Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 39. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 39.

Wakiwa njiani mama yake alipomuona anaendelea kutetemeka kwa hofu akajaribu kumtuliza tena. “Funga macho ukimtafakari Mungu aliyekufikisha hapa, Pendo. Usikumbuke zile namba za presha tulizozipata baada ya kukupima. Kumbuka ukuu wa Mungu tu. Utajisikia unatulia. Funga macho kabisa.” Pendo akatulia kabisa akafunga na macho kama alivyoshauriwa na mama yake, wakielekea hospitali ya karibu. Walipofika akamueleza daktari matatizo yake, akapimwa usiku huo, wakaona wampumzishe kabisa mpaka papambazuke, pressure ishuke ndipo aende kwa daktari aliyekuwa akimuhudumia. Pendo akapewa kitanda, akapewa dawa, akalala.

Asubuhi akashituka kutoka usingizini wakati nesi akimpima tena pressure. Akakuta ujumbe kutoka kwa Willy akiuliza kama waliamka salama. ‘Tupo salama. Asante.’ Akajibu. ‘Basi nitawaona baadaye. Nitawahi kutoka kazini ili kuhamisha mizigo.’ ‘Sawa.’ Pendo akajibu na kurudi kulala.

Jioni.

W

illy anafika nyumbani Salasala jioni hiyo, akaanza kuingiza vitu vyake kwenye chumba alichokuwa akikitumia zamani kama ofisi yake. Sifa alijua anajua alipo Pendo akamuacha akiendelea na shuguli zake kuingiza vitu. Alishamwambia amefurahi amerudi nyumbani. “Tulikuwa wapweke kweli!” Willy akacheka. Akaingiza kila kitu ndipo akaenda chumbani kwa Pendo. Akashangaa Pendo hayupo chumbani. Akatoka kumfuata Sifa jikoni. “Dada yako yuko wapi?” “Tokea walivyompeleka hospitalini, hawajarudi mpaka sasa hivi.” Willy akashituka sana.

“Pendo ni mgonjwa!?” “Mimi najua unajua kaka! Usiku bibi na babu walikuja kugonga, nikawafungulia. Wakaniambia wamekuja kwa sababu dada aliwapigia kuwa ni mgonjwa. Hata mimi nilikuwa nimelala, sikuwa najua kama ameanza kuumwa huko chumbani. Nikaongozana nao chumbani kwa dada, babu akampima presha, wakakuta ipo juu. Tukasaidiana na bibi kumvalisha, wakampeleka hospitalini. Ndio hawajarudi mpaka sasa hivi.” Willy akashangaa sana. Aliwasiliana na Pendo!

Willy kwa mama yake Mkwe.

Hapo hapo Willy akampigia simu Pendo aliyekuwa akichat naye asubuhi asimwambie kama yupo hopitalini. Ikaita bila kupokelewa. Ndipo akajikaza kumpigia mama yake. Uzuri bado alikuwa na namba zao. Ikaita mara mbili tu akapokea. “Shikamoo mama.” “Marahaba baba, pole na kazi.” “Asante, lakini niliwasiliana na Pendo,hakuniambia kama yupo hospitalini!” Akasikika akilalamika. “Wamempumzisha. Presha ilikuwa juu. Lakini naona jioni hii yupo sawa. Tulimuhamisha kule tulipokuwa tumempeleka hospitali ya mwanzoni, tukamleta kwa daktari ambaye alikuwa akimuhudumia tokea mwanzo. Naona amempumzisha.” Willy akashangaa sana ni kwa nini Pendo hakumwambia.

“Sikujua mama! Mimi nilimuulizia hali yao, akaniambia wanaendelea vizuri. Kwa hiyo nikawa...” “Subiri kidogo Willy.” Kimya. Akasikia mlango unafunguliwa nakufungwa taratibu. “Willy?” Akamsikia akimuita, akaitika. “Nipo mama.” “Nilikuwa natoka nje, amelala. Daktari ameshauri alale kabisa, kupumzika. Sikutaka tumuamshe.” “Samahani mama, sikukusudia kusumbua.” “Hata kidogo, lakini Willy.” Willy alishapanda kwenye gari, kuelekea hospitalini alipolazwa Pendo. “Nipo mama. Na nipo njiani nakuja huko. Kuna kitu chochote labda kinahitajika?” “Hapana. Kama ni chakula, daktari ameshauri ale cha hapahapa hospitalini kwanza ambacho wataangalia chumvi, na maji tu. Asante.” Mama mkwe wake akashukuru.

“Nakusikiliza mama.” “Nilimuuliza Pendo kama amekwambia kama amelazwa, alichonijibu ni kama maadamu watoto wapo salama, hutakuwa na wasiwasi.” “Mama!” Willy akashangaa kwa kuumia sana. “Ndivyo alivyoniambia. Na kwa kuwa wamemfungia mashine tumboni kuangalia mapigo ya watoto na wamemfanyia hata Ultrasound wameona watoto wapo salama kabisa. Tena daktari wake ni kama amemwambia vile vimbe zinanywea kitu ambacho si chakawaida, hajawahi ona! Kwetu ni muujiza.” Kimya. Willy akifikiria. “Hizo ni habari njema Willy. Inamaana hizo vimbe zikinywea, zinawapa watoto nafasi ya kukua.” “Naona kila mtu anajua nimerudi kwa Pendo sababu ya watoto!” “Si ndicho kilichokuondoa?” Huyo mama akauliza bila kuzunguka mpaka Willy akapoa.

“Wewe uliondoka sababu ya watoto. Mwenzio hakuwa akishika mimba. Leo tunakuona umerudi kwenye maisha yake akiwa mjamzito, sasa hata kama ungekuwa wewe, ungefikiri nini Willy mwanangu?” Kimya. “Nafikiri ndio maana hata yeye Pendo anaona akupe habari za watoto tu ambao ndio anajua unajali zaidi, sio yeye.” “Sio sawa mama na si kweli.” “Unakataa nini Willy mwanangu? Labda sijaelewa kwamba sasa hivi tunazungumzia nini!” “Kweli mama umesahau mapenzi yangu kwa Pendo!?” “Siwezi kusahau hata kidogo na ndio maana tulielewa ni kwa nini uliweza kumuacha mwanamke unayempenda na kwenda kuzaa nje. Nafikiri hilo uliliweka wazi na lilieleweka. Au kuna kitu kingine hapa kilijificha ambacho sisi tumeshindwa kuelewa?” Mama yake Pendo akauliza taratibu tu.

“Hapana mama. Ila najua nimemuumiza sana Pendo, kwa kitendo cha kama kumpa mwanamke mwingine mimba tukiwa kwenye ndoa.” “Kwani wewe ndio ungekuwa wa kwanza, Willy? Watu wanakuwa na ndoa zao, wanakosea. Wanaomba msamaha kama linakuwa ni kosa, uponyaji unachukua muda kwenye ndoa, lakini penye nia ya ndoa pakiwepo, ndoa zinapona, na kuendelea. Lakini wewe ulikusudia kutupilia mbali kila kitu na kwenda kuanzisha familia yako Willy. Ulipima kwenye mizani ukaona mapenzi peke yake hayatakutosha maishani, unahitaji familia na ndio maana ukaondoka kwa haraka sana. Hukutaka hata kupoteza muda, ukasaini talaka na kwenda kuanza upya. Halafu hukusikika hata kwa salamu, au kupotea njia kumwangalia mwanamke uliyekuwa naye kwa miaka yote hiyo, kujua anaendeleaje! Unakuja kutokea akiwa mjamzito. Unafikiri habari utakazokuwa ukipewa ni zipi kama si hizo?” Pendo hakuwa na tofauti kuzungumza kama mama yake, ila Pendo aliongezeka na deko, mtoto wa mwisho.

“Naomba nikwambie ukweli mama bila kukuficha na kwa heshima zote.” “Nakusikiliza.” Akajibu kwa kutulia mama Kenton. “Narudi kwa Pendo si kwa kuwa ana watoto wangu. Ni wangu aidha nipo na mama yao au la. Na wala wao hawatakuwa watoto wa kwanza kuwa na wazazi waliotengana.” Huo ukawa ukweli. Mama Kenton kimya. “Kushindwa kwa Zelda kunibebea mimi mtoto, sio mwanamke wa mwisho hapa duniani. Naamini mama yangu utakubaliana na mimi wapo wanawake wengi tu wangekubali niwaoe na wanizalie watoto zaidi ya wawili ambao nawatarajia kwa Pendo. Zelda aliangalia picha kubwa kwa haraka, akatumia akili. Alijua mama angekufa, baba ana mali nyingi kunizidi mimi ambaye kila pesa itakayoingia sasa hivi ipo kwenye kujijenga. Mzee ameshamaliza kujijenga, pesa inayoingia sasa hivi ni matumizi tu. Zelda ameliona hilo na kwa kuwa wote tumeshakuwa wakubwa, njia pekee yakuipata pesa yote ya baba na mali ni kumzalia yeye mtoto ambaye hata baba akifa leo, anajua mali zote atamwachia yeye na huyo mtoto.” Willy akaamua kuzungumza.

“Ninachotaka kusema, nipo kwenye maisha ya Pendo, au nimerudi kwenye maisha ya Pendo kwa sababu ndiye mwanamke ninayempenda. Nampenda Pendo na ni my SOULMATE. Hakuna idadi ya watoto itakayochukua nafasi ya Pendo maishani mwangu. Hata azae hao halafu atake tena wengine, au asizae hata hao alionao sasahivi, Pendo ni my Soulmate. Nampenda Pendo na ndio maana nimerudi na nitabaki hata kama hakuna anayefurahia. Nitabaki na Pendo na nitafanya kila niwezalo aamini nimerudi kwa ajili yake yeye sio hao watoto wanao muendesha kama gari bovu!” Akaanza kukasirika.

“Nyinyi wote mnanifanya hata nichukie watoto niliowasubiri na kuwahangaikia kwa muda wote huo!” “Wewe Willy!” “Kweli mama. Mnaniharibia mahusiano yangu na Pendo. Kila kitu ninachofanya hamumuoni mke wangu mnamuo...” “Aliyekuwa mke wako.” Mama K, akamkatisha kwa kumsahihisha. “Nitamuoa tena Pendo. Na nitamuoa hivi karibuni. Najua Pendo bado ananipenda. Mnambana mpaka nakosa raha! Swala limekuwa watoto tu mchana na usiku na si Pendo mwenyewe! Kila kitu ni watoto tu, mnajisahau. Mnafanya kila kitu kunikomoa na kusahau mimi ndiye baba yao! Mnahangaika na vitu vya watoto wangu na kunipuuza mimi mwenyewe!” “Si haukuwepo! Ulitaka maisha yasiendelee kwa kuwa wewe umeondoka?”  Akashangaa mama K. “Basi nimerudi. Na nimerudi sababu ya Pendo. Na Ninampenda.” Willy akaongea kwa ukali, akashangaa kimya. Akakumbuka anaongea na mama mkwe, kipenzi cha Kenton, mtoto wake mkorofi haswa. Akapoa.

Alishafika hospitalini. Mida hiyo ya jioni foleni ya kurudi mjini haikuwa kubwa. Akaegesha gari. “Samahani mama yangu.” “Hapana. Umeongea moyo wako. Ila sijui sasa unataka  sisi tufanyaje, Willy!? Uliondoka, ndio umerudi!” “Basi naomba mtambue kama nimerudi mama yangu. Hilo tu.” “Hakuna anayejua haya uliyoniambia sasa hivi. Na nina uhakika hata Pendo mwenyewe hajui hayo unayosema, Willy.” “Kwa maneno naona itakuwa ngumu kuamini na kuelewa kwa haraka. Naombeni nafasi kuyathibitisha hayo.” “Sawa Willy, mwanangu.” Mama huyo hakuwa na mambo mengi. Akakubali na kuagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Willy akaingia hapo chumbani alipokuwa amelazwa Pendo na mama mwingine kitanda cha pembeni. Akamkuta mama K peke yake kwa upande wa Pendo. “Mbona mashine nyingi wakati umeniambia anaendelea vizuri, mama!?” “Hizo mashine zisikuogopeshe. Wanafuatilia mapigo ya moyo ya watoto na pressure yake huyo wanataka irudi kawaida kabisa ndipo wamruhusu, ndio maana unaona yupo usingizini saa hizi na wamemuwekea catheter ili asiamkeamke kwenda chooni. Tena hiyo ilikuwa kabla ya Ultrasound na daktari wake kuona hizo vimbe zinanywea. Hamna aliye hatarini hapo.” Mama K akamtuliza. Willy akabaki amesimama pale akimtizama Pendo.

“Utakuwa hapa kwa muda gani?” Willy akamgeukia mama K aliyekuwa akinong’ona. “Nataka nirudi nyumbani angalau nikaoge na kubadili, ndipo nirudi. Tulikuwa hapa na kina Nancy muda wote nikapitiwa na wazo lakurudi nyumbani wakati wao wapo hapa.” Ndipo Willy akajua kila mtu kwenye familia alikuwepo hapo kasoro yeye ndio hakuambiwa, kwa kuwa kinachomuhusu ni watoto wake, na ameshaambiwa watoto wake wapo salama, wakaona wamuache wasimtaarifu. Akaumia kuona hajataarifiwa habari za kuugua kwa Pendo. “Sasa nataka kujua kama wewe utakuwepo. Na sitakawia.” “Nitakuwepo mama. Nenda tu hata ukapumzike kidogo. Nitakuwepo.” Willy akajibu akisikika kuumia. “Sawa. Asante na ikitokea unapatwa na dharula kabla sijarudi, tafadhali usiondoke bila kunitaarifu ili nimtume hata Kenton ambaye yupo karibu aje akae naye mpaka nirudi.” “Nitakuwepo mama. Hakuna dharula nyingine kwa sasa isipokuwa hii ya Pendo kuwepo hapa hospitalini.” “Basi nitawaona baadaye.” Mama K, akaondoka.

Willy na Pendo Hospitalini.

W

illy akasogeza kiti mpaka karibu na kitanda alicholazwa Pendo, akakaa. Alikaa hapo akiwa ameinama amepotelea mawazoni kama lisaa, aliponyanyua uso akamkuta Pendo ndio anaamka. “Watoto wote wapo sawa Willy. Usiwe na wasiwasi. Hiyo unayoona na kusikia hapo.” Akanyooshea kidole mashine nyingine iliyokuwa imesimama pembeni na kufungwa kuzunguka tumbo lake. “Ni mapigo yao ya moyo. Huo mlio si unausikia?” Willy kimya akimsikiliza. “Huo ni mlio mzuri, inamaana wapo sawa.” Pendo akaendelea kwa sauti ya chini kama asiyetaka kumsumbua mgonjwa wa kitanda cha pembeni. Willy akabaki kimya akimsikiliza wala asitazame hizo mashine. “Na Mungu amenitendea muujiza mwingine, vimbe zimeanza kupungua, zinanywea, kwa hiyo nafasi ya kukua kwao inaongezeka. Hawapo hatarini.” Pendo akaongeza taratibu kama kutaka kumtoa yeye wasiwasi.

Willy akasimama na kumsogelea. “Naomba nisaidie maji ya kunywa. Baba na wengine wako wapi?” “Nilimkuta mama tu. Na amekwenda nyumbani kuoga, amesema atarudi kuja kulala na wewe.” Willy akamsaidia kumpa maji. “Asante.” Akaona anavuta simu pembeni ya kitanda, akapiga. “Baba!” Akamsikia anasikiliza. “Najisikia vizuri, ndio nimeamka.” Akamuona akisikiliza tena kwa muda kidogo kama akielezwa kitu, akamuona anajishika tumbo na kujifuta machozi. “Asante baba. Usiku mwema.” Akakata na kujifuta tena machozi.

Willy akatulia kidogo kama kumpa nafasi atulie kisha akamuuliza. “Kwa nini hukuniambia kama umelazwa?”  Akauliza taratibu tu. “Nilipoona hakuna hatari ya watoto, nikaona nisikusumbue. Nikuache ufanye kazi tu.” Pendo akajibu taratibu tu. “Halafu baba ameniambia mama atakuwa hapa kama kwenye saa nne, Willy. Ungeenda kupumzika. Naamini kila kitu kitaendelea kuwa sawa. Nikisikia taarifa nyingine za watoto, nitakutaarifu.” Kimya Willy akimtizama. “Kapumzike Willy, najua umechoka na kazi za siku nzima. Kila kitu kitakuwa sawa.” Pendo akasisitiza.

“Sipo hapa kwa ajili ya watoto tu Pendo!” Pendo akamwangalia kama asiyemsadiki. “Najua unaweza usiniamini, lakini sipo hapa eti kwa kuwa nina wasiwasi sana kuwa kuna kitu kibaya kitatokea kwa watoto! Na hata kama kikitokea, uwepo wangu hapa hautasaidia chochote kile. Kwa sasa sina uwezo wa kufanya chochote kwa hao watoto, isipokuwa wewe.” “Lakini sivyo ulivyosema jana wakati tunaagana, Willy! Jana usiku ulisema unataka kurudi nyumbani si kwa ajili yangu ni kwa ajili ya watoto.” Willy akashituka sana.

“Pendo! Ni wakati gani niliongea hivyo!? Hata usingizini nikiwa nimelala, nina uhakika nitakuwa sijaropoka kwa kuwa silo lililojaza moyo wangu! Sina sababu yakutokuwa hapa isipokuwa niliona umeniongelesha vizuri na kunipokea siku ya kwanza kabisa kuonana tokea tuachane. Kama ungenikatalia kuja nyumbani siku ile wala nisingekusumbua! Kwanza swala la watoto kama ni wangu au sio wangu lilikuja kujijibu baadaye kadiri nilipokuwa na wewe.” “Unawezaje kufikiria hata kama watoto sio wako!?” “Subiri kwanza Pendo naomba usilie unisikilize. Tafadhali. Nataka tuzungumze na si kukuudhi.” Akamfuta machozi.

“Unakumbuka ni mara ngapi wamechukua mbegu zangu na kukupandikizia kwa bomba?” Willy akauliza taratibu tu. Pendo kimya. “Unakumbuka mazungumzo yetu siku moja na daktari ya kuwa wapo kina mama ambao hawajaolewa wananunua hiyo huduma na wanapandikiziwa watoto, wanazaa?” Kimya Pendo akimsikiliza. “Sasa nikwambie ukweli tu, na Mungu wangu nishahidi. Nilipokuona mara ya kwanza kabisa. Nikajua baada ya kuachana na mimi ulirudi kwa yule daktari, akupandikiziwa watoto kwa kutumia mbegu nyingine walizo na uhakika nazo kuwa zina nguvu. Nikajisikia vibaya baada ya kuona na kwako nilishindwa. Lakini nikaona upo sawa, na unazungumza tu na mimi. Hukuweka dharau yeyote ile kwangu, ndio maana nikapata ujasiri wakurudi nyumbani, wala nisijue kama watoto ni wangu, ila tu sikutaka kukupoteza na wewe, kwa kuwa nimepoteza ndugu wote na marafiki pia.” Willy akaendelea taratibu tu.

Akamshika mkono kwa upendo. “Nimerudi kwako si sababu ya watoto, ni kwa ajili yako Pendo. Nahesabu watoto ni kama nyongeza Mungu anataka kunipa. Sisemi wewe ni muongo, lakini kwa hakika sikumbuki kukwambia narudi nyumbani sababu ya watoto, Pendo!” “Basi labda nilielewa vibaya pale uliposema unataka tu kurudi nyumbani, na si kuwa unataka kunioa.” “Na pia sikusema hivyo Pendo. Nilisema hivi, naomba tu kurudi nyumbani, sio kwamba nakuomba kukuoa. Tena nilisema hivyo baada yakuona unasita kuniruhusu kurudi nyumbani na ndio maana nilikwambia naweza hata kutumia ile iliyokuwa ofisi yangu ili niwepo tu pale karibu na wewe niweze kukusaidia. Na hayo yote ni kwa sababu kama hii. Yakuona watu wote wanaweza kuacha shuguli zao na kuja hapa, mimi nakuwa sina taarifa!” Pendo akanyamaza.

“Watu wote wakaribu yako, ambao hawaishi pale nyumbani kama mimi, walipata taarifa kama wewe ni mgonjwa, isipokuwa mimi, Pendo. Mimi sikuambiwa, nakuja kuambiwa na Sifa ambaye na yeye alidhani najua! Ndio maana nikaomba kuwepo pale karibu ili mengine ambayo unashindwa kuniambia sababu ya kutokuniamini, niyaone mwenyewe kwa macho.” “Si kwamba sikuamini Willy.” “Ni hivyo tu Pendo. Nimepoteza uaminifu kwako, nimepoteza sifa nyingi sana. Hilo najua, na ninajua itachukua muda kuja kuniamini tena. Lakini nakwambia na kukuhakikishia nipo hapa kukusubiri wewe wala si watoto. Nitasubiri mpaka uamini nimerudi kwenye maisha yako, tuishi kama zamani ambapo tulikuwa tukiambiana mambo yetu wenyewe na kuyatatua. Mpaka yakiwa mazito, ndipo ulipokuwa ukiwaambia wazazi. Lakini mara zote mimi ndio nilikuwa kimbilio lako kwanza ndipo wazazi. Najua itachukua muda kujengeka kama ilivyokuwa zamani tokea chuoni. Naamini kuna hatua nilifika, ukajenga uaminifu kwangu, simu za nyumbani zikapungua, zikawa zinaishia kwangu. Na nafikiri imekuwa hivyo kwa muda mrefu sana isipokuwa hii miezi mitano nilipokugeuka.” Pendo kimya.

“Lakini nimerudi Pendo. Na sina ninapokwenda. Watoto wawepo au wasiwepo. Nimerudi nyumbani ambako kuna utulivu. Sijashindwa kabisa nje. Najua na wewe unajua. Nimeshindwa kwa Zelda, lakini sio kwamba nitakosa mwanamke kabisa! Hapana. Kurudi kwangu nyumbani ni kwa ajili yako ili angalau uone nimetulia na ninamaanisha. Ukinifukuza leo, ukaniambia hutaki kuniona tena, nitaondoka na kukuacha kwa amani kabisa nikijua niliharibu mimi mwenyewe, nitawajibika na matokeo. Akaunti ya watoto ninayo, nilipiga picha kile kikaratazi cha benki ulichonipa siku ile nikusaidie kuweka pesa. Nitaendelea kuwatunza wanangu na sitawasumbua mpaka wewe uone upo tayari kuwakutanisha na mimi. Lakini sitawatelekeza mpaka wafike umri wakujitegemea, kama Mungu atanipa uhai. Na sitawasumbua hata kidogo. Nitaondoka Pendo, na kukuacha uwe na amani.” Pendo akapoa kabisa.

Willy hakuwa akidanganya. Aliongea ukweli. Willy kwa muonekano analipa vizuri tu. Ana kazi nzuri na pesa ipo. Zelda alikimbia kwa kuwa alidhani amefilisiwa na mkewe wakati wakiachana, akadhania Willy ni mlala hoi, hana hata pakuweka kichwa chake kumbe Willy anajenga mjengo wa maana. Pendo akakumbuka picha alizokuwa akionyeshwa na Willy usiku uliopita. Kwa hiyo akimuachia tu hapo, atakachokuja kusikia ni kuoa kwa Willy. Akawa mpole. Na kwa kuwa Willy naye alimjua vizuri sana Pendo, akajua kwa hakika mazungumzo ya usiku uliopita ndiyo yamempandisha presha mpaka kulazwa hapo.

“Sijui umenielewa Pendo? Tafadhali uliza popote na zungumza kile kilichopo moyoni ili tuwe ukurasa mmoja. Nilishakuumiza kwa kukusaliti mwanzo, sitaki kuona nikiendelea kukumiza. Hustahili. Wewe ni mtu mzuri, umejawa upendo na mema. Sitaki mimi ndio niwe chanzo cha matatizo kwako. Kama ukiona nakuwa tatizo na si msaada, nipo tayari kukupa nafasi mpaka utakapokuwa tayari.” “Natamani ubaki Willy. Usiondoke.” Pendo akaongea kwa upendo bila hata kujivunga. Willy akainama na kuanza kumbusu midomoni. Akambusu tena na tena. Akambusu tena. Kisha akaendelea kumbusu akiwa amelala hapohapo. “Nakupenda Willy. Nakupenda sana mpenzi wangu.” Willy akamuhurumia na kuzidi kuhukumiwa.

“Najua unajua kama nakupenda Pendo. Nilikosa na mama aliniwekea pressure, nilikuwa siwezi hata kuhema. Simu na jumbe za kifo chake akiniambia anakufa bila kuona watoto kutoka kwangu tu, katika watoto wake wote watano zilikuwa haziishi, mpaka nikasalimu amri. Nikajiambia kama nikuzaa tu, nizae huyo mtoto aonekanike, sisi tuendelee na maisha yangu. Nilisogwa Pendo! Sina jinsi nikakwambia ukaelewa. Ilibaki ikawa hiyo ndio habari inazungumziwa tu pale nyumbani wala si ugonjwa wa mama tena. Walipojua tu kuwa mama hatapona, agenda ikageuka kwangu. Nilikuwa sina raha!” “Pole Willy, ndio maana ukageuka ukawa mtu wa hasira kwa vitu vidogo ambavyo havikuwahi hata kukusumbua!” “Hata sikuwa najua Pendo. Samahani sana. Ila amini nilikuwa nimevurugukiwa haswa. Gafla maisha yangu yakakosa maana kabisa sababu ya mtoto! Nikakubali ili kutulie, kumbe ndio najiingiza kwenye matatizo zaidi!” Pendo akatulia. Yakaendelea mabusu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mama K alirudi akakuta bado wanapeana mabusu. Akajua habari ya Pendo na Willy ndio imerudi upya. Akaona ajisogeza karibu ili wajue ni yeye ameingia, Willy aondoke, amuache Pendo apumzike. Akaona hawamwangalii, Willy amemuinamia Pendo pale kitandani akiendeleza mabusu. “Pengine ataruhusiwa kesho.” Pendo na Willy wakacheka na kuachiana. “Naona ukapumzike baba, ili na huyu naye alale, kesho kila mtu arudi kwake.” Wakazidi kucheka. “Basi naomba nimuage mama yangu. Nitaondoka.” “Dakika tano tu Willy mwanangu, ili alale huyo.” Mama K, akatoka kama kuwapa nafasi. Naye Willy akawa muungwana hata hakuchukua muda mrefu, akatoka kumfuata mama K nje.

Willy anataka kurudisha Majeshi kwa Upya.

“Usiku mwema Willy mwanangu.” “Nina shida kidogo mama. Naomba unisaidie.” Willy akamsogelea. “Kwa sasa sina rafiki wakaribu wala ndugu. Tumesambaratika sina wakumtuma kwenu. Nataka kumuoa Pendo.” Mama K akaanza kucheka. “Nataka taratibu za mahari.” “Unataka kuanza uppya?” Willy akacheka. “Vyovyote mtakavyoniambia mimi nitafanya wazazi wangu. Nisaidie tu kuzungumza na Mzee, nijue taratibu.” “Kwa nini usimtumie yule msimamizi wenu wa harusi?” Mama K akauliza. “Kwanza ile harusi waliyotusimamia, niliivunja. Pili wale walimuumiza sana Pendo. Japokuwa mimi nilikuwa nikizungumza na mwanaume, lakini ilikuwa ni kama tunalazimishia tu. Mahusiano yalibadilika. Naanza upya mama yangu.”  Mama K akacheka akifikiria. “Nitazungumza na baba K na Kenton, kisha tutakujibu.” “Nitashukuru ikiwa mapema.” “Sawa Willy.” Wakaagana safari hii wakicheka sio kama mwanzo alipokuwa njiani.

Asubuhi ya siku inayofuata, Willy alianzia hospitalini na maua mazuri, safari hii na kadi kubwa sana ya ‘I Love You’. Mama K akacheka Willy alipokuwa akiipanga mezani upande alipolazwa Pendo. “Bado amelala.” “Vipi lakini, wamelalaje?” Akauliza Willy wakati akiweka na maua hapohapo mezani. “Wamelala vizuri tu. Daktari wa zamu alipita usiku, akawaangalia wote, akasema wapo sawa na Pendo naye pressure ipo sawa sasa. Amesema kila kitu kikienda sawa, daktari atakayepita zamu asubuhi hii atamruhusu.” “Afadhali. Wametoa masharti yeyote?” “Na mimi niliuliza, hakuna jambo kubwa zaidi ya kuwa waangalifu tu na vitu vya msingi. Kama chumvi na kupumzika. Swala la kunywea kwa vimbe ndio linashangaza karibia wote. Naona swala la hatari ya hao watoto linaanza kupungua.” “Afadhali hata swala la honeymoon nalo litawezekana.” Mama K akacheka. “Kweli umekusudia!” “Kabisa mama. Naamini hapatakuwa na ugumu kwenye kuoa.” “Sio kwa baba yake.” Willy akasogea vizuri, akajua wamezungumza.

Wakatoka hapo ndani. “Kwa hiyo hakuna masharti?” “Yeye amesema hatapokea tena mahari ya pili. Heshima unayotaka kumpa Pendo, kumuoa tena kihalali, inatosha.” “Kweli mama!?” “Kabisa Willy mwanangu. Si mngerudi tu kuishi kwani nani angezuia? Lakini kurudi tena kuomba baraka za Mungu ni jambo zuri sana. Baba K amefurahi sana.” “Nashukuru sana mama yangu. Basi nitataka hata kutoa zawadi ya shukurani kwenu nyinyi wazazi, kwa kuwa naye kipindi mimi nilipomuacha. Angalau niwashike tu mkono.” “Hilo hatuwezi kukuzuia Willy mwanangu.” “Sawa. Lakini naomba swala la kumvalisha pete Pendo liwe la siri kidogo. Angalau apate kitu kipya na kizuri. Na yeye apate suprise ya kuchumbiwa.” Mama K, akacheka akionekana kuridhika. Wakazungumza kidogo, wakarudi ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa amevunja ndoa ya kanisani, Willy anamtaka tena Pendo. Atafanikiwa? usikose kufuatilia kuon Ilivyo rahisi kuvunja/kubomoa kuliko Kujenga.

 Jack & Sabrina nao?

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment