Siku hiyo Pendo alirudishwa nyumbani akiwa amejawa furaha haswa. Mzima kabisa. Willy alikuwepo hospitalini wakati wakiruhusiwa. Lakini alikwenda kazini. Kwa kuwa alishapata baraka za wazazi, ikabakia yeye tu. Akaanza kupanga mipango ya kumvalisha pete. Mtu sahihi aliyemfikiria kwa haraka ambaye angemsaidia kuweka sawa mipango ambaye alijua Pendo ana mkubali akawa amebakia Sabrina pekee. Akaamua kumpigia simu.
Kwanza
Sabrina hakuamini kama ni Willy. “Kwema!?” “Kwema
kabisa. Habari za familia?” Willy akauliza. “Tunamshukuru
Mungu hatujambo.” Sabrina akawa amemaliza. “Nataka
kumuona Pendo.” Sabrina akacheka sana. “Sasa
nataka kumvalisha pete ya uchumba. Najua furaha yake itakamilika, wewe
ukiwepo.” “Mbona Mungu akubariki! Maana nilikuwa natafuta sababu yakunitoa humu
ndani, sikuwa nayo.” Willy akacheka.
“Sasa wewe mpigie simu Jack. Mwambie lazima mimi niwepo. Ukimuweka
sawa huyo, nakuja na timu yangu yote. Nimechoka kukaa humu ndani, na kucheza na
watoto tu.” Willy akazidi kucheka. “Kwani hauji tena Dar kufanya baby shower ya huyo
mtoto mwingine?” “Ukitaka kumuudhi Jack, mwambie mambo ya kuja Dar kwa baby
shower.” “Kwa nini?” “Sijui walimwambia nini mume wangu juu ya baby shower
ya hawa wanae wawili, naona amechukia, hataki tena. Kwanza hataki nije huko
nisije nikajifungulia huko Dar.” Ndipo Willy akakumbuka hekaheka ya
alipojifungua hao mapacha wakizungu pamoja na fujo alizosikia mama Misindai alitaka
kufanya siku ya baby shower yao hao watoto lakini Jacinta akamtuliza.
“Wewe mpigie simu
mpange. Na uweke msisitizo Willy, lasivyo Jack hawezi kukubali. Hataki nifanye
chochote au kwenda kokote, nalea tu hii mimba! Nimenenepa kwa kula na kulala
kama Pendo ambaye yupo bed rest wakati mimi sina tatizo jamani!”
Willy akazidi kucheka. “Nitafanya hivyo.”
Wakazungumza kidogo, wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Uzuri
ikawa jumapili hiyo ndiyo birthday ya mapacha wa Jack na Sabrina. Sabrina ana mimba
ya miezi nane tayari, watoto wake wakawa wanatimiza mwaka. Ikawa rahisi kuweka
mipango ya huko kuchumbiwa kwa Pendo kwa siri bila Pendo mwenyewe kujua. Wakamwambia
Pendo wanakwenda kuwafanyia birthday yao Dar ambako yeye yupo, kwa kuwa hawezi
kusafiri. Pendo alifurahia sana. “Na nguo zao mimi ndio
nitanunua na...” “Sasa usianze shuguli Pendo, mwishowe Willy atatufukuza kwenu.”
Wakacheka. “Aunt yao, Jacinta na Joy wamesema wataandaa
sehemu ya kufanyia pamoja na keki. Wewe naomba upumzike.” “Waambie nguo ni
mimi.” Pendo akaweka msisitizo. “Nguo tu, basi.”
Wakacheka na kuendelea kuzungumza wawili hao ambao walikuwa hawakosi
chakuzungumza.
Birthday ya
Mapacha,
Na
Kuchumbiwa tena Kwa Pendo.
S |
abrina na familia
yake walishukia nyumbani kwa Pendo ambako walishakuwa na chumba chao hapo. Wote
na watoto wao walikuwa wakilala chumba kimoja. Ukiwaweka chini, wanasambaa kila
mahali. Pendo alijitahidi kuwaandalia vitu kutokana na umri wao. Bado hawakuwa
wakiweza kutembea wenyewe, wanashika sehemu ndipo wanatembea. Jacinta
aliwaambia ameweka reservation, Cliff Hotel meza karibu na mchangani baharini
ili watoto wote wacheze, hilo likawa limekaa vizuri. Wakakubaliana familia zote
wakutane hapo kuanzia saa 9 mchana. Uzuri wakati wanafika hapo siku ya ijumaa
jioni, ndugu wa Pendo nao walikuwepo. Kwa kuwa wote Sabrina alijua wana watoto,
akawaomba mbele ya Pendo kuwa wawalete watoto wao ili wawaimbie Jeiline na Keiline.
Bila kujijua Pendo naye akaweka msisitizo kwa mama zao wasikote. Basi mpango
ukakamilika vizuri tu. Pendo hajui kama mlengwa ni yeye.
Ilipofika
mchana, Sabrina na familia yake wakaondoka na gari ya Pendo, Willy na Pendo
pamoja na msichana wao wa kazi wakaondoka na gari ya Willy. Familia hizo hawakuchelewa.
Wakajikuta wamekuwa wengi. Familia ya Msindai wote mpaka wazazi. Junior waziri
naye akawepo na familia yake. Familia ya Pendo wote. Mpaka wazazi, familia ya
Kenton, na Nancy pia. Wazazi wa Sabrina wote wawili na Sabina pamoja na rafiki
yake nao wakawepo.
Usingeshindwa
kuzungumza na mzee Msindai. Alikuwa mcheshi mno na mtu wa utani. Hata baba yake
Sabrina ambaye hakuwa msomi, alijisikia vizuri kuwa naye. Mazungumzo yake
yalikuwa yakawaida sana ambayo hayakuhitaji kufikiria ila kucheka tu. Akiwa
katikati ya kundi na hivyo alikuwa daktari wa watoto, mngecheka tu. Sasa
wakakutana na Jackson mwanae wote wanapenda watoto. Michezo ikaanza ni vicheko
hapo, Pendo asijue wote wamekusanyika hapo kwa ajili yake yeye.
Jack
alikuwa busy na watoto wake hao wakizungu, utafikiri amezaa na mzungu. Na hao
watoto walimjua Jack. Akiwepo mahali, akili na mawazo yao yote yapo kwa baba
yao tu. Na hawatakubali mtu awaguse ila baba yao tu. Jack aliwabebea michezo
yao akaisahau kwenye gari. “Sasa hapa tutafukuzwa Jack. Watazagaa hapa na
kuvuta wageni wa watu. Naomba ukawaletee michezo yao, akili iwe kwenye michezo
yao tu, tutulie.” Walishafika meza za pembeni na kusimama kwenye viti
wakichekea watu huku wakimwangalia baba yao. “Waoneni jamani! Acha kuwapungia
mkono bwana Jack! Waite.” Watu wakazidi kucheka. Jack akanyanyuka ili akafuate
michezo. Walikuwa wakifuatana kila mahali kama mchwa.
Walipomuona
baba yao ananyanyuka tu, wote wakaanza kurudi kwa haraka. “Nakuja sasa hivi,
nisubirini.” Jack akawaambia, wote wakaanza kulia. Pendo akawaita ili wamfuate yeye.
“Hapo walipo hakuna anayekumbuka jina lake hata mmoja.” Sabrina akafanya
wacheke. “Njoo Jeiline, mama.” Bibi yao akaita. “Mimi nakwambia hapo hajijui
kama yeye ni Jeiline, mama. Acha tu.” Na kweli huyo mtoto hata hakumwangalia
bibi yake, macho kwa baba yao wakilia. “Kwa nini unasema hivyo?” Akauliza
Pendo. “Labda baba yao aondoke ndio akili zao zinawarudia. Hata uwaite mpaka
sauti ikauke, hakuna atakayekugeukia, akili na macho yao ni kwa baba yao tu.
Mimi ninachofanya wakiwa wanacheza na baba yao nakwenda kuwakwapua.” Wakazidi
kucheka. “Na hawatanyamaza mpaka baba yao awachukue hapo. Ukiwagusa ndio
watazidi kulia.” Jack akarudi kuwachukua walishakuwa wekundu.
“Sasa
Jack akitaka kutoka?” Akauliza Junior. “Inabidi kuwakimbia. Anawaingiza
chumbani, anacheza nao na mimi naingia hapo. Michezo ikikolea. Ndipo Jack
anatoka taratibu.” “Hawalii sasa wakigundua ameondoka?” “Na wao wanatoka hapo
chumbani, wanaanza kumtafuta. Watamtafuta mpaka wakutane na mchezo mwingine,
ndio wanatulia. Wanaingia kwenye kila chombo, kila mahali.” Wakacheka.
“Muulizeni Sifa. Leo kawakuta wapo kwenye madroo ya jikoni. Wakifika, kama
umeweka vitu humo, wanasaidiana. Wanatoa kila kitu, halafu wanaingia ndani na
kukaa. Kama kuna sufuria wanazoweza kutoa kabatini, wanatoa, halafu wanaingia
wao humo ndani. Na wanasaidiana mpaka kila mmoja apate pakuingia, ndio
wanatulia.” Watu wakazidi kucheka. Ungependa kuwaona hao watoto. Walishakuwa na
nywele ndefu za kuanguka mabegani. Lakini kwa kuwa bado zilikuwa zakizungu,
zinateleza kusukika, walikuwa wakiegeshwa riboni tu zenye ua. Ungependa
kuwaangalia.
Willy
na Jack wakaongozana kwenye gari huku Jack amewabeba juu akiwaendesha kama
ndege, basi walikuwa wakicheka sana na machozi shavuni. “Ila wana michezo yao
ya kujenga. Hiyo ukiwawekea sehemu wanayomuona baba yao, wanatulia na kujenga
kwa muda mrefu tu, hutawaona wanazunguka.” Sabrina akaendelea kujibu kila
wakiuliza juu ya hao watoto. Kwa kuwa wao ndio walikuwa watoto zaidi pale,
walivuta macho ya wote na masikio.
“Jack
anawapenda hao watoto! Kutwa anatuma video zao na story zao haziishi. Ukitaka
Jack acheke, muulizie wanae.” Jacinta akaongeza. “Na ukita mzungumze jambo la
maana, asiwe na hao watoto. Hana cha maana anachoongea. Akiwa nao hapo
nyumbani, nakuwa na watoto watatu. Ukimwambia watoe watoto ndani ya masufuria,
anakwambia na yeye mwenyewe anatamani kama angekuwa na uwezo wa kukaa humo
ndani ya hayo masufuria ili apate ule ubaridi wake.” Mpaka mama yake Jack
akacheka. “Hana analozungumza la maana mkaelewana akiwa na watoto. Wala hana
analofikiria. Mkiwapeleka watoto kucheza ziwani, ujue unarudi na watoto watatu
wote wamejaa mchanga ni wakusafisha usiku kucha!” “Na Jack?” Pendo akauliza
huku akicheka. “Na Jack, ndiyo. Mnalala usiku mito inajaa michanga, basi
hamuwezi tena kulala. Inabidi uamke uanze na yeye kumkwangua kichwa kumtoa
michanga!” Wakazidi kucheka. Jack akarudi na wanae akiwa amewashika mkono
wanatembea.
Joy
akaona alete keki wakate, wamalize la watoto ili kumpa nafasi Willy. “Nilikuwa
namuuliza mke mwenzangu juu ya baby shower ya dume.” Joy akamchokoza
Jack wakati anasimama. Jack akamwangalia Sabrina. “Mbona unaniangalia mimi,
wakati anazungumza na wewe?” “Sabrina akakujibuje?” Jack akauliza wote
wakacheka. “Sijaelewa jibu lake.” Joy akatumia akili kwa haraka akajibu hivyo.
Jack akamwangalia tena Sabrina. “Sasa mimi nimefanya nini Jack!?” “Wameshaanza
kukushawishi na wakati tulikubaliana kabisa, Sabrina.” Wakaanza kucheka.
“Hakika sijashawishika.” “Kwani hamtaki baby shower?” Sabina akauliza.
“Hatutaki
baby shower. Au sitaki baby shower. Anayetaka kumpa mtoto
zawadi, anakaribishwa. Lakini sitaki baby shower, na huyo mtoto
anazaliwa Singida wala si hapa. Sitaki hekaheka nyingine.” Jack akaweka
msisitizo. Kila mtu akakumbuka walipozaliwa hao wazungu. “Na masharti ya mimi
kuwepo hapa leo ni nisije kushawishika hata mama Msindai aseme nini!” Sabrina
akaongea kwa sauti ya chini lakini wote wakacheka. “Wewe msikilize tu Jack.” “Umeanza
mama. Nilishakwambia hapana, na tunabakia na hapana. Si ndivyo
Sabrina?” “Yeah! Kama alivyosema Jack.” Jibu ya Sabrina ikawafanya wote
wacheke. “Mimi naona muda wakuondoka hapa unakaribia. Joy naomba keki, wanangu
wakate, tuwahi ndege ya Singida, jioni hiihii.” “Acha hizo Jack!” “Sabrina
anakosa msimamo kaka. Atashawishiwa na mama, utashangaa tunarudi hapa wakati
hali yake sio yakusafiri safiri! Atazalia kwenye ndege bure!” Jack akakaa chini
kabisa mchangani na watoto wake. Wakaangaliana hao watoto na kucheka kama kawaida
yao wakipiga makofi.
“Sasa
huko Singida mnadaktari mzuri wa kukusaidia siku ya kujifungua?” “Nakusikia
mama. Naomba hayo maswali niulize mimi, wewe muache Sabrina.” Kila mtu
akacheka. “Na huko Singida watoto wanazaliwa kila siku wala Sabrina hatakuwa wa
kwanza. Na kujibu swali lako, anaye daktari mzuri sana. Hata baba anamfahamu na
kumsifia.” “Na wewe Msindai mambo mengine usiwe na haraka kujibu, uwe
unaniuliza mimi kwanza!” Wakazidi kucheka. “Ili anidanganye na kunitia hofu?”
Jack akauliza huku akijenga mchangani na wanae. “Jiachie tu mama. Hiyo baby
shower wala haitakuwepo.” “Wala siachi. Si kirahisi hivyo!” “Wala
hadanganyi huyo Sabrina. Niulize mimi.” Wote wakacheka Jacinta alivyosema
hivyo. Walimjua mama Msindai.
“Naomba
muache Sabrina mama. Wewe zungumza na mimi.” “Ndio usikilize sasa. Kila mtoto anakuja
na baraka zake na furaha yake. Kwa nini huyu asikaribishwe vizuri?” “Basi
tutaandaa kule Singida, tutawakaribisha mje. Lakini sio hapa Dar. Hiyo pesa
tunayotumia kwa tiketi za kwenda nakurudi si tungenunulia hizo diaper?” Jack
akasimama. “Twendeni wanangu tukacheze mbali na mama Msindai.” Wakazidi
kucheka. “Hutaki tena?” “Mimi namjua mama, hatakunywa maji leo mpaka nikubali.”
“Joy ameenda kuleta keki.” “Mtatuita.” Jack akabeba wanae, akamuomba Claire
ambebee michezo ya wanae wakaondoka watu wakicheka.
Keki
ikaletwa, Joy akaandaa meza vizuri wakaitwa wote. Wakawaimbia Jeiline na Keiline
wakiwa wamekaa juu ya meza wanapiga makofi huku wakimwangalia baba yao tu. Jack
akawasaidia kuzima mishumaa. Wakaingiza mikono wala sio kisu. “Ustaarabu wa Singida
huu!” Sabrina akaongea wakicheka. Wote wawili wakawa wanataka kumpa Jack.
Wanashindana. Wakamshika shati na kusimama wakiwa na keki mkononi. Kila mtu
anacheka. “Sasa mpeane zamu jamani. Dad atakulaje hivyo?” Jack akafungua mdomo,
Keiline akawa wakwanza kumuwekea keki baba yake, Jack hakufunga mdomo, Jeiline
naye akamlisha. Ndio Jack akafunga mdomo kila mtu akacheka. “Ndio kazi yao hata
nyumbani. Sasa subirini muone, hawajamaliza.” Wakashangaa wote kwa pamoja
wanambusu kila mmoja shavu lake, halafu wakajipigia makofi. Kila mtu akacheka
na kupiga makofi.
Ungejua
tu hao watoto wanampenda Jack. Akili na mawazo yao yote yako kwa Jack kila
wakati. “Haya mlisheni na mama yenu nyinyi watoto!” Pendo akawageuzia kule
kwenye keki tena. Wakachukua keki na kufanya kama walivyofanya mwanzoni.
Wakampa Jack. Watu wakazidi kucheka. “Mbona hapo kazi washamaliza!a Mimi tena
ndio basi. Waone wanavyocheka kama mazuri.” “Watakupa mama, njaa za nini? Acha
mimi nilishwe.” “Basi utamaliza keki nzima wakati wenzio tunataka na sisi
kula.” Jack alijazwa keki mdomoni. Akawalisha na wao kwa pamoja. Wakacheka na
kupiga tena makofi. Akawashikisha keki na kuwasaidia kumlisha mama yao.
“Umeridhika sasa?” Jack akamuuliza Sabrina. “Mbona mimi mara moja tu!” Watu
wote wakacheka. “Basi hiyo keki mtamaliza wenyewe na watoto wenu.” Jacinta akafanya
wacheke. Wakawa na wakati mzuri hapo wakicheka.
Penzi La Mpaka Kifo.
W |
akati bado
watu wamekusanyika hapo, wakila keki wakati wanasubiria chakula kiletwe, Jack
akaomba watulie kidogo. Kwa kuwa walijua kinachoendelea wote wakawaambia watoto
wao watulie. Pendo akashangaa Jack aliyesema watu watulie, anamwangalia Willy.
Willy akamsogelea Pendo pale alipokuwa amekaa, akapiga goti. Pendo akashangaa
sana, akamwangalia baba yake na kukunja uso. Baba yake akacheka na kurudisha
macho kwa Willy aliyekuwa amepiga goti mbele yake. Akahema mara mbili na ya
tatu. Watu wakcheka. “Daah!” Akasikika Willy na kufanya watu wacheke. Akamvuta
mikono yote Pendo aliyekuwa amekaa na tumbo lake hapo kitini.
“Pendo,
maisha yamenipa nafasi ya pili mbali na wewe. Nikazunguka na kuhangaika, lakini
bado moyo wangu unajikuta nakuchagua wewe tu.” Watu wakapiga makofi kushangilia.
“Na ninajua kabisa, hata nitoke tena, bado nitakuchagua tu wewe, tena na tena.
Narudi kwako si kwa sababu ya watoto, lakini ni kwa ajili yako wewe Pendo.”
Hapo watu wakatulia.
“Kuna
siku nililala kwenye gari nikiwa peke yangu sijui pakwenda. Nimechanganyikiwa,
lakini mtu pekee niliyekuwa nikimfikiria ni wewe. Nikatamani kukupigia
kukwambia ninapopitia na nilipo, lakini nikajua nastahili kila pigo
ninalopitia.” Willy akaendelea. “Nikapata kazi nzuri, nikatamani kumwambia mtu
kuwa ndoto zangu zimetia, lakini nikajikuta ni mpweke zaidi kwa kuwa haukuwepo
kwenye maisha yangu, Pendo. Ninachotaka kusema, nataka kurudi nyumbani, kwako.
Sio kwenye kile chumba ninacholala sasa hivi.” Watu wakacheka. “Nataka kukuoa
tena, uwe mke wangu. Ni sawa?” Chozi la Pendo lilishafika kifuani. Hakutegemea
wala kutarajia. Akamwangalia Sabrina, Sabrina akacheka. “Nakupenda Willy.” Pendo akajibu wote wakashangilia. Willy
akamvalisha pete nzuri sana ya uchumba na kuanza kumbusu.
“Kwani
kila mtu anakuwa bibi harusi mara mbili, dad?” Claire akamuuliza baba yake wote
wakacheka. “Na mimi nataka kuwa bibi harusi mara mbili.” Claire akaongeza
nakufanya wazidi kucheka. “Mjibu sasa mtoto.” Mama Msindai akafanya wazidi
kucheka. “Mwanao anataka harusi mbili kama auntie Pendo.” “Mimi naona kwa sasa
tuombe uwe unasimamia tu. Utakuwa umesimamia mara mbili.” Baba yake akajibu
nakufanya wote wazidi kucheka. “Kwa hiyo utaniombea?” “Nitawaomba baadaye.”
Baba yake akamtuliza. “Kwani tunaoana tena kama zamani?!” Pendo akauliza kwa mshangao, wote wakacheka.
“Kabisa. Nimeuliza taratibu za mahari, naona nimesamehewa mahari.” Wakacheka.
“Lakini nataka kuwapa mkono wa shukurani wazazi wangu kwa kuwa na wewe kipindi
hicho cha miezi mitano nilipokuwa sipo.” Akamfanyia ishara Jack, Jack akaelewa.
Akatoka hapo akiwa amebeba watoto wake.
“Naomba
msubiri kidogo.” Willy akaongea akisugua mikono kama aliyepatwa wasiwasi tena
na anachotaka kufanya. Watu wakacheka wakisubiria. Baada ya muda kidogo, Jack
na wanae wakarudi na muhudumu akiwa amebeba mifuko, wazi ilionekana ni ya nguo.
Wakasogea mpaka pale. Kenton naye alikuwepo. “Hii ni suti ya baba, akipenda
anaweza kuvaa siku ya harusi yetu.” Willy akamkabidhi, watu wakapiga makofi.
“Na hii ni nguo ya mama. Shemeji yangu Nancy amenisaidia kuchagua. Asante sana
mama.” Wakapiga tena makofi yakushangilia. “Jamani mimi nilibarikiwa wakwe
wazuri, najua wote ni mashahidi.” Willy akafanya watu wacheke na kushangilia.
“Sijamaliza. Na hii ni bahasha yao. Najenga. Kwa hiyo hiki ni kidogo tu, kusema
asante.” Akamkabidhi baba yake Pendo. Pendo akiwa haamini. Wakashangilia hapo
na pongezi zikaendelea.
“Sasa
mbona wasimamizi wenu hawapo?” Akauliza
Joy. “Ile ndoa ilikufa, tunaanza upya. Ndoa mpya, na watu wapya.” Akajibu Willy.
“Nataka Sabrina na Jack watusimamie.” Pendo akafanya wacheke. “Sasa na tumbo
hili wewe Pendo!” “Nataka huo upako wako Sabrina. Tumepita kwingi sana mimi na
wewe, nataka uwepo kwenye maisha yangu daima.” Sabrina akasimama na kumkumbatia
Pendo. “Wale wasimamizi wa kwanza waliniumiza sana. Walinikatisha tamaa na
kumwambia Willy anajidhalilisha kuendelea kwenda kutoa mbegu hospitalini, mimi
sina uwezo wa kuzaa.” “Jamani!” Wote wakashangaa. “Kweli tena. Muulizeni Willy.
Lakini Sabrina amekuwa na mimi, akaamsha ari ya kuwa mjamzito. Akaniombea, tena
ndani ya gari nikiwa na mimi naongea lugha yakushindwa kama wengine na akiwepo
daktari pia aliyekuwa akisema sitaweza kuja kushika mimba.” Pendo akaongea kwa
upole.
“Nikamkatisha
tamaa Sabrina. Nikamwambia asijisumbue hata kuomba. Umri umepita na sina mayai.
Sabrina akaniambia yeye ana mwita Mungu anayependa kutembea kwenye magumu
na mtenda miujiza. Akaniambia nitembee kwenye imani yake yeye, atanibeba
tu. Mimi nitulie nishuhudie kile Mungu atafanya. Nakumbuka akaanza kuniombea
kwenye gari mpaka Jack akaja, akatukuta kwenye gari akaungana kuomba na sisi.
Ilikuwa siku ya baby shower yake.” “Unakumbuka na maombi aliyoomba
Sabrina siku ile ukumbini?” Akauliza Jacinta.
“Na
kweli ulipokea kwa kiwango ulichokuwa umejitoa Pendo. Ulijitoa sana kwa
Sabrina.” “Mpaka leo Pendo anajitoa kwangu mimi na Jack pamoja na watoto wetu.
Mungu amekutendea dada yangu na amekurudishia ndoa yako.” Wakacheka, “Na
unakumbuka usemi wako wa Mungu atanitendea jambo zito, mpaka
watakaosikia masikio yatawasha?” Wote wakacheka. “Jamani Mungu
ananitendea, acheni niwape ushuhuda juu ya yale Mungu amenitende.” Watu
wakatulia.
“Huyu
Mungu wa Sabrina, anashangaza watu na madaktari wanaotuhudumia mimi na wanangu.
Vimbe nilizokuwa nazo, muulizeni mama. Zilikuwa Zimeota huko tumboni kama uyoga!
Watoto wakikua, na zenyewe zinakuwa zinamaliza damu mwilini mwangu. Majuzi
nilipandisha pressure, nikajua ndio shetani anataka kumaliza wanangu, kumbe
ndio ilikuwa njia ya mimi kurudi hospitalini kupewa habari njema. Nikidhani
watoto wangu watatoka kabla ya siku sababu ya pressure, waliponifanyia ultrasound
ndio wakakuta zinanywea. Jana tumerudi tena na Willy hospitalini, wakatuthibitishia
kabisa kuwa ni kama zimenywea kabisa, wanangu wananafasi yakukua. Na...” Wakati
Pendo akishuhudia, Jack akashangaa mkewe amepotea pale kimawazo, anaangalia kwa
wasiwasi kwenye kona ingine kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Taratibu
na yeye akageuka. Akashangaa hakuna kitu cha ajabu kinachomfanya mkewe ashangae
huko alipokuwa amepotelea mawazoni ila wateja tu wakawaida. Akazunguka kule
alipokuwa amekaa mkewe, akambusu kichwani na kumsugua na mguu wa Keiline
aliokuwa amewabeba wanasinzia. Sabrina akanyanyua uso kumtizama. Akamuona
amebadilika kabisa usoni. Akajua kuna jambo. “Twende ukanisaidie kuwabadilisha
hawa, niwapakate walale.” Akamnong’oneza kwa sauti ya chini. Ilikuwa njia
yakumtoa pale. Sabrina akamuaga Pendo wakatoka.
Wakaelekea
ndani ili kutafuta sehemu ya kusafisha hao watoto na kuwabadilisha nguo hizo
zilizokuwa zimejaa michanga na keki ili wapate usingizi wa mchana, Jack alikuwa
amewabeba wote wawili. Wamejilaza kila mmoja pembeni ya shino ya baba yao. “Upo
sawa?” “Naona nikuchoka tu.” Jack akasimama mbele yake na kumwangalia kama vile
anayemwambia nipe ukweli. Sabrina akahema kwa nguvu na kugeuka nyuma kama
kuangalia kama kuna mtu anawasikiliza.
“Ni
nini hicho kilichokuogopesha gafla?” “Nina uhakika yule aliyekuwa amekaa pale
akikuangalia sana jinsi unavyocheza na watoto ni Tino.” Kwa sekunde kadhaa Jack
akabaki akimtizama. Sabrina naye akabaki kimya kama hajui aseme nini tena. “Kwa
hiyo!?” Jack akauliza kwa mshangao kidogo. “Sijui Jack! Nahisi sikutegemea
kumuona au sitaki kumuona tena. Na jinsi alivyokuwa akikuangalia ulivyokuwa na
hao watoto, sijapenda.” “Niambie wasiwasi wako ulipo.” Jack akawa ametulia tu. “Itakuaje
akianza kutusumbua? Tino ni mtu wa kesi kesi sana.” Jack akakunja uso.
“Anatusumbuaje? Labda sielewi Brina. Kuwa muwazi zaidi.” Sabrina akavuta pumzi
kwa nguvu na kutafuta jinsi yakueleza.
“Napenda
familia yangu Jack. Napenda amani na utulivu tulionao mimi na wewe pamoja na
watoto wetu. Sitaki ije itokee siku moja tunapoteza hiki tulichonacho sasa hivi.”
“Labda kifo. Lakini hivi wanne tulivyo, tutabakia hivyo labda Mungu atuongezee
mwingine au amchukue mmoja wetu.” Jack akaongea kwa uhakika lakini Sabrina
akabaki na wasiwasi usoni.
“Niangalie
mimi Brina.” Sabrina akamwangalia. “Tino hana chake hapa. Aliua watoto wake
yeye mwenyewe kwa pesa yake. Hawa watoto ni wangu Mungu amenipa, hakuna
atakayeninyang’anya. Asikutishe kwa kesi za kipuuzi alizokuwa akishinda. Hawa
ni wanangu, hakuna mwanasheria wala pesa itakayoweza kutoa hawa watoto mikononi
mwangu.” Ikamgusa sana Sabrina. “Kweli Jack?” “Hujanijua linapofika swala la familia
yangu. Kwanza nashangaa hata kwa nini umuhofie! Huna anachokudai. Alikuacha
akiwa ameridhika mmeua watoto wenu. Hawa ni wangu mimi na wewe. Usitishwe na
uzungu wao, hawa.” Sabrina akacheka na kuwaangalia wanae.
“Kila
siku natamani niamke niwakute wamebadilika angalau wafifie hiyo rangi, tufanane
nao kidogo!” “Mimi nataka waendelee kuwa hivi hivi binti zangu. Wakati Mungu
alipotupa hawa watoto, alitupa wakiwa wamekamilika. Hakufanya kazi nusu.
Aliwaleta kwetu akijua sisi ni weusi, wao weupe. Watakuwa wakijipenda na
kujithamini vile walivyo jaliwa na Mungu. Siwaonei aibu, na wala sina sababu yakujificha
nao. Ni wanangu, na nitawalinda na kila mtu hata iweje.” “Akitaka kuwa anawaona?”
“Huyo Tino!?” “Ndiyo Jack.” Jack akacheka kwa kujiamini. “Hivi wewe Sabrina
nahisi hujanielewa vizuri. Awaone kina nani!? Yeye akiwa kama nani kwanza!?”
Jack akauliza kwa mshangao sana.
“Eti
Brina? Wewe ulishaona wapi mtu anakwenda kwenye familia za watu na kuanza kudai
kuona watoto wao? Yeye si rafiki yangu, wala ndugu yangu mimi wala wewe. Anaona
wanangu wa nini? Haitakaa ikatokea Brina. Kama vile nilivyomkatalia mwanasheria
wake usoni ndivyo itakuwa kwake hivyo hivyo. Hakika mwache aje. Namsubiria kwa
hamu sana.” Jack akaongeza kwa uhakika kabisa.
“Nitataka
aje atuambie sisi kama wazazi wa hawa watoto na aelezee uma hicho kitakachokuwa
kimebadilika ni kipi! Atake kuwaua tena kwa kukubembeleza, mpaka kukusindikiza
hospitalini na kulipia garama zote za mauji yao. Akajiridhisha wamekufa ndipo
akapata amani ya kukuacha kuwa huna mnachodaiana, halafu eti leo huyo muuaji
atake kuwaona! Wewe unanitania Sabrina! Hakuna mahakama nitashindwa kuingia
kulipigania hilo na kuhakikisha namuwekea restrain order, hata
asiwasogelee wanangu. Akitimiza adhima yake ya kuwaua pindi atakapofanikiwa kuwa
nao karibu! Usinitanie kabisa. Hakika mwache aje, ndipo atanitambua.” Sabrina
akajishika tumbo na kulipapasa kama aliyeridhika.
“Na
wewe wala usimuogope. Hata ukikutana naye uso kwa uso, tembea kama jasiri. Hakudai
na wala huna watoto wake. Alilipa pesa nyingi sana muue watoto wake. Na
walishakufa, hawa watoto ni wetu mimi na wewe, na kaka yao anakuja. Na hatutaki
baby shower.” Sabrina akacheka sana. “Naomba uwe na msimamo katika hilo
Brina bwana! Acha kuwa njia panda.” “Mimi nataka.” Jack akatoa macho. “Huyu
mtoto atazaliwa tu bwana, Jack! Acha kuwa na wasiwasi na wewe.” “Hapana
Sabrina. Unakumbuka shida tuliyopata ulipojifungua hawa? Walikugeuka.” “Sasa
huyu Msindai mwenyewe, watanigeuka nini na wewe?” Jack akashangaa sana.
“Wewe
huoni kama wanafanya upendeleo!?” “Ndiyo, wanafanya upendeleo, lakini si wote
ni wetu! Acha mama amfurahie mjukuu wake. Wewe unakumbuka alipopitia Willy na
mama yake?” Jack akanyamaza. “Hawa wazee wanapenda wajukuu zao Jack. Maamuzi na
maisha mabaya niliyoishi mimi zamani, yasimpunje na kumfanya huyu mwanangu
akalipa garama yake.” Akajishika tena tumbo.
“Acha
bibi yake amfanyie kile atakacho. Hayo mengine sisi tutajua jinsi ya
kuyasawazisha tukiwa na watoto wetu nyumbani. Lakini usimzue kwa kuwa anachokifanya
si kibaya. Ukubali ukatae, huyu ndiye mjukuu wake.” “Sasa hapo unataka kuharibu
Brina.” “Ni ukweli ambao unataka kuupinga kwa nguvu nyingi bila sababu! Mwache
dume langu likaribishwe kwa furaha zote. Kwanza wewe umeona wabibi wangapi wanahangaika
na wajukuu zao kwa kiasi hiki? Hii ni baraka ya mwanangu, Mungu ameruhusu kwa
makusudi kwa ajili yake yeye Briyan, mwache mwanangu apokee.” Sabrina akaongea
bila wasiwasi.
“Hivi
unajua ule mfuko aliokuja nao asubuhi pale nyumbani umejaa nguo zake huyu kaka
yao?” “Haiwezekani Sabrina!” Sabrina akacheka. “Kabisa. Ila akaleta na vibanio
vya nywele vya hawa wadada. Sasa kuna hasara gani, wakati na huyu ni wetu?”
“Sikujua! Mimi nilijua ameleta zawadi za kina Jeiline!” Jack akashangaa sana.
“Hata mimi. Lakini akanifuata chumbani na kuniambia kabisa, anataka nguo za
kwanza atakazovaa Briyan ziwe zakutoka kwake.” “Haiwezekani Brina!” “Kabisa.
Lakini wewe jiulize Jack, ubaya upo wapi!? Angekususia kabisa kwa kuwapokea
hawa na kujitenga moja kwa moja! Ungefanya nini? Ungepoteza mahusiano mazuri
sana uliyonayo na mama yako. Na ninakujua Jack, ingekutesa sana. Sasa Mungu
amekurudishia mama, tena anataka na mjukuu niliyezaa mimi! Tatizo liko wapi?”
Jack akanyamaza akimtafakari mama yake.
“Mwenzio
nikacheka na kufurahia. Alete tu. Briyan ni mwanangu kama Jeiline na Keiline. Na
yeye ni mama yako. Huwezi kumbadilisha atakachojisikia kwao, na maadamu sasa
hivi anawaita wajukuu, unataka nini tena! Mambo mengine yaache tu kuwe na
amani. Hautakaa ukapata mama mwingine. Naomba tumchukulie hivyo hivyo
atakavyotujia.” “Ila sifurahii Brina. Sipendi.” “Mimi sijui ni kwa nini Jack!
Hata hainikeri hata kidogo! Nina amani, sana tu. Sijui ni kwa kuwa naona
wameshapata upendo mkubwa sana kutoka kwako!” Jack akamwangalia.
“Kweli
Jack. Waangalie hapo walipo.” Jack akawachungulia akakuta wametulia kimya.
“Wanasinzia.” “Sasa ndio nakuuliza Jack, unavyowaona hao watoto, wanahitaji
upendo mwingine zaidi ya huo?” Jack akacheka. “Kwanza wenyewe hawataki!” Wote
wakacheka. “Akili na mawazo yao yapo kwa mtu mmoja tu, wewe. Basi. Sasa leo
unataka iweje? Mimi mwenyewe nadhani ningekuwa nao peke yangu nisingeweza
kuwapenda hivyo.” Jack akajisikia vizuri
sana kuona Sabrina anaona na kuthamini mapenzi aliyonayo kwa hao watoto. “Kama
wewe umeridhia sawa Brina. Mimi sikutaka upendeleo.” “Wewe mwache mwanangu apate
upendeleo. Ndilo aliloandikiwa na Mungu.” Jack akacheka huku akifikiria.
Wakaelekea sehemu ya kubadilishia nguo watu wanaenda kuogelea. Nje tu.
“Tukiwaogesha
watachangamka, heri tuwafute tu.” Jack akacheka. “Si ndio vizuri wacheze! Leo
siku yao bwana! Waache.” “Wanazagaa sana bwana, watu wanashindwa kufanya mambo
yao inakuwa ni wao tu!” “Hata! Si kosa la wanangu. Kama wao wanavutiwa na uzuri
wao ni tatizo lao, nitashindwa kuwasaidia.” “Basi na wewe uwafundishe kukubali
watu Jack. Watoto gani hawataki kuguswa.” “Hawawajui je! Unataka wawakubali ili
iweje? Wawasalimie hivyohivyo kwa mbali. Wawaache wanangu.” Wakasaidiana
kuwasafisha na kuwabadili. Wakachangamka kweli na kuanza kupiga makofi. “Si
nilikwambia wewe! Ona walivyotoa macho.” Jack akawa anacheka nao bila wasiwasi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Umelichulia
vipi swala la nyumba aliyokwambia shem? Hiyo bei ni rahisi sana Jack. Tunaweza
tusipate dili nzuri kama hilo tena.” “Kwa hiyo upo tayari tukope kwa ajili
hiyo?” “Sasa hivi hatuna hiyo pesa, ila huwezi kujua kesho yetu mpenzi wangu.
Kwanza unaweza kujikuta hiyo nyumba ikaja kujilipa yenyewe. Tuichukue, kama
kuna kukarabati, tukarabati na kuikodisha. Hata kama sasa hivi pesa inasumbua,
lakini huwezi kujua kesho! Tukiwa na nyumba kule Singida na Dar, sio jambo
baya. Na uzuri unamkopa kaka yako, hakuna riba, hatuna chakupoteza.” Jack
akashawishika. “Basi kabla yakuondoka, nitamwambia atusindikize tukaone nyumba
yenyewe tusije uziwa mbuzi kwenye gunia.” Hilo wakakubaliana bila shida.
“Lakini
ujue mama atakuomba uje ujifungulie nyumbani.” Sabrina akatulia kidogo. “Ndivyo
alivyokwambia?” Sabrina akauliza. “Aliniomba kama mwezi umepita, nikamkatalia.
Akaja kukumbushia tena na akaniambia atazungumza na wewe.” Hapo Sabrina akapoa.
“Huna sababu ya kukubali.” “Nafikiria tu.” “Unafikiria nini?” “Nilitaka mama
awepo kunisaidia. Ukumbuke nitakuwa na watoto watatu Jack! Halafu ukweni! Naona
kama sitakuwa na uhuru.” “Tunaweza tusikae sana. Hata juma moja tu.” Sabrina
akajua na yeye anataka.
“Kwa
hiyo na wewe ndivyo unavyotamani iwe?” “Sio lazima.” Akajitoa Jack kama kuepuka
lawama. “Lakini unatamani iwe hivyo?” Sabrina akambana. “Sio mbaya. Lakini
unajua mimi nitakuwa na wewe Brina. Usiogope.” Sabrina akacheka moyoni. Akambusu
mdomoni. “Wakati wote upo na mimi Jack. Na ndio maana unaniona naishi bila
hofu. Umekuwa kimbilio langu tokea chuo. Sasa kama hili ndilo unataka liwe kwa
huyu au bibi yake anataka iwe hivyo, sawa. Mimi sina shida na wala sina
kinyongo. Watoto wote ni wangu. Na hata hao uliowapakata hapo wakikuchekea na
kukulamba kama pipi ni wangu tu!” Jack akacheka na kuwabusu kichwani. “Bwana
mimi napendwa!” Jack akajisifia. Sabrina akacheka huku akiwatizama wanae. “Basi
hata hao yupo atakayewapenda tofauti tofauti. Ujiandae na kwenda na upepo.” Wakasimama
huku wakirukaruka hapo miguuni kwa baba yao.
“Sasa
tusikae hapa wakati watu wapo kule Jack. Twende.” Wakaanza kukusanya vitu vya
watoto pale. “Umesikia tunatakiwa kusimamia harusi?” “Hata sijui itakuaje na
hili tumbo! Kwanza tujue ni lini ndipo tujipange.” “Willy anaonekana anataka
iwe mapema kabla mkewe hajajifungua.” “Sio mkewe bwana!” “Aaah! Vinachanganya
hata huelewi! Juzi alikuwa mkewe, jana wakaachana, leo anamchumbia, sielewi.”
Sabrina akacheka huku akiendelea kukusanya vitu vya watoto, Jack amebeba hao
watoto akimfuata kwa macho akimtizama anachokifanya.
Palipo na Amani, Na
Uharibifu Kunyemelea!
Wanasimama
baada ya kukusanya kila kitu, na Tino naye akawasimamia mbele yao. Sabrina
akaduwaa, kwa muonekano ule na vile alivyo Tino, Jack akajua ni yeye tu.
“Tukusaidie nini?” Jack akamuuliza akimtizama machoni akiwa amebeba watoto
wake. “Naitwa Tino.” “Kwa hiyo!?” Jack
akamuuliza kama anayemshangaa. “Nilitaka kusalimia tu.” “Ukimwangalia Sabrina
hivyo alivyo, anaonekana anataka salamu yako?” Tino akamtizama Sabrina. “Habari
za siku Sabrina?” Jack akacheka. “Achana na mke wangu, wewe. Twende Sabrina.”
Wakasogea mbele kidogo wakiwa wanaondoka, Tino akaanza tena.
“Mbona
hasira wakati ni salamu tu.” Jack akageuka na kucheka. “Hujaniona nikiwa na
hasira, na ninauhakika hutataka kuniona. Narudia tena, achana na mke wangu. Na
kama unalo jambo jingine lizingumze sasa hivi, au..” “Au nini? Au nini Jack? Utanifanya
nini?” Tino akauliza kama anayemwambia sikuogopi. Jack akacheka na kurudi
nyuma. Sabrina akamshika. “Utajua utakapofanya nilichokuonya. KAA MBALI NA MKE
WANGU.” Jack akaweka msisitizo huku akimtizama machoni.
Tino
akacheka. “Twende Jack. Twende. Hana hata hadhi ya kuzungumza naye huyo. Atakupotezea
muda tu na kukuharibia siku.” “Mbona wewe sijawahi kukuharibia siku ila
kukuachia faraja mpaka sasa mnafurahia matunda yangu!” Tino akaongea kwa kejeli
akiwacheka wote wawili huku akiwatizama. “Si nilikwambia Jack? Twende. Hana
jema litakalomtoka kinywani mwake isipokuwa maovu yaliyojaza moyo wake. Twende
mpenzi wangu.” Sabrina akamshika Jack, Tino akacheka huku akiwatizama. “Twende
Jack.” Jack akaona ni heri aondoke tu kama Sabrina alivyomshauri lakini
alionekana ameshakasirika sana na kama anayezuia maneno.
Lakini
wakati wanaondoka wakamsikia tena Tino akisema. “Mtasikia hivi karibuni kutoka
kwa mwanasheria wangu.” Sabrina akashituka sana karibu adondokwe na vitu
alivyoshika mkononi. Akajua maji
yameshamwagika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Katikati Ya Ndoa Tulivu, Kwenye Amani, Tino Amerudi.
Nini Kitaendelea? Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment