Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 52. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 52.

Damu nzito kulikio maji.

Sabina alishapanga na Tino usiku uliopita mara tu alipotoka nyumbani kwa Pendo, kuwa kesho yake atapokwenda kumchukua mama yake na watoto, wakati Sabrina yupo harusini, basi wao wakutane sehemu ili Tino apate muda na watoto wake. Sabina alichofanya ni kushusha vitu vya kina Sabrina na wanae pamoja na mama yake nyumbani kwake, na kuondoka nao wote mpaka sehemu Tino aliyojua watoto wake watapata sehemu ya kucheza na kaka yao kukaa bila shida. Wakakutana hapo bila hata kumwambia Sabrina. Hata Sabrina alipopiga simu kujua hali ya wanae, hawakumwambia sehemu walipo.

Tino alifurahi kuwaona hao watoto mpaka machozi. “Wamefanana sura na mama yao ila damu ya kwetu kabisa! Hizo nywele nyingi mpaka kwenye ngozi ni za kwetu. Si umemuona mama yangu mdogo? Ananywele hivyohivyo.” “Hata mama yako alikuwa na nywele nyingi.” Sabina akaongeza maana alimuonyesha picha za marehemu mama yake pia. “Kabisa, kama mama pia. Nimefurahi Sabina! Asante sana. Sikujua kama naweza kuja kupata nafasi ya kuja kuwasogelea kwa karibu hivi.” Mama yake Sabina kimya akiwatizama hao watoto na Tino.

“Nifanyaje ili wanisogelee?” “Hawa watoto wanapenda michezo ya kimyakimya. Kama hivyo unavyoona wanajenga hapo, sasa usianze maneno mengi. Kajenge nao, hapo ndipo utaweza kuwavuta.” Mama Sabrina akamsaidia Tino. “Hawajaweza kuzungumza tu!?” “Bado. Ila wanaelewa kila kitu, wazito tu wakuzungumza.” “Kama Tino mwenyewe.” Sabina akaongeza. “Katika moja ya vitu nilivyomwandikia Sabrina pia ni hivyo. Kuwa anapoona wanachelewa kuzungumza, asiogope, sisi kwetu huwa tunachelewa sana kuongea, ila tunavipaji vikubwa sana vya uchoraji. Ndio kazi ambayo hata mama mdogo inayomtajirisha. Kwa hiyo tupo hivyo.” Hayo Tino anazungumza macho kwa watoto hao wakizungu.

Mwishoe akawasogelea. Bibi yao alikuwa akitembea na begi lao la michezo kama mama yao ili wasisumbue mtu. Na kweli wakiwa na michezo yao, utakachosikia ni kupiga makofi tu na kucheka. Watajenga vitu vyao kimyakimya bila kuzungumza wala kusumbua mpaka wachoke. Walikaa nao hapo mpaka jioni kabisa bila kumsikia Sabrina kitu kilichomshangaza mama yao na kuanza kumpigia wakiwa njiani kurudi nyumbani kwa Sabina.

~~~~~~~~~~~~~~~~

W

alifika nyumbani kwa Sabina na kumkuta amekaa tu nje, amejiinamia. Alipowaona akasimama kwenda kusaidia kutoa watoto kwenye gari. “Hawa watoto wananukia harufu ya Tino. Mlikuwa na Tino?!” Mama yake na Sabina wakaangaliana kwa hofu maana Sabrina aliuliza swali la moja kwa moja. Sabrina akapata jibu. “Haya naomba umpigie nataka kuzungumza naye.” “Naomba utulie Sabrina. Aliniomba tokea jana, nikaona kwa kuwa hautakuwepo, mimi ndio niwapeleke.” “Una namba yake ya simu?” “Naomba adhabu yake unipe mimi Sabrina. Tino yupo kama mgonjwa, mimi ndiye niliyemruhusu. Anakuogopa kupita kiasi. Tafadhali Sabrina. Naomba..” “Unanipa namba yake au hutaki?” “Mimi naona umpe tu.” Mama yake akamwambia Sabina lakini akiwa amepooza kama na yeye ameingiwa hofu.

Sabrina akarudisha watoto kwenye gari na kuwafunga vizuri, akachukua namba ya Tino na kumpigia hapohapo. Tino akapokea. “Haloo!” “Mimi Sabrina.” Pakazuka ukimya. “Unakumbuka pale tulipokuwa tukiishi Moshi, ukaniacha peke yangu ukiwa umejiridhisha nimeshaua hawa watoto?” Kimya. Sabina na mama yake wakaangaliana wakiwa bado ndani ya gari.

“Wewe Tino? Unasahau pale tulipokuwa tukiishi Moshi mpaka ukawa unanilazimisha niue hawa watoto?” “Nakumbuka Sabrina. Na ninaju..” “Sasa, sehemu kama ile kwa hapa Dar, naweza kupata wapi? Kwa mwezi mmoja tu, nataka nikodi, nikae wakati najiuguza.” Kidogo Sabina na mama yake wakatulia. “Zipo sehemu nyingi tu, inategemea unataka kuishi mtaa upi.” “Sasa sio unitajie sehemu za mamilioni ya pesa, maana mimi ni mama wa watoto watatu, ukichanganya na wale uliotaka niwauwe.” “Sabrina jamani!” “Asije akafikiri wale aliotaka niwauwe niliwauwa. Ndio namwambia pale aliponiacha hospitalini, akakimbilia huku Dar akiwa amejiridhisha nishaua watoto wangu, bado ninao.” “Mimi naona wewe Sabina ungenyamaza maana mnaharibu zaidi.” Mama yao akaingilia.

“Najua sehemu ya pesa nzuri tu. Ulitaka kwa lini?” “Si ndio nimekupigia simu hapa!” “Kwa hiyo usiku huu?” “Unakumbuka nilipokuja mjini kupumzika nikaishia kukuuguza wewe mchana na usiku bila kupumzika, halafu MIMI ukaniacha matatizoni?” Wote kimya. “Basi tokea wakati ule mpaka leo sijapumzika, nakimbizana tu. Sasa sijui kwa hali hiyo ulitaka iwe lini?” “Iwe haraka Sabrina.” Akajibu Tino kwa upole.

“Sasa mimi nina wazo. Unakumbuka ile hoteli tulikaa pale kabla ya kwenda Moshi?” Tino akauliza kwa uzuri tu, Sabrina akampokea. “Pale kwenye ile hoteli tulipokuwa pamoja, ukawa ukinidanganya kama unanipenda sana, umri na mali si tatizo. Tutaendelea tu na tutakuwa na maisha mazuri na matulivu, kumbe ulikuwa uongo wa kutaka kunitumia tu ili uweze kujitegemea halafu unitupe bila kuacha chochote kwangu, hata  watoto niue?” Kimya kidogo. “Wewe Tino? Si pale siku ile ukakasirika na kulia kabisa ukidhani nimekuacha kumbe nilikwenda tu saluni nikaacha sim...” “Ni hapohapo Sabrina. Hapohapo. Nilikuwa nikishauri pengine usiku huu ukalale hapo na watoto, wakati tukishughulikia hiyo Villa. Mimi natangulia hapo kukuchukulia chumba, utanikuta hapo.” “Sasa sio tumekubaliana hapa, ukaanza ule mtindo wako wa kubadilika badilika kama kinyonga. Mtu usiye na msimamo. Unaongea hili leo, halafu kesho unapanga mauaji kabis...” Mama yake akaenda kumpokonya simu. “Inatosha Sabrina.” “Sawa.” Bila shida Sabrina akakubaliana na mama yake na kugeukia wanae.

“Nani anahamu na mama?” Akauliza wanae, mapacha wakaanza kupiga makofi. “Muanze kuongea nyinyi warembo, tuwe tunawasiliana. Mkoje nyinyi! Ona mlivyojaa michanga! Haya twendeni mkapumzike na mama. Mama anataka likizo ya mwezi mzima, mbali na kelele za watu. Nani anakwenda na mama?” Wakajipigia tena makofi na cheko kubwa. Sabrina akacheka. “Naomba nisogeze mpaka sehemu ya taksii dada, mimi na mama tukapumzike.” “Mbona unabadili mawazo wakati tulikubaliana vizuri!?” Sabrina akatoa kichwa garini.

“Naomba nisikilize dada yangu. Maisha yangu yote yamekuwa kuhangaikia watu bila kushukuriwa ila lawama tu. Sijawahi tenda jema hapa duniani, ikabakia sifa ila karaha. Nikakaa nikajifikiria leo siku nzima. Ni kwa nini niendelee kuteseka hivi! Sijapata jibu. Nikajiambia nawajibika mimi mwenyewe kwa Sabrina. Acha nijipe raha. Hii hangaika na mishono ya uzazi mpaka Singida, sasa hivi, kwa nini haswa!” Mpaka Sabina akacheka.

“Sabrina!” “Kweli dada. Sasa twende mama yangu, ukalee uzazi kitajiri, kwenye mahoteli ya wenye pesa zao. Tukipata Villa, nitakwambia umelete na baba, apumzike na yeye hata mwezi tukihudumiwa na sisi kama wagonjwa. Tukitoka huko ndipo tutajua chakufanya. Ila sasa hivi, sitaki kelele kabisa. Mimi na watoto wangu tu. Sitaki kumsikia yeyote yule ila wanangu. Na wewe dada wakikutafuta, tafadhli tafuta hekima yakuwajibu, ila chonde, usiwaambie mimi na mama tulipo. Acha nipumzike kidogo, nipate tena nguvu ya kuendelea na haya maisha, lasivyo nitarukwa na akili, niache wanangu wakiteseka.” “Mimi nipo na wewe Sabrina. Ila kumbuka umeolewa mama, na mahari ya watu tulichukua.” “Usijali. Hayo tutakutana nayo baada ya hata mwezi. Acha nijiuguze mimi mwenyewe kwanza nipone. Au dada utashindwa kunifichia siri? Kama utaona shida, basi hata usijue ninapokwenda.” “Siwajui, hawanijui. Wewe ndio unanihusu Sabrina. Siwajibiki kwao.” “Asante dada yangu.” Wote wakaondoka hapo kwa Sabina, wakiwa na vitu vyote vya Sabrina na watoto wake, pamoja na mama yao kuelekea huko hotelini.

“Jamani Brayan ni mpole mwanangu! Amelia kweli huyu leo?” “Kidogo tu. Lakini kimya hivyohivyo.” “Ubakie mpole hivyohivyo mwanangu, mama apumzike.” Sabrina akamvuta mkono na kumbusu. Akamfunika vizuri akatulia. “Sijui tunapokwenda Sabrina.” Sabrina akamtajia. “Haiwezekani Sabrina!” “Kasema mwenyewe Tino. Acha nikapumzike dada. Nilihangaika naye sana yule mwanaume.” “Ila anaonekana hata huko amefanikiwa!” Sabina akaongeza. “Nimemsikia kwenye mazungumzo yake.” Mama yake akaongeza tena. Sabrina kimya ametulia  na watoto wake kiti cha nyuma.

~~~~~~~~~~~~~~~~

          Wakafika hotelini na kumkuta Tino akisubiria nje kama Valet. Sabrina alishituka sana alipomuona Tino. “Natamani kukuuliza lakini nimejikumbusha kuwa hayanihusu.” “Hongera kwa mtoto. Mtulivu kweli.” Sabrina akamwangalia na kushusha wanae kwenye gari. “Acha nikusaidie kuwabeba hawa wawili.” “Sitaki. Sihitaji msaada wako.” Tino akajivuta nyuma. “Kwanza ile barua ya restrain order bado unayo au nikakutafutie nyingine?” “Nimewapatia chumba kizuri, nenda kapumzike na watoto.” Sabrina akamwangalia na kurudisha uso ndani ya gari kufungua wanae. Sabina na mama yake kimya wakisikiliza.

“Nasubiri ushushe watoto na mizigo ili nikaegeshe gari.” Sabina akaongea akiwa bado amekaa kwenye kiti cha dereva. “Nenda tu kapumzike dada. Uje kesho asubuhi tuwe wote.” “Kweli hamtahitaji msaada kwa sasa?” “Hapana dada. Najua unasubiriwa mahali. Nimesikia ukiambiwa kwenye simu wakati tupo njiani. Wewe nenda, mimi na mama tutakuwa sawa kabisa. Kesho.” “Sawa. Ila mkiwa na shida mnipigie.” “Sawa.” Sabrina akakubaliana na dada yake. Mama yake akashuka garini baada ya kuagana na Sabina.

“Basi ngoja mimi nikalete Cat yakubebea mizigo.” “Ukiongea hivyo unasikika kama mtu mzuri, usiyejawa hila na huwezi hata kufikiria mabaya kwa viumbe wasio na hatia!” Tino akaondoka kwa haraka, kweli akarudi na Cat, gari yakubebea mizigo. “Acha mimi nikusaidie kuipanga hapa na kukuingizia ndani.” “Sitaki Tino. Kwanza ondoka.” “Umetoka kufanyiwa upasuaji Sabrina, acha kubeba vitu vizito! Acha nikusaidie, nitaondoka tu. Mimi silali hapa.” “Sasa hivi ndio unataka kunisaidia wakati uliniacha hospitalini na dripu ya maji, huku ukinipokonya vitu vyako na ukiwa umeridhika nimefanya uovu wako.” “Sasa unataka niendelee kuwa mtu mbaya au mzuri?” Sabrina akamwangalia na kunyamaza. Akatoa watoto wake garini, wakike akawasimamisha pembeni ya gari, Tino na mama yake wakaanza kutoa mizigo garini huku wakipanga kwenye kigari chakubebea mizigo.

Walipomaliza Tino akamuita muhudumu na kumuomba yeye ndio asukume ile Cat ya mizigo. “Naomba nikusaidie kubeba watoto Sabrina. Kwanza wanasinzia, sio sawa kutembea mpaka huko chumbani na wakati...” “Sitaki. Kwanza wameshazoea. Na bibi yao yupo hapa. Akiona wamechoka atawabeba. Usiguse watoto wangu. Kwanza ondoka Tino.” “Sasa huko chumbani utapajua?” “Wewe nielekeze, uondoke. Nipe kadi ya chumba, uondoke.” “Nakusaidia tu, Sabrina! Sina nia ya kuendelea kukukera.” “Unakumbuka uliponiita mimi ni mnyanyasaji?” “Kwa nini nisibebe watoto mpaka chumbani, kisha niwaache mkiwa ndani, kuliko kuwaacha hapa nje! Watu wanapita hapa wanatuangalia! Ona mpaka mlinzi hapo mlangoni hatuelewi! Mpe mama mtoto huyo mdogo, mimi nibebe hawa wawili, twende.” “Wewe mwenyewe umechoka, sidhani hata kama unanguvu yakubeba watoto wawili. Utaniangushia wanangu bure!” Mama yake akaenda kumchukua Brayan mikononi mwa mama yake.

“Naomba mimi mnionyeshe huko chumbani, huyu kaka akabadili nguo, ale, alale vizuri.” Bibi yao akaongoza njia. “Niwabebe?” Tino akaendelea kusihi. “Hawataki kubebwa na wewe.” “Au tuwaulize wenyewe?” “Hawaongei.” “Ila wanaelewa kila kitu hawa watoto. Wanaufahamu mkubwa sana.” Sabrina akamtizama, na kuondoka. Tino akabeba wanae na kumfuata. “Mmechoka sana?” Tino akawauliza kwa upendo, wakajilaza begani. Akaendelea kutembea kumfuata Sabrina kwa haraka ili yeye ndio aongoze njia.

“Na kesho usirudi hapa, wewe Tino. Sitaki wanangu wakuzoee. Wewe ni mpita njia, na ubakie hivyohivyo.” “Ile Villa yakuishi japo kwa mwezi nimeanza kushugulikia.” Tino akatupia akitembea nyuma yake. “Basi usirudi hapa mpaka uwe umekamilisha.” “Sitaki kukuudhi zaidi, Sabrina. Nitafanya kila kitu unachotaka, ila ukumbuke mimi nipo.” “Na hilo ndilo tatizo langu.” Sabrina akajibu. Wakawa wamefika kwenye lift. Wakaingia wote na mama yake Sabrina. “Ungeniacha nimalizie. Kwamba ukihitaji kitu chochote, muda wowote hata kama ni usiku, nipigie.” “Nataka ufute ule uongo na utapeli wako wote ulionidanganya wakati unashida na...” “Namba ya simu nimeandika kwenye simu ya mama, Sabrina. Hata ukitaka dawa ya maumivu, kurudi hospitalini kwa uangalizi tu, wewe nipigie, nitakupeleka.” “Leo ndio unakumbuka kuwa kama wanadamu wengine? Uliniacha hospitalini wewe.” “Najutia mpaka nimekuwa mgonjwa Sabrina.” Sabrina akamwangalia.

“Kweli Sabrina. Najutia na naugua kwa huo ubaya. Sijawahi kumtenda mtu ubaya niliokufanyia wewe na watoto wangu. Huwa nashituka usiku, nikikumbuka, nashindwa kurudi kulala, mpaka kwa madawa. Sili vizuri, Sabrina.” Sabrina akamwangalia vile alivyokonda kama mgonjwa na kunyamaza. “Ila nashukuru Mungu nilikosa nikiwa na wewe Sabrina. Kama ningekosa kwa ukubwa ule nikiwa na mwanamke mwingine, sasa hivi tusingekuwa na hawa watoto.” Hapo Sabrina akawa amefungwa mdomo kabisa. Akanyamaza. Mama yake kimya ametulia hapo ndani ya lift na Brayan akiwa amelala kama dada zake begani kwa baba yao. Wote wakanyamaza mpaka wakafika kwenye chumba.

“Asante.” Sabrina akashukuru na kupitiliza chumbani. Tino akatabasamu tu. “Nikusaidie nini mama yangu? Naona hawa wamejaa michanga sana. Naweza kukusaidia kuwaogesha na kuwabadilisha nguo, wakati wewe ukimsaidia Sabrina kwa huyo kaka yao.” “Una uhakika Tino? Umekuwa nao siku nzima, sijakuona ukila vizuri! Nashauri ukapumzike.” “Usijali mama yangu. Hata hivyo mimi si mlalaji wa mapema hivi. Acha nikusaidie kidogo tu. Nipe nguo zao zakubadili baada ya kuwaosha.” “Sawa.” Tino akaelekea kwenye moja ya bafu la karibu na vyumbani akijua huko yapo mataulo pia. Sabrina na yeye akaingia kuoga kwenye bafu la moja ya chumba, master.

Wakati amejilaza baada ya kuoga, Tino akaingia. “Unajisikiaje?” Sabrina akabaki akimwangalia. “Kuna aina moja ya shampoo na conditioner, nzuri sana kwa ajili ya aina ya nywele zao hawa. Naomba nilete kesho asubuhi pamoja na aina nzuri ya brashi kwa ajili ya aina ya nywele zao pia.  Nimeona aina ya chanuo mnachotumia, sio kwa ajili ya aina ya hizo nywele zao.  Itawasaidia hata wao.” “Hebu njoo hapa karibu Tino.” Tino akasogea na hofu kidogo. Sabrina akakaa.

Unashida gani wewe? Unataka nini tena!? Tafadhali naomba niambie, usinipotezee muda.” “Najutia nilichofanya Sabrina. Nimepata kila kitu mpaka ile leseni niliyokuwa nikihangaikia ya Italy. Sasa hivi nauza picha zangu kimataifa. Kazi zangu zinauzika vizuri. Nina hela Sabrina, lakini majuto yananifanya kuwa kama hivi unavyoniona. Mgonjwa nisiye na dawa, ndio daktari amenishauri nirudi, nitengeneze na wewe kwanza, niweke amani na wewe niliyekukosea kwanza, ndipo tuone tunaendelea vipi!” “Unataka nikusamehe kwenye lipi Tino? Msamaha huo unataka ufike wapi?” “Popote utakaponisaidia kunisamehe Sabrina. Nimekosa, naomba nisamehe.” Tino akapiga kabisa magoti.

“Tafadhali acha kunikosanisha na Mungu wangu. Usinipigie mimi magoti ila Mungu tu. Simama.” Tino akasimama. “Nimekosa kwako zaidi na nitakavyokiri hapa. Najuta Sabrina.” “Sasa naomba uniache nipumzike Tino. Nipo kwenye wakati ambao hata mimi mwenyewe siuelewi. Nahitaji muda wakutafakari mengi  kwenye maisha yangu. Kwa mara ya kwanza nataka nijifikirie mimi kwanza.” “Naahidi sitakubughudhi Sabrina. Nataka tu kusaidia. Najua sistahili, lakini najua kwa hakika hata wewe hustahili kulea peke yako. Watoto wawili si kazi ndogo! Kuanzia kiuchumi na hata maisha yao ya kila siku. Naomba upokee kila msaada nitakaoweza kukupa, kwa muda nitakao weza. Ni hilo tu. Naondoka, nashauri na wewe ufikirie juu ya hili.” “Sawa.” Hilo likamfurahisha Tino, hakutegemea. “Nashukuru sana Sabrina. Basi nitakuona kesho. Na ninachukua kadi moja ili nikirudi asubuhi nisisumbue.” Sabrina akamwangalia na kurudi kujilaza bila kumjibu.

Tino aliondoka hapo akiwa amejawa furaha asiamini kama hajafukuzwa tena. Sabrina alikuwa kama amepoa kwa kiasi fulani, kitu kilichomtuliza na yeye na kumfanya angalau usiku huo akalale kwa amani.

Kwa Kina Msindai.

J

ack alikuwa kama amepigwa na butwaa hajui afanye nini tena. Alikuwa amemkasirikia Sabrina akidhani amemsaliti, kumbe mama yake ndiye amemdanganya. Ameshaharibu mpaka hapo, akaona ni bora amalize tu, ndipo amtafute tena Sabrina angalau akiwa ana habari njema za kuwa Mbunge. Alijua kwa hakika atafanikiwa tu kwenye swala la ubunge. Upepo wote ulikuwa ukionyesha unavuma kwa heri kwake. Akaona arudi kwa Sabrina akiwa ameshamaliza yote na ahadi ya kutulia naye. Alijua kwa hakika Sabrina hana pakwenda, amejifungua na ana watoto watatu wadogo, akajua yupo tu, amalize yake, atamkuta tu. Alishaambiwa na kaka yake kuwa Sabrina anampango wa kurudi Singida na watoto, akaona atulie mpaka akitoka Dodoma ndipo arudi Singida.

Baada ya kufukuzwa harusini, na yeye akaenda kutafuta sehemu akakaa huko mpaka giza lilipoingia ndipo akarudi nyumbani kwao akiwa ametulia kabisa. Hakutaka kesi wala kumuuliza mama yake. Alimkuta chumbani kwake, baba yao sebuleni tu akisoma magazeti kama kawaida yake na kuangalia taarifa ya habari. Akamsalimia na kupitiliza chumbani kwake. Akabadili suti aliyokuwa amevaa, akatoka na yeye akakaa hapo sebuleni. Kimya. Hakuna aliyemsemesha mwenzie mpaka Jack alipoaga kwenda kulala. Mama yake hakutoka chumbani.

Asubuhi siku ya jumapili alichelewa kutoka chumbani mpaka kwenye saa 4 asubuhi alipomsikia baba yake akimgongea chumbani kwake. “Huendi kanisani?” “Hapana baba. Shikamoo.” “Marahaba. Basi ungetoka upate kifungua kinywa.” “Naelekea Dodoma muda si mrefu.” “Basi uwe na safari njema. Acha mimi niwahi. Mama yako naye yupo chumbani.” “Asante baba.” Mzee Msindai akaondoka. Akaenda kuoga na kuchukua mizigo yake baadhi pamoja na suti nzuri akatoka hapo chumbani kwao na kwenda chumbani kwa mama yake. Akakuta amemaliza kifungua kinywa, sinia lipo pembeni.

“Shikamoo mama, mimi ndio nakwenda Dodoma.” “Uwe na safari njema.” “Asante.” Jack akaondoka bila kuzungumzia jingine lolote. Akapewa lifti na dereva wa hapo nyumbani kwao kumpeleka uwanja wa ndege kuelekea Dodoma. Akiwa kwenye ndege alibaki akifikiria jinsi alivyokuwa amefurahia hilo swala la ubunge na jinsi lilivyomgeukia vibaya sana. Amepata ukweli wote wa kilichoendelea kati ya Sabrina, mama yake, Jena na Pendo. Akajidharau kupita kiasi kujiona safari hii amewezwa kirahisi hivyo! Hakuwa na wa kumlaumu ila yeye mwenyewe.

Alifika hotelini. Sehemu nzuri tu, lakini akaanza kusikia upweke wa hali ya juu. Akamkumbuka Sabrina na watoto wake. Akasikia kummisi. Ghafla kila kitu kikakosa maana. Akasikia mzigo mkubwa moyoni, hata huo ubunge na ahadi zake vikakosa maana. Jack asiyejua kumuudhi mtu ghafla anaangukia kumuumiza mwanamke moja tu na wa pekee aliyempenda na kumsubiria kwa muda mrefu sana. Mama yake akilijua hilo, anampokonya! Akasikia hasira asijue anamkasirikia mama yake au yeye mwenyewe aliyeamini kwa haraka na kusahau maneno ya Sabrina tokea mwanzo kuwa angependa babyshower ya Brayan na pia japokuwa asingekuwa huru ukweni, lakini alimwambia wazi kwa ajili yake atakwenda tu, kwa uzazi huo wa Brayan. Alisahau vipi na kuamini kuwa Sabrina ni kigeugeu! Akapoa.

Jumapili.

H

uku kwa Sabrina mida ya saa nne asubuhi, Tino aliingia hapo na mifuko mingi ya vitu vya watoto wake. Akakuta bibi yao akiwapa kifungua kinywa. “Acha nikusaidie.” Akakaa yeye na kuanza kulisha binti zake huku akiwaongelesha na kucheka walivyokuwa wakicheka. Sabrina alikuwa ametulia kimya chumbani akiwasikiliza na mtoto wake wakiume amelala. Alishaamka akala na kunyonyesha na kurudi kujilaza. Tino anaingia hapo alimsikia muda wote.

Ilikuwa ni hoteli nzuri sana na Tino aliwachukulia suite. Chumba na sehemu ya sebule yenye kila kitu. “Sabrina na mtoto wameamkaje leo?” “Vizuri tu. Naona amerudi kulala. Alikuwa hapa na wanae, akaenda kupumzika.” “Jana nilihisi kama yupo na maumivu, anazo dawa?” “Mmh! Sabrina si mzungumzaji wa matatizo yake. Ngumu kujua. Ukimuuliza atakwambia tu yupo sawa. Na ndivyo alivyonijibu hata asubuhi hii kuwa yupo sawa. Ila ameniaga hapa kuwa anakwenda kupumzisha mgongo. Sasa nikusubiri mpaka aseme mwenyewe.” “Sabrina ni mtu mzuri sana mama. Aliniuguza nikiwa sina mtu. Natamani kumsadia sasa hivi, lakini najua ni ngumu kwa niliyomtendea.” “Sabrina ni msiri sana. Sana. Si kama Sabina au watoto wangu wengine. Sasa mpaka afunguke yeye mwenyewe, ndipo utajua kinachoendelea. Mchukulie taratibu tu.”

Tino akabaki akilisha binti zake huku akifikiria. Akamgeukia mama yake Sabrina. “Unafikiri Sabrina atakubali nitoke na watoto wakaogelee kidogo? Nimewanunulia life jackets. Hawawezi kuzama au kudhurika. Nitakuwa nao majini.” “Muulize mwenyewe.” “Tunaweza kwenda wote. Na wewe ukakaa pale na kupata chakula wakati sisi tukiogelea.” “Mimi nashauri uzungumze na Sabrina mwenyewe Tino. Hata jana nilikwambia, si sawa kuchukua watoto bila idhini ya Sabrina mwenyewe. Hata kama umerudi sasa hivi, lakini usisahau amehangaika nao hao watoto tokea hawajazaliwa. Nashauri kwenye kila jambo linalohusu hawa watoto, zungumza naye yeye mwenyewe.” Tino akanyamaza.

Walipomaliza kula, akasaidia kuwasafisha kisha akaenda chumbani. “Vipi Sabrina?” “Hao watoto sijawahi kuingia nao kwenye maji kwa kuwa mimi mwenyewe ni muoga sana wa maji. Hata baba yao huwa namkataza asiwaingize majini tukiwa ziwani.” “Nimenunua lifejackets za kuwavalisha wakiwa ndani ya maji na mimi najua kuogelea. Watakuwa salama. Ila kama ukikataa, sitalazimishia.” “Unataka kwenda nao wapi?” “Kwenye pool ya hapahapa hotelini. Nitakwenda na mama pia.” “Naomba uwe mwangalifu Tino. Tafadhali sana.” “Usiogope, watakuwa sawa kabisa. Kuna muda maalumu unataka niwarudishe?” “Lazima waje wapate usingizi wa mchana. Ikifika kwenye saa 7 na nusu watakuwa wapo tayari kwa usingizi. Naomba warudishe mapema kidogo ili waoge pia na kula.” “Sawa ila naona nitawalisha hukohuko. Unataka uletewe chakula gani?” “Naomba uwe mwangalifu tafadhali. Kusiwe na bahati mbaya huko.” Tino akaelewa hataki amuulize chochote juu yake.

“Sabrina.” Akamuita taratibu, Sabrina akamwangalia. “Nashukuru.” Sabrina akanyamaza wala hakumjibu. Tino akabaki akimwangalia. “Unazo dawa za maumivu?” “Ninazo. Asante.” “Una kila kitu unachohitaji kujihifadhi wewe binafsi?” “Kwa sasa ninavyo, pengine mpaka kesho.” “Niandikie ili nikiondoka jioni, nikajaribu kutafuta madukani.” “Huhitaji kufanya hivyo. Mimi nitaenda kujinunulia mwenyewe.” “Najua unaweza. Lakini kwa kuwa mimi nina usafiri na ninapita huko madukani, naweza kukuchukulia.” Sabrina akanyamaza. “Basi acha niandae watoto, watakuja kukuaga.” “Sawa.” Tino akatoka.

Baada ya muda wakaingia watoto wake na bibi yao. “Jamani mmependeza!” Wakajipigia makofi. Sabrina akacheka na kukaa vizuri. “Sasa hizo kofia za nini tena?” “Nywele zisiwasumbue zikiingia maji. Niza kuogelea.” Tino akajibu akiwa nje ya chumba. “Unashughuli wewe na hawa watoto! Sasa vyote hivi umenunua?” “Jana nilipotoka hapa. Kila kitu walichovaa hapo ni salama kwa ajili yao. Hata hivyo viatu ni maalumu ili wakiloa, wasiteleze. Bibi yao ameniambia hawapendi kubaki miguu tupu bila viatu au soksi.” “Sio hawapendi tu, hawatembei kabisa hao. Lazima miguu iwe angalau na soksi ndipo wanasimama.” “Niliwaona jana wakati Sabina alipowavua na kuwaambia watembee mchangani, wakagoma. Sasa hivyo vitawafaa maana wanaweza kuingia navyo majini na pia wakatembea navyo nje. Nimewanunulia na sun screen cream kwa ajili ya kulinda ngozi yao wakiwa juani, wasiungue.” “Ukiondoka, uniachie hiyo sun screen cream, maana ilibidi kuwabadilishia muda wakuwapeleka ziwani, iwe jioni kwa sababu wanababuka wakikaa sana juani.” “Basi utaona leo wakirudi, hawataumia kabisa.” Sabrina akawaangalia na kucheka.

“Hivi mnajua mnakwenda wapi?” Akawauliza na kucheka, wakajipigia makofi. “Muanze kuongea bwana! Njooni mumbusu mama, na msimsumbue bibi pamoja na Tino. Muwe wasikivu. Sawa?” Wakaenda kupanda kitandani. “Tarabu kaka amelala.” Wakamwangalia mtoto. Tino akaenda kuwasaidia kupanda vizuri hapo kitandani. “Mnaanza kuongea lini?” Wakacheka. “Watazungumza tu. Mama mdogo ameniambia nikwambie huwa kwetu watoto wa kike wanachelewa sana kuzungumza. Hata yeye na mama walichelewa kuzungumza mpaka mama yao akaingiwa na wasiwasi. Bibi akajaribu kuwatafutia wataalamu wa speech, matamshi, lakini na yeye bibi akaambiwa na mama yake ni vya kuridhi.” Sabrina akabaki akimsikiliza.

“Ila kwetu tunakipaji cha uchoraji, Sabrina.” “Sitaki watoto wangu wateseke kama wewe Tino. Wewe unaamini njia yakufanikiwa ni moja tu, huo mkono wako na si vinginevyo. Hapana Tino. Sitaki wanangu wawe watumwa.” “Si utumwa! Na hata hili mama mdogo ameniambia nikwambie, kwetu ni wachoraji sana. Angalia hawa watoto unapowapa michezo yao. Kama umekaa chini ukachunguza, jinsi wanavyopangilia blocks zao, ni kifasaha si kama watoto wengine. Ni kipaji Mungu amekiweka kwetu, huwezi kuwazuia. Hawa hawajafundishwa na mtu. Angalia hata wakikuta hata na vyombo au viatu mahali, ona jinsi wanavyopangilia vizuri! Ni kipawa kipo ndani yao. Ni aidha kukitambua na kuwasaidia kukikuza au kitakuja kujitokeza baadaye sana, kwa kuchelewa.” Sabrina akawaangalia wanae na wao wakawa wanamwangalia. Wote wakacheka.

“Sasa nyinyi mnacheka nini?” Wote wakaenda kumbusu mama yao kwa pamoja. “Halafu hawa wanao Sabrina, utafikiri ubongo wao upo sehemu moja! Wanafanya mambo mengi kwa pamoja tena bila kuambizana.” Mama yake akaongeza. “Na Jack alishasema hivyo. Kuna mambo wanafanya kama kope za macho. Bila kupanga, wanafanya pamoja.” “Nakufanana mpaka mimi mwenyewe huwa kuna wakati nawachanganya. Wakitoka kuoga ndio kabisa mpaka niwaite majina kama ulivyonifunisha. Naanza na Keiline anayeitika kwa haraka, najua ndio yeye na kumtia alama hata ya kitu kidogo tu.” Wakacheka.

“Nikija kurudi tena nitakuletea vitu vya kuwasaidia kwenye makuzi yao. Vyakuchora, kuzungumza na mengine mengi kutokana na akili yao. Watakua vizuri tu.” “Sasa huko kuzungumza ni mpaka lini? Na wakianza kuzungumza ndio itakuwa kama hivyo wewe!” Mpaka mama yake akacheka. “Ndiyo na hapana. Upande wa wanaume hawana shida ya matamshi, mimi ni makuzi mabovu ndiyo yaliyonifanya kushindwa kuzungumza. Mama mdogo yeye ni mzungumzaji mzuri tu. Ipo siku utamsikia, lakini anasema yeye na mama ni kweli walichelewa sana kuongea.” Wakatulia kidogo. “Acha sisi twende kabla jua halijawa kali sana.” “Mama, naomba macho kwa wanangu tafadhali.” “Na Sabina naye anakuja. Usiwe na wasiwasi.” Wakambusu tena mama yao, wakaondoka.

Siku hiyo Sabrina alijikuta hapo chumbani yeye na mwanae huyo wa wakina Msindai, wengine wote wakashinda sehemu ya kuogelea karibu siku nzima. Ilipofika mchana mama yake alirudi kumwambia wanae wana wakati mzuri, anashauri awaache tu, wakichoka ndipo wawarudishe. Sabrina alikubali akijua hata yeye mama yake amefurahia huko walipo. Akawaacha tu.

Jumatatu.

W

akati Sabrina yupo mapumzikoni akiepuka maneno ya mama Msindai akimpa nafasi na mwanae na mapumziko ya uzazi, akifurahia pesa ya Tino huko hotelini, na kumpa Tino mwenyewe wakati mzuri wakulala usiku huo baada ya kuwa na wanae siku nzima na kupigia simu ndugu zake huko Italy akiwatambulisha wanae akitaka wawasalimie na kuwatambua, huko kwa Jack jijini Dodoma ilikuwa tofauti. Alishindwa kulala kwa mawazo. Akajaribu kumtumia ujumbe usiku huo. ‘Nipo mpweke Brina, moyo unauma. Sijui chakufanya! Natamani ungekuwa hapa na mimi, Brina. Nimeharibu, sijui chakufanya.’ Akautuma huo ujumbe na kusubiri ufike lakini akasubiri zaidi ya lisaa, ukawa haujafika.

Akampigia na kugundua simu yake imefungwa asijue Sabrina alifanya kwa makusudi. Alimtumia ujumbe Pendo na kumwambia anajipa likizo ya mwezi mzima, atamtafuta baada ya hapo. Akamtakia mwanzo mwema na Willy, ndipo akazima simu rasmi. Jack akaangalia simu kwa muda akisubiria kuona ujumbe unafika, mpaka akachoka. Akaweka simu chini na kuanza kufanyia mazoezi yale atakayokwenda kujibu bungeni kwenye usahili. Akajiuliza maswali na kujibu akiangalia muda asipitishe akaongea mengi yasiyo na maana. Akajikosoa kwa hili na lile, ilimradi tu kujinoa vizuri. Ilipofika karibu saa 11 alfajiri ndipo usingizi ukaanza kumsumbua. Akasinzia kidogo na kuwahi kwenye usahili akiwa anataka kufanya kwa ajili yake na familia yake.

Baada ya wenzake kadhaa kuingia na kujieleza mbele ya wabunge wote na yeye akaitwa kuwa imefika zamu yake, akaingia. Ukweli alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake akiamini atafanikiwa tu na jina lake pia alijua linambeba. Msindai! Kaka naye yupo kwenye uongozi! Akajua nafasi ni yake. Alikuwa amekaa hapo huku macho kwenye simu akitegemea kuona ujumbe umefika kwa Sabrina lakini mpaka mida hiyo wakiendelea kwa usahili yeye na wenzie, hakuona ujumbe kufika. Akajua kama kawaida ya Sabrina kumblock anapokuwa amemkasirikia. Akaomba simu ya mtu mwingine, akajaribu kumpigia na kumkosa.

Usahili uliisha wakasubiria hapohapo majibu kuona nani amepita nani amekosa, Jack akiwa ametulia hana wasiwasi ila tu kwa familia yake. Ila si kwa kinyang’anyiro hicho alichokuwa amejiaminisha na kuaminishwa hata na mama yake kuwa NI LAZIMA atashinda tu. Muda wa matokeo kufika, Jack akawa hajafanikiwa. Hakupata nafasi ya Ubunge wa Afrika Mashariki. Alishituka na kubaki kama amemwagiwa maji ya baridi. Hakuna kupinga ila kukubali tu matokeo. AMESHINDWA.

~~~~~~~~~~~~~~~~


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment