Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 42. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 42.

Walitoka hapo kimya kimya wakaingia garini bila hata kusemeshana. Willy akaondoa gari hapo kanisani. Pendo akashangaa Willy anasimamisha gari pembeni ya barabara. Akamgeukia. “Si unanipenda?” Pendo akashangaa. “Nataka kujua Pendo.” “Wewe unajua nakupenda. Kwa nini?” “Na wewe unajua kama nakupenda na nimekusudia kuwa na wewe?” “Najua Willy ila sijui kwa umbali gani?” “Kwa kila umbali unaoweza kufikiria na unaokuogopesha sasa hivi, maana na mimi nimeingiwa hofu. Naomba tu uniahidi kwa chochote tutakachokutana nacho kuanzia sasa, hakitatutenganisha. Tutasimama pamoja.” Pendo akavuta pumzi kwa nguvu. “Nikwambie ukweli Willy?” Pendo akauliza huku akipapasa tumbo lake, kama aliyepata nafuu.

“Nini?” “Nilishaingiwa hofu yakupitiliza nikijua kibao ndio kinanigeukia. Hayo maneno nilitamani nikwambie wewe, lakini nikaishiwa ujasiri.” “Kuwa chochote tutakachokutana nacho kuanzia sasa, hakitatutenganisha?” Willy akamuuliza. “Ndiyo, lakini nikaona nitakuwa mbinafsi endapo ukimpata Zelda, ukagundua mtoto alikuwa wako, ukamtelekeza kwa ajili yangu ambaye hata watoto hawajazaliwa!” “Kwa hiyo bado huamini kama nimerudi kwako kwa ajili yako ila watoto?” Willy akauliza kwa kuumia. “Nipo njia panda Willy. Upande mmoja unaamini, upande mwingine nakuwa na wasiwasi hata naogopa chochote kisije kutokea kwa hawa watoto, nikakupoteza.” Willy akavuta pumzi kwa nguvu akajirudisha nyuma ya gari akaegemeza kichwa na kugeukia nje. Pendo naye akanyamaza kimya.

Mtaka Cha Uvunguni, Sharti Ainame.

A

kamuona anatoa simu yake na kupiga. Ikaita kwa muda mrefu mpaka ikakata. Akamuona anapiga tena. “Samahani kwa usumbufu baba. Lakini nilitaka kuomba namba ya simu ya Zelda, nahitaji kuzungumza naye.” “Sina.” Akajibu mzee Ngoi kwa jeuri. Pendo akajua kweli Willy amekusudia kuwa naye. Kumpigia simu mzee Ngoi! Ni jambo la mwisho kabisa angetamani kufanya. Hata mchungaji alimkatalia. “Pengine unafahamu sehemu anapoishi kwa sasa?” “Kwa nini unafikiri hivyo?” Mzee Ngoi akauliza kwa jazba. “Nauliza tu baba yangu. Je alipokuwa akiishi zamani unapakumbuka?” “Keko, karibu na yale magorofa ya National Housing. Kuna nyumba upande wa nyuma yake, wanalima michicha nje, ndiko alikokuwa akiishi hapo kabla hajaja kwangu na mke wangu na kuwa tapeli.” “Amekutapeli!?” Willy akauliza nakuweka spika ili Pendo asikie.

“Sina muda wa kipuuzi na kuzungumza vitu vya kipuuzi.” “Nilitaka tu kusikia upande wako baba, kabla sijakwenda kuzungumza naye.” “Huna utakachopata kwa malaya yule, mbwa anayeweza kulala na yeyote na muongo wakupindukia.” Willy akajua walishageukana. “Unajua alichokuwa akiniaminisha mimi?” Willy kimya. “Kabla yakulala na wewe, eti alikuwa akisema anataka mimi nimlale kwanza ili nisije kula makombo yako na pia akitaka eti mimi niridhike kwanza kwakuwa ananipenda mimi na anataka mtoto wake wa kwanza awe wangu. Unajua na ahadi yake?” Willy kimya.

“Msichana yule ni tapeli la mchana kweupe. Alifikiri atanizidi mimi! Hata kidogo. Anataka kunufaika hapa mjini kwa jasho langu mimi!” “Ni nini alikuahidi baba?” Willy akamkatiza maana hasira ilizidi kupanda akataka kusikia ya Zelda zaidi. “Eti hata kama mama yenu asingefariki pengine angepona, wewe ukaachana na mkeo mkaoana naye, bado sisi tungeendelea kama kawaida na kuolewa na wewe ndio ingekuwa njia rahisi yakutufanya tuzidi kuwa karibu kwa kuwa ananipenda sana na mama yenu ndiye anatutenganisha kumbe muongo tu. Ananiibia akitaka kunufaika kote kote huku akitumia madawa yakunipumbaza! Nashukuru Mungu huyu msichana tuliyekuwa naye tokea zamani akitusaidia kazi mimi na mama yenu, ndiye amenifungua macho.” Willy akajua mapenzi yameshageuka.

“Pole sana baba. Hukufanikiwa kubakisha namba yake?” Willy akauliza tena kinyenyekevu kama kumtuliza. “Nafikiri naweza kuwa nayo. Subiri.” Pendo na Willy wakaangaliana. Gafla mzee Ngoi akasikika ametulia kabisa. Akawatajia hiyo namba, Pendo akawa akiandika. “Nakushukuru sana baba. Asante.” Willy akajishusha kabisa lakini moyoni alishamchukia huyo baba yake wala hakutaka wala kupanga kuja kumsikia tena.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Huyu Mzee ni mtu wa mwisho kabisa ambaye nilitaka kuja kuzungumza naye, zaidi kuja kumuomba chochote hata maji!” Pendo akamwangalia. “Nafanya hivi kwa ajili yako Pendo. Nataka kuwa na wewe. Na ndio maana nazungumza na kujishusha kwa hawa wote ambao sikutaka hata kuja kuwasikia tena.” Pendo akabaki ametulia. “Nakupenda wewe Pendo, na nimekusudia kutulia na wewe hata iweje.” “Nashukuru Willy.” “Mbona kama unaongea ukiwa unamashaka!?” Willy akalalamika. “Hapana Willy. Nimeshukuru ila sijui kinachotukabili mbeleni.” “Hapo sasa unanitia nguvu ukijiweka na wewe. Angalau unanitia moyo. Naamini tukisimama pamoja kuanzia sasa, hatutashindwa.” Pendo akatulia. “Si ndio?” “Naamini hivyo Willy. Naamini kuwa hutabadilika tena.” Willy akajua bado anamashaka. “Basi naomba kuanzia sasa matendo yazungumze.” Willy akatoa gari hapo.

“Tunakwenda wapi tena?” “Nataka kutimiza yote, leoleo. Mchungaji amesema nizungumze kwanza na Zelda ndipo niendelee. Naomba tuongozane mpaka kwake. Na yeye nimsikilize, niweke kikomo naye. Ni sawa?” “Umeshafikiria kama ikitokea mtoto ni wako!” “Nitajua mbele ya safari Pendo. Tafadhali tusimame wote.” Pendo akamwangalia na kunyamaza. “Nini?” “Nafikiria tu.” “Juu ya nini?” “Nasema itakuwa mipango yako imetimia. Kuzaa na Zelda na kuwa na mimi.” Willy akashindwa hata azungumze nini tena. Akanyamaza kabisa na kugairi hata kwenda kwa Zelda.

Pendo akamuona anabadili njia nakurudi nyumbani. “Vipi tena?” “Naona turudi tu nyumbani Pendo, pengine tujipe muda wakufikiria kujua nini tufanye kuanzia hapa. Acha mimi niende nikazungumze na Zelda. Kama kuna kufanya DNA, nifaye kabisa mpaka kieleweke, ndipo nirudi kwako nikupe majibu ili uweze kuamua kuwa na mimi Willy peke yangu au mimi Willy na huyo mtoto. Nisikubebeshe mizigo isiyokuhusu.” Pendo akajua amekasirika.

“Umekasirika?” Akamuuliza taratibu tu. “Hapana, ila sijui natakiwa kufanya nini tena Pendo! Nahisi akili imefika mwisho. Acha nitembee na kufanya kile ninachoweza.” “Samahani Willy, naomba usikasirike.” “Hapana Pendo. Nilikosa, acha niwajibike peke yangu.” “Hapana. Nahisi nimeingiwa na hofu pamoja na wivu tu. Nilifurahi nilipojua mtoto si wako. Sasa sasahivi kunakuwa na mazingira yote yakuonyesha mtoto ni wako. Nina hofu ya kukupoteza tena.” “Naomba uniamini hutanipoteza Pendo. Nimerudi na sitaondoka tena. Hata kama mtoto ni wangu, mimi na wewe tutafute njia pamoja ya jinsi yakukabiliana na hiyo hali. Nitakusikiliza wewe.” “Basi twende pamoja.” “Una uhakika?” “Ndiyo. Twende. Sasa hivi ujasiri umeongezeka.” Akamvuta mkono na kuubusu. “Asante Willy.” Pendo akashukuru na tabasamu. Willy akajua amefungua moyo. Akageuza gari tena kutafuta Keko.

Kwa Zelda.

“Nashauri tumpigie simu kwanza.” Pendo akatoa wazo. “Sawa.” Pendo akabonyeza namba kwenye simu ya Willy, ikaita Zelda akapokea. “Hallo!” Kwa heshima kubwa sana kama si Zelda. “Unaendeleaje Zelda?” “Naendelea vizuri, ila mtoto ndiye alikuwa akiumwa.” “Nini?” Willy akauliza. “Malaria. Akaishiwa maji, tukalazwa kama siku mbili hivi. Lakini sasa hivi anaendelea vizuri.” “Mnaishi wapi?” “Kule kule nilikokuwa nikiishi mwanzoni, sikuachia chumba changu. Nilikifungia na vitu vyangu.” “Unajua mimi sifahamu ulipokuwa ukiishi! Labda unielekeze, nataka kuja.” Zelda akatulia kidogo. “Zelda.” “Nipo. Nafikiria jinsi ya kukuelekeza.” “Kwani ni mbali na barabarani?” “Hapana. Gari inafika mpaka hapa.” Akamuelekeza kwa upendo na ahadi ya kumfuata barabara kubwa, kama atashindwa kuelewa na kufika kwake. Asijue na Pendo yupo. Wakaagana.

Wakamkuta barabara kubwa amesimama na mtoto amemfunga mgongoni. Willy akamwambia apande awaonyeshe njia ya mpaka kwake. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwake. Ilikuwa nyumba ya wapangaji watatu. Na yeye akawa wanne. Willy aliegesha gari yake nje, akaenda kumfungulia Pendo mlango, akamsaidia kushuka, baadhi ya wapangaji wengine, majirani na Zelda wakiwatizama. Wakasalimia waliowakuta hapo nje, Zelda akawakaribisha ndani. Willy akamtanguliza mkewe, wakawa wanamfuata Zelda nyuma mpaka chumbani kwake. Kilikuwa chumba kizuri tu kilichokamilika kila kitu. Makochi mazuri, kitanda safi, kabati kubwa zuri tu na tv yake. Pasafi kabisa.

“Si ninaweza kukaa?” Akauliza Pendo. “Karibuni.” Zelda huyu alijawa na heshima kama Zelda aliyekutanishwa naye Willy mwanzoni kabisa. “Pole na kuuguza.” Akaanza Willy, Pendo kimya. “Asante. Lakini naona anaendelea vizuri.” “Mara ya mwisho kuachana pale kwa mzee, mlikuwa mfunge ndoa. Na ukasema mtoto alikuwa ni wa mzee kwa kuwa ndiye uliyekuwa naye mwanzoni kabla yangu. Swali, kwa nini upo hapa na mtoto na si kule kwa mzee?” Willy akaenda moja kwa moja kwenye kilichowapeleka.

“Chonge amenigeuka.” Akaanza Zelda. Willy akakunja uso. Chonge ni msichana wa kazi wa nyumbani kwao kwa miaka takribani 12. Amekaa na mama yake kwa muda mrefu sana. “Chonge?!” Willy akataka uhakika. “Ndiyo yule msichana wa kazi. Na sasa hivi yeye sio msichana wa kazi tena, ndiye mwanamke wake mzee Ngoi, ameleta ndugu yake kutoka kwao ndiye anayemfanyia kazi.” Pendo akajiweka sawa. Willy akachoka kabisa. “Muda wote mimi nipo pale kumbe yeye Chonge ananionea wivu na kunipigia mahesabu yakunitoa pale. Akawa ananung’unika moyoni na kwa yule kijana wa usafi kuwa kama baba anataka kuoa, yeye ndio alitakiwa arithi nafasi ya mama sio mimi niliyekuja juzi tu hata simjui baba. Sasa analalamika hivyo lakini huku kwangu akawa kama ananichekea na kujidai ananiheshimu mimi kama mama mwenye nyumba wake.” Akaendelea Zelda. Pendo na mumewe wakisikiliza.

“Sasa nilipojifungua tu, akaanza kunijaza maneno kwamba niwe makini. Watoto wa mzee Ngoi wanaweza kunichezea kwa kuwa baba amewafukuza pale nyumbani kwa ajili yangu na pia mkeo wewe hawezi kukubali kwa kuwa nimewavunjia ndoa.” Pendo akashangaa sana. “Unamaanisha nini ukisema kuchezewa!?”  Akauliza Willy akionyesha uso wa hasira kidogo. “Yaani kuwa mkeo anaweza kuniloga mimi na mtoto wangu kwa kuwa nimewavunjia ndoa yenu, na yeye hazai. Kwa hiyo akisikia mimi nimezaa, ataniloga mimi na mwanangu.” Pendo akacheka taratibu kwa kusikitika Zelda akamwangalia kidogo na kuendelea.

“Eti na dada zako wanaweza kuniloga mimi na mtoto wangu, sababu baba yenu aliwafukuza akaniambia niwe makini na niwawahi kwa kuwa hamuwezi kukubali mali yote nipewe mimi na mwanangu.” Willy akatulia tu akimsikiliza. “Mwezi huo wa kwanza Ngoi akawa ananijali mimi na mtoto. Ananipa matumizi pale nyumbani na kunisaidia maswala ya mtoto kwa mapenzi mazito sana. Kumbe Chonge anaumia. Akawa anasema hajawahi kumuona baba yenu hata akipenda hivyo wajukuu zake! Mimi nikamwambia mapenzi ya mtoto na wajukuu ni tofauti, mimi sishangai kwa kuwa yule ni mwanae. Lakini yeye akwa ananing’ang’ania lazima niufunge ule upendo usije badilika.” Willy akakunja uso. Zelda akaelewa.

“Yaani niende kwa mganga kumfunga Ngoi ili asije kubadilika.” Willy akapandisha nyusi zote kwa mshangao. “Ndio mimi nikamwambia siwezi kutoka kwenda kutafuta mganga wakati nina mtoto mdogo. Akaniambia yeye atanisaidia kwenda kumtafuta. Akaanza kwenda yeye sasa kwa huyo mganga. Mara ya kwanza akarudi na kuniambia anachohitaji huyo mganga. Nikampa ili ampelekee.” “Nini?” Willy akauliza bila kujua. Zelda akasita kidogo. Hapo ndipo Willy akataka kujua zaidi. “Kama umeamua kuongea, ongea kila kitu, acha kuficha mambo.” Akaongea Willy kwa ukali. “Ilikuwa nguo yangu ya ndani na ya Ngoi.” Willy akashituka sana. “Kwa hiyo ukampa zote mbili!?” “Ndivyo alivyoniambia ametumwa na huyo mganga ili ayafunge hayo mapenzi. Mimi nikakubali nikampa na pesa juu!” Willy akabaki ameduaa. Zelda akaona aendelee.

“Akarudi na dawa, akaniambia mganga ameshaanza kazi yake. Hizo dawa nizakumuwekea kwenye chakula chake. Basi, ikawa rahisi, Chonge akipika, tunamuwekea. Sasa nikashangaa baada ya muda, Ngoi ni kama anaanza kunibadilikia mimi! Akaanza ukali hata kwangu, na akawa hana muda na mtoto. Akija nyumbani anakuwa busy na taarifa ya habari na magazeti kama unavyomjua baba yako kwa magazeti wakati ni kama mtindo huo alipunguza nilivyokuwa naye. Nikimtaka kimapenzi, ananitolea sababu. Ikabidi kurudi kwa Chonge na kumwambia mbona zile dawa ni kama zinambadili Ngoi na kumfanya kinyume nami! Akaniambia labda niende mimi mwenyewe kwa mganga nikazungumze naye. Atanisindikiza, yeye na mtoto watabaki kwenye gari.” Wakamuona anaguna kwa kusikitika.

“Jamani Chonge ni mshenzi yule msichana, msimuone mpole au amenyamaza vile. Mbaya kuliko shetani!” “Naomba uendelee.” Willy akamkatisha. “Basi, ndio akanichukua siku hiyo asubuhi kama kwenye saa nne hivi. Akanipeleka mpaka kwa mganga wake. Akaniambia mimi nishuke,  niingie ndani kwa mganga, nisiwe na wasiwasi alishazungumza naye, yeye atabaki na mtoto kwenye gari. Mimi nikashuka. Hapo aliniambia nijifunge khanga chini na ingine nijifunike. Basi, kumbe mimi nashuka, nakwenda kwenye ile nyumba ya mganga, mpaka naambiwa nikae pale nje nisubiri kama wenzangu. Maana nilikuta kama kina mama wanne hivi. Nikaambiwa ni kwa foleni, na mimi nikae hapo mpaka zamu yangu ifike. Nikaka hapo. Kumbe mwenzangu Chonge ananipiga picha tu!” “Anakupiga picha!?” Akauliza Willy kama ambaye ashapotezwa.

“Ndiyo. Anatumia simu yake kunipiga mimi picha kila ninachokifanya. Najua anabembeleza mtoto wangu kumbe ananipiga picha tu. Zamu yangu ikafika, nikaaguliwa na kubadilishiwa dawa. Nikarudi kwenye gari akawa ananiuliza maswali, kumbe ananirikodi tu jinsi ninavyomjibu mimi sijui! Nikamsimulia kila kitu tulichomfanyia Ngoi na huyo mganga, mwenzangu yeye kumbe anajirikodi kama anashangaa vile, mimi sina habari jinsi anavyoniuliza yale maswali. Najua tupo pamoja!” Zelda akaendelea.

“Tukarudi nyumbani tukapika, nikampa zile dawa sasa ili amuwekee. Akapokea na kuniambia ni heri azifiche yeye huko jikoni, ili iwe rahisi. Nikampa dawa zote. Sasa nikashangaa Ngoi anazidi kuwa mkali na hali nyumbani. Anagomba mfululizo, nyumbani ni kama anapakimbia. Hataki nimguse wala nimsogelee. Nikamwambia Chonge mbona mambo yameharibika zaidi! Akasema labda sikumsikiliza yule mganga vizuri, nirudi nikamuulize tena labda kuna sharti nimekosea. Mimi nikamwambia ndio itakuwa mara yangu ya mwisho. Nikirudi havijafaa, dawa zote alizonipa, nachoma moto. Chonge akaniitikia tu vizuri.” Zelda akacheka tena kwa masikitiko.

“Baada ya kama siku 5 nilipotoka kwa mganga, Ngoi akaniaga kuwa anasafiri na hajui atarudi lini. Akaondoka bila maelewano. Hasira zisizo na sababu, tena hapo alishaniambia nihame chumba kwa kuwa mtoto analia usiku, yeye anashindwa kulala na kesho anatakiwa kwenye majukumu yake, mimi nina uwezo wakulala mchana. Nikaona ni sawa. Nikashangaa anaondoka bila kuniachia pesa mimi, eti amemuachia Chonge! Halafu akaja chumbani nilipokuwa nimelala na mtoto ananiaga na kuniambia pesa za matumizi amemuachia Chonge! Nikamuuliza kwa nini iwe hivyo na mimi ndiye mkewe! Akanijibu moja kwa moja, bado hatujafunga ndoa, nisijisahau. Akaondoka na kufunga mlango kwa nguvu. Jamani nilishituka karibu kuchanganyikiwa.” Pendo na Willy kimya wakimtizama.

“Nikamfuata Chonge nikamuuliza ameachiwa kiasi gani na kwa nini iwe yeye si mimi?  Akanijibu hata yeye hajui, lakini akanisisitiza lazima nirudi kwa mganga haraka kabla hajapotelea kwa mwanamke mwingine huko nje, nishukuru hata akili yake imemtuma kwangu. Na mimi nikaona ni jambo jema. Ilipofika kwenye saa sita mchana tukarudi kwa mganga. Kama alivyofanya mwanzo, akabaki kwenye gari na mtoto, mimi nikashuka. Sikukuta watu wengi sana. Nikakaa kidogo nikaingia. Nimefika naaguliwa, nashangaa Ngoi naye anaingia na mtoto wangu. Akanikabidhi mtoto wangu pale pale nilipokuwa nimekaa nikiaguliwa, na kuniambia amepata ushahidi wakutosha, hataki kuniona tena. Akaniambia za mwizi arobaini. Akanionyesha picha zangu za kwanza na kunisikilizisha mazungumzo yangu na Chonge yale niliyokuwa nikimwambia Chonge kuwa safari hiyo nimemfunga kabisa Ngoi. Mganga amenihakikishia ni wangu daima. Ngoi akaondoka na kuniacha palepale.” Zelda akaanza kulia taratibu.

“Nikatoka nje, sikumkuta Chonge wala gari halikuwepo pale nilipokuwa nimeegesha. Nikarudi pale kwa mzee Ngoi, mlinzi akaniambia amesema hataki kuniona tena na niondoke. Basi, mimi nikarudi kwa wazazi maana hata funguo za hapa zilikuwa pale kwenu. Nikakaa kama siku kumi ili angalau kumpa nafasi mzee Ngoi atulie ndipo nirudi nijieleze nikiwa na wazazi. Baba na mama wakanisindikiza nikiwa na mtoto. Bwana nilijuta. Mzee Ngoi alikuwa mkali mno, heshima hakuna kwa wazazi wangu.” “Ilikuwa kama siku ile kwetu?” Willy akauliza kwa kejeli.

“Ila sasa mimi Chonge alinigeuka! Akaitwa kutoa ushahidi. Akaeleza yote ila yeye akajitoa kabisa. Akasema mimi ndiye niliyekuwa nikimuwekea dawa Ngoi ili kumuharibu akili na akasema nilishamwambia hata huyu mtoto sio wake Ngoi. Nilimfanyia tu uchawi kumdanganya kuwa mimba ni yake akakubali. Halafu eti nimemfanyia dawa huyu mtoto, hata akienda hospitalini kupimwa, ataonekana ni wa Ngoi tu. Kwa hiyo akaniambia hamtaki huyo mtoto tena na wala nisiwahi kumsogeza pale.” Zelda akalia kwa uchungu sana.

“Wakatoa ushahidi wote wa picha na sauti yangu nikisema kama nimemloga Ngoi. Ndio Ngoi akatufukuza na kusema akija kuniona pale tena, ananipeleka polisi na ushahidi anao. Hataki kuniona mimi wala mtoto wangu. Na hata nikimshitaki popote, anatoa ushahidi kuwa mimi nimemloga na hamtaki huyu mtoto kwa kuwa haamini na hatakuja kuamini kama kweli ni wake kwa kuwa nishamloga. Chonge ndiye mwanamke anayemtakia mema tokea zamani, amekuwa akiwasaidia bila tamaa. Akasema pale mbele ya wazazi kuwa Chonge ndiye atakayekufa naye, kwa kuwa wamekuwa naye na ni mwanamke mvumilivu. Akatufukuza pale pale.”

“Mimi nikaomba mizigo yangu, Chonge akasema haniamini tena, akawa ananisindikiza kila mahali ananisimamia kila ninachofanya huku akiniharahisha. Akamuita yule kijana anisaidie kubeba vitu vyangu na vya mtoto, aniachie nje. Tena nguo tu. Vitu kama vitanda vya mtoto akanikatalia nisibebe.” “Nani sasa?” Willy akauliza. “Si Chonge huyo! Akaniruhusu kuchukua nguo tu, bila aibu wala huruma! Tukatoka pale na wazazi nao wakaniambia itabidi nirudi tu kwangu. Nimewatia aibu mno na kuwafedhehesha kwa tamaa zangu. Nilikuwa na kila kitu, lakini sikuridhika. Wazazi wangu nao wakaniacha palepale. Wakaondoka. Ndio mimi nikarudi hapa. Lakini namshukuru Mungu sijatetereka, naishi vizuri tu.” Willy akavuta pumzi kwa nguvu nakubaki kimya hata hajui aseme nini tena. Akabaki ameinama.

“Willy!” Pendo akamgusa begani kama kumrudisha pale. “Mmmh! Hata sijui niseme nini tena!” Willy akabaki kama anafikiria zaidi. “Labda mimi niulize kama naruhusiwa.” Pendo akaanza taratibu. “Uliza tu. Labda utanisaidia na mimi kujua chakuongea. Maana nahisi nimeingiwa hofu na hayo mazingaombwe, sijui uchawi! Sijui lipi la kweli na lipi silo!” “Wewe sijawahi kukuloga. Chonge ndiye aliyenipeleka.” Zelda akajitetea. “Lakini si ulikubali na kufanya, tena mpaka kutumia madawa!?” Willy akamuuliza kwa ukali kidogo. Hapo Zelda akashindwa kujibu.

 “Nashindwa hata kuendelea kukuuliza chochote kwa kuwa unasura nyingi sana Zelda, ambazo kila nikikutana na wewe, zinajifunua! Zelda niliyetambulishwa na mama, siye niliyekutana naye nilipokwambia tuishi pamoja, ili tulee mtoto! Hiki unachosema alikufanyia Chonge, nafikiri ndicho alichokuona ukitufanyia sisi watoto wa baba. Alikuona vile ulivyomudu kugeuza moyo wa baba, ukawa mkatili kuliko kawaida. Ukafurahia kumuona baba anatufukuza nyumbani kwetu. Tulipozaliwa na kukulia. Chonge ameiga ulichokifanya Zelda. Hakikuwa kitu kigeni. Na pengine Chonge hakuwa na hilo wazo ila alilipata kwako.” Zelda akanyamaza na hapo akashindwa cha kujitetea.

“Ulitaka kuuliza nini Pendo?” Willy akamgeukia Pendo. “Nilitaka kujua kwa mchungaji alizungumza nini na kwa nini alikwenda tena kwa mchungaji Swai?” Pendo akabakia na kile kilichowapeleka pale, hakuyumbishwa na habari nyingi za Zelda. “Swali zuri sana. Amenichanganya mpaka nimesahau swali la msingi. Ulifuata nini kwa Mchungaji Swai, na ulimwambia nini?” Willy akarudia swali kwa msisitizo. “Ilikuwa tufunge ndoa pale kanisani kwa mchungaji Swai. Tulishakwenda tukazungumza naye mimi na Ngoi kwa pamoja. Akatuuliza maswali na kuzungumza na sisi. Tukaweka kabisa tarehe yakufunga ndoa. Sasa Ngoi aliponifukuza ndio nikarudi kwa Swai ili kuzungumza naye.” “Ulizungumza naye kama hivi?” Willy akauliza. Zelda akababaika sana na kushindwa kutoa jibu la moja kwa moja.

“Usipoteze muda Zelda. Tafadhali jibu swali.” “Sio kwa undani na uwazi hivi.” Zelda akajibu kwa kubabaika. “Labda utuambie ni nini ulimwambia, sisi wenyewe tutajua ni nini uliacha.” “Mimi nilimweleza ule mwanzo kabisa kabla mama hajafa na makubalino yetu.” “Yapi Zelda?” Willy akauliza kwa ukali. “Yale ya kukubebea wewe mimba, lakini naweza kulala na Ngoi pia ili kuhakikisha nashika mimba, ili kukufanya wewe utulie kwangu, umuache mkeo, unioe mimi.” “Hivyo tu ndivyo ulivyomwambia!?”  Akauliza Willy kwa ukali na mshangao. “Nikamwambia lakini baada ya kifo cha mama, baba akanibadilikia, sasa hivi yupo na msichana wa kazi, hanitaki mimi na mtoto.” “We Zelda!?” Willy akashangaa sana.

“Naomba subiri kwanza Willy.” Pendo akamtuliza ili yeye aongee. “Ukamwambia nini juu ya Willy?” Pendo akauliza. “Mimi sikuongea mengi juu ya Willy zaidi ya kumwambia pia nililala na Willy, ila Willy aliondoka sijui alipo.” “Hukumwambia kuwa mtoto ni wa nani?” Pendo akamuuliza swali la kumtenga tu, lakini akitaka na yeye jibu. “Ukweli mpaka sasa hivi nimechanganyikiwa.” “Usinitanie Zelda!” Willy akapaniki. “Naomba utulie Willy. Tafadhali mpenzi. Tupo hapa kwa mazungumzo. Tulia mimi nizungumze na Zelda.” Willy akatulia.

“Unaposema umechanganyikiwa, unamaanisha nini?” Pendo akamuuliza kwa sauti yake ya taratibu bila kuonyesha jazba. “Maana ukumbuke nilikuwa nikilala nao hawa wote wawili.” Pendo akaumia lakini akajikaza, ila sio Willy. “Sio wewe ulisema mbele ya ndugu zangu kuwa mtoto ni wa mzee kwa kuwa siku zako za hatari, ulikuwa ukianza na baba?” Kimya. “Wewe Zelda?” Willy akaita kwa ukali, Zelda akaanza kulia. “Ni muongo huyu Pendo. Ameona kwa baba ameshindwa, ndio anataka kuniharibia na kwangu kwa kunikimbilia sasa hivi. Hukumuona siku ananikana.”  Pendo akamshika mkono Willy kama kumtuliza. Willy akanyamza tena.

“Naomba usilie Zelda. Tulia tuzungumze ili tufikie muafaka. Willy ni mpenzi wangu, nasitataka atelekeze mtoto kama ni wake. Eti nijidai kama huyu mtoto hayupo halafu ulee peke yako! Hapana Zelda. Lazima tutamtunza kwa namna yeyote ile.” Hapo Zelda akaanza kutulia. “Nashukuru dada.” Zelda akafuta machozi akijua ameshapata ulaji. Pendo akaendelea. “Sasa ili kusiwe na kurukana na kubadilika tena, haya mambo lazima yaende kwa maandishi. Kuwepo na kukabidhiana matumizi ya kila mwezi ili usilemewe. Ataingizwa kwenye matibabu ya kazini kwa Willy ili akiwa anaugua kama hivi, awe anapewa matibabu mazuri na kuhakikisha anawekewa akiba benki, ya kuja kusoma baadaye.” Mpaka Willy akamgeukia Pendo kwa mshangao. Pendo akamminya ule mkono aliokuwa amemshika, Willy akatulia.

“Sijui kama unanielewa Zelda? Sitakubali Willy akuachie majukumu ya mtoto kama ni wake.” “Nakushukuru dada. Asante. Mungu na wewe akubariki.” Pendo hakutaka hata kuitika. “Sasa, itabidi kumpima huyo mtoto na Willy.” Hapo Zelda akashituka sana. “Haya mambo yanakwenda kisheria Zelda. Leo Willy hawezi kutokezea na jina tu la mtoto ofisini kwao nakusema naomba kila mwezi kiasi hiki cha pesa kiende kwa huyu mtoto, na mnipe kadi nyingine ya matibabu kwa ajili ya mtoto wangu! Haitawezekana. Lakini mtoto akipimwa, akajulikana ni wa Willy, zile karatasi, Willy atazichukua na kuzipeleka ofisini kwao, kuanzia hapo utaratibu wa matunzo ya mtoto uanze. Sijui kama umenielewa?” Zelda akanyamaza.

“Au hutaki msaada, unataka umlee mtoto wako mwenyewe?” “Nataka msaada. Maisha magumu, halafu ndio nimeanza tu kazi kwenye hiyo shule hata hawalipi vizuri.” “Basi twende hospitalini hata sasa hivi. Na ndio vizuri mtoto wako atafanyiwa vipimo zaidi kujua afya yake. Na utakutana na daktari wa watoto akushauri vizuri.” Hapo Zelda akakubali lakini Willy akawa na wasiwasi.

“Majibu yakija yakawa kama vile alivyosema baba!” Pendo akamwangalia kama hamuelewi. “Kama kufanyiwa uchawi sijui mazingaombwe, vipimo vionyeshe ni wangu kumbe si wangu!” “Ndipo tutakapoomba hayo mazingaombwe yasije kuisha ili abakie kuwa mtoto wako kama anavyofanya mwenzio Jack. Hajapungua mahali popote. Anahesabu ni baraka kupata wale watoto. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Si wewe wala mimi tutakuwa wa kwanza. Kwanza huyu mtoto mmoja tu atatugarimu nini Willy?” Willy akapoa.

“Hakuna tutakapopungua kumsaidia mtoto mmoja tu hapa duniani. Akala vizuri, akasoma vizuri na kukua kwenye mazingira mazuri! Sidhani kama ni jambo baya.” Zelda akazidi kufurahi, akajitayarisha haraka na kuchukua begi dogo la mwanae, wakatoka na kukuta watu wengi nje ya mlango kama wamekaa wakifanya shuguli zao, lakini wakajua walikuwa wakisikiliza. Wakatoka kimya kimya, Zelda akafunga mlango wake, nakuwafuata kwenye gari. Willy akiomba kikombe alichokwisha nywea kimuepuke. Kuzaa na Zelda! Willy alijawa na wasiwasi mpaka akaonyesha, ila Pendo akamuacha tu maana alijiambia aliyafuata yeye mwenyewe huko kwa Zelda! Apambane na hali yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mtoto Wa Nani? Itajibiwa  Sehemu Inayofuata.

Usipitwe.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment