Jack akiwa ofisini kwake
akaambiwa anamgeni anahitaji kumuona. Akatoka mpaka mapokezi. Akakutana na mtu
mtanashati. “Nikusaidie nini?” “Nimekuja kutafuta amani.” Jack akakunja uso.
“Tunaweza kukaa kidogo?” Jack akatafuta sehemu wakakaa. “Mimi ni mwakilishi wa
bwana Maximilian Kundi na mkewe.” Jack akacheka na kutulia. “Nimekuja kuomba
amani na kuomba kumaliza mambo bila kufikishana kwenye vyombo vya sheria.”
“Nafikiri hilo tumeshachelewa.” Jack akajibu. “Basi labda niseme, tusiende
mbali.” “Nilimwambia Tino, ambaye alishawishiwa na huyo unayemwakilisha ili aje
anifanyie mimi fujo, labda hakukwambia wewe au Max. Ila nitarudia kwa manufaa
yako na wewe.” Yule wakili akakaa sawa kusikiliza.
“Hakuna
umbali nitakao shindwa kwenda ambako kutanisaidia kulinda familia yangu.
Nitafanya lolote na chochote kulinda familia yangu. Sijui walikushirikisha nini
na kwa umbali gani, lakini hao uliowataja, wametishia familia yangu, na siwezi
kufumbia macho. Ushahidi ninao. Na ninakutuma kwao, waambie chochote
kitakachompata mke wangu, watoto wangu, mimi mwenyewe na familia ya Msindai,
wao watakuwa watuhumiwa wa kwanza. Wakili wetu anao ushahidi wote na wengineo wanao
ushahidi pia, ili chochote kikimtokea hata huyo wakili wetu, kuwepo na ushahidi
mwingine.” “Lakini nafikiri tunaweza kuzungumza tu.” “Si ndio tunazungumza
hapa! Ulitaka kusikia nini? Au kuna ujumbe mwingine ambao hujaufikisha kwangu?”
Jack akawaka. Ujasiri uliongezeka kwa kuwa aliwawahi kwa ushahidi. Kwa mara ya
kwanza Max akafikishwa magotini.
“Kama
hakuna ujumbe mwingine, naomba nirudi kwenye kuwajibika.” “Samahani kwa kuwa
najua upo kazini. Lakini naomba niombe msamaha na nikuhakikishie kabisa, hiyo
familia itakaa mbali kabisa na familia ya Msindai. Naweza hata kuweka kwenye
maandishi ili tu kufanya haya mambo yasiende mbali.” “Nakwambia haya mambo yapo
mbali zaidi ya hivi tunavyozungumza. Vitisho vyao vimenaswa na vyombo vya Usalama
wa taifa! Hawakukwambia hilo!?” Jack akauliza na kuendelea bila kusubiri
jibu. “Kunifuata mimi mtu mdogo sana, muhasibu wa serikali tu, tena mkoani
Singida, ukiwa umemtishia waziri wa hii nchi, unafikiri itabadili kitu? Au
kusaidia kweli!?” Jack akazidi kumtisha.
“Nafikiri
unataka kunipotezea muda ambao nalipwa na serikali kuwajibika.” “Naweza kukufuata tena baada ya
kazi.” Jack akakunja uso. “Nipo hapa na wewe. Nimekupa nafasi ya kuzungumza.
Tena kwa kutumia muda wa mwajiri wangu. Halafu unataka tena nikupe na muda wa
familia! Ni nini ungetaka kusikia kutoka kwangu?” “Natafuta amani kati yako na
kina Kundi.” Jack akashangaa sana. “Mnamfanya nani mtoto mdogo hapa!? Upo leo
kutafuta amani kwakuwa wamekamatwa. Wamekwambia lakini ni nini walipanga dhidi
yangu na familia yangu?” Kimya kwa kuwa Jack alishapandwa sana na hasira.
“Nakuuliza?
Unajua mipango mibaya waliyokuwa wamepanga kwa siri huyo Max na mkewe kumtenda
kaka yangu ambaye hakuwa na hatia?” Kimya. “Walikusudia kumuharibia kazi kwa
kumzulia kashifa nzito! Kwa ajili ya Max kujinufaisha tu yeye mwenyewe kifedha
na ajira. Mtu kama huyo aachwe na kazi yenye nguvu sana kwenye jamaii, unafikiri
ataangamiza wangapi? Na wewe unajiharibia kuja hapa kutetea uovu wao, si
inamaana unahalalisha uovu wao?” “Hata kidogo.” “Basi acha sheria ichukue
mkondo wake. Kama na wewe unalipwa ili kuwatetea, basi simama kisheria ujipange
kuwatetea siku watu wa Usalama watakapokamilisha uchunguzi wao.
Nakutakia siku njema.” Jack akasimama na
kuondoka.
Kwa Sabrina.
J |
ack akaingia
ndani na kumpigia simu Sabrina. “Upo mzima baba watoto?”
Akaanza Sabrina. “Mzima. Mbona kimya?” “Nilikuwa
nimesinzia hapa sakafuni, hivi umepiga
ndio nimeamka. Makinda yako sijui yametawanyikia wapi! Ngoja nianze kusaka.”
Sabrina akakaa Jack akacheka. “Walikuwa wanaongea hapa
huku wanarukaruka tumboni, nikaishia kuloa mate, nikaona nilale tu maana
sielewi.” “Mlango wa mbele wa hapo sebuleni umefungwa lakini?” Sabrina
akashituka kidogo akasimama. “Umefungwa, watakuwa..
Jeiline!” “Muite Keiline kwanza ndio atakuja kwa
haraka.” “Na kweli.” Sabrina akaanza kuwasaka huku akimuita Keiline,
akamuona anatokea chumbani. Akacheka. “Kama ulijua. Keiline
ndio katoka. Walikuwa chumbani kwao.” Sabrina akainama na kumbusu.
“Mtoto
mzuri wewe! Mlikuwa mnaharibu nini chumbani?” Akaanza kucheka. “Muone!” “Weka kwenye video nimuone.” “Naona hiyo shuguli niifanye
nikiwa nimejilaza kabisa chini sakafuni hapo chumbani kwao. Haya twende
Keiline.” Kuingia chumbani, wamevuruga kuliko kawaida. “Hapa chumbani kwao ni kama kumepigwa bomu!” Jack
akacheka. “Nalala hapa hapa. Haya, njooni watoto wa Jack, mumuone baba yenu,
mimi nilale.” Sabrina akaweka video akajilaza chini, wote waliposikia sauti ya
Jack akiwaita wakatambaa mpaka kwenye simu, wakaanza kupiga makofi, kila mtu
akiongea lake. Jack moyo safi, amejishindia vibinti viwili. Tena vinaafya
nzuri. Jack aliporidhika wote wapo salama, akarudi kuendelea na kazi.
Sabrina na
watoto jijini Dar.
S |
iku
zilipokaribia za harusi ya Pendo na Willy, ikabidi Sabrina atangulie na watoto
Dar amuache Jack kazini ili kutunza siku za likizo. Akashukia nyumbani kwa
Pendo kwa makubaliano baada ya harusi atahamia ukweni. Ukweli ni kwamba Sabrina
alijua maisha yake na hao watoto wakizungu huko ukweni bila Jack, itakuwa shida
tupu. Hapatakuwa na uhuru na watoto hao wanaofika kila mahali kama si kwa
kutambaa, basi kwa kutumia vigari vyao wakisuma mpaka watakapo. Sabrina
akamwambia Jack, atajifungua kabla ya siku kwa wasiwasi. Ndipo Jack akamwambia
mama yake kuwa Sabrina atakuwepo Dar lakini nyumbani kwa Pendo kwa ajili ya
kumsaidia maandalizi ya harusi, ila harusi ikiisha atahamia kwa mama Msindai. Yote
hayo Sabrina alijua mumewe atakuwa yupo naye jijini. Wakaelewa.
Alifika
Dar na wanae akiwa ameshatafutiwa daktari wa wakina mama, baba mkwe wake
akamwambia lazima aanze mara moja ili ikitokea anajifungua mapema, basi huyo
daktari ajue anamsaidia mama wa namna gani na mtoto. Pendo alimsindikiza
kliniki kwa mara ya kwanza hapo jijini Dar. Sabrina alimuomba mama yake aje
akae nao hapo kwa muda akimsaidia swala la watoto ili msichana wa kazi, wa
Pendo asilemewe. Kwa hiyo siku wanafika na mama yake naye akaletwa na Sabina.
Kwahiyo wakati anakwenda kliniki na Pendo, aliwaacha watoto wake na mama yake akiwa
hana wasiwasi.
Walitoka
na Pendo wakiwa wamejawa furaha, moja kwa moja mpaka kliniki. Sabrina akaanza
upya kwa huyo daktari kama hajawahi kuhudhuria kliniki kabla. Akafanyiwa vipimo
vyote na ultrasound. Akaambiwa mtoto alishageuka kabisa. Siku zilikuwa
zimekaribia. Daktari alimwambia kila kitu kipo sawa. Wakatoka hapo akamtaarifu
Jack na kumtumia picha za ultrasound. ‘Mwanao huyo! Mzima,
wanasema yupo tayari kuja kukuona dady.’ Jack akafurahia na kumpigia simu
baada yakuona picha. Wakazungumza. “Binti zangu?” “Wako
na bibi yao, amesema leo atawalisha ugali. Kama nawaona watakavyolala!”
Jack akacheka. Akamsalimia na Pendo wakaagana baada ya kuwaambia watakwenda
sehemu wakae na kula ili kupata muda wao.
Sabrina
akamtumia na mama mkwe wake hizo picha za mtoto za ultrasound. Kisha akampigia
kumshukuru kwa kumtafutia daktari mzuri. “Walikuangalia
kila kitu lakini?” “Kila kitu mama. Utafikiri ndio mara ya kwanza ninaanza
kliniki!” Mama Msindai akacheka. “Nilimwambia
huyo daktari aweke umakini maana mimi huyo daktari wenu mliyekuwa mkimuona huko
Singida hata sijamuelewa vizuri.” Sabrina akacheka tu akimjua mama
Msindai. Jambo lake yeye ndio huwa linaeleweka. Akaulizia wajukuu zake. “Wapo na bibi yao. Amesema leo atawalisha ugali.”
Wakacheka. “Watakubali sasa?” “Tunashangaa sisi huwa tukiwalisha
wanatukatalia, lakini bibi yao akiwalisha huwa wanakula bila shida! Na huwa
wanalala mpaka mnasahau.” Wakacheka tena. Na yeye akamsalimia Pendo na
kutaka kujua anaendeleaje na watoto wake. Akawatania. “Bibi
harusi na msimamizi wote mnashindana matumbo!” Wakacheka na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakafika
kwenye hoteli nzuri wawili hao stori zikaanza. Sabrina akamwambia muhudumu kile
kilichopo tayari kwa haraka kiletwe aanze kula ndipo ataagiza anachotaka. Pendo
akaanza kucheka. “Huogopi kunenepa?” “Hata sina hilo wazo na wasiwasi. Mwili
wenyewe naona umegoma!” “Kwa hiyo hapo unakula kila kitu!?” Pendo akauliza kwa
mshangao. “Nakwambia kila kitu, tena sana. Mpaka uji wa ulezi nakunywa kama
wale watoto wa Jack.” Pendo akacheka sana. “Ukinikuta nakula ugali, utafikiri
nimetoka shamba.” “Sasa mbona hunenepi?” “Mama anasema nimechukua mwili mkavu
kama shangazi zetu. Halafu chakushangaza, ni mimi tu nyumbani ndio sina mwili.”
“Namuona Sabina na ndugu zako wengine.” “Basi. Mama alikuwa akinilisha
nilipokuwa nanyonyesha, niliongezeka kidogo tu, tukadhani mwili utasogea lakini
ulipoishia ndio ikawa basi.” Pendo akacheka. “Basi mimi nikila hivyo, nafumuka
kama nyumba.” “Na hupendi?” Sabrina akaendelea huku akinywa juisi ya embe
ambayo walishaletewa.
“We
Sabrina! Si nitatisha?” “Ulivyo na umbile zuri hivyo Pendo, dada yangu!
Utapendeza kama mama yako.” “Sasa ndio ninachokwepa na sitaki kinitokee.”
Wakacheka sana kwani ni kweli Pendo alifanana na mama yake. “Hongereni kwa
nyumba nzuri, tulipita na Willy juzi.” “Kweli ile nyumba nzuri! Mpaka nahisi
wanaweza kubadili mawazo na kuja kutudai!” Wakazidi kucheka. “Jack anamuharakisha
kaka yake amsaidie iwe kwa majina yetu haraka kabla hawajaabadilika hao ndugu.”
“Mtahamia sasa au mnakodisha?” Pendo akauliza. “Mmmh! Mimi nahisi kuna ambalo
linaendelea, Jack anasita kuniambia.” “Kwa nini?” “Maana na mimi nilimuuliza
swali hilo hilo. Tunaanza kutafuta mteja lini na wapi?” “Akajibu tusubiri
kidogo, tunaweza tusiikodishe. Sasa nikamshangaa kidogo, kwamba pale Joy
alisema tukikodisha tutapata pesa nyingi, na yeye akalifurahia hilo, ni nini
kimegeuka gafla!” Sabrina akaendelea kula kwanza.
Max aharibu
zaidi.
M |
ara
Sabrina akashangaa Max anawasogelea. Kitu kikampanda Sabrina, akashikwa na
hasira ya ajabu sana baada yakumuona Max. Pendo akamuona ametulia akimtizama
anapowasogelea. “Unamfahamu?” “Sana.” Akajibu Sabrina macho kwa Max. “Hujambo
Sabrina?” “Sijambo kabisa, namshukuru Mungu.” Akajibu Sabrina macho kwa Max
bila tabasamu. “Familia haijambo?” Max akauliza tena kama anayebabaika hajui
chakuzungumza. “Unataka nini kwangu Max!? Ni nini unataka?” Sabrina akauliza.
“Naweza kukaa kidogo, nina shida yakuzungumza na wewe.” Sabrina akakunja uso.
“Sitakuchukulia muda mrefu.” Max akavuta kiti na kukaa.
“Tunafahamiana
vizuri kwa muda mrefu sasa ndio maana nimeona nikufuate tuzungumze.” Sabrina
kimya akimtizama kwa hasira. “Najua unaelewa kinachoendelea kati yetu na kina
Msindai. Nimekosa Sabrina. Hata nimemtuma mtu kwa mumeo kuniombea msamaha ili
haya mambo yaishe, kuwe na amani. Nipo tayari hata kuweka kwenye maandishi
kuwahakikishia kuwa sitawaingilia tena familia ya Msindai. Tafadhali nisaidie.”
Sabrina akakunja uso tena akimwangalia Max kwa mshangao. “Ni hivyo tu Sabrina.
Najua nilizungumza maneno ambayo sikutakiwa. Nahisi nikutokana na hasira tu
siku ile. Nikampigia simu Tino nikiwa na hasira, nikaongea maneno mabaya.
Lakini wote tunajua sina uwezo wa kuwadhuru nyinyi.” Sabrina akazidi
kukasirika.
“Kweli.”
“Umemaliza Max?” Sabrina akauliza. “Ni hilo tu.” Max akajibu wazi alionekana
yupo kwenye hali mbaya. Midomo ilikuwa imemkauka kama siye Max aliyekuwa
akinukia vizuri na shati jeupe haswa kila wakati mpaka usiku. “Cha kwanza mimi
na wewe hatufahamiani kabisa. Unafahamiana na Sabrina yule mliyekuwa mkimuona dhaifu
ambaye angekukwamisha kwanza wewe kupata pesa baada yakushinda kesi ambayo,
pili sasa, Tino alikuwa akihangaika kujinufaisha dhidi ya Lela. Ukazungumza
naye na kumshawishi aondoe kikwazo ambaye ni mimi, si kwa manufaa yake tu, ila
yako pia. Ushinde kesi, ulipwe na Tino, na Tino apate nyumba.” Max akataka
kukataa. “Usikatae Max. Kwa kuwa mimi nilikuwa na Tino Moshi nilikuwa nikisikia
na kujua njama zako ulizokuwa ukipanga kwa kumfundisha Tino, dhidi yangu.” Max
akapoa.
“Kutoka
mlipotuaga wewe na mkeo, mimi na Tino kututaka tujipange vizuri, ukarudi
kinyumenyume na kumwambia Tino kwa siri kuwa mimi ndio tatizo pekee
litakalomfanya asifanikiwe kwenye kesi uliyokuwa ukiitengeneza dhidi ya Lela na
mengine mengi unayoyajua wewe, yaliyombadilisha kabisa Tino. Bisha Max.”
Kimya. “Mkaanza mipango ya kutonihusisha. Kila ukipiga simu swali lako la
kwanza si hata kujua ninaendeleaje mimi niliyekuwa nikimtunza mtu unayetaka
pesa yake, unamtaka atoke au awe mbali na mimi ili mzungumze. Na mimi kwa
kutaka kujua kinachoendelea, mimi ndio nikawa nikiondoka kumpa Tino nafasi ya
mazungumzo, lakini nikiacha simu yangu alipo Tino, iwarikodi mazungumzo yenu
yote. Baadaye nilipokuwa nakuwa peke yangu, nilikuwa nikisikiliza kila kitu.”
Max kimya na kuzidi kuamini mambo yamemgeukia haswa na hila yake ipo mwangani.
“Nilijua
ushauri wako wote wa kikatili uliokuwa ukimshauri Tino kuwa aachane na mimi ila
anilipe ili nisije mgeuka baadaye. Ukamsisitiza aweke ushahidi wote wa pesa
atakayonilipa mimi ili ikitokea nina madai yeyote yale, muwe na ushahidi. Bisha
Max. Nakukaribisha ukanushe haya ninayozungumza.” Kimya. Sabrina akazidi
kupandisha hasira. “Ulimpanga Tino vizuri, akawa akitembea na kufanya kila unachomshauri
wewe. Na kwa kuwa na yeye roho yake ni mbaya sana, amejawa na ubaya
moyoni mwake, akatekeleza yote uliyokuwa ukimtaka anifanyie bila shida, tena
akaenda umbali mrefu tu kukufanikishia kila kitu. Ukampongeza. Si ni kweli?”
Kimya.
“Upo
hapa leo, kwa kuwa umekamatwa kwenye uovu wako, na mipango yako mibaya
uliyokuwa ukiipanga dhidi yetu. Na aliyekukamata ni Mungu aliye hai Max. Wala
si kina Msindai. Ni Mungu. Na ubaya wako umekufuata, unatakiwa kulipa
ndio maana unahangaika kila mahali.” Kimya, Pendo akisikiliza. “Mungu amekuweka
kweupe kabisa Max. Hakika amekuweka pabaya. Yale uliyokuwa ukiyafanya
kwa siri dhidi yangu nikiwa sijakutendea kosa wewe ambaye ulikuwa ukinufaika
na pesa mnazotengeneza kesi na Tino ambaye nilimtoa katika hali ya kufa,
mkanitenda ubaya, Mungu ameamua kukuweka mwangani na kukulipiza. Visa
vyako na ubaya wako wote, ndivyo vipo mlangoni vikikulilia Max. Wala si
Sabrina na mumewe.” Sabrina akaendelea.
“Huu
msamaha unaoutafuta kwangu na Jack, nashauri uanze kwa Mungu mwenye nguvu na
uweza mkubwa sana Max. Yeye pekee atakutoa kwenye shimo kubwa ulilopo sasa
hivi, na hakika nakuhakikishia, hutatoka isipokuwa kwa msaada wa Mungu, endapo atakurehemu. Kwa kuwa hila yako
imechukua sura kubwa zaidi ya unavyodhani Max. Hila yako, uchochezi
wako, na njama ulizokuwa ukitaka kumuangusha kiongozi mzuri sana ambaye
anasifiwa hata na raisi, imebebwa na usalama wa taifa, wala si mimi.
Nilimwambia hivi Tino.” Sabrina akamgeukia Max vizuri.
“Nilimwambia,
sijui ni kwa nini Mungu alinikutanisha na yeye akiwa kwenye ile hali ambayo
Mungu alitaka kunitumia kumtoa pale. Nikamwambia, nilitoka kwenye maombi ya
karibia mwezi. Hivi unaelewa Max? Mwezi mzima mimi nakula mara moja tu kwa
siku, tena nikiwa nafanya kazi ngumu sana, nikimuomba Mungu anisaidie anitoe
kwenye ile hali. Halafu eti Mungu ananitoa kwenye kutunza ngombe, kusafisha
mavi ya ng’ombe na kutibu madonda yao, majibu ya Mungu ananipeleka kwa Tino
aliyekuwa amejawa madonda na kinyesi mwili mzima! Sijui kama unanielewa Max?”
Sabrina akauliza kwa ukali.
“Yule
ambaye ulikuwa ukimfundisha anikimbie, na kumwambia endapo nitafanya madai
kwake, utamtengenezea kesi na kunishinda. Yule uliyekuwa ukijinufaisha na pesa
yake bila kumjali yeye mwenyewe, na kutumia uovu wa moyo wake vizuri sana,
ukimpandikizia chuki dhidi yangu, nilimtoa kwenye mauti. Au nisema Mungu
alinitumia kumtoa kwenye mauti. Alijawa nywele mwili mzima kama mnyama
wa porini! Alijawa kinyesi kilichogandana na madonda, mikojo! Hata mkewe
alinizuia nisiingie kwenye chumba chake. Lakini mimi nikamtii Roho wa Mungu.
Nikaingia chumbani kwake, nikamsaidia Tino. Sikuwahi kukusikia wewe wala mkeo
mkija pale kumsalimia wakati mlijua ni mgonjwa. Ukasubiri nilipomrudisha tena
kwenye uhai, mkaanza kumtumia tena ili kujinufaisha.” Sabrina alijawa jazba.
Akawa mkali, mpaka Max akaogopa.
“Basi
Sabrina. Mimi nilitaka...” “Nakuamuru ukae Max, unisikilize mpaka nimalize.
Lasivyo nitahakikisha unarudishwa kwangu unisikilize kwa lazima. Usinitanie.
Umekuja hapa mwenyewe tena bila kukuruhusu kukaa, umekaa. Sasa nakuamuru ukae
mpaka nimalize ndipo nitakuruhusu. Usinifanye mimi mjinga. Nilinyamaza
nikiwa nakujua sana kuwa wewe ni mbaya Max.” Max akarudi kukaa, kwani alitaka
kuondoka watu walipoanza kuwageukia.
“Hivi
unajua nilikuwa silali?” Sabrina akaanza tena. “Mchana na usiku nilikuwa silali
nikimuhudumia ‘chanzo chako cha pesa’, aliyekuwa hawezi hata kushika
kijiko! Mimi nilihangaika naye kutafuta jinsi ya yeye kujisaidia bila kinyesi
na mkojo kumshika mwilini. Nikamtibu madonda na kumsafisha kutoka kwenye hali
aliyokuwa nayo kama mnyama wa porini, mpaka akarudi kuwa Tino aliyekuwa
akikulipa wewe mapesa mengi, mimi sinufaiki naye mpaka mwisho wakati unamshauri
jinsi ya kuniacha! Mikono hii miwili, bila pesa, kwa kutumia akili na uwezo wa
Mungu, vilimfufua Tino. Na ndipo nirudi kwa kile nilichomwambia Tino mwanzoni
kabisa wakati nikimfariji na kumtia moyo mpaka pressure yake ikapona.
Nilimwambia hivi, sijui ni kwa nini Mungu amenipeleka pale wakati nilikuwa
nafanya kama kile anachotaka tena nikifanye. Tena nikiwa nimeomba kwa muda
mrefu sana, lakini, nikamwambia Tino sasa, nitafanya kwa uaminifu bila kuchoka,
bila kumfanyia yeye ubaya, kama nafanya kwa Mungu mwenyewe.”
Sabrina akatulia.
“Unanielewa
Max?” Kimya. “Nilimwambia na ndivyo nilivyofanya kwake, kwa uaminifu wote, kwa
kuwa Tino hakuwa hata akiweza kuzungumza. Sikuwa namjua hata sura kwa kuwa kama
nilivyokwambia, alijawa nywele kama mnyama. Usingeweza kumsogelea wewe Max. Nina
uhakika kabisa. Alikuwa anatisha mno. Tino anapona, ndipo nakuja kugundua
kumbe anao uzuri wa kibinadamu! Sikuwa nikijua namtunza mtu wa namna gani!
Lakini Max, nilinyenyekea kwa yule kiumbe, vile alivyo kama namuhudumia Mungu
mwenyewe. Mchana, usiku bila kuchoka wala kunung’unika ila mkewe kunishauri
kumuacha. Na mkewe alipoona simuachi, naye akanikimbia akiwa ameniachia mgonjwa
mahututi. Lakini nilimwambia Tino, nitamdai Mungu wala si yeye.” Sabrina
akacheka.
“Paliponishangaza
zaidi vile njia za Mungu zilivyo za ajabu, eti Tino ananiacha hospitalini mimi
mgonjwa na dripu inanining’inia! Ananiacha hospitalini na kunidai vitu vyake!”
“Hiyo mimi sikujua Sabrina?” “Acha unafiki Max! Wewe ulimshauri Tino ahakikishe
wakati anaondoka akiniachia gari lake anirikodi nikiwa nakiri kuwa gari lake
ninalo na anirikodi nikiwa nakubali kumpa mtu atakayemtuma kuja kulichukua. Kanusha
Max.” Max akashituka sana. “Nakwambia hivi, nilikuwa nikijua na kufuatilia kila
mazungumzo yenu Max. Mpaka nikawa namuuliza Mungu, ni kwa nini anaruhusu
hata tu ile kujua ubaya mnaopanga dhidi yangu wakati sijawatendea ubaya
ila wema!” “Lakini mimi sikumwambia akupokonye ukiwa mgonjwa.” Max akajaribu
kujitetea.
“Unabisha
nini Max wewe!? Tino aliniacha kama ulivyomshauri wewe. Tena bila kujali
nitakwenda wapi wakati alinipeleka mji wa ugenini kwa ajili ya kumuhudumia yeye
mwenyewe! Aliniacha nikiwa sijui pakwenda na wala sijui chakufanya! Kama
mwanadamu nikaumia sana. Roho wa Mungu akanikumbusha ninayemdai si Tino
wala wewe, ni Mungu. Ndipo nikasamehe, na kumgeukia sasa kumdai mdeni
wangu. Nilimlilia Mungu, Max! Mchana na usiku nikimwita bila kuchoka kwa
kuwa kwanza nilikuwa siwezi kulala tena kwa hofu. Kazi ikabakia kumuita
Mungu anitetee. Bila kula wala kunywa maji, nilimuita Mungu wangu mpaka akanitumia
Jack.” Sabrina akakaa vizuri.
“Huyu
Jack uliyetaka kumdhuru huyu, ni Mungu wangu hapa duniani. Mungu anamtumia
kunilipa hapa duniani. Pengine hujaelewa kama mimi mwanzoni. Ninapomuona Jack
mume wangu na yale anayoyafanya kwangu, namuona Mungu akinilipa Max. Umbali ule
niliokwenda kwa Tino na kukunufaisha wewe, ndio anakwenda Jack mpaka mimi
naogopa! Jack ni Mungu aliyepo kazini. Huna utakalopanga dhidi ya Jack ukafanikiwa
Max. Nakuhakikishia na ninakwambia, umecheza na Mungu, na wala hatakuacha kwa
kuwa unajaribu kusimama kwenye kusudi la Mungu, ndio maana wakati wote umekosa,
hujalipwa kama safari hii.” Sabrina akaongea kijasiri.
“Kama
unafikiri upo matatizoni, umekosea Max. Bado. Ulikuwa ukitayarishwa tu,
na kutambulishwa kuwa, umecheza na moto. Wewe si ni mzuri wa
kutengeneza kesi, nakushauri jipange. Huna utakapokimbia au
utakapojificha, usionekane. Hata hapa ulipo sasa hivi, unajulikana upo
hapa. Nina uhakika barua yako ya restrain kama aliyopewa Tino, inakuja.”
Max akazidi kuingiwa hofu zaidi. “Hiki ulichokifanya hapa, ni kosa ambalo Jack
alikuonya uwanja wa ndege siku ile, ukakasirika na kwenda kupiga simu za
uchochezi dhidi yetu. Kwa kuwa wewe ni mkorofi, umekiuka alichokuagiza mume
wangu, akikuonya ukae mbali na mimi, umemdharau.” “Hapana Sabrina.
Nimekuja kwa amani kabisa. Mungu wangu ni shahidi.” Sabrina akazidi kukasirika.
“Amani
ipi Max!? Unatafuta amani baada ya kukamatwa! Ubaya wote ule uliokusudia
kuufanya dhidi yetu kama usingekamatwa si ungetenda tena kama ulivyonitenda
mimi nilipokuwa Moshi?” Max kimya. “Upo hapa kwa kuwa umekamatwa. Halafu
najiuliza Max, hata kama unapenda pesa kiasi hicho jamani! Kwa nini umenuia kuniangamiza
mimi kwa kiasi hicho!? Nilikukosea nini Max wewe isipokuwa kukuheshimu wewe na
mkeo?” Sabrina akaanza kulia. “Ulipanga mipango
mibaya sana, ya hila ili Tino aniache. Sikulalamika kwako wala kukuuliza.
Nikakuachia Tino. Ukaenda umbali wakumwambia ahakikishe haniachi hata na
ujauzito. Ukamtafutia mpaka daktari wa kunitoa mimba. Ukahangaika mpaka
ukafanikiwa na hilo. Tena unarudi tena kuja kumtaka Tino anifanyie fujo!
Unataka nini kwangu Max?” “Naomba utulie Sabrina.” Pendo akajaribu
kumtuliza.
“Hapana dada. Hujui huyu mtu kitu alichonipokonya. Wala si kwa
Tino, ila sasa hivi amevunja familia yangu dada. Nilitaka familia moja, ya
baba mmoja tu ambaye atajulikana kote mpaka kifo, kuwa ni Jack. Lakini huyu
mwanaume amenipokonya dada! Kulikuwa na amani, yeye amevuruga tena. Kila
nikitulia sehemu, ananifuata kunitenda ubaya mkubwa sana. Hayupo hapa kutafuta
amani, yupo hapa kwa kuwa safari hii uovu wake umefika mbele ya kiti cha enzi
cha Mungu wangu, amekamatwa ndio unamuona hapa. Ni muuaji huyu dada.
Simaanishi muuaji wa maneno, namaanisha mmwaga damu kabisa wa vitendo.
Hawezi kuniona nimetulia mahali nina amani, akatulia. Lazima avuruge kwa
manufaa yake. Sasa hivi mambo yamekuwa makubwa mno! Mambo yaliyokuwa yametulia.
Ameyachokonoa chokonoa mpaka yamekuwa makubwa! Tena ni yeye mwenyewe
aliyaanzisha tukiwa Moshi, nikaamua kumuachia Mungu tu. Unarudi tena nyuma
nyuma kuvuruga!? Ni nini unataka kwangu wewe mtu? Kwa nini unaumia kuniona
nimetulia!” Sabrina akazidi kulia.
“Hakika Mungu akulipe Max mpaka ujue ni Mungu anashugulika na
wewe. Umenionea vyakutosha. Ubaya wako, uovu wako na dhuluma mlizokuwa
mkifanya na Tino mkijinufaisha moja kwa moja kupitia mimi, Mungu anashugulika
na wewe. Ubaya uliotaka kunifanyia mimi, mume wangu na watoto wetu, unakurudia
wewe na familia yako. Hutatoka hapo, kwa kuwa kila siku inayokwenda kwa Mungu, unapikwa,
ukishamalizwa kwenye vyombo vya usalama, ulimwengu utakutambua, na utakuwa
fundisho Max.” Sabrina akaongea kwa hasira na uchungu sana. Akajifuta
machozi.
“Hakika hutasimama Max. Na Jack alimwambia Tino, atawashugulikia
nyinyi wawili, mpaka anamalizana na wewe, hutakaa ukawa na uwezo wa kumdhuru au
kutumia usomi wako kumuangamiza mtu mwingine tena na wala ukawa na uwezo
wakusimamia kesi ya mtu hapa mjini ila kubeba jembe na kurudi migombani.
Akamuhakikishia Tino ambaye amekimbia.” Max
akashangaa mpaka usoni akaonyesha. “Hajakuaga eeh!” Sabrina akamkejeli. “Mwenzio alipopata tu ujumbe wake kuwa ushahidi wake wote
upo, na atashugulikiwa kikamilifu. Jack akamwambia mpaka anamalizana naye,
atajua Sabrina si tambaa lakufutia matapishi kila akihitaji. Aliposikia
hivyo, akasalimu amri. Sasa bado wewe
mchochezi, unayejinufaisha kwa kupitia machozi ya watu, hukumu yako inakuja
Max. Damu uliyokusudia kuimwaga bila hatia kule Moshi, yale mauti uliyoita
kwangu kule Moshi, inakuwinda wewe na familia yako. Imekusimamia mlangoni,
ikikutaka kukumaliza wewe na familia yako kama ulivyofanya kwangu na Tino.
Mungu anakulipa. Nimemaliza, naomba utupishe na siku nyingine,
usirudie kunivizia kwenye mahoteli.” Max akasimama na kuondoka kimyakimya.
Hakuna
Msiba Usiokuwa Na Mwenzie!
S |
abrina
akiwa na hasira vilevile akageukia chakula chake ili ale, hata hakumeza chakula
alichoweka mdomoni, akaanza kujisikia vibaya. Jasho likaanza kumtoka. “Najisikia vibaya da Pendo. Moyo unaenda mbio mpaka
naona shida kufungua macho!” Pendo akaingiwa hofu, akamuita muhudumu.
“Naomba...” Kabla hajamaliza, Sabrina akakaa chini kabisa sakafuni. “Sabrina!”
“Najisikia vibaya dada. Sitaki nianguke nimuumize mtoto wangu. Usigope, ila
naomba mpigie simu Jack.” “Nikupeleke hospitalini?” “Jack kwanza dada.” Sabrina
akasisitiza. Pendo akampigia simu Jack kwa haraka.
“Sabrina anajisikia vibaya, lakini amesema nikupigie kwanza wewe
simu.” “Nipe nizungumze naye.” Pendo akamkabidhi
simu Sabrina. “Vipi Brina, mama!?” Jack akaanza
kwa wasiwasi. “Najisikia vibaya sana Jack. Mapigo ya
moyo yanakwenda mbio, hii hali haijawahi kunipata. Na ninapatwa kizunguzungu!”
“Ngoja nimpigie simu baba watume gari. Usikate.” Ndani ya nusu saa gari
ya wagonjwa ya usalama wa taifa na mama Msindai, Mzee Msindai na Jacinta wakawa
wameshafika hapo Masaki walipokuwa wamekaa wakila.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment