“Umeshaona
ile sinema ya ‘Simba’?”
Jack akamuuliza, Tino kimya. “Kaitafute, uitizame. Utaona jinsi lile dume
linavyomlinda mtoto wake huyo Simba. Wala si mama ndio mlindaji, ila baba! Kwa
hiyo kama mnafikiri mnatengeneza kesi dhidi ya Sabrina, nakusaidia, mnapambana
na Jackson Msindai. Baba niliyepewa hicho cheo na Mungu na kukipokea kwa
heshima kubwa sana. Nitapambana kwa kila pumzi niliyonayo hapa duniani, na
Mungu atanisaidia na kunitetea. Nitapambana kwa uwezo wangu wote kuhakikisha nikimalizana
na wewe, unaelewa na kujua, huna ulilobakiza hapa duniani. Kwa hiyo mkajipange
sawasawa.” Jack akaongea kwa ujasiri mkubwa sana.
“Na
nitahakikisha mpaka namalizana na wewe utakuwa kila ukisikia jina la Sabrina,
utajua sio tambaa la deki la kusafishia matapishi kila unapotapika.” Jack
akamsogelea zaidi akamkazia macho zaidi. “Utajua, utajuta na nitahakikisha
unaelewa kuwa bahati huwa zinakuja mara moja tu. Na kwako ililetwa na Mungu,
ukaiua kwa pesa yako mwenyewe. Sikutishi, ila nakuthibitishia, UTAELEWA. Nakukaribisha
NIJARIBU.” Jack akatulia kama kumpa nafasi akimtizama. Mapacha wake waliokuwa
wamejilaza begani wakatoa uso walipomsikia baba yao ameongeza sauti wakati
anasema ‘NIJARIBU’. Wote kwa pamoja wakambusu Jack shavuni na kupiga makofi
kama wanaojipongeza kwa walichofanya wenyewe kwa dad wao. Jack akarudisha akili
kwao, akawabusu pale pale Tino akiwaangalia. Wakajirudisha begani.
Sabrina
akasikika akicheka, kitu kilichomuudhi zaidi Tino mpaka akawa mwekundu. “Kama
nilikuwa sijakutambulisha, basi huyo ndio Jack niliyekuwa nikikwambia habari zake.
Na ndiye mume wangu.” Sabrina akawa kama amepata ujasiri akajisogeza mbele
kidogo ili amuone vizuri Tino usoni. “Na nyinyi mtanitambua. Nikejelini tu,
lakini nazijua haki zangu. Na mahakama itanitetea.” “Itakutetea kwenye haki
yako. Na ndio kazi ya mahakama, kutoa haki za wananchi. Kama unahisi unahaki
yako, hujaipata, au umenyang’anywa, basi kimbilia mahakamani kama ilivyo
desturi yako. Maana nasikia wewe ni hodari wakudai hata visivyo halali yako kwa
kumtumia mwanasheria wako Max, anayekusaidia kusuka kesi. Sasa safari hii, ujue
umekutana na Simba. Nitanguruma, hutakaa ukanisahau wala kusogelea familia
yangu tena.” Mpaka Sabrina akashangaa.
“Nimedai
nini kisicho changu!?” Akauliza Tino kwa hasira. “Kudai mshahara usiofanyia
kazi. Unaishi kwa jasho la watu wanaoamka kila siku asubuhi na kwenda kazini
kufanya kazi na kuingizia kampuni faida, wakati wewe unajiliza kama mtoto mdogo
kuwa ni mgonjwa. Unafikiri sikufahamu? Nakufahamu sana. Najua ulikuwa nchini
Italy ukifanya shuguli zako binafsi, lakini wewe na mwanasheria wako
mkidanganya upo kwenye matibabu uendelee kulipwa, wakati unafanya mafunzo ya
uchoraji upate leseni ya kimataifa na kujifunza lugha, na ndio umerudi.”
Sabrina akazidi kushangaa. Tino akaonekana ameingiwa hofu.
“Nakujua
au ninawajua vizuri sana. Na ninazo picha ambazo Max alikutumia za watoto wangu,
akikushauri uje uwadai.” “Ni damu yangu na mshahara ninaolipwa ni haki yangu.”
Tino akajitetea akionyesha hasira ya waziwazi lakini wazi alionyesha kuishiwa
nguvu, anajikaza tu. “Na ndivyo anavyokudanganya Max. Sasa mwambie Max,
ninakuja kama moto, nikimalizana na yeye, hatakaa akawa mwanasheria tena hapa
nchini. Nitahakikisha anawajibika kwa kosa lakuchukua picha yangu na watoto
wangu na kusambaza bila idhini yangu huku akikuchochea wewe uje ufanye fujo
kwetu. Mchochezi, mvunja amani na mvunaji asipopanda. Anatumia vifungu vya
sheria vibaya, kujinufaisha. Kwa hiyo mwambie Maximilian Kundi, wakati anakutengenezea
kesi dhidi yetu, ambayo kwanza kabisa hata kesi yenyewe tu, haipo. Kwa
kuwa ulishaua watoto wako na ushahidi wote ninao na ukiri wa video wa daktari aliyeua
watoto wako upo. Sasa mwambie ajiandae na kesi yake na yeye. Mwambie ninakuja,
na sitamuacha.” Sabrina akashangaa sana na kuogopa. Tino mwenyewe
akabaki ametoa macho.
“Ulifikiri
nilipokwambia nakusubiria kwa hamu unafikiri nilikuwa nakudanganya? Uliona
kimya kwa kuwa nilijua utasimamia ule usemi wako uliomjibu Max na kumkatia simu,
alipokupigia simu ukiwa nchini Italy akikushawishi urudi nchini kudai
watoto wangu, ili yeye atengeneze pesa zaidi kupitia wewe, ukajibu kwa hakika
kabisa, watoto si wako, ni wa Sabrina.” Tino akazidi kuchanganyikiwa. “Nikajua
unajielewa na kwa hakika ulikusudia kweli kutokuwa na watoto na mke wangu. Maana
ulihatarisha maisha ya mpenzi wangu haswa ili tu kuwaua watoto! Na hilo nitakuja kukulipiza tu.
Ipo hukumu yake juu ya hilo. Endelea kunifuata fuata, nakuhakikishia utalipa
ulichomtendea mke wangu.” Sabrina akajisikia vizuri, Jack akaendelea.
“Lakini
kwa ule usemi wako uliompa Max kuwa, ‘watoto si wako ila ni wa Sabrina’,
hakika nilikuheshimu sana. Nikajua hata kama wewe ni shetani mwenye roho mbaya
ya namna gani, lakini unajielewa na unajua unachokitaka. Ndio maana nikakuacha.
Sasa leo unakuja kunifanyia fujo mbele ya mke wangu na binti zangu! Hakika umeharibu
Tino. Umemfungulia Simba mwenye njaa! Hamtabaki salama.” Junior kaka yake Jackson
akaja. “Mmepotelea wapi nyinyi?” Akauliza
na kusogea pale waliposimama. Akakuta ile hali ya tension pale, ila wote
kimya. “Vipi Dogo? Kila kitu kipo sawa hapa?” “Oooh yeah! Like never before!”
Jack akajibu huku akimtizama Tino kibabe. Tino akaondoka akiwa mwekundu mpaka
macho. Wakabaki wakimsindikiza kwa macho mpaka akapotea machoni kwao.
Jack
akamgeukia kaka yake. “Naona tumefikia muafaka juu ya nyumba, kaka.” “Kwanza
tukushukuru kwa kutufikiria shem. Asante sana.” Sabrina akadakia. “Na nyinyi
mnajitahidi. Zaidi wewe Sabrina. Ni mke mzuri. Unamsaidia sana mwenzio. Am
so proud of you two. Popote mtakapo kwama, mniambie.” Wakaangaliana.
“Nini?” Junior akauliza. “Tunahitaji msaada wa fedha ili kuinunua hiyo nyumba
kaka. Tukisema tutoe tu pesa kwenye akiba sasa hivi, wanangu watalala njaa.”
Wakacheka.
“Na
niwaambie kabisa, nyumba ni hazina ambayo hamtajutia. Hiki mlichoamua ni muhimu
sana kwa kuwa hamjui maisha yatawapeleka wapi. Mnaweza kujikuta mnapata kitu
kizuri zaidi huku Dar, ikawalazimu kurudi. Hamtaki kurudi mnaanza kuhangaika
pakuishi.” “Ni kweli.” Sabrina akakubali. “Na pia mnaweza kufanyia biashara
kama mimi na Joy tunavyofanya. Na nashauri kabla yakununua, mkaingalie. Joy
aliipenda sana kwa kuwa imekamilika na ipo sehemu nzuri. Mwenye nayo alifariki,
alitangulia mke, akaja yeye, ndio ndugu wanauza ili wagawane ndio maana bei ipo
nzuri. Kesho nitawapeleka, leo inabidi niondoke. Nimeitwa.” Wakaelewa ni mambo
yake ya kikazi. “Ila kesho nitakuwa na nafasi asubuhi kabla hamjaondoka.”
“Tunashukuru sana kaka. Tutamshukuru na shem.” “Sawa sawa.” Akawaaga na
kuondoka.
Jack Ampe
kwa ufupi kilichokuwa kikiendelea kati ya
Max, Mama
Kundi, & Tino. Sasa Usalama wa Taifa.
S |
abrina
akamwangalia Jack. “Nina mengi yakukuuliza, lakini naona tutazungumza vizuri
usiku, baada ya kukupongeza vizuri tena kwa kituo.” Jack alicheka sana.
“Nahitajika pongezi?” “Kubwa sana. Leo usiku ujiandae, utachoka wewe!” Jack
akazidi kucheka. “Najilaumu wewe! Acha tu Jack. Nimejichelewesha mno! Lakini
wewe! Hakika wewe ni wangu. The best dad and sweetheart in town.” Jack
akajisikia vizuri sana. “Daah!” Sabrina bado hakuamini utetezi alioufanya Jack
kwao. Jack alisimama kama dume kweli kweli akitetea familia yake, mpaka
akamshangaza Sabrina.
“Turudi
kwenye shuguli, wasije ona wametufanikishia ya watoto wetu, tumekimbia kumbe
huyu mwendawazimu ndio ametuchelewesha hapa.” Wakaanza kuondoka. “Kwanza
amenifanya niongee kitu ambacho nilitaka kuwashitukiza. Kosa la kusambaza picha
zangu na wanangu!” “Ulijuaje Jack!?” “Umesahau mimi siku hizi mtu mkubwa sana?
Nafikishiwa habari bila kuzitafuta.” Akajisifia kidogo Jack na kumfanya Sabrina
acheke huku akimwangalia alivyojivuna. “Lakini Sabrina, acha tu. Niseme ukweli ni
Mungu tu. Baada ya kuachana na Max siku ile uwanja wa ndege nikiwa nimemkatalia
mawasiliano na wewe, kile kitu kikaendelea kunisumbua. Jinsi alivyokuwa
akiwaangalia wanangu na wewe! Nikasumbuka sana moyoni. Nikapuuza kwa muda,
lakini nikasema hapana. Lazima nimchunguze Max, kumjua yeye ni mtu wa namna
gani. Nikamuomba mtu wa usalama anisaidie kumpeleleza.” Sabrina akajua ni dada
yake tu ndiye aliyemuomba ampelelezee, maana Jacinta ni mtu mkubwa sana huko
Usalama wa taifa.
“Sikutaka
kukwambia ili nisikuogopeshe. Lakini Sabrina!” “Nini?” Sabrina akauliza. “Watu
ni wabaya mke wangu. Yaani acha mama! Huyo mtu alipoanza uchunguzi, akakutana nao
hao watu wawili pamoja na mkewe Max, yaani yule mtu mwenyewe akaniambia
nijiandae kwa vita inayonijia mimi na familia yangu. Yalinaswa mazungumzo yao
yote na mipango ya Max, kwa Tino na mkewe pia. Lakini alipoishia ushawishi kwa
Tino, Max akiwa ameshamtumia picha za watoto wangu, ni kama aligonga mwamba. Kwa
kuwa Tino alimjibu kwa ujasiri kabisa kuwa watoto ni wa Sabrina. Max
alipoendelea kumlazimisha, Tino akawa mkali kabisa, akisisitiza kuwa watoto
ni wa Sabrina na kumkatia simu kwa kuwa Max aliendelea kumsisitiza arudi
watengeneze kesi kudai watoto wake kwani ni wazuri sana.” “Haiwezekani Jack!”
Sabrina akashangaa sana kwa kuumia.
“Hakika
Brina. Ndio kaka akasema lazima kuongeza umakini na kujipanga.” Sabrina akashituka
sana. “Kwani Junior anajua!?” “Ilibidi Sabrina. Haya mambo yamechukua sura
nyingine kubwa sana, kwani wamenasa na mazungumzo ya Max na mkewe ambaye
anafanya kazi ofisi moja na kaka.” “Nakumbuka Max alisema siku ile.” “Sasa
mkewe alionekana kumuonya Max asimshawishi Tino kudai watoto. Si kwa wema, ila
kuhofia kazi yake. Sasa utachoka Max alichokusudia kukifanya dhidi ya Junior,
kama bosi wa mkewe na waziri. Hapo sasa ikabidi kaka aambiwe na usalama
wajulishwe rasimi ili akitekeleza sasa, kaka awe salama.” “Nini Jack!?” Sabrina
akazidi kuchanganyikiwa kwani hakutaka kabisa mtu amjue baba wa watoto wake,
ibakie tu Jackson Msindai.
“Max
alimwambia mkewe, kabla kaka hajamgusa kumuharibia kazi wakati yeye Max anadai
watoto wa Tino kwetu kisheria, wamtengenezee kesi kubwa na nzito.” “Junior!?”
“Ndiyo. Mbaya eti hata wamtumie yeye mwenyewe mke wa Max. Sasa sijui aseme
anamtaka kimapenzi au amembaka ofisini, hawakuweka wazi lakini alisikika Max
akimwambia mkewe watamtengenezea kesi nzito dhidi ya huyo mkewe. Ili kwanza
atumbuliwe na kumchafua haswa, ili kaka awapishe mjini.” “Jackson Msindai wewe!
Max?” “Ni mbaya yule! Mimi mwenyewe sikuamini. Anaonekana anazisaka pesa kwa
kila namna na ndio maana amemshikilia sana Tino ili kujinufaisha.” “Na Tino
anamsikiliza sana. Yuko kama mjinga kwa Max.” Sabrina akachukia kabisa kila
alipokuwa akimkumbuka Max na mazungumzo aliyokuwa akiyasikiliza kwa siri kati
ya Max na Tino.
“Sasa
kuanzia hapo ndipo ikabidi sasa uchunguzi wa kina uanze ili kujua tunapigana na
nani. Ndipo sasa habari zao zikaanza kusakwa kwa kina tena zoote. Kwa kifupi, wanatizamwa
kwa karibu mno na kesi yao imechukua sura kubwa zaidi nitakavyokwambia.
Uchunguzi ukikamilika, utasikia tu. Lakini ujue Max alikuwa akipanga vita dhidi
yetu. Angetushitukiza vibaya sana. Ni Mungu.” “Kweli ni Mungu Jack. Lakini nimeumia
sana. Max amenipokonya kitu kikubwa na cha muhimu sana. Sikutaka uma umjue Tino
kabisa. Sikutaka habari zake zijulikane na zihusishwe na familia yangu. Max alimshauri Tino vibaya sana
juu yangu. Kama haitoshi, amerudi tena kwenye hiki Mungu alichonibariki! Hakika
naumia Jack.” Sabrina akalalamika kwa uchungua sana.
“Nisikilize
Sabrina. Labda ni katika kujulikana tu Tino, lakini nitahakikisha hiki
tulichonacho, hakuna atakayetupokonya hata Tino mwenyewe na Mungu atatusaidia.”
Sabrina akanyamaza. “Hili jambo halipo chini yetu tu. Nakuhakikishia Max
hatawahi kuja tena kuwa tatizo kwetu na kwa mtu mwingine. Subiri uone. Na
sidhani hata kama atabakishiwa leseni ya uanasheria tena. Kikubwa na cha msingi
ni sisi kujipanga na kuwa ukurasa mmoja pale tutakapohitajika kusimama
mahakamani endapo Tino atatushitaki. Lakini napo tutamuwahi.” “Sijui Jack!
Hakika Mungu aingilie kati. Tino hakutaka hawa watoto kabisa. Na Max alihakikisha
anamshawishi Tino akiita ujauzito ni tatizo au niseme kosa. Akamwambia kwa
kumsikia mwenyewe, ahakikishe haniachi na ujauzito. Asimamie na ahakikishe
ananiacha na pesa tu, tena kwa maandishi. Iweje leo aanze tena kuibua kesi?”
“Yeye anataka pesa tu. Wala si kwamba anakusuduia zuri kwa yeyote. Ukisikiliza
mazungumzo yake na mkewe, ni pesa tu na umaarufu. Lakini Sabrina, Mungu yupo na
sisi, hata hili litapita kwa namna ambayo Mungu atatupigania.” “Ni kweli Jack.
Hapo umesema kweli. Mimi nitamlilia Mungu wangu mpaka nibakiwe na haki yangu.” Wakazungumza
kidogo na kuamua kurudi walipoacha watu wengine.
Mama
Msindai na Shower ya Briyan.
W |
akati
wakitembea simu ya Jack ikaanza kuita mfukoni. “Nisaidie kutoa.” Akatoa. “Mama Msindai
huyo.” “Pokea.” Sabrina akapokea. “Ni mimi Sabrina,
Jack huyu hapa amebeba watoto.” Sabrina akawahi asije akasema neno
lisilomuhusu. “Nataka kujua hiyo tarehe ya baby
shower. Haitakuwa kubwa kwa kuwa ni mtoto wa tatu. Tunafanyia tu nyumbani.”
Sabrina akaanza kucheka. “Mimi sijakupatia mwenzio
mama! Ni nini lakini?” Jack akauliza kwa kulalamika. “Nataka nifanye maandalizi mapema. Kwanza nishachelewa kuwapa
watu tarehe kamili. Unataka nianze kuonekana mbambaishaji?” “Kwamba ushawaambia
watu kuwa kuna baby shower!?” Jack akashangaa sana. “Ndiyo! Hee! Ulitaka sasa nishitukize watu! Wewe mtoto vipi?
Wewe niambie tarehe mtakayokuja, nijipange.” Wakamfikia alikuwa
amesimama kama mlangoni kutokea upande wa beach. Sabrina akakata simu akicheka,
nakuirudisha mfukoni kwa Jack.
“Kwa
hiyo hapo ulikuwa ukitufuata?” Jack akamuuliza. “Ndiyo! Naona hatufikii muafaka
halafu nasikia kesho mnaondoka, na sijasikia mipango ya kuja nyumbani! Umekuaje
Jackson wewe!” “Naomba kabla hujapenyeza agenda ya kuja nyumbani kesho wakati
unajua kabisa kilichotuleta hapa ni Pendo, naomba tumalize hilo la shower
mama.” Sabrina akazidi kucheka pembeni ya Jack. “Sawa. Kwahiyo mnakuja lini kwa
shower na kujifungua? Au mkija mnakuja moja kwa moja?” “Ni nini
kinachokufanya ujue kama na kujifungua itakuwa ni huku na Singida?” “Bwana wee!
Tushapita huko muda mrefu sana. Naomba nipe tarehe acha kupoteza muda.” Jack akamtizama
mama yake asimmalize.
Akamgeukia
Sabrina. “Unakuja lini? Mumeo anaweza akakufuata sio lazima ukamsubiria mpaka
apate likizo kazini.” “Naomba zungumza na mimi mama.” “Wewe mbishi sana bwana!
Jambo dogo tunavutana weee! Niambie Sabrina.” Akamgeukia Sabrina tena.
“Tukifika tu Singida, tutakupa tarehe zote mama, wala usijali.” “Ona mambo
yalivyo rahisi! Unataka kufanya mipango inakuwa migumuuu!” Akamalizia hivyo
mama Msindai na kurudi kwenye kundi la watu, akamuacha Jack akimwangalia.
Sabrina akaendelea kucheka.
Jumapili.
Kesho
yake kabla yakuondoka jijini, Joy ambaye alikuwa akifanya biashara ya Real
estate. Ananunua nyumba, anakarabati na kuuza au kupangisha, yeye ndiye
aliyeona hiyo nyumba, akata wainunue wao sababu kwanza ilikuwa sehemu nzuri sana, ilishakuwa na kisima
kilichochimbwa na kujengewa vizuri, akapenda uzio wake, na bado ilikuwa mpya,
haikuhitaji marekebisho yeyote, ni usafi tu na kuhamia hapo. Bei ndio
iliyomchanganya zaidi. Alipomwambia mumewe, akamwambia hiyo itawafaa Jack na
Sabrina.
Sabrina
alipoiona, tamaa yakurudi kuishi Dar ikamwingia. “Hapa tunapata chumba cha kaka
Briyan na dada zake wanapata chumba chao, na bado tunabakiwa na vyumba viwili
mbali na chetu! Mungu atupe nini?” Joy akawa anacheka tu huku akiwaonyesha
uzuri zaidi wa ile nyumba. Wakakubaliana wataichukua, waandikishane kila kitu,
wao watatuma pesa kiasi, nyingine wawakopeshe. Joy akawahakikishia mpaka
ifikapo jumatano nyumba itakuwa yao. Joy alikuwa na kampuni yake na wafanyakazi
kabisa kwenye hiyo kampuni yake wanaomfanyia kazi. Kwa hayo alikuwa na uhakika
wakuwakamilishia hiyo nyumba bila shida tena kwa haraka.
Wakakutana kwa mama Msindai kwa chakula cha
mchana. “Umefurahi sasa?” Jack akamuuliza mama yake. “Uwe unakumbuka kwenu,
uache kujisahau.” Mama Msindai akamjibu hivyo. Lakini wote walishamjua huyo
mama, akitaka kitu chake, atakaba mpaka kiwe. Jack na familia yake wakaondoka
jijini kurudi nyumbani kwao.
Willy&Pendo.
Jumapili
hiyo hiyo Willy na Pendo nao baada ya ibada wakaomba kuzungumza na mchungaji juu
ya ndoa yao. Hawakuwa washirika wanaojihusisha sana na mambo ya hapo kanisani
lakini walijulikana na watu baadhi. Na mchungaji alifahamiana na familia ya
kina Ngoi zaidi. Aliwafahamu. Na ndipo kwenye kanisa hilo hilo walifanya ibada
ya mazishi ya mama Ngoi. Kwa hiyo aliwajua Mzee Ngoi na mkewe zaidi. Alijua
mengi yanayoendelea kwenye familia hiyo na alishafika mara kadhaa nyumbani kwa Ngoi
enzi za uhai wa mama Ngoi akiwa mgonjwa kwa maombi hata hospitalini alipokuwa
akilazwa, alikuwa akienda kuomba pamoja naye kwani mama Ngoi alikuwa mmoja wa
viongozi walio mstari wa mbele hapo kanisani. Hata ndugu zake wengine walikuwa
wakishiriki hapo japo sio washirika wa kila jumapili.
“Ni
kama mmesambaratika sana Willium!” Mchungaji akaanza na Willy baada ya kutoa
pongezi kwa Pendo. “Tupo.” Willy akajibu kwa ujumla. “Unawasiliana na ndugu
zako? Sijawaona kanisani.” “Nafikiri majukumu yamekuwa mengi tu, lakini wapo.”
Mchungaji akatulia kama kumpa nafasi kumsikia, maana majibu yake yalikuwa ya
jumla kama anayeficha ukweli. Wakatulia tena kidogo Willy akitafuta pakuanzia.
Akajiweka sawa, Pendo kimya na mchungaji kimya.
“Nataka
kumuoa tena Pendo.” Akaanza Willy. Mchungaji akatulia. “Nataka utusaidie
tufunge ndoa hapa kanisani. Nilitaka kujua utaratibu unakuaje.” “Ndoa ya kwanza
nilifungisha mimi hapahapa kanisani. Labda niulize sababu ya kuvunjika.” Hapo
likawa swali gumu sana. Willy akafikiria akatulia kidogo. “Kulitokea matatizo
kidogo.” Akajibu Willy. “Udogo gani uliosababisha kuvunjika kwa ndoa, Willy?”
Mchungaji akambana. “Kwa kurudi kanisani inamaana unakusudia kuanza upya. Sasa
nilazima nijue kilichosababisha kuharibika kwa mwanzoni, ili turekebishe
kabisa, pasitokee tena hilo tatizo unapoanza upya.” “Nilitoka nje ya ndoa,
nikajua nimempa msichana mwingine mimba. Lakini mpango haikuwa kuachana na
Pendo. Ilikuwa mtoto azaliwe, nizungumze na Pendo, akinisamehe, tuendelee huku
nikilea mtoto wangu. Lakini mambo hayakwenda vizuri tukaishia kuachana, lakini nikarudi
kwa Pendo, nimemuomba msamaha, amekubali turudiane, ndio nataka tufunge tena ndoa.”
Willy akajieleza.
“Na
unayemzungumzia hapa ni Zelda?” Wote wakashangaa kidogo mchungaji alipouliza
hivyo. “Nataka uhakika.” “Ndiyo.” Willy akajibu. “Ni kitu gani
kilikuthibitishia kuwa mtoto si wako?” Kidogo hilo swali likamfanya Willy
kuingiwa na wasiwasi, akanyamaza. “Namfahamu Zelda na baba yako. Ukumbuke
wazazi wako walikuwa washirika wazuri sana hapa. Hata ndoa ya baba yenu ya
pili, alitaka ifungwe hapa.” “Walitaka!?” Willy akawa hajaelewa.
“Nashauri kabla ya kuendelea na mpango huu wa Pendo. Kwa kuwa nimezungumza sana
na Zelda. Kwa muda mrefu sana. Najua kilichokuwa kikiendelea. Na hayupo kwenye
wakati mzuri na mtoto. Unahitaji...” “Sielewi mchungaji. Nini kinaendelea!?” Willy
akawa haelewi, Pendo kimya.
“Ndio
maana nakushauri kabla hujaendelea na hili lililowaleta hapa na Pendo, ili
kusitokee kosa kama kosa la kwanza, mtafute Zelda mzungumze kwanza.” Wote
wakabaki wakimtizama. “Siwezi kuzungumza mambo ya watu wanayoniamini nayo. Wewe
nenda kazungumze naye yeye mwenyewe Zelda.” “Si bado anaishi pale kwa mzee?” Willy
akauliza. “Sidhani. Nashauri umpigie.” Wasiwasi ukazidi kumwingia Willy, Pendo
ndio zaidi. “Sina namba yake ya simu na wala sijawasiliana nao wote wawili
tokea watufukuze nyumbani.” “Basi anzia kwa mzee wako.” “Siwezi.”
Mchungaji akabaki kimya.
“Hao
watu nilishachana nao muda mrefu sana na sitaki kurudi kwenye maisha yao.” “Nafikiri
hilo huwezi kukwepa tena Willy. Na sitaweza kuendelea na hili mpaka nijue
umefikia mwafaka na ulilolianzisha wewe mwenyewe kwa msaada wa mama yako, ndipo
nitaweza kuwaunganisha nyinyi wawili tena. Lasivyo tutarudia mchezo
uleule.” Wakatoka hapo kwa mchungaji wakiwa wamepoa, hawajui kwa uhakika ni nini
kinaendelea. Pendo akajihisi anamkosi wakupitiliza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini Kinaendelea kati ya Mzee Ngoi na Mpenzi
Zelda?
Kilichobadilika kwa Tino na kurudi kudai watoto
tena ni nini?
Mazito na
ya kusisimua yapo mbele.
Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment