Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 43. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 43.

 Zelda, Willy & Pendo hospitalini Kwa DNA.

Wakati wapo njiani kila mmoja akiwaza lake, Pendo akapata wazo. “Nashauri majibu ya hii DNA tukayafungulie kwa mchungaji Swai na kuweka naye mipango yote ili kila mmoja atoke hapo akiwa ameridhika, au unaonaje Zelda?” Willy akamtizama Pendo na kurudisha macho barabarani. “Mimi nakushukuru sana dada yangu, maana ingekuwa mtu mwingine kwa tulichokutendea, usingesamehe. Nilikuwa na mahusiano na mumeo, nika...” “Hukuwa kwenye mahusiano na mimi.” Willy akapinga kwa jazba.

“Mimi sijui wewe unaitaje! Naomba nisamehe. Lakini mimi namaanisha ile tu kulala na wewe tena zaidi ya mara mbili na yeye kujua na kusamehe! Binafsi namshukuru.” Pendo akanyamaza kimya na kugeukia dirishani. Willy akajua kimemuumiza. “Chochote utakachonishauri dada yangu nitakusikiliza.” Zelda akaongeza kwa unyenyekevu, Pendo akabaki kimya. Akarudisha mawazo kwa watoto wake, akaendelea kujisugua taratibu tumbo lake. Pakatulia.

“Hongera dada, naona na wewe Mungu amekujalia.” Zelda akavunja ukimya. Pendo akatamani asijibu lakini akaona awe muungwana. “Asante.” Akajibu Pendo taratibu tu, Willy akitamani amwambie asizungumze chochote huko nyuma alipokuwa amekaa. “Mungu mkubwa, ndio maana mimi nimemgeukia. Nimeshajua maisha, nimeamua kutulia kabisa.” Akaendelea Zelda taratibu tu. Kimya kwa Pendo na Willy wanasikiliza. “Maana mama Ngoi alikuwa akinihakikishia kuwa nisiwe na wasiwasi kumbembea mimba mumeo maana huna kizazi na wala hutakuja kuzaa.” Willy alitamani kuchanganyikiwa, akafunga macho na kutingisha kichwa wakiwa wamesimama kwenye mataa. Pendo kimya.

“Hata wifi Stella na..” “Tafadhali nyamaza Zelda. Tafadhali sana.” Willy akamkatisha. “Kwani nimeongea baya gani mimi! Nimemtukuza Mungu kwa kile alichokifanya! Amemuabisha shetani na kazi zake. Sasa mimi nimekosea wapi!?” Zelda akauliza taratibu tu. “Maana kuna kazi za Mungu. Akifanya jambo lake utajua tu, ana...” “Nimekwambia nyamaza Zelda. Wewe ni mtu gani huwezi kusikia na kutii!? Utapungua wapi ukinyamaza? Nimekwambia nyamaza, tafadhali nyamaza. Upo ndani ya gari yangu mimi, nimekwambia nyamaza. Kamtukuze huyo Mungu wako sehemu nyingine lakini si hapa. Umenisikia na kuelewa?” Willy akaongea kwa kugomba, Pendo macho nje ya gari ametulia kimya. “Sawa. Na samahani kama nimewaudhi. Nia..” “Basi. Nyamaza na usizungumze tena. Usiombe msamaha wala usieleze chochote. Sitaki kukusikia hapa. Tukafanye kinachotupeleka hospitalini, basi.” Willy akamkatisha kwa haraka sana tena kwa ukali. Zelda akanyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Walifika hospitalini gafla Pendo akawa anajisikia kochoka kabisa kama asiyetaka kuwepo pale. Akawa ametulia kabisa, amejishikilia tumbo lake. “Kwa kuwa leo ni jumapili, sidhani kama tutachukua muda mrefu.” Willy akamwambia kwa upendo, Pendo kimya akitembea kuelekea mapokezi. Wakaandikisha na kupelekwa kumuona daktari na kufanyiwa vipimo, Willy akitumia kadi yake ya hospitalini. Waliambiwa vipimo vitachukua siku tatu mpaka saba, Willy atapigiwa simu yakiwa tayari. Akaomba hayo majibu yafungwe ili waje wayafungue pamoja. Kisha Pendo akawa muungwana. Akahakikisha Zelda anapata daktari wa watoto. Akalipia matibabu yote, akampa na pesa ya taksii yakumrudisha nyumbani kwake.

“Lakini kabla hatujaachana, naomba nisaidie simu yako mara moja.” Willy na Zelda wakawa hawajaelewa, lakini kwa pesa aliyopewa na msaada, Zelda akamkabidhi. Wakamuona anapekua hiyo simu na kufuta namba ya simu ya Willy. Akatafuta kama kuna jumbe, akafuta kila kitu mpaka mawasiliano na jumbe za zamani bila kusoma. Aliporidhika hakuna alichobakisha cha Willy kwenye ile simu, akamrudishia. “Majibu yakitoka, nitakupigia ili tukutane kwa mchungaji tuwekane sawa. Sijui una swali?” “Naomba usimuulize hivyo Pendo. Wewe umeshahakikisha mtoto ameangaliwa, hana tatizo. Umempa pesa zaidi ya nauli yakumrudisha tulipomtoa, inatosha. Naomba tuachane kwa sasa.” Pendo akanyamaza. “Asante dada.” Akawa kama amemkasirikia Willy, Zelda akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakarudi kwenye gari Willy akifikiria chakuzungumza. Pendo alikuwa ametulia kimya. “Asante kusimamia hili na kuhakikisha linakamilika.” “Bado halijakamilika.” Pendo akajibu. “Lakini hata ulichofanya mpaka sasa ni kikubwa na wazo la kumalizana kwa mchungaji nimelipenda. Ni la busara na litatusaidia kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja.” Pendo akajua anajaribu kujirudi. Lakini alishakuwa amechafuka moyoni kupita kiasi. Zelda alimtibua kupitiliza. Hakujua aseme nini tena. Mpaka hapo hamu ya hiyo ndoa ilishamuisha. Akanyamaza bila ya kujibu.

“Nakupenda Pendo. Nakupenda sana mpenzi wangu.” “Lakini haibadilishi kuwa umenisaliti Willy!” Machozi yakaanza kumtoka Pendo. “Tena uliniacha kwa sababu ya matatizo niliyokuwa nayo wakati tuliahidiana tutasimama pamoja kwenye maisha yetu yote Willy! Uliniahidi tokea chuo kuwa utakuwa na mimi katika maradhi na furaha, lakini ukanikimbia! Moyo wangu unauma sana na nashindwa kupinga wazo la kuwa upo na mimi hapa sababu ilishindikana kwa Zelda. Inamaana kama Zelda angekukubalia mkaanze maisha na wewe, kwa hakika usingekuwa na mimi sasa hivi Willy. Najisikia mimi ndio chaguo la pili kwa kuwa huko kulishindikana.” “Najua ni hasira tu Pendo, lakini nina uhakika sivyo moyo wako unavyokwambia. Unazungumza kwa kupitia hisia zilizoumizwa. Lakini moyoni unajua kwa hakika sina mwanamke ninayempenda hapa duniani isipokuwa wewe. Najua hilo unalijua kwa hakika.” Willy akaongea kwa uhakika kabisa. Pendo akanyamaza nakuendelea kujifuta machozi.

Jumapili hiyo ikataka kuisha tofauti na walivyotarajia Pendo na Willy. Waliianza kwa furaha hata wazazi wa Pendo wakijua wanakwenda kuandikisha ndoa. Lakini wawili hawa wanarudi nyumbani hawaongeleshani! Walipofika nyumbani Willy akamfungulia mlango wa gari, akashuka na pochi yake. “Asante.” Akashukuru Pendo kwa sauti ya kinyonge, akaingia ndani moja kwa moja jikoni. Akajiwekea chakula chake na Willy mezani, akaanza kula chake. Willy akaja, na yeye akaanza kula kimya kimya. Pendo akamaliza yeye wa kwanza. “Nakwenda kuoga nijipumzishe mpaka asubuhi. Usiku mwema.” Akaaga na kuondoka. Hawakuwa wakilala chumba kimoja bado. “Asante na wewe.” Willy akajibu wakati Pendo akielekea kwenye chumba kilichokuwa chao wote wawili.

          Willy na yeye akaoga, akakaa chumbani kwake akijiuliza hili na lile. Kwa hakika alimuhitaji Pendo, msichana waliyekuwa wote miaka yote. Anampenda Pendo. Pendo amempokea na kumpa sehemu ya kuishi bila shida. Willy hakutaka apoteze tena ile hali ya utulivu pale. Akatoka na kumfuata chumbani kwake, akamkuta amelala. Amezima taa kubwa ya juu, amebakisha ndogo ya mezani. Akapanda kitandani akajilaza akijua wazi hajalala.

“Samahani nimekusaliti, nilitoka nje ya ndoa na kukuacha kipindi ukinihitaji Pendo. Nisamehe nilikosa sana.” Kimya. “Kwa sababu yeyote inayokujia sasa hivi. Unayosikia kutoka kwa watu, naomba ujue ni kweli nimekwama huko nje, lakini nimekurudia wewe kimbilio langu. Najua ni kwako tu ndipo nitakuwa salama Pendo. Ningeweza kujificha popote na aibu yangu, lakini nakujua utanisitiri aibu yangu, utasimama na mimi kwa kuwa ndivyo ulivyokuwa ukifanya wakati wote.” Willy akaendelea taratibu akimbembeleza.

“Katika ahadi zetu tuliahidiana kuwa pamoja kwenye shida na raha. Nimerudi kwako nikiwa nipo kwenye shida. Naomba usinitupe.” “Sikutupi Willy, ila nimekasirika.” “Naomba nikukumbatie vizuri na kukubusu, pengine hasira itapungua.” Willy alimjua Pendo, mpenda kubembelezwa. “Pendo?” Kimya. “Au umenichukia kiasi hutaki nikuguse kabisa?” “Nataka Willy.” Pendo akajibu kwa kudeka, Willy akajisogeza kwa haraka, akamkumbatia na kuanza kumpapasa taratibu. “Nisamehe Pendo. Nataka tubaki pamoja.” “Na mimi nataka tubaki wote Willy, lakini bado nina maumivu. Nipe muda naamini nitakuwa sawa.” “Ilimradi tupo wote, sina tatizo. Nitakusubiri mpaka utakapokuwa tayari. Ila mipango ya harusi si inaendelea kama kawaida?” Akamuona amenyamaza.

          Akamnyanyua uso na kuanza kumbusu midomoni kwa muda kidogo, kisha akamuachia. “Usibadilike bwana!” Akambembeleza. “Labda tusubiri hili lipite Willy. Tusijichanganye.” “Naomba yote yatupite tukiwa ndani ya ndoa. Nilikuomba Pendo. Naomba hasira isitutenganishe na kusahau tulichonacho. Mwenzio nilizidiwa nguvu na kina mama. Lakini unajua nakupenda Pendo. Nilisimama na wewe wakati wote! Tokea chuo mimi nilikuwa mtu wako nikikuuguza ukiumwa tumbo. Usinisahau tafadhali.” “Siwezi kusahau.” “Basi tufunge ndoa. Usibadili mawazo. Niangalie.” Pendo akanyanyua uso akamwangalia.

“Tuambiane chochote kitakachotokea baada ya hapa, tutasimama pamoja kama Willy na Pendo wale wa zamani. Ulisema hiki chumba hakijawahi kukosa kutupa majibu ya mambo magumu. Naomba kisianzie kwangu. Nakuhitaji Pendo. Niahidi utaendelea kusimama na mimi hata katika hili.” Akasindikiza na busu la muda mrefu, mikono ikasambaa kila mahali kwenye mwili wa Pendo. Akamvutia kwake zaidi, hali ya Pendo ikabadilika, akamkumbatia Willy kwa nguvu kama anayetaka amshike kwa nguvu zaidi. Willy akaendelea kumpapasa kila alipofikia na kumbusu hiyo midomo kwa utulivu. Midomo ikahamia kwenye shingo ya Pendo akaendelea na romance Pendo akifurahia.

Gafla Pendo akashangaa anamwachia. “Willy bwana! Ndio nini!?” “Safari hii honey moon tunakwenda wapi?” “Bwana Willy! Malizia ulichoanza.” Willy akacheka na kumfunika vizuri. “Honeymoon wapi?”  Willy akaendelea kuuliza. “Sijui. Lakini hatuwezi kusafiri. Na ninaomba uondoke hapa. Unanitesa tu.” Willy akacheka na kusimama. “Ushanihakikishia ndoa, kaa mkao wakusubiri.” “Kwani sasa hivi kuna nini?” “Uridhike sasa hivi, ukose sababu yakusubiri? Nguvu hiyohiyo uitunze kule kwa mchungaji usimamie kwa hekima zote atufungishe ndoa. Halafu ukafaidi honeymoon.” Pendo akamwangalia, Willy akacheka na kutoka.

Jumatatu.

Jackson Msindai Afanya kweli Kwa Max na Tino.

Kwa Max.

W

akati Max ndio amerudi tu nyumbani akizungumza na mkewe ambaye naye pia, ndio alikuwa amerudi nyumbani kutoka kazini, mlinzi akawagongea kuwa wanamgeni na amesema nilazima aonane na Max mwenyewe. Max akamwambia amkaribishe baada ya kuuliza maswali na kujiridhisha ni mtu mzuri. Akafika mlangoni na kumuomba asaini kuwa amepokea barua aliyokuwa ameshika mkononi. Max akiwa na mshangao akaipokea na kusaini baada ya kujiridhisha ni yake kwa jina lililokuwa limeandikwa juu ya bahasha. ‘Maximilliun Kundi.’ Mjumbe akaondoka, Max akiwa amekunja uso akarudi ndani.

“Ni nani na anataka nini?” Akauliza mkewe. “Ameleta hii barua.” Akajibu akiifungua. Moja kwa moja akaenda kwenye kichwa cha habari. ‘SHITAKA.’ Max akashituka sana mpaka mkewe akamuona. “Vipi?”  Akauliza mkewe lakini safari hii hakupata jibu. Barua ilieleza dhumuni lakutaka kushitakiwa na Jackson Msindai kwa kosa la kumpiga picha yeye akiwa na watoto wake bila idhini ya Jackson mwenyewe, na kisha kuzisambaza kwa uchochezi. Nyuma yake ziliambatanishwa karatasi zenye hizo picha zikuwa na siku, pamoja na muda alipomtumia Tino hizo picha. Na ikaandikwa kuwa mazungumzo kati yake na Tino akimpa ushawishi akimtaka Tino arudi nchini kwa haraka kuwadai watoto wa Jackson na Sabrina Msindai, huku Tino akimthibitishia kuwa watoto si wake ila wa Sabrina. Ila  yeye bwana Max aliendelea kumshawishi kichochezi bwana Tino, aliambiwa mazungumzo hayo yapo yalinaswa.

Barua ikaendelea kusema, hata mazungumzo kati yake na mkewe pia yalinaswa wakiwa wanaweka mipango hatari tena yakutisha kwa familia ya Msindai, wakimlenga moja kwa moja waziri wa Jamuhuri ya Muungano wa nchi ya Tanzania. Mwanasheria huyo aliyemwandikia hiyo barua kwa niaba ya Msindai, alimthibitishia mazungumzo hayo yapo na yalinaswa na watu wa Usalama wa Taifa. Ndugu Maximilian Kundi akatajwa kama mchochezi, muharibu amani, na mtu hatarishi.

Max alihisi kizunguzungu akakaa kwenye kochi la karibu. Mkewe akasimama na kumpokonya zile barua. Akasoma. “Mungu wangu Max umeniponza wewe!” Mama Kundi akashika kichwa. “Nilikuonya Max. Nilikuonya kabla hujaanza hii vita na kina Msindai, mume wangu! Ni nini umefanya?” “Nilituma na kuzungumza nikiwa kwenye hasira!” Max akajitetea akiwa ameishiwa nguvu kabisa. “Lakini pia nilikuonya siku ile Max. Unakumbuka lakini? Kwa nini kujiingiza kwenye mambo yasiyokuhusu?” Mama huyo akaendelea kulalamika huku akirudia ile barua akitamani hiki na kile kisingeandikwa na kujitoa kabisa kwenye mpango mzima na kumtupia lawama mumewe.

Kwa Tino!

Kilichompata Max ndicho kikampata Tino. Ni kama kuna mtu alikuwa akisubiria warudi majumbani kwao. Akahakikisha Tino anapokea na kuweka saini ndipo akaondoka. Yake ilikuwa ‘Restrain order’ na barua kutoka kwa mwanasheria wa Jackson Msindai akimtaka akae mbali na familia ya Jackson Msindai, kwa vitisho alivyofanya siku iliyopita, ya jumapili, kwa familia hiyo. Barua hiyo ikaeza kuwa vyombo vya usalama vimenyaka mazungumzo kati yake na Max akimshawishi arudi nchini kudai watoto wa Jackson na Sabrina Msindai. Barua ikaeleza majibu yake kwa Max, baada yakuona picha zilizoambatanishwa nyuma ya waraka huo, yalisikika Tino mwenyewe akijibu ‘watoto si wangu ni wa Sabrina’, aliambiwa yapo na sauti zao wote wawili zikiwa zimenaswa vizuri bila shida.

Waraka huo ukaendelea kueleza kushangazwa na hofu iliyowapata familia ya Jackson Msindai kurudi kudai tena watoto baada ya ukiri wake yeye mwenyewe kwa Max, alipomthibitishia kuwa watoto si wake, lakini jana yake aliwafuata na kudai watoto wa Jackson na Sabrina huku akitoa vitisho. Mwanasheria huyo akaeleza, kwa alichokifanya jana baada ya kukataa yeye mwenyewe kuwa watoto si wake, na uthibitisho wa kuwa ni kweli watoto wa Jackson si wake kwani alishaua watoto wake yeye mwenyewe na uthibitisho wa mauaji wa watoto wake upo, inaashiria kuwa amekubali kushawishiwa na mwanasheria wake na amekusudia kufanya fujo kwa familia hiyo ya Msindai.

Kwa mshituko mkubwa sana Tino akaangalia karatasi ya nyuma. Ilikuwa na zile picha alizotumiwa na Max zikionyesha muda na siku sahihi zilipotumwa. Akaambiwa mazungumzo yapo yamenyakwa. Alionywa na kutakiwa kukaa mbali na familia hiyo au atachukuliwa hatua kali za kisheria na kushitakiwa kwa kosa la mauaji, na vitisho kwa familia hiyo ya Jackson Msindai. Tino hakuamini akabaki ameduaa, hajui kama ni hofu au ni mshituko ndio unamsababishia baridi. Akakaa na yeye kwenye kochi la karibu. Akaamini kuwa Jack hakuwa akimtania na amewawahi kuwashitaki na kweli anao ushahidi. Tino akabaki ametulia.

Picha za binti zake, vile walivyo wazuri ikamjia. Akakumbuka vile walivyombusu Jack kwa pamoja na kupiga makofi. Jack akarudisha mabusu kwa watoto wake. Akakumbuka vile walivyokuwa wamejilaza begani kwa Jack. Kisha akakumbuka jinsi Jack alivyokuwa amewashika mkono na kutembea nao baada yakumlilia asiwaache. Jack akarudi akawachukua. Akakumbuka jinsi walivyokuwa wamemganda Jack hata mchangani kule baharini. Na mabusu ya hapa na pale. Akaumia sana Tino na kujuta mno moyoni.  Akumchukia Max kwa ushauri wake. Akaitazama ile nyumba. Jumba zuri sana. Kweli ameshinda kesi, lakini yupo peke yake! Akazidi kuumia na kumchukia Max kuliko kawaida. Tino akabaki akiwaza.

Jumatano.

Zelda, Willy & Pendo Mbele Ya Mchungaji Tena.

W

illy alishampigia simu mchungaji na kumuomba kikao siku hiyo ya jumatano. Akamwambia atakuwa na Zelda. Lakini hakumwambia maswala ya DNA. Mida ya saa nne asubuhi Willy alikwenda kuchukua majibu hospitalini, akabaki nayo mpaka jioni. Akaenda kumfuata Pendo nyumbani ndipo wakaelekea kanisani. Walimkuta Zelda ameshafika kanisani na mtoto wake akisubiria. Mchungaji alikuwa na watu wengine ofisini, wakabaki nje ya ofisi wakisubiri. Pendo akamuona Willy anawasiwasi sana. Anasugua mikono bila kutulia. Akajua anawasiwasi na majibu hayo ya DNA. Gafla Willy akawa hataki tena mtoto kutoka kwa Zelda aliyemkimbilia kwa kutupa ndoa ya kanisani. Pendo akamuacha kabisa wala hakumtuliza. Akahangaika kwa hili na lile akijituliza, mwishoe Pendo akamuona anamshika mkono. “Nakupenda Pendo.” “Najua Willy.” Zelda akabaki kimya akiwasikiliza.

Willy akambusu Pendo kwenye mkono aliokuwa ameushika, midomo ikitetemeka, macho mekundu, mishipa ya kichwa imesimama. Pendo akamuhurumia. Alikuwa amepatwa hofu ya kupitiliza. “Naamini tutakuwa sawa Willy.” “Kweli?” Willy akataka uhakika. Pendo akaelewa ni ombi kwamba hata mtoto akiwa wake, basi asimuache. “Naamini hivyo.” Pendo akajibu taratibu. Willy akabaki akimwangalia. “Itakuwa sawa Willy.” Hapo Willy akaridhika. “Nashukuru Pendo. Na nina uhakika tutakuwa na wakati mzuri honeymoon.” Pendo akacheka taratibu. Alikuwa amependeza vilivyo na mimba yake ya mapacha. Na vile alivyo mtulivu, kila alichoweka mwilini mwake kilitulia. “Si hata wewe unasubiria honeymoon kwa hamu?” Willy akauliza akibembeleza.  Pendo akamwangalia akacheka. Mlango wa mchungaji ukafunguliwa, waliopo ndani wakatoka, mchungaji akawaita ndani.

Baada ya salamu, Willy akaanza. “Tulipotoka hapa siku ya jumapili, tulikwenda nyumbani kwa Zelda. Tukazungumza naye kwa urefu na undani. Lakini tukagundua katika mazungumzo kati yenu, kuna mambo mengi sana hakukushirikisha. Tukamuomba kama leo anaweza kuja hapa, tuzungumze kwa pamoja ili ujue ukweli wote.” Mchungaji akamkaribisha Zelda. Akaanza Zelda kuongea kuanzia mwanzo mpaka mwisho bila mtu yeyote kumwingilia.

“Na mimi si mvunja ndoa za watu. Kama mama Ngoi asingeniambia kama mke wa Willy hazai, mimi nisingekubali tokea mwanzo. Mama Ngoi ndiye aliyeniingiza matatizoni mchungaji. Nimebaki njia panda kwa mipango yake!” Zelda akaanza kulia. “Alinihakikishia ndoa na malezi ya mtoto! Amenitoa kwenye maisha yangu ambayo hayakuwa ya juu sana, lakini nilikuwa najitosheleza. Ona sasa hivi nahangaika na mtoto na sina kazi ya maana wakati kila mtu ananilaumu mimi! Nimebaki peke yangu nikiteseka, wakati niliahidiwa mengi tu. Yule mama amekufa na kuniacha nahangaika, hakuna asiyemtaka huyu mtoto!” Zelda akaendelea kulia.

“Naomba kuzungumza na mimi.” Pendo akaingilia. Alikuwa kimya muda wote. “Karibu Pendo.” “Asante. Labda nirudie nilichomwambia Zelda, ili ajue sikuwa nikimdanganya. Tumefanya vipimo kujua kama mtoto ni wa Willy au la, ili kuwa na uhakika.” “Mmefanya vizuri sana maana ndicho nilichotaka kuwashauri.” “Majibu ninayo tayari, tulitaka uje utusaidie wewe kusoma ili kuondoa utata.” Willy akaweka ile bahasha mezani.

“Endelea Pendo.” Willy akamtaka Pendo aendelee. “Nilimwambia Zelda, kama mtoto ni wa Willy, nina uhakika bado Willy anamtaka mtoto wake. Si ndio Willy?” Hapo Willy akapoa. Kimya. “Najua wamepitia kwenye ugumu na Zelda, lakini mimi kama mpenzi wa Willy na ninayekusudia kuwa na Willy, kama mtoto ni wa Willy, nakuhakikishia mchungaji huyo mtoto atatunzwa vizuri tu. Sitakuwa na amani kuona Willy yuko na sisi, halafu mtoto wake anateseka huko na mama yake. Itakuwa ni laana hata kwa watoto wetu. Atatunzwa na kusomeshwa kadiri atakavyoweza huyu mtoto aliyezaliwa na Zelda, kwa kuwa yeye hana hatia. Lakini kama ni wa Willy. Ila kama si wa Willy, basi hapo hainihusu tena. Itanihusu tu, pale atakapokuwa ni mtoto wa Willy.” “Nashukuru dada. Na ninaomba usinilewe vibaya. Mama Ngoi na wale watoto wake wa kike ndio walio nisukumia kwa mmeo.” Akaongea Zelda kwa unyenyekevu. Willy kimya akisugua mikono.

“Mimi naona huko tulishapita. Naomba mchungaji tusaidie tuendelee mbele. Mama hayupo, tuliobaki ni sisi. Na hatuwezi kukwama kwa jambo lililokwisha tokea. Tusimfanye huyu mtoto ni laana wakati Zelda umepewa na Mungu kwa upendo tu. Mimi nimehangaika miaka na miaka kutafuta mtoto. Wewe umepewa, naomba uchukue ni kama zawadi ya thamani sana. Usije mchukia mtoto kwa mazingira uliyoyasababisha wewe mwenyewe.” “Sio mimi dada!” Zelda akabisha. “Usikatae kuwajibika Zelda. Mtu wa kawaida hawezi kulala na baba na mtoto wake kwa wakati mmoja! Hata kama mama Ngoi alikushawishi yeye na watoto wake hao wakike, pamoja na mumewe na hata Willy mwenyewe, bado ulikuwa na nafasi ya kukataa. Lakini ulikubali wewe mwenyewe. Usimfanye mtoto wako akawajibika kwa maamuzi yako machafu.” Pendo akawa mkali.

“Lakini Mzee Ngoi alisema anataka kumsaidia kijana wake pia.” Zelda akaendelea kujitetea. “Zelda! Huna jinsi ukajitoa katika hili. Yule mzee hakuanzia kwako. Alianza na mimi pia.” Mchungaji na Zelda wakashangaa sana. “Mahusiano uliyoyakubali kuwa nayo na mzee Ngoi mpaka kukimbia naye kwenye mahoteli, kumfungia kwako tena mkewe akiwa hai, hayakuwa ya kulazimishwa wala yakutafuta huyu mtoto. Ulitaka mahusiano na yule baba, ukakataa kuwa na Willy kwa kuwa ulitaka kunufaika na mzee Ngoi, ila mwenzio amekuzidi akili.” Pendo na sauti yake ya upole akawa mkali.

“Na usifikiri nia ya mzee Ngoi ni kumsaidia Willy, aliona umejirahisisha kwake na yeye akajinufaisha akijua mwisho wa siku utaondoka na Willy, yeye maisha yake yaendelee kama kawaida. Ngoi hana shida na watoto. Kama ameweza kuwafukuza watoto wake aliolea na mkewe, ulifikiri atashindwa nini kwa mtoto wako? Tena ukawatoa watu wawili muhimu kwenye maisha yako! Stella na Prisca waliokuingiza kwenye familia. Ulitegemea nini!? Kweli wewe ulidhani mzee Ngoi na umri ule aanze kulea mtoto na wewe! Kwa nini Zelda? Kwa kipi? Alikuwa akifurahia kampani yako tu. Mzunguke naye kwenye biashara zake, basi. Hakuanza na wewe na wala hataishia kwa Chonge. Alianza kwangu akiniomba mahusiano nikiwa mke wa Willy tena akiniambia sababu kama yako. Kumsaidia kijana wake.” Wote wakashangaa.

“Kwamba na wewe alikutongoza!?” Akauliza Zelda kama asiyeamini. “Ulifikiri kwako ni mapenzi Zelda!? Samahani nazungumza hivi kwa baba yake Willy, lakini yule Mzee hajatulia Zelda! Ni vile wewe humfahamu. Hata wanae wanamjua baba yao. Alihangaika sana na mimi mpaka nikamtisha kuwa nitamwambia baba yangu na kuja kumtisha pia kuja kumwambia Willy ndipo akaniacha kwa kuwa anamuogopa sana Willy kuliko watoto wake wote. Anajua Willy anauwezo wakusimami jambo na akashinda. Sio tegemezi wala hana shida na mali zake kama watoto wake wengine. Willy alianza kujitegemea akiwa bado mdogo sana. Wewe ndio uliyefungua mwanya wa yule mzee kumtukana Willy, lakini hata yeye anajua Willy hana shida na mali zake. Kwa kifupi anajua hana kitu anaweza kumtisha nacho Willy kama watoto wake wengine waliozoea kumkopa pesa mara kwa mara na ndio maana anawanyanyasa kila wakati na kuwadhalilisha. Kwa mara ya kwanza, wewe Zelda, ndiye uliyefungua mlango mzee Ngoi akapata jambo la kumtukania Willy. Ila anamjua Willy si mjinga wala hajashindwa maisha. Na anajua kwa hakika Willy wangu sio muhuni.” Hapo Willy akajisikia vizuri na kuanza kutulia.

“Si mzee Ngoi wala mkewe, wote wanajua Willy sio muhuni. Na pia usifikiri wewe ndiye mwanamke wa kwanza kushawishiwa pale nyumbani kuwa na Willy. Ila wenzio walikuwa na akili. Waliokuja kujaribu walipogundua mapenzi ya Willy kwangu, walikataa kabisa na kuondoka. Wewe mwenyewe tokea mwanzo ulisema Willy alikwambia atazaa tu na wewe. Si ndivyo?” Zelda kimya. “Sasa ulitegemea nini kama si kulea huyo mtoto peke yako?” Kimya.

“Hakuna uchawi uliofanyika Zelda. Wewe ndio ulishindwa kucheza karata zako vizuri, umeshindwa. Hamuwezi nyinyi kumloga mzee Ngoi. Anaakili sana yule mzee wewe hujui na nafikiri hata Chonge hajui. Anapoteza pesa zake bure huko kwa waganga. Utakuja kuniambia na yeye akishika mimba, kama hatakalia hicho kiti ulichokaa hapo akimlilia mchungaji hapa. Mzee Ngoi ana watoto wa kike na wa kiume. Tena amesomesha wote, na amewaweka mkononi wote kasoro Willy. Wanafanya kile anachotaka yeye. Sasa unafikiri kwa nini atake mtoto mwingine?” Kimya.

“Samahani nimezungumza sana mchungaji.” “Lakini ni heri umeweza kutufungua macho na kuelewa ukweli mzima kwa undani. Pengine niende kwenye jambo hili la msingi litakalotupa dira nyingine kuanzia sasa.” Akafungua ile bahasha. Akaisoma kwanza yeye mwenyewe. Wakamuona anavuta pumzi. Wote wakabakia na hali ya wasiwasi usoni. Uso wa mchungaji ukapooza kabisa. Akasoma tena, na tena. “Hivi vipimo mlifanyia wapi?” Willy akajibu. “Inamaana basi ni vya kweli.” Wote kimya wakimtizama. Akabaki ametulia.

“Niambie tu mchungaji nijue moja. Nishamjua Ngoi alivyo, nishamjua Willy na mkewe. Nataka kujua hayo majibu ili nijipange upya.” Zelda akaongea kinyonge. Mchungaji akasoma tena na kujibu, “Huyo ni binti wa Ngoi.” “Asante Mungu wangu.” Willy akashukuru kwa sauti na kusimama kabisa akiwa amenyanyua mikono juu. “Willy wewe!” Pendo akashangaa, na kumvuta arudi kukaa. Zelda akaanza kulia. “Nitafanyaje sasa?” Zelda akauliza akilia. “Naomba nisaidie kuzungumza na Mzee Ngoi, dada.” “Najua ulisikia malalamiko ya wifi na mama Ngoi kuwa sipendi kwenda nyumbani kwao? Si ndio?” “Waliniambia unakimbia majukumu ya ugonjwa.” Zelda akajibu. “Sawa sawa. Lakini si hivyo. Ni nilikuwa nikimkwepa mzee Ngoi. Mimi na yule baba tuliacha kuzungumza muda mrefu sana na huwezi hata kutukuta tumekaa sehemu moja peke yetu. Kwa sababu ya kutaka kunibaka, na kunishika shika kimapenzi.” Wote wakazidi kushangaa, Willy kimya.

“Na ujue wazi kabisa, ndipo ugomvi wangu na mama Ngoi ulipoanzia. Alijua mimi natembea na mumewe kwa kuwa alishatukuta mimi na mzee Ngoi kwenye kile chumba mama alikuwa akiwekea vitu vyake vya thamani na vipya. Alitukuta mumewe akiwa na hali mbaya, na mimi nipo hapo. Akadhani kuna kilichokuwa kikiendelea hapo chumbani ametufumania, kumbe yule baba alikuwa amenifungia hapo, tunakimbizana anikamate, lakini sikupiga kelele. Hiyo ni mara ingine, ingine nahisi yule mama aliniona wakati mumewe akinishika makalio, tena aliingiza mkono ndani ya gauni, tukiwa nje, yule mama akiwa ndani na unajua nyumba yao inamadirisha ya vioo. Hakusikia tulichokuwa tukizungumza ila kushuhudia kitendo cha mumewe kuingiza mkono ndani ya gauni na kunishika makali.”

“Hatukuwahi kuwa marafiki na yule mama tena, na akaacha kunikaribisha nyumbani kwake, na akaweka mazingira ya mimi hataki nifike nyumbani kwake, japo kwa wengine hakusema moja kwa moja, ila mimi mwenyewe aliniambia kwa kinywa chake mwenyewe. Ndio maana usingeniona mimi nakwenda kwa yule mama kama sipo na Willy. Ninachotaka kukwambia ni kwamba, kwa yule mzee sitaweza kukusaidia, labda mchungaji.” Mchungaji akacheka kwa kusikitika.

“Mimi mwenyewe ndio maana nimeumia sana nilipogundua ni mtoto wa Ngoi. Namjua Ngoi tokea kina Willy ni watoto wadogo kabisa. Ni mkorofi asiyebadilika. Na akisimamia jambo lake, kumbadili ni neema. Mwanzoni alihangaika sana mkewe, mpaka akakubali kuishi naye vile alivyo. Mtu pekee anayeweza kumsikiliza kwenye maisha yake ni yeye mwenyewe.” Hapo Zelda akazidi kulia. “Natamani angekuwa mtu mwingine, lakini si Ngoi.” Wote wakanyamaza kwa muda Zelda akisikika akilia.

          “Na Willy je?” Akauliza Zelda huku akilia. “Unanitania wewe!?” Willy akashangaa sana. “Si ulikuwa naye siku akitufukuza pale nyumbani tena ukimsaidia kwa maneno machafu sana kwangu na dada zangu! Au umesahau?” Willy akamuuliza tena kwa ukali sana. “Willy!” Pendo akaita kwa upole. “Hapana Pendo. Anajidai analia hapa, ni muongo. Hakuna anayemjua Zelda wa ukweli ila mimi. Ni mbaya huyu, kuliko hivi anavyoonekana na kusikika. Ana maneno machungu, hujawahi kuona. Mkatili asiye na hata chembe ya ubinadamu. Ana matusi yale ya nguoni. Mazito ambayo mdomo wake umeshindwa au haujui kuyachuja. Zelda akikutukana, hapepesi jicho.” Willy akaongea kwa jaza akitetemeka.

“Ninafuraha si kwa kuwa mtoto si wangu. Nataka sana mtoto. Lakini nilikuwa nikiwaza kuwa na mtoto na wewe! Natamani leo iwe mwisho wa sisi kukutana, ili usinipatie sababu hata yakunisalimia.” “Willy naomba utulie.” Pendo akamshika. “Nikwambie kabisa mchungaji Swai, kwake huyu labda kanisa limsaidie, lakini si ndugu. Yeye ni shahidi wa hiki ninachokwambia. Sisi kama watoto, hawa wawili, yeye na baba, walivyotufukuza vibaya vile, tulitafuta wazee wa ukoo. Watu ambao wanaweza kumkalisha mzee Ngoi wakazungumza. Mzee alitukaribisha nao nyumbani, lakini muulize Zelda kama atakuwa mkweli, fujo, matusi na dharau alizoonyesha mbele ya wale wazee na sisi.” Kimya.

“Ilikuwa inatisha mpaka aibu. Ikabidi tuondoke. Zelda alitukana waziwazi mbele ya wale wazee. Akanikashifu mimi akisema ndio maana hashangai ni kwa nini mke wangu hakushika mimba, sijui  mapenzi, nipo kama mwanamke.” Pendo na mchungaji wakashangaa na kushituka kwa sauti. “Haaa!” “Mungu wangu nishahidi. Alisema huyu mbele za wale wazee na ndugu zangu. Tena akasisitiza hata shuguli yenyewe siiwezi, sina nguvu za kiume zakutosha, hata dakika 5 sifikishi!” “Mungu wangu!” Pendo akashangaa sana. “Kama mimi naongopa, akanushe hapa. Mama mmoja akamuomba atulie, atumie tafsida kwani pale kuna wazee. Lakini Zelda akamjibu vibaya yule mama, tena kama shangazi yetu, japo si tumbo moja na baba lakini sisi tumekua tukimuita shangazi. Akasema yeye pale haoni mtoto mdogo ambaye hafanyi mapenzi.” “Haiwezekani Willy!” “Si huyu hapa muulize. Muulizeni.” Willy akaweka msisitizo.

“Sasa huyu leo anarudia mlango upi na kwa nani wakati alitufukuza pale kwa mzee? Sisi na wale wazee wote.” “Siku ile sikuwafukuza.” Zelda akajitetea. “Kilichopungua ni neno ondokeni. Lakini ulitukana mpaka yule mama akasema hawezi kuendelea kusikiliza ukitutukana, yeye yupo na mumewe pale, na sisi ni kama watoto aliotuzaa kwani alitulea. Hakukwambia hivyo yule mama na kuondoka na mumewe, ndio baba akasema na sisi tuondoke haraka?” Kimya.

“Tafadhali mchungaji, mimi nataka kuoa. Nataka kumuoa Pendo mpenzi wangu. Naamini tatizo au kipingamizi kilikuwa Zelda tu. Sina mwanamke nimelala naye, hata kuwa na mahusiano naye tokea nianzane na Pendo isipokuwa huyu Zelda. Na Pendo wangu hivyo hivyo. Mimba ya Pendo ni yangu mimi. Mpenzi wangu alitulia hata tulipoachana hakuwa na mahusiano. Tatizo lilikuwa mimi kwa huyu Zelda. Umeshapata ukweli juu ya Zelda. Naomba akutafute kwa wakati wake, sisi tumalize yetu. Naomba Pendo, uumpe nauli aondoke.” “Nilimrushia pesa ya nauli yakuja na kurudi. Labda nimuongeze tu.” “Hapana. Naomba atupishe tafadhali. Hiki ni kikao chetu.” “Mimi naomba nikusubirie hapo nje mchungaji. Lasivyo sitakubali kushindwa kirahisi hivi.” Zelda akaongea wasimuelewe anamaanisha nini. “Sawa. Bila shida unaweza kunisbiria tu.” Zelda akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

·         Zelda Atakubali Kuachwa  Njia Panda?

·         Pendo Na Willy Safari Hii Watafanikiwa?

·         Mama Kundi Amejua Amesikiwa Na Bosi Wake. Na Yeye Anakabiliwa Na Lipi?

·         Tino & Max?

Itaendelea.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment