Alimkuta
Pendo akimsubiria kwenye gari. “Mtoto yuko wapi!?” “Bado yupo na bibi yake.”
Sabrina akajibu akipanda garini. “Pole Sabrina.” Sabrina akacheka taratibu ila
mpaka usoni alikuwa amebadilika. “Umekunywa dawa za maumivu?” “Haya ni maumivu
ya moyoni dada. Nimetoka kumuomba Mungu anisaidie. Maana naumwa! Kuliko
nitakavyokwambia. Naumwa dada, ni Mungu ndiye aniponye, wala si dawa.”
“Pole sana Sabrina. Pole.” “Nashukuru.” Sabrina akajiegemeza kwenye kiti
akafunga macho, akatulia kabisa. Pendo akavuta pumzi kwa nguvu na kunyamaza.
Kimya.
Baada ya muda Jack akaja na mtoto.
“Huyu mtoto aliandaliwa kila kitu kule kwa mama, Sabrina! Kwa nini hukusema
mapema kuepusha usumbufu usio na sababu wa matayarisho yake? Kwanza pale
nyumbani kwa Pendo hakuna nafasi yakutosha. Nyumba imejaa sasahivi.” Sabrina
kimya kama Pendo. “Kama ni mambo ya Ubunge, sikukwambia kwa nia nzuri tu na
kwanza ni kwa sababu ya kuwa na chaguzi nyingi. Hakuna ubaya kuwa na chaguzi
nyingi.” “Tafadhali ukipata nafasi uniletee nguo zangu na za kaka pale nyumbani
kwa Pendo.” Sabrina akaongea hivyo huku akimpokea mtoto.
“Nashukuru kwa kila kitu Jack.
Kunilipia gharama hapa hospitalini na...” “Mbona unaongea kama hatutakuja
kuonana tena!?” “Naomba nisaidie kufunga mlango, tafadhali.” “Sasa mbona
umemleta mtoto bila kiti chake na wewe Jack!?” Pendo akauliza kwa hasira
kidogo. “Naomba tu twende dada. Natamani kulaza huu mgongo. Kiuno kinauma na
tumbo nalo linakata. Nahisi nimechafuka tena.” “Wewe Sabrina! Tena!?” “Inatoka
kama bomba!” “Si uliniambia usiku kuchwa hakuna iliyotoka?” “Sijui dada! Twende
tu, labda nikitulia itapungua.” “Kwa nini tusimuulize daktari kabla
yakuondoka.” “Nashukuru Jack, ila acha nikawahi wanangu. Twende dada.” Sabrina
akaweka msisitizo, Jack akaweka mfuko wa dawa miguuni na kufunga mlango, Pendo
akaondoa gari, Sabrina akiwa amepakata mtoto wake.
“Kwa nini hukutaka kumwambia ukweli
Jack?! Ungemwambia tu. Maana wenzio watamjaza maneno yasiyo ya kweli mwishowe
wewe utaonekana mbaya.” Wakiwa njiani Pendo akaanza. “Tayari mimi ni mbaya
dada. Historia yangu inajirudia tena. Ilikuwa hivihivi kwa Tino. Tulikuwa na
mipango mizuri sana na Tino. Max alipoona Mungu ametenda, ndipo na yeye
akaingilia ili kujinufaisha yeye binafsi. Sasa ndicho kinachotokea kwa Jack.
Mama yake anatamani sana abakie yeye mwenyewe kwa Jack. Kama ulivyomsikia,
anaumia kuona niliyomfanyia mimi Jack ndio yamekuwa makubwa na kuingia kwenye
historia ya maisha ya Jack halafu yeye hatajwi. Anachotaka kufanya sasa hivi ni
kumfanikisha Jack kwa njia alizobuni yeye, ili abakie yeye ndio amemfanikisha
Jack kwenye aina hiyo ya Ubunge, si ubunnge wa Singida ambako atajulikana ni
Sabrina, si yeye.” “Sabrina! Ujue ni kweli! Wewe umesema. Mama Msindai ni mtu
wakupenda sana sifa.” Akaongeza Pendo kama aliyefunguliwa macho.
“Hata kwenye ile babyshower ya mapacha
wako alitaka kufanya ugomvi, sema wanamuogopa sana Jacinta. Jacinta akawa mkali
na kumwambia waziwazi kabisa kama hawezi, aondoke. Aliumia mambo yalikwenda
vizuri bila yeye kuhusishwa na akakuta kuna wakubwa wengi tuliwaalika siku ile
wakakubali bila hata kumtumia yeye.” “Sasa ndicho kinachompata na kilichotokea
Singida siku wa uzinduzi wa kile chama kwa upya. Dada ule mji ulifurika watu
wazito wenye majina na vyeo ambao hata mimi sikutegemea! Halafu na yeye
hakuhusishwa kuombwa akaribishe mtu hata mmoja. Yaani akaja kukutana nao pale
kwenye shuguli. Mambo yaliyotendeka siku ile pale na watu kunitambua na mimi,
hata mwanae pia kusema yote yasingewezekana bila mimi, kinamuuma
sana mama Msindai, ndio maana anahangaika.” “Sabrina wewe umesema kweli!” Pendo
akaendelea kuamini.
“Lakini
dada si mimi. Ni Mungu. Sabrina mimi sina uwezo hata
wakuwa na mtu kama wewe dada!” “Usiseme hivyo Sabrina!” “Mimi sikudanganyi
dada. Najijua mimi ni nani na kile Mungu ananitendea. Sina uwezo wowote ila
Mungu.” “Sasa kwa nini humwambii Jack.” “Hata kidogo. Jack si mtoto mdogo,
dada. Halafu mahusiano ya Jack na mama yake ni ya muda mrefu sana, hayatavunjwa
na mimi kamwe. Sitataka mimi kuingia katikati yao. Mwache Mungu ashughulike
nao. Sijawahi kufanikiwa kwenye kujitetea dada. Tokea mtoto mimi ni mbaya sana
kwenye kujitetea. Sijui ni kwa nini! Tunaweza tukawa tumefanya kosa wote pale
nyumbani, wenzangu wakajitetea na kupona, mimi nikaishia kuingia matatizoni na
wazazi kunichapa kabisa. Nilipongundua huo udhaifu wangu, nikaacha kujitetea
kabisa. Nilipomfahamu Mungu kwa undani, nikamuomba awe mtetezi wangi.” Mpaka
Pendo akaanza kulia.
“Hajawahi kuniacha hata kwenye yale
magumu mno. Huwa ananitetea kimyakimya na kuniinulia msaada mpaka huwa
nashangaa. Tino aliponiacha mjamzito, peke yangu, niliingiwa na hofu kubwa
sana, na nilikuwa na maumivu kama hivi. Nililia dada, na mbaya zaidi
nilijua nilimkosea Mungu. Niliishi na Tino kimapenzi nikiwa nimetoka kufunga na
Mungu kunikutanisha naye. Nilimlilia Mungu kwa toba nikimsihi asiniache, mbona
alinitumia Jack! Huyu Jack nililetewa na Mungu. Wala sitapambana nao, dada.
Nilifanya mengi kwa Jack, si kwa ajili yake. Kama ilivyokuwa kwa Tino, ndivyo
kwa Jack. Nilimtengenezea jina pale Singida, nikiwa najinyima mno na mimba ya
huyu mtoto. Nikifunga na kuomba huku mjamzito, bila kumwambia Jack, mpaka Mungu
akafanikisha kwa kiwango cha juu sana.” “Lakini Jack alisema. Bila wewe
asingejulikana. Kabla ya kuanza kumuhangaikia, alikuwa tayari kurudi huku
mjini.”
“Sasa hicho ndicho kinachomuuma mama Msindai
na kumshangaza mpaka anasema ni uchawi kumbe mwenzie naanzia magotini.”
Hapo akamgusa Pendo. “Huyu simba wa kabila la yuda, dada!” “Si mchezo.” “Acha
dada. Ana mtindo wa kunguruma! Akinguruma mahali, hamtabaki kama ilivyo. Watu wanachanganyikiwa.
Wala si Sabrina. Ingekuwa mimi nisingeumia hivi. Lakini ni yeye ananguruma
dada, mpaka na mimi naumia kwenye masikio ya rohoni! Ila acha dada. Nimetoka
kumwambia pale hospitalini kuwa, amenguruma kupita kiasi, mpaka masikio
yangu ya nafsi yameumia. Yeye ndio aniponye.” “Jamani Sabrina!”
“Kweli dada. Ni yeye tu. Yesu aingilie
kati. Maana kama isingekuwa yeye kujibu kwa MOTO, nani angeona moshi
mkali hivi na kuwafanya watokwe na machozi yasiyo koma!” Pendo akacheka sana.
“Sabrina una maneno!” “Nakwambia kweli dada. Moshi huwa unamtindo wakuumiza
macho mpaka machozi. Ndicho kinachompata mama Msindai. Aliyoyatenda Mungu mpaka
sasa masikio yanawasha, moshi unamuumiza macho yeye na Jena, wanalia bila
kujijua. Namuachia Mungu. Nitanyamaza kimya, nimemsihi mtetezi wangu aanze kazi
yake. Hakika atasimama na kunitetea TENA.” “Nilikuwa nimeumia
Sabrina, lakini umeniinua nafsi yangu mpaka nakuhurumia wewe.” “Hata mimi huku
kuongea hapa kumenifanya nimepata faraja.” Wakaanza kucheka.
“Ila nasikia maumivu dada!” “Acha
kabla hatujafika nyumbani kwenye ile fujo ya wanao, tupate muda wa maombi.
Tumsihi mtuliza bahari, atulize dhoruba ndani yako.” “Niombee na ndoa yangu.
Shetani anataka kupenya.” Pendo akatafuta sehemu wakaegesha gari. Yakaanza
maombi hapo. Wawili hao waliomba zaidi ya nusu saa. Mpaka wanamaliza hapo,
vicheko. “Mama wewe ni muombaji!” “Wewe hujioni?” “Wewe ndio umeniambukiza
Sabrina.” Wakacheka. “Basi najisikia moyo umetulia kabisa mpaka mwili!” “Amen.”
Pendo akatoa gari pale kuelekea kwake wakiwa wanacheka. “Mwanao mtulivu!
Amelala hata hageuki!” “Halafu nahisi amejisaidia. Nitambadilisha nyumbani.”
~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika
nyumbani kwa Pendo na kuwashangaza, zaidi mama yake Sabrina. “Basi mimi nikajua
uzazi huu, ukweni!” “Naona kazi bado unayo wewe bibi wa wajukuu watatu.”
Akajibu tu hivyo Sabrina wakacheka. “Haya mlete kaka.” Mama Sabina kampokea Brayan
kwa furaha zote bila swali la ziada. Wanae wakafurahi sana kumuona mama yao.
Wakaanza kurukaruka. Sabrina akacheka. “Na mimi nilikuwa na hamu na nyinyi!
Mmependeza! Nani amewasuka?” “Nimewavizia wakati wamelala.” “Asante mama.
Wamependeza kweli. Waone na macho yao.” “Kweli wamependeza. Una watoto wazuri
Sabrina!” “Sasa dada Pendo si useme tu wazuri kama mimi!” Wakacheka sana.
“Siamini Sifa! Hata wewe unanipinga!” “Dada mimi nimefurahi kukuona.” “Mmmh!”
Sabrina akaguna na kupitiliza chumbani.
“Pendo dada yangu, naomba uje huku uzungumze na hii timu yangu, wakati naoga.” “Na mimi nakuja kujilaza hapohapo kwenye godoro lao.” “Si upande hapo kitandani tulale wote?” “Sasa si na wao watataka kupanda kitandani wakati kaka naye anataka kulala!” “Hapo kweli. Basi mama mwenye nyumba wewe karibia hapo kwenye godoro.” Wakacheka wakati Pendo na watoto wote wakimfuata Sabrina huko chumbani. Na mama yake akiwa na Brayan wakawa wanaingia ili kumbadilisha. Walipata chumba kimoja hapo kwa pendo. Sabrina na watoto wake wote wakapata chumba kimoja. Mama Sabina ikabidi ahamie chumbani kwa Sifa kwani alikuwa akilala hapo kwenye chumba na watoto wa Sabrina. Willy alikuwa na chumba chake. Pendo ndio anatumia chumba kikubwa humo ndani, master bedroom. Cha mwisho ndio hicho kilijazwa vitu vya watoto watarajiwa wa Pendo. Nyumba ikawa imejaa haswa.
Kwa Msindai.
J |
ioni
Junior, Joy na Jacinta wakaelekea nyumbani kwao moja kwa moja wakijua Sabrina
aliruhusiwa na kuelekea nyumbani kwa wazazi wao. Walimkuta Jena yupo hapo. “Wewe
kazi vipi?” Kaka yao akauliza akikaa. “Nimefika na mimi muda si mrefu.” “Na
hospitalini pia ulikuwepo?” Akauliza Jacinta. “Mbona maswali mengi hivyo!?”
Jacinta akamwangalia na kuelekea kwenye kabati. “Hakuna wine huko. Nimeishiwa
nategemea kesho ndio nikanunue.” “Nilivyo na kiu! Mzazi yuko wapi?” Jacinta akauliza
na kumgeukia Jack aliyekuwa kwenye simu yake.
“Kabadili mawazo, yupo kwa Pendo.”
Akajibu Jack nakufanya wote wamgeukie. “Kwa nini tena!?” “Halafu kama yupo kwa
Pendo kwa nini wewe uko hapa!?” Junior akaongeza swali kutoka kwa Jacinta.
“Kwani kila alipo Sabrina ndipo awepo Jack!?” Akadakia mama Msindai na
kumshangaza kila mmoja mle ndani. “Hebu subiri kwanza mama. Pengine mimi ndio
hamjanielewa. Nauliza hivi, kama Sabrina yupo kwa Pendo, kwa nini Jack
anaonekana yupo hapa?” “Tena anaonekana amekuwepo hapa na pensi yake hiyo
anayoshindia hapa! Kuna nini?” Akaongeza swali Jacinta.
“Wanaumia kuona safari hii wamepitwa.
Hawajui mambo ya Jack. Washazoea wao kuwa washauri wa Jack, wampotoshe vile
wanavyotaka wao. Sasa mtajibeba.” Jena akasimama na pochi yake. “Una uswahili
wewe kama sio daktari! Umejawa maneno maneno ya uchonganishi na ushabiki!
Hujui unaongea nini wala na nani!” Jena akamcheka Jacinta na kuongeza bila
kujibu shutuma zake. “Mmepitwa safari hii. Haya nendeni makwenu, Jack
yupo na mama yake. Hamna wakumuharibu kichwa.” “Unazungumza nini wewe Jena!?”
Akauliza Junior akionyesha hasira na sintofahamu. “Sitaki maneno na wewe
Junior. Mimi nimeletwa na yangu, naondoka. Mambo ya Jack na familia yake, mwacheni
Jackson mwenyewe. Yeye anajua nini chakufanya, acheni kumfuatilia kila wakati
na kumwambia mnachotaka nyinyi afanye.” “Nani huwa anafanya hivyo kama sio
umbea tu?” Akauliza Jacinta.
“Nyinyi wawili. Junior na wewe
Jacinta.” Akajibu mama Msindai, Jena akacheka sana kwa kuwakera. “Mwenye mtoto
amekataa na mtoto wake. Kafanyeni yenu yanayowahusu.” Jena akaongeza na kutoka
akicheka. Junior na Jacinta wakaangaliana. “Hata mkiangaliana, mtanifanya nini
sasa?” Akauliza mama Msindai. “Jamani sisi tunaona tuondoke. Twende Joy mke
wangu.” “Naona na mimi pia niondoke.” “Muwe na usiku mwema.” Akaongeza mama Msindai,
Jack kimya ameinamia simu yake.
Kwa Pendo.
M |
ama Sabina
akashangaa mpaka giza linaingia Jack haonekaniki pale, ila Willy akarudi kutoka
kazini, Pendo amelala kitandani na Sabrina. Willy akacheka. “Sasa hapa timu
imekamilika.” “Umeona eeh! Hapa roho kwatu!” Akajibu Pendo. “Pole na kazi.”
“Asante. Mzee Msindai atapita hapa muda si mrefu kumuona tena mtoto.” “Yule
baba ana upendo jamani!” “Ni daktari wa watoto pia. Hataki kufanyike kosa.”
Willy akajibu. “Lakini pia anao upendo wa kibaba.” “Mtu mzima pia. Hana mambo
ya kitoto. Ila nahisi hata Junior amechukua moyo wake. Mstaarabu sana yule
kaka.” Mama Sabina alikuwa akiwabadilisha nguo wajukuu zake hao wawili ili
walale. Akabaki akisikiliza tu, Sabrina kimya amejilaza na mwanae.
“Vipi na wewe Sabrina?” “Tumbo
lilikuwa likiuma, ila limepoa. Nililala tokea nitoke hospitalini, ndio tumeamka
na Pendo sasa hivi.” “Sasa mtoto! Mtamuua mtoto kwa njaa nyinyi wawili.” Pendo
na Sabrina wakacheka. “Huyu Sabrina anabaraka ya maziwa. Yanamwagika kama bomba!
Alikamua na kumuachia mama. Ndio akawa anayatumia kumpa mtoto wakati tumelala.
Halafu mwanae mpole kweli. Si mlizi.” Wakati wanazungumza wakasikia sauti ya
Mzee Msindai. “Ngoja nikamkaribishe.” Willy akasimama na kutoka.
Baada ya muda wakaingia hapo ndani na
kuanza kutania watoto kwanza. Aliwajulia watoto, mpaka kina Jeiline wakawa
wanamchekea. Na yeye akapewa mabusu. “Hapo sasa roho imeridhika. Mbona
mnapendeza usiku huu?” Wakajipigia makofi wakicheka. “Mwambieni babu urembo huu
ni wakitandani!” Akajibu bibi yao. “Kweli nyinyi ni warembo! Hapo ndio
mnakwenda kulala?” Wakajipigia tena makofi, Pendo na Sabrina wakazidi kucheka.
“Hiyo ndio kazi yao hao. Kupiga tu makofi. Karibu baba.” “Kaka yao
anaendeleaje?” “Mlalaji kweli!” “Acha nimwangalie kidogo.” “Nashukuru baba
yangu.” “Karibu Mzee Msindai.” Pendo akamkaribisha akimpisha hapo kitandani.
“Sasa na wewe Pendo unapata usingizi wa mchana au usiku.” Pendo akacheka.
“Nishapata wa mchana, hapohapo, wa usiku naenda kuupata chumbani kwangu.”
Wakataniana kidogo na Msindai, wakamuona anaanza kumpima mapafu.
Akatulia akimsikiliza akitumia stethoscope.
“Naona hiki kifua ni cha mkimbiaji kabisa! Apewe jembe akalime.” Wakacheka.
“Nashukuru baba yangu.” “Karibu. Usiwe na wasiwasi kabisa. Huyu naona mzima
kabisa. Baba yao yuko wapi? Simuoni hapa!” “Nilimuacha hospitalini na mama.”
Akajibu tu hivyo Sabrina. “Basi naona kila kitu kinakwenda sawa. Mlale vizuri,
nitakuja kuwaona tena kesho.” “Nashukuru sana baba yangu. Usiku mwema.”
Akacheza kidogo na watoto, wakati Willy anamsindikiza nje, Jack naye akawa
anaingia na mizigo.
“Tuzungumze kidogo hapo nje Jackson.”
“Sawa baba.” Willy akampokea mzigo na kutoka na baba yake. “Pole na kazi baba.”
“Asante. Nilitaka kukushauri uongoze umakinifu kidogo tu. Unafanya vizuri, lakini
kuwa makini zaidi. Ni hilo tu.” Jack alimjua baba yake si mwenye maneno mengi.
“Naamini unaelewa.” “Katika nini? Labda unisaidie kufafanua kidogo.” “Familia
ndio msingi mkubwa wa kila kitu. Nikimaanisha kila kitu. Mafanikio ya
aina yeyote ile, yanaanzia kwenye familia. Ikishashindikana nyumbani, au
familia ikiyumba tu, hakuna mafanikio yeyote yale huwa yanasimama. Hata
kama yatasikika ni makuu sana, kama msingi wa familia ukiwa mbovu, hakuna kinachosimama.”
Akatulia mzee Msindai akimtizama kama kumpa nafasi.
“Sijui kama unanielewa?” “Nakuelewa baba.”
Akajibu Jackson. “Hapo ulipo, Junior alipita lakini kilichomsaidia yeye ni
msingi mzuri, ndio maana mpaka leo unamuona yupo kwenye mafanikio. Hana cha
ajabu sana na watu wengine au mawaziri wengine, lakini msingi wa familia yake ndio
unamuona ametulia vile. Akifanya mambo sahihi, na ufahamu wake upo wazi akiwa
na uwezo mkubwa sana wa kuelewa mambo magumu, hata kuyafanya yaliyo magumu ndio
maana hata wakimtafuta na kosa hawapati, ila siri ipo kwenye msingi.
Pakiwa bado pabichi kabisa, tengeneza msingi mzuri na imara. Ni
hivyo tu. Usiku mwema.” Mzee Msindai akaondoka na kumuacha Jack amesimama hapo
nje akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo
yalishaiva. Alishachukua fomu za kugombea ubunge wa Afrika mashariki kama
alivyoambiwa na mama yake. Kesho yake ndio anatakiwa kwenda kujinadi. Alifanya
kila kitu kama alivyoshauriwa na mama yake akimwambia asubiri asiseme lolote
juu ya hilo mpaka atakapofanikiwa. Alipomwambia hawezi kumficha Sabrina, mama
Msindai akatumia hekima ya kimama kwa kiziwanda wake mpaka Jack akakubali. Ila sababu
kubwa aliyompa mwanae ni kumwambia kutosema kwa haraka ili asimchanganye
Sabrina ambaye amewekeza sana huko Singida. Ahangaike kimyakimya mpaka akipata
ndipo amwambie ili wachague pamoja ila lengo la mama Msindai ni kama
alivyomgundua Sabrina. Ilikuwa ni hila tu.
Sasa
Jackson akabaki akifikiria. Akahisi ameshakosea. Mambo yameshajulikana kabla.
Sabrina amekasirika. Na pia hakupenda kabisa jinsi walivyoachana na kaka yake
pamoja na Jacinta usiku huo nyumbani kwao. Akahisi amekuwa msaliti kwa watu
waliosimama naye kwa kipindi chote hicho! Ghafla akajikuta kwenye kambi ya mama
yake na Jena ambao wote wanajulikana ni wapinzani tokea mwanzo! Baba yake naye
anampa maonyo ya mafumbo lakini alijua wazi ni nini anamaanisha. Asimamie wapi!
Afanye nini! Akawaza Jackson. Mambo yameshafika mbali. Na yeye
ameshashawishika. Ubunge anautaka tena kwa haraka. Na ahadi ya kuupata upo! “Hakika
siwezi kurudi nyuma. Hangaika yote hii itakuwa bure kabisa. Nikishaupata na
Sabrina akaona mafanikio yote haya, lazima yeye mwenyewe ataunga mkono tu!”
Jack akafikia muafaka wa kuendelea. Alisimama hapo nje kwa muda akifikiria,
ndipo akarudi kwenye gari aliyokuwa amekuja nayo na kuchukua mizigo mingine,
akaingia nayo ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliingia
ndani akakuta nyumba imetulia kama kawaida ya nyumbani kwa Pendo. Willy na Pendo walikuwa mezani wakila. Wao
wawili tu. “Karibu Jack.” “Mimi nimeshakula. Sabrina yuko wapi?” “Naona
wamelala na mama yake huko chumbani pamoja na watoto.” Akajibu Willy, Pendo
kimya. “Hiyo mizigo labda uiweke tu hapo, na uitolee maelezo kama yapo.
Vinginevyo Sifa ataiingiza huko chumbani kesho.” “Sabrina amelala muda mrefu?”
“Ndiyo.” Akajibu Pendo akimtizama Jack kama aliyekwisha mkera.
“Na naomba upunguze sauti Jack, watoto
wamelala. Bibi yao amewabembeleza muda si mrefu na yeye anataka kumpumzika.
Alikuwa nao hapa siku nzima kama Sabrina
tu. Ungetaka, ungewahi kuja. Acha kelele.” Pendo akawa mkali kwa Jack.
Jack alibakia akimtizama na kumsikiliza. Pakatulia kwa muda. Willy na Pendo
wakaendelea kula. “Usiku mwema.” Mwishoe Jack akaaga. “Sasa kesho tunatakiwa
kanisani Jack, kwa ajili ya kukutana na mchungaji kwa mara ya mwisho kabla ya
harusi. Nimesikia unamipango mingine ya ubunge kesho hiyohiyo. Sasa
nataka kujua kama utaweza au nitafute mtu mwingine? Maana Sabrina amesema yeye
ataweza, ukishindwa itaeleweka tu. Naweza kumuomba kaka Junior anisimamie
badala yako.” Willy akaongea bila kubembeleza.
“Ni saa ngapi?” “Tuliweka miahadi ya
saa nne na nusu asubuhi.” “Hatuwezi kusogeza?” “Hapana kwakweli. Wa muhimu
alikuwa Sabrina. Pendo alisema nilazima Sabrina, ndio maana tulimuomba
mchungaji isiwe leo ila kesho. Mimi sina ulazima au chaguzi ya mtu
wakunisimamia, nataka kuoa. Kwa hiyo sitaki kumyumbisha tena
mchungaji kwa mara ingine tena. Ni kesho saa nne na nusu asubuhi. Kama
hutaweza, uwe na amani kabisa, uniambie nitafute mtu usiku huu huu nikamilishe
hili swala. Sitaki kuyumbishwa.” “Sikuwa najua Willy, ningejipanga! Muda huo
nitakuwa kwenye..” “Kama nakuelewa sawasawa ni kwamba kwa muda huo hutaweza? Ndiyo
au hapana. Nijibu kwa ufupi tu ili tujaribu kuokoa hili swala, nisikwame
kwa ajili ya msimamizi.” Jack akawa kama amebanwa.
“Nafikiri
mchungaji ataelewa kwa kutokufika kwangu kwa kesho tu. Ila jumamosi
nitakuwepo.” “Wewe unataka kunikwamisha Jack na maswala yako ya sirisiri.
Mimi katika hili sitayumbishwa aisee. Najua ninachotaka, na si siri.
Nilikupigia muda mrefu tu kukuomba, ukakubali. Huu ujuaji unaotaka kuuweka
mpaka kanisani kusema mchungaji ataelewa, hapo nikutaka jambo langu likwame
wakati mambo ya siasa mimi nayajua. Nyinyi wanasiasa huwa mnaongea chochote
hata kama mnajua kabisa si kweli, ilimradi tu kufanikisha mambo yenu. Sasa hapa
unataka kunipiga siasa mimi, nikae nikijua na sisi tumepatana katika hili kumbe
mwenzetu unamipango yako mingine ya siasa.” “Hakuna jingine Willy! Mbona hivyo!?”
“Acha kuniuliza kama hujielewi
Jackson. Swala la harusi yangu kuwa ni jumamosi wewe ulilifahamu tokea lini?” Kimya.
“Zaidi ya majuma mawili! Kila anayenihusu alifahamu likawa wazi. Nikawauliza
kabisa kama mtaweza. Sabrina akakubali, na wewe ukakubali. Wewe swala lako la huu
ubunge ulilijua lini? Kinachoendelea kesho si chakushitukizwa kwako ila
kwetu sisi uliyetukubalia! Huwezi ukaniletea siasa kwenye ndoa ninayoitaka
Jack. Sio hapa, na si katika hili. Tafadhali nikushukuru tu, nitatafuta mtu
mwingine. Wewe endelea tu. Acha nipige simu mbili tatu kuona mtu mwenye
utayari.” “Mimi nipo tayari Willy. Acha hasira. Nitasimamia harusi yenu.” Willy
akacheka akivuta simu yake.
“Nakushukuru muheshimiwa Jackson Msindai,
lakini hapana. Mimi siasa nazijua kaka. Huwa hazinaga macho. Haziangalii
utu wala mtu, ni kufanikisha maswala ya siasa kwanza, mengine baadaye. Mimi nilishaharibu,
nimepata neema, acha niitumie. Wewe kila la kheri Muheshimiwa. Ila
katika hili ulilokwisha onyesha mashaka hata yakuwepo kesho kwa muda wetu, hapana.
Hutanisimamia tena. Ila karibu harusini kama utakuwa na nafasi. Ibada ni saa
nne asubuhi pale kanisani. Tukitoka hapo tunakwenda kwenye kupiga picha.
Chakula cha mchana tutakuwa hotelini na ndugu wa Pendo, pamoja na Jacinta,
Sabrina na watoto wake, na familia ya kaka Junior. Ukiweza karibu. Ukishindwa
sisi wote waelewa tu. Siasa si ngeni kwetu. Wote tunajua ni mchezo mchafu.”
Jack akacheka na kutingisha kichwa. Pendo akasimama na kuondoka kabisa pale
mezani. “Wapi tena?” Willy akamuuliza. “Naenda kuoga. Nijilaze. Si utakuja.”
“Nikimaliza kufunga milango baada ya Jack kuondoka.” Jack akajua ndio
anafukuzwa. Akashangaa sana vile anavyogeukwa.
“Isingekuwa hiyo ratiba ya kesho,
hakika ningekuwepo kanisani Willy. Naomba usinielewe vibaya. Na ujue wazi
jumamosi hakuna kitakachoharibika. Nitakuwepo.” “Kama mgeni, karibu. Ila
si kama msimamizi wangu. Umeshindwa kesho, inatosha. Wale wasimamizi wetu wa ndoa
ya kwanza nao walianza dalili kama hivi wewe, nikawafumbia macho, mwishoe
wakaja kuwa tatizo kwenye ndoa yetu. Sasa wewe endelea tu. Nashukuru kwa maneno
yako ya utayari.” Jack akaona aondoke. Ni kweli alikuwa kwenye wakati mgumu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment