Jack
alikuwa na wasiwasi, hakutaka baba yake akate simu. “Nitakutaarifu
tukifika hospitalini Jackson. Lakini usiwe na wasiwasi, wataweza kuishusha tu.”
“Tafadhali usikate simu baba.” “Sasa nitawasiliana vipi na madaktari wengine
ili kumsaidia mkeo, Jackson?” “Weka comference call.” Baba yake akajua
amepaniki. “Nisikilize Jackson. Haitasaidia ila
utaongeza hali ya wasiwasi hapa. Madaktari wote wataongea lugha za kidaktari
hata ukiwa kwenye simu hutaelewa. Naomba utulie, tutakuta...” Mzee
Msindai akaona simu imekatwa. Kabla hajamwambia mkewe, akaona simu ya mkewe
inaita. “Mwanao huyu hapa, amehamia kwangu!” Mama Msindai akaongea akiitizama
simu yake. “Sasa leo hakuna kitakachofanyika ila kumtuliza yeye!” “Wewe mwambie
atulie, bwana Jackson! Mkewe na mtoto watakuwa sawa!” Baba yake akaanza kupiga
simu kuomba msaada wa haraka kwa madaktari aliojuwa ni wazuri na hawapo kazini.
“Mama!” “Jackson, baba yako anahangaika kutafuta madaktari wa
kukutana na Sabrina huko hospitalini. Ameondoka hapa na gari ya wagonjwa ya
usalama, anapelekwa usalama wa taifa ambako atakuwa ni yeye tu na madaktari.
Ameshawekewa dripu, nina uhakika mpaka tunafika hospitalini Sabrina atakuwa
yupo sawa. Ni pressure ndiyo ipo juu baba.” Mama yake
akajaribu kumtuliza. “Wewe usikate simu. Mimi narudi
nyumbani kujiandaa. Naomba niombee kwa kaka, tiketi ya ndege yakuondoka leo
huku.” “Nisikilize Jack. Umepaniki, na sidhani
kama ni sawa kuendesha hata kurudi nyumbani.” “Mama! HUU SIO WAKATI
WAKUNIFIKIRIA MIMI ILA HALI YA MTOTO WANGU NA SABRINA. NAONDOKA SASA HIVI.”
Jack akagomba mpaka mama yake akaweka simu pembeni akawa anasikiliza simu akiwa
ameishika mkononi wala si sikioni. “Mama!” “Nimeelewa
baba. Nampigia simu sasa hivi Junior akutafutie usafiri wa kukuleta leo Dar.
Ila naomba taratibu huko njiani Jack.” Simu ikakatwa. “Leo kazi ipo.”
Akaongea mama Msindai.
Akimpigi
simu Junior. “Junior baba, naomba msaidie Jack afike
Dar leo. Lasivyo hakuna kitakachofanyika leo ila kujibu simu zake tu.” “Na simu
yake hiyo inaingia hapa kwangu. Ananipigia sasa hivi.” “Kila la kheri!
Anawasiwasi sana.” “Na mimi nipo njiani nakuja huko hospitalini, Jacinta
ameniambia.” Wakaagana, ili apokee simu ya Jack. Jacinta ndiye aliyekuwa
ni mfanyakazi wa usalama wa taifa, tena kiongozi aliyeshika wadhifa wa juu
sana, na Mzee Msindai ambaye alikuwa daktari hapo kwa muda mrefu akihudumia
watoto na hospitali kuu ya Muhimbili pia, mpaka akastaafu na kufungua hospitali
yake mwenyewe.
Sabrina Hospitalini.
S |
abrina
alifikishwa hospitalini matibabu ya kaanza. Hapakuwa na kitu kigeni sana na
chakutisha ila ni kweli pressure ilikuwa juu. Mzee Msindai alishaomba vipimo
alivyofanyiwa kutoka hospitali ya Muhimbili siku hiyo asubuhi vitumwe hapo ili anayemuhudumia
hapo ajue anamshugulikia mama mjamzito wa namna gani. Akaja huyu akafanya kile
ilimradi Sabrina alikuwa kwenye mikono salama na sahihi.
Hali
ya mtoto ikaonekana sio nzuri, wakaombwa wote watoke nje akabaki mzee Msindai
tu na madaktari wengine ndani ya chumba alichokuwa akihudumiwa Sabrina, kina
Mama Msindai, Jacinta na Pendo wakatoka nje wakisubiria Sabrina ahudumiwe.
Wasiwasi sasa ukawaingia wote baada ya daktari aliyekuwa akiangalia mapigo ya
mtoto kutopata vizuri. Jacinta akaanza. “Huyu Sabrina mbona nilisikia habari
zake masaa machache yaliyopita kutoka kwa mumewe akanitumia na picha za mtoto
wao kuwa ni mzima kabisa! Na Jack akasema daktari alimwambia Sabrina mtoto ni
mzima hata amegeuka! Jack akawa ananiringishia kuwa dume lake linataka kuwahi
kutoka kumuona! Imekuaje sasa hivi nasikia madaktari wananong’ona tena kuwa
hawasikii vizuri mapigo ya mtoto?” Jacinta akauliza. Pendo kimya.
“Eti
Pendo, kulitokea nini hapo katikati maana na mimi Sabrina alinitumia picha za
mjukuu, nikampigia akase...” “Na mimi nilikuwepo mama wakati mkizungumza. Si
unakumbuka ulitutania tunashindana matumbo?” Pendo akaongea akionekana
ameingiwa na yeye na wasiwasi. “Hakika Jackson atachanganyikiwa chochote
kikitokea kwa huyo mtoto. Mimi mwenyewe nahisi nita...” “Mama tulia bwana.
Akija hapa Jack na kuona wewe umepaniki ndio atapaniki mara mbili.” “Junior
amempatia usafiri?” “Niliona kuna ndege Dodoma. Kuna mkubwa anarudi huku jioni
hii. Junior amemwambia apitie Dodoma, watakuja naye.” “Sasa atapata ndege
yakumtoa Singida mpaka Dodoma kweli?” “Junior ameshugulikia kila kitu mama. Na
mimi nikisaidia kwa kadiri ya uwezo wangu. Naomba utulie, Jack atakuwepo hapa
kabla ya saa 11 jioni.” “Na hizo foleni za uwanja wa ndege mpaka hapa!” Mama
Msindai akaendelea kuweka wasiwasi. “Mama Msindai! Nimekwambia ninashugulikia
Jackson awepo hapa kabla ya saa 11 jioni. Naomba utulie mama.” Jacinta
akamtuliza. Akanyamaza.
Pendo
naye alikuwa kimya. “Eti Pendo? Au alianguka huyu Sabrina?” “Hapana dada. Tena
vile kukutwa sakafuni ni yeye mwenyewe aliwahi ili asije kuanguka. Nafikiri
alipandisha hasira baada ya mazungumzo yake na mtu aliyekuwa akimtaja kama
Max.” Jacinta akashituka sana. “Subiri kwanza Pendo. Maximilian Kundi!?” “Sijui
dada, ila yeye alikuwa akimtaja kama Max tu.” “Kwani wewe Jacinta unamjua huyo
Maximilian Kundi kama nani kwa Sabrina?”
Akauliza mama yake. Jacinta hakujibu akamsogelea karibu Pendo.
“Walikuwa
wakizungumza kwa simu au alimfuata?” “Huyo Max alitukuta tunakula pale akakaa
akisema anataka kuzungumza na Sabrina akisema anataka kuomba amani. Lakini
Sabrina akaanza kulia sana akimshutumu Max. Sikuelewa ni nini anaongelea, kwa
kuwa ndio na mimi kwa mara ya kwanza namsikia na kumuona huyo Max ila ni kama
nakumbuka Sabrina akimsema pale kama ni mwanasheria.” “Ni yeye. Ngoja
nimtaarifu Junior.” “Kuna nini!?”
Akauliza mama Msindai na wasiwasi akiona amepitwa.
“Wewe
mama angalia mambo ya mjukuu, mengine yaache.” “Wewe unajua sitaacha na
sasahivi nitajua. Aidha kutoka kwako, au kwa Junior, au kwa Jackson mwenyewe au
nitapiga simu sasa hivi habari zinifikie hapahapa tukiwa tumesimama hapahapa.”
“Kuna mambo mengine mama Msindai jifunze kuyaacha yakupite. Junior na Jack
wameomba kabisa na kunisihi usiambiwe.” Jacinta akamsihi mama yake. “Sasa hapo
ndipo nitakapotaka kujua, tena sasa hivi. Jambo linalotaka kuhatarisha maisha
ya watu wanaonihusu! Mjukuu ambaye nimekuwa nikisumbiria! Huna utakaloniambia
Jacinta, nikanyamaza. Na unanijua mimi, nitafanya makubwa, patanguruma hapa au
nitaagiza niletewe huyo Max mwenyewe ajieleze yeye ni nani na anataka nini.”
Jacinta akabaki akimtizama mama yake, na yeye akamtizama.
“We
Jacinta?” “Basi naomba Junior aje azungumze na wewe, mama. Yupo njiani
anakuja.” “Sawa.” Akakubali mama Msindai na kutulia kidogo. “Au...” “Hapana
mama. Umeshakubali kusubiri, naomba subiri tafadhali.” “Kwani yanamuhusu nani?”
Jacinta akatingisha kichwa na kutaka kuondoka. “Unanipuuza mimi Jacinta!?”
Jacinta akageuka. “Umekubali kusubiri mama yangu. Ni nini!?” “Nataka sasa kujua
yanamuhusu nani. Naona kusubiria hilo jibu sitaweza na sitaki kuzungumza na mtu
asiye sahihi.” “Yanamuhusu mwanao Jack na familia yake. Tena yeye ndio
amenisihi haswa usiambiwe mama. Tafadhali acha.” “Sasa Junior ameingiaje?” Akaendelea
kudadisi. Jacinta akavuta pumzi kwa nguvu, akainama kama anayefikiria.
“We
Jacinta? Au unataka nikamtoe Msindai ndani anisaidie kunitafutia habari kamili
kwa kinachoendelea kati ya huyo Maximilian Kundi na familia ya Msindai au
unaniambia?” “Umeshamshika jina lake kamili, mama jamani! Mbona unataka
kunigombanisha na kina Junior walioniamini, na...” “Kwa hiyo na Junior
anahusika?” Jacinta akanyamaza. “Au yeye ndio mama yenu siku hizi, anayeambiwa
mambo yenu, mimi sina maana tena?” “Mama Msindai usiende mbali. Yanamuhusu
Junior pia.” Mama Msindai akakunja uso.
“Jambo
gani linalomuhusu Jackson na familia yake, halafu tena limuhusu na Junior?!” Akafikiria
kwa sauti. “Yanamuhusu kama Junior Msindai au kama Waziri?” Akauliza kwa sauti
akimtizama Jacinta. “Naenda kupiga simu mama, naomba tulia na usimtoe baba
ndani, acha amuhudumie mtoto wa Jack, usije ukazua jingine.” “Ninao watu wa Usalama
wengi tu. Wala si wewe na baba yako ndio ninaowafahamu huko Usalama wa Taifa.
Ulinikuta nikifahamiana nao. Nyinyi kina Msindai msinibabaishe. Mnajidai
mnanificha mimi mnafikiri sifahamiani na watu! Nawajua watu wakubwa kuliko
nyinyi kina Msindai.” “Sawa mama.” Jacinta akaondoka pale wala hakutaka
kubishana naye tena. Alijua akibaki pale, atamtoa ukweli wote na kujikuta
akimwambia kila kitu.
Jacinta
& Junior.
J |
acinta alitoka
pale na kurudi ofisini kwake, kwenye jengo jingine tu lakini paleplae ndani
Usalama wa Taifa, akampigia simu Junior. “Nimetoka
kuzungumza na Pendo. Bahati mbaya nilimuuliza nini kilitokea mpaka Sabrina
aanguke wakati alikuwa mzima kabisa, lakini mbele ya mama!” “Na mimi
nilishangaa. Jack alinitumia picha za mtoto wake akasema ni mzima kabisa. Sasa
hivi baba ananipigia simu kuniulizia Jack amefikia wapi, anatakiwa aje atoe
maamuzi hali ya mtoto sio nzuri!” “Junior!” “Kweli. Wanasema mapigo yake ya moyo
si mazuri kwa sababu ya pressure ya mama yake.” “Jack atachanganyikiwa Junior.
Sasa amefikia wapi?” “Sina chakufanya, nilazima asogee mpaka Dodoma kama
ulivyosema. Mbaya zaidi hakuna ndege ya sasahivi yakumtoa Singida. Nimemuomba
baba wahangaike kwanza, kumtaarifu yeye iwe jambo la mwisho, lakini kwa jinsi
nilivyosikia kwenye sauti ya baba, nahisi hali si nzuri.” “Baba huwa sio mtu wa
kupaniki au kukata tamaa.” Akaongeza Jacinta. “Ndio
hicho sasa, ukimsikia akiwa amepaniki ujue hicho kitu si kizuri.” Wakatulia
wakifikiria.
“Ulitaka kusema nini juu ya Pendo na mama?” “Mmmh! Mpaka nilisahau!
Nilimuuliza Pendo ni nini kilitokea kutoka Sabrina anatoka hospitalini mpaka
pressure kuwa juu kiasi hicho!” Junior kimya
akisikiliza. “Akasema Max alimfuata.” “No way!” Junior akahamaki. “Alimfuata wapi!?” “Wakati wanakula baada ya kutoka huko
hospitalini kwa kliniki. Anasema Sabrina akagomba na kulia sana kwa Max, mpaka
pressure ikapanda.” “Hapana Jacinta. Huyu mtu lazima kumshugulikia sasa hivi.
Hatuwezi kuendelea kusubiri.” “Na mimi naona hivyo. Nilitaka kukutaarifu hicho
na kukwambia...” “Simu ya mama hiyo!” Jacinta akamsikia kaka yake. “Ndio hicho nilitaka kukwambia. Usipokee kwanza nisikilize.”
Jacinta akataka kumpanga kaka yake kwanza.
“Mama anataka nini!?” “Anataka umwambie huyo Max ni nani na
anahusika vipi kwako na kwa familia ya Jack.” “Mama angetulia kwanza!” “Hapa
nimemkimbia. Ashawaka, hamna utakachomwambia tena akasikia. Amesema yupo radhi
akamtoe baba ndani anakomuhudumia Sabrina na mtoto, au apige simu kwa watu wake
wengine wa Usalama kuulizia habari za huyo Max.” “Acha nimpigie nimtulize,
nimwambie nitakuwepo hapo baada ya muda mfupi sana. Na wewe naomba ukamilishe
swala la Max tafadhali, Jacinta. Huyu mtu atatuangamiza kweli!” “Sasa hivi
natuma akakamatwe.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado
mapigo ya mtoto yalikuwa chini. Yanapiga na kupotea, na kwa kuwa mtoto
alishakomaa, na pressure ya Sabrina ilikuwa imeanza kushuka, daktari akamshauri
mzee Msindai watoe mtoto kwa haraka. “Sidhani kama ni sawa kuendelea kusubiri
Mzee. Tunajiweka kwenye hatari pasipo sababu.” “Acha nimtaarifu mumewe kwanza.”
Mzee Msindai akatoka na kumkuta mkewe hapo nje. “Naomba usipaniki ila
unisikilize.” “Sasa hapo ndio unanipanikisha na wewe.” Mama Msindai akawaka kwa
mumewe. “Sasa wewe ukiwa juu hivyo, nani atakuwa msaada kwa hawa watoto?” “Wewe
niambie Msindai.” “Pressure ya Sabrina imeanza kushuka ni kitu kizuri. Inabidi
mtoto atolewe ili kuepuka madhara kwake.” “Mmepata mapigo yake ya moyo?” Mama
Msindai akauliza. Willy naye akaja hapo akiongozana na Joy.
“Poleni
jamani.” Wote kwa pamoja ndio ikawa salamu yao. “Ndio Msindai anatoa taarifa
hapa.” “Naomba tuzungumze na Jack ili atoe baraka zake, mkewe apelekwe chumba
cha upasuaji.” “Kupasuliwa tena! Kwa nini?” Mama Msindai akazidi kupaniki,
Junior naye akaingia. “Naomba utulie mama. Sauti yako inasikika mpaka huko
nje.” Junior akamtuliza. “Mimi sijali maswala ya sauti nataka kujua.” “Naomba
nizungumze na Junior hapo pembeni.” Baba yake akamvuta mkono, mama Msindai naye
akasimama na kufuata. “Naomba usubiri kwanza, mama J. Hali hiyo tukimpigia simu
Jack ndio atapaniki zaidi.” Mumewe akamsihi. “Subiri mama.” Mama Msindai
akarudi kukaa.
“Nataka
kumpigia simu Jackson na wewe ukiwepo, akubali sasa hivi mkewe afanyiwe
upasuaji na pengine azungumze naye. Anatetemeka sana wakati pressure imeanza
kushuka, au niseme sio mbaya. Nafikiri ameingiwa na hofu. Lakini tukifanikiwa
kumtuliza Jack, akazungumza na mkewe akatulia, hawatapoteza mtoto.” “Ndio
tumefikia hapo?!” Junior akaingiwa na wasiwasi. “Yaah! Mapigo ya mtoto sio
mazuri amepatwa fetal distress. Na mbaya zaidi mama yake alishaanza
tayari uchungu tokea hawajamfikisha hapa. Aliyehusika kumpima kule walikomtoa
kabla hawajambemba kwenye gari, anasema alianza kuona dalili za uchungu. Wakajua
ni sababu ya hiyo pressure kwenda juu sana, ndio iliyosababisha kuanzwa kwa
uchungu. Lakini hata hivyo mtoto amekomaa, amebakisha siku chache sana
kuzaliwa, hata 10 zisingefika. Ndio maana wanaona atolewe tu.” “Mungu asaidie.
Jack atachanganyikiwa, baba. Acha tumpigie.” Junior akampigia.
“Jack?” “Vipi kaka? Umefika kumuona mke wangu?”
Jack akauliza na wasiwasi. “Nipo hapa na baba alikuwa
akinipa maendeleo ya mama na mtoto.” Jack akatulia. “Pressure ya Sabrina imeanza kushuka kitu ambacho nikizuri.
Na kwa kuwa mtoto amekomaa, wanaona ni heri wamtoe tu.” “Wanamtoaje mtoto,
kwani Sabrina ameshaanzwa na uchungu?” Baba yake akapokea simu. “Ndiyo. Lakini wanaepuka asisukume, wanataka kumsaidia
ajifungue kwa upasuaji.” “Sijaelewa! Nahisi sijui nimepaniki! Kwa nini upasuaji
tena!? Naomba mniambie ukweli kama mke wangu na mtoto wapo matatizoni.”
Junior akamtizama baba yake.
“Tukichelewa ndipo watakuwa matatizoni ndio maana tumekupigia ili
utoe idhini yako afanyiwe tu.” “Siwezi kufikiria mpaka nimuone Sabrina, baba.
Nahisi napaniki sijui niseme nini! Naomba kumuona Sabrina.”
Junior akachukua simu. “Sasa mkeo yupo kwenye hali
mbaya Jack. Anakuhitaji wewe umtie moyo ili kuweza kupita hapa. Lasivyo
mtapoteza mtoto na utamtesa mkeo. Unanisikiliza Jack?” “Nasikia ila naomba
unielewe na mimi, nimeingiwa hofu kaka. Nilikuwa kwenye kujiandaa kuja Dar,
kumpokea huyo mtoto kwenye hali ya utulivu. Sasa
hivi nimekwama huku, mtoto wangu anazaliwa huko! Tena anazaliwa kwa njia ambayo
muda mfupi uliopita hata haikuwa ikifikirika!” “Nisikilize
Jack na ujikaze uache kulia mbele ya mkeo. Haya mambo yanatokea. Na uzuri kama
ipo njia ya kusaidia, ni vizuri utoe ruhusa, mkeo na mtoto wahudumiwe. Ni sawa?” “Sawa.” “Basi naomba
utulie, baba anampelekea mkeo simu umtulize. Anasema ameingiwa na hofu sana.”
“Piga kwa video basi nimuone.” Kaka yake
akamwangalia baba yao.
“Lazima nimuone na yeye anione ili kumtuliza!”
Jack akaweka msisitizo. “Basi tulia Jack ili aweze
kuona tumaini kwako.” Junior akakata na kupiga kwa video, akamkabidhi
baba yake, akarudi ndani kwa Sabrina. “Mumeo huyu hapa.” Akamkabidhi simu. “Brina?” “Unakuja?”
Sabrina akauliza na machozi. “Nipo njiani nakuja. Vipi
lakini wewe?” “Naogopa sana Jack. Mapigo ya
mtoto hayasikiki vizuri.” “Ingekuwa ni mtu mwingine
mwenye huyo mtoto, hata mimi ningeingiwa hofu, lakini kwa kuwa ni wewe, najua
utaweza tu.” “Kweli?” “Kabisa. Hata hilo lipo ndani ya uwezo wako. Tulia kabisa na
uzuri upo na wataalamu hao, watakusaidia tu.” Sabrina akavuta pumzi kwa
nguvu kujaribu kutulia.
“Kwani wewe uko wapi sasa hivi?” “Nakuja Brina. Nipo njiani.” “Bado upo Singida?!”
“Niombee nifike salama na mimi nakuombea kila kitu kiende salama.” “Nimesikia wakimwambia baba wanataka kunifanyia upasuji. Sasa
itakuaje kama wewe hautakuwepo?”
“Kila kitu kitaenda sawa. Baba ameniambia hata ningekuwepo, wasingeniruhusu
kuingia.” “Lakini nilitamani
ungekuwepo tu nijue upo na tuagane kabla sijaingia. Nisipotoka hai je?”
Jack akaingiwa na hofu, na yeye akaanza kulia kama mkewe. “Naogopa Jack. Naogopa sana.” Jack akabaki kimya
akilia. Baba yake akachukua simu.
“Naomba nyinyi wawili wote mnisikilize. Hakuna hatari kubwa kwa
sasa. Wanachotaka nikumsaidia mtoto. Na kama Sabrina angekuwa na tatizo,
ningekwambia Jackson. Mmesikia?” Kimya
wakiendelea kulia. “Jack safiri kwa utulivu ukijua
unakuja kumkuta mke na mtoto wako, na Sabrina utulie kabisa ili kutuliza hiyo
pressure waweze kukusaidia kumtoa mtoto. Hofu yeyote sasahivi haitamsaidia
mtoto wenu. Sijui kama mnanielewa?” Hakuna aliyejibu. “Na wameanza kumtaka Sabrina wamwandae kumwingiza chumba cha
upasuaji. Usiogope hata kidogo. Hakuna hatari.” Mzee Msindai akawapisha
wauguzi waliotaka kumuandaa Sabrina kumpeleka chumba cha upasuaji.
Mipango Ya Mungu Si Ya
Mwanadamu.
S |
abrina
alitolewa akiwa anapelekwa chumba cha upasuaji, analia hakuna anayemsikiliza
hapo nje walipokuwa wakimsubiria kumuaga na kumwambia wanamuombea asiwe na
wasiwasi. Sabrina alikuwa akilia sana. “Sasa Sabrina mama, watakufanyiaje
upasuaji unalia hivyo! Tulia ukijua ukitoka utamkuta mumeo.” Mama Msindai
akajaribu kumtuliza wakiwa wanamfuata nyuma akiwa amelazwa kwenye kitanda. “Jack hajatoka hata Singida, mama!” “Lakini
anakuja. Naomba utulie na uamini kila kitu kitakwenda sawa.” Sabrina akaendelea
kulia wala asimsikilize mtu tena. “Nakuombea Sabrina. Kila kitu kitaenda sawa.
Na nimezungumza na mama pamoja na Sabina. Watoto wapo sawa. Nimewaambia
wamuachie Sifa watoto, wao waje. Ukitoka utawakuta. Kwa hiyo usiwe na
wasiwasi.” Pendo akamuongelesha kwa upole na upendo, Sabrina akatingisha tu
kichwa na kuendelea kulia. “Sasa
atafanyiwaje upasuaji analia hivyo!?” Mama Msindai akamuuliza mumewe. “Hatuwezi
kumsubiria Jack, lasivyo watapoteza mtoto. Watamchoma sindano, atalala tu.
Hakuna jinsi.” Sabrina akaingizwa chumba cha upasuji wengine wote wakasubiri
hapo nje.
“Naomba
mpigie tena Jack kujua amefikia wapi, Junior mwanangu. Asije akatoka tena,
asimkute mumewe.” “Mwanao huyo ameniangusha kabisa! Mimi namwambia azungumze na
mwenzie amtulize, na yeye analia bwana!” Mzee Msindai akalalamika. “Anaogopa.
Kila mtu ameingiwa na hofu. Msimlaumu mtoto.” Wote wakamgeukia mama Msindai
wakimshangaa. “Ndio ni mtoto na ninaomba mumpigie simu sasahivi kujua amefikia
wapi.” Junior akatingisha kichwa na kuondoka pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya muda mama yake na Sabina wakawa wamefika pale. Wakakuta wanasubiria hapo.
Willy ndiye aliyekwenda kuwapokea na kuwaleta walipo. Kila mtu alikuwa kimya
akisubiria kivyake. Baada ya kama dakika 25 mtoto akatolewa akiwa ameshikwa na
daktari wa watoto. Wote wakasimama. “Amefanana na baba huyo!” Wote
wakakubaliana na Jacinta. Jacinta akampiga picha kwa haraka, mtoto akatolewa
pale. “Inabidi akawekwe kwenye mashine na apewe oxygen kwa haraka, ili kumsaidia
upumuaji. Vinginevyo amezaliwa na uzito mzuri tu na amekomaa kama mnavyomuona.”
“Asante sana, nashukuru. Naomba tuongozane.” “Bila shaka.” Mzee Msindai
akafuata nyuma.
Mama
Sabrina akamkimbilia yule daktari kabla hajapotea. “Vipi mama yake huyu?” Akauliza
kwa wasiwasi. “Wanamalizia. Atatolewa muda si mrefu. Kila kitu kimekwenda sawa.
Usiwe na wasiwasi. Samahani nilikuwa na haraka nimeshindwa kutoa taarifa za
mama.” “Asante.” Mama Sabrina akarudi kwenye kundi wengine wakajisuta. Hata
walisahau kuuliza habari za Sabrina. “Afadhali umeulizia mama kuliko hivi
tulivyokuwa tumebaki hapa na wasiwasi.” Akaongea mama Msindai, mama Sabina
akarudi kukaa na kuinama.
Muda
ukazidi kwenda. “Jacinta, Jackson amefikia wapi?” Mama Msindai akauliza. Akaona
Jacinta na Junior wanaangaliana. “Mnanikera mimi nyinyi wawili na vijisiri
visivyoisha! Sasa kama sasa hivi mlitaka kunificha nini?” Akalalamika kwa ukali
mama Msindai. “Tulitaka kupunguza wasiwasi mama.” Junior akamtuliza. “Jackson
yuko wapi, Junior?” Akauliza tena kwa ukali. “Hajapata ndege yakumtoa Singida.
Leo hakuna ndege mama.” Mama Msindai akabaki ameduaa.
“Lakini
tumemshauri kama anaweza kusogea hata kwa basi mpaka Dodoma au Arusha, atapata
ndege hata ya usiku.” “Yaani nyinyi wawili na akili zenu zote mnashindwa
kumfikisha mtoto hapa!? Nimewapa kazi moja tu. Moja! Na
imewashinda. Mme..” “Mama, naomba utulie. Jacinta alitafuta ndege na
akazungumza na watu wamsubirie Jackson Dodoma, ili waje nae. Wakakubali. Hakuna
jinsi nyingine yakufanya kwa kuwa hakuna ndege Singida. Na hawawezi kuendelea
kumsubiria Jackson Dodoma wakati hiyo ndege inamleta mkubwa huku Dar.” Junior
akajaribu kumtuliza mama yake na kuondoka kuzungumza tena na Jack. Mama Msindai
naye akasimama.
“Najua
umekasirika mama, ila nakusihi hivyo ulivyo usimpigie simu Jack sasahivi.
Nimetoka kuzungumza naye, yupo na hali mbaya kuliko hivi alivyo Sabrina.
Imebidi kumsindikiza kwa simu mpaka ameingia kwenye basi.” “Anaelekea wapi sasa?”
Mama yake akamuuliza Jacinta. “Amesema Arusha ndio kuna ndege nyingi.” “Sasa si
atafika hapa kesho! Mnamshaurije mtoto lakini nyinyi?” “Naomba tulia mama. Maana ameshaondoka Singida,
tumuombee afike hapa salama.” “Kuendesha?” Jena akauliza. “Kuendesha Junior
amemkataza. Amepaniki sana.” Jacinta akajibu. Junior ameenda kumpigia tena
kumuangalia na kumpa habari za mtoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment