Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 48. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 48.

Sabrina akaona Pendo ameingiwa hofu, asijue mama yake mkwe ndio zaidi. Akamfariji Pendo bila hila. “Tutaomba dada. Usitie shaka. Bibilia inasema, ‘hakuna silaha itakayoinuka juu yetu ikafanikiwa!” “Ndio maana nampenda Sabrina wangu. Sasa na wewe toka hapo ili ukanisimamie harusi bwana!” Wote wakaanza kucheka upya.

“Naona hatutoki hapa bwana! Kaka mwenyewe ana kazi ya kula tu hapa! Wala simuoni mwenye tatizo la mapafu mimi! Akija mzee Msindai, naomba mama Msindai muwekee msisitizo kesho tuondokeni hapa.” Wote wakacheka lakini si mama Msindai akawa kama amepotea kabisa pale kimawazo. Kimya. “Hata mimi nishachoka dada. Namisi vile vicheko vya wale kina dada, kesho lazima tutoke hapa.” “Na mabusu.” Akaongeza mama K. “Maana na mimi mwenyewe nikipita kuwaangalia na bibi yao, nagawiwa mabusu na kupigiwa makofi.” Akaongeza mama K. Wakacheka, hawana habari. “Na Jack naye ana kazi ya kwenda kuyafuata, na kuja kuniringishia hapa. Mimi naona nitoke tu hapa, nikalee wanangu wanne.” Wakacheka zaidi. “Unamaanisha wa nne na Jack?” “Yeye ndio zaidi. Naona huyu Brayan atakuwa na nafuu kuliko hiyo timu ya watu watatu!” Sabrina akawafanya waendelee kucheka lakini akaaanza kugundua ukimya wa gafla wa mama Msindai, akashindwa kuelewa ila stori zikaendelea.

Siku ya Kuruhusiwa Hospitalini.

Jumatano.

K

wa juhudi alizozionyesha mama Msindai hapo hospitalini, kila mtu alijua Sabrina akitoka hapo anakwenda nyumbani kwake. Alikuwepo hapo hospitalini na Sabrina bila kuchoka wala hakuona aibu kana kwamba ndio mtoto wao wa kwanza. Alijaa hapo akiongoza mambo, ilimradi kila mtu ajue yeye ndio muhusika. “Chumba kilishaandaliwa kabisa. Eti baba! Msindai mwenyewe wewe! Ushaandaliwa mji wako!” Sabrina akamwangalia Jack, Jack akatabasamu tu. Lakini Sabrina alijua ni jambo analolihitaji sana Jack. Wawepo nyumbani kwao kwa muda huo. “Sasa ugeni huu mbona anatajwa mtoto mmoja tu! Wale mabinti zangu je!?” Akajiuliza Sabrina wakati akimtizama mama Msindai na mjukuu wake. Na alikuwa akimvalisha nguo zake yeye tu. Kila kitu alichovaa huyo mjukuu, kilitoka kwa bibi yake. Sabrina akatulia tu akijitizamia.

          Tayari zilishapita siku tatu tokea afanyiwe upasuaji. Na kwakuwa alijua Pendo naye anamsubiria, ikabidi kujikaza kuweza kutembea vizuri. Walikuwa wakizunguka na Pendo muda wote kufanya mazoezi ya kutembea huku wakizungumza mambo yao yasiyoisha. Walishajikuta wameshikana haswa kana kwamba wapo rika moja na ni marafiki wa muda mrefu.

          Siku hiyo ya nne mama Msindai akaweka msisitizo kwa mumewe mpaka wakaruhusiwa. Sabrina kimya akitaka kujua kitakachoendelea ila hakuwa na furaha kabisa kwenda kwa mama Msindai. Kwanza alimuogopa sana huyo mama alimuona ni kama hajamfungulia moyo wake ila kujitahidi tu tena mbele za watu si wanapokuwa peke yao. Na alishaonyesha wazi mtoto aliyeandaliwa chumba ni huyo Brayan tu. Sabrina akabaki akiwaza wale wazungu wake, na fujo zao huko ukweni!

Jena alipoingia hapo wodini, chumba alichokuwepo amelazwa Sabrina, alisema anapita tu siku hiyo hatakaa sana, yupo kazini. Alimkuta Pendo, mama Msindai, Sabrina na mtoto. Kwa kuwa Jena na yeye ni daktari wa watoto, akataka kumtizama tena mtoto kabla hajaondoka. “Namvua nguo zote. Ili kumtizama vizuri.” “Kama ndio hivyo namuandalia maji kabisa ili nimuogeshe. Baba yake akimaliza kulipia, tunaondoka tu.” Akajibu mama Msindai kwa shangwe zote. Sabrina akaona yeye na Pendo wakatembee kupata mazoezi wakati wao wakiendelea na mtoto. Wakatoka hapo na kuwaacha wao wawili na mtoto. Watu wote walijua Jena na mama yake wapo karibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mtakuwa kwa mkweo kwa muda gani?” Pendo akauliza walipofika mbali kidogo. “Hata sijui dada. Lakini namuona Jack amefurahi kweli! Sitaki kuanza kumuuliza maswali yakuondoka wakati hata bado sijafika!” “Wewe usiwe na wasiwasi. Una Jacinta na Junior upande wako, tena wote hao wanasikilizwa sana kwao, wa kali na wanamsimamo, utakuwa sawa tu.” “Tatizo ni pale nitakapotakiwa kubaki na huyo mama peke yetu, siku nzima! Hayupo hivyo unavyomuona hapo tukiwa tunabaki wawili tu. Sina jinsi yakumuelezea, lakini moyo wake si mzuri kwangu.” “Jack si yupo! Na mimi nitakuwa nikija kila siku asubuhi. Nalala hapo mpaka Willy akija kunichukua jioni. Hamtakuwa peke yenu kwa muda mrefu.”

          “Kweli dada?!” “Kabisa. Na hivi sina tatizo lolote!” Wakacheka. “Kweli Mungu mkubwa Sabrina! Vimbe zimesalimu amri!” “Wewe usifanye mchezo na Mungu anapotaka kujipatia utukufu! Mbona anagawanya bahari mbele ya kila jicho ili wamjue kama yeye yupo! Sasa amefanya njia humo tumboni ili mapacha wake wapite, watoke watu washuhudie ukuu wake! Usifanye mchezo wewe!” Wakafurahia kwa pamoja, wakati wakizunguka kwa  mara ya mwisho wakati Jack akimalizia kulipia hapo hospitalini. Wakazunguka kidogo, wakaamua kurudi.

Moyo Wa Mtu Msitu.

W

alipokaribia chumbani wakasikia wakicheka kwa sauti ya chini. “Mama!” “Hakika! Asiniletee upuuzi mimi!” Jena akasikika tena akicheka kama asiyetaka kusikika. “Sasa unawachukua na wale watoto wakizungu?” Wakasikia Jena akiuliza tena. Sabrina akamfanyia ishara Pendo anyamaze wasikilize kwanza. “Yaani hapa nawapigia mahesabu jinsi yakuwakwepa.” Sabrina alishituka nusura akae chini. Akasikia maumivu makali yamepita chini kabisa ya tumbo. Akajishika.

“Wewe niambie mwenyewe nawatolea maelezo gani wale watoto jumamosi jioni watu wakija kwenye hiyo babyshower?!” Jena akacheka kishabiki. “Baba na mama weusi pamoja na mtoto huyu mmoja, wakike wakizungu!” “Hebu niambie! Jack kaenda kulitafuta balaa mpaka kalipata! Na nitalikomesha tu. Wewe subiri.” “Weza kukuta yaliyompata Ngoi na yeye yamempata mama! Watu wanabisha tu.” Pendo akaumia sana. Akamtizama Sabrina.

“Mbona hilo nimelithibitisha Jena! Nimefikiria vile Ngoi alivyokuwa mbishi na msimamo kwenye mambo yake, leo aje ayumbishwe tu na kasichana!” “Eti mama! Yaani mkewe mwenyewe alikuwa akimshindwa, eti gafla Ngoi kawa mjinga kwa mapenzi!” “Sasa mfikirie Jack na mzee Ngoi hali zao, niambie zinatofauti gani?” “Kweli hakuna mama.” Jena akamuunga mkono mama yake. “Sasa na mimi nishaanza mikakati ya kumtoa mwanangu. Wasinichezee akili! Jackson amekuwa kama mjinga jamani! Sabrina! Sabrina! Ukimtizama huyo Sabrina hata mkononi hajai!” “Eti mama jamani! Jack kakataa wanawake wazuri eti sababu yake! Hakika kuna jambo.” “Sasa watanijua kama mimi ndiye niliyebeba miezi 9 au mganga wao. Nimeanza taratibu tena na huyohuyo Junior wanayemuona Mungu mtu! Najua nikimuweka sawa Junior mshauri wao, watafuata tu. Sasa subiri!” Mama Msindai akasikika kupania kwa uchungu.

 “Mmmh!” Wakamsikia mama Msindai akiguna kwa uchungu. “Nini?” “Si Junior huyo! Amemuunganisha Sabrina na marafiki zangu wale wa hali ya juu na vyeo, karibu wote! Tena bila kunitaarifu! Mimi nakuja kuambiwa na wao wenyewe!” “Mama!” “Kweli tena! Junior ameniweza sio mchezo. Sasa sijui na yeye Sabrina kawafanyaje, wana kazi yakunipigia simu kumsifia tu! Huko Singida wanamsifia Sabrina kuwa ndio anafanya mambo, na Jackson naye anasema bila Sabrina yote hayo yasingefanyika na wala asingefika alipo!” “Mama! Jack amesahau jinsi unavyotuhangaikia kweli!” “Nakwambia amesahau kabisa imekuwa ni Sabrina wala si mimi! Sasa ngoja nimtoe Jack huko Sing..” “Lakini mama huyu binti ana kitu bwana! Umeona jinsi alivyombadilisha hata Pendo!” Sabrina na Pendo wakaangaliana.

“Namuona! Pendo amebadilika ameku..” “Subiri kwanza mama. Unakumbuka siku ile ya birthday ya wale watoto wao wakizungu na kuchumbiwa tena kwa Pendo?” “Nakumbuka sana.” “Eti Pendo anasema bila Sabrina asingeshika mimba!” “Nilimsikia na wakakumbatiana!” “Mimi nikajiuliza, hivi huyu Pendo anasahau vipi shida nilizopata naye kwa madaktari mpaka kuacha kazi zangu kuwa naye! Unakumbuka mama mpaka ukaniambia niwe mwangalifu nisije nikashika la mimba ya mwenzangu tu na kazi ikanishinda?” “Nakumbuka. Sasa leo eti ni Sabrina!” “Nakwambia huyu msichana ana kitu, mama. Si bure. Sijui utafanyaje mama yangu!” “Nakwambia nimeshaanza mikakati yangu. Wewe subiri tu.” Mama Msindai akasikika.

          “Nasikia kichomi dada, acha nikajipumzishe kidogo.” Pendo alibadilika mpaka rangi. Ndani wakanyamaza ghafla walipomsikia Sabrina akilalamikia vichomi wasijue walikuwa hapo nje ya mlango kwa muda wakutosha tu. Pendo na Sabrina wakaingia. “Vichomi tena! Au umetembea sana! Pole.” Mama Msindai akamuwahi kwa upendo mara tu walipoingia, kama si yeye. “Nahisi hivyo. Hata hivyo nahisi nimechafuka sana. Acha niingie bafuni nijisafi kidogo. Dada Pendo nisindikize.” Wakapitiliza bafuni. “Pole Sabrina. Pole sana mdogo wangu.” Pendo akanong’ona. Sabrina akabaki amesimama akiwaza. “Badili basi.” Pendo akawa kama anamkumbusha kilichowaingiza hapo upande wa bafuni. Sabrina akajisafisha na kubadili.

Majembe Yamegongana.

Wakati wanataka kutoka  chooni mara wakamsikia Jack amerudi hapo chumbani. “Niambie muheshimiwa wa Bunge la Afrika Mashariki! Mzee wa dola.” “Mshabiki wewe!” Akamsikia Jack akijibu hivyo na kushituka sana. Sabrina akakunja uso na kumwangalia Pendo kama akimuuliza. “Sijui Sabrina!” Sabrina akatoka.

          “Tokea lini wewe Jack ni mbunge wa Afrika Mashariki?” Sabrina akauliza taratibu tu akiwa anapanda kitandani. “Kumbe upo! Nilijua bado mnatembea.” Jack akauliza akionekana kushituka kidogo. “Mumeo yupo kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Afrika ya Mashariki, usahili ushakaribia. Na hivi alivyo maarufu sasa hivi, hata Junior anaamini atapata tu.” Jena akadakia na kuongeza swali kwa Sabrina. “Kwani wewe hujui kama siku zimeshafika!?” Sabrina akashangaa sana.

Akamwangalia Jack. “Sina taarifa hizo! Sijui siku wala huo Ubunge!” “Mama wewe naona safari hii umepitwa! Wenzio mpaka mavazi ya shughuli yakuapishwa akipata huo ubunge, tunayo!” Jena akaongea kishabiki kama kumuumiza Sabrina. “Na kweli naona nimepitwa! Mimi bado nipo na mambo ya Singida kumbe...” “Mambo yanabadilika bwana! Tena nilimshauri Jack baada ya kuzungumza na wakubwa wengi tu. Kwa kuwa ameshajitengenezea jina, kwa asilimia kubwa sana atapata. Anazo sifa zote. Huko Singida ni kutuma tu lori na kuwachukulia mizigo yenu, mrudi mjini. Kilichompeleka huko Jack kishakamilika. Inatosha.” Akaongea mama Msindai macho kwa mjukuu wake akimuweka sawa ili amnyanyue hapo alipokuwa akimvalisha.

          “Eti Pendo mwanangu, utakuwa ukiwaleta wajukuu kila siku asubuhi pale kwangu ili wawe wanakuwa na kaka yao? Wakue pamoja sio mbalimbali.” Sabrina akaumia kama Pendo. “Wala usiwe na wasiwasi. Jackson huyu ndio atakuwa na hiyo kazi ya kukuletea huyu kaka kila utakapomuhitaji.” Sabrina akajibu kwa haraka akiwa ameshakasirika. “Mbona sielewi!? Nani natakiwa kumpeleka wapi!?” “Brayan kwa bibi yake.” Akajibu Sabrina huku akitoka tena kitandani, akavaa viatu.

          “Sijaelewa!” Jack akawa kweli hajaelewa. “Sasa si Brayan atakuwa na bibi yake!?” Akadaki Jena kwa kuhamaki. “Popote nilipo mimi, ndipo watakapokuwepo watoto wangu wote watatu, bila kuachwa wala kufichwa hata mmoja wao, kwa kuwa wote watatu ni watoto niliozaa mimi Sabrina. Ni wangu. Kwa hiyo wakati nikisubiria harusi ya Pendo, nitakuwa na watoto wangu wote pale kwa Pendo, kama mama alivyoshauri hapa, ili WAKUE pamoja. Mkimtaka Brayan, muda na wakati wowote mtampata. Jack, tunaweza kuzungumza hapo nje kidogo?” Sabrina akaanza kutoka.

          “Jamani na mimi nitarudi baada ya muda mfupi kidogo.” Pendo akatoka kwa haraka na kumpita hata Sabrina ambaye alishaanza kuongoza njia. “Hakika haiwezekani! Nilivyojiandaa hivyo!” Mama Msindai akasikika akiongea kwa mshangao mkubwa, Sabrina hakujibu. Akatoka. “Kwani kuna nini!?” Jack akauliza. “Muulize huyo mkeo anayekuwa kigeugeu wakati alishakubali na mama akaingia gharama kubwa za matayarisho. Jack akakunja uso akatoka akiwa na mshangao usoni.

          Hakumkuta Sabrina hapo nje, akajua amekwenda upande mwingine. Akaongeza mwendo kumfuata. Akamkuta anaendelea kwenda. “Vipi tena Brina!? Mbona sielewi?” Sabrina akaendelea kutembea bila hata kugeuka nyuma mpaka alipojiridhisha amefika mbali kabisa, hakuna atakayewasikia. Jack akamkimbilia.

SABRINA AWEKA MSIMAMO WAKE KWA JACK.

          “Nini kinaendelea?! Halafu mbona ni kama upo na maumivu?” “Nimekuomba tuzungumze, lakini nikutaka unisikilize Jackson.” Jack akatulia akimtizama maana kuitwa jina lake zima na Sabrina, si alivyozoea. Akajua amekasirika. Alionekana amejawa hasira na maumivu. “Uliponikuta Moshi kipindi kile, sikuwa pale kwa bahati mbaya. Tuliweka mipango na Tino, tena mipango mizuri tu, yakueleweka. Katikati ya mipango yetu, akatokea Max na mipango mingine kwa Tino. Tino alipopima, akaona ya Max ndio inamanufaa kwake, akaamua kufutilia mbali mipango tuliyokuwa tumeweka pamoja.” Jack Kimya.

          “Hakuniacha tu. Lakini alihakikisha ananiuzia mipango yake mipya na kutaka na mimi niendane nayo. Nikamwambia haiwezi kuwa kwa haraka kiasi hicho, nahitaji muda wa kufikiria kama yeye ili niweze kufikia maamuzi, kama yeye.” Sabrina alikuwa amejawa hasira Jack aliweza kumuona jinsi anavyo tetemeka. “Nilipofikiria, sikuafikiana naye, ndipo akaondoka na kuniacha pale uliponikuta, yeye akarudi huku Dar, akafanya alichoona au alichoshauriwa ni chema kwake, na kweli akafanikiwa kukipata.” “Kweli leo unanifananisha mimi na Tino kwa sababu ya Ubu..” “Tafadhali nimekuomba kuzunngumza, usiniingilie Jackson. Mimi ndiye niliyekuita hapa.” Jack akapoa.

          “Ni nini nataka kukwambia juu ya haya?” Sabrina akaendelea. “Kwa sababu yeyote ile utakayokuwa umekubaliana na ushauri wa mama yako, juwa ni kati yenu nyinyi wawili, usifanye maamuzi kwa familia nzima. Kama nilivyomwambia Tino, na kwambia na wewe pia. Wewe ulishauriwa, ukapata muda wa kutafakari, ukakubali na kuchukua hatua. Ni wewe. Mimi kama Sabrina, nikiwakilisha vichwa vya Jeiline, Keiline na Brayan, peke yangu lakini nikisimama kwa niaba ya hao watu watatu. Namaanisha ninapozungumza na wewe, nawakilisha hao watu watatu, hufanyi maamuzi kwa niaba yetu.” Jack akashituka sana moyoni.

          “Wewe unapofanya maamuzi, popote ulipo, muda wowote, jua unafanya maamuzi kwa niaba yako wewe peke yako. Ila mimi ninapofanya maamuzi, nafanya maamuzi kwa niaba ya watu wanne mpaka hao watu watatu watakapofikisha umri wa kujitegemea! Kwa maana ambayo nataka uelewe leo, jua hivi, endapo tunakaa mimi na wewe tukaamua jambo, hapo ujue ndipo tunapofanya maamuzi ya familia nzima, si vinginevyo.” Ikabidi Jackson aweke mikono mfukoni na kumtizama Sabrina vizuri.

          “Sasa basi, wakati mama yako anapokwenda kufuata mizigo Singida, hakikisha unamwambia achukue ya kwako tu. Yangu na watoto wangu ibakie Singida, kwa kuwa mimi bado sijamalizana na Singida.” “Mpaka lini?” “Mpaka MUNGU atakaponiambia vinginevyo.” Sabrina akamjibu na kumtizama machoni. Wakatulia kidogo wakitizamana, kisha  Sabrina akaendelea.

          “Uliponikuta Moshi, na si kwingineko, ni kwa kuwa Mungu wangu alitaka niwepo pale. Huna utakaponipeleka hata kama ni Ulaya, kama Mungu hayupo na mimi.” “Umekasirika tu Brina, kwa kuwa sikukwambia maswala ya Ubunge wa Afrika Mashariki, lakini ulikuwa tayari kuhamia Dar! Na sikukwambia kwa sababu...” “Nakwenda kuishi kwa Pendo. Nikisema nakwenda, ninamaanisha kama nilivyokwambia, mimi na watoto wangu wote, mpaka harusi ya Pendo itakavyoisha nitakuwa nikirejea Singida. Mkimtaka Brayan, muda na wakati wowote mnaweza kumfuata. Kwa hiyo, kwa kuwa mama yako hajui jibu la hapana, nashauri safari hii tafuta hekima ya kuzungumza naye. Ila naondoka sasa hivi na PENDO.” “Mbona kama unazungumza kwa kufunga mjadala hunipi hata nafasi ya mimi kutoa maamuzi yangu!? Wale watoto wote watatu ni wangu pia!” “Tafadhali naomba usisahau jambo la msingi. Vitu vyangu na wanangu visiondolewe Singida. Nisipovikuta Singida, nitajua natakiwa kuanza upya. SITASUBIRI.” Sabrina akamalizia na kugeuka na kuanza kuondoka.

          “Sabrina!?” Sabrina akamgeukia. “Tafadhali usinifuate Jack. Niache kwa muda.” “Mpaka lini na kwa nini!? Mbona kama unakuza mambo bila sababu!? Unakuwa kama mtu uliyekuwa ukinitafutia sababu tu!” Sabrina akaondoka bila yakujibu. “Kuna dawa za kutuliza maumivu. Rudi ndani unywe.” Sabrina hakugeuka kabisa, akaendelea kutembea kwenda upande mwingine kabisa wa hiyo hospitali.

Pendo  kwa Willy.

Huku kwa Pendo yeye alitoka hapo na kuanza kulia. Akalia Pendo kwa uchungu kisha akampigia simu Willy ambaye alikuwa ofisini. Akalia hapo kwenye simu mwishoe akamsimulia kila kitu Willy. “Haiwezekani Pendo! Jack amegairi Ubunge wa Singida bila kuzungumza na mwezie wakati anajua mwezie alihangaika sana!” “Kazi ya mama yake kama nilivyokwambia.” “Hapana Pendo. Hawa kina mama tunawasingizia tu na kuwapa nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu ambayo hata Mungu aliamuru tuwaache, tukaungane na wake zetu. Sisi wenyewe tunatakiwa kufikiria na kuondokana kwa wazazi kuwa mwili mmoja na wake zetu. Jackson ataharibu nyumba yake vibaya sana. Anitizame mimi!” Pendo akamcheka moyoni akajua yamempata, imekuwa fundisho.

“Ila nimeumia sana aisee!” “Juu ya Jena kukusimanga?” Willy akauliza. “Vyote Willy! Nahisi pia wameamua kumkataa kabisa Sabrina bila yakumpa nafasi jamani! Wanampangia mabaya bila sababu! Na safari hii naona wamefanikiwa kwa Jack.” “Sawa. Sisi tutakuwa watizamaji. Ila nakuomba Pendo utulie bwana. Sitaki mambo ya Pressure tena.” “Acha nikamtafute Sabrina wangu, amesema ataondoka na mimi.” “Huogopi kugombana na mama Msindai?” “Baada ya kumsikia leo kumbe walikuwa wakinisema na mwanae, sijali tena Willy. Wanadamu hata ufanye nini huwezi kuwaridhisha, heri Sabrina huwa anasimama na mimi.” “Ni kweli. Uwe mwangalifu mpenzi wangu.” “Sawa. Kazi njema.” “Ukinihitaji tu, nipigie.” Pendo akacheka na kukata. Akaanza kurudi wodini.

MAMA MKWE NA WIFI

VITA YAKISOMI.

P

endo alifika kwenye chumba alichokuwa amelazwa Sabrina akakuta tena wakimsema vibaya sana Sabrina. “Najua hayanihusu, lakini mimi naomba nizungumze jamani.” Pendo akaingilia maneno kati ya Jena na mama yake waliyokuwa wakimrushia Jack kama kumsemelea Sabrina. “Sabrina si kigeugeu!” “Na wewe si utamtetea tu.” “Hapana Jena. Wewe umebeba chuki na Sabrina na umeshindwa kumfungulia mlango moyoni mwako ndio maana unamsema vibaya sana.” “Nimemsema nini na wewe kama sio unafiki tu?” Jack kimya kama asiyeelewa tena.

“Mimi niite vyovyote vile Jena, lakini Mungu wa Sabrina mnayekazana kumuita ni mchawi, anawaweka kweupe! Ila naumia kuona ni kwa nini anaruhusu kuwasikia jamani! Kila mkimsema vibaya, mwenyewe anawasikia. Jamani acheni nyinyi! Mnamtafuta Mungu wa yule bint..” “Subiri kwanza Pendo. Acha kulia tafadhali. Usije ukapandisha pressure, mumeo akatulaumu. Kuna nini tena?” Jack akasimama. “Analia nini sasa na yeye kama si...” “Naomba nyamaza Jena.” Jack akawa mkali. “Anataka kuzusha mambo ya ajabu hapa!” “Unaniuma Jena wewe, basi tu! Kwa nini nyinyi mnashindwa kujifunza kwa yaliyotupata mimi na Willy jamani!” “Ndio tunajifunza na kuchukua hatua.” Mama Msindai akajibu kwa jazba. “Basi Sabrina amewasikia yote.” “Amesikia nini tena?” Jack akauliza.

“Nakuonya Pendo acha uchonganishi wewe mtoto! Kama yalishindikana kwako, uache kwetu.” Mama Msindai akawa kama anamtisha asiseme. “Acha maneno ya uchonganishi na uzushi kwenye familia zisizokuhusu. Angalia ya kwako ambayo hata hayajakaa sawa, unarukia ya kina Msindai, utayaweza wapi!” “Sawa  mama Msindai. Mimi nanyamaza ila ujue Sabrina amewasikia na ndio maana amegairi kuja kwako wala si kigeugeu maana alipanga sana kuja kuishi kwako bila shida.” “Juu ya nini?!” Jack akazidi kuuliza. “Anaumia huyo mkeo kuona amepitwa kwa habari za Ubunge. Sisi wote tunajua, yeye hajui ndio ametuziria! Yeye alitegemea...” Sabrina akaingia. Wakanyamaza.

“Dada, naomba twende nikapumzike.” “Na usisahau hata huyo Pendo ni sisi tumekutambulisha.” Sabrina akamgeukia Jena. “Unasema nini Jena? Samahani sijakusikia.” “Nakwambia hivyo unavyokataa kwenda kwa mama unakimbilia nyumbani kwa Pendo kana kwamba na sisi Pendo hatuhusu!” Sabrina akabaki akimtizama na kukunja uso. “Sijaelewa.” “Kwamba isingekuwa sisi, na huyo Pendo usingemfahamu.” “Ni kweli kabisa.” Sabrina akajibu hivyo na kuendelea kufuata vitu vyake.

“Nisaidie kubeba hili kapu dada. Mimi nitabeba mtoto.” “Tunaweza kuzungumza Sabrina?” “Naomba isiwe sasa hivi tafadhali. Nina maumivu, naomba dada Pendo anipeleke nyumbani kwa wanangu, nikapumzike.” “Ungekunywa dawa.” Sabrina hakumjibu Jack akamsogelea mama Msindai. “Namuomba mtoto, mama.” Sabrina akaongea kwa upole tu. “Hivi unajua nina uwezo wa kukukatalia huyu mtoto na kumwambia Pendo asikukaribishe nyumbani kwake?” Mama Msindai akamuuliza kibabe. “Hapana. Sikuwa nikijua hivyo.” Sabrina akamjibu taratibu tu. “Umeona dharau zake?” Pendo akatoka na kapu bila kujibu lakini kama kumwambia mama Msindai yeye ameamua kumchukua Sabrina hata akipinga.

“Jena, naomba nyamaza tafadhali. Mwache Sabrina. Acha kujibishana naye na kumtupia maneno.” Jack akaingilia. “Anadharau sasa hivi kwa sababu marafiki wa mama wote amewageuza mioyo.” “Unaongea nini wewe!?” Jack akashangaa kidogo, kabla Jena hajajibu akamgeukia Sabrina. “Tangulia kwenye gari nitakuletea mtoto.” Sabrina akatoka kimyakimya. “Ni nini kiliendelea wakati mimi nilipotoka kwenda kulipia? Wewe Jena umezungumza nini tena? Kwanza mimi nilijua tunafuata ushauri wa mama. Mpaka nikichukua fomu na mambo yakikaa sawa ndipo tuwaambie watu ili kupunguza ushindani au vikwazo. Tukishakuwa na chaguzi mbili ndipo kuwaambia watu! Sasa mbona na wewe unazungumza hata kabla mambo yenyewe hayajawa tayari! Nini kinaendelea tena?!” “Weee! Niache kabisa usiniingize kwenye mambo ya ajabu. Mkeo mwenyewe kisirani kakasirika kupitwa kwenye hili. Anataka muendelee kumficha mama mambo yenu, awe anajua yeye tu ili akutawale. Amekasirika ndio maana anaonyesha jeuri yake waziwazi kwetu kwa sababu sasa hivi anafahamiana na watu wakubwa! Hana shukurani hata kidogo. Mama amemuuguza hapa bila kuchoka, yeye...” Sabrina alikuwa akisikiliza nje ya mlango. Akaona aondoke tu. Asijiumize roho yake zaidi maana ni kama Jena alikuwa akificha ukweli kwa kuongea maneno mengi kumchanganya Jack. Akamuacha Jack na ndugu zake.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Katikati Ya Furaha Ya Kupata Mtoto Mwingine tena kwenye familia, Mtoto Anatolewa Hospitalini Akiwa Mzima, Mama Yake Akiwa Hai, Hawana Tatizo Lolote, Mungu Mtenda Miujiza Ameshakamilisha Yake, Na Shetani Naye Amepenyeza Agenda Yake.

Ni Nini Kitaendelea?

Kama Kwa Tino Tu Mizani Iliemea Kwa Max, Tena Kirahisiii, Kwa Jack Na Mama Yake Kipenzi, Je?

Inaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment