Jackson alipotoka tu Willy akampigia simu
Junior. “Samahani kaka. Najua usiku na umepumzika. Ila
nimekwama. Nina shida.” “Hamna shida. Karibu.” “Naomba
unisimamie harusi siku ya jumamosi, ila kesho ambayo ni siku ya kazi
tunahitajika kwa mchungaji mida ya saa nne na nusu asubuhi. Nimekwama kaka,
ndio maana nakuomba wewe. Sina watu. Nilipoteza ndoa na marafiki pia.” “Pole
sana. Labda niulize kwa Jackson imekuaje tena? Nilisikia yeye na mkewe
wangewasimamia!” “Kwanza nafikiri Sabrina
anakaribia kuwa aliyekuwa mkewe, pili Jackson kesho ana mambo ya Ubunge
wa Afrika Mashariki. Kesho ndio siku yenyewe.” “Hebu twende taratibu Willy.”
Ikabidi Junior akae sawa.
“Ndio hivyo
kaka.” “Tuanze taratibu. Unasema Jackson Msindai anagombania kwenye Ubunge wa
Afrika Mashariki!?” “Ni siri yake na mama yenu hata sisi wenyewe tumejua leo.
Hata mkewe amesikia leo wakiwa hospitalini, Jena aliropoka tu kama kawaida yake
unavyomjua Jena.” “No way! Yaani Sabrina mwenyewe amejua leo!?” “Acha
kaka, ni mambo yakusikitisha.” “Sabrina amehangaika sana na Jackson!” Kidogo
kikaonekana kumsumbua Junior. “Ndio chakuumiza na hapa
tunavyozungumza, yupo kwa mama yake, ameacha mzazi hapa.” Willy
akamueleza mengi mno ya uchungu na kumshangaza sana Junior.
“Kwa hiyo
nimekwama kaka. Naomba msaada wako unisimamie.” “Hilo halina shida. Lakini
naomba nikuombe kitu Willy.” “Nakusikiliza kaka.” Walimjua Junior kwa
hekima. Akatulia akitaka kusikia hizo hekima zake usiku huo akiwa hajui hatima
yake na msimamizi wake. “Tafadhali usimkatie Jackson
tamaa. Naomba mvumilie. Najua unaweza usimuelewe sasa hivi, lakini atakuwa
kwenye kipindi kigumu sana, ambacho atatuhitaji tu. Naomba mimi nije kesho hapo
kanisani. Nifanye yote yanayohitajika, ila kwa niaba ya Jackson, na nitamwambia
mchungaji. Mafundisho yote mimi nitarikodi kwa ajili yake. Akishindwa kutokea
kabisa kesho, basi akimaliza shughuli zake nitampa ajue ni nini mchungaji alitaka asikie yeye kama
msimamizi.” “Sasa na jumamosi siku yenyewe ya harusi asipotokea?” Willy
akasikika kutoridhika.
“Atakuwepo
kwenye harusi. Na kama asipokuwepo basi mimi nitasimama badala yake. Tafdhali
Willy. Nikuombe kwa niaba yake. Sisi ni ndugu, tusikatiane tamaa. Na unamjua
Jack. Anampenda mke wake na watoto wake, pamoja na familia yako. Katika hili
naomba tumsaidie. Ili jambo jema lisigeuke kuwa baya.” “Ndio nashangaa sasa!”
“Ni kweli anachofanya ni kitu kizuri sana, ila utekelezaji wake ndio umekuwa
mbaya tu. Lakini anafanya kitu sahihi. Tafadhali mvumilie.” “Nimekusikia kaka.
Na asante. Najua unamajukumu mengi.” “Hata hilo ni moja ya jukumu la muhimu
sana. Ndoa ni msingi wa kila kitu. Nakupongeza sana.” Willy akacheka
akisikika ametulia sio jazba kama alivyoanza. Akashukuru na kukata simu akiwa
ametulia kabisa.
Jacinta.
M |
ida ya saa
12:30 asubuhi Jacinta akawa amefika hapo nyumbani kwa Pendo. Sifa akamfungulia.
“Wote bado mmelala? Nimekuja kumuona mzazi kabla siku haijawa na mengi.” “Mimi
na bibi tulishaamka. Hata dada Pendo yupo macho chumbani kwake, amepita hapa
sasa hivi kutoka kumwangalia mzazi.” “Basi acha nianzie kwa Pendo.” “Umependeza
dada!” Jacinta akacheka. “Asante Sifa. Mama shikamoo.” Mama Sabina akaitika na
kutoka kusalimiana na Jacinta. “Na kweli umependeza.” “Asante. Acha nizungumze
na hawa warembo wawili kabla sijachelewa kazini.” “Karibu dada Jacinta. Kama
kawaida yako umependeza.” “Asante. Sasa mbona asubuhi asubuhi na mifuko?”
Jacinta akamuuliza Pendo. “Nampelekea Sabrina. Twende, yupo macho.”
“Hatutaamsha watoto?” “Wanae wana mida yao yakuamka. Hapa tulikuwa tukizungumza
tokea saa 11 asubuhi usingizi uliponiishia.” “Naona mtakuwa na kazi yakucheka
tu.” Willy naye akatoka chumbani kwake na kumsalimia Jacinta, ndipo wakaelekea
chumbani kwa Sabrina.
“Karibu. Nasikia sifa za kupendeza
kwako, nikawa nakusubiria. Shikamoo.” “Marahaba Sabrina, hujambo?” “Mimi
naendelea vizuri, namshukuru Mungu.” “Mshono?” “Naona unaendelea vizuri
kwakweli. Njoo ukae hapa kitandani, usisimame muda mrefu na kiatu kirefu.”
“Nishazoea. Majukumu niliyonayo yanataka kiatu kirefu muda wote kazini.
Usijali. Ila nakaa ili mniambie nini kilitokea jana hospitalini.” Sabrina na
Pendo wakaangaliana. “Ni nini?” “Sabrina hataki kusema eti anaogopa kuwa
mchonganishi.” “Wala si uchonganishi, ni ili na wewe ueleweke Sabrina. Umesikia
wifi yangu?” Sabrina akanyamaza.
“Usiache watu wakakusema vile
watakavyo. Iwe wamechagua tu, lakini ukweli ujulikane. Niambie nini kimetokea.”
“Mama Msindai hataki hawa wanangu wawili, wifi.” “Unamaanisha nini?” Jacinta
akakaa pembeni ya kitanda. “Acha mimi nikusimulie dada.” Pendo na yeye akakaa.
“Jana sisi wawili tulikwenda kutembea kama mazoezi, tukawaacha Jena na mama
yenu wakiwa na mtoto. Jack alikwenda kulipia. Wakati tunarudi tukawasikia
wakimsema Sabrina vibaya sana. Pamoja na mimi.” Pendo akamasimulia Jacinta
mwanzo mpaka mwisho, Jacinta akabaki ametoa macho.
“Haiwezekani!” “Ila hata Jack hajui
haya.” Sabrina akaongeza. “Kwa nini?!” “Wifi, Jack yupo kwenye ushindani. Mama
yake akitaka afanye anachotaka, sitaki tena mimi nikazidi kumchanganya halafu
ikawa lawama. Acha afanye anayoshauriwa na mama, mpaka afike mwisho, nisije
laumiwa baadaye.” “Wala hutaacha kulaumiwa.” “Asante dada Jacinta. Na mimi
nimemwambia hivyohivyo Sabrina.”
“Nisikilize Sabrina. Mimi namjua mama.
Ulipo hapo na Joy, wifi yetu alifikishwa kasoro tu, Junior sio mtoto wa mama
kama Jack, ndio maana Joy alipita. Mumewe alisimama naye mpaka mama akaelewa
kuwa Junior hataki mchezo kwenye ndoa yake. Sasa kwa Jack ni tofauti. Jack ni
mtoto wa mama yule ambaye hakui, na ni marafiki wa kuzungumza hata saa sita
usiku. Kwa miaka yote unayojua Jack anayo, mama ni rafiki wake wakaribu mno,
ndio maana unamuona safari hii amekamatwa na hana jinsi yakujitoa. Nilimkuta
jana nyumbani, Jackson hakuwa na furaha
kabisa. Ni kama aliyekuwa njia panda. Na mama akahakikisha anatuonya kabisa na
kututenga na Jack. Hakutaka kabisa tujue kinachoendelea.”
“Yaani mimi, ndio nimeambiwa na Junior
jana usiku baada ya kuzungumza na Willy kuwa Jack anagombea Ubunge na wewe
hujui. Ndio tukaelewa ni nini kinaendelea, ila hatukujua kama mama hakutaka
watoto waende pale, ndio maana mimi na Junior tukaona nije tuzungumze vizuri na
wewe. Na ujue ni kweli mama hataki kumshiriki Jack na yeyote yule hata sisi
ndugu zake pia hataki. Mimi na Junior ndio maadui wakubwa wa mama sababu ya
Jackson. Na anafanya hivyo kwa mapenzi tu aliyonayo kwa Jackson. Naomba
umsamehe Jack. Tafadhali Sabrina. Muhurumie tu na uelewe alipo sasa
hivi. Mama ana ushawishi wa hali ya juu, najua kwa sehemu na wewe umeshamfahamu.”
Sabrina akacheka na kunyamaza.
“Na wote tunajua jinsi Jackson
anavyokupenda Sabrina. Si kwa kinafiki, Jack anakupenda. Alikosana na mama kwa
ajili yako. Ili tu kukuoa.” Sabrina akajifuta machozi. “Kweli. Mimi
nilikuwepo wakati Jack akikugombania. Yupo kwenye wakati mgumu na haya
yote pia anaona yatakuwa na manufaa kwenu wote ndio maana unamuona ameangukia
kwenye mtego kirahisi. Na mama ametumia hiyo njia makusudi akijua udhaifu wa
Jackson. Mama yetu anaakili Sabrina, anayo akili ile ya kufikiria kwa haraka na
mbali. Ngumu kumshinda, mpaka uwe na akili na moyo kama wake, ndipo utamuweza.
Hivihivi, sio mrahisi. Kwa hiyo vumilia tu. Ila huu ndio msimamo wetu
mimi na Junior.” Sabrina akamwangalia.
“Safari hii hatutazungumzia chochote
kama mama anavyotaka. Tutawaacha tu waendelee mpaka mwisho. Akifanikiwa,
tutatoa pongezi kama wengine, ili mama apate huo utukufu anao
uhangaikia, pengine atatulia. Hatutazungumza lolote ila kuwa watizamaji
tu. Kwa hiyo tunaomba na wewe usikate tamaa. Ukweli jambo analofanya ni zuri
sana tu. Ubunge wa Afrika Mashariki sio jambo baya, na lingemuongezea sifa na
bado angerudi kugombania huko Singida. Ila tu mama amelifanya liwe baya mpaka
kutenganisha familia! Tena bila sababu mpaka linashangaza! Ukitaka chochote
kile, mimi na Junior tupo kwa ajili yako.” “Nashukuru
Wifi yangu. Ila naomba mimi nikasubirie huko Singida.” Sabrina akajifuta
machozi.
“Naweza
kurudi huku kama itahitajika, lakini tuna miradi mingi na muhimu sana
tulianzisha na Jackson. Siwezi kuiacha katikati tu! Mimi ndivyo nilivyo wifi.
Nikianza jambo najisikia lazima kumaliza.” “Inaeleweka Sabrina, na hiyo nayo ni
sifa aliyokusifia Jack pale nyumbani.” Sabrina akacheka na kuinama.
“Sasa kwa muda gani?” Akauliza Pendo.
“Ni kwa
muda tu dada. Ikishasimama, tukapata wasimamizi wazuri, sio ikafa mara tu
tutakapoondoka! Nikijiridhisha ipo sawa na imesimama, na Mungu amenipa
kibali chakuondoka, basi nitaondoka. Lakini sio sasa, tena ghafla! Sitaweza.”
“Basi popote ulipo jua mimi na Junior simu yako itapokolewa wakati wowote.” “Nashukuru sana wifi yangu, na asante kunisikiliza.”
“Karibu na acha kulia. Usilie tena. Una watoto wanao kuangalia. Tulia kabisa
fanya kile unachoweza kufanya. Mengine yatasubiri tu.” Sabrina akajifuta
machozi na kutulia. “Ewaa!” Wakacheka vile Jacinta alivyosema kama kufurahishwa
na Sabrina kutulia kwake. “Basi acha mimi niwahi kazini, tutaonana baadaye.
Pendo unitafutie wine bwana. Nikitoka kazini niikute.” “Usijali dada yangu.
Nikitoka kanisani nitaenda kukununulia, uikute hapa.” “Hayo ndio maneno.”
Jacinta akatoka.
Kanisani.
P |
endo na
Sabrina walitoka nyumbani bila yakuchelewa kwa makubaliano wakutane na Willy
pamoja na Junior huko kanisani. Wakamkuta Willy alishafika. Pendo akaanza
kucheka. “Kweli mpenzi wangu ameamua kuoa jamani!” Sabrina akacheka wakati
wakiegesha gari. Waliwahi dakika 20 kabla ya miahadi na mchungaji, kwa hiyo
hata mchungaji hakuwa amefika bado. “Acha nikamchokoze wakati wewe unasubiria
hapa.” “Msalimie.” Pendo akaegesha gari vizuri na kushuka, akamuacha Sabrina
amepoa garini.
Baada ya muda kidogo wakaona gari ya
Junior ikiingia. Akaegesha na yeye, kisha akatoka kwenda kumsalimia Pendo na
Willy, akazungumza nao kidogo akamfuata Sabrina pale garini alipokuwa amekaa.
“Niambie shemeji! Umemuacha wapi kaka?” “Babu yake alipokuja kumuona jana
usiku, akampima mapafu, akasema ni wa kupewa jembe akalime uwele. Si wakupakata
tena.” Junior akacheka sana. “Kama mtaalamu Msindai ametoa baraka zake, basi
anastahili kwenda shamba.” Wakacheka kidogo.
“Naomba niingie garini tuzungumze
kidogo.” “Karibu shem.” Junior akapanda garini. “Hapa mlipo wewe na Jack, mimi
na Joy tulishapitishwa. Ila sisi tukasimama, Joy akanivumilia mpaka mama
akaelewa. Ninachotaka kukwambia ni hivi, Jackson anakupenda sana, mnayo ndoa
nzuri mno, usikubali kuipoteza. Na usifikiri ni kwa hili tu, itachukua zaidi ya
hili na mengine mengi mpaka mje kuwa ukurasa mmoja na mama, na pengine pia
mnaweza isije ikatokea mkawa ukurasa mmoja kwa maisha yenu yote, lakini simama
na mumeo.” “Nasimama naye vipi wakati sijui linaloendelea shem!? Mimi nimesikia
jana! JANA! tena kwa bahati mbaya, hata Jack hakuju kama nipo chooni, Jena
aliropoka tu.” Sabrina akalalamika.
“Kwanza nataka ujue hiki anachokifanya
Jackson ni jambo zuri sana. Binafsi natamani angenishirikisha ili nimshauri
vizuri na kumsaidia maandalizi mazuri akajiongezea nafasi kubwa yakushinda!
Lakini imetokea kama ulivyoona. Hakuna jinsi yakubadilisha tena. Sasa hivi yupo
huko, amenipigia kuniomba nikutafute hata kwa simu nijue unaendeleaje kisha
nimjulishe.” Sabrina akaona machozi yanamtoka. “Naweza kuelewa wakati mgumu
alionao yeye Jack, zaidi hofu yakuona ameharibu na anajisikia kama ni msaliti.
Mimi na Jacinta tumeamua kutomwingilia kabisa mpaka mwenyewe azungumze.
Asipolizungumzia, hatutamuuliza wala hatutataka kujua.” Sabrina akanyamaza.
“Kwa sasa, unahitaji kitu chochote?”
“Labda nikuombe msaada wakunirudisha mimi, watoto na mama yangu, Singida. Kama
nilivyomwambia wifi Jacinta, kuna mambo nasimamia. Nikiyaacha sasa hivi, kazi
yote ile mpaka na nyinyi mkaja kutuunga mkono, itakuwa bure kabisa. Naomba
nisaidie hilo tu.” “Unataka kuondoka lini?” “Sitaki Pendo na Willy watoke
kwenye fungate, wakute nyumba yao bado imejaa. Hata yule msichana wao wa kazi
wamempa likizo. Baada ya harusi tu, anakwenda kwao. Na mimi naomba iwe hivyo.
Ikipatikana ndege ya jioni, ningeshukuru.” “Na mshono huo utaweza kusafiri?”
“Kabisa shem. Acha nikatulie nyumbanni na wanangu walipopazoea na patulivu.
Huku kwenye majumba ya watu ni kama wanakuwa kero.” “Basi acha niangalie,
nitakujibu jioni nikija kumuona kaka na dada zake.” “Nashukuru sana.” wakamuona
mchungaji amefika, wakashuka garini. “Acha nimuwahi nizungumze naye.” Junior akaongeza
mwendo kwa haraka akimfuata mchungaji.
“Waziri Msindai!” “Heshima yako mzee
wangu.” Akampa mkono. “Unafanya nini hapa!?” Wengine wakasogea. “Nikuombe tu.
Jackson, mdogo wangu, ndiye msimamizi wa hii harusi. Amebanwa kwenye majukumu
mida hii ameshindwa kufika hapa. Naomba niwepo hapa kwa niaba yake. Nichukue
hekima zote kutoka kwake, kwa makini mpaka na kukurikodi kabisa, kisha
nikamuhamishie yeye. Tafadhali sana mchungaji. Najua sio utaratibu wenyewe, ila
nikuombe tu.” “Haina shida kabisa. Na kama ningejua, tungebadili muda.” “Willy
anataka kuoa. Hilo lakubadili muda tumelitoa kwenye mjadala.” Wakataniana
kidogo, ndipo wakaingia ofisini na kuendeleza ratiba ya siku hiyo.
I |
lipofika
jioni chumba alichopewa Sabrina kikawa kimejaa kelele na vicheko. Joy na wanae
walifika hapo mara baada ya kuwatoa tu shule. Jacinta naye akafika hapo na
kudai wine aliyoagiza. Akawa amekaa akinywa huku wakicheka, Willy naye alitoka
kazini akawepo hapo, na Junior naye akafika hapo. Vicheko vikaendelea wakati Sabrina
amejilaza. Mara na Jack naye akaingia. Binti zake walikuwa wakicheza na Claire,
wote walipomuona ameingia wakanza kilio wakimtaka. “Hapo tena habari
imebadilika. Si mlikuwa mmetulia nyinyi!?” Jacinta akawachokoza lakini hata
hawakumwangalia. Wote wakamsogelea Jack, akawabeba na kuwabusu. “Hata mimi
nimewasi. Mnaendeleaje!” Wote wakambusu kwa pamoja, watu wote wakacheka.
“Haya mabusu ndio nayamisi zaidi.
Haya, mbusuni tena dad!” Wakarudia tena na kujipigia makofi, kila mtu akacheka.
Angalau akakuta mazingira ya hakuna anayemwangalia tofauti, akasogea nao mpaka
pale kitandani. “Vipi Brina?” “Safi tu.” Akajibu Sabrina kwa sauti ya chini
macho kwa watoto wake. “Sasa hayo machozi si mjifute nyinyi wawili!” Wakajifuta
na kushangaza wote. “Kumbe wanaelewa!?” “Wanaelewa sana. Ila tu wamegoma
kuongea. Sasa sijui sababu ya shuguli!” Sabrina akaongeza. “Brayan
anaendeleaje?” Jack akaendelea kuuliza. “Naona huyu mlalaji. Na kelele zote
hizi hajaamka hata kidogo.” “Kunyonya?” “Ukimsogeza kwenye ziwa anafungua mdomo
na kunyonya bila shida.” “Hata chupa yake ni hivyohivyo. Ukimuwekea tu mdomoni,
ananyonya.” Akaongeza mama Sabina. “Afadhali.” Akamalizia Jackson, na kurudisha
macho kwa binti zake.
Stori
zikaendelea na vicheko. Jack kimya na binti zake wakatulia hapo begani kwa baba
yao. Uchangamfu wao ulitegemeana na baba yao. Akiwa amechangamka, na wao
wanachangamka, Jack akitulia, na wao wanatulia. Wakatulia kimya wengine
wakizungumza mpaka bibi yao alipowataka wakale, Jack akatoka nao kwenda
kuwalisha. Sabrina hakuwa hata akimwangalia Jack.
Ilipofika
kwenye saa mbili baada ya wote kumaliza kula Joy akaaga na watoto wake kwa
ajili ya shule kesho. “Kuna watakaolia kuamka hapa kama wasipopata usingizi
wakutosha.” “Ni Claire huyo! Mimi siliagi.” “Sasa kwa nini umtaje ili aanze
kulia hapahapa! Utalia wewe Clei!” “Mimi siliagi
asubuhi. Muongo tu Clei.” Akaanza kulia Claire. Watu wote wakaanza
kucheka. “Umefurahi sasa?” Mama yake akamtisha, Clei akakimbia pembeni. “Basi
mwanangu. Lakini pia naona muda wako wa kulala umeshaanza kupita. Si hata macho
yameanza kuwa ....” “Na machozi.” Akamalizia Clei kwa baba yake nakufanya
wazidi kucheka.
“Hakika
uatalia Clei wewe!” Clei akakimbilia nje, mpaka baba yake akacheka. “Mimi macho hayajajaa machozi mimi!” Hapo Claire
anaongea machozi yapo kifuani. “Njoo mama. Wanakusingizia?” Baba yake
akamuuliza, kidole akapeleka mdomoni akamwendea baba yake akilia. “Kwani dad mimi macho yangu yamejaa machozi?” “Njoo
mama. Mimi nilitaka kusema yamejaa usingizi. Si ndiyo?” Akatingisha kichwa
kukubali. Shangazi yake akawa anacheka mpaka machozi. “Mimi naona kuna wanao
onewa kwa kuwa wakweli.” Akaongea Jacinta kwa sauti ya chini.
“Clei mchokozi, anti. Anapenda kunichokoza tu.”
“Na mimi nimemuona anti. Usilie basi, asije sema kweli macho yako yamejaa
machozi.” Mpaka mama yake akacheka. “Mimi silii
tena.” “Nakujua wewe sio mliaji, Claire wangu.” “Clei
ananisingizia?” Akamuuliza anti wake akiwa amepakatwa na baba yake.
“Nikuulize Claire, kipenzi changu?” Jacinta akamuuliza kwa upendo, akatingisha
kichwa kukubali, kidole mdomoni. “Eti kwani ukiamshwa asubuhi kwenda shule wewe
huwa unalia?” “Kidogo tu, halafu nanyamaza.” Walicheka
wote mpaka Sabrina akashika tumbo asitoneshe mshono. Walicheka sana. “Mimi
naona dad atusindikize kwenye gari, asije akalala hapahapa. Si ndio Claire
mwanangu?” Akamkubalia mama yake kwa kutingisha kichwa, Junior akasimama na
mwanae huku akicheka.
“Sasa
maadamu nishakula hapa, nikifika ni kuoga na kulala, siku imeisha. Nashukuru
Pendo mdogo wangu. Mzazi wewe, kesho tena. Acha na mimi nikalale naona na mimi
macho yameanza kujaa usingizi.” Wakacheka tena. “Basi raha yake Clei ni kumuona
mwenzie analia hivi kila wakati.” “Sasa kaka yao mbona mtulivu sana?” Sabrina
akauliza. “Huwezi kumsikia.” Akaongeza Jacinta akisimama. “Yupo kama baba yao,
ukimya.” “Halafu nahisi anajiona mkubwa sana kwao hawa wawili, hawafuati nyuma
kama hivi unavyomuona Cleiton kutwa nyuma ya Claire mwanangu akitafuta
chakumliza. Halafu anapenda sana kusoma vitabu. Hapo yupo chumbani kwa Willy
amekutana na vitabu huko, ndio maana umemuona amekuja hapa kwa baba yake,
amemuonyesha kile kitabu na kumuuliza kama kinafaa kusoma. Baba yake alipokiangalia
na kukipenda, ndio ukamuona anamnong’oneza Willy, pale alikuwa akimuomba kile
kitabu.” “Kumbe!” “Ndivyo alivyo mwanangu yule. Hapo anakisoma, hatatoka hapo
mpaka amalize au nikamtoe huko. Huwezi kumkuta akimfanyia fujo dada yake.”
“Kwanza hataki kumuona hivi akilia.” Akaongeza Junior kwa mkewe.
“Sasa
starehe ya Cleiton yeye ni mpaka mwenzie alie.” Wakaendelea kucheka. Junior na
Jacinta wakijiandaa kutoka. “Usiku mwema Sabrina. Ulale salama na watoto. Na
mimi naona niondoke nao hawa, tufike nyumbani pamoja.” “Nashukuru shem. Mungu
akubariki. Na Joy asante kwa supu. Nzuri kweli naona mwenzangu Pendo ana kazi
yakuongeza tu!” Wakacheka. Wote wakawa wakiondoka. Willy na Pendo ikabidi
kuwasindikiza, Sabrina akabaki hapo na mtoto wake.
Jack
akarudi ndani kwa haraka. “Jana nilikuja nikakuta mlisha lala.” Sabrina
akatulia tu. “Naona nyumba imejaa sana, mpaka unalala na mama hapahapa!”
akaendelea Jack, Sabrina kimya hata hakuwa akimtizama. Akamuweka sawa mtoto,
akasimama kuelekea chooni. “Vipi maumivu?” “Naendelea vizuri.” Hapo Sabrina
akajibu. Jack akawa anamfuata nyuma. Ikabidi Sabrina asimame na kumgeukia.
“Nakwenda chooni Jack!” “Najua. Ila nakupenda Brina. Mimi sitakusaliti. Na mimi
sio kama Tino.” “Nimebana haja ndogo kwa muda mrefu sana sababu ya wageni.
Naomba nikajisaidie tafadhali.” “Sawa. Ila kaka alinitumia mafundisho yote ya
kanisani, harusi nasimamia mwenyewe.” Ikabidi Sabrina aondoke tu.
Choo
kilikuwa nje tu ya chumba hicho anachotumia na wanae. Jack akaendelea kumfuata
hata Sabrina hakugeuka tena. Akamfuata mpaka chooni, akasimama nje ya choo.
“Kungekuwa na nafasi hapa, leo ningelala hapa. Ila naona nyumba imejaa! Au
tuhamieni wote kule kwa mama?” Jack akaendelea kuzungumza, Sabrina akawa akimsikiliza
kule ndani chooni. “Nimewamisi Brina. Nina hamu na wanangu. Kwa nini tusiende
wote kule kwa mama?” Sabrina kimya, mama yake akisikiliza tu asielewe.
“Brina!”
Sabrina akatoka na kumpita hapo mlangoni. “Basi mimi niondoke na kina Jeiline.
Maana nimeambiwa wanalala chini.” “Usithubutu. Nilipo mimi ndipo na wao
watakuwepo. Hata kama ni sakafuni.” Sabrina akajibu huku akirudi chumbani, Jack
akimfuata nyuma. Pendo na Willy wakarudi ndani. Pendo akapitiliza chumbani kwa
Sabrina, akamkuta na Jack akataka kutoka. “Njoo dada, unisaidie kitu.” Sabrina
akamuwahi kabla hajatoka.
“Nini?”
“Huu mfuko ulioniletea sijaelewa.” “Sasa mwenzio hizo zilikuwa zikinifaa haswa.
Maana nilikuwa nikianza hedhi ni mpaka kwenye mashuka. Basi nikivaa hizo pullup
diaper, nalala bila wasiwasi yakuchafuka. Kwa hiyo jaribisha. Utalala
vizuri.” “Kwani bado unapata hedhi nyingi?” Hakuna aliyemjibu Jack. Sabrina na
Pendo wakaendelea kungalia mfuko. “Nenda ukaoge, ujaribu.” “Kweli nikaoge ndio
nije ninyonyeshe.” “Au turudi hospitalini, Brina.” Jack akaendelea bila kuchoka
akijikomba. Sabrina akachukua taulo na nguo pamoja na mfuko, akarudi bafuni,
Jack naye akamfuata. “Unataka nikusaidie nini, Brina?” “Kunyamaza Jack!” “Mpaka
saa ngapi?” Sabrina akanyamaza. “Brina?” “Nenda kapumzike Jack, tuache wenye
nyumba na wenyewe wapumzike, tafadhali.” “Basi niogeshe watoto ndio niondoke.”
“Bibi yao ameshawaogesha ndio maana unaona wapo kwenye nguo za kulalia.” “Kweli!” “Hii nyumba tunawahi kulala na
hatutaki kelele na wewe unajua Jack. Nenda kwenu.” Pendo akamfukuza.
“Namsubiria
Sabrina.” “Huna haja yakusubiria. Nenda kalale.” Sabrina akajibu. “Haya nenda
ili Willy wangu afunge milango, tulale. Kesho anakwenda kazini kama kawaida.”
“Halafu kaka Junior alinitumia mafundisho yote ya kanisani. Nishayasikiliza na
nimeyafanyia mazoezi.” “Wewe nenda bwana Jack. Unakuwa msumbufu tu. Unakuja
mida watu tunataka kulala!” “Basi acha nimsubirie Brina nimuage.” “Nakusikia
Jack.” “Kesho basi. Nikujie na nini?” “Sihitaji kitu.” “Basi kesho. Mlale salama.
Acha nikaage wanangu. Nahisi wapo chumbani kwa Sifa.” Kimya. Jack akaondoka
bila ya kujibiwa.
Ijumaa.
Siku
ya ijumaa Jackson hakutokea kabisa pale nyumbani wala hakupiga simu. Mida ya
mchana Sabrina na Pendo walikwenda saluni kufanyiwa matengenezo ya nywele,
kucha na uso kwa sababu harusi ilikuwa asubuhi ya siku inayofuata, hawakutaka
kuchelewa kanisani wala kwenye chakula ambako ndipo walipokuwa wamealika wageni
wao wote. Willy alikwenda kazini kama kawaida, likizo yake ilikuwa ikianza
rasmi siku ya jumatatu.
Alirudi
nyumbani wakaanza kusaidiana na mama yake kufungasha sababu ya safari ya kurudi
Singida kesho yake. Mama yake akashindwa kuvumilia, ikabidi kumuuliza Sabrina.
“Nataka tu kujua Sabrina mwanangu. Ni nini kinaendelea kati yako na Jackson? Maana
ulitakiwa ukakae huko kwao kwa uzazi, umerudi hapa na yule mama simuoni wala
mumeo!” Ikabidi Sabrina akae chini amueleze mama yake. “Una maumivu?” “Hata.
Naona nipumzike wakati nakwambia. Kiiuno kinauma.” Sabrina akaweka na nguo za
mtoto pembeni alizokuwa akikunja.
“Jack
ni mtoto wa mama yule wakuambiana siri zile za ndani. Mama yake hataki mtu
yeyote awe karibu na Jack isipokuwa yeye. Jack kunipenda mimi ambaye
nilishamkataa mara nyingi tu na yeye kujua, akaja kunioa wakati nina mimba ya
hawa mapacha, na Jack kunisifia kuliko yeye, kinamuuma yule mama. Haamini kama
ni jambo la kawaida ila natumia nguvu za giza kwa mwanae. Ndio vita hiyo
iliyokuwepo. Na naomba kukwambia tu ukweli mama yangu. Maana nimekuona umesimama
na mimi kwenye ulezi wa watoto wote bila kuchoka. Yule mama ameshindwa kabisa
kupokea hawa watoto wakizungu.” Ikabidi mama Sabina akae sasa.
“Maadamu
umeanzisha haya mazungumzo, acha niulize. Maana nilikuwa sijui naulizaje.”
“Kujibu maswali yako yote na mengine ambayo pengine utashindwa kuniuliza, hawa
watoto nilipata mimba mtaani tu. Baba yao amezaliwa na mama mwenye asili ya
kizungu kama unavyowaona hawa. Hawa ndio wamebeba damu kali ya huko kwa bibi
yao kuliko hata huyo baba yao. Sasa huyo baba yao hakutaka nizae hawa watoto
ila kutoa mimba. Mimi nikaachana naye, nikaamua kutunza hawa watoto yeye akiwa
ameridhika niliitoa mimba maana aliniacha hospitalini akidhani nimetolewa mimba
kumbe nilimuomba daktari tumdanganye. Kufupisha stori, Jack aliniomba anioe na
ujauzito wa hawa kina dada wawili, ndio mama yake anahangaika sasa hivi.”
Sabrina akaendelea.
“Nilimkuta
Jack kule Singida panamshinda. Nikamtia moyo na kuanza kufanya mengi kwa upande
wa mambo ya siasa. Kama unavyomsikia Jack kwenye vyombo vya habari akimshukuru
sana mkewe, bila hila na kwao hivyohivyo, basi yule mama anatafuta na yeye
kuyafuta yote hayo abakie akisifiwa yeye na Jack.” “Mmmh! Sasa atafanyaje?” “Kwanza
kumtenganisha na huyu kaka yake waziri na huyu dada yake unao waona kutwa wapo
hapa kunitembelea. Maana wao wanamshauri tofauti na anavyotaka yeye kummiliki.
Na pili, kumtafutia aina nyingine ya ubunge ambao yeye mama Msindai ndio
atajulikana amemwezesha, apate sifa. Ndio hekaheka unayoona inaendelea, Jack
hayupo, yupo kwenye kinyang’anyiro cha Ubunge wa Afrika Mashariki. Tena kwa
siri wote tulikuwa hatujui.”
“Mbona
jambo la kheri analifanya vibaya!” “Kila mtu anashangaa mama yangu! Sasa
kujibu swali jingine ulilouliza mwanzoni, yule mama hataki hawa watoto wangu wa
kizungu wakaishi pale kwake. Tuliwasikia wakinisema na wanangu kule hospitalini
kuwa hawawataki wakaishi pale kwake, eti wawe wanakuja kunisalimia mimi na Brayan
kwa muda mimi nitakao kuwa pale. Ndio na mimi nikawaambia sitakwenda
tena kwake. Nilipo mimi, ndipo watakapokuwepo wanangu wote!” “Haiwezekani!”
“Hakika mama.” “Sasa Jackson akasemaje?” “Hakuwepo na wala hajui. Hapo alipo
anahasira kwamba nimembadilikia, sikwenda kwao. Ndio maana unamuona
hivyo.” Mama Sabina akazidi kushangaa.
“Sasa
kwa nini na wewe hukumwambia?” “Asante mama.” Pendo akaingia. Sabrina akacheka.
“Da Pendo na wewe umo!” “Mama amekuuliza swali kama la dada Jacinta. Mjibu.”
“Nisikilize vizuri mama yangu. Jack tayari yupo kwenye siri na mama yake. Wapo
kwenye mipango ambayo mama yake amefaulu kumteka moyo mpaka amekubali. Sasa
wameshaanza mchakato, sitaki nikawa sababu ya mimi kuwachonganisha katikati ya
haya yote, akashindwa huko, nikaonekana mimi ndiye niliyeingilia na
kumchanganya. Nimemuomba Jacinta na yeye asiwaingilie kabisa. Tubakie sisi ni
wabaya mpaka hili la Ubunge liishe. Kwani ubaya huwa unajificha mama yangu?
Utakuja kujulikana tu.” “Mimi nakuunga mkono Sabrina. Mahusiano ya mama na
mtoto huwa hayaishi hata iweje. Usijiingize katikati yao. Acha yawashinde
wenyewe.” “Asante kunielewa mama yangu.
“Mwache
yeye akatae wajukuu zangu wa kizungu. Ninavyojivunia mimi!” Pendo na
Sabrina walicheka sana. “Hakika tena. Hata magazetini wanitoe nao. Nawapenda
kweli! Na naona wenzangu kila kukicha wanazidi kuwa wazungu!” Sabrina alicheka
sana. “Basi mimi nilikuwa nikimuomba Mungu siku moja waje waamke weusi.” “Koma
wee!” Mama Sabina akamkemea mwanae kwa mshituko kabisa. Pendo alicheka mpaka
akakaa. “Mama hutaki tena weusi?” Akauliza Pendo akicheka. “Kwani yeye Sabrina
ndiye kawaumba! Asitafute balaa. Muumbaji mwenyewe kataka wazaliwe wazungu, leo
unaomba nini! Si hao wanakuwa bila huyo mama? Watakuwa tu, na lile
alilokusudia Mungu juu yao litatimia.” “Amina mama yangu. Nakushuru. Na
asante.” “Amina.” Na Pendo naye akapokea
neno la baraka wakaendelea kufungasha.
Ilipofika jioni ndugu wakaanza kuingia tena.
Upande wa Pendo na Msindai. Bwana harusi yuko wapi?” Pendo akaanza kucheka.
“Sitaki Nancy.” “Mbona mimi nimeuliza kwa wema tu.” “Kaenda harusini.” Watu
wakaanza kucheka. “Mzee Ngoi kapatikanika!” “Willy katoka kunipigia simu,
anasema kumbe ni harusi ya ukumbini kabisa. Anakaribia kurudi. Anasema kuna
shangwe utafikiri Zelda anaolewa na kijana!” “Waw! Ndugu zake je?” “Anasema
hajawaona mahakamani labda ukumbini hapo baadaye. Ila Willy mwenyewe
nimemlazimisha angalau atokee tu.” “Bora. Mambo mengine ni kuepuka lawama tu.
Mzee kama yule kupiga simu kabisa si jambo dogo.” “Halafu bado ni baba yao.
Hata wafanye nini bado ni baba tu.” Akamalizia baba yao hapo kwa mkewe.
Stori
zikaendelea Jack hakuonekanika na hakuna hata aliyemzungumzia hata kumuulizia
kama alitokea pale. Bado mama Msindai na Jena pia hawakutokea pale, ila mzee Msindai
alifika tena kumwangalia mtoto na Sabrina. Akampakata mtoto na kucheza na
wajukuu zake wengine, kisha akaondoka.
Kumbuka Shuka Kumekuchwa!
M |
zee Msindai
alipoondoka tu Sabina akamsogelea Sabrina na begi dogo alilokwenda kulifuata
kwenye gari wakati Mzee Msindai akiaga, akamkabidhi Sabrina. “Ni nini hii!?”
“Amenipa Tino.” Sabrina alishituka karibia kutupa chini. “Nakushauri upokee tu
Sabrina. Tino ametoka Italy amenitafuta na kunisihi nikukabidhi hili begi kwa
wema tu, si matatizo.” Hapo akavuta
masikio ya kila mtu hapo chumbani kwake ambako walikusanyika na bibi harusi
mwenyewe akiwa amelala na mzazi. “Amesema hakuna haraka. Ila amesema
itakusaidia sana. Hata kama ni baada ya miaka hata mitatu, anashauri ubaki nalo
tu, uje ulifungue na kuona alichoweka humo ndani. Ameahidi hatakusumbua kwa
lolote lile. Ila ameomba upokee hilo begi.” Wala Sabina hakuwa akizungumza kwa
sauti kubwa, ndogo tu kama kunong’ona, lakini kila mtu aliweza kusikia.
“Kuna
leo na kesho mdogo wangu. Akili kumkichwa.” “Kwani wewe umezungumza
naye!?” Sabrina akamuuliza kama anayetaka kujua kama anajua kilichoendelea kati
yake na Tino! “Sana tu. Tena hakunificha
kitu hata kimoja. Mimi mpaka ikabidi kuomba hekima za mama. Tino yupo na hali
mbaya ya majuto kupita kiasi. Anasema ameandika barua kabisa akikiri watoto ni
wako na hakuna atakayekusumbua tena, ila anataka kukusaidia akitambua malezi ya
watoto wawili ni gharama na mengine mengi amesema ameandika vipo humo ndani.
Nia anasema ni kusaidia tu si kukuvuruga. Anasema alifanya kosa ambalo
linamgharimu mno maishani, ila hataki kuendelea kutenda kosa.” Sabrina akabaki
kama amepigwa na butwaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
v
Mungu Wa Sabrina Safari Hii
Anajibuje?
v
Sabrina Ataelewaje
Majibu Ya Mungu Wake Aliyemuomba Kwa Mara Ingine Tena, Akiwa Kwenye Uchungu
Akiwa Hospitalini, Akiwa Na Maumivu Ya Makali Ya Kujifungua Mtoto Kwa Upasuaji Na Kusemwa
Vibaya Na Mama Mkwe Na Wifi, Pamoja Na Jack Aliyemficha?
v
Nini Kitaendelea Kwenye Ndoa
Hii Iliyoingiliwa Na Mama Mkwe Kukiwa Na Ahadi Nzito Ya Mafanikio Kwa Jack?
v
Wakati Jack Akiwa Kwenye
Kinyang’anyiro Cha Ubunge, Tino Arudi Kwa Upya?
Usipitwe Na Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment