Maisha
yangu yamebadilika kabisa, nimekuwa kama sijao sababu ya kosa la kutaka
maendeleo!” Sabrina akatoka na kufunga mlango wa chumbani. “Mimi ningefanikiwa,
ungefurahi Sabrina.” “Nani alikwambia sikuwa na furaha?” “Namaanisha zaidi.”
Sabrina akamwangalia na kurudisha macho kwenye simu. Akapiga. “Sasa mbona mimi
hunisikilizi tena!?” “Nampigia simu Tino, kumruhusu aende atakako, asibakie
maeneo yale akidhani bado nahitaji...” Wakati akimjibu Jack huku kwenye simu
Tino akapokea.
“Halow!”
Akamsikia Tino. “Mimi nilishatoka maeneo ya
huko, Tino. Wewe kuwa huru kwenda utakako. Nilipata usafiri.” “Sijui kwa nini! Jeiline
amelala kabisa! Mpaka naona shida kumwamsha.” “Jana alikaa ndani ya maji muda
mrefu sana. Atakuwa amechoka. Nashauri uwarudishe tu.” “Nikiwarudisha sasa
hivi, utanipa tena jioni tukaangalie movie?” “Baba yao yupo hapa, Tino. Sijui
atasemaje tena!” Tino akanyamaza na kushindwa chakujibu. Lakini Jack
akafurahi sana.
“Mimi nashauri uwarudishe kwa sasa, halafu tujipange tena.” “Hata
hivyo nakushukuru sana, Sabrina. Asante. Nahisi sababu ya furaha ya kuwa nao, nilikosa
kuwa na kiasi kwao, nikawashindisha majini kwa muda mrefu.” “Na wenyewe
wanapenda maji, ila wamelemewa.” “Basi tunarudi.” “Sawa.”
Sabrina akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Nani Anabakia Baba Kwa Hao Mapacha Wasiotakiwa Na
Mama Msindai? Itakuaje Kwa Tino, Sabrina Na Jack Aliyerudi? Wanakutana kwenye
Villa anayolipia Tino.
Inaendelea..
0 Comments:
Post a Comment