“Inabidi
aachwe apumzike.” Nesi akashauri. “Naombeni kuzungumza na Jack. Atakuwa na
wasiwasi sana.” Sabrina akaongea kwa upole. “Ni kweli. Pengine akikuona hivyo
atatulia na yeye. Pole sana Sabrina.” “Asante shem. Nawashukuruni sana.”
“Usijali, tupo pamoja.” Wakampigia video Jack. “Mkeo
anataka kuzungumza na wewe.” “Ameshatoka!?” “Kila kitu kilienda sawa. Ila
anatakiwa kupumzika. Mkizungumza tu, na sisi tutamuacha alale.” “Nawashukuruni sana kuwa naye.” Jack akasikika
akianza kulia. Mama yake kimya. Jacinta akapokea simu. “Baba
wewe mimi unanishangaza! Mwanao huku analia, na baba huko unalia!” Angalau
wakacheka.
“Mbwembwe zote zile za ubaba za asubuhi, zimekwisha kabisa!”
“Nilitamani niwepo bwana!” “Sasa haupo sisi ndio tupo huku. Usiwe na wasiwasi
bwana. Tunashukuru Mungu kaka amekuja salama, mzima, na mama yake huyu hapa
nakupa, yupo salama. Mkeo amejikaza sana mpaka amekufikishia dume lako,
umshukuru sana sio kuendeleza wasiwasi. Hapa ni furaha tu.” “Nashukuru.”
Kidogo Jack akasikika ametilia.
Wakampa
Sabrina simu. Jack akamuona mkewe. “Pole.” “Ni hongera
bwana! Namshukuru Mungu kila kitu kilienda sawa. Ila sijamuona mtoto. Na
wamesema sitamuona leo.” “Kwa nini tena!?” Jack akashituka sana. “Amewekwa kwenye mashine. Wanasema ni kwa uangalizi tusiwe na
wasiwasi.” Jack akanyamaza. “Usiwe na wasiwasi
Jack, baba yuko naye huko. Na hata ungekuwepo wasingekuruhusu kwa sasa kwa kuwa
ndio kama wanaanza matibabu yake. Hata kunyonyesha nimewaulizia hawa waliokuwa
wananihudumia hapa baada ya upasuaji, wamesema siwezi kumnyonyesha sasa hivi
mpaka baada ya masaa 48.” Sabrina
ndio akawa sasa faraja kwa mumewe kila mtu akisikiliza, hayo hata wao walikuwa
hawajui.
“Kwa nini tena jamani!” Jack
akaendelea kulalamika. Wote wakamgeukia mama Msindai. “Sasa nini? Lazima awe na
wasiwasi.” Mama yake akamtetea Jackson. Wote wakacheka kwa masikitiko. Na
Sabrina akacheka na kushika tumbo. “Acha bwana wasiwasi
Jack. Wanasema ni kwa ajili yakutochosha mapafu yake. Wanataka atulie kabisa.
Mengine utamuuliza daktari mwenyewe ukija.” “Afadhali.” Wote wakaitika
kwa pamoja na kucheka. Jena akachukua simu na kumueleza jinsi inavyokuwa kwa
mtoto anayezaliwa na fetal distress. Angalau wote sasa wakaelewa. “Kwa hiyo ni utaratibu mzuri kwa ajili ya mtoto lakini sio
kwamba yupo kwenye hatari.” Jena akamalizia. “Hapo
sawa sasa.” “Nakurudisha kwa mkeo.” Akampa simu Sabrina. “Nasinzia Jack.” “Basi pumzika. Nitakuona karibuni. Pole.”
“Asante. Lakini usiwe na wasiwasi kila kitu kipo sawa.” “Umewasiliana na mama
huko nyumbani na watoto?” “Mama yuko hapa.” Sabrina akajibu taratibu
akiwa anasinzia. “Tena! Sasa watoto wangu wameachwa na
nani!?” “Naomba utulie Jack. Nakupa mama akwambie habari zao. Wazima, hawana
tatizo. Na amewaacha wamelala.” Sabrina akampa simu mama yake.
“Samahani mama yangu, sikujua kama wameachwa peke yao.” “Hawapo peke
yao baba.” Mama Sabrina akajibu akicheka. “Huna
utakachomwambia huyo sasa hivi mkaelewana.” Sabrina akaongea taratibu. Wakacheka.
“Lakini naona kama kuachwa na mtu baki asiyewawezea,
watateseka sana!” Jack akaendelea kulalamika. “Watoto
wenu wanashida na wanakataa watu nyinyi wenyewe mkiwepo. Lakini wale watoto
wanamkubali kila mtu. Mchana Sifa alinisaidia kuwaogesha baada ya kula ugali
wakawa wanambusu tu na kumpigia makofi.” “Ndio kazi yao hiyo. Hawana
jingine wawezalo na cheko lao.” Sabrina akaongeza akiwa amefunga macho.
Wakacheka.
“Hawana shida kabisa. Bora washibe na wawe wasafi. Usiwe na wasiwasi
baba. Na nimewaachia chakula chakutosha, wala hawatapata shida.”
Mama Sabina akaendelea kumtuliza. “Nimemtuma na mama
awapitie pale kuwaangalia kabla hajaja hapa. Usiwe na wasiwasi Jack.”
Pendo akaongeza. “Nashukuruni sana. Labda tu na kupiga
simu sasa hivi kujua wanaendeleaje! Inawezekana walionekana sawa kwa kuwa
walikuwa na wewe mama ambaye wanakufahamu. Sasa wakija kuamka wajikute na watu
wote wageni! Watakuwa, watashituka sana na..” Wote wakacheka.
“Niliwaambia
mimi. Jack hawezi kuridhika hata mumwambie nini! Ni mpaka yeye mwenyewe awepo
hapa. Naomba mumtumie tu namba ya simu ya Sifa tafadhali. Ili apige na kuwaona
sura zao, hapo ndipo atatulia. Lasivyo hakuna lugha mtamwambia mkaelewana.”
“Naona kweli.” Jacinta akaongeza. “Nakutumia Jack. Ila nilimwambia Sifa hata wakianza
kulia tu, anipigie. Na mimi narudi huko sasa hivi kwenda kumtengenezea Sabrina
supu. Nikifika pia nitakupigia mzungumze.” “Nakushukuru Pendo. Asante sana.”
Wakaagana, pakatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
J |
ackson mpaka
anafika Arusha, ilishakuwa usiku, akakosa nafasi ya ndege. Sabrina anaamka
jioni walipomletea supu, swali la kwanza baada ya uchovu na madawa ya usingizi
sasa kuisha akafungua macho kuangaza, Jackson mumewe hayupo, kila mtu yupo.
“Jack yuko wapi?” Wakaangaliana. Jacinta ambaye yuko karibu nao hao wawili kwa
upande wa Msindai akasogea hapo kitandani. “Jack amekosa ndege leo anakuja na
ndege ya kwanza kesho asubuhi.” Hapo hapo Sabrina akajifunika. Hakujua hasira
ilipotokea, akaanza kulia hapo wakwe zake wakimtizama. Alilia Sabrina kama
aliyefiwa. “Labda mumpigie Jack azungumze naye.” Sabrina akapandisha mabega
kukataa. Akaendelea kulia.
“Mimi
naona nitoke hapa, niende nikamuulize dokta hukusu huku kuvimba kwake.” Wote
wakamgeukia Jena kwa mshangao. “Kwani ilikuwa lazima utangaze mpaka umtie hofu!?”
Mama Msindai akamuuliza binti yake huyo daktari kwa mshangao sana. Sabrina
akajifunua kutoka kwenye shuka, akajiangalia vizuri mikono. Kweli alikuwa
amevimba, akazidi kulia. “Nitakufa hata sijamuona
Jack, jamani!” Kilio kikaongezeka. “Umefurahi sasa?” Mama Msindai
akamuuliza tena Jena kwa hasira. “Jamani mama! Mimi nilitaka kusaidia tu.”
“Sasa mbona bado umesimama hapo?” Mama Msindai akamuuliza kwa ukali zaidi, Jena
akaona atoke bila kuongeza neno.
“Mama!”
Mzee Msindai akamsogelea Sabrina. “Usilie kabisa, wala hutakufa kwa hili. Ni
kawaida ya hayo madawa waliyokupa huko chumba cha upasuaji. Wengine inakuwa
hivyo. Mwili wako utarudi kama kawaida. Wamekuwekea maji hayo yanasafisha mwili
wako kutoa sumu yote. Usiogope.” Mzee Msindai akaongea kumtuliza Sabrina
aliyekuwa akilia huko ndani ya shuka. “Hata mimi ilinitokea nilipojifungua
Cleo, Sabrina. Usiogope huwa inatokea. Junior si unakumbuka?” “Nakumbuka. Na
labda kumuhakikishia Sabrina, mumewe atakuwa amefika hapa kwenye mida ya saa
nne asubuhi. Una maumivu yeyote?” Sabrina akaendelea kulia.
“Mtoto sijamuona! Jack mwenyewe simuoni, nimebakiwa na maumivu
tu.” “Umetoka kufanyiwa upasuaji leo mama.
Ukiendelea hivyo vizuri, kesho wakatoa hiyo catherter ukiweza kutembea, utakwenda
kumuona mtoto wako. Wamempa maziwa, ametulia kabisa hana shida.” Hapo Sabrina
akajifuta machozi. “Sasa wanampa maziwa gani?”
Wakacheka kidogo. “Hivi sivyo tulivyopanga na Jack
jamani!” “Kwani nyinyi mlipanga nini?” Ikabidi aulizwe. “Tulipanga tuwe wote wakati najifungua halafu tukate keki
siku hiyo hiyo!” Wote wakaelewa sasa. “Yaani
tulipanga kuwe mpaka na mchukua video ili kupata ukumbusho wa Brayan. Mimi ndio
nilitaka niwe mtu wa kwanza kumnyonyesha Brayan sio maziwa ya kina mama ng’ombe!
Ona sasa hivi tulivyvosambaratika! Mipango yote imebadilika! Angalau hata Jack
angekuwepo!” Sabrina akaendelea kulalamika huku akilia.
“Pole
sana Sabrina. Lakini katika yote, naomba tumshukuru Mungu. Mpo mbali mbali
lakini wote mpo salama. Willy amechukua video ya kila kitu tokea Brayan anatoka
chumba cha upasuliwaji.” “Nilianzia wakati yeye mwenyewe anapelekwa.” Willy
akaongeza. “Umeona sasa. Wewe ulipotoka. Na sasa hivi pia kabla hatujaja hapa
tulikwenda kumuona Brayan. Tumeshindwa tu kumshika, kwa kuwa hatukuruhusiwa.
Lakini amemchukua video vizuri, mwanao amelala, safi. Ukiacha kulia
tutakuonyesha.” “Na bado hakuna kilichoharibika. Akitolewa kwenye hiyo mashine,
tutakata keki hapahapa baba yake, na dada zake wakiwepo. Wapige makofi mpaka
wachoke.” Mama Msindai akaongeza kwa Pendo, angalau Sabrina akatabasamu.
Wengine wakacheka.
“Naomba mnisamehe jamani! Nashukuru kwa kuwa hapa, lakini
nilitegemea Jack angekuwa ameshafika. Natamani angekuwepo hapa.”
Sabrina akaongea kwa upole na kujifuta machozi. “Ni sawa kabisa Sabrina na ni
haki yako mumeo kuwepo hapa. Hata yeye anatamani angekuwepo hapa. Lakini
imetokea gafla, ni mipango ya Mungu. Na uzuri Mungu amekusaidia wewe na mtoto,
mengine yaendelee hivyo hivyo taratibu.” “Halafu mipango yetu si ya Mungu,
Sabrina. Pole.” Sabina akaongeza.
“Mama
naye yuko wapi?” Wote wakacheka. “Mumeo ameomba kwa kubembeleza arudi nyumbani,
akakae na watoto. Naona haamini yeyote na wale wanae.” “Mmh! Yaani Jack jamani!
Naomba tu umsamehe da Pendo. Na ubaya wa Jack hajuagi kunyamazia jambo.” Wote
wakacheka. “Na alikazana huko nyumbani, mpaka ikabidi nimuombe Willy aje
amchukue hapa mama.” “Jamani Jack! Kwamba na wewe ulikuwepo pia pale nyumbani?”
Sabrina akauliza kwa kushangaa. “Si tuliondoka hapa karibu wote kasoro mama
yako na mama Msindai. Ili upumzike. Wengine wakarudi makazini, mimi nikarudi
nyumbani kukupikia. Mumeo akaanza. Mbona hawaamki? Nikamwambia bibi yao amesema
huwa wakila ugali huwa wanalala sana. Akataka awaangalie hivyo walivyolala.”
Watu wakazidi kucheka.
“Nikaenda
na simu mpaka chumbani, ikaanza sasa kazi ya kuwapanga. Mara aseme Jeiline
awekwe hivi, mdogo wake vile.” Sabrina akaanza kucheka. “Ndivyo alivyo Jack
kama hajalaza yeye watoto! Pole dada.” “Sasa kwani hao watoto huwa hawageuki!?”
Mama Msindai akauliza. “Wewe mama hutamuweza Jack.” Sabrina akamalizia. Pendo
akaendelea. “Mimi sikubisha kwani ulishaniambia habari za Jack za kuamka usiku
pia kupanga watoto chumbani kwao.” Wakacheka. “Na nyumbani pia!?” “Hivyo hivyo.
Kila siku usiku lazima aamke akawaangalie. Sasa mimi huwa namwambia wakiamka,
asirudi nao pale chumbani maana huwa wakimuona tu, wanachangamka. Wanataka
waanze kucheza, wakati mimi mwenzie nimeshinda nao siku nzima nataka
kumpumzika. Kwa hiyo namwambia awaache, na kama anaona hawezi akiwaamsha akae
nao huko huko. Lakini kwani utalala! Kunakuwa kama ndio kumekuchwa.” “Na hapo
ndio ikawa hiyo kazi.” Pendo akaendelea.
“Mara
ya kwanza akaridhika. Tukaagana. Niko katikati yakupika, akapiga tena anaomba
nikawatizame tena. Nikakuta watoto wapo vilevile wamelala. Nikajua hajaridhika.
Ila nikaona nimwache nipike. Akapiga mara ya tatu anawaulizia kama hawajaamka
pengine wamepatwa na tatizo. Nikamwambia naenda kuamsha wanae ili wote
tutulie.” Wote wakacheka. “Na yeye akacheka lakini akakubali niwaamshe. Sifa
akabeba mmoja mmoja mpaka sebuleni. Akaanza tena, hawajachangamka!” “Jamani!
Watoto waliotoka kulala!” Sabina akashangaa. “Wewe hujamjua Jack. Anaweza akakupigia
simu mchana, yeye yupo kazini, labda ndio umejipumzisha tu, anakupigia umelala
mchana, anakuamsha ukaangalie watoto wanaocheza. Na yeye awaone.” “Basi kazi
ipo, wanakuwa watatu!” “Mbona yeye ndio watatu, wanne ndio Brayan.” Sabrina
akaongeza wote wakamwangalia mama Msindai. Akacheka.
“Sasa
ndio kazi yakumtaka bibi yao ikaanza. Akaanza fujo sasa. Mwenzie napika, yeye
analalamika. Eti watoto wake huwa hawazubai muda mrefu hivyo, lazima wameingiwa
na hofu. Kwa muda huo wangekuwa wameshanifuata pale jikoni, wamechangamka. Ule
sio uzubaifu wao.” Kila mtu alikuwa akicheka wakati Pendo akisimulia. “Kila nililokuwa
nikimwambia anajibu lake. Akaona simuelewi, akaenda moja kwa moja kwenye shida
yake. Yeye anataka bibi yao ndio awe nao pale.” Kila mtu akacheka. “Namwambia
yupo na Sabrina kule hospitalini, anasema yeye anamjua mkewe, atakuwa sawa tu
na sisi, ila wanae watateseka ugenini. Anaomba bibi yao arudi hapo. Nikamwambia
namtuma Willy atoke ofisini amfuate bibi yao hapa, amrudishe nyumbani ili watu
wote tutulie.” “Hapa napo alishampigia simu bibi yao akajieleza weee. Mimi
nikamnong’oneza hapa huyo bibi yao, nikamwambia maneno hayo yooote juu ya
wanae, anamtaka arudi tu nyumbani, yeye ndio awe nao.” Mama Msindai akafanya
wote wacheke zaidi. Angalau stori zikaendelea, Sabrina akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi
na mapema Sabrina akatolewa kila kitu na kuambiwa anaweza hata kutembea kidogo.
Mama Msindai alirudi kulala naye. Ndugu walipopita asubuhi wakiwa wanawahi
makazini, wakamkuta mama Msindai anampeleka chooni. “Anatembea!” “Naona
mwenyewe ametaka aanze kutembea ili akamuone mtoto wake.” Mama Msindai akajibu.
“Vipi maumivu?” “Naona ni kawaida yale ya kufanyiwa upasuaji. Yapo lakini sio
sana.” Wakasalimia wote asubuhi hiyo kila mtu akawahi majukumu yake. Akabakiwa
na mama Msindai tena peke yao. “Nipeleke nikamuone mwanangu mama.” “Wewe
Sabrina! Sio tungojee kidogo!” “Nitafika mama. Sijui mwanangu hata anafananaje
jamani! Wanampa vitu ambavyo hata sivijui! Baba
yake hayupo na mimi pia nishindwe kwenda kumuona! Acha niende mama.”
“Basi usilie. Twende taratibu tu, naamini tutafika. Na mumeo ameshaondoka
Arusha, anakuja. Mtakuwa pamoja hivi karibu. Na Msindai atakuja tena baadaye
atupe picha kamili ya Brayan.” “Nashukuru mama.
Asante.” Wakaanza safari ya kumfuata mtoto.
Wakatembea
mpaka alipokuwa amewekwa huyo mtoto na vitoto vingine. Sabrina akafurahi sana
kumuona mwanae. “Brayan amezaliwa mkubwa kuliko dada zake! Niombee nimshike
kidogo mama.” Mama Msindai akacheka. Akazungumza na wale manesi, wakamfunika
vizuri mtoto na Sabrina mwenyewe, akamshika Sabrina akafurahi sana, akatafuta
mahali akakaa. Akamshukuru sana Mungu wake huku amemshika. Mama Msindai kimya akimtizama.
Akambusu wee, na kumfunua kidogo. “Kweli anafanana na babu yake!” Wakacheka.
“Msindai amefurahi huyo. Namwambia watoto wanabadilika aache kuniringishia,
ananiambia lakini kwa sasa amemfanana sana.” Wakacheka. “Amekuja kukaa naye
hapa usiku akimwangalia, mpaka tukamwambia akapumzike, sisi tutakuwa naye.”
Muuguzi mmoja akaongeza, wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
kwenye majira ya saa tano na nusu asubuhi, Jack na dada yake Jacinta wakaingia
hapo hospitalini. Sabrina hakujua kama ni furaha au uchungu, akaanza kulia
tena. Akalia hapo mumewe akiwa amemkumbatia mpaka akatulia. “Mbona umevimba
sasa?” “Wamesema nitakuwa sawa tu. Nimefurahi Jack!
Pole.” “Pole na wewe. Nilikuwa nakuhurumia upo peke yako!” “We Jack?”
Mama yake akamuita kwa ukali, akihamaki. Wakacheka. “Kwani sisi sio watu hapa?”
Akauliza mama Msindai. “Mwenzio kalala uwanja wa ndege huyo.” Jacinta
akaongeza. “Jack!” “Sikutaka niende hotelini, halafu nipitiwe na usingizi,
niachwe na ndege ya asubuhi!” “Pole. Ila nimefurahi!”
Wakacheka na Jack akambusu mkewe. “Hongera Brina. Ila kwa jinsi baba
alivyonionyesha picha zake Brayan, heri ulimzaa kwa upasuaji! Mkubwa sana.” Wakacheka
kwa furaha. “Twende wote tukamwangalie.” “Nashauri uoge kwanza Jack. Umekuwa na
safari ndefu, na mtoto bado yupo kwenye uangalizi.” Mama yake akamuwahi.
“Kweli.” Jack akakimbilia hapo bafuni kuoga ili kwenda kumwangalia mtoto wao.
Atafutaye Hachoki,
Jumanne!
K |
atika
hekaheka hizo za hospitalini, maandalizi ya harusi yao, Pendo na William kama
marafiki wa karibu wa Sabrina na Jack, hawakuwa wakikosa hospitalini pia. Siku
ya tatu ambayo mtoto alionyesha nafuu kubwa na ahadi ya kutolewa siku
inayofuata, endapo mambo yasipobadilika kwa mtoto, kwani alishaweza kunyonya
bila shida. Willy na wengine wakiwa ndani ya hicho chumba stori na vicheko
vimekolea mida hiyo ya jioni wafanyakazi wakiwa wametoka kazini na kujikuta
wote hapo hospitalini kumuona Sabrina na mtoto, mzee Ngoi akampigia simu Willy.
Willy akakunja uso na kumtizama Pendo. “Nani?” “Mzee Ngoi huyu! Sijui anataka
nini kwangu!?” Willy akaongea akiitizama simu yake kama aikate tu.
“Msikilize.” Pendo akashauri kwa
utulivu. Willy akamtizama na kupokea. “Shikamoo.”
“Marahaba Willy. Hujambo?” Mpaka Willy akashangaa. “Kuna nini baba!? Maana hapa nipo hospitalini.” “Ni salamu tu
na kukutaka wewe na Pendo mfike nyumbani kuna habari njema.” “Kama
nilivyokwambia, nipo na mgonjwa na maandalizi ya harusi yangu. Tafadhali
niambie tu.” “Nani tena mgonjwa?” Mzee Ngoi akauliza swali
lililomshangaza zaidi Willy. “Ni nini kinaendelea
baba?!” “Nataka kujua tu! Kwani kuna ubaya gani?” “Kwani wewe unamfahamu rafiki
yangu yupi? Kwa nini usiniambie ulichonipigia?” Pendo akamshika kidogo
kama kutaka kumtuliza. “Mimi sielewi!” Willy akamlalamikia Pendo, simu sikioni.
“Taratibu.” Pendo akamsihi.
“Ni habari
njema tu. Si kutaka kukuudhi. Najua hatukuwa kwenye mahusiano mazuri, lakini
naona mama yenu mdogo anaona ni vizuri tuwe na mahusiano kama familia.”
“Subiri kwanza baba. ‘Mama yetu mdogo’ ndio nani!?” Hilo swali la
Willy likavuta masikio ya watu wote pale chumbani ila akasikika mzee Ngoi
akicheka kidogo. “Ndio habari njema nilitaka ukija hapa
na wenzio niwaambie. Ila kwa kuwa upo na mgonjwa na mambo hayo ya harusi kama
alivyoniambia mchungaji, acha tu nikwambie.” Willy kimya akisikiliza.
“Nimeamua
kutekeleza ushauri wa mama yenu. Alinipa baraka zote kumuoa Zelda, naona nitekeleze.”
Willy alishituka nusura kuangusha simu. “Subiri kwanza
baba.” Ikabidi Willy atoke nje maana alivuta masikio ya wote mle ndani,
akahisi atawasumbua. “Ni jambo alilolitaka mama yenu,
ila Chonge naona aliniyumbisha kidogo kwa ushirikina. Naona yamemrudia yeye
mwenyewe, amegeuka mwendawazimu kabisa yule wakuvua nguo mbele za watu.”
“Mungu wangu!” Willy akashituka sana. “Kabisa.
Huwezi kucheza na mipango ya Mungu. Yule msichana alitaka nitelekeze damu
yangu, ili niwe naye! Mabaya yote aliyomfanyia mama yenu mdogo, yamemrud...”
“Tafadhali mwite Zelda tu.” Willy akamkatisha akiwa amejawa mshituko,
hasira na hofu.
“Sasa tulirudi
kwa mchungaji kumuomba atufungishe ndoa kwa
haraka hata kabla yenu ili unapoa uwe na wazazi wote.” “Zelda sio mama
yangu na hatakaa akawa mama yangu. Kwanza sitaki mtu yeyote yule kwenye harusi
yangu. Mnataka...” Willy alikuwa akiongea kwa sauti ya juu akigomba mpaka
ndani wanasikia. “Samahanini jamani. Acha
nikamtulize.” Pendo akasimama na tumbo lake akatoka taratibu akijivuta.
“Naiomba hiyo simu Willy.” Wakamsikia Pendo na sauti yake ya chini na ya
taratibu. “Nakaribia kuitupa mimi!” “Sasa kabla hujaitupa, naiomba mimi.”
Akamkabidhi Pendo kwa hasira.
“Hellow.”
Wakamsikia Pendo. “Ni mimi Pendo. Naomba Willy akupigie
baadaye tukitoka hospitalini.” “Kumbe na wewe upo? Tena Zelda anakushukuru sana
kwa kumsaidia kipindi akiwa kwenye shida. Ameomba usikose kwenye harusi.”
“Naomba tuzungumze baadaye, tafadhali.” Wakamsikia Pendo ametulia.
Wakajua anasikiliza. “Siwezi kuahidi kwa kuwa sijui
itakuwa lini na mimi najiandaa...” “Naomba mumuache Pendo, tafadhali.”
Willy akagomba kwa sauti ya juu na kuchukua simu kutoka kwa Pendo.
“Ni nini
jamani!? Kwa nini mnalazimishia?” “Sitaki mpitwe na kitu cha muhimu kama hiki
na itakuwa kumuenzi mama yenu.” Willy akafunga macho. “Sasa kwa kuwa kanisani wanaka kutangaza kwanza, tumeona
tukafungie tu mahakamani siku ya ijumaa kisha tutakwenda kubariki kanisani
wakiwa tayari na sisi.” “Haraka ya nini jamani!? Mnaharaka gani nyinyi mnaoshindwa
kusubiri kanisani?” Willy akauliza. “Hatutaki
kuendelea kuishi dhambini.” “Kwamba Zelda amesharudi hapo nyumbani!?” “Kabisa,
pamoja na mdogo wenu.” “Hakika natupa hii simu.” “Nipe mimi Willy.”
Pendo akasikika tena.
Willy akampa na kuondoka kabisa pale. “Ni mimi Pendo, tena. Tunashukuru kwa mwaliko.” “Ni ijumaa ya
kabla ya harusi yenu hiyo jumamosi.” Akaongeza mzee Ngoi na kuendelea. “Ndio maana tuliona mfike leo jumanne, tupate upatanisho kwa
familia nzima, ndipo tuanze upya. Hatukuachana vizuri. Hawa ni ndugu, damu
moja. Hakuna jinsi mdogo wao akakua bila ndugu zake.” “Nashukuru sana. Asante kwa mualiko. Willy atakupigia
baadaye. Lakini kwa binafsi yangu sitaweza. Kama ulivyosikia harusi yetu
ni siku ya jumamosi, yaani siku inayofuata baada ya harusi yenu.” “Na Zelda
ameshauri tufanye harusi yetu siku hiyo makusudi kabla yenu ili siku ya harusi
yenu kuwepo na wazazi wakueleweka. Hatutachukua michango. Nitagharamia harusi
yetu, mimi mwenyewe.” Pendo akachoka kabisa baada ya kusikia mzee Ngoi
akizungumza hivyo.
“Lakini mimi nimeshauriwa na daktari nipumzike. Sitaweza shughuli
mfululizo. Harusi yenu na yangu! Sitaweza kwa kweli. Ingekuwa siku zimepishana,
angalau kwa juma moja hapo ingekuwa afadhali ningeweza kuhudhuria harusi yenu.
Lakini hivyo sitaweza. Naomba niwatakie maandalizi mema, mfanikiwe.” “Nashukuru
sana Pendo na umetoa sababu ya msingi sana. Inaeleweka kabisa.” Pendo
akakata na kubaki ameduaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Haya
njoo Pendo utujuze ya ukweni.” “Nancy! Acha bwana. Unataka kumliza bure.” Baba
yake akamuwahi. “Hawezi. Eti Pendo, mdogo wangu? Maana tumesikia kila kitu ila
si kwa undani.” Wote wakaanza kucheka. Pendo akaingia akicheka taratibu. “Jack
naomba kanitafutie Willy wangu. Asije akaenda kujirusha baharini bure!” Jack akacheka
na kutoka. “Haya! Nimesikia umepata mama mkwe mwingine!?” Wote wakacheka.
“Nancy umekazana!” “Dada Jacinta kila familia ina vijimambo, lakini ya Ngoi ni
kiboko! Hutakaa ukaipatia mwenzie. Tangia Pendo ameolewa huko, tunajionea
mambo. Inageuka aina ya viroja kila kukicha! Si misibani si kwenye masherehe,
lazima washangaze uma.” Nancy akaongeza na kufanya wacheke tena.
“Pendo mdogo wangu?” Nancy akaendelea
kusihi akitaka kujua zaidi, watu wakacheka vile anavyobembeleza. Pendo akacheka
kidogo kama anayefikiria. “Ila kwa nilivyomsikia mzee Ngoi! Mmmh!” “Nini?”
“Hayupo sawa bwana. Amekuwa kama sio yule Ngoi mkorofi! Sijawahi muona Ngoi
huyu! Mnyenyekevu na mvumilivu mpaka akamaliza ujumbe wake kama aliyesimamiwa
lazima aseme! Sasa najiuliza, Ngoi ni wakulazimishwa kusema jambo kweli!”
“Mkewe mwenyewe alikuwa anamshindwa!” “Sawasawa Nancy. Huyu baba ameshindikana
kila mahali! Mchungaji mwenyewe alituambia walimnyanyulia mikono hata pale
kanisani! Walimshindwa yule! Halafu alimfukuza vibaya sana Zelda. Ghafla Zelda
amerudi na ndoa juu! Tena ya haraka hivyo, na mwenzie aliyekuwa aolewe na Ngoi
kawa kichaa jamani!” “Haaa!” Hapo kila
mmoja akahamaki nakutaka kujua zaidi.
“Kweli! Yaani Chonge alifanikiwa
kuteka moyo wa Ngoi mpaka kumfukuza Zelda na mtoto kabisa!” “Kisa nini?” “Mmmh!
Yaani mama Msindai, ndio utachoka kabisa. Mambo ya ushirikina.” Pendo
akawasilimulia kwa ufupi, wote wakajua lipo jambo kwa hakika. “Basi safari hii
uchawi umempata. Atulie na yeye yule mzee! Khaa!” “Nashauri Nancy na wewe
utulie.” Wote wakacheka. “Sawa baba. Maana ni baba yake mkwe Pendo?” Nancy akamuuliza
baba yake kishabiki. “Wameambiwa na mama mdogo anakuja.” Wote wakacheka. “Mama
K na wewe kumbe umo! Umetulia hapo kimya kumbe unasikiliza! Haya baba, mama
naye kasikia.” Nancy akafanya wazidi kucheka lakini kumbe wameamsha wasiwasi na hofu kubwa kwa mama Msindai,
wasijue.
“Ila
naona Willy hataki tena!” Nancy akaongeza, Pendo akacheka mpaka machozi. Wote
wakaanza kucheka tena kwa sauti ya kimyakimya ili Willy mwenyewe asije kuwasikia.
“Nancy mshabiki wewe! Mwache mpenzi wangu!” Pendo akaendelea kucheka. “Sasa
wewe nawe umkazanie maombi. Maana hao watu wanaonekana sio wazuri. Umesikia
Pendo?” “Kweli mama!” “Haya! Wewe cheka tu. Kama wamemuweza Ngoi, ujue...”
“Bwana mama!” “Mimi nakutahadharisha. Vita imeanza.”
~~~~~~~~~~~~~~~~
- v Zelda Amerudi Enzini, Akitaka
Undugu Na Watoto Wa Ngoi. Nani Atakuwa Upande Wake Nani Atakua Kinyume Naye? Na
Je, Atakayekuwa Kinyume Naye Kama Chonge, Ambaye Amegeuka Mwendawizimu,
Kitampata Kipi? Nini Kilitokea Na Nini Kitaendelea Kwa Familia Hiyo Ya Ngoi Iliyoachwa
Na Mama Ngoi Mikononi Mwa Zelda?
- v Kile Alichodhania Amefanyiwa
Mwanae, Jack, Wanakithibitisha Kwa Mzee Ngoi Na Kuinua Wasiwasi Mkubwa Na Hofu Kwa Mama Msindai. Nini Kitatokea Katikati Ya Furaha
Kubwa Hivyo?
v
Bado Shetani Yupo Kazini.
o
Usikose Muendelezo….
0 Comments:
Post a Comment