Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 44. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 44.

“Poleni kwa matatizo.” Mchungaji akaanza pale walipobaki wao watatu. “Kwangu nachukulia ni fundisho nililopitia baada ya kupotoka.” “Labda niseme tena kidogo. Sitaongea sana.” Pendo akaongea na tabasamu. “Karibu Pendo. Binafsi napenda kukusikia kwa kuwa pengine ni kwa kuwa huzungumzi sana!” Pendo akacheka. “Kweli. Labda leo ndio kwa mara ya kwanza nimekusikia ukizungumza. Nyinyi wote mmekuwa na ndoa nzuri sana. Na wakati wote nilikuwa nikiwaambia. Hicho mnachokifanya na kukishikilia, msikiache. Ni msaada kwa wengine. Mkadumu sana hapa. Hata mlipotengana, bado Pendo uliendelea kuja kanisani. Unakumbuka mazungumzo yetu ya mara ya mwisho ulipokuja kwenye maombi?” Pendo akaanza kulia. Willy akawa hajaelewa.

“Mungu amekurudishia na zaidi. Si Willy tu, na watoto.” Pendo akacheka na kujifuta machozi. “Wakati ule ilikuwa hata haileti maana!” Pendo akaongea na kushika tumbo lake, akajifuta machozi. “Mambo ya Mungu huwa hayaelewiki kwa akili za kibinadamu.” Pendo akanyamaza. “Ulisema kuna kitu ulitaka kuzungumza.” Pendo akavuta pumzi kwa nguvu na kucheka kidogo. “Majuzi nilipata muda wakufikiria sana. Nikakumbuka mwanzo wangu na Willy. Najua alikosa, lakini Willy amenibeba jamani!” Machozi yakaanza kumtoka tena Pendo. “Alinibeba mpaka nikawa nashangaa! Alisimama na mimi akinitetea kwa ndugu zake hata kwa mama yake bila kuchoka. Na wala Zelda hakuwa msichana wa kwanza mama yake kumtafutia Willy. Walitafutwa wazuri na warembo tu, lakini Willy alikuwa na msimamo akisimamia agano alilonipa si siku ya ndoa, zamani sana tukianza mahusiano tukiwa  chuoni.” Pendo akaendelea taratibu.

“Tokea chuo, mimi ni shahidi wa Willy, wasichana walikuwa wakimtongoza kwa siri, lakini Willy alibakia kuwa mwaminifu kwangu. Hata tulipojua mwenye tatizo linalosababisha tusipate watoto ni mimi, bado Willy alisimama na mimi. Aliniambia hivi, sijui kama atakumbuka! Kuwa ni bora abaki na mimi mpaka kifo, kuliko watoto bila mimi.” Willy akabaki ameinama. “Na ndivyo ilivyokuwa kwa Willy. Yeye hakuwa na wasiwasi kama mimi. Aliridhika, ila pressure ya familia ndio nahisi ilimzidi. Willy ni mwaminifu sana na ananipenda bila kujitahidi. Hilo sina shaka nalo.” Pendo akacheka na kujifuta machozi.

“Ninachotaka kusema ni hivi mchungaji, unatujua sisi. Kile ulichokuwa ukikiona hapa kanisani ndicho kilichokuwa nyumbani. Hatukuwa na matatizo ya siri. Na hata alipoanza mahusiano na Zelda...” “Hayakuwa mahusiano Pendo!” Willy akakanusha. “Basi niseme hata ulivyoanza kulala na Zel..” “Haina nafuu Pendo.” Willy akamkatisha tena kumsihi aache tu. “Basi niseme hata Zelda alipoingia kwenye picha, hapakuwa na utofauti nyumbani. Willy alijua Zelda amebeba mtoto wake, lakini bado aliendelea kuwa mtulivu nyumbani, japo niliona mabadiliko, ila nakiri kulikuwa na heshima kubwa tu. Willy ananiheshimu. Sijui kitakachotokea mbeleni kati yetu, lakini...” “Hakuna kingine kitatokea mbele yetu Pendo.” “Usiseme hivyo Willy. Sisi ni binadamu.” “Labda kifo au wewe unigeuke. Mimi nimejifunza kutokana na kosa.” Pendo akamwangalia, akaamua aendelee.

Anyway, ninachotaka kusema ni kuwa, najua wapo wanandoa wanatoka nje ya ndoa na kuumizana sana kipindi hicho wakiwa na mahusiano ya nje. Najua pia ndoa zinachangamoto zake nyingi, lakini nilipenda ndoa yangu. Nampenda Willy. Kama Mungu akitusaidia tukarudi kwenye ndoa ya namna ileile, nitashukuru. Ningependa watoto wangu wazaliwe na kukua kwenye mazingira ambayo Willy yupo kwenye maisha yangu. Waone na kuonja ule upendo alionao. Tabia ya uadilifu na kujituma katika mambo. Kwa hiyo nilikuwa naomba utusaidie ikiwezekana wanangu wazaliwe tukiwa ndani ya ndoa.” Pendo akaongea kwa upole. Akawa amemaliza.

Mchungaji akavuta pumzi kwa nguvu na kujiweka sawa kitini. “Na mimi naahidi hutakaa ukafungisha tena ndoa yangu na Pendo. Hii ni mara ya pili na ya mwisho kwa kuwa haitakaa ikavunjika tena.” Mchungaji akacheka akimtizama Willy. “Unauhakika Willium?” Mchungaji akamuuliza. “Kwa asilimia 100.” “Labda nikuulize Willy. Nijibu tu bila kuuliza au kwenda mbali na swali.” “Sawa.” Willy akakubali.

“Watoto aliobeba Pendo ni wa miujiza haswa. Hilo kila mtu anajua mpaka madaktari wake kama sikosei, si ndio?” Pendo akatingisha kichwa kukubali. “Siombei kitu kitokee. Lakini hawa watoto ni wa Mungu na nyinyi mmepewa tu dhamana. Sasa je, mwenye nao akiamua kuwachukua?” “Inamaana mimba itoke na watoto wafe?” Kama kawaida ya Willy akaenda kulitengeneza swali na kuliweka wazi kabisa. “Ndiyo.” Ikabidi mchungaji akubali tu. Pendo kimya. “Nakujibu jibu ambalo nilimjibu Pendo mwenyewe na ndugu zake. Sijarudi kwa Pendo sababu ya watoto. Nimerudi kwa Pendo kwa sababu amenipokea. Angenifukuza Pendo, na akaniambia watoto alionao ni wangu, ningewatunza bila shida na yeye angeendelea na maisha yake na mimi hivyo hivyo. Mimi bado nikijana mchungaji. Kama mzee Ngoi mpaka leo anaweza kuoa, nashindwaje mimi!?” Hapo Willy akawa ameongea uhalisia.

“Kwa hivi nilivyo, ninauhakika ningeweza kutafuta mwanamke mwingine yeyote nikaoa na nikaanzisha familia bila shida. Lakini Pendo ni Soulmate wangu. Hakuna jinsi nikawa nafuraha na mwanamke mwingine, nikijua Pendo wangu yupo! Narudia tena, labda ingekuwa Pendo amenikataa. Kwa hiyo nipo hapa mbele yako si kwa sababu ya watoto aliobeba Pendo, ni kwa sababu ya Pendo wangu. Nampenda Pendo. Japo sitaona haya kusema nimefurahia kumkuta Pendo na watoto. Hilo sitadanganya kwa kuwa najua litampa utulivu Pendo mwenyewe aliyekuwa akiwataka hao watoto mchana na usiku. Muulize Pendo kama mimi nilikuwa namsumbua kwa swala la ujauzito!” “Amekiri mwenyewe.” Akajibu mchungaji.

“Na ni kweli. Na penda watoto, lakini si kama Pendo. Nilifikia hatua mimi nikamwambia Pendo, tena kwa kumuomba Pendo tuachane na maswala ya watoto, maana niliona namkosa na Pendo mwenyewe! Kulia kila wakati, na kila nikiwa naye anachozungumzia ni watoto tu! Nikamuomba tuache kabisa. Akalikubali hilo, tukatulia. Nikaenda umbali wa kuonya kila mtu nyumbani, asizungumzie lolote na mke wangu juu ya watoto. Wakakubali japo ilikuwa kwa shida na kubishana sana, lakini wakaliheshimu hilo, angalau tukatulia. Muulize Pendo kama kuna hata mtu alimsumbua tena juu ya watoto.” Pendo kimya.

“Nikashangaa wakati Zelda ni mjamzito, akaanza tena kitu ambacho tulishafunga mjadala. Akaanza tena habari za watoto wakati mpaka nilimwapisha asizungumzie tena swala la watoto isipokuwa mapenzi yetu sisi tu wenyewe. Tukakubaliana wakija sawa, wasipokuja pia ni sawa. Na kweli Pendo akatulia kabisa, na kurudia hali yake ya zamani kabisa. Kwani maswala ya watoto yalianza kumfanya azeeke, mpaka usoni alikuwa kama amechoka! Kwa mara ya kwanza alipolirudisha hilo la watoto nikawa mkali kwake japo yeye anafikiri ilikuwa sababu ya Zelda. Lakini ni kwakuwa nilijua itaanza tena shida ileile. Mahangaiko yaleyale wakati tulisharidhika. Kumbe mwenzangu alikuwa akitembea kwenye imani kwa maombi aliyofanyiwa na Sabrina! Ndiye aliyemrudishia tumaini la hawa watoto. Kwa hiyo naomba nikuhakikishie mchungaji, mimi nitatulia. Na Mungu anisaidie.” “Hapo umeongea.” Mchungaji akamalizia.

“Nataka Sabrina anisimamie harusi. Ndiye aliyesimama na mimi kipindi nimeachika, na ndiye aliyerudisha imani ndani yangu mpaka nikapata hawa watoto. Amekuwa akiniombea kuanzia mwanzo mpaka sasa. Ni mtu wangu anayesimama na mimi mchana na usiku. Ila anajifungua mwezi ujao. Nilitaka harusi kabla hajajifungua. Haitakuwa kubwa, ndogo tu, lakini lazima Sabrina awepo.” Mchungaji akacheka. “Kisheria nilazima tutangaze. Tupange tarehe ya harusi, na tuanze matangozo angalau hata mara mbili tu kuweka nafasi kwa uma.” “Sawa.” Wakazungumza hapo ofisini kwa mchungaji na kuweka tarehe ya harusi kabisa, wakatoka wakiwa wameridhika. Wakampita Zelda hapo nje ya ofisi, wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakarudi nyumbani wakiwa wamejawa furaha. Kwani hata walipokuwa kwa mchungaji waliombana tena msamaha, wakasameheana. Mchungaji alizungumza nao kwa kina tu, na kuwaombea. Wakatoka hapo wapo ukurasa mmoja, wamejawa amani wanazungumzia ndoa tu. Pendo alipofika tu kitandani kwake, akaanza kupiga simu akitangaza tarehe yao ya harusi. Pendo akataarifu ndugu zake wote akiwa amejawa furaha, akisema haamini kama Mungu amemrudishia Willy wake. Alijawa vicheko na kilio kwa furaha. Wakati Pendo anaongea na watu wake, Willy akatoka hapo chumbani.

Willy akaanza kufikiria amtaarifu nani kwenye familia yake. Hawakutaka kualika watu wengi, ni watu wa karibu tu na wenyewe mahusiano ya mara kwa mara sio ndugu wakutafutana mara moja kwa mwaka! Hao walikubaliana wawaache. Hawakutaka kitu kikubwa na wala hawakutaka kutumia pesa nyingi kulisha watu. Walitamani hata wasizidi 30. Willy alikaa pale akifikiria ndugu zake, akaanza kuwachuja mmoja baada ya mwingine. Ubaya waliomtendea yeye tokea alipokuwa na Pendo mpaka kuja kumuuzia mbuzi kwenye gunia! Zelda! Wote akaona asiwarudishe tena kwenye maisha ya Pendo kwa wakati ule anao tarajia watoto, na afya yake haijakaa sawa. Akaona upande wake yeye asialike yeyote hata marafiki. Bado kazini alikuwa mgeni hakuwa na rafiki wa karibu wa kiasi hicho. Akaamua atulie tu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Na huku kwa Sabrina na Jack walipopata tarehe ya harusi ya kina Pendo, ilikuwa karibu kabisa na Sabrina kujifungua. Kama week hiyo hiyo. Ikabidi Jack kuweka mipango ya kueleweka ya yeye na familia yake kuwepo Dar kwa muda wakutosha mpaka Sabrina na mtoto huyo atakayezaliwa watakapokuwa tayari kwa safari ya kurudi tena Singida. Wakawekeza nguvu kwenye kukamilisha nyumba. Na kwa jinsi walivyoiona, haikuhitaji marekebisho mengi. Akamuomba shemeji yake amsaidie kutafuta watu watakayoisafisha vizuri. Ndani na nje. Maswala ya maji na umeme kuhakikisha pako sawa. Wakatuma kiasi cha pesa walichonacho na wanachotaka kitumike kwenye hiyo nyumba. Joy akawaambia atawasaidia. Huo mpango ukakaa sawa.

Kina Jacinta, Nancy na Jena pamoja na wazazi wakawasaidia kuandaa hiyo harusi. Kuanzia Pendo mwenyewe, mavazi na maswala ya saluni. Hawakutaka wasimamizi wa watoto, lakini Joy na Junior wakabembeleza mpaka wakakubaliwa mtoto wao asimamie. Kwa hiyo wakagaramia mtoto na maua. Wakati huo Willy anatafuta sehemu ya fungate.

Hakuna Msiba Usiokuwa na Mwenzie.

W

akati ofisi za serikali zinahamia Dodoma mji mkuu wa Tanzania, mama Kundi na baadhi ya wenzake wakabahatika kubakishwa Dar. Likawa jambo la furaha kwa kuwa hawakujua ingekuaje kwa familia kutengana. Lakini wakiwa kwenye hofu ya Msindai, na bosi wake akipita na kuendelea na shuguli zake bila kuonyesha kuna tatizo lolote lile, siku ya alhamisi mama Kundi akapokea barua ya uhamisho. Barua ilimtaka akaripoti katika kituo kipya cha kazi kwenye ofisi zao jijini Dodoma, jumatatu inayofuata. Alishituka karibu kuchanganyikiwa. Akatamani kumpigia simu Max, lakini akaogopa tena mawasiliano yao yasije kamatwa.

Akaamua kwenda kulalamika kwa meneja wake. Meneja akamwambia ni agizo lililokuwa limetolewa kutoka zamani kuwa serikali ihamie Dodoma, ila wao walikuwa wakitekeleza kwa awamu. Zamu yake imefika, anatakiwa akaripoti kazini. Akamshauri kama anayo malalamiko yeyote yale, aandike barua kupinga agizo la kuhamia Dodoma. Mama Kundi alikuwa kwenye hali mbaya kwani biashara zake zote zilikuwa jijini Dar. Anaondokaje kuacha biashara zake, mume na watoto wanaosoma! Nani atasimamia nyumba yake! Lakini alitakiwa aondoke, au aache kazi. Kuacha kazi napo ikawa ngumu kwani alishatumikia serikalini kwa miaka mingi sana. Kuacha kazi kwa kukataa kazi ni kupoteza haki zake nyingi sana ambazo angepewa kama angesubiri mpaka kustaafu kwake!

Kwa Tino.

Alibakiwa na ile hali mpaka alipotoka kazini bila kumtaarifu yeyote kwa simu kwa hofu ya kusikilizwa mazungumzo yao. Hofu ilizidi kuwaangia walipofika wote nyumbani na kuzungumzia hiyo hali na kinachowakabali. Hapo ndipo wakajua maji yamezidi unga. Waliotangulia wametangulia, na kina Msindai wanacheza mchezo wa kiutu uzima, kihalali kabisa. Wakajua wao wameshika kwenye makali, wanaumia. Mama Kundi na mumewe ikabidi sasa kumfuata Tino wazungumze na wajipange.    

Wanafika kwa Tino, wakagundua na Tino naye alishapewa barua kutoka kwa mwanasheria wa Msindai. “Kwa nini hukuniambia!?” Max akalalamika akishangaa. “Hapa nimechanganyikiwa, nilikuwa nikifikiria jinsi yakujipanga upya.” Ndipo wakaomba kusoma barua yake. Baada ya kuwazungusha kwa hili na ile akishindwa kuwaonyesha barua yake, Max akahisi lipo jambo.

“Nini kinaendelea Tino?” “Mimi nilikuwa Cliff kwa mambo yangu ya kikazi. Ndipo nikawaona wanangu na Jack. Hakika ile ni damu yangu. Ilikuwa ni birthday yao yakutimiza mwaka! Nikaumia! Nahisi ni kupaniki, nikatafuta muda ambao wametoka katikati ya kundi ambalo walikuwa wamekusanyika kwa ajili hiyo, mimi nikawafuata. Mambo hayakuwa mazuri, nikapaniki na kuongea hata ambayo sikuwa nimekusudia. Nikawatisha nikitumia ushawishi wako kwangu kuwa nirudi huku nchini, tuwadai hata kisheria wale watoto ni haki yangu na mimi. Hapo ndipo nafikiri yule jamaa akakasirika sana. Kaka yake akaja, akanikuta nimesimama nao pale tunaongea.” “Kaka yao waziri Msindai!?” Wakauliza kwa pamoja. “Ndiyo.” “Basi wewe ndio umeharibu Tino.” Wakaanza kumlaumu Tino kwa kumshambulia.

“Hebu subirini kwanza!” Tino akawakatisha kwa kuwashangaa sana tena kwa ukali. “Mbona mnataka kunichanganya sasa hivi? Maswala kama nina watoto huku nchini niliyatoa wapi kama sio wewe Max kunipigia mwenyewe!?” Tino akauliza kwa ukali.  “Tena ulinipigia simu kwa ushawishi mkubwa sana ukitaka nirudi kudai watoto wangu na ukaniambia unayo mipango mizuri tu. Ulinishawishi na kuniambia ninahaki kisheria kudai watoto wangu! Nimekutana na kina Jack na Sabrina. Nikaeleza nia yangu juu ya watoto wangu. Kaka yao alikuja mwisho kabisa tumemaliza mazungumzo. Akauliza kama ni kwema, mimi nikaondoka bila hata yakujibu. Sasa kosa langu lipi!?” Tino akawashangaa kwa ukali.

 “Wale ni ndugu Tino! Unafikiri hawatazungumza?”  Akauliza mama Kundi akiwa amepoa sio jazba tena ila akilaumu. “Halafu na mazungumzo yetu tulimtaja huyo waziri, kama watu wa usalama walinyaka hayo mazungumzo na kumpa Jack, unafikiri watashindwa vipi kumfikishia waziri mwenyewe!” “Subiri kwanza Max. Msitake kunichanganya mimi!” Tino akawakatiza tena. “Unazungumzia nini!? Mimi na wewe hatukuzungumzia swala lolote juu ya waziri, isipokuwa watoto wangu. Maswala ya waziri mimi sipo kabisa na sifahamu ni nini mnazungumzia!” “Ni mimi na mke wangu.” Max akajibu akiwa amepoa kama aliyeishiwa ujasiri. “Hapo sasa sijui! Huko sipo. Mimi nimedai wanangu kama ulivyonishauri, basi. Sikutishia familia ya Msindai.” “Kwa nini hutaki tuone barua yako Tino?” Akauliza mama Kundi. “Nahisi haiwahusu.” Wakashangaa sana.

“Tokea lini mambo yako hayatuhusu wewe Tino?” Akashangaa sana mama Kundi. “Isingekuwa kukuthamini, wala usingekuwa hapa leo! Max alikufanyia uungwa kukutaarifu swala la watoto, leo unamkana!” “Hapana. Alifanya kwa ridhaa yake na sababu zake anazozijua yeye mwenyewe. Mimi nilishamwambia watoto ni wa Sabrina! Kwa nini yeye aliendelea kuning’ang’ania, akinitafuta hata nilipomkatia simu!?”  Hapo ukalipuka ugomvi haswa. Kukanana kukaendelea. Mama Kundi akilia na kutukana wote wawili. Max mumewe, na Tino ambaye alimuita hana shukurani na ndio maana Lela alimtenda. Wakagombana haswa!

“Subiri kwanza mama Kundi. Naona unakwenda kusiko kweli.” Hapo Tino akaamua kuvua uvivu na kuzungumza. “Mimi sijui huwa mumeo anakwambia nini au alikushirikisha nini juu ya kesi yangu, lakini nipo hapa, hivi unavyoniona peke yangu kwenye hili jumba, sababu ya ushauri ambao najutia sana kuusikiliza na kuutendea kazi, kutoka kwa mumeo.” Tino akaendelea akiwa anatetemeka kwa hasira. Max akataka kukana, akamkatisha. “Kwanza nilikushangaa sana uliponipigia simu na ndio maana nikakukatia simu. Ni kama unayetaka kunichanganya tu.” “Kivipi wakati mimi ndiye niliyekusaidia?” Max akahamaki.

“Katika lipi na sasa hivi unataka nini?” Tino akauliza kwa ukali. “Ni wewe mwenyewe uliniambia niachane na Sabrina.” Mkewe akashangaa sana. “Haiwezekani Tino! Wewe ni muongo. Mpaka leo Max hajui kilichotokea kati yako na Sabrina!” Tino akashangaa sana. “Unanitania mama Kundi!? Ndivyo anavyokudanganya mumeo?” Mama Kundi akatulia kidogo na kumwangalia mumewe.

“Sikumleta kwenu Sabrina na kuwaambia nimepata mwanamke anayenipenda na kunijali?” Tino akauliza na kuendelea. “Umesahau mama Kundi tulitoka kwenu tukiwa tunakwenda kuanza upya?” “Mpaka nikawapa na ushauri!” “Basi mumeo alikuja kubadilika kabisa na kunishauri tofauti na hivyo. Akanishawishi na kunichanganya kabisa. Yaani simu yake ya mwisho akinishawishi nirudi kudai watoto kuna sehemu kidogo alijichanganya ndipo ikabidi kuanza kujipa muda kwa upya na kukumbuka neno moja hadi jingine juu Sabrina, kwangu. Mumeo, anaakili sana. Yaani nikitafakari sasa hivi, huwa nashangaa mpaka mapigo ya moyo yanabadilika! Najiuliza, hivi ilikuaje! Hakika sijapata jibu mama Kundi! Kutoka kwenye kumpenda Sabrina, alihakikisha anatembea na mimi hatua kwa hatua, akinipa shutuma chungu sana za Sabrina, mpaka akanifikisha sehemu nikamgeuka Sabrina na kumuacha Sabrina kabisa. Tena vibaya sana.” “Haiwezekani!” Mama Kundi akapinga akimtetea mumewe.

Tino akacheka kwa masikitiko akaendelea kama anayejaribu kukumbuka hila za Max. “Hakika wewe ni kiboko Max! Mimi ni mjinga kwa kukusikiliza ushauri wako wa kinyama, lakini wewe ni katili aisee! Yaani alikuwa ananikaba, sihemi, akisema nihakikishe sifanyi kosa la kumuacha Sabrina na mimba yangu.” “Kwa nini aseme hivyo!?” Mama Kundi akauliza kwa kushangaa sana. “Wakati huu nimetulia ndio naamini kile alichoniambia juu ya Sabrina hakikuwa cha kweli, japo sina uthibitisho, ila kwa jinsi ambavyo nimeanza kuujua moyo wa mumeo kwangu kuwa ni pesa tu wala si kunijali mimi, nahisi nia yake ilikuwa ni ashinde ile kesi ili nimlipe ile pesa niliyomlipa. Alikuwa masikioni mwangu masaa yote akiniambia maneno mengi ya kumchafua Sabrina kwangu akisema ni uchunguzi ameufanya. Ila kila nikikumbuka ushawishi wake kwangu juu ya Sabrina, hakika ni kosa langu mwenyewe kwa kuwa ni mimi mwenyewe nilishindwa tu kumsikia vizuri kwa wakati ule. Nilichagua cha kusikia na kuamini. Maana alikuwa akisisitiza sana akisema kama nishafanya kosa la kumpa Sabrina mimba basi nirekebishe haraka kabla kesi kutajwa ili Lela asije nizidi kwenye MALI, ikaonekana mimi ndiye nimetoka nje ya ndoa sio yeye.” “Kwamba urekebishe kwa kutoa mimba!?” Mama Kundi akawa ameelewa ila anapingana na ukweli. “Abishe Max sasa hivi.” Mkewe akamgeukia Max akitamani akanushe.

“Max?” Mkewe akaita kwa ukali. “Haikuwa hivyo moja kwa moja.” “Acha kumdanganya mkeo Max. Swala la kuwa Lela alikujia ofisini akiwa si mjamzito kama ilivyokuwa imesemekana, kwa hiyo na mimi niwe makini kabisa tena nisirudi na Sabrina Dar, lilitoka wapi?” “Haiwezekani Max!” Mkewe akasikika akiwa ameumia sana. “Mama Kundi, mumeo ndiye aliyenishawishi na kusimamia kumtoa mimba Sabrina. Sikuwa napumzika! Mchana, asubuhi na usiku yupo kwenye masikio yangu akitaka nimsafishe kabisa Sabrina, asibakiwe na mimba yangu ili tushinde kesi, huku akisema tuhuma nyingi za Sabrina ikiwepo ya uchawi kwamba kwao ni wachawi pamoja na shutuma za Sabrina na dada yake kunilia njama ili wampindue Lela, niwe na yeye Sabrina anufaike na pesa yangu. Akanithibitishia Sabrina ni tapeli hana mapenzi ya kweli kwangu, kama ilivyokuwa ikionekana. Sasa ili kumzibiti ni kumtoa mimba asije rudi na watoto na kunidai mali!” “Mungu wangu Max!” Yule mama akazidi kuumia.

“Na hakutulia Max mpaka alipohakikisha nimemfikisha Sabrina hospitalini kwa daktari wa kutoa mimba ambaye ni yeye mwenyewe Max alinisaidia kumtafuta. Sijui alimpata wapi, lakini alinipa jina na namba za simu. Wakakubaliana na huyo daktari mpaka kiwango cha pesa cha mimi kumlipa huyo daktari kwa kazi ya kumtoa mimba Sabrina. Sijui Sabrina alifanya mchezo gani! Hakika mpaka leo nimeshindwa kuelewa. Lakini mimi nilifanya kama Max, mumeo, alivyoagiza. Kumpeleka Sabrina mpaka kwa huyo daktari wake wa kuua watoto wangu, na nilimuacha Sabrina hospitalini akiwa amewekewa dripu kama mgonjwa kabisa aliyetolewa mimba. Nikamuacha hapo maana Max aliniambia na hilo, nihakikishe sirudi naye Dar. Kwa kuwa Lela anamsaka sana Sabrina kama shahidi wake. Akaniambia nisije onekana na Sabrina popote pale. Basi nikamuacha Sabrina hospitalini, akiwa kama mgonjwa na nikashuhudia ana dripu kabisa amewekewa ile sindano ya mkononi.”

“Mpaka leo nashindwa kujisamehe kumuacha Sabrina hospitalini wakati yeye aliniuguza mkiwa nyinyi wooote, mmenisusa. Mkaja kurudi na ushauri wenu mlipojua nipo hai, bado pesa yangu itawasaidia. Alichofanya Max mumeo ni kuhama tu upande. Kutoka kula pesa yangu kwa kupitia Lela aliyekuwa akimsaidia madai yangu wakati mimi nipo mahututi kitandani, na kuhamia upande wangu mimi mwenyewe alipoona nimerudisha uhai, nachukua pesa yangu kwa Lela, na yeye atakuwa upande wa Lela, usio na masilahi.”

Anyways, aliponifanya mumeo, nianze kufikira kwa makini sasa, ni ile simu yake ya kurudi nchini nije kudai watoto, na kuendelea kunitafuta  japo nilimkatia simu. Ikabidi nianze kujiuliza kwa upya. Hivi huyu Max aliyehangaikia mpaka tiketi yangu kuhakikisha narudi Dar bila Sabrina, baada ya kuua watoto wangu mwenyewe, inakuaje tena mtu huyuhuyu aliyenishauri na kusimamia kuua wanangu hatua kwa hatua, bila aibu wala huruma, iweje leo anarudi tena kuniambia nikadai tena watoto walewale aliosema tuwauwe ili wasije rudi kudai MALI! Hapo nikabaki kujiuliza bila jibu. Lakini nikajiuliza tena au huyu Max, mwenzangu pengine kwa kuwa yeye watoto wake hakuna aliyemshauri awauwe na anaye mke wake, ametulia kwake, ni kwamba amesahau au la! Lakini. LAKINI. Nikaja kukumbuka tena pale aliponipigia tena simu ya kurudi kudai watoto wangu, alibadilika tena pale nilipomwambia watoto si wangu ni wa Sabrina, akanishauri tena tumtengenezee tena Sabrina kesi, tuseme wakati ule nafanya yote yale sikuwa kwenye akili timamu, nilikuwa mgonjwa.” “Mungu wangu!” Mama Kundi mikono kichwani.

“Yaani tena mumgeuke tena sabrina huyohuyo!?” “Yeap! Tena si kumgeuka tu Sabrina, hapo ukituliza mawazo na kufikiria, ni kwamba hata mimi ananigeuka. Ananiambia yote yaliyotokea Moshi, yeye hausiki ni mimi tu.” Tino akamjibu mkewe macho kwa Max. “Huo ndio ushauri kutoka kwa mumeo, huyo hapo mpaka mimi mwenyewe nikamkatia simu. Na ndio maana mmeona nimerudi lakini nimeshindwa hata kuwatafuta.”

“Namtafakari mumeo sipati jibu! Najilaumi ni kwa nini nilimruhusu anifanye mimi kama mjinga! Tena mjinga wa kiasi hiki! Hakika namuwaza Max mpaka silali kwa hofu. Na hofu kubwa niliyonayo nahisi ni yale maovu yangu mimi mwenyewe. Halafu kuja kuona hao watoto nilioshauriwa na mumeo niwauwe! Hakika nimeshindwa kulala. Nakunywa madawa ya usingizi ili niweze kulala.” Tino akazungumza kwa uchungu sana.

“Na ndio maana hata nilipopata hii barua kutoka kwa kina Msindai, nilibaki kimya. Kila nikiwaza, najuta na kubakia nikijiambia tatizo kubwa na aliyenifikisha hapa mpweke hivi ni Max.” “Ni kweli ni Max!” Mkewe akaongea kwa uchungu sana. “Max amenitenda kwa faida yake yeye wala si ya mtu mwingine. Amenishindia hii nyumba lakini amenipokonya Sabrina ambaye nilimwambia wazi kuwa ni mwanamke pekee aliyenipenda kwa dhati. Lakini Max alihakikisha anamtoa kwangu vibaya sana na kuua watoto wangu! Leo anakuja nyumbani kwangu anataka kujua kinachoendelea tena kwenye maisha yangu! Hakika ondokeni kabla sijamuita mlinzi. Kama ulifikiri utatengeneza pesa nyingine kupitia kesi yangu, hapana. Acha kwa mara ya kwanza, na mimi nifikirie kwa akili zangu nikiwafikiria binti zangu na Sabrina ambaye ulinifanya nimtelekeze vibaya sana.” Tino akasimama na kufungua mlango. Akamuita mlinzi. Mama Kundi alipoona hivyo akasimama kwa haraka na kutoka. Max akafuata kimya kimya akijua hata nyumbani kumeharibika.

~~~~~~~~~~~~~~~~

 Itaendelea....

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment