Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 53. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 53.

Jack hakujisumbua hata kumtaarifu mama yake akijua atayapata tu matokeo. Akarudi hotelini. Ile hali ya uchovu ikachanganyikana na mshituko. Akawa amechoka ila hana njaa wala usingizi. Akaanza kufuatilia swala la usafiri wakumrudisha Singida kesho yake.

Jumanne.

Aliondoka mji mkuu wa Tanzania akiwa ameshindwa. Alichohangaikia mpaka kuvunja mahusiano mazuri aliyokuwa nayo na kaka yake, Jacinta dada yake pamoja na Sabrina, watu wake wa karibu sana, hajapata! Hakuwa amewasiliana na hao watu wala na wao hawakumtafuta kama waliojionya kama walivyoonywa na mama yao. Kama isingekuwa hivyo, wangeshampigia na kumpa maneno yakumtia moyo. Jack alikuwa amepoa lakini na tumaini la familia. Akajua hata kama Sabrina atakuwa amemkasirikia, basi angalau hiyo likizo aliyokuwa amechukua kumsaidia kulea mtoto, basi atalea watoto kwa juhudi zake zote, mpaka kumfurahisha Sabrina, asijue Tino ndiye ameshika usukani.

Walikuwa na mipango mzuri, lakini kosa dogo tu, likabadilisha kila kitu na kujikuta akimrudishia Tino asiyestahili, damu yake. Jambo zuri na la maana, likakosa baraka za Mungu, mke, hata jamii yake ya karibu kwa sababu ya ushindani wa mama yake.

Alifika Singida moja kwa moja mpaka nyumbani kwake na kushangaa hakuna mtu. Akazunguka kila chumba kukaonyesha wazi ni kama alivyopaacha mara ya mwisho alipoondoka baada ya kumruhusu na msichana wao wa kazi aondoke na yeye kwa likizo mpaka watakapokuja kurudi hapo nyumbani ndipo na yeye wangempigia arudi. Msichana wa kazi aliondoka na kumuacha Jack peke yake hapo ndani kwa siku chache akijiandaa kwenda kuungana na familia yake huko Dar ndipo ikatokea kujifungua Sabrina kwa gafla, Jack akaondoka hapo bila kuweka sawa. Kwa hiyo akakuta nyumba vilevile kama alivyoacha. Akaanza kazi ya kupiga simu ya Sabrina bila mafanikio. Jioni mlinzi alipokuja hapo kwa ajili ya kulinda, alimwambia Sabrina hakufika hapo na watoto. Hakuna aliyeingia hapo. Jack akaanza kuingiwa hofu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

H

uku kwa Tino na Sabrina pamoja na watoto, aliwaacha wakakaa hapo hotelini kwa muda wa siku 6 ndipo wakahamia kwenye Villa nzuri sana. Hapo napo wakapapenda. Ilikuwa sehemu ya vyumba viwili, ndipo Sabrina akamuomba baba yake na yeye aende wakapumzike. Maisha hapo yakaendelea kwa utulivu tu, Sabrina na watoto wake, na Tino akisaidia kwa hali na mali.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Huku kwa Jack juma lilipoisha akaamua kurudi jijini kumsaka mkewe na watoto akijua kwa hakika Pendo atakuwa akijua walipo. Jack alitua jijini moja kwa moja nyumbani kwa Pendo. “Usinisumbue Jack. Umeshindwa na mipango yako na mama yako, ndipo unamkumbuka Sabrina sasa hivi! Alitoka hospitalini akakaa hapa hata kuhumtafuta, sasa hivi ndio unajidai kumtafuta?” “Naomba niambie alipo.” “Sijui, na hata ningejua, nisingekwambia.” Jack akaondoka hapo nyumbani kwa Pendo njiani akawatumia ndugu zake wote ujumbe akiomba wakutane kwa wazazi wao jioni.

Akaelekea mpaka ofisini kwa Sabina mida hiyo ya karibu kutoka kazini siku ya ijumaa. “Sabrina na watoto wako wapi?” “Ni swali gani hilo Jack, au umechanganyikiwa wewe!?” Sabina akaweka mshangao mkubwa. “Unaniuliza swala la mkeo, kwani mimi ndiye niliyemuoa?!” “Sabrina hayupo nyumbani.” “Yuko wapi?! Na umewaambia wazazi?” Hapo Jack akaingiwa hofu kidogo. “Wewe Jack? Tokea lini?” Sabina akazidi kumkaba. Jack kimya. “Kwani mlikuwa na matatizo? Kwa maana mimi nilihisi tatizo tokea alipojifungua. Eti mtu kajifungua kwa upasuaji, eti ukamuacha na watoto wote akiishi kwa Pendo, nikaambiwa wewe huishi pale unaishia kwenu! Mama akajiuliza na kushangaa sana. Akasema hata kama wewe ni mnyama wa kiasi gani, basi ungeamua kumuacha angalau akiwa amepona! Unamuacha mzazi na kidonda kibichi!” “Nilikuwa sijamuacha. Kulitokea kutoelewana tu.” “Ndio hasira mpaka ukamtelekeza mke na watoto! Yaani baba yako aliweza kufika kuangalia mtoto, wewe mwenye mtoto umekasirika unajificha kwenu! Sasa hasira zimeisha au unataka kumpa talaka yake?” Sabina akaendelea kumkaba.

“Hapana! Nani amesema nataka kumuacha Sabrina!?” “Wewe mwenyewe kwa vitendo vyako. Au umegairi kwa kuwa umekosa ubunge?” Jack akaona aondoke. “Sasa wazazi wapo kwa mdogo wangu yule wakiume, wameenda kumtembelea. Wapigie simu, uwataarifu kutoonekana kwa Sabrina na wajukuu zao.” Jack akatulia kidogo na kugeuka tena akiondoka. “Mbio za sakafuni, zimeishia ukingoni. Ulifikiri utashinda kwa kuwa wewe ni Msindai, ukamtelekeza Sabrina, umeshindwa ndio unaanza kumtafuta tena! Muulize Pendo uliyemuachia familia yako.” Jack alikuwa amesimama na kumgeukia tena Sabina  wakati alipoanza kuzungumza tena kwa kumkejeli, akabaki amesimama tu, Sabina akarudi zake ofisini, akamuacha hapo nje.

Kwa Kina Msindai.

I

lipofika majira ya saa mbili na nusu ndipo Jack akaingia nyumbani kwao na kukuta ndugu zake wakimsubiria. Akasalimia na kukaa. “Samahanini kwa kuchelewa.” Akaanza Jack. Kimya. “Nakumbuka mwanzo niliposema namuoa Sabrina, mama alipinga kabisa akiwa ametoa sababu zake. Nikalazimishia mpaka nikamuoa Sabrina. Alipojifungua wale watoto, napo ikaleta shida sana, nafikiri wote tunakumbuka. Mama akakata mawasiliano na mimi mpaka Sabrina aliposhika mimba ya Brayan na maswala yale aliyoyafanya Sabrina kule Singida yalipoiva, Brina akashauri nimpigie mama simu, ili asipitwe kwenye vitu muhimu sana vinavyotokea kwenye maisha yangu.” Kila mtu kimya akisikiliza.

“Sikutegemea kwa ule ushauri. Nikamuuliza Brina kama anao uhakika, akasema yeye anajua mama ananipenda sana, na amehangaika sana na mimi mpaka kufika pale. Hadhani kama ni sawa mama akapitwa na mambo yangu ya muhimu. Tofauti zake na mama, akaniambia hazinihusu mimi. Hataki kumnyima Brayan mapenzi ya bibi yake au kuvunja mahusiano yangu na mama, kwa makosa aliyofanya yeye nyuma. Kufupisha habari, nilimtafuta mama, yeye mwenyewe mama akaomba kufika nyumbani kwetu akiwa na zawadi za Jeiline na Keiline. Nikajua amefika mahali, amewapokea.”

“Ukaanza mchakato wa babyshower ya Brayan. Kuhofia kilichotokea kwa mapacha kisitokee tena, mimi nikakataa kabisa. Sabrina akanilazimisha na kurudia tena usemi wake uleule, maisha na maamuzi mabaya aliyofanya yeye, yasimnyime Brayan baraka kutoka kwa bibi yake. Nikamwambia mbona kama kuna upendeleo! Akasema watoto wote ni wake, haimsumbui kama mmoja akipendelewa. Sisi wazazi tutafute jinsi ya kubalansi huo upendo, lakini tusimnyime Brayan alichoandikiwa na Mungu. Tukakubaliana kila kitu na mama alichotaka ila bila kujua kwamba ukaribisho huo hapa nyumbani si kwa wale mapacha!” “Unaaza ufitini Jackson. Mimi ndivyo nilivyokwambia au unaleta maneno ya mtaani hapa nyumbani kwangu?” “Naomba nimalizie mama.” “Sitaki ufitini mimi.” “Sawa.” Jackson akaendelea.

“Ukaja mchakato wa Ubunge wa Afrika Mashariki. Ukaanza kama unakuwa siri. Nikauliza ni kwa nini hata kaka asiambiwe, yeye ndio mshauri wangu. Sasa baada ya kukaa baada ya haya yote kutokea ndipo nagundua kulikuwa na hila nyingi tu ndani yake tokea mwanzo. Hata majibu niliyojibiwa wakati ule nashindwa kuyaeleza hapa. Ndipo nikalazimishia kusema nilazima nimuulize kaka, anishauri. Nikaonywa nisiende kwa undani ili kuepusha kuja kuonekana kuna upendeleo.” “Na mkeo?” Akauliza Jacinta. “Si amesema asiingiliwe huyu Jack? Sasa maswali ya nini?” “Swali hili ni la Jack, Jena. Acha kunijibiza.” “Wote tumeitwa hapa. Nani amekuweka wewe ndio muuliza maswali?” Jena akamuuliza dada yake.

“Kwa Sabrina niliambiwa nisimchanganye. Sio mbaya kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja. Nikimwambia kabla ni kama kumvunja moyo kwenye juhudi tunazoweka Singida. Nifanye kimyakimya, nikishafanikiwa ndipo nimwambie. Ila kwa hakika sikujua kama zile simu za kuulizwa mchana na usiku kama nimemwambia Sabrina, zinahusiana na ushirikina. Kwamba anahisiwa kuwa ataniloga nisifanikiwe.” Junior na Jacinta wakacheka kwa kusikitika. Mzee Msindai kimya, ametulia kabisa.

“Mnachocheka kwa dharau ni nini?” Mama yao akauliza, hawakujibu, wakanyamaza kabisa. “Kufupisha habari nzima, binafsi nilishangaa sana hili jambo lilivyokuja kugeuzwa kuanzia hata na Jena huyu hapa mbele ya Sabrina! Ikawa tena kama kuna ushindani!” “Acha kuniingiza kwenye mambo yako Jackson. Mkeo mwenyewe yamemshinda, analia wivu.” “Sawasawa. Tukubaliane kabisa kuwa Sabrina ni mchawi, mbaya sana kwangu, ana watoto wa kizungu ambao ni aibu kubwa sana kwa hii familia. Hata hivyo ameondoka na watoto wake.” Wakashangaa sana.

“Ndiyo. Sabrina ameondoka.” “Ameona umeshindwa Ubunge, ndio amekukimbia.” “Hivi wewe Jena kichwa chako kimejaa wadudu au unafikiria kweli?” “Ningekuwa daktari? Nafikiria, na mimi naongeaga ukweli, si mnafiki mimi. Ameona mwenzie ameshindwa ndio ameondoka.” “Labda mimi nisaidie kwenye kuongeza ubaya wa Sabrina hapo kwa Jena kwa kusahihisha. Tokea alipoondoka siku ile ya harusi ile ya kina Pendo, hata kabla sijakwenda Dodoma kwenye kinyang’anyiro hicho cha ubunge, sijawaona tena.” “Hakwenda Singida kama alivyosema?!” Kaka yake akauliza kwa mshangao. “Hapana kaka. Hakuna aliyemuona Sabrina na wanangu kule Singida tokea walipokuja huku kwa ajili ya harusi ya kina Pendo, babyshower ya Brayan na kujifungua. Lakini hilo sio tatizo. Nimewaomba mfike hapa ili muwe shahidi.” Wote wakatulia.

“Nimefanya mengi mno aliyokuwa amenishauri mama. Nafikiri tokea mtoto, jibu analojua mama kutoka kwangu ni ‘ndiyo’. Na nimekuwa mwaminifu sana hata katika hili la Ubunge japokuwa nilikuwa nimevurugukiwa haswa, nikajiambia nitii tu. Nifanye kile anachonishauri.” “Kwani na wewe mwenyewe hukutaka? Acha kunigeuka kama vile nilikulazimisha! Kama ni kokosa huo Ubunge safari hii ni wengi tu wamekosa, halafu nafasi nyingine zipo tu zinakuja. Utapata.” “Sawa mama.” “Halafu sio kila kitu alichokushauri mama umefanya wewe Jack. Alikwambia nini juu ya huyo Sabrina na ukang’ang’ania?” Jena akaongeza bila aibu.

“Hivi wewe Jena huwa unafikiria lakini kabla hujazungumza kweli?!” “Subiri kwanza kaka. Ni kweli kabisa Jena. Sasa ndio nimerudi hapa kwa mama na wewe Jena. Nimekuwa peke yangu kwa zaidi ya siku 10. Tokea Jena ulipomwambia Sabrina kuwa amepitwa, nyinyi wote mnajua swala la ubunge kasoro yeye, mpaka leo sina familia. Nipo Singida peke yangu. Sina hata wakuzungumza naye. Sasa ndio nimerudi kuomba mawasiliano ya yule mwanamke mnayeona atanifaa, niombe tena nioe.” Hapo pakawa kimya. Jack akatoa simu.

“Sabrina ameondoka na wale watoto wake wakizungu na hata huyu wangu. Sasa sasahivi nipo huru kuoa kabisa. Tena hata sheria ipo upande wangu kwa kuwa Sabrina yeye ndiye aliyeondoka. Sijamfukuza. Sasa katika wale wanawake ambao mlikuwa mkinishauri, yupi ambaye sasa hivi mama, unadhani atakufaa awe mkwe wako?” “Unanivunjia heshima Jackson!?” “Hata kidogo mama yangu. Ninachotaka ni hiki kilichotokea kwa Sabrina kisitutokee tena. Safari hii nioe chaguo lako, ili wote tupumzike. Sasa hivi nipo tayari kwa yeyote utakayemchagua wewe, nitajie tu, nianze kutongoza upya, nioe.” “Utajijua mwenyewe!” “Nilijijua mwenyewe, ukaingilia mama, mpaka sasa hivi nimekimbiwa. Nilikuwa nikiheshimika nina familia nzuri. Kule Singida kila mtu alikuwa akinipongeza kwa heshima Sabrina aliyokuwa ameniwekea kwenye jamii. Sasa kama nilipata heshima kwa mwanamke mbaya ambaye hafai vile, bila shaka kwa huyo utakayenichagulia wewe, itakuwa zaidi.”

“Mimi sijakwambia umuache mkeo.” “Hata kidogo mama yangu. Ameondoka yeye mwenyewe kwa kuwa yamemshinda. Viwango vyetu vitukufu vimemshinda yeye aliyezaa watoto wa kizungu, akaloge kwingine. Ndio naomba sasa ushauri wa mwingine hata bikra, mimi nitaoa.” “Naona umeanza kunitukana.” Akasimama mama yake. “Naomba usubiri mama. Kwa maana nyingine. Kuondoka kwako hapa leo, mbele ya familia, ni kwamba unasema swala langu na mwanamke nitakayeoa tena, halikuhusu?” “Linanihusu vipi mimi!?” “Tafadhali naomba fikiria majibu yako na uyakumbuke siku utakapokuja kunikuta na mwanamke wangu. Narudia tena mama, naomba nipe mwanamke ambaye wewe unajua ni mcha Mungu, asiye na mimba, atakayenipenda na kunihudumia kwa uvumilivu kuliko Sabrina.” “Kwani na wewe mwanamke ni mmoja tu? Siku zote tulivyokuwa tukikushauri juu ya Phina hapa!? Mama alikushauri mara ngapi hapa ukaishia kwa....” “Subiri Jena.” Jack akamkatiza na kuchukua tena simu yake.

Jack kwa Mke, Chaguo la Mama Yake.

W

akamuona anapiga simu na kuweka kwenye spika. Wote kimya. “Upo mzima Phina?” “Mzima Jack. Mama watoto na kichanga wanasemaje?” Akauliza Phina vizuri tu akisikika ametulia na yupo kwenye mzingira tulivu. “Tumeachana ndio maana nimekupigia.” “Aisee pole. Ndio maana ile shower ilifutwa! Maana nilisikia tu watu siku za mwishomwisho wakisema hawatakuja, nikasikia mpaka mama Mkapa naye amegairi, ndio nikauliza kwa nini tena na tumealikwa na mama Msindai mwenyewe! Sikupata majibu yakueleweka, kumbe ndoa ilishindikana! Pole Jackson. Inatokea.” Wote hawakuwa wakijua hata kama watu wengi wakubwa aliotaka mama Msindai wahudhurie kwenye hiyo tafrija, walitoa udhuru wakutohudhuria. Kumbe tena walimkatalia siku za mwishoni, akabakia kumlaumu Sabrina tu.

“Huyo naye atakuwa mbeya.” Kwa haraka Jack akabonyeza Mute ili Phina asimsikie mama yake. “Wala hakuna aliyeghairi kuja! Ni vile Sabrina alivyokataa ndipo nikaifuta. Lakini wageni wote nilioalika walikuwa tayari kuja. Mbeya tu.” “Tena! Mkwe mwenyewe anayependwa tena na yeye mbeya!?” Jacinta akauliza na kuanza kucheka. “Upo Jack?” Wakamsikia Phina akiita kwenye simu. Jack akamtoa kwenye mute. “Nipo. Samahani nilikuweka kwenye mute. Sasa kwa kuwa tumekuwa tukifahamiana kwa muda mrefu, na umezoeleka hapa kwenye familia, naomba tuoane.” Wakamsikia Phina akicheka.

“Sikutanii Phina. Kweli. Ukikubali, mwezi ujao tunafunga ndoa.” “Acha masihara Jack! Yaani wewe siku zote hizo, ushakuwa mpaka na watoto ndio unataka unipe mimi wegazi! Ulikuwa wapi miaka yote hiyo! Akuu! Na uache utani wa usiku usiku bwana! Pole kwa matatizo, lakini mimi sina mpango wakuingia kwenye ndoa za namna hiyo. Sina shida kihivyo! Yaani ushindwe ndoa ya mwanamke mliyepambana vile siku ya harusi, mkae mpaka mzae, mje mshindwane ndipo uje kwangu! Acha masihara wewe! Mimi mwenyewe nataka mume wangu, tuje tulee watoto wetu, sio wegazi! Naamini utaelewa tu Jackson. Sitaki kuwa chaguo la pili kwa yeyote yule. Na umama wa kambo sio wito wangu.” Jack alikuwa ametulia kabisa akisikiliza, na kuweka speaker kila mtu asikie.

“Hata hivyo na yeye ni mtu mzima sana. Hee!” Mama Msindai akaongeza, wakasikia simu imekatwa. “Naomba ushauri wa mwingine ambaye si mtu mzima, mama.” “Wewe tulia utapata mwanamke mzuri tu. Acha haraka.” “Wala si haraka mama. Sirudi kuwa mdogo na kama ulivyosikia ni kama soko langu linaanza kuisha sokoni sababu si kijana tena.” “Sasa na wewe huyo Phina ni mwanamke wa kutulia na kuoa huyo?” Jacinta akacheka sana.

“Na huyo naye pia hamfai Jack? Maana ndiye aliyekuwa chaguo lenu wewe na Jena, ghafla amekuwa mtumzima? Wakati ukimng’ang’aniza Jack amuoe, hukujua kama ni umri wa Jena?” “Hayakuhusu Jacinta wewe! Acha kunivunjia heshima.” “Samahani mama yangu. Nimefurahi tu.” “Kwahiyo...” “Naomba turudi kwangu mama. Kwa hiyo huna ushauri mwingine tena?” “Mimi nilikuwa nakusaidia Jackson. Unaweza kuwa umekasirika kwa kuukosa huo Ubunge uliokuwa ukiutaka sana. Lakini...” Jack akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko, kisha akauliza. “Mimi ndiye niliyekuwa nikiutaka sana Ubunge na si wewe mama? Hukunikuta nimetulia na ndoa yangu, tukiwa na mipango inayoeleweka na Sabrina, umenivunjia ndoa na mipango yote, sasa hivi nimerudi kuwa kama kijana niliyemaliza chuo! Nipo sifuri kabisa!” “Wewe rudi ukatulie, endeleza jimbo lako. Uchaguzi unakuja baada ya miaka michache sana. Upo pazuri. Huko Singida huwezi kushindwa. Sabrina si Mungu wako. Alikuwa akikutafutia sababu, ameipata kwa haraka na ndio maana amekukimbia.”

“Mimi labda niulize japokuwa unaweza ukanichukia sana mama.” “Sasa kwa nini uulize?” Mama yake akamuuliza Junior. “Humuhurumii Jack hapo ulipomfikisha? Kwamba huhisi kama unahusika kumfikisha hapo alipo?” “Kwa lipi!? Sijamwambia Sabrina andoke mimi! Yeye kama si mchawi, anakimbia nini? Anakimbia kwa aibu zake, kuona amegundulika ubaya wake! Na swala la watoto wa kizungu kwani ni uongo? Hata Jack akijidai kuwapenda, kweli wale watoto si wake. Na ni mzigo unaomgharimu Jackson. Kwa pesa ipi anayoingiza Jackson itakayomtosha kutunza na watoto wa wanaume wenzie waliopita hapo kwa Sabrina? Mimi ni mama, lazima niumie. Sasa kosa langu ni kutoa malalamiko yangu? Yeye huyo Sabrina hakumtaka Jackson tokea zamani, ila Jackson ndiye aliyeenda kumlazimisha.” Jackson akashangaa sana.

 “Ndiyo, kwani uongo? Wewe mwenyewe ulikuwa ukiniambia jinsi alivyokuwa akikukataa. Amemlazimisha, wameingia kwenye ndoa, yamemshinda, ndio kakimbia. Halafu mnataka kunitupia mimi lawama! Kama kweli yeye ni mwanamke kweli na anamapenzi na Jack, angebaki tu. Umeoa usipopendwa. Acha kutafuta mchawi wako. Nilikuonya kwa kuwa nilimjua huyu msichana si mwanamke wakuwekwa ndani, hukunisikiliza. Sasa sasahivi yamekurudia, ndipo unanitafuta mimi ili unilaumu! Si kwa hili Jackson. Mchawi wako kamtafute kwenye kioo. Huyo ndiye wakumlaumu, maana amekuponza kwa kuwa king’ang’anizi. Nakwenda kupumzika, msinipandishe pressure kwa shutuma za kijinga mimi. Na iwe mwisho kuniitisha kikao cha kiupuuzi kama hiki.” Jena akaanza kucheka, mama yake akiondoka. Na yeye akachukua pochi yake, akaondoka. Wakabakia wao watatu na baba yao.

“Mzee Msindai, upo baba yangu?” “Nipo Jacinta, mama. Za kazini.” “Mimi naendelea baba. Nachapa kazi. Umekula baba yangu au nikuletee chakula hapohapo ulipokaa.” “Nitashukuru.” Jacinta akasimama kwa haraka na kuanza kumpangia baba yake chakula. “Umemuuliza Pendo kujua Sabrina na watoto walipo?” Junior akamuuliza Jack. “Hajui. Nimemfuta na Sabina, pia hajui.” “Kwa wazazi?” Akauliza baba yake. “Hawapo Chalinze. Wazazi wapo kwa yule kaka yao. Acha mimi nikapumzike.” Jack akasimama, wakamuona anatoka. “Wapi tena!?” “Naona hapa nimekosa mke, baba. Acha nikatulie hotelini kesho nirudi Singida, nikaanze kazi, nisije nikakosa vyote. Usiku mwema.” Hakuna aliyejibu, kimya. Jack akaondoka.

Jacinta akamaliza kumpangia baba yake chakula. “Sasa wewe kula baba yangu, na mimi nikapumzike, kesho nina vikao vya kuanzia alfajiri. Nitakupigia mchana.” “Nashukuru mama yangu mzazi. Uwe mwangalifu huko barabarani.” “Nitafanya hivyo. Sasa muheshimiwa Msindai?” Akamgeukia kaka yake. “Acha na mimi niondoke pengine nitamuwahi Joy kabla hajalala. Usiku mwema baba.” “Na wewe. Salimia familia, zaidi Claire.” “Huyo sijui kama nitamkuta sasahivi. Nitamwambia kesho akupigie kwa kuwa haendi shule.” “Hapo sawa.” Wawili hao wakaondoka na kumuacha baba yao akila hapo sebuleni peke yake, mke chumbani.

Singida.

J

ack akarudi Singida na kuanza kazi.  Lakini na huko Singida nako akakuta habari zake za kukosa ubunge wa Afrika Mashariki zimeenea tena zikisambazwa vibaya sana na mmoja wa mwanasiasa ambaye naye aliona muelekeo wa kurudisha hilo jimbo kwa chama chao, akatamani yeye ndio awe mbunge hapo lakini akakuta Jack ameshajijengea sifa na ni kama kila mtu alishajua yeye ndio atachukua jimbo pale. Kitendo cha kugombania ubunge wa Afrika Mashariki bila hata kuwaambia vijana wake wa chama wale wa karibu tu, huyo mpinzani wa Jack wa ndani ya chama hichohicho akatumia huo mwanya vibaya sana. Akawatangazia watu kuwa Jackson Msindai ni msaliti kwa watu wa hapo. Alikuwa na tamaa ya pesa na alikusudia kuwakimbia pindi atakapopata ila Mungu alimuweka mwangani. Na kweli majina yote ya walioingia kwenye kinyang’nyiro hicho yalikuwa yakitembe tu mitandaoni, walioshindwa walijulikana kwa wazi tu, na waliochaguliwa kuiwakilisha nchi ya Tanzania kwenye Bunge la Afrika ya Mashariki majina yao yalitangazwa na pongezi zao ziliendelea kumiminika.

Akamchafua Jack vilivyo akipita kugeuza mioyo ya wapambe wa Sabrina na Jack akitaka wamgeukie au wawe upande wake ili yeye aje achukue nafasi ya Jackson Msindai kwenye hilo. Akaweka chuki na ufitini. Singida pakaanza kuwa pachungu kwa Jack. Hana majibu ya kueleweka juu ya alipo Sabrina na wanae, na wala hakuwa na sababu ya msingi ya kutoweka wazi nia ya kugombea Ubunge wa Afrika ya Mashariki, ambalo hata halikuwa jambo baya kama anavyosema Waziri Msindai. Jambo jema, wakalifanyia hila bila sababu! Na kama wangeliweka kwa wazi, kushindwa kwa Jack wala isingekuwa jambo la ajabu. Ni kawaida tu, na si Jackson Msindai peke yake ambaye hakuchaguliwa!

 Jack akabaki hajui chakufanya tena. Mama yake ameshamaliza yake, hataki kupandishwa presha. Alichokitaka kwa kijana wake kwa kiasi fulani kimetimia. Mwanae yupo Singida akiingiza pesa yake anayolalamikia ni ndogo, sasa safari hii haitumiwi na Sabrina wala watoto wake Sabrina. Kumetulia. Lake na Jena limetimia. Sabrina amewapisha kwenye maisha yao.

Watu wawili waliokuwa wakiendesha familia moja na kusaidia jamii, shetani ameingilia kati. Si wao tu wanaojiharibia familia yao, na jamii ambayo ilikuwa ikiwatizama kwa muongozo kiajira, kwenye miradi walioanzisha wao wenyewe, Sabrina na Jack.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Je, Sabrina ameyarudia matapishi yake? 

Usikose Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment