Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 51. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 51.

“Sabrina!?” Sabina akamuita akitaka kujua msimamo wake. “Nipo kwenye wakati wakutulia mbele za Mungu, anisaidie dada. Angalau nitulie kabisa, pengine akiongea yeye Mungu nitamsikia nijue chakufanya. Kumekuwa na kelele nyingi, sijui nimsikilize nani na niamue nini! Kwa hali niliyonayo sasa hivi, siwezi kufanya maamuzi sahihi. Acha nimalize siku zangu za maombi kwanza.” “Wewe Sabrina kumbe unafunga ndio maana huli! Si maziwa yatakauka!?” Pendo akashangaa sana. Wote wawili na Sabina wakamgeukia Pendo, wakajua wanasikilizwa. “Nina maziwa mengi dada! Mpaka mama ananishangaa. Hapa nimekamua, nimejaza chupa zote, na bado yanamwagika.” “Mmmh! Ila kufunga katikati ya kunyonyesha!” “Na mimi namwambia hivyohivyo, lakini hanisikii.” Mama yake akadakia.

 “Naomba mjumbe nimalize ujumbe wangu ili niwahi kuondoka, nina miahadi mahali.” Sabrina akamgeukia tena dada yake. “Mwenzio amesema yupo anasubiri. Hataondoka kuona kama utapokea au unataka nimrudishie vitu vyake. Anasema hilo begi lina vitu vya thamani sana ambavyo hakuna pesa inaweza kununua.” Sabrina akakunja uso kwa mshangao. “Hataki vije vitupwe tu. Amesema ukikataa, nimrudishie.” “Wewe, Sabina!” Wote wakamgeukia mama yao. “Nipe mimi hilo begi nikae nalo wala usirudishe.” Wakabaki kimya wakimshangaa yeye mama Sabina.

“Jamani tusidanganyane. Kuna maisha na uhalisia wake. Si haya sasa hivi tunayashuhudia! Wakati mwingine mapenzi yanashindwa na uhalisia wa maisha. Leo mnakubaliana hivi, kesho tutakuja kumkuta Sabrina amebaki peke yake kama hivi na watoto. Atafanyaje?” Chumba kizima kimya, maana ni kweli Jack hakutokea hapo siku nzima.

Mama Sabina alipoona ukimya mkubwa katikati ya wasomi hao, mama wa Chalinze, mtaji wake ni watoto wake, akasimama yeye mwenyewe akaenda kuchukua hilo begi pale alipokuwa ameliweka Sabina, kitandani ila amelishikilia. “Kamwambie Tino mimi ninalo hili begi. Sabrina atakapokuwa tayari atalifuata nyumbani kwao.” Akalichukua na kuanza kutoka. Wajukuu zake wote pale walipokuwa wamekaa karibu na bibi yao wakicheza na Claire, wakaanza kumlilia bibi yao pale walipomuona akitoka. “Naona mapenzi yamehamia kwa bibi!” Akadakia Pendo kwa nia nzuri tu, kama kubadili ile hali ya hewa. “Ndiye niliyebaki! Watafanyaje?” Akajibu mama Sabina. Ukimya mwingine tena ukapita. “Simameni sasa mumfuate bibi, acheni kulia bwana.” Wakamgeukia mama yao. “Haya Keiline anza kusimama.” Kweli huyo mtoto akasimama na dada yake akafuata. “Taratibu msianguke sasa, nendeni kwa bibi.” Wakajipigia makofi, angalau watu wote pale wakacheka.

“Ila humo ndani kuna kadi za benki za kila mtoto, amesema kuna pesa. Usizire Sabrina mdogo wangu.” “Dada Sabina! Bado una ujumbe tu!” Wakacheka kidogo.  “Nimekaa naye karibia masaa matatu akijieleza. Na wewe unamjua Tino si muongeaji. Kwa hiyo lazima nimalize ujumbe, ndio niondoke maana na yeye anasubiri jibu. Nimesubiri ili tubakie peke yetu, naona hamna dalili. Sasa Tino anasema zitakusaidia kuwatunza watoto.” “Acha nimuombe Mungu hekima dada. Najua wewe ni mjumbe, lakini natamani isingekuwa wakati huu. Naomba tuyaache tu. Maadamu wanakua, na wanafuraha, naomba tuyaache kama yalivyo kwa sasa. Ila nashukuru.” “Sawa. Na mimi nitakuwa nikiondoka. Nitakuja kesho kuja kuwachukua.” “Nashukuru dada. Asante.” Sabina akaondoka, Sabrina akaendelea kukusanya vitu vyake na watoto. Pakazuka ukimya wa muda.

Junior akavunja ukimya. “Halafu Sabrina, usifikiri nimekusahau. Bado nashugulikia swala la usafiri wa kukurudisha Singida.” “Hamna neno shemeji. Sisi tutakuwa sawa tu.” “Utafanyaje!?” Akauliza Junior kwa mshangao kidogo. “Kesho wakati tunakwenda harusini, nitamuacha hapa mama na hii chekechea yangu yote. Nikitoka kwenye tafrija ya Pendo na Willy, nitarudi hapa. Sabina atatuchukua, tukalale kwake, naona tuondoke siku ya jumapili nikiwa nimepumzika.” “Mtaondoka na usafiri gani!? Ungesubiria niangalie hata ndege ya jumatatu!” “Sabina anaye mtu anayefahamiana naye anakatisha tiketi za ndege. Amemuahidi anaweza kutupatia tiketi siku ya jumapili. Ndio tunasubiria. Usihangaike tena shemeji yangu. Najua una mambo mengi. Naona mimi na timu yangu tupo vizuri kabisa.” Pakazuka ukimya mwingine.

Mkewe Junior akavunja tena huo ukimya mwingine, akiaga. “Jamani tutaonana kesho kanisani. Acha msimamizi wa harusi, akalale. Naona marafiki wameondoka wamemuacha hapo, anasinzia.” “Naona na vidole vishawekwa mdomoni.” Pendo akadakia. “Eti Claire?” “Mimi nitaenda kutengenezwa nywele zangu asubuhi. Mama amesema ataniamsha kama nakwenda shule.” “Hutalia?” Shangazi yake akamchokoza, wakacheka kidogo. “Ata...” “Cleiton, bora usijibu. Maana lasivyo!” Mama yake akamkatisha kaka yake kwa haraka, Clei akaweka mkono mdomoni kama anayejiziba mdomo nakufanya wote wacheke sana. “Mimi silii siku hizi. Nimekuwa dada mkubwa, anti. Na mama amemwambia Clei akiwa ananichokoza na kunifanya nikalia, yeye ndio atalia zaidi.” Walicheka humo chumbani kila mmoja akiwaangalia hao watoto wawili. Siku hiyo nayo ikapita.

Harusi ya Willy & Pendo.

W

akati wapo kanisani, Jack akaingia kama aliyekuwa akikimbia. Ila amependeza haswa. Msafi na amenyoa vizuri, suti safi. Sabrina alimuona ila akatulia tu. Ibada ilikuwa nzuri, ila fupi tu yenye watu wachache. Wakatoka hapo na kwenda kwenye kupiga picha, wakaelekea sehemu ya kula. Hakuna aliyemsemesha Jack hata hapo ndani ya gari wakiwa maharusi na wao kama wasimamizi, yeye mwenyewe akaanza. “Vipi Sabrina?” Sabrina akamwangalia. “Salama.” Akajibu taratibu tu. “Vipi na watoto?” “Hawajambo kabisa.” “Mbona kama sijawaona hapa?” “Wapo na mama na Sabina. Sikutaka vilio kwenye shughuli ya muda mfupi. Nikaona niwaache tu.” “Nilikuwa Dodoma, nimeingia muda si mrefu. Na bado sijamaliza, natakiwa kurudi tena.” Kimya. Hakuna aliyemjibu.

“Mimi nishukuru kwa kutusimamia jamani. Sabrina, asante sana. Najua bado ni mgonjwa na mambo ya operation, lakini ilikuwa lazima wewe uwepo ili nioe.” Pendo na Sabrina wakacheka. “Usijali Willy. Mimi mwenyewe nimefurahi nimeshuhudia kuwekwa historia kwa mara ya pili, tena kanisani! Sikujua kama ndoa za kanisani huwa zinavunjika!” Sabrina akawa kama anashangaa. “Kiukweli hazikutakiwa ziwe zinavunjika, hata maandiko hayaruhusu. Ni basi tu. Ni kosa, haitakiwi kuwa hivyo.” “Lakini nyinyi Mungu aliwakusudia muwe pamoja. Ilikuwa lazima awarudishe pamoja.”  “Ni kwa neema Sabrina. Hata sisi tunakiri ni Mungu tu.” Wakatulia mpaka wakafika sehemu ya chakula.

          Hawakuwa watu wengi. Walishaweka reservation. Wakakuta meza yao ilishaandaliwa. Pendo hakuvaa shela, ila nguo nzuri tu ya rangi ya maziwa. Wakakaa, Sabrina naye akakaa pembani ya Pendo, Jack pembeni ya Willy, Sabrina akainama na kunyamaza. Wakaagiza vinywaji, wakati wanasubiria vyakula wakitoa pongezi zao kwa Willy na Pendo, wakamuona mama Msindai na mumewe wakiwasogelea. 

~~~~~~~~~~~~~~~~

          Pakazuka ukimya. Maana hawakuonekana kanisani. Hata Jena hakutokea kanisani. Hata maharusi wenyewe hawakumtegemea huyo mama maana mara ya mwisho hawakuachana vizuri na bibi harusi mwenyewe, yaani huyo Pendo. Walipofika hapo mezani, wakasalimiwa na kila mtu. Uzuri kuliwekwa viti kwa idadi ya watu. Waliomba meza sehemu ya ndani, lakini ya kuweza kukaa watu 25 mpaka watoto. Kwa hiyo waliweza kuonana.

          Willy na Pendo wakasalimia kwa heshima na kushukuru kufika kwao. “Asante kwa kufika.” “Ulifikiri kwa sababu umeungana na huyo mwenzio kunihujumu kwenye shughuli yangu ndio sitakuja?” Akauliza mama Msindai akiweka napkin yake vizuri. Pakazuka ukimywa wa ghafla, Sabrina macho chini. “Wengine tukisema ‘ndiyo’ kwenye jambo, huwa tunasimamia ‘ndiyo’ zetu, hatuwi vigeugeu.” “Sidhani kama hii ni sehemu yake mama. Tafadhali mambo mengine tuyazungumze wakati mwingine.” Junior akaongea kwa sauti ya chini kama kumtuliza mama yake.

          “Halafu hapa ni harusini jamani! Tusisahau kama sisi tumealikwa.” Akaongeza Jacinta na kuharibu zaidi. “Kukiwa harusini ndio watu hawazungumzi! Hee!? Tena nyinyi ndio mnampa kichwa huyo mwanamke, ananifanyia jeuri mimi kwa kuwa nyinyi watatu na huyo Pendo mmeungana kumkingia kifua.” Sabrina akamtizama.

          “Hata unitizame kwa dharau, lakini Mungu atakulipa wewe. Unanidhalilisha mimi hapa mjini! Naalika watu kumfanyia shower mjukuu wangu, unanikatalia wakati tuliwafanyia shower watoto wako!” “Mama! Unakwenda mbali pasipo sababu!” Jackson akashituka sana. “Samahani, pengine sikuwa nimeeleweka au sikuwa nimeelewa. Mimi sijakataa shower ya Brayan. Hata Jack nilimwambia, ningependa na Brayan afanyiwe shower.” Sabrina akaongea taratibu tu.

                   “Huo ni unafiki mbele ya watu ili uonekane mwema kumbe ni...” “Hapana mama. Acha kumtukana Sabrina. Hata kama amekataa shower lakini...” “Samahanini jamani. Mimi naomba niondoke, ili kuleta amani hapa.” “Umesha...” “Ila kama nilivyosema hospitalini, muda na wakati wowote ule mtakaomtaka Brayan, tafadhali tuwasiliane tu. Na sijakataa shower. Brayan ni mtoto wangu kama Jeiline na Keiline. Sikatai baraka zozote kwa mtoto wangu. Tafadhali, mnijulishe tu. Ni lini, wapi na muda gani natakiwa kufika na Brayan, bila shida nitafika ila kulala nilazima nilale walipo watoto wangu wengine wote.” Sabrina akamalizia.

          Akamnong’oneza kitu Pendo ambaye alikuwa akilia, akachukua pochi yake na kuondoka taratibu. “Kweli mama Msindai, kwa ajenda zako binafsi unakuja kuniharibia harusi ya mtoto wangu!?” Akalalamika mama K. “Mimi nafahamiana na wewe mama Msindai na familia yako kwa muda mrefu sana, lakini leo umevuka mipaka. Unakuja kumtusi binti yangu siku ya harusi yake kwa kuwa tu amemchagua Sabrina kuwa rafiki! Umetuvunjia heshima vibaya sana, mama Msindai.” “Mimi nahisi ametudharau sana. Pengine ametuona sisi wote hatuna maana, ila hao wageni aliokuwa amewaalika kwenye hiyo babyshower yake.” Akaongeza Kenton kwa mama yake.

          “Umepokelewa kwa heshima kubwa sana hapa, na ukashukuriwa. Umegeuza harusi ya mdogo wangu sehemu ya kutolea dukuduku lako!? Kilichoshindikana ni nini kumuita Sabrina pembeni na kuzungumza naye?” Akaendelea kulalamika Kenton. “Hakutaka kuzungumza ila kumuadhibu Pendo, kwa kumpokea Sabrina. Kile kinachoendelea pale kwa Pendo, akilia kwenye harusi yake, ndicho alichokuwa akikitaka. Na amekipata.” Akaongeza Nancy. Mzee Msindai kimya.

          “Hiyo ni dharau ya hali ya juu sana. Kama wangekuwa wamekaa hapa kwenye hii tafrija, watu wa hadhi zenu nyinyi, kwamba na sisi tungekuwa tumealika maraisi hapa, pamoja na wake zao. Mawaziri wenye vyeo kama vyenu hivyo, kweli mama Msindai ungefanya ulichokifanya hapa?” “Kwani nimeongea nini cha ajabu?” “Hivi unajua hii harusi ilibidi kusogezwa mbele ili Sabrina awepo hapa na Pendo?” Akauliza tena Kenton. “Kwani mimi nimemfukuza Sabrina? Dhambi zake mwenyewe ndizo zimemkimbiza!” “Jamani, acheni mimi nimuwahi Sabrina. Yule binti amejifungua kwa upasuaji, nahisi leo ndio amemaliza juma. Sidhani kama ni sawa...” “Nenda Jacinta. Tafadhali sana.” Akadakia Junior, Jacinta akaondoka kwa haraka, Jack akawa kama ameduaa.

Jack akasimama kama mshale. “Subiri kwanza Jack. Acha kukimbia kimbia na wewe kama usiyejielewa.” Pendo akajifuta machozi. “Kwa kuwa mama yako ameanza kuvunja amani kwenye hii tafrija akimshutumu Sabrina bila kosa.” “Pendo nakuonya wewe mtoto.” “Hapana mama Msindai. Umekwenda mbali mno na najua mwisho wa haya yote ni kutaka kuvunja ndoa ya Jack.” “Navunja!” “Nyamaza mama Msindai. Umekuja mwenyewe kwenye shuguli yangu na kuanza fujo. Heshima haiombwi.” Pendo akawa mkali mpaka akashangaza  wote. Willy akamshika.

“Pendo!” “Kabisa mama Msindai! Unampotosha Jack kwa kisingizio cha maendeleo huku ukipanda mbegu za chuki katikati yao! Unamdanganya Jack ili kumchukia mkewe...” “Nilikuonya acha uzushi Pendo wewe!” Pendo akamgeukia Jack. “Haya CJ, nenda na watoto kule baharini mkacheze.” Mtoto mkumbwa wa Junior akachukua watoto wote wakaondoka kama alivyoagiza mama yake.

“Sasa wewe jidai unataka ubunge, halafu ukawa mbunge, ukajikuta huna mke wala watoto. Mama yako anakudanganya Jack. Anachotaka ni ushindani, alichofanya Sabrina kule Singida na kukusanya watu, ndio anataka na yeye akifanye apate sifa kama alivyosifiwa Sabrina. Hapo alipo anachuki kwa kile alichokifanya Sabrina Singida na kufanikiwa akasifiwa yeye Sabrina na si yeye.” ‘Unaongea nini wewe Pendo?!” Jack akauliza. “Mnafiki huyo na mchonganishi.” “Sasa kama ni muongo, si umuache amalize kuzungumza ndipo ukanushe? Eti mama Msindai? Umeanza mwenyewe, tumekusikiliza mpaka mwisho, acha na Pendo naye azungumze. Kwanza ni harusi yake, umeshaiharibu, hakuna cha ziada.” Akasisitiza Kenton.

“Haya ninayokwambia Sabrina hatakwambia kwa kuwa amekataa. Hataki kukuchanganya, anaona ni bora yeye abakie mbaya, ili utulie na mama yako. Mfanikiwe kwa hila zenu. Lakini Sabrina si kigeugeu Jack. Mimi siwezi kukuficha. Alimsikia mama yako na Jena wakimsema vibaya sana. Maneno machafu mno siwezi kurudia hapa itakuwa kama kumdhalilisha tena Sabrina. Ila walikuwa wakilalamika kuwa wale mapacha wanakufilisi wewe, na hawataki pale nyumbani kwake.” “Haiwezekani! Si kweli Pendo. Mama aliwaandalia...” “Acha kuwa kama toto linalonyonya na wewe! Tumia akili zako wewe Jack!” Pendo akawa mkali kabisa. “Siwezi kukaa hapa na kusikiliza uongo wa kipuuzi mimi.” Mama Msindai akasimama.

“Ondoka tu, lakini wote tunajua unakimbia ukweli.” Akamgeukia Jack. “Wewe ulifikiri siku ile hospitalini mama yako alikuwa akiniomba niwe nawaleta kina nani pale nyumbani kwake?” Jack akawa anajaribu kuvuta kumbukumbu. “Walikujaza maneno mengi ya uongo wakimsingizia Sabrina eti anakataa kwenda kwake mama Msindai kwakuwa ulimficha siri yenu ya ubunge wa EALA. Wakakujaza huo uongo ili kukupoteza tu kwenye lengo. Lakini walitaka Sabrina aache watoto wake nyumbani kwangu, yeye akaishi kwenu kama kuwaficha wale mapacha wake eti marafiki zake hao waheshimiwa wasije kuona watoto wa kizungu pale kwenu.” “Haiwezekani! Maana mama alishavuka huko kwenye swala la wale watoto, hata alikuja Singida akakaa nao!” “Si huyo hapo akanushe.” Akaongea kwa hasira. “Sina muda wakujibu shutuma za kijinga.” Mama Msindai akaondoka.

“Hawataki kabisa wale watoto na anafanya kila awezalo kukutenganisha na Sabrina. Na kwa taarifa yako tu unacheza mchezo wa hatari sana Jack, mpaka nakuhurumia. Aliponitenda Willy, alinitenda nikijua ananipenda. Sikujua mapenzi ya mtu mwingine isipokuwa ya Willy, aliyekuwa akinipigania kwao mchana na usiku ndio maana tulirudiana kwa urahisi. Lakini wewe Jack, unapita kwenye moyo uliojaa madonda. Hujaweka hata mizizi, hujatoa hata sababu ya msingi yakuvumiliwa na kupendwa kweli mpaka kifo, unacheza michezo ya visa vya mama mkwe wewe! Unachokifanya wewe unatofauti gani na Tino?” “Acha kunifananisha na Tino, Pendo.” “Haa!” Pendo akakaa vizuri.

“Hujamuacha Sabrina nyumbani kwangu akiwa na hedhi mbaya, mshono wa uzazi akiwa na watoto watatu, wewe unanyonya kwa mama yako mkifichiana siri?” “Ni jambo...” “Acha ujinga Jack. Wewe ni kama mdogo wangu. Lakini nakwambia ukweli kabisa, samahani naongea hivi mbele ya baba yako na kaka yako, lakini sikujua kama unaakili ndogo kiasi hiki!” “Pendo unanitukana.” “Hakika wewe ni mjinga wa mwisho kabisa Jack. Kasirika mpaka urukwe na akili. Sijui utakuwa mbunge wa namna gani unayeshindwa hata kufikiria! Unauchu wa madaraka mpaka unakuwa mnyama wakupitiliza!” “Sio uchu wa madaraka.” “Ni uchu huo na mama yako amegundua huo udhaifu wako ndio anaoutumia. Sasa nikwambie kabisa, umecheza kijinga, na mama yako amekuingiza pabaya na wewe umeingia kama likondoo.”

“Kwanza wewe una katoto kamoja tu na Sabrina, pamoja na mama mkwe mwenye matusi makali akimdhalilisha vibaya sana. Mwenzio Tino anao...” “Tino si mwenzangu.” “Na kweli si mwenzako maana yeye anao watoto wawili na Sabrina, na amejirudi akijutia makosa yake. Hana baba wala mama mkwe wakumkera Sabrina. Anamtaka Sabrina na watoto wake, tena kwa machozi. Ndipo mtajua kama Sabrina ni mchawi au ni Mungu wake. Sasa nenda Dodoma, nenda kokote ukawe mbunge, acha wanaume wenzako waliokwisha shiba pesa, wakayaishi maisha, wakajua familia ni bora kuliko mengine yote, wakushikie kile mama yako anachokuaminisha hakina umuhimu. Tutakuona mitandaoni na ubunge wako. Huna aibu wala shukurani kabisa wewe Jack.”

“Maisha yako yote ulikuwa Msindai. Hakuna hata gazeti lililotaka kukuweka. Kaka yako na mama yako si wapo na nyadhifa za juu za uwaziri! Mbona hukuwahi kuitwa bungeni? Swala la ubunge wa afrika Mashariki kwani limeanza leo? Mbona hushangai mama yako hakukuweka huko mpaka alipoona Sabrina amekutoa huko mavumbini Singida, ndio mnaanza fujo za kipuuzi hapa! Mnajidai tu, lakini hamna lolote wanafiki wakubwa nyinyi mnapenda kutumia watu bila aibu. Haya ondoka, nenda kamfuate mama yako.” Jack akabaki amesimama.

“Baada ya dakika 5 ukiwa umesimama hapo, nakuitia askari akutoe hapa kwa nguvu, kesho uonekane magazetini. Toka na nisikuone tena Jack. Mbaya kabisa wewe, mwanaume usiye na msimamo, ila uchu wa madara.” “Tulia Pendo mama yangu mzazi. Utapandisha pressure.” “Hawa si watu baba. Wanyama kabisa, hawa! Huyu Jack anahangaikiwa na Sabrina akiwa mjamzito mpaka anafanikiwa, hata mwaka haujaisha, anajidai yeye ni Msindai, mtoto wa mama anamtelekeza Sabrina akiwa mgonjwa! Huna akili kabisa Jack. Na kaburi mama yako alilomchimbia Sabrina, linakuzika wewe mwenyewe tena ukiwa hai. Subiri utaona ‘Muheshimiwa Msindai!’ Siku yako inakuja.” Pendo akamdhihaki kwa kumwita ‘Muheshimiwa’.

“Na msiba huo utalia mwenyewe, maana mama yako pamoja na Jena watakuwa busy wakisherehekea ushindi wa kumrudisha Sabrina na watoto wake wakizungu kwa Tino, wewe wamekukabidhisha huyo msichana wanaetaka umuoe.” “Tena naona kama Tino ameshapata baraka za mama yake Sabrina!” Jack akakunja uso na kumgeukia Nancy. “Mimi naona wewe upambane tu upate Ubunge, umfurahishe mama yako, mheshimiwa Msindai. Naona maswala ya ndoa yanahitaji wanaume kwelikweli, wewe huyawezi. Kapige tu siasa. Sasa kama alivyokwambia Pendo, hapa sisi njaa zinauma. Tunaomba utupishe, sisi wanandoa tuendelee kudumisha ndoa, wengine siasa hatuwezi.” Nancy akaongeza.

“Nashauri Jackson uondoke.” Akaongeza mzee Msindai aliyekuwa kimya kabisa muda wote. “Na pengine niombe radhi kwa wote. Najua hii si picha mliyokuwa nayo kwa siku ya leo. Mtuwie radhi. Binafsi nishukuru kwa heshima mliyotupa, acha tupishe hapa, ili mjaribu kuimaliza hii siku vizuri. Naamini Sabrina atakuwa salama. Muwe na wakati mzuri.” Jacinta akarudi wakati baba yake ndio amesimama tu. “Jamani sijampata Sabrina. Nimempigia simu baada ya kumkosa hapa, simu yake haipo hewani. Na nimezunguka kila mahali hapa mpaka nikauliza walinzi wa pale nje, hawajamuona. Mwenye simu ya Sabina, naomba.” “Mimi ninayo ya mama yake. Acha tumjaribishe.” Ikabidi  mzee Msindai asubiri.

Pendo akampigia mama Sabina. “Bibi harusi!” Ikabidi Pendo acheke tu. “Mpo na Sabrina hapo?” “Alinipigia muda tu kuniuliza kama bado tunamaziwa ya mtoto. Alipojua tulishaondoka pale kwako na watoto wapo sawa, akaniambia anakwenda mahali, atatutafuta baadaye. Nilifikiri mpo naye!” “Nashukuru mama yangu. Tutawasiliana.” Pendo akakata bila kutaka kumtia wasiwasi. “Sasa atakuwa amekwenda wapi?” “Sasa hivi ndio unajidai kuuliza!? Acha kunitia kichefuchefu Jack. Please.” Akamjibu kwa hasira na kumgeukia Jacinta. “Nahisi naweza kujua alipo, lakini sitawaambia. Yupo salama dada Jacinta. Nashukuru kujali.” “Unauhakika?” Akauliza kwa kujali Jacinta. “Kabisa. Wewe kaa ule dada yangu.” “Na kunywa.” Jacinta akavuta kiti na kukaa.

“Mbona baba na mheshimiwa Msindai mmesimama?” Jacinta akauliza akivuta glasi yake ya magarita. “Mimi nilikuwa nikiondoka, mama.” “Bila kula baba yangu!? Mambo yako yote yapo hapa. Wanyama wa baharini, washaokwa, kazi kutafuna tu baba yangu. Au nikawaombe wakufungie uende navyo?” “Wewe uniletee nyumbani.” “Usitie shaka baba yangu. Nikilewa kiasi chakujua sitafika kwako, nitamuomba kaka yangu hapa akupitishie.” Ikabidi wacheke. “Nashauri usiendeshe baada ya hapa.” “Hilo wazo zuri baba yangu. Nitalifikiria.” “Naomba utilie maanani, Jacinta. Tafadhali mama.” “Sawa baba yangu. Mimi mtiifu.” Jacinta akasindikiza za kinywaji mdomoni, Mzee Msindai akamwangalia huyo binti yake nakuondoka.

Tushatia aibu hapa, bora tu kulewa, yaishe.” Jacinta akaendelea huku akinywa, wote wakacheka. “Kunywa kidogo Junior, kaka yangu. Hamna jinsi.” “Natamani kama kuondoka!” “Sasa hiyo ndio aibu mara mbili hapa. Au nadanganya Kenton?” Jacinta akafanya wazidi kucheka. “Kweli tena. Ushaona watu wanaofanya fujo kwenye harusi za watu, tena tupo tu wachache hapa, halafu tena tuondoke! Jamani tunyweni, tu.” Akanyanyua glasi juu. “Jamani, kwa Willy na Pendo.” “Kwa Willy na Pendo!” Wote wakanyanyua glasi na kugongesha.

“Pendo naomba tuzungumze pembeni kidogo.” “Acha kunisumbua Jack. Nilikuwa nyumbani tokea tulipoachana hospitalini. Ungekuja.” “Nashauri Jackson uondoke.” Kaka yake akaweka msisitizo. “Unanisikia Jackson?” “Sawa. Lakini mimi si msaliti, nampenda Sabrina na wala sijamtumia tu. Hapa nilitaka kujua Sabrina alip..” “Kwa nini sasa hivi Jackson? Kwa nini iwe kwenye shughuli ya mwenzio?” Junior akawa mkali kabisa. “Uharaka huo unatoka wapi?” “Basi kaka. Lakini nia ilikuwa nzuri tu tokea mwanzo. Sikuwa nafanya siri. Ila..” “Nafikiri unazungumza na watu ambao sio sahihi kabisa Jackson. Hayatuhusu. Sijui kama unaelewa?” “Sawa kaka. Na samahanini sana jamani.” Kimya. “Mimi naona wewe ungeondoka tu, washawachoka kina Msindai.” Jacinta akajibu akiendelea kunywa huku akizungumza. Jackson akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment